Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kuwepo katika Bunge hili. Haikuwa rahisi lakini kwa uwezo wake leo niko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati ya moyo wangu napenda sana niwashukuru wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi, kwa kuchagua kwa kura nyingi viongozi wanaotokana na CCM. Wamempa kura nyingi Mheshimiwa Rais, lakini wamechagua Wabunge wote wanaotokana na CCM, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niahidi mbele yako kwamba nitashirikiana na Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wanaotokana na CCM nikiamini kwamba wao wamechangia uwepo wangu katika Bunge hili. Ninaahidi kufanya nao kazi hasa zinazohusu akina mama usiku na mchana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabla sijaendelea kusema niunge mkono hoja, lakini nianze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Naomba nipongeze sana hotuba hii imekaa vizuri lakini kwa kuwa ni wajibu wetu kusema neno na mimi naomba niseme neno.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la shilingi milioni 50 za kila kijiji. Sote tunafahamu kwamba Mheshimiwa Rais wetu alitoa ahadi kwa wananchi wetu kwamba Mwenyenzi Mungu akimjalia kushinda katika nafasi hii…
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sikudhani, naomba ukae.
KUHUSU UTARATIBU......
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie kwamba miongoni mwa mabingwa wasemaji bila kusoma ni pamoja na mimi. Naomba nimhakikishie hilo na ili kuthibitisha naomba niendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuzungumzia shilingi milioni 50 ambazo Mheshimiwa Rais alitoa ahadi kwa wananchi wetu. Namuomba awe anaangalia ahakiki kama hapa nilipo sisomi ili kumthibitishia kwamba niko vizuri na sina shaka, nimepikwa nikapikika. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu wakati anaomba kura alitoa ahadi ya kutoa shilingi milioni 50 kila kijiji na mimi napongeza ahadi hii na sina shaka ahadi itatekelezwa na kwa bahati nzuri kwenye hotuba ya Waziri Mkuu imeelezwa. Kwa kuwa zoezi hili la ugawaji wa hizi pesa wamesema watahakikisha zinatolewa kupitia SACCOS na baada ya utaratibu huu kukamilika kinachofuata sasa ni utekelezaji. Nashauri kabla hatujafika kwenye hatua ya utekelezaji maelekezo yatolewe kwa wananchi wetu ya namna njema ya upatikanaji wa pesa hizi ili kusitokee mkanganyiko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo mbele ya Bunge lako kwa sababu hivi tulivyo hapa kule vijijini tayari akina mama wanaendelea kuchangishana pesa na kufungua akaunti. Inawezekana kabisa wakafungua akaunti lakini mwishoni mtu akajikuta hapati kile alichokusudia. Kwa hiyo, naomba yatolewe maelekezo wakati tunaingia kwenye utaratibu huo kila mmoja anajua vigezo gani vitatumika vya kutoa hizi pesa. Sina shaka na Serikali yangu, naamini watatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia pia masuala ya Mfuko ule wa TASAF. Mheshimiwa Waziri Mkuu atakubaliana na mimi kwamba jambo hili ni jema na kwa kweli linasaidia kaya maskini na kwa bahati nzuri wameelezea kaya ambazo zimenufaika na kiasi ambacho kimetolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama vile ambavyo tunahakiki watumishi hewa, naomba na katika eneo hili turudi tuhakiki wanufaika. Kwenye eneo hili kuna watu ambao wananufaika lakini siyo maskini kama vile ambavyo tumekusudia. Kwa hiyo, inawezekana kabisa jambo likawa jema lakini lisilete manufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Ofisi ya Waziri Mkuu kama vile ambavyo tunahakiki watumishi hewa basi na kwa upande wa TASAF kwa kuwa tumekusudia kusaidia kaya maskini, twende tusaidie kaya maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la ugawaji wa maeneo ya utawala. Kama nilivyosema kwamba mimi natokea Mkoa wa Ruvuma lakini naomba niizungumzie Wilaya ya Tunduru. Wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa Wilaya kongwe katika nchi hii, ina Kata 39 na Majimbo mawili. Tumezungumza