Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Devotha Methew Minja

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Awali ya yote niwashukuru akinamama wa Mkoa wangu wa Morogoro kwa kunipa fursa ya kuwa mwakilishi wao. Hali kadhalika nikishukuru Chama changu kwa kuniona kwamba nafaa kuwakilisha katika Bunge hili, bila kuwasahau wapambanaji wenzangu wa ITV. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia vizuri sana Mpango ulioletwa mbele yetu. Yako mambo mengi sana, lakini hakika mambo haya nilikuwa nikijiuliza tu, mikakati na mipango mingi kiasi hiki tunaifanya kwa ajili ya watu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikapata jibu ni kwa ajili ya wananchi na maendeleo ya Taifa lao, lakini hivi tunavyojadili mambo haya muhimu ambayo yanakwenda kulenga kuleta maendeleo ya wananchi, tukiwa tumejifungia, lakini wananchi hawajui ni kitu gani kinachoendelea, kwa kuzuwia chombo cha umma kutangaza matangazo haya moja kwa moja, naona kama hatuwatendei haki wananchi. Hali kadhalika naona kama tutakwama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mataifa mbalimbali yaliyoendelea ni yale ambayo yametumia vizuri vyombo vya Habari. Mfano Malaysia, ukienda ukimuuliza hata dereva tax, National Goal ni ipi na ni njia gani ya ku-achive National Goal? Watakueleza kwa sababu wako informed na wanatumia vyema vyombo vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunakuja na Mpango hapa tunasema ni kwa ajili ya wananchi na maendeleo ya Taifa, lakini wananchi hawa hawana fursa ya kupata na kuelewa tunajadili nini! Tumezungumza mambo mbalimbali ambayo ni ya vyanzo vipya vya mapato, tumezungumza habari ya mambo ya retention, lakini mambo hayo hamuoni kama wananchi wangepata fursa ya kufuatilia moja kwa moja kujua na sisi tunafanya nini, ingeweza kutusaidia pengine mipango hii ikaweza kutekelezeka kwa uzuri na kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata taarifa hapa kwamba, TBC Chombo cha Umma ambacho kilianzishwa kwa lengo la kutoa huduma kwa umma; TBC inasema ni gharama kuendesha matangazo haya ya moja kwa moja! Hata hivyo, tumekwenda mbali zaidi kuangalia mchakato, ukiaangalia Air Time kwa TBC kwa kipindi cha saa moja gharama yao ni 7,080,000/=, lakini tukiangalia saa ambazo tumekuwa tukizitumia hapa kuanzia masaa sita mpaka saba kuendesha Bunge live. Pia tumejaribu ku-calculate kwa vipindi vinne vya Bunge kwa maana ya vipindi vitatu vifupi na kipindi kimoja cha Bunge la Bajeti ambacho ni kirefu, tukapata ni sawa na saa 290 za kurusha Air Time na ukizidisha unapata 2.2 billion na siyo 4.2 kama tulivyoelezwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika tunakumbuka Serikali, kamera tunazoziona huku zilifungwa na Star TV enzi hizo, lakini hivi sasa ikatokea mambo mengine mengine hapo wakasema siyo vema ni lazima taarifa hizi zirushwe na vyombo vya umma. TBC ikajengewa uwezo kwa kupewa bilioni 4.6 inunue vyombo vya kisasa na kutumia kamera hizi ambazo zimefungwa na Star TV, lakini matokeo yake hiyo 4.6 haijafanya chochote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii TBC wanakuja na crew ya watu 20 kurusha live hapa, kitu ambacho kinaongeza gharama. Hamuoni sasa ni wakati wa kuruhusu hivi vyombo binafsi vifanye kazi vizuri, kuhakikisha vinasaidia kusukuma mipango hii kama TBC imeshindwa? Hamuoni kama sasa ni wakati wa Serikali kupunguza hivi vikwazo kwa vyombo hivi binafsi na kupewa hizi ruzuku ambazo TBC inashindwa kufanya kazi? Ruzuku zielekezwe kwa vyombo binafsi vifanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niende kwenye mipango mbalimbali niliyoiona kwenye kitabu hiki; nimeona habari ya reli, miundombinu, barabara, lakini sijaona mahali popote ambapo tumezungumza jinsi ya kusaidia wananchi ambao wameathirika kutokana na miundombinu hii. Nikizungumzia Kilosa hivi sasa kuna wananchi wanaishi kwenye mahema kwa zaidi ya miaka mitano, wameathirika kwa sababu reli ya kati ilikatika katika eneo la Godegode, tuta la Kidete lilivunjika ambalo nimeona mpango mnalitengeneza, lakini kuvunjika kwa tuta lile ambalo lilisababisha mafuriko kwa wananchi hamjaweka mpango wa kuwapa hata viwanja wananchi leo hii, tangu 2010 wanaishi kwenye mahema, wakiwemo wananchi wa Kidete, wananchi wa Mateteni na wananchi wa Magole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni wakati umefika wakati tunaandaa mipango hii tuwafikirie na wananchi hawa ambao waliathirika kutokana na kuharibika kwa miundombinu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mna mpango wa kufanya Tanzania kuwa ni Tanzania ya Viwanda. Tunavyozungumza hivi Morogoro viwanda vilikuwa vingi, leo hii viwanda mbalimbali vimekufa, lakini hamjatueleza kwamba, viwanda hivi vitafufuliwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha Canvas, kiwanda cha UNAT cha matunda ambacho akina mama walikuwa wanatumia kwa ajili ya matunda yao! Leo hii akinamama ndiyo wanaotembea na mabeseni kichwani, haikuwa kazi yao! Kiwanda cha Asante Moproko, Kiwanda cha Ceramic, Kiwanda cha Tanarries, ambavyo vyote hivi vilikuwa vinatoa ajira kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye suala la maji; limezungumzwa kila mahali, lakini Mkoa wa Morogoro ni Mkoa ambao una mito mingi sana, lakini Mkoa wa Morogoro ndiyo unaoongoza kwa kukosa maji. Nikianza katika Manispaa ya Morogoro pekee, ambayo kwa sasa inategemea Bwawa la Mindu ambalo limejengwa mwaka 1984 wakati huo idadi ikiwa ndogo sana; leo hii Serikali imekuja na mkakati mpya wa kujenga Bwawa la Kidete, hatukatai! Imekuja na mpango mpya wa kujenga mabwawa mengine ya Vidunda, hatukatai! Lakini kweli mipango hii ni kwa manufaa ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii inatumia mito ya Morogoro ambayo maji yatakwenda sehemu nyingine, sisi wana-Morogoro wenye mito yetu tunabaki bila maji! Nenda katika Manispaa nimesikia majibu ya Naibu Waziri leo asubuhi, Kihonda, Area Five, Kilakala, kote huko hakuna maji japo anasema kwamba, mpango wa MCC ulisaidia, lakini tunavyozungumza hivi sasa huo mpango wa MCC wananchi hivi sasa ni kuandamana kila wakati wakienda MORUWASA kudai maji! Kwa nini sasa kwa mito hii mingi wasifikirie kujenga bwawa jipya kwa kutumia hii mito yetu iliyopo, ili kuhakikisha kwamba wanamaliza tatizo hili la maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye masuala ya migogoro ya wakulima na wafugaji, nazungumza hili kwa masikitiko makubwa. Hivi karibuni kupitia vyombo vya habari tumesikia jinsi mauaji ya mifugo na wananchi yakiendelea katika Wilaya ya Kilosa na Mvomero.
Hivi karibuni nimetembelea vijiji vya Kunke kule Mvomero, wananchi wa vijiji sita wamechangishwa shilingi mia tano kila mmoja eti kwa ajili ya kufanya operation ya kuwaondoa wafugaji. Kazi ya kufanya operation ya kuwalipa Polisi ni kazi ya wananchi? Wananchi kila mmoja alitozwa shilingi mia tano ili wawaondoe wafugaji, zoezi ambalo linapaswa kusimamiwa na Serikali kupitia Wizara husika, lakini leo hii wananchi wanaambiwa kama ninyi hamtaki migogoro hii basi wachangie ili wafugaji waondolewe. Hii ni kuendelea kuongeza uhasama katika makundi haya mawili kwa kuwa yote yanafanya shughuli halalli ambazo zinachangia pato kwa Serikali.
Tukirudi kwenye suala la Mpango wa NFRA wa kuuza mazao, hivi sasa Serikali imeanzisha soko la Kibaigwa ambalo linatoa huduma kuwezesha wakulima wa Morogoro, Dodoma na Manyara kufanya biashara ya mazao, lakini hivi sasa wakulima wa Morogoro hawapeleki mazao yao pale kwa sababu ushuru...
MWENYEKITI: Nakushukuru sana.
MHE. DEVOTHA MATHEW: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hoja zangu katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa Walimu hauwiani katika ya shule za mijini na vijijini ambapo katika Wilaya ya Kilosa Shule ya Msingi Mabwegere kwa zaidi ya miaka 10 ilikuwa na Mwalimu mmoja hali iliyosababisha baadhi ya wazazi wasio na taaluma ya elimu kujitolea kwenda kufundisha watoto wao, hali hii ilisababisha shule hiyo kushindwa kufanya vizuri. Ipo haja ya kuangalia upya mgawanyo huu wa Walimu badala ya kurundikana katika Manispaa ya Morogoro wakati Wilayani hakuna Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la X-ray mashine katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro unategemea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ili kutoa huduma za matibabu zilizoshindikana katika Wilaya saba za Mkoa lakini X-ray mashine iliyopo imenunuliwa zaidi ya miaka 14 iliyopita na haina ufanisi hali inayolazimu wagonjwa kwenda nje ya hospitali (private) kufanya kipimo hiki. Aidha, kutokana na matukio mengi ya ajali wajeruhi pia wanategemea hospitali hiyo. Naomba Serikali ione umuhimu wa kununua X-ray machine mpya kwa ajili ya hospitali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya zahanati zimefunguliwa na Mwenge miaka mitano iliyopita na baada ya Mwenge zimefungwa badala ya kutoa huduma kwa wananchi licha ya kuwa zimejengwa kwa nguvu za wananchi. Mfano wa zahanati hizi ni Bigwa iliyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la mafuriko ya mara kwa mara katika Mto Mkondoa, Wilayani Kilosa. Serikali iliahidi tangu mwaka 2010 kuwa wangejenga tuta ili kuzuia mafuriko lakini mkandarasi alipewa fedha kazi haijaisha na wananchi wanaendelea kupata madhara makubwa ya nyumba kujaa maji kila msimu wa masika pamoja na kusomba reli ya kati maeneo ya Godegode.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa TASAF katika Wilaya ya Kilosa na Mvomero, baadhi ya kaya zisizo maskini zimepewa fedha bila utaratibu na wenye shida na maskini wanakosa nafasi hizo. Ipo haja kwa watathmini wa TASAF kufanya upya uhakiki wa kaya maskini zinazostahili kusaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wa Viti Maalum kukosa ofisi katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kama Waziri wa TAMISEMI alivyoeleza Bungeni. Ipo haja ya Waziri wa TAMISEMI kuwaandikia Wakuu wa Mikoa kutoa ofisi hizo ili kuwezesha Wabunge wa Viti Maalum kufanya kazi zao za kisiasa kwa wananchi badala ya kutumia ofisi za chama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufukuzaji wa watumishi wa umma bila kutumia haki za msingi za binadamu. Tumeshuhudia Serikali ikiwafukuza watumishi kwa madai ya kutumbua majipu, hatupingani na utumbuaji huu, lakini haki za msingi za binadamu zizingatiwe. Mfano, Mkurugenzi Kabwe wa Dar es Salaam kutumbuliwa mbele ya mkutano wa hadhara bila kujali staha yake, familia, mke, watoto na marafiki, hali hii ni ya kukemewa. Utaratibu mwingine ungeweza kufuatwa kwa Waziri mwenye mamlaka kumshughulikia badala ya kumuaibisha hadharani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufukuzaji huu wa watumishi umewakumba pia Mabalozi ambao walipewa saa 24 wawe wamerudi nchini. Lazima haki za mtumishi zizingatiwe mfano kuangalia utu na familia. Mfano, kuna watoto ambao wapo shuleni nje ya nchi na wazazi wao bila kumpa muda wa kujiandaa kuhamisha familia inakuwa sio sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzuiaji wa vyombo vya habari kufanya kazi zake mfano waandishi wa TV hawaruhusiwi kuingia Bungeni na kamera badala yake wanapewa taarifa ambazo ni edited. Huu ni ukiukwaji wa Katiba na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi juu ya Bunge lao linaloendeshwa kwa kodi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama kubwa za Mwenge. Mwaka huu uzinduzi wa Mwenge umefanyika Mkoani Morogoro ambapo tumeshuhudia kila halmashauri zimeelekezwa kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia maandalizi hayo na halmashauri zote zimetoa fedha za wananchi na kuzipeleka katika shughuli za Mwenge. Kama hiyo haitoshi Walimu wa shule za msingi na sekondari wamelazimishwa kutoa mchango wa Sh.10,000 ili kuchangia maandalizi ya uzinduzi wa Mwenge. Hii si sahihi, si haki fedha za wananchi walipa kodi kutumika kukimbiza Mwenge ambao bado hauna tija kwa wananchi huku wanafunzi wakikosa masomo ili kuhudhuria shughuli za Mwenge.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi hewa kudumu katika Wizara mbalimbali kwa miaka mingi ni udhaifu kwa watendaji wa Serikali waliopewa dhamana na Serikali. Badala ya kuwakamata watuhumiwa pekee ni muda muafaka kuwatia hatiani wasimamizi na maafisa wa idara tofauti walioshindwa kutimiza wajibu wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia agizo la Rais kuhusu watumishi kulipwa mshahara usiozidi milioni kumi na tano ni lini utekelezaji huu utaanza?

