Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Selemani Said Bungara

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amenipa mimi umaarufu na kuwa Selemani Bungara Bwege, pia kwa kukupa Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa mjanja kwa hiyo, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, nawashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Kilwa Kusini, mwaka 2010 nilishinda kwa kura 500 kuna watu wakasema wewe umemuonea tu Madabida nitamwita Mhindi Bin Asineni, mwaka huu nimempiga kwa kura 5,595. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba CCM mjiandae mumlete mgombea mwingine nimpige tena. Kwa mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili mambo mengi yamesemwa hapa, lakini naomba vijana wangu wa upande wa UKAWA msiwe na wasiwasi, humu ndani sasa hivi hatupambani na Serikali ya CCM, humu tunapambana na Serikali ya Magufuli na tunapambana na Serikali ya Mapinduzi, CCM hamna Tanzania sasa hivi, hii ni Serikali ya Magufuli na Serikali ya Mapinduzi.
Sasa mkitambua kwamba tunapambana na Serikali ya Magufuli, tusimlaumu sana Magufuli kwamba ndiyo kwanza anaanza na wamekubali wenyewe Serikali ya CCM kwamba tulifikia hapa na udhaifu huu ni kwa ajili ya Serikali iliyopita ya CCM, hii sasa ni Serikali ya Magufuli. Kwa hiyo, tutamwona Mheshimiwa Magufuli kwa miaka yake hii mitano atafanya nini akishindwa na yeye tutamwajibisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nawashukuru sana vijana wangu wa UKAWA tushirikiane tuzidi ili 2020 tuielekeze kibla Serikali ya Magufuli maana yake CCM tena hakuna nchi hii. Waheshimiwa nimepokea pole, kuna watu hapa wametaka kulia hapa eti kwa sababu…
Bunge lisioneshwe live wanataka kulia, aah, mimi nilifikiri wanataka kulia kwa sababu watu hawapati maji vijijini…
TAARIFA....
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa siipokei kwa sababu anapingana na mwenyewe Mheshimiwa Magufuli, kila siku anasema kwamba Serikali yangu, wakati mwingi anasema Serikali yangu hasemi Serikali ya CCM, kwa hiyo siipokei taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu bado saba ilikuwa tatu tu, narudia kusema kwamba napenda sana Wabunge msililie kwamba Bunge lisioneshwe live mlie kwa kuwa watu hawapati maji, hawapati tiba vizuri, hawapati elimu. Nashangaa sana mtu anayelia anaomba kulia, mimi ninavyojua kulia kuna mambo mawili tu, utamu au uchungu, na ukipata utamu au uchungu huombi kulia unalia tu, ukimwona mtu anaomba kulia au anatamani kulia hataki kulia huyo. Ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naanza na mambo ya viwanja vya ndege, katika kitabu ukurasa wa 99 nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwamba anaanza mchakato katika Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko, nimefurahi sana, lakini Uwanja wa Kilwa Masoko walikuja kutathmini mwaka 2013 na tathmini ya uwanja ili upanuliwe bilioni mbili, milioni themanini, laki nne na sitini elfu mia mbili na sitini mpaka leo, wametathmini watu wale hawajawalipa. Leo wanasema wanafanya mchakato ili wapanue sasa kabla bado hawajafanya mchakato huo wakawalipe wapiga kura wangu, 2,080,460,260, mkawalipe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013/2014, 2015/2016, wanawaambia wasiendeleze majumba wala wasilime mashamba yao mwaka wa tatu sasa hivi au wa nne. Naomba sana katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri aniambie kwamba lini watakwenda kuwalipa wale watu ili waendelee na mchakato wa kuupanua uwanja huo. Kama hawakuniambia lini wanataka kuwalipa nashika shilingi. Najua mtapiga kura nyinyi mko wengi, lakini shilingi mimi nitaishika safari hii isipokuwa katika majumuisho yake akiniambia watawalipa lini kesi imekwisha kwa sababu Serikali ya Magufuli ndiyo kwanza inaanza, sisemi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili barabara, katika ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyepita kulikuwa na ahadi ya barabara ya kwa Mkocho – Kivinje, lakini mpaka leo. Mheshimiwa Majaliwa alikuwa Waziri akasema kabla ya Uchaguzi, uchaguzi umekwisha, naomba Waziri Profesa, Msomi leteni hela hizo barabara ya kwa Mkocho – Kivinje ijengwe, maana yake kuna watu hapa wa CCM wanasema Majimbo upinzani usipeleke hela, jamani ehee mimi nilipata kura elfu kumi na tano, Asineni elfu kumi, Mheshimiwa Magufuli alipata elfu kumi, Mheshimiwa Lowassa alipata elfu kumi na nne, haya hizi elfu kumi za Mheshimiwa Magufuli ndiyo zimemfanya yeye ashinde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukisema kwamba Jimbo la Kilwa huleti maendeleo kwa sababu Magufuli hakushinda mnawaumiza elfu kumi waliomchagua Magufuli, haki sawa kwa wote timizeni. Sina wasiwasi, kama hamkuleta hayo nitashinda zaidi kwa sababu kila ukimuumiza mtu wa Kilwa basi anazidi kupata uchungu anaipiga CCM, leteni Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nangurukuru – Liwale itiwe lami, sisemi sana amesema Mheshimiwa Bi Lulida hapa, Naiwanga – Nainoko – Ruangwa