Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Maria Ndilla Kangoye

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naitwa Maria Ndila Kangoye, ni Mbunge wa Viti Maalum kutokea Mkoa wa Mwanza nikiwakilisha vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuanza kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusimama siku hii ya leo hapa nilipo. Pia nipende kuwashukuru wapigakura wangu ambao ni vijana wa UVCCM Mkoa wa Mwanza pamoja na wanawake wa UWT ngazi ya Taifa kwa kunipa dhamana ya kuwakilisha vijana ndani ya Bunge hili la Kumi na Moja. (Makofi)
Mhehimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya. Nampongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na wasaidizi wake ambao ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Manaibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze katika kuchangia hoja iliyopo. Kwanza, nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kwani hotuba ya Mheshimiwa Waziri imesheheni mambo mazuri yenye kuleta matumaini katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba Kilimo kimeajiri takriban asilimia 70 ya Watanzania na wengi wao wakiwa ni vijana. Hivyo basi, napenda kuungana na Wabunge wenzangu wanaotokana na Kanda ya Ziwa hasa wale walioongelea zao la pamba kwa kusema kwamba ni kweli zao la pamba limeanza kupunguza uthamani wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa pamba wamekuwa wakikatishwa tamaa na changamoto nyingi zinazolikabili zao hili. Baadhi ya changamo hizi ni ukosefu wa masoko ya uhakika, lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa pembejeo hususan mbegu na kumekuwa pia na usambazaji wa mbegu ambazo hazioti. Hii imewakatisha tamaa sana wakulima wa pamba. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, labda kwa kwa kutoa mfano, tatizo hili limewahi kutukumba hata kule Wilayani kwangu Magu, katika vijiji vingi vikiwemo kijiji cha Shishani, Kabila, Mwamanga, Ndagalu na vingine vingi. Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kujikita katika viwanda napenda kuiomba Serikali ifufue viwanda vya nguo ili kuweza kupata soko la ndani kwa wakulima wa pamba. Naamini viwanda hivi vitaweza kutoa ajira kwa vijana, kama Rais wetu alivyoweza kuajiriwa katika Kiwanda cha Mwatex enzi za ujana wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, napenda kuipongeza Serikali kwa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Naamini sasa vijana wengi waliojiajiri katika sekta hii wataweza kupata mikopo ya bei nafuu na kuweza kupanua kilimo chao kulingana na teknolojia ya hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kubwa inayomkabili mkulima wa Kitanzania ni ile ya kutozwa kodi nyingi mpaka mazao yake yanapofika sokoni. Namshukuru Waziri Mkuu, wiki iliyopita amesimama hapa mbele yetu na kutuhakikishia kwamba kodi hizi zitapunguzwa, na mimi ninachoiomba Serikali ni kwamba ianze kutekeleza agizo hilo kwa uharaka ili wakulima waanze kunufaika mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo lingine kubwa. Wakulima hawa wanapofika masokoni, wanakutana na madalali. Madalali hawa wamekuwa kama miungu watu ndani ya masoko haya. Wao ndio wapangaji wa bei na wamekuwa wakitengeneza mazingira ya kukabidhiwa mazao haya; wao ndio wanaouza, ndio wanaopokea pesa na mara nyingi wamekuwa wakiwatapeli wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali kuweza kuanzisha chombo maalum ambacho kitakuwa chini ya Halmashauri za Wilaya ambacho kitawatambua hawa madalali na ikiwezekana na wao walipishwe kodi kwa sababu hata hiyo pesa wanayopata haina jasho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Ziwa hususan Mkoa wa Mwanza ni maarufu kwa ufugaji, lakini kumekuwa na uhaba wa viwanda vya kusindika nyama, maziwa na kuchakata ngozi. Naiomba Serikali itoe kipaumbele kwa kuanzisha viwanda hivi ili kuweza kunufaisha jamii ya ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ifike mahali tuachane na kusafirisha mifugo, ila tujikite katika usindikaji wa nyama, maziwa na usafirishaji wa ngozi ambazo tayari zimekuwa processed. Hili ni suala ambalo linawezekana na nina uhakika kwa Serikali hii inawezekana kabisa. Labda kwa kutoa tu mfano, kuna Ranchi ya Kongwa hapa ya NARCO, imekuwa ikisafirisha nyama kutoka kwenye ranchi yake kwenda sehemu mbalimbali, hata kwenye maduka ya kuuza nyama (butcheries)yaliyoko Dar es Salaam.
