Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Aida Joseph Khenani

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kushiriki Bunge hili kwa mara ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda siyo rafiki sana, dakika kumi naziona chache, napenda kuanza kuzungumzia suala la utawala bora. Tunapozungumzia utawala bora tunamaanisha, usiwe utawala bora wa maandishi uwe wa vitendo. Tunapozungumzia vitendo, amezungumza mzungumzaji aliyepita sasa hivi, kazi yetu sisi siyo kupongeza Serikali, kazi yetu ni kuikosoa na kuisimamia Serikali. Hatuwezi kuogopa polisi pale ambapo tunaona kuzungumza ni haki yetu, hatuwezi kuogopa kupigwa pale tunapoona Serikali imekosea, tutaisimamia na tutaikosoa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utawala bora, nianze na suala la maslahi ya walimu. Walimu wa nchi hii ni watumishi kama watumishi wengine. Kama kweli utawala ni bora, kwa nini madai yao imekuwa ni wimbo wa nchi hii? Kila Mbunge anayesimama hapa akizungumzia Jimbo lake anazungumzia masuala ya walimu. Leo ukitazama hata kwenye vyuo, kwa sasa wanachuo wakikosa haki zao muhimu, wanaposimama kudai haki yao wengi wanafukuzwa vyuoni, je, huo ni utawala bora? Tukisimama hapa tukidai haki zetu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa tuisaidie Serikali na nchi yetu kuboresha mapendekezo ya Mpango. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniongoza kwa sababu najua ni kazi yako. Ninapozungumzia suala la utawala bora hatuzungumzi kwa sababu ya uoga na nidhamu ya uoga sisi wengine hatuna. Mnapozunguka mnatazama nchi zinazounda Umoja wa Afrika utawala bora wanafanyaje, lakini utawala bora wa Tanzania tunauzungumzia kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele mlivyoleta kwenye Mpango, Serikali makini haiwezi kuwa na vipaumbele vingi visivyokuwa na idadi. Inaonyesha ni jinsi gani mmeandika tu lakini utekelezaji ni sifuri. Nikianza na suala la kilimo. Natokea Mkoa wa Rukwa, tunalima sana mahindi na maharage. Leo hii wakulima wa Mkoa wa Rukwa wanajiona kama wakimbizi ndani ya nchi yao. Pembejeo ni tatizo kwao lakini hata vile vichache wanavyopata kwa nguvu zao ili angalau kuzisaidia familia zao kuna ushuru usiokuwa na tija. Tunapozungumzia ushuru, huyo Mtanzania wa Rukwa ambaye ni mkulima, amekosa pembejeo, amejikongoja akalima kilimo chake tena kwa mkono lakini na kilekile kidogo Serikali inatoza ushuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini watakapoanza kuwathamini wakulima wa nchi hii hasa wa Mkoa wa Rukwa? Wamelima mahindi na mnajua walikosa soko, mmezungumzia hapa, lakini huyu mkulima wa Tanzania ili ajue kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inamthamini, inamthamini kwa lipi, kwenye pembejeo ni shida, kwenye masoko ni shida.
Naishauri Serikali, kama kweli tunaamini asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima, tutengeneze mazingira rafiki ya wakulima hawa. Isibaki stori za kwenye madaftari na vitabu yanabaki kwenye makabrasha, tunataka vitendo vifanyike. Kama kweli ni kazi tu mmemaanisha mfanye kazi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala la maji, nikiwa natazama Bunge kwa njia ya TV, Mheshimiwa Keissy imekuwa ni wimbo wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, iko Mkoa wa Rukwa. Watu wa Nkasi Kaskazini na wenyewe ni Watanzania kama Watanzania wengine, kwa nini kila siku iwe ni wimbo tu wa maji? Kwenye Mpango mnaoleta mtuambie ni mikakati gani mipya mliyokuja nayo ukiachana na nyimbo mnazoimba kila siku. Mikakati mipya iko wapi ambayo itatufanya sisi tuwaamini kama kweli mnakwenda kutenda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wananchi, imefikia mahali wamechoka na nyimbo hizi sasa wanataka utendaji. Ukitazama Bunge hili Wabunge wengi wanasimama wanazungumzia suala la maji, sawa, yawezekana tunazungumza na tunaleta kwa maandishi kama hivi, ni kitu gani kinawazuia sasa mnapoandika mnashindwa kutenda? Kama kweli ni Serikali sikivu na siyo kinyume, tendeni sasa, muache kupiga story.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miundombinu. Mkoa wa Rukwa umesahaulika kwa kila kitu. Watu wa Rukwa siyo Watanzania? Ukizungumzia Nkasi Kaskazini na Kusini barabara ni hadithi. Amezungumza hapa Mheshimiwa Mipata na anazungumza kila siku lakini sisi tunapozungumza hatuombi, tunaitaka Serikali ifanye kwa sababu ni wajibu wenu kufanya na msipofanya tunajua hamsikii na hamuelewi. Msifikiri Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongoza ni kwamba mnapendwa sana, no, lazima mjitafakari. Pale mliposhinda kwa haki mjitafakari lakini mapito mliyoyapata katika kipindi hiki mnajua kwamba ni jinsi gani mmekosea step, lazima mjipange. Sasa kwenye Mpango mnaokuja nao tunahitaji mikakati madhubuti ambayo kweli inamaanisha kwenda kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la elimu. Suala la elimu haliwezi kufanikiwa kama mnakurupuka lazima mtafakari kabla ya kusema. Mnasema elimu bure, elimu bure itakujaje wakati walimu wenyewe madai yao yako palepale? Sawa wanafunzi wamefika shuleni lakini sasa hivi wanafunzi idadi yao ni kubwa kuliko walimu. Hii elimu bure inakwenda sambamba na yale mnayoyasema au mnasema tu ili kutimiza wajibu? Mimi naamini hata hili mmeibuka tu kulisema, hamjajipanga. Ni mipango gani madhubuti ambayo mmetuonyesha hapa kama kweli mmekusudia kutoa elimu bure? Mimi nawashauri msiwe mnakurupuka, mjipange kwanza. Mkiona UKAWA wamekuja nayo wanazungumza msifikiri na nyie mnaweza mkafanya.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi yangu kuiambia Serikali pale walipokosea lazima wajirekebishe na wasikurupuke lazima wajipange. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa na maneno mengi kuliko kutenda na Watanzania wanaona. Haya wanayoyazungumza inaonyesha ni jinsi gani kweli wamekurupuka, hawajajipanga. Vipaumbele ambavyo wanashindwa kuvitekeleza, vipaumbele vingi, hakuna Serikali inayoendeshwa kwa staili hii. Lazima uwe na vipaumbele unavyojua utatekeleza. Ni kipi ambacho mlikileta kwenye Mpango uliopita na mmetekeleza kama mlivyokuwa mmepanga, hakuna! Imekuwa ni maneno ya kila siku ya kuandikwa yanashindwa kutekelezeka. Tunaitaka Serikali ya Chama cha Mapinduzi iachane na porojo, ifanye kazi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Napenda kushauri mambo machache katika Wizara hii ya Ardhi. Mheshimiwa Waziri imeonekana kama ana mikakati kabambe kwenye maandishi yake, lakini sijajua alivyojipanga kwa sababu suala la migogoro ya ardhi lipo kila sehemu nchini na halijaanza leo na sitapenda sana kama Waziri anasubiri na Mkoa wa Rukwa yatokee kama yanayotokea Morogoro ndiyo achukue hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wamekuwa na utaratibu mmoja wa kusubiri matukio ndiyo wamnakuja na matamko na mikakati. Nafikiri ni vema kwenye maeneo ambayo haijatokea migogoro, wakaweka mikakati thabiti kuonyesha kwamba wako serious na suala hili. Tatizo wanasubiri matukio ndiyo wanakuja na kauli ambazo hazisaidii chochote, watu wanakuwa tayari wameangamia, wamepoteza maisha, hawana tena cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mgogoro wa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga na mwekezaji EFATHA, limekuwa ni kero sana kwa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Rukwa, tumezungumza mara nyingi sana. Mheshimiwa Waziri amezungukia maeneo mengi lakini Mkoa wa Rukwa bado hatujamwona. Hili suala limeleta shida sana kwani kuna watu wameumia sana pale, kuna watu wamefungwa, sijajua shida ni nini? Hili suala sijui halijafika mezani kwa Mheshimiwa Waziri au kama limefika ni kitu gani kinazuia asije Mkoa wa Rukwa kuangalia nini kifanyike? Nimeona jitihada za Waziri, lakini napenda kuziona pale atakapofika kuzungumza na wananchi wenyewe. Napenda kumshauri ili afanikishe masuala haya, asifanye kazi kama Wizara nyingine wanaopewa maandishi wanaridhika kwa maandishi yale bila kwenda sehemu husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna migogoro ambayo inaendelea mpaka sasa, Jimbo la Kalambo kuna mauaji yametokea hivi karibuni. Migogoro hii iliyopo kwa Wafipa ilikuwa haipo sana kwa sasa ipo kati ya Wafipa na Wasukuma lakini shida siyo makabila, elimu mnaitoa kiasi gani? Mmegundua shida ya migogoro hii ni nini? Yawezekana mmekosa suluhisho kwa sababu hamjaja na njia ya kusuluhisha migogoro hii ila mnakuja na matamko ambayo hayana tija. Ni vema mkajua tatizo la migogoro ni nini na mkaja na suluhisho la kudumu siyo la muda mfupi kwa ajili ya kampeni, mkaja na suluhisho ambalo litaondoa migogoro kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la kuwapa ramani viongozi wa Serikali alilozungumzia hapa Mheshimiwa Waziri. Mkoa wa Rukwa nimeangalia hapa pesa zilizorudishwa kwao, kwenye kitabu cha hotuba, ukurasa wa 83 anasema marejesho, ile asilimia 30, Manispaa nzima ya Sumbawanga kiasi ambacho kimerejeshwa pale sijajua kama kinaendana na Manispaa, kuna shida kubwa sana hapa. Yawezekana ni mawasiliano mabovu kati ya Wizara yenyewe ya Ardhi na Manispaa husika. Kama siyo rushwa basi kuna shida kubwa sana kwenye Wizara au kwenye Manispaa pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wanaowaweka kwenye Manispaa na Halmashauri zetu wamekuwa wakijitukuza kama Miungu watu ambapo wananchi wanapokuwa na shida wanashindwa kuwahudumia kwa uharaka, wanaangalia ni nani anasema, anasema nini, ana kiasi gani. Sasa nchi haiwezi kwenda kwa staili hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama eneo ninalotoka mimi Kata ya Chanji, ni ya muda mrefu sana kwenye Manispaa ya Sumbawanga, iko katikati ya mji lakini Mheshimiwa Waziri akitazama maeneo yaliyopimwa atashangaa lakini property tax inakusanywa! Halafu baadaye ndiyo watakuja na hili la bomoabomoa, Sumbawanga haijafika lakini wananchi wako kwenye tension kubwa sana kwamba sijui mimi nitaondoka au nitabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri ni vizuri elimu ikatolewa kwanza kwa watu hawa na elimu tunayoizungumzia ni bora wakapewa Wenyeviti wa Serikali au Vitongoji na Vijiji, wale ndiyo wako karibu na wananchi kuliko hawa mnaowapeleka. Hawa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vitongoji au Vijiji wataweza kueleweka vizuri na wananchi wao kwa sababu wanajua maeneo na wanajua ramani vizuri za maeneo hayo. Kama tutachukulia mambo haya juu juu hatutaweza kukomesha tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana Waziri ana nia njema lakini watendaji wake wa chini ndiyo wanaomwangusha lakini yawezekana na wao ni kwa sababu elimu hawana au yawezekana hawa watu ambao wanaweza wakafikisha ujumbe ni wachache kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, kuna haya mambo yanawezekana yanakurudisha nyuma kwa sababu aidha, watu kwenye Halmashauri ni wachache au hata waliopo hawatimizi wajibu wao. Kwa hiyo, ni vizuri katika haya anayotaka kuyafanya akagundua kitu gani kinakwamisha pengine ni bajeti anayopewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefikia mahali nchi hii haitambui kwamba migogoro hii inapelekea kukosa amani katika nchi yetu, kwa sababu unapotokea mgogoro kati ya shule na wananchi unategemea ni nini kinaendelea? Siyo kwamba wale Walimu wanatambua maeneo yale wao wamekwenda pale kufundisha, lakini nani anayatambua yale maeneo? Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa haelewi ramani halisi ya pale ikoje. Sasa inapotokea migogoro kama hii nani alaumiwe Serikali, Halmashauri ya Mji au Manispaa ambayo inahusika na lile eneo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri kabla hatujachukua hatua na migogoro mingine haijajitokeza, elimu itolewe kwa watu wetu na elimu hiyo tusi-base tu kwa watu ambao wako Wizarani, tu-base kwa watu ambao wako na wananchi wetu ambao ni Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la asilimia 20 kwa Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa, yawezekana maeneo mengine wanapewa, Manispaa ya Sumbawanga kuna shida katika suala hili. Inafikia mahali Watendaji wa Kata wanasema wanaopaswa kukusanya ni mgambo, sheria inasema nini juu ya suala hili, ni akina nani wanaokusanya hii property tax? Sheria inasema nini, inawezekana ni mkanganyiko. Sasa Wenyeviti wanapata shida, wanakusanya pesa hizi kwa amani kabisa, wanapokwenda kule hawapewi, sasa shida nini Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana naona kwamba Waziri ana nia njema katika maelezo yake, lakini yawezekana watendaji wake ndiyo wanaokwamisha mambo anayotaka kufanya. Pia hata bajeti anayopewa haifanani na migogoro ambayo ipo kwenye nchi yetu, haifanani kabisa. Ndiyo maana muda mwingine tunaona kama kiini macho au kama story za miaka yote. Yawezekana ana kusudio jema, tunataka tuone haya mambo kwa vitendo na pale Waziri anapoona amezidiwa asisite kusema. Kazi yetu hapa siyo kumshangilia, tutamshangilia pale atakapofanya vizuri, lakini kama atakuja na haya mabegi aliyotupatia leo na documents nyingi halafu akashindwa kutimiza kile alichopanga, haitatusaidia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninachotaka kusema ni kwamba, suala la rushwa kwenye Wizara hii ni kubwa sana. Yawezekana hata Waziri katika maeneo aliyokwenda ameliona lakini maeneo mengine akashindwa kuona kwa sababu sijajua kama anapewa ushirikiano wa kutosha. Huu ushirikiano ni lazima kuwepo na semina elekezi ili Mwenyekiti wa Serikali ajue wajibu wake, ajue anapata nini na anapaswa kufanya nini kwenye suala la ardhi, lakini ajue wananchi wake wanapaswa kutimiza wajibu gani kwenye kumiliki majengo yao au wanapokuwa wanataka umiliki wa ardhi. Mheshimiwa Waziri wananchi kwa sasa wanatamani maeneo yao yapimwe lakini anapokwenda pale mpaka aje apate hiyo hati ya kumiliki ardhi ni shida, tatizo ni nini, kuna shida gani hapa na bado inakuwa ghali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri hata hizi nyumba tunazosema za National Housing bei wanazotoa hazifanani na mazingira halisi ya maeneo husika. Huwezi ukauza nyumba kwa shilingi milioni 30, kwa Manispaa ya Sumbawanga, unategemea Mfipa anayepata gunia tatu kwa mwaka ataweza kununua hiyo nyumba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hizo nyumba zijengwe kulingana na mazingira halisi ya eneo husika. Kama ni Manispaa ya Sumbawanga waaangalie watu wa Manispaa ya Sumbawanga uwezo wao wa kipato ni kiasi gani. Wasichukue mazingira ya Dar es Salaam wakayapeleka Manispaa ya Sumbawanga haitawezekana. La sivyo hizo nyumba watakwenda kujenga kwa ajili ya wafanyabiashara lakini kusudio la zile nyumba ilikuwa ni watu wa hali ya chini waweze kupata nyumba za kuishi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri katika hilo, awatazame watu wa Sumbawanga kwa jicho lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa kumaliza hii migogoro, Mheshimiwa Waziri ana nia njema na ameonesha njia, napenda kushauri tena kuwe na ushirikishwaji. Manispaa ya Sumbawanga siyo lazima twendaemahakamani, sisi tunaheshimu sana mila na desturi, anaweza akaa na watu wa pande zote mbili wakamweleza shida ni nini badala ya kusubiri migogoro mpaka ifike mahakamani na watu kuuawa. Kwa hiyo, ushirikishwaji ni suala jema sana na litasaidia kumaliza migogoro hii. Yawezekana sheria zipo, lakini zimepwaya au usimamizi ni mbovu. Kwa hiyo, hata kama zitakuja hapa zikawekwa kwa staili nyingine, inawezekana ikawa ngumu kwenye utekelezaji.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunijaalia uzima, kuweza kusimama tena ndani ya Bunge hili Tukufu. Pia napenda kupongeza na kushukuru kwa dhati Ofisi yako kwa kuweza kuokoa maisha yangu.

