Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Lucy Thomas Mayenga

All Contributions

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia leo kusimama hapa na kwa kweli nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa sababu hiki ni kipindi changu cha tatu ndani ya Bunge, namshukuru sana Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya na Baraza la Mawaziri. Watu wamekuwa wanafanya kazi vya kutosha, wanapiga kazi ambayo inasifika sana na kila mtu kwa kweli anaona utendaji wao, ingawa kuna wengine wamezidi zaidi, wengine viwango vyao ni vya juu sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumzia kuhusu suala la makato ya kwenye kiinua mgongo. Hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha amegusa pabaya kwa Waheshimiwa Wabunge. Hata hivyo, nafahamu kwamba una busara sana, kwa hiyo utafikiria tena upya ili angalau mambo yakae vizuri sina haja ya kueleza zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza bajeti hii ni bajeti ambayo ina kila sababu ya kutuonesha na kutupa imani kwamba huko mbele tunakokwenda pako vizuri sana. Naisifu kwa sababu angalau imetuonesha na inatupa picha kwamba huko mbele yale ambayo tunayafikiria yameanza kidogo kuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala zima la uchumi wa viwanda. Tunapozungumzia suala zima la uchumi wa viwanda, najiuliza, kwamba tunazungumza kuhusu suala la uchumi wa viwanda je, tuko tayari? Kwa sababu tunaweza tukakaa tukazungumza mambo mazuri sana na tukawa na mipango mizuri sana, tukapiga makofi hapa tukawa na sifa nyingi sana lakini tusipofunga mikanda na kusema kwamba hapa sasa tumeamua kufanya kazi vya kutosha, haya masuala yataishia kwenye makaratasi na utekelezaji wake utakuwa ni mgumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu lipo jambo moja ambalo sijapata picha sawasawa, suala hilo ni la Inter-Ministerial Coordination. Wizara hii na Serikali hii kwa ujumla kwenye suala hili la uchumi wa viwanda, Wizara ya Kilimo inashirikiana vipi na Wizara ya Elimu, Wizara ya Nishati, Wizara ya Maji na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu tunapozungumzia uchumi wa viwanda, huu ni uchumi na ni biashara ambayo ni mkakati wa muda wa kati na muda mrefu. Sisi wengine siyo wafanyabiashara wakubwa, lakini angalau tunajaribu jaribu kidogo. Kwa hiyo, ninapozungumzia hivi ni kwa sababu tukisema kwamba tunazungumzia viwanda lazima tujiulize, Wizara ya Elimu imejiandaa kwa kiwango gani? Wizara ya Maji licha ya kwamba Tanzania ni Taifa ambalo ni la tatu duniani kwa wingi wa maji, imejiandaa kwa kiwango gani ili kuweza ku-facilitate? Kwa sababu kiwanda bila maji ni kitu ambacho hakiwezi kwenda. Wizara ya Kilimo imejiandaaje? Wizara ya Nishati imejiandaaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipokuwa makini tutajikuta kwamba watu wanakuja, wanasema sisi ni wawekezaji tunataka kuwekeza, mimi nataka kuja kuwekeza labda pengine kwa wananchi wangu wa Shinyanga kule, nataka nifungue kiwanda cha kitu fulani, lakini akikaa anaanza kwanza kujiuliza wakati anafanya due-diligence, hivi maji hapa nitayapataje? Anajiuliza hivi umeme bei yake na upo kwa kiwango gani? anajiuliza hivi kwa mfano, kama nikifanikiwa kama endapo nitawekeza kwenye kilimo, masoko yako wapi? Anajiuliza hivi, hapa nikifungua kiwanda human resource nitaitoa wapi? Kwa hiyo, haya ni maswali ambayo inatakiwa kama Serikali kwa ujumla wetu tujiulize kwa pamoja ili tuweze kuwa wote na kauli moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu sisi kama Watanzania, wapo Watanzania ambao tunafanya kazi vizuri sana, lakini wapo watu ambao wamezoea business as usual. Wao kazi yao mtu anaingia ofisini, tunaona hata kwenye ofisi na taasisi za Serikali, mtu anaingia asubuhi saa mbili anatoka saa tisa, uvivu na ile kukaa tu kwa kujiona kwamba mimi sina tatizo lolote yaani mtu anakaa tu ile laissez-faire imekuwa ni tatizo letu. Kwa hiyo, hatuna budi sisi kama Viongozi na Wanasiasa tuseme kwamba tumejiandaa vipi kwenye hili suala.