Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Ritta Enespher Kabati

All Contributions

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha , Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa ili tuweze kuujadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo naomba Serikali iweze kunipatia ufafanuzi wake:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza viwanda; ni imani yangu kuwa kama viwanda vitaimarishwa nchini, Serikali itaongeza pato la Taifa na tutaongeza ajira kwa vijana wetu nchini.
Ningeomba kujua, nchi yetu ilikuwa na viwanda vingi sana, ambavyo vingi vyao vilibinafisishwa na wawekezaji wengine wamebadilisha matumizi ya viwanda hivyo. Je, nini mpango wa Serikali kwa viwanda hivyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tulikuwa na kiwanda cha kuchonga almas cha Tancut Iringa, ambacho kilikuwa kinatumia malighafi za ndani, lakini leo hii almas yetu inapelekwa nje kuchongwa. Tungependa Serikali iweke Mpango wa wazi unaoeleza jinsi ya kuanzisha viwanda vitakavyotumia kununua bidhaa za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, miundombinu ya barabara; ningependa kujua Serikali imejipangaje kuhakikisha barabara zote za kiuchumi zinapitika wakati wote ili kuweza kuchukua mazao na malighafi kama Mgololo kilichopo Iringa, hiyo ingejengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Iringa ni kati ya Mikoa ya kiuchumi. Kwa mfano, tunalima mahindi kwa wingi, vitunguu, nyanya, chai na tuna msitu mkubwa sana wa miti, lakini barabara zake zote zinazokwenda kwenye maeneo hayo zina hali mbaya sana! Ningependa jambo hili, Serikali itoe kipaumbele. Pia zipo barabara kama ile inayokwenda kwenye Mbuga ya Wanyama ya Ruaha National Park iwekewe lami ili tupate Watalii wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, umeme; Viwanda vitakapoanzishwa vitahitaji umeme wa uhakika, umeme usio katikakatika kama tulionao hivi sasa na kuwepo umeme, mijini na vijijini ambao ni wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, kilimo; kwa kuwa nchi yetu, wananchi wake asilimia kubwa sana wanategemea kilimo na tunategemea Serikali yetu iweke mpango mahususi kwa ajili ya kusaidia wakulima. Wakulima wapatiwe elimu ili walime kilimo cha kisasa na chenye tija na kitakachoweza kusaidia malighafi katika viwanda vyetu pamoja na kupatiwa mikopo katika Benki yetu ya Kilimo. Je, ni kwa nini Serikali isifungue Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Dodoma ili Benki hii iweze kufikiwa na mikoa yote kuliko ilivyo sasa, Benki hii ipo Dar es Salaam tu?
Mheshimiwa Naibu Spika, tano, uimarishaji wa miradi ya vyanzo vya mapato; Serikali iwe na mpango madhubuti wa kumalizia miradi ambayo imechukua muda mrefu sana, ambayo inaweza kuongeza pato la Taifa kwa sababu tumekuwa tukianzisha miradi mipya wakati miradi ya zamani inasuasua!
Mheshimiwa Naibu Spika, sita, ujenzi wa reli na viwanja vya ndege; bila Serikali kutoa kipaumbele katika ujenzi wa reli bado tutaendelea kusuasua sana katika ukuzaji wa pato letu la Taifa. Reli itaponya hata barabara zetu nchini na kupunguza hata bei ya bidhaa. Pia Serikali ieleze wazi mpango hata kuhakikisha viwanja vyetu vya ndege vinajengwa ili viweze kusaidia kukuza pato la Taifa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha Hotuba yao ili tuweze kuijadili. Yapo mambo ambayo naomba kupata ufafanuzi na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maboresho ya maabara katika shule zetu. Katika Mkoa wetu wa Iringa kuna shule nyingi sana za sekondari bado maabara zake hazijaweza kuboreshwa vizuri ili kuweza kumsaidia mtoto anayesoma masomo ya sayansi. Pamoja na kutokamilika kwa majengo kwa baadhi ya shule, lakini hata vifaa vya kutumia katika maabara kwa baadhi ya shule bado havikidhi haja. Vile vile pamoja na Sera ya Serikali kupeleka umeme wa REA katika taasisi kama shule zetu za sekondari na vyuo, bado hakuna umeme. Sasa tunategemea hawa watoto wakifanya mtihani kweli watafaulu kwa mtindo huu, tutapata kweli wataalam wa sayansi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule kongwe na maboresho ya shule maalum. Katika Mkoa wetu wa Iringa tunazo zile shule kongwe za sekondari kama Shule ya Lugalo, Shule ya Tosamaganga, Shule ya Malangali, hizi shule zinahitaji ukarabati wa hali ya juu.
Ningeomba sasa Serikali itoe kipaumbele katika ukarabati wa majengo ya shule hizi tu. Shule ya Sekondari Lugalo sasa hivi ni shule maalum, inachukua watoto wanaofundishwa elimu maalum, kama watoto wenye ulemavu wa ngozi, watoto viziwi, watoto wasioona, lakini inasikitisha sana kuona shule hii hawa wenye elimu maalum hawana vifaa vya kujifunzia. Je, ni utaratibu gani unatumika ili hawa vijana waweze kupata vifaa vya Walimu wao kuwafundishia na vifaa vya kujifunzia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho ya mitaala kwa Walimu. Serikali imekuwa ikibadilisha mitaala lakini Walimu hawapati semina au elimu kwa ajili ya kuweza kuielewa hiyo mitaala ili waweze sasa kufundisha kwa watoto. Hivyo, Serikali kama inabadili mitaala iende sambamba na kuwafundisha Walimu hao hiyo mitaala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni ya wazabuni. Naomba Wizara ifanye utaratibu wa kulipa madeni yote ya wazabuni. Wazabuni wanapata shida kwa muda mrefu sasa. Ningeomba Waziri anapojibu atueleze mkakati wa Serikali wa kulipa madeni ya wazabuni, yamekuwa ni ya muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia mada iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimwa Rais alipokuwa anapokea ile ripoti ya makinikia ya pili aliomba sisi Watanzania tumuombee, hasa na mimi nikaona nitayarishe vifungu ni nukuu kidogo hapa katika Bunge letu ili wale ambao wanakuwa hawasomi Biblia waweze kusoma na naomba nisome Timotheo wa Pili Mlango wa Kwanza mpaka wa Tatu; “Basi kabla ya mambo yote wataka dua sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya Wafalme na wote wenye mamlaka ili tuishi maisha ya utulivu na amani.”

