Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Rose Cyprian Tweve

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuchangia, naomba kwanza kuanza kwa kutoa shukurani. Moja kwa Mwenyezi Mungu; pili, kwa wazazi wangu; baba yangu na mama yangu, kwa kunilea, kunisomesha na zaidi ya yote kwa kunipa ujasiri mpaka nimeweza kufika hapa leo. Baba na mama nawashukuruni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nachukua fursa hii kuwashukuru akinamama wote wa Mkoa wa Iringa kwa kunidhamini, kwa kuniamini niwe mwakilishi wao. Kweli mmenipa heshima kubwa sana. Naomba mwendelee kuniombea Mwenyezi Mungu anipe nguvu, hekima na busara ili tuweze kushirikiana vyema tuisaidie Iringa yetu iweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, pia nitoe pongezi zangu kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa na ngumu anayoifanya kwa kujitoa muhanga, awe kimbilio, awe macho ya maskini na wanyonge. Mheshimiwa Rais, nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa niaba ya wanawake wote wa Mkoa wa Iringa, namshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kumchagua Mama yetu Samia, kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii inadhihirisha anatutambua sisi wanawake, anatambua mchango wetu kwa nchi hii na anataka tuendelee kushiriki kikamilifu katika maamuzi yatakayohusu Serikali ya nchi yetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais tunakushukuru sana. Mama Samia hongera sana; najua utatuwakilisha vyema na sisi wanawake wa Tanzania tupo nyuma yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja, niunge mkono hoja iliyoletwa mbele yetu na Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji. Natambua kuwa Serikali yetu inajipanga kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda ili tuweze kupambana na hili tatizo sugu la ajira na umaskini hasa kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kuwa asilimia 75 ya Watanzania, wanategemea aidha kilimo, uvuvi na ufugaji. Sasa wakati Mpango wa Maendeleo umeletwa hapa kujadiliwa, wengi tulishauri kuwa corner stone ya huu uchumi wa viwanda, viwe vikubwa au vidogo lazima vitumie raw materials ambazo zitakuwa zinazalishwa na hawa wakulima wadogo wadogo ambao wanatoka vijjini. Lengo lilikuwa, kusaidia kupata soko na ku-add value ya hizi hizi raw materials ambazo zitakuwa zinazalishwa na hawa wakulima wadogo wadogo. Kwa kufanya hivyo, tutasaidia kuinua uchumi wa wakulima na kuisaidia Tanzania iweze kufika kwenye huu uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi kama Malaysia na India, zilikuwa nchi maskini. For example Malaysia was one of the poorest country kuliko hata Tanzania, lakini wenzetu wameweza kupiga hatua na sekta ambayo imeweza kuwafikisha hapo ni Sekta ya Kilimo. Waliwatengenezea mazingira mazuri wakulima hawa wadogo na wafugaji wadogo wadogo. One of the things they did ni kutengeneza hizi collection centers; zikawa ni kiunganaishi kati ya wafugaji, wakulima na viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi collection centres zinasaidia huyu mfugaji au mkulima anapoamka asubuhi wazo lake kubwa ni kuzalisha na siyo soko la mazao yake; lakini hapa Tanzania bado kidogo tuko nyuma. Kwa mfano, mifugo; Tanzania is one of the leading countries kwenye mifugo, lakini bado tuna-import maziwa kutoka nchi nyingine. What is problem here? Hatuna viunganishi, hatuna collection centers ambazo zitawaunganisha hawa wafugaji na viwanda vilivyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano kidogo tu. Pale Mkoani kwangu Iringa tuna kiwanda kikubwa cha Asasi, kina-process products nyingi zinazotokana na maziwa; mengine tunatumia hapa kwenye restaurant yetu ya Bunge, naomba mwendelee kutuunga mkono. Kiwanda hiki kinaweza ku-process lita 100,000 kwa siku, lakini mpaka leo hii kinapokea