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Naomba na mimi nichangie mawili, matatu kwa dakika hizi tano ambazo umenipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwa uzito wa bajeti hii ya kilimo ambayo tunafahamu pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 70 inategemea kilimo. Ninachokiona katika kujadili bajeti hii, wakulima na wafugaji hawajui ni nini tunachojadili, ikizingatiwa kwamba changamoto ni nyingi katika sekta hii. Nafikiri, hatuzungumzii habari ya televisheni tu, tunazungumzia pia habari ya redio. Mkulima anapaswa akiwa shamba leo hii ajue mpango wa Serikali wa kununua maelfu ya tani za mahindi; mkulima ajue kwamba ni kiasi gani cha fedha kimetengwa kwa ajili ya kusaidia pembejeo, lakini leo hii tunawanyima fursa wakulima hawa kujua wakati tunakabiliwa na matatizo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo suala tu la kusikiliza redio mkulima akiwa analima, watu wako kwenye bodaboda wanasikiliza redio, wako kwenye daladala wanasikiliza redio, wanajua ni nini hatma ya sekta hii muhimu ambayo inachangia pato zaidi ya asilimia 70.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Morogoro. Hivi karibuni Waziri wa Kilimo alifika Mkoani Morogoro; mauaji makubwa yametokea, wananchi wameuawa, mifugo imeuawa, lakini hatma ya kutatua migogoro hii kule Mvomero wameamua kujenga korongo la kilometa 13 linalogharimu shilingi milioni 147, lenye urefu wa futi zaidi ya sita kwenda chini, upana zaidi ya ekari moja kutenganisha wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi shilingi milioni 147 zingejenga Zahanati mbili, zingejenga malambo matatu ambayo yangesaidia wananchi hawa ambao migogoro yao mikubwa ni kutokana na kukosa vitu muhimu ikiwemo haya malambo. Leo tumeamua kuanza kuwagawa Watanzania hawa badala ya kutafuta suluhu ya kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, enzi za Mwalimu Nyerere migogoro hii haikuwepo, lakini hivi sasa watu wamehodhi maeneo makubwa, wakulima hawana sehemu ya kulima, ranchi zilizokuwa za Serikali zimehodhiwa, Serikali ilitoa maamuzi kwamba zaidi ya ekari 5,000 zigawiwe wananchi hawa lakini hakuna kitu, wamegawana vigogo, sasa hivi wanakuja kuamua kuwatenga wakulima na wafugaji. Sijui tunakwenda wapi katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Berlin wameamua kuvunja ukuta ili kuwaunganisha watu, leo sisi tunasema tunajenga korongo kumtenganisha mkulima na mfugaji! Watu hawaombani chumvi, hawaombani kibiriti! Shule wanafunzi wanashindwa kuvuka upande wa pili! Naongea kwa masikitiko makubwa; wananchi hawa wangejengewa mikakati ya kutatua migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu alifika pale, wananchi wanamnyooshea vidole Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, RPC, DC, migogoro inatokea hawana habari kinachoendelea, matokeo yake Mahakama ilitoa rulling kutengeneza buffer zone Halmashauri/Serikali iliamua kujenga korongo kwamba sasa korongo litengenezewe. Hata mipaka ya nchi zetu, hakuna makorongo. Inasikitisha sana! Fedha hizo ambazo ni mapato ya wananchi ambayo yangesaidia lakini sasa hivi yanakwenda kutengeneza makorongo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, korongo hili halikuzingatia hata ushauri wa Madiwani wala NEMC zaidi ya kuharibu mazingira. Kwa hiyo, naomba Serikali ifikirie upya jinsi ya kusaidia jamii hizi kurudisha utamaduni.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na siungi mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kwa maandishi tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro katika Kijiji cha Kambala. Serikali imeshindwa kutatua mgogoro huu. Serikali imejenga korongo la kuwagawa wakulima na wafugaji kufuatia migogoro ya mara kwa mara. Korongo hili limetumia zaidi ya shilingi milioni 147, fedha za mapato ya halmashauri ilizokuwa inadai Kiwanda cha Mtibwa Sugar.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zingeweza kusaidia kujenga zahanati na majosho ya mifugo badala ya kujenga korongo la kuwatenganisha wakulima na wafugaji, tunatengeneza Taifa la namna gani? Tunahubiri amani na ushirikiano lakini tunakuja na maamuzi ya kuwagawa Watanzania kwa kutenganisha jamii hizi. Nashauri Serikali itumie busara kupitia maamuzi haya ili kurudisha mahusiano kwa jamii hizi. Tatizo la wakulima na wafugaji lingeweza kutatuliwa kwa njia ya majadiliano badala ya kutumia nguvu. Serikali iangalie mashamba yaliyohodhiwa bila kuendelezwa kwa muda mrefu pamoja na ranchi zikiwemo za Wami Dakawa zitumiwe na wananchi baada ya Serikali kufanya utaifishaji na kugawa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliyopita iliagiza zaidi hekari 5,000 zigawanywe kwa wananchi ili kuondoa kero ya upungufu wa maeneo ya kilimo na ufugaji. Eneo hilo limechukuliwa na vigogo wamegawana badala ya kutolewa kwa wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali ichukue hatua kama ilivyoagizwa wananchi wapate ardhi hii badala ya vigogo kujinufaisha na maamuzi ambayo yameshatolewa na Serikali. Ni wakati wa Serikali kusimamia maamuzi yake yaliyokwishatolewa na si kuyabatilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, NFRA - stakabadhi ghalani. Ukopaji wa mazao kwa wakulima mwaka jana umesababisha usumbufu mkubwa na wakulima walikopwa mazao kwa muda mrefu lakini walicheleweshewa malipo yao. Wengine wamelazimika kutumia nguvu kudai jasho lao. Tumeshuhudia wakulima wa maeneo ya Kibaigwa, Mbeya, Morogoro waliandamana kudai malipo yao. Zoezi la kuwalipa wakulima hao limechukua muda mrefu huku wakulima wengi wakipata hasara katika taasisi za fedha walizokopa kwa ajili ya kilimo na walitegemea kurejesha baada ya msimu wa kilimo badala yake iliwachukua miezi na miaka kudai malipo pasipo kupata jibu.
Nashauri Serikali iwalipe fidia wakulima kwa kuwa mazao waliuza kwa shilingi 500 na kuuza kwa 800, Serikali ilitengeneza faida kwa nini Serikali isingetoa fidia/kifuta jasho kwa wakulima hao? Mfumo huu wa NFRA unapaswa kuangaliwa upya na kwa mwaka huu Serikali ije na mpango/mfumo mpya wa kuwalipa wakulima mara baada ya kuuza mazao yao. Pia ikiwezekana NFRA iwe na mfumo wa kuwakopesha pembejeo na mbegu wakulima ili walipie baada ya kuvuna mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru wa mazao, hii imekuwa kero ya muda mrefu kwa wakulima na ni ukandamizaji wa wakulima ambapo kuna milolongo ya ushuru wa mazao kutoka shambani kwenda sokoni, sokoni kwenda stoo za soko na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri huu unaendelea kuwakandamizi, wakulima wanakata tamaa badala ya kuuza mazao yao sokoni mfano soko la mazao Kibaigwa sasa wanakwepa ushuru na wanauza mazao mashambani kama lumbesa na kuendelea kupata hasara. Imefikia wakati sasa Serikali kuangalia upya viwango vya ushuru wa mazao, kuondoa mageti ya ushuru kwenye vijiji ili kuwezesha wakulima kuwa na ushuru mmoja tu usiowaumiza na pengine ushuru mwingine wapewe wafanyabiashara wanaonunua mazao toka kwa wakulima au kwenye masoko.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa njia ya maandishi juu ya hoja ya Viwanda na Biashara kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufa kwa viwanda Morogoro; Mwalimu Nyerere alipendekeza Mkoa wa Morogoro kuwa Mkoa wa viwanda tangu miaka mingi iliyopita kwa lengo la kusaidia Jiji la Dar es Salaam kutokana na miundombinu iliyopo ikiwemo umeme, barabara, reli, maji na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vilitegemewa na wananchi wa Morogoro, vilisaidia kupunguza tatizo la ajira, ambapo hata wananchi wale waliweza kuendesha maisha na kupeleka watoto shule, hali hii ilisababisha population na kupelekea kuwepo kwa vyuo vingi vikuu ambavyo vilitengeneza wanafunzi waliofanya kazi katika viwanda, lakini viwanda hivi leo hii vimekufa baada ya Serikali kuvibinafsisha!
