Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. James Kinyasi Millya

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya watu wa Simanjiro, kwanza kwa sababu nasimama mara ya kwanza niwashukuru sana kwa kunichagua na kunipa heshima ya kuwa Mbunge wao na kusaidia kuwaondolea kelele hapa Bungeni. Mimi namshukuru Mungu sana kwa hilo na nawashukuru kwa ajili ya heshima waliyonipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Frantz Fanon wakati fulani alinukuliwa akisema haya, nanukuu kwa kiingereza; “every generation out of relative obscurity must find it’s own mission and either fulfill it or betray it.” Kwa tafsiri isiyokuwa rasmi sana kwamba kila jamii kwa wakati fulani lazima ikubali kutafuta njozi yake na labda waamue kuikamilisha au kuikataa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la nchi yetu ni kubwa na tatizo hili kwasababu limetokea CCM wakati fulani si lingine bali ni unafiki na uongo. Unakuta viongozi wanaotegemewa na Taifa hili wanaongea uongo kwa sababu ya kujipendekeza, nilishindwaga mimi, nilishindwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasemahaya? Ugonjwa huu ni mkubwa kwa sababu unakuta makada ninaowafahamu kwa majina wanajaribu kujivua u-Membe, wanajaribu kujivua u-Lowassa kwa kujipendekeza na Serikali iliyoko madarakani wanawaacha wananchi wanateseka hawasemi ukweli. Huu ugonjwa ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mifano michache wengine wanasema nisitaje lakini kwasababu sitaki kuwa mnafiki, alikuja Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba, ugonjwa huu ni mkubwa. Katoka kwa wananchi akatetea Katiba nzuri, iliyotoka kwa wananchi kwa mapendekezwa ya wananchi baadaye alipoguswa mahali na CCM akakana matokeo ya wananchi, ni unafiki mkubwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili ni kubwa na kama viongozi hatutapona katika hili nchi hii itaenda pabaya. Ninamkosa Baba wa Taifa kama Nyerere, kama Sokoine ambao wakisimama kwa ukweli, watasimamia hiyo kweli na hiyo kweli itawaweka huru milele. Nimewakosa watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye hoja za madini. Sisi watu wa Simanjiro tuna madini ya Tanzanite, kwa miaka mingi sana ukienda Naisinyai, kuienda Mererani – Simanjiro watu ni maskini kweli kweli. Eneo lenye watu karibu 50,000 Mererani na Naisinyai hawana maji, Tanzanite ipo pale, wanachukua wazungu, wanachukua wazawa, watu wetu wanaachwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, Mheshimiwa Profesa Muhongo ninakuheshimu sana na unajua, nikuombe hata kutokana na yale ambayo yanasemekana si hasara, corporate social responsibility, tusimamie, watu wetu wanaumia sana, wanaonewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa leo hii niongee kwa masikitiko makubwa. Tulikuwa na mgodi mkubwa unaoitwa Tanzanite One, hata Kamati imegusia na kwenye taarifa mbalimbali ipo. Mgodi ambao Serikali ni mbia, STAMICO na mwekezaji uliuzwa kiholela na mimi najiuliza kama Mbunge na ningeomba nipate majibu wakati unakuja kuhitisha hotuba na hoja yako; hivi mgodi ule na ubia ule ulipatikanaje kwa Kampuni ya Sky Associates ambayo nimeaminishwa na najua kwenye maandiko si Kampuni ya Tanzania, wametokea wapi watu hawa? Je, tender hii ilitangazwa lini ili watu wote wa-compete fairly halafu wapewe. Sky Associates kama alivyokuwa anasema Dkt. Mwakyembe kuwa wakati fulani aki-present hoja yake ya DOWANS hii ni kampuni ya mfukoni, ni ya watu wachache waliotengenezewa ulaji na baadhi ya Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa, sintachelea kusema Simbachawene anahusika kwenye hili. Kampuni hii leo hii inanyanyasa wananchi wote, wachimbaji wadogo naomba niwataje kwa majina, Simbachawene amesainije mkataba kampuni iingie kwenye ubia na Serikali lakini hakuna mtu alieshindana naye? Eti walitangaza kule London Stock Exchange, Watanzana wangapi wangeweza kuona London Stock Exchange? Leo wachimbaji wadogo wanaonyanyaswa kwenye mkataba huo, Mathias Mnama, Sunda, One, Olomi, Mwarabu na mwingine kapoteza maisha kwa sababu ya mitobozano. (Makofi)
Mheshimiwa Profesa, wewe uliunda Tume wakati fulani, Tume mbalimbali zimeundwa kwa ajili ya mitobozano huko ardhini lakini bahati mbaya kuna Tume yako wewe, kuna Tume ya Dkt. Kipokola, kuna Tume ya Jenerali Mboma, wachimbaji wadogo wanaonewa na mgodi huu kwa muda mrefu.