maziwa lita 15,000; na hizi zitoke Mikoa mitatu; pale Iringa, Njombe na Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha zaidi, pale Iringa kuna wafugaji ambao maziwa yanaozea ndani. Tatizo hapa ni nini? Ni kile ambacho nimesema kwamba hatuna viunganishi, hatuna collection centers ambazo zitawaunganisha hawa wafugaji na hiki kiwanda kilichoko pale. Kwa hiyo, Waziri Mheshimiwa Mwigulu nakuomba, umefanya kazi kubwa kwenye Mkoa wangu wa Iringa, naomba ufike pale tuwe kiunganishi, tuwatengenezee hizi collection centers kwenye Wilaya yangu ya Mufindi, Wilaya ya Iringa Mjini, Iringa Vijijini na Kilolo. This will be a win-win situation. Tutakuwa tume-create soko kwa wale wafugaji wadogo wadogo na pia tutam-assure raw material huyu mwekezaji ambaye amefungua kiwanda pale Mkoa wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho ningependa kushauri, tu-invest kwenye elimu. Wakati TAMISEMI wanawasilisha bajeti yao, ilionesha kuwa kuna hawa Maafisa Ugani, less than fourteen thousand, kuna thirteen thousand five hundred and thirty two. Hii ni namba ndogo and this can be easily solved.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna watoto wengi ambao wamemaliza Shule za Kata, tuwape incentives. Hizi ruzuku tunazotoa kwenye pembejeo, tuhakikishe tunawekeza kwenye elimu. Hawa Maafisa Ugani ndiyo watakaokuja kuwa Walimu wa kuwafundisha huyu bibi na babu kwa sababu lengo ni kuhakikisha hii asilimia 75 inaendana na huu uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Waziri wa fedha kwa kutambua unyeti wa Sekta hii ya Kilimo akaahidi kutoa nyongeza ili iweze kutusaidia kufikia malengo ya uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nihitimishe kwa kusema yafuatayo:-
Tanzania ya viwanda inawezekana, Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana; uzuri Sekta hii imepewa Waziri Mheshimiwa Mwigulu aliye makini, ambaye yuko competent, ambaye atatufikisha pale tunapotaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii nyeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja niunge mkono hoja iliyoletwa mbele yetu leo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Sote tunatambua Tanzania kuna uhaba mkubwa wa Walimu hususani kwenye masoma ya Mathematics na English. Tanzania hatuna Chuo cha Ualimu kinachoandaa Walimu wa English watakaofundisha shule za msingi. Maana yake kuna 100% lack of trained English Medium Primary School Teachers.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Teachers Colleges za Primary Schools zinafundisha kwa Kiswahili. Sasa changamoto inakuja kwamba, pamoja na kuwa Wizara ya Elimu inatambua mapungufu hayo hakuna coordination na Wizara zingine kama Wizara ya Kazi.
Wizara ya Kazi ina charge $500 kutoa class B work permit regardless wewe ni Mwalimu au ni Injinia wa Dangote Cement au Barrick Gold Mine. Kinachosikitisha zaidi, Wizara ya Mambo ya Ndani yaani Uhamiaji wao wanatoza $2000 fee ya resident permit kwa hawa Walimu ambao tunawahitaji sana. Hii fee imeongezwa kutoka $600 iliyokuwa wanatozwa mwanzo mpaka $2,000 kwa sasa na hii fee ya $2,000 ni kwa miaka miwili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli Taifa letu linataka kusaidia watoto wetu, napenda nishauri yafuatayo:-
(i) Hizi fee zifutwe ili kuvutia kupata Walimu bora watakaoweza kufundisha vijana wetu; na
