Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Khadija Hassan Aboud

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mama yetu, dada yetu mpendwa, Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie na suala la kutatua kero na changamoto za muungano. Naomba kuipongeza Serikali kwa hatua zake na Kamati na Tume zilizoundwa katika kutatua kero na changamoto hizi za Muungano mpaka hapa tulipofikia ambapo sasa Zanzibar iko huru kujiunga na taasisi zozote za Kimataifa, inaruhusiwa kukopa, Tume ya Haki za Binadamu imeanzishwa Zanzibar na mengi mengineyo. Ninachosisitiza tu harakati hizi ziendelee katika kuboresha maslahi ya Watanzania nje na ndani ya Zanzibar.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira si suala la Muungano lakini mazingira na mabadiliko ya tabianchi ni suala la Kimataifa. Zanzibar imo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo naomba jitihada zile za kuisaidia Zanzibar katika kunusuru visiwa vile iendelee. Kwa sababu utafiti uliofanywa tayari maeneo 48 ya visiwa vya Unguja na Pemba yameathirika kimazingira. Baadhi ya visima vya maji matamu vinatoa chumvi, baadhi ya mashamba yanatoa chumvi na kuna mmomonyoko wa ardhi. Hivyo basi, naomba jitihada hizi ziendelee katika kuinusuru Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila ya mazingira hakuna nchi. Hivyo naomba Wizara hii ya Mazingira iongezewe fedha katika kuinusuru nchi yetu na hasa katika maeneo ya fukwe za bahari na visiwa tengefu. Katika maeneo hayo wavuvi wanatumia uvuvi haramu, wanaharibu matumbawe na kuathiri mazingira ya visiwa hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa, humu ndani ya Bunge tumekuja kutete maslahi ya Watanzania wote, lakini bado kuna wenzetu wanang‟ang‟ania madaraka. Tayari Kisiwa Panza na kwingine maji yameanza kufukia visiwa hivyo watatawala nini hawa visiwa hivi vikishafukiwa na bahari? Mimi naomba Jamhuri ya Muungano iingize nguvu zake zaidi katika kunusuru visiwa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze katika suala la Muungano. Imesemwa hapa Muungano wetu umefifia na hauna hali ya kuridhisha na wakati wowote unaweza ukavunjika. Mimi naamini Muungano wetu kwa nguvu za viongozi wetu na Watanzania wote umeimarika zaidi na una nguvu zaidi na unajulikana Kimataifa zaidi kuliko hapo mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie katika suala la majeshi. Kwanza napenda kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania. Napenda kumpongeza Waziri wa Ulinzi kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kulinda uhuru na usalama wa wananchi wa visiwa vya Zanzibar katika chaguzi zote mbili. Uchaguzi wa Zanzibar umefanyika kihalali kwa kufuata Katiba na sheria zote za uchaguzi. Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ndiye Rais wa Zanzibar mpaka mwaka 2020. Naomba Bunge lako lisitumike kama mahali pa kujadili masuala ya Zanzibar, masuala ya Zanzibar yako kwenye Baraza la Wawakilishi.Wamesusa, watu wamekula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasikia malalamiko mengi kwamba Tume imevunja uchaguzi. Napenda niwakumbushe katika mwaka 2008 chama kimoja cha upinzani hapa Tanzania kilifuta matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Vijana kwa sababu tu hawakumtaka ambaye anapendeza kwenye chama chao na wakakaa hawana Mwenyekiti mpaka mwaka 2011, hao pia wanafuata demokrasia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea suala la ulinzi katika maeneo tengefu, naomba litumike Jeshi la Ulinzi la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kulinda hayo maeneo tengefu ya visiwa ambavyo wavuvi haramu hutumia kujificha kufanya uharibifu wa mazingira na pia maficho ya wahalifu. Naomba jambo hili litiliwe maanani kwa sababu wao ndiyo chanzo cha uharibifu wa mazingira katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kupitia Bunge lako Tukufu viongozi wetu mahiri wataendeleza mshikamano, udugu, upendo uliojengeka kwa miaka mingi mpaka kufikia miaka 52 ya Muungano wetu kwa vitendo. Mimi sina shaka na hilo, Serikali iko tayari na sisi raia tuko tayari kutii sheria za nchi. Kwa wale ambao hawatii sheria za nchi basi sheria itachukua mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nimalizie kwa kuwaombea nguvu zaidi viongozi wetu wote, Mawaziri wetu wote na sisi Wabunge, sote tutekeleze majukumu yetu tuliyotumwa na wananchi na si kuwa walafi wa kutafuta madaraka kwa njia za mgongo wa nyuma. Uchaguzi umeshafanyika, wananchi wanahitaji maendeleo, hawahitaji porojo za kisiasa au za mwanasiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kuwapongeza viongozi wote wa Wizara kwa juhudi kubwa za kuendeleza elimu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama cha Walimu Tanzania, CWT ishauriwe kupunguza mchango kwa Walimu au kuondoa kabisa. Pia michango waliochangisha waoneshe ni kwa namna gani imewasaidia walimu ili walimu wanufaike na michango yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bodi ipange mpango mkakati wa kufuatilia wanafunzi ambao wamepata ajira au kujiajiri lakini mpaka sasa hawajarejesha mikopo ili fedha hizo zisaidie kuongeza idadi ya wanafunzi kukopeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,, wanafunzi wa kike waliopata bahati mbaya ya ujauzito nashauri Wizara iwaruhusu kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara isaidie ujenzi wa mabweni ya wasichana katika maeneo ya vijijini ili kuwanusru wasichana wetu wadogo.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara iwasaidie wakulima wa mazao ya baharini:-