Mheshimiwa Spika, namshukuru pia Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano waliouonyesha na nitakuwa sio mtu mwema sana nisipowashukuru Wabunge wa Mkoa wa Rukwa na Katavi kwa upendo waliouonyesha bila kujali itikadi za vyama vyao.

Mheshimiwa Spika, pia naungana na wazazi, Walimu, ndugu na jamaa katika kuomboleza msiba uliotukuta juu ya wanafunzi ambao walituacha. Tunasema kazi ya Mungu hatuwezi kuhoji, lakini tumepokea, ingawa mambo haya hayazoeleki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakwenda kuchangia mambo machache nikianza na upande wa habari. TBC ni Television ya Taifa wote tunajua, lakini inachangiwa na walipa kodi wa nchi hii wakiwepo wa Mkoa wangu wa Rukwa, leo tunapokuwa tunajadili bajeti, wanashindwa kujua wawakilishi wao wamezungumza nini? Je, wamezungumza yale waliyowaambia? Kwa sababu hawawezi kuona tena Bunge live.

Mheshimiwa Spika, yawezekana hata nia njema ya Serikali hasa anapokuwa anazungumza Mheshimiwa Rais kwamba watu wafanye kazi, lakini tunafahamu fika kwamba Rais anapokuwa anafanya jambo lolote anaonekana live. Rais huyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alichaguliwa kwa kura za Watanzania, Wabunge wamechaguliwa kwa kura za Watanzania. Sijajua utofauti mkubwa uliojitokeza hapo katikati.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Mawaziri pamoja na sisi Wabunge, mimi bado linanichanganya kwenye kichwa changu. Tofauti ni nini? Ni nafasi au ni kazi kama alivyozungumza? Kwa sababu ule muda anapoonekana yeye, wananchi wanaacha kazi wanamsikiliza, basi angalau hata kipindi hiki cha bajeti sasa ili wananchi waweze kuwaona Wawakilishi wao wanafanya nini? Je, wanazungumza yale waliyowaambia wazungumze au inakuwaje? Sidhani kama itakuwa busara au uzalendo anaousema yeye aonekane, Waheshimiwa Wabunge wasionekane, wakati wote walikwenda kuomba kura na wananchi ni wale wale ambao wanatakiwa waone nini kinazungumzwa na nini kinatendeka. Sidhani kama uzalendo uko mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri labda aje atuambie kwamba pesa zinakuwa nyingi sana kuonyesha Bunge, lakini upande wa Rais na vitu vingine pesa zinakuwa siyo nyingi. Wakati huo huo TBC inaweza kuonyesha mambo mengine. Napenda tupate taarifa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up kwamba kwa mara ya mwisho ni lini taarifa za Upinzani zilionyeshwa TBC? Nimekuwa mfuatiliaji sana wa TBC. Sasa kama TBC imekuwa na ubaguzi, ni vyema Mheshimiwa Waziri aje kutuambia tujue. Ni lini kwa mara ya mwisho TBC ilionyesha habari za Upinzani, wakati wote ni Wabunge na wote ni Wawakilishi wa wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili kwa upande wa habari, ni juu ya Waandishi wa habari. Pamoja na Bunge kutoonyeshwa live, Watanzania hawa wanategemea kupata habari kwenye vyombo mbalimbali. Leo waandishi wa habari wanakuwa na hofu ya kutoa habari. Hatujasikia tamko kutoka kwa Mheshimiwa Waziri linaloonesha moja kwa moja uzito juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari. Tumeangalia matukio kadhaa, achana na hayo ya huko nyuma ya akina Mwangosi na watu gani, lakini bado hatujaona jitihada za Serikali juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie mikakati yake aliyoipanga juu ya Waandishi wa Habari. Wananchi hawawezi kujua chochote bila kuwaona au kuwasikiliza Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wangu wa Rukwa kuna maeneo hakuna TV, wanategemea kusikiliza redio. Hizo redio zenyewe sasa hivi habari haziendi kama zilivyo; sijui mpaka zichujwe wapi, zifanywejwe! Sasa haya mambo inafikia mahali yanakuwa na ukakasi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie ni mikakati gani ameiweka juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari? Sambamba na hilo, ile ripoti ya Mheshimiwa Nape tunataka tuisikie, kwa sababu hapa ndiyo mahali pake, aje atuambie nini kinaendelea juu ya kile kitu? Kama kuna kiini macho tujue kwamba imeshindikana, lakini imeshindikana kwa nini?

Mheshimiwa Spika, upande wa michezo, hatuwezi kuboresha michezo tukiwa hatujaboresha viwanja vya michezo. Hapa tutapiga story siku zote na kutafuta mchawi. Kwa sababu huwezi kusema watu waje wacheze, unategemea kwamba waje wacheze Dodoma tu; kwa sababu hawa watu wanatoka kwenye Wilaya na Mikoa. Huko kwenye Wilaya na Mikoa hali za viwanja ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, katika viwanja hivyo kuna viwanja vinamilikiwa na Chama Tawala; siyo dhambi, basi viendelezeni. Viko kwenye hali mbaya! Shida ni nini? Yawezekana bado hakujawa na mikakati thabiti kwa sababu hatutegemei kuangalia Serengeti boys wale wale wakae miaka 20, tunataka mikakati ya wale ambao wanaandaliwa sasa kuja kuwa Serengeti Boys wa mwaka 2020. Hawa watu wanapatikana wapi? Wanapatikana kwenye Wilaya na Mikoa. Ni utaratibu gani umewekwa ambao utakuwa rafiki kwa hawa vijana wanaotoka kwenye mikoa na wilaya?

Mheshimiwa Spika, siamini kwamba Mkoa wangu hakuna wachezaji wazuri. Mkoa wa Rukwa wanakula samaki, kuna watu wanacheza vizuri sana. Ni lini utawajua? Utawajua kwa kufuata ule utaratibu uliokuwepo zamani. Kulikuwa na michujo inafanyika shule za msingi na sekondari. Nakumbuka kwa mara mwisho UMITASHUMTA pamoja na UMISETA wakiwa wanakwenda Geita nafikiri, ilitokea tamko hawarudi wale watoto. Tunaomba mtuambie sasa, hiki kitu ndiyo kimefutwa moja kwa moja au kuna mikakati gani inaandaliwa juu ya suala hili? Maana imeshakuwa sasa hatuelewi, tupo tu.

Mheshimiwa Spika, siamini kama wachezaji wengi wanatoka Dar es Salaam na Mwanza tu; na Mikoa mingine wachezaji wapo. Wekeni mikakati, wekeni mazingira rafiki ya kuwapata wachezaji wazuri na wapo, wanapatikana maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, vile vile tusiwekeze kwenye mpira peke yake. Kama tumeshindwa kwenye mpira, lazima tuwe na plan B. Tutafute mchezo mwingine ambao hatutaitwa shamba la bibi Tanzania, haiwezekani! Naamini vipaji vipo vingi tu, lakini ni namna ya kupata hivyo vipaji na kuvifuata kule viliko. Kwa hiyo, kumekuwa na shida kidogo.

Mheshimiwa Spika, vazi la Taifa limekuwa likizungumzwa sana. Siamini kwamba mpaka leo tumeshindwa kupata vazi la Taifa. Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kufanya majumuisho atuambie, maana nimeona huku pembeni nyuma ya hiki kitabu, lakini haijaonesha kwamba ndiyo hili, sijui! Nafikiri ndiyo utaratibu unaandaliwa. Muda umekuwa mrefu, mpaka lini kwa mwendo huu unaokwenda? Kama ndiyo hili limepitishwa, basi mtuambie lilivyopitishwa.

Mheshimiwa Spika, hiki kitu inatokea, hata ukiangalia kwenye muziki, watu wengi hasa wanawake unakuta mavazi wanayovaa pale ni tofauti na wanaume, wao watavaa suti nzuri na tai safi kabisa, lakini wanawake wanavaa vibaya! Leo mtawaambia nini wakati hakuna vazi lililoteuliwa? Tunaomba mtakapokuja, tena Mheshimiwa Naibu Waziri,yeye ni mwanamke, kwa sababu inapotokea kudhalilishwa, hawadhalilishwi wale walioko pale na wanawake wengine wote wanaozunguka kwenye jamii hizi tunapata aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, lilizungumzwa sana siku ya Ijumaa suala la Mwenge. Naomba Mheshimiwa Waziri aje anipe ufafanuzi kidogo. Kwenye Mkoa wangu wa Rukwa Wenyeviti wamekamatwa kwa kutochangisha pesa za Mwenge. Naomba kujua, ni sheria ipi ilitumika kuwakamata Wenyeviti hawa kwa kutochangisha pesa za Mwenge? Kwa sababu kitu kinachoitwa mchango kwa mimi ninavyoelewa, ni hiari siyo lazima. Sasa ni sheria ipi ilitumika kuwakamata Wenyeviti hao wa Serikali ambao hata mshahara hawalipwi; na kila siku tunajadili hapa, hakuna siku imepitishwa Wenyeviti wataanza kulipwa mshahara au posho. Sasa ni sheria gani ilitumika kuwakamata Wenyeviti hawa? Naomba kauli ya Serikali Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kichwa changu bado hakijakaa vizuri. Ahsante kwa nafasi uliyonipa kutoa mchango huo.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini napenda pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunifikisha siku ya leo salama na kuchangia Wizara muhimu sana kwa wananchi wangu wa Mkoa wa Rukwa. Tunapozungumzia kilimo, tunazungumzia kitu muhimu sana ndani ya Taifa letu, tunazungumzia kitu muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa, lakini pia tunatazama hali ya uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika haya mazingira tunapozungumza kilimo kunajambo la msingi ambalo ni bajeti. Bajeti ni tatizo; na hata tutakapochangia mambo mengi hapa tunarudi pale pale kwenye bajeti, tutatoa maelezo mengi ushari mwingi suala linarudi pale pale kuhusu bajeti.

Naomba utakapokuja Mheshimiwa Waziri wa Kilimo utuambie mikakati uliyonayo tofauti na miaka iliyopita. Hali ya chakula umeiona, hali ilivyo mbaya unajua ingawa imefikia mahali sasa mnatoa kauli za kufurahishana tu unamfurahisha aliyekutua wakati wananchi wanaumia, tukizungumza hapa zinakuwa story tu kama story zingine za kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kilimo; sasa hivi ukiwatazama watumishi wa Serikali hawategemei tu mshahara, wamejiingiza kwenye kilimo kwa sababu wanajua kilimo kinalipa; kilimo ndiyo kila kitu. Sasa kama tutashindwa kuwekeza kwenye kilimo tutaondokaje kwenye hii hali tuliyonayo? Pembejeo ni shida, kuna suala tunazungumzia kila kipindi cha bajeti; Benki ya kilimo. Kama maeneo ambayo yanazalisha hiyo Benki haipo, hata wakulima hawaijui tunamalizaje tatizo hili? Hawajui waanzie wapi wala waende wapi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kila tunapozungumza majibu yanakuwa ni yale yale. Mimi naomba utakapokuja utuambie angalau mikakati mipya ambayo unayo ili kukitoa kilimo hapa kilipo na hatimaye tuinue uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuzungumzia kilimo kwamba wananchi wa Rukwa wananufaika wakati hujawaambia kwamba kwa kipindi hiki ambacho wanategemea kuvuna watauza wapi. Suala la masoko ni muhimu kuliko suala lingine. Sasa hivi tunaendeshwa kwa matamko tu, akipita Mheshimiwa Rais anasema hivi, halafu wewe Waziri wa Kilimo unakuja na matamko mengine, sasa hawa wakulima wamebaki dilemma, yaani hawajui wamsikilize nani? Wamsikilize Mheshimiwa Rais wakusikilize wewe Mheshimiwa Waziri wa Kilimo?

