Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Emmanuel Papian John

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. EMMANUEL J. PAPIAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Maana nimekaa muda mrefu naona wanaongea mara mbili mara tatu mimi nakosa nafasi, lakini nashukuru kwa kupata hiyo nafasi.
Kwanza niwapongeze wananchi wa Kiteto kwa kunichagua, wale wananchi wamenipa kura nyingi, wameniamini. Wananchi wa Kiteto nawashukuru sana na naendelea kuwaombea na naahidi kwamba nitawatumikia kama ambavyo wameniamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia upande wa kilimo kwa sababu kwanza ni bwana shamba, ni mkulima, ni mfugaji, nina uzoefu kwenye kilimo zaidi ya miaka 25. Kilimo cha nchi hii kimeshindikana, lakini nadhani kuna mahali ambapo yawezekana tumejichanganya, hebu tufikirie ni wapi tumekosea. Nchi hii sasa hivi tuna- import zaidi ya asilimia 60 ya mbegu za mahindi na mbegu za aina nyingine. Tunapolalamika, tumejiuliza kwamba sasahivi tumejiuliza habari ya pembejeo, lakini hata huyo msambazaji wa pembejeo atapata wapi hizo pembejeo. Nchi nzima hakuna mbegu asilimia 60, tunayo ardhi ya kutosha, tunao wataalamu, tunazo benki kwa nini watu wetu hawawezi ku-invest kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali haijachukua jukumu la kuwabinafsishia watu maeneo wakaweza kuendesha kilimo cha kuzalisha mbegu kiasi kwamba mbegu zikatosha na usumbufu ukapungua kwa wakulima wetu. Kuna Kanda ya Ziwa ukiangalia Kigoma, ukaangalia Kagera, ukaangalia ile kanda ya Kibondo nzima, mvua zinatosha, tungeweza kutenga maeneo, ule ukanda wote tukaweza kuzalisha mbegu, zikaweza kusaidia nchi yetu kwa maana ya kilimo, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Benki ya Kilimo imeanzishwa, ukiangalia mtaji wa Benki ya Kilimo, ukikopesha watu utakopesha watu ambao hawazidi 10, 20 hii benki na jinsi ambavyo tunawakulima na asilimia kubwa ya watu wetu ni wakulima na wafugaji hebu niambie kwa mtaji huu tunakwenda wapi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hamisheni pesa zilizoko kwenye ile Benki ya TIB, zipelekwe kwenye Benki ya Kilimo, kopeni pesa ingiza kwenye ule Mfuko, ruhusu wananchi wetu wakakope waweze kufanya kazi. Hata tutakapokwenda kutoza kodi, kuna kitu cha maana cha kutoza kwa sababu watu watakuwa wamezalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, benki nyingi za kibiashara zimeweza kukopesha wakulima na wakulima wengi wamefeli kwa sababu ya riba kuwa juu. Hata hivyo, jambo kubwa na shida kubwa hapa inaonekana ni kwa sababu hizi benki, Benki Kuu imekuwa inakopa, inaweka government guarantee na bado hazilipi zile benki na zile benki kwa sababu zinaogopa kufilisika haziwezi kushusha interest, mkulima na mfugaji wataponea wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Benki Kuu haiwezi ku-gurantee, iki-guarantee hailipi zile benki, hicho kilimo kitaenda wapi, watapunguza riba waende wapi na wanapesa za watu! Naomba kushauri, Benki ya Kilimo iimarishwe, mitaji ihamie huko, watu wakakope huko, wakachape kazi. Ukimaliza unawaandikisha VAT na TIN halafu wanalipa kodi kwa raha zao, wanaendelea kutambaa kwenye nchi yao kwa neema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto tunazalisha mahindi kwa maana ya kulisha central zone including Dar es Salaam, Morogoro, Arusha na Manyara. Awamu iliyopita, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alizungumza suala la kutujengea lami kutoka NARCO kwenda Kiteto ili mazao yaweze kutoka kwa salama. Mpaka leo hii barabara tumeimba, tumeomba, nimemwambia Ndugai, Ndugai amelia Bungeni, imeshindikana barabara, hebu niambieni hii barabara inajengwa lini niende kuwaambia wananchi. Maana Magari yanaanguka sasa hivi madaraja yemekwisha, magari yameanguka, chakula cha msaada kimeshindwa kwenda, watu watakufa njaa, barabara imekufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa mniambie leo, mimi sijui cha kuwaambia. Maana wananchi watakuja wenyewe hapa hapa maana Kiteto ni karibu hapo, wakiamua saa nne wako hapa, sasa mniambie niwaambie nini, hii barabara kwa nini haijengwi na sisi tunalisha watu? 90 percent ya mazao yanayokuja NFRA hapa yanatoka Kiteto, lakini Kiteto imegeuka vumbi, sisi hatuna benefit yoyote kwa sababu hata wananchi wetu hizi barabara wamezikosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu amani; Kiteto ni Darfur ndogo. Bunge lililopita wame-debate, mapigano ya wakulima na wafugaji watu wamekwisha. Nataka kuiuliza Serikali iniambie leo tunafanya nini ili kuhakikisha kwamba amani inatengemaa Kiteto, wakulima na wafugaji waweze kubaki salama?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Emmanuel hebu tulia kidogo. Tafadhali usiite Kiteto ni Darfur ndogo, wote tunajua nini kinaendelea Darfur, tafuta mfano mwingine tafadhali.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Haya nimefuta, lakini si zilipigwa na wewe unajua? (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ukishafuta usiendelee tena na maneno mengine, futa uendelee kutoa hoja yako.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Haya nimefuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto watu wameumizana, lakini katika mambo ambayo yamesababisha ile Kiteto watu waumizane ni pamoja na viongozi, watendaji wa Serikali kushindwa kufanya kazi. Katikati ya mgogoro wa wakulima na wafugaji kuna watu wana-benefits ndani ya haya. Wanashindwa kufanya kazi za sehemu zao ili amani iweze kupatikana na kusema ukweli na kuusimamia. Hapa watendaji wa Serikali tuamini, tuseme waliteleza na walishindwa Serikali kuchukua hatua kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu NGOs. Kiteto kuna NGOs zinapenyeza penyeza zinakuja, wanazungumza, mara tunataka hifadhi ya nyuki, mara pingos, mara nini, kila siku wamo, wanazunguka, wanaita makundi machache, wanafanya vikao, wanalipana posho. Mmoja akiulizwa Mbunge wenu yuko wapi, wanasema, Mbunge tumechelewa kumpa taarifa kwa sababu ilikuwa ni haraka haraka. Mipango na haya mambo yanayopangwa ndani ya ile Wilaya, ndiyo matokeo ya kumaliza watu yanayoendelea sasa hivi.