kwenye vikao vyetu na tumeomba kupata Wilaya nyingine. Niombe kupitia ofisi yake wakati utakapofika basi waiangalie na Wilaya ya Tunduru kwa kuiweka katika mgawanyo ule wa kuongeza Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri huwa tunaongeza maeneo ya utawala kwa ajili ya kurahisisha kutoa huduma kwa wananchi wetu. Kwa dhati ya moyo wangu na kwa bahati nzuri Waziri Mkuu ni msikivu na naamini pale alipo Waziri Mkuu ananisikia, wakati utakapofika wataangalia na kuipa umuhimu Wilaya ya Tunduru. Wala hapigi story Mheshimiwa Waziri Mkuu pale ananisikiliza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la asilimia 10 ya mikopo ya wanawake na vijana. Kwenye eneo hili wachangiaji wamesema kwamba utaratibu wa siku za nyuma tulikuwa tunaziagiza Halmashauri zetu zitenge asilimia 10 kwa ajili ya kusaidia mikopo ya wanawake na vijana. Mimi naomba ukubaliane na mimi kwamba yako maeneo hayafanyi vizuri. Naomba sana sana tusisitize Halmashauri zetu zitenge hizi pesa kwa ajili ya kusaidia wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mengi ya kusema lakini naomba niseme mimi ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI. Wewe utakuwa shahidi, Kamati ya UKIMWI imewasilisha taarifa yake hapa, miongoni mwa mambo ambayo tumekuwa tukiyajadili kwenye vikao vyetu ni kwamba utaratibu wa uendeshaji wa Bunge hauna tofauti sana na utaratibu wa uendeshaji wa Halmashauri. Utakubaliana na mimi kwenye Halmashauri zetu Kamati hizi haziko kama zilivyo kwenye Bunge. Tulileta maombi kwako, tulikaa na wewe, nikubali inawezekana kabisa kabla sijawa Mjumbe wa Kamati pengine nilikuwa sijajua ugumu na tatizo kubwa lililopo la dawa za kulevya na UKIMWI lakini nilipokuja kwenye Kamati hii nimeona kwamba hili tatizo ni kubwa na Wajumbe wenzangu watakubaliana na mimi kwamba ni tatizo kubwa. Tumewasilisha hapa bajeti yetu, tutaomba Bunge liridhie kwa kile ambacho tumeomba na wakati utakapofika basi kitolewe kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba kwa heshima na unyenyekevu na tunaamini nyie viongozi mlioko mbele ni sisi ndiyo ambao tumewaweka na kiongozi msikivu ni yule anayesikia kilio cha watu anaowaongoza, tunaomba sana Kamati hii irudi kwenye mfumo uliokuwepo huko nyuma ambapo Wajumbe wa Kamati hii walikuwa wanapata nafasi ya kushiriki kwenye Kamati nyingine. Wanakuwa na nafasi ya kwenda kuzungumzia masuala ya barabara, maji, zahanati lakini leo sehemu kubwa sisi ni ku-deal na masuala ya maboksi ya condom, masuala ya dawa za kulevya na uingizaji wa vidonge hivi vinavyowasaidia wenye UKIMWI. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikuombe kwamba katika eneo hili, naamini wewe ni msikivu na Spika ni msikivu na wote nyie ni wasikivu na mmekaa hapo kwa ajili ya kusikiliza kilio cha watu mnaowaongoza na sio wengine ni pamoja na sisi Wajumbe wa Kamati hii, tuko tayari kufanya kazi. Kwa nafasi hii naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama lakini nimpongeze na Naibu wake wametupa ushirikiano sana, pale tulipowataka kwenye Kamati yetu wamekuja wametupa maelezo, niombe sana mliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini liko tatizo lingine la MSD. Tumefika sisi mpaka MSD wanadai pesa na inawezekana kabisa itafika wakati watashindwa kabisa hata kupakua mizigo bandaraini. Kuna pesa ambayo wanaidai Serikalini na kwa bahati nzuri Naibu Waziri wa Afya tulikuwa naye wakati tumeenda MSD na yeye aliahidi kwamba kile kiasi cha pesa kitatolewa. Niombe watekeleze ahadi yao ya kuwalipa MSD.