Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Esther Nicholus Matiko

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipatia fursa hii kuweza kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/2017.
Awali ya yote, nachukua fursa hii ya kipekee kabisa kuwashukuru wananchi wa Tarime Mjini, kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe kuweza kuchagua mwanamke tena kutokea Chama cha Upinzani. Wameudhihirishia ulimwengu kwamba wamechagua mtu ambaye atawasemea na kuwatumikia na siyo jinsia. (Makofi)
Vilevile nawashukuru wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kuonesha kwamba wana imani kubwa na UKAWA; na CHADEMA wote mtakumbuka kwamba Bunge ililopita alikuwepo Mbunge mmoja tu wa kuchaguliwa, lakini sasa hivi tupo Wabunge wanne kutoka Mkoa wa Mara licha ya dhuluma nyingi nyingi, lakini nafikiri CCM mmeisoma namba kidogo kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuchangia na nianze na utawala bora. Kwenye utawala bora, wakati wa uchaguzi yalijitokeza mambo mengi sana. Cha kusikitisha, hata Mheshimiwa Rais Magufuli alisema uchaguzi umeisha na mambo yameisha; lakini mpaka leo wale ambao wanaonekana walikuwa washabiki wa vyama vya upinzani, wameendelea kunyanyasika, wanakamatwa na wanabambikiwa kesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea hili nikizungumzia Jimbo langu la Tarime Mjini. Kuna wananchi wamebambikiwa kesi, wengine wamepewa murder case ya binadamu ambaye anaishi na ameenda akasema kabisa huyu mtu sijawahi kukosana naye na wala sijafa na nipo hai. Huyu anaitwa Charles Kitela Chacha na amepewa mashitaka ya murder mwenye PI No. 37/2015. Utawala bora uko wapi? Mtu ambaye wanasema ni Marehemu ameuawa anaitwa Wambura Ryoba Gucha, yupo hai wa Kijiji cha Turugeti, Tarime. Tunaomba muwe na utawala bora ili haki itendeke; na kama tutaenda kwenye demokrasia na uchaguzi muweze kupata haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, Chama tawala kinasikitisha. Mnapoona wapinzani wameshinda, mnawawajibisha watendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninavyoongea, Tarime, Watendaji wanawajibishwa, walimu wanasumbuliwa, RPC amehamishwa, OCD amekuwa demoted kisa Mheshimiwa John Heche kashinda Tarime, Mheshimiwa Esther Matiko ameshinda Tarime; Halmashauri ya Mji wa Tarime upo CHADEMA; Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, upo CHADEMA. Utawala bora upo wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata watu wakisimama hapa wakaongea yanayotokea upande wa pili, nami nikipata muda baadaye nitazungumzia, mnabaki mnaona kwamba wanaongea ndivyo sivyo mjichunguze, mwitendee haki Tanzania. Tunataka amani, tusiimbe amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine sasa nichangie kuhusu uchumi na viwanda. Tumekuwa tukishauri; Bunge lililopita nilikuwa Waziri Kivuli wa Mipango na kwa bahati nzuri sana ambaye ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mpango alikuwa akituletea. Atakuwa ni shuhuda na amekidhihirisha hiki ambacho naenda kuongea kwamba mnapanga vitu bila uhalisia. Hiki kitu ambacho tunasema uchumi na viwanda hakiwezi kufanikiwa kama tunapanga vitu bila uhalisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Tunajua kabisa ili tuweze kuwa na uchumi na viwanda ni lazima tuwe na barabara ili hata wale wazalishaji, wakulima waweze kusafirisha mazao yao na kufikisha kwenye viwanda. Lazima tuwe na reli imara, lazima tuwe na umeme, maji na vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara ukiangalia ukurasa wa 27 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 mnatuambia kipengele cha pili ujenzi mpya wa barabara zenye urefu wa kilometa 5,427 na kukarabati barabara zenye urefu wa kilometa 1,055 kwa kiwango cha lami. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 mnaweza mkajenga kilometa 5,427 iwapo kwa miaka mitano mmetujengea kilometa 2,700.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhalisia gani? Ndani ya mwaka mtajenga Kilometa 5,400! Let’s be realistic! Ndiyo maana leo tutapoteza nguvu nyingi kuwashauri hapa; tutapoteza fedha nyingi za Watanzania, mnachokiandika hakioneshi uhalisia. Kwa hiyo, naomba kabisa, tuwe tunaonesha uhalisia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmeainisha reli nyingi, nyingi! Mimi natokea Kanda ya Ziwa na ningependa kabisa reli ya kati iweze kukamilika ili tuweze kupunguza ajali. Siyo tu kukuza huu uchumi wa viwanda ambao mnasema; jana walisema hapa miundombinu ya barabara haichangii vifo, lakini kiuhalisia tunapoteza nguvu kazi ambazo tumezisomesha, wengine ni ndugu zetu ambao ni wajasiriamali wa kawaida, wanakufa barabarani kwa sababu ya barabara mbovu. Malori yanapita hapo hapo, ajali nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imarisheni reli ili tusafirishe kwa reli. Kwanza tunakuza uchumi lakini hatutapoteza Watanzania. Ninachokiona mmeainisha hapa, tutarudi hapa mwezi wa sita mwakani, mtaanza kusema hatukupata fedha na asilimia nyingi za maendeleo zilikuwa zinatoka kwa wahisani; na sijui sekta binafsi; tutaanza kuimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bora mwandike mtajenga kilometa 300 za lami tutawaelewa, kuliko kutuandikia 5,400 halafu tunakuja hapa mwakani hamjafanya chochote. Tunapenda sana Watanzania tuwe na hiyo mnayosema uchumi wa viwanda; tunapenda kuona Watanzania wengi wakiwa kwenye uchumi wa kati na siyo wachache wapo juu, wachache ni masikini wa kutupwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na uchumi wa viwanda nimeshataja. Kuhusu kilimo chetu; zaidi ya 70% Watanzania tunajishughulisha na kilimo, lakini kilimo ambacho hakina tija. Ile kauli mbiu ya kilimo kwanza tumeiimba, tumeicheza hakuna mafanikio. Mkisoma ripoti zenu zenyewe kuhusu kilimo inaainisha dhahiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni shida ingawa mmesema Mpango ulioisha umekamilisha kwa 68% vijijini na 95% mjini. Ndiyo maana nasema tuwe wakweli. Leo kule Tarime Mjini ukiyaona maji utafikiri ni ubuyu, tuje na uhalisia! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pensheni kwa wastaafu. Mwaka 2015 tulipitisha tukasema walipwe shilingi 100,000/=, lakini kuna watumishi tena Mapolisi ambao mnawatumia sana, wanalipwa shilingi 20,000/= mpaka leo. Sasa mlipokaa hapo mjiulize, hawa Watanzania wanaishi vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kampeni Mheshimiwa Magufuli alisema na hata kwenye Star TV mlikuwa mnarusha sana; ushuru wa kero kwa maana mboga mboga, matunda, mama ntilie na wengine wote mnaenda kuondoa. Leo Watanzania hawa wananyanyasika; na alisema pia mgambo watatafuta kazi nyingine. Mimi nasema mnisikilize na mwondoe wale mgambo kwenye Jimbo la Tarime Mjini. Watanzania wote, wamama, wababa, vijana wanaojitafutia wamachinga, mlisema ushuru mdogo mdogo mtaondoa. Tubuni vyanzo mbadala tusiwakamue hawa ambao wana kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure, mimi naomba mseme mmepunguza makali ya elimu, lakini siyo elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda ni mchache, nimalizie kwa Zanzibar; ingawa watu walisimama hapa wakasema sisi wa Bara tusizungumzie ya Zanzibar. Kiukweli tujichunguze, kiuhalisia, tena nianze na Mheshimiwa King siku ile alisema kwamba maiti walipiga kura. Kama maiti walipiga kura, ajiulize na yeye huyo maiti alipiga kura tano. Yeye kama Mbunge wa Jamhuri amefuata nini hapa na yeye alipigiwa kura na maiti? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni sawa na kumwambia muislamu, umepika kitimoto, umechanganya na kuku, unamwambia achukue kuku, aache kitimoto, wakati ile supu yote imechanganyikana. Mmechambua kuku ambao ni wale Wabunge wa Jamhuri na Rais, mmeacha wale Wawakilishi kwamba ndio kitimoto. Jichunguzeni! Kama ni maiti alipiga kura, amepiga kote. Tutendee haki Watanzania wa Zanzibar, tusiingize nchi kwenye machafuko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi. Mmeainisha mtapima ardhi, tunaomba mfanye hivyo. Ardhi imepimwa kwa 10% tu, kule Tarime Mjini tunahitaji mpime ardhi ili tupate thamani tuweze kukopa na kujishughulisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Mheshimiwa Magufuli kwenye kampeni alisema atatoa shilingi milioni 50 kwa kila Kijiji na Mtaa. Sijaona mmeainisha; naomba mwainishe, wananchi wa Tarime mimi nina Mitaa 81, ili tuanze kuzipata hizo shilingi milioni 50 kuanzia mwaka huu wa fedha, tuweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia kwanza kwa kuangalia ni nini kimetekelezwa kwa Mpango wa Kwanza. Ukiangalia kiuhalisia Mpango wa Kwanza haujatekelezwa kwa asilimia 60 kama ambavyo mmeandika. Ni kwa nini nasema hivi? Mfano mdogo tu kwenye hotuba ya Waziri anatuambia kwamba maji vijijini yameenda kwa zaidi ya asilimia 72 kwamba wananchi wa vijijini zaidi ya milioni ishirini wamepata maji.
Mheshimiwa Spika, sasa mimi nikawa nauliza ni Tanzania ipi imepata maji safi na salama? Mkoa wa Mara, Wilaya ya Tarime, Mji wa Tarime siyo tu vijijini hata mjini hakuna maji. Ile Sera ya mwaka 2002 kwamba maji unapata ndani ya mita 400 ni ndoto. Kwa hiyo, kama takwimu zenyewe ndiyo hizi ni dhahiri mtakuja mtasema mmetimiza kwa asilimia 60 lakini kiuhalisia hakuna kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo mme-document hapa kwamba fedha za maendeleo sasa hivi zitakuwa zinaenda kwa asilimia 40 ya bajeti. Mkumbuke Mpango wa Kwanza tulisema asilimia 35, lakini mtu asimame aniambie kama Serikali hii na naomba sana msiwe mnasema Serikali ya safari hii ya Awamu ya Tano imedhamiria as if sasa hivi ni chama kingine, ni Chama hicho hicho cha Mapinduzi ndiyo mlikuwepo miaka yote…
MHE. ESTHER N. MATIKO: Msitake kutu-fake Watanzania mnakuja hapa mnasema ooh, sasa hivi tumedhamiria, nikiangalia cabinet iliyopo sasa hivi over sixty percent ni ile iliyokuwepo Awamu ya Nne. Mkumbuke kwamba hata Awamu ya Nne tulikuwa tukiongea hapa tukiwashauri, baba yangu Mheshimiwa Wasira alikuwa anakuja hapa anatubeza kwenye Mpango, nilikuwa Waziri Kivuli wa Mpango na bahati nzuri aliyekuwa kwenye Mpango ndiyo Waziri wa Fedha na Mpango sasa hivi. Halafu mkikaa mnasema sasa hivi hii Serikali ina dhamira ya dhati, come on, are you serious? Watu wale wale, chama kile kile tumekishauri, over sixty percent Mawaziri mliokuja madarakani ndiyo wale wale labda mmebadilishwa tu, ulikuwa Waziri wa Katiba na Sheria sasa hivi ni Waziri wa Afya, ulikuwa sijui wapi sasa hivi umeenda pale. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, sasa leo tukisema kwamba tulidhamiria kuimarisha miundombinu ya barabara ambayo ndiyo inaenda kuchochea uchumi wetu na mtu aka-document tukasema Rais, Mheshimiwa Magufuli ndiye aliyekuwa Waziri kipindi hicho na nakumbuka katika vitu ambavyo vilipewa kipaumbele ni ujenzi wa barabara, lakini ndiyo mmejenga kwa asilimia hamsini na tatu.
Mheshimiwa Spika, hivyo ambazo hatukuvipa kipaumbele sana asilimia 20, asilimia sijui ngapi! Asilimia tatu! Halafu tunaishia kuwa na mipango. Kwanza nilikuwa najiuliza, kuanzia jana na-postpone tu. Maana yake nasema nachangaia nini? Tunatoa ushauri, tunasema but nothing is going to be done. Tunachangia nini?
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba sana, tukisimama tuwe kama Wabunge, acha Mawaziri watakuja watajibu kama Serikali. Nashangaa Mbunge anasimama anatetea kweli! Kaka yangu wa Mkuranga, documents za Kambi ya Upinzani, tulicho-document kimetokana na alichokiandika Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, sasa ukianza kusema, nikasema anajidai aah, sijui zimeongezeka 500. Ongeza hizo 500, zinakuwa ni 3000. Sasa 3000 kwa miaka mitano, leo unazitekeleza vipi?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, taarifa!
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, naomba nishauri na naomba...
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, taarifa!
SPIKA: Taarifa iko upande gani?
MBUNGE FULANI: CCM.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Kulia kwako.
SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Mabula....