(i) Kuwatafutia masoko ya uhakika wakulima wa zao la mwani;
(ii) Kusaidia kuwapatia elimu juu ya mbegu bora ya mwani inayokubalika katika masoko ya nje ya nchi; na
(iii) Kuhamasisha wawekezaji wawekeze katika kujenga viwanda vya usindikaji wa mazao ya bahari, mfano mwani na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iongeze juhudi katika kudhibiti uingizaji wa bidhaa zisizo na ubora unaokubalika kwa matumizi na zinazohatarisha maisha ya mtumiaji na hasa bidhaa za chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishaji wa viwanda uzingatie ujenzi wa viwanda visivyoharibu mazingira, malighafi zake ziwe zinapatikana hapa nchini, Wizara iweke vipaumbele vya aina ya viwanda tutakavyoanza navyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napongeza juhudi za Wizara katika juhudi zake za kufufua viwanda na kuanzisha vipya kwa nia ya kuongeza pato la Taifa na kupunguza tatizo la ajira kwa wananchi na kuweza kunyanyua hali zao za maisha. Ahsante.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na uongozi wote wa Wizara na taasisi zake na wasanii wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sanaa za kazi za mikono na sanaa za ufundi zipewe msukumo zaidi ili kuwawezesha vijana wengi kutengeneza na kujifunza sanaa hizo ili waweze kujiajiri na kupunguza umaskini wa kipato pamoja na kuongeza Pato la Taifa. Maigizo na filamu zinazokiuka maadili ya Mtanzania zisiruhusiwe kuoneshwa katika jamii ili kupunguza mmomonyoko wa maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya Kiswahili ipewe msukumo zaidi ili Kiswahili kiweze kuwa ni mojawapo ya lugha yenye nguvu na iweze kuzungmzwa na nchi nyingi duniani. Hivyo itapelekea Watanzania kupata ajira zaidi katika kufundisha lugha ya Kiswahili. Pia Kiswahili kitaongeza umaarufu wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zake za kuhakikisha Wizara inatekeleza majukumu yake kama inavyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utalii naishauri Wizara iweke mkakati madhubuti katika kudhibiti mapato yatokanayo na utalii. Watalii wanaotembelea Tanzania walipie hapa nchini kuepusha upotevu wa mapato. Elimu na matangazo juu ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini ipewe kipaumbele ili kuongeza idadi ya watalii kuitembelea Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu misitu, upandaji wa miti uwe mara mbili zaidi ya miti inayokatwa. Nishati mbadala ya kupikia itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa ambapo itasaidia kupunguza miti kuchomwa kwa kutengeneza mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafirishaji wa mbao nje ya nchi udhibitiwe zaidi pamoja na kupunguza kiwango cha mbao zinazosafirishwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vibali vya ukataji na uvunaji miti katika mashamba ya miti, kwa mfano SAO Hill na kwingineko upatikanaji wake ni wa shida sana, hata muombaji aliyetimiza masharti yote. Kuna upendeleo na wanyonge ni shida sana kupata vibali hivyo. Nashauri upangwe utaratibu mzuri katika utoaji vibali vya uvunaji miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nawatakia kazi njema.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Wizara kwa kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania. Nina ushauri ufuatao:-
(i) Abiria wanaosafiri nje ya nchi wakaguliwe kwa uhakika ili kudhibiti Watanzania kukamatwa na madawa ya kulevya;
(ii) Wizara itenge fedha kwa ajili ya dharura kwa Balozi zetu kwa madhumuni ya kuwasaidia Watanzania wanaofika Ubalozini kuomba wasaidiwe baada ya kupata matatizo makubwa huko ugenini; na
