Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri

All Contributions

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Naomba nitangulize shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kuweza kusimama hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutimiza ahadi yake. Alisema kipindi cha kampeni, yeye akiahidi anatekeleza. Kwa Wana-Dodoma ametuletea Makao Makuu na kweli Serikali imeshahamia. Kipindi cha kampeni wananchi waliilalamikia CDA kwamba amethubutu, ameivunja mamlaka ya ustawishaji. Sisi tunamwambia tuko naye bega kwa bega, tunasema uungwana ni vitendo asubirie 2020, Dodoma tuko naye pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyongeza tu ni kwamba Serikali tunaomba sasa muda muafaka umefika wa kuleta muswada wa Sheria ya Makao Makuu. Leo hii tunajadili Wizara nyeti, tunajadili maisha robo tatu ya Watanzania. Kwa mujibu wa hotuba yako Mheshimiwa Waziri, umesema kwamba sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, imeajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania.

Waheshimiwa Wabunge, everybody is entitled to his/ her opinion, lakini lazima tuseme ukweli. Wao wanaosema tumeganda wakati Sudan inategemea chakula kutoka Tanzania, Kenya wanategemea mahindi kutoka Tanzania, Uganda wanategemea mahindi kutoka Tanzania na mazao mengine! India wanategemea chorosho, choroko, dengu, mbaazi zote zinatoka Tanzania. La msingi ni kwamba tunatakiwa tuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii naomba niwaambie, Waziri wa Fedha na Naibu Waziri, naomba mnisikilize. Mipango yenu ni kwamba tunataka kupeleka nchi kwenye uchumi wa viwanda, tunataka kuwa na uchumi wa kati, tuwekeze kwenye kilimo, mifugo na uvuvi. Kilimo, mifugo na uvuvi ni afya, kilimo, mifugo na uvuvi ni ajira, itampunguzia kaka yangu Antony Mavunde adha aliyokuwa nayo. Kilimo, mifugo na uvuvi ni fedha na uchumi, kilimo, mifugo na uvuvi ni amani. Tukiwa na njaa tutaweza kuwa na amani?

Kwa hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, ukipeleka hela kwenye kilimo, mambo yako yote, mpango wa maendeleo utafanikiwa kwa asilimia 200. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi, lawama nyingi sana zimemwendea Mheshimiwa Waziri. Namfahamu Mheshimiwa Waziri. Nimeshalima naye, ni mkulima mzuri sana. Tena bahati nzuri analimia hapa hapa katika Mkoa wetu wa Dodoma. Mheshimiwa Waziri amekua kama mtoto wa mfugaji, kazaliwa kwenye jamii ya ufugaji, anatoka Kanda ya Ziwa, anaelewa uvuvi. Ukikaa na Mheshimiwa Waziri, maono aliyokuwanayo kwa Wizara yake ni makubwa, lakini hana fedha, atafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze umuhimu wa utafiti, sayansi na teknolojia katika kilimo. Kwa Kiingereza tunasema, science and technology innovation in agriculture. Tunasikitika, bajeti ya ugani iko wapi? Bajeti ya utafiti ikoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu chote, leo hii nchi yetu ina watu takriban milioni 50, baada ya miaka 10 tutakuwa na watu zaidi ya milioni 65. Hakuna mpango mkakati wa kutuvusha kutupeleka huko na yote Mheshimiwa Waziri siyo kosa lake; huna utafiti, uta-project vipi? Utapangaje mipango yako vizuri kama hujafanya utafiti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote, niwaambieni, dunia nzima kati ya watafiti wanaoheshimika ni Tanzania. Kigoma Watanzania walifanya utafiti wa mbegu ya michikichi ambayo Malyasia ndio wanatumia. Leo hii niwaambieni, kuna Mtanzania mmoja alikuwa Serikalini, amefyatuliwa risasi juu, amechukuliwa na Bill Gates Foundation Marekani kama mtafiti na aliombwa abaki kule afundishe masomo ya kilimo, lakini amechukua uzalendo wake, amerudi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa utafiti naomba niwaambieni Serikali, leo hii mjiulize kwenye uvuvi, Ziwa Victoria sisi ndio wenye sehemu kubwa, lakini ukienda kwenye statistics za dunia, Uganda imetupita, yenyewe ni ya sita katika uvuvi wa Ziwa Victoria. Sisi ni wa nane, kwa nini? Leo hii tujiulize Bukoba kahawa mwaka 1978, miaka 30 na kitu iliyopita walikuwa wanazalisha zaidi ya tani 140,000, lakini leo kwenye kitabu mmeona, tuna-project kuvuna tani 47,000 kwa sababu hatujafanya tafiti ya kuendeleza hizi kahawa. Miche imekuwa mikuu, haizalishi, imekuwa dormant. