Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Martha Jachi Umbulla

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja hii. Kwanza kabisa na mimi nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa na afya njema na kuwa mahali hapa leo hii, na kwa moyo wa dhati nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa hotuba nzuri na zaidi kwa mengi ambayo anawatayarishia Watanzania kupitia hotuba yake.
Mheshimwia Naibu Spika, wananchi wa Tanzania wamemuunga mkono sana Mheshimwia Rais kupitia hotuba yake na kwa hakika Tanzania nzima inampongeza, Afrika inampongeza na dunia inampongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ameainisha maeneo mengi muhimu kwa maendeleo ya haraka ya nchi yetu. Vilevile ameainisha kero na malalamiko mengi sana ya Watanzania na baada ya kuainisha kupitia hotuba yake akatuletea sisi Wabunge wasaidizi wake ambao anatutarajia tuweze kumsaida katika kutatua kero hizo na malalamiko ya wananchi, alijua mahali pa kupeleka akijua kwamba Wabunge bila kujali kwamba ni wa chama gani wote ndiyo wananchi wanawategemea. Sasa kilichonishangaza mimi na kunisikitisha ni kujiuliza kwamba hivi wananchi wameiopokea na kuipongeza hotuba ya Rais na bila kujali itikadi. Amekwenda kila Jimbo akaainisha kero na malalamiko ya wananchi, sasa hawa wenzetu ambao hawakutaka kusikiliza hizi kero na malalamiko ya wananchi wanamwakilisha nani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningewaona mashujaa kama siku ile wangemsikiliza Mheshimiwa Rais, wakaona hotuba ile inasema nini na basi leo ama jana tulivyoanza kuchangia kwa kuona kwamba haiwafai basi wakatoka. Lakni tukashangaa wanaendelea kunga‟nga‟nia kujaribu kuchangia jambo ambalo hawakuweza kukubaliana naye. Lakini ya Mungu mengi niachie hapo.
Mheshimwia Naibu Spika, naomba nichangie kidogo sekta ya ardhi. Ardhi yetu imekuwa na thamani kubwa sana na inaendelea kuwa na thamani, tena kwa kasi kubwa sana, na hivyo kadri watu tunavyoongezeka na mifugo na mahitaji ya ardhi, kunakuwa na mahitaji makubwa ambayo ardhi inaendelea kuwa finyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa mfano, kule kwetu Manyara kuna migogoro kila Wilaya na hasa kufuatia uhaba wa ardhi. Ukienda Wilaya ya Kiteto kuna migogoro, ukienda Wilaya ya Mbulu, ukienda Wilaya ya Hanang, ukienda Wilaya ya Babati, Simanjiro kote kuna migogoro kutokana na uhaba wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mapendekezo mazuri ya Mheshimwia Rais na maainisho yote ya kwenye framework ya mpango wa miaka mitano mimi naomba kutoa mawazo ya ziada. Nchi yetu tumejaliwa kuwa na mapori makubwa sana ambayo mengineyo yana-potential kubwa ya kuweza kuzalisha mazao na hasa kutumika kwa ufungaji. Sasa ninaomba kwa sababu wananchi wenyewe hawawezi kuyawezesha hayo mapori ili yaweze kutumika kwa kilimo na ufugaji, naiomba Serikali itenge bajeti ya maksudi kabisa, ili iweze kusaidia kuwezesha haya mapori makubwa ambayo ni potential yaweze kutumika kwa ajili ya kilimo na kwa ajili ya ufugaji na zaidi sana kwa ajili ya uwekezaji vilevile kwa sababu tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda.