(iii) Ofisi ya Makao Makuu ya Kiswahili ipewe vitendea kazi na fedha ili ifanye kazi zake kwa umahiri mkubwa ikiwa ni pamoja na kukitangaza Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namtakia Waziri kazi njema katika kutekeleza majukumu yote.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza utendaji kazi mzuri kwa Viongozi na Watendaji wote wa Wizara na Taasisi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TTCL, iimarishwe zaidi kwa vitendea kazi vya kisasa ili iweze kufanikisha malengo yake kwa kufikia kutoa huduma za mawasiliano katika maeneo na vijiji vyote ndani ya Tanzania kwa ufanisi mkubwa. Mitandao ya simu ya Tigo, Airtel, Vodacom haina nguvu katika baadhi ya maeneo na maeneo mengine mawasiliano hakuna kabisa huko Zanzibar, hivyo waongeze nguvu ili wateja wapate huduma katika sehemu zote huko Zanzibar mfano, Chukwani, Mji Mkongwe na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi za Serikali na Taasisi zake watumie huduma za simu za TTCL pia wahimizwe kulipa madeni kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Posta, liongeze nguvu na kujipanga zaidi katika huduma ya kusafirisha pesa na kupokea fedha kwa njia ya haraka ili watu wavutike kutumia huduma yao badala ya kutumia mawakala wengine wa kupokea na kupeleka fedha nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Nawatakieni kazi njema na nguvu katika kutekeleza majukumu ya kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa na mimi napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Wizara ya Ulinzi, Mheshimiwa Waziri na jopo lake lote, napenda pia kuwapongeza Mkuu na Wakuu wa Majeshi yote ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya ya ulinzi wa raia na Tanzania kwa jumla ndani na mipaka yote ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuanza kuchangia sasa hivi ni kuhusu kuvamiwa kwa maeneo ya kambi za Jeshi. Kama ilivyoelezwa na Wajumbe waliotangulia, kambi zetu nyingi zimevamiwa na maeneo ya raia. Nataka kuishauri Wizara yako Mheshimiwa Waziri tuangalie kambi ambazo zimeathirika sana na kuvamiwa na raia, tuombe Serikali tubadilishe maeneo ya kambi tupeleke maeneo mengine ambayo yapo nje zaidi na maeneo ya wananchi. Hayo ni kwa sababu ya kunusuru maisha ya wananchi waliozunguka katika maeneo yale, lakini pia usalama wa jeshi lenyewe, pamoja na vifaa vilivyokuwemo ndani ya kambi za Jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie kidogo kuhusu mapato yanayopatikana na shughuli za utendaji katika majeshi. Naomba Wizara yako kwa kupitia Wizara ya Fedha kama kuna mapato yanazalishwa na majeshi yanakwenda Serikalini, basi iwekwe percent kidogo ibakie pale ili waweze kujiendesha kwa shughuli nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa limezungumzwa suala la wanajeshi wastaafu kuwa waganga wa kienyeji. Baada ya mtu kustaafu kazi ya aina yoyote, ana uhuru wa kufanya analolitaka; na uganga wa kienyeji ni fani, siyo kila mtu anaweza. Kama mtu ana fani yake, sheria haimbani kuwa mganga wa kienyeji, kuwa mshona cherehani, kuwa mtengeneza baiskeli, kuwa fuundi makenika, anaweza! Huo ni uhuru wa raia kufanya anachokipenda! Katika uganga wa kienyeji huo anapata mapato mengi kuliko mimi ninayefanya kazi Serikalini nilivyokuwa kwa wakati huo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nizungumzie kidogo suala hili la majeshi kwenda Zanzibar, kubakwa kwa demokrasia, kuingilia uchaguzi. Ninachosema, Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni Jeshi la Wananchi wote wa Tanzania kama jina lake lilivyo. Lina uhuru na lina haki ya kikatiba ya kufanya kazi popote ndani ya Jamhuri ya Tanzania kuanzia Kigoma mpaka Kisiwa Panza mpaka Tumbatu na kazi ya ulinzi ni kazi ya jeshi hili. Kwa wale ambao hawakufurahishwa na kitendo kile, mimi nawahesabu ndiyo wale ambao walikuwa wanataka kuhatarisha amani ya nchi. Kwa sisi ambao tulikuwa tunataka tuwe huru, tufanye uchaguzi kwa amani, tulifurahi sana kuwepo kwa jeshi letu la ulinzi wa Tanzania kuja kutulinda. Wananchi walifurahi, walikuwa wako huru, hawana mashaka kama walivyokuwa mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Zanzibar ilikuwa inajulikana, wakati wa uchaguzi hali ilikuwa tete, wananchi wanaogopa hata kwenda kununua sukari nje, wanashindwa. Kila asubuhi kukicha unasikia milipuko Kibanda Maiti; milipuko Darajani; milipuko, kumezungushwa uzio. Hivi ninyi mlikuwa mnataka kufanya nini hasa? (Makofi)
Mimi nauliza kulikuwa kuna nia gani na nchi yetu hata leo imekuwa jeshi kila mahali linazungumzwa. Jeshi nalipongeza wamefanya kazi nzuri, wameilinda Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano ambayo ni wajibu wao na wamelinda raia wa Zanzibar kama ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda kulipongeza kwa dhati jeshi letu liendelee na juhudi zake hizo za kulinda amani ya nchi na nchi yetu ya Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchaguzi wa Zanzibar umefanyika kwa kufuata sheria zote za uchaguzi za Zanzibar. Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ndiye Rais wa Zanzibar, ataiongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Nawashauri, tunasikia maneno mengi hapa kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, lakini kama kweli walikuwa na nguvu ya umma inayowakubali kwa nini walikataa kuingia kwenye uchaguzi na wao wana mtaji wa kutosha? Kwa nini wamekataa mechi ya marudio? Kama kweli wana mtaji wa kutosha wa wapiga kura, ilikuwa hakuna sababu ya kukataa kuingia kwenye uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Zanzibar …
TAARIFA....