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kubinafsisha lilikuwa ni kuongeza uzalishaji na kupanua viwanda, lakini hivi sasa viwanda vimebaki kuwa magodauni, vingine vinafuga mbuzi na vingine vimebaki tupu baada ya wawekezaji wasio na nia njema kuuza vyuma vilivyopo ndani ikiwemo kiwanda cha Kanivas cha maturubai na kiwanda cha Asante Moproko kilichokuwa kinatengeneza mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijitapa kuwa inataka kuingia katika uchumi wa viwanda, lakini tutafikaje bila ku-review upya matatizo yaliyosababisha kufa kwa viwanda hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa Serikali, ipitie upya mikataba ya ubinafsishaji, ambapo baadhi ya wawekezaji wasio na nia njema walichukua viwanda kwa lengo la kujinufaisha ambapo wengine walichukua viwanda kwa lengo la kupata mikopo katika mabenki, ambapo wengine walichukuwa mikopo na kufungua biashara zingine zikiwemo biashara za mabasi na malori badala ya kuwekeza kwenye viwanda na matokeo yake viwanda vimekufa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi zaidi ya 4000; mpaka sasa wengine wameshakufa, walikuwa wanadai fidia baada ya ubinafisishaji kwa lengo la kuwaendesha na kulipa vinua mgongo, lakini wafanya biashara hawa hawakuwalipa Wananchi hao hadi leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka ama kupitia upya mikataba, ukaguzi wa viwanda vya Komoa, Kanvas, Asante Moproco, Ceramic Unats, Tanaries, Tanzania Shoe, ambavyo vyote vimekufa na vimegeuzwa kuwa mazalia ya popo na kufugia mbuzi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kufungia viwanda vya Plastics nchini; hivi sasa kuna zaidi ya viwanda 20 vya kutengeneza plastics vinavyotengeneza mifuko, ambavyo vingi vimefungiwa kwa sababu vinasababisha uchafuzi wa mazingira, kiwanda kimoja cha mfuko wa plastic kinaajiri watu 200 kwa viwanda, hivi 20 tunawanyima ajira watu 4000! Kwa nini Serikali isije na plan B ya kuwataka wawekezaji hawa wa viwanda vya biashara kama vya mifuko kuagiza material ya kuozesha mifuko badala ya kuja na hoja ya kuongeza micro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imevifungia viwanda hivi kwa kuvitaka vitengeneze mifuko minene yenye unene wa macro 50 kutoka kwenye micro 30 ya hivi sasa. Wawekezaji hao wana mikopo na walifuata utaratibu wote wa kupata vibali na kuwekeza, lakini badala ya kuja na mkakati rahisi kusaidia nchi iendelee kuwa na viwanda sasa inaua viwanda!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Uingereza, Kenya, Ethiopia, viwanda vya Plastics ndiyo vinasaidia kuongeza ajira na kuinua uchumi. Katika hili wamefanikiwa kutokana na ubunifu ambapo ungesaidia kuwezesha mifuko hii badala ya hapa nchini kuja na mkakati wa kufungia viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ije na plan B ya kusaidia viwanda hivi kwa kuruhusu ku-import material kuwezesha mifuko na hii itasaidia hata bidhaa zingine zinazotumia mifuko kama chumvi, viroba, sanzu na kadhalika. Lakini tukija na mpango wa kuwa na mifuko macro 50 mifuko hii itakuwa ghali na watu wa kawaida hawataweza ku-afford.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kupata nafasi hii. Awali ya yote niipongeze kwa namna ya pekee hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni ambayo imefafanua mambo muhimu na imeitendea haki sekta hii ya habari. Nianze kwa kupongeza kazi nzuri ambazo zinafanywa na waandishi wa habari hapa nchini, kazi zinazofanywa na wasanii, kazi zinazofanywa na wanamichezo mbalimbali hasa wale wanaojitolea kwa nguvu zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Mheshimiwa Zitto kwamba hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na kuisahau timu ya Taifa Stars hata Twiga Stars wamefanya kazi nzuri sana na walifuzu South Africa baada ya kuichapa Eritrea kwa bao nne kwa mbili, tulipaswa tuwaenzi kinadada hawa ambao wanafanya vizuri na wapo katika list ya timu nane bora za Afrika zinazofanya vizuri.
Baada ya kusema hayo vilevile Mheshimiwa Waziri ameshindwa hata kutueleza ni jinsi gani hii Wizara inaendelea kuwaenzi wanamichezo ambao wametumia nguvu na jasho lao kwa mfano Ndugu Francis Cheka, ambaye baada ya kumchapa Mserbia, hivi sasa Ndugu Francis Cheka, anaokota chupa, ndiyo ajira yake aliyonayo hivi sasa mkoani Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoka Morogoro ninamfahamu, nimekuwa mwandishi na nimekuwa nikiandika habari zake, kungekuwa na mpango wa kuendelea kuwaenzi watu hawa siyo tu pale baada ya kumaliza pambano, angalau awe role model aendelee kufanya kazi zake vizuri na vijana wengine wavutiwe na kazi nzuri ambayo anaifanya kwa maana tuone ni yapi manufaa ya yeye kupigana na kupata ushindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niende kwenye suala ambalo mwaka huu Aprili 15, Idara ya Habari, Mawasiliano ya Bunge ilitoa taarifa zake kwa vyombo mbalimbali vya habari, kwamba inaanza mpango wa kuwa na feed maalum ambayo tv itakuwa inarushwa na Bunge. Hali kadhalika Waziri naye alifika Bungeni na akatudhihirishia hilo, kwamba hivi sasa taarifa za Bunge zitakuwa zinawafikia wananchi kwa uhalisia, kwa high quality na tukawa tunaamini hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu ambao wanasema wameutoa katika Mabunge ya Jumuiya za Madola, utaratibu huu hapa kwetu kidogo ni tofauti, feed maalum zinatumika kwa nchi ambazo hasa waliangalia wingi wa vyombo vya habari, kuondoa congestion ya waandishi wa habari wote kuingia kwenye Bunge kupiga picha, ikizingatiwa kwamba waandishi wa television lazima awe mwandishi na mpiga picha, achana na redio achana na magezeti, sasa wakawa na mpango maalum ambao utasaidia Bunge liwe na television yake isaidie vyombo binafsi kila mmoja kwa wakati wake aweze ku-rely hizo information na kuzisambaza katika vyombo vyake. Wakati huo huo wananchi wawe na uwezo wa ku-access hiyo television na kuangalia ni kitu gani kinachojiri Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwetu ni tofauti na kinachofuata hivi sasa, tangu kuanza kwa mpango huu tumefanya monitoring ya day to day, kuna vitu ambavyo tumevibaini, mojawapo ni kufanya editing ya kupitiliza, taarifa tunazozizungumza, taarifa ambazo zinakosoa Serikali hazipewi nafasi, uchujaji huu wa namna hii ambao mwishoni mnatoa vitu vile ambavyo tu vinapendeza Serikali hatuwatendei haki wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeangalia hata uwiano wachangiaji wa upande wa Serikali na kambi pinzani, hakuna uwiano sahihi, tuna ushahidi, tunarekodi, na tumefanya monitoring za kutosha. Waziri Kivuli wa Ulinzi Mheshimiwa Juma Hamad Omar akiwasilisha taarifa yake hapa, amepewa dakika tatu tu, tena za mwishoni za kushukuru, waandishi wa habari wameshindwa kuiandika ile habari, na kama mli-monitor saa mbili habari hiyo haikuweza kutokea, sasa uchujaji wa namna hii tunakwenda wapi, kama tuna mambo ya feed maalum? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini sasa waandishi wapiga picha wasiruhusiwe wakaingia wakachukua kile ambacho wanafikiri kitafaa, kuendelea kuwaruhusu waandishi wa magazeti na wapiga picha kuingia, huku waandishi wa television wakisubiri nje na baada ya kurekodi wanapelekewa clip kwenye external ambazo tayari zimeshachujwa, waandishi hawa wataandika nini, ushahidi upo na tunafuatilia na tunajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hilo mpango huu wa feed maalum bado quality yake ya picha siyo nzuri, mfumo unaotumika waandishi wa habari wakichukua ni lazima waende waka-condense lazima waende waka-convert kwenye adobe kwa maana hiyo wakatanue picha quality inapungua, hiyo ndiyo hali halisi. Kwa maana hiyo, kuna haja sasa ya kufikiria ili kuondoa utata kwa waandishi hawa wa television pamoja na kuwepo huu mfumo wa Bunge lakini wawe na uwezo wa kupiga picha kwa quality ambazo wanafikiri zinakidhi vigezo kwenye vyombo vyao vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isiruhusu mpango huu pamoja na hoja za awali kwamba ni gharama, Mheshimiwa Nape alituambia ni shilingi bilioni nne tulifanya assessment za kutosha, tukagundua wala haifiki bilioni Nne ilikuwa ni shilingi bilioni 2.1, wadau wamejitokeza wako tayari kusaidia wamezuiwa, mpango huu bado unaendelea kuwakwamisha waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru, hili ni jambo ambalo Serikali inapaswa kuliangalia upya. Televisheni ya Taifa (TBC) inafanya nini kama inaendeshwa kwa kodi za Watanzania, kwa nini haipewi jukumu hili la kupeleka hizi taarifa kwa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi, katika taarifa ya Waziri amezungumza mambo mbalimbali, lakini sijaona mahali ambapo amekuja na mpango wa kuwasaidia waandishi wa habari ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu. Waandishi wa habari wanafanya kazi kutwa nzima, hawana mikataba, hawana maslahi mapana, lakini amekuja na mkakati kwamba lazima walipie Press Card kwa shilingi 30,000 ili kuingiza mapato katika Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema siyo hilo tu, Wizara kama inataka kumsaidia mwandishi wa habari ingekuja na mpango ambao ungewabana wamiliki wa vyombo vya habari walau kutenga asilimia fulani ya kuwasaidia waandishi hawa wawe na bima za afya, wawe na security za kazi, waweze kufanya kazi yao kama kweli tunatambua mchango wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli mnatambua mchango wake wewe mwenyewe binafsi Waziri kila unapopita, kila unachofanya, hufanyi bila waandishi wa habari, lakini inapokuja kuhusu masuala yao hapa hatujaona sehemu ambayo umejikita kupambania maslahi ya watu hawa! Zaidi ya hayo umenukuliwa ukisema sasa unataka kuja na mkakati wa waandishi wa habari kuwa na degree, ni jambo la ajabu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea nyingi watu wenye taaluma ya diploma ndiyo wazalishaji wakubwa na hata hapa nchini tunatambua mchango wa walimu wenye diploma, wauguzi, madaktari wenye level ya Assistant Medical Officer (AMO) wanafanya kazi nzuri sana, lakini ni kwa nini inapokuja kwa waandishi wa habari kije kigezo cha degree? Tulitegemea kuona mikakati kwamba nini kifanyike walau wapate muda wa kujiendeleza…