Mheshimwia Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Manyara pia sasa hivi, kuna wimbi kubwa la wizi wa mifugo, wafugaji wanawaibia wakulima mifugo yao ikiwa ni njia mojawapo ya kuwafukuza wale wakulima ili waweze kuwaachia maeneo hayo waweze kuingiza mifugo yao. Sasa hii ni tabia inayopelekea mauaji, naiomba Serikali iweze kubuni ni namna gani wanaweza wakaikomesha hii tabia ya wizi wa mifugo ambayo pia inapelekea mauaji. Itakapotoa tamko ya kuhakisha kwamba Serikali imetoa tamko kuhakikisha kwamba inatoa adhabu kali kama fundisho wimbi hilo la wizi wa mifugo linaweza likapungua na wananchi watafanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya viwanda tunaiona na kwa hakika mimi nakubaliana nayo, viwanda vitajenga uchumi wetu kwa haraka na kuongeza Pato letu la Taifa. Ninakubaliana na mapendekezo yote yaliyopo kwenye Hotuba ya Rais wetu, lakini vilevile niombe kwamba Mkoa wetu sisi wa Manyara ni maarufu sana kwa kilimo cha mazao hasa vitunguu swaumu. Najua vitunguu swaumu siyo zao lililozoeleka, niwahakikishie lina soko hata nje ya nchi. Ninaiomba Serikali wakati ukifika tuweze kufikiria kuweka kiwanda katika Mkoa wetu wa Manyara hususani Wilaya ya Mbulu ambapo tunalima kwa wingi sana zao hili ambalo kwa sasa hivi soko lake halina uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu matumizi ya shilingi milioni 50 alizoahidi Rais wetu. Tuna mifano mingi sana ya fedha za aina hiyo ikiwepo mabilioni ya Kikwete ambayo tuliyasikia kipindi kilichopita, lakini vilevile asilimia 10 ya fedha zinazotengwa na Halmashauri kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi kwa bahati mbaya hazikuwekewa mfumo mzuri ambao ungeweza kuwafikia walengwa. Ninaiomba Serikali itakapofikia wakati huo wa kutupa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na hasa kwa kuwawezesha wanawake na vijana na makundi mengine. Tuangalie isije ikaenda kwenye mfumo huo huo wa upotevu bali tuiwekee utaratibu mahsusi, bila haraka yoyote kuhakikisha kwamba kunakuwa na taaluma ya kutosha ili fedha hizi ziweze kuwafikia walengwa waweze kufanya kazi iliyokusudiwa na hivyo kufikisha dhamira ya Rais iliyo njema ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo waweze kufanya kazi yao kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa na haya machache naunga mkono hoja na naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa juhudi kubwa anayoiweka katika kuliongoza Taifa letu, ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia uzima na kuweza kusimama hapa kuchangia hoja
hii ya Wizara ya Elimu. Naomba na mimi nichukue fursa kama wenzangu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako, na Naibu Wake Mheshimiwa Stella Manyanya, aidha nimpe pole kwa msiba wa mama yetu na Mungu ampe subira.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ni ufunguo wa maisha na lazima Watanzania wapate elimu itakayowafungua katika maisha yao. Aidha, niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, kwa sababu imekwisha anza kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu wote na wanakuwa na ufunguo wa maisha kwa sababu ya kuanza mfumo wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya msingi pamoja na sekondari hadi kidato cha nne ni kama msingi wa nyumba, na kama msingi wa nyumba ni imara basi elimu yetu ya msingi na sekondari itakapokuwa imara tutakuwa na elimu iliyo bora hadi vyuo vikuu na hatimaye Watanzania wote watakuwa na elimu bora Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini elimu bora pia inatokana na walimu walio bora, na wenye moyo wa kufundisha kwa sababu walimu ndio watakaoweza kuboresha elimu yetu na kwa hivyo ni lazima tuhakikishe kwamba changamoto zote zinazokabili