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja. Nawatakia kila la kheri na kazi njema, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Wizara ya Ardhi mwaka 2011/2012 Bunge lilipitisha matumizi ya kuanzisha mabaraza ya ardhi na nyumba Wilaya ya Matano na Tunduru ikiwa ni mojawapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Baraza la Ardhi la Nyumba halikuanzishwa na Serikali kutokana na bajeti ya Wizara kwa muda uliopangwa. Ndipo Halmashauri kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ikafuatilia Serikalini mipango hiyo ya uanzishwaji wa Baraza. Jibu lililotolewa ni kwamba Serikali kwa sasa haina uwezo wa kuanzisha Baraza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kwamba wananchi wa Tunduru wanapata taabu ya kusafiri kilometa 264 hadi Songea kufuata huduma za baraza. Halmashauri ikaona ni vema itoe jengo miongoni mwa majengo ya Idara ya Ujenzi na samani japo chache ili angalau Baraza liweze kufanya kazi. Je, ni lini Serikal itaajiri Mwenyekiti wa baraza la Ardhi la Wilaya ya Tunduru? Kwa
sasa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Songea Mheshimiwa Norbet Ndimbo ndiye anaetembelea Baraza la Tunduru kila baada ya mwezi mmoja na mara nyingine miezi miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaajiri watumishi na wahudumu wa Baraza? Kwa sababu sasa kuna mtumishi mmoja Bi. Vumilia Chipasura anafanya kazi ya Uhudumu, Ukarani na Uchapaji. Ikiwezekana basi, hata huyo kibarua aangaliwe kama ana sifa aajiriwe na aongezewe watumishi wengine kwani amejitolea kwa muda wa miaka miwili sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Serikali ijenge jengo la kudumu kwa ajili ya Baraza la Ardhi badala ya kuazima jengo Halmashauri. Hii iendane na ununuzi wa thamani za Ofisi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukurasa wa 31 – 32 amezungumzia jukumu la kuanzisha na kusimamia Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kwa lengo la kutatua migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti ya Wizara ya mwaka 2011/2012 Bunge lilipitisha matumizi ya kuanzisha Mabaraza matano ya Ardhi na nyumba ya Wilaya na Tunduru ikiwa ni mojawapo. Hadi sasa Halmashauri imetoa jengo miongoni mwa majengo ya Idara ya Ujenzi na samani japo chache ili angalau Baraza lianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waziri anapohitimisha michango mbalimbali ya Wabunge naomba mambo yafuatayo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iajiri Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Tunduru kwa sababu kwa sasa mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Songea Mheshimiwa Norbet Ndimbo ndiye anayetembelea Baraza la Tunduru kila baada ya mwezi mmoja na mara nyingine baada ya miezi miwili. Hili halileti tija kwa wananchi wa Tunduru.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iajiri watumishi na wahudumu wa baraza; kwa sasa kuna mtumishi mmoja tu Bi Vumilia Chipasura, anafanya kazi kama kibarua, hajaajiriwa na anafanya kazi zote za uhudumu, ukarani na uchapaji, ikiwezekana hata huyo aajiriwe.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijenge jengo la kudumu kwa ajili ya Baraza la Ardhi badala ya kuazima jengo Halmashauri, hii iendane na ununuzi wa samani za ofisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kuwa si vizuri kuendelea kuanzisha mabaraza mengine ya ardhi na nyumba ya Wilaya ikiwa haya yaliyopitishwa na Bunge hayajakamilika.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia siku ya leo, na hasa katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani ambapo waislamu wote kote nchini wanatimiza miongoni mwa nguzo tano zile ni pamoja na kufunga Ramadhani. Namshukuru Mungu, nawatakia kila la heri wale wote ambao wamewajaliwa kutimiza nguzo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa dhati ya moyo wangu na kama sikusema haya hakika sitaietendea haki nafsi yangu, naomba binafsi nikupongeze sana kwa kazi nzuri unayoifanya. Kuna usemi wanasema usimdharau usiyemjua. Awali wakati unaingia kwenye nafasi hii nilipata shida sana kuona kweli Naibu Spika utamudu nafasi hii! Kwa kweli, umeitendea haki nafsi zetu, lakini umetufurahisha akinamama wenzako, hakika unatuwakilisha vizuri endelea kuchapa kazi tuko pamoja na wewe na Inshallah tunakuombea uendelee kuwa salama mpaka tarehe Mosi tunapomaliza kufunga Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana niwapongeze, Waziri wa Fedha na Naibu Waziri, wamewasilisha mpango mzuri na wametupa nafasi hata sisi Wabunge ya kuona nini kimeandaliwa katika bajeti hii. Naomba niwapongeze sana kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini yako mambo mengi yamezungumzwa mazuri. Miongoni mwa mambo mazuri lazima kuwe na changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie upande wa afya. Waheshimiwa Wabunge, wenzangu wengi wamezungumzia kuhusu ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, niwapongeze sana na mimi nakubaliana nao moja kwa moja, lakini mimi naomba sana nizungumzie suala la ikama ya watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuwa shahidi na Mheshimiwa Waziri anayehusika atakuwa shahidi kwamba tunalo tatizo la watumishi wachache katika Idara hii ya afya. Mimi niombe sana tuliangalie jambo hilo, kwa kuwa tunalo tatizo la hawa watumishi ni vizuri kupitia vile vijiji vyetu wako kule vijana ambao wamejifunza uhudumu wa afya, ni vizuri tukawaangalia wale kuwapa mafunzo, ili wawe wanasaidia kutoa huduma za afya kwenye zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiofichika, hata tukienda sasa hivi kwenye vijiji vyetu unaweza ukakuta mhudumu mmoja, huyo huyo ataandika cheti, huyo huyo atachoma sindano, huyo huyo ataenda kuhudumia kusafisha vidonda, kazi zote anatakiwa azifanye. Kwa hiyo, mimi binafsi niliona sana kulingana na muda huu mfupi nijikite sana kwenye eneo hili katika kuhimiza kupata watumishi wa afya kwenye vituo vya afya na zahanati zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naomba nilizungumzie ni suala la miradi ya maji. Tumekuwa tukizungumza sana kuhusiana na suala la miradi ya maji, siyo siri iko miradi ambayo tayari wananchi wetu wamekabidhiwa, lakini upo ukweli usiofichika kwamba, miradi ile mpaka sasa iko miradi mingine haifanyi vizuri, haitoi maji ipasavyo. Mimi naomba sana, kupitia Wizara husika, ufanyike uhakiki wa kuona ni miradi gani ambayo imekabidhiwa kwa wananchi, lakini haitoi maji ipasavyo kuona sasa hatua zichukuliwe katika kuhakikisha tunaifanyia ukarabati na wananchi wetu wanapata maji ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yamezungumzwa mambo mengi, lakini naomba pia nizungumzie suala la kupunguza tozo kwa wakulima. Kwenye taarifa yao wamezungumza na hasa kwenye suala la wakulima wa korosho. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mpango wake kwamba watahakikisha wanapunguza tozo mbalimbali kwa wakulima na mimi nakubaliana nao kwa sababu, zipo tozo ambazo zilikuwa zinawakandamiza sana wananchi wetu. kwa kuwa wameanza kupunguza baadhi ya tozo nasisitiza sana waendelee kuziangalia hizo tozo ambazo hazina maslahi kwa wananachi wetu, ni vizuri kuziondoa ili wakulima waone waone tija ya kile wanachokifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala zima la bajeti. Hapa tunazungumzia bajeti tumeweka mipango mingi ambayo tunakusudia tupige hatua, lakini kama hatujasimamia ukusanyaji mzuri wa mapato, mimi naamini haya yote tunayozungumza hayawezi kuzaa matunda. Mimi nasisitiza sana kwenye haya mambo ambayo tumekusudia kwenye hivi vyanzo vya mapato ni vizuri tuvisimamie ili hii miradi ambayo tunaikusudia ifanyike, ifanyike kwa jitihada na itafanyika vizuri kama kile ambacho tumekusudia kukikusanya kitakusanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala zima la bajeti. Hapa tunazungumzia bajeti tumeweka mipango mingi ambayo tunakusudia tupige hatua, kama hatujasimamia ukusanyaji mzuri wa mapato naamini haya yote tunayozungumza hayawezi kuzaa matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasisitiza sana katika haya mambo ambayo tumekusudia katika vyanzo vya mapato ni vizuri tuvisimamie ili hii miradi ambayo tunaikusudia ifanyike, ifanyike kwa jitihada na itafanyika vizuri kama kile ambacho tumekusudia kukikusanya kitakusanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie jambo…..

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja.

