Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Tauhida Cassian Galoss Nyimbo

All Contributions

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia toka Bunge hili lianze, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa na wananchi kwa kura nyingi. Pia nimpongeze Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia kwa kuteuliwa, imani yetu wanawake hatatuangusha maana tuna uhakika na kazi anazozifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa wakati huu nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Ali Shein kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi na kwa imani yake na Wazanzibari. Nasema nampongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa sababu ameonesha hakika yeye ni kiongozi na kiongozi wa kupigiwa mfano. Uvumilivu wake, utu wake, ubinadamu wake umefanya leo Zanzibar iwe ni nchi ya amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais huyu hakuwa kiongozi ambaye ni mchu wa madaraka, hakuwa kiongozi ambaye anashibisha tumbo lake, amekuwa kiongozi mwenye kuitakia wema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Ukimya wake kwa muda wote na maneno yote kwa muda wote aliokaa kimya lengo lake lilikuwa ni moja kuhakikisha Zanzibar iko salama, kuhakikisha Tanzania iko salama. Kama Rais alikuwa na mamlaka tosha na alikuwa na kila cha kufanya na alikuwa na aina ya sababu ya yeye pia kujitangaza lakini hakufanya hivyo, alitaka kwenda kwa utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Waziri Mkuu kwa kuteuliwa kwake na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Niwashukuru Mawaziri wote, imani yangu kwenu ni kwamba tutapiga hatua, hapa tulipo tutaendelea kusonga mbele. Tunaitegemea Tanzania mpya katika miaka mitano hii ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani zangu pia ziende kwa wapiga kura wangu ambao ni Wanawake wa UWT, Mkoa wa Magharibi. Nawashukuru kwa kunirudisha Bungeni na kuniamini kama mtoto wao naweza nikafanya kazi, nawaahidi sitowaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe kama mwanamke, ujasiri wako tumeuona na tumeona ukifanya kazi kama mwanamke ambaye hutuangushi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze moja kwa moja kwenye kuchangia. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, kwa bajeti yake nzuri aliyoileta na nipongeze kikosi kizima cha Jeshi la Wananchi wa Watanzania. Kazi zenu ni nzuri zinaonekana ndiyo maana ukaona watu wanapiga kelele, mngekuwa hamfanyi kazi watu wangenyamaza kimya lakini kwa kuwa mnafanya kazi ndiyo maana watu wakapata fursa ya kunyanyua midomo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na wananchi wake kwa ujumla, niwapongeze kwa kumrudisha kila siku Bungeni kwa mbwembwe. Hii yote inaonesha ujasiri wake na uwezo wake wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sura ya tisa katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri imezungumzia suala zima la maendeleo ya viwanda, kilimo na ajira kwa ujumla. Vijana tumaini kubwa liko kwake. Akitaka kujua kama Tanzania vijana matumaini yako kwake aone wakati unapofika wa kuchukua watakaojiunga na JKT au jeshi kwa ujumla. Vijana wengi huhangaika na nafasi hizi kwa sababu matumaini yao kama vijana wa Tanzania yako kwake. Nadhani ni vema wakashirikiana na Wizara ya Viwanda na Kilimo wakaona ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia vijana wa Tanzania. Naamini kwa kufanya hivyo tutaendelea zaidi kama vijana wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye suala zima la uchaguzi. Toka tulipoanza Bunge hili hoja kubwa na michango ya Wizara zote zilizochangiwa ni hoja ya uchaguzi wa Zanzibar. Uchaguzi wa Zanzibar umekwisha, Rais yupo, anatawala, tunaendelea kama kawaida. Sasa hizi kelele unaenda kumpigia Jeshi la Wananchi wa Tanzania amekufanya nini? Kwa sababu wanaposema wanadhani hawana uwezo wa kuingia humu ndani ili kujibu. Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeitendea haki Zanzibar. Kati ya vyombo ambavyo tunastahili kuvipongeza Tanzania ni pamoja na Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sikuwa na shida ya kuzungumza hapa, nazungumza kwa sababu jeshi hili halikumpiga mtu, halikumchapa mtu, halikumtukana mtu, halikufanya kitendo chochote cha kuweza kuzungumzwa kwenye Bunge hili. Jeshi lile limekaa Zanzibar kwa amani, limepita kwa mbwembwe, hivi jeshi linapita wewe unaogopa nini? Una masuala gani ya kukufanya uliogope Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Hebu tuambie hoja yako ya msingi juu ya Jeshi hili ni nini ili tuwapeni majibu ya uhakika. Toka Bunge lianze tumekosa jibu la kuwapa kwa sababu hatukuona suala la msingi juu ya masuala yenu mnayozungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi limekaa Zanzibar…
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa nane wa kitabu cha hotuba ya Waziri wa Jeshi la Ulinzi kimezungumzia suala zima la kuimarisha muungano, mlidhani muungano unaimarishwaje? Mlidhani ile kuoa na kuoana tu kunatosha kuimarisha muungano? Muungano utaimarishwa na Jeshi la Ulinzi. Mimi niwapongeze, kati ya mtu ambaye anajisikia ufahari mkubwa leo kusimama hapa kuziona zile kofia zipo pale mmoja wao ni mimi. Tunawapenda, fanyeni kazi na kila uchaguzi ukifika msimsubiri Waziri awapeni amri. Jenerali upo, viongozi wote wapo tunataka mshuke iwe kwa boti, iwe kwa ndege na kadhalika lakini muingie Zanzibar kufanya kazi. Hata uchaguzi ukirudiwa warudi, wakitaka kuja kesho waje, kitakachotokea tunakuombeni mje msisubiri amri, fanyeni kama wajibu wenu, fanyeni kama kazi zenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumzia mambo mengi kuhusu uchaguzi lakini tu tungependa kuwaambia kwamba uchaguzi pamoja na kwisha, kulikuwa na hoja zinazongumzwa na Tume, Mwenyekiti wa Tume alikaa kwenye TV zikachambuliwa kasoro, kila kitu kilichoonyeshwa kule, hamkuwa na hoja na ninyi kutafuta Kipindi mkajibu, mbona mlinyamaza kimya? Kama masuala mnayozungumzia kwamba document mnazo, mna ushahidi hata sisi document tunazo mpaka leo, kura mbili mbili zipo, saini wanaweka watu wawili wawili zipo, hakuna kilichokuwa hakipo! Mmebaki mnawinda lakini hayo mawindo yenyewe mnayowinda hakikisheni kwamba hayapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo yangu yalikuwa hayo machache, nakushukuru kwa kunipa fursa hii.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Waziri Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake Waziri Dkt. Kigwangalla, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya ndani ya Wizara hii. Pia nimpongeze Rais wangu aliyetokana na Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya katika Taifa hili la Tanzania. Wananchi wa Tanzania tuna furaha kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na kuwatendea haki Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ni kubwa, Dada yangu Ummy Wizara ni kubwa, kazi na majukumu uliyokuwa nayo ni makubwa, lakini haina budi ukiwa kama mwanamke mwenzangu nikupongeze kwa ufanisi mkubwa wa kazi na uwezo uliokuwa nao wa kazi, kuweza kumudu Wizara hii kubwa na Wizara ambayo imebeba watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumza watu wote, majigambo ya Wabunge, majigambo