Mheshimiwa Naibu Spika, na haya mambo lazima yawekewe utaratibu. Tunajua itifaki zilivyo, lakini tunapozungumzia uchumi kuna watu ambao ni wataalamu panapokuwa na siasa pia tuwasikilize wataalamu hawa, wakulima tunawakatisha tamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pembejeo tumekuwa tunalizungumza kila siku na hakuna majibu ambayo yanaonesha mwelekeo moja kwa moja wa kuondokana na haya matatizo ambayo wanayapata wakulima juu ya pembejeo. Tunaomba Serikali ipeleke pesa kwa wale wanaonunua pembejeo kwa wakati ili muda ukifika yale maduka yauze kwa bei ya ruzuku na wasaidie wale wakulima. Nilizungumza hapa, ukitazama Mkoa wa Rukwa mkiwapa pesa wale wakulima wanaopata shida, hawana hata pesa za pembejeo, mkiwapa kipindi cha mwenge hamjawatimizia malengo yao; wapeni kipindi cha kilimo ziwasaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, zitawasaidia wanawake zitawasaidia vijana pia. Kuhusiana na suala hilo utakaa tu wewe na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, mkatoa tu mwongozo ukafika kule. Sijajua Kiswahili ambacho kinaweza kikawasaidia ni kipi kwa sababu kama maneno tunasema mambo mengi tunazungumza lakini bado utekelezaji unakuwa mgumu. Kipindi nasema nakuja kuchangia Mbunge mmoja akaniambia unaenda kuchangia nini? Nikajiuliza maswali kwa nini ananiambia naenda kuchangia nini, nikamwambia naenda kuchangia kilimo; nini kwenye kilimo, bajeti yenyewe ndio hii! Nimetafakari sana, lakini tutasema tu kwa sababu ndiyo kazi yetu kusema, kama mtasikia sawa msipo sikia sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ajira Tanzania ni shida kwa vijana, vijana hawa wanategemea kilimo, kilimo chenyewe kina matatizo, tuambieni hawa vijana mnawapeleka wapi? Yaani kilimo hamjawasaidia, ajira hakuna mnataka waende wapi?

Mheshimiwa Waziri tunaomba mikakati ya kutosha, yaani hali ya kilimo haifurahishi ingawa unakuja hapa unatuambia hali ya chakula iko vizuri, siju iko vizuri wapi? Kwa sababu ukiangalia bei ya mahindi ya mwaka wa jana, bei ya mahindi kwa kipindi hiki sasa msimu huu wa kilimo bei yake unaiona halafu unasema hali ya chakula, Mheshimiwa Waziri unamfurahisha nani yaani?

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani haya mambo unakuwa unamfurahisha nani kwa sababu hali halisi inaonekana. Ni bora ukasema ukweli tukusaidie kama suala ni bajeti hupewi pesa sema tukusaidie ndiyo kazi yetu. Lakini ukija hapa ukafanya mambo ya kufurahishana hatimaye tutaanza kuonana wabaya hapa, tunaweza tukakutuhumu kumbe kosa si wewe kosa ni bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya wakulima na wafugaji yaani umekuwa waimbo, hivi mnataka mtuambie kwamba mmeshindwa kabisa kuwa na mikakati ya kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji? Wataalamu wanafanya kazi gani? Yawezekana ninyi ni wanasiasa, wataalam wenu wameshindwa kuwasaidia jinsi ya kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji au mpaka leo hamjajua tatizo lililopo kati ya wakulima na wafugaji ni nini? na kuna migogoro mingine inachangiwa na ninyi wenyewe Serikali kwa kutokufanya maamuzi haraka ya kumaliza midogo kabla haijawa mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali tena leo yawezekana ikawa mara ya mwisho. Suala la ardhi, ardhi tunajua ni ndogo na watu wanazidi kuongezeka tupeni sasa mikakati ya kumaliza migogoro hii yawezekana ndugu zenu hawajaumizwa, lakini kuna watu wamekufa .
Roho inakuwa inauma tunapokuja kuwaambia nyinyi hamsikii mnataka tuseme nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningefurahi kama Mheshimiwa Waziri wangu vile ambavyo huwa anaonyesha anasikia tukizungumza leo tunapokuja kipindi kingine tunakuja na kauli nyingine lakini kauli ni hizi hizi na mambo haya haya hivi usikivu unafanyika wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishauri tu, yale maamuzi ya kwenda kununua ndege yawezekana yalikuwa sahihi, lakini kama kilimo ni kipaumbele maamuzi yale yalikuwa batili. Huwezi kupanda ndege una njaa, huwezi kupanda ndege una utapiamlo, kama kilimo kilikuwa cha kwanza ni bora basi mngechukua nusu kwanza muingize kwenye kilimo na nyingine iende huko kununua hiyo ndege. Kwa sababu tunasema kilimo ndiyo kipaumbele. Sasa maji ni shida, kilimo cha umwagiliaji kinapatikanaje?

Pembejeo ni shida, bajeti yenyewe uliyopewa shida, haya kwenye masoko yenyewe mpaka leo hamjasema lakini toka acha wakulima wauze bei wanayotaka, sawa watauza halafu wakiuza hiyo bei kwa sababu shida sio bei shida ni pesa hakuna hata hiyo bei atakayopanga nani ataenda kununua hela hamna. Kwa hiyo, kunamazingira mengine matamko haya hayasaidii na yenyewe yanatengeneza migogoro tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya hali ya hewa imekuwa ndiyo kisingizio, hawa watabiri wa hali ya hewa nao wanaweza wakatusaidia au wakatuathiri, kwa sababu wakulima wanapokuwa wanakwenda kulima wanataka kujua mwaka huu mvua ni nyingi au chache, wanatakiwa kuambiwa walime nini kulingana na hiyo hali ya hewa ya kipindi hicho. Sasa hayo mazingira yanapokuwa yanajitokeza na wakulima nao wanaanza kulima kwa mazoea. Ukitazama hii bajeti ina maana kwa kipindi hiki cha mwaka 2016/2017 wakulima walikuwa wanafanya kazi wao binafsi, ni kama Wizara haipo, kwa utekelezaji huu, Wizara haijawasaidia chochote.