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano tu mdogo nitolee, National Housing ni Shirika letu la Umma, lakini siyo wawekezaji, National Housing, wanajenga nyumba za Serikali wanaziuza, Wabunge tumekuwa mara nyingi sana tunapiga kelele kwamba nyumba hizi bei yake ni kubwa sana, lakini ukikaa na National Housing wanakwambia kwamba tunapokaa wakati tunaanza hii project ya kuanza kujenga nyumba sehemu, tunajikuta kwamba maji mimi mwenyewe National Housing ndiyo nivute, umeme mimi mwenyewe ndiyo nikae nifanye hizo jitihada, kwa hiyo unajikuta ile pesa ambayo unaiweka pale ni kubwa sana kiasi ambacho baadaye inabidi irudi kwa mlaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu suala zima la mifumo yetu pia. Mifumo yetu na system yetu ya nchi ya kuchukulia mambo, lazima tubadilishe pia sheria zetu za kazi kabla ya kuanza kukaribisha hawa wawekezaji. Sheria ya Kazi iliyopo sasa hivi inatakiwa iwe fair kwa mwajiri pamoja na mwajiriwa. Hivi sasa unakuta Sheria ya Kazi ime-base zaidi kwa yule mwajiriwa kiasi kwamba anajiona kama Mungu mtu, sasa nini kinachotokea?
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea sasa ni kwamba, watu wanafanya kazi, mtu anajua kwamba kwa mfano, mimi kama labda nafanya kazi kwenye shirika lolote labda pengine tigo, airtel na kadhalika, anaweza mwingine aka-misbehave, mwingine anafikia kiwango hata cha kuiba lakini haya mashirika na haya makampuni, hiki naomba Serikali kwa kweli tujitahidi sana, tuwe makini sana, tukae tujiulize na ikiwezekana tuunde timu ya kuangalia hawa wawekezaji tu tulionao hapa, sasa hivi kabla ya kuwakaribisha hawa wengine kwenye uchumi wa viwanda, wana matatizo gani? Maana kinachotokea sasa hivi, mtu anaiba airtel au anaiba tigo kwa mfano au anaiba sehemu nyingine yoyote lakini kinachotokea ni kwamba lile shirika au hiyo ofisi wanamchukua yule mtu wanamwambia tu naomba u-resign.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kutoa
mchango wangu. Nianze kwa kutoa shukrani zangu nyingi
sana kwa Waheshimiwa Wabunge wote walioko katika
Bunge hili kwa support kubwa waliyonipa na hatimaye sasa
nimekuwa Mrs. Jamal, ahsanteni sana. Haya makofi naomba
yaendelee mpaka mwisho najua kuna sehemu yatagoma.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe pongezi za
dhati sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa
Jenista Mhagama na Naibu wake Mheshimiwa Mavunde,
wanafanya kazi nzuri sana na kazi kubwa sana. Leo
nimesimama hapa, kwanza kwa kweli nina hasira kwa
sababu kuna baadhi ya vitu ambavyo havijanifurahisha hata
kidogo na kuna baadhi ya vitu ambavyo nikiviangalia
unamwangalia mtu halafu unasema; hivi huyu anategemea
nini? Unakosa majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa nafasi ya
kipekee nimpe pongezi zangu za dhati sana Mheshimiwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa sana
ambayo anaifanya yeye pamoja na Baraza lake la Mawaziri,
wanafanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi ambayo asilimia
32 ya mapato ya ndani yanakwenda kulipa madeni, katika
nchi ambayo malimbikizo ya madeni yapo asilimia sita, katika
nchi ambayo Mheshimiwa Rais anapozunguka au Waziri
Mkuu au Mawaziri wanapozunguka Rais anaanza kuombwa