ya Makatibu Wakuu, majigambo ya waendesha boda boda yote yanategemea afya zao na umezibeba wewe dada yetu Ummy pamoja na kaka Kigwangalla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiache pia kuzungumza suala zima la afya kwa watoto. Mheshimiwa Waziri umelizungumza katika kitabu chako, umelizungumza na kuliongea kwa kina suala zima la afya ya watoto katika ukurasa wa tano, umelizungumza na umelitendea haki, ila dada yangu nikuombe ukiwa kama mwanamke kumbuka unapokwenda labour unapofikwa na uchungu. Unayoyafanya yote ni mazuri lakini wajibu wetu kukukumbusha kuna baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatupaswi kulaumu, tunapaswa kukuambia ili ukumbuke na kuangalia maeneo mengine. Unapokwenda labour mwanamke unaujua uchungu na dada yangu Ummy una watoto uchungu unauelewa. Watoto wamefikwa na janga kubwa linalowasumbua sasa la kubakwa, hatuna budi kama mwanamke angalia kwa jinsi ya pekee tatizo hili tunalitatuaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalizungumza Dada Ummy huwezi kulitatua peke yako, lazima kuna baadhi ya watu mshirikiane au Wizara mshirikiane. Lazima ushirikiane na Wizara ya Mambo ya Ndani, lazima ushirikiane na Wizara ya Katiba na Sheria. Dada Ummy ni nafasi yako kama mwanamke kaa nazo Wizara hizi muone tatizo hili mnalitatuaje. Leo kilio cha kila mwanamke ndani ya Nchi hii, ubakaji wa watoto na unyanyasaji wa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna njia nyingi za unyanyasaji wa watoto, lakini kwa sasa yenye sura ya pekee ndani ya Tanzania ni suala la ubakaji. Nimeambiwa jana Dada yangu Faida amesimama mpaka amefikia kulia, suala la ubakaji ni suala kubwa, Dada Ummy unafanya kazi kubwa lakini kaa na Wizara zingine hutalitatua peke yako na kulimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalizungumza hivi kwa sababu, Wizara hizi imefika wakati unapokwenda Mahakamani unaambiwa limekwama Wizara ya Mambo ya Ndani kwa maana polisi, lakini polisi ukifika ukifuatilia unaambiwa limekwama hatuna maelezo ya kutosha ndani ya Wizara ya Afya. Tulione suala hili linakwendaje na suala hili Dada Ummy linahitaji pia elimu ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wenzetu wengine hawafahamu kwamba mtoto unapompeleka ukamtia maji, tayari baadhi ya uthibitisho unaufuta kabisa. Inapaswa lazima kama mwanamke usimame na kutoa elimu ya kutosha ili tuone tatizo hili kama Serikali na kama viongozi tukiwa tuna nia moja na lengo moja ya kulitatua tatizo hili limalizike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 26, ulizungumza kwa makini na kwa kuitolea maelezo ya kutosha hospitali ya Muhimbili. Ndani ya mwezi mmoja uliokwisha nilikuwepo Muhimbili kwa muda wa siku tatu, ilinibidi nikae pale. Panapostahili sifa binadamu apewe sifa. Mmefanya kazi kubwa lakini naamini kazi hii anayewatia nguvu na kukuwezesheni ni Mheshimiwa Rais. Inapofika wakati kama viongozi tusiwe wingi wa kulaumu tukakosa kushukuru. Unapoizungumzia hospitali ya Muhimbili uwe umekwenda umefika. Kuna tofauti kubwa ya nyuma tulipotoka na sasa hivi, lakini kwa sababu kuna baadhi ya watu nilipoenda, nilifanya kazi nikiwaona nisiache kuwataja kwa majina, lazima niwasifie. Kiongozi unapopata muda, posho tunayowalipa haitoshi kwa madaktari lakini basi...