Ninaomba kwa mara ya kwanza unisaidie kama Mbunge na unisaidie kama mwananchi mwakilishi wa wananchi wengi wanaotaka kunufaika na mgodi wao. Hawa Sky Associate waundiwe tume, ni wezi, hawanufaishi Simanjiro. Ninakuomba, wanaiba madini, wananunua mpaka Maafisa wetu wa Serikali, wengi! Naomba Mheshimiwa Profesa utusaidie kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine; Mheshimiwa Profesa madini yanaibiwa kila siku na kampuni hii. Na bahati mbaya, mimi nimeahidi mara nyingi nitakuwa mkweli mpaka nitakapokufa. Wanapata wapi kiburi cha kufukuza wafanyakazi 201 halafu wamewafukuza, baada ya kuwafukuza wanawapeleka mahakamani hawajawalipa mafao na sheria za kazi zinajulikana, bahati mbaya mama yetu Mhagama naye anatajwa humu ndani kwamba ni shemeji wa mmoja wa mbia wa hapo. Dada anaitwa Asia Gonga ameolewa na Martin Mhagama au Yusuph Mhagama, sasa sijui….
TAARIFA...
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba ukoo wake ni mkubwa na mimi ni kwamba nimepata taarifa. Nimetaja taarifa tu kwamba anatajwa. Angesema tu mimi huyo sihusiki naye, simple. Lakini watu hawa wanapatiwa kiburi na nani? Wanafukuza Watanzania halafu sekta yako inayosimamia wafanyakazi haiwasaidii, kwa nini nisihusishe jina hilo na jina lako? (Makofi)
Baada ya kusema haya mgodi huu tunataka tunufaike nao. Madini haya yamechukuliwa kwa muda mrefu lakini kampuni hii ya kitapeli iondolewe mara moja, Wanasimanjiro na Mheshimiwa Waziri nikuombe ukutane na wananchi hawa ukutane na wachimbaji wadogo usikie kilio chao. Tanzanite kwa mara ya kwanza na EPZA, kwa nini msijenge EPZA, madini yetu yanatoroshwa kila siku. Tumeto aeneo kama Simanjiro, liko eneo la EPZA, mnachelewa kulijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba kuwasilisha. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi naomba nichangie haya yafuatayo:-
(a) Mashamba pori na kutapeli ardhi ya watu ambao hawakuridhia; na
(b) Makazi, ujenzi wa NHC na tatizo la mishahara midogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba pori na ulaghai kupitia Wenyeviti. Kuna mashamba pori Simanjiro naomba utusaidie kwani wananchi wanateseka na mifugo yao na hivyo kusababisha migogoro kati ya wananchi na mbuga za wanyamapori (National Park). Shamba Namba 24 linasumbua wananchi wa kijiji cha Lobosoit „A‟. Mheshimiwa Waziri anafahamu tatizo hili na tayari maelekezo yale tumeshaanza kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa zaidi ya miaka mingi shamba hili halitumiki na halilimwi na juzi kwenye Kikao Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Bwana Brown Ole Suya alileta barua ya kubatilisha matumizi ya ardhi kutoka kwenye kilimo na mifugo kwenda mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba siyo suala la mazingira na wananchi wa kijiji cha Lobosoit “A”, siyo tu hawakumpa mtu huyu hiyo ardhi ya kilimo na mifugo lakini hawapo tayari ardhi yao ihalalishwe ili mtu huyu aiuze ardhi hii kwa wageni (wazungu).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenyeviti wa Vijiji Simanjiro ambao sio waaninifu wameuza ardhi ya wanakijiji bila ridhaa yao na hili limepelekea mpaka wao kupata hati miliki. Waliomilikishwa kimakosa wamepewa mpaka hati miliki na Wizara ya Ardhi. Tutasaidikaje ili wale Wenyeviti wa Vijiji ambao sio waaminifu wachukuliwe hatua na wananchi warudishiwe ardhi yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Laangai, mbali na tamko la mahakama la kuzuia ardhi ya wafugaji isiibiwe na isigeuzwe kuwa eneo la mapambano kama ilivyotokea Kiteto, naomba Wenyeviti