kuanzia vidonge kwenye hospitali mpaka kwenye ndege
watu wanalalamika, Rais huyu kwa kazi hizi anazozifanya kwa
kipindi hiki kifupi alichofanya kazi, anastahili pongezi kubwa
sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukakaa hapa
kukaanza kuongea kirahisi rahisi kwamba Rais huyu amefanya
hivi, Rais huyu hafai, Rais huyu sijui amefanya hivi ni rahisi sana
kuongea namna hiyo, lakini Wabunge baadhi
wamezungumza; hivi sisi Waheshimiwa Wabunge maana nianze hata na mimi mwenyewe kwa sababu nipo humu
ndani; katika kipindi hiki cha 2016 mpaka sasa hivi mmefanya
nini kwenye Majimbo yenu? Hivi kila mtu akisema akae hapa
aanze kuulizwa orodhesha ulichokifanya atasema amefanya
nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema makofi
yaendelee najua yatagoma; mimi nimekaa hapa Bungeni
kwa kipindi cha miaka 12 kuanzia mwaka 2005 mpaka leo hii
niliingia hapa Bungeni nikiwa mdogo sana. Naomba kutoa
tahadhari kubwa sana kwa Wabunge ambao ni wapya na
hasa Waheshimiwa Wabunge ambao ni vijana. Wako watu
ambao ni Genuine kabisa kutoka pande zote mbili; kutoka
upinzani na pia na huku. Kuna watu ambao wakiongea
unajua kabisa huyu anaongea ni kwa kutoka kwenye
dhamira yake lakini kwa experience yangu kuna watu
nimeshuhudia tangu nimeingia hapa Bungeni miaka 12 hii
kuna watu wananunuliwa na ni Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wana interest zao
nyuma, mambo yao yameharibika, wanakuja hapa
wanataka kutuvuruga. Kuna mtu anakuja hapa anasimama
kwa sababu mume wake alikuwa fisadi ameondolewa
kwenye madaraka anasimama hapa anataka kutuvuruga.
Kuna mtu anakuja anasimama hapa kwa sababu alikuwa
anapewa pesa na mafisadi, mambo yamekuwa magumu
anakuja hapa anataka kutuvuruga, kila saa Serikali mbaya,
Rais mbaya, sijui vitu gani vibaya; tunaomba samahanini sana
hayo maneno yenu mnyamaze mkaongee huko barabarani.
Hapa tunataka tukae tuongee masuala ya maana, masuala
ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeishi Rwanda kwa kipindi
cha miaka kadhaa siwezi kusema ni miaka mingapi na kule
walikuwa wanajua mimi ni Mnyarwanda. Nimeishi uswahilini
ya Rwanda na nimeishi Masaki ya Rwanda; watu ambao ni
viongozi wanakuwa wazalendo, kuna mambo ambayo ni ya
msingi, mtu anakaa nazungumza kwa ajili ya nchi yao. Watu
wanakaa wana-discuss issues ambazo ni za maana leo hii tumekuwa viongozi ni mambo ya Twitter, sijui Whatsapp,
meseji za kipumbavu pumbavu ni aibu kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatakiwa tutumie muda
ambao huu tunao kukaa, kufanya mambo ambayo ni ya
maana. Kwa nini hatukai tukashauriana kwamba jamani
hebu tufundishane ujasiriamali tunafanyaje, hebu jamani
twende tukamfuate Mheshimiwa Waziri wa Fedha, jamani
Mheshimiwa hebu tusaidie, tunataka tujiunge Wabunge 20
tufungue kiwanda, Mheshimiwa Waziri wa viwanda hebu
tusaidie Wabunge 50 tunataka tukae tuweke mitaji yetu,
tunataka tufanye biashara ya maana, matokeo yake watu
mnakaa mnaanza kuchanganyikiwa, mnakuwa hamna hela
mkitoka hapa maisha magumu, mmekaa wengine hapa
mnapiga makelele, mnapata hizo nguvu kwa sababu mpo
ndani ya vyama vyenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatakiwa watu muweze
kukaa kila mtu amekuja hapa kwa nguvu yake na kila mtu
amekuja hapa kwa moyo wake na anajua yeye mwenyewe
nini kilichomleta. Sasa msikae hapa mnaanza ku-insight other
Members of Parliament to turn against the Government hii ni
adabu mbaya, mbaya, mbaya kupita kiasi. Kama mna
mambo yenu huko pembeni nendeni mkayamalize, kama
mna jambo lenu huko pembeni nendeni mkakae mkaongee
huko, lakini siyo mnakuja hapa eti Bunge zima likae liongee
mambo ya ajabu ajabu…
Taarifa....
