Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Pauline Philipo Gekul

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweke mawazo yangu katika hoja ambayo iko mbele yetu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa afya njema ili tuendelee kutekeleza wajibu wetu ambao Watanzania wametukabidhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Jambo la kwanza ambalo Serikali imeona na naomba ninukuu na hili jambo limenishtusha. Ukurasa wa 22 katika kitabu cha Hotuba ya Waziri, anasema kwamba; “Mapato yote yatakusanywa na Wizara ya Fedha, mapato ambayo yanatoka katika Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa watatakiwa kuwasilisha mapato yote yatakayokusanywa yawasilishwe kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na yatagawiwa kulingana na bajeti za mafungu zitakazoidhinishwa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni kubwa sana, picha ninayopata hapa Halmashauri zetu zitakufa. Amesema mapato yote na kimsingi ukiangalia tunakwenda kuua Serikali za Mitaa. Leo tutakusanya mapato ushuru wa stendi, wa wafanyabiashara, chochote ambacho Halmashauri zetu wanakusanya tuweke kwenye Mfuko wa Serikali. Tukumbuke historia ya ugatuaji madaraka katika Serikali zetu (decentralization).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1982 Baba wa Taifa alijuta tulivyofuta mfumo mzima wa Serikali za Mitaa; barabara hazikwenda, hospitali zilikuwa mbaya na mwaka 1980 wanakumbuka wale waliosoma historia, kwamba ilifikia hatua hata outbreak ya cholera ilishindikana kuzuiwa huko chini kwa sababu kila kitu kilifanywa na central government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunarudi kule ambako Muasisi wa Taifa hili aliona kulikuwa na tatizo na alijutia na akasema hili jambo halitojirudia tena. Serikali hizi za Mitaa wamepewa mamlaka kwa mujibu wa Sheria zetu za mwaka 1982. Wana mamlaka ya kuajiri, mamlaka ya kukusanya mapato na kuyatumia kwa kiasi fulani, lakini wana mamlaka pia ya kutunga sheria mbalimbali ambazo zinasaidia katika kukusanya ushuru huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapotaka pesa zote katika nchi hii tukusanye at central level, halafu tutengeneze bajeti zetu huku chini, tupeleke Serikali Kuu wao ndiyo waanze kutupimia, athari yake ni nini? Athari yake tutaua morali ya wale wanaokusanya hizo kodi ndogo ndogo huko chini, kwa sababu maendeleo hayataonekana; kutakuwa na ubaguzi wa kupeleka fedha hizo katika Halmashauri hizo, japo watu wengine wanakusanya, lakini pia hapatakuwa na maendeleo huko chini kwa sababu fedha haziendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli; ukiangalia bajeti ya Serikali kwa muda mrefu, fedha za own source katika Halmashauri zetu ndiyo zinasaidia miradi ya maendeleo mbalimbali, miradi midogo midogo. Hizo fedha ndiyo zinasaidia kuchonga barabara zetu, lakini angalia fedha zinazotoka Hazina haziendi kwenye Halmashauri zetu kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kwenye bajeti ya mwaka jana, mwaka juzi, hata katika hivi vitabu, inaonyesha fedha za wafadhili ndiyo zinakuja kuliko fedha zinazotoka Hazina. Nitoe mfano, katika Halmashauri yangu ya Mji wa Babati, 11% tu ya fedha za Hazina ndiyo zimeingia na ni miaka yote fedha zinazotoka Serikali Kuu haziingii. Kwa kubariki kila kifanyike at central level, huku chini watu wakusanye tu halafu watu wachache wapange, tupeleke sehemu fulani, tusipeleke sehemu fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo nakuhakikishia tunaua Halmashauri zetu, hakuna maendeleo yatafanyika, mtafanya mambo yenu makubwa makubwa katika central level, lakini yale yanayohusu maslahi ya wananchi wa hali ya chini na maendeleo yao nakuhakikishia tunarudi kwenye historia ya mwaka 1980 ya jinsi ambavyo decentralization, Baba wa Taifa Mwalimu aliona kwamba ni jambo muhimu sana kwa sababu central level hawawezi kufanya wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imebariki kwamba hizo sheria ziangaliwe, maana yake Sheria inayotajwa ni mwaka 1982 ya Serikali za Mitaa, kwamba sasa tunachukua uhuru wa Serikali za Mitaa kukusanya kodi zao na kuzifanyia matumizi, Serikali Kuu ndiyo inafanya. Naomba Bunge hili tusithubutu kufanya hivyo, bali tusaidie Serikali za Mitaa kubainisha vyanzo ambavyo hawakusanyi, tuviimarishe na Sheria hizo ziimarishwe badala ya Serikali kuu kuchukua madaraka yote. Sasa tunakusanya kila kitu at central level, hatuwezi tukapitisha kitu kama hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa retention premium ya ardhi 30%, hizo fedha huwa hazirudi. Tunauza viwanja huko, tunapeleka makusanyo yote ardhi, Wizara ya Ardhi hawapelekewi hizo pesa na Wizara ya Ardhi wao wakipata chochote na wanajitahidi chochote wanachopata kutoka Hazina wao wanapeleka 30% katika hizo Halmashauri, lakini Serikali Kuu, Hazina hawapeleki hizo fedha hata hiyo tu premium ya ardhi hawapeleki. Iweje leo tuwapelekee eti fedha zozote tunazokusanya kwenye Halmashauri zetu, tupeleke kwenye Serikali Kuu. Tunaua Halmashauri zetu na maana yake tunaua suala zima la Serikali hizi mbili Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, wanataka sasa kila kitu wafanye wao. Hiki kitu Bunge hili tusifanye vinginevyo maendeleo yatakwama katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la service levy. Wamezungumza hapa ushuru wa huduma na vitu kama hivyo. Kwa muda mrefu tumeishauri Serikali, suala la mitandao ya simu ni chanzo kimojawapo katika Halmashauri zetu. Leo mitandao hii wamiliki wa makampuni haya ya simu ushuru wa huduma wanaolipa haueleweki kwa sababu Halmashauri imefikia hatua wanakusanya sijui ushuru wa nguzo, sijui service levy, hiyo asilimia zero point three Wizara ya TAMISEMI mwaka jana na Wizara ya Mawasiliano walikaa chini wakasema watashauriana na wakaandikiana barua kwamba wakusanye katika central level. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pata picha mpaka leo hawajawahi kukaa, hawajawahi kupeleka kwenye hizo Halmashauri kwamba ni kiasi gani wanastahili kupitia kwa makampuni haya ya simu, hata hilo kama tulishindwa, tunathubutuje leo, eti kwenda kuchukua hata vile vyanzo ambavyo kidogo tunajitahidi Halmashauri zetu zinakusanya, lakini sisi at central level kitu ambacho Wizara mbili walitakiwa wakae wa-reconcile wapi ambapo haya makampuni hayalipi, halafu zile asilimia zigawanywe zipelekwe kwenye Halmashauri zetu equally hawapeleki.
Leo tunaua Halmashauri zetu tunasema tunafanya sisi, wakati ya premium ya ardhi mmeshindwa, hii service levy mmeshindwa, halafu Serikali Kuu, hivi kweli hiki kiburi kinatoka wapi cha kusema kwamba, sasa ninyi mnakusanya, halafu mtugawie sisi tuwaletee tu bajeti. Hili ni jambo kubwa sana na ninaona kama hatujalipitia na hatujalielewa vizuri, lakini kama tukipitisha jambo hili ambalo linapendekezwa katika ukurasa wa 22, tumeua Serikali zetu za Mitaa totally.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize sana kuhusu hili tusilipitishe na tuliangalie kwa upya, lakini suala zima la kurasimisha biashara zetu ni kwa nini sijaona Mpango unaoonesha vijana wetu ambao wanafanya biashara ndogo ndogo waweze kuboreshewa maeneo yao. Kwa muda mrefu hata kwenye Hotuba ya Rais alizungumzia suala zima la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa vijana wetu, Wamachinga. Hawa wakipangwa pesa zikatengwa, zikajengwa shopping malls ambazo zitasaidia vijana wetu tukawapanga, watalipa ushuru katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea leo, hawa wafanyabiashara wanaokuwa taratibu, hawajawahi kupangwa kokote, hawajawahi kutengewa maeneo, lakini kingekuwa ni chanzo kizuri ambacho tukakaa tukawaangalia jinsi gani Serikali za Mitaa wakapanga maeneo kwa ajili ya hawa vijana, wakafanya biashara wakalipa ushuru mbalimbali na tozo mbalimbali, itasaidia sana kuongeza mapato ya Serikali. Kwa hiyo, nishauri kwamba inawezekana Serikali inawaza mambo makubwa, bandari, sijui ndege, sijui vitu gani wakati kuna watu ambao wakipangwa tu wanaweza wakasaidia kuleta marejesho katika Mfuko wetu na katika Halmashauri zetu ili tuone ni jinsi gani ambavyo tunaweza tukafanya maendeleo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda vidogo vidogo ambavyo vinaweza vikaajiri hawa vijana, limezungumziwa lakini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru ili na mimi niweze kuchangia machache katika Wizara hii ya Elimu, Wizara muhimu sana na awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya ambayo anayoendelea kunijaalia ili niweze kutoa mchango wangu katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Babati Mjini ambao wamenipa dhamana ya kuwa Mbunge wao wa Jimbo na niwaahidi sitowaangusha na baada ya Bunge tutaendelea kuwa pamoja ili tuendeleze Jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niombe Waziri anisaidie kwa sababu hapa tunazungumza suala zima la bajeti. Naomba tu anisaidie katika bajeti yake kabla sijaenda mbele zaidi katika kitabu chake cha Development, kwenye Vote 1003, amezungumzia suala zima la rehabilitation of the schools and colleges. Ametenga shilingi 8,153,000,000 lakini ukienda kwenye randama hii, Mheshimiwa Waziri ulichokiandika huku kwamba unafanya marekebisho ya shule zetu sicho ulichoandika, unaomba na nafikiri umefanya hivyo kwa sababu mkijua wengi Wabunge hatusomi randama, umeandika fedha hizo shilingi bilioni nane unajenga ujenzi wa ofisi ndogo ya Wizara Dodoma pamoja na ukarabati wa Makao Makuu ya Wizara shilingi 6,153,000,000 lakini ukaandika kwamba ni ukarabati na upanuzi wa Taasisi ya elimu ya Watu wazima shilingi bilioni mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo shilingi 8,153,000,000 huku ulivyotuandikia kwamba unafanya rehabilitation ya schools, sicho kabisa ni uongo na niombe majibu ya kina kwa sababu shilingi bilioni nane ukigawa kwa idadi ya madarasa ni zaidi ya madarasa 1,000 yanatakiwa yajengwe kwa fedha hizo na nasema hivyo kwa sababu mmekuja na sera ya elimu bure, watoto wanakaa chini Mheshimiwa Waziri kipaumbele chako ni kujenga ofisi yako kwa shilingi bilioni sita na shilingi bilioni mbili ilihali ukijua watoto wa Kitanzania wanakaa chini, chini ya Wizara yako.
Kwa hiyo, nahitaji uniambie ni kwa nini Waziri mwenzetu, mwanamke mwenzetu, mwenye uchungu kwa watoto wa Kitanzania unatenga fedha zaidi ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya ujenzi wa ofisi yako ilihali watoto wanakaa chini na Wizara hiyo unaongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa la Kitanzania literacy level yetu ni asilimia 67. Watanzania wengi zaidi ya asilimia 30 bado kusoma na kuandika ni tatizo. Lakini kwa hali ya kawaida Taifa hili ambalo linapigana vita, maaskari hawa ambao wako vitani wamesahauliwa kwa asilimia zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu kama Mbunge wa Jimbo nilikaa na walimu wangu kuwafikia kwenye shule zote zaidi ya 30 katika Jimbo la Babati Mjini. Wala haya ninayoyachangia siyabahatishi na maaskari na walimu hawa ambao wanapambana na ujinga katika Taifa la Tanzania na naamini haya nitakayosema ambayo nimeambiwa na walimu wangu wa Babati ndiyo wanayopata walimu katika nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la madaraja walimu wetu. Mmetoa miongozo kwa miaka mitatu mnapandisha madaraja lakini walimu wanaofundisha huko katika shule zetu wanakaa miaka minne hawajapandishwa madaraja, lakini Mheshimiwa Waziri mnawapandisha madaraja kwa ceiling ya bajeti. Mimi naomba niishauri Serikali, kwanini mnawagawa walimu na maaskari hawa ambao wanapigana katika Taifa la Tanzania kuondoa ujinga? Kama hakuna fedha msiwagawe walimu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna walimu wanaajiriwa pamoja, kwenye madaraja wanatofautiana, kwenye mishahara wametofautiana, kwa nini? Mnapeleka wachache eti ukomo wa bajeti wengine wasubiri, nani kakwambia hivyo Mheshimiwa Waziri? Huu ni ubaguzi, walimu hawa kama hakuna fedha subirini mkipata muwapandishe hata kwa miaka mitano wote au miaka minne badala ya kuwagawa, hilo naomba majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wanaohamishwa kutoka Mkoa mmoja kwenda mwingine, Halmashauri nyingine kwenda nyingine akifika anaanza upya, daraja halipandi, anaambiwa huko ulikotoka ndiko ambako mambo yako yamekosewa, hebu Waziri tuambie leo hivi kuhamishwa ni dhambi kwenda kusaidia sehemu nyingine? Kwa nini walimu hawa wakihamishwa kwenda Halmashauri nyingine madaraja yao wanaanza upya, hawaendelei na madaraja waliyonayo? Unaongoza hiyo Wizara tupe majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti lakini lingine, hivi Serikali haina mpango kazi kwa walimu? Transport allowance? Leo anaibuka Makonda anasema walimu wapande mabasi bure. Msiwalipe transport allowance kwa nini? Yaani Serikali mmeacha walimu yeyote aamue kwamba hawa leo wapande bodaboda, hawa wapande mabasi bure, hawa wakejeliwe hivi kwa nini? Muwalipe walimu wetu transpot allowance. Sitting allowance hamuwalipi, yaani mwalimu hana shift yoyote, kwanza wanalalamika muda wanaingia saa moja wanatoka saa kumi, hawana wa kuwapokea wakati madaktari, manesi na fani zingine wana-shift lakini pia wanalipwa on call allowance, mwalimu halipwi housing allowance, sitting allowance wala transport allowance, umempeleka kijijini kule hakuna nyumba. Hivi kweli Mheshimiwa Waziri umekaa kwenye Wizara hiyo kwa muda mrefu, haya matatizo unayafahamu, leo nahitaji majibu kwa ajili ya walimu wa Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Waraka wa Elimu Bure, sawa, mmeiga kutoka kwetu UKAWA elimu bure mkakurupuka mkaanzisha. Haya mtuambie na mimi niliuliza swali kwa Waziri Mkuu, ni kwa nini mmekurupuka katika hili la elimu bure? Mnachokifanya sasa hivi shule zetu hakuna pesa. Shule ya wanafunzi 800 mnapeleka OC ya shilingi 200,000. Madeni katika shule zetu, Mheshimiwa Waziri tangu mwaka jana shule zinadaiwa pesa za ulinzi, za maji, za umeme kila shule yangu niliyopita inadaiwa zaidi ya milioni tano. OC ya shilingi 200,000 inaendeshaje shule? Mnaua elimu ya Tanzania. Mmetuachia huko kwa TAMISEMI mnasema kwamba huko tutafute pesa, hakuna. Mnabadilishia gear angani. Mlituambia kwenye waraka kwamba madawati wazazi hawatachanga leo wazazi wa Babati wanachangishwa Madawati, mnageuzia gear angani. Mtuambie kwanini mnatudanganya? Na hizi fedha mnapeleka lini tunahitaji mtuambie msitudanganye Watoto wetu wanakaa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa walimu wa sayansi. Mheshimiwa Waziri, zaidi ya walimu 30,000 wanahitajika wa sayansi katika nchi hii. Nimepita kwenye shule za sekondari, ninauliza hata mwalimu aliyesoma BAM (Basic Applied Mathematics) A-level aniambie kama yupo afundishe mathematics, hakuna mwalimu wa hesabu kwenye shule za sekondari halafu Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako unasema ujenzi wa maabara katika shule zetu za sekondari utakamilika mwaka 2018/2019 ndiyo vifaa vya maabara utapeleka huko. Tunapataje walimu wa sayansi ilihali hata maabara huko hakuna vifaa na hampeleki? Mnajenga ofisi zenu kwa shilingi bilioni nane, mnataka walimu wa sayansi wa mathematics, wa chemistry hawapo kwenye shule zetu, mnategemea mtabadilisha Taifa hili kweli elimu ya nchi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha shule hatuna walimu wa sayansi. Mheshimiwa Waziri nikushauri tu, walimu wa arts tunao wakutosha. Boresheni VETA, pelekeni vijana wetu huko VETA muwadahili walimu wa sayansi, mtupelekee walimu wa sayansi kwenye shule zetu. Msitegemee watapatikana huku juu, huku chini hata hayo maabara mmeshindwa kujenga. Waziri nakupa tu ushauri wewe ni Mwananmke mwenzangu naomba tu nikupe ushauri labda utanielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine niurejeshaji wa mikopo. Mheshimiwa Waziri Bunge lililopita tulikuwa tunalipa, mimi ni-declare interest, mimi nimelipa nimemaliza. Lakini Bunge lililopita tuliandaliwa mpango hapa, Wabunge wote tumelipa, tumekuwepo Bunge lililopita. Hivi nchi hii kodi mpaka ikusanywe mpaka Magufuli aende na polisi na mbwa kama alivyoenda bandarini ndiyo mkusanye? Ndiyo mtakusanya?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti mbona sijaona mkakati wa ninyi kukusanya fedha hizi, mtuambie wazi wazi, halafu mnasema mtu akichelewa kulipa eti mnampiga interest ya 10% kwa sababu amechelewa, ajira ziko wapi? Wamekaa mtaani hawana ajira baadae unampiga eti penalty ya 10%, kweli Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani muache kuimba Serikali ya Magufuli, hii nchi ni ya kwetu sote! Isiwe ni one man show kwamba Magufuli asipofikiria ninyi Mawaziri mnasubiri leo anaamkaje anasemaje, njoo na mpango kazi wako wa kukusanya hizo fedha, hata hapa basi ungetuita Wabunge wote hapa tujue nani anadaiwa, tulipe hizo pesa. Lakini pia utuambie na hao wengine ambao wameajiriwa kwenye sekta ambazo sio rasmi wanalipaje, sio tunamsubiri Rais akisema basi wote ndiyo tunaenda huko, hapana! Hatuwezi mkaendesha nchi kwa show ya kiasi hicho! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la shule za awali. Mheshimiwa Waziri najua utasema iko TAMISEMI, jamani mmechukua sera ya elimu bure, basi tembeleeni! Mtoke na Simbachawene muende hizo shule. Walimu kwanza hawana mitaala na watoto wetu wanakaa chini ya miti, hakuna darasa, mmewaambia Wakurugenzi watafute hizo fedha wajenge, hawana! Collection za Halmashauri ndiyo hizo mnasema mnaenda kukusanya wenyewe, mpaka zitoke lini? Watoto wananyeshewa na mvua!
Naomba leo mniambie Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Elimu iko chini yako, sera na mambo mengine naomba leo utuambie kwenye hili Bunge, una mkakati gani kwa ajili ya watoto wetu wazuri? Wale wa miaka mitano ambao wanakaa chini, mkituachia Halmashauri tujenge hayo madarasa tutajenga kwa muda gani kama Serikali ya CCM mmejenga VETA kwa miaka 10 hata VETA moja kwa Wilaya haijakamilika! Mnategemea hao watoto…
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Mnategemea watajenga shule hizi za msingi….
MWENYEKITI: Mheshimiwa ni kengele ya pili hiyo!