Mheshimia Naibu Spika, suala hili sasa hivi mawakala kule Mkoa wa Rukwa hawajalipwa mpaka leo, kuna watu wameuziwa nyumba zao, kuna watu wamefilisiwa. Lakini kosa sio la kwao ni kosa la Serikali kwa nini inashindwa kuwalipa. Mheshimiwa Waziri ni vyema ukawa mkweli na muwazi tukusaidie. Tukiwa tunazungumza hapa masuala ya kilimo uti wa mgongo sijui kilimo kwanza yaani kauli nyingi ambazo haziendani kabisa na mazingira ya kilimo chenyewe kinavyokwenda. Ni vyema mkawa mnatoa matamko yanayoendana na mazingira mliyonayo. Lakini ukisema hamna pesa wala si dhambi kwa sababu utakuwa umesema ukweli… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naunga mkono taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo na taarifa zote zilizowasilishwa. Siko mbali sana na wajumbe waliotangulia, kwanza nampongeza Mheshimiwa Goodluck kwa mara ya kwanza ameonesha ukomavu wa kisiasa kwamba msimamo wake unabaki pale pale. Kila mhimili unapaswa kuheshimiwa na lazima tulisimamie hilo, hatuwezi kukubali. Kuna kitu kimenishangaza sana, Maazimio ya juzi tu hapa lakini naona kuna watu wameanza kugeuka, Bunge hili hili, juzi tu hapa, kuna nini kimetokea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado tutaendelea kusema ukimtuhumu mtu ambaye ana watu wengine nyuma hujamtuhumu yeye, tunachokizungumzia sisi ni kwamba sheria zifuatwe. Kuna watu wanaohusika na hayo mambo wafuate utaratibu, sheria ziko wazi. Makonda hawezi kumwita mtu yeyote angeagiza Jeshi la Polisi lifuate utaratibu kuwaita hao watu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika mazingira ya kawaida kama kuna Mbunge ametuhumiwa, sisi tulivyoambiwa tunalala msifikiri ni mtu mmoja alisikia, ni wananchi ambao wako nyuma yetu wamejua kwamba sisi tunalala usingizi. Sasa kama tunakubaliana na Makonda kwamba kweli tunalala usingizi, kiukweli mimi binafsi kama Aida, sisi Wafipa tuna misimamo yetu, mimi siwezi kukubaliana hata siku moja. Kama kuna mtu anajua amefanya vizuri kwa kusubiri uteuzi, sisi wengine hatusubiri uwaziri hata siku moja hatusubiri, tutasimamia ukweli. Kama kuna watu wanafanya hayo mambo hakuna mtu anafurahishwa ila afuate utaratibu mambo mengine yaendelee. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye taarifa ya Kamati, niongelee kuhusu Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Ndugu zangu Wabunge pale ndipo sheria zinachapwa, mtu yeyote ambaye unahusika na mambo haya ukienda kuona pale na ukaacha unafiki, ukatimiza wajibu wako kama Mbunge utaelewa hiki ninachokizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa Jenista Mhagama kama kweli kuna utumbuaji kitu gani kinazuia kumtumbua yule mtu pale kwa sababu mambo yako wazi kabisa inakuwaje siri za Serikali zinakwenda kutolewa nje, kuna kitu gani kinaendelea? Tunaishauri Serikali ifanye utaratibu unaowezekana, kama mmefanya haraka kuhamia Dodoma mpaka kwenda kwenye Chuo cha UDOM, fanyeni haraka kutafuta utaratibu wa kudhibiti mazingira ya pale, kwa sababu tu moja, kwa maslahi ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la wanasheria wetu, yawezekana shida ni taaluma waliyo nayo au hakuna utaratibu wa kuwaangalia hawa wanasheria wa Halmashauri jinsi wanavyowajibika. Kuna watu wamehukumiwa kwa sheria hizi za Halmashauri ambazo ziko kinyume kabisa na sheria mama. Tunaishauri Serikali kuna kila sababu ya kufanya semina kwa hawa wanasheria wa Halmashauri kama kweli tuna nia njema. Kwa sababu yawezekana wanafanya kwa kutojua au kwa makusudi kwa sababu wanajua mmewatelekeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukiangalia hata kesi nyingi za Halmashauri, nimewahi kukaa siku moja nikajiuliza kwa nini kesi nyingi za Halmashauri tukienda mahakamani tunashindwa? Kuna mambo mawili hapa, yawezekana wanasheria wenyewe wanapiga deal na hawa watu waliopeleka kesi mahakamani au Wakurugenzi wanapokuwa wanafanya shughuli zingine wanashindwa kuwashirikisha wanasheria. Haya mambo lazima tuyatazame kwa maslahi ya Taifa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawasiliano ya Simu. Kulingana na umuhimu wa mawasiliano kwa binadamu ili kuweza kutimiza malengo yao kwa wakati ni vema Serikali ikamaliza tatizo kwa kupeleka minara ya simu kwenye maeneo ambayo bado hayajapata mawasiliano. Kwa mfano Jimbo la Nkasi Kusini, Wilaya ya Nkasi iliyopo Mkoa wa Rukwa, Kata ya Kala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Meli ya MV Liemba. Meli hii imekuwa ya muda mrefu na imechoka, Serikali kwa nini isituletee meli mpya ili kuokoa maisha ya wananchi wa Ziwa Tanganyika? Suala la barabara inayotoka Sumbawanga – Kanazi limechukua muda mrefu na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotoka Namanyere, Kilando, Kabwe na maeneo mengine ya Wilaya ya Nkasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Kiwanja cha Ndege cha Manispaa ya Sumbawanga. Mpaka sasa wananchi wa Sumbawanga wanashindwa kuendelea na shughuli zao wakisubiri kulipwa baada ya tathmini. Nashauri Serikali baada ya tathmini, iwalipe wananchi hawa na kama kuna matatizo ya kifedha basi waruhusiwe kuendelea na shughuli zao za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Usalama katika Bandari; kuna kila sababu ya Serikali kufanya tathmini ya kutosha katika maeneo ya bandari, kwa sababu kumekuwa na changamoto na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wafanyakazi wa bandari. Suala la fedha kutofika kwa wakati, nalo linakera, ni tatizo kwenye maeneo mengi nchini na kupelekea usumbufu mkubwa kwa kutomaliza miradi mbalimbali ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Barabara Kujengwa Chini ya Kiwango; suala hili limekuwa endelevu katika mikoa yetu. Nashauri Serikali iwachukulie hatua wakandarasi wote wanaofanya kazi chini ya kiwango na kutoa taarifa kwenye maeneo mengine ili wawafahamu wakandarasi wazuri na wabaya ili wasirudie kuwapa kazi wakandarasi wasio na sifa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kusimama wakati huu nikiwa na afya njema. Napenda kumshukuru aliyewasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani na Waziri kwa kutambua umuhimu wa kilimo nchini Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napenda kusema miongoni mwa wakulima tunaowazungumzia leo ni pamoja na wakulima wa Mkoa wa Rukwa. Kuna shamba ambalo Wabunge wangu wa Mkoa wa Rukwa wamelizungumza kwa miaka kadhaa humu ndani, tena ni wa Chama cha Mapinduzi, yawezekana hamkuwasikiliza kwa sababu ni Chama cha Mapinduzi leo nasimama kupitia CHADEMA kuzungumzia shamba hilo hilo ili mtambue kwamba ni suala ambalo linawagusa wananchi moja kwa moja, shamba la EFATHA, Manispaa ya Sumbawanga, Kijiji cha Isesa imekuwa ni sehemu ya watu kwenda kufanya kampeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili limetamkwa hapa ndani akiwa Waziri Mkuu Pinda kwamba anakwenda kulishughulia, lakini mpaka leo hakuna kilichofanyika. Sijajua speed mlionayo Chama cha Mapinduzi na kama mna nia njema na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga. Wananchi wale kwa sababu ni miongoni mwa watu waliowapa kura na sasa mnajiita ni kazi tu mmeacha porojo nendeni mkashughulikie suala lile, muache story mfanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitazungumzia suala moja ambalo ni kero kubwa kwa Watanzania hasa wakulima. Mimi ni miongoni mwa watoto waliotoka kwa wakulima tena wanaolima kilimo cha mkono. Nasikitika Waziri hayupo hapa alisema anataka jembe likae kwenye jengo la kumbukumbu, lakini angejua kwamba Manispaa ya Sumbawanga asilimia kubwa ya wakulima wanalima kwa mkono wanapata gunia mbili au tatu kwa mwaka lakini wanalipa kodi kwenye nchi hii wakati huo huo ni miongoni mwa wakulima ambao wanapata mateso mpaka wanajiona ni kama wakimbizi ndani ya nchi yao. Analima kwa mkono, kutoa mazao yake shambani kuyapeleka sokoni anakamatwa njiani alipie kodi. Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Rais alipokuja hapa alipokuwa anazindua Bunge alizungumzia habari ya tozo zisizokuwa na tija, lakini mpaka leo kama mlikuwa serious mngekuwa mmeonyesha hatua. Hakuna kitu, zimekuwa ni story za miaka yote.