na Serikali za Vijiji vya kitapeli zichukuliwe hatua. Iandaliwe orodha ya Wenyeviti wezi wa ardhi ili wachukuliwe hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya ardhi inapandisha bei za nyumba; riba za kibenki ni tatizo kubwa la bei ghali za nyumba hizi. La pili, mwanafunzi aliyepata kazi/ajira mwaka huu atapataje nyumba iwapo mshahara wake ni mdogo sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya Angola wana mpango mzuri wa kuiwezesha jamii yake kupata makazi bora. Naomba mkajifunze hayo ili wananchi wasaidiwe kupata nyumba bora na nzuri kwa mishahara yao midogo. Hawawezi kukodi nyumba za NHC kwa bei za sasa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze masikitiko yangu makubwa kwamba wafugaji wanapambana na nini? Wanapambana na dola nyingi dhidi ya uhai wa watu. Wizara hii ni Wizara pekee yenye dola nyingi kweli ambazo interesting group, zingine ambazo ziko nje ya nchi zina-interest, na mimi hapa imebidi nitoe kidogo leo elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumeanza utalii nchini mwetu? Mwaka 1892 alikuja Muaustralia mmoja anaitwa Oscar Bowman, mwaka 1913 akaja mwingine anaitwa Stewart Edward White mzungu wa Kiingereza, akaja mwingine anaitwa Bernard Dimezec pamoja na mtoto wake anaitwa Michael wakaandika kitabu kimoja kinachoitwa Serengeti shall never die. Baada ya wazungu hawa kuandika vizuri kitabu hicho, Waingereza, mwaka 1959 wakaamua kuwaondoa wafugaji wa Kimasai Serengeti, wakasema wala hawafai. Tumewatunzia mazingira hayo kwa damu na jasho letu tukiwapa na ng‟ombe wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe takwimu nyingine, kwa nini kuna migogoro ya wafugaji na wakulima nchi hii! Serengeti zimeondoka square kilometers 14,750 kutoka kwa wafugaji, Mkomazi - square kilometers 3,500 za wafugaji, Ngorongoro zimeondoka square kilometers 8,300 za wafugaji, Tarangire National Park zimeondoka square kilometers 2,850 za wafugaji, watu hawa mnawapeleka wapi! It’s a calculated genocide, mnataka maisha yetu yasiwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hii, Edward Moringe Sokoine, kati ya mwaka 1948 na 1958 ndipo wakati alikuwa anamaliza shule ya msingi na sekondari. Mikataba hii inaingiwa, mnaondoa maeneo haya makubwa kutoka kwa watu wetu. Where were there any informed consent? Naongea hivi, kuna wafugaji wako Zambia wanasuka watu nywele, kuna wafugaji wako Dar es Salaam wamekuwa walinzi, Serikali mnawaonaje, tunaanza kuwa watu wabaya kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnatupiga, tumewahifadhia mazingira haya yote tukiamini kwamba tunatunza maisha yetu. I declare interest, siamini kwamba utalii ni mbaya, lakini utalii mbaya unaoumiza maisha yetu ni utalii usiokubalika na nitakuwa wa mwisho kukubali utalii wa namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanauliza maswali mengi, wanasema mifugo inaharibu mazingira, mmoja amezungumza hapa, hivi ni ng‟ombe gani anayeua tembo, ni ng‟ombe gani anayeua simba. Lakini geuzeni swali upande wa pili, watu wanaotegemea mifugo, karibu watu milioni mbili nchi hii, geuzeni usemi kwamba hawa mifugo wamekufa, its their livelihood, leo Serikali ianze kuwalisha hawa, mnaongelea 17 percent ya GDP ya nchi. Je, mkianza kuwalisha watu hawa kwa sababu hawana mifugo, hawana maisha, itakuwa ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitika kwenye kauli ya Mheshimiwa Waziri juzi na bahati mbaya wafugaji wa Kimasai wamekupigia kura kwa takribani miaka15 kule Same. Unasema mifugo haifai, mifugo inaumwa, wanyama wasisafirishwe. Sasa