Sasa ikiwa suala kama hili tayari lilishaanzishwa tena na vyombo vya Serikali, je, inashindakana vipi kuweka mlologo mzuri ili nyama ya ng‟ombe inayotoka Mwanza iweze kufika Dar es Salaam ikiwa fresh na kuwafikia walengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuhitimisha mchango wangu kwa kuiomba Serikali kuiangalia Wilaya ya Ukerewe kwa jicho la pekee. Ukerewe ina visiwa 38; kati ya hivyo, 15 ndivyo vyenye makazi ya kudumu na 23 ni makambi ya wavuvi; na wavuvi wengi ni vijana. Nasikitika kusema kwamba vijana hawa ambao ni wavuvi wamekuwa wakihangaika kutafuta masoko mbali na Ukerewe, ukizingatia kwamba viwanda vya samaki vipo Musoma na Mwanza. Vilevile tukiangalia hali ya usafiri wanaotumia siyo usafiri wa uhakika, yaani usafiri ule siyo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tumekuwa tukiwaokota pembezoni mwa ziwa na hii kwa kweli…
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Nianze kwa kumpongeza Waziri pamoja na Naibu wake kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini kwa Watanzania, lakini niwapongeze sana kwa kazi nzuri waliyokuwa wanafanya kwani haifichiki. Tumeona ujenzi na ukarabati wa hospitali zetu za rufaa lakini tumeshuhudia pia uanzishwaji wa hospitali maalum ya Benjamin Mkapa Ultra Modern Hospital iliyopo hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, napenda kuikumbusha Serikali kwamba bado haijafikia lengo lililowekwa miaka 15 iliyopita ndani ya Azimio la Abuja linaloitaka Serikali kutenga asilimia 15 ya bajeti yake ya Taifa kwa ajili ya afya. Hapa ninavyoongea sasa Wizara hii imetengewa bajeti chini ya asilimia kumi ya bajeti ya Taifa. Napenda kuiomba Serikali iweze kufikiria upya suala hili na kurejea katika msimamo wa makubaliano hayo na kuwezesha Sekta hii ya Afya kufanya vizuri kwani tutakapowezesha sekta hii tutawezesha pia sekta nyingine kuweza kukua na kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoani Mwanza zipo changamoto nyingi ambazo zinaikabili sekta hii ya afya. Changamoto hizi tayari zimeshatajwa na Wabunge wenzangu lakini na mimi nitaweka msisitizo japo kwa ufupi. Kuna changamoto ya ucheleweshaji wa dawa kutoka MSD; kumekuwa na wafanyakazi wachache katika sekta hii ya afya; kumekuwa na ucheleweshwaji wa mishahara ya wafanyakazi; kumekuwa na ukosefu wa maduka ya dawa katika hospitali zetu za wilaya na lipo tatizo ambalo limekuwa likisumbua sana la ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa wagonjwa wa wilaya zote za Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Magu ina magari manne ya wagonjwa lakini katika magari manne ni gari moja tu la kituo cha Lugehe ndilo linalofanya kazi, mengine matatu yote ni mabovu na magari haya yamekuwa yakikarabatiwa mara kwa mara bila mafanikio. Kwa kuwa pia Wilaya ya Magu haina mapato ya kutosha, magari haya yamesababisha deni la shilingi milioni 38 kwa ajili ya service zilizokuwa zinafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ilani ya Chama changu cha Mapinduzi iliahidi kwamba, itaboresha mazingira ya wafanyakazi wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta hii ya afya, napenda kuikumbusha Serikali kwamba ni wajibu wake sasa kutekeleza Ilani hiyo kwa kuweza kutatua changamoto hizi ili wafanyakazi waweze kufanya kazi katika mazingira yanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Sengerema nayo inahitaji ruzuku stahili. Mheshimiwa Ngeleja amesimama mara kwa mara na kuhamasisha suala hili na kuiomba sana Wizara na napenda kuungana naye katika vita hii. Hospitali ya Wilaya ya Sengerema inapata ruzuku ya vitanda 150 tu wakati hospitali hiyo ina vitanda zaidi ya 370 na inategemewa na wakazi wengi wanaoishi ndani ya Jimbo hilo la Sengerema. Ombi hili tayari lipo Wizarani na ni matumaini yetu kwamba Wizara itatupatia jibu zuri ambalo litatuletea matumaini kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimebahatika kuzunguka katika baadhi ya shule za msingi na sekondari ndani ya Mkoa wa Mwanza nikiwa na wanaharakati wanaotoa elimu ya afya ya uzazi. Kwa fursa hiyo ya muda mfupi, nimegundua kwamba ipo haja ya Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wa