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu niwaeleze umuhimu wa science and technology innovation. Leo hii tunafurahi hapa kusema kwamba tunalisha East and Central Africa, lakini tusipojipanga vizuri, tunu hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu tutaikosa, Malawi wamejipanga kwenye pamba. Malawi ni nchi ndogo, lakini leo hii inaenda kutupita kwenye uzalishaji wa pamba kwa sababu ya tafiti na kujipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuongelea suala la mbegu. Tumejaribu sana kuendeleza kilimo. Nashukuru Serikali ilijaribu kutoa matrekta, lakini hebu tuweke azimio, Mheshimiwa Waziri, kaa chini. Vituo unavyo, mahitaji unayajua, sitaki kuzungumzia sana yaliyokuwemo humu. Hebu tusonge mbele, tuwafunge watu midogo. Tuweke azimio kwamba Serikali ihakikishe kila mkulima anapata mbegu bora. Wakulima wetu wamekuwa wanatumia nafaka. Nendeni mkasome muone tofauti ya mbegu na nafaka (seed and grain). Mkulima analima heka yake moja, akivuna mahindi, yale yale aliyoyavuna, anahifadhi anaifanya mbegu. Siyo mbegu! Atajikuta alivuna mawili atabaki na moja. Kwa hiyo, tuweke azimio, uwezo huo tunao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba kuzungumzia Mkoa wangu wa Dodoma. Mkoa wa Dodoma unafanya tremendous kwenye kilimo, ingawa watu wanajua kwamba ni kame. Msimu wa mwaka 2013/2014 Tanzania iliuza tani 860,000 China, kati ya hizo tani 300,000 ufuta umetokea hapa Dodoma. Tuna maonyesho ya Nane Nane. Pale inaonekana mazao yote yanawezekana. Kwani ile ardhi ya Nane Nane ni ya wapi? Ni Arusha? Siyo ya Dodoma! Lakini humu sijaona Mheshimiwa Waziri. Nina vijana wengi na kila siku nawapigia kelele waingie kwenye kilimo. Hebu tuhamishe basi ile Nane Nane tuipeleke Chamwino, tuipeleke Kondoa, tuipeleke Chubi. (Makofi)

Mheshimiwa Ally Saleh kauliza kuhusu shamba kubwa, twende Chubi kwa Mheshimiwa Kijaji ukaone shamba kubwa za hizo heka unazosema na mwekezaji ujifunze. Tembea, no research, no right to speak. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongea kwa sababu niko field, najua raha ya kilimo, najua machungu ya kilimo, najua mafanikio na ninajua tukiweka nguvu kidogo, tutafika mbali. Nataka sana vijana. Vijana wanataka red market, wanataka mitaji, hatuna sehemu ya kuwapeleka zaidi ya kilimo. Tuwekeze jamani! Leo hii haiwezekani, nchi ya Egypt ina River Nile peke yake. Source ya River Nile ni Lake Victoria. Kale ka-Nile kanatokana na Lake Victoria wanakatumia, wanafanikiwa vibaya mno! Sisi wenye Ziwa Victoria, wenye Ruvu na mito kibao hatuongei, kwa nini tunashindwa kutumia hizi fursa? Tumeona mwenyewe Mheshimiwa Waziri umeshasema hii ndiyo sekta ambayo inaleta pesa kuliko zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie kwenye uvuvi katika Ziwa Victoria, kuna samaki anaitwa sangara. Sangara jamani…(Makofi)

(Hapa kengele ililie kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma mwenye kurehemu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kukushukuru wewe, Mheshimiwa mtani wangu, maana niliona mbona napitwa, muda unazidi kwenda na mimi sipati nafasi. Napenda ni-declare interest, mimi ni mkulima. Tumezoea kusikia mtoto wa mkulima, mtoto wa mfugaji, mimi ni mtoto wa kishua, lakini ni mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwa kusema, naipongeza Tanzania, napongeza Serikali zote za Chama cha Mapinduzi kuanzia Awamu ya Kwanza, ya Pili, ya Tatu, ya Nne na hii ya Tano.