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu kazi ya jeshi ni ulinzi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la ajira. Naomba kama yalivyozungumzwa, hawa vijana waliokwenda kupata mafunzo ya JKT ndio wafikiriwe kwanza katika ajira za jeshi. Pia napenda kushauri kwamba hili jeshi letu la JKT ligawe aina ya mafunzo. Kuwe na mitaala ambayo inawahusisha wanafunzi wa vyuo wanapokwenda kupata mafunzo yawe ya aina nyingine na mafunzo ya vijana wanaoandaliwa kuwa wanajeshi au askari yawe ya aina nyingine kwa maana kwamba hapa tutaepuka kuwafundisha mambo yote ya kijeshi vijana ambao baadaye watakwenda kuajiriwa kwenye taasisi nyingine za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu nyumba za askari wetu wa Jeshi, na mimi nasisitiza kwamba awamu hii nyumba zijengwe Unguja. Nashauri kutokana na uhaba wa ardhi wa Kisiwa cha Unguja, basi sijaona ramani zao lakini nashauri nyumba hizi zisiwe nyumba ndogo ndogo badala yake ziwe nyumba za ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa nyumba nyingi na baadaye eneo litakalobaki huko mbele lije litumike kwa nyumba nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi letu ni kubwa, limekua, tofauti na jeshi la mwaka 1964 na 1967. Kwa hiyo, kwa sababu jeshi letu limekua, lazima kutakuwa na mahitaji mengi na changamoto nyingi. Kwa hiyo, la kufanya tu ni Serikali kuongeza bajeti katika jeshi hili katika Wizara hii na ifikirie zaidi kutatua matatizo mbalimbali ya Wanajeshi wetu na hasa wakati wa kustaafu walipwe viinua mgongo vyao kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami napenda kuipongeza Wizara hii ya Mambo Nchi za Nje kwa juhudi kubwa inayofanya pamoja na Mabalozi wetu walioko nchi za nje wanaoiwakilisha Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Balozi zetu zilizoko nchi za nje zinafanya kazi kubwa wakati fedha zinazopelekwa ni chache ukiachilia mbali kucheleweshwa kwa baadhi ya mahitaji yao. Pia Balozi zinafanya kazi kubwa kuwapokea Watanzania wanaopata matatizo wakiwa nje ya nchi mfano kama Oman, India, Marekani, Uingereza ambapo wengi wao huenda kwa sababu zao binafsi kama kutafuta ajira baadaye kutelekezwa na waajiri wao, wengine wanakwenda kwa matibabu wanaishiwa fedha na wanakimbilia kwenye Balozi zetu za Tanzania na Balozi zinafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi hao wanarejea Tanzania. Napenda kuzipongeza sana Balozi zetu zilizoko nchi za nje kwa uvumilivu wao huu na upendo kwa Watanzania wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri tumearifiwa kwamba Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki imehamia rasmi Zanzibar. Mimi napenda tu kusisitiza kwamba Kamisheni hii ipewe kipaumbele cha vitendea kazi ili iweze kufanya kazi zake vizuri. Kwa sababu kwa kutumia lugha yetu ya Kiswahili tutaongeza ajira kwa vijana wetu, pato la Taifa na tutaitangaza nchi yetu Tanzania duniani kote. Kwa hivyo, kuamua Kiswahili makao makuu yake kuwa ndani ya nchi yetu ya Tanzania ni fahari kwetu sote Watanzania katika umoja huu wa Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kuliongelea sasa hivi ni elimu juu ya fursa za kiuchumi na biashara katika masoko ya Afrika Mashariki. Wananchi wetu wa Tanzania wengi hawaelewi ni mbinu gani na njia gani za kufanya biashara katika masoko hayo ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kulizungumza hapa kwa mashirikiano ya pamoja kwa Wizara hii ya Mambo ya Nje na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha wanadhibiti wasafiri Watanzania na abiria wengine wanaopitia Tanzania kupitia viwanja vyetu vya ndege kwa usafirishaji wa madawa ya kulevya. Tatizo hili linalipa aibu sana Taifa letu wanapokwenda nchi za nje tukaambiwa watu hawa wametokea Tanzania au ni raia wa Tanzania. Udhibiti ufanyike pale kwenye viwanja vyetu vya ndege, madawa haya ya kulevya yasitokee nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba kwa Mabalozi wetu walioko nchi za nje watumie fursa hiyo kuitangaza Tazania na kutafuta mialiko mbalimbali kama matamasha ya kiutamaduni na biashara yanayokuweko katika nchi hizo wawalete Tanzania ili wananchi wetu waweze kufika huko. Hili nina ushahidi nalo kwa sababu mimi mwenyewe nilishawahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Utamaduni na Mambo ya Sanaa nilikuwa natafuta mwenyewe mialiko kwa viongozi na wasanii kutoka Zanzibar kwenda kuitangaza Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapofika katika baadhi ya Balozi na vikundi vyangu vya utamaduni hata wao wanakuwa hawaelewi kwamba kuna fursa za namna hiyo katika nchi zao. Kwa hiyo, ninachoomba wafanye utafiti na wawe wanatafuta mialiko kama hiyo ya maonesho mbalimbali ili Watanzania waweze kushiriki na kuitangaza nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali na Wizara kwa ujumla katika juhudi zake za kuendeleza michezo, sanaa na utamaduni nchini. Serikali iweke mkazo zaidi katika kuipa nguvu lugha ya Kiswahili kwa kutumia lugha hii katika shughuli na hafla mbalimbali za kitaifa na kimataifa ili lugha yetu hii iweze kuongeza idadi ya watumiaji na pia kuongeza soko la ajira kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, utamaduni; Serikali iendelee na juhudi za kutoa elimu kwa wananchi juu ya mila potofu zinazoathiri afya za wananchi. Serikali iendelee na juhudi za kutoa elimu kwa wananchi juu ya tamaduni zinazokandamiza wanawake, watoto na jamii kwa ujumla. Wasanii wapewe elimu ili wasiitumie sanaa kudhalilisha wanawake kwa mavazi