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Siungi mkono hoja.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nichangie katika Mpango wa Serikali wa Maendeleo 2017/2018 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza sana Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, lakini ni lazima tuseme ukweli, hali ya maisha ya wananchi vijijini ni ngumu zaidi na wanaishi kwa kula mlo mmoja na wengine wanashindwa hata kupata mlo kutokana na mazingira magumu. Zipo taarifa kutoka vyombo mbalimbali yakiwemo magazeti, mitandao kwamba Septemba, 2015 mabenki yalikuwa na faida ya shilingi trilioni 64, lakini Septemba, 2016 faida za mabenki ni shilingi trilioni nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Waziri anasema uchumi umekua! Hivi kweli uchumi umekua, difference ya shilingi trilioni 60 ni gap kubwa. Serikali lazima ijitathmini, imekosea wapi? Hivi sasa mabenki yanajiendesha kwa hasara, hayatengenezi faida. Kama hayatengenezi faida, Serikali inakosa kodi na pia, hata wananchi nao wanakosa mikopo katika benki. Benki za Serikali ndiyo zipo hoi zaidi, TWB, Twiga Bancorp, TIB, ndiyo zimesinzia kabisa kwa kuwa na mtaji wa negative. Tumeshuhudia Serikali kuichukua Twiga na kuipa jukumu BOT kusimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi ya kujiuliza katika Serikali hii wakati kuna hali ngumu za maisha kwa wananchi, lakini Serikali imeshindwa kuzuia matumizi ya hovyo hovyo yanayogharimu fedha na kusababisha hasara kwa Taifa. Mfano halisi ni Benki ya TIB ambayo malengo yake ilikuwa ni kuendeleza kilimo, kutoa mikopo, kusaidia katika miradi ya umwagiliaji, kujenga na kuwekeza katika miradi ya kilimo, lakini zilizokuwa idara zake sasa hivi nazo zimekuwa ni benki kamili; TIB Cooperate, TIB Commercial, TABB Bank ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, benki zote hizi ma-CEO wao wote wanalipwa zaidi ya shilingi milioni 20 na kama imeshuka ni baada ya Mheshimiwa Rais kutoa tamko la kupunguza mishahara. Pia, katika hili, benki zote hizi zina Wakurugenzi wanaolipwa zaidi ya shilingi milioni 10, lakini hakuna wanachofanya; kuanzia asubuhi hadi jioni wanahudumia watu wawili au watatu tu kwa siku kwa sababu, benki hizi Makao Makuu yake yapo Dar es Salaam badala ya benki hizi kuwa vijijini kuwasaidia wakulima ambao kwa zaidi ya 80% kilimo hicho kinatengeneza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ugumu wa maisha unaonekana waziwazi katika uwekezaji wa viwanda; Bakhresa ameripotiwa na vyombo vya habari kuwa, zaidi ya 70% ya biashara zake zime-freeze na anatarajia kuhamishia hub zake katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha TTPL hivi sasa kilikuwa kinasindika zaidi ya tani 46,000, sasa hivi kiwanda hiki kinasindika tani 16,000 lakini cha kushangaza Serikali haitazami viwanda vya ndani vilivyo ndani, lakini inaangalia kujenga viwanda vipya badala ya kuangalia kwa jicho lingine viwanda hivi. Badala ya Serikali kutegemea kuanzisha viwanda vipya visivyo na tija na kuacha vya zamani vikiendelea kuteketea, lazima Serikali ikubali kuelezwa ukweli, ikae chini na kujipanga na kuweka vipaumbele vya kuendelea kutafuta mbinu za kufufua uchumi na kuwaondolea wananchi mateso ya ugumu wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, priorities za Serikali kwa wananchi wake hazieleweki. Tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu; kama uchumi umekua, kwa nini wasikopeshwe kama tunakusanya shilingi trilioni saba? Kwa nini Mfalme wa Comoro asingesaidia kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Vyuo Vikuu? Priority ni uwanja wa mpira wa kisasa Dodoma au kujengewa Msikiti na siyo kusaidia wahanga wa Kagera ambao hawajui hatima ya maisha yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kama takriban zaidi ya mwaka watumishi hawajui hatma ya maisha yao. Hawajui lini zoezi hili litamalizika; hawakopesheki na mabenki, kisa uhakiki. Hii siyo sawa. Serikali ina watumishi wa umma siyo zaidi ya 5,000, uhakiki gani usioisha? Uhakiki gani unazuia watumishi kupanda madaraja na kushindwa kupata haki yao ya msingi ya kupata mikopo?

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na nikiri kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii lakini katika taarifa ya Mwenyekiti aliyowasilisha utashangaa kwamba hakuna suala lolote linalozungumzia juu ya Faru John, hakuna suala lolote linalozungumzia juu ya Loliondo, ni burning issues kwa sasa hivi, Watanzania walitaka wapate majibu, lakini Kamati haikuweza kwenda ili kuweza kupata kielelezo ili kuleta Bungeni, ni jambo la kushangaza. Sijui ni Kamati ipi ambayo inaweza ikalifanyia kazi zaidi ya Kamati ambayo ilikuwa maalum kwa ajili ya kuleta masuala haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa haraka, niongelee suala la kulinda corridors wanakopita wanyama, kama tulivyosikia kwenye taarifa ya Kamati ya Maliasili na Utalii, Wizara iliamua kuzuia maeneo ambayo ni mapito ya wanyama. Nazungumza hili kwa sababu wanyama ambao wanatoka Saadani kwenda Wamimbiki, Mvomero, Mikumi kuelekea mpaka Ruaha wananchi wamevunjiwa nyumba zao katika Wilaya ya Mvomero wakijumuisha pia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kutokana na kupisha hizi corridor za wanyama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kushangaza Serikali imewavunjia wananchi nyumba hizi, haikuwalipa fidia lakini Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imejengwa kwenye mapito hayo ya wanyama. Kama ni sheria ni lazima ikate pande zote mbili. Kuendelea kuwavunjia wananchi nyumba zao bila kuwalipa fidia huku Serikali ikiendelea kuweka majengo ya Halmashauri na kujenga nyumba za wafanyakazi si kuwatendea haki wananchi. Naomba Wizara iangalie upya suala hili na kama kuna uwezekano walipe fidia kwa wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mambo mengine ya migogoro ya wakulima na wafugaji Mkoani Morogoro. Ziko Kamati mbalimbali ambazo zimeundwa na Bunge hili lakini mpaka sasa hivi hakuna taarifa zozote ambazo zimefanyiwa kazi kusaidia kupunguza migogoro hii. Tunashuhudia watu wanapigwa mikuki ya midomoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Rais akifuta hati mbalimbali za mashamba. Tatizo ni ardhi, kwa nini mashamba hayo yasirudi yakawasaidia wananchi wa Wilaya za Mvomero na Kilosa ambako ndiko kwenye matatizo na migogoro ya kila siku? Hati hizi ambazo zimefutwa kwa nini ardhi hizi zisigawanywe kwa wananchi? Mpaka sasa ardhi zile zimeendelea kuwa mashamba pori pamoja na kufutwa huku wananchi wanaendelea kuwa na migogoro kutokana na uhaba wa ardhi. (Makofi)
Suala lingine ni kuhusu korongo lililojengwa la kuwatenga wakulima na wafugaji Wilayani Mvomero. Suluhu ya migogoro hii si kuendelea kuwatenga wakulima na wafugaji. Jamii hizi zinategemeana, hawa ni Watanzania, wanashirikiana lakini Serikali imeendelea na msimamo wake wa kuendelea kujenga korongo lile mbali na kwamba tulisema lisitishwe ili kutafuta suluhu kati ya makundi haya mawili ambayo yameendelea kuwa na migogoro ya siku hadi siku. Serikali imeendelea kutumia fedha zaidi ya shilingi milioni 17 kuendelea kuchimba korongo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo ambayo tunahitaji Wizara husika iyafanyie kazi ione. Kuna Kamati Maalum ya kutataua migogoro ya…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia sana hotuba zote tatu ikiwemo ya Waziri, hotuba ya Kamati na hotuba ya Kambi ya Upinzani. Katika hotuba zote hizi, kila hotuba iligusa kuwapongeza madaktari kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwa Watanzania. Tunafahamu kazi yao ni ngumu kazi ya kutetea uhai wa wanadamu siyo kazi rahisi. Kazi ya kuahirisha kifo siyo kazi rahisi ni kazi ambayo kwa kweli inatoka moyoni katika kuhudumia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia madaktari wakifanyakazi katika mazingira magumu, tumeshuhudia wengine hata waki- risk kwenye kazi zao magonjwa, kupata maambukizi, lakini madaktari hawa hawakati tamaa wanaendelea kuwahudumia Watanzania. Kwa kweli, niwapongeze sana madaktari kwa kazi ngumu wanayoifanya. (Makofi)

Pamoja na kazi hii sasa wanayoifanya lakini kuna mambo ambayo tukiyaangalia yanakatisha tamaa. Daktari anafanya afanyavyo kuhudumia wagonjwa walio wengi, lakini inatokea viongozi kama DC, RC anamtumbua hadharani Daktari - DMO akishasikiliza malalamiko ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara, anasema kuwanzia leo hana kazi. Nafikiri ifike mahali tuwape moyo watu hawa ambao wanajitoa kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaktari wana madai yao ya msingi, kwa zaidi ya mwaka mmoja hivi sasa Daktari Bigwa kwenye zile call allowance kwa maana mgonjwa kazidiwa saa nane saa tisa ya usiku analipwa shilingi 25,000 na dakitari wa kawaida analipwa shilingi 15,000. Madaktari hawa kwa zaidi ya mwaka hospitali nyingi hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwa Mkoa wa Morogoro. Hospitali ya Mkoa wa Morogoro inahudumia wagonjwa 500 kwa siku na hii ni baada ya hospitali ile kuwa ya rufaa kwa maana inahudumia wagonjwa wanaoshindikana katika Wilaya zake zote. Hospitali hii pamoja na ukubwa kuhudumia wagonjwa 500 ni sawa na wagonjwa 15,000 kwa mwezi, lakini hospitali hii haina x-ray machine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, x-ray machine iliyopo ni ambayo imenunuliwa tangu vita ya pili ya dunia, kwa sababu hospitali ile ilikuwa ya Jeshi. X-ray inagharimu siyo zaidi ya shilingi milioni 100, hospitali hii haina. Wagonjwa wanatoka na drip wanakwenda Mazimbu, wanakwenda hospitali ya Jeshi kwenda kufanya x-ray. Hilo nimelishuhudia mwenyewe na tumefuatilia na tumewahi hata kusema hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mortuary, hivi leo ndugu yako akipoteza maisha katika Mkoa wa Morogoro utalazimika kumsitiri pasipo hata kusubiri ndugu, kwa sababu mortuary hazifanyi kazi. Kweli kwa hospitali hii ambayo ina hadhi ya kuwa ya rufaa inashindwa kutengeneza tu mortuary kwa ajili ya kuwaifadhi wapendwa wetu ili basi walau waweze kuagwa kwa heshima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala lingine la Madaktari Bingwa. Tumekuwa na ajali nyingi sana Mkoa wa Morogoro, Daktari Bingwa wa mifupa hakuna, theatre kwa ajili mifupa hakuna, theatre iliyopo ni moja na inategemewa kwa maana ya magonjwa yote, akina mama wanaojifungua ndiyo hiyo hiyo. Watu wenye vidonda ndiyo hiyo watu wa ajali ndiyo hiyo. Nafiki Waziri alitizame kwa namna nyingine suala hili ili kuipa hadhi hospitali ya Mkoa wa Morogoro iweze kuwa na theatre room.