Waheshimiwa Wabunge wenzangu, huu mchezo hauhitaji hasira na msema ukweli mpenzi wa Mungu. Kama wewe unasema tupo nyuma, India wanatambua korosho bora inapatikana Tanzania, dunia inatambua mwaka 2015 kwa mujibu wa FAO kati ya nchi 10 duniani zinazoongoza kwa kuzalisha ndizi, Tanzania imo. Pamoja na yote, tumo kwenye ramani. Serikali zetu zimekuwa zikihangaika na kilimo na zinazidi kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, ametuletea wahusika ambao watatuvusha. Nina uhakika kipindi hiki cha 2015 na ninamwomba Mheshimiwa Rais, hii timu wasiibadilishe mpaka tufike 2025; Mheshimiwa Mwigulu na mwenzake watatuvusha mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ya kuyaboresha ili tufike mbali. Cha kwanza ni sera, kwa sababu kuna vitu tunashangaa tu. Leo hii haiwezekani mbegu inayozalishwa hapa nchini iwe inatozwa ushuru mkubwa kuliko mbegu inayoagizwa kutoka nje. Kwa sababu wataalam wanasema, mbegu inatakiwa ifanyiwe tafiti mahali husika. Kuna factors nyingi za hali ya hewa na aina ya udongo uliopo. Kwa hiyo, tukibadilisha hizi sera zetu, namwomba Mheshimiwa Waziri akae chini apitie sera zilizopo, je, zinaendena na wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi zitamsaidia yeye maana kuna watu wameshaanza kumtisha, na mimi nikakumbuka, ametaja baadhi ya Mawaziri ambao walipitia Wizara yako leo hii hawajarudi, nikakumbuka na baba yangu mdogo yumo kipenzi changu Mheshimiwa Adam Malima, na yeye alipita huko hajarudi, lakini nasema kwamba Mheshimiwa Mwigulu utaiweza na itakufikisha sehemu ambapo wewe unapaota, angalia hizi sera! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja limechangiwa sana na watu hapa, mimi ni mwana maendeleo, ni kijana, ninalinda interest ya kundi kubwa ambalo lina-constitute hii nchi. Kuna watu mnawasema vibaya, jamani wafanyabiashara wamo humu, kuna biashara ambayo haina channel of distribution? Kwenye biashara lazima una producer, una mtu wa katikati ambaye anapeleka kwa final consumer. Kwa nini kwenye kilimo huyu mtu wa kati anapigwa sana vita? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba ridhaa kwa Wana-Dodoma hususan vijana kuja kuwawakilisha, mimi mkisema hivyo mnaniumiza. Nina vijana wengi sana ambao wanafanya biashara za mazao na naomba kuwasemea, wanafanya kazi kubwa kuisaidia Serikali kuendesha kilimo. Hawa watu wana-invest kule. Ninyi mnapochelewa kupeleka mbegu, hawa ndio wanaenda kuwapa wakulima mbegu na muda mwingine inaweza kutokea mvua hazijatosha, hawajapata kitu. Hela zao wao ndio zinakuwa zimepotea.
Naomba tuwaendeleze hawa, tuone ni namna gani ya kuimarisha mahusiano baina ya wakulima na hawa vijana wetu. Haiwezekani leo hii tumsifie kijana Mtanzania anayeenda kuchukua nguo China kuja kuuza, tumkandamize huyu ambaye aliamua kufanya kazi na mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi, nimeshauri sana tangu niwe Mbunge kwa sababu nina interest na kilimo na ninajua kilimo ndiyo cha kututoa.