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ili na mimi nitoe machache ya kwangu katika Wizara hii ya Maji, Wizara muhimu sana katika maisha yetu ya kibinadamu na ni Wizara ambayo kwa kweli ina mgusa kila mmoja. Jana na juzi tulizungumzia Wizara ya Elimu jinsi gani inagusa maisha ya kila mmoja lakini maji kwanza, usipokuwa na maji hauwezi ukaenda darasani wala hauwezi ukaenda kazini wala hauwezi ukafanya chochote. Kwa hiyo, nitoe mchango wangu katika Wizara hii muhimu sana ambayo inagusa maisha ya kila Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nisemee yale ambayo wananchi wa Jimbo la Babati Mjini wamenituma kuyasema. Hadi sasa hali ya maji katika nchi yetu siyo nzuri na Mheshimiwa Waziri unazungumza kuhusu kufikia asilimia 80 katika miaka hii mitano maji katika vijiji vyetu katika nchi nzima. Lakini Mheshimiwa Waziri kinachokukwamisha ni bajeti ya Serikali na mimi niombe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu hakuna sababu ya kukaa na kujadili bajeti ya Serikali wakati hazipelekwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu anafanya vizuri ana nia njema lazima umpongeze. Mheshimiwa Waziri, tangu umeingia kwenye Wizara hii walau tumeanza kuona fedha zimeanza kufika katika maeneo yetu, bajeti iliyopitishwa ya Serikali ya mwaka huu inayotekelezwa kwenye shilingi bilioni 400 za maendeleo, zimeletwa tu bilioni 130 na kitu asilimia 28, hivi hata kama ungekuwa na nia njema ungefanyaje hiyo kazi? Ndiyo maana mchango wangu siku ya leo niwaombe Wabunge wote tujadili hii bajeti lakini tukijua adui mkubwa wa Wizara hii ni Wizara ya Fedha. Wizara ya Fedha hawapeleki pesa katika Wizara hii tunatenga bajeti pesa haziendi, na ndio maana miradi yetu haiendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru pia katika vijiji vyangu vya Nakwa, Malangi, mliniletea pesa yale maji yameanza kutoka Mheshimiwa Waziri, lakini kama ungeletewa pesa zote shilingi bilioni 400 maana yake miradi ingekamilika yote. Kwa hiyo, niiombe Serikali tusiiachie Wizara ya Maji tukawanyima fedha tukajua watu wetu kule wako salama. Kama mpaka sasa nusu ya Watanzania vijijini hawana maji mnategemea tunasongaje mbele na Serikali ya CCM mkae chini mfikirie hili. Watanzania hawana maji, na mkimyima Waziri huyu, siyo kwamba mnaikomoa Wizara hiyo, mnatukomoa sisi na wananchi wetu huko chini, kwa hiyo niiombe Serikali Wizara ya Maji tuipe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi viporo, tulikuwa na vijiji kumi kwa kila Halmashauri na Wilaya, kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Babati, zaidi ya vijiji vitatu sasa tumesubiri kwa muda mrefu sana. Mheshimiwa Waziri nimeona kwenye bajeti hii zaidi ya shilingi milioni 900 mnakwenda kunipatia kwenye kijiji cha Imbilili, kijiji cha Hala na Haraa. Ninaomba bajeti hii ya zaidi ya shilingi bilioni 900 unaoiomba kwenye Bunge hili, basi hivyo vijiji uvipatie kipaumbele kwa sababu tumekaa zaidi ya miaka minne watu hawana maji. Kata nzima kijiji kimoja tu sasa ndiyo naanza kuona kwamba kuna mwelekeo katika hizo shilingi milioni 900 lakini Kata nzima kina mama wanachota maji makorongoni, wanahangaika.(Makofi)
Mheshimiwa Waziri, shilingi bilioni 900 unaomba ni jambo jema, asilimia 75 ya fedha za ndani umetenga kwa mara ya kwanza kwa ajili ya miradi ya maendeleo, haijawahi kutokea, hizo asilimia 75 zikitoka za shilingi bilioni 900, shilingi bilioni 600 fedha za ndani basi zije moja kwa moja kwenye hivyo vijiji, haiwezekani miaka 55 wananchi wanachota maji kwenye makorongo. Kata nzima hawana maji, hawajui hata bomba la maji linafananaje, ndiyo sasa kijiji kimoja walau unaanza kuona mwanga kwa miaka 55 haiwezekani. (Makofi)
Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kwa ujumla wake, angalieni suala la maji, suala la maji halisubiri, watu wanateseka. Walimu tuliokuwa tunawasemea juzi kwenye Kata hii Sigino anakuambia Mheshimiwa Mbunge ninakwendaje kufundisha wakati tu hata vyoo mlivyotujengea vya maji hakuna maji tunatoka na maji kwenye madumu. Naongea kwa masikitiko makubwa kwa sababu wananchi hawa wameteseka kwa muda mrefu, ninaomba Mheshimiwa Waziri hivi vijiji vyetu, ambavyo vimesubiri kwa muda mrefu uvipe vipaumbele hizo pesa zije mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madeni ya taasisi. Wizara hii inadai zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa taasisi mbalimbali za Serikali. Mfano, katika Jimbo langu la Babati Mjini, Magereza tu tunawadai shilingi milioni 100, Polisi tunawadai zaidi ya shilingi milioni 30, Halmashauri yangu inadaiwa zaidi ya shilingi milioni 12 katika hospitali, kwa nini taasisi hizi wanashindwa kulipa, sababu ni hizi zifuatazo:-
Kwanza Serikali hampeleki pesa za OC. Kwenye Magereza hampeleki, Polisi hampeleki, hospitali zetu tunaendesha kwa shida hata madaktari na manesi wanashindwa kulipwa, fedha za OC na on call allowances, watalipaje maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, naona leo dada yangu Susan Lyimo ndiyo amekaimishwa hongera dada, niombe Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu hebu taasisi na Wizara hizi waweze kulipa fedha hizi, mkiwapa Magereza na Polisi maana yake hizi shilingi bilioni 30 Mheshimiwa Waziri una uwezo kwamba hizi pesa sasa zinafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wezangu wa BAWASA Babati wameshindwa kufanya kazi kwa sababu wana nia njema, waliniambia Mheshimwa Mbunge tunapeleka Maji Gadueti, Managa, kila mahali kwenye vijiji vyako, lakini tunadai zaidi ya shilingi milioni 100 Magereza, Polisi tunawadai Halmashauri mmekata mpaka OC tunashindwa kuendesha, Serikali itupatie hizi pesa tukalipe.
Mheshimiwa Waziri, unasema solution ni prepaid meters, hivi unaweka prepaid meters hizi kwa pesa zipi yaani walipe kabla pesa ziko wapi OC haziko, hili ni la Serikali. Serikali tuleteeni pesa, lipeni hili deni la shilingi bilioni 30 ili tupate maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la madeni ya wakandarasi, Mheshimiwa Waziri katika shilingi bilioni 200, shilingi bilioni 100 umeshalipa, ninakuomba hizi shilingi bilioni 105 zilizobaki ulipe ili nikamilishe mradi wangu wa Nakwa, mradi wa Malangi, mradi wa Kiongozi wa maji, kwa sababu kwenye hizi shilingi bilioni 100 naamini pia Wakandarasi wangu ambao wanaendesha mradi wa Nakwa wanadai zaidi ya shilingi milioni 252. Kijiji cha Malangi zaidi ya milioni 280 hizi pesa zikija shilingi bilioni 100 ambazo Wakandarasi wanadai na Serikali mkapeleka Wizara ya Maji, maana yake wananchi hawa wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Serikali bado, wala sina ugomvi na Waziri wa Maji, kwa sababu unagombanaje na mtu ambaye Serikali kwenye shilingi bilioni 400 inampelekea shilingi bilioni 100, nitakuwa mwenda wazumu! Mimi nahitaji Serikali pelekeni pesa Wizara ya Maji ili tuone kama Waziri anatosha au hatoshi. Lakini kwa kile alichokipata naamini kila mmoja hapa alikuwa anauliza walau kuna fedha zinafika kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe haya madeni Waziri wa Fedha naamini Mungu akitujalia tutachangia kwenye Wizara yako, kitu cha kwanza, tuone shilingi bilioni hizi 105 za maji za wakandarasi unalipa lini ili watu wetu waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvunaji wa maji, Mheshimiwa Waziri umesema taasisi za Serikali watengeneze matenki ya kuvuna maji. Hivi Halmashauri hazina pesa, OC haipelekwi unategemea hata kwenye fedha zile za miradi ya maendeleo watajenga matenki kwa fedha zipi? Serikali msirushe tu mpira Wizara ya Maji, hampeleki hata fedha za maendeleo, kama hampeleki mnategemea matenki hayo ya kuvuna maji kwenye maeneo ambayo visima haviwezi kujengwa, vinajengwa kwa namna gani? Kwenye package yenu hamuweki ujenzi wa hayo matenki ya kuvunia maji! Hili ni la Serikali, niishauri Serikali tatizo la maji ni kubwa sana, basi pelekeni fedha Wizara ya Maji ya matenki hayo maeneo ambako hakuna visima na maji ya mtiririko ili tuhakikishe kwamba maji hayo yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine muhimu sana ni suala la upangaji wa bei za maji. Mheshimiwa Waziri, utaratibu unajulikana kwamba wananchi wanahusishwa, lakini maji yamekuwa yakipanda katika taasisi za maji wananchi hawahusihwi, hata wakitoa maoni yao bado unit ya maji ni pesa nyingi sana. Hivi hawa Watanzania wanawezaje kulipa hizi bili?