elimu ya msingi na elimu ya sekondari tuweze kuzitatua ili dhamira yetu ya kuboresha elimu kuanzia msingi na sekondari iweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze kuzungumzia mazingira wezeshi kwa ajili ya walimu wetu hasa wa sekondari za kata. Walimu wetu wa sekondari za kata wako katika mazingira magumu sana, hasa sisi ambao tunatoka katika mikoa ya pembezoni. Walimu wengi wa sekondari hizi za kata wako katika maeneo ambayo hakuna umeme, maji, huduma mbali mbali za jamii, hospitali ziko mbali na hatimaye hata mitandao hizi ambazo vijana wengi wanazitumia hazipo; na kwa hivyo utaona changamoto nyingi zinazowakabili vijana hawa walimu ili waweze kufanya kazi katika Sekondari hizo ama maeneo hayo, inahitajika ushawishi ili waweze kuendelea kufanya kazi katika shule ama maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naiomba Serikali kwamba iweze kuangalia uwezekano wa kuwapa walimu wa sekondari za kata, na maeneo mengine yenye mazingira ambazo ni mbaya, waweze kupata hardship allowance ili iweze kuwapa motisha. Hili ni muhimu sana, najua walimu wengi wote wana matatizo ya hapa na pale, lakini hawa ambao wako katika sekondari hizi zenye mazingira ambayo sio wezeshi n wanahitaji uangalizi ama huruma ya Serikali kwa kuweza kuwapa motisha waweze kufundisha kwa sababu elimu bora kama ambavyo nilianza ni pamoja na mwalimu ambaye atakuwa na moyo wa kufundisha baada ya kuwezeshwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia mengi yameisha zungumzwa. Lakini ni suala zima la kutenga maeneo ya shule ambayo yatawezesha kilimo ya mashamba na bustani. Tuki-refer elimu za hapo awali, shule zetu nyingi zinakuwa na mashamba ama maeneo ambayo wanafunzi wanalima na kilimo hicho kinaweza kikasaidia pia kuwapatia chakula cha mchana, ama matunda ambayo yatawajenga wanafunzi wetu kiakili, kimwili na kiafya. Kwa hiyo, najua changamoto ya ardhi ambayo inakumba nchi yetu hasa kwa maeneo ya mjini lakini bado kwa maeneo ya mikoani tuna ardhi ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo uanzishwaji wa shule ziende sambamba na maeneo ambayo wanafunzi watapata kulima na kuweza kujijenga kimwili na kiafya. Lakini vilevile kupata chakula kwa bei nafuu. Tukisema wazazi waendelee kuchanga kwa ajili ya chakula cha mchana cha wanafunzi, bado ni mzigo na kwa hivyo tutafute namna rahisi ya kuweza kuwapatia wanafunzi wetu chakula cha mchana, kupunguza pia utoro shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia upungufu wa walimu wa sayansi. Hili limezungumzwa sana. Lakini mkoa wetu wa Manyara una upungufu mkubwa sana wa walimu wa sayansi, najua pengine na maeneo mengine lakini ya kwetu lazima niisemee, hatuna walimu kabisa wa masomo ya sayansi, kwa hivyo tunaomba Serikali iweze kuangalia inapo-allocate walimu, iweze kufikiria maeneo ambayo tayari kuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itafute kila mbinu, jinsi ambavyo ilipata mbinu ya kujenga maabara nchi nzima, tukaweza kujenga kwa kipindi kifupi. Hiyo ni hatua ya kwanza na tumemaliza, na mimi naipongeza Serikali, wanaoibeza wana lao, lakini tayari tuna maabara zetu, nina hakika kwamba walimu wa sayansi watapatikana. Serikali iweke juhudi ya hali ya juu, kuhakikisha kwamba walimu wa sayansi wanapatikana ili waweze kufundisha masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa maabara umefanikiwa, lakini ninajua kwamba suala hili lilikuwa suala kama la zimamoto na imetumia fedha ambazo zilikuwa zimekusudiwa kwa madhumuni mengine. Kwa mfano, huko katika Wilaya yetu ya Mbulu ama Mkoa wetu wa Manyara, maabara tumezijenga katika Wilaya zote, lakini tumetumia fedha ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya miradi