nina maswali mawili; maana yake ni kwamba hawafai kuliwa na kwamba maisha ya watu ni ya bei rahisi kuliko pesa? Swali la pili, je, tuambiwe kwamba ni kauli ya Serikali kwamba wale wote wanaotegemea nyama nchi hii na wale wanaosafirisha kwenda Mataifa mengine wasisafirishe nyama kwa sababu wanaumwa, itoke kauli ya Serikali? Mheshimiwa Waziri amenisikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, kuna WMAs, tunachoomba wafugaji wa Kilindi, Mheshimiwa Msigwa ameongea hapa milioni 25, ndugu yangu naomba upate hili, tuna ng‟ombe milioni 25, hatutaki kuongezewa eneo, mipaka ambayo iliwekwa kabla sisi hatujawa na akili ya kisheria na ndiyo maana unaona Wamasai wengi, Mheshimiwa Ole-Nasha, wengine wote wanasoma sheria kwa sababu ya uonevu mkubwa. Sisi hatuli wanyamapori hao, hatuli simba, hatuli swala, tunawatunzia, lakini basi let it be fair, na ninyi msituumize. Kimotorok mnatufukuza, Emoret mnatufukua, Same mnatufukuza, Kilosa mnatufukuza, Bukombe mnatuumiza, Hanang‟ nina picha hapa, maskini wa Mungu mfugaji anatoka Katavi ameumizwa, kuna PF3 hapa. Mnatuumiza, mmetufanya watumwa kwenye nchi yetu. Naomba Serikali mkae chini mtufikirie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba utalii ni kitu kizuri, lakini Waheshimiwa Wabunge iwe fair. Naomba Sheria za WMA zilianzishwa na jamii, Kifungu kile cha 12 kilichoanzisha sheria hiyo badilisheni. Tunapata hela zetu, Simanjiro tumekataa WMA, lakini Kiteto na Longido wanafanya WMA. Mheshimiwa Waziri, hela zinachelewa sana, tunaomba mtume hizi hela mapema. Lakini kile Kifungu cha 51 cha sheria hiyo, ongezeni percentage, imekuwa ni kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeumia sana, Wamasai hawajasoma nchi hii, sheria za nchi hii hazijaangalia bado watu hawa. Kule Afrika Kusini wakati wa ukombozi, mwaka 1994 wakasema tuleteni an affirmative action. Tunacholilia hapa, wengine tumesoma siyo kwa sababu ya sera za CCM, ni bahati za makanisa na bahati za wengine wazungu tu. Mmetusahau muda mrefu, mnatuumiza muda mrefu, naombeni mfikirie kwamba Bunge hili lianze kutenda haki kwa ajili ya watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, fikirieni mifugo, its not about business, it is a livelihood. Mimi nisipokuwa na ng‟ombe siangalii kuhusu hela. Lakini lingine ni lile linahusiana na Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Sumaye, Wakili mwenzangu ameongea, ninasikitika sana, watu hawa wanasahau records. Mwaka 2006 Lowassa akiwa Waziri Mkuu wa CCM alifukuza mifugo Ihefu, hapakuwa hata siku moja na tamko la Kiserikali kutoka kwa Lowassa na Sumaye kutapanya mifugo yote nchi hii, msipotoshe umma. Nimuombe Wakili mwenzangu anapoanza kusimama aongee na authority, tunatetea utu, hatutetei biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, Mungu awabariki sana. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina nafasi gani katika ushirikiano wa kibiashara kwenye ukanda wa Kusini mwa Afrika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu wa kifugaji wanaokwenda Zambia na Afrika ya Kusini, wamekwenda kwa ajili ya kusuka nywele za akinamama kwa “style ya kimasai.” Ni sisi pekee nchi hii na Afrika ambao tunaweza kusuka nywele hizi na hazisukwi na mtu mwingine yeyote. Matatizo na adha wanayokumbana nayo wenzetu wa Kimasai katika nchi hizi mbili ni haya yafuatayo:-
(1) Wanakatwa, wanapigwa na kuhukumiwa bila kupewa usaidizi wa kisheria;
(2) Zambia kama nchi, imekuwa ikiwahukumu “Wamasai” bila kuwapa msaada wowote wa kisheria “fair hearing” trial hazifanyiki.