(ii) Tuwape support ya kutosha hawa ndugu zetu wenye private schools wakati Serikali yetu inaendelea kuboresha hizi government schools kwa sababu utafiti unaonyesha private schools ndizo zinatoa elimu bora zaidi kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, naomba maslahi ya Walimu wetu yaboreshwe ili kuwapa motisha ya wao kuendelea kuwasaidia vijana wetu. Pia tuhakikishe shule za msingi wanapewa madawati ya kutosha hususani Mkoa wangu wa Iringa watoto wetu bado wanakaa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hoja iliyoletwa mbele yetu siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri sana. Vilevile nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Wizara hii. Hii inadhihirisha kuwa Wizara imepata Waziri pamoja na Naibu Waziri walio makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende moja kwa moja, niunge mkono hoja iliyoletwa mbele yetu. Natambua kuwa Serikali yetu imefanya mambo mengi na inaendelea kuhakikisha kuwa utamaduni, sanaa na michezo inapewa kipaumblele hasa kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya msingi ningependa kuishauri Serikali. Kwanza tuhakikishe kwamba sanaa na michezo inapewa kipaumbele toka shule za msingi. Lazima tuhakikishe vijana wetu wanapewa vifaa vya michezo na sanaa. Shule nyingi hazina viwanja vizuri vya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuhakikishe tunawekeza kupata walimu wazuri wa kuwafundisha hawa vijana wetu. Lazima sisi kama Taifa tuhakikishe tuna academy kuibua vipaji vya vijana wetu katika michezo mbalimbali kama vile basketball, volleyball, mbio na sanaa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo tutajihakikishia Taifa letu litakuwa na uhakika wa kuwa na vijana ambao wataweza kushindana na mataifa yaliyoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Naomba niende moja kwa moja, niunge mkono hoja ambayo imeletwa leo hapa mbele yetu na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri Lukuvi na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya kuongoza na kusimamia wizara hii nyeti. Matunda ya kazi yao kweli yanaonekana, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, personally naomba nimshukuru Mheshimiwa Lukuvi kwa kuwa mfano wa kuigwa hasa kwangu mimi nikiwa kijana kiongozi. Amedhihirisha ni jinsi gani tunatakiwa kuwajibika pale tunapopewa majukumu yetu, ahsante sana Mheshimiwa Lukuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Ardhi ya kuhakikisha Watanzania wanapata hati zao na kutatua hii migogoro inayojitokeza katika maeneo mbalimbali, napenda kushauri suala la elimu ya ardhi litiliwe mkazo. Watanzania lazima watambue haki na thamani ya ardhi yao. Hili limekuwa ni tatizo kubwa linaendelea kujitokeza hususan kwenye Mkoa wangu wa Iringa. Kumekuwa na wajanja wachache ambao wanafika kwenye maeneo ya vijijini na kuwashauri hawa wanavijiji kuwauzia haya maeneo, moja kwa bei ya chini na pili wengine wamediriki kuwashawishi hadi kuuza maeneo yao yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea hawa wanavijiji wanakosa hata maeneo ya kuzalisha mazao ambayo yanaweza kuwasaidia wao kuendelea kupambana na kukidhi mahitaji ya familia zao. Kwa hiyo, hili suala la elimu Mheshimiwa Lukuvi naomba tulipe kipaumbele sana. Hii elimu isitoelewe tu kwa wale wanakijiji lakini hata hawa wawekezaji wanaokuja kununua haya maeneo kule vijijini waambiwe kuwa wanapopewa yale maeneo wahakikishe hawa wananchi wanaachiwa eneo ambalo wataendelea kuzalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nakazania hii elimu? Tumesema tunataka Tanzania sasa iwe nchi ya viwanda na wote tulikubaliana kuwa hawa wakulima wadogo wadogo, hii asilimia 75 ambao wako kijijini wanaotegemea kilimo ndiyo wangetumia hiki kilimo kuzalisha raw materials ambazo zitapelekwa kwenye hivi viwanda. Kama haya maeneo yote yatakuwa yamebebwa na hawa watu chache, tutakapoanzisha hivi viwanda watakaonufaika ni wale ambao watakuwa na maeneo makubwa ya kuzalisha hizi raw materials na hii dhana nzima ya kuwasaidia hawa wakulima wadogo wadogo waweze kufikia ule uchumi wa kati itakuwa ni vigumu kufikiwa. Kwa hiyo, naendelea kusisitiza lazima suala la elimu lipewe kipamumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la hati miliki hasa hizi za kimila limechangiwa kikubwa sana na Wabunge hapa ndani na mimi ningependa niongezee. Naomba hizi hati miliki za kimila zipewe uzito na ziwe zinatambuliwa kisheria. Hata nchi za wenzetu zilizoendelea, mtu anayemiliki ardhi anapewa heshima kubwa na hiyo heshima inatokana na kuwa ile hati yake popote anapokwenda, hata kwenye hizi financial institutions anaweza kukopesheka lakini hapa nyumbani kwetu bado ni changamoto kubwa sana hususan kwa wanawake. Sisi ni asilimia kubwa hapa nchini, population yetu ni zaidi ya asilimia 51 lakini ni asilimia 19 tu…