Mimi nawashauri, siku hizi Watanzania wanaelewa mnapotamka kitu mwende kwa vitendo, msitamke tu halafu mkanyamaza, mnapotamka tayari Watanzania wamesikia wanabaki kusubiri utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao haya tunayozungumzia ndugu zangu Wabunge tukiwa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo kuna mkulima analipia mpaka mwenge, huu mwenge unakwenda kumsaidia nini mkulima, unammulikia nini shambani? Imefikia mahali hizi tozo hata wanaosimamia inaonekana kama kuna hali fulani ya upofu wa kutokutazama mbele. Wakulima hawa ni miongoni mwa watu ambao wanachangia pato kubwa la Taifa katika nchi hii, mmekuja na kauli mbiu nyingi sana lakini kauli mbiu hazijasaidia chochote imebaki story tu na mnaongoza kwa kupanga vitu kwenye karatasi, lakini utekelezaji mna zero positive. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la masoko, unapozungumzia viwanda, Waziri wangu naona ametoka, alisema Sumbawanga atajenga kiwanda, mimi nataka nimwambie Mkoa wa Rukwa tunalima mahindi, maharage, ngano na ulezi na pia kuna wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapozungumzia Serikali ya viwanda mpaka leo mmetoa elimu kiasi gani kuonesha kwamba mko serious na viwanda mnavyovizungumza? Kwa sababu hata wakulima wataona mnachokizungumza ni sawa na story za siku zote walizowahi kusikia. Kama elimu hamjatoa, halafu mnawaambia kwamba wao wanatakiwa kujenga viwanda wakati hawajaona utofauti wa wao walivyokuwa wanalima na leo unavyowaambia kwamba wapeleke kwenye viwanda, viwanda vinawasaidia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikaji wa pembejeo, sidhani kama huwa hamsikii siku zote tunavyokuwa tunawashauri. Kabla sijaingia kwenye hili Bunge mmeshauriwa mara nyingi sana. Kuna sehemu mpaka mnawaambia Wenyeviti wa Serikali washiriki kuandaa zile Kamati. Ukitazama Mkoa wa Rukwa hasa Manispaa ya Sumbawanga, huyo Mwenyekiti anayeshughulikia pembejeo, halafu mnapokuja mnakuwa mmeweka watu wenu mnaowajua, analipwa shilingi 5,000 baada ya miezi mitatu. Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa leo inamkopa hiyo shilingi 5,000 kwa miaka mitano..
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niwaambie Serikali ya Chama cha Mapinduzi kama mko serious na mnatambua umuhimu wa kilimo katika nchi hii nendeni mkafanye utafiti kwanza. Unapozungumzia viwanda lazima ujue kabla ya viwanda wananchi walikuwa na changamoto zipi. Kama soko mlishindwa kutafuta mlipokujana na kauli mbiu ya kilimo kwanza ikawa kilimo mwisho, viwanda leo vitakwenda kumkomboa Mtanzania kwa style ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la hawa Maafisa Kilimo kuna wengine wako mjini na Mkoa wa Rukwa utakuta wale wakulima hawamfahamu. Yeye faida yake kuwepo kule ni nini, hakuna faida ambayo mkulima anaiona. Inabidi tusiwalaumu wataalam hawa, yawezekana hamjawawezesha wanawafikiaje wakulima hawa. Kwa hiyo, nawashauri Chama cha Mapinduzi kama mna nia njema na wakulima wa nchi hii hasa wa Mkoa wa Rukwa wawezesheni hawa Maafisa Kilimo wakatimize wajibu wao wa kutoa elimu kwa wakulima hawa ili kilimo hiki kilete tija ndani ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la utabiri wa hali ya hewa, yawezekana ni Nyanda za Juu Kusini peke yake, Mkoa wa Rukwa kipindi cha nyuma walikuwa wanalima kutumia utabiri wao wa kawaida, wa Kifipa ule, wakitazama ndege wanajua kwamba safari hii kuna mvua nyingi au chache lakini walikuwa wanapata vizuri kuliko leo wakiambiwa kuna mvua nyingi wanapolima mvua haiji. Naomba hawa watabiri wa hali ya hewa utabiri wao uwe ni wenye tija, usiwe na hasara kwa Watanzania na wanapofanya utabiri wasifanye utabiri wa Dar es Salaam kwani huko hakuna wakulima, wafanye utabiri kwa kuangalia wakulima wa vijijini hasa Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la uvuvi kwa sababu wavuvi pia wako Mkoa wa Rukwa. Wavuvi katika Taifa hili hususani Mkoa wa Rukwa imekuwa ni Mkoa ambao wamenyang‟anywa sana vifaa vyao kwamba ni haramu, hivi viwanda vinavyozalisha hivi vitu hamjui viko wapi? Yawezekana hata kodi mnachukua lakini mkifika mnawaambia vifaa vyao ni haramu, kwa nini msiende kwenye viwanda vinavyozalisha?
Mimi naomba kuwaambia hawa Watanzania wapo kama ninyi ambao leo ni Mawaziri lakini mlikuwa kama wao na mlitazame hili kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia kwamba na wao wanastahili kuishi kwa amani katika nchi yao wasijione kama wakimbizi ndani ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Ziwa Rukwa amelizungumza jana Mama Maufi, yule ni Mbunge wa Chama cha Mapinduzi, hili suala limesemwa sana humu ndani na Mbunge wa Kwela, sasa tunaomba tunapowaambia mchukue hatua. Inafikia mahali mnapokuwa mnajiita ninyi ni Serikali sikivu hata mtu ambaye alikuwa haelewi anajitokeza kuja kusikiliza kwamba huyu anayesema anasema kitu gani kwa sababu kama mmeambiwa mara moja, mmeambiwa mara ya pili kitu gani kinazuia msiende kutekeleza, shida ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bajeti ya kilimo mnayokuwa mnatenga kama mna nia ya kuboresha kilimo, hizi fedha ni za wapi, mkitegemea fedha za nje mnakwenda kufanya nini au mnakuja kucheza comedy hapa ndani ya Bunge na kutudanganya? Huwezi kupanga kwenda kufanya kitu unategemea mhisani akupe fedha wakati wewe hujajipanga una kiasi gani? Kama mko serious kweli basi Taifa litazame kwamba kilimo ni uti wa mgongo kama mlivyokuwa mmesema mara ya kwanza. Mambo mnayofanya hayafanani na hiki mnachokizungumza. Niombe kauli mbiu zenu ziendane na kile mnachokifanya. Hatutachoka kuwashauri lakini msiposikia tutatumia kauli nyingine ya kuwaambia maana kauli ya kawaida naona ni ngumu sana kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu, hivi mnaweza mkaboresha kilimo bila kuwa na miundombinu ya uhakika? Kwa mfano, Wilaya yangu ya Nkasi pale Namanyere toka Mheshimiwa Rais wa leo akiwa Waziri alitamka hapa akasema Wafipa hawajawahi kuona hata lami, nilijua anatania maana alisema watani wangu mpaka leo hakuna lami, kwa hiyo, alikuwa serious kwamba kweli Wafipa watabaki kuwa hivyo. Kwa hiyo, nawashauri hawawezi kulima halafu hawana barabara ambayo itawafanya wafike sokoni kupeleka mazao yao. Muwe serious kutazama kwamba kilimo kinakwenda sambamba na miundombinu na mfanye hayo mkiwa mnamaanisha kwamba kweli mpo serious kuboresha kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri mambo kadhaa katika Wizara hii muhimu katika maendeleo ya nchi yetu ili kuleta tija kwa kizazi hiki na kizazi kijacho, kuboresha maslahi ya Walimu kulingana na umuhimu Mwalimu katika kuboresha elimu nchini ni lazima Mwalimu aweze kulipwa stahiki zinazostahili kulingana na hali halisi ya maisha kwa sasa. Kulipa madai ya Walimu kwa wakati kulingana na Sekta ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanapocheleweshwa kulipwa madai yao kwa wakati inapelekea Walimu wetu wengi kukosa utayari wa kufundisha kama ilivyokuwa mwanzo, wanakata tamaa. Mfano, Manispaa ya Sumbawanga iliyoko Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia ya kutowalipa Walimu pesa ya likizo na kupelekea kuona kama wanatengwa. Suala la Afisa Elimu kumwadhibu Mwalimu, hali hii imeendelea kuonyesha manyanyaso makubwa kwa Walimu wetu kwa mfano dalili iliyojitokeza hivi karibuni katika Wilaya ya Sumbawaga Mkoa wa Rukwa. Serikali inachukua hatua gani kwa Afisa Elimu huyu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuleta ufanisi katika Wizara ya Elimu katika Taifa letu, suala hili la kodi kwenye Wizara hii imepelekea ada kuwa kubwa zaidi na hivyo Watanzania wa hali ya chini kushindwa kumudu katika ada husika. Mwingiliano wa Wizara kuwa na chanzo cha tatizo kutokana na changamoto nyingi zinazowapata Walimu wanafuzi pamoja na miundombinu kutokana na mambo hayo kutoshughulikiwa na Wizara moja, imekuwa changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Kitengo cha Ukaguzi kutokuwa na vifaa vya kuweza kuwafikia Walimu na kutimiza majukumu yake na kupelekea kuleta matokeo chanya katika Wizara moja ambayo itashughulikia haya yote, suala la mikopo katika Elimu ya Chuo Kikuu kuna vigezo gani vinavyotumika kutoa mikopo hii ambayo imekuwa na malalamiko makubwa hasa kwa watoto wanaotoka familia za kimasikini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI, upandishwaji wa madaraja katika Sekta hii ni lazima Wizara ifanye marekebisho. Suala hili linaleta mkanganyiko mkubwa hasa katika Manispaa ya sumbawanga. Hii ilitokana tu na uzembe wa vyombo husika. Hatua zichukuliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Waraka Na. 5, elimu bure, liende sambamba na miundombinu, ada elekezi kulipa madai yote ya Walimu, mikopo hata kwa Walimu walioamua kujiendeleza ili kuondokana na ujinga na kukomboa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha elimu tujiulize mambo yafuatayo katika Wizara hii ya Elimu. Nini chanzo cha elimu yetu kushuka? Nini kinazuia kulipa madai ya Walimu? Kwa nini Walimu hawawezeshwi katika matibabu? Kwa nini mitaala yetu ni tatizo? Kwa nini ada elekezi leo? Lini Wizara itatoa Motisha kwa Walimu wa vijijini? Ni lini Serikali italeta mashine ya kuchakata vyeti nchini?