Niombe Serikali iliangalie hili, Serikali ifungue macho ione lakini ichukue hatua za haraka na za makusudi kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni wanasiasa. Siasa zinazochezwa Kiteto zimekuwa ni za kihuni, sasa hivi tuko salama. Sasa niombe Serikali inisaidie, wale wanasiasa uchwara wanaokuja kutembeza siasa pale, tupige siasa wakati wa siasa, lakini wakati wa kazi, tuchape kazi badala ya kugombanisha wakulima na wafugaji. Wewe ukitafuta siasa, njoo wakati wa siasa tupige, tukimaliza tuhimize amani, tuhakikishe kwamba watu wote wana uwezo wa kufanya kazi, mkulima aende shambani, mfugaji aende shambani. Niombe Serikali inisaidie kupima ardhi ya Kiteto vizuri, iipime yote, mkulima ajue anaishia wapi na mfugaji ajue anaishia wapi, mwisho wa siku sisi tuijenge amani na Serikali isimame katikati kutekeleza hilo, huu muda wenyewe ni mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie afya, hospitali ya Kiteto, tumeomba pesa, tumeahidiwa, tumeambiwa, sasa tumechoka. Tunaomba jamani ile hospitali ikarabatiwe maana sasa hospitali itakuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko pale. Wodi ya wanaume iliyoko pale imechanganya na wale wagonjwa wa TB (Tuberculosis), wote wanachanganyika humo humo, sasa wale watu wataponea wapi? Aliyejeruhiwa ameanguka na pikipiki humo humo, aliye kwenye dozi ya TB yumo humo humo. Sasa tutajengewa lini hii wodi za wanaume zitenganishe hawa watu ili wananchi wasiweze kuambukizana magonjwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali inisaidie na Waziri wa afya, hakikisheni kwamba mnaweza kunitatulia huu mgogoro na ile hospitali ikarabatiwe maana sasa imefika mahali tunafanya repair tunazibaziba wenyewe, tunakwenda huko tunakarabati mahali, tunasogezasogeza ili lile jengo lisije likaangukia wagonjwa halafu tukaongeza wengine tena wodini, tukaongezea yale magonjwa wanayoumwa, halafu tunaongezea mengine tena ya jengo kuwaangukia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine tulilonalo Kiteto ni la maji. Kata za Dongo, Songambele, tumechimba visima, ile nchi ni kame. Hebu Serikali iangalie mfumo mpya wa kutusaidia, ile nchi ni kame, wamechimba visima havifiki. Visima vilivyochimbwa vikipatikana maji havifungwi mapampu ili watu waweze kupata maji. Niombe Serikali iweze kuliona hili kwamba kama inawezekana, tuchimbiwe mabwawa ya kutosha, watu watatumia maji na mifugo itatumia maji hayo hayo ili angalau tuweze kuokoa maisha ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ndani ya Mji wa Kibaya; ule mji Rais ametuahidi visima kumi, ametuahidi pesa, vile visima vimeshindikana. Sasa ule Mji wa Kibaya mnataka watu waende wapi, imeshindikana, watu hawapati maji na tumeahidiwa maji muda mrefu sana. Naomba Serikali iweze kuliona hili ule Mji wa Kibaya uweze kuokolewa maana watu wameongezeka, maji hatuna, tuna visima viwili, maji hayatoshi, watu wanabeba ndoo, akinamama wameota vipara. Na mimi niliwaahidi akinamama nikiwa Mbunge mtaota nywele mwanzo mwisho. Naomba Serikali ichukue jukumu la kuhakikisha kwamba hawa akinamama wanaota nywele kichwani. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha. Sasa atafuata Mheshimiwa Jamal Kassim Ali.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kushukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo imejaa mambo mengi ambapo yote yanakidhi matarajio ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la kilimo. Wizara ya Kilimo nilidhani ingeweza kutusaidia kwa maana kwamba Benki ya Kilimo ingeweza kubeba zile pesa ambazo ziko TIB ili kuongezea mtaji ambao ni ile shilingi bilioni 60 inayotajwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Fedha nyingine nilizotaka ziweze kuhama ni zile za Mfuko wa Pembejeo wa Kilimo ambazo ziko Exim Bank. Zile pesa kama zingehama zingeweza kuongezea capital kwenye ile bilioni 60 ili wananchi waweze kukopa kwa urahisi kwa sababu itakapokuwa fedha zote ziko mahali pamoja itatusaidia kuweza kukopa na wananchi wetu wengi ambao ni asilimia 80 wako vijijini wangeweza kukopa pesa hizo, hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili NFRA wamesema watanunua tani laki moja. Tani laki moja ni kiasi kidogo cha chakula, naomba Serikali iweze kununua chakula karibu tani laki mbili ili itakapotokea shortage tuweze kukabiliana na uhaba wa chakula. Hata hivyo, tutakapokuwa na excess wana uwezo wa kuuza nje kwa maana kwamba kurudisha pesa ili waweze kwenda kwenye season nyingine ya ununuzi wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo za kilimo. Hebu tuangalie ni njia ipi ambayo inaweza kutusaidia. Kwenye kilimo ningeshauri tuangalie ni namna gani ya kuweza kuzalisha mbegu zetu wenyewe kuliko importation ya mbegu ambapo tunatumia foreign currency kuziingiza hapa nchini, ni gharama kubwa. Pia Serikali iangalie ni namna gani ya ku-invest kwenye kilimo cha mbegu ili tuweze kuzalisha mbegu wenyewe nchini na kupunguza hali ya kutegemea mbegu za nje ambazo mara nyingine ni hatarishi kwa maana ya kilimo chetu hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni dawa za ruzuku za mifugo. Ukiangalia dawa za ruzuku za kuogesha mifugo hapa nchini zinasumbua, haziui isipokuwa kwenye ile zero grazing (ng’ombe wale wa majumbani) lakini ukienda kwenye wale ambao wanafuga nje mifugo mingi kupe hawafi. Nashauri na kuiomba Serikali iangalie importation ya dawa hizi au wale watengenezaji basi waangalie mara mbili kwa sababu kupe hawafi, ng’ombe wanazidi kuumwa na hii inachangia sana kusababisha mifugo yetu kutokuwa na afya na mwisho wa siku tunakuwa na mifugo ambayo haiko kwenye kiwango kwa sababu ya dawa ambazo hazikidhi kiwango cha kuweza kutibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuomba ujenzi wa Kiwanda cha Nyama pale Ruvu. Naomba Serikali ijikite kuangalia namna gani ya kujenga Kiwanda cha Nyama ili mifugo yote inayoweza kuingia Pugu iishie pale Ruvu ikachakatwa, nyama zikaingia kwenye supermarkets na masoko yetu tukawa na nyama bora. Hii itasaidia kuwa na nyama ambazo zimepimwa na ziko kwenye viwango. Pia tutaweza kujua ni mifugo kiasi gani tumechinja lakini hata ili revenue yetu haiwezi kupotea kuliko kwenda kushindana pale Pugu. Hilo ni jambo ambalo ningeomba Serikali ijikite kulishughulikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba soko la mazao Kiteto, sisi tunazalisha mazao mengi sana. Ukiangalia central zone nzima inategemea mazao ya Kiteto, Dar es Salaam inategemea Kiteto, Tandale nzima inategemea Kiteto kwa asilimia karibu 50 lakini hatuna soko.
Naomba Serikali ilione hili itujengee soko ndani ya Wilaya yetu hata kama kuna soko la Kibaigwa lakini tuwe na soko letu la ndani. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda alione hili, tuwe na soko letu la ndani tuweze kuwa na internal collection yetu, tuweze kuona ni namna gani na sisi tunaweza kuvuka huko mbele tunakokwenda ili tuweze kupata namna gani ya kuweza kuingiza mapato lakini na watu wetu waweze kufaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na hilo, lile soko pamoja na NFRA kwa mfano inanunua mazao Kiteto zaidi ya tani labda 10,000 au 15,000 ile transportation cost ya kuja NFRA tungependa wapewe wananchi wetu wenye magari wasafirishe kile chakula kuliko kumpa zabuni mtu akasafirisha kile chakula na wananchi wakabaki pale. Ni mojawapo ya creation employment kwa vijana wetu. Watu wetu waweze kufaidi hata hii asilimia ndogo ya kusafirisha hicho chakula kwa sababu na wao magari wanayo. Hii inaweza kusaidia kwa sababu tenderer anaweza kusafirisha kwa gharama kubwa wakati wale wananchi wanaweza kusafirisha kwa gharama ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shilingi milioni 50 kila kijiji, plan yake vyovyote vile itakavyokuwa kwa Kiteto tumejitahidi kufungua VICOBA, SACCOS na vikundi mbalimbali lakini ningeomba nitengeneze commitment. Hebu twende tuangalie kwenye maeneo hizi pesa zikienda, je, kwa mfano Kiteto tunaweza kutengeneza commitment yetu ya kutumia pesa hizi, tukazalisha, zikazunguka kwa wananchi, tukazisimamia wenyewe, kukaja returns kwa kufikiria muundo wetu wa namna gani ziweze kuzunguka zikafikia watu. Maana tukienda kwa maana kwamba kuna watu wale ambao watakuwa ni wajasiriamali ndiyo wapate hizo pesa then wale ambao siyo wajasiriamali katika ile routine ya mzunguko wa zile pesa wao watakuwa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sisi Wilaya ya Kiteto tulete plan yetu mkiona inafaa basi tu-guarantee, tu-sign contract, mtupe hizo pesa tuzizungushe kwa maana ya wananchi wetu katika zile SACCOS and then tuzalishe ile riba na bado tuoneshe ile flow ya matumizi ya zile pesa na jinsi ambavyo zinavyoweza kurudi Serikalini ili ziwasaidie wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyo trend ni kwamba tutakapokuwa tumeweza kuwapa watu wengine wale wazee ambao hawawezi kupata hizo pesa basi watakwenda kwenye ile role ya TASAF. Ile asilimia 10 ya vijana na wanawake ambayo itakusanywa kutokana na ile collection ya Halmashauri basi itasaidia vijana. Lengo letu ni ku-make sure kwamba tunaweza ku-monitor wenyewe, tukajua ni watu gani wanaweza kupata pesa hizo na nani hana, nani anastahili na nini kifanyike ili mradi ile community nzima iweze ku-benefit kutokana na hiyo collection na zile generation ya income ambazo tutakuwa tumezipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie kuhusu mapato. Tumekubaliana ndani ya Serikali zile electronic machines zitatumika kukusanya mapato. Kuliko sasa hivi kwenda kwenye ku-tender, sijui tenderer amepata pesa, nashauri kwamba Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Halmashauri wasimamie kwa kutumia electronic machines tukusanye mapato wenyewe. Hii ni creation of employment, tujue tumepata nini, Halmashauri zetu zinaweza kukusanya zaidi kuliko tenderer ambaye anaweza ku-benefit zaidi kuliko Halmashauri zetu ambazo zingeweza kusimamia zenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna barabara ambayo inatoka NARCO hapa njiapanda kwenda Kiteto. Hii barabara wakulima wengi wanaitumia, tunaomba Serikali ituone. Ni ahadi ya Serikali tangu mwaka juzi, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alituahidi kwamba angeweza kuitengeneza barabara hii. Tunaomba Serikali ya awamu hii kupitia mpango wake wa fedha hebu tuoneeni huruma, hii barabara haina shida kabisa, ina madaraja mawili tu au matatu. Mheshimiwa Waziri Mkuu uko hapa, tuokoe kidogo angalau na sisi tupitishe mazao yakafikie walaji kwa gharama nafuu lakini na mkulima aweze ku-benefit kale ka-profit kwa sababu transportation cost zitashuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Handeni – Kilindi – Kiteto – Chemba – Singida. Barabara hii inafungua mikoa mitano, inafungua Tanga, Manyara, Dodoma na Singida. Ile pipeline ya mafuta wanayosema ya kutoka Uganda itapita pale. Hebu Serikali tuoneni huruma, tunaomba hii barabara muiweke kwenye mpango. Barabara hii itakapofungua mikoa hii itapunguza hata msongamano wa hii barabara ya Dar es Salaam ili watu wengine wapitie kule lakini tutakuwa tumefungua mikoa kwa maana ya programu ya kufungua mikoa yote kwa barabara za lami na watu wote waweze kupita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu CDA naomba Serikali ijaribu kuona ni namna gani inaweza kutengeneza plan ya EPZ zone kubwa hapa Dodoma ili vitu vingi na investors wengi waje Dodoma wakuze mji wetu na ivutie watu ili tupunguze msongamano Dar es Salaam. Hilo la msongamano linaweza kuhamia Dodoma, tukaweka kijiji kingine ambacho ni business city center ndani ya mji wetu wa Dodoma na ikapanua mji na kuongeza ajira na watu wakaongezeka Dodoma na sisi tukaendelea ku-benefit. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu ni mchache naona umekwisha, naomba kuishukuru Serikali. Nimpongeze Rais Magufuli kwa kazi anayoichapa, wote tumuunge mkono. Tulimuomba Mungu atupe Rais ambaye anatufaa Watanzania kwa sasa. Hebu tumuunge mkono, tukubaliane naye, maamuzi anayoyafanya tumuunge mkono, tusibaguane kwa itikadi za vyama, tuhakikishe kwamba tunamuunga mkono, tumpe full support ili aweze kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Watanzania kule tunakotakiwa kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri Mkuu, anachapa kazi, yuko makini, hana mjadala, kazi lazima iende, tusiwakatishe tamaa viongozi wetu. Tunawaunga mkono Mawaziri wetu, chapa kazi tuko nyuma yenu, fungulieni speed zote, fanana kama gari linaloshuka mlima halina break tusonge mbele, huko tutakakoishia Watanzania wote tutakuwa tumekubaliana kwamba lazima maendeleo yapatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Spika naomba kuchangia kwa kushauri mambo yafuatayo:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Serikali isaidie ujenzi wa ofisi ya Tume ya Maadili, wasaidiwe vyombo vya usafiri angalau gari moja kila mwaka, ikibidi wakope kwenye Mifuko wajenge na Serikali ilipe polepole ili waache kupanga kama sehemu ya kupunguza gharama kwa Serikali pia kama sehemu ya kutunza siri na ulinzi wa kutosha kwenye ofisi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni kuhusu Ofisi ya Nyaraka za Serikali. Hiki ni kitengo muhimu sana naomba wapewe fedha kwa awamu, pia wajenge na kwa sababu wana maeneo wasaidiwe. Watumishi kwenye Wilaya na Mikoa huonesha uzembe mkubwa katika utunzaji wa nyaraka katika maeneo yao, nashauri watumishi wazembe kupitia DED watambuliwe na kupewa onyo kali.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. EMMANUEL J. PAPIAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hata kama ni dakika kidogo. Nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ninalotaka kuzungumzia, nimekuwa nashauri sana juu ya Benki ya Kilimo. Nimeomba mara nyingi sana kwamba hii Benki ya Kilimo ina mtaji mdogo, nimeomba zile pesa za TIB zihamie Benki ya Kilimo; nimeomba zile pesa za Mfuko zilizoko Exim zihamie Benki ya Kilimo ili benki yetu iwe na mtaji wakulima na wafugaji wetu waweze kukopa kwenye benki moja ili waende kwenye chombo kimoja, wapate huduma mahali pamoja, warejeshe malipo yao mahali pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hii benki ihamie Dodoma. Kwa nini benki ikae Da es Salaam kwenye yale majengo maghorofa yanayolipa gharama kubwa! Majengo yapo Dodoma katikati ya nchi, anayetoka kusini aingie, anayetoka Kaskazini aje, anayetoka Magharibi aje lakini naomba hii Benki ihamie Dodoma. Hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nililotaka kuzungumza ni hili suala la migogoro ya wakulima na wafugaji. Migogoro ya wakulima na wafugaji mara nyingi ukikuta mahali kuna mgogoro, wakulima na wafugaji wanapigana, mwanasiasa anafaidika na ule mgogoro. Watendaji wa Serikali wanafaidika na ule mgogoro!
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iangalie ni namna ipi tunaweza kufanya ili kuhakikisha kwamba mgogoro unapotokea mahali, unakabiliwa kwa wakati, wale Watendaji wa Serikali, Mwanasiasa anayeshiriki katika hilo, achukuliwe hatua haraka na Serikali ijulishwe na wananchi wajue ili kuweza kuhakikisha kwamba tunakabiliana na migogoro inayotokea baina ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nizungumzie NARCO. Ukitaka kuitafuta Wizara ya Mifugo, lazima utaitafuta NARCO; ukitaka kuzungumzia mifugo nchini, lazima uitafute NARCO. Wabunge wengi wamezungumza habari ya mashamba yaliyoko huko Kalambo, Kagera, Arusha, Tanga; NARCO ndiyo yenye maeneo makubwa, lakini NARCO haipewi mtaji. Kwa nini haipewi mtaji? Nilishaomba nikasema, NARCO iombewe pesa za nje zenye riba nafuu ikopeshwe, mashamba yajazwe mifugo, tuajiri wataalam waingie pale, tuwasainishe mikataba, wakishindwa, ni Magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mashamba yako wazi, wafugaji pembeni wanayavamia, mwisho wa siku inaleta migogoro. Ndiyo maana inafika mahali watu wengine wanasema haya mashamba yachukuliwe, yanyang‟anywe. Haya mashamba yanakwenda wapi na ndiyo jicho la Wizara! Hakuna mahali pengine unaweza kuiona mifugo au kufanya researches? Watu wengi, sasa hivi wataalam wetu na vijana wengi wanaofanya Ph.D, Masters, kwenye fields wanakwenda kwenye hayo maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na kuishauri Serikali kwamba iombe pesa za nje kwa ajili ya NARCO, i-inject pesa za kutosha, iongeze wataalam tuweze kusimamia hayo maeneo na tuweze kufanya kazi kwa kuingiza mapato kwa maana nzima ya hiki Kitengo chetu cha Mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa kwenye Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, mikoa ilipokuja juzi Dar es Salaam, nilikuwa nawaambia kila mkoa ujaribu kuainisha ni mazao gani yanaweza kustawi lakini ambayo ni commercial. Tusi-base kwenye mahindi, mwisho wa siku tukivuna, yanakuwa mengi, hayana soko. Mikoa ikiweza kuainisha yale mazao kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, yale mazao ya biashara; ufuta, alizeti na kadhalika yanaweza kusaidia mazao yakatoka nje tukaingiza foreign currency badala ya ku-depend on haya mazao ambayo asubuhi na jioni hatuna bei, bei imepatikana, haipo na internal collection bado haipo.
MHE. EMMANUEL J. PAPIAN: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushukuru, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kazi nzuri, ambayo inaifanya baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais. Napenda kushauri mambo machache yafuatayo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kwenye elimu Serikali imefanya mambo mengi, lakini na mengi yamezungumzwa humu ndani ambayo yanaelekeza ni jinsi gani ambavyo elimu inaweza kwenda na jinsi gani iwe na watu wote wametoa ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba aanze na Primary Schools. Ile mitaala ya Primary Schools ya zamani tuliyoizoea airudishie ule mfumo kwamba ukikuta Kitabu cha Darasa la Kwanza anachokisoma Mwanafunzi aliyeko Nkasi Tanzania, kule Rukwa, Sumbawanga, kitabu hicho hicho tukikute Lindi cha Darasa la Kwanza, kinachofanana na kinachosomeka vile vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri a-plan Primary Schools kwanza, asiende haraka! Sekondari pumzika, Vyuo pumzika, taratibu tu, kule kunakwenda kuna Makamishina, kuna watu wanafanya, wewe nenda na Primary Schools, jenga misingi; hakikisha Walimu wanafundisha, hakikisha shule zinakaguliwa, hakikisha kuna utaratibu wa elimu kwa zile ambazo ni Sekondari, za Kiingereza Primary Schools wawe na mitaala inayofanana. Zile za Kiswahili zirudi vile vile kama zamani. Sayansikimu; mtoto afundishwe kutengeneza mwiko, chungu, afundishwe kupika, kulima; tunataka hiyo ianze Primary School bila haraka kwa mwaka huu. (Makofi)
Mwaka kesho wewe nenda Secondary School, Form One mpaka Form Six, panga mambo vizuri, usiwe na haraka, pesa hazitoshi na sisi ndiyo wakusanyaji, hazipo! Hicho kidogo kinachopatikana, mwaka kesho plan for Secondary School, Form One mpaka Form Six. Mwaka unaofuata, plan kwa ajili ya vyuo, nenda tena mpaka Vyuo Vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri awatafute wale Walimu wa zamani waliokuwa wanafundisha zile shule za primary; kaa nao, zungumza nao wakupe tactics na the way kuingia katika huu mfumo wa kutengeneza elimu bora kama ile ya zamani ambayo tunahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri akae na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Tunao Mabalozi nje, wafanye kazi ya kutafuta scholarships kwa ajili ya wanafunzi wetu waende wakasome nje. Kila mwaka Balozi yeyote kwenye nchi aliyomo ambayo ina uwezo, aweze kuita na kutafuta wafadhili wasaidie watoto wetu wakasome nje. Lengo kuu la kusomesha watoto wetu nje, Watanzania wamejifunga; Watanzania wako magereza, wamefungwa; hawatoki nje! Wanafikiri hapa panaweza. Waende nje wakapigwe, wapigwe baridi, wapate shida, walale njaa, wakirudi Tanzania watashughulika na uwekezaji. Mheshimiwa Waziri, hebu jitahidi zungumza na hao watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, hawa wawekezaji mnaowaona ni kwa sababu wameona fursa huku, tupeleke watoto wetu kule. Wale watoto ukikaa nao ukiwaambia nenda kasome au nenda Netherlands, ukimaliza degree shawishi mfadhili ndugu yako mwingine apate nafasi umlete huko huko. Mkibaki huko, sawa; mkirudi Tanzania, sawa. Tutakuwa tumetengeneza Watanzania kwenye exposure ya dunia hii nao watoke nje wakaone vilivyoko huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkaguzi mmoja Kiteto alikuja ametoka kwenye kanda, ana gari, hana mafuta, hana nini. Nikamuuliza, sasa vipi? Anasema sasa nitakagua nini? Anataka kukagua na anayeombwa mafuta ni Mkurugenzi na akienda kuomba Mkurugenzi mafuta Mkurugenzi haiwezekani akamnyima mafuta kwa sababu anakwenda kumkagua; akimkagua anamletea madudu; akimletea madudu, hawataelewana. Matokeo yake anakosa mafuta, anakaa mezani analipwa mshahara bure. Hii ndiyo mishahara hewa ambayo tunazungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hawa Wakaguzi waanze na Primary School wakutengenezee kitabu, wakuletee ujue matatizo ya Primary School kwa nchi nzima kwa mwaka huu ili ujue sasa shida za ku-tackle matatizo ya Primary School yanaanzia wapi na yanakwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto tuna shule za mabweni chache, lakini watoto wetu kwa sababu ya maeneo ya kifugaji, ni mbali. Shule nyingine ni kilometa 14, shule nyingine 15, sasa watoto kwenda shuleni ni ngumu.