MWENYEKITI: Ahsante, kwa heri, dakika tano zako zimekwisha mlikubaliana kugawana dakika na mwenzako Mheshimiwa Juliana Shonza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono hoja, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia siku ya leo. Kwa kuwa hoja iliyoletwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2016/2017 inagusa maslahi mapana ya wananchi wa Mkoa wa Iringa hususani wanawake ambao wameniwezesha kufika hapa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa Wabunge wanaowakilisha wananchi wa Mkoa wa Iringa. Sasa ndani ya huu Mkoa wa Iringa tunahifadhi kubwa ya Msitu wa Taifa wa Sao hill. Kwa muda huu niliopewa nina jambo moja kubwa ambalo nitalizungumzia, ni suala zima la TFS na utaratibu mzima wa utoaji wa hivi vibali vya kuvuna msitu wa Sao hill. Hili limekuwa ni tatizo kubwa sana. System nzima ya utoaji wa hivi vibali haieleweki. Vibali hivi vimekuwa vinawanufaisha wachache. Watanzania ambao ni wazawa, wavunaji wadogo wadogo, kundi la akinamama, vijana na walemavu hawapewi kipaumbele. Hawa wazawa ndiyo waliolima msitu huu, hawa ndiyo wameweza kuutunza huu msitu mpaka umefikia hapo ulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka Serikali inatoa cubic meter 600,000 kwa Watanzania waweze kuvuna msitu huu. Hapa ndipo nina tatizo napo na ndipo panaposikitisha. Watanzania hawa ambao ni wazawa hawanufaiki na huu mgao, ni wawekezaji ambao wanapewa kipaumbele kuweza kunufaika na huu msitu. Nitatoa mfano mmoja, tuna hawa Wawekezaji ambao wamepewa kuendesha Kiwanda cha Mgololo, wanajiita RAI-Group. Hawa ndio wamekuwa beneficiary wakubwa wa huu mgao wa vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii 600,000 inayotolewa na Serikali RAI-Group wanapewa cubic meter 250,000 na kinachosikitisha zaidi, hawa RAI-Group wanalipa nusu ya bei ambayo wanatakiwa kulipia vibali hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibali kimoja, Mtanzania, Mwanairinga, Mwanamufindi analipa sh. 28,000/=, RAI-Group wanalipa sh. 14,000/= tu. Sasa ukipiga mahesabu kutoka kwenye hizo cubic meter 250,000 wanazopewa, ukizidisha mara hiyo Sh. 14,000/= maana yake wanalipa bilioni 3.5 kwa mwaka. Sasa wangeweza kulipa hiyo Sh. 28,000/= ambayo Mtanzania wa kawaida analipa, Serikali ingeingiza bilioni saba kwa mwaka. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri anipe maelezo, ni vigezo gani wanatumia kuwapunguzia bei hawa RAI-Group na ni vigezo gani wanafanya hawa Watanzania waendelee kulipa hii Sh. 28,000/=? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nipewe maelezo ni kwa sababu gani hawa RAI-Group wanapewa kipaumbele? Wanapewa hizi cubic meter 250,000 wakati hawa Watanzania wa kawaida Wanairinga hawawezi kunufaika na msitu huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nipewe ufafanuzi wa ukusanyaji wa kodi kutoka kwa hawa wawekezaji wa hiki Kiwanda cha Mgololo. Cha kusikitisha zaidi hawa RAI-Group wanapasua haya magogo, wanatengeneza hizi raw materials wanapeleka Kenya, wanaenda ku-process makaratasi ndipo waturudishie sisi hapa kununua wakati haya makaratasi yangekuwa processed hapa Tanzania, tungetengeneza ajira kwa vijana wetu. Kwa hiyo, naomba majibu yanayonitosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa RAI-Group walishakuwa na Kiwanda Malawi, wamefukuzwa