Lakini ukisoma Waibrania 13 mpaka 17 inasema; “Watiini viongozi wenu na kuwa wanyenyekevu maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu kama watu watakaotoa hesabu ili kwamba wafanye kazi yao kwa furaha na kwa manufaa yenu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Magufuli ni zawadi kwa Watanzania ni Mussa wa Watanzania kwa vile Mungu alivyosikia kilio cha watu wa Taifa la Israel kuwakomboa toka utumwani na kuwapeleka Kanani vivyo hiyo Mungu amesikia kilio cha Watanzania wanyonge amemleta Rais Magufuli ili awe mkombozi wa kututoa katika utumwa, umaskini na kutupeleka katika neema kwa kudhibiti wizi wa madini na rasilimali za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitumie fursa hii sasa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika nchi yetu na niombe Watanzanila bila kujali itikadi zetu tuunge mkono kwa yote anayo yafanya kwa ajili ya Taifa letu. Nawapongeza Watanzania wote waliomuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu na hatua wanazozichukua kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali katika sekta ya madini, nawapongeza Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa azimio lao ambalo walilitoa juzi kuunga mkono juhudi hizi za Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kumpongeza Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri katika Ofisi yake Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu wake Mheshimiwa Mavunde kwa kuaamua kuupatia heshima Mkoa wetu wa Iringa kuja kuzindua mafunzo ya ufundi kwa vijana wetu katika Chuo cha Don Bosco; mafunzo ambayo yatawanufaisha vijana karibu 3,440 na yataendelea kwa nchi nzima tena bure kabisa. Vijana 1,000 Mwanza, vijana 1,000 Morogoro, vijana 2,000 Dar es Salaam na vijana 4,000 ambao wamekuwa wakifanyakazi bila kupata mafunzo watapata vyeti vyao. Kwa hiyo, ni jambo jema ambalo Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inatakiwa iungwe mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeza sasa katika madaa nimpongeze Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango, Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Kijaji na watendaji wote wa Wizara kwa hotuba yake ya bajeti nzuri na yenye mashiko, na ambayo imejali watu wote wakulima, wafanyakazi, wote imewajali kwa kweli. Lakini naomba kabla sijaanza kuchangia kabisa na mimi ni nukuu katika hotuba ya msemaji wa Kambi ya Upinzani ukurasa wa tatu maneno ya hayati Nelson Mandela “No easy walk to freedom.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie wenzangu Wapinzani kuwa nchi hii ilikwisha pata uhuru kwa njia ya amani na utulivu. Sasa sijui wenzetu wanapigania uhuru wa nchi gani maana nchi yetu ilikwisha kombolewa kutoka kwa wakoloni kwa jitihada za TANU na sasa hivi ndio CCM na hao hao NAC tuliwasaidia Watanzania kupata uhuru kutoka kwa makaburu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali katika bajeti hii kwa kuwatambua rasmi wafanyabishara wadogo wadogo wasio rasmi na wanafanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi kama mama lishe, wauza mitumba wadogo wadogo, wauza mazao ya kilimo kwa kuwapatia vitambulisho maalum kazi wanazozifanya. Lakini nilitaka kujua je kuhusiana na vijana wa bodaboda na wenyewe wako maana yake kwenye kitabu kile hawajasema maanake nao wamekuwa wakitoa kodi naomba na wenyewe labda watakapokuwa wanajibu watuambie kama na bodaboda na wenyewe wapo.