yasiyoendana na maadili ya Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, TBC iongezewe nguvu ya vitendea kazi, rasilimali fedha, watumishi wa kutosha ili redio na TV ziweze kusikika na kuonekana nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla katika utekelezaji wa kazi za kuendeleza utalii hapa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni/ushauri; Wizara iendelee na kazi ya kuibua vyanzo vipya vya utalii na kuvitangaza duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tanzania Forest Fund (TFF), Kamati iliyoundwa kuangalia jinsi ya kutoa fedha za utafiti wa kuendeleza misitu Tanzania, uhifadhi wa misitu na viumbe wadogo wadogo kuna malalamiko kwamba wanaopewa fedha hizo baadhi yao hawakidhi vigezo na baadhi hawajishughulishi na shughuli hizo kabisa. Nashauri ufuatiliaji wa karibu juu ya fedha hizo za Serikali zilizotolewa kama zimetumika zilivyokusudiwa. Kabla ya kutolewa fedha hizo ukaguzi ufanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nawatakia utekelezaji mwema wa majukumu yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Na mimi napenda nikuunge mkono kwa kazi yako unayoifanya ya kusimamia sheria na kanuni zetu za Bunge. Endelea kusimamia sheria na kanuni za Bunge ili kulinda heshima ya Bunge letu. (Makofi)
Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Fedha, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa Wizara hii kwa juhudi zao za kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua za maendeleo. Naomba niwatie moyo, endeleeni na kazi, sisi tuko nyuma yenu kuwasaidia pale ambapo panahitajika kutoa msaada wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kutoa mchango wangu kwenye Tume ya Pamoja ya Fedha. Napenda tu kutoa msisitizo kwamba Tume hii ifanye kazi zake na kama kuna upungufu urekebishwe na kama kuna upungufu wa watendaji basi nafasi hizo zijazwe ili Tume hii ifanye kazi yake vizuri na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu mashirika ya Serikali kama NIC na TTCL. Haya ni mashirika yetu ya Serikali lakini hali yake siyo nzuri kiutendaji na katika ukusanyaji wake wa mapato au kupata mapato. Ni vyema sasa taasisi za Serikali ikayatumia mashirika yetu ya Serikali ili kuongeza mtaji na fedha zaidi katika mashirika hayo. Mfano TTCL, taasisi zote za Serikali zikitumia mitandao hii ya TTCL nafikiri tutaweza kuwaongezea mtaji wa kuendesha shughuli zao na litaanza kunyanyuka pamoja na mashirika mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taasisi ambazo zinafanana katika shughuli zake za utendaji mfano TRL na RAHCO, TBS na Weights and Measures Agency. Hebu Serikali sasa iangalie taasisi za namna kama hiyo ambazo kazi zake zinafanana au zinakaribiana iziunganishe ili zifanye kazi kwa pamoja na kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu ukusanyaji wa mapato katika bandari bubu. Ni kweli kabisa fedha nyingi zinapotea katika bandari bubu. Kwanza ni kuziorodhesha bandari zote bubu za Tanzania na baadaye kujua ni mbinu gani ambazo wanatumia katika kupitisha bidhaa. Kwa kufanya hivyo tutaweza kudhibiti upotevu wa mapato na bidhaa za magendo. Kwa kupitia bandari bubu si ukwepaji tu wa kodi uliopo huko bali pia zinatumia kupitisha bidhaa ambazo haziruhusiwi mfano nyara za Serikali zinapitishwa na zinakwenda katika maeneo mengine na zinasafirishwa. Mfano, zinaweza zikapitishwa bandari bubu za Tanga na Zanzibar na kusafirishwa huko zinakokwenda kama China na kwingineko. Kwa hivyo, ulinzi na ukaguzi madhubuti ufanyike katika bandari bubu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi natilia mkazo Sheria ya Manunuzi kama wenzangu walivyoiongelea, iletwe hapa ili ifanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitilie mkazo kuongezewa mtaji Benki ya Kilimo kwa sababu benki hii kutokana na mpango kazi wake imejipanga kwenda katika mikoa yote ya Tanzania. Tatizo lao ni mtaji wa kufika na kufungua ofisi katika mikoa yote ya Tanzania. Kama itaongezewa mtaji itaweza kuwafikia wananchi wote huku waliko ili kuwasaidia wananchi katika miradi midogo midogo ya kilimo, uvuvi, ufugaji na mingineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tutilie nguvu ukwepaji wa kodi, najua hili mnalifanyia kazi. Nataka kuuliza, kulikuwa na uwakala wa ukusanyaji wa VAT kati ya Tanzania Bara na Visiwani kila mmoja ni wakala wa mwenzake. Sasa sijui mpango huu mpaka sasa unaendelea au umesimama? Pia naomba tudhibiti mfumko wa bei, kila kukicha mfumko wa bei unakuwa mkubwa na unakuwa mzigo mkubwa kwa wananchi katika kununua bidhaa za kujikimu kimaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mifuko hii ni vema ikaangalia masharti ya wanachama wake ili kupunguza baadhi ya masharti ili isiwe mzigo kwa wananchama wa mifuko hii. Mfano umri wa kulipwa pensheni wakati wa kustaafu inamlazimisha mwanachama lazima afikishe miaka ile waliyoitaka wao na pengine kungekuwa na nafasi ya kustaafu mapema akalipwa haki zake angeweza kustaafu na nafasi zile zikajazwa na vijana wengine ambao wanataka kuajiriwa. Kwa kipengele hicho kinafanya mtu abakie tu kusubiri kulipwa pensheni kwa sababu kama hukufikisha umri huo huwezi kulipwa pensheni yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize kuhusu ukusanyaji wa mapato kwa jumla. Naomba wafanyabiashara wahamasishwe zaidi kutumia hizi mashine za kieletroniki na mashine hizi zisiwe kwa baadhi tu ya watu, ziwe kwa wafanyabiashara wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja, nawatakia kheri katika ufanisi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naanza na NFRA. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo hayatabiriki naomba sasa hii NFRA iongezewe nguvu, iongezewe fedha ili kwanza iweze kununua mazao ya kutosha na kwa wakati na kwa bei muafaka. Pili iongezewe fedha ili tuweze kuhifadhi mazao yetu kwa njia za kisasa zaidi na tuepukane na ile kuhifadhi katika maghala twende kisasa zaidi ambapo mazao yetu yatakaa kwa muda mrefu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu ukulima na ufugaji unaohifadhi mazingira. Nashauri Wizara ya Kilimo ishirikiane na Wizara ya Maji hawa wafugaji ambao wana mifugo mingi wahamasishwe na wapewe elimu ya kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya mifugo yao huko wanakoishi. Katika ukulima nashauri Serikali ihimize zaidi hasa wale wanunuzi wakubwa mfano wa tumbaku, waje na yale majiko ya kisasa ya kukaushia tumbaku ili kuepusha ukataji wa miti yetu kiholela ambayo inatumika kukaushia tumbaku. Naomba yale majiko ya tumbaku yapewe hamasa zaidi ili yatumike tumbaku yetu ikaushwe kwa majiko ambayo hayahitaji kukata miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza uvuvi wa bahari kuu kwa Serikali kuamua kwa makusudi kujenga au kuendeleza gati namba sita na gati namba tatu ya kule Zanzibar kwa ajili ya kupokea na kuhifadhi samaki wa bahari kuu. Naomba hili Serikali ilitilie mkazo, hizo bandari zimalizike kwa haraka ili nchi yetu iweze kupata mapato ya fedha za kigeni na ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba Serikali yetu ina dhamira ya dhati kabisa katika kumsaidia mkulima na mvuvi wa Tanzania. Kwa maana hiyo kwa makusudi imeondoa tozo mbalimbali na kodi mbalimbali zitakazomsaidia mvuvi na mkulima. Dhamira nyingine ya dhati ni kuweka ununuzi wa pamoja wa mbolea, hizi zote ni mojawapo ya dhamira za dhati za kuwasaidia wakulima wetu na mvuvi ili waondokane na tabu ndogo ndogo zinazowakabili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na naipongeza Wizara kwa marekebisho ya baadhi ya kanuni za mamlaka katika uvuvi wa bahari kuu. Naomba Kanuni hizi zitumike kwa haraka ipasavyo ili ziweze kutuletea mapato katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongeza kwenye Benki ya Kilimo, nashauri benki hii iongezewe mtaji ili iweze kusaidia wananchi kulima ikiwemo kuhamasisha vikundi vidogo vidogo vya vijana na wanawake kuwapa mkopo ili Wizara ya Kilimo itoe utaalam wa ukulima na utengenezaji wa mbegu bora ili wananchi wetu wapate mbegu bora ambazo zitaendana na soko, uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwa dhati kabisa kuwapongeza Viongozi wetu Wakuu wa nchi, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Viongozi wote wa Serikali pamoja na Wizara hii ambayo leo tunajadili bajeti yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira ni suala pana na linahitaji mbio za haraka ili kunusuru nchi yetu. Kama lilivyoelezwa na Wizara yenyewe na hatua mbalimbali ambazo wanachukua napongeza kwa jitihada hizo ziendelee na wazo la kuongeza fedha katika bajeti ya Wizara hii ni muhimu kwa sababu ndiyo urithi wa nchi yetu na vizazi vijavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya Muungano ni pana, hivi sasa vizazi vingi tuliopo tumezaliwa baada ya Muungano. Kwa mantiki hiyo, vijana sisi ambao wengi wetu ni raia wa Tanzania tunaoishi sasa tunaupenda na tuko tayari kuupigania kwa nguvu zote Muungano wetu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie changamoto za Muungano. Nashauri changamoto za Muungano pale zinapotatuliwa zitangazwe bayana kila mwananchi azielewe, kwa sababu ni changamoto nyingi zimefanyiwa marekebisho na zimeshafanyika kazi lakini bado wananchi hawaelewi. Nasisitiza pia ushirikiano wa sekta ambazo siyo za Muungano, kwa sababu raia wa nchi mbili hizi au wa Jamhuri ya Muungano wanatumia fursa mbalimbali kwa nchi zote mbili Zanzibar na Jamhuri ya Muungano kama hospitali, elimu na mengineyo, pamoja na utamaduni na mila zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa jina la sasa Tanzania una umri wa miaka 53, ni chombo muhimu sana kwa maisha na maendeleo ya Watanzania na hasa Wazanzibari wapenda amani, utulivu na maendeleo. Yeyote anayebeza au kudharau Muungano huu na kuwa hautakii mema tunamjua ni mmoja katika maadui wa nchi yetu. Dunia, Afrika na majirani zetu wanafahamu kwamba Tanzania ni nchi ya amani na hususan ikiwemo Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Muungano huu na Mapinduzi ya Zanzibar, majaribio mengi ya vitimbakwiri yalifanyika kutaka kudhoofisha au kuondosha kabisa, lakini kwa uimara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania majaribio hayo yameshindwa. Moja kati ya jaribio hilo ambalo limeshindwa lilisababisha kifo cha muasisi wa Mapinduzi na Muungano Mheshimiwa Abeid Amani Karume, lakini kwa uimara wa Serikali zetu majaribio hayo yameshindwa na yataendelea kushindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi ambayo inatokana na fedha na mambo yanayohusu Muungano. Naomba nichukue nafasi hii kwa kifupi sana kwa wale wasiofahamu umuhimu na maendeleo ya Muungano. Kwanza ni ulinzi na usalama, hilo sina shaka nalo ni faida moja ya Muungano, nikigusia kwenye elimu kuna miradi mikubwa ya uanzishwaji wa shule za sekondari 19 pamoja na ujenzi wa Chuo cha Benjamin Mkapa kule Pemba, hizo ni faida za Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa shule sita za sekondari zikiwemo shule tatu zilizomo katika Jimbo la Mheshimiwa Ally Saleh shule ambazo ni Forodhani, Hamamni na Tumekuja, zimo ndani ya Jimbo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mifuko hii ya Muungano tumepata mafunzo ya Walimu ambapo jumla ya Dola za Kimarekani milioni 42 zilitumika kwa mkopo wa Benki ya Dunia zilizokopwa na SMT. Pia kuna dola milioni 10 kwa ujenzi wa school mpya sita Unguja na nne Pemba. Hayo ni matunda na mafanikio ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, kuna miundombinu ya barabara ikiwemo Mkapa road Mkoa wa Mjini Magharibi, kuna barabara Pemba zilizojengwa kwa Mfuko huu wa Muungano.