Napenda kuzungumzia vijana. Kuna kundi moja la vijana ambao ni wahitimu wa Vyuo Vikuu, imekuwa kwao tatizo ni ajira, lakini wapo ambao wanajitolea, mmojawapo ni mimi. Tangu nilipomaliza diploma niliamua kuingia kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, lakini hawa vijana kutumia vile vyeti vyao tu kama collateral na Serikali iwasimamie vizuri, waweze kuwezeshwa kufanya kilimo chenye tija na cha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaunda kundi la hawa wahitimu mmoja akiwa mtaalam kutoka SUA mwingine awe accountant, mwingine awe mtu wa procurement, mwingine awe marketing; wakiungana hao wakaenda shambani na ukawawezesha kwa nyenzo, wakaenda kulima, wakauza, watafanikiwa na wao wenyewe watakuwa ni source ya ajira kwa vijana wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mengi sana ya kuchangia, nitaandika kwenye mchango wa maandishi. Tunataka kumtoa Mtanzania kwenye kilimo cha jembe, Mheshimiwa Mwigulu thubutu na utaweza. Weka sera ya kila kijiji kiwe na trekta. Tuna vijiji 19,200 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012; ukipiga hesabu ya trekta moja farm track ya milioni 35 na hiyo ni bei ya hapa Tanzania, inakuja hesabu ya kama shilingi bilioni 600.7. Ukithubutu utaweza kwa awamu, sio vijiji vyote vitahitaji! Utaweza na utakuwa umeacha trade mark ambayo haitafutika mioyoni mwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, kwa kuwa tunataka tuweke uchumi wa viwanda, tufanye kilimo cha biashara. Naomba tuanzishe agricultural zones, ifahamike. Ukanda ambao unalima ndizi, u-concetrate, uboreshe mbegu nzuri za ndizi ambazo tutaweza ku-export. Tunaweza kwenda Bukoba na Mbeya hawa wakawa zones za kulima ndizi, machungwa kwa watani zangu Tanga, mananasi kwa watani zangu Wasukuma Geita, pamoja na kwa kaka yangu Mheshimiwa Ridhiwani, ikawa ni zone kwa ajili ya mananasi. Tuna kilimo cha maua, leo hii Songwe, Mbeya, Iringa Arusha na uzuri miundombinu ipo, kuna airport, we can export fresh flowers to Europe and elsewhere in the world. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwetu Kanda ya Kati tukazanie kwenye alizeti, ufuta, choroko, dengu, mbaazi and I tell you Tanzania ni nchi ya tatu katika Afrika ku-produce mbaazi. Tunatengeneza mbaazi nzuri kweli! Mpwapwa kwa Mzee Lubeleje ndio wanatengeneza the best karanga in the world ambayo inatoa mafuta mazuri. Kwa nini tusitumie fursa hii kwa ajili ya kupata kipato kikubwa katika nchi yetu?
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Kwa hiyo, nashukuru sana. Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti ni suala muhimu linalowezesha kupata taarifa sahihi na kuwezesha kuweka mipango mbalimbali ya nchi. Ili kupata maendeleo endelevu katika michezo, ni muhimu kuwa na taarifa sahihi zilizofanyiwa utafiti. Serikali imefanya tafiti nyingi kama vile michezo kwa watu wenye ulemavu, michezo na UKIMWI, haiba na michezo na kadhalika. Bado kuna maeneo mengi ya michezo yanahitaji kufanyiwa tafiti ili kuongeza tija katika sekta ya michezo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo la kukosekana mfumo endelevu wa kuviendeleza vipaji vinavyoibuliwa na kuwa na miundombinu isiyokidhi mahitaji. Vilevile somo la elimu ya michezo limekuwa halifundishwi kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2002 hadi 2007 kulifanyika utafiti uliofanywa na Idara ya Elimu ya Michezo na Utamaduni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ulioonyesha kwamba vipindi vya masomo ya michezo katika shule za sekondari za Serikali na binafsi vimekuwa vikitumika kufundisha masomo mengine badala ya elimu ya michezo na michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tafiti hizi zilibainisha ukosefu wa walimu wenye sifa stahiki za kufundisha elimu ya michezo kuwa ni changamoto kwa shule za Serikali na binafsi nchini. Nashauri Mheshimiwa Waziri aanze na shule za binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwepo kwa mfumo na utaratibu mzuri wa ufuatiliaji na tathmini katika michezo kumeendelea kuathiri upatikanaji wa taarifa na mapato halisi yanayotokana na ajira za wanamichezo. Hali hii imeathiri wachezaji