Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Agnes Mathew Marwa

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama katika Bunge hili Tukufu siku ya leo. Kwa umuhimu zaidi nawashukuru sana wapiga kura wangu, wanawake wa Mkoa wa Mara, walionipigia kura nyingi sana za kishindo hadi leo hii kuwepo hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru kwa upekee mama yangu mzazi na baba yangu, pamoja na Mashirika ya Kikristo yaliyonifanyia maombi, pamoja na Mashekhe na wanamaombi wote na watu wote wa Mkoa wa Mara waliokuwa wanafurahia leo hii niwe Mbunge. Nawashukuru sana, nawaahidi sitawaangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kunukuu kidogo Hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa sababu sikupata nafasi ya kuongea siku ile. Kwa ruhusa yako naomba ninukuu. Hotuba ya Mheshimiwa Rais iliwakumbusha watumishi wengi wa umma ambao wengi walijisahau wajibu wao, hivyo aliwakumbusha watumishi wengi kuwajibika kwa umma kwa taaluma na weledi kwa kuzingatia usawa bila upendeleo kwa watu wote, bila kujali itikadi ya vyama na dini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, nampongeza Mheshimiwa Rais Magufuli kwa hotuba yake ambayo imehimiza kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa umma (integrity). Hivyo basi, kwa hotuba hiyo nzuri ya Mheshimiwa Rais tunatarajia kwamba kila mtumishi mahali pake pa kazi atimize wajibu wake ipasavyo na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza ndoto na matarajio ya Watanzania walio wengi hasa wa kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza moja kwa moja kwa kuongelea au kuchangia kwa suala la ujasiriamali. Wajasiriamali au ujasiriamali ni suala ambalo linatakiwa liangaliwe kwa macho ya ziada, kwa maana katika Mpango wa Taifa au Mpango wa Maendeleo, wajasiriamali ndio wanatoa mchango mkubwa sana kwa Taifa hili; na haswa naanzia na akina mama wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wa Mkoa wa Mara ambao wanafanya biashara ndogo ndogo, ikiwemo wafanyabishara wa dagaa, ikiwemo wale wanaouza mboga mboga na wengine wa masokoni wananyanyasika sana kutokana na kutozwa ushuru usiokuwa na sababu. Kwa hiyo, naomba tuangalie sana hawa wajasiriamali kwa macho ya huruma, kwa maana na wao wanatoa mchango mkubwa sana katika Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niende kwenye suala la maji. Suala la maji limekuwa ni ni kilio cha kudumu katika Taifa hili la Tanzania. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangazie sana macho yake na itoe kipaumbele katika suala la maji, kwa maana suala la maji limesababisha matatizo na majanga makubwa hasa kwa wanawake wetu wa Mkoa wa Mara, kwa kuvuruga au kuachanishwa kwa ndoa zao kutokana na umbali mrefu wanakwenda kutafuta maji. Vilevile limekuwa likiwasababishia ulemavu wa migongo, limekuwa pia likiwaletea shida sana katika uzazi. Kwa hiyo, kwa namna ya kipekee sana liangaliwe suala la maji na hasa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia naungana na Waheshimiwa walioongea jana, Mheshimiwa Zitto Kabwe pamoja na Mheshimiwa Lugola, kuhusiana na suala la reli. Ni kweli katika mazingira ya kawaida, utaratibu ambao unatakiwa katika kuunganishwa kwa reli ili nchi ya jirani au ndugu zetu wa jirani wapate unafuu, ni kitu ambacho siyo kizuri sana, kwa sababu kwanza itatupotezea sisi Pato la Taifa na wao kwa ujanja wao, wanachotaka kukifanya ni kwamba wataunganisha kule juu kwa juu nchi nyingine ili malipo haya yasije Tanzania. Kwa hiyo, hilo suala liangaliwe au lipewe kipaumbele, liwe kama lilivyoongelewa na Mheshimiwa Zitto au