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kwa heshima zote kabisa mdogo wangu katika hili Bunge, hajitambui. Ikumbukwe CCM ikichukua takwimu za Urais wanapataje, imeanzia 81% imeshuka mpaka Mheshimiwa Magufuli amepata 58%, tena questionable! Questionable! (Kicheko/Makofi)
Kingine, huyo huyo wakati Uenyekiti unabadilishwa badilishwa, wakati Mheshimiwa Mnyika anasema kwamba ule uongozi wa Mheshimiwa wa Kikwete ni dhaifu, ninyi mlisimama na kusema na kufedhehesha kila kitu! Leo yaani mnajikosoa ndani yenu wenyewe. Tunafurahi sana na wananchi wanawaona na wanasikia kwamba hamfai! Niendelee! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kwenye nishati ambacho ni kichochezi kwenye viwanda. Mpango uliopita, yaani mlikuwa mmedhamiria mnaleta Megawatt 2,780, lakini mpaka tunavyoongea miaka mitano ni Megawatt 496 tu. Hivi viwanda tunavyoongea tunaenda kuvipataje, kama nishati yenyewe bado ni goigoi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo kule kwetu Tarime ni wakulima na wafugaji. Tunahitaji hata viwanda, tuwe na umeme. Kwa mwendo huu, tutafikaje? Halafu tukiishauri Serikali hapa kwamba tuwe na vitu ambayo tukiviongea vina tija, watu wanaweka… nyie Wabunge, mmekuja kama Wabunge, wajibikeni kama Wabunge, acha Mawaziri watende. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yaani kiuhalisia nikipitia sekta zote, kwenye elimu ndiyo kabisa! Siku ile Mheshimiwa Rais alisema hapa kwamba viwanda ambavyo anadhamiria na ambavyo vitaajiri Watanzania, vitatumia nguvu kazi zaidi kuliko teknolojia ya kisasa. Kwenye Mpango, matarajio yetu kwenye VETA tu hayajafikiwa kwa kiwango kikubwa sana. Sasa leo tuseme tuna Mpango mkakati upi ili uweze kutuaminisha kwamba hii dhamira ya dhati tuliyonayo tutafikia? Mimi mwenyewe natamani sana Tanzania tuweze kukua kiuchumi, wananchi wengi hawana ajira. Tuna rasilimali nyingi, lakini zilikuwa zinakumbatiwa tu na wachache huko, zinatumika vibaya.
Mheshimiwa Spika, sasa kama kweli hiyo awamu ya tano ina dhamira ya dhati na kwa sababu bajeti hii tunaenda kuongea mambo mengi Wizara mbalimbali, tutaenda kuipima kama ina dhamira ya dhati. Kweli kama ina dhamira ya dhati ya kuwasadia Watanzania, Mheshimiwa Waziri tunaomba hayo uliyoyaandika utuainishie kwamba tunamaanisha. Asilimia 40 zinaenda kwenye maendeleo, tumejizatiti vipi kwenye kodi?
Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 wakati nachangia bajeti hapa nilimweleza mfano tu, Mama Sada. Nenda hapa kwenye supermarket moja Dodoma, umenunua vitu, hakupi ile risiti ya TRA, akaenda, akafuatilia akapata.
Mheshimiwa Spika, hawa Usalama wa Taifa, leo ukinunua vitu hawakupi risiti za TRA. Juzi tu nimenunua kitu Kariakoo Sh. 620,000/= nikawaambia wanipe risiti ya TRA, ooh, risiti ya TRA tukikupa inaenda zaidi ya hapo. Sasa si hii ndiyo bei umeweka kwenye duka lako? Ndiyo! Unajua aliniambia basi naomba nikupe sh. 100,000/= halafu sh. 520,000/= nikuandikie ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, Usalama wa Taifa, ninyi kama Wizara mnadhibiti vipi hilo? Tunapoteza mapato mengi sana. Hii mnayosema sijui risiti za electronic, hazifanyi kazi, wanaziweka kando. Mtanzania akienda, anamwambia nitakupa hiki, fanya punguza, shell, yaani kote tunapoteza mapato and then mnakuja tu mme-document ma-paper; tupe sign mnakusanya vipi kodi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haitoshi tu Mheshimiwa Rais kusimama kwenye TV, Tanzania lipa kodi. Mmeweka mechanism gani kuendeleza hii ya Mheshimiwa Rais anayosema kila siku kwenye TV kwamba kodi itakusanywa kweli? Wekeni watu waende kwenye maduka! Ajidai kama ananunua kifaa, aone kama atapewa hiyo risiti au atapewa lugha gani? Kamata, fanya vyote nchi nzima, watu walipe kodi, siyo kuwanyanyasa watu wadogo wadogo, wajasiriamali wenye vimbogamboga, wenye miradi midogo midogo ndio wanaoleta fedha kwa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilisema mwaka 2015 kwamba, worthiness ya mtu i-reflect ulipaji wa kodi yake. Sijui hata wamefanya nini? Mnatangaza watu wawe na TIN, sijui kila mtu awe na TIN: Je, kweli kila Mtanzania ana-TIN? Mimi kwa mfano, Esther Matiko, worthiness yangu ina-reflect nalipa kodi vipi? Do you trace that? Kama hamtaweza kukusanya mapato ya ndani na wafadhili wenyewe ndiyo hivyo, hii mipango, miaka mitano tunakuja hapa, patupu! Tena leo bora tunaambiwa zimepikwapikwa ziko asilimia 60. Tukija mwaka 2019 hapa tunaelekea 2020 tutaambiwa story zile zile.
Mheshimiwa Spika, nimalizie. Tuwe na nishati, tuboreshe miundombinu ya barabara kama mnataka hivi viwanda kuanzia kule kwa mkulima, barabara zipitike. Tuboreshe reli.
Mheshimiwa Spika, ukija kwenye Air Tanzania, aibu! National Carrier, aibu! Ukisafiri, ukaenda na hizi ndege, ukifika Nairobi, wanashuka watalii wote mnakuja Tanzania wachache. Wakishafika pale, ina maana zile hoteli za Kenya ndio wanafaidika. Wanaletwa na magari kuja kwenye mbuga zetu za Tanzania. Hata juzi niliona wanasema, hata daraja la Kigamboni ambalo mmelizindua jana, watasema liko Kenya. Mlima Kilimanjaro Kenya, mengine yote Kenya. We are not branding our Nation. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Samatta ni mchezaji sijui wa wapi huko, what are we doing? Tuwe serious! Tutafute vyanzo ambavyo vinatuletea mapato. Sekta ya Utalii, let„s have our National Career. Hatuna National Career! Ni wafanyakazi tu wamebaki na jengo pale city center tena ambalo lipo kwenye prime area, mliendeleze basi! Tunabaki tu na vijistori, tutaleta, tutaleta. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa Jimbo langu la Tarime. Kwanza kabisa, naomba kabisa kipekee nimshukuru Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Najua kama wanavyojinafasi humu ndani, mkijivua kweli, ile ambayo tumekuwa tukiwashauri miaka yote, mnasema kelele za chura hazimnini sijui nini; sasa kweli mkiamua kufanya hivyo, siyo kama maigizo kwa sababu mnaona Mheshimiwa Magufuli anavyofanya, mtafika mbali.
Mheshimiwa Spika, ndugu yangu pale huwa anavaa zile scarf za Kitanzania na nini, kweli yule ni mzalendo sana. Amekuja Tarime, ameongea mambo mengi sana na Wanatarime.
Kama kweli hiyo dhamira itaenda kutendeka kama ni ya Serikali hii, rasilimali tulizonazo zikageuzwa kuwasaidia Watanzania, maana yake tumekuwa tukiongea, pale kuna Soko la Kimataifa, tumekuwa tukipiga kelele humu mimi na Mheshimiwa Nyambari, limechukua miaka mingi kumalizika, liko Lemagu; lile soko lingemalizika, ingekuwa ni kipato kikubwa sana kwa nchi yetu. Liko border pale! Mnachukua muda mwingi sana kumaliza lile soko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzetu Kenya wanachukua hiyo opportunity, ukienda upande wa pili wa Kenya ni tofauti kabisa na Tanzania. Lile soko likikamilika, ule mnada ukafunguliwa, kipato ndani ya Mji wa Tarime, kipato ndani ya Wilaya ya Tarime kitaongezeka na Taifa linaenda kupata fedha ambazo leo zitatumika kusaidia hayo madawati na kujenga Maboma. Maana yake mmesema elimu bure, kule kwetu hakuna vipato. Havipo Tarime Mjini! Sasa mnahangaisha watu kujikusanya maskini wale wajenge viboma; watoto wanasoma 200 kwenye darasa moja. tupeni lile soko lifunguliwe, mnada ufunguliwe, kipato kiongezeke.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kipekee kabisa namshukuru ndugu yangu, kaka yangu pale, naomba na Mawaziri wengine, mmepewa ridhaa na Watanzania, mnatumikia nchi. Maana kuna mwingine nilisikia ooh, pale sijui CHADEMA, sijui CUF hatupeleki maendeleo. What?
Mheshimiwa Spika, hizi rasilimali ni za kwetu wote. Wale Watanzania wote wametuweka wote madarakani. Ninyi mmepewa ridhaa ya nchi, kuna wengine wamepewa ridhaa za Majimbo na Halmashauri. Tunatakiwa tuwatumikie wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nafikiri ushauri wangu mkiuzingatia, vichochezi vya kuanzisha viwanda, viwepo; nishati, miundombinu ya barabara na kilimo mkiboreshe, Sekta ya Elimu ili tuweze kupata hao watu ambao tunasema tunaenda kuwatumia, reli na usafiri wa anga. Ndoto ya Waziri wa Fedha na hii Mipango mnayotuletea, itatimia. Kinyume cha hapo, tutakuwa tunacheza vidogoli tu siku zote. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwa ufupi tu kuhusiana na maombi yangu ya kupandisha hadhi Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC) kilichopo Tarime Mjini kuwa VETA. Chuo hiki kwa sasa kinatoa huduma kwa wananchi wa Tarime nzima Rorya na Serengeti. Hivyo ili kuendana na azma ya Serikali ya Tanzania ya viwanda ni lazima vyuo vya ufundi viwe vingi. Tumekuwa tukiomba chuo hiki kuwa cha ufundi ili tuweze kukidhi hitaji la muda mrefu wa kuwa na chuo cha ufundi, tutashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni wimbi kubwa la walimu toka Kenya wanakuja kufundisha shule binafsi za Tarime. Hiyo tunaomba Wizara iingilie kati maana tunao Walimu wa kutosha kuweza kuajiriwa, hivyo vibali vinatolewaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa elimu kuanzia sera za elimu, mitaala yetu pamoja na miundombinu yetu, inatoa taswira pana ya nini tufanye kama Taifa kwa ufupi tu. Tarime tumejenga Maabara hatuna vifaa wala wataalam wa maabara, tuna uhaba wa Walimu wa Sayansi na ndiyo maana watoto wanafeli. Tusiangalie Quantity tuangalie Quality. if we need to have quality education then input lazima ziwe effective. Madaftari, vitabu, madawa, madawati, walimu wenye motivation, nyumba za walimu na posho ya ziada, posho ya pango, posho ya safari na usafiri, kupandishwa madaraja, chakula mashuleni, ukaguzi wa shule zetu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi ni hayo, mengi yamechangiwa naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja hii katika kuonesha ni jinsi gani sanaa na michezo inaweza kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa. Leo hii Taifa lingehakikisha tuna viwanja vya kutosha kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Mikoa na vyote ni vya kisasa, si tungekuza soka na michezo mingine kama ridhaa, basketball, volleyball, netball na mingine mingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, enzi zetu wakati tunasoma, michezo ilikuwa na hamasa na shule zote za msingi na sekondari zilikuwa na viwanja vya kutosha. Michezo mbalimbali ilikuwa ikichezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni wakati sasa viwanja ambavyo vinahodhiwa na CCM virudi kwa Serikali ili viendelezwe na kuweza kuleta tija. Ni muhimu kwa sababu hivi vilijengwa enzi ya chama kimoja ambapo ni fedha za Watanzania zilitumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuiomba Serikali angalau watusaidie kuboresha uwanja wa Wilaya Tarime ambao upo pale Tarime Mjini, kwani umetelekezwa na kubaki kutumika kwenye mikutano ya hadhara badala ya michezo husika. Uwanja una sifa zote za kuweza kuchezwa ligi za daraja la kwanza na ukiboreshwa utasaidia sana kukuza uchumi. Hivyo, natoa rai yangu kwamba Serikali ishirikiane na Halmashauri ya Mji wa Tarime ambayo tayari wameshatenga fedha kiasi kidogo kwa ajili ya uboreshaji wa uwanja wa Serengeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni dhamira ya Halmashauri ya Mji wa Tarime kujenga shule ya michezo kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini. Hivyo tumeomba Serikali ione umuhimu wa sports accessory ziweze kuwepo nchi nzima na kwa wale walio tayari kama Tarime Mjini wapewe vipaumbele. Bila shule za michezo huwezi kukuza vipaji kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tuwekeze kwenye sanaa na wasanii wa kuigiza na kuimba nyimbo ambazo zitakuwa na tija kwao. Mfano, wanamuziki wetu wana vipaji vizuri sana lakini uhalisia wa maisha yao hayaakisi kipato ambacho Watanzania wengine wanavyopata nje ya nchi ni nyingi tofauti na wanazopata hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tuwekeze kwenye tamaduni zetu ambazo zinaweza kuwa pia kumbukumbu ya tamaduni zetu. Siku hizi tamaduni zinapotea kabisa; ngoma za jadi zinapotea na mambo mengine ambayo yangekuwa kivutio kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi naomba majibu, ni jinsi gani Serikali imejipanga katika hoja hii na nyingine?