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la sakata la madaktari. Serikali ya Awamu ya Nne, kipindi cha nyuma ilikuwa ikihamasisha kwa maana ya ule mpango wa brain bridge kutoka nje, madaktari wetu ambao wamesomeshwa na kwa fedha za Tanzania watoke nje, waje nchini, tena nakumbuka Rais wa Awamu ya Nne, ndiyo ulikuwa mkakati wake wa kuwaomba Watanzania walioko nje warudi hapa nchini watoe huduma kwa Watanzania wenzao. Nakumbuka walikwenda Cuba, Botswana Uingereza na kwingineko na baadhi ya madaktari nafikiri waliitika wito wa Rais wa Awamu ya Nne wakarudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii cha kushangaza Tanzania ambayo ina upungufu wa madaktari, inawachukua madaktari kwenda kutoa huduma kwa Wakenya. Tumeushangaza ulimwengu kwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia daktari mmoja kwa takwimu nimepitia hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa vijijini daktari mmoja anahudumia watu zaidi ya 78,000 na nane, kwa mjini anahudumia watu 25,000. Wenzetu Kenya daktari mmoja anahudumia watu 15,000. Leo hii sisi ndiyo wa kupeleka Madaktari Bingwa, madaktari wetu, watoto wetu, waende wakahudumie kuwaponyesha Wakenya wakati wamesomeshwa na kodi za Watanzania! Kuna mahali ambapo tunabidi kukubali kwamba tumefanya makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, najaribu kuwatizama wale ambao hawakujitokeza kwa maana walikuwa na nia pengine ya kutoa matibatu kwa Watanzania, kuwaajiri madaktari 258 kati ya wale ambao walitahiniwa na kuwaacha wale wazalendo ambao walikuwa na nia ya uzalendo siyo sawa. Nafikiri priority ingekuwa kwa wale ambao walisema wana nia ya kuwatumikia Watanzania zaidi, kubaki nchini na kusaidia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya Serikali inasema ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya, hivi sasa tuna kata zaidi ya 3,900, hospitali ambazo zinamejengwa katika kata hizi ni hospitali 448 ambayo ni sawa na asilimia 11 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu unatekelezeka kwa namna hii? Yako mengi ambayo tunataka kuyajua, flyover ndiyo ni maendeleo, flyover moja ambayo ni shilingi bilioni 100 ni sawa na kujenga hosptali ngapi za Kata? Ni zaidi ya hospitali 250. Priority kwa Watanzania walio wengi ni flyover au ni kupata hospitali ili wapate huduma za afya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu suala la upungufu wa vifaa. Ukienda kwenye hospitali kifaa cha kupima wingi wa damu baadhi ya hospitali za private unapata, siyo hospitali za government. Ukienda kupima hospitali za government itakuchukua siku tatu kufahamu wingi wa damu, private ndani ya saa kadhaa unapata jibu, kwa sababu hospitali za government zinazidiwa na wagonjwa, ni kwa nini vifaa hivi muhimu visiwepo kwenye hospitali za government zikaweza kuwasaidia wagonjwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa naliangalia sana suala...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niwapongeze waandishi wa habari ambao wanafanya kazi yao vizuri sana. Tuna kila sababu ya kuwapongeza waandishi kwa sababu tujiulize tu kama Taifa hili lingekuwa halina waandishi hakuna vyombo vya habari sijui tungekuwa kwenye giza la namna gani. Tunapenda tuwapongeze kwa kazi ambayo wanaifanya, japo tunajua wanafanya kazi katika mazingira magumu kuliko ilivyo kawaida. Tunaendelea kuwapa moyo waendelee kupambana kuendelea kutoa elimu na kuelimisha taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani (Waziri Kivuli) alikuwa ametoa pongezi nyingi kwa harakati mbalimbali ambazo Waandishi wa Habari wanaendelea kufanya katika kujaribu kujitetea na kuhakikisha kwamba wanaendelea kuifanya kazi yao. Pamoja na kwamba hotuba ile imechinjiwa baharini lakini mimi nawapa comfort kwamba tutaendelea kuwasemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Waziri wakati wa hotuba yake, amewasifu wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari, wanamichezo lakini sijasikia mahali akizungumza kuhusu habari ya mateso ya waandishi wa habari. Waandishi wa habari ambao walivamiwa na kuumizwa wakiwa katika press conference ya Chama cha Wananchi (CUF) ambao nao ni wadau muhimu nilitarajia angewapa pole. Hali kadhalika kwa wasanii, Ney wa Mitego na Roma Mkatoliki nao waliteswa ambao nao pia ni wadau wake, alipaswa nao awape pole kwa kazi kubwa ambayo wanafanya pamoja kupitia madhila mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri amenukuliwa akisema kwamba yeye ni msikivu na yupo tayari kuhakikisha kwamba anaendelea kusaidia tasnia hii ya habari iendelee kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni zaidi ya waandishi 30 wamepitia manyanyaso makubwa, wengine wakiwekwa ndani na Wakuu wa Wilaya, vyombo vya habari vikivamiwa ikiwemo redio ya Clouds, tunamuomba Mheshimiwa Waziri wakati ana windup hapa atueleze ni nini hatma ya ripoti iliyoandaliwa na Mheshimiwa Nape Nnauye wakati akiwa Waziri kuhusu sakata la kuvamiwa Clouds. Si hiyo tu pia atuambie ni sheria ipi ambayo inamruhusu DC kumzuia mwandishi wa habari asiingie katika Wilaya eti apate kibali cha kuandika habari.

Tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze kwa hii sheria ambayo RC, DC ana uwezo wa kumuweka mtu rumande kwa saa 48 iletwe Bungeni irekebishwe kwa sababu imekuwa ikitumika kama kigezo cha kuwaumiza waandishi wa habari. Tumeona Ndugu Mnyeti ambaye ni DC wa Arumeru amewaweka Waandishi wa Habari ndani kisa wameingia katika eneo lake la kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo waandishi wa habari walitambuliwa rasmi kwa maana ya kuhakikisha professional hii ya waandishi wa habari inafanya vizuri. Tunashukuru hivi sasa Serikali inatambua kwamba tasnia ya habari ni muhimu na inafanya kazi. Hata hivyo, yapo mambo mengine ya msingi ambayo tunajiuliza, kama uandishi wa habari ni tasnia muhimu kama ilivyo professional zingine mfano za udaktari, wanasheria kuna mambo ya msingi sana ambapo yanatufanya tunashindwa kuielewa sheria hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea mwandishi wa habari amefanya makosa ya kitaaluma sheria hii inasema akamatwe na polisi afikishwe mahakamani, lakini taaluma kama ya udaktari, endapo daktari atafanya makosa ya kitaaluma kuna sheria kwamba bodi inapitia, inamuajibisha lakini hakuna harakati za haraka haraka za kumpeleka polisi na kumfikisha mahakamani. Imewahi kutokea daktari ambaye alikuwa afanye operesheni ya kichwa akafanya ya mguu, lakini alifikishwa mahakamani? Kwa nini tunapokuja kwenye suala la uandishi wa habari wakamatwe na polisi wafikishwe mahakamani, tunaona hapa kuna double standard. Tunaomba kama kweli hii ni sheria na tumeamua kuitambua tasnia ya waandishi wa habari basi kama mtu atakuwa amefanya kosa la kitaaluma bodi zihakikishe zinamwadhibu kwa kuangalia taaluma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu ukata wa hivi sasa kwa vyombo vya habari, hii haijawahi kutokea. Hivi sasa waandishi wa habari hawana kazi za kufanya, kuna poromoko kubwa la waandishi kuachishwa kazi. Kampuni za The Guardian, Free Media, Azam na New Habari Cooperation zimepunguza waandishi. Ni kwa nini waandishi hawa wanapunguzwa? Ni kwa sababu hali imekuwa ngumu, wanafanya kazi katika mazingira magumu. Gazeti ambalo lilikuwa linatengeneza nakala 26,000 sasa hivi linatengeneza nakala 5,000. Hali hii inakuwa ngumu zaidi kwa sababu Serikali haipeleki matangazo kwenye hivi vyombo vya habari hususani vya private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Rais akihitaji kufanya press conference anaita vyombo vyote, Mkuu wa Wilaya au RC wakitaka kufanya press conference anaita vyombo vyote lakini ikija kwenye suala la matangazo vyombo vya binafsi vinabaguliwa. Kwa nini tusitende haki tuwezeshe hizi private sector zifanye kazi zipate matangazo ziweze kuhudumia Taifa hili? Kama kuna mkakati wa kuhakikisha kwamba tunadumaza vyombo hivi tuelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima Serikali iangalie imetoa mamlaka hivi hivi sasa kwa Idara ya Habari - Maelezo yenyewe ichuke jukumu la kuratibu matangazo yote. Katika matangazo ambayo yanakwenda kwenye vyombo vya habari, Idara ya Habari - Maelezo ambayo imepewa jukumu ya kuratibu matangazo inapata commission ya asilimia 10, kwa hiyo imeacha kazi yake ya msingi sasa hivi inahakikisha inatafuta matangazo. Hii ni kama ilivyo sasa hivi traffic ambapo wameacha kazi zao za msingi za kuhangaika na ajali inahangaika na tochi za kukusanya. Tunaomba tusaidiwe tujue kama kweli suala hili la kuratibu matangazo ambalo linakwenda kwa njia ambayo ni ya kibaguzi kupitia Idara ya Habari - Maelezo, ni kwa nini utaratibu wa zamani usitumike na vyombo vyote vipate haki katika kupata matangazo ili viweze ku–retain waandishi ambao wameajiriwa katika vyombo hivi vya habari. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, tukitoka hapo tuzungumze kuhusu hofu iliyopo hivi sasa kwa vyombo vya habari. Hakuna uhuru kabisa wa vyombo vya habari hapa nchini. Tumemsikia Mheshimiwa Rais katika ziara zake Mkoani Shinyanga alisema yapo magazeti matatu ambayo yupo karibuni kuyafungia, japo hakuyataja lakini hii moja kwa moja kama mkuu wa nchi inaleta hofu kwa waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kuona kwamba pengine ni mimi au yule. Kwa hiyo, waandike habari ya kuipendeza Serikali na kuacha kuandika habari za kukosoa Serikali pale ambapo inakwenda kinyume na utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sakata la Bashite kuvamia Clouds, Rais alinukuliwa kwamba vyombo vya habari haviko huru kwa kiasi hicho na kutoa karipio kali. Tulitegemea kwamba Rais angesaidia kwa mtu kama huyu ambaye amekiuka maadili ya utumishi wa umma kwa sheria ya mwaka 1995 mpaka sasa hivi asingekuwa kazini. Kwenda kuivamia studio na waandishi wa habari ambao wanafanya kazi zao kihalali na kuhakikisha waandishi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, sekta hii muhimu kwa uchumi wa Taifa. Kiwango cha kutangaza utalii kipo chini hali ya kuwa na tozo nyingi zinazotozwa zikidaiwa matumizi yake ni promotion kupitia Bodi ya Utalii mfano watalii wanalipa dola moja per head wanapolala kwenye hoteli per night na zinapelekwa Bodi ya Utalii. Matozo mengi yanafanya watalii wengi kukimbilia Kenya na mpaka Kenya wana-captalize Mlima Kilimanjaro ni wao na watalii wanafikia kwao due to number of charges zisizo na sababu. Katika eneo la matangazo mfano ndege za Kenya zimeandikwa Kilimanjaro na zinakwenda nchi nyingi duniani, kwa hiyo, ni rahisi kuwaaminisha wageni kuwa Mlima Kilimanjaro upo Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwe na strategies nzuri za ku-promote utalii na kuondoa siasa kama za kusema tunanunua ndege kubwa ya Dreamliner itakayoruka Ulaya mpaka Kilimanjaro ikiwa na watalii is this a strategy? Hapo hapo mkoa wenye utalii umejaa siasa za chuki mpaka kukera wageni, kwa mfano RC kaweka mtu ndani muda mrefu kwa zaidi ya miezi minne bila dhamana kwa kesi ambayo ina dhamana, yote haya wageni wanayaona na wanatushushia value.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA wafanye kazi na kupunguza matumizi yasiyo na lazima. Kwa mfano kuna Mawaziri walikuwa wanatumia mali za TANAPA kama magari, ndege kama mali zao binafsi na zikatumika mpaka kwenye kampeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Faru John na Faru Fausta ambapo Faru Fausta gharama za matunzo yake ni kubwa wakati matukio ya ujangili ni makubwa na yanaendelea. Hata taarifa ya Faru John namna alivyopotea inajulikana ila imefunikwa funikwa na imepita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoteli nyingi za kigeni zina- charge gharama kubwa na masharti yake ni magumu. Hoteli hizi zinawalenga hata wazawa ambapo huendi bila appointment na ndiyo hao faru wanapotelea kwenye hizo hizo hoteli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maliasili na nishati, matumizi ya mkaa yanaendelea kuongezeka nchini na hii inatokana na kupanda kwa gharama za gesi. Serikali huwezi kuhimiza matumizi ya nishati mbadala wakati gesi na umeme gharama yake ipo juu. Makaa ya mawe,
wawekezaji kama Dangote amepewa achimbe kwa nini yasitumike pia kwa wazawa kama nishati ili waache kuchoma mkaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro maeneo ya hifadhi namna ambayo wawekezaji wanapewa vipaumbele kuliko wazawa na mwisho huwa ni migogoro isiyoisha. Wawekezaji wana viwanja vidogo vya ndege ndani ya hifadhi mfano Serengeti wanavifanyia nini kama siyo vinatumika kuhujumu uchumi wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi ambayo ipo Mtwara tulihakikishiwa kuwa itakuwa muarobaini wa mambo mengi ikiwemo matumizi ya nyumbani ili kunusuru ukataji misitu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya gesi ya majumbani na bei itakuwa chini. Kuna sehemu kama Dar es Salaam yalitandazwa mabomba ya gesi mitaani lakini hakuna lolote, mkaa tani na maelfu ya tani kila siku yanapelekwa Dar es Salaam.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa maisha na maendeleo ya Watanzania. Vision ya viwanda, Mwalimu Nyerere aliwahi kuiona na ilikuwa implemented kuanzia miaka 1967, ambapo mikoa mbalimbali ilionesha kwa vitendo kwa kuwa na viwanda na vilikuwa vikifanya kazi. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa Mikoa ambayo ilinufaika na vision hiyo kwa kuwa na viwanda zaidi ya 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunavyozungumza viwanda vilivyokuwa vimewekeza katika Mkoa wa Morogoro kwa miaka hiyo ya 1960 viliwezesha wananchi wa Mkoa wa Morogoro kupata fursa za kupata ajira. Ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupata house girl; ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupita kukuta watu wanacheza bao; ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupita kukuta Wamachinga; ilikuwa siyo rahisi kupita Mkoa wa Morogoro ukakuta watu wamekaa vijiweni, kwa sababu kulikuwa na viwanda na viwanda vile vilikuwa vikitoa ajira kwa wananchi walio wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo sasa, namwomba Mheshimiwa Waziri, nimejaribu kupitia sana katika taarifa yake hii, iko wapi mikakati ya kufufua viwanda vya Mkoa wa Morogoro vilivyokufa? Ubinafsishaji wa viwanda badala ya kuongeza efficiency, ubinafsishaji wa viwanda umekuwa ni wa kunufaisha watu wachache ambao wamechukua viwanda kama collateral kwenda kukopa katika mabenki, kunufaika wenyewe na wananchi kukosa ajira. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha, atuambie uko wapi mkakati halisi wa kuvirudisha viwanda vya Mkoa wa Morogoro? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Morogoro hivi sasa kuna viwanda, kwa mfano, Kiwanda cha Canvas ambacho kilikuwa kikinua hata pamba kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa, lakini hivi sasa wameacha kulima pamba kwa sababu kiwanda kimekufa. Kipo kiwanda cha Asante Moproco cha Mafuta; kiwanda hiki wananchi walikuwa wanalima alizeti kwa sababu walikuwa na uhakika wa sehemu ya kuuza. Hivi sasa wananchi hawalimi alizeti kwa kuwa hakuna kiwanda. Kipo kiwanda cha Komoa, kipo kiwanda cha CERAMIC, Morogoro Leather Shoe, UNNAT cha Matunda ambacho kilikuwa kikinunua matunda ya wananchi wa Mkoa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atupe mkakati wa kufufua viwanda hivi. Siyo hivyo tu, atuambie Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua wawekezaji hawa ambao kwa makusudi waliviua viwanda hivi? Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha watu hawa ambao wengine kwenye viwanda vile wameuza vipuri, hivi sasa yamebaki kuwa magodauni na wengine wanachunga mbuzi. Je, ni sahihi kwa watu hawa kutumia collateral kupata faida lakini wanaviua viwanda badala ya kunufaisha? Atuambie, Mheshimiwa Rais alipita Morogoro akasema atalishughulikia, tunataka kuona kwa vitendo kwamba hawa wamiliki wa viwanda ambao wameziweka ajira za wananchi wa Mkoa wa Morogoro mfukoni, wanachukuliwa hatua gani kama kweli mna nia ya kuleta viwanda kwa nchi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la nyumba. Wakati wa ubinafsishaji zipo nyumba ambazo zilikuwa zinamilikiwa na viwanda vile na zilikuwa ni nyumba za Serikali. Zile nyumba hivi sasa zinamilikiwa na watu ambao ndio waliobinafsishiwa viwanda, lakini hivi sasa wafanyakazi wa Serikali hawana nyumba, hawana pa kuishi. Wale watu wamepeana nyumba zile kinyemela, hawalipi pango na hawalipi kodi. Maofisa wanakosa mahali pa kuishi lakini watu waliobinafsishiwa wanang’anga’nia kuishi kwenye nyumba hizi. Hii siyo sahihi kabisa. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri amulike, aangalie ili hatua mahususi ziweze kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia biashara ya mwendokasi; mabasi ya Dar es Salaam, tuna mengi ya kujiuliza. Biashara hii imekuwa kama ni ya watu wachache. Serikali imeamua kuleta mabasi ya mwendokasi kwa lengo la kusaidia kupunguza msongamano, lakini kuna wazawa, kuna Watanzania ambao walikuwa wakifanya biashara za daladala ambao nao walikuwa na uwezo wa kupata fursa ya kuwekeza katika mwendokasi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mimba kwa watoto wa kike walio chini ya miaka 18 waliopo shuleni, lazima Serikali ikubali kwa kuweka mkakati maalum wa kuwaendeleza watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni. Kupata mimba hatukubaliani nako, si kitu kizuri, lakini sasa tuwalaani watoto wa kike?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pamoja na kuja na sheria ya kifungo cha miaka 30, lakini bado watoto wanaendelea kupata mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu kwa shule za msingi zinaonesha wanafunzi 251 wamepata mimba, takwimu hizo bado kwa wanafunzi wa shule za sekondari. Kuwaondoa shule watoto kwa kupata mimba bila kuwa na mpango wa kuwaendeleza ni sawa na kuendelea kutengeneza Taifa la mbumbumbu. Tujue watoto wanaopata mimba ni dhahiri hawajapata uelewa wa masuala ya afya ya uzazi kwa maana ya kujua uzazi wa mpango, afya ya mama na mtoto, elimu ya kulea mtoto, umuhimu wa chanjo na kadhalika. Ni wakati wa Serikali kuweka mkakati wa mpango wa kuwarudisha shule watoto wa kike wanaopata mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwiano wa walimu katika shule zilizopo mjini na vijijini haupo sawa. Ipo haja Serikali kuona jinsi ya kugawa walimu kwa uwiano ili kukidhi mahitaji ya walimu kwani shule nyingi vijijini zina upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tatizo la mkanganyiko wa vitabu, kutokana na makosa makubwa yaliyopo kwenye vitabu na bado vinaendelea kutumika kuharibu watoto wetu, ni vizuri Serikali ikachukua hatua kuvikusanya vitabu vyote na kuviondoa kwenye shule na kuja na utaratibu wa haraka wa kutengeneza vitabu vingine visivyokuwa na makosa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara hii muhimu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Nimefuatilia sana taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji lakini katika hotuba yake hakuzungumza mkakati wa kufufua viwanda vilivyokufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la Tanzania ya Viwanda lilikuwepo na Mwalimu Nyerere miaka 1967 alikuwa na vision hiyo na ali-implement wakati ule kwa kuhakikisha viwanda vingi vinaanzishwa katika mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro pekee ulikuwa na viwanda zaidi ya 40, lakini hivi sasa viwanda vingi vimekufa vikiwemo viwanda vya Canvas, Komoa, Asante Moprocco, Ceramic Tanzania, Leather Shoe, Unnats na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aje na majibu, upi mkakati wa Serikali wa kufufua viwanda vya Mkoa wa Morogoro ambavyo vilikuwa vikitoa ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro?