Mheshimiwa Lugola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie sana suala la polisi kuhusiana na makazi au vituo vya kazi. Vituo vya kazi na masuala ya makazi ya polisi wetu imekuwa ni shida sana. Hivyo, Serikali ingechukua taratibu za ziada ili iingie mkataba na Shirika la Nyumba la Taifa ili kuwajengea nyumba za kudumu hata baadaye watakapomaliza kuzilipa ziwe za kwao hata pale wanapokuwa hawapo kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba ndugu zangu wa upinzani, tumtie moyo Rais wetu Mheshimiwa Magufuli. Ameanza vizuri. Siyo kila kitu tunaongea maneno machafu, maneno ya kashfa, maneno ya dharau, kiasi kwamba hata wewe ukiombwa kitu huwezi ukakubali kama mtu ameongea maneno ya dharau. Hata Mwenyezi Mungu anatoa pale unapomsifia; ndiyo maana unasema; “Baba yetu uliye Mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimie, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni,” ukimaliza unampiga kibao Mungu, halafu ndiyo unamwomba, “utupe riziki yetu ya kila siku.” Siyo ninyi kila siku mnatoa matusi tu. Kesho msipofanyiwa maendeleo mnalalamika.
Ndugu zangu Wapinzani nawaomba sana; mmefanyiwa mambo mengi sana kwenye Majimbo yenu kuliko hata sisi wa CCM. Mfano ni Arusha au Mkoa wa Kilimanjaro, uko wazi kabisa, mmefanyiwa mambo mengi mazuri, hata barabara mlizonazo ni kama barabara za Kimataifa, mikoani kwetu, hatuna. Mnatakiwa muwe na Shukurani, lakini pia mnatakiwa mkubali kwamba aliyeshinda, kashinda, ninyi mmeshindwa. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Muda wako umekwisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mungu kwa kunijalia kuchangia siku ya leo katika Wizara ya Afya. Namshukuru kwa nafasi ya kipekee Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya yeye na Serikali nzima, kwa kuonesha kwamba anaweza na kwa kuonesha kwamba sasa Tanzania mpya yenye matumaini inawezekana.
Meshimiwa Mwenyekiti, Mkoani kwangu Mara kuna matatizo makubwa sana ya vituo vya afya, ukizingatia kwamba Mkoa wa Mara umepakana na mipaka mingi ambayo wenzetu wa nchi za jirani pia wanategemea huduma za afya kutokana na Mkoa wetu wa Mara. Kwa mfano, Wilaya ya Tarime kwa sasa imegawanyika katika sehemu mbili; tuna Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya. Hospitali tuliyonayo ni moja tu, ambayo haikidhi mahitaji kutokana na wingi wa watu waliopo Wilayani hapo Tarime. Kutokana na hali halisi ya matatizo hayo ya hospitali, Mgodi wa Acacia uliopo Wilayani Tarime, ambao uko chini ya North Mara wameamua kutujengea Kituo cha Afya katika Kijiji cha Nyamwaga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Tarime, kaka yangu Mheshimiwa Luoga, alikaa nao chini wakafanya maongezi, pamoja na Halmashauri ya Tarime. Wakaongea wakakubaliana kwamba badala ya kutengeneza au kujenga Kituo cha Afya, wakakubaliana kwa majengo yale yale na kwa gharama zile zile, tuiombe Serikali ikubali majengo yale baadaye yawe Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa dada yangu Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla bahati nzuri mpo hapa, nawaomba watukubalie Wilaya ya Tarime, yale majengo yatakayojengwa na Kampuni ya Acacia yawe ni Hospitali ya Wilaya kwa sababu wamejitolea wao wenyewe. Kwa hiyo, pia yanakuwa yametusaidia sisi kupunguza gharama ambazo tungezipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya kipekee zaidi, kama mnakumbuka, naamini hata Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliopita wameiongelea sana Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kwangwa. Hospitali ya Kwangwa ilikuwepo hata kabla hatujazaliwa, tunasikia