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwanza kabisa kabla sijachangia nitoe masikitiko yangu kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo kwa kweli inajisifu kwamba ni Serikali ya Hapa Kazi Tu. Imezuia television isionyeshwe lakini yet tuko ndani tumejifungia sisi wenyewe, bado mnazuia taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani isisomwe. Inaonesha ni jinsi gani hamjiamini, hamjajipanga na hamjajua ni nini mnataka mlifanyie Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi; kuna mambo makuu mengi sana ya kuyazungumzia na kwa sababu ni dakika kumi, naomba nianze na Jeshi la Magereza. Ni dhahiri kwamba kwenye Jeshi letu la Magereza sheria ambazo zinatumika sasa hivi ni zile ambazo zilikuwa zikitumika wakati wa ukoloni; ni sheria ambazo zimepitwa na wakati. Leo unaweza ukakuta Askari Magereza kwa bahati mbaya, mahabusu au mfungwa ametoroka, atapewa adhabu labda ndani ya miaka mitatu tuseme, ambayo adhabu moja ya mfungwa kutoroka anatakiwa akatwe mshahara wake, nusu ya mshahara au robo ya mshahara, anatakiwa ashushwe cheo, anatakiwa asiende masomoni kujiendeleza na hata ikitokea huyo aliyekimbia amekamtwa, bado huyu Askari Magereza atatakiwa atumikie hiyo adhabu kwa miaka yote ambayo amepangiwa. Hii ni dhuluma na haikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo mzima wa uendeshaji wa Jeshi la Magereza kiukweli unatakiwa ufumuliwe upya. Tunahitaji kufumuliwa upya kama walivyofanya kwenye idara nyingine. Kuna malalamiko mengi sana ambayo yamekuwa yakiendelea. Hata bila kufumba macho, ni dhahiri kwamba Commissioner General wa Prison amekuwa akilalamikiwa sana. Naomba kabisa mchunguze hayo malalamiko ambayo yako dhidi yake, myafanyie kazi. Kwa sababu tumekuwa tukizungumza, mnapuuzia, baada ya muda ukija kuchunguzwa, ripoti ya CAG inatoa yale ambayo tunayalalamikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wote wa Umma tumekuwa tukijaza hizi fomu za maadili, mwachunguze mali wanazomiliki, mishahara wanayopewa ina-reflect uhalisia wa mali ambazo wanamiliki? Kuna ufisadi mkubwa sana ambao unaendelea kwa Viongozi Wakuu wa haya Majeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, makazi ya Askari ni duni sana. Mwaka 2015 wakati wa bajeti nilizungumza hapa na mkasema kwamba mlikuwa mmetenga kujenga zaidi ya makazi 9,000. Leo tunavyozungumza, Waziri umekuja unatuambia mnajenga makazi 4,000. Tunapenda kujua yale ya mwaka 2015, hayo makazi 9,000, yamejengwa kwa kiasi kipi? Leo ninavyozungumza, kule Tarime Askari Magereza makazi wanayoishi hata ukienda kumweka sungura, atalalamika kwa nini anaishi kwenye ile nyumba. Leo unamweka binadamu, tena Maaskari Magereza ambao wana familia, kinyumba ambacho kilijengwa mwaka 1942, enzi za ukoloni mpaka leo hujaboresha na zaidi kipindi hicho walikuwa wakikaa Askari Magereza wachache, leo wanakaa wengi kwenye kijumba hicho kimoja, wana familia na mnajua kuna mambo mengine ya staha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuta saa nyingine Askari Magereza wanawajibika kujijengea wenyewe vijumba. Tunaomba mnapokuwa mnasema nyumba 4,000, basi wajalini wale ndugu zetu ambao wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Serikali hii ya Hapa Kazi Tu inakwepa kuzungumzia Lugumi ya Jeshi la Polisi, lakini inasemekana kuna Lugumi nyingine kwenye Jeshi la Magereza. Inasemekana kwamba kuna fedha zilitolewa kwa ajili ya mfumo wa utambuzi wa ndugu zetu ambao wapo Magereza; wafungwa na mahabusu, wanaojulikana kama OMS (Offender Management System), ilitolewa ili hizi system ziweze kufungwa kwenye Magereza yote nchini, lakini inasemekana hadi leo hakuna system ambayo imefungwa kwenye hayo Magereza. Nataka kujua kama ni kweli, hizo fedha zimekwenda wapi? Au hii ndiyo ile dhana ya kuendeleza Lugumi ndani ya Jeshi la Polisi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, inasemekana pia kuna fedha zilitolewa kwa ajili ya kununua magari ndani ya Jeshi la Magereza ya kuwabeba mahabusu kutoka Gerezani kwenda Mahakamani na pia wale ambao unakuta wana-escort. Mheshimiwa Waziri amesema hapa kwamba watajitahidi kutenga fedha na kuna baadhi ya wilaya mmenunua, lakini inasemekana kwamba kuna fedha zilitengwa. Sasa nataka nijue, kama hizo fedha zilitengwa na mzabuni alikuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, zimeweza kununua hayo magari mangapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli zilitolewa, maana yake inasemekana zilitengeneza magari mabovu ambayo sasa hivi hayafanyi kazi na tunaendelea kuona kwamba Askari Polisi ndio wanasindikiza watu kwenda Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ni cha fedheha, ni uniform. Uniform mara ya mwisho kutolewa kwa hawa Maaskari Magereza, ambao nimefanya nao mazungumzo, ilikuwa ni 2009, mpaka leo hamjaweza kuwapa uniform.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hawa Maaskari Magereza, labda hata na wa Jeshi la Polisi, ukiwatazama na wengine wamekuja hapa Bungeni, wana uniform tofauti. Viatu vyao vinatofautiana, maana yake wanajinunulia, uniform zao ziko tofauti. Halafu Serikali ambayo inawatumia hawa ndugu zetu, tena vilivyo katika kuwakandamiza wapinzani, mnashindwa hata kuhakikisha kwamba mnawastahi na mavazi yao, angalau waonekane ni watanashati, mnawadhalilisha! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza, kama mmeshindwa kuleta uniform kwa hawa Askari, kwenye mshahara wao waongezeeni fedha za posho ya kununua uniform zao ambazo wataweza kununua uniform zenye kiwango cha juu. Maana inasemekana kuna mtu mmempa tenda ya ku-supply uniform; na ni mke wa kigogo wa Jeshi la Magereza. Anafanya kazi BOT, uniform zenyewe anazoleta ni za kiwango cha chini, yet hawa Maaskari wetu wanakwenda kununua vile vitambaa, wakifua siku mbili havina kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza bado, hii Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba chombo hiki muhimu kwa mustakabali wa maisha ya Watanzania inawaboreshea makazi yao? Inawapa mazingira mazuri ya kufanya kazi? Siyo tu mnawatumia halafu mnawaacha wanaishi kama watumwa kwenye nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni ucheleweshaji wa malipo; mafao ya Askari wastaafu na Mheshimiwa Waziri nimekupa copy. Kuna baba, ni Askari mstaafu sasa hivi ana miaka 70, tena bila huruma, ametumikia Jeshi kwa zaidi ya miaka 32; kuanzia mwaka 1962 mpaka 1995, anaitwa Simon Mirumbe. Amekuwa akihangaikia mafao yake kuanzia 1995 mpaka leo 2016, mnamzungusha tu. Mmemtumia lakini mnashindwa kumpa mafao yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike wakati Serikali ya Chama cha Mapinduzi itambue umuhimu wa Jeshi hili la Polisi, msiwatumie tu, bali muwajali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni msongamano wa mahabusu kwenye Magereza yetu. Leo ukienda Tarime, lile Gereza limejengwa 1942, uwezo wake ulikuwa ni kubeba wafungwa na mahabusu 209, lakini kuna siku unakuta wapo zaidi ya 500 mle ndani. Miundombinu ni mibovu, choo hakitamaniki, watu wanabanana, magodoro yenyewe ni aah! Tumekuwa tukishauri humu ndani; kuna kesi nyingine hazihitaji hata kumpeleka mtu kwenye Gereza, lakini unakuta mnalundika. Leo ukienda Tarime, kufuatia uchaguzi wa Oktoba, kuna kesi za kisiasa watu wako mle zaidi ya mia, wakati mnajua kabisa ile ni hatarishi kwa afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, nataka kujua; na Mheshimiwa Ummy kama angekuwepo; unakuta mwanamke labda amekamatwa kwa bahati mbaya akiwa mjamzito, anapelekwa mahabusu Gerezani, inatokea anajifungua, yule mtoto aliyezaliwa naye anakuwa ni mfungwa au mahabusu kwenye lile Gereza. Nataka nijue Serikali mnajipanga vipi angalau miezi sita huyu mama muweze kum-excuse atoke Gerezani, aweze kumzaa mtoto wake ili mtoto asiathirike kwa yale… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Aah, mmenibania eeh! (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa na mimi fursa hii niweze kuchangia kwenye bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia maeneo kadhaa kwa sababu dakika 10 ni chache sana. Nianze na suala zima la utawala bora na utawala bora wenyewe nitaanzia suala la kuwanyima fursa Watanzania kuweza kuona ni nini wawakilishi wao wanafanya Bungeni. Ni dhahiri kwamba tumesikiliza michango mingi sana na mingine kwa kweli inasikitisha, ukimwona Mbunge anasimama, anaunga mkono hoja hii dhalimu ya kupoka haki ya uhuru wa wananchi kuweza kujua wawakilishi wao wanafanya nini then unatakiwa ujiulize mara mbili mbili kwamba hata hao wananchi waliomleta huyu mwakilishi huku walifanya makosa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilisikitishwa na Mheshimiwa kijana kabisa Halima Bulembo, anasema tukionekana kwenye televisioni ni kwamba tunatafuta umaarufu. Nikasema labda nitembee kwenye hoja yake hiyo hiyo nimuelimishe kidogo huyu mdogo wangu. Akumbuke kwamba sisi wengine tuliweza kupata morale ya kutaka kuingia kwenye siasa baada ya kuwaona wanawake wenzetu akina Mama Abdallah, Anna Kilango, Halima Mdee na wengine na hata ukiwaona watu waliogombea Udiwani na Wenyeviti wa Mitaa wanapata inspiration wanapomwona Esther Matiko anachangia nini, fulani anachangia nini, wanaona kwamba hata sisi wanawake kumbe tunaweza tukiingia kwenye uwanda huu wa siasa. Sasa leo mwanamke kabisa anapiga vigelegele hiyo fifty fifty mnafika vipi? Yaani mnaungana na wanaume ambao wanaona hii ni njia pekee ya kuwakandamiza ninyi msifikie lengo lenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wengine tuna malengo makubwa, kuna Mheshimiwa mwingine alichangia kaka yangu Chegeni anasema kwamba twende tukafanye kazi Jimboni. Mimi lengo langu siyo kulitumikia Jimbo la Tarime tu kuna siku nataka niwe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, ninachokiwakilisha hapa nataka Tanzania nzima itambue Esther Matiko anafanya nini kwa Taifa lake wala siyo Tarime tu.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Kwa hiyo, kama ninyi mna short vision ya Jimbo tu na mnaamua kuwanyima Watanzania haki zao, jitafakarini mara mbili na mkienda pale mnaapa kuitumikia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halafu mnaikiuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani alisema na Wabunge wengine wamechangia mkubali, msikubali suala hili liko wazi na nitaomba mpitie hii Katiba, tulipokuja tulipewa kibegi kina hivi vitu vyote msiende kuweka ndani ya uvungu pitieni hii Katiba. Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Fedha na wengine waliochangia juzi hapa mlikuja mkapotosha lakini ni dhahiri Rais hawezi kuhamisha fungu moja kwenda lingine bila idhini ya Bunge tunaopitisha hapa, Mwenyekiti wewe ni Mwanasheria unajua, ni Mfuko wa Dharura tu. Kasomeni vizuri kuanzia Ibara ya 135 mpaka 140, kama hamna Katiba nitawatolea copy niwape ili tuweze kumshauri Rais asivunje Katiba na sheria yetu ya nchi. Inawezekana kabisa Rais ana lengo zuri aje sasa watuletee statement ya reallocation tuipitishe, mwenye mamlaka hayo ni Waziri au ndiyo hiyo tunasema kwamba hamna instrument kwa hiyo Rais inapoka mamlaka ya Waziri wa Fedha na kufanya anachokifanya ninyi mnapiga makofi, haikubaliki! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie sasa, TAMISEMI na nachangia kwenye Jimbo langu, nimechangia Kitaifa narudi sasa kwenye Jimbo langu.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure ni sawa sawa na mgonjwa yuko ICU. Kuna siku nilisema tuseme tumepeleka unafuu kwa wananchi, tusiseme elimu bure. Kwa sababu leo utasema elimu bure lakini Serikali Kuu mnasema Halmashauri ndiyo ijenge maboma, ihangaike kupata madawati lakini hazina uwezo. Kwa mfano kwangu Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pitia uone, kadri tunavyozidi kwenda mbele Halmshauri ya Mji wa Tarime kwa mwaka huu unaomalizika makusanyo ni shilingi milioni 300. Leo Halmashauri hiyo ijenge maboma ya shule za msingi za Tarime, ipeleke madawati na afanye na mambo mengine kwa fedha zipi? Walau mlitoa Waraka Na.5 wananchi walikuwa wameshaanza kujitolea mara tena Rais Magufuli akasema usichange labda upate kibali, wameacha, watoto wetu wanakosa mahali pa kusomea. Kama mnataka kutoa elimu bure jipangeni tunahitaji madarasa ya kutosha watoto wa Kitanzania wasome. Leo ukienda Tarime watoto zaidi ya 200 kwenye darasa, madarasa yenyewe hayapo. Walimu wanakaa kwenye miti, Tarime Mjini pale ofisi inatazamana na ofisi ya Chama cha Mapinduzi, walimu ofisi zao ni miti. Halafu mnakuja mnasema elimu ni bure. Mheshimiwa Cecilia Paresso hapa kasema do you have seven hundred billions kuweza kufanya elimu bure i-take off. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hamna madawati, hamna madarasa, Sera ya Elimu inasema walau watoto 45 kwa darasa moja wanakaa zaidi ya 200. Walimu wenyewe hawawi-motivated, hawana nyumba, umesema umejenga nyumba 183; sijui 188 kwa sekondari, mimi najiuliza mwalimu apange mjini, achukue sijui ni pikipiki au gari aende kufundisha Kenyamanyori hiyo fedha ni ya kwake kwenye kamshahara kale unakompa hana motivation allowance yoyote ile halafu mtasema elimu bure inaenda kuwa elimu ambayo haina manufaa yaani bora amefika la saba au la kumi na mbili lakini anarudi kitaa hajapata elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mtu afanye kazi vizuri lazima walau ufanye akili yake itulie yake, mwalimu anayekwenda kumfundisha mwanafunzi ni lazima awe ametuliza akili. Mwalimu hana nyumba na wenye vinyumba vyenyewe wakikaa wananyeshewa nilisema mwaka jana hapa, shule ya sekondari nyumba zao zinavuja wanahamisha vigodoro huku na huku halafu leo useme kwamba watoto wale wa maskini watafundishwa waelewe, hata siku moja. Tuwe na vitabu vya kutosha, tuwe na madawati, tuwe na madarasa ya kuweza kuhakikisha wanafunzi wanakaa walau 45 ili mimi mwalimu ninavyofundisha waweze kunielewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye afya. Sera ya Afya inasema walau kila kijiji au mtaa wawe na zahanati, mmeonyesha mna zahanati 4,500 tangu uhuru mpaka sasa hivi bado kuna upungufu wa zahanati 8,043. Vituo vya afya mnavyo 488 upungufu wa 3,506 na mnajua Maazimio ya Abuja walau asilimia 15 ya bajeti ya Serikali iende kwenye afya tumekuwa tukiimba, you don’t do that. Leo mnasema mnaboresha afya, kama imewachukua miaka 50 tuna vituo vya afya 484 itatuchukuwa zaidi ya miaka 350 kutimiza hivi vituo vya afya vinavyohitajika, watu wetu wanakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwa Tarime kuna Zahanati ya Gamasara ambayo iko Kata ya Nyandoto inahudumia wananchi wa Kata ya Nyandoto kama kituo cha afya wakati ni zahanati, inahudumia wananchi wa kijiji cha Kongo na Ketere hiyo ni Wilaya ya Rorya na inahudumia wananchi wa Kewamamba na Nyagisya hiyo ni Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Jimbo la Vijijini). Zamani walau mlikuwa mnapeleka shilingi milioni nne kwenye Halmashauri ya Mji leo mnapeleka shilingi166,000 baada ya miezi mitatu, hawa Watanzania tunawapenda au tunachezea afya zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije tena kwenye Hospitali ya Mji ambayo mliishusha hadhi kutoka Hospitali ya Wilaya mkaifanya Hospitali ya Mji na niliuza swali hapa nikasema ilitakiwa iwe Hospitali ya Rufaa maana inasaidia wananchi wa Rorya, Serengeti na Tarime kwa ujumla siyo mji tu, mnapeleka ruzuku ya shilingi milioni 51 halafu Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mnapeleka shilingi milioni 91 wakati mkijua kabisa kwamba ile Hospitali ya Mji iliyoko mjini inahudumia huko kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 51 iweze kutibu Wilaya nzima maana kiuhalisia haitibu wananchi wa Mji wa Tarime tu. Ndiyo maana nasema hivi mna watendaji na watu wenu wanafanya kazi ku-check uhalisia? Halmashauri ya Wilaya ya Tarime haina hospitali, wanakuja kutibiwa kwenye Halmashauri ya Mji wa Tarime, kwa nini mnaweka allocation za kitoto namna hii? Mnachezea afya za Watanzania, tunaendelea kushuhudia wananchi wakifa, waoneeni huruma. Nipeni mwanga maana sioni na mniongezee dakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo. Halmahsuri ya Mji wa Tarime tuna Mogabiri Extension Farm...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Nitachangia siku nyingine kwenye Wizara zingine, nina nondo nyingi sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipatia fursa hii kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba Wizara hii ndiyo imeshikilia uchumi wa Tanzania, tukisema Tanzania ya viwanda ina maana Wizara hii ndiyo inatakiwa ifanye vema. Tukienda hata kwenye sekta ya afya, tumeshuhudia mikoani hasa katika Wilaya ya Tarime kwenye vituo vya afya ambavyo vipo kando kando ya mji wanawake wakienda kujifungua vituo hivi vinatumia tochi kuwazalisha wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea kwamba Wizara hii iweze kweli kuonesha kama ilivyosema kwenye hotuba yake kwamba asilimia zaidi 98 zimekwenda kwenye fedha za maendeleo na nje ya hizo 98 ambazo ni trilioni 1.54; trilioni 1.32 zinaenda kwenye nishati. Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba itaenda kuwatendea haki Watanzania kwa kuwapatia nishati mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye madini; Halmashauri ya Mji wa Tarime au Wilaya ya Tarime imebarikiwa kuwa na madini pamoja na kwamba Profesa alisema dhahabu siyo kitu siku hizi, lakini bado tunaithamini dhahabu na tukiitumia vizuri inaweza ikatusaidia sana kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ina migodi midogo midogo ya Nyabori, Kebaga na Buguti. Hii migodi ya Kebaga, Nyabori na Buguti; mgodi wa Buguti bado ulikuwa na leseni ya Acacia ambao walisema inakwisha Disemba. Kwa hiyo, natumaini kwamba kama itakuwa imekwisha basi watapewa wachimbaji wadogo wadogo ambao tayari wapo field.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata mwanzoni mwa mwaka huu nilimwambia Profesa wakati ameweka ziara ya Tarime atembelee ule mgodi nafikiri nafasi haikumtosha. Hao wachimbaji wadogo wadogo wanapata changamoto nyingi sana na tukirejea Sera ya Wachimbaji Wadogo ya 2009 ambayo ilielekeza kwamba waweze kupatiwa mitaji kwa maana ya ruzuku ambayo wameonesha kwamba wanaitoa lakini ruzuku hizi ambazo wanazitoa hazifuati utaratibu au utaratibu wake ni mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, walengwa siyo wale wachimbaji wadogo wadogo, wale ambao tunawa-target bali ni wajanja baadhi wanakuja wanajivisha umbrella ya wachimbaji wadogo wadogo, wana-benefit kwa hizi fedha na wale ambao ni targeted group hawapati. Kwa hiyo, ningependa sana utaratibu huu uweze kufuatiliwa vizuri, waweze kupata wale Watanzania ambao kweli ni wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tuna GST kwa maana ya Geological Survey of Tanzania (Mawakala wa Jiolojia) hawaendi kuhakikisha wanasaidiana na hawa wachimbaji wadogo wadogo kujua kwamba sehemu fulani kuna madini. Kwa mfano, sasa hivi wachimbaji wa Buguti na Nyabori ambao nimewaainisha hapa wanachimba kwa kubahatisha; kwanza wanatumia vifaa duni, wanatumia nguvu zaidi kuliko teknolojia ya kisasa; lakini wakifika chini wanakuta hakuna madini wanahama tena wanakwenda kwenye shimo lingine hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa hii GST ijielekeze kule iwasaidie hawa wachimbaji wadogo wadogo waweze kujua bayana kwamba nikichimba hapa nitakwenda kukutana na madini. Ukizingatia kwa mfano Buguti water table ipo juu sana, wanatumia vifaa duni, kutafuta jenereta na kuanza kutoa maji na kuchimba na hakuna umeme maeneo hayo yote ambayo nimeyaainisha, zile Kata hazina umeme kabisa. Hao wachimbaji kwanza hawajaweza ku-benefit na hiyo ruzuku wanajikongoja kwa kuchangishana vikundi vile, lakini wakichimba bado hawawezi kupata kinachostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba huwa kuna Wakaguzi wa Madini ambao wanakagua teknolojia ya uchimbaji. Hawa watu hawawafikii hawa wachimbaji wadogo wadogo kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, unakuta hawa wachimbaji hawapati ushauri mbadala kutoka kwa hawa wataalam wetu. Ningependa kuelekeza Wizara hii kama tumeamua kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo wadogo tuhakikishe kwamba tunawafikia, tunashauriana nao, ikiwezekana tunawapatia elimu mbadala na tunawapatia na vifaa ili waweze kuchimba kwa teknolojia ya kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosikitisha zaidi kupitia uchimbaji mdogo mdogo ule uchenjuaji wa madini mineral processing mnaita, unakuta wanachukua yale madini, wanatia mercury ili kuweza ku-process na kupata ile dhahabu yenyewe; hii inawaua Watanzania kidogo kidogo, leo hata ukienda kwenye haya maeneo ya dhahabu au madini , utakuta kuna watu vipofu, maana yake haya madini yakiingia kwenye damu yana affect zile chromosome macho yataharibika. Unakuta watoto wanazaliwa wana vichwa vidogo, unakuta wengine ngozi zao ukiziona hazitamalaki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika huu uchimbaji mdogo mdogo tusipowekeza vizuri, tukawapa kinu cha kufanya direct smelting mwisho wa siku tunawaua hawa Watanzania, baada ya muda mchache Watanzania wengi wanakufa kwa sababu wanatumia zile mercury. Leo ukienda Buguti, ukienda Kebaga, ukienda Nyabori unawakuta akinamama wengine hata ni wajawazito wanashika shika ile mercury, inawapa direct effect kwa kiumbe aliyepo tumboni ,lakini na yeye mwenyewe after five, ten years wanafariki dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fanya research kwa wote nenda Geita, nenda Nyamongo, njoo kwenye hii migodi midogo midogo pale na Profesa unajua mercury effect yake, lakini wanatumia. Hivyo basi tuwawezeshe, tuwape modern instruments za kufanya hiyo process ya madini wasitumie mikono yao moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Nyamongo kabla sijakwenda kwenye nishati. Nyamongo kwa kweli na naongea hii kama natokea Tarime, tumekuwa tukiongea huku kwa muda mrefu sana ule mgodi siyo neema kwa watu wa Tarime bali ni majonzi kwa watu wa Tarime na hata Watanzania wengine ambao wanafanya shughuli zao pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba ukienda nchi za wengine kama kuna migodi ni neema, hivi leo kweli ukija Tarime huwezi ukaona reflection kwamba kuna mgodi ambao unatoa dhahabu ya kutosha kilometa kadhaa kutoka Tarime Mjini, hatuna barabara za lami, wamejitahidi ndani ya ile Kata ya Matongo pale ndiyo kuna shule wamejenga na kile kituo cha sungusungu, lakini hata ukienda hospitali ile ya mji ambayo mnaisema ambayo ndiyo inatoa huduma hata kwa asilimia kubwa kwa Wilaya nzima ya Tarime haioneshi uhalisia kwamba kuna mgodi upo kwenye hii Wilaya ya Tarime.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukiangalia huduma za jamii maji walikuwa wanatoa kwa kupeleka ile buldoza lidumu la maji lile, ina maana hawajawachimbia kuhakikishia kwamba wanawapa maji ambayo yapo salama. Kwa hiyo naomba sana kikubwa mwaka 2011 baada ya watu zaidi ya sita kuuawa Nyamongo aliyekuwa Waziri wa Nishati Mheshimiwa Ngeleja, Mama Nagu Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji na Mheshimiwa Wasira walikuja Nyamongo wakawaahidi wale Watanzania kwamba watawapa maeneo mbadala ya kuchimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wakaongea na mgodi na wakawaahidi kwamba watachukua yale mawe wawe wanakuja kuwamwagia kwenye maeneo yao, maana wakienda kuokota mawe mnawapiga risasi. Wameshindwa kutimiza yale ambayo waliahidi, kwa sababu naamini Wizara hiyo ni institution hata kama ametoka yule Waziri amekuja mwingine, mnabukua ma-file mnaona mliahidi nini kwa wale Watanzania mkawatimizie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la nishati; Jimbo la Tarime Mjini au Wilaya ya Tarime kwa asilimia zaidi ya 70 wananchi wake hawana umeme. Leo tunavyoongea Mheshimiwa Profesa Muhongo, tumeshaleta mapendekezo yetu kupitia REA l pia na hizo njia nyingine za kuweka umeme kwa hawa Watanzania. Kama tunataka kukuza uchumi wetu tuhakikishe tunasaidia, mathalani Tarime Mjini Kata ya Nkende, Nyandoto, Kitale na Kenyamanyoli asilimia zaidi ya 98 hawana umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Nkende kuna soko tunalijenga la Afrika Mashariki hamna umeme, kuna uwanja wa ndege pale, kuna mnada wa Magena, lakini kuna machinjio ya kisasa Nkende na huduma zingine za jamii. Zaidi kwa upande wa pili wa Tarime ni Kenya; wenzetu Kenya ukija usiku ni taa zinawaka tu, ukija usiku upande wa Tanzania ni giza kama vile ni pori. Kwa hiyo, ningependa kuwaomba sana hizi trilioni 1.32 Tarime mtukumbuke, mtuletee hii nishati ya umeme, sisi ni wakulima, sisi ni wafugaji tuweze kusindika mazao yetu, tuweze kukuza uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Watanzania wengine ni wajasiriamali wadogo wadogo wamewekeza, leo mtu mwenye saloon kama hana umeme hawezi kumudu kununua jenereta, leo wale wafanyabiashara wadogo wadogo hawawezi kumudu bila umeme. Tukiwaza Tanzania ya viwanda, pia tuwaze Tanzania ya wajasiriamali wadogo wadogo ambao nishati ya umeme ndiyo mbadala wa kuweza kuwakomboa Watanzania. Tuwaze huduma za jamii kama shule, tuwaze huduma za jamii kama hospitali, tuwaze huduma za jamii zinginezo, magereza na vituo vya polisi bila umeme huko vijijini, hata hao wahalifu mnakwenda kuwaweka pamoja na Polisi mnategemea nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba sana Serikali hii ya CCM kupitia kwa Profesa Muhongo wawekeze na nina imani labda alikaa hawajampunja bajeti yake na akajiridhisha kabisa hii trilioni 1.32 inatosha kuhakikisha wanaleta umeme zaidi ya asilimia 70 kwa Watanzania ili tuweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa lolote lile lenye nishati mbadala ya umeme utaona uchumi wake utaji-reflect kwa sababu umeme ndiyo kila kitu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atuangalie Tarime, Kata nilizozitaja za Kenyamanyoli na mgodi ukiwapelekea umeme hiyo migodi itaenda kufanya kazi bila kutumia jenereta. Apeleke umeme Kitale, Turo, Nyamisangula, Nyandoto na kwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu kwenye maeneo makuu mawili, yaani nishati na madini. Naomba nianze na Sekta ya Madini ambayo tunajua kuwa, kuna Watanzania wamejiajiri kwenye sekta hii, lakini pia, kuna wawekezaji toka nje wamewekeza kwenye sekta hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Tarime Mjini limebahatika kuwa na migodi midogo kwenye Kata ya Kenyamanyori na Turwa. Wilaya ya Tarime tumebarikiwa kuwa na Mgodi wa North Mara ambao ni mkubwa na muwekezaji wa kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya uwekezaji wananchi walikuwa wakifanya uchimbaji mdogomdogo, lakini baada ya uwekezaji ule wamepata adha kubwa sana, hawana maeneo yaliyotengwa dhahiri kwa ajili ya kuwapa maeneo ya kuchimba bali wameendelea kuuawa pale wanapokuwa wameenda kuona chochote kwenye mabaki (vifusi).