Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Zainabu Nuhu Mwamwindi

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, tingatinga letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nianze kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu walivyoanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mungu mwenye rehema ambaye ametuwezesha leo na mimi Zainabu Mwamwindi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano nawakiilisha wazazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Ni hotuba ambayo ilikuwa ina mashiko mazuri na makubwa sana, ni hotuba ambayo ilisheheni kila kitu na ni hotuba ambayo siyo tu kwamba sisi Wabunge wa CCM ndiyo tunaipongeza au tunasema kwamba ilikuwa ni hotuba nzuri bali ndiyo ukweli uliojitokeza siku Mheshimiwa Rais alipokuja kutufungulia au kutuzindulia Bunge letu la Jamhuri ya Muungano. Hotuba hii siyo sisi tu, hotuba hii kuanzia wale wengi wanaoishi vijijini waliipongeza sana. Pia wasomi baadhi yao waliipongeza hotuba hii lakini na wale ambao wanaishi mjini nao pia waliipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwenye macho haambiwi tizama na mwenye masikio haambiwi sikia, Mheshimiwa Magufuli Watanzania kumchagua hatukufanya kosa. Pia niseme tu kwamba Watanzania kukichagua Chama cha Mapinduzi ndiyo usahihi wenyewe, ni chama
ambacho wamekiona kina sera nzuri, Ilani inayotekelezeka lakini pia ndiyo Chama kinachosema ukweli, hilo ni sahihi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Katika hotuba yake, aliongea kwa uchungu na Wabunge wengi wamechangia sina sababu ya kurudia lakini niseme yako mambo muhimu ambayo alikuwa ameyakazia sana, alikazia sana suala la maji.
Kule Tosamaganga, Kata ya Kalenga ambayo ina vijiji vitatu na vitongoji sita ule mradi wa maji ni wa mwaka 1974 miundombinu imechakaa. Nitoe ombi kwa Serikali ya CCM, Serikali sikivu, Serikali ambayo ina huruma na wananchi isaidie mradi huu. Tosamaganga ni sehemu ambayo imetoa viongozi wengi sana ambao wanalitumikia taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1974 wakati mradi wa maji unawekwa kule Tosamaganga ulizingatia uwepo wa watu waliokuwepo kwa wakati ule. Sasa Tosamaganga imekuwa na idadi kubwa sana ya watu hivyo maji hayatoshelezi kutokana na wananchi kuongezeka kwa kiwango kikubwa. Tosamaganga pia ina shule nyingi sana ambazo watoto wanasoma pale. Imezungukwa na mito lakini kuna mlima mkubwa, watoto wanashuka kwenda kufuata maji kule wengine wanatumbukia. Hivi karibuni amekufa mtoto mmoja wa kiume anaitwa Onesmo kwa sababu alikuwa amekwenda kufua siku ya Jumamosi, kwa bahati mbaya nguo yake ikateleza kwenye maji wakati anaifuatilia akazama kwenye maji. Kwa hiyo, bomba za Tosamaganga pamoja na vijiji vyake maji hayatoki kabisa. Kwa hiyo, namuomba Waziri wa Maji uiangalie Tosamaganga kwa jicho la huruma, maji yale hayatoshelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikuombe Mheshimiwa Waziri, kule Unyangwila na Irangi, wale watu wameanza wao kwa nguvu zao kuchimba mtaro kwa ajili ya kutafuta maji na wameshafikisha kilomita tatu na nusu lakini hawajui watapata wapi mabomba na maji kwenda
kuyafikia ni kilomita sita na nusu. Mheshimiwa Waziri nakuomba katika ufalme wako iangalie Tosamaganga na Kalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati akiwa Mbunge Marehemu Dkt. William Mgimwa, alikuwa ameahidi kupeleka gari la wagonjwa katika Hospitali ya Ipamba, ni Hospitali Teule ya Wilaya ya Iringa. Hospitali ile ni kubwa kwani inatoa huduma kwa wananchi wanaotoka maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Iringa na pengine hata Mikoa ya jirani lakini cha kusikitisha hakuna gari la wagonjwa. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, hebu tazama Hospitali Teule ya Ipamba ili waweze kupatiwa gari la wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara yangu ya kwanza leo nimeshuhudia Mbunge akilidanganya Bunge Tukufu. Mbunge wa Iringa Mjini amesimama hapa kwa kujiamini kabisa, akizungumzia habari ya Iringa Mjini yeye kama mwakilishi wa wananchi wa Iringa.