wamekuja hapa, sasa sisi tunawa-protect, moja tuwape vibali vingi, mbili bei ya chini, hii kweli inahuzunisha, inatukatisha tamaa sisi Wanairinga, inatukatisha tamaa sisi Wanamufindi, naomba tulifanyie kazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, hawa RAI-Group wapande misitu yao na kama bado wataendelea kupanda msitu huu wa sao hill basi walipe bei moja sawa na Watanzania. Hata kama wakilipa bei hiyo moja lazima hivi vibali vipunguzwe, viende kwenye makundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua asilimia kubwa ya wanawake na vijana sasa hivi wako kwenye hivi vikundi vya ujasiriamali. Tatizo la hivi vikundi ni maskini, havina pesa, hakuna miradi endelevu ambayo ingeweza kuwasaidia wao kuendelea kupambana na hizi changamoto zao za kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri angewawezesha hawa vijana, angewawezesha hawa akinamama katika Wilaya zote, Iringa Mjini, Iringa Vijijini, Kilolo na Mufindi waweze kutumia hivi vibali angekuwa; moja, amewainua kiuchumi; pili, hivi ndivyo vitakavyokuwa vikundi darasa vya kuwashawishi watu wengine waendelee kupanda miti kwa sababu watakuwa wameona matunda na benefits ambazo zinatokana na upandaji na upasuaji wa miti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa RAI-Group tunawapa vibali vikubwa. Hawajihusishi na mambo yoyote ya kijamii, barabara mbovu, madawati watoto wanakaa chini, kuna manufaa gani ya kuendelea kuwashikilia watu hawa wakati pale Mufindi tuna wavunaji wazuri wana viwanda, wamekuwa msaada mkubwa kuchangia madawati, kuchangia hospitali, hebu tuwape kipaumbele watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri please, doesn’t get me wrong. Najua ndiyo umepata kuongoza Wizara hii, so prove to me kuwa unakasirishwa na jambo hili, tuwapiganie Watanzania wetu waweze ku-enjoy matunda ya nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, after all Mheshimiwa Waziri tunasema tunataka Tanzania iende katika uchumi wa kati, Wizara hii ina nafasi kubwa ya kuwainua hawa wananchi, tuwawezeshe, tuwape kipaumbele hii ita-trickle down sasa tukiendelea kuwashikilia hawa RAI-Group tunawapa vibali cubic meter 250,000, hawa wengine hawanufaiki tutafikaje huko, lazima tuwaonjeshe matunda ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti sasa kwa kumalizia namwomba Mheshimiwa Waziri, najua yeye ni msikivu, he is competent. Naomba tufike Mufindi, hawa wavunaji wanajua matatizo ya hivi vibali, wanajua solution ya kuweza kutatua hili tatizo…
MWENYEKITI: Ahsante.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia tena siku ya leo. Naomba nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango na Naibu Waziri Mheshimiwa dada yangu Ashatu, kwa kuandaa na kuwasilisha bajeti hii elekezi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni ya kuungwa mkono kwa sababu kwa mara ya kwanza kabisa kama Waziri wa Fedha alivyosema asilimia 40 ya hii shilingi trilioni 29.53 inategemewa kujielekeza katika miradi ya maendeleo. Kama kweli bajeti hii itakwenda kama ilivyopangwa na kama kweli mipango na malengo tuliyoyaweka yatakwenda kama yalivyopangwa, basi Serikali hii ya Awamu ya Tano ina nafasi kubwa ya kubadilisha maisha ya Watanzania na kuwajengea tena imani ambapo tunatambua karibu watu milioni 10 wanaishi katika hali ya umaskini hususani wanawake, watoto na vijana wetu. Kwa hiyo, namuunga mkono sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niongelee suala la TRA, mimi binafsi naunga mkono TRA waende kwenye hizi Halmashauri zetu na kukusanya mapato haya. Naziomba Halmashauri za Mkoa wangu wa Iringa watoe ushirikiano wa kutosha na nina sababu zangu za msingi.
Moja, tunatambua kabisa Halmashauri zetu hazina watumishi na wataalam wa kutosha wa kuweza kukusanya mapato haya kwa wakati na kwa kiasi kinachotakiwa.