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na mgodi iliahidi ndani ya Bunge hili Tukufu wakati nilipotaka mkakati wa Serikali kutatua wimbi la mauaji ya Watanzania kwenye huo mgodi 2011, waliahidi kutenga maeneo pamoja na kumwaga vifusi vile kwenye maeneo ya wananchi, pamoja na ku-support vikundi mbalimbali ili vijishughulishe na ujasiriamali kuweza kukukuza uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yalisemwa na kurudiwa na Mheshimiwa Nagu, aliyekuwa Waziri wa Uwekezeaji, Mheshimiwa Wasira aliyekuwa Waziri wa Mahusiano na Uratibu na Mheshimiwa Ngeleja aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini. Ni vyema sasa Serikali ikatimiza haya kwa wananchi na Wilaya ya Tarime na Watanzania waishio Nyamongo na maeneo jirani na North Mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime kuna migodi ambayo wachimbaji wadogo wadogo wanashughulika na uchimbaji wa madini. Maeneo hayo ni Nyabhori na Kebaga, Kata ya Kenyamanyori na Mgodi mwingine ni ule wa Bajeti ambao upo mpakani mwa Turwa na Kenyamanyori. Kwa ajili ya kuboresha au kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji hawa wadogo ni muda muafaka Serikali kuhakikisha hizi ruzuku za zaidi ya bilioni 500 zinawanufaisha walengwa na sio matajiri wachache wanaojivisha joho la uchimbaji mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo wadogo ambazo naomba Serikali kujitahidi ndani ya bajeti ya mwaka huu waweze kupatiwa ruzuku, sambamba na vifaa muhimu vya kurahisisha uchimbaji. Changamoto ya kwanza ni juu ya teknolojia inayotumika kuchimba madini, ni ya kienyeji ambayo ni hatarishi sana kwa maisha yao; mfano kuchoronga miamba inabidi watumie nguvu nyingi badala ya morden equipments.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni changamoto ya maji. Aina ya uchimbaji ni underground ambapo unakuta water table ipo juu sana, hivyo inawawia vigumu kufanya shughuli za uchimbaji sababu ya maji na ikizingatiwa vitendea kazi vyao ni duni sana. Ni rai yangu sasa, Serikali itambue maeneo haya na kutoa ufadhili wake kwenye mashine za kuvutia maji kama vile motor, generator na waweze kutoa kwenye vikundi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ni miundombinu mibovu ya barabara kuelekea kwenye migodi hii. Nashauri Waziri akae na Wizara husika kuweza kushawishi ujenzi wa barabara angalau kwa ngazi ya changarawe ukizingatia migodi hii inachangia kwenye pato la Serikali kupitia leseni za uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine lenye changamoto kubwa ni juu ya kuweza kupata mitambo ambayo hupima udongo na miamba, ili kujua upatikanaji wa dhahabu au madini mengine. Maana kwa sasa wachimbaji wadogo wadogo wanajichimbia kienyeji na kwa kubahatisha tu na hivyo kujikuta wanapoteza nguvu kazi nyingi sana na haina ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Wilaya ya Tarime tumekuwa hatupatiwi sehemu ya mrahaba toka ACCACIA, kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa kutoa kiasi cha fedha ambacho hutumika kuleta maendeleo ya kijamii. Baadhi ya maeneo ya huduma za jamii ambazo ACCACIA wanapata ndani ya Mji wa Tarime ni Hospitali ya Mji, soko, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Uhamiaji, Stendi, Mahakama, hivyo kwa kuwa wafanyakazi wa ACCACIA wanapata huduma tajwa hapo juu ni dhahiri kuwa ACCACIA wana wajibu wa kuhakikisha Halmashauri yetu ya Mji wa Tarime inapata huduma muhimu za kijamii pamoja na mrabaha toka mgodi wa North Mara. Mji wa Tarime una ukosefu wa maji na barabara za mitaa ni mbovu mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mchana huu nichangie katika Sekta ya Nishati ya Umeme; Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa asilimia zaidi ya 70 hawana nishati ya umeme. Halmashauri ya Mji wa Tarime ina mitaa 88, ambapo kiuhalisia kuna kata nne ambazo zipo na vijiji na hamna nishati ya umeme kabisa. Kata hizi ni Ketare, Kenyamanyori, Nandoto, Nkende na baadhi ya maeneo ya Kata ya Turwa na Kata ya Nyamisangura.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishapeleka barua kuelekeza maeneo yenye uhitaji mkubwa wa umeme, hivyo naomba kujua kama REA Phase III imeyafanyia kazi na ukizingatia Kata ya Kataer, Nyandoto na Kenyamanyori wanajihusisha sana na kilimo ambacho kitasaidia kwenye dhana nzima ya Tanzania ya Viwanda, tuweze kusindika mazao yetu, kufungua viwanda vidogo vidogo. Kata ya Nkende ndio yenye soko la Kimataifa ambalo linajengwa pale, pia kuna uwanja wa ndege ambao unatumiwa na watalii waendao Nyamongo na hata Viongozi wa Serikali na kisiasa, hivyo taa ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Kata ya Nkende ndiyo yenye Mnada wa Magera ambao Serikali imeahidi kuufufua. Pili, ni katika Kata hii ya Nkende ndiyo tuna machinjio ya kisasa, ofisi ya Uhamiaji inajengwa karibu na Mgena Airport na Remague East Africa Market, lakini pia wajasiriamali wadogo wadogo wanategemea nishati hii ya umeme ili kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ijulikane kuwa mahitaji muhimu ya kijamii, kama shule za sekondari na msingi, hospitali, vituo vya afya, zahanati, vituo vya polisi, viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao; hivyo, naomba sana Wizara hii itoe kipaumbele katika Halmashauri ya Mji wa Tarime ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Tarime. Hivyo nishati ya umeme ni ya muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba Wizara hii ichukue hatua ya kuhakikisha hakuna ukatikaji wa umeme mara kwa mara bila kutoa taarifa kwa mteja/wateja kitu ambacho husababisha uharibifu wa vifaa vinavyotumia umeme na kusababisha hasara kwa mlaji. Utolewe Waraka toka ngazi ya Wizara ukiamrisha uboreshaji wa utoaji wa nishati ya umeme bila kuleta madhara kwa mlaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha kwa kutoa ushauri kwa Serikali kuhakikisha fedha za maendeleo zilizotengwa zitumike kwa ajili ya bajeti iliyotengwa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu mbadala kwa wachimbaji wadogo wadogo, ili wapate elimu mbadala kwa uchimbaji wenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara hii juu ya mambo muhimu matatu yanayohitajika ndani ya Wilaya ya Tarime na hasa Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tarime kwa kiasi kikubwa haijapimwa. Mfano, Halmashauri ya Mji wa Tarime kwenye kata nane, ni kata mbili tu ndiyo zimepimwa. Hilo eneo lingine halijapimwa licha kuwa sasa hivi vijiji na vitongoji vyote vimekuwa mitaa na tuna idadi ya mitaa 81. Hivyo upangaji wa mitaa ni muhimu na uhitaji wa kupanga mitaa ni lazima ili tuweze kupima viwanja na kupandisha thamani ya ardhi yetu. Tunaweza kutumia ardhi ile ili kukopa katika taasisi za kifedha; vilevile mji ukipangwa vyema utavutia wawekezaji mbalimbali kuja katika Halmashauri yetu na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali kama vile viwanda, ufugaji, uwekezaji kwenye majengo ambapo tunahitaji strategic master planning ya mji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ni Kata ya Bomani kwa sababu tu ndiyo zimepimwa. Tunahitaji upimaji wa haraka kwenye Kata za Turwa, Nyamisangura, Nkende, Kenyemangori, Ketare na Nyandoto ziweze kupimwa ili kuweza kuruhusu utoaji mwingine wa huduma za kijamii kama umeme, barabara, shule, vituo vya afya, vituo vya biashara, maeneo ya viwanda na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za upimaji wa ardhi ni ghali sana kwa Mtanzania wa kawaida kuweza kumudu, maana ni kuanzia shilingi milioni moja na kuendelea. Vilevile taratibu hizo zinachukua muda mrefu sana na zina mlolongo na urasimu. Hivyo tunaomba sana upimaji wa viwanja kwenye Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kipindi cha mwaka huu. Hii itaweza kupunguza kasi ya migogoro kama ule uliopo kwa wananchi wa Mtaa wa Mafarasini, Kata ya Bomani ambapo walipimiwa ardhi kwa ada (gharama) ya shilingi 20,000, shilingi 40,000, shilingi 70,000. Cha kushangaza baada ya muda Serikali inawaambia walipie tena upya gharama za kumiliki ardhi kuwa ni kuanzia shilingi 2,000,000 na kuwaambia kuwa wanaoshindwa kulipia gharama hizo watanyang‟anywa ardhi hizo na kupewa wenye uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halikubaliki kwa maskini wale waliomilikishwa ardhi kwa kufuata sheria na walilipia. Iweje leo tena mnawapoka? Hadi sasa wananchi hawa wa Mafarasini wanashindwa/huogopa kuendeleza makazi yao kwa kuhofia kupokwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ni juu ya waraka ambao umetoka Serikali Kuu (Wizarani) kwenda kwenye Halmashauri ya Mji ikitaka kutokutumia matumizi ya ardhi pale inapoona inafaa. Hili kiukweli limekuwa kikwazo kikubwa sana na ukizingatia Halmashauri yangu ni changa na hivi katika upangaji wa mji kuna maeneo yanaweza kubadilishwa matumizi ili yaweze kutumika katika shughuli za kijamii kama vile mashamba na hata viwanja vya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inarudisha nyuma maendeleo ya Tarime Mjini. Mfano Ofisi ya Mbunge iliandika barua kwenda Halmashauri ya Mji kuomba eneo ambalo litatumika kujenga maktaba ya umma ambayo itasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu. Vilevile kuongeza idadi ya Watanzania wanaosoma vitabu ili kupanua uelewa. Cha kushangaza na kwa masikitiko, Mkurugenzi wa Halmashauri wa Mji kasema kwamba Serikali imezuia ubadilishwaji wa matumizi ya ardhi. Hii inarudisha nyuma maendeleo ya Tarime Mjini. Naomba Wizara ione umuhimu wa kupatiwa eneo la kujenga maktaba ambayo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ni tatizo sugu ni juu ya kucheleweshwa kwa malipo ya fidia kwa wananchi ambao ardhi yao imepokwa na JWTZ. Wananchi hawa walifanyiwa tathmini tangu mwaka 2012 hadi leo hawajalipwa na walizuiliwa kufanya shughuli za maendeleo tangu mwaka 2007 na wakapora hadi mkataba wa mnara wa Airtel, kinyume kabisa na sheria za nchi hii. Je, katika tathimini itakayofanywa tena itafidia mkataba wa mnara pamoja na uhalisia wa mali tangu mwaka 2007? Kutakuwa na riba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawataka Serikali imalize malipo ya Ranchi wa Ronsoti, Msati (Nyamisangura) Kenyambi (Nkende) na nyinginezo. Ni aibu kuwapoka wananchi ardhi kinyume na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 lakini mkashindwa kulipa fidia. Vilevile Serikali ione umuhimu sasa ya kuhakikisha Bodi ya Mifuko ya Fidia inaundwa mwaka huu ili tuepushe ucheleweshaji wa malipo ya fidia. Tunaomba NHC waje kuwekeza Tarime, maeneo tutawapatia ili kuweza kupunguza adha ya malazi na kukuza mandhari ya mji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile fidia za wananchi wa Nyamoyo ambao walifanyia tathmini tangu mwaka 2011/2012 waweze kulipwa fidia zao maana waliondolewa na kwenda kutafuta makazi mengine ambapo ilibidi wakope fedha benki waweze kuanzisha makazi mengine. Hivyo wameshindwa kulipia mkopo na kubaki na adha kubwa sana. Hawa sasa ni wakazi wa mji wa Tarime, hivyo tufuate Sheria za Ardhi bila kunyanyasa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inachukua muda mrefu kweli kurejesha retentions katika Halmashauri husika, mfano Halmashauri yangu ya Mji wa Tarime ambayo haina mapato ya kutosha. Hivyo hizo fedha za upimaji ardhi ni vyema ziwe zinapelekwa mapema kuliko kucheleweshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuwasilisha.