Nakuomba, kuna shule za Dongo za sekondari, tunaomba hizi shule za bweni, za kifugaji basi mtusaidie waweze kusoma kwa maana ya kupata hela ya chakula ili wale watoto tuweze kuwa-accommodate kule kwa sababu wakirudi majumbani mwisho wa siku wanaolewa. Kule kuna ndoa ambayo Mkuu wa Shule akipewa ng‟ombe mmoja anaachia mtoto anakwenda anaolewa na anaolewa underage. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba zile shule zangu za Dongo, kuna Engusero, kuna Resoit Secondary School, kuna Rarakin Primary School. Hizi shule tunaomba zipate msaada wa kupata hela ya chakula ili watoto waweze kulala bwenini na wote tuwabebe wakae huko wasiweze kutoka kwenda kuolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, ali-plan na sasa tumefikia, changamoto zipo, ni nyingi, lakini tuna hakika kwa kushirikiana tutaweza. Naomba niseme, Bunge hili lilikwenda likazuia kidogo fimbo za makalio kidogo na kwenye mikono, hebu turudishe fimbo watoto wajue kwamba jamani kuna malezi. Turudishe bakora kidogo kwenye mikono; Walimu wanadharaulika! Wakisema, hawasikiki! Hebu turudishe huo utaratibu jamani, turudi tulikotoka. Sisi ni Waafrika. Ni lazima kuwa na nyenzo kidogo twende, hatutafika!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hebu ajitahidi aangalie namna ya kuliweka hili, fimbo zirudi kidogo. Aombe huko juu fimbo zirudi halafu watoto waanze kuogopa, hata wawahi shuleni wakasome wakiambiwa wasome; wakikemewa wakimbie, wakiitwa waje wanakimbia. Discipline iwepo. Walimu wanatukanwa shuleni na mtoto wa Darasa la Tano na wazazi twende tukaseme. Waheshimiwa Wabunge nanyi semeni huko tushinikize hili tuondoe tabia utovu wa nidhamu, halafu watoto warudishiwe fimbo kidogo halafu mambo yasonge mbele.
Mheshimiwa Waziri, naomba kusema kwamba nakushukuru lakini anza na primary mwaka huu, umalize matatizo ya primary; mwaka kesho sekondari, mwaka kesho kutwa vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninalopenda kuzungumzia ni juu ya reli hii ambayo imepangwa kujengwa lakini napenda kushauri kwamba ujenzi wa reli hii uwe kwa awamu kwa sababu kila anayesimama anazungumzia reli, lakini reli haiwezi kujengwa kwa wakati mmoja, nafikiri tujenge reli kwa awamu kama ni Dar es Salaam - Tabora, kama ni Dar es Salaam – Mwanza. Hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kuna barabara ya kutoka Handeni - Kibirashi - Kijungu - Kibaya - Njoro nimeiona kwenye mpango. Barabara hizi kuzijenga ni gharama kubwa kwa Serikali na ukiangalia gharama na jinsi zinavyotakiwa kwa maana kwamba kila mtu anaomba barabara, ningeshauri mambo yafuatayo:-
Naomba Mheshimiwa Waziri safari hii ajenge barabara kutoka Handeni - Kibirashi aishie hapo, mwakani ajenge Kibirashi – Kibaya - Kiteto aishie hapo, mwaka unaofuata ajenge Kibaya - Chemba aishie hapo, mwaka unaofuata ajenge Chemba – Singida, ndiyo njia pekee inayoweza kusaidia barabara hizi kuisha. Hizi barabara unaweka upembuzi, pesa inaingia, feasibility study baada ya muda fedha zikikosekana mnaanza upya tena, hizi zote ni gharama kwa Serikali na tunapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kushauri barabara zijengwe kipande kidogo kidogo na kwa awamu. Barabara itakayopata mfadhili wa nje kama ni kilometa 400, 500 akiianza amalize yeye mwenyewe lakini kama ni fedha za ndani tujenge kidogo kidogo ili na maeneo mengine yapate na fedha nyingine zitumike kujenga barabara hizi za vumbi na changarawe katika maeneo mengi ikiwa ni sehemu ya kufungua barabara zetu za vijijini. Hilo ni jambo la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti jambo la tatu, naomba kushauri kama inawezekana tubadilishe mfumo wa manunuzi itusaidie kwenye mambo haya yafuatayo; hizi fedha zinazotengwa kwenda kwenye halmashauri zetu kwa ajili ya barabara hebu toeni asilimia 20 tukopesheni vifaa kwa ajili ya barabara. Mkoa mzima wa Manyara kama umetengewa shilingi bilioni tatu au shilingi bilioni nne, asilimia 20 Serikali tukopesheni vifaa, weka government guarantee tupate katapila na vifaa vingine vya ujenzi wa barabara, sisi wenyewe tu-fuel halmashauri zetu kutokana na collection za ndani, tutumie gharama nafuu kutengeneza barabara zetu za halmashauri vinginevyo ni gharama kubwa kwa Serikali. Tusipobadilisha hii sheria hatuwezi kupata hiyo guarantee na kuweza kununua vifaa vyetu. Najua hii inaokoa fedha nyingi za Serikali lakini kama kuna mikono ya watu wanaotafuna haiwezi kupita. Naomba Wabunge mniunge mkono kwa hili tuweze kuwa na vyombo vyetu vya kutengeneza barabara zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Arusha – Kibaya - NARCO, nimekuwa namwambia Mheshimiwa Spika barabara ya NARCO - Kiteto mbona huizungumzii anasema nimebanwa. Sasa Mheshimiwa Waziri useme leo umembanaje Spika, kwa nini hutengenezi barabara hii? Barabara hii ni ahadi ya Serikali, ni ahadi ya Mheshimiwa Kikwete mwaka 2013 mpaka leo imeshindikana. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, jenga barabara ya NARCO – Kongwa na NARCO - Dosidosi tu. Jenga Kongwa kwa mwaka huu mwaka unaofuta jenga Dosidosi mpaka Kibaya kilometa 39, kidogo kidogo mwisho wa siku utafika Oljoro, Arusha. Mimi naomba tujenge barabara kwa awamu ili hii barabara itengenezeke, lengo ni kufungua barabara hii ili mazao yaweze kutoka. Kiteto ndiyo inayolisha Tanzania kwa maana ya Dar es Salaam, ndiyo inayolisha Kanda ya Kati, kwa nini hamfungui barabara hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa pili ndani ya barabara ile zimeanguka gari saba kwa siku moja zikipeleka chakula cha msaada. Sasa kwa nini msifungue hii barabara tukaweza kupita, ni zaidi ya kilometa 91 tu. Nadhani jitihada za makusudi hazijachukuliwa kukamilisha ujenzi wa barabara hii. Barabara ya Oljoro - NARCO iliwahi kutengewa shilingi milioni 900 mwaka 2013 za upembuzi mpaka leo hatujui zilienda wapi. Tunaomba hii barabara iangaliwe na itengenezeke, tutaamini kama Thomas tutakapoona wakandarasi wako site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya ndege, ndege tunazihitaji, tunahitaji Watanzania watembee lakini kuna jambo nataka kushauri. Viwanja vyote vya ndege ambavyo sasa vina vumbi, vimekwanguliwa hebu suburini kwanza, jengeni hivi viwanja vyote ambavyo mmeanza vya Dar es Salaam, Arusha, KIA, Mwanza ili vimalizike, tujenge kwa awamu na tutakapomaliza tuanze kiwanja kimoja kimoja kwani kushika miradi mingi kunatupotezea mambo mengi. Bajeti ya nchi ni ndogo, fedha zinazokusanywa ni kidogo, tufanye jambo liishe tukirudi hapa tuseme liliisha. Kila siku unazungumzia habari ya kiwanja cha Mwanza, miaka 10 unahangaika na nini kama kimetushinda kiacheni! Jenga Dar es Salaam ukimaliza hamia Arusha, ukimaliza hamia Mwanza, ukimaliza hamia Kigoma, ukimaliza hamia Kagera, maliza kwanza kimoja ujue kwamba kiliisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndege. Rwanda ina ndege mpya 14 na ni nchi ndogo, ATC imebaki alama, kwa nini? Mmeonyesha mpango wa kununua ndege lakini kama tunanunua ndege, niwashauri Wabunge wenzangu tukubaliane tutafute CEO wa kampuni au shirika hilo kutoka nje, siyo Mtanzania watalifuta, litaliwa! Watafunaji ni wengi na kwa sababu hakuna anayeiunga mkono Serikali, leo tunalalamika ndege, ndege, tumeuwa wenyewe, tunatafuna wenyewe, kilichoko kinaliwa, mashirika kutoka nje yanatutafuna, tuna-sign wenyewe, mnahangaika na nini? Tu-import wataalam watufanyie kazi tuwalipe ili tuokoe vinavyowezekana. Naomba kushauri hizi ndege zitakazonunuliwa punguzeni watumishi wote wa ATC bakiza wachache, zitembee ndege chache, zifanye kazi, wakope wanunue nyingine ziweze kutembea ndani ya nchi yetu at least kwa hesabu tukijua kwamba wamekopa watalipa, wakishindwa magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbunge mmoja amesema barabara za lami wanabandua wanabandika, ndiyo! Kitaalam