jinsia ya kike wanapata taulo za kujisitiri ili kupunguza changamoto kubwa ya wanafunzi hawa kutokuhudhuria masomo wakiwa kwenye siku zao. Kwa sababu tayari Serikali inatoa vitabu na madawati mashuleni, naomba suala hili pia liweze kupewa kipaumbele ili kuweza kunusuru wasichana hawa kukosa masomo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri wapo vijana wa Mwanza ambao wamejitolea kufanya utafiti na wakatengeza washable sanitary towels yaani pedi ambazo zinaweza kufuliwa na kutumiwa zaidi ya mara moja kwa muda mrefu. Naomba Serikali iwasaidie vijana hawa ili bidhaa zao ziweze kuthibitishwa na TBS na endapo zitatufaa bidhaa hizi ziweze kununuliwa na Selikali na kusambazwa katika shule mbalimbali hasa zile zilizopo vijijini. Napenda kumwomba Waziri wa Afya anipokee nitakapowaleta vijana hawa ofisini kwake kwani ni fahari kwa Tanzania kuwa na vijana wabunifu tena wenye kujituma kwa niaba ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Wizara hii kwa hotuba nzuri iliyojieleza vizuri kwa maslahi ya Watanzania kwa ujumla, pamoja na yote naomba Serikali iweke makazi katika suala lifuatalo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana hasa katika maeneo yanayozunguka migodi yetu. Suala hili limesababisha mauaji ya vijana hawa wanaparamia migodi kuweza kupata chochote kama tunavyosikia mara kwa mara kwenye mgodi wa Nyamongo, Mkoani Mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali yangu sikivu, Serikali inayotekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi inayoahidi kupanua wigo wa ajira kwa vijana, iweke mikakati maalum ya kuhakikisha kwamba, migodi mikubwa kama Nyamongo inauza mchanga ambao hauhitajiki na mgodi kwa wananchi ili nao waende kusafisha na kupata japo kidogo katika rasilimali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini suala hili linawezekana na naamini kwamba, Serikali hii, haitashindwa kuweka utaratibu huu wa wananchi kupata mchanga huo kutoka migodini.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu asubuhi hii ya leo, nikushukuru wewe pia kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Naibu wake Dkt. Angelina Mabula kwa kazi nzuri wanayofanya, niwape pole kwa changamoto nyingi wanazokumbana nazo ndani ya Wizara hii, kwani zipo nyingi zikiwemo zile za migogoro ya ardhi ambazo zimekuwa ni za muda mrefu na zenye kuhitaji hekima na busara katika kuzitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa gender sensitivity nipende kumshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kumteua mwanamama Dkt. Angelina Mabula kuwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Baada ya salamu hizi naomba nijielekeze katika kuchangia hotuba iliyoko mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina hekta milioni 88.6 za nchi kavu na kati ya hizo ni hekta milioni 60 ambazo ni mbuga na zina uwezo wa ku-accommodate ufugaji. Pamoja na kuwa na eneo kubwa la kututosheleza bado kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na migogoro hii imekuwa ikisababisha ulemavu vifo, upotevu wa mali lakini hata wananchi kuhama makazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua jitihada ya Wizara hii katika kutatua migogoro hii lakini naiomba Serikali ikae itafakari, itafute mbinu mbadala na rafiki kutatua matatizo haya. Hata pale inapowezekana ishirikishe wazee wa kimila katika kuwashawishi wakulima na wafugaji kutumia maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli zao. Niishauri Serikali kutengeneza mifumo ya kuzuia kuliko kutengeneza mifumo ya kupambana baada ya matatizo haya kufumuka. Kubwa zaidi niishauri Serikali kuhakikisha inafanya utafiti ili iweze kujua vyanzo halisi vya migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaisihi Serikali kuona haja ya kutambua ufugaji wa asili katika Sera ya Taifa ya Ufugaji ya mwaka 2006, kwani ufugaji huu umekuwa ukichangia asilimia 7.4 ya Pato la Taifa. Kikubwa ni kutengeneza mfumo madhubuti kuhakikisha kwamba ufugaji huu haugeuki kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Sheria ya Ardhi kumekuwa na changamoto kubwa ya wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha wa