mtengeneze, mjenge. Kilanjelanje na Njilinji mmepanga milioni 85, jamani ehee milioni 85 haifai, haitoshi tuongezeni hela, mvua ya mwaka huu, mafuriko ya mwaka huu barabara yote imekufa tunaomba hela iongezwe, naomba sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, siisemi sana Serikali ya CCM kwa sababu tayari ishashindwa na wenyewe Mawaziri mmesema kwamba Serikali yetu ilikuwa dhaifu, ilikuwa haikusanyi hela, ilikuwa hivi, lakini Serikali ya Magufuli inakusanya hela haina udhaifu, wala siilaumu Serikali ya CCM iliyopita, najua nitailaumu Serikali ya Magufuli mwakani siyo mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kuna vijiji kumi havina mawasiliano ya simu Nainokwe, Liwitu, Kikole, nawaomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri watuletee mawasiliano watu wapige simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya, bandari, nimeangalia humu Bandari ya Kilwa haipo, lakini gesi ya Kilwa akisimama Mheshimiwa Muhongo hapa, gesi ya Kilwa italeta mambo, ehee, lakini watu wenyewe wa Kilwa thuma amanu thuma kafara. Naomba bandari nayo muiangalie, sasa gesi hiyo mngeipitisha wapi? Naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, sisi watu wa Kusini mnatuonea, maendeleo yote mnawapa watu wenye maneno mengi tu huku. Sisi wengine hatujui kusema, wanyonge, tunaomba Serikali ituangalie. Kuna mradi wa maji, kuna wafadhili kutoka Ubelgiji, basi mpaka leo hawataki kutuletea, tangu mwaka 2014, Mbelgiji amesema anatuletea maji hamtaki kutuletea maji. Kwa sababu gani, sisi watu wa Kusini tu! Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini awali ya yote, napenda kukupongeza kwa kuchaguliwa tena kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Wizara nyeti na muhimu katika Tanzania yetu. Mwenyezi Mungu akuzidishie busara na hekima.
Pia napenda kukupongeza kwa katika hotuba yako ukurasa wa 36 mpaka 37 kwa kuturejeshea mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea, mradi utakaogharimu Dola za Kimarekani bilioni 1.98 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 411.24. Natoa shukrani kwa Serikali kwa kutupatia mradi huu mkubwa kwa maendeleo ya Kilwa na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote hayo, Jimbo la Kilwa Kusini, pamoja na gesi inatoka katika Jimbo la Kilwa Kusini lakini katika mradi wa umeme vijiji REA, kwenye Jimbo la Kilwa Kusini ni Kijiji kimoja tu cha Matanda ndicho kimepata umeme katika mradi wa REA. Mheshimiwa Waziri naomba vijiji vifuatavyo vipate umeme wa REA: Pande, Mtilimita, Namwando, Nakimwera, Nangao Malalani (Kata ya Pande), Rushungi, Kisongo, Ruyaya, Lilimalya Kaskazini na Kusini, Namakongoro (Kata ya Linimalyao), Makangaga, Nakia, Nanjilinji „A‟ na „B‟ (Kata ya Nanjilinji), Likawange, Mirawi, Nainokwe (Kata ya Likawaga) Kilole, Ruatwe, Kisangi, Kimbarambara (Kata ya Kikole).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Wilaya ya Kilwa Jimbo la Kilwa Kusini ndilo Jimbo litowalo gesi asili kwa heshima na taadhima lipewe kipaumbele katika mradi wa umeme vijijini. Natanguliza shukrani. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukuwezesha wewe kuwa Mwenyekiti wa kikao hiki na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa Urais Mheshimiwa Magufuli na kuapa kwamba atailinda Katiba ya Jamhuri ya Tanzania, lakini kwa bahati mbaya tu Katiba yenyewe kidogo anaipindisha pindisha kwa sababu hatoi haki kwa Vyama vya Siasa kufanya mikutano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si nimetoa shukrani? Mimi nimetoa shukrani tu wala sikumtukana mtu yeyote. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa shukrani hizi kwa Mwenyezi Mungu leo najielekeza kuchangia katika sehemu mbili tu katika hotuba hii. Tunakumbuka 2010 Rais aliyemaliza muda wake Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Mungu amzidishie, aliahidi kwamba katika kampeni yake ya 2010 aliahidi kwamba atatengeneza barabara ya Kwa Mkocho – Kivinje barabara ya kilomita 4.2 kwa kiwango cha lami, mpaka leo nisemavyo barabara kwa mvua za jana tu na juzi gari zilikuwa hazifiki katika Hospitali ya Wilaya kutokana na barabara hiyo kuwa chafu na haipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti ya 2016/2017, tulitenga milioni 800 kwa ajili ya barabara hiyo ili ikamilike kwa kiwango cha lami, lakini mpaka sasa hivi nisemavyo ndege zimenunuliwa lakini fedha hizo za bajeti hazijaingia katika Wilaya ya Kilwa ili barabara hiyo itengenezwe. Pamoja na ndege mlizonunua hizo lakini mkumbuke kwamba kuna barabara ambazo ni muhimu sana zinaenda katika hospitali za Wilaya, nazo zikumbukwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri naomba hizo milioni 800 zipatikane ili babaraba ile iishe. Tena kwa bahati nzuri tarehe 2 Machi, 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Dkt. Magufuli alifika Kilwa na nikamwambia tatizo hilo kwamba kuna kiporo cha Rais aliyepita na nikamwomba kiporo hicho amalizie yeye. Akaahidi na kumuagiza Injinia kwamba hiyo barabara iishe.