lami life span yake ni miaka 15, ikiisha biashara imekwisha lazima ubandue. Ukiona imedemadema mkandarasi alikuwa mzuri, unashukuru Mungu. Leo hii reli ya kati life span yake ilishaisha, ukiona inademadema Mungu ametusaidia. Mimi naomba watu wazungumze kwa data, tuone ni jinsi gani tunatakiwa tutoke hapa, hizi barabara nyingi kushindikana kwake ni kwa sababu hata wakandarasi wetu wengi wamekuwa wachakachuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri leo, kama leo Dangote Mtwara simenti inaweza kuwa shilingi 8,000; kwa nini tusijenge barabara za zege? Kama tunaweza kupasua mawe, tukachukua simenti ya gharama nafuu, mwaga zege barabara toka Mtwara kwenda Songea, kwenda Ruvuma pasua huko kote, una haja gani ya kuhangaika? Kama tuna kiwanda Tanga, jenga barabara ya zege kutoka Handeni njoo mpaka Singida watu watambae huko. Una haja gani ya kuagiza lami Ulaya ambayo tunatoa pesa za nje wakati pesa hizo hatuna? Internal collection yetu, simenti ni yetu, mawe ni yetu, mwaga zege barabarani wakandarasi tunao ili barabara ziweze kupitika kwa muda ambao sisi tumekusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kushukuru na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hatuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kwa asilimia mia moja. Tatizo kubwa la umeme Kiteto ni umeme wa REA katika Kata ya Kijungu, Kata ya Songambele, Kata ya Magungu, Kata ya Dongo na Kata ya Sunya. Kata hizi zote zilikuwa za REA II, sasa tunaomba majibu ni lini Kata hizi zitapatiwa umeme, maana sasa tumeingia REA Awamu ya III haya maeneo yakiwa bado?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kwa kazi anayoifanya kwenye Wizara yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naomba kumshukuru Waziri kwa kunipa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kiteto. Tumekuwa na migogoro mingi kwa muda mrefu Kiteto lakini sasa ameshatupa Baraza la Ardhi, tunakushukuru sana na tunakupongeza sana. Tunakuomba meza na vifaa vingine vya ofisini halafu uje ulifungue lianze kuchapa kazi, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi wamefanya kazi kubwa sana. Mpaka leo Kiteto hali ya amani inayoendelea ni kwa sababu waliweza kupima baadhi ya vijiji, mipaka ikabainishwa na watu wakaweza kuishi kwa amani kwa kipindi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi iliyobaki Kiteto si kubwa sana. Namuomba Waziri aje na wataalam wake atusaidie kupima ardhi yote ili finally migogoro yote iweze kufika mwisho. Wafugaji wapate pa kukaa, wakulima wapate pa kukaa, kila mtu ajue kipande chake cha ardhi, mwisho wa siku itapunguza muingiliano ambao kwa sasa umekuwa unatuletea migongano ya kila wakati. Najua ni gharama kubwa, lakini kwa mazingira na hali iliyojitokeza kiteto tunaomba tupewe priority ili tusirudi huko tulikokwishatoka, hilo ni jambo la tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ile Tume ya Waziri Mkuu ya Askofu Mhagachi, ilifanya kazi Kiteto ikamaliza, ripoti imekaa. Tunaomba mumshauri Waziri Mkuu ile ripoti ije, Waziri Mkuu afike, tumalize ule mgogoro, watu wajue nini kilitokea katika ripoti ile na hatimaye watu waweze kujua wapi wanatakiwa wasimamie na nini kifanyike kwa watu wote na atakayeyasababisha matukio mengine basi aweze kushughulikiwa kulingana na ile document itakavyokuwa inaeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Kiteto kuna NGOs nyingi ambazo zinanitia mashaka. Siku nyingine tutakuja kukuta Tanzania ilishauzwa hatujui na hivi vibali vinatolewa Serikalini. Kwa kweli NGOs ni nyingi, unashtukia NGO imezaliwa asubuhi watu wanafukuzwa asubuhi wanasema ni CBOs, jioni ni WMAs na hifadhi, sasa tumeshindwa kuelewa kipi ni kipi. Watu wameshalima mashamba, wamejenga, ni vijiji asubuhi wanakuambia hii ni hifadhi au ni WMA, hawa watu tutawapeleka wapi? Asubuhi watu wanaanza kushikiana mikuki na mapanga. Haya siyahitaji Kiteto, naomba Waziri aje hizo NGOs nyingine azipunguze, zifutwe na zijulikane zinafanya nini. Kwa sababu NGOs hizi zinafanya chokochoko za chini na ndizo zinazoibua migogoro ya wakulima na wafugaji Kiteto na kupelekea watu kupigana wakaisha. Tunaomba zifanyiwe kazi zile ambazo hazifanyi kazi vizuri zifutwe na zile zinazofanya kazi vizuri basi ziendelee na ziratibiwe kwa nini zinafanya kazi hizo na vyanzo vyao vya mapato vinatoka wapi ili tuweze kujua hawa watu wanakwendaje na wanatoka wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hati miliki za kimila. Tunataka tujue, hizi hati miliki za kimila wananchi wetu wamepewa, wanajua mipaka ya maeneo na ni title, benki haziwakopeshi watu hawa, hazizikubali hizi title. Tunaomba Waziri mwenye dhamana azibane benki zinazokataa hizi title, azidhibiti, iende Serikalini, itungwe sheria, wasipewe vibali vya kufungua matawi mengine kama wanakataa hizi title. Tunahitaji watu wetu wapewe mikopo kutokana na title walizonazo kwa sababu ardhi ni yao, wana hati miliki kwa nini wasipewe mikopo kwa kutumia hizo documents zao kwa sababu wana haki nazo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Waziri amejitahidi katika kunyang‟anya watu ardhi ambao hawaitumii, kutatua migogoro kwenye maeneo mbalimbali, kwa kweli Mheshimiwa Waziri Lukuvi amethubutu lakini naomba niishauri Serikali, Mheshimiwa Lukuvi apewe ulinzi. Akienda na kasi hii Mheshimiwa Lukuvi watampiga mshale, haki ya Mungu, mshale hauna leseni, mshale haulipiwi kodi, anaweza kutembea huko maporini Kiteto na sehemu nyingine ambako watu wana hasira wakampiga mshale kwa sababu anachapa kazi, hongera sana, amethubutu kufanya hayo. Tuombe Mawaziri na viongozi wengine na Wabunge hebu tumuunge mkono Mheshimiwa Lukuvi, tumsaidie kumtatulia migogoro na sisi, kule tuliko na sisi tufanye, tusiwe ni part ya complain. Viongozi wengi wanalalamika sana, tuko kwa wananchi, migogoro mingine inamalizwa na Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto leo iko stable kwa sababu niko pale, hata kama kuna differences zozote zile lazima iwe stable, lazima itulie, wameniamini lazima watii kwa mamlaka na sheria za nchi. Wabunge twende kwa wananchi tukachape kazi, migogoro mingine ni differences tu za makabila, tabaka, uchumi, tumezidiana, amelima pakubwa, amelima padogo, ana ng‟ombe wengi, unakaa chini, mnavuta tumbaku, mnakunywa pombe, msivute ile sigara nyingine kubwa, tatua migogoro ya wananchi kabla haijaenda kwa Waziri, kabla haijaenda kwa Mkuu wa Mkoa, kabla haijaenda huko juu kwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia National Housing. Nashukuru sana kuna mchangiaji mmoja amesema National Housing ina kodi kubwa, ina vitu vingi inavyolipa lakini naomba ni-create awareness, National Housing kuna siku moja inaweza kuanguka, ikashindwa kulipa mikopo. Tuwapongeze wamechapa kazi, lakini naomba ni-create awareness kwa Serikali, Marekani iliwahi kuanguka benki zikatingishika ika-shake mpaka dunia nzima na Afrika tukapata shida. Napenda kuwaambia leo wana-flow ya mikopo mikubwa, wana hizi riba na kodi wanazotakiwa kulipa, nimshukuru Waziri mwenye dhamana alishaona na amewasimamisha kuendelea na development, wajenge hizo walizonazo wakae chini, wa-plan upya kwa maana kwamba watengeneze vision wakijua kabisa kwamba wana mikopo ya kulipa, waone capability yao ya kuilipa bila baadae kuja kuitegemea Serikali na kuwa mzigo. Mheshimiwa Lukuvi naomba ulisimamie hilo na uliangalie sana kwa sababu inaweza kutokea ukawa mzigo kwa Serikali, leo ni safi, kesho shimo. Naomba muangalie sana kwa sababu wana amana za mabenki wanaweza kusababisha yakaanguka, huo ni ushauri mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine naomba nishauri Mheshimiwa Waziri, migogoro mingi ya ardhi imekuwepo lakini tukubaliane kwamba katika maeneo mengi watendaji wa Serikali wanaolipwa mishahara, Maafisa Ardhi wanahamisha beacon. Kiteto