kwa hiyo baadhi ya miradi sasa hivi imekwama kwa kukosa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kulikuwa na ujenzi wa madaraja muhimu sana katika maeneo ya vijijini kama Daraja la Gunyoda kule Mbulu, ujenzi wa kituo cha afya kule Endagikoti, Mbulu, tayari miradi hii na miradi mingi ya umwagiliaji imekwama kwa sababu ya kukosa fedha, kwa sababu fedha zile zilikuwa diverted kwenda kujenga maabara. Naiomba Serikali iweze kuangalia hili na ihakikishe kwamba fedha hizi zinarudishwa ili miradi hii ya maendeleo iweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala zima la matatizo ya walimu wastaafu. Hili ni tatizo sugu na wengi wamelizungumzia, lakini ni kilio cha wastaafu walimu wengi ni lazima Serikali iwe sikivu, wananchi wanapolalamika kwa kipindi kirefu na kilio hiki cha wastaafu ambao hawapati stahili zao ni cha muda mrefu sana. Walimu wengi kipindi kile cha kupandisha madaraja kiliposimamishwa, wengi walikuwa wanaendelea kufanya kazi na huko wanastahili na wanapaswa kupandishwa daraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala hili lilikuja kufikia kupandishwa madaraja wakati wengi wameshastaafu vilevile, ninaiomba Wizara iangalie walimu ambao tayari walistahili kupandishwa na wamekaa katika cheo kimoja zaidi ya miaka 15, lakini hadi wanastaafu hawakuweza kupata stahili zao. Na sasa wako wengine ambao wamesimama kwa kipindi kirefu, mishahara yao inatofautiana na walimu ambao walikuwa nao wameajiliwa hata baada yao, lakini wana mishahara ambayo ni midogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nachukua fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Maliasili Utalii Profesa Maghembe, Naibu wake Engineer Ramo Makani kwa kazi nzuri sana wanayofanya kwa Wizara hii, kumbukeni methali ile isemayo mti wenye matunda hauishi kutupiwa mawe. Hata hivyo mmeweza na tunawatakia kazi njema na ya ufanisi kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazo hoja zangu kadhaa ambazo naomba mnapo-wind up mnipatie majibu.
(i) Burunge Game Control Area iliyoko Makuyuni na Babati Vijijini ni eneo kubwa sana igawanywe ili ibakie sehemu ndogo tu na nyingine irudishiwe wananchi na hivyo sheria iliyoko ibadilishwe kuruhusu mapendekezo hayo.
(ii) WMA iliyoko eneo la Vilima Vitatu Babati ni mateso makubwa kwa wafugaji walioko eneo lile, kiasilia eneo hilo lilikuwa la wafugaji na hata baada ya kushtakiana na WMA wafugaji walishindwa kesi. Hadi leo wananchi hao hawajapewa haki yao, naiomba Wizara ilishughulikie suala hili kuwapa wananchi wa Vilima Vitatu utulivu wa maisha na usalama wa maisha yao na mifugo yao. Naomba kauli ya Wizara.;
(iii) Vijiji 16 vinavyozunguka hifadhi ya Tarangire na Magugu walipoondolewa waliambiwa watapewa kifuta jasho hadi leo kati ya fedha walizoahidiwa Tanzania zaidi ya shilingi milioni 100 wamepewa shilingi milioni 12 tu. Huu ni unyanyasaji wa wananchi. Naomba msaada wako Professa na naomba kauli ya Serikali.
(iv) Wananchi wanaozunguka Hifadhi za Ayamango, Gedamar na Giijedabonga – Babati wako pale tangu Operesheni Vijiji, leo na kwa muda mrefu ndani ya hifadhi isitoshe wengi wao hawajaonyeshwa maeneo ya kuhamia kila mara ni mapambano na askari na wanyamapori. Mheshimiwa Profesa na Engineer (Wizara) naomba sana mtoe suluhu ya migogoro hii, fidia wanayopewa haijengi hata choo.
(v) Wakati wa Operesheni Tokomeza aliuwawa mwanamke kwa maelezo yaliyotolewa hata hapa Bungeni na kwenye vyombo vya habari, Serikali iliunda Tume ya Kijaji na hadi leo hii hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Serikali. Mheshimiwa Jitu amewaandikia barua bila majibu yoyote, naiomba Wizara itoe kauli juu ya jambo hili linalosubiriwa na wananchi wa Babati na Mkoa wa Manyara.