Naomba sana naomba, kwa kuwa Mheshimiwa Magufuli hasemi uwongo na alisema kwamba barabara lazima naomba barabara hiyo iishe ili watu wapate kutumia barabara hiyo na kufika katika hospitali kwa njia ya usalama. Bila hivyo watu wa Kivinje na Wilaya ya Kilwa kwa ujumla tutaona kwamba hatutendewi haki tunaonewa bila sababu ya msingi. Naomba Mheshimiwa Waziri barabara hiyo iishe na fedha hizo milioni 800 zipatikane katika mizezi mitatu iliyobaki ili barabara hii iishe. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni uwanja wa ndege. Kilwa Masoko kuna uwanja wa ndege, uwanja huo kulifanywa tathmini kwa wananchi wangu tarehe 19 Machi, 2013 ili walipwe fidia ili uwanja upanuliwe. Mpaka leo ninavyoongea tangu 2013 mpaka leo 2017 wananchi wangu hawajapata fidia. Naomba sana katika kuhitisha hotuba yake Mheshimiwa Waziri atuambie hawa wananchi wangu watapata lini fidia hiyo ya uwanja wa ndege na kama haiwezekani mseme kwamba haiwezekani.
heshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ingawa dakika tano hazijatimia lakini imeeleweka.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwingi wa huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Rais katika Serikali ya Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Kikwete aliahidi kujenga barabara ya Singino (Kwamkocho) - Kivinje ya urefu wa kilometa 4.2, barabara hiyo inaelekea katika Hospitali ya Wilaya. Ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kwa umuhimu wa barabara hiyo ya kiwango cha lami, lakini kwa bahati mbaya mpaka leo, hiyo barabara ni tatizo. Katika bajeti ya 2016/2017, ilipitishiwa sh. 800,000,000/= kwa ajili ya kumalizia barabara hiyo lakini hadi leo hakuna kilichopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, mwaka huu wakati alipotutembelea nilitoa kilio changu hiki cha barabara ya kiwango cha lami katika Hosopitali ya Wilaya. Alimwagiza Meneja wa TANROAD Mkoa wa Lindi amalize kero hii ya muda mrefu. Kwa heshima na taadhima naomba fedha ya bajeti ya 2016/2017, sh. 800,000,000/= zipatikane ili mradi huu wa barabara muhimu ya Kwamkocho - Kivinje ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, pia asimamie agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli aliyoagiza Nangurukuru kuwa Meneja wa TANROAD kuwa awasiliane na Wizara ili kero hii imalizike. Naomba kwa heshima na taadhima asimamie barabara hii muhimu kwa ajili ya faida ya kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaona katika bajeti hii mwendelezo wa Uwanja wa Ndege na Bandari ya Kilwa Masoko. Naomba katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri anipatie taarifa ya Uwanja wa Ndege na Bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vile vile Mheshimiwa Waziri anifahamishe, malipo ya wananchi waliotathminiwa katika eneo la Uwanja wa Ndege. Katika majumuisho yake napenda kujua malipo ya wananchi hawa kwa muda sasa wa miaka mitatu hawajalipwa, ni lini watalipwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda kusisitiza:-

(a) Barabara ya Kwamkocho – Hospitali, ambayo ni ahadi ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Kikwete.

(b) Bandari na uwanja wa ndege.