(3) Tunaiomba nchi ya Zambia ituambie wafugaji hawa wafanye nini ili wakidhi vigezo vya kufanya kazi nchini huko?
(4) Balozi wa Tanzania (Lusaka) amekuwa “reluctant” katika kuwasaidia vijana wetu wanaopata matatizo nchini Zambia. Naomba Balozi wa SADC atazame hili ili watusaidie kuwaondolea vijana wetu shida wanayokumbana nayo.
(5) Tunaomba vijana wetu waliofungwa kwenye Magereza ya Zambia wasaidiwe. Wapo wengi Magerezani na sijui kama Wizara ina takwimu zozote. Please hili lifuatiliwe pia.

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niweke msimamo kwamba na mimi pamoja na Kambi yetu Rasmi tunakubaliana kimsingi kwamba mkataba huu kwa muda huu usisainiwe na Serikali.
Mheshimiwa Spika, lakini hilo lisitunyime nafasi ya kuweza ku-criticize mkataba mzima objectively. Maprofesa watatu walikuja Jumamosi, ninawaheshimu sana. Mheshimiwa Profesa Kabudi, ni mwanasheria nguli, ni mwalimu wetu kwa namna yoyote, lakini walipowasilisha upande mmoja wa shilingi, kisomi haikubaliki.
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye article 101 pale inaposomeka; “resources mobilization.” Nataka tu niwaoneshe faida ya mkataba huu pamoja na madhaifu yake mengi, lakini kuna faida fulani.
Mheshimwa Spika, nenda kifungu cha pili; “The objective of joint resource mobilisation is to complement, support and promote in the spirit of interdependence, the efforts of the East African Community Partner States in pursuing alternative sources of funding to support regional integration and the development strategies, in particular the EPA Development Matrix.” Hiyo matrix hatujaletewa.
Mheshimiwa Spika, Maprofesa wangetuonyesha Waheshimiwa Wabunge hiyo development matrix ni kitu gani? Tunapoungana na EU tunakuwa na nafasi kubwa ya ku-negotiate for funding kwa ajili ya miradi ya maendeleo; mkataba huu unasema hivyo. Mkataba huu kwa kiwango chochote una madhaifu makubwa lakini sisi kama nchi tusifikie mahali tukawa ni watu wa kukataa siku zote.
Mheshimiwa Spika, alipoanza Profesa siku ile, alisema kitu kimoja kwamba nchi ya Tanzania na Afrika ya Mashariki kwa ujumla, itapoteza revenue.
Waheshimiwa Wabunge, naomba niwakumbushe kitu kimoja, mwaka 2004 tuliingia mkataba wetu na Kenya na Uganda; East African Customs Union Protocol. Tuliwaachia nchi ya Kenya kwa miaka mitano walipe kodi.
Mheshimiwa Spika, mkataba huo uliisha mwaka 2009. Mwaka 2009 Kenya ikaanza kuingiza bidhaa zake bila kulipa kodi Tanzania, baada ya Tanzania na Uganda kuruhusiwa kuingiza Kenya bidhaa zao wanazotengeneza kwa miaka mitano bila kodi yoyote.