Mheshimiwa Naibu Spika, ubinafsishaji wa viwanda ulikuwa na lengo la kuongeza ufanisi wa uzalishaji na si kuua viwanda. Sasa kwa nini uwekezaji umetumika kuongeza tija kwa mwekezaji na kuua ajira? Wawekezaji kwa masikitiko makubwa wametumia viwanda hivi kama Collateral kuchukua mikopo mikubwa katika mabenki badala ya kuendeleza kwenye biashara za malori, mabasi na kuua viwanda hii sio sawa. Tunataka kuona Serikali inachukua hatua mahsusi kwa wawekezaji hao kwa makusudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba za Serikali zilizonunuliwa na wawekezaji hata baada ya kuua viwanda kwa nini wawekezaji hawa wasirudishe nyumba hizo zikatumika kwa wafanyakazi wa Serikali? Hawalipi kodi hawalipi pango, huku wameua viwanda; ni kwa nini Serikali isichukue nyumba hizi zikatumika kwa maofisa wa Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya Mwendo Kasi Jiji la Dar es Salaam, ni kama imekuwa monopolized na watu wachache. Kabla ya mwendo kasi wapo wamiliki wa mabasi ya daladala ambao walikuwa wakifanya biashara tena kwa mkopo na wengine wakijifunga mkanda kuuza nyumba, mali na kuingia kwenye biashara ya daladala. Serikali imekuja na mpango wa mabasi yaendayo kasi; kwa nini wasiwape fursa wafanyabiashara wa daladala nao kama wana uwezo wawekeze katika mabasi hayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa mabasi ya mwendo kasi ambayo yalikuwa yanatoa huduma kwenye njia pekee sasa hivi yanafanya biashara kwenye njia ambazo si maalum; wa mfano Mbezi Louis, Muhimbili; hali hii inawaweka pembezoni wafanyabiashara wanyonge wa daladala ambao nao wangeweza kupata fursa hizo kama wazawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya viwanda sasa itekelezwe kwa vitendo ambapo tunatarajia kuona Serikali inafanya kazi kwa pamoja na Wizara nyingine mtambuka kama vile Wizara ya Kilimo na Mifugo, Nishati na Madini pamoja naWizara ya Maji na Umwagiliaji. Hakuna viwanda bila uhakika wa umeme na malighafi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa maandishi Wizara hii muhimu kwa mustakabali wa uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu importation ya mbegu za kilimo, kwa nini tunaendelea kuruhusu makampuni makubwa kama Panner SIDCO ambayo hurb zao zipo nje ziendelee kushika kasi katika soko la mbegu? Serikali lazima ifikirie kuwezesha makampuni ya ndani na wakulima wetu kupitia Vyuo vya Utafiti kama Ilonga, ASA, kuwasadia wakulima kuzalisha mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhakika wa chakula unaenda sambamba na uhakika wa mbegu. Lazima Taifa lijitafakari na kutenga bajeti ya kudumu kuwezesha makampuni ya ndani kuyajengea uwezo wa kutengeneza mbegu hasa zinazoendana na hali ya hewa ya mazingira tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako malalamiko ya wananchi juu ya mfumo wa NFRA na hii inatokana na urasimu wa Viongozi wa Vyama vya Ushirika ambao wanatumia mfumo huu kuwapa fursa wafanyabiashara wa mazao kuuza mazao badala ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Maafisa Kilimo katika ngazi za Kata watumike kusaidia kuwatambua wakulima na kuwawezesha kupata fursa badala ya sasa hivi ilivyo kwa mfumo huu kwa nje unaonekana kuwasaidia wakulima, lakini wengine wanaumizwa na urasimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbegu feki masokoni; mamlaka zinazohusika kwa nini zinashindwa kufanya kazi? Wakulima wananunua mbegu madukani hawana utalaam wa mbegu, lakini hakuna hatua za dhati za kuwakamata, kukagua maduka ya pembejeo za kilimo
na mifugo ili kubaini mbegu feki na mbegu zilizoisha muda wake wa matumizi. Mfano, viuatilifu holela vinavyoingia madukani kwa njia ya panya, mfano Mkoani Mbeya na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Morogoro katika Wilaya ya Kilosa, Mvomero, Kilombero na Wilaya ya Morogoro Vijijini. Serikali, Wizara ya Ardhi isaidie kufuta mashamba pori yasiyoendelezwa kwa miaka mingi. Mfano, Mvomero na Kilosa, Serikali ichukue hatua kubadilisha matumizi ya mashamba hayo. Mfano, NAFCO Kilosa yagawiwe kwa wakulima na wafugaji ambao migogoro yao inatokana na uhaba wa maeneo ya kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlundikano wa kodi au ushuru wa mazao kwa wakulima mfano, soko la mazao Kibaigwa. Ni kilio cha wakulima wengi wa Mikoa ya jirani na Morogoro; Kiteto na Dodoma ambao wanashindwa kupeleka mazao yao kutokana na ushuru wa mazao wa kila kituo cha kizuizi cha ushuru wa mazao. Ushuru huu ukiondolewa, utawasaidia wakulima kuacha kuuza mazao yakiwa mashambani na badala yake ushuru huu watozwe wafanyabiashara. Vinginevyo, wakulima wataendelea kuuza mazao yakiwa shambani na kwa lumbesa.

The Access to Information Bill, 2016

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Na mimi nichukue fursa hii kuchangia muswada uliopo mbele yetu. Katika Bunge lililopita Mheshimiwa Waziri alikuja na mikakati yake akisema atakuja na muswada hapa ambao utakuwa ni mwarobaini; muswada wa habari. lakini matokeo yake sasa imekuwa ni muswada wa taarifa, sijui imekuwaje ghafla ukabadilisha gia hewani. Lakini tunachosema tu ni kwamba huu ni mkakati si muswada kama vile tunavyoufikiria; huu ni mkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa muswada huu, kwa hali halisi na mambo yanavyoendelea hivi sasa ni kwamba unakwenda kupewa rungu. Tumeshuhudia mengi ikiwemo wewe mwenyewe binafsi kuvifungia vyombo vingi vya habari. Na muswada huu unakwenda kufunga midomo; muswada huu unakwenda kukupa mamlaka ya kufanya utakavyoweza kufanya kwasababu kuna baadhi ya vipengele ambavyo vinaonesha kwamba endapo mtu hataweza kupewa taarifa, Waziri ndiye msemaji mkuu na ndiye mwenye mamlaka ya mwisho. Muswada huu unakwenda kukupa wewe mamlaka hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, endapo mtu atakosa taarifa sahihi atakwenda kukumbana na Waziri ambaye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho. Na kwa mamlaka hayo sasa haitoi fursa kwasababu Waziri anasimami Wizara. Inawezekana kabisa taarifa zinavyotafutwa zipo chini ya Wizara, sasa itakuwaje Waziri aweze kutetea hili? Tunaomba, kwa mujibu wa sheria kwasababu mahakama ndio yenye kuingilia kati, yenye mamlaka; suala hili lingekwenda huko badala ya kumuachia Waziri kuwa ndio msemaji mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikianza kifungu kile cha 19 ambacho kinamtaka Waziri kuwa wa mwisho katika…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 107A ambayo inaitaka Mahakama kuwa ndicho chombo pekee cha kutoa haki inayogombaniwa na si Waziri sasa. Endapo Waziri atapewa mamlaka haya, endapo mtu atakuwa amenyimwa taarifa mahali fulani pa kwenda kulalamikia isiwe ni Waziri; itoe fursa kwamba mtu aweze kwenda mahakamani na mahakama itoe haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 4 kina mgongano juu ya ni nani anapaswa kupewa taarifa. Kifungu hiki kinasema kwamba mpewa taarifa awe ni raia na si mtu. Tafsiri yake ni nini hapa? Wakati Mheshimiwa Waziri anaeleza alisema kwamba mlijaribu ku-relay nchi nyingine kwa mfano South Africa, Malaysia, Uingereza na kwingineko ambapo mnasema kwamba mtu yeyote anapaswa kupewa taarifa. Kwa hizo nchi za wenzetu kwa maana ya Uingereza, Malaysia na South Africa sheria zao zinasema hivyo. Lakini hapa mmekuja na hoja kwamba mtu anayepaswa kupewa taarifa ni raia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ni raia sisi wenyewe tunaji-contradict kwasababu gani? Yapo matukio kadhaa, kwa mfano issue ya RADAR, wakati huo sisi Tanzania tuliomba information kutoka Uingereza, na imetusaidia kupata taarifa kwa wenzetu; zikatuwezesha kupata change ya dola milioni 12. Sasa kama sisi tutasema mtu anaetaka kupata taarifa ni lazima awe raia kwa maana hiyo tunajifunga. Kama kuna watanzania ambao ni wawekezaji wapo hapa na wakafanya madudu; wakahitaji kupata taarifa hapa hatuwezi kuwapa taarifa kwasababu sheria hii itakuwa inawabana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahivyo, tunacho sema ni kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18(d) kwamba:-
“Kila mtu ana haki ya kupata taarifa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi tunasema kila raia kwa mujibu wa muswada huu. Kwahivyo, kuweka neno raia ni kwamba ni kichaka ambacho tunakwenda kujificha. Tumeona issue mbalimbali mfano sakata la ESCROW tuliweza kupata taarifa kwa wenzetu kutoka Malaysia kwasababu gani? Wao Katiba yao inasema kupata taarifa ni mtu yeyote na si raia. Sasa tutakapokuja na kipengele kwamba tunasema kwamba ni raia sasa tutakuwa tunajifunga kwamba baadhi ya taarifa hatuwezi kuzipata lakini pia hii ni kuleta ubaguzi; hamuwezi mkaja na muswada huu mnatuambia nchi zingine zimefanikiwa kwa mfano Malaysia na South Africa ambazo sheria yao ni tofauti na hii; haizungumzii raia inasema mtu kupata taarifa ni haki ya kila mtu. Hata Katiba yetu inasema hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kifungu cha kwanza kinasema sheria ianze kutumika mara tu Waziri anapoitangaza. iko miswada mingi ambayo imepita, zipo sheria nyingi ambazo zimepitishwa na Bunge hili lakini bado hazijaanza kufanyiwa kazi. Lakini kwenye hili kwasababu ni mkakati ikishapitishwa tu tayari ianze kufanya kazi; lakini kwanini isingepewa muda kanuni zikatengenezwa? Sisi tunasema ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge lazima tuungane katika hili kwasababu muswada huu unakwenda kunyamzisha vyombo vya habari; ni lazima tufikirie upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii vyombo vya habari vinafungiwa, mtu akiamka tu asubuhi anavyoamua anafungia vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Tanzania kwa level tuliyofikia sasa maendeleo tuliyo nayo tunajivunia ni vyombo vya habari. Ni nani ambae sasa hivi atakubali kuwekeza kwenye vyombo vya habari kama tunakwenda kuwa na sheria ya namna hii? Radio moja ikifungiwa ina waajiriwa permanent labda 20, hujaweka wale ambao wanakwenda kujifunza, hujaweka watu wale ambao wanakuwa wanafanya mawasiliano ya moja kwa moja; kwa maana kuchangia hoja, hujaangalia familia za hao watu. Tunaathiri zaidi ya watu 100 kufungia redio moja; wafanyakazi tu peke yake achana na Watanzania. Sasa leo hii tunakuja na sheria hii ambayo mtu akifanya kosa tu dogo lazima afungiwe. Kwahiyo, tunasema, kwa wakati tulionao na hali tulizonazo tunaona huu ni mkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Lakini vilevile kifungu cha sita tunapendekeza kiondolewe kabisa, kwanini? Mnasema kwamba mtu ambaye ata-distort information yoyote anapaswa kuhukumiwa kama zilivyo Sheria za Usalama wa Taifa. Ni kwanini tujifiche nyuma ya hizi sheria za usalama wa taifa wakati tunayo sheria ambayo inazuia hali hiyo ya mtu kama akisema uongo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunasema kwamba mtu atafungwa kifungo cha miaka 15 mpaka 20. Kwanini mtu kama ametoa information tu akakutane na kifungu kikubwa namna hii? na hakuna sehemu ambayo inazungumzia kwamba endapo hakuna fine, moja kwa moja kwamba mtu ni lazima akakumbane na kifungo cha ndani kwa maana miaka 15 mpaka 20; kwanini hakuna fine katika hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengine kwa mfano informers wanakupa habari nzuri ambazo zinaweza zikasaidia na zikajenga lakini kama siye msemaji atakumbana na kifungo hiki. Sisi tunasema kifungu hiki kiondolewe kwasababu kitakwenda kutunyima kupata taarifa; so long mtu ambaye ana information ambazo ni reliable zinaweza zikasaidia nchi, zikasaidia taifa; kwa mfano issues za njaa na mafuriko; tukasubiri afisa ambaye ameteuliwa na Serikali aende akatoe taarifa hizi. Hii ni kwenda kunyima vyombo vya habari kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwenye uchaguzi, tutakwenda kwenye uchaguzi mwaka 2020, kwa maana hiyo taarifa za awali za uchaguzi mwandishi hataruhusiwa kuzitoa ni mpaka asubiri Afisa Habari wa Wilaya? Tunachosema kwamba kuna mambo ya msingi ambayo kwa hofu tu ya kukumbana na hili ni lazima tuyaangalie, na tunapendekeza kabisa kifungu hiki cha sita kiondolewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mmezungumzia kuhusu utoaji wa taarifa kwa maana ya mtu atakapoomba taarifa apewe siku 30, hivi hiyo itakuwa ni taarifa au itakuwa ni kitu gani, kwa sababu uende uombe taarifa kwenye taasisi, ukae siku 30 usubirie kupata jibu kwamba hiyo taarifa ipo au haipo, ni kwa nini msingeweka siku tatu au siku moja kama ilivyo TAMISEMI. Siku 30 halafu unajibiwa kwamba taarifa unayoihitaji haipo. Tunachotaka kumuambia Mheshimiwa Waziri, Muswada huu utakwenda kunyamazisha vyombo vya habari, utakwenda kuumiza wamiliki wa vyombo vya habari, utakwenda kuvunja morali kwa watu ambao wana interest ya kuwekeza kwenye tasnia ya habari, tunaomba kama kuna uwezekano wowote Muswada huu uondolewe tusubiri tupate maoni upya. Wadau mbalimbali wa habari walishiriki lakini maoni yao hayamo humu, hayakuzingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunasema, mtaupitisha kwa sababu ya wingi, lakini tunachosema kwamba tutafika kwenye hali ambayo, kama wenzetu Uganda ilivyo Rais anaamka asubuhi anafunga magazeti, anafunga redio. Sasa kwa sasa hivi graph ya vyombo vya habari ambapo kwa Afrika, Uganda ilikuwa inashika nafasi kama ya sita, sasa hivi inakaribia kuwa mwishoni kwa sababu ya vyombo vya habari kufungwa midomo na Serikali. Tunaomba ili Muswada huu uwe na maana, ni lazima Serikali ikubali kwamba kuna baadhi ya vitu ambavyo ni lazima vifanyiwe marekebisho makubwa, vinginevyo uwekwe pembeni tusubiri mpaka muda utakapofikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Tanzania ya leo hii, kwa teknolojia ilivyokua sasa hivi, mtu akipata taarifa mtu ataogopa, watu wataingiwa woga, tutakosa taarifa muhimu. Mbona tunashuhudia kwenye baadhi ya vyombo ambavyo vinakuwa biased, matukio makubwa wanaacha kwa sababu ya woga. Kwa hiyo, tunakwenda kutengeneza sheria ambayo itaendelea kudidimiza vyombo vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokiomba ni kwamba Serikali iko haja ya kuangalia upya jambo hili. Yapo mambo mengi ambayo tungeweza tukayafanyia kazi kwanza kabla ya kuja na muswada huu, zipo haki nyingi za watu za kupata taarifa, mngeangalia badala ya kujificha…
MWENYEKITI: Ahsante sana.