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa hizi dakika tano japo ni chache sana nitajitahidi kwenda katika point form. Kwanza kabisa niseme kwamba naunga mkono taarifa zote mbili za Kamati ya PAC na LAAC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kikubwa nichangie kwanza kabisa kwenye misamaha ya kodi. Tumekuwa tukiongea kama Bunge na kuishauri Serikali kwamba walau misamaha ya kodi iwe angalau chini ya asilimia moja ya Pato la Taifa. Ukisoma taarifa ya PAC utaona kabisa wameainisha misamaha ya kodi isiyokuwa na tija kwenye Taifa letu na mbaya zaidi inatolewa kwenye makampuni mengine ambayo hayana leseni, mengine wanasema yameghushi. Sasa swali hapa ambalo tungetaka tujue hawa watu ambao wamepewa hizi fedha, Serikali imechukua hatua gani, wameshazirudisha na kwa wale watendaji ambao waliidhinisha hii misamaha ya kodi ilhali watu wameghushi nyaraka, leseni zime-expire na mambo mengine wamechukuliwa hatua gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine ni suala zima la madeni ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii. Siku Mheshimiwa Rais anaongea na wanahabari alisema kabisa kwamba mifuko hii inafilisika kikubwa ni kwa sababu wanasiasa na mbaya zaidi akasema Wabunge sisi ndiyo tunafilisi mifuko hii kwa sababu tumekopa. Kwenye ripoti hii ya PAC imeanisha kabisa zaidi ya shilingi trilioni 1.5 Serikali inadaiwa na Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea kuna wafanyakazi fedha zao hazijapelekwa kwenye mifuko husika, kwa mfano, Askari Magereza na Polisi na wafanyakazi wengine tangu mwezi wa nne mpaka sasa hivi makato yao hayajaenda kwenye mifuko husika. Sasa tunauliza ni kwa nini Hazina wasipeleke hizi fedha za michango kwenye mifuko husika? Yaani mnakopa kwenye michango ya wafanyakazi bado mnakopa kwenye uwekezaji halafu Rais anauambia umma kwamba Wabunge ndiyo wamefilisi mifuko ya jamii, is he serious? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, tumekuwa tukilalamika kuhusu kukaimishwa kwa watendaji kwenye mashirika ya umma lakini pia imekithiri kwenye Halmashauri zetu. Ni wakati sasa Serikali ione umuhimu wa either kuwajiri watu wenye uwezo kwenye vitengo mbalimbali, kwa mfano kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Tarime mara nyingi nimekuwa nikimfuata Waziri husika, kuna watendaaji wanakaimu kule, ufanisi ni zero, Halmashauri inakuwa haiwezi ikafanya vizuri. Naomba kabisa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ufanye juhudi na wale wengine ambao wanasimamia mashirika mbalimbali tusiwe tunakaimisha hizi nafasi inapunguza ufanisi wa kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 20 za ruzuku ambazo zinatakiwa kwenda kwa Serikali za Mitaa na Vijiji. Tumekuwa hata tukiuliza maswali humu ndani, wale Wenyeviti wa Mitaa hawalipwi posho, unakuta hata hawana stationary kwa hiyo wanashindwa hata kufanya kazi. Fedha ambazo mnapeleka kule kwenye Halmashauri haziwafikii Serikali za Mitaa au za Vijiji. Tunaomba sasa Wizara husika muweze kuwa na ufuatiliaji kama ni ripoti inakuwa inatolewa kuhakikisha kwamba hizi asilimia 20 kweli zinatengwa au hazitengwi na kama hazitengwi ni kwa nini zisiende kule chini na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho kinahuzunisha zaidi ni zile asilimia kumi kwa ajili ya vijana na wanawake. Kikubwa hapa kinakuja unakuta Halmashauri haina mapato, fedha wanazokusanya wanapeleka sehemu zingine. Kwa hiyo, hii ipo tu kwenye makaratasi kwamba wanawake wanapewa asilimia tano na vijana wanapewa vijana asilimia tano lakini kiuhalisia hakuna. Mfano kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Tarime hiyo kitu haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ni kwamba vyanzo vya mapato ni vichache, lakini kingine mnaelekeza kwamba fanya kitu fulani kwanza, kwa hiyo, priority ya kutoa fedha kwa ajili ya Mfuko huu kwa ajili ya vijana na wanawake haipo na hii inakuwa inayumbisha. Tunaomba sasa utiliwe mkazo kama nilivyopendekeza kwenye ruzuku ya asilimia 20 na kwenye hii ruzuku ya asilimia kumi ya vijana na wanawake napo Serikali kupitia Wizara husika wahakikishe wanawake na vijana wanaenda kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho nilitaka nizungumzie…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Esther.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hoja hii kwenye maeneo ya maliasili na utalii, elimu, kilimo, viwanda, afya na uchumi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa masikitiko makubwa kuona mpango huu haujaweka Sekta ya Maliasili na Utalii kama moja ya maeneo ya vipaumbele licha ya kwamba sekta hii huchangia zaidi kwenye kuingiza fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutolewa kwa maliasili na utalii katika vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ni fedheha na masikitiko makubwa kuwa sekta hii haipo katika Mpango wa mwaka 2017/2018. Tunaomba Serikali itoe sababu za msingi, ni kwa nini Sekta ya Maliasili haipo ilhali ndiyo sekta iliyokuwa ikichangia kukuza uchumi wa ndani kwa miaka yote na ndiyo inayotoa ajira kwa vijana na haihitaji gharama kubwa sana za uendeshaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, kupungua kwa watalii wanaoingia nchini na hali mbaya ya Sekta ya Utalii; mfano watalii wamepungua kwa 8% kutoka watalii 1,140,156 mwaka 2014 mpaka watalii 1,048,944 mwaka 2015 na bado hali inazidi kuwa mbaya kwani watalii wanazidi kupungua kila siku hasa baada ya uwepo wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za Maliasili na Utalii. Pia kumekuwepo na upungufu wa idadi ya watalii wa hotelini 1,005,058 mwaka 2014 mpaka 969,986.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupungua kwa mapato ya utalii kutoka dola milioni 1,982 mpaka 1,906; na hizi ni kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014/2015. Vile vile kwa wastani wa siku za kukaa watalii, zimepungua kutoka siku 12 mpaka kumi na kwa sasa hali imezidi kuwa mbaya zaidi baada ya kuwepo kwa VAT, maana Sekta ya Utalii imekuwa na mlundikano wa kodi nyingi sana takriban 32. Hizi zote zinaongeza gharama na kusababisha watalii kuona ni ghali sana kuja kupumzika na kujionea utalii wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kumekuwepo na matatizo makubwa kwenye Sekta ya Utalii yanayochangia kushuka kwa mapato yatokanayo na utalii. Mfano tu, ninavyoongea sasa, Mamlaka ya Ngorongoro imekataza wamiliki na magari binafsi yanayotoa huduma za kitalii kwa kutumia magari binafsi ambayo kimsingi yamesajiliwa kibiashara na yamekidhi vigezo vyote vya magari ya utalii ila tu siyo magari ya Kampuni, yawe ndiyo kama masharti ya leseni ya utalii inavyotaka. Kama barua yenye Kumbukumbu Namba NCAA/D/584/Vol.XIII/20, pamoja na barua TNP/HQ/L.10/22 iliyohusu zoezi la uhakiki wa leseni kwa makampuni yanayofanya shughuli za utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa takriban magari 300 yamezuiwa kufanya kazi za kupeleka wageni ndani ya hifadhi. Makampuni yaliyokuwa yanafanya biashara kupitia magari haya tayari yalikuwa yana wageni ambao wanapaswa kwenda hifadhini, hivyo watalii wengi wanataabika ilhali tayari wameshatoa pesa zao na wanahitaji huduma. Hii ina athari ya moja kwa moja katika soko zima la utalii nchini ambalo mpaka sasa linakumbwa na changamoto lukuki.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua hitaji la kisheria katika kupata leseni ya utalii, lakini tujiulize, tunawasaidia vipi Watanzania hawa ambao wamejichanga na kupata fedha kidogo kwa ajili ya mtaji wa kuanzisha biashara hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nichukue fursa hii kuishukuru Wizara kwa kuwa Waziri Profesa Maghembe na Watendaji wake waliweza kuona ni fursa nzuri za kuendelea kuwaajiri watu kwenye Sekta ya Utalii ya Usafirishaji kwa kulifanyia kazi pendekezo letu tulilolitoa wakati wa bajeti, ambapo tulipendekeza Serikali angalau iweke sharti la magari kuwa matano badala yake yamekuwa mawili au matatu. Kwa taarifa nilizonazo, ni kuwa magari matatu ndiyo hitajio. Hii ni hatua tatuzi kwa vijana maskini wa Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu ni kwamba, kufuatia barua ya Ngorongoro ni kuwa, Serikali ipate uhakika wa uwepo wa magari matatu katika kuanzisha biashara, iwe ni magari matatu bila kuwa na kigezo cha umiliki, bali ieleze kuwa kampuni ni lazima iwe na magari matatu, iwe ni magari ya kukodi au ya kibiashara lakini ni lazima kampuni ioneshe uwezo na uhakika wa magari hayo; na yabandikwe sticker. Msingi wa hoja hii ni kuwa siyo Watanzania wote wana uwezo wa kumiliki magari matatu yenye viwango elekezi, bali wanaweza kukodi magari yenye viwango elekezi na biashara hii ikaendelea na kutoa ajira na kukuza uchumi ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwenye sharti la leseni ya biashara (TALA License) hiyo kuna hitaji la kampuni kulipa dola 2,000 kwa makampuni ya ndani na dola 5,000 kwa makampuni ya nje, havijalishi idadi ya magari ambayo kampuni hiyo inamiliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali isihakikishe kuwa linalipa dola 100 kwa mwaka bila kujali idadi ya magari? Serikali itapata fedha nyingi zaidi kwa kuwa yapo makampuni yana magari zaidi ya 300 na yanalipa dola 2,000 na mengine yana magari matano na yanalipa kiasi sawa cha dola 2,000. Endapo kila kampuni italipa dola 100 kwa mwaka, ina maana kwamba kwa makampuni yenye magari 300 kwa mwaka watalipa dola 3,000 badala ya 2,000 kama ilivyo sasa. Hii itasaidia wafanyabiashara wadogo pia kuweza kumiliki magari yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nashauri hii Sekta ipewe kipaumbele. Tulishauri kuwa kodi ya ongezeko la thamani ni bomu kwa uchumi wetu na sasa athari imeanza kuonekana. Tuliwaiga Kenya, lakini wenzetu waliondoa hiyo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na nature ya utalii ya Kenya ni kama kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni juu ya zoezi zima la uhakiki wa wafanyakazi hewa ambalo limechukua muda mwingi, nalo linaendelea kuwaacha Watanzania wengi bila ajira na kwa wale waliokuwa wanasubiri ajira pamoja na wale walioajiriwa mwezi wa Nane, 2015 ambapo walisitishiwa ajira kupisha uhakiki tangu Februari, 2016 hadi leo hawapo kazini na hawalipwi mshahara. Unategemea hawa Watanzania wataishi vipi? Tunataka majibu kwenye hili maana Mheshimiwa Rais alisema akiwa BoT kuwa zoezi la uhakiki wa wafanyakazi hewa kuwa ni kati ya miezi miwili au mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachoonekana sasa ni dhahiri Serikali hii haina fedha ama inaelekea kufilisika na hivyo kuamua kwa makusudi kujificha chini ya kivuli cha uhakiki ili kuondoa aibu ya kutokuwa na fedha ya ajira mpya. Fedha za nyongeza kwenye kupandisha madaraja, kuongeza mishahara kwa mujibu wa Sheria na Mikataba, hakuna watumishi kwenda masomoni wakilipiwa na mwajiri wake. Tunaomba majibu katika hili, maana bila Walimu wenye motivation, Madaktari, Manesi na kadhalika, hii nchi tunaiweka kwenye bomb. Hatua stahiki zichukuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya viwanda bila mikakati ya elimu yenye kutoa elimu na wanafunzi wa kada mbalimbali ili waweze kwenda kwenye viwanda tarajia; bila mikopo kwa kada zote kwenye elimu ya juu ni bomb. Bila kuwekeza kwenye motisha za Walimu kama nyumba, ofisi, Transport Allowance and Hardship Allowance; pia bila kuwa na uhakika wa maji ni ndoto kuzungumzia Tanzania ya viwanda kama hakuna umeme, miundombinu imara ya barabara, kuwekeza katika kilimo chenye tija ili kiweze kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda tarajiwa, itakuwa ni ndoto ya Abunuwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni juu ya kutokuwekwa asilimia za pato la Taifa kwenye Mpango wa Maendeleo, sababu na Sheria ya utekelezaji ya Mpango wa Maendeleo. Mpango wa mwaka 2011/2012 – 2015/2016 tuliazimia 35% ya pato la Taifa ziende kwenye Mpango wa Maendeleo lakini kwa sasa mpango hausemi chochote. Hii ni hatari sana maana tunaweza kukuta mpango huu ukitegemea wahisani zaidi, kitu ambacho ni hatari kama nchi tusipowekeza kwenye maendeleo yetu wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni juu ya umuhimu wa kuona review kwenye mdororo wa kutokuwa na mizigo Bandarini ambayo inatokana na tozo mbalimbali, wharfrage tunatoza dola 240 kwa futi 20 lakini wenzetu dola 70 na VAT on Transit na kadhalika.