watu wamekwisha kwa sababu wali-divert beacons za hifadhi wakasababisha watu kuendelea kugombana. Maeneo ya wakulima yakasogea ndani watu wakaanza kupambana, huyu anasema ni hifadhi huyu anasema ni mashamba, mwisho wa siku watu wakamalizana. Hawa Maafisa Ardhi wako wahuni tunaomba uwaondoe wakae pembeni, ajiri vijana wapya, wako mtaani wana vyeti kwapani, tunaomba uwasaidie hao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nishukuru, nimuombe Mheshimiwa Angeline Mabula, Naibu Waziri, amsaidie Mheshimiwa Lukuvi, kwa kazi namjua akiwa Muleba alikuwa anachapa kazi, kulikuwa na migogoro mingi Kagoma alisimama kidete akaeleza ukweli hadharani wananchi wanakukumbuka sasa chapa kazi kwa Tanzania nzima. Pia kuna Dkt. Yamungu, Katibu Mkuu wa Wizara, ni mchapakazi, chini yake kuna Makamishna tunawapongeza, chapa kazi nchi isonge mbele migogoro ipungue hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushukuru na kuwasilisha, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. EMMANUEL J. PAPIAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nampongeza Waziri mwenye dhamana na Mambo ya Nchi za Nje, Mheshimiwa Mahiga kwa kazi nzuri anayoifanya. Pia nawapongeza Mabalozi wetu kwa kazi nzuri wanazofanya huko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu machache ni ushauri tu. Napenda kushauri Wizara ya Mambo ya Nje wakae na Mifuko ya Jamii. Vile viwanja vyetu vilivyoko nje ambavyo vinahitaji kujengwa wakae na Mifuko ya Jamii wapate pesa wajenge zile nyumba halafu zile pesa wanazolipa kwa maana ya zile nyumba wanazokodi waweze kulipa hiyo Mifuko na kurejesha ili tuweze kuwa na nyumba zetu kwenye Balozi zetu kote duniani ambapo tuna Balozi. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili naomba Mheshimiwa Mahiga ajaribu kuhakikisha kwamba Mabalozi wetu tulionao nje ambao wanatusemea sisi wajitahidi kutafuta nafasi kwa ajili ya vijana wetu watoke nje waende kusoma, kutafuta washirika, misaada, matajiri walioko nje waweze kutu-support kusomesha watoto wetu katika vyuo vikuu vya nje ili waweze kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu nataka kuzungumzia Chuo cha Diplomasia, napenda kushauri Wizara ijitahidi kuona ni namna gani inaweza kufanya training kwa ajili ya viongozi wetu hata wale wa kisiasa ambao tuko humu Bungeni. Watuletee wataalam tuelimishwe tujue namna gani ya kuishi kwenye mazingira haya ya kidiplomasia kwa maana tujue namna gani ku-behave kwenye community nje ya hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine nataka kushauri Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, soko letu la East Africa ni kubwa sana, lakini naomba niseme kuna challenge kubwa sana kwenye East Africa ambayo Tanzania haiendani na nchi nyingine. Ukiangalia kwa mfano Kiwanda cha Maziwa Musoma kilikuwa kinapeleka maziwa Kenya, kilipigwa mizengwe mpaka kikafa lakini leo Kenya ina-import maziwa Tanzania na tunakunywa. Unaweza ku-imagine ni namna gani nchi nyingine ndani ya East Africa zinajaribu kuhakikisha kwamba wawekezaji wao, biashara zao, sisi Tanzania ni market kwao lakini sisi kupeleka kwao inakuwa ni ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo ukipeleka mahindi Kenya lazima upitishe kwa mtu mmoja anunue hayo mahindi hakuna mtu mwingine mpaka yeye anunue. Mkenya akitoka Kenya kuja hapa lazima aingie Kiteto anunue kwa mkulima aende Hanang, Simanjiro, Iringa hakuna control, it means wao wako aware.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Wizara hii ijaribu ku-create watu ambao ni business attaché kwenye hizo embassies, wawe aware, waangalie ni namna gani ya ku-control wale watu wanaokuja lakini na wale watu ambao wako kule ili wananchi wetu waweze kupeleka biashara huko na sisi bidhaa zetu ziuzike huko kama ambavyo bidhaa zao zinavyoweza kuuzika hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa Wizara hii wanafanya lakini liko jambo moja nimejiuliza nikashindwa kupata majibu. Kama miaka miwili iliyopita magari yetu mengi yalikuwa yanapeleka mizigo Congo, Rwanda na Burundi. Leo naomba niwape swali moja jepesi, ukitoka Dar es Salaam kukanyaga Dodoma unakutana na magari ya Rwanda zaidi ya mia, nimejiuliza ni kwa nini? Sisi wakati tunapeleka ile mizigo madereva wetu walikuwa wana kazi, turnboy kazi, magari yetu yanakunywa mafuta hapa, creation ya employment ipo, sasa leo kwa sababu ya kushindwa kukabiliana na uwezo wa kupeleka mizigo, kuleta mizengwe mizengwe hapa katikati tumesababisha na kuwaamsha wale sasa wako kikazi zaidi. Hebu jiulizeni tumepoteza shilingi ngapi kwenye nchi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe na kuwashauri mjaribu kuwa watu wa kukabiliana na hali ya soko, tuko kwenye East Africa, soko linatosha, opportunities zilizopo nyie ndiyo mnatakiwa mtuambie kuna hili, fanyeni hili ili Watanzania wetu waweze ku-benefit kwenye hizi nchi ambazo sisi ni Wanajumuiya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri jambo lingine. Huko nje Mabalozi wetu wanazo kazi lakini kazi kubwa ambayo wanatakiwa kuifanya sasa ni ya ku-market Tanzania kwa maana ya uwekezaji, kwa maana ya kututafutia mashirika makubwa na ku-monitor pesa zao zinakuja kufanya nini hapa. Hawa watu wanaokuja kwa kujipenyeza tutashtukia siku nyingine watu wanaingiza pesa hapa, wananyonya uchumi wetu na hatujui na wanajiita wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, laundry money zitatembea hapa, uchumi na shilingi yetu itashuka, Watanzania tutabaki maskini wenzetu wakichakachua pesa. Niombe Waziri mwenye dhamana na Mabalozi wetu wajaribu kusimamia hili, waliangalie kwa ukaribu na wajitahidi kuhakikisha kwamba nchi yetu haipotezi na sisi tuna-benefit kutokana na hizo nchi ambazo wao wanaziwakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niwashukuru sana, niwaombe kwa jinsi wanavyoweza wajitahidi kufanya kazi hiyo. Watu wanabeza kwamba Tanzania haijafanya kitu, hatuwezi ushirikiano, hatuwezi umoja, hebu angalieni siku ya kukumbuka Uhuru wetu wageni wa kimataifa wanaokuja kushangilia nchi yetu. Hii ni indication kwamba Tanzania ina heshima ndani ya Afrika, ina heshima ndani ya dunia, kubali usikubali Tanzania kuna kitu imefanya katika investment ya umoja na diplomacy ndani ya dunia hii. Niwaombe mnaotubeza na nyie njooni na njia mbadala ya kutuambia tutoke hapa twende vipi badala ya kubeza yale ambayo tumekwishayafanya, hongereni sana kama Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushukuru sana na naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nampongeza Waziri wa Fedha kwa hotuba nzuri ya bajeti ambayo inatupa matumaini ya huko tunakokwenda kwa kipindi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ninalotaka kuzungumzia ni kushukuru kwa bajeti hii kwa sababu hii bajeti itafanya Watanzania waweze kufanya kazi. Naomba na kushauri sana wabane, watafute vyanzo vingine, hata hivi ni kidogo, pesa zishindikane kupatikana Watanzania waanze kufanya kazi kwa sababu hawataki kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona speech ya Rais akizungumza juu ya vijana ambao wanazunguka, watu hawataki kufanya kazi. Naomba Mheshimiwa Waziri Mpango na Naibu Waziri wajitahidi wahangaike kiasi kwamba pesa iwe ngumu ili watu waamke wanatafuta pesa badala ya kufikiri kuangalia runinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msamaha wa kodi kwenye makanisa na mashirika ambayo yanatakiwa kusamehewa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi hiki ni kipindi ambacho watu wengi wamekuwa wana diverge kodi wanakwepa kwa sababu siyo waaminifu kama zamani. Mtu anaweza kuleta kontena nne anasema hii tunajenga kanisa, ni tiles, ni vioo, kontena moja ndio inayofanya kazi, kontena tatu zinapigwa mtaani, halafu mkimaliza mnasema tunakwenda kusali kumbe kodi imepotea. Hiyo