sheria hiyo, kumekuwa na tafiti nyingi ambazo zimebainisha kwamba wananchi wanaoishi katika ngazi za msingi hususani vijijini wakiwemo wanawake, wakiwemo wafugaji, wachimbaji wadogo na wakulima wamekuwa wakikosa haki katika kumiliki ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi zipo mila ambazo zinamkandamiza mwanamke katika kumiliki ardhi, mila hizi zimekuwa zikimwaminisha mwanamke kwamba yeye ni wa kuolewa na kusubiri kurithi ardhi kutoka kwa mume wake. Hii tumeona changamoto yake kwamba, yapo baadhi ya makabila yanasadikika kwamba wanawake wao wanawaua waume zao ili waweze kurithi mali. Hii imekuwa ikiwanyima wanawake haki ya kupata, kutumia na kudhibiti ardhi moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iweke mpango mkakati wa kutoa elimu ya Sheria hii ya Ardhi katika ngazi ya vijiji ili wananchi waweze kujua haki zao katika kumiliki ardhi. Kama Sheria ya Ardhi Na. 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 za mwaka 1999 zinavyoainisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wawekezaji na ardhi; kumekuwa na tatizo la wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi na baadhi yao wamekuwa wakitumia sehemu ndogo tu ardhi hiyo, wapo ambao hawajaendeleza kabisa maeneo hayo na kusababisha mapori katikati ya vijiji na mara nyingi mapori haya yamekuwa yakitumika na wahalifu kama maeneo ya kujifichia. Vijana wa Kitanzania wana uhitaji mkubwa wa ardhi ili kuweza kufanya shughuli za kiuchumi, tukumbuke kwamba vijana hawa wa Kitanzania wamelelewa katika mila na desturi za Kiafrika ambapo mali zote ikiwemo ardhi ni za baba, hata pale wanapojitahidi kwenda shule na kuhitimu vyuo vikuu bado wanakuwa hawana fursa kubwa ya kupata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Wizara hii isitengeneze utaratibu wa kuwagawia maeneo ya ardhi vijana ili nao waweze ku-contribute katika uchumi wa nchi yetu. Kwa kufanya hivi tutakuwa tumepunguza tatizo ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara la wananchi kuvamia maeneo kama haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa kumiliki ardhi, kumekuwa na mlolongo mrefu katika umilikishaji wa ardhi, aidha kwa kupata cheti cha hakimiliki ya kimila ama kwa kupata hati. Hii imesababisha wawekezaji kukosa uvumilivu na kukimbilia katika nchi ambazo zina unafuu katika kumilikisha ardhi. Mlolongo huu mrefu umesababisha Watanzania kuwa wavivu wa kumiliki ardhi kihalali na kwa namna moja au nyingine tumekuwa tukiikosesha Serikali yetu mapato yanayotokana na ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 37(a) inasisitiza kuimarisha utoaji wa huduma za ardhi. Napenda kuiomba Serikali hii iweze kutekeleza Ilani hiyo ili kuweza kumsaidia Mtanzania kuweza kumiliki ardhi ndani ya muda mfupi. Hili linawezekana kama tu tukiziwezesha Halmashauri zetu za Wilaya kuajiri vijana wa kutosha na Wizara ijikite zaidi katika kampeni nyingi zikiwemo zile za upimaji wa ardhi kuanzia ngazi za Vijiji mpaka za Miji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijahitimisha napenda kuikumbusha Serikali kwamba ilikuja Wilayani kwetu Magu Jimbo la Mheshimiwa Kiswaga ikaomba eneo kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wananchi. Napenda kuwataarifu kwamba eneo hilo tayari lipo tunawasubiri tu ninyi mje muwekeze ili wananchi wetu waweze kunufaika kwa kupata nyumba bora kwa bei nafuu. Hata Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu tayari wameshawatengea eneo, tena eneo lipo halihitaji hata fidia ni kazi kwenu kuja kujenga nyumba hizo ili wananchi waweze kupata nyumba bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha, napenda kuungana na wenzangu wote kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa ya kuchangia kwa maandishi. Napenda kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri, lakini pamoja na yote, napenda kuwataarifu Waziri na Naibu wake kwamba kwa haraka haraka inaonekana watendaji wa Wizara hii wanafanya kazi kwa mazoea na ni wakati sasa wa watendaji hawa kusimamia Katiba ya nchi pamoja na Sera Taifa zinazoigusa Wizara hii ikiwemo Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Wizara hii kuhakikisha