(vi) Halmashauri ya Wilaya zinazopaswa kupata asilimia 0.3 ya service levy za hoteli za kitalii zinazopaswa kulipa Halmashauri lakini hoteli zimegoma kulipa kiasi hicho mpaka Mahakama ya Rufaa, lakini Wizara imekaa kimya. Tunaomba ufumbuzi wa malipo haya ya asilimia 0.3 service levy kwa Halmashauri husika hapa nchini ni imani yangu Mheshimiwa Waziri utatolea kauli.
(vii) Tanzania Forest Service wanakusanya ushuru mkubwa kutokana na mkaa wa magogo. Naiomba na naishauri Serikali kuwa taasisi hii irudishe kiasi fulani cha mauzo haya ili kuendeleza upandaji wa miti itafika mahali misitu itaisha.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kupata nafasi hii na mimi nichangie hoja iliyoko mbele yetu. Na mimi nichukue fursa hii kwanza kukupongeza wewe binafsi kwa umahiri wako na ushupavu wako wa kuliongoza vyema Bunge letu, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja iliyoko mbele yetu ni mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti ya 2016/2017 na katika kuliangalia hilo, ni lazima tuangalie utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 ili tuweze kujifunza tulikosea wapi na vipi tujisahihishe ili tuweze kwenda vizuri kwa bajeti yetu ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vipaumbele vilivyowekwa katika bajeti ya 2015/2016 mimi nimevichukua viwili ili niweze kuvichambua tuone ufanikiwaji ulikwenda kwa kiwango gani? La kwanza kabisa, kipaumbele chetu cha kwanza ilikuwa kupunguza umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la kupunguza umaskini, tukiangalia katika jamii zetu, kwa mabilioni na matrilioni ya fedha tulizowasomea wananchi mwaka 2015, ni kwa kiwango gani umaskini umepungua baina ya jamii yetu ya Watanzania. Hali bado ni mbaya sana vijijini, wananchi wetu bado hawana milo mitatu, wananchi hawana nyumba bora za kuishi, wananchi wetu bado hawana vyanzo vya uhakika vya fedha na kwa hiyo, ni vizuri kutafakari, ni kwa namna gani umaskini utapungua katika nchi yetu hasa kwa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujipima hivyo, ni vizuri pia tukaangalia changamoto zilizojitokeza, changamoto kubwa ambayo imejitokeza katika kupunguza umaskini baina ya jamii zetu, kubwa ambalo limeonekana ni upatikanaji wa rasilimali fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Serikali imeweka mfumo thabiti wa ukusanyaji wa fedha katika bajeti ya mwaka huu na zaidi sana ni hili la kutumia electronic machines. Mfumo huu bado una changamoto kubwa sana. Pamoja na kuweka mikakati na adhabu zitakazotolewa kwa ajili ya watakaokiuka kutoza kutumia mashine hizo, bado mimi nina wasiwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vituo vya petroli, kwa mfano, wakikwambia mashine hii ni mbovu ama iko out of order na ni kweli utakavyodhihirika hivyo, bado utakapomchukulia hatua mfanyabiashara ambaye mashine yake hiyo ni mbovu, utakuwa hujamtendea haki. Kwa sababu utakuta ni ukweli na umempa adhabu na kutakuwa na msururu wa watu kutaka huduma na watakapokosa huduma ya kupata petroli na dizeli wataleta lawama tena kwa Serikali. Kwa hiyo, nadhani tuangalie ni namna gani tutaboresha mfumo mzuri wa ukusanyaji kodi ili tuweze kutekeleza miradi yetu ya maendeleo katika Vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nililotaka kuishauri Serikali ni kwamba bajeti iendane na tathmini halisi ambayo tumeiona katika utekelezaji wa kipindi kilichopita. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona kwamba pamoja na jitihada za kupunguza umasikini ametenga shilingi milioni 50 kila kijiji. Dhamira yake ni njema na itakapotekelezwa itakwenda vizuri. Utekelezaji watatengeneza wataalam, lakini bado ametenga fedha hizo ili kuona ni namna gani umasikini utapungua katika jamii zetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kipaumbele cha pili, kilikuwa upatikanaji wa huduma za jamii. Kilio kikubwa cha Waheshimiwa Wabunge tangu waanze michango humu tumeona ni kilio cha maji. Maji bado ni tatizo kubwa katika jamii zetu na kwa hiyo, kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ni vizuri kuendelea kubuni mikakati bora ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. Sasa utaratibu uliopo, naipongeza pia Serikali kwa kutenga hiyo asilimia ndogo ya kuongeza kwenye tozo ya mafuta ya shilingi 100. Nina uhakika shilingi bilioni 250 zitakapopatikana, shilingi bilioni 220 zikienda kwenye usambazaji wa maji vijjijini itasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni mkatakati mzuri na mimi nauamini kwa sababu tozo ya kwenye mafuta na petroli ni tozo yenye uhakika, kwa sababu huduma hiyo ipo kila siku na tumeona kwenye miradi ya REA pia. Tozo zilizowekwa kwenye REA imetusaidia kusambaza umeme vijijini na kwa hiyo, hiki ni chanzo ambacho kinaweza kikatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huduma nyingine ya jamii ni suala la elimu. Nampongeza tena Mheshimiwa Rais kwa kuleta mfumo wa elimu bure, nina hakika tathmini mwisho wa siku itakwenda vizuri katika kuboresha elimu katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima la huduma za afya. Huduma za afya ni kipaumbele kingine cha pili baada ya maji. Suala la afya hasa kwa kabrasha hili ambalo limetolewa na TAMISEMI kwa Mkoa wangu wa Manyara, ni masikitiko makubwa sana. Nimeona katika taarifa hii iliyotolewa na TAMISEMI na hasa ikishirikiana na Wizara ya Afya; Mkoa wa Manyara katika mlolongo wa kuodhoresha zahanati na uboreshaji na ukarabati wa vituo vya afya, nimesikitika kuona Wilaya ya Simanjiro imewekewa zahanati moja tu, wakati Mikoa mingine na Wilaya nyingine zina zahanati mpaka 10 hadi 15. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Wilaya ya Kiteto kubwa kama hiyo, imewekewa zahanati tatu tu. Tena cha kusikitisha fedha ambazo zitakwenda kukarabati majengo hayo ni Capital Development Grants ambazo mara nyingi wala hazipatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha kwa Mkoa wa Manyara, sijui mikoa mingine imetumia mbinu gani kuhakikisha kwamba wamewekewa fedha za kutosha, lakini naiomba Wizara na Serikali na hasa maeneo husika kwamba waangalie hili. Wilaya ya Mbulu ina Majimbo mawili, lakini zahanati na vituo vya afya vilivyoorodheshwa hapa na vya Jimbo la Mbulu Mjini; tunaishukuru Serikali kwa hilo kwa sababu na mimi natokea huko, lakini ni vizuri kuiona Mbulu Vijijini kwani hakuna hata zahanati moja iliyoorodheshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeliona kabrasha hili nikadhani kwamba ni makosa yamefanyika, naamini kwamba wahusika watakwenda kuiangalia vyema na kuhakikisha kwamba kila Wilaya inanufaika na usambazaji ama upatikanaji wa huduma za afya ikiwepo kujenga zahanati na vituo vya afya katika kila kijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo…