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na nimshukuru Mheshimiwa Silinde ku-share na mimi dakika chache ili na mimi niweze kutoa maoni yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niunge mkono asilimia mia moja hotuba za Kamati zetu zote mbili. Wamezungumza mambo mazuri ya kujenga na naamini Mawaziri wanasikiliza ili wakayafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pale Mheshimiwa Silinde alipoishia kuhusu TIB Bank kwamba hawa wadaiwa wanatukwamisha, fedha hizo zisitufikie maeneo mengine. Basi sasa kama Bunge tuazimie kwa nguvu zote kwamba hili litekelezwe na tuwafahamu hawa watu na waweze kulipa hizi fedha ili ziendelee kusaidia maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala ambalo nilitaka kulizungumzia siku ya leo, ni asilimia tano ya akina mama na vijana. Naungana na maoni ya Kamati kwamba walete marekebisho ya sheria kwa vile ule ni mwongozo umeshashindikana. Nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI kipindi kilichopita tulilisimamia hili sana lakini Wakurugenzi hawapeleki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na upungufu huo, jambo ambalo nahitaji kuishauri Serikali siku ya leo ni kwamba kwanza ule mwongozo una upungufu. Kwa mfano, wazee wa jinsia ya kiume wao hawapati zile fedha, akina mama wazee wanapata upande wa wanawake na vijana pia wanapata lakini wazee wa jinsia ya kiume (me) hawapati. Nimepita kwenye Jimbo langu na kila nilipopita wazee walilalamika kwamba hawanufaiki kabisa na mfuko huu na wenyewe wanaomba wapate hizo fedha kwa sababu sio wazee wote wenye wake na wenye watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono mapendekezo ya Kamati kwamba marekebisho yafanyike au ule mwongozo sasa tuuache. TAMISEMI kupitia miscellaneous amendment kama ni muswada mzima mtuletee ili na hao wazee wapate fedha hizo tofauti na sasa ambavyo wanahangaika kupata upande wa TASAF wakati TASAF haifiki maeneo yote. Pia mnafahamu TASAF kila baada ya miaka mitatu ndiyo wanabadilisha zile kaya maskini kwa hiyo hawa wazee hawatafikiwa. Kwa hiyo, hili mtuletee na naunga mkono kabisa mapendekezo ya Kamati ili na wazee wa jinsia ya kiume (me) waingie wapate hizo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kukazia siku ya leo ni suala la safari za Wakurugenzi. Kwa kweli Wakurugenzi mliotuletea hawakai kwenye Halmashauri zetu, akitoka kwa DC yuko kwa Mkoa wa Mkoa, akitoka kwa Mkuu wa Mkoa yuko kwa RAS. Ametoka kwa RAS anarudi kwa DAS ametoka hapo anaenda kwa OCD, ametoka kwa OCD yuko kwenye safari anasafiri Dar es Salaam au Dodoma, hawakai kabisa kwenye vikao vyetu. Wizara upande wa TAMISEMI muwaandikie basi muwape miongozo kwa sababu hawakai na ndiyo maana baadaye wanapoanza kutumbuliwa wanashangaa kama yale madudu yalifanywa na watu ambao waliwakaimisha wao. Kwa hiyo, niunge mkono maoni ya Wabunge wenzangu ambao jana walizungumza kwamba kuna tatizo kubwa sana kwa Wakurugenzi wetu, muwape mafunzo lakini wakae kwenye vikao vyetu vya Halmashauri waweze kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kuzungumza siku ya leo ni suala la madeni katika Halmashauri zetu. Mlivyotuletea Waraka wa Elimu Bure, kiukweli Serikali hampeleki pesa. Shule ya watoto 300 au 400, mnapeleka shilingi 200,000, huko huko wanunue mipira kwa ajili ya michezo, huko huko fedha za administration. Niliuliza swali kwa Waziri Mkuu jamani hiki kitu mfanyie review kwa hali ya kawaida shule zetu kuna madeni na Halmasahuri hizi zinadaiwa wakati huo huo mmechukua vyanzo vikubwa vya mapato. Kodi ya ardhi sasa inakusanywa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina hata zile asilimia 30 hamrudishi tena na ndiyo maana juzi nikasema kama ninyi ni waungwana kaeni chini muangalie zile asilimia 30 ambazo mlitakiwa kuzirudisha na mnafahamu zaidi shilingi bilioni 50 hamkuzirudisha, ni shilingi bilioni 4 tu mmerudisha juzi, basi leteni vifaa vya upimaji ardhi katika maeneo yetu kwa sababu huko kwenye Halmashauri zote kwa hali ya kawaida hawana vifaa hivyo.
Mimi niishauri Serikali acheni kuua Halmashauri zetu, kwanza mmepeleka sasa eti bima ya afya wazee tukawalipie kwa fedha gani? Kodi ya majengo mmechukua, TRA mpaka sasa hawakusanyi mnapoteza tu muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kodi ya majengo ndiyo hiyo tena inakusanywa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Wakati huo kuna madeni, Waraka wa Elimu Bure unataka tulipie madeni ya walinzi, maji katika shule zetu yameshakatwa kwa sababu Halmashauri haina fedha na fedha hampeleki hebu kaeni chini muangalie hizo Halmashauri mnaziweka upande gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nisisitize, kama mnahitaji kujenga hizi Halmashauri mkumbuke mlifanya decentralization kwa sababu wakusanye, walipe na wasimamie. Leo mnapochukua fedha hizo zote, mnatubakisha na ushuru tukimbizane na mama lishe, bodaboda na bajaji, kwa nini? Mtuachie hizo kodi ndiyo zilikuwa zinatusaidia tuendeshe hizo Halmashauri. Muwa-empower hao Wakurugenzi na Madiwani wetu wasimamie hizo fedha muone kama kazi hazitoenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho jamani leteni pesa za maendeleo, hakuna fedha kabisa. Halafu mnategemea hizo barabara tutachonga na nini? Pia kwenye miscellaneous mnazotuletea kila siku mtuletee ile ya TANROADS asilimia 70 tuiondoe, asilimia 30 ziende kwenye Halmashauri zetu kuchonga hizo barabara haiwezekani. Nilisema kwenye Bunge hili kwamba TANROADS watusaidie kwenye zile asilimia 70 ili tuchonge hizo barabara lakini ile ni wao wenyewe wapende au wasipende. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi nina mambo machache, naomba dakika zangu tano nimgawie Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, tembo wanamsumbua Jimboni kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni suala la chakula. Wakati Waziri wa Kilimo akieleza hali ya chakula nchini alisema kuna Wilaya zaidi ya 56 kama sikosei zina upungufu mkubwa, lakini Wilaya hizo hatujapewa list, ninaitake Serikali watupe majina ya Wilaya hizo tuzifahamu na ni lini sasa chakula kitaenda, kwa sababu wananchi wetu wana hali mbaya sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea wananchi wangu wa Jimbo la Babati Mjini debe moja la mahindi wananunua kwa shilingi 20,000. Naomba nifahamu mnapeleka lini hicho chakula kwa wananchi wetu kwa sababu hali ni mbaya na mliwambia kwamba wauze ng’ombe hata watatu wanunue debe moja, hao ng’ombe watatu hata bei haifiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeenda Karatu tumeona ng’ombe wamedondoka barabarani wamekufa, sasa hata ng’ombe kumi hawatoshi kupata shilingi 20,000. Mtuambie mnapeleka chakula lini hasa kwa wananchi wangu wa Babati wana hali ngumu kweli na mvua hazijanyesha. Wakati mwingine viongozi wa juu tuangalie kauli zetu, huenda hata Mungu anatuadhibu kwa ajili ya kauli zetu, mlisema hamtoi chakula, mvua ikaacha kunyesha, saa hizi hali mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Kamati iliyoundwa. Hii Kamati ya Migogoro ya Ardhi ya Wakulima na Wafugaji ni Kamati ambayo inahusisha Wizara zaidi ya tano, mpaka leo hamtuambii hiyo Kamati imefika Wilaya ipi? Hamtuhusishi Wabunge na Madiwani huko chini tufahamu hiyo Kamati, tuliuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, lakini huko kila tukizungumzia migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji mnatuambia Kamati iko site, mtuambie iko wapi? Imeanzia wapi? Imefikia wapi? Hiyo schedule mtupatie Wabunge ili tufuatilie, mkitujibu tu humu ndani mkatuambia Kamati iko site, watu wanauana haina maana yoyote Waheshimiwa Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtuambie iko wapi, mje na Babati huku, anzieni huko pia. Morogoro kule watu wanauana, Wabunge tushirikishwe hiyo Kamati tuipe ushirikiano mgogoro huo wa wananchi wetu kuuana uishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni suala la kodi ya ardhi. Katika bajeti iliyopita Waheshimiwa Wabunge kodi ya ardhi tukasema TRA ikusanye, sasa hivi Halmashauri zetu hawakusanyi tena lakini TRA hawana manpower,haya maduhuli ya Serikali hayakusanywi tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri tu Wizara ya Ardhi, mlikuwa mnatuletea asilimia 30 retention ya premium, sasa hivi hizo pesa zingetusaidia hata kununua vifaa, Halmashauri zetu hatuna vifaa vya upimaji ndiyo maana ardhi kubwa ya Tanzania haijapimwa. Leo badala ya kuwezesha Halmashauri zetu wabaki na hizo retention za 30 percent mlipitisha kwenye bajeti mwaka jana, wakati mmetufukuza mkapitisha, mkasema TRA wakusanye. TRA hawakusanyi, hawana manpower. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali kwamba rudisheni sasa kazi hiyo kwa Halmashauri zetu ili kazi ya upimaji ardhi katika Halmashauri zetu iende sambamba na suala zima la upatikanaji wa fedha. Kwa sababu ile 30 per cent ilikuwa inatusaidia. Kama TRA hawakusanyi mwaka mzima kwa nini msifanye maamuzi? Kazi kwenu, wakati wa bajeti kaeni chini mfikirie siyo kodi tu ya ardhi, lakini pia hata kodi ya majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni suala la fedha za maji, fedha za maji kuna mlango wa Wizara ya Maji, mna bajeti yenu huko haiko wazi sana, lakini kuna TAMISEMI na kuna Halmashauri zetu. Kwenye Halmashauri mnatupa ceiling ndogo sana Mheshimiwa Waziri. Kaeni chini muweze ku-reconcile pamoja vyanzo vyote vya fedha za maji ili Wabunge tujue kwamba miradi mikubwa tupitishie milango ipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Babati katika Jimbo langu, pale Kata ya Sigino, uliona Kata nzima hawana maji kabisa vijiji vyote vine. Tukiwafuata mnasema kuna fedha upande wa Wizara ya Maji, kuna TAMISEMI, wakati huo huo ceiling hazitoki mapema saa hizi Mabaraza wameshaanza kukaa kwenye bajeti, ceiling hazijulikani. Toeni ceiling mapema, lakini onesheni mapema kwamba Wizara ya Maji tunaweza tuka-access fedha hizo kwa kiasi gani? Kama tutaendelea kutokuweka mambo haya wazi, tutaendelea kuimba wimbo wa kwamba hakuna maji katika Taifa letu kwa miaka zaidi ya 50 na akina mama wanaendelea kuchota katika makorongo na ndoo hazijashuka katika vichwa vyao.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