kwamba utalii wa nchi yetu unaimarika kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo ile ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona nchi nyingine zikijitangaza kuwa na baadhi ya vivutio vilivyopo ndani ya nchi yetu kama come to Kenya and see Mount Kilimanjaro. Hili ni suala la kusikitisha sana pale nchi yetu inaposhindwa kukemea masuala haya kupitia Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashangaa kwa umri wangu sikuwahi kusikia kitu chochote kuhusu mjusi wa aina ya dinosaur aliyewahi kupatikana hapa nchini Tanzania Mkoa wa Lindi na kupelekwa Ujerumani. Nimekuwa na maswali mengi juu ya hili. Nimekuwa nikijiuliza ni kiasi gani cha fedha Ujerumani inaingiza kupitia huyu mjusi? Katika hizo fedha ni kiasi gani kinaletwa Tanzania na ni kiasi gani kinapelekwa Lindi kwa ajili ya maendeleo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana kuona hata mashuleni hili halitajwi popote na kibaya zaidi hata huko Ujerumani hatuna uhakika kama hawa wanataja mnyama huyo katokea Tanzania na kibaya zaidi historia ya mjusi huyu haijulikani na ipo mbioni kupotea kabisa tukizingatia uwepo wa kizazi hiki na kijacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara husika kutueleza ni shilingi ngapi tunaingiza kama nchi kutokana na mjusi huyu na ni jinsi gani tunafaidi kwa yeye kuwepo huko Ujerumani? Ninaisihi Serikali kumrudisha mjusi huyu nchini ili tuongeze kipato cha Serikali kupitia utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Wizara hii kuwapeleka Madiwani wa sehemu husika alipopatikana mjusi huyu na baadhi ya Wabunge wakiwemo wanaotoka Lindi kwenda kumuona mjusi huyu ili waje watuhakikishie uhai wake, lakini kikubwa zaidi tupate taarifa ya kujiridhisha juu ya kipato anachoingiza nchini humo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia napenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya chini ya Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wengi wana imani kubwa na Serikali hii ya Awamu ya Tano, lakini Watanzania wengi pia wana matumaini makubwa sana na bajeti ya kwanza ya Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupongeze wewe pia kwa ujasiri ulionao. Nikuhakikishie kwamba Watanzania wote wanaona ni jinsi gani unavyokitendea haki Kiti hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika kuchangia hoja iliyopo mezani nikianza na sekta ya elimu. Kumekuwa na changamoto kubwa katika ugawaji wa fedha inayotengwa kwa ajili ya elimu. Mara nyingi tumekuwa tukiona kwamba fedha nyingi zimeelekezwa katika matumizi ya kawaida huku maendeleo ya elimu yakipata pesa ndogo na wakati tunajua kwamba maendeleo yamekuwa na changamoto kubwa na nyingi kama za ukosefu wa madawati, madarasa, vyoo, nyumba za Walimu, mabweni na maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata tukirejea katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, tunaona kwamba asilimia 84 ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya elimu ilielekezwa katika matumizi ya kawaida huku asilimia 16 tu ikielekezwa katika fungu la maendeleo ambapo nusu yake ilielekezwa katika mikopo ya elimu ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii imeathiri sana elimu katika shule zetu za sekondari, primary lakini na vyuo vyetu vya VETA ambapo vimeshindwa hata kukidhi haja ya kuwa na teknolojia ya kisasa. Kwa mfano, mwanafunzi anayejifunza ushonaji katika Chuo cha VETA anatumia cherehani ya kawaida yaani ile ya kutumia miguu na mara nyingi wanafunzi hawa wamekuwa wakitamani kuajiriwa katika viwanda vikubwa let me say kama A to Z cha kule Arusha ambacho kina teknolojia ya kisasa na mashine zake ni za umeme. Ina maana tunawapa mzigo hawa wawekezaji kwa kuanza kuwa-train upya hawa wanafunzi kwa muda mrefu mpaka hapo watakapoanza kufikia ile quality ya ku-produce kile kinachohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali katika ugawaji wa fungu la sekta katika mwaka wa fedha ujao itenge fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo ya elimu. Kwa kufanya hivi, maendeleo yetu yatasonge mbele, lakini pia tutapata nafasi kubwa ya kupata picha ya matumizi ya fedha ya maendeleo