historia yake. Kama mnavyojua, Mkoa wa Mara kuna matatizo mengi sana, ukizingatia kule kwetu kulikuwa na mfumo dume ambao hadi sasa haujakwisha, kwa hiyo, kuna matukio mengi sana ambayo yanategemeana na Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma Hospitali ya Kwangwa, wanawake, watoto na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kwa ujumla wanapata shida sana. Tangu mwaka 2012, mkoa ulikuwa unaomba shilingi bilioni mbili na point, lakini hizo fedha zilikuwa hazifiki kama zilivyokuwa zinaombwa. Toka kipindi cha mwaka 2012, mwisho imekuwa 2013; na mwaka 2014, Serikali imejitahidi kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mara, wamejenga hospitali, imefikia ilipofikia, lakini mpaka sasa imekuwa kitendawili; na fedha ambayo imeshatoka ilikuwa ni sh. 3,334,967,000/= na fedha nyingine za kipindi hicho bado hazijatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu zaidi, wananchi wa Mkoa wa Mara, kwa kuiona Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina umuhimu, pamoja na kuwa baadhi ya Majimbo wamewachagua Wabunge wa Upinzani, lakini Rais wetu aliongoza kwa kura za kishindo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Rais aiangalie sasa hospitali ya Mkoa wa Mara ili sasa ifikie mwisho kwa sababu ni hospitali ambayo inaweza kutoa msaada mkubwa sana, lakini pia ikapunguza matatizo ya wananchi wa Mkoa wa Mara kutoka Mkoa wa Mara kwenda Mkoa wa Mwanza, wakati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza pia inazidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, wananchi wa Mkoa wa Mara wengi wao akinamama ndiyo wanaotunza familia zao na akinamama hao hawana vipato vya kutosha; wanakosa hata nauli ya kuwatoa kutoka Mkoa wa Mara kwenda Mwanza. Kwa nini hili suala Serikali isiliangalie kwa nafasi ya kipekee zaidi ili hospitali hiyo itengewe sasa kiwango cha kutosha ili kuisaidia japo ianze kufanya kazi, hata kama majengo mengine yatakuwa bado, basi yatamaliziwa baadaye, lakini ianze kazi, iitwe Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy, baada ya Bunge, kama inawezekana twende wote Wilayani Tarime, aende akaangalie yale majengo ambayo Acacia imeshakubali kujenga ili muipe hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kwa nafasi ya kipekee sana, kuna wanawake wenzetu ambao ni ma-nurse mishahara yao ni midogo sana, haitoshi. Mwaangalie na mwaongezee mishahara. Pia Wizara ya Afya kwa ujumla muiangalie bajeti yake iongezwe kwani bajeti iliyopo ni ndogo sana, haitoshi kukidhi mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi nyingine tena ya ziada, nasema MSD ni jipu kwa sababu, ni kweli kuna baadhi ya maeneo wanakosa pesa ya kuwalipa, lakini kwa mfano Wilayani Serengeti wametenga bajeti ya kuwalipa lakini wao madawa ndiyo hawana. Kwa hiyo, naomba kama inawezekana, urudishwe utaratibu wa zamani, twende tukanunue madawa au hospitali ziruhusiwe kununua madawa kwenye maduka makubwa ya wengine, ambapo madawa yanapatikana, kuliko wananchi wetu wanakufa wakati madawa hakuna MSD. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusiana na Bima ya Afya, wananchi wangu wa Mkoa wa Mara wanapata shida sana na wamekuwa mstari wa mbele kujiunga na Bima ya Afya. Katika mazingira ya kawaida, unapojiandikisha, kwa mfano umejiandikishia hapa hapa Bungeni, ukienda kituo kingine huwezi kutibiwa. Kwa hiyo, wananchi wangu wa Mkoa wa Mara wanapata shida. Mwanamke akijiandikishia Nyamongo mgodini au akijiandikishia Mtaa wa Mkendo, hawezi kwenda kutibiwa Mtaa wa Ilingo, kwa sababu Bima yake inaishia kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru sana na nimpongeze sana Mheshimiwa Nape Nnauye kwa jinsi alivyoanza vizuri katika Wizara yake, anaonesha ni jinsi gani anavyopenda michezo na jinsi gani anavyoiweza Wizara hii kwa sababu anaonekana kabisa kwamba anaitendea haki, Mheshimiwa kaka Nape tunakutia moyo, watu wasikuvunje moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee sana naomba niongelee kuhusu suala la Miss Tanzania. Miss Tanzania ni kati ya sanaa inayoitangaza nchi yetu, ni kweli kwamba kulikuwa kuna madoa ambayo wanapaswa kurekebisha, wanatakiwa wayarekebishe, lakini Mheshimiwa Waziri unatakiwa ukae nao, wewe na Wizara yako kuweka sawa ili sanaa hii isipotee, waendelee kuonesha mashindano ya Miss Tanzania kwa sababu ni kati ya mashindano yanayoitangaza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za wasanii ni kazi ambazo zinapaswa kutetewa sana na Waheshimiwa Wabunge na nchi kwa ujumla. Nchi za wenzetu sanaa ndiyo inayoleta uchumi wa nchi, kwa mfano Nigeria na nchi nyingine, sanaa ni kitu cha muhimu sana.
Kwa hiyo, tunatakiwa tuangalie wasanii kwa macho mawili au kwa macho ya mbele zaidi ili tuwape moyo wasanii wetu. Tuangalie kazi zao, tuangalie jinsi ya kutengeneza utaratibu ili jasho lao na kazi zao zionekane, wasiwe wanafanya kazi halafu watu wanatoka tu huko pembeni, wanapata pesa kutokana na jasho la wasanii. Namuomba sana Mheshimiwa Rais awaangalie wasanii hawa kwa macho ya huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wasanii wa Tanzania wako chini sana, wanadharaulika sana ni kwa sababu hawana mtetezi. Mheshimiwa Waziri uliangalie sana hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee zaidi narudi kwenye suala la kuonesha matangazo ya Bunge live. Kuhusiana na suala la kuonesha matangazo ya Bunge live hii ilipelekea Wabunge tukawa (Wabunge waliopita) maana nisiseme tukawa sikuwepo kipindi hicho, mimi pia nilikuwa naagalia televisheni. Wabunge walikuwa wanakaa tu hapa kwenye tv wakiuza sura hapo! Hawaendi kufanya kazi majimboni mwao! Kwa hiyo, ni suala ambalo wananchi wanatakiwa waelewe, utaratibu huu umefanyika ili kuwarudisha Wabunge waende kufanya kazi majimboni mwao! Siyo wanang‟ang‟ania kuonekana kwenye tv! Wanataka waonekane ili iweje? Mkitaka muonekane nendeni mfanye kazi majimboni kwenu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu mbaya sana, Wabunge tunawadanganya wananchi kwa sababu wananchi hawajui. Sasa hivi mnaonekana majimboni kwani uwongo? Mnakwenda majimboni sasa hivi na mnatakiwa muende mkafanyekazi majimboni! Siyo mnadanganya wananchi waungane na ninyi wawa-support eti ooh, Serikali ya CCM, Serikali ya CCM haitaki muone maovu! Maovu mbona ninyi ni waovu kuliko mtu yeyote!
Mheshimiwa Naibu Spika, natamani hata kulia! Mnatutia aibu! Najisikia uchungu sana! Mnadanganya wananchi….
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana ndugu zangu wananchi waliotuchagua waelewe kwamba huu utaratibu katika mazingira ya kawaida ni kweli, wanaweza wasielewe lakini waelewe kwamba sasa hivi Wabunge tunatakiwa turudi kwao kufanya kazi na tukae karibu nao wananchi, ndiyo maana na wananchi wanatakiwa na wao wafanye kazi zao watakuwa wanatuangalia kwenye tv baadaye. Utaratibu huu ni mzuri sana na utawafaidisha wananchi na kuwanufaisha, tutakwenda kila siku majimboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina la zaidi ahsante sana na nashukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kipekee zaidi naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Muhongo kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli Mheshimiwa Muhongo unastahili sifa na nafasi hiyo