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kuunga mkono hoja, ingawa nimeambiwa nina dakika kumi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii kwa kuchangia Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa na jitihada yao wanayoifanya, kwa kweli sisi kama Watanzania tunaiona wenyewe kwa macho. Kinachonifurahisha na kuniridhisha zaidi ni kwamba Mawaziri wote wawili ni wanawake. Mara nyingi wanapofanya kazi wanawake mimi kama Tauhida huwa najisikia ufahari mkubwa lakini hatuachi kusema mambo madogo madogo ili waweze kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mimba kwa watoto wa kike linahitaji umakini kwenye kutoa uamuzi. Ukiangalia suala hili kwa pande zote mbili kwa hoja zinazojengwa basi kila mmoja ana tafsiri yake. Naamini kwamba Waheshimiwa Wabunge ni watu makini na watatoa maamuzi sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye ukurasa wa 28 na 29 wa Taarifa ya Kamati, kuna sheria zinazomhusu mtoto wa kike, naomba ziangaliwe na zifanyiwe kazi. Nasema zifanyiwe kazi kwa sababu sheria ambayo ilitakiwa iletwe ni anayempa mimba mtoto wa kike kuwekwa ndani. Imani yangu ni kwamba atakayempa mimba mtoto wa kike akiwekwa ndani nina uhakika kwamba suala la mimba kwa wanafunzi litakoma au suala la mimba kwa watoto wa kike litakoma kwa sababu mtiaji mimba ataogopa kuwekwa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kwamba ifike wakati kama wananchi na Watanzania tukubaliane kwamba mtoto wa kike anatakiwa apewe elimu ya kutosha, tusiwe watu wa kufumba maneno. Suala la kufumba maneno ndiyo limetufikisha hapa leo kutokubaliana.

TAARIFA...

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mchengerwa kwa ufafanuzi na maelezo mazuri, nayakubali kwa kuwa mwanasheria ametoa jambo la ziada zaidi kutukumbusha, naikubali taarifa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Mheshimiwa Waziri amesikia kwa sehemu, naomba aweke mkazo kwenye maeneo hayo, yeye ni mama, ni mwanamke, hatupendi kuwa na Taifa wanawake wakakosa fursa ya kufanya kazi, kwa sababu tu ya hali ambayo wao hawakupendezewa nayo na wala hawakukubaliana nayo. Umri mtoto anaopata mimba ni mdogo, anarubuniwa, nafikiri ni wakati wa kulishawishi Bunge hususan wanawake wenzangu tuliotoka kwenye Viti Maalum kwamba tuje na mikakati ya makusudi na sheria za makusudi, mtoto mwanamke atafutiwe jinsi ya kulindwa aendelee na masomo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiamue kwa utashi tu, tusifikie wakati tukaamua bila kujua nini athari yake mbele. Ningeridhia sana kama ingekuwa bakora hii na sisi tuliokuwemo ndani ingetukamata. Nazungumza kama ingetukamata kwa sababu watoto wengi wanaothiriwa na hili ni watoto wa vijijini, watoto wa kimaskini. Nazungumza hivi Mheshimiwa Waziri kwa kuwa tunaishi mitaani tunaelewa nini kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtoto yeyote wa mtu aliyepo humu ndani, tena namshangaa baba yeyote anayesimama humu ndani akadhani kwamba hakielewi kinachoendelea kule nje. Mtoto anayepata fursa ya kusoma ni mtoto wa mwenye pesa, ndio anayepata fursa ya kusoma, tufikie wakati tuwafikirie na walioko chini. Nazungumza mtoto yoyote wa mwenye pesa akishika ujauzito, ikifika mwezi mmoja au miwili anaenda kutolewa mimba kimya kimya inapita, baba ndani ya nyumba yake haelewi mtoto wake kama katolewa mimba maana haugui lakini isitoshe mtoto huyo huyo atatafutiwa shule ya mbadala kwenda kusoma. Inaniwia vigumu kutokuitendea nafsi yangu haki, nataka apewe fursa mtoto wa kike kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, kwangu mimi ni kigezo Wabunge wangapi wa kike humu mnaendelea kusoma. Wabunge mmebeba mimba zaidi ya tano ya sita mmezaa na mnakaa na waume zenu. Tuwatafutie mustakabali watoto wa kike tunawafanyaje, tunawasaidiaje? Huwezi kuwa Mbunge wa Viti Maalum uliyeteuliwa na wanawake wenzio… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's