The Media Services Bill, 2016

MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikiliza sana Waziri wakati anawasilisha Muswada huu. Waziri amesema anaenda kuandika historia, nikubaliane nae anaenda kuandika historia ya kutengeneza Muswada ambao wadau hawakushirikishwa. Tumewahi kuona wapi? Tumejaribu kujifunza na kuangalia katika Mataifa mengine yenye sheria kama hii; wadau wanapewa nafasi, wadau wanapewa kipaumbele kwa maana ya kutoa mawazo yao na michango yao, lakini kwa Muswada huu tunakwenda kuupeleka kwa jinsi ambavyo Serikali imeamua, watekelezaji wa sheria hii wako kando. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iingie tu kwenye rekodi na ieleweke hivyo kwamba wadau waliomba waongezewe muda, ni kwa nini wadau wanataka muda? Muswada huu ulisomwa mara ya kwanza tarehe 16/9/2016 wadau wakaomba watoe mawazo yao, wakafika kwenye Kamati, wakaomba waongezewe muda. Kwa nini wanataka muda? Kwa sababu tasnia hii ya habari ina wadau wengi wakiwemo waandishi wa habari ambao ndiyo watekelezaji wa Sheria hii. Tunazungumza hivi sasa tukiwa na redio zaidi ya 200 ziko vijijini, tunahitaji kupata michango yao badala ya kupata michango ya waandishi walioko mjini Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wakaomba waongezewe muda, Muswada huu uje Bungeni hapa katika Bunge lijalo lakini waliongezewa siku kumi. Hii imekuwa novel ya kusoma kwa siku kumi? Hii ni Sheria ambayo kila mmoja alipaswa aje na mawazo. Utaweza kuona katika Muswada huu Waziri anatuambia kwamba una maslahi mapana ya waandishi. Yako wapi maslahi ya waandishi hapa? Tumeshuhudia waandishi wa habari wakipigwa, wakiuawa, wakimwagiwa tindikali, sheria hii inasema wapi kuhusu kuwalinda hawa waandishi wa habari wakiwa kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo, Waziri anasema kwamba anakwenda kutengeneza historia. Historia gani ambayo hakuna michango na mawazo ya hawa waandishi? Historia gani ambayo hakuna popote palipozungumza hata kima cha chini cha mwandishi wa habari alipwe nini, iko wapi? Tuseme basi Muswada huu unatetea kwa maana ya kuwa na sehemu ambayo inaonesha mwandishi wa habari alipwe kiasi gani, awe na mazingira gani ya kutekeleza kazi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu ya wadau ni nini? Hofu ya wadau Mheshimiwa Waziri ameandika historia ya peke yake. Katika kipindi cha mwaka mmoja ya Uwaziri wake, amekwenda kufunga magazeti, amefunga redio, hana mikono misafi na ndiyo maana waandishi wana hofu, wanataka wahakikishe kwamba Muswada huu wanausoma vizuri, wanatoka na majibu ambayo watajua ni nini hatma ya vyombo ambavyo ndivyo wanavyovitumikia na ndivyo vinavyowapa kula yao asubuhi na jioni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu nyingine ya wadau katika hili, ni kwa nini Serikali haikuona kwamba kuna haja ya kuwapa nafasi. Nimeshiriki kwenye hii Kamati, baadhi ya michango ya wadau ambayo niliiona ni kutoka kwa TWAWEZA na kutoka kwa TLS, halafu tunasema hii ni michango ya wadau. TLS anafahamu, TWAWEZA wanafahamu shida, adha ya waandishi wa habari ambao wanatembea kwa miguu barabarani wakitafuta habari? TWAWEZA wanayaelewa haya? Ungeniambia UTPC wanaelewa, ungeniambia TAMWA wanaelewa, ungeniambia MCT wanaelewa, ningeelewa, lakini TWAWEZA?
Mheshimiwa Mwenyekiti, TWAWEZA wanafahamu a, b, c za uandishi wa habari? TWAWEZA wanajua shida waandishi wanayoipata? Kwa hiyo, tunakuja na mawazo kwamba TWAWEZA wametoa na TLS wametoa. Hii tunaifananaisha na kama, wao ni wadau walioalikwa tu kutoa mawazo yao lakini wadau halisi ambao walipaswa kuingia hapa hawakushirikishwa. Ni kama tuseme mtu unaandaa harusi waalikwa wanashiriki lakini bwana harusi na bibi harusi hawamo halafu unaita ni harusi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu unakwenda kumpa mamlaka Waziri ya kuamua ni nini ambacho waandishi wa habari wanataka waripoti, kwa nini? Kuna vipengele ambavyo vinasema kwamba Waziri ndiyo mwenye mamlaka ya kuangalia ni kitu gani kinaripotiwa kwa muktadha, kwa maslahi ya usalama wa Taifa, usalama wa Taifa ambao una sheria zake, ambazo zinafuatwa lakini Waziri ndiyo anasema kwamba yeye ndiye atakayeenda kupewa mamlaka ya kuhakikisha kwamba kila kinachoripotiwa yeye ana mamlaka ya kujua ni kitu gani ambacho kinaenda kuandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tumeona kwenye hotuba yake Mwenyekiti wa Kamati anasema mazingira mazuri yanayoenda kutengenezwa kwa waandishi wa habari ni pamoja na kuweka dressing code. Leo hii Taifa hili ambalo tunaona umuhimu wa vyombo vya habari tunahitaji kwenda kuwa na dressing code? Waandishi wa habari wamekuwa wakifanya kazi za utafiti, wanahitaji kuvaa nguo kufahamika wanafanya nini? Tunafikiri ni vitu ambavyo Serikali imejenga mikakati kuhakikisha wanaenda kudhibiti, kuhakikisha waandishi wa habari hawafanyi kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Bima ya Afya kwa waandishi wa habari tumeliona na sisi tunasema kwamba hilo halitoshi pekee kusema kwamba ndiyo maslahi ya waandishi wa habari. Tumeweza kuweka misingi gani ambayo itawabana hawa wamiliki wa vyombo vya habari kuwasaidia hawa waandishi wa habari kwa maana ya kuwalipa mishahara ambayo inaendana na kazi wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kuna kipengele kingine kwamba Waziri ndiyo atakwenda kutengeneza kanuni ambazo zitakwenda kusaidia baada ya Sheria hii kutungwa. Tuliomba kwamba iwekwe wazi hapa tujue ni regulation zipi ambazo zinawekwa kwa sababu ya matamko mbalimbali ya Waziri ambayo amesikika akiyazungumza kwenye vyombo vya habari kwamba anataka uandishi wa habari lazima uanze na level ya degree.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Taifa gani ambalo lina sheria hizi ambalo limeweka kwamba kigezo cha mwandishi wa habari lazima awe na degree. Tumeona Mataifa mengi ambayo hata uchumi wake unaimarika, kuna level mbalimbali, kuna watu wa certificate, wapo watu wa diploma, wapo watu wa degree lakini wanatambulika kutokana na michango yao wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani tukizungumzia suala la kazi za udaktari, kuna madaktari wa AMO, kuna madaktari wa MD, kuna madaktari wenye masters lakini wote wanafanya kazi, lakini council ndiyo yenye mamlaka ya kuhakikisha kwamba wanatengenezaje madaraja ya hawa waandishi wa habari, lakini kuja na vigezo vya degree kama mbinu ya kuwagawa waandishi wa habari, leo hii wazee ambao wamefanya kazi iliyotukuka hasa ya kupigania uhuru wa Taifa hili basi wasionekane kama nao ni waandishi wa habari kisa hawana degree ya uandishi wa habari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tunataka Sheria iseme wazi kwamba ni kanuni zipi ambazo zinakwenda kutengenezwa kwa ajili ya kusimamia sheria hii. Kanuni ziwe wazi, zieleze kwamba mwandishi wa habari atakwenda kuwa ni mtu wa namna gani na sisi tunasema kwamba mwandishi wa habari awe ni mtu yeyote ambaye amemaliza form four, mtu yeyote ambaye amesoma certificate, advanced certificate ya uandishi wa habari, mtu ambaye hata ana diploma atambulike, hata ana degree atambulike kwa sababu vyuo hivi vilisajiliwa na NACTE, kwa maana hiyo Serikali inatambua ni vyuo ambavyo vinafanya kazi ya kuwatengeneza waandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuja na mkakati wa kwamba sasa tunakwenda kukomesha kwa kuleta suala la degree katika uandishi wa habari, hii itafanya waandishi wengi wenye passion ya kufanya kazi hii kuhakikisha wanatoka kwenye hii na sijui; tunasema tuna mpango wa kuongeza ajira lakini tunaenda…
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's