(c) Malipo ya wananchi waliotathminiwa katika eneo la Uwanja wa Ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufafanuzi katika hizo kero zangu na naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukurani kwa kunipa nafasi hii ili nichangie. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi ili tuitumie sisi binadamu katika maendeleo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya maji na kila kiumbe ana asili ya maji, sisi binadamu tumepatikana kutoka na asili ya maji. Hata hivyo miaka 56 ya Serikali ya CCM tunazungumzia habari ya maji. Tunakwenda vijijini kuomba kura ajenda yetu kubwa ni kwamba mkinichagua kuwa Mbunge mtapata maji, miaka 56.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema Mheshimiwa wa Mtama hapa, Ilani ya CCM mliwaahidi Watanzania kwamba mtapata maji kutoka asilimia 67 mpaka 85. Mimi Jimbo langu au Wilaya yangu ya Kilwa maji vijijini ni asilimia 48.3. Tunaomba sana maji safi na salama. Tunaomba sana, bajeti ya maji lazima iongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa 2016/2017 tulipangiwa au tulipitisha bajeti ya bilioni mia tisa hamsinitukapata asilimia 19, mwaka huu bilioni mia sita sasa ukipata asilimia 16 utajua mwenyewe itakuwa shilingi ngapi maana itapungua. Naomba sana bajeti hii ya maji irudi iende ikaongezwe fedha kama zilivyoongezwa mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia Mradi wa Maji wa Mavuji. Katika bajeti ya 2016/2017, ukurasa wa 142 kulikuwa na mradi wa maji katika Mji wa Kilwa Masoko. Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa chanzo, mitambo ya kusafishia na kutibu maji, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa matanki, ukarabati wa upanuzi wa mabomba ya kusambaza maji. Mahitaji ya fedha euro milioni 61.67. Maelezo, majadiliano ya Serikali na Ubeligiji kupitia kampuni ya Aspec international yanaendelea. Usanifu umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya! Nataka nijue toka kwa Mheshimiwa Waziri, mazungumzo kati ya Aspec na ninyi yameishia wapi? Mradi huu ungesaidia upatikanaji wa maji katika miji midogo miwili ya Kilwa Kivinje na Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, lakini sasa hivi ni miaka mitano maneno tu, maneno tu, kesho, kesho kutwa, kucha maneno tu. Oh haa! Mheshimiwa Waziri leo nataka aniambie mchakato huu umefikia wapi ama sivyo kwa mara ya kwanza nataka nitoe shilingi;.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana. Serikali ya CCM kwa miaka 56 imeshindwa, tunataka kuiangalia Serikali ya Magufuli, maana Serikali CCM haipo, sasa hivi kuna Serikali ya Magufuli. Tunataka tuione Serikali ya Magufuli kwa miaka hii mitano itamaliza tatizo la maji? Kama haikumaliza tatizo la maji katika Tanzania, basi Magufuli bye bye (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali ya Magufuli ikishindwa kutatua tatizo la maji bye bye mwaka 2020, kwa herini. Waheshimiwa maji si mchezo, huwezi kuishi bila maji, huwezi kulala na mama bila maji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, bila maji hakuna kila kitu, watoto hawapatikani bila maji. Tunaomba hilo jambo la maji na hii bajeti lazima irekebishwe ili Watanzania tupate maji. Naunga mkono kabisa; utampata wapi mtoto bila maji? (Vicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kule Kilwa kuna mradi wa maji tangu mwaka 1992, Kilwa sehemu ya Mpala. Watu walitathminiwa lakini tangu 1992 mpaka leo hawajalipwa fidia, mpaka leo! Maji wameyachukua Mpala wameyapeleka Masoko lakini Mpala penyewe pale maji hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana katika majumuisho leo Mheshimiwa Waziri aniambie watu wa Mpala fidia yao watalipwa lini? Naomba sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji alikuja Mpala na akawaahidi watu wa Mpala kwamba lazima hela zao watapata, nataka nijue leo Serikali sikivu ya Mheshimiwa Magufuli mtoe kauli leo nisikie kama si hivyo sijapata jibu sawasawa nasema kweli Serikali ya Mheshimiwa Magufuli si Serikali sikivu. Kama sikivu kweli nijue kwamba watu wale fidia zao zimetoka au zitatoka lini. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, naomba sana msimtie aibu Mheshimiwa Magufuli, Magufuli ni mzuri pengine wabaya ni ninyi hapo. Magufuli mzuri ana tatizo moja tu, anabinya demokrasia, hapo tatizo analo, lakini mengine hana matatizo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana; kuna matatizo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Riziki Saidi Lulida

Special Seats (CUF)

Contributions (15)

Profile

Hon. Shamsi Vuai Nahodha

Kijitoupele (CCM)

Contributions (4)

Profile

View All MP's