ya sekta ya elimu. Kama inawezekana hili fungu la mikopo ya elimu ya juu litolewe katika fungu la maendeleo lihamishiwe katika fungu la matumizi ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika kuchangia masuala yanayohusu Mkoa wangu wa Mwanza. Nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kututengea fedha kwa ajili ya meli mpya katika Ziwa Viktoria lakini nishukuru pia Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa daraja litakalounganisha Kigongo na Busisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, napenda kutanguliza salamu zangu za masikitiko makubwa kwa Serikali juu ya Mkoa wa Mwanza kuwa mkoa unaoongoza kwa umaskini, kwa kweli ni suala la kushangaza sana na ukizingatia ripoti kutoka BOT inaonesha kwamba Mkoa wa Mwanza ni wa pili katika kuchangia mapato kwa Serikali. Je, hii inamaanisha kwamba Serikali haithamini watu wa Mkoa wa Mwanza? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwa kukutaarifu tu ni kwamba watu wa Mwanza ni watafutaji wazuri tu na wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji kule Sengerema na Misungwi, utalii pale Saa Nane Island, ukienda Magu utakutana na museum kubwa ya kabila la Wasukuma lakini ukienda Ukerewe pia utakutana na mawe yanayocheza. Nikuhakikishie kwamba shughuli zote hizi zimekuwa zikichangia mapato kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina nia nzuri na Mkoa wa Mwanza, narudia kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina nzuri na Mkoa wa Mwanza naiomba katika mwaka wa fedha ujao itenge fedha ya kutosha kwa ajili ya miradi ambayo tayari imekwishaainishwa ndani ya mkoa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna miradi ambayo tayari ilikwishaanzishwa ila haijakamilika na mara nyingi tumekuwa tukipata majibu ya danadana. Naiomba Serikali iweze kuikamilisha miradi hii ili watu wa Mwanza waweze kunufaika na matunda ya michango yao katika pato la Taifa. Miradi hiyo ni kama ule wa maji wa Sengerema, Ukerewe, Misungwi na Magu pale Kisesa na Bujora na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa na miradi mingine ya umeme ambayo bado haijakamilika mpaka hivi sasa. Ipo pia miradi ya barabara ambayo imekuwa ikiongelewa mara kwa mara kama mradi wa barabara ya kutoka Kamanga - Sengerema ambao pia upo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi na mradi wa barabara kutoka Kisesa - Usagara na barabara nyingine nyingi ndani ya mkoa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali imeweza kutoa maji Ziwa Viktoria ikayapeleka Shinyanga iweje leo mtuaminishe watu wa Mwanza kwamba Serikali imeshindwa kutoa maji Ziwa Viktoria kuyapeleka Sumve, Magu ama Sengerema, kwa kweli suala hili linatuweka katika hali ya sintofahamu. Serikali inaposema kwamba ina mradi wa maji vijijini imaanishe siyo tusikie kwamba miradi hii inapelekwa mijini kama ilivyokuwa huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina maji mengi sana, tukiachana na maji yaliyopo kwenye maziwa, mito na bahari yapo maji yanayotokana na mvua ambayo mara nyingi yamekuwa yakisababisha maafa ya mafuriko katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Serikali kuanza kufikiria kujikita katika miradi ya kuhifadhi maji katika mabwawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na matumizi mengine. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Serikali kukubaliana na wazo la Kamati ya Bajeti la kuongeza Sh. 50 katika tozo ya mafuta ili tuweze kuiwezesha sekta hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya kilimo tunafahamu kwamba asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima na wengi wao wakiwa ni vijana na wanawake. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa dhamira yake ya kupunguza ama kuondoa kabisa ushuru mbalimbali katika mazao ya kilimo. Nimesoma hotuba iliyopo mezani inaonesha kwamba sekta ya kilimo imetengewa shilingi trilioni 1.56 ambayo ni sawasawa na asilimia 4.9 tu ya bajeti ya Serikali tukitoa deni la Taifa. Napenda kuishauri Serikali kuongeza fedha hii kwani haiendani na watu wanaotegemea kilimo. Kwa sababu Serikali…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's