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na umuhimu wa Wizara ya Ardhi napenda kushauri mambo yafuatayo ili kuepukana na migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika Mkoa wa Rukwa na nchi nzima kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi yaboreshwe kulingana na utendaji wanapokuwa katika Mabaraza ya Ardhi. Kutokuwa na elimu ya kutosha kumepelekea kupata migogoro mingi katika Halmashauri zetu. Hati za kimila, mara nyingi zimekuwa hazitambuliki kwa baadhi ya watendaji katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Manispaa ya Sumbawanga iliyopo katika Mkoa wa Rukwa na Wilaya zake, kata na vijiji pamoja na mitaa na vitongoji vyake. Serikali ina mkakati gani wa kuwapa semina watu hawa ili kuondoa migogoro, kuwawezesha Maafisa Ardhi, kwa kuwapa vitendea kazi. Maafisa Ardhi hawa wamepelekea migogoro mikubwa sana katika Halmashauri zetu kwa kutomaliza mogogoro kwa wakati na mahali pengine kutokea migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya wawekezaji na wananchi, kulingana na migogoro hii kutokea kila eneo katika nchi yetu, nashauri Serikali kutafuta njia sahihi ya kumaliza migogoro hii ya wawekezaji na wananchi kwa kuweka njia shirikishi kuanzia ngazi ya chini ili kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro kwa wananchi wa Isesa na mwekezaji, huu ni mgogoro wa muda mrefu uliopo katika Manisapaa ya Sumbawanga Mjini na Vijijini, suala hili limechukua muda mrefu hata kwenye kitabu cha Waziri mgogoro huu haupo, naomba Wizara ichukue hatua haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fidia kutokuwa wazi, kutokuwalipa wananchi fidia kwa muda muafaka inapelekea migogoro mingi katika Halmashauri zetu kutokana na taarifa tufauti na kupelekea migogoro isiyo ya lazima, nashauri Serikali kutoa fidia kwa wananchi na kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kutoa hati kuchukua muda mrefu, kutokana na hali hii kushamiri hasa katika Mkoa wa Rukwa, Manispaa ya Sumbawanga na ili kuondoa tatizo hili Serikali imegundua tatizo hili, imegundua ni nini linalochelewesha? Pia migogoro kati ya wakulima na wafugaji nashauri Serikali kupima maeneo nchi nzima ili kuepukana na tatizo la migogoro inayoendelea na kupelekea vifo mbalimbali vinavyotokana na migogoro hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi ya ardhi katika Manispaa ya Sumbawanga kulingana na suala hili kuwa na hali ya kutokuwa na usimamizi mzuri wenye uwazi ili kuondoa migogoro isiyokuwa na tija. Suala la ushirikishwaji ngazi za mitaa, hali hii ya kutokushirikishwa hasa kupewa ramani na kuyajua maeneo ya wazi ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza bila sababu.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa watumishi katika hospitali zetu nchini suala hili limekuwa ni tatizo kubwa sana katika Wilaya zetu. Kwa mfano, Wilaya ya Kalambo, Nkasi, Sumbawanga Mjini na Sumbawanga Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu saratani ya shingo ya kizazi, suala hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa wanawake wa Kitanzania na kasi yake ni kubwa sana, lakini bado hatujaona Serikali ikiipa kipaumbele kulingana na tunavyopoteza wanawake wengi hasa walioko vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukosefu wa dawa kwenye hospitali zetu, hili limekuwa ni tatizo kubwa, Serikali ifanye utaratibu wa kufuatalia kama dawa zipo katika hospitali za vijijini. Wizara ipeleke dawa ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sheria ya Ndoa, kuna sababu ya kuleta mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ili kuokoa maisha ya watoto wetu wa kike kwa kukosa mambo ya msingi ikiwemo elimu, kwani wakiingia kwenye ndoa wakiwa na miaka 18 itapelekea kukosa elimu.