ulistahili hasa ndiyo maana umerudishwa tena pamoja na majungu yote yaliyotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kuishukuru au kupongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kazi kubwa wanayomsaidia Waziri Muhongo pamoja na Naibu wake kwa sababu kumekuwa kuna mgogoro wa muda mrefu sana kati ya wananchi wa Tarime kule mgodini na wawekezaji wa Mgodi wa Acacia. Lakini Mheshimiwa Waziri amekuwa ni chachu kubwa ya kuonyesha yeye anasababisha ule mgogoro unafikia mahali anaumaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo basi Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zake nilizoziona au wananchi walizoziona Mheshimiwa Waziri alituma watu waende wakaangalie matatizo ya wananchi, Mheshimiwa Waziri alimteua akiwemo Mbunge wa kule kule mgodini kaka yangu Heche na yeye pia alikuwa kati ya watu walioenda kule kuangalia matatizo ya wananchi, kwa hiyo nafikiri mambo yatakuwa mazuri tu nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri endelea hivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona hapa kwenye mkataba wa Mgodi wa Acacia. Mgodi wa Acacia ulikuwa na leseni ya utafutaji wa madini ndani ya Halmashauri ya Tarime katika Kata ya Turwa na Kinyamanyori. Kwakuwa leseni hiyo muda wake ulishakwisha naiomba Serikali ikabidhi maeneo yale kwa wananchi ili waendelee na uchimbaji mdogo mdogo. Na Serikali kwa mpango wake endelevu iliyonao mzuri wa kuwasaidia hao wachimbaji wadogo wadogo, wachimbaji hao watakaporudishiwa eneo hilo iwasaidie mashine za kisasa kama ilivyo kwa maeneo mengine ili uchimbaji wao uwe na tija na uwanufaishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri, pamoja na juhudi zake kubwa sana za kuanzisha mradi wa REA ambao umewasaidia ndugu zetu wengi sana Vijijini ikiwemo Mkoa wa Mara; Mheshimiwa Waziri nikuombe kuna baadhi ya vijiji mkoani Mara ambavyo vimebaki; kwa mfano Wilayani Rorya kuna vijiji vya Kemwame, Kibui, Mkengwa na Baraki Tarafa ya Suba vimekwama baada ya kuwa vimewekewa nguzo toka mwaka 2015 na kinachoendelea wananchi wale hawakijui mpaka sasa hivi wamebaki kwenye sintofahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atakapofunga hoja yake anipe majibu juu ya suala hili la umeme, ni lini wananchi wa Wilaya ya Rorya wataupata umeme? Lakini pia anipe majibu ya kuwarudishia wachimbaji wadogo wadogo wa Tarime eneo lao ili nao waifadike nalo? Kwa sababu kuna wachimbaji wengi wadogo wadogo kule ambao wanaitwa tu wachimbaji wadogo wadogo lakini hawana maeneo ya kuchimba kwa sababu yale maeneo ni ya watu, watu ndio wameyamiliki. Kwa hiyo, nikuombe kipekee zaidi unishughulikie sana suala, hili usiliache.
Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu zangu wapendwa, Wabunge wenzangu; mwisho naomba kumalizia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao wameniwekea wimbo kwenye simu yangu unasema CHADEMA, CHADEMA peoples power nina imani kabisa ni wale majirani zangu. Lakini watani wangu naomba niwaambie mimi ni nyara ya CCM, kwa hiyo huo wimbo hautafanya chochote. Tunapoingia humu ndani Bungeni bangi tuweke pembeni na kazi tuweke pembeni.
Kwa hiyo, ndugu zangu niwaambie hamtanikatisha tamaa, CCM ina vijana, ina wazee ina watoto ina kila mtu na CCM ni ile ile mwaka 2020 mtaisoma namba. Ahsante mimi ndiye Agness kutoka Mkoa wa Mara, nyara ya CCM ahsanteni.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Suleiman Masoud Nchambi

Kishapu (CCM)

Supplementary Questions / Answers (4 / 0)

Contributions (3)

Profile

Hon. Lazaro Samuel Nyalandu

Singida Kaskazini (CCM)

Contributions (1)

Profile

View All MP's