NAIBU SPIKA: Kengele ni ya pili hiyo Mheshimiwa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara ya hii ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamezungumzwa na wazungumzaji wamenifilisi kidogo lakini niendelee kusisitiza kwamba kwanza naishukuru Serikali yangu kwa kuhakikisha kwamba bajeti ya mwaka asilimia 40 zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo. Hii ni hatua ambayo imekuwepo kwa mara ya kwanza na kabla kabisa ya utekelezaji, kadri wenzangu walivyosisitiza tunaomba na kwa muda mrefu tumesisitiza kwamba Sheria ya Manunuzi iletwe haraka sana Bungeni tuweze kuifanyia marekebisho ili asilimia hiyo 40 iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo iweze kuwa na impact kwa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupanga matumizi ni jambo moja lakini kutekeleza yale yaliyokusudiwa ni jambo la pili na la muhimu zaidi. Nishauri Wizara kuhakikisha kuwa yale yote yaliyokusudiwa, yaliyopangiwa matumizi yaweze kutekelezwa jinsi ambavyo Bunge litapitisha na kuidhinisha matumizi hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hadi kufikia Machi 2016 fedha zile zilizokuwa zimepangwa kwa bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa mfano mafungu 62 yale yaliyoko chini ya Serikali Kuu ni mafungu 33 yaliweza kupewa fedha kwa asilimia 50. Kwa hiyo, ni wazi kwamba bajeti hiyo haitakidhi matarajio yale ama matumizi yale ambayo yamepangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria ya bajeti ambayo ni ya 2015 mwaka jana tu, tunatarajia kwamba sheria hiyo italeta impact kwa bajeti ya mwaka huu. Kwa kuwa kuna sheria, tuna imani kwamba matumizi ya fedha ambazo zimepangwa kufikishwa katika miradi yetu yatasimamiwa na sheria hiyo. Zaidi sana kwa kuwa tuna mid term review ya bajeti yetu, tunaamini kwamba Sheria ya Bajeti itaisimamia kikamilifu kuhakikisha kwamba jinsi Bunge litakavyoidhinisha fedha hizo zitaweza kufikishwa jinsi zilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu spika, nizungumzie na mimi mradi wa Village Empowerment maarufu kama shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Kwanza ni-declare interest kwamba mimi nina utaalamu kiasi fulani wa micro-finance na kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu kwa kubuni mradi huu wa shilingi milioni 50 kila kijiji. Pia nieleze hofu yangu, sijajua vizuri kwamba hiyo shilingi milioni 50 ambazo zitatolewa kama mikopo kwa wajasiriamali ni pamoja na fedha zitakazotumika katika kuhamasisha wananchi ama zitakazotumika katika kuweka wataalamu watakaosimamia miradi hiyo ama ni fedha zitatengwa na bajeti nyingine ili kuweza kuhakikisha kwamba shilingi milioni 50 kwa kila kijiji inamfikia kila mwananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze wasiwasi wangu pia kwamba je, shilingi milioni 50 zinavyokwenda kwenye kijiji ni kwa jinsi gani kila mwanakijiji atafikiwa na fedha hizo? Kama hivyo ndivyo ilivyo na nadhani ndiyo matarajio ya Rais wetu kwamba kila mtu atapaswa kupata mkopo hasa wale waliolengwa wanawake na vijana. Kwa hiyo, ni lazima kuwe na mkakati madhubuti kuhakikisha kwamba hizi fedha zinawafikia walengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, fedha hizo zinawafikiaje? Mimi siamini utaratibu huu wa SACCOS, naamini zaidi utaratibu wa revolving loan fund ili fedha hizi zitakapotolewa kwa awamu ziweze kuzunguka zimfikie kila mwananchi. Kwa sababu tuna uzoefu tumeona kwamba katika mifuko mingine ambayo tumeahidiwa na viongozi wetu, kwa mfano mabilioni ya JK, bahati nzuri mimi nilikuwa mmoja wa walioteuliwa kati ya Wabunge saba kushauri katika ile National Executive Empowerment Council lakini tukaishia kupata barua na hatukuweza kuitwa hata siku moja na hatukujua hata yalikwendaje na yaliishia wapi. Kwa hiyo, tuna hofu kutokana na uzoefu wa kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba fedha hizi za sasa zikiwekewa utaratibu madhubuti, zikawekewa na riba kwa sababu riba ni suala muhimu sana katika kukopesha wananchi, unapoweka riba inazalisha