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kuweza kupata fursa hii ili niweze kutoa maoni yangu kufuatia ripoti ya Kamati ya Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nionyeshe masikitiko yangu ya kwamba katika ripoti hii ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ni robo moja tu ndiyo tumeletewa katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu. Tuko robo ya tatu sasa hivi kwa hiyo nilitarajia kabisa tungeweza kupata mpaka robo ya pili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017. Cha kusikitisha zaidi tunaona ni kwa kiasi gani bajeti hii haitekelezeki kama vile ambavyo tuliletewa hapa. Ikumbukwe wakati tumeleta hii bajeti mwanzoni nilisema kabisa kwamba hii bajeti haina uhalisia na nitashangaa sana kama hata itafikisha asilimia 70 ya utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoongea hivi leo, fedha za maendeleo hazijakwenda kwa kiasi kikubwa sana lakini zaidi madeni. Juzi wakati Waziri anatoa kuhusu hali ya madeni na hapa nisikitike kidogo kwa mwanafunzi wangu Stanslaus anasifia kwamba wanalipa sana madeni. Nizungumzie tu baadhi ya haya madeni ya Watanzania wa ndani ambao wanaidai Serikali na inapelekea hata hawa Watanzania wanauziwa mali zao na wengine wanajiua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa aliyotoa Waziri mwenyewe hapa ndani anaeleza kabisa kwamba mathalani wakandarasi wanadai shilingi trilioni moja, bilioni moja na milioni mia nne na mpaka sasa hivi wamelipa tu shilingi bilioni 360. Wanaotoa huduma za ndani wanadai shilingi bilioni 237 na wamemaliza kulipa shilingi bilioni 11 tu. Wazabuni wanadai shilingi bilioni 900 na kwa mujibu wa taarifa ya Waziri ya tarehe 19 wamelipa shilingi bilioni 49 tu. Hivi tunavyoongea hawa watu wanaotoa huduma hospitalini, shuleni, majeshini wanasitisha kwa sababu Serikali mmeshindwa kuwalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti sasa ningependa kujua mkakati wa utekelezaji wa ulipaji madeni haya ukoje. Jana mnasema madai ya Walimu mnafanya uhakiki yaani sasa hivi Serikali inajificha kwenye kufanya uhakiki. Madeni ya pembejeo tunafanya uhakiki, madeni ya Walimu tunafanya uhakiki, madeni ya wazabuni mnafanya uhakiki, kuajiri watu mnafanya uhakiki, muwe wazi mseme Serikali haina fedha ili Watanzania wajue kwamba Serikali haina fedha, kama wanauziwa mali zao ni kwa sababu Serikali haitaki kuwalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho kinasababisha hata Serikali isipate mapato kama ilivyokuwa ime-project, tulisema hapa kuna kodi zingine mmeziweka ambazo hazina uhalisia, hazitekelezeki, kodi kwenye sekta ya utalii, kodi kwenye transit goods. Ikasikitisha zaidi Mheshimiwa Rais anasema kabisa ni bora aje mtalii mmoja lakini alipe kodi, waje watalii wachache walipe kodi kuliko kuacha tusiweke hizi kodi ili watalii waje wengi. Mtalii akija alikuwa analipa hiyo kodi, akilala hotelini analipa na sehemu zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa tumewekeza kimkakati kwenye utalii kuhakikisha tunakuwa na angalau watalii hata milioni tatu, milioni nne ingesaidia kwani ni sekta pekee ambayo inatoa ajira nyingi, ni sekta pekee ambayo ingekuwa inaingiza fedha za kigeni. Leo Tanzania tuna vivutio vingi sana, tuna utalii wa fukwe, ukilinganisha hata na Afrika Kusini tu, wenzetu on average wana watalii zaidi ya milioni 15 sisi Watanzania eti milioni moja, halafu tunakaa hapa tunafikiri nchi yetu itaenda, tuna utalii wa kila aina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Afrika Kusini pale Soweto utakuta watu wamepanga foleni kuangalia sehemu aliyoisha Baba wa Taifa Mandela lakini hapa kwetu ukienda Butiama ambayo ni makumbusho ya Baba wa Taifa utashangaa. Uwanja wa ndege wa Musoma tumesema mturekebishie ili watalii waweze kwenda pale watu wanaenda kujenga Chato, ndiyo vipaumbele! Yaani badala uboreshe Musoma, uboreshe na kwa Baba wa Taifa ili watalii waje wengi kwenye makumbusho unaenda kujenga Chato! Vipaumbele vya nchi hii, inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweke mkakati wa kuhakikisha angalau tunapata watalii milioni tatu, milioni nne, Taifa letu litasonga mbele. Tuna vivutio vingi sana, eti vi-table mountain vya South Africa, sisi tuna milima mingi tu hapa, tuna fukwe nyingi. Leo Brazil fukwe zao wanazitumia vizuri sisi Watanzania tupo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, uwekezaji kwenye bahari kuu, wanasema Chenge report na vitu kama hivyo. Serikali ingeamua kujielekeza kutafuta wawekezaji kwenye uvuvi wa bahari kuu ingekuwa ni chanzo kingine kizuri tu ambacho kingeweza kutupatia mapato. Hii ina maana wale watu wavue wale samaki, tuwe tumejenga viwanda hapa hapa waweze ku-process hapa hapa itatoa ajira nyingi lakini pia tukisha-process na ku-pack tutasafirisha ina maana tutapata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote hayaonekani kama ni chanzo, tunabaki kusubiria Watanzania wakamatwe kwa boda boda, matrafiki siku hizi wanakaa kwenye magari wanasema kabisa sijui mnawa-promote, leo nimekusanya shilingi bilioni moja kutokana na makosa ya barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi huko mikoani, walala hoi waendesha pikipiki wanakamatwa, Tarime mfano hata tumeona Mheshimiwa Lacairo wa Rorya analalamika, mtu ameajiriwa na kapikipiki kake unamwandikia faini Sh. 90,000 atoe wapi wakati mwisho wa siku anatakiwa apeleke Sh.10,000 kwa tajiri wake, akishindwa pikipiki inachukuliwa na magari hivyo hivyo. Yaani sasa hivi Serikali hii ya Awamu ya Tano chanzo kikuu cha mapato ni kupitia makosa ya barabarani, aibu! Kama Taifa tuwekeze kwenye bahari, viwanda viwe vikubwa, kama nilivyosema vichakate hapa hapa, ajira zitapatikana tutasafirisha nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kingine cha mwisho ni kilimo. Zaidi ya Watanzania 80% wamewekeza kwenye kilimo lakini kilimo chetu hakina tija kwa sababu hata vichocheo vya kuhakikisha kilimo kina take over vyenyewe bado viko hoi. Huwa tunaimba hapa kuboresha miundombinu ya usafirishaji, kwa sababu mimi nikilima niko kule kijijini lazima niwe na barabara ambayo itanisababishia lori kubwa lifike niweze kusafirisha mazao yangu kutoka point A kwenda point B, barabara ni mbovu, hazijatengenezwa kabisa. Tunaona lami tu za kwenye highway, mkatengeneze na huko ambako ndiko wakulima wako wengi ili waweze kusafirisha mazao yao kutoka vijijini kuja mijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine ni umeme. Kaka yangu hapa Profesa Muhongo alisema ame-invest kwa mwaka huu ni zaidi ya shilingi trilioni moja na bilioni mia ngapi kwamba tutaona umeme unawaka vijijini. Ni matarajio yangu kwamba tutaona umeme unawaka huko ili hao wakulima wanaolima waweze kusindika yale mazao yasiharibike, waweze kujenga viwanda vidogo vidogo kuviongezea thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiwa na umeme, tukiwa na miundombinu mizuri ya barabara, maji yakawa yanapatikana tutaweza kuona kweli tunasonga mbele vinginevyo hatutaweza kuwa na mapato kabisa. Tutakuja hapa tunatoa bajeti, mapato ni hayo unaelekeza kwenye vinywaji, unaelekeza kwenye vikodi vya utalii kwa hiyo watalii hawaji mnakosa, tuwe na watu ambao wamesomea mambo haya waweze kuishauri Serikali na kuleta bajeti ambayo inaakisi uhalisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nimekuwa nawatetea sana hawa ndugu zangu wa Magereza. Naambiwa Askari Magereza wanaidai Serikali kuanzia mwaka 2012/2013, 2013/2014, 2015/2016 ndiyo nimesikia sasa hivi mmewapelekea ya 2015/2016 nataka kujua 2012/2013 na 2013/2014 ni lini mtaenda kuwalipa? Pia tuweze kujua fedha za kuweza kufidia yale maeneo ambayo mmechukua…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa sababu ni dakika tano nitakwenda kuongea kwa kifupi sana. Kwanza kabisa naunga mkono ripoti za Kamati zote mbili, lakini zaidi naomba Serikali ifanyie kazi ripoti ya Kamati ya Uwekezaji kwa yale yote ambayo tumeshauri pale na ambayo tumeyaona field. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa haraka haraka nisisitize kwa yale ambayo tumeandika kwenye Kamati yetu. Ni kweli kabisa tumeona athari ambazo zinajitokeza kwa kutokuwa na bodi kwenye taasisi na mashirika ya umma. Taratibu zinataka kwamba mchakato wa kuweza kuwa na bodi baada ya ile nyingine kukaribia kuisha walau uanze miezi sita kabla, lakini tumeshuhudia Serikali hii taasisi zinakaa bila bodi zaidi ya miaka miwili hadi miaka mitatu. Na mfano tumetolea Bodi ya TANAPA, imekaa zaidi ya miaka mitatu tunaona kabisa ile kesi ya concession fee ilihukumiwa tarehe 12 Septemba, 2014, lakini Serikali ikaona ni bora Taifa liendelee kupoteza kila mwaka zaidi ya shilingi bilioni 10 kuliko kuunda Bodi ya TANAPA ambayo ingeweza kufanya maamuzi na kuweza kupata fedha ambazo ni takribani zaidi ya shilingi bilioni 20 zimepotea, ambazo zingeweza kwenda kujenga zahanati na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kumekuwepo na watumishi kukaimu kwenye nafasi za watendaji wakuu kwenye mashirika yetu na taasisi kinyume kabisa na sheria inavyosema. Unakuta mtu amekaimu zaidi ya miaka miwili hadi mitatu, wakati inatakiwa ndani ya miezi sita mtu aweze kupatikana kwa nafasi husika. Hii inasababisha mashirika yetu, taasisi zetu zisiwe na ufanisi katika utendaji na tutaendelea kuona mashirika yakiwa yanajiendesha kihasara kwa sababu hatujaweza kutengeneza management ambayo kwanza kabisa imebobea na inajua ni nini inafanya. Ukimkaimisha mtu hawezi akafanya decision kwa sababu hajua kwanza ultimatum ya nafasi yake ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kuhusu madeni ambayo Serikali inadaiwa na hazi taasisi. Unakuta imepata huduma lakini inashindwa kulipa madeni haya. Kwenye Kamati tumeainisha; mfano ni madeni makubwa kutokana na mifuko ya hifadhi ya jamii, tumeona madeni takribani kwenye PSPF ukiyachukua yote kwenye categories zile tatu ni takribani shilingi trilioni 3.47 za wanachama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuja Naibu Waziri wa Fedha akatuahidi kwamba watatoa hati fungani ya takribani shilingi bilioni 290 ambayo ilikuwa ni deni linalotokana na miradi, lakini mpaka leo hawajaweza kutoa hiyo hati fungani, hawajaweza kulipa malimbikizo ya madeni ya mwajiri kwenda PSPF, hawajaweza kulipa takribani shilingi trilioni 1.7 ya yale madeni ambayo waliyachukua kwa wastaafu wale wa kabla ya mwaka 1999. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuishii hapo tu, Shirika kama DAWASCO ni shirika dogo sana, lakini unakuta linadai shilingi bilioni 16 kutoka kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Hizi shilingi bilioni 16 zingeenda DAWASCO zingeweza kusaidia na kuboresha huduma ya maji Dar es Salaam na Pwani, lakini unakuta hawalipi wakiambiwa hawalipi kwa sababu ni Jeshi basi linaendelea tu wanapata huduma. Ifike wakati hizi taasisi kama hazilipi na zenyewe zikatiwe maji, haiwezekani Mtanzania anashindwa kulipa 20,000 mnamkatia maji, lakini taasisi ya Umma inadaiwa mpaka shilingi bilioni 16 hamuwakatii maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uonevu na Mtanzania wa kawaida akisikia anashangaa sana, yaani akishindwa kulipa bili ya maji ya shilingi 10,000, 20,000 anakatiwa maji lakini unakuta mnadai zaidi ya shilingi bilioni 16 na bado huduma ya maji inaenda. TANESCO wanawadai, TSN wanadai, LAPF wanadai, Serikali mnadaiwa madeni mengi sana. Tuweze kulipa haya mashirika ili yaweze kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kwa haraka haraka kabisa, wakati tumepitia kwenye hizi taasisi tumegundua kwamba hizi taasisi zinajiendesha kihasara. Tatizo lingine ni kwamba fedha wanazozipata wanazitumia kwenye matumizi ya kawaida badala ya uwekezaji. Kwa mfano, kama ilivyoainishwa kwenye baadhi ya mashirika; tumeona NSSF walitumia zaidi ya asilimia 17 kinyume kabisa na vile ambavyo matakwa yanataka asilimia 10 kwa mwaka wa fedha 2015/2016; lakini pia kamati imeainisha AICC na mashirika mengine. STAMICO inajiendesha kwa hasara, wanaweza wakawa wanakopa benki wanakuja wanajitumia kwenye matumizi ya kawaida ambayo ni kinyume kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu mikataba ambayo mashirika yetu yanaingia, taasisi zetu zinaingia hasa zikiwa kwenye ubia na wawekezaji wengine. Hii imekuwa inalipeleka taifa letu kwenye shimo siku zote. Na ninashindwa kuelewa wataalam wetu ni kwamba tunakuwa hatujui ni nini tunafanya au hatuna uzalendo wa kutosha. Kwenye taarifa yetu umetolewa mfano wa mkataba wa Mlimani City; kwamba sisi tunakubali kuingia mkataba wa kupata gawio la asilimia 10 ya faida na tunasema kwamba tunaingia mkataba mpaka baada ya miaka 50 ndipo tunaweza tukapata ile mali, na ukiangalia ubora wa yale majengo ya Mlimani City ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, ni dhahiri kabisa ndani ya miaka 50 tutakuwa tunapata mabua. Yaani wale wawekezaji watafaidika wataondoka sisi wakitupa asilimia 10 tu, Taifa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante,

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii niweze kuchangia. kwanza kabisa, naunga mkono ripoti za Kamati zote mbili lakini nitajielekeza sana kwenye suala la elimu kama ambavyo tunajua elimu ya Tanzania iko ICU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kushauri baadhi ya maeneo ambayo Serikali inatakiwa iyafanyie kazi ili walau tuweze kuwa na elimu iliyo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Dunia ilishauri ili Taifa liweze kuwa na elimu bora walau tuweze kuwekeza 5% ya Pato la Taifa. Ukiangalia nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wenzetu wamewekeza vya kutosha. Kwa mfano, Kenya wamewekeza 6% ya pato la Taifa, Rwanda wamewekeza 5%, Uganda wamewekeza 4%, Burundi wamewekeza 3% lakini sisi Tanzania tumewekeza 1% tu ya Pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutashikana uchawi hapa, Wakuu wa Mikoa watawafukuza walimu kama tulivyosikia Mtwara, wanasiasa wataingilia, watawaghadhibu walimu lakini uhalisia ni kwamba hatujawekeza vya kutosha kwenye elimu ya Watanzania. Kama Taifa lazima tuwekeze vya kutosha. Kamati hapa imesema tunatenga fedha lakini haziendi.