na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hii ikilinganishwa na nchi kama Nigeria, Ivory Coast, Ghana na Afrika ya Kusini ambazo zimefanikiwa kupitia michezo. Mheshimiwa Waziri, hili linaendana sambamba na sanaa, hususan muziki wa kizazi kipya. Kwa mfano, Diamond ndiye msanii anayelipwa zaidi kuliko msanii yeyote Afrika Mashariki na Kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka Disemba, 2015, Tanzania ilikuwa na wachezaji takribani kumi wanaocheza michezo ya kulipwa nje ya nchi. Tisa ni wa soka na mmoja wa mpira wa kikapu. Hata hivyo, mtazamo wa jamii haujajielekeza kutambua kuwa michezo ina michango katika kukuza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri, tuweze kutafuta wabia zaidi tuweze kujenga sports academy kama ile Jakaya Kikwete Sports Academy, ikiwezekana kila mkoa au angalau kila kanda kwa kuanzia.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia katika hoja zilizo mbele yetu. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, kwa kuniwezesha kuwa mwakilishi wa vijana katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite moja kwa moja kwenye mchango wangu. Naanza na asilimia tano ya mikopo kwa vijana kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri zetu. Naomba kuishauri Serikali kwamba hili jambo ni la kutilia mkazo maana limekuwa kama ngonjera. Kila siku watu wanaongelea kwamba kuna 10% Halmashauri zinatakiwa zitoe 5% iende kwenye vikundi vya akinamama na 5% ziende kwenye vikundi vya vijana lakini haifanyiki hivyo.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano na kasi yake iliyoanza nayo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi basi tunasema na hawa watu wa Halmashauri wajue kwamba huu ni wajibu, ni lazima watoe hizi fedha. Pia siyo kutoa tu zipangiwe utaratibu maana hii ni mikopo, lengo lake ni kwenda kuwasaidia hawa vijana waweze kufanya kazi, waweze kuinua kipato chao na vilevile hizi pesa zirudi ili vijana wengine wapate hiyo fursa. Kwa hiyo, uwekwe utaratibu mzuri wa kuzikopesha na kuzirudisha ili ziwe endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri awaambie Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya walisimamie kwa karibu jambo hili. Huu ni mpango wa Serikali lakini tumeona kuna vyama vingine vya siasa sijui wanalewa madaraka, juzi tu wameanza kutoa hundi, ooh, mapesa ya UKAWA, mapesa ya UKAWA ya wapi? Basi na sisi wa CCM kwenye Halmashauri tunazoziongoza tuanze kusema ni hela za CCM. Kwa hiyo, naomba ifahamike kwa wananchi kwamba huu ni mpango wa Serikali na siyo mpango wa vyama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye elimu. Napenda kuipongeza Serikali hii, tangu tulipokuwa tunaomba ridhaa kwa wananchi tulisema kwamba tuko kwa ajili ya kuwasaidia wananchi. Mmethubutu na mmeweza kuleta elimu msingi bila ya malipo, kazeni buti mwende mbele. Kitu chochote chenye neema lazima kiendane na changamoto. Tumeona udahili umeongezeka baada ya kuwawezesha wananchi kwani ile Sh. 20,000/= tu ya kumpeleka mtoto wake shule ilikuwa inamshinda.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutokana na neema hii kuna vitu vimeambatana nayo, kuna upungufu wa madarasa, Walimu, matundu ya vyoo halikadhalika na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya hawa Walimu wetu. Nashauri katika kila Halmashauri waweke mpango mzuri wa kuweza kutatua matatizo ambayo yanaambatana na neema hii bila kusahau madawati. Pia niwakumbushe tu ameshaongea Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kila Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi zile mbao mlizozikamata jamani ziende zikatengeneze madawati, ameongea bosi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee kuhusu sekta ya afya katika upatikanaji vifaa tiba na dawa. Hii imekuwa changamoto ambayo najua Serikali inajaribu kuikabili kutwa kucha. Tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, tukaeni chini tuna wataalam, Wizara yetu ya TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara kwani hatuwezi sisi kama Tanzania kuwa na viwanda ambavyo vitatengeneza dawa? Nina uhakika malighafi za kutengenezea dawa zipo.