Pia nilikuwa naomba Halmashauri zetu ziandae sasa mazingira rafiki kwa hawa wafanyabiashara waweke miundombinu rafiki, kuwepo na maji, kuwepo na umeme na waangalie sehemu ambazo hawa wanaweza wakafanya biashara zao na wakapata faida. Kwa sababu utakuta Halmashauri zetu zimekuwa zikitenga maeneo ambayo sio rafiki na biashara na kuwasababisha vijana wetu kushindwa kufanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi pia niungane na wote waliochangia kuhusiana na tozo ile ya shilingi 40 katika mafuta mimi nilikuwa naomba kweli ipelekwe moja kwa moja katika mradi wa maji. Kwa sababu maji vijijini ili dhamira ya kumtua ndoo kichwani mwanamke iweze kutimia kwa sababu ukiangalia katika Mkoa wetu utakuta miradi hii ya maji mingi sana imekwama, visima vingi vimechimbwa lakini havitoi maji na vilevile unakuta kuna vyanzo vya maji vingine ambavyo bado sio salama, kwa hiyo, kuna maziwa na mito mingi lakini bado hatujaweza kupatiwa maji vizuri katika Mkoa wa Iringa maji vijijini ni tatizo kubwa sana. kwa hiyo nilikuwa naomba ile tozo iende moja kwa moja kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuchangia kuhusiana na hoja hii nafikili tunaelekea katika uchumi wa viwanda lakini bila kutoa kipaumbele katika barabara zetu za kiuchumi bado tunapatashida sana, kwa sababu ndizo ambazo zenye malighagfi, utakuta katika Mkoa wetu wa Iringa barabara nyingi sana za kiuchumi hazina lami. Kwa hiyo, utaona kwamba zile malighafi wakati wa mvua malori yanakuwa yanakwama ukienda kule Mufindi, Kilolo unakuta kwamba yale malori yanakwama kule kwa hiyo mimi nilikuwa naomba Serikali itoe kipaumbele ihakikishe kwamba barabara zote za kiuchumi zinawekewa lami ili kusaidia hata kukuza uchumi huu wa viwanda kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipochangia mara ya kwanza nilichangia kuhusiana na Benki ya Wanawake; kwa kweli hii Benki ya Wanawake sisi kwa Wanawake ni mkombozi na nilisema kwamba imeshafungua baadhi ya madirisha katika baadhi ya Mikoa ambayo sio ming, ningeomba Serikali kwa kweli iangalie kwa karibu ili iweze kuipatia ile pesa ambayo ruzuku ambayo ilikuwa Serikali imeamua kuwapatia ili Wanawake wote wafaidike kwa sababu Wanawake wengi sana walikuwa wanaaibishwa, ndoa nyingi sana zimevunjika kwa sababu wanaenda kuchukua kwenye taasisi za fedha nyingine ambazo zinawafanya wanawake wanadhalilika wanawake ndoa zimevunjika, wanauziwa mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naamini kwamba kwa sababu Serikali na tulikaa kwa pamoja na tukaamua kwamba Benki ya Wanawake iwanufaishe Wanawake wote basi Serikali iweze kutoa pesa ambayo ruzuku ilikuwa imeahidi kwamba ingeweza kuwa inatoa kila bajeti ili madirisha mengi sana yaweze kufunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu kinu chetu cha Iringa pale National Milling, nililisema siku ile kwenye swali, kile kinu tuna imani kwamba NSSF walisema kwamba wangetusaidia ili kile kinu kiweze kusaidia wakulima wa Iringa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kwa kweli hili nalo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwamba makinikia yetu sisi Iringa ni vinyungu, utaona Wabunge wengi sana wamechangia hapa wakizungumzia kuhusu vinyungu. Vinyungu ndio mkombozi wa wana Iringa sasa nisipozungumza sasa hivi wanawake wote wanashindwa, maana yake ilikuwa mwaka mzima unalima, mwaka mzima unafanya biashara kupitia vinyungu vile, hata mimi mwenyewe nimesomeshwa kwa vinyungu. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi naomba Serikali iangalie upya hili suala la vinyungu maana yake hata kwa Wasukuma kule wanaita majaruba maana mimi nimeolewa na Wasukuma wanaita majaruba kwa hiyo kila nchi wanaita kwa majina yao, kwa hiyo ningeomba hivi viangaliwe upya ili wananchi waendelee kutumia maana yake naona Wabunge wengi wa Iringa pia wamezungumzia kwa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza haya kwa kweli kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu na niseme kwamba Waziri wa Fedha kanyaga twende, fanya kazi, tunajua kwamba tunakuamini, wewe ni Waziri ambaye umekuwa ukitusaidia sana, kwa hiyo, endelea na Naibu wako, fanyeni kazi leteni bajeti na niombe sasa pesa zifike kwa wakati kwenye Halmashauri zetu ili ile miradi ya muda mrefu iweze kumalizika kwa wakati kwa sababu tumekuwa na miradi mingi ya muda mrefu ambayo sasa mkichelewesha pesa gharama inakuwa inaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nikushukuru na ninaunga mkono hoja kwa asilimia 150.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri walio katika Wizara yake kwa kutuletea bajeti ili tuweze kuijadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii imegusa kila eneo lakini yapo baadhi ya mambo ambayo nataka nipatiwe ufafanuzi:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watu wenye ulemavu; niipongeze Serikali katika ukurasa wa 21 inasema inathamini mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo na kwamba wana haki sawa ya kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Hata hivyo, bado watu wengi wenye ulemavu wanapata mateso sababu Serikali haijaweza kutunga sheria kuhakikisha watu wanaomiliki vyombo vya usafiri wanahakikisha miundombinu inakuwa rafiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walemavu wengi wamekuwa wakipata mateso makubwa sana hasa wale wenye baiskeli kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine wanapokuwa wanasafiri umbali mrefu. Bado majengo mengi sana hayajaweza kuwa na miundombinu rafiki ya kumfanya mtu mwenye ulemavu aweze kuyatumia kama vile shule, hospitali, vituo vya afya hata ofisi zetu za Serikali, mtu mwenye ulemavu anapotaka huduma katika majengo hayo imekuwa ni mateso kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua ni lini Serikali itaweka sheria kuhakikisha zinalinda haki ya mtu mwenye ulemavu. Pia bado wetu wenye ulemavu wengi na hasa wale wasio na uwezo wa kupata baiskeli wapo nyumbani hawapati hata haki ya kusoma. Nashauri Serikali ihakikishe kila mwenye ulemavu anapatiwa baiskeli bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilianzisha program ya kuwasaidia watu wenye ulemavu katika mkoa wangu, niliamua kuwathamini, kuwajali na kuwasaidia pale walipo, naelewa changamoto nyingi sana ambazo Serikali yetu inatakiwa kuzitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu ya bure; niendelee kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kutoa elimu bila malipo nchini, imesisitiza kila mzazi kupeleka mtoto shule na asiyepeleka mtoto hatua kali itachukuliwa dhidi ya mzazi/mlezi huyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imeweka mkakati gani kuhakikisha hawa watoto wa mitaani au watoto wanaojulikana kama ombaomba nao wanapata hiyo haki ya kusoma? Ni nani anayewajibika ili watoto hawa wasome? Swali hili huwa najiuliza kila siku lakini huwa nakosa jibu, ningependa kujua mkakati wa Serikali kuhusiana na hilo.