Amezungumzia mradi wa maji wa Iringa Mjini na kujidai kwamba Iringa Mjini maji yanapatikana kwa kiwango cha asilimia 98 lakini akasema Iringa kuna barabara za lami, akaenda mbali zaidi akasema taa Iringa Mjini zinawaka bila shida barabarani. Mheshimiwa Mbunge
amelidanganya Bunge lako Tukufu. Naomba tumwogope Mungu, Mchungaji Msingwa ni Mchungaji na nafikiri ana hofu ya Mungu lakini anapozungumzia vitu hata anaposema tunajikomba ndiyo tuna haki sisi tumsifu Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Iringa Mjini mpaka sasa maji ni asilimia 95, ni mradi ambao ulianzishwa na Mheshimiwa Monica Mbega wakati wa kipindi chake na hata wakati wa uzinduzi wa mradi huu alikuja Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne. Mbunge wa Iringa Mjini, Mheshimiwa Peter Msingwa hakushiriki katika uzinduzi wa mradi huu kwa sababu mradi huu alikuwa hautaki na hakuukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la barabara vilevile Mheshimiwa Msigwa amezikuta barabara za lami zikiwa tayari zipo. Ni mradi uliotoka Serikali Kuu na siyo yeye. Taa za barabarani ni package ya mradi wa barabara…
NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa Mwamwindi naomba ukae.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ZAINAB N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kukushukuru wewe mwenyewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia leo katika Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye ameniwezesha leo nami niweze kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli; nampongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu; nampongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na timu yake yote ya Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo wanatukonga nyoyo zetu Watanzania, wametuonesha umahiri wao na kwamba wana ari kubwa ya kulitumikia Taifa na wananchi wote wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna moja au nyingine, naitumia nafasi hii pia kuwashukuru wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia mimi uwepo wangu au wamerahisisha mimi Zainab Mwamwindi kuwepo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Nawashukuru kwa namna ya pekee na nasema Mungu awabariki sana, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inahitaji kwenda kwa kasi na ari kubwa. Tunasema tunahitaji Tanzania yenye viwanda. Kilimo kinatajwa kama uti wa mgongo wa nchi yetu na kinatajwa kwa sababu ya kwamba hakuna hata mmoja kati yetu Wabunge wa Jamhuri ya Muungano ambaye hatujui kwamba bila kilimo nchi haitasonga mbele. Ni lazima tulime na tuweze kupata mafanikio mazuri, lakini pia ndoto yetu ya kuwa na viwanda vingi itatokana na uzalishaji mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea Mkoa wa Iringa. Mkoa wa Iringa kuna Kiwanda kikubwa cha Karatasi cha Mgololo. Kiwanda kile kinazalisha karatasi, lakini namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho yake, atueleze au awaeleze wananchi wa Tanzania kwamba ni kwa nini Kiwanda cha Mgololo kinachotengeneza karatasi soko lake halipo lakini pia karatasi zake hazipatikani sokoni na hata kama zitapatikana, karatasi zake huwa ghali sana? Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Mwijage naomba atusaidie sisi wananchi, ni kwa nini Tanzania hii tunatengeneza karatasi lakini kwa bahati mbaya sana karatasi zile zikipatikana bei inakuwa ghali kuliko zile ambazo zinaingizwa kutoka nchi za nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la kinu cha kusindika au kusaga sembe kilichoko Manispaa ya Iringa. Ni kiwanda ambacho kinasaga sembe. Inawezekana kikawa ni kiwanda pacha, kinahusiana na kilimo vile vile. Kiwanda kile kilikuwa kinafanya kazi vizuri sana huko nyuma wakati wa NMC lakini mara baada ya Shirika la NMC kufa, kiwanda kile sasa kimekuwa hakifanyi kazi kama ambavyo inatakiwa. Pia kuna vijana wetu na akinamama pia wapo ambao nao walikuwa wanapata ajira na wengi wao wakiwa ni akinamama ambao ndio wanaotunza familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana, naomba Mheshimiwa Waziri, atusaidie katika kiwanda hiki, Serikali iweke mkono wake kwa asilimia mia moja ili iweze kuwakomboa wananchi wa Mkoa wa Iringa ambapo wananchi wa Mkoa wa Iringa hasa ni wakulima wa mazao ya mahindi, wanazalisha mahindi kwa kiwango kikubwa sana, lakini mara nyingine tunakosa soko la kupeleka mahindi, tukauze wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, Serikali itie mkono wake kwa asilimia mia moja katika kiwanda kile ili tuweze kukuza ajira kwa vijana wetu, lakini pia wakulima wa Mkoa wa Iringa na mikoa jirani waweze kunufaika na kiwanda kile kwa kuuza mahindi yao pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mama. Vazi la mwanamke yeyote wa Kitanzania ni Kanga. Namwomba Waziri wa Viwanda atusaidie sisi wanawake wenye maumbile kama mimi, tumekuwa sasa hatuvai kanga, kwa sababu Kanga zinazidi kuwa ndogo siku hadi siku na akinamama wamenituma nije niseme katika Bunge lako hili. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, kanga zilizopo sasa zinatosha kuvaa wasichana wadogo na Tanzania hii wanawake wameshiba, wako vizuri, wanahitaji kuvaa kanga wapendeze watoke katika shughuli mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, hilo aliwekee kipaumbele sana maana wanawake ndiyo jeshi kubwa na tegemeo la Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ni mara yangu ya kwanza leo kuchangia, naomba kusema naunga mkono hoja ya Waziri wa Viwanda na Biashara. Nasema ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inahitaji kwenda mbele kwa kasi. Ni jambo linalofahamika duniani kote kuwa tofauti muhimu ya nchi tajiri na masikini ni uzalishaji bidhaa za viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kimetajwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu; kilimo hakiwezi kustawi bila ya viwanda. Wakati Serikali imelivalia njuga suala la viwanda hapa nchini, naomba kuishauri Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kutazama nyuma wapi tulikwama kama Taifa na wapi tulipo na changamoto ipi tunazokabiliana nazo. Kwa mfano, mimi nimetoka Iringa ambako kuna kiwanda kikubwa cha karatasi kilichopo Mgololo Wilayani Mufindi. Namwomba Waziri wakati wa majumuisho anisaidie kuwaeleza Watanzania, ziko wapi karatasi za Mgololo katika soko? Kwanini zikipatikana bei yake huwa ghali kuliko karatasi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinu cha kusaga unga Iringa Mjini kilikuwa chanzo muhimu cha ajira na soko la uhakika la zao la mahindi Mkoani Iringa na mikoa jirani. Mheshimiwa Waziri pamoja na kuwa na ulinzi, kinu hicho kipo katika sekta pacha ya kilimo na viwanda, tunaiomba na kuishauri Serikali kuhakikisha kuwa kinu hicho kiwe katika asilimia mia moja ya uzalishaji ili kukuza ajira na uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake amebainisha kuwa Sekta ya Viwanda ni msingi wa maendeleo wa Sekta ya Kilimo umetueleza kuwa asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo sana na viwanda vidogo Iringa kama ilivyo baadhi ya Mikoa nchini kama vile Tanga, Morogoro na kwingineko, kuna uzalishaji mkubwa wa matunda ambayo mengi huishia kuoza mashambani kwa kukosekana kwa viwanda vidogo vya kati katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kuhusishwa kwa viwanda vidogo hasa katika maeneo ya uzalishaji ni ukombozi mkubwa kwa wakulima ambao wengi wao ni wanawake. Ufufuaji na uanzishaji wa viwanda utakuwa na maana endapo Wizara husika itaweka vipaumbele, kwani mwisho wa siku tunachotaraji ni kuwepo kwa viwanda vyenye tija. Tunapofufua kiwanda cha mbolea tutakuza ajira na kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima na kuongeza uzalishaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiona ari na hamasa kubwa aliyonayo Mheshimiwa Waziri ya kuhakikisha kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana. Wanawake wa Tanzania vazi lao ni khanga, naomba kushauri kwamba kifufuliwe Kiwanda cha Mutex na Urafiki.
Viwanda vilivyopo vimesababisha wanawake wengi sasa hawavai khanga kwa sababu ukubwa wa khanga kiurefu na upana ni mdogo sana. Namtakia kila la kheri Mheshimiwa Waziri na timu yake Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. ZAINAB N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu na Makatibu wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni barabara itokayo Iringa Mjini kwenda Ruaha National Park. Barabara hii ni muhimu sana kwa watalii, naomba ipewe kipaumbele kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, natanguliza shukrani.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyeniwezesha na kunipa afya njema na uzima wa kuniwezesha leo hii nichangie kwa maandishi katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii ni moja ya sekta muhimu sana na kwa hakika ni sekta ambayo ikipewa msukumo wa nafasi ya kipekee, italiongezea Taifa letu fedha nyingi. Mbuga zetu za hifadhi ambazo ni vivutio vya watalii zinahitaji kuwekewa mazingira mazuri ambayo yatawavutia watalii, naomba nitoe mifano miwili ya mbuga za Ruaha na Saadani, barabara ya kutoka Iringa Mjini kwenda Mbuga ya Ruaha siyo ya kiwango cha lami, na vivyo hivyo barabara itokayo Tanga kwenda Pangani hadi Saadani ni mbuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii naiomba Serikali iangalie kwa jicho la kipekee kama biashara nyingine zilivyo na ushindani, Serikali iongeze kasi katika kuutangaza utalii wetu. Bodi ya Utalii ishirikiane na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kufanya jitihada hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa hotuba nzuri yenye kuonesha mwelekeo, nampongeza pia Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara na nawatakia kila la kheri, wasonge mbele na kasi hii ya hapa kazi tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja mia kwa mia.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's