Pili, kama ripoti ya CAG inavyoonesha, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa na ufisadi ambao unaendelea kwenye hizi Halmashauri zetu na tunajua miradi mikubwa ya maendeleo kama vile zahanati na maji inategemea sana kodi ambazo zinatoka ndani ya hii Halmashauri yetu. Kwa hiyo, kwa hili mimi namuunga mkono Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ombi, Serikali ihakikishe inapeleka hizi pesa kwenye hizi Halmashauri kwa wakati na kwa bajeti ambayo itakuwa imependekezwa na Kamati ya Bajeti kutoka kwenye hizi Halmashauri husika. Vilevile ningeomba hii Ofisi ya CAG ipewe pesa ya kutosha, kwa sababu hii ndiyo macho na masikio ya Serikali yetu, ndiyo itakayoweza kuhakikisha pesa hizi zilizotengwa zinakwenda kufanya yale malengo ambayo yamekusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme machache. Najua nia na lengo la Waziri ni zuri. Naomba nishauri machache ili tuweze kuiboresha hii bajeti yetu kwa sababu na mimi lengo na nia yangu ni kuhakikisha Watanzania wanaishi vizuri. Kwenye ukurasa wa 39 wa hotuba Waziri alikiri kabisa kuwa huduma za afya na maji bado ni changamoto na akaenda mbali zaidi akasema upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama bado ni changamoto hususani majumbani na viwandani. Naomba nimkumbushe alisahau eneo moja nyeti la hospitali kwani hospitali zetu nyingi bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tukubaliane na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti, wao wameshauri tuongeze tozo ya Sh. 50 kwa kila lita ambayo itatusadia sisi kupata shilingi bilioni 250 na wakaenda mbali zaidi kusema shilingi bilioni 230 itakwenda kwenye miradi ya maji na shilingi bilioni 30 itakwenda kuboresha zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waziri wa Afya hapa anasoma hotuba yake alieleza kabisa kuwa hali ya zahanati bado ni mbaya na vifo vya akinamama na watoto bado vinaendelea. Mwaka 2010 watu 454 walikuwa wanapoteza maisha wakati wa kujifungua, sasa hivi 2015 ni watu 398 bado wanaendelea kupoteza maisha. Sasa hili ni jambo la kusikitisha si jambo la kujivunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wakati nachangia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii nilisema yafuatayo:-
Mkoa wa Iringa kuna hifadhi kubwa ya msitu wa Sao Hill. Serikali inapoteza takribani shilingi bilioni sita kwa mwaka na hii ni kuanzia mwaka 2007 na Mheshimiwa Cosato alilisemea hili pia. Kwa taarifa nilizopata jana, hawa wawekezaji wa RAI Group sasa hivi wanafanya lobbying Dar es Salaam kuhakikisha wanaendelea kulipa hiyo Sh.14,000 kwa cubic metre. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ahakikishe hao watu wa RAI group wanalipa fair share sawa na Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zahanati ziko katika hali mbaya, Wilaya yangu ya Kilolo hawana hata Hospitali ya Wilaya na wanahitaji shilingi bilioni 2.2 ili kuweza kukamilisha hospitali hii na nimesema tutapata shilingi bilioni sita kwa mwaka kutoka kwa hawa wawekezaji wa RAI group waweze kuchangia pato la Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wameweka imani kubwa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano, wananchi wa Iringa wana matumaini makubwa sana kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano. Sasa kama tutaendelea kuwabeba hawa wawekezaji na kuwatwisha mzigo Watanzania wanyonge, wauza mitumba, waendesha bodaboda, tukawaacha hawa RAI Group waendelee kuvuna matunda ya nchi hii kweli itatusikitisha. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha afuatilie kuhakikisha hawa RAI Group wanalipa fair share. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. (Makofi)

Awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Dada yangu Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla, mmekuwa mabalozi wazuri, kweli hilo jina linawafaa. Ni matarajio yangu Watanzania hasa wanawake na watoto wanatambua na wanajivunia mchango mkubwa ambao mnautoa kwenye Wizara yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niende moja kwa moja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 55 anasema: “Maendeleo endelevu ya Taifa lolote yanategemea uwekezaji katika makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 idadi ya watoto ni asilimia 51.6 ya Watanzania wote.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ambazo zimepiga hatua, zilifanya jitihada za makusudi kuhakikisha zinawekeza kwenye hii rasilimali watu. Kwa hiyo, kwa hotuba hii Mheshimiwa Waziri naungana na wewe kabisa kuwa ni jukumu letu kama Taifa kuhakikisha kuwa tunawatengenezea mazingira mazuri hii asilimia 51.6, kwa sababu tunasema tunataka Tanzania iweze kufika uchumi wa kati na hii ndiyo nguvu kazi ambayo itatusaidia kuweza kufika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utafiti ambao umefanywa na World Health Organization wakishirikiana na World Bank wanasema, Taifa kama tunataka kuhakikisha tunawekeza kwenye watoto umri ambao unafaa ni kuanzia mwaka sifuri mpaka miaka miwili. Sasa Mheshimiwa Waziri nikupongeze kwa kuleta takwimu hizi, imetupa picha kamili kuwa sasa ni zaidi ya nusu ya Watanzania ni watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ningependa turudi nyuma kwa kutumia huu utafiti na ushauri ambao umetolewa na World Health Organisation. Turudi nyuma sasa tujue katika hii asilimia 51.2 ni watoto wangapi wako kwenye umri wa mwaka sifuri mpaka miaka miwili, kwa sababu hii ni critical age ndiyo maana wamesema kama Taifa tunatakiwa kuanza kuwekeza hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunasema ni critical? Kama hotuba yako ambavyo inaonesha mortality rate ya watoto wa mwaka sifuri mpaka miwili ni kubwa sana, tunapoteza watoto 21 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa.

Pia umekiri kabisa kuwa udumavu ni tatizo kubwa sana kwa Taifa letu, tumekuwa na watoto ambao uelewa wao unakuwa ni mdogo sana. Tunajua kabisa tatizo la udumavu linafanya mtoto ashindwe kufikiri, kutunza kumbukumbu na hata kufanya maamuzi inawawia vigumu sana.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tuna kazi kubwa kama taifa kuhakikisha tunalinda hawa watoto wetu ili tuweze kufikia malengo hayo ya uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo kwa Serikali yatakuwa kama yafuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema hii age ya mwaka sifuri mpaka miwili ni critical na tunataka tuwe na watoto ambao wataweza ku-grasp hizi concept, sasa hivi kumekuwa na frustration. Mtoto anakwenda shuleni, mwalimu ameandaliwa na tumetengeneza miundombinu mizuri lakini watoto hawa bado wanashindwa ku-grasp hizi concept zinazofundishwa shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali na kama wizara naomba tupitie hizi sheria, tuzilete hapa ili tuweze kufanya mabadiliko na tunaweza tukaanza kidogo tu, hizi maternity leaves tunazipuuzia, tunasema zipo vizuri, hazipo vizuri, ukiangalia nchi ambazo zimeendelea kwa mfano, Scandnavian countries wanatoa kipaumbele kikubwa sana kwa wamama wajawazito, si ndiyo. Wengine wanapewa hadi siku 480 sisi hapa bado ni siku 120, siku hizi hazitoshi kwa sababu tunatakiwa kumlinda huyu mama ili aweze kumlea mtoto wake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze juhudi za Serikali za kuhakikisha tunatoa elimu kwa mama mjamzito juu ya lishe ya motto, lakini hii haitoshi tunatakiwa kwenda mbali zaidi. Tumesema kuna viwanda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja nitaleta mapendekezo yangu kwa maandishi. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu iliyoletwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Mheshimiwa Spika, tatizo la maji limekuwa ni changamoto kubwa kwa Taifa letu hususan, Mkoa wangu wa Iringa.

Mheshimiwa Naibu Spika, shida hii ya maji inamgusa mwanamke moja kwa moja. Wanawake wamekuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji badala ya kujitafutia maendeleo yao ya kiuchumi. Tatizo hili la maji si tatizo mjini tu, bali vijijini nao wamesahaulika kwa muda mrefu. Ili nchi yetu iweze kufikia malengo ya Tanzania ya uchumi wa kati lazima tuhakikishe hii nguvu kazi (wanawake) ambao ndio wazalishaji wakubwa tunawaondolea adha hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, naomba tuongeze tozo ya sh.50 kwa lita, ili tuwe na chanzo chenye uhakika. Kama hii haitawezekana, basi tupunguze kwenye other sources kama Road Funds na REA. Nina imani kubwa na Serikali na Wizara kuwa watapokea ushauri wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's