Mheshimiwa Spika, Watani zangu Wahaya mtu akiumwa kichwa hanywi panadol ana dawa zake anazitumia. Nina uhakika malighafi za kutengeneza dawa tunazo, hiyo itatuokoa kwanza tutakuwa tunazalisha dawa zetu hapa, tutapata kipato soko lipo na pia dawa zitakuwa zinapatikana kwa bei nafuu na tutawaepuka hawa matapeli ambao wanatafuta fursa ya kuleta dawa ambazo zimepitwa na muda na siyo nzuri kwa matumizi ya binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia mradi wa uendelezaji miji ya kimkakati. Kwa Mkoa wetu wa Dodoma huu mradi umetusaidia sana kwenye maeneo ya Kisasa, Nkuhungu, Mjini Kati na Kikuyu. Kwa kweli mradi huu ulivyotekelezwa hapa mmetupa moyo, kweli mnatuheshimu kwamba hapa ni Makao Makuu ya Chama na Serikali. Kwa hiyo, naomba mradi huu uendelee kwenye sekta zingine za miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kugusia Tume ya Utumishi wa Walimu. Hiki kimekuwa ni kilio kikubwa sana kwa Walimu wetu. Tunajua mchango wao katika maendeleo ya Taifa letu kwa sababu aliyekuwa anaajiri Mwalimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na kuwalipa Walimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na kumpandisha cheo Mwalimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na malipo ya Mwalimu ni mwingine, lakini Tume hii ya Utumishi itakuja kuwa mkombozi wa Mwalimu, hongera sana kwa Serikali yetu. Kwenye bajeti hii tumeona mmeshawawekea fungu lakini tunaomba kwa siku za karibuni muweze kukamilisha taratibu zote ili hii Tume ipewe meno ianze kazi haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nigusie kidogo mipango ya matumizi bora ya ardhi. Wataalam wetu katika Halmashauri wakishirikiana na Viongozi wa Vijiji, Kata, pamoja na Wilaya na Madiwani wapange mipango bora ya ardhi kwa sababu huko ndiko kwenye wananchi na wanajua changamoto zinazotokea na ambazo zinaleta ugomvi kati ya wakulima na wafugaji. Tukikazania huko hili tatizo litakuwa historia kwa sababu wananchi wanaumia jamani. Sisi tupo huku lakini wananchi wa Kongwa tunaumia sana kwa hii migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda tu kugusia kwa hawa watumishi wa Halmashauri, kuna hawa Mabwana Kilimo, Mabwana Mifugo na Maafisa Biashara, majipu tusiangalie wale wanaofuja pesa tu tuwaangalie hata wale watumishi ambao hawatoi deliverance. Wananchi wetu wanajitahidi kujikwamua kwa kuendesha shughuli za kilimo na biashara lakini hawa wataalam hawawasaidii. Vijana wengi wapo hapa Dodoma wanafanya biashara ya uchuuzi wa mazao lakini hakuna Afisa Biashara hata siku moja kamfuata kumpa ushauri wa kitaalam. Vilevile Serikali ifike kipindi iwasaidie na kuwa-guarantee hawa vijana waweze kupata mikopo na wakopesheke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuongelea makusanyo ya mapato. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshaongea, Halmashauri wasipofikisha 80% ya ukusanyaji wa mapato waliokadiriwa zitafutwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu hii kauli iwe ni ya kweli, kama Halmashauri haijafika hicho kiwango basi ifutwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kugusia kwa juu tu kuhusu TASAF III, TASAF inasaidia sana. Tumeona TASAF I, TASAF II na sasa hivi tupo kwenye TASAF III ni kweli inasaidia wananchi wenye kipato cha chini na kaya maskini. Tunaomba TASAF iendelee na moyo huohuo, kelele nyingi na matatizo tuliyokutana nayo huko ni ya kisiasa kwa sababu wenzetu walisema, ooh, hizi hela zinakuja kwa ajili ya kampeni, siyo kweli, zinasaidia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuongelea PCCB, tumeona utendaji kazi wao mzuri, wanashughulikia masuala ya rushwa lakini kwenye ripoti zao tumeona wakiongelea, ooh, tume-save fedha kiasi fulani lakini kuna rushwa fulani sijui kwa nini inafichwa. Rushwa hii inaumiza kweli kweli, inawaathiri watu kisaikolojia, inasababisha watu wapate magonjwa, wengine hata wakate tamaa za maisha, ni section 25, rushwa ya ngono hasa kwa mtoto wa kike.
Mheshimiwa Spika, mtoto wa kike tangu elimu ya msingi anasumbuliwa na rushwa ya ngono, kwenye elimu ya sekondari anasumbuliwa na rushwa ya ngono, akija chuo kikuu anasumbuliwa na rushwa hii ya ngono, akija kwenye kazi anasumbuliwa na rushwa ya ngono. Jamani kama kesi zipo tunaomba zielezwe ili hawa mabinti wasifiche na waseme haya matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia mbili.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's