HE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na Wizara ituambie ni kwa muda gani wale nyumba zao zilizopigwa (X) zilizopo au zilizokutwa na sheria ya mwaka 2007 zitafidiwa kwa kuwa sasa hawaruhusiwi kabisa kufanya maendeleo yoyote. Ni vyema wakaruhusiwa kufanya ukarabati not ujenzi wa nyumba hizo kwa kuwa hata zikidondoka kwa sasa hawaruhusiwi kukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ng’ombe, punda wanachungwa pembezoni mwa barabara wanasababisha sana ajali, hivyo TANROADS kote nchini watakiwe kuweka doria kwa wanaochunga ng’ombe, punda, mbuzi, kondoo pembezoni ya barabara wachukuliwe hatua kali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, minara ya simu kwenye vijiji vyenye kuwa na tatizo la mawasiliano wasaidiwe upesi kama vile vilivyopo Babati. Mfano, Himiti, Chemchem, Imbilili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgao wa fedha za Mfuko wa Barabara TANROAD; asilimia 70 za fedha za Mfuko wa Barabara upunguzwe hadi asilimia 50 ili wananchi wa Tasime wenye barabara nyingi wasaidiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, all the best brothers.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kunipa nafasi na mimi nitoe maoni yangu katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Pia ninamshukuru Mwenyenzi Mungu kutupa afya njema, sisi wote katika Bunge hili ili kuishauri Serikali.

Pili, niendelee kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Babati Mjini kwa msiba ambao tulipata wa wale watoto ambao walipata ajali na Watanzania wote niwape pole, siku ya leo ni mazishi pale mtaa wa Mrara, Mungu awatie nguvu, ni msiba mzito sana ambao kwa kweli ni kazi kuupokea katika mioyo yetu, lakini Mungu atupe faraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, haya ninayochangia ni ambayo naona niyaseme kutoka moyoni mwangu. Naomba niseme neno moja la kiswahili kwamba Wabunge tuko hapa kwa ajili ya kusimamia Serikali, lakini kama hatutaacha unafiki toka moyoni, haya malalamiko ya wanajeshi na wananchi wetu hayawezi kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hili kwa sababu unafiki huu tusipouacha tutaendelea kusema Magereza ya Jimboni kwangu, Polisi wa Jimboni kwangu, Zimamoto wa Jimboni kwangulakini wenye matatizo ni sisi Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii bajeti yake ni shilingi bilioni 930, lakini bajeti ya maendeleo ni shilingi bilioni 40, kati ya shilingi bilioni 940 ndio za maendeleo. Waheshimiwa Wabunge tunaongea hapa kinafki, tunaongea tu kwa kupapasa wakati wa kupitisha vifungu tunaongeaongea tunakwenda kwenye guillotine haya hatuyaongei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatufiki kwenye vifungu, hatuongei kwa dhati ya mioyo yetu na kama tukisimama kuisimamia Serikali niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na mimi tuache unafiki. Ikifika saa ya kupitisha vifungu tuitake Serikali waongeze fedha za maendeleo kwa sababu kila Mbunge analalamika kuhusu Polisi kwenye Jimbo lake, Magereza kwenye Jimbo lake, Polisi kwenye Jimbo lake, na Jeshi la Zimamoto kwenye Jimbo lake hawana magari, hawana maji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifika kwenye kupitisha vifungu tunaenda mtu anatoa shilingi baadaye anarejesha kishkaji, wakati fedha hazipo huku kwenye maendeleo. Kwa hiyo, ni aibu Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo inalinda Tanzania, fedha za maendeleo shilingi bilioni 40 wakati wanajeshi wanakaa kwenye mabanzi, kwenye bati ndiyo nyumba zao. Unafiki huu utatupeleka pabaya. Mimi ninawaomba Waheshimiwa Wabunge leo, bajeti hii isipite wanongezewe fedha wanajeshi hawa na magereza na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe pole Mheshimiwa Waziri wetu Kivuli Mheshimiwa Godbless Lema, jana alibaguliwa kule Arusha na maeneo mengine. Nimtie moyo tu kwamba ubaguzi huu siyokwa sisi peke yetu, ubaguzi huu upo hata kwa wanajeshi wetu. Nitoe mfano, Jeshi la Magereza katika bajeti hii, hivi tunavyoongea nimeona kwamba Jeshi la Magereza hawajawahi kusikilizwa mambo yao. Niwape mfano, Mheshimiwa Rais mwaka jana mwezi Novemba, alizungumza kuhusu duty free hizi bidhaa ambazo zinapelekwa kwenye majeshi yetu, akasema hizi fedha badala ya kuwaletea vinywaji tutakuwa tunawaletea kila baada ya miezi mitatu shilingi 300,000. Ninavyoongea hapa Jeshi la Magereza hawajawahi kupewa fedha hizi, lakini majeshi mengine wamepewa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri utuambie kwa nini mnabagua Jeshi la Magereza. Jeshi la Polisi mmewapa Januari, Aprili mmewapa awamu mbili. Jeshi la Wananchi mmewapa mwezi wa Novemba, Desemba, awamu mbili. Jeshi la Magereza hamjawahi kuwapa hizi fedha,kwa nini mnawabagua jeshi hili? Wakati Jeshi la Magereza ndiyo linakaa na wananchi ambao wanaonewa, wanabambikiziwa kesi, wanawalinda wahalifu, wanakaa na watu kule wanawavumilia. Wengine hawa mahabusu na wafungwa mnawapeleka kule.

Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikuambia hawana hata uniform, hawana hata nguo, mnawapeleka mnawafunga. Wafungwa wetu katika magereza nilifanya ziara katika Gereza la Babati, mtu mzima unakwenda pale unapewa suruali na shati la juu tu hakuna nguo nyingine yoyote ni mfungwa huyo! Jeshi hili wanakaa na watu hawa wasiokuwa na nguo mnawapa suruali tu na shati la juu, nguo zingine pull neck na nguo za ndani hamuwapi, halafu watu hawa hawapewi fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mnaita Jeshi la Magereza mnawapenda, mnawasikiliza, hata kwenye nyumba kwenye kitabu cha development nimekwenda, nyumba zote ambazo mnakwenda kujenga mnafanya renovation ni nyumba za polisi, sina tatizo na polisi wetu lakini Jeshi la Magereza mmewasahau kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie kwa nini ubaguzi huu mnaotufanyia sisi, sasa mnaupeleka kwenye majeshi yetu? Mtakuwa salama vipi? Wewe ni mfungwa mtarajiwa kaka yangu, kesho na kesho kutwa, utakuwa mahabusu pia, uko hapo tu wengine walikuwa hapo na wengine walishaondoka unafahamu, usicheze na Jeshi la Magereza wapelekeeni mahitaji yao na hizi pesa mlizowaahidi muapelekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo niliseme, hizi shilingi bilioni 40 ambazo ninasema tusipoacha unafiki, ndiyo hizi ambazo zinatakiwa ziende kwenye maendeleo. Wafungwa na mahabusu wapate magodoro. Gereza la Babati wafungwa wetu na mahabusu wanalala kwenye magodoro kama slice za mikate. Wanaunganishaunganisha vipande vya magodoro halafu havitoshi wanalala chini. Ukitaka kwenda kupeleka pale mlolongo ni mrefu mpaka uende Magereza Makao Makuu. Mkuu wa Gereza pale hatakuruhusu kupeka hivyo vitu mpaka uandike barua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mnaleta mlolongo kwa nini hamnunui vitu hivyo? Magodoro hamnunui, uniform hampeleki lakini pia hata chakula ration wanazokula hazitoshelezi! Mtuambie ni kwa nini hizi fedha za maendeleo msiongeze kwa sababu kila mmoja ni mfungwa na mahabusu mtarajiwa. Hakuna magodogo huko.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu alifika babati, alifika pale Jeshi la Polisi, nashukuru alienda pale rangi ikapigwa pigwa kwa sababu alienda pale, lakini nilimweleza masuala ya Gereza la Babati, hali ni mbaya na Magereza ya nchi nzima hali ni mbaya, hata magodoro hakuna. Ni vizuri tukakubaliana kwamba fedha hizi ziongezwe.Mfano, Jeshi la Magereza wanatakiwa nyumba 10,526 asilimia 71 hizi nyumba hazipo.Achilia mbali Magereza wanakokaa, lakini asilimia 71 ya Jeshi la Magereza hawana hizo nyumba.Polisi hawana hizo nyumba, Wilaya tano tu ndiyo mmeweka katika bajeti hii. Hivi kweli Waheshimiwa Wabunge tukae tu tunalalamika, kwamba jimboni kwangu, jimboni kwangu, nafikiri hili tulichukue kama Wabunge. Kwamba Wizara hii tunataka fedha za development angalau hata bilioni 200 ili tuache kelele za nyumba za Polisi wetu, tuache nyumba zetu za Magereza zijengwe, vinginevyo mnatuachia mzigo mkubwa sana na hili halitokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Magereza Wilaya moja kutokuwa na Gereza. Mfano, Babati pale tuko Makao Makuu ya Mkoa, lakini wenzetu wa Hanang’ hawana gereza tunaletewa mahabusu, gereza la Babati sasa lina watu zaidi ya 400 wafungwa pamoja na mahabusu, wanakaa mahabusu wa Hanang’ wiki tatu hawapelekwi Mahakamani, OCD wa Babati na wa Hanang’ hawana mafuta, Polisi wetu hawa wamewaachia mzigo mkubwa sana, kwenye ziara zao wakubwa wakija pale, wanawaambia watafute magari, wanaanza kuomba matairi yako wapi, mafuta yako wapi, hata fedha hawapeleki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanashindwaje kujenga Gereza Hanang’ wanarundika pale, watu wanasukumana pale, chakula hakitoshi, hawapelekwi Mahakamani, wanakosa haki zao. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu, naomba nifahamu na atuunge mkono kwa kweli, siyo baadaye aseme hela hazitoshi wakati anajua Hanang’ hakuna gereza, Babati msongamano ni mkubwa kwenye Gereza letu la Wilaya. Atuambie ni lini la Hanang’ litajengwa ili wananchi wa Babati wanapoingia kwenye lile Gereza, wasisongamane kiasi hicho kwa sababu hizi fedha hazitoshi na yeye atuunge mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine suala la Zimamoto. Jeshi la Zimamoto wanafanya kazi nzuri na wanakusanya…

TAARIFA...

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nisaidie tu kulinda muda wangu. Naomba nipokee taarifa ya Mheshimiwa Nagu ni dada yangu, naomba tu nikwambie dada ulikuwa haujalisemea ndiyo maana mpaka leo hakuna Gereza, kwa hiyo acha nikusaidie mdogo wako nikusemee.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwakunipa dakika tano angalau niseme machache kwa ajili ya Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli kama kuna Mbunge atasimama kwenye Bunge hili na kusema bajeti ya maji isiongezwe basi huyo Mbunge labda alipata Ubunge kwa kupendelewa na alipewa zawadi tu, hakutafuta kura, lakini kama alikwenda kwa wananchi akaona kero zao hatathubutu akasimama na kusema bajeti hii iziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja za Wabunge wote wanaosema kwamba ile Sh.50 iongezwe mpaka Sh.100 ili wananchi wetu wapate maji. Wale ambao majimbo yao, mikoa yao ina maji, tafadhali mtuache sisi ambao bado wananchi wetu hawana maji ili tuunge mkono hoja hii ya kwamba fedha ziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hili kwa sababu mimi niko Jimbo la Babati Mjini lakini nina Kata nzima ya Sigino yenye vijiji vinne haina maji. Asubuhi nilikuwa naongea na Mbunge mmoja ananiambia Mheshimiwa Mbunge inawezekana sana fedha hizi zisiongezwe au zikaongezwa, nikamwambia lakini hebu tupige picha siku moja Wabunge tukae wiki nzima humu ndani tusioge na tusiwe na maji itakuwaje? Akaniambia hivi, tutanunua maji ya Kilimanjaro tutaoga. Nikamwambia okay, una uwezo wa kununua maji ya Kilimanjaro lakini mama na bibi yako uliyemwacha kijijini kule hana uwezo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tusiweke itikadi zetu katika suala hili. Niombe Serikali isikilize kilio hiki cha Wabunge wote kwamba fedha hizi ziongezwe ili wananchi wangu wa kata ya Sigino, Jimbo la Babati Mjini wapate maji. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika, wale akinamama walimvika mpaka na mgoroli akawaahidi kwamba katika bajeti hii fedha zitakwenda katika Vijiji vya Sigino, Singu, Dagailoi na Imbilili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye kitabu zimetengwa shilingi milioni 600 tu hazitatosha, lakini fedha zikiongezwa tutapata shilingi 2,700,000,000 ambazo tumeziomba. Kwa hiyo, niunge mkono kabisa hoja ya Wabunge kwamba fedha hizi ziongezwe na wananchi wa Tanzania wapate maji. Ni aibu, akinamama wanateseka, wanachota maji kongoroni, ndoo zao zinavunjika, wengine wanarudi usiku, wengine wanabakwa, wanahangaika wanatafuta maji halafu sisi wanawake humu ndani tuseme fedha zisiongezwe, inasikitisha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kabisa Serikali kama mnaona tozo ya mafuta haitoshi twendeni hata kwenye mitandao ya simu, tuna 0.03 ya service charge ambayo siku zote wamekuwa hawalipi. Tumekuwa tukizungumza hata kwenye TAMISEMI hizi fedha haziendi. Hebu Serikali kaeni chini muangalie fedha hizi hata kama ni shilingi 20, 30, 50 tuzipeleke kwenye Mfuko wa Maji ili zipeleke maji kwa wananchi wetu. Wananchihawa wamevumilia kwa miaka hamsini, kwa nini tusiwatendee haki fedha zikaenda wakapelekelewa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sina ugomvi na Mawaziri, wao wamepelekewa asilimia 19, lakini Serikali kama mngepeleka asilimia 100 ya shilingi bilioni 900 ambazo zilipangwa maana yake kero hizi zingepungua. Kwa hiyo pia niombe Waziri wa Fedha pamoja na Serikali kwa ujumla wake Wizara ya Maji wapelekeni pesa. Pamoja na kwamba tunaomba fedha hizi ziongezwe, lakini fedha zile zilizopangwa ambapo miradi iko kwenye mchakato pia ziende.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kwenye Jimbo langu la Babati Mjini, Vijiji vya Haraa na Imbilili tulishampelekea Mheshimiwa Waziri bado kusaini tu mikataba, lakini tunaambiwa zimeenda asilimia 19 tu, bajeti ya Wizara ya Maji ilitakiwa ziende asilimia hata 50, 60, 70 au 80 mbona Wizara ya Ujenzi fedha zimeenda? Kwa nini Wizara ya Maji ambayo inamgusa kila mwanamke katika nchi hii msipeleke fedha?Wangapi waonapita kwenye barabara zenu za lami mnapeleka asilimia zaidi ya 70 au 80 lakini akinamama hawawezi wakapelekewa fedha zao?Kwa hiyo, niunge mkono hoja hii lazima Wabunge tuwe serious kwamba Wizara hii waongezewe fedha.