zaidi na kupunguza uzito kwa Serikali kwa sababu ile riba inaweza ikatumika katika kuhakikisha kwamba kunakuwepo na wataalamu watakaolipwa ili wasimamie kwa kikamilifu utoaji wa mikopo na urejeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilishikwa na wasiwasi kama Wajumbe wengine wa Kamati yangu, ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, kwa shilingi milioni 50 zinapaswa ziende shilingi bilioni 980 na zitafikia jumla ya vijiji 19,600. Hata hivyo, tunaona kwamba zimetengwa tu shilingi bilioni 59.5 ambazo hazitoshi kabisa. Kwa hiyo, naishauri Serikali yangu iongeze bajeti hiyo ili azma ya kufikia kila kijiji kwa shilingi milioni 50 iweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile fedha hizi ziwekewe utaratibu ili zisiweze kupotea kama ambavyo tunaona utaratibu wa mikopo ya Halmashauri inavyopotoea kwa sababu haina ufuatiliaji, haina riba, haina hata namna yoyote ili ya kufuatilia nani kapewa, nani karejesha na kwa muda gani urejeshaji ufanyike. Mkopo ni fedha unayompa mtu kwa matarajio ya kurejesha kwa hivyo ni lazima uwe na utaratibu madhubuti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamekwishasemwa lakini nashauri kwamba utaratibu huu wa revolving loan fund ni sawa unapompa mtu mwenye njaa samaki ukitarajia kwamba kesho atakuomba tena, lakini kumbe ni vizuri basi ukampa mtu vifaa vya kuvulia samaki ili aendelee kupata chakula badala ya kumpa samaki ambaye atakula leo tu na kesho atakuwa hana kitu. Kwa hivyo, mimi nashauri, revolving loan fund ndiyo utaratibu ambao utawezesha kila mwananchi kufikiwa ndani ya kijiji na hatimaye mradi utakuwa endelevu, hata Rais atakapokuwa amemaliza muda wake wa miaka kumi, atakuwa ameacha legacy ya mikopo hii inaendelea ndani ya nchi yetu, wananchi wanaendelea kukopeshana na hatimaye tunapunguza umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na haya machache mengine yamezungumziwa sina sababu ya kurudia, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. MARTHA J.UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa mchango wangu kwa hoja hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuthamini shughuli ndogo ndogo za wananchi katika kuzalisha mali, lakini naomba kutoa masikitiko yangu kuhusu wajasiriamali wadogo wanaonyweshea mbogamboga kutumia maji machafu yanayotiririka kwenye mifereji, Jijini Dar es Salaam. Mboga hizi huuzwa kwenye mahoteli mbalimbali jijini humo na kusababisha madhara kiafya pia inasababisha kinyaa kwa walaji. Kero hii inajulikana na watu wengi wakiwepo viongozi wanaoweza kufanya uamuzi kupiga marufuku kutumia maji hayo. Vinginevyo Serikali ishughulikie kusafisha mifereji yote michafu ili maji yanayotiririka humo yawe salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Sekta ya Kilimo, kuna athari kubwa sana ya uharibifu wa mazingira kwa mfano robo tatu ya ardhi ya Wilaya ya Kiteto imelimwa, (kuacha mapori yasiyofaa kwa kilimo na ufugaji) kwa sababu hiyo miti yote katika maeneo hayo yamekatwa na ardhi kubakia tupu (bila miti). Nini mikakati ya Serikali katika kunusuru Wilaya hiyo (ardhi yake) kugeuka kuwa jangwa? Tuliambiwa ardhi hiyo imepimwa miaka mitatu iliyopita, lakini hadi leo wakulima wakubwa wanaendelea kulima na ardhi inaendelea kuwa finyu pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Sekta hii; sehemu kubwa asilimia 80 inategemea fedha za nje, hali inayohatarisha kutekelezeka kwa miradi ya mazingira kwa sababu fedha za nje mara kwa mara haziletwi kwa wakati. Naomba kujua Serikali inasemaje kuhusu hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's