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi tu tarehe 4 Julai, Mkopo wa India wa USD 92.1 milioni kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji Mkoa wa Mjini Magharibi. Pia kuna uimarishaji wa miundombinu ya maji mijini na vijijini kwa mkopo wa ADB wa dola milioni 21. Pia tumesikia leo miradi ya mazingira kupitia TASAF na mifuko mingineyo kuhifadhi mikoko, ujenzi wa kuta, kuzuia bahari, bahari inakula visiwa vyetu lakini Mifuko ya Muungano inakwenda kusaidia kulinda bahari isile visiwa vyetu kule Zanzibar. Pia kuna miradi mikubwa ya mikopo ya SMT ndiyo inayodhamini Zanzibar pale ambapo itashindwa SMT inalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoona Mifuko ya TASAF imesaidia wajasiriamali wetu wadogowadogo, pia imesaidia masoko, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, imesaidia kaya maskini, yote hayo ni matunda na faida za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. Muungano wetu imara tutaulinda, tutaudumisha, kwa maslahi wa wananchi wote wa Tanzania, vizazi vya sasa na vizazi vijavyo. Dunia inaona, Afrika inaona na sisi tuko imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha ahsante sana na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika. Awali ya yote, nachukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati sana Mawaziri wetu wawili hawa; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Maji kwa ufuatiliaji wao wa karibu na kutenda kazi kwao kwa umakini katika kusaidia Taifa letu kuondokana na shida ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni moja kati ya nchi tano za Afrika zenye wingi wa maji na maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu. Tatizo letu labda ni kwenye changamoto za utaalam na rasilimali fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijielekeze kwenye hii taasisi ya Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA). Hii ni taasisi ya Serikali, unapokuja ushindani mara nyingi wanashindwa kwa sababu wana bei zao ambazo zimewekwa kwa kiwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoshauri ni kwamba Halmashauri zetu zitumie hii Mamlaka ya DDCA katika uchimbaji wa visima na mabwawa, kwa sababu hawa wana utaalam wa kutosha na pindi wamechimba kwa bahati mbaya maji hayakutoka, huwa hawadai malipo. Taasisi binafsi wanatuchimbia visima na mabwawa na baadaye wanadai malipo na maji huwa hayatoki. Nashauri iongezewe nguvu na vifaa vya kisasa kabisa ili zile kanda ambazo wameweka ziweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwenye mfuko wa maji. Nami nakubaliana na waliotangulia kwamba ile shilingi 50 sasa iongezeke kwenye bei ya mafuta, ya kukatwa kwenye mafuta, ile tozo ili ifikie shilingi 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishauri Serikali iangalie zaidi kwenye simu. Kwenye simu kuna fedha nyingi sana, tuangalie vyanzo vingine vya kuongeza huu mfuko na tuangalie haya Mashirika ya Simu. Mashirika ya Simu yanaingiza fedha nyingi, lakini wanavyowekeza kwenye maendeleo ya wananchi ni kidogo. Katika huu Mfuko wa Maji nashauri kwamba vijijini wapewe asilimia kubwa ili kuimarisha miundombinu ya maji huko Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninaloliona hapa kwenye VAT ni katika madawa ya kutibu maji. Kwenye madawa ya kutibu maji hii VAT inapelekea sasa maji yawe bei kubwa ambapo kuna baadhi ya mamlaka wanashindwa kujiendesha hata kulipa bill za umeme. Naomba liangaliwe suala hilo kwenye madawa ya kutibu maji ili kumshushia mwananchi mzigo wa kulipa bill kubwa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye mikoa yetu, mkoa wa chini zaidi unaolipa bei ndogo ni 640 Moshi, na DAWASCO wanalipa 1,663 kwa unit, lakini bei hizi bado kwa Tanzania ukilinganisha na nchi za nje, mfano Denmark kwa unit ile ile inayolipwa Moshi shilingi 650 wao wanalipa shilingi 7,658. Ukienda nchi ndogo ambayo inalipa bei ndogo na ina utaalam wa kutosha, ni China; inalipa shilingi 902, lakini Moshi tunalipa shilingi 640. Hili nataka kutoa mchanganuo mdogo zipo nchi mbalimbali na bei zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia Chuo cha Maji. Chuo hiki kiongezewe nguvu na vifaa vya kutosha ili tupate wataalam wa maji huko vijijini na kwenye Manispaa zetu. Kikiimarishwa Chuo hiki tutapata wataalam watakaosaidia kwenye Mikoa yetu na Wilaya zetu; mfano kwenye kitengo cha drill cha uchimbaji wa Visima, hiki kipewe msukumo mkubwa wa wataalam ili tuweze kuwatumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niongezee kuchangia kwenye uvunaji wa maji ya mvua ambapo suala hili liwe ndiyo kauli mbiu yetu. Tuanze na sisi Wabunge humu ndani kwenye majumba yetu na maeneo yetu tujiwekee akiba ya maji ya mvua. Nafahamu kuna nchi baadhi ya maeneo maisha yao yote wanaishi kwa maji ya mvua tu, hawana maji mengine yanayotumia, kwa sababu wapo juu ya milima, milima ni jiwe hawapati maji, maji yao ni ya mvua tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni afya. Kwa kuwa maji ni afya tukiwekeza zaidi kwenye maji, tutapunguza hata ununuaji wa madawa ya kutibu binadamu na hasa watoto wadogo ambao wanaathirika sana na maradhi mbalimbali ya maambukizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukipata maji tutamsaidia mwanamama au mwanamke kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi, atapata muda wa kutosha wa kulea familia, atapata muda wa kutosha wa kujiajiri na kuinua kipato chake, badala ya kutumia muda mrefu kuhangaika kutafuta maji. Kwa hiyo, nashauri tuwekeze zaidi kwenye Mfuko huu wa Maji ili tuweze kumsaidia mwananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea, naamini kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Rais wake, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na Mawaziri wote, wana nia na dhamira ya dhati kabisa katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanaondokana na shida ya maji na shida mbalimbali zinazotukabili. Mambo huenda kwa awamu, awamu baada ya awamu, hatua baada ya hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Wizara imejipanga vizuri katika kutekeleza mpango kazi wao waliotuandikia katika bajeti yao. Naishauri Serikali zile pesa walizoomba zitoke na zitoke kwa wakati...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote kwanza naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na Kambi ambazo zimezungukwa na maeneo ya raia. Naomba Serikali ilishughulikie suala hili kwa haraka kwa sababu tayari kuna baadhi ya maeneo ya kambi ukipita nje yanayofanyika ndani ya Kambi ya Jeshi yote raia wanayaona. Mfano Kambi ya Mwanyanya inahitaji ukarabati wa kujengewa ukuta. Pia naomba Serikali sasa ilipe fidia lakini pia izungumze na Serikali kupata maeneo mengine kwa ajili ya Jeshi, maeneo yawe ni ya Serikali yasiyohitaji watu kulipwa fidia ili kuweka akiba kwa hapo baadaye kwa ujenzi wa Kambi na matumizi mengine ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira za JKT, nashauri pia isiwe kwenye vikosi vya Jeshi tu lakini pia hata ajira za taasisi nyingine za Serikali na Serikali kwa ujumla iwafikirie vijana wetu hawa wanatoka katika Jeshi la Kujenga Taifa ili wapewe kipaumbele kwa sababu vijana hawa tayari wameshafunzwa uzalendo, ujasiri pamoja na maandili ya kuitumikia nchi na Taifa kwa jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipongeza Jeshi letu kwa kukabiliana na vitendo mbalimbali viovu vinavyofanyika katika mipaka yetu ndani na nje ya Tanzania ikiwemo kudhibiti mambo ya uharamia na mambo mengine yote yanayojitokeza yanayoashiria mambo ya kigaidi na mengineyo. Nalipongeza sana Jeshi letu kwa kazi nzuri linayoifanya katika kusaidia mambo mbalimbali yakiwemo majanga na maafa yanayotokea ndani ya nchi, wamekuwa mstari wa mbele sana kutoa msaada wa hali na mali na nguvu zao zote katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Waziri wa Ulinzi, Mkuu wa Majeshi, Kamanda wetu wa Majeshi na Majeshi yote nchini Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda nchi yetu, mipaka yetu na raia kwa ujumla. Kama ilivyotokea kuashiria kwa uvunjifu wa amani uliotokea Zanzibar wakaenda pale kwa ajili ya kulinda amani ya nchi na hawakwenda kushiriki uchaguzi wamekwenda kusimamia amani ya nchi na wameifanya kwa uzalendo mkubwa na nchi sasa iko shwari nchi iko salama, mipaka ya nchi yetu iko salama, tunawashukuru wanajeshi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba mahitaji yao ya msingi tuwasaidie, yakiwemo marupurupu na mambo mengine ya kupandishwa vyeo na madaraja ili waweze kufanya kaz zao kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninaloliomba, mwenzangu alichangia kuhusu vituo hivi vya afya, ni kweli vituo vya afya na Hospitali za Jeshi zinatoa msaada mkubwa sana kwa raia. Naomba ziongezewe vifaa na ziongezewe watalaam na kuwapatia mafunzo zaidi ikiwemo kuwapatia mafunzo wanajeshi wetu ili kukabiliana na hatari zinazojitokeza za kimataifa za uharamia na ugaidi. Naomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa zaidi kwa wanajeshi wetu na hasa vijana wadogo ambao ni nguvu kazi kubwa ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niongezee tu kwa kusema kwamba Jeshi letu ni imara, Jeshi letu linafanya kazi nzuri, na ninakipongeza kwa dhati kikosi kile ya Makomandoo wa Jeshi. Mheshimiwa Waziri kikosi kile ukione kwa jicho lingine zaidi la huruma kwa sababu ndicho kikosi ambacho tunakitegemea yatakapotokea majanga na maafa makubwa ndani ya nchi yetu, lakini Mwenyenzi Mungu naomba yasitokee hayo, nchi yetu iendelee kuishi tuishi kwa amani na salama, mipaka yetu iwekwe salama, na nchi yetu iwekwe salama. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali, Wizara ya Elimu na viongozi wote wa Wizara ya Elimu kwa juhudi kubwa za kuendeleza elimu nchini kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na waliopendekeza watoto wa kike wanapopata ujauzito wakiwa bado wanafunzi waruhusiwe kurejea shuleni baada ya kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima iimarishwe zaidi ili kuwasaidia wale vijana walioacha shule mapema na waliokosa kwenda shule kwa sababu mbalimbali zikiwemo umaskini wa familia zao.


Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi ipewe nguvu na shule za ufundi zipatiwe vifaa vya kisasa ili wanafunzi wanapomaliza waweze kujiajiri, pia waweze kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na nawatakia kazi njema.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's