The Access to Information Bill, 2016

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nami nitoe machache katika Muswada ambao uko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika Muswada huu katika Ibara ya Pili kwamba, sheria hii itatumika Tanzania Bara, kwa sababu sheria hii tunayotaka kuitunga sasa katika Muswada ni kwamba, inatumika Tanzania Bara tu, naomba nipate ufafanuzi kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaonesha mambo ya Muungano, ukurasa wa 128.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni Katiba ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Hili jambo ni la pande zote, siyo la upande mmoja tu, lakini jambo la pili ni kile kipengele cha sita, suala zima la uraia, hakuna uraia wa Zanzibar wala wa Tanganyika, tunazungumza masuala ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nipate justification ya kwa nini sheria hii, Muswada huu ubague Wazanzibari ubaki kwa Tanganyika tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza suala zima la kupata taarifa na huu Muswada umezungumzia hata raia, huyu raia ni wa namna gani. Maana yake ni hatujaangalia kwa mapana ni kwa nini tumewatenga Wazanzibari wasishiriki kama jambo hili ni jema na ndiyo maana kama tunaona Katiba inakiukwa lazima tuseme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema nia ya Muswada huu ni Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 18(d) kwa maana ya kwamba, Katiba hii ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumza suala la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unazungumza raia, unazungumza Katiba na vifungu vyake, kwa nini unakiuka upande wa pili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naona huu Muswada wa ni wa Kitaifa, huu Muswada usingepaswa kutenga Zanzibar, ulipaswa pia na wenyewe uwe applied kwa sababu raia wa Zanzibar ni Watanzania, anaweza akahitaji kupata taarifa au anaweza akahitaji kufuata zile taratibu ambazo ziko kwenye Muswada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, to be honest, huu Muswada umeletwa kwa makusudi maalum, huu Muswada haujaletwa kwa nia njema ya Ibara ya 18(d) kama alivyosema Mheshimiwa Waziri. Huu Muswada umeletwa kwa ajili ya kufunga watu midomo. Huu Muswada umeletwa kwa sababu ya kuzuia taarifa za Serikali ambazo ni ovu, ambazo mara nyingi zimekuwa zikivuja. Ndiyo maana kama lengo ni jema nisome hiyo Ibara ya 18(d) inasema, “Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Muswada huu umeleta visingizio, umeleta hatua na vikwazo vya Ibara hii ya 18(d). Kimsingi Muswada huu, kwa maoni yangu umekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu Katiba inasema kila mtu anayo haki ya kupewa! Muswada unasema uombe! Huyu raia analazimishwa kwa sheria hii, kama tutapitisha, siyo kupewa kama Katiba inavyotaka, ni kwamba, aombe. Hatua sasa zinaanza kuoneshwa uombe kwa maandishi, uombe sijui kitu gani, mara sijui siku 30, lakini Katiba inasema una haki ya kupewa taarifa wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema mmeleta huu Muswada, mmejisahau tu ni juzi, mlipitisha kwenye Bunge lililopita Sheria ya Whistle Blowers! Mnawafunga sasa midomo wakiwa na taarifa fulani wasizitoe kwa sababu mtawabana kwa sheria hii mtawaambia mliomba wapi? Taarifa za maandishi ziko wapi? Binafsi naona Serikali imekuja na Muswada huu kutimiza na unajua wameshindwa kujificha, tuwe wakweli, mmejianika kwenye Kifungu cha 6(2) kwenye Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 6(2) kinasema kwamba, taarifa iliyozuiwa inaweza kuzuiliwa kama utolewaji wa taarifa hiyo unaweza kusababisha mambo yafuatayo, mambo mengi sana (a) mpaka (i)! Jambo la kwanza ambalo limenisikitisha (g) inasema, “Kuzuia au kusababisha madhara makubwa kwa Serikali katika kusimamia uchumi.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmejificha hapa, yaani mmejificha kweupe kabisa! kwenye Kifungu cha 6(2)! Halafu lingine mnaandika mnasema kuwezesha au kuhamasisha kufanya kosa! Kuingilia upelelezi unaofanywa na vyombo vya uchunguzi! Kudhoofisha kwa kiasi kikubwa uwezo wamiliki wa taarifa na bla-bla nyingi tu, mmejificha hapo! Mnazuia mambo yenu yasipekuliwe tena! Wale whistle blowers wasitoe tena kama kuna kitu, ufisadi unafanyika katika Serikali hii wasiseme tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao ni wema sana katika Taifa hili, aidha ni wafanyakazi wa Serikali au siyo wafanyakazi wa Serikali, wanapogundua kuna ufisadi mahali wamekuwa wakitoa ushirikiano katika Taifa hili, lakini Muswada huu unakwenda sasa kuwafunga midomo kwa sababu, mnataka msemaji awe tu ni Afisa Habari katika taasisi fulani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli tu, Kifungu cha 16, kuahirisha utoaji wa taarifa, naomba tu ninukuu, “Mmiliki wa taarifa ambaye amepata ombi anaweza kuahirisha kutoa taarifa husika mpaka linapotokea tukio maalum ikiwemo kuchukua hatua za kisheria au kiutawala au mpaka kwisha kwa muda uliowekwa,” tumeweka hapa muda siku 30, lakini hapa kifungu cha 16(1) mnamlinda huyu mtu ku-delay hata zaidi ya siku 30 au asitoe kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, atasema aah! mmeomba taarifa ya wafanyakazi hewa, Waziri wa Utumishi ametoa miezi sita tufanyie kazi, wewe unaomba ndani ya siku 30! atakwambia bado kuna taratibu hazijafuatwa hapa, kuna mambo hayajakamilika hapa! Mmempa mandate ya kuzuia hata hizo taarifa katika Kifungu cha 16(1). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, nenda Kifungu cha 18(1), matumizi ya taarifa, inasema, “Bila ya kujali masharti ya Kifungu cha 6 mtu aliyepewa taarifa kutoka kwa mmiliki wa taarifa hatatakiwa kuipotosha taarifa hiyo.” Hata kile ambacho kimetolewa kama kimepotoshwa kutoka kwenye chanzo, anayekuja kuadhibiwa katika Muswada huu ni yule mtumiaji wa mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote mmewabana Watanzania hata wakipata kile walichopewa waendelee, mpaka kifungo mmeweka, lakini aliyepotosha aliyetoa taarifa, yaani chanzo hakijapangiwa adhabu, mnampangia adhabu yule mtumiaji wa mwisho! Ndiyo maana nasema mmejificha kwenye Kifungu cha 6(2), yale ya kwenu yote ambayo hamtaki yaguswe mfunge watu midomo yako pale, mengine ni haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda vifungu vya 20, 21, 22, 24 ndiyo usiseme. Hata wale Maafisa wanaotoa zile taarifa wamepewa mamlaka whether watoe au wasitoe na wakifanya au wasipofanya, Kifungu cha 24 kwa nia njema! Haijawa defined hiyo nia njema! Hawatachukuliwa hatua, wanalindwa! Kwa nini mnataka mtumie Bunge hili kupitisha kitu kibaya kiasi hiki ambacho kiko against Katiba yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu, kama Serikali iko honest, walikuwa wana nia njema kuleta Muswada huu, nilifikiri huu Muswada base yake inakubaliana kwamba, ni Ibara ya 18(d) ya Katiba, lakini nilifikiri huu Muswada usingezidi vifungu vitatu. Kifungu cha kwanza kingeeleza jambo hili, njia za mtu kupata habari, mtaeleza pale kwamba Serikali itawajibika, Baraza la Madiwani litawajibika, Taasisi yoyote ya Umma itawajibika kutoa taarifa kwa wananchi hawa kama Ibara inavyosema. (Makofi)
Jambo la pili ingekuwa ni taarifa zipi ambazo raia hao wanatakiwa wapate kwa wakati kama ilivyoeleza kwenye Ibara hiyo ya 18(d); hamjaeleza mmekimbilia kujilinda kwenye Kifungu cha 6(2), mngeeleza ni taarifa zipi hasa na ni zipi ambazo Mtanzania hatakiwi kupewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ingekuwa ni adhabu ambazo angepewa huyu ambaye ni Afisa Habari au ni Mtumishi wa Serikali anayekataa kutoa taarifa hiyo kwa wakati, hamjasema adhabu. Mmesema tu anaweza aka-appeal, akaenda sijui kwa Mkuu wa hiyo Taasisi, akaenda kwa Waziri ndiye msemaji wa mwisho. Tena mnathubutu kusema Waziri ndio msemaji wa mwisho! Kwa sababu Mkurugenzi labda na Waziri wanawasiliana Mkurugenzi atamwambia sijamaliza kufanyia kazi, Waziri atatoa majibu hayo hayo. Mnathubutu kusema na Waziri ndiyo msemaji wa mwisho, ndiye mwenye maamuzi ya mwisho, lakini hamjasema adhabu ya mtu ambaye atakiuka ibara ya 18(d) ya Katiba kwa kushindwa kutoa taarifa kwa wananchi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuwaite mna nia njema? Kwa nini tuwaone mna mambo mazuri sana kuhusu Muswada huu, kwa nini tusiwaone kwamba lengo lenu kubwa ni kufunga vyombo vya habari midomo, ni kufunga whistle blowers, ni kuwatisha wananchi ambao hawajafuata taratibu kwamba hizi taarifa kwanza umezipataje achukuliwe hatua na mtafanya, kwani mangapi mmepitisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho naweza kuwashauri Serikali hii, hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, na hakuna jambo ambalo halina mwanzo na mwisho, mnatumia wingi wenu vibaya, lakini yameanza kuwarudi taratibu. Hii ni movie tu ambayo mnacheza ila siku zinahesabika, kwa sababu hamuwezi mkawa mnakiuka Katiba kiasi hiki Watanzania waendelee kuwaangalia. Hawa Watanzania siyo wajinga hata siku moja, hata kama mnaona hawawezi kufikiria, lakini ipo siku watapata ufunuo kwamba haya mnayoyafanya kwa ajili yao siyo mazuri hata kidogo.
Mheshimiwa Waziri hayo ni maoni yangu, huu Muswada haufai kabisa na vifungu vyote vimetungwa kwa ajili ya kuwabana wale watumiaji siyo Serikali kuwajibika kwa wananchi kutoa taarifa vile ambavyo Katiba yetu inataka. Nawaomba tu kwa sababu mna muda mkatafakari, kama mmeona kwamba mtuletee mambo haya ndiyo tuyapitishe hiyo damu haitadaiwa mikononi mwetu, mtapitisha kwa wingi wenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawahakikishieni ipo siku haya mambo mnayopitisha yatawarudi. Ahsante.

The Valuation and Valuers Registration Bill, 2016

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuweka mawazo yangu katika muswada huu muhimu kwa maslahi ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye muswada nikihitaji ufafanuzi labda ni-declare tu interest, mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo, lakini kwa sababu hiyo sikatazwi pia kuweka mawazo yangu katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate ufafanuzi. Suala la kwanza, mwanzoni tulikuwa na utaratibu kwamba taarifa zie za uthamini zinapokuwa zimeshakwenda kwa ngazi za juu, kunakuwa na nafasi za Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa inaporudi wana-verify pia, lakini katika muswada huu hawajatajwa popote. Sambamba na hilo, naomba nifahamu tu kama sasa nafasi zao pia hazipo, lakini pia huyu mwananchi akate rufaa wapi pale ambapo anakuwa hajaridhika na uthamini ule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Wizara itusaidie kujibu; kuna wananchi wengi ambao kwa muda mrefu sasa leo tunatunga hii sheria wao wamekuwa wakisubiri fidia zao hazijalipwa kwa muda mrefu na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani imesema kwamba kuna wale ambao wanasubiri fidia katika maeneo ambayo yametengwa kwa akiba ya barabara na maeneo mengine; hawa watu wamekaa kwa muda mrefu hawajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya sheria hii kupitishwa, sawa mtapata ule muda ambao unapandekezwa na baadaye Bunge tutapitisha, hao wengine wanachukuliwa wapi au wanakuwa wamesahaulika? Napenda kufahamu kwa sababu wako wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye vifungu vya Muswada huu, katika kifungu cha 7(1). Kifungu hiki kinasema; “Iwapo Mthamini Mkuu ameridhika kwamba uthamini haukufanyika ipasavyo, atapendekeza kwa mamlaka husika nidhamu na hatua zinazopaswa kuchukuiwa dhidi ya Mthamini aliyesajiliwa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo yangu, ni vizuri sasa kwa sababu tunatunga sheria, tukaweka adhabu wazi wazi. Mheshimiwa Waziri ulikuwa umeeleza katika hotuba yako kwamba nia ni njema, kulikuwa na Wathamini wanafanya ndivyo sivyo na vitu kama hivyo, ndiyo lengo mahususi la muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini mnataka kumwachia Mthamini Mkuu apendekeze hatua na kwa nini tusiweke sasa kwenye muswada huu au kwenye sheria hii kwamba huyu ambaye amekuwa akifanya under valuation kwa watu wetu na mali zao; huyu mtu adhabu yake iwe ni kiasi hiki? Kwa nini tumwachie Mthamini Mkuu yeye apendekeze? Hiyo mamlaka husika inaweza isimwadhibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza tu au nashauri kwamba hii adhabu tuiweke kwa sababu tunatunga sheria hii pia kulinda watu wetu ili zile thamani za majengo yao na hadhi zao zisichezewe hovyo hovyo na hawa Wathamini. Kama lengo ni kuwabana hawa Wathamini, basi tupendekeze adhabu na tusiache hivi ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kifungu cha 52; Mheshimiwa Waziri amependekeza kutoka kile ambacho mwanzoni kiko kwenye kifungu cha 52 kwamba muda Waziri atabainisha, lakini umeenda kwenye miaka mitatu katika suala zima la kulipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba huu muda ambao wananchi wetu wanasubiri fidia usiwe zaidi ya mwaka mmoja na tunafahamu kwa muda mrefu sana kwamba wananchi wamekuwa wakitwaliwa maeneo yao, lakini wanasubiri kwa muda mrefu, hawapati hizo fidia; tuwasaidie pia kwa sababu hii ardhi ndiyo rasilimali pekee Mtanzania anayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomwacha kwa miaka mitatu akisubiri fidia hiyo, anaweza akawa amesha-mess-up na hajui kwamba afanye nini. Baadaye unakuja kusema kwamba unamlipa au haumlipi, wakati huo umeshampotezea muda kama hao wa reserve ya barabara tumewaacha sasa, hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napendekeza kwamba endapo ardhi imetwaliwa, lakini huyu mtu baada ya mwaka mmoja hahitaji tena ardhi hiyo, basi alazimike kama ni ile interest ambayo ina-accrue baada ya miezi sita, ilipwe hata kama haihitaji ile ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hivi kwasababu zifuatazo: kuna baadhi ya watu binafsi ambao labda wanataka kujenga shule au taasisi fulani, wanataka kuwekeza kitu fulani, anahodhi ardhi ya wananchi kwa miaka miwili, mitatu au minne kama tutapitisha mwaka mmoja au kama mtapitisha pia kwa wingi wenu hiyo miaka mitatu mnayoipendekeza, lakini kuna watu watatumia ardhi hizo, atakaa nayo, hajalipa fidia, baadaye anasema siihitaji tena ardhi hiyo. Huyu mwananchi anakuwa katika hali gani? Miaka mitatu umempotezea muda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashawishi Bunge hili kwamba pia tuweke charge fulani kwa mtu atakayehodhi hiyo ardhi kwa lengo la kutaka kuendeleza, lakini baadaye aka-reject, akawarudishia wananchi, asiseme tu ardhi yenu hiyo hapo, sihitaji kuwalipa tena fidia kwa sababu siihitaji na siitumii tena. Tuwalinde hawa wananchi ambao watakuwa wamapotezewa muda, angalau awajibike hata some amount aweze kulipa ili tuepushe wimbi kubwa la watu ambao watahodhi ardhi, baadaye wanawarudishia wananchi wakati wameshawapotezea muda na wameshindwa kuendeleza ardhi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba miaka mitatu ni miaka mingi sana, kama lengo ni kuwasaidia Watanzania, Mheshimiwa Waziri akubaliane na maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba isiwe zaidi ya mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwenye kifungu cha 55; hiki kifungu kinasema, Mthamini aliyesajiliwa endapo atataka kuingia kwenye eneo lolote au kwenye jengo lolote lile, hatakiwi kukataliwa. Pia Mheshimiwa Waziri akaleta marekebisho katika jedwali lake kwamba aweze kutoa taarifa; inaweza ikawa ya maandishi au taarifa yoyote ile. Niongezee kwamba iwe ni kwa ridhaa ya yule anayehodhi eneo hilo, iwe ni ardhi au jengo, kwa sababu taarifa inaweza isimfikie kama hajatoa ridhaa kwamba nakubali tukafanye uthamini wa haya niliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, kuna Wathamini watakwenda watasema mmiliki anafahamu, lakini hawa wamiliki hawafahamu. Nitoe mfano mzuri wa wananchi wa Jimbo langu la Babati Mjini eneo la Bagara Ziwani, Mheshimiwa Waziri analifahamu sana. Wale wananchi walithaminiwa maeneo yao bila wananchi wengi kufahamu hata kama Wathamini wameingia kwenye maeneo hayo, wakabaki kuwafukuza kwa silaha. Maana yake ni nini? Wakaja wakatoa taarifa ya uthamini ekari ifidiwe kwa shilingi 240,000. Wananchi wengi wakakataa kuchukua zile fidia kwa sababu haikuwa ridhaa yao pia na hawakushirikishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika kifungu hiki cha 55, iwe pia pamoja na taarifa ya maandishi, pawepo na ridhaa ya mwenye mali hiyo, iwe ni ardhi au jengo kwamba sasa hili lifanyike. Tusipofanya hivyo, taarifa zitapikwa mezani na baada ya hapo wananchi watakataa na mchakato wa fidia utachukua muda mrefu sana na matatizo yatakuwa mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upesi upesi kifungu 55(2), nipendekeze kwamba hiki kifungu tukifute kabisa na tufanye vice versa. Kinataka mtu ambaye amekataa kwamba eneo lake lisithaminiwe, hajatoa ushirikiano, kifungu 55(2)(d) inapendekeza adhabu, kwamba atatozwa fine isiyopungua shilingi milioni moja na isiyozidi shilingi milioni tatu au kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miezi 24 au vyote kwa pamoja; fine na kifungo. Naomba hii adhabu iwe nikwa hao Wathamini. Watakapokuwa wamekosea…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru nitaleta amendment.