usibadilishe yeyote anayesema kodi ilipwe kwanza, watakapomaliza kulipa kodi atakaporejesha zile risiti kwamba hivi vitu vimetumika, basi wewe mrudishie kilicho chake lakini msamaha usiondoe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo na mifugo. Na-declare interest kwamba, mimi ni mkulima na ni mfugaji, si mdogo ni mkubwa. Naomba na kuzidi kusisitiza ili Watanzania watoke kwenye huu umaskini waende kufanya kazi, wafanye kazi kwa bidii watafute maisha ni lazima Benki ya Kilimo iongezewe mtaji ili tuweze kuondoa wale watu wanaosongana mijini, wanashinda vijana wenye vifua wanatembeza nguo za akinamama za elfu mbili mbili. Ili warudi vijijini ni lazima hii benki iweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la matrekta. Hebu tuingizieni matrekta ya kutosha watu wetu wakope waende mashambani maana hawatalima Dar es Salaam. Tusaidieni ruzuku za pembejeo, hakikisha kwamba tunainua mashamba yote ya kilimo ambayo yanaweza kuzalisha mbegu ili mbegu tunayo-import zaidi ya asilimia 80, zaidi ya bilioni kadhaa zinazotoka nje zibaki hapa ndani ili kuwe na creation ya employment na watu wao watafanya kazi mashambani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na kitengo cha kilimo-anga. Zamani tulikuwa na wataalam wazuri wa kilimo-anga ambao ma-pilot wetu ndio wa kwanza East Africa na Central kwa kuendesha ndege za kumwaga madawa, lakini leo hatuna pilots, hatuna ndege, na kesho kutwa mwezi wa tisa Kondoa inaomba chakula cha msaada. Naomba msikie hapa, tukirudi Bungeni Waziri wa chakula ataombwa chakula kupeleka Kondoa, ndege wamemaliza chakula. Niwaombe, kwenye bajeti yao wafikirie kununua ndege ya kilimo, wapelekeni vijana wetu wakasomee kuendesha ndege za kumwaga madawa Uingeza badala ya kukodi wataalam wa kuja kumwaga dawa hapa, huo ndio ushauri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ATC. Tunanunua ndege tunapongeza kwa mpango huo ndege na zije Watanzania wafanye kazi na shirika lifanye kazi. Naomba kushauri tangazeni nafasi ya Chief Executive Officer wa ATC ambaye atasimamia. Atoke nje hatutaki ubabaishaji kwenye hili shirika tena. Madeni yote yanayodaiwa weka pembeni wataendelea kudaiana na Serikali, wataendelea kudai mishahara huko huko shirika lianze upya, akaunti mpya, CO mpya, watendaji wapya, tusonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Mazingira. Nchi ya Tanzania ni chafu sana. Niombe kushauri wametenga pesa kwa ajili ya kupanda miti milioni kadhaa nchi nzima. Kwa nini wasifikirie ni namna gani tunaweza kufuta mifuko ya plastic nchi nzima ili tuokoe kwanza udongo, tuokoe ardhi, tuondoe uchafu, tuokoe magonjwa, tuokoe uhai kabla ya kupanda miti? Maana hizi plastic bag zimesambaa na ni nyingi sana madhara yake ni makubwa hatuwezi kuyaona leo lakini ukiangalia nchi yetu kwa uchafu huu ni mara mia tutumie disposable paper ambayo inaweza kwisha na udongo wetu ukabaki salama, huo ndio ushauri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, CAG tunaomba aongezewe pesa, ndilo jicho letu, ndilo jicho la Mheshimiwa Rais, ndilo jicho la Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndilo jicho la Mheshimiwa Waziri wa Fedha; hiki kitengo kipewe pesa. Lakini naomba kushauri jambo, kumekuwa na mrundikano wa madeni; mara tunaangalia yalienda wapi, yakaenda wapi miaka kumi bado CAG anakagua haviishi vilipanda vilishuka. Hebu mshaurini CAG afute haya matakataka yaliyoliwa huko nyuma, maana yameliwa na Watanzania hawa hawa wamemaliza, ayafute ili hiki kitengo kiweze kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi. Ni kwamba kipunguziwe mzigo wa ku-audit. Ana-audit miaka kumi ishirini iliyopita huku mbele vinaliwa, huku nyuma ameshindwa kuzuia sasa afanye nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu wafute hivi vitu, Mheshimiwa Waziri afute haya matakataka yote haya yaishe tuanze upya mafaili mapya, tukamatane kwa upya, CAG aweze kufanya kazi kwa ukaribu vinginevyo unamfanya ana-audit vitu wiki mbili tatu hawezi ku-cover nchi kumbe ana audit vitu vya 2013, 2012 huko, badala yake tungekuwa tunakwenda mbele ili aweze kukabiliana na uovu ambao umetokea kwa wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo nataka kushauri, hawa auditors wa CAG wangeweza hata kukabiliana na watendaji wetu wahalifu kwa wakati. Sasa otherwise ni kwamba anapokwenda ku-audit anakuta mtumishi alihama aliiba, akapandishwa cheo, akaua zaidi badala ya kuokoa pale. Watu wakamatwe kwa wakati kwa sababu tunahitaji hawa watu tuweze kuwakamata kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA. Tunaomba isaidiwe watumishi wengi wa TRA wanapata vitisho kutokana na walipa kodi, kudai kodi siyo kazi rahisi wamefunga roho. Hawa watumishi wetu wa TRA wasaidieni ili waweze kulindwa na usalama wao, otherwise wanaweza kuyumbishwa na wafanyabiashara na viongozi wanasiasa watendaji, mwisho wa siku wakafanya uhalifu wa kuhujumu nchi bila wao kutaka. Naomba wasaidiwe maana wanakutana na shida nyingi na maamuzi mengine wanayafanya bila wao kutaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, watakapofanya hivyo itatusaidia sisi kujua na kukagua vitu vyetu ambavyo vyote vinawezekana na makusanyo mengi yatakuwa makubwa kiasi kwamba, tutakuwa tumeweza kukusanya kiasi ambacho sisi tulikuwa tunakitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati. Kiteto tumepewa zahanati tatu, sasa wale Wamasai wangu wa kule porini naenda kilomita 150 watakutana lini na dawa? Simangilo zahanati moja watakutana lini na dawa, clinic watakutana nayo wapi, sasa Mheshimiwa Waziri tunaomba hili suala mliangalie…
Mheshimiwa Naibu Spika, muda umekwisha? Yesu wangu! Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. EMMANUEL J. PAPIAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, naunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya na jinsi anavyosukuma gurudumu la maendeleo kwenye nchi yetu. Siku zilizopita kwenye mwaka 2010 - 2015 wenzetu wa Kambi ya Upinzani walikuwa wanasifia sana utendaji wa Kagame. Walikuwa wanasifia sana jinsi anavyochapa kazi na jinsi ambavyo amenyanyua Shirika la Ndege; na ATC yetu imekufa wakiwa wanalaani pamoja na Rais wetu Mstaafu JK. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nashangaa leo, Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amenunua ndege za kutosha, leo anapingwa. Jambo lingine ni kwamba, wakati wanasema anashauriwa na Kagame, wakati anajenga barabara Magufuli akiwa Waziri, swali ni
je, alikuwa anashauriwa na Kagame? Wakati anakamata meli zilizokuwa zinatuibia samaki kwenye bahari kuu, alikuwa anashauriwa na Kagame? Nawaomba, mkikumbuka kudanganya siku nyingine mkumbuke pia namna gani ya kujibu hoja zenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie jambo dogo tu la Utawala Bora. Leo Jimboni kwangu Kiteto siyo salama sana. Siyo salama kwa sababu ya utawala bora tu, ambao tuna-miss watu ambao kwenye sehemu zao hawafanyi ipasavyo. Kiteto kulitokea mauaji na sasa baada ya Waziri Mkuu kutoka juzi tu miezi miwili wameshakufa watu wawili. Mashamba yameshachomwa zaidi ya thelathini. Tuna viongozi; tuna Mkoa, tuna Wilaya, tuna OCD tuna Mahakama na tuna Ofisi ya DC. Kwa nini vitendo hivi vinaendelea?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niambiwe kwa nini vitendo hivi vinaendelea na Serikali haijachukua hatua? Suala hili ni uzembe wa Watendaji wetu. Excuse ndiyo nyingi. Unaambiwa wamekamamatwa ugoni, wameshikana wapi, lakina umma uliteketea. Siku za hivi karibuni, hapa Jimbo la Kibajaji waliuawa wananchi watatu. Kile kijiji watu walitawanywa, walikamatwa, waliwekwa ndani na Serikali ilionesha jitihada zake. Kwa nini Kiteto hizi jitihada hazifanyiki ili mauaji yaweze kukoma? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, Kiteto kuna watu wanafikiri kwamba ile amani ilitengenezwa tu. Hata wakati mauaji yanaendelea, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilikuwepo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ilikuwepo, Watendaji wote wa Serikali walikuwepo. Leo wanatumia camouflage kwamba