Kwa hiyo, naomba kabisa Waheshimiwa Wabunge tuazimie na kwenye bajeti ya 2017/2018 tuhakikishe walau tunatenga 3% ya Pato la Taifa kwenye elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kushauri Rais aone kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuunda tume ya kuweza kuchunguza hali ya elimu nchini ili waje na mbadala wa nini kifanyike kuweza kufufua elimu yetu. Pia ni wakati sasa Waziri aweze kuteua Wajumbe wa Baraza la Kumshauri kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 1995 ambao watakuwa wanamshauri Waziri kitaalamu maana tumekuwa tukishuhudia sasa hivi Mawaziri wanatoka tu na matamko. Kwa hiyo, tunaomba kabisa aunde lile Baraza liweze kumshauri kitaalam ni vipi tuweze kusonga mbele katika elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuwathamini walimu, mimi ni mwalimu. Walimu wasipokuwa na motisha hatuwezi kuwa na elimu bora. Imeelezwa hapa kwa mujibu wa takwimu za CWT ni zaidi ya shilingi trilioni 1.06 walimu wanadai. Wale ambao wamerekebishiwa mishahara ni walimu 5,000, walimu 80,000 bado hawajarekebishiwa mishahara wanadai zaidi ya shilingi bilioni 300, kuna wale walimu ambao wamestaafu takriban 6,000 wanadai zaidi ya shilingi bilioni 480 na kuna wanaodai madeni ya likizo ambayo hata bado hayajaboreshwa. Malengo ya BRN walisema walimu waweze kulipwa madeni yao ndani ya siku 90, sasa ni kwa nini Serikali inachukua muda mrefu sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu kwa Wote (Universal Secondary Education). Kwa maoni yangu nashauri sera hii tusiitekeleze sasa hivi kwa sababu Serikali haijajiandaa. Kwa mfano, ukisema elimu ya msingi iishie darasa la sita na waendelee kwenda sekondari kwa wote, tumejenga sekondari zipi za kuweza ku-absorb hawa watoto wanaotoka shule ya msingi na kuendelea moja kwa moja, bado hatujajiandaa! Ni dhahiri sasa tuweze kujiandaa kwanza kama nchi, kwa baadaye ndiyo tuweze kutekeleza hii Sera ya Elimu kwa Wote.
Kwa hiyo, iendelee watoto kujiandikisha shule wakiwa na miaka saba na elimu ya msingi iendelee kuwa darasa la saba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni wanasiasa kuingilia masuala ya kitaalam ya walimu. Utakuta Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa anajaziwa mafuta eti anaenda kukagua shule wakati huo huo wakaguzi ambao ni wataalam wanakagua kwa 30% tu na wanasema hawana fedha za kuweza kuwazungusha kukagua shule. Sasa hawa Wakuu wa Wilaya na Mikoa wengine hata hawana utaalamu huo, wako busy wanajaziwa mafuta kuzunguka kukagua shule. Tusiingilie kabisa kwenye masuala ya kitaalamu tupeleke fedha kwa wakaguzi waweze kukagua na kutoa mapendekezo ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kwenye afya kuhusu Taifa la vijana kuteketea na viroba. Kamati hapa imesema na mimi Jimboni kwangu kabisa waliniambia nilete Hoja Binafsi. Hivi viroba na sasa hivi hali imekuwa ngumu vijana asubuhi tu na mmewakataza wasiende kwenye bar mpaka saa kumi, kwa hiyo, wenyewe wakiamka tu asubuhi na pikipiki zao wamekamatwa na polisi na wengine kazi ngumu ngumu wanakunywa viroba vile. Viroba kwanza havina standard! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu nilivyokuwa nimekwenda baada ya hii likizo fupi tumezika vijana zaidi ya wanne na wananchi wamenituma kama Bunge tuazimie viroba vifutwe Tanzania, visizalishwe wala visiingizwe Tanzania.
Kwa hiyo, naunga mkono kabisa mapendekezo ya Kamati kuhusiana na viroba viweze kupotea kabisa vinginevyo tunateketeza Taifa letu, vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa wanateketea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine na cha mwisho ni kuhusu dawa za kulevya, zimezungumzwa kwa upana wake. Kama Taifa tujiulize ni kwa nini tumekuwa tukiimba, hatutekelezi. Kabla ya mwaka 2010 hata sijawa Mbunge tunaona kuna ma-champions walikuwa humu wakizungumzia dawa za kulevya na wengine wakataja kabisa, Marehemu Amina alitaja baadhi ya watu hapa. Tukaja Bunge la Kumi wengine tukawa Wabunge, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Mheshimiwa Bulaya, Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Rais Kikwete akasema ana orodha….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti,
nakushukuru sana kwa kuweza kunipatia fursa hii nami niweze
kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Naomba
Waheshimiwa Wabunge kama tunatambua ni nini wananchi
wametutuma kufanya kwenye Bunge hili Tukufu, basi
tuwatendee haki kwa kufanya yale ambayo wametutuma
kufanya na kutokujitoa ufahamu na kufanya kinyume na
ambavyo tumetumwa na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono
hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni na ninaomba
Waheshimiwa Wabunge msome hotuba zote pamoja na
kwamba mtakuwa mnayo mengine kichwani, lakini hotuba
ya Upinzani kwa kweli imeeleza mengi na mazuri kwa Taifa
letu, tuweze kuishauri vema Serikali ili tuweze kusonga mbele
kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 nilisema kabisa
wakati wa bajeti imepitishwa na niliandika kwenye mtandao
wa Bunge, nikasema hii bajeti ikitekelezwa hata kwa asilimia
70 tu, nikatwe kichwa changu. Mbunge mmoja, ndugu yangu
Mheshimiwa Chegeni akaingia inbox akaniambia
unamaanisha nini? Sasa napenda nimwambie
nilichokimaanisha ndiyo tunachokiona leo, kwamba mpaka
leo bajeti ya maendeleo hata asilimia 40 hatujafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kwamba
kuliko kuja na bajeti ambazo hazina uhalisia, kama mpaka
leo hatujafika asilimia 40, ile bajeti ya mwaka jana, tuchukue
nusu yake ndiyo tuilete. Tulete bajeti ambazo zinatekelezeka.
Tusiandike matumaini kwenye makaratasi mwisho wa siku
hata asilimia 50 tu hamfikishi. Tuwe na uhalisia ili hata
unapokuwa umeelezwa kwamba mathalan Mkoa wa Mara
Jimbo la Tarime Mjini kwenye maendeleo kwa mwaka wa
fedha 2017/2018 tutaleta shilingi bilioni moja, basi na hiyo
shilingi bilioni moja tuweze kuitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo
ningezungumzia tuliondoa duty free kwa majeshi kwa maana
Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi, Askari wa
Uhamiaji, Askari wa Majini na Magereza. Cha ajabu mpaka
leo kumekuwa na double standard. Kuna wengine
wameshalipwa mara mbili, kwa maana ya kila mwezi laki,
laki; wameshalipwa shilingi laki sita. Jeshi la Wananchi wa
Tanzania na Askari Polisi, lakini Askari wa Uhamiaji, Majini na
Magereza mpaka leo hawajalipwa. Ndugu zangu, tunataka
kujua ni kwa nini kunakuwa na double standard?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba kabisa
Mheshimiwa Waziri Mkuu awaangalie ndugu zetu Magereza,
wamekuwa wakionewa sana. Unakuta Askari Magereza ana
degree lakini bado analipwa mshahara kama yule askari wa
kidato cha nne. Leo mnawalipa hawa wengine, lakini hawa
Askari Magereza niliowatja mpaka leo hamjawalipa. Wale
watu ni muhimu sana na ikizingatiwa kuna watu
mnawapeleka kwa kesi za kubambikwa kule Magereza.
Hawa watu wakiamua kugoma, wale watu waliopo
magerezani kule kutakuwa hakukaliki. Kwanza mngekuwa
mnatumia busara zaidi, mngewalipa wale kabla hata
hamjawalipa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Naomba
mzingatie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna madeni wanadai
ya mwaka 2012/2013; 2013/2014 mpaka leo hawajalipwa. Leo
mfungwa akitoroka, hawa ndugu zetu wanapewa adhabu
kutokwenda masomoni, wanapewa adhabu ya kukatwa
fedha, maisha wanayoishi ni duni na kipato chao ni duni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu na
Waziri husika tunaomba hawa ndugu zetu muazingatie na
wenyewe waweze kupata hiyo package ambayo mliiondoa
ya duty free nao waweze kupata stahiki zao kama
mnavyowapa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Waziri
Mkuu ametanabaisha kwamba wamejitahidi sana katika kuwawezesha wananchi, lakini ukisoma ameainisha kwamba
kuna shilingi bilioni moja sijui pointi ngapi wamewapa vijana
kwa mfuko wa vijana na shilingi bilioni 4.6 kupitia
Halmashauri, kwamba ndiyo hapo wamewezesha
wananchi. Hatuko serious na Serikali hampo serious.
Mlituambia mmetenga milioni 50 kwa kila kijiji au mtaa,
mpaka leo mtuambie mmetekeleza vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waziri Mkuu akija
akasema kwamba Halmashauri zimejitahidi kupeleka 4.6
billion kuwezesha wananchi ilhali mkijua kuna Halmashauri
nyingine hazina kipato cha kutosha, mathalan Halmashauri
ya Mji wa Tarime, tumejitahidi, hapo zamani walikuwa hata
hawatoi hela. Kwa mwaka huu, tumejitahidi tumetoa ten
million. Ten million only; leo mnasema tunaweza
kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali itekeleze ile ahadi
yao ya shilingi milioni 50 kila mtaa na kijiji; tumehamasisha
wananchi wameunda vikundi mbalimbali na SACCOS
tunazihitaji hizo shilingi milioni 50. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye elimu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndugu yangu amesema kabisa
tumejitahidi kutoa elimu bure na vitu kama hivyo. Ni dhahiri
baada ya kuja hii elimu bure sijui, wakasema kwamba
usipopeleka motto, unafungwa; kweli tumeandikisha watoto
wengi sana mashuleni, lakini hatuangalii idadi. Tunatakiwa
tuangalie quality ya ile elimu ambayo tunaitoa. Leo mmesajili
wanafunzi wengi, lakini walimu wanadai madeni mengi na
hamjawapa mazingira mazuri ya kuwafanya wafundishe
watoto wetu waweze kuelewa, hawana motisha yoyote ile,
leo mnategemea kutakuwa na ufaulu mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesema mmerekebisha
madawati. Sawa, madawati kwanza kuna sehemu nyingine
bado hayajatosheleza, madarasa hayatoshi. Wananchi
wanajenga, Serikali inashindwa kwenda kuezeka, vitabu
hamna pamoja na kwamba TWAWEZA jana wamesema ratio
ni moja kwa tatu, lakini mimi kwangu darasa la kwanza na la pili ni moja kwa tano; darasa la tatu mpaka la saba,
kitabu kimoja; wanafunzi 50 mpaka wanafunzi 100. Hapo
tunategemea elimu bure itatoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe serious, kama tunataka
tutoe elimu ambayo ni nzuri kwa wanafunzi wetu, elimu bora,
tuwekeze na walimu wawe na motisha, wapewe fedha
stahiki, walipwe madeni yao na wawe na mazingira mazuri
ya kufundishia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee afya. Hospitali ya
Mji wa Tarime mmeandika kwamba bado ni Hospitali ya
Wilaya ya Tarime, lakini mnaleta OC na basket fund ambazo
zinatumika idadi ya wananchi wa Mji wa Tarime, wakati
kiuhalisia wanahudumia wananchi wa Wilaya nzima ya
Tarime, watumishi mmepunguza idadi wakati wanahudumia
wananchi wa Wilaya nzima ya Tarime, wengine wanatoka
Rorya na wengine Serengeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwepo na vigezo
stahiki. Kama mnaona ni vyema hospitali ile iwe ya Wilaya,
basi tunaomba OC na basket funds zije kwa idadi ya
wananchi wa Wilaya ya Tarime na siyo idadi ya wananchi
wa Mji wa Tarime. Mnawapa kazi kubwa watumishi, unakuta
daktari anafanya masaa zaidi ya 30 wakati alitakiwa awe
kazini kwa saa nane tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye maji. Kuna
mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria ambao usanifu
ulishafanyika na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa wapo
tayari ku-sponsor huo mradi ambao unaanzia Shirati, Ingili Juu,
Utegi, Tarime mpaka Sirari. Kuanzia mwaka 2011 watu
wamefanya design mpaka leo haujatekelezwa. Napenda
kujua ili kutatua tatizo la maji Tarime, ni lini huu mradi utaanza
kufanya kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, fidia ya ardhi ya
wananchi ambao Jeshi la Wananchi wa Tanzania
wamechukua. Nimekuwa nikiimba sana hapa Bungeni na
Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba unisikilize katika hili.
Mheshimiwa Mama Ritta Kabati mwache Waziri Mkuu
anisikilize, maana nimekuwa nikiimba hii kuanzia mwaka 2007.
Jeshi la Wananchi wa Tanzania limechukua maeneo ya
wananchi wa Nyandoto, Nyamisangula na Nkende mpaka
leo hawajalipwa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante,

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's