Mheshimiwa Spika, tujiulize kama nchi, hivi baada ya ule mkataba mwaka 2009, viwanda vingapi Mheshimiwa Mwijage tumeanzisha kuanzia siku hiyo? Tumepeleka nini Kenya? Leo hii mnatutuhumu wengine, tumepeleka kabichi, nyanya na vitunguu lakini hatujaanzisha viwanda vya aina yoyote.
Mheshimiwa Spika, wengine mnasema tunautetea mkataba huu kwa sababu tuna maslahi binafsi na nchi za Ulaya, wala siamini hata kidogo. Mimi ni mzalendo na ninaamini ni mzalendo, lakini hivi mfano Tanzania, Waziri wa Fedha anajua, kati ya mataifa matano makubwa yanayochangia Tanzania bajeti yake, ni nchi zipi? Kama kati ya tano hizo, Ulaya zipo nchi tatu.
Mheshimiwa Spika, nafikiri wakati tunakataa mkataba huu, tujiulize maswali ya msingi, moja, hivi ni viwanda gani hivyo ambavyo tunavitetea kwamba tukiingia kwenye mkataba huu tunapoteza bidhaa?
Pili, kwa muda gani nchi yetu ya Tanzania itaweza kujenga viwanda vyake peke yake na kuweza kushindana na masoko haya mengine ya East Africa na Ulaya pia, itatuchukuwa muda gani kujenga viwanda kwa sababu viwanda vingi vipo mfukoni.
Tatu, kama hatutaanzisha viwanda kama nchi, hivi hamuoni kwamba Ulaya wakiingiza bidhaa zao kwenye uchumi kuna kitu kinachoitwa basket of goods, kwa sababu vitaingia kwa bei rahisi mwananchi wa kawaida atakuwa na uwezo wa kuvinunua kwa wingi zaidi.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunapata kutoka China tunavitoza kodi ambavyo ni vya hali ya chini kweli, lakini wote tunafahamu, leo ukiletewa bidhaa kutoka Ulaya na China, wote ambao mmesafiri humu duniani, mtakubaliana na mimi kwamba bidhaa ya China na Ulaya vinatofauti kubwa, quality wise, I will go for European goods for sure!
Mheshimiwa Spika, nne, naomba pia nishauri badala ya kukutaa mkataba huu, Bunge tumshauri Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais kwenye kikao cha mwisho cha Marais wa Nchi za Afrika Mashariki -Summit ya juzi Arusha au Kenya kikao kimoja cha mwisho, ndiye aliyewaomba wenzake kwamba jamani mkataba huu sisi hatujapitia, ninaomba niunde Technical Committee ambayo itapitia mkataba huu itushauri kama nchi.
Mheshimiwa Spika, Technical Committee ndiyo ile nafikiri ambao wamewasilisha upande mmoja wa shilingi nafikiri siyo vema sana tukawa ni nchi ya kususa na kukataa wakati hatuchukuii hatua madhubuti ya kuweza kubadilisha nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nishauri kitu kimoja…
TAARIFA...
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, naomba nipokee taarifa hiyo kwa nia njema kwamba anajaribu kuniambia kwamba ni kweli Mheshimiwa Rais alivyoomba kwamba iiundwe Technical Committee ya kuishauri Serikali imeundwa, lakini bado haijawasilisha mapendekezo yake.
Mheshimiwa Spika, hilo halitunyimi fursa kama Bunge kuiomba Serikali, mkataba huu kwa sasa usitishwe lakini tusikatae moja kwa moja. Uende ukapitiwe tena tuangalie kama negotiating team ya Tanzania inaweza ikabadilisha baadhi ya mambo ambayo tunayataka na bidhaa ambazo tunataka kuzitetea kwa muda na baadaye urudishwe Bungeni.
Mheshimiwa Spika, pili, ninaomba Serikali yetu badala ya kupiga kelele ya kusema tunaandaa viwanda, sasa ifikirie ni muda sahihi wa kuwekeza kwenye viwanda. Hili jambo la kukimbia na kuwa na protection policy kila saa hautatufikisha mahali. Waingereza wanasema, you better run the hard way kwa sababu the easy way you do not go it, kwa sabubu ninyi hamuwezi hata kidogo. Tukiwaachia hata miaka 100 humuwezi kuanzisha viwanda vya kushindana na Ulaya. Ni changamoto kama nchi kwamba, ni lazima kwa muda huu tuamue wote kama jamii tuungane tuwaambie Mawaziri hawa wenye viwanda mifukoni, walete viwanda ili tusiwe wapiga kelele kwenye soko la Afrika Mashariki.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo Arusha ukienda kwenye maduka yote vifaa vya Kenya vimejaa, ukiuliza tunapeleka nini Kenya? Utaambiwa maembe na machungwa ya Tanga na unga wa Azam.
Mheshimwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba mkataba huu usisainiwe, lakini kama nchi tuangalie faida ambazo tunaweza tukazipata kutokana na mkataba huu, badala ya kuanza kulialia na kupiga kelele kwamba sisi hatuwezi, hatuwezi siku zote! Muda unatosha ni muda sasa wa kushindana na Mataifa mengine kama nchi.
Mheshimiwa Spika, tumeingia kwenye AGOA, mmesikia jana Mheshimiwa Mwakyembe amesema tumeuza asilimia nne soko la Marekani, wakati Kenya wameuza 98% they are taking advantage of their industrial power na Tanzania tunabaki kulalamika ni nchi ya kulalamika tu Kiongozi analalamika, wananchi wanalalamika, kama alivyosema Mheshimiwa Lowassa wakati fulani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nimshukuru saana Mungu kwa kunipa nafasi hii leo lakini niendelee kuwashukuru watu wa Simanjiro kwa kuniamini kuwa Mbunge wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye Wizara hii na kuanza na maneno haya tu, kwamba ni lazima Wizara hii itambue pamoja na maslahi mapana ya nchi ni muhimu kutambua pia kwamba wale waliosaidia sekta hii ya kiuchumi ya maliasili kutunzwa mazingira yake na wenyewe waheshimiwe; maana imekuwa na fikra kubwa sana kwamba wale ambao wanaishi pale, maslahi yao sio mapana sana na sio makubwa kwa Taifa ukilinganisha na Taifa kubwa. Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie sana kwasababu mimi ni mfugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niungane na Wabunge wenzangu, mipaka hii kuanzia mwaka 1954 mpaka leo haijaangaliwa tena, jamii imeongezeka na mimi niko kwenye msimamo mmoja kwamba haiwezekani tufike mahali kwamba kesho tukiwa bilioni moja kama Wachina tuseme na mbuga zetu ziliwe, haiwezekani! Ni lazima tukubaliane.Lakini wakati mipaka hii ikiandaliwa watu wetu walikuwa hawajui kinachotokea, hawajui thamani ya ardhi, hawajui nini maana ya mipaka hii na wanyama hawa. Ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri na zile Wizara ambazo zimeungana Wizara tano, mifugo, kilimo tuje na wawakilishi (wote sisi wawakilishi) tukae pamoja tuweke mipaka ya kudumu na tuwafundishe wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Simanjiro vijiji vya Kimotoro, kijiji cha Lobosiret, Emboret na baadhi ya maeneo ambayo mbuga hizi zimezunguka nipo tayari kuwaongoza wananchi wangu tutakapokubaliana na Serikali kwamba mipaka hii sasa huu ndiyo uwe mwisho, kwa maisha ya sasa na maisha ya baadae ya watoto wetu. Ni muhimu sana tukae wadau wote tukubaliane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nitambue kimsingi kazi kubwa iliyofanyika Ngorongoro, Loliondo. Nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri lakini bahati mbaya nimeona pia kwenye Kambi yetu Rasmi ya Upinzani. Wananchi wamekaa na watumishi wa Serikali, wamekubaliana njia ya kwenda mbele ili kumaliza migogoro. Mheshimiwa Waziri ninaona hutaki kutambua nguvu hii. Mimi nafikiri ni vyema sana wanyamapori na Wizara yako ikae na wananchi tukubaliane wote kwamba kuanzia sasa na maisha ya baadae tunakaaje ili kuhifadhi wanyama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mtalii, nikuambie tu ukweli, mimi nazunguka sana lakini namshukuru Mheshimiwa Nape na yeye siku moja nimeenda mbuga moja nikasikia na yeye yupo kwenye hoteli mojawapo. Ni lazima sisi kama Bunge, hii Wizara tuibebe, kazi kubwa tuifanye. Viongozi hamtalii, hamuendi mahali, lakini ni vyema sana Wizara hii iwepo Ngorongoro