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa ushauri au pendekezo langu kwa Serikali, kwa kuwa kuna shule za watu binafsi na shule nyingi zimekuwa zikitoza fedha nyingi lakini nazo zimekuwa zikitozwa kodi na Serikali, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuwapeleka hawa watoto katika shule hizo ili zile shule zinazokubali kuwachukua na kuwasomesha hawa watoto wa mtaani shule hizo zipunguziwe kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya wazabuni, wazabuni wa nchi hii bado wana mateso makubwa sana pamoja na kuwa walijitahidi kutoa huduma kwa Serikali yetu, kuna baadhi ya wazabuni ambao toka awamu zilizopita wamekuwa wakifuatilia malipo yao bila mafanikio. Serikali itambue kwamba wazabuni hawa wengi wao ni wale waliochukua mikopo benki na kuna wazabuni ambao wamesababishiwa kutaka kuuziwa dhamana zao walizoweka rehani ili wapatiwe mikopo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itambue kuwa wazabuni hawa pia wanadaiwa na kodi ya mapato, kwa sababu sheria inasema ukishatoa invoice kwa mzabuni wako unatakiwa ulipe kodi, sasa wanalipa kutoka wapi wakati bado hawajalipwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuhakiki madeni ya wazabuni bado hatma ya malipo haijajulikana. Ningependa kujua Serikali hii ya Awamu ya Tano imejipanga vipi kuhakikisha wazabuni wanalipwa kwa wakati ili kumwondolea adha ambayo mzabuni amekuwa akiipata na imesababisha wazabuni wengi kufilisika na kufunga biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali wa kutoa milioni hamsini kila kijiji; naendelea kutoa pongezi zangu kwa Serikali na Rais wa Awamu hii ya Tano kwa kuwa na mpango wa kupeleka milioni 50 kila kijiji. Sasa napenda kujua, Serikali imejipangaje kutoa elimu ya kuwatayarisha walengwa ili kuhakikisha pesa hizi zitakapoanza kutolewa zinawafikia walengwa na zinawasaidia, pia kuweza kurudishwa ili ziweze kuwa na mzunguko, kwa kuwa ukimpatia mlengwa akazirudisha zitasaidia walengwa wengi kufikiwa. Tuna rundo kubwa sana la akinamama ambao wameweza kuwa na uthubutu wa kufanya biashara, lakini hawana mitaji, sasa hili jambo litakuwa ndiyo suluhisho ya mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira zisizo rasmi; napenda kujua ni lini Serikali itarasimisha ajira zisizo rasmi? Kwa mfano, Mkoa wetu wa Iringa ni Mkoa ambao vijana wengi wamekuwa wakipata ajira ya kufanya kazi za ndani (house girl au house boy), pia tumekuwa na mkataba wa Kimataifa na nchi yetu kuridhia, bado ajira hii haijarasimishwa imekuwa ikisababisha vijana wengi kufanyiwa vitendo vya kikatili, kunyanyaswa, kubakwa, kupata mimba zisizotarajiwa na kuambukizwa UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua ni lini ajira hii itarasimishwa ili vijana wetu waweze kutendewa haki na hata kujiunga katika Mifuko ya Jamii, kuwekewa bima ya afya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mauaji ya vikongwe; haya mauaji ya vikongwe hasa Mikoa ya Kanda ya Ziwa yamekuwa ni tishio na mauaji haya yamedumu kwa muda mrefu sana. Ningependa kujua Serikali imejipanga vipi kukomesha ukatili huu wanaofanyiwa vikongwe kwa kushirikishwa na imani za kishirikiana? Je, toka mauaji haya yameanza kufanyika ni vikongwe wangapi wameuawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kumaliza miradi ya zamani. Ningependa kujua mpango wa Serikali kuhakikisha inamaliza miradi iliyochukua muda mrefu kukamilika. Kwa mfano, katika Halmashauri yetu upo mradi wa machinjio, mradi huu umechukua muda mrefu sana kukamilika. Ni imani yangu kuwa mradi huu ukikamilika Manispaa yetu itakuwa na chanzo kizuri sana cha mapato na pia Halmashauri itaongeza ajira kwa vijana wetu, hivyo ningeshauri Serikali ifanye tathmini ya vile vyanzo ambavyo vinaweza kutuongezea mapato na miradi yake ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji; niendelee kuipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma ya maji safi, salama na ya kutosha. Imani yangu ni kuwa, kama program hiyo itakamilika, nia ya Serikali kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani itatimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Iringa hauna tatizo la maji, bali tatizo kubwa ni usambazaji wa maji. Kwa mfano, Wilaya ya Kilolo ina mito mingi, Serikali inashindwaje kutoa maji kutoka kwenye Mto Lukosi, Ruaha na Mtitu? Nina imani kabisa kama Serikali ingesambaza maji kupitia vyanzo vya mito hii, ingeweza kutumia gharama nafuu sana ya uhakika kuliko kuchimba visima visivyokuwa na tafiti za kutosha na kusababisha pesa nyingi kutumika katika tafiti badala ya kutumia vyanzo vya mito, kwa sababu maji yanapokosekana ni mwanamke ndiye anayeteseka. Tunaomba ile ahadi ya kumtua mama ndoo kichwani ikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma muhimu katika Wilaya mpya; kuna Wilaya ambazo zimeanzishwa muda mrefu sana, lakini bado hazijapatiwa huduma muhimu. Kwa mfano, Wilaya ya Kilolo ilipata hadhi ya kuwa Wilaya toka mwaka 2002, mpaka leo hii Serikali haijaweza kujenga Hospitali ya Wilaya, Makao Makuu ya Polisi, Mahakama ya Wilaya, pia barabara inayounganisha Makao Makuu na Wilaya mpaka leo hakuna lami pamoja na Halmashauri kuweka jitihada ya kutenga maeneo kwa ajili ya huduma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi hata hizi ahadi za Serikali za kujenga Wilaya mpya kama zitatekelezeka, ningependa kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha hizi Wilaya zilizoanzishwa muda mrefu utekelezaji wake upo vipi, ukamilishaji wa hizo huduma katika Makao Makuu ya Wilaya, kwa sababu wananchi wamekuwa wakipata shida sana kuzifuata hizo huduma na hasa kutokana na changamoto za miundombinu ya barabara zetu za vijiji zilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti iliyoletwa Mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kurudi tena kwa mara ya pili katika Bunge hili maana bila yeye nisingekuwemo.
Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia bajeti hii, naomba kwanza nishukuru na nikipongeze sana Chama changu cha Mapinduzi kwa ushindi wa kishindo na niwapongeze Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi. Vilevile niendelee kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya. Nimpongeze pia Waziri Mkuu na Mawaziri wote wamekuwa wakifanya kazi nzuri na kwa umakini mkubwa sana. Nimpongeze Spika, nikupongeze na wewe Naibu Spika, nipongeze pia na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Rais wa Zanzibar kwa ushindi wa kishindo kikubwa alichokipata kwenye uchaguzi wao na sasa hivi Baraza la Uwakishilishi ni wana-CCM watupu. Najua sasa watafanya kazi nzuri sana kwa sababu tulipokwenda China labda niwakumbushe wenzangu walioenda China wenzetu wa China walisema kwamba Tanzania mnachelewa kwa sababu ya upinzani. Wenzetu kule chama ndiyo kinachoongoza Serikali, kwa hiyo tulivyokwenda hata na wapinzani walisema kwamba hawa kazi yao ni kuwinda yale mabaya. Kwa hiyo, naamini kwamba Zanzibar watafanya kazi nzuri sana, waendelee kufanya kazi wawakilishe vizuri chama chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kushukuru tu, naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa ujenzi wa daraja la Igumbilo ambalo lipo katika Jimbo la Iringa Mjini. Lile daraja kwetu lilikuwa ni tatizo kubwa. Kila mwaka watu walikuwa wanakufa kwenye lile daraja kwa sababu kuna shule ya sekondari, kuna chuo sasa ujenzi wa lile daraja najua kwamba maafa ya vifo vya kila siku pale Iringa tumekombolewa. Kwa hiyo naamini kwamba uchaguzi ujao, najua Mama Mbega alitolewa kwa ajili ya lile daraja, tumeshajenga Jimbo litarudi tu kwenye Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kuchangia kuhusu ucheleweshaji wa fedha za miradi katika Halmashauri zetu. Kumekuwa na ucheleweshwaji mkubwa sana wa fedha za miradi katika Halmashauri na kusababisha miradi hii kuongezeka gharama kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Manispaa yetu ya Iringa Mjini uko mradi ule wa machinjio ya kisasa wa Ngelewala. Ule mradi kwa kweli ulipoanza gharama yake ilikuwa ndogo lakini sasa hivi kadri unavyocheleweshwa ule mradi unaendelea kuongezeka gharama. Kwa sababu mpaka mwaka jana bajeti iliyopita tulitakiwa tutumie shilingi milioni 700 ili kumaliza mradi ule, lakini sasa hivi zinahitajika shilingi 1,400,000,000 ili mradi ule uishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ule mradi utatunufaisha sana sisi Wanairinga kwa sababu kwanza tunategemea kupata ajira kama ya vijana 200 mradi utakapokamilika. Vilevile tunajua kwamba mradi ule utakapokamilika Halmashauri yetu itaongeza mapato. Pia kwa sababu yale ni machinjio ya kisasa tunategemea kwamba nyama itakayochinjwa pale itasafirishwa nje tutaongeza pia pato la fedha za kigeni. Kwa hiyo, labda Serikali ingefanya upembuzi yakinifu kuangalia ile miradi ambayo itasaidia kuongezea mapato kwenye nchi hii au kwenye Halmashauri zetu, hii ingemalizika kwa haraka zaidi ili iweze kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kuchangia kuhusiana na Serikali kutokamilisha miundombinu katika wilaya zetu. Katika Mkoa wetu wa Iringa, Wilaya ya Kilolo, nilishawahi kuuliza swali la nyongeza kwamba ilipata hadhi mwaka 2002 lakini mpaka leo miundombinu yake mingi sana bado haijakamilishwa katika makau makuu. Kwanza, Jimbo lile lina changamoto kwamba kuna wananchi wanaoishi mabondeni na kuna wanaoishi milimani. Kwa hiyo, utakuta kwamba kutokuwepo miundombinu kwenye makao makuu wananchi wanapata shida sana. Hakuna Hospitali ya Wilaya ya Serikali, hakuna Mahakama, Mahakama ya Wilaya wanaendeshea kwenye Mahakama ya Mwanzo. Vilevile Makao Makuu ya Polisi hayapo katika Makao Makuu ya Wilaya. Kwa hiyo, Serikali ingeangalia kwa sababu nia ya Serikali kuanzisha Wilaya ni kusogeza huduma kwa wananchi. Sasa kama hamuweki huduma kwa wananchi hata ile nia ya kuanzisha hizo Wilaya inakuwa bado haisaidii kitu chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwazungumzie wazabuni. Madeni ya wazabuni kwa kweli yamekuwa mwiba sana. Wazabuni wengi wanadai sana na wengi wao kwanza wamekopa benki na wengi wao wanadaiwa mpaka kodi za mapato. Kwa hiyo, sasa nia ya kuwasaidia hawa wananchi wenye kipato cha chini inakuwa hamna kwa sababu kama wamekopa wakauziwa zile dhamana zao kwa ajili ya madeni ambayo wanadai Serikali naona itakuwa hatuwasaidii. Kwa hiyo, naomba suala hili lipewe kipaumbele ili wazabuni kwenye halmashauri zetu zote au kwenye Serikali yetu yote waweze kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine labda nielezee kuhusu barabara zetu za Halmashauri. Kumekuwa na tofauti kubwa sana kati ya barabara za Halmashauri na za TANROADS. Huwa najiuliza ni kwa nini kwa sababu hata kule kuna wataalam, labda kama mnapeleka pesa kidogo mngepeleka pesa nyingi ili na zenyewe ziwe na uimara kwa sababu barabara za Halmashauri zinajengwa temporary sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa…….