The Media Services Bill, 2016

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweke mawazo yangu katika muswada huu wa Sheria Huduma za Habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kamati husika ilivyokuwa inachambua muswada huu, tulikuwa tunasoma mambo mengi na mapungufu yake, lakini mimi binafsi nilikuwa siamini kama kweli yako kwenye muswada. Nilipopitia muswada huu niliogopa sana kama Bunge hili tunakwenda kupitisha pamoja na marekebisho ya Serikali yale machache, kama Wabunge hatutasimama na tukawa wakweli kwa Taifa letu tukapitisha muswada huu tunakwenda kuzika tasnia ya habari katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu kwa hali ya kawaida, ukiufungua vifungu vyote vina mapungufu. Hakuna kifungu hata kimoja kina nafuu na nitaenda kwenye muswada, sitapiga porojo, kwa hiyo, mtulie siyo mnapiga kelele. Muswada huu kwa hali ya kawaida unakwenda kinyume kabisa na Ibara ya 18(d) ya Katiba; haki ya kila mtu kupewa taarifa kwa wakati. Huu muswada kama nia yake ni njema, kama nia yake tunataka tuwasaidie hawa wenzetu wanaotupa habari na waandishi wa habari na vyombo vyake, huu muswada leo ungekuwa unazunguzia maslahi ya waandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu muswada umezungumzia tu suala la bima kwa waandishi wa habari, bima tu! Yaani, kama tunazungumza kwamba tumeleta kwa ajili ya kusaidia watu hawa na kuwalinda wapate haki zao, wawe huru walindwe katika Taifa hili ni uongo mtupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii movie imeanza siku nyingi sana, Watanzania tulikua tukiangalia inaendelea na mnakaribia kuhitimisha hii movie, leo kwa kuleta muswada huu. Ninasema hivi kwa sababu gani, Serikali hii mlianza na movie ya kufungia Bunge hili tukawa gizani Watanzania wasituone mkafanikiwa. Hii yote mliwanyima Watanzania wasijue ni nini kinaendelea katika Bunge lao. Bunge ni mkutano wa Watanzania, tunakuja wawakilishi wachache tunajadili bajeti, tunatunga sheria Watanzana waone, mkaanza kizima Bunge hili tuko gizani mkafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya hapo mkawanyima Watanzania haki ya kupata taarifa mbalimbali kupitia vyama vya siasa kwa kuwazuia wasiende kwenye mikutano. Leo katika Taifa hili katika Awamu hii ya Serikali ya Tano, vyama vya siasa hawana nafasi tena ya kuwapalekea Watanzania habari mbalimbali, mmewafungia wananchi, mmewanyima fursa hiyo. Lakini hamkuishia hapo mkaenda kwenye televisheni, redio mbalimbali magazeti mkayafungia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kupitia muswada huu mnakwenda kukamilisha azma yenu ndugu zangu Wabunge wa chama hiki tawala kama tutapitisha muswada huu; kufungia mitandao ya kijamii mbayo ndiyo ilikuwa pekee imebaki kuwapelekea Watanzania taarifa. Haya ninayosema yapo kwenye kifungu cha 3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachilia mbali redio, televisheoni magazeti, mkazungumza suala zima la mitandao ya kijamii. Lakini wakati mnajadili kwenye Kamati, Mheshimiwa Waziri ulikua unabisha hata hili kwamba huku hatuendi, lakini leo iko kwenye kifungu cha 3 na inaeleza wazi kwenye hicho kifungu cha 3 katika kueleza maana mbalimbali kwamba mitandao hii ya kijamii ni mawasiliano yalianzishwa na watu hao kwa ajili ya kubadilishana habari. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, maana yake ni nini? Sisi Wabunge tuna group letu la whatsapp tunapashana habari mbalimbali, kuna facebook na ma-group mengine. Leo hata admin wa group la Wabunge inabidi apate leseni. Ndicho mnachopitisha kwenye kifungu cha 3. Chochote mtakacho…
Kifungu cha 3 hujasoma, tulia na wewe utachangia kwa wakati wako. Tulia na wewe utachangia kwa wakati wako, soma kifungu cha 3. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo huyo anaeongea ni admin wa group hilo. Kwa hiyo, tulia ukiwa hujui, sasa ndiyo nakwambia. Unajua hata hayo ma-group leo lazima wawe na leseni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lengo la muswada huu ilikuwa ni kuweza ku-impose fine mbalimbali ambazo mtataka kutoza kwa hao watu ambao angalau wanatoa taarifa mbalimbali kwa ajili ya Taifa la Tanzania. Kulikuwa hakuna hizo fine, leo mmeweka hizo fine za shilingi milioni tatu, shilingi milioni kumi, shilingi milioni 15 na shilingi milioni 25. Mnafungia Taifa la Tanzania kwenye giza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwneyekiti, huu muswada ni wa kuogopwa, wala siyo wa kupitishwa hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapitishe kwenye vifungu mbalimbali. Kifungu cha 7(1), yaani kwa hali ya ajabu kabisa ni kwamba watu wote wanatakiwa wapewe taarifa, lakini huu muswada haujazungumzia zile televisheni ambazo siku zote zimekuwa zikichuja taarifa mbalimbali. Televisheni ya Taifa (TBC) ambayo tunalipia kodi inaamua kutokurusha taarifa fulani, inarusha taarifa fulani, hawajaweka adhabu hata kidogo. Kama lengo lenu ni jema, kwa nini hamuelezi kwamba TBC kwenye kifungu hiki siku zote imekuwa ikionesha ubaguzi wa wazi kwa taarifa fulani fulani, mnasema kwenye kipengele cha 7(1) kwamba vyombo vya habari vina haki ya kutoa taarifa kwa wote bila kubagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nia yenu ni njema mbona msiseme TBC adhabu yake ni nini kutokutoa taarifa ambayo inachuja na kubagua vyombo vingine na taasisi nyingine? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 7(b)(iv), Muswada huu unazungumzia suala la Serikali kuchuja taarifa na iandikwe taarifa ambayo Serikali itakayoelekeza. Yaani televisheni za binafsi Serikali itaelekeza kwamba ni taarifa ipi waandike. Ninyi binadamu hii nchi ni ya kwetu sote, siyo yenu peke yenu. Mnataka muwafunge midomo televisheni na magazeti binafsi na vyombo binafsi mpaka Serikali ielekeze. Huu muswada ni mzuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza kabisa, Ibara ya 7(2) mme-copy kifungu kinachotoka kwenye Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya Namba 6 ya 2016. Mme-copy each and everything kutoka kwenye sheria ile tuliyopitisha juzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hiki kifungu cha 7 wakati tunapitisha sheria hii tulileta amendment vitu vyote vile; Taarifa ya Baraza la Mawaziri, hali ya uchumi, sijui Serikali imeyumba, isikosolewe, yaani kile kifungu kipindi kile tulipowaletea amendment, sasa hivi mmekileta kizima kizima. Mme-copy na ku-paste kama kilivyo, maana yake nia yenu ilikwama kipindi kile wakati tunapitisha ile sheria, leo mmeleta tena huku mnatuchosha tulete tena marekebisho wakati vile vitu tulishaviweka sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la muswada huu ndugu zangu ni kuingiza nchi yetu katika giza, Watanzania wasithubutu kuandika chochote, wasikosoe chochote; chochote unachoandika uwe na leseni na mlishaanza by the way. Vijana wetu wakikosoa tu kidogo, mmeshawakamata mnawapeleka Polisi wakatoe maelezo; wengine wako ndani. Umekosoa tu kwamba hapa hakijaenda vizuri, yaani mnatengeneza Serikali ya nchi hii Rais asikosolewe, Mawaziri msikosolewe, yeyote asikosolewe, ndiyo mnachotaka! Ndiyo maana mmepanga hizi fine humu ndani ambazo mnajua Watanzania hawawezi kuzilipa. Huu muswada ni wa ajabu sana! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Bodi; hii Bodi kwanza Waziri anateua. Mheshimiwa Waziri asubuhi umerekebisha umeingiza wale watu wawili; watu binafsi na taasisi nyingine ambazo ni za umma. Umeingiza tu hao wachache lakini the whole component ya watu saba wote ni wateule wa Waziri. Halafu huko sasa ndiyo unataka eti hii Bodi itoe vitambulisho. Wakitoa vitambulisho hivyo, mtu umenyimwa, hujui mahali pa kwenda kukata rufaa. Hata kama umenyimwa, hakuna popote unaweza kukata rufaa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 14 inasema hivi, itaajiri kwa idhini ya Waziri Mkurugenzi Mkuu. Waziri anaweza akaamua kufanya hata delay; si hajaamua. Mpaka atakapoamua! Hivi bado mnabisha kwamba Waziri sasa ndio ameweka miguu yake yote humo, chochote kinachofanyika, mpaka yeye awepo. Uhuru uko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa hali ya kawaida, hata kama mtapitisha, kama mlivyopitisha bajeti ya juzi, hatutakaa muda mrefu tu mtakuja kulia kama tunavyolia sasa hivi. Mnalia sasa hivi hakuna fedha huko; si mlipitisha kipindi kile? Kelele zote na kila kitu mkapitisha; lakini leo Halmashauri zenu hazina fedha miezi mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 18(1) kuthibitishwa kwa wanahabari. Hakuna vigezo vyovyote ambavyo vimewekwa hapa katika ibara hii. Kama ninyi mnataka fair play, kwa nini msiweke vigezo? Ili mimi nikijua kwamba kigezo ni hiki; maana kanuni hizo mnazozitunga, sio wote ambao wanaweza wakazi-access. Hapa tunatunga sheria, wekeni basi vigezo hapa tujue kwamba mtu anapoonewa kwa kigezo hiki, anajua kwamba hiki kigezo ndiyo kimenitoa mimi kwenye ligi. Hakuna vigezo, hamviweki. Mnataka Bodi yenu mliyoiteua ndiyo iweke vigezo. Hamwatendei haki Wanahabari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 20(2) ni mbaya zaidi, tena inaenda kinyume na Ibara ya 22 ya Katiba, kwamba mtu yeyote ambaye atakuwa amesimamishwa kufanya kazi hii, hataruhusiwa kufanya kazi hii tena. Yaani unamzuia kabisa asifanye hiyo kazi ya habari. Hicho kifungu cha 20(2) mnawanyima hata Watanzania ajira. Mmeshindwa kutoa ajira huko mtaani huku tena mnaendelea kuweka vifungu kwamba hata akionewa, basi hawezi akafanya kwenye chombo kingine. TBC mkimfukuza, ITV hawawezi kumchukua, ndicho ambacho mmeweka kwenye kifungu cha 20(2). Muswada huu kama utapitishwa na kwa wingi wenu mtapitisha…
Mheshimiwa Mwenyekiti, watapitisha tu, kwani walishapewa shilingi milioni kumi hizo! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 50(1)(d) cha muswada huu, adhabu ya kuchochea uasi na maneno ya kichochezi, fine kwa mtu atakayeandika huyo, ni shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni kumi au kifungo cha miaka saba mpaka 20. Mnaenda…
MWENYEKITI: Ahsante.