Conservation Area Authority, iwepo TANAPA kwa ujumla wake, kina KINAPA wote, mfanye juhudi za kipekee za kusaidia Watanzania watalii na viongozi wa nchi hii muanze kutalii kwenye mbuga zetu ili tupate mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nitambue leo Simanjiro, kijiji cha Kimotoro pamoja na kupoteza maisha ya mfugaji mmoja, kuuawa na wanyama, anafidiwa kijana wetu mmoja leo kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe. Mimi naendelea kusema fidia hii haitoshi, lakini leo anafidiwa mmoja. Naomba Wizara muangalie uhalali wa binadamu, heshima ya binadamu vis a vis mnyamapori. Haiwezekani anapouawa, shilingi milioni moja tu! Badilisheni sheria hizi, tubadilishe ili tuheshimu ubinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa kwenye Wizara hii, leo mimi sitaongea sana against you,kubwa na imeandikwa kwenye Biblia na Qurani amri kubwa kushinda yote ni upendo. Ninyi wahifadhi kaeni na sisi, nami nitambue kazi kubwa ya Tarangire iliyofanya pale Kimotoro wakati mnapitapita pale Kimotoro tumeweka mahusiano mazuri, Mhifadhi na Afisa Uhusiano wa Tarangire ninaomba nitambue kwamba tumeanza kukubaliana vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee Makumbusho ya Taifa. Bahati nzuri nimesoma mwaka 2006/ 2007 Misri, nimetembelea makumbusho yao. Watu hawa wanaingiza watalii wengi sana kwa Makumbusho ile ya Cairo. Lakini Ujerumani wanaongoza pia kwa ajili ya makumbusho.

Ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuanzia ukurasa wa 12 mpaka 51 inaongelea wanyamapori, ukiangalia ukurasa wa 53 mpaka 89 kurasa 36 na 39 inaongelea nyuki. Lakini Makumbusho yetu ya Taifa mnaongelea kwa kurasa saba tu, hamuipi uzito utamaduni wetu wa nchi yetu. Makumbusho ya Dar es Salaam hayana maana kubwa ukilinganisha na makumbusho mengine yanayotuzunguka kwenye nchi yetu. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, weka nguvu kubwa kwenye makumbusho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Misri pale bajeti ya 2017/2018 wanapitisha almost one billion USD wamepata msaada kutoka JINCA wanaboresha makumbusho yao. Mwalimu Nyerere na ninyi bahati nzuri wazee kama ninyi mmeishi na Mwalimu Nyerere sisi wengine tunamuona kwenye makumbusho tu. Kwa nini hampendi kuutunza utamaduni wetu, alianzisha Makumbusho ya Taifa letu. Ninaomba kwa nguvu zote, bajeti ya Makumbusho iongezwe. Ninaombeni tuwape Watanzania heshima hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili kuna suala la utozaji, lakini Mabalozi wetu nimeshuhudia nchini Canada, Balozi wa Kenya anaenda kwenye shule za sekondari na vyuo vikuu vya nchini Canada anawaita watalii wakati wa low season wanafunzi anatangaza utalii, imefika wakati sasa nchi yetu tunapomteua Balozi wetu pamoja na hadidu za rejea za kumpa moja ni kutangaza nchi na kutangaza nchi yetu kwenye mataifa ambayo wanaenda. Haiwezekani Mabalozi wakakaa kule maofisini na ofisi kubwa na wanapewa kila kitu, lakini hawatangazi nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu hatupati watalii wa kutosha Zanzibar is just amazing, ukiangalia Ngorongoro ni nzuri, ukiangalia Mlima Kilimanjaro, hamna mlima kama huo duniani. Lakini hatutangazi vizuri, mabalozi wetu ni vizuri Serikali iweke hadidu za rejea za kusaidia utangazaji wa utalii katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu mbili naomba nimpe Mheshimiwa Ester.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's