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.
MHE. RITTA E. KABATI: Naomba niunge mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na kumpongeza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na watendaji wake kwa kuwasilisha hotuba ya bajeti yao hapa Bungeni ili tuweze kuijadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ambayo nilikuwa napenda kupatiwa ufafanuzi na kutoa ushauri kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, viwanda vilivyobinafsishwa. Serikali iliamua kubinafsihsa viwanda vilivyokuwa vya Serikali na kubinafsishwa kwa wawekezaji lakini bado tunaona licha ya kuwa viwanda hivyo havifanyi kazi lakini vingine vimebadilishwa hata matumizi na vingine vimegeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia bidhaa au mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango mkakati gani kwa sababu awamu hii Serikali ina mpango wa kufufua viwanda na ningependa kujua hatua gani watachukuliwa wawekezaji hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ningependa kujua katika ujenzi wa viwanda je, itazingatia katika maeneo yenye malighafi ili kupunguza gharama za kusafirisha malighafi kutoka zinakopatikana mpaka viwandani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Iringa hasa katika Jimbo la Kilolo asilimia kubwa kuna kilimo cha nyanya, pilipili na vitunguu, lakini wakulima wamekuwa wakipata shida sana kupata masoko kwa kuwa Serikali inahimiza ujenzi wa viwanda na kuna eneo la EPZ je, mkakati wowote umewekwa na Serikali ili kupata mwekezaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, maeneo yaliyoteuliwa na EPZ. Kwa kuwa Serikali ilitenga maeneo mengi sana kwa ajili ya uwekezaji katika viwanda lakini maeneo mengi bado wananchi hawajalipwa fidia likiwemo lililotengwa katika Mkoa wetu wa Iringa. Nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanalipwa ili maeneo hayo yaweze kutumika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubovu wa barabara zinazokwenda katika viwanda. Nini mpango wa Serikali kuhakikisha barabara zote zinazokwenda katika viwanda zinajengwa kwa kiwango cha lami na barabara hizo zinahamishwa kutoka kuwa za Halmashauri na zinakuwa za TANROAD.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha bajeti hapa Bungeni ili tuweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ambayo nilikuwa naleta ili kupatiwa ufafanuzi na kutoa ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanja vilivyojengwa kwa ajili ya michezo, naomba Serikali inipatie majibu kuhusu viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya michezo na Halmashauri zetu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja hivi watendaji wa Halmashauri waliamua kuvigawa na vikafanyiwa uvamizi yakajengwa majengo na baadaye Serikali ikatoa tamko kuwa wavamizi na maeneo ya wazi yaliyotunzwa kwa ajili ya michezo wabomoe lakini tamko hilo halijatekelezeka mpaka leo. Na kila siku tumekuwa tukiuliza maswali kuhusiana na jambo hilo lakini yanajibiwa kisiasa zaidi. Sasa naomba kujua jambo hili, Serikali imelichukulia vipi kwa sababu hatuwatendei haki vijana wetu, vipaji tunavitengenezea vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kujua sheria za vyombo vya habari ni lini italetwa hapa Bungeni, kwa sababu tunaamini kuwa sheria hii ndiyo muarobaini wa matatizo yote katika vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu michezo ya UMISETA na UMISHUMTA. Michezo hii kwa sasa haina ari kabisa, ni imani yangu kama Serikali ingeamua kuwekeza mikono katika shule za msingi na sekondari zingeweza kuibua vipaji na tungeimarisha michezo yetu hapa nchini na kupata wachezaji bora. Inasikitisha kuona kuwa michezo ya shule za sekondari na msingi inapoanza shule nyingi watembeze mabakuli ya kuomba omba vifaa vya michezo mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Tanzania tutakuwa na Vazi letu la Taifa?. Serikali imekuwa kila mara ikitupatia taarifa kuwa Vazi la Taifa lipo katika mchakato. Ifike wakati tuambiwe kama imeshindikana tuambiwe ili tusiendelee kusubiri jambo lisilo na mwisho. Ni fahari kubwa kutambulika kwa mavazi kama zilivyo nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini Serikali bado haiwezi kutoa kipaumbele timu ya wanawake, mbona timu ya Taifa inatafutiwa mpaka kocha wa kigeni kwa nini timu ya Twiga bado mpaka leo wanatembeza bakuli tu wanapokuwa na mashindano? Ni lini watapewa fungu au kutengewa katika Bajeti ya Serikali? Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha bajeti yao hapa Bungeni. Yapo mambo ambayo nilikuwa napenda kupata ufafanuzi wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya ndege; ukisoma kitabu cha hotuba ya Waziri, ukurasa wa 90 – 91 unaeleza kuwa kupitia TCAA Serikali itaendelea kusimamia uboreshaji wa viwanja vya ndege na kiwanja cha ndege cha Nduli kikiwa kimojawapo. Lakini ukiangalia hali halisi ya kiwanja cha ndege cha Nduli kipo katika hali mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanja kina matatizo makubwa sana katika njia ya kurukia na kutua ndege (runways), kiwanja hakina fence, kila siku mifugo inapita katikati ya kiwanja. Kutokana na mafuriko yalijitokeza mwaka huu kiwanja kimeharibiwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2015 safari za ndege zilikuwa 2,300. Idadi ya abiria kwa mwaka 2015 walikuwa 8,300 hivyo ni ongezeko la asilimia 198 kwa safari za ndege katika kipindi cha miaka mitano. Kuna ongezeko la wasafiri wanaosafiri kwa ndege, ni asilimia 90 kwa kipindi cha miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mbuga ya wanyama ya Ruaha; kama kiwanja hiki kitakamilika kwanza tutaongeza utalii na pia tutakuza uchumi wa Mkoa na Taifa zima. Naomba kujua kama kiwanja hiki kitajengwa kwa sababu katika mpango kipo, lakini muda ndiyo leo Waziri atupe jibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara za kiuchumi mkoa wa Iringa. Serikali ya Awamu hii ya Tano, sera yake ni ujenzi wa viwanda ili kukuza kwa uchumi wa nchi na kutengeneza ajira kwa wananchi. Katika mkoa wetu wa Iringa barabara nyingi za kiuchumi bado hazijaweza kujengwa kwa kiwango cha lami pamoja na kwamba katika hotuba yake kuna baadhi zimetengewa fungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kilolo; barabara ya Ipogolo - Kilolo, makao makuu, hii barabara inaunganisha Mkoa na Wilaya kilometa 37, lakini iliyojengwa kwa lami ni kilometa saba tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mufindi; kuna kiwanda cha karatasi, viwanda vya chai, msitu mkubwa; barabara zake ni Mafinga - Mgololo - Changalawe kupitia vijiji vya Sao Hill, Mtila - Matana kutokea Nyororo, Nyororo – Kibao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu reli ya kati; ili kuponya barabara zetu ni vema Serikali ikaijenga. Ushauri wangu ni kuwe na TANRAIL ambayo itafanya kazi kama TANROADS kuweza kusimamia masuala ya reli nchini, mfano reli ya kati, reli ya TAZARA, reli mpya kwenda DRC, hii ya Tanga - Uganda, Tanga - Kigali; itasaidia kubeba mizigo mingi, itasaidia kulinda barabara zetu, itasaidia kupunguza gharama, itasaidia kufungua fursa ya ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya TAZARA; muda mrefu Serikali inazungumzia kupitia upya mkataba wa Sheria za TAZARA, je, Serikali imefikia wapi? Ni kwa nini kwa upande wetu tusitumie reli ya TAZARA kwa usafirishaji wa ndani ya nchi, tuliambiwa upande wa Zambia wanafanya hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mishahara ya wafanyakazi wa TAZARA imefikia wapi, hakuna tena mgogoro? Naomba kupata majibu ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii adimu. Kwa sababu nilishaongea naomba nianze moja kwa moja kwenye mada, naunga mkono hoja ya hotuba hii ya miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze moja kwa moja na ujenzi wa viwanja vya ndege na moja kwa moja nielekee katika Mkoa wangu wa Iringa. Kiwanja cha Nduli ni kiwanja ambacho toka nimeingia hapa Bungeni miaka mitano iliyopita, siku zote nimekuwa nikichangia hotuba ya Uchukuzi lakini kiwanja hiki tumeambiwa kwamba kipo katika mpango wa ujenzi wa vile viwanja 11. Haya majibu tulishapata toka hotuba ya Bunge lililopita, sasa ni lini hasa Kiwanja cha Nduli kitajengwa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hakijajengwa hiki kiwanja kina changamoto nyingi sana na najua kwamba ujenzi wa hiki kiwanja utasaidia sana kukuza uchumi wa Mkoa wetu wa Iringa, hata Taifa zima. Kwa sababu tunategemea sana ile hifadhi ya Ruaha ambayo tunajua kwamba watalii wengi sana tungewapata na tungeweza kupata ajira kwa vijana wetu na vilevile tungeweza kabisa kuongeza kipato cha utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja huu una changamoto nyingi sana. katika njia zile za kuruka na kutua (running way) kuna makorongo, yaani sio ma-corrugation, zile njia ni balaa, kwa sababu mwaka 2012, mwaka 2015 kulishawahi kutokea ajali ya ndege ya Auric. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri au na ile Kamati ingepita kuona, wakati wowote tunaweza tukapata matatizo. Ule uwanja sasa hivi hauna uzio, mara nyingi sana mifugo inakatiza katikati ya uwanja na vilevile bei ya ndege ni kubwa sana kwa sababu hakuna kituo cha mafuta. Kwa hiyo, inasababisha nauli inakuwa kubwa sana. Ningeomba kabisa uwanja huu ukakaguliwe mapema na ikiwezekana katika vile viwanja 11 basi kiwe cha kwanza kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia na ujenzi wa barabara za kiuchumi katika Mkoa wetu wa Iringa. Kwa kuwa Serikali hii ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele kabisa kujenga viwanda kwa ajili ya kujenga uchumi na kufufua viwanda vyetu nchini ili kuongeza ajira