The Finance Bill, 2017.

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Finance Bill ambayo iko mbele yetu.Awali ya yote niombe wale wanaotunza muda watutendee haki upande wa pili. Kumekuwa na tabia ya kukata muda, last time nilichangia badala ya dakika 10 nilipewa dakika saba na nusu. Kwa hiyo, nami naona kabisa muda pale nimeanza ngapi, muache kutukata muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Nategemea kuchangia mambo matano. Mafuta ya taa, kodi ya majengo, ushuru wa hoteli, ushuru wa mazao na vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya haya, niseme machache ambayo yamejitokeza juzi. Kwa hali ya kawaida naamini Bunge letu linaongozwa kwa Kanuni pia, kura ya bajeti ni kura ya imani na iko wazi. Ninyi ni Serikali ni Chama mnachoongoza sisi ni Wapinzani tunaotegemea kuingia madarakani, hatuwezi tukaunga bajeti yenu, ni Kanuni ni wazi, hata keshokutwa ninyi mkawa upinzani mnaweza mkawa na mawazo yenu mbadala na msiunge ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilishangaa sana kwa mara ya kwanza, huu ni mwaka wangu wa sita au wa saba, haijawahi kutokea mwongozo mtu mmoja akiomba wanapewa watu wengine sita nyuma yake, the same mwongozo. Ndiyo maana ilitushangaza sana na bahati nzuri mlifanya zile siasa mkiwa mmeachia television wazi, Watanzania wameona ubaguzi mnaoufanya wa wazi wazi. Hata kama mnakutana kwenye vikao vyenu vya caucus ni vizuri mkakumbuka critical thinking and argumentation, mmeletewa jambo lakini ni vizuri mkajiongeza, hivi kwa hali ya kawaida leo nchi nzima Miji mikubwa tunaongoza Wapinzani tukiamua kwa kauli zenu za ubaguzi ndugu zetu mlioko madarakani, tukaamua kukusanya zile kodi wenyewe, maendeleo tutashindwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ya majengo mnayochukua ninyi, kodi ya mabango mnayochukua ninyi, kodi ya ardhi mnayochukua ninyi ambayo hamrudishi tutafanya maendeleo na wananchi wetu watapata barabara, watapata hospitali, watapata kila kitu. Mkajisahau, mkaona mfanye siasa za kibaguzi, maana yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, mnawaambia Watanzania kwamba mtakusanya kwenye miji yetu hamtoturudishia na how if sisi tukaenda kwa Watanzania tukawaambia msilipe kodi, maana ninyi ndiyo mmeanza na waliwaona. Leo ukiwaambia kwamba wasilipe kodi, kwanza mlishawaambia kwa sababu mmesema hamtapeleka kwenye Majimbo ya Upinzani maana yake ni nini, mmewaambia wasilipe kodi. Ninyi ndiyo mnaleta matatizo kwenye Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfikirie ndiyo maana nikasema kwa wale ambao walisoma siasa; critical thinking and argumentation, ways and methods of decision making, maamuzi mliyofanya mmejichonganisha, mmejichora kwa Watanzania na ni aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu mlishaanza siku nyingi ndiyo maana hata hela za Mifuko ya Jimbo huku Wapinzani mmeanza kutukata, mmejiongezea ninyi. Mfuko wa Jimbo nikatolea mfano nikaombea mwongozo hapa, mmeshaanza iko wazi na hizi pesa mkianza kukusanya hamtotuletea, we are ready kwa hayo mnayotaka kuyafanya. Niwakumbushe tu, msifanye siasa za kitoto Watanzania wanawaona, inatia uchungu, mnaligawa Taifa hili. Naomba hayo yatoshe na Mawaziri wala msiendelee kuyaongelea hapo ni aibu kwenu, mnaligawa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mchangiaji amesema Serikali ni sikivu, eti ndiyo maana mkaleta sheria mkabadilisha badilisha sana, kwa sababu mmeya-accommodate mawazo ya Wabunge, kama ndivyo hili la mafuta ya taa, limewashindaje? Hayo mafuta ya taa nani asiyejua kwamba road licence haihusiani na mafuta ya taa? Hoja si ni kwamba Serikali ni sikivu, mmeya-accommodate mawazo ndiyo maana mkaleta yale marekebisho kwenye Finance Bill. Mafuta ya taa ndugu zenu wanawasha taa, vibatari, hakuna gari linalotumia mafuta ya taa, lipo? Mbona hili hamrekebishi kama Serikali ni sikivu! Nawashauri tu kama ninyi ni wasikivu toeni hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii na Finance Bill hii maana yake kila Mtanzania atalipa kodi, wala msijifiche, maana yake ni nini? Hata yale ambayo mnasema mmefuta sijui road licence, motor vehicle mmehamisha hata kwa watu ambao hawana hayo magari. Kwa hiyo, hili la mafuta ya taa naomba nipate ufafanuzi kama mlikuwa wasikivu kwa nini mpaka leo hamjafuta? Kwa hiyo, iondoke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la kuwatambua Wamachinga, MC, Mama Lishe, wauza mbogamboga, jamani! Lengo lenu ni jema kama mnavyosema, lakini siyo jema. Mmeshindwa tu kuandika mstari mmoja kwamba mnaenda kuwatoza kodi, hivi unaweza ukaniambia kwamba unataka kumtambua MC leo yuko kwenye kitchen party, kesho yuko kwenye harusi, kesho kutwa yuko kwenye msiba, kesho kutwa yuko kwenye ubarikio, eti unataka kumtambua! huyu movement yake unamtambuaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mama anayeuza mboga kichwani eti hata wauza mbogamboga hata aibu hamna mnaandika! Wengine, wanatembeza nyumba kwa nyumba unamtambuaje? Unampa kitambulisho ili iweje? Eti wauza mitumba hawa, mnataka kuwatambua muwape vitambulisho kweli? Semeni mmeamua kupeleka kodi kwa hawa wafanyabiashara wadogowadogo, Mama Lishe watalipa, kwa nini mnamumunya, mbona liko wazi, andikeni pia tujue? Tukienda kuwaambia Watanzania hao mmeshajiharibia sana kwenye bajeti hii. (Makofi)

T A A R I F A...

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa imetumia dakika tatu, muda wangu uwe pale pale. Kwanza sina sababu ya kubishana naye.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa siipokei kwa sababu hata Waziri wakati ana-wind up alisema lengo la kuwatambua ni nini, kwamba baadaye wakawe walipa kodi, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge hakuwepo Hansard ipo itatafutwa, kama hakuwepo wakati ana-wind up tutatafuta Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kuwatambua mkawatambue, mkijua mmeshindwa kukusanya kodi kwenye makampuni ya madini, mnataka mkawalipishe hawa wanaotembeza mboga mboga, it is ok tutawaambia tu, tutakutana huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja nyingine ya ushuru wa hoteli. Mkanganyiko mwingine ni huu kwamba miaka sita niliyokuwa kwenye Bunge hili kulikuwa na mkanganyiko wa ushuru wa huduma kwa makampuni ya simu, mkasema mtakwenda kuyarekebisha, mtaangalia hilo mkashindwa, lakini hata huu ushuru wa hoteli, kulikuwa na mkanganyiko wa hoteli za five stars na hoteli zingine. Miaka mingi Halmashauri zikawa hazikusanyi, this time mmeleta tena mkanganyiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tu Mheshimiwa Waziri aangalie na mwongozo utoke mapema ushuru huu wa hoteli unakusanywa kwa kiasi gani na Halmashauri zikusanye, kwa sababu mlivyoandika maana yake hata ukusanyaji wake ni mkanganyiko mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Halmashauri zetu mmeondoa vyanzo vingi, hata hivi vingine vinavyobaki muwe mnaondoa mkanganyiko, haisaidii, mnasema isikusanywe, huku ikusanywe, sijui hoteli gani hampeleki mwongozo! Pelekeni mwongozo hili likae sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ushuru wa mazao, hili la ushuru wa mazao Mheshimiwa Waziri amesema kwamba tani moja imesamehewa mazao ya chakula, pia mmeshusha kwa asilimia mbili kutoka asilimia tano sasa ni asilimia tatu. Kimsingi Halmashauri zote zilikuwa zinakusanya asilimia tatu walikuwa hawajafika hata asilimia tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, toeni vitambulisho, kwa mfano Babati Mjini, wakulima wengi wanalima Babati Vijijini Galapo, lakini huu usumbufu siyo kwamba iwe ni tani moja, kama nimelima tani kumi ni mazao ya chakula yapitishwe kwa Halmashauri zote mbili, kukaa chini na kuwapa kitambulisho wakulima wanaotoka Halmashauri nyingine wanao-cross border. Hili la kusema iwe chini ya tani kumi haitosaidia wakulima wetu, kwa sababu pia kule wanakokodi mashamba wanakuwa wameshalipa fedha na wamechangia hiyo Halmashauri. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba wapatiwe vitambulisho sivyo ambavyo imekaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la kodi ya majengo, kuna watu wanasema kwamba Halmashauri za Wilaya ziko excluded, siyo kweli. Mmesema Miji Midogo, Miji Midogo iko kwenye Halmashauri za Wilaya! Mimi sijui uelewa wa watu ukoje? Hata huko wanasema nyumba ikiwa ya tofali na ya bati mtachaji. Kwa hiyo, Halmashauri za Wilaya zipo na huu mkanganyiko ulikuwepo hata juzi wakati mnahitimisha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's