The Tanzania Fisheries Research Institute Bill, 2016

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na kuwepo katika kikao cha leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi kwanza napenda niipongeze Serikali yangu na Wizara husika kwa kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania 2016. Kwa nini nalazimika kuipongeza Serikali na Wizara? Ni kwa sababu nafahamu Muswada huu unalenga kuendeleza, kuongeza na kuboresha uelewa wa wakulima wetu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Muswada huu yamezungumzwa mambo mengi katika kufanya utafiti. Naomba nijikite kwenye suala la utafiti wa mbegu bora. Waheshimiwa Wabunge wengi jana wakati wanachangia wameeleza sana uwepo na mbegu bora za mazao ya chakula na biashara. Mimi mwenyewe nimewahi kutumia mbegu za mahindi ambazo zinaletwa na haya mashirika mbalimbali, cha kushangaza nilipanda kama heka 10 lakini shamba lote mahindi hayakuota.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inawezekana jambo hili lilinigusa mimi lakini pia liliwagusa wakulima wetu, mambo kama haya kwa kweli yanakatisha tamaa. Kwa hiyo, binafsi naamini kwa kupitia taasisi hii ambayo itafanya utafiti tutakuwa na mbegu bora. Miongoni mwa vitu ambavyo mimi binafsi nasisitiza ni kupatikana kwa mbegu bora ambazo hazitakatisha tamaa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutokuwa na mbegu bora maana yake tunawafanya wananchi wetu waendelee kutunza mbegu zile kwa teknolojia ambazo zimepitwa na wakati labda kwa kufutika mbegu kwenye moshi ili mwaka mwingine ikasaidie. Kwa karne hii ambayo tunakwenda nayo binafsi naona sio jambo jema. Kwa hiyo, nasisitiza sana katika eneo hili la utafiti tuzingatie upatikanaji wa mbegu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na jambo hilo pia naomba nisisitize suala la uhifadhi wa mazao. Wakulima watalima mashamba, watapanda mbegu na hatimaye watavuna. Katika eneo hili, wakati wakulima wetu wa mazao ya biashara na chakula wanasubiri soko mara nyingi Serikali imekuwa ikiwasisitiza wasiuze mazao yao. Katika kipindi kile ni wajibu wetu sasa kuwaelimisha njia bora ya uhifadhi wa mazao ili viwango na ladha ile isipotee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu nimeshuhudia tumekuwa tukiunda Bodi mbalimbali lakini mara nyingi hatuzisimamii. Mfano mzuri ni Bodi ya Korosho. Hivi karibuni tumefanya kikao cha wadau wa korosho Bagamoyo, kwa bahati nzuri Waziri mwenye dhamana alikuwa mgeni rasmi katika kikao kile, alizungumzia masuala mengi na changamoto zilizopo kwenye Bodi na Mfuko ule wa Wakfu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mwenyekiti wa Bodi amepata fursa ya kujibu maelezo ambayo mgeni rasmi aliyaeleza, alimwomba Waziri kwamba siyo vizuri kusubiri mikutano ya wadau, ni vizuri Wizara iwe inashirikiana moja kwa moja na Bodi katika kutatua changamoto zilizopo na kutoa ushauri. Kwa hiyo, nasisitiza katika jambo hili kwamba tunapounda hizi Bodi ni wajibu wetu kuzisimamia ili kubaini changamoto zilizopo na kuzitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Muswada huu pia tumezungumzia masuala ya uundaji wa Bodi na upatikanaji wa Wajumbe. Kwenye ile Bodi tumezungumzia upatikanaji wa wakulima kuwa wawakilishi kwenye Bodi. Kamati imependekeza kwamba kuwepo na wakulima wawili badala ya mkulima mmoja kama ulivyopendekeza Muswada. Hata hivyo, dada yangu Mheshimiwa Sakaya wakati analijadili hili na mimi binafsi nilipenda sana mchango wake alizungumzia kuhusu hizi Bodi na alifika mbali, alipendekeza kwamba Bodi hizi ni vizuri zikaenda Kikanda. Binafsi nilishawishika lakini baadaye nilipata shida nikasema tunaweza tukafika mahali tukaweka kikanda lakini kila kanda ina mazao mchanganyiko hatma yake tunaweza tukafika mahali sasa kila mwakilishi wa zao aingie kwenye Bodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nikubaliane moja kwa moja na mapendekezo ya Kamati kuwa badala ya yule mjumbe mmoja aliyependekezwa kwenye Muswada basi kuwepo na wajumbe wawili wakulima ambao wataingia kwenye hii Bodi. Sote tunafahamu kwamba kidole kimoja hakivunji chawa kwa kuingia wakulima wawili kutasaidia kutatua changamoto zilizopo. Hata hivyo, kubwa zaidi naomba tuangalie sifa za wale wakulima ambao wata…

MWENYEKITI: Ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's