wametengeneza. Wakati ule Mbunge alikuwa anaunga mkono hiyo hoja, DC aliyekuwepo alikuwa anaunga mkono, ofisi nzima, ndiyo maana umma uliteketea. Leo amani ipo kwa sababu tumefanya changes za utawala wa pale. Kila anaponyanyuka, nipo. Leo nimetengenezewa zengwe, nashughulikiwa. Nami watakaoshughulikiwa kukamatwa au kuwekwa ndani yawezekana nami nimo. Mimi nitakwenda kama Mandella. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukihisi kwamba naweza kudanganya na kusema uongo, siyo sehemu. Ukihisi kwamba naweza kuulinda uovu, siyo sehemu! Kiteto chama pekee, Kamati ya Siasa ya Wilaya ndiyo iliyookoa na kulaani vitendo viovu na Serikali ilikuwepo. Waziri Mkuu aliunda Tume; tunaomba ile ripoti itoke. Ile ripoti ina mambo mengi ndani yake. Ile ripoti itoke kwa sababu gharama ya Serikali imetumika, lakini kumefanyika heavy investigation juu ya matukio yaliyosababisha ile hali kuwa pale. Inaonesha vitendo vingi ambavyo vimefanywa na baadhi ya Watendaji mle ndani katika ile ripoti. Inaonesha involvement ya wale wanasiasa waliofanya hayo mambo pale ili itusaidie way forward tujue namna gani ya kukabiliana na matatizo yaliyoko pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, Kiteto wanasema imevamiwa sana. Leo wanafukuza watu kule, amani inaanza kupungua. Mtu amekaa miaka 20 au 15, maisha yake yako kule, hajui kwingine kwa kwenda, leo anaambiwa aondoke, anakwenda wapi? Wanasema ni
wavamizi, lakini wanasahau kwamba leo wale tunaowafukuza kule; leo Wilaya yangu nusu ya wafugaji wako Kilindi kwa Mheshimiwa Omari Kigua, naye awafukuze?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapozungumza, Kata yangu ya Dosidosi inayopakana na Kongwa, robo tatu ya wakulima wake wanalima Kongwa wakati ni wananchi wa Kiteto. Leo tuwafukuze? Wana zaidi ya miaka 30. Ukikaa unaulizwa, “ehee, leteni document ya shamba; hili shamba lako ulilipata lini?” Mtu ana miaka 30, ameoa, ana wajukuu analima Kongwa; ni mwananchi wa Dosidosi Wilaya ya Kiteto. Leo tufukuze watu kwa miaka 20 waliyokaa pale; kisa ni nini? Kwa sababu kuna mazingira ya rushwa, kwa sababu kuna ukabila. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo naomba mkubaliane nami, Bunge hili ikitokea kafa mtu Kiteto, namba msimame tuahirishe Bunge tuendelee na mchakato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishakutana na vitu vigumu sana kwenye yale mazingira. Ukiona mgogoro hauishi, jua kuna watu wanachochoea huo mgogoro. Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hoja na napongeza jitihada zako ikiwemo upatikanaji wa dawa katika hospitali zetu. Niombe gari la wagojwa katika tarafa ya Matui ambayo ina population kubwa ya watu. Gari hilo likae kituo cha afya Engusero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba daktari wa Anesthesia katika kituo chetu Engusero ili operations ziweze kuendelea. Pia tunaomba madaktari na ma-nurse, Wilaya ina upungufu wa watumishi hao ikiwemo Daktari wa Kinywa na Meno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ujenzi wa maabara ya Wilaya maana iliyopo ni chumba kidogo Prime Minister alikiona akashangaa na akaniambia nikuambie.

Mheshimiwa Waziri, tunaomba upanuzi wa kituo cha afya cha Sunya maana kinabeba wagonjwa zaidi ya 30,000 tunaomba maabara na upanuzi wa majengo (wodi).

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. EMMANUEL J. PAPIAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza napongeza kazi inayofanywa na Wizara na watalaam wake na pili nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya na jitihada nyingi zote za kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambayo imetengwa hii ya shilingi bilioni 600 ambayo tunalalamika kwamba iende shilingi bilioni 900, mimi ninaona kwamba Wizara imepanga bajeti ambayo ndiyo halisi, kwa sababu hata hii shilingi bilioni 600 yenyewe tukisema leo tuiombe yawezekana hizo fedha zisifike. Fedha ambazo zimetoka ni chini, asilimia 19, ina maana kwamba hata hii tukiiomba yenyewe yawezekana isiwe halisi. Sasa mimi niombe na kushauri kwamba Bunge lako hili likubali tutengeneze ile shilingi 50 iongezeke kwenye mafuta ambayo ndiyo pesa halisi ambayo yawezekana ikawa ni halisi ya kwenda kupeleka kwenye miradi yetu ya maji, angalau ikaongeza Mfuko wa Maji kupata pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji wa wizara wanafanya kazi kwa nguvu kubwa, lakini huku chini kwenye halmashauri zetu watendaji wa Idara za Maji hawafanyi kazi ipasavyo. Idara ya Umwagiliaji Wizarani kuna tatizo la watu kukaimu, watu wengine wamestaafu. Hili suala la umwagiliaji nchini naomba litizamwe kwa kiwango kikubwa, suala la kukaimu linasababisha watu kushindwa kufanya kazi na kufanya maamuzi kwenye maeneo yao. Wale waliostaafu, kama hakuna watu wengine ambao wamewarithi ambao mmekuwa trained na kujua namna ya umwagiliaji nchini basi wale wapewe contract kwa muda wafanye training ya hao wengine ili waweze kusukuma kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa linalofanya nchi yetu ipoteze fedha nyingi ni tathmini ya miradi ya maji kuwa gharama kubwa sana. Mradi mdogo wa shilingi milioni 20 mtu ana tender shilingi milioni 200, hizi fedha zinavyotoka inalazimisha mradi kuwa nusu nusu na haifiki mwisho na mwisho wa siku miradi mingi ya maji nchini inakuwa viporo na haifiki mahali inapotakiwa.

Kwa hiyo tunaomba tulitazame hili, lakini kwenye tendering documents Wizara iangalie, Serikali iangalie ni namna gani tunaweza kwenda kwenye uhalisia unaoweza kufanya miradi hii iweze kukamilika na fedha za Serikali zisiweze kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wafadhili, miradi mingi ambayo inakuwa supported na wafadhili mimi nadhani hawa wafadhili na wenyewe kuna jinsi wanatupiga chenga. Leo wameleta fedha, kesho wameahidi, keshokutwa wame- cancel, miradi haiwezi kuendelea, hii ni danganya toto. Nchi ijitizame upya ni namna gani tunaweza kutokana na haya masuala ya wafadhili, asubuhi amekushika tai, jioni amekuachia tunakuja Bungeni tunaahidi vitu ambavyo haviwezekani. Tujitizame upya tupunguze hili suala la utegemezi wa wafadhili ambao wanatufikisha mahali ambapo sipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kiteto wameniomba niiombe Wizara ya Maji, maeneo ya Ndido, Makame, Loolera tupewe bwawa moja angalau kwenye hii tarafa ili basi wale wafugaji wapate maji. Kanda hii ya maeneo ya hizi kata tatu hawahitaji maji safi na salama, wanahitaji ilimradi ni maji, ukinywa usiharishe, usife, ng’ombe wasife, yawe meupe, yawe meusi, yawe blue wao wanahitaji kitu kinachoweza kuitwa maji na Serikali ikawaambia haya ndiyo maji, kwa sababu wamelia miaka mingi hakuna mabwawa, mifugo inakufa, wananchi hawawezi kupata maji ya kutumia. Maji haya yote sisi tunayatumia kwa maana ya binadamu na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napendekeza na naomba Wizara yako kwamba tupate bwawa moja la maji kwenye tarafa moja kwa mwaka huu, hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunaomba, kuna mabwawa ambayo wananchi wanachimba wenyewe; ukichukua fedha Wizarani, ukaangalia namna gani ya ku- rescue situation kwa haraka, uka-fund wale watu wanaochimba yale mabwawa kwa mikono yao tunaweza
kuwa na mabwawa madogo madogo kwenye maeneo ambayo wakati Serikali haijapanga ile miradi mikubwa basi wananchi wana mabwawa madogo madogo ambayo wanaweza kuwasaidia maji kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nishukuru kwa Bwawa la Dongo ambalo limeingizwa kwenye mpango, lakini niiombe Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's