Kuhusu ukatili kwa wanawake, kwa kuwa ukatili huu umekuwa ukiendelea kwa kasi hasa kwa watoto wa kike wakiwa shuleni, mitaani na nyumbani, je, Serikali inaleta mkakati gani wa kumaliza tatizo hili la ukatili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vya wanawake wajawazito hakuna mkakati wa dhati wa kumaliza tatizo hili na kuona wanawake hasa waliopo pembezoni na wanawake wa vijijini, Serikali iweke kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uzazi wa mpango, kuna kila sababu ya Serikali kutoa semina elekezi hasa kwa maeneo ambayo bado elimu hii haijawakomboa kwani kumekuwa na upotoshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kwa kupitia Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Afya ili kuboresha na kujenga vituo vya afya kwa kila kata na hospitali za Wilaya hasa katika Mkoa wa Rukwa hakuna Hospitali za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kuzingatia, kukosekana kwa hospitali hata moja ya Wilaya katika Mkoa wa Rukwa kunapelekea mlundikano wa wagonjwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Rufaa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naungana na wachangiaji wote waliopita kwa suala la kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Tusipoanzisha Wakala wa Maji Vijijini, tutaimba nyimbo za siku zote ambazo hazitapatiwa majibu. Tukianzisha wakala tutaepusha malalamiko mengi ambayo yanajitokeza kwenye vijiji.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo ni vigumu sana kuweza kuyakamilisha kwa sababu suala la maji linahitajika maeneo yote. Wanafunzi hawawezi kukaa darasani kwa muda wote kama maji hayapo. Pia, kilimo tunachokisema kila siku kama uti wa mgongo na majina mengi ambayo tumejipa, hatuwezi kukidhi malengo kama suala la maji halitapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali, unajua tumekuwa na vipaumbele vingi, hebu tukae tuangalie kipaumbele ambacho Watanzania wanakizungumza. Leo kama maji ni kipaumbele cha nchi hii, hatuwezi kupunguza bajeti, tungeongeza bajeti. Inaonesha ni jinsi gani mambo tunayoyazungumza hapa ni kama kuna watu wengine washauri tena tofauti na Bunge. Suala la maji tulizungumza, tunazungumza tena, lakini kuna mambo ambayo yanapewa vipaumbele nje na yale ambayo Wabunge wanazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Serikali, ni vyema wakazingatia basi yale ambayo tunayazungumza. Ukitazama hili suala la maji haliko upinzani, haliko chama tawala, wote tunazungumza maji, maji, maji. Tunaomba basi tupate mikakati ya Serikali, angalau basi wawe wanatusikia na kutusikia ni pale wanapojibu yale tunayoyazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia vyeti fake, kuna bili fake, sijui kama Waziri anajua. Kama maji hayapo lakini bili zinasoma, zinasomaje? Kwa hiyo, kipindi wenziwe wanazungumzia vyeti fake, yeye ajue kuna bili fake! Naomba aje hapa atuambie kama maji hayapo bili zinakujaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye Mkoa wa Rukwa lazima wakae pamoja Wizara tatu, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Mazingira. Mkoa wa Rukwa hatujawahi kulia njaa hata mwaka mmoja lakini kinachotokea saa hizi kwa ajili ya kufurahishana, yaani anakuja mtu wa mazingira, wananchi wamelima mahindi, anawaambia wakate wamelima kwenye vyanzo vya maji. Ni kweli hatukubali kulima kwenye vyanzo vya maji lakini watuambieni Serikali wametenga eneo gani mbadala wananchi wakalime? Hatulimi bangi bali mazao ya chakula. Tunahitaji wakae pamoja waje na majibu ya kueleweka ya kuwasaidia Watanzania. Ni kweli wanaepusha vyanzo vya maji visiharibiwe lakini wanataka watu wafe na njaa? Waje watupe majibu ya uhakika Watanzania wa Rukwa wajue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nimwambie kwa taarifa tu Mheshimiwa Waziri, mwaka jana tu wanawake 12 wamepoteza maisha kwa kufuata maji umbali mrefu. Leo tunazungumzia maji hayohayo tena tayari bajeti imepungua wakati maji bado hawajapata. Leo mimi nakujaje


namshangilia hapa Mheshimiwa Waziri wakati wanawake walionipigia kura wanapoteza maisha na bado hana mikakati yoyote ya kuonesha mazingira rafiki ya kuwasaidia maji. Tunaomba majibu ya kuridhisha ambayo yatawasaidia Watanzania.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huu tunazungumza kuna wanawake ambao wamefariki, kuna wanawake ambao wamebakwa, kuna wanawake ambao wameathirika kuhusiana na ndoa zao, kuna wanawake ambao wamepoteza mapato, huu muda wanaofuata maji wanashindwa kufanya biashara wanaanza kuhangaikia maji. Mheshimiwa Waziri tunaomba na Waziri anayehusika na upande wa watoto, Wizara ya Afya, hakuna kitu kitawezekana bila maji. Kwa hiyo, wanapokaa pamoja waangalie basi, maji ni kipaumbele hakuna mambo mengine. Nakushukuru.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na umuhimu wa Wizara hii ya Maliasili na Utalii ambayo inachangia pato kubwa kwa Taifa letu, kuna kila sababu ya kubadilisha utaratibu wa kuendesha Wizara hii ili kuongeza idadi ya watalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubadilisha aina ya matangazo kutokana na hali ya ushindani ni mkubwa sana, ni vyema Serikali ikabadilisha utaratibu wa matangazo kwa vivutio vilivyopo nchini kwa kutumia njia kama shuleni, ngazi ya msingi, sekondari na vyuo vikuu na vyuo vya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu ili kupata watalii wengi nchini kwa kutengeneza miundombinu ambayo itakuwa rafiki kwa watalii wanaokuja nchini ili kuongeza idadi ya watalii na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wananchi kulingana na migogoro ambayo inaendelea nchini katika maeneo mbalimbali ikiwemo Simanjiro ambao umechukua muda mrefu sana kupeleka mifugo na wananchi kuuawa, ni vyema migogoro hii ikamalizwa kwa wakati na bila kuathiri haki ya binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya hifadhi ichunguzwe upya kwani idadi ya watu imeongezeka lakini maeneo ya hifadhi pamoja na mapori tengefu wakati ardhi ni ile ile. Hivyo, nashauri Serikali kupitia upya mipaka hiyo ya maeneo ya hifadhi ili kuwatendea haki wananchi wanaoishi karibu na hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na uzoefu na matatizo mengi yanayotokea katika maeneo ya hifadhaji ili utekelezaji wa yale waliyokubaliana yafikie malengo, suala la bajeti kufika kwa wakati kulingana na umuhimu wa Wizara hii ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu za kiuchumi katika nchi yetu, ni vyema bajeti ikatolewa kama ilivyotengwa na kupitishwa na Bunge na iende kwa wakati.

Suala la kushirikiana na Wizara nyingine ambayo ni Wizara ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Kilimo ili kuweza kuwa na mkakati wa kudumu wa kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi na watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, manyanyaso kwa wananchi wanaopita katika hifadhi kulingana na hali iliyopo katika maeneo mbalimbali wanatakiwa kupewa elimu na siyo maamuzi na hatua kali zinazochukuliwa kwa mifugo na wananchi wetu.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda na elimu. Kulingana na umuhimu wa kuwa na viwanda nchini kwetu, ni lazima kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuanzisha viwanda na faida zitakazopatikana baada ya kuwa na viwanda nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuboresha kilimo. Kulingana na utaratibu wa viwanda ni vyema wananchi wakabadili utaratibu wa kilimo cha mazao na badala yake walime au kuanzisha kilimo chenye tija kwa ajili ya kuhudumia viwanda vitakavyokuwa vinazunguka maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda na ajira kwa vijana. Ili suala la viwanda lifanikiwe ni vyema elimu ikatolewa zaidi kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa ambao watanufaika na viwanda badala ya kuchukuwa vijana wa nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha elimu ya viwanda mashuleni. Kulingana na umuhimu wa suala la kuanzisha viwanda ni vyema kama wanafunzi katika masomo wakawa na elimu au mada juu ya kuanzisha na kuendeleza viwanda nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwawezesha wakulima. Kwa kuwa viwanda vingi na kwa asilimia kubwa vinategemea kilimo na ili suala hili la viwanda lifanikiwe ni vema wanawake wakulima wawezeshwe kuanzisha viwanda hata kama ni vidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda na mazao ya biashara. Ni vema Wizara ya Viwanda na Biashara kuwa na mkakati wa kudumu na endelevu kwa kuwa na viwanda bora vya kuandaa mazao ya biashara ili kilimo kiweze kuwakomboa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha vyuo vya VETA Mkoa wa Rukwa. Vyuo hivi vitasaidia vijana kupata ujuzi utakaosaidia kuendesha viwanda vitakavyoanzishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, masoko ni tatizo kubwa kwa wakulima hasa wa Mkoa wa Rukwa mpaka wanaelekea kukata tamaa kutokana na changamoto hii. Naomba Serikali ishughulikie suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ifufue viwanda vilivyokufa vya nguo, nyama, maji na kilimo (pembejeo).