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
nilichokisema nilisema kwamba, katika kipindi ambacho
nimekaa hapa Bungeni nimeshuhudia Wabunge wa aina hiyo
wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa
Waziri Mkuu afikishe salamu zetu kwa Mheshimiwa Rais aende
akamwambie kwamba tuko nyuma yake, tunajua kazi kubwa
ambazo anazifanya, tunajua Serikali hii kazi kubwa ambayo
inaifanya na tuko nyuma yake kwa njia yoyote ile. Hatuwezi
kunyamazishwa lakini ninachoweza kuwaambia, hawa
ambao wanaweza kupambana naye, yupo mpaka 2025
ambao wanadhani kwamba 2020 ni mwisho, they are very
wrong na wanajidanganya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwaambia hata
baadhi ya Wabunge ambao tuko huku kwenye Chama
chetu, kila siku nasema na kuna mtu mmoja nimeshawahi
kumwambia; You cannot win the fight with your Boss, you
are messing up with the very wrong person katika Awamu hii
ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo hapa Bungeni,
kipindi cha uchaguzi uliopita, wote tulikuwepo hapa labda
hawa wengine wageni ambao hawakuwepo lakini walikuwa
wanafuatilia. Baadhi ya Wabunge tulikuwa tunaona tabia
za ajabu ajabu walizozifanya ukiwa humu ndani, watu na
heshima zao. Mimi nimeingia hapa kwa mara ya kwanza
ulikuwa unamwona Mheshimiwa Mbunge unadhani kwa
sababu ya umri wake ni mtu mzima, ‘shikamoo Mheshimiwa’
baadaye unakuja kukaa baada ya mwaka mmoja, baada
ya miaka miwili, unasema kumbe hata ‘mambo’ hastahili kwa
sababu ya jinsi vitu anavyovifanya vya aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua na wala siyo
siri, tulikuwa tumekaa hapa, watu wakati wa uchaguzi,
makundi yaliyokuwepo, sasa mimi nasema hivi; kama yale
makundi yalikuwepo, kama ni masuala ya interest nyingine
ambazo tunazo tuachane na hizo biashara sasa hivi tukae tujenge nchi yetu. Tukae tufanye kazi, tukae tuanze kuangalia
maendeleo ya nchi yetu yanakwendaje, wengine hapa
kwanza hata muda wenyewe wa kuuliza maswali hatuna kwa
sababu unawaza biashara tu sasa unamshangaa mtu
mwingine kila saa amekaa ‘Serikali hii sijui imefanya hizi’ mimi
nasemaga hivi hawa watu wanatoa wapi muda? Mwisho
mtakosa Ubunge mrudi nyumbani kule maisha yaanze kuwa
magumu, shauri zenu. Ndiyo ukweli wenyewe si nyie mnajijua?
Niliwaambieni haya makofi yatafika mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata siku moja Simba
Wazungu wana msemo kwamba; “The lion does not turn
around when a small Dog barks” Kwa hiyo, naomba
Mheshimiwa Waziri Mkuu wala msihangaike na hawa watu
ambao wanapiga makelele ya ajabu ajabu, maneno ya
ajabu ajabu, wanasema vitu vya ajabu ajabu, ninyi kaeni,
fanyeni kazi mwendelee kuwepo kwenye mstari na tuko
pamoja, tunaowaunga mkono ndani ya hili Bunge ni wengi
zaidi kuliko hawa wachache ambao wanapiga makelele.
Tuwaache waendelee kupiga makelele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niseme;
watakuja siku moja kula matapishi yao, wapo watu ambao
tumewashuhudia leo mtu anasema hivi kesho anakuja
unamshangaa huyo huyo anasimama Serikali hii nzuri sana.
Unashangaa haya maneno ametolea wapi, watakuja kurudi
kula matapishi yao lakini wakati huo tutakuwa tayari
tumeshawajua.
Mheshimimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nina hasira
sana. Naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's