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, bili ya maji. Kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba bili za maji ni tofauti na ilivyokuwa awali, pia hata kusoma wanakuwa wanakadiria tu na kupelekea kuleta hali ya sintofahamu kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mita za maji kuchezewa. Suala hili limekuwa ni tatizo na mambo haya yanafanywa na watumishi wenyewe wa Idara ya Maji au watu wanaokuwa wafanyakazi wa Ofisi za Idara ya Maji kwenye Halmashauri zetu na mikoa yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uharibifu wa vyanzo vya maji. Elimu inatakiwa kutolewa kwa wananchi wetu ili wajue athari za kuharibu vyanzo vya maji kwani hatuwezi kukomesha tatizo hilo bila kutoa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya maji ni mibaya. Suala hili linahitaji Wizara tatu kukaa kwa pamoja ili kuimarisha tatizo la maji katika Halmashauri zetu. Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya uvunaji maji ya mvua. Kumekuwa na matatizo sugu ya ukosefu wa maji katika Mkoa wa Rukwa wakati mvua zimenyesha na kusababisha mafuriko na kuua watu na maafa. Kwa nini Serikali isiwe na utaratibu wa kuhifadhi maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo, Mifugo na uvuvi na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kukaa pamoja na kupanga utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka vyanzo vya maji kulima mazao ambayo hayataathiri vyanzi vya maji na pia kutowaathiri wananchi kupata njaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa Idara ya Maji wasio waaminifu wamepelekea malalamiko makubwa kwa wananchi kwa kuwapa vifaa vibovu au kuchezea mita na kusababisha bili zisizo na uwiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji itengeneze mita kama ilivyo LUKU za umeme ili kuondoa malalamiko kwani kila mtu au mteja anajua amelipa kiasi gani na ametumia kiasi gani kumaliza kabisa malalamiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu. Ili kulinda vyanzo vya maji, wananchi wakielimishwa vizuri juu ya kulinda vyanzo vya maji matatizo mengi yataisha au kupungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa iliyotengwa ni ndogo iongezwe kulingana na umuhimu wa maji katika maeneo mengi nchini. Pesa iliyotengwa haiwezi kumaliza tatizo la maji nchini. Nashauri Serikali iongeze pesa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na nchi yetu kuwa na mahusianao na nchi mbalimbali duniani kuna kila sababu ya kuboresha maeneo muhimu ili kudumisha mahusiano makubwa na yenye manufaa kwa nchi yetu ikiwemo yafuatayo:-

Kwanza, kuunganisha soko la ndani ya nchi yetu na masoko ya nje kwa kufanya uboreshaji wa mazao yanayozalishwa nchini, kuyapandisha thamani ili yaweze kutumika nchi nyingine ambazo tuna uhusiano mzuri na nchi yetu, kupata manufaa kwa kupitia masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kupeleka wanadiplomasia wenye uwezo. Kutokana na mazingira halisi ya nchi yetu ni vema wanadiplomasia nafasi zao zikawa na faida kwa nchi yetu, kwa kutumia uwezo wao kuchukua mambo ya nchi nyingine na kuyaleta nchini kwetu yalete manufaa. Kuwa na utaratibu wa kuunganisha Watanzania wanaoishi nchi za nje kulingana na kauli mbiu ya Awamu ya Tano, kauli mbiu ni viwanda ni vema Wizara hii ya mambo ya nje kuangalia ni jinsi gani watasaidia Taifa kuendana na kauli mbiu ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni namna gani Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi kubeba ajenda ya utalii ili Taifa letu liweze kunufaika na watalii, endapo kama Wizara itaweza kutangaza na kubeba ajenda ya utalii ili kupata fedha za kigeni pamoja na kujenga uhusiano mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Watanzania wanaoajiriwa nje ya nchi hususan kazi za ndani, wamekuwa wakiuawa na kuteswa na kunyanyaswa ni vema Wizara ikawa na mipango endelevu ya kumaliza na kufuatilia kwa ukaribu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa wanafunzi wanaosoma nje ya nchi ni mdogo sana, Wizara ni vema pamoja na Mabalozi waweze kuangalia kwa ukaribu wanafunzi wote na kuwapa misaada ambayo inaweza kuwa ndani ya uwezo wao.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ni kitu muhimu sana katika nchi yetu na dunia nzima kwani kila kiumbe kinachoishi duniani kiko chini ya ardhi ambapo kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zinaikabili Wizara hii ambayo ni lazima kuwepo na mikakati ya makusudi kumaliza changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji; suala hili limekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi yetu ambayo imesababisha madhara makubwa sana ikiwemo vifo kwa wakulima na wafugaji na pia kwa wawekezaji hasa kama hakukuwa na ushirikishwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mipaka, ni vyema Wizara ikawa na utaratibu madhubuti wa kupitia upya mipaka ya maeneo mbalimbali ikiwemo vijiji na vitongoji lakini maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji pamoja na maliasili zote ili kuondoa migogoro mbalimbali inayoweza kujitokeza katika maeneo yetu. Upatikanaji wa hati miliki, suala hili limekuwa na changamoto kubwa hasa kwa wananchi wa vijiji ambao makazi yao hayajapimwa, na kumekuwa na urasimu mkubwa kwa maafisa wa ardhi katika Halmashauri mbalimbali nchini ikiwemo Mkuu wa Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Maafisa Ardhi kwenye Halmashauri ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga; nashauri Serikali kuongeza Maafisa Ardhi kwenye Halmashauri mbalimbali nchini ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima. Kutolewa mafunzo kwa Maafisa Ardhi na Maafisa Mipango Miji ili kuweka ufanisi katika maeneo na kazi zao ambao hazitaleta usumbufu kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upimaji wa ardhi, suala hili limekuwa na changamoto kubwa, lakini linatokana pia na maafisa ambao sio waaminifu kwa kujipatia viwanja ambavyo Halmashauri na Serikali kwa ujumla hazinufaiki kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa hati kuchukua muda mrefu na kupelekea mianya ya rushwa suala hili limekuwa likiwakatisha tamaa wananchi ambao hawana hati miliki. Nashauri Serikali kufuatilia suala hili kwa ukaribu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba; kuna changamoto kubwa hasa kwa suala la gharama kwani gharama za nyumba zinazojengwa ni kubwa ambazo wananchi wakiwemo wa Mkoa wa Rukwa hawawezi kumudu kabisa nyumba zijengwe kulingana na jiografia husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji wapewe ramani ili wayajue maeneo yao. Hii kwa kiasi kikubwa itachangia kuondoa migogoro isiyo na sababu.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na kauli mbiu ya Serikali ya viwanda ni vyema tukaboresha Benki ya Kilimo na kuifikisha mikoani ili wakulima waweze kukopesheka ili waweze kujikomboa kimaisha na kufikia malengo ya viwanda katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu soko la uhakika la mazao, kutokana na nchi yetu kuwa na idadi kubwa ya wananchi ambao ni wakulima wamejikita kwenye kilimo cha mazao ya chakula na mazao ya biashara ambayo yamekosa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta binafsi, Serikali inapaswa kushirikisha sekta hii katika taratibu za kukuza uchumi katika nchi yetu ili waweze kuwa mfano na wengine waweze kuwekeza katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya maliasili na utalii, kulingana na umuhimu wa sekta hii ya utalii ni muhimu ikatazamwa kwa umakini mkubwa kwani tukiwekeza kwa kufanya tafiti za kutosha tutaweza kupata fedha nyingi za kigeni kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ipewe kipaumbele katika shughuli zote za maendeleo kwa kuwawezesha wakulima kwa kuwapa pembejeo, mtaji na elimu ya kuachana na kilimo cha mazoea badala yake kiwe cha kisasa. Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, Serikali ijielekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuelekea kwenye nchi ya viwanda kuepuka kilimo cha msimu ambacho hakitabiriki na kinaweza kisifikie malengo ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya madini, kulingana na umuhimu wa viwanda ni vyema Serikali ikawekeza kwenye utafiti ili wanavyuo wanapomaliza masomo yao waweze kusaidia Taifa la Tanzania kwa upande wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Deni la Taifa, ni vyema kama Taifa tukawa na utaratibu wa kukopa mikopo ambayo haiwezi kuwatesa Watanzania wote. Tutaweza kuepuka kero hiyo kwa kukopa kwa wazabuni wa ndani ambayo haitakuwa na kero kubwa.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's