na pia kuongeza uchumi katika nchi yetu. Katika Mkoa wetu wa Iringa zipo barabara za kiuchumi ambazo siku zote Wabunge wangu wa Mkoa wa Iringa wamekuwa wakizizungumzia kwamba zijengwe kwa kiwango cha lami ili ziweze kupitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kwenye Mkoa wetu wa Iringa, kwanza kabisa kuna Kiwanda kile cha Mgololo cha Karatasi, kuna Viwanda vya Chai ambavyo viko pale Mufindi na kule Kilolo. Vile vile kuna msitu na kuna hifadhi, lakini barabara zake zote za kiuchumi hazina lami, sasa utakuta malori yanapokwenda kuchukua bidhaa na kuna malighafi nyingi tu ambazo zingesaidia kwenye viwanda lakini wanapokwenda kuchukua zile malighafi wakati wa mvua malori yanakwama mno. Kwa hiyo, naomba kabisa Serikali sasa iangalie na izipe uzito. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwenye kile kitabu, kuna baadhi ya barabara zimetengewa japokuwa ni finyu sana, lakini naomba sasa ungefanyika upembuzi yakinifu, ile miradi ya kiuchumi, barabara zile za kiuchumi zianze kujengwa ili kusaidia uchumi kwenye nchi hii. Labda hata nizitaje kidogo, kuna barabara hasa inayokaa katika hifadhi, Ruaha National Park, hii nafikiri ipewe kipaumbele kikubwa sana katika mkoa wetu, kwa sababu ile hifadhi ni ya pili katika Afrika. Halafu katika Wilaya ya Mafinga kuna ile barabara ya Mafinga-Mgololo, kwenda Shangalawe kupitia Sao Hill, Mtula – Matana kuelekea mpaka Nyololo, kuna ile barabara ya Nyololo - Kibao, hizi zipewe kipaumbele katika Wilaya ya Mufundi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukienda Kilolo, barabara inayounganisha mkoa na Makao Makuu siku nyingi sana, hata Profesa Msola alikuwa anaisemea sana, haina lami kabisa. Ile inaanzia Ipogolo- Ndiwili- Ihimbo- Luganga- Kilolo, hii nayo ipewe kipaumbele. Pia kuna ile ya Dabaga- Ng‟ang‟ange- Mwatasi- Mufindi, hizi barabara ni za kiuchumi, naomba zipewe kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nizungumzie kuhusu reli ya kati. Mimi nimeolewa na Wasukuma, ni vizuri nikiwazungumzia. Huu ujenzi wa reli ungesaidia sana kuponya barabara zetu, tumekuwa tukitenga pesa nyingi sana kwa ajili ya barabara lakini kama hakuna reli tumekwenda kuona kwenye nchi za wenzetu, nchi nyingi zenye miundombinu mizuri hata uchumi unakwenda kwa haraka sana. Kwa hiyo, ningeomba kwa kweli reli safari hii ipewe kipaumbele cha hali ya juu kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pengine ningetoa tu hata ushauri wangu, pengine kungekuwepo na TANRAIL ambayo itafanya kazi kama TANROADS. Hii TANRAIL ishughulikie tu masuala ya reli, reli ya kati, reli ya TAZARA na ijenge hizi barabara ya Tanga, Tanga mpaka Kigali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niizungumzie kidogo reli ya TAZARA, kwamba, kulikuwa kuna ile sheria ambayo muda mrefu sana tulijua kwamba hii sheria ingeletwa mapema ikabadilishwa tungeweza pia kuwasaidia hii Reli ya TAZARA. Mara ya mwisho Waziri aliyekuwepo alikuwa amefanya mpango kwamba wale Wajumbe wa Miundombinu wangekwenda Zambia wakakutana ili warekebishe hii sheria. Sasa nataka kujua imefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo nataka kulizungumzia, ni kuhusu hizi nyumba za Serikali zilizouzwa. Ukisoma kitabu cha Kambi ya Upinzani ukurasa wa tisa unaelezea, lakini nataka kwanza kunukuu kwamba unapozungumzia kitu, nimesoma neno la Mungu kwa sababu Mbunge wangu ni Mchungaji, anasema kwamba toa kwanza boriti kwenye jicho lako ndipo utaona kibanzi kwenye jicho la mwenzio. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimeangalia, hizi nyumba zimeuzwa lini, mwaka 2002, wakati huo Waziri Mkuu alikuwa Mheshimiwa Sumaye na sasa hivi yuko kwenye Kamati Kuu ya CHADEMA. Vile vile nikaona kwamba mgombea wa upinzani naye aliuziwa Plot No. 68 na nikaona kwamba mgombea wa Upinzani, Mheshimiwa Lowassa na yeye pia anahusika. Aliuziwa kwenye 590, sasa ningeomba ushauri huu wangerudisha kwanza wao…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kabati muda wako umekwisha!
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea bajeti ili tuweze kuijadili. Yapo mambo ambayo nilikuwa nataka kuishauri Serikali pia na mengine kupatiwa ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni ya makazi, wananchi wengi sana wanaoishi katika maeneo yasiyopimwa Serikali iliweka mpango wa kuwapatia leseni za makazi ili waweze kutumia ardhi yao kupata mikopo ya benki au taasisi mbalimbali za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini muda wa miaka mitatu ni kidogo sana, ni kwa nini Serikali isiweke angalau hata miaka mitano mpaka kumi ili kusiwepo na usumbufu wa mkopaji kama anachukua mkopo wa muda mrefu? Naomba hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za pango la nyumba za Shirika la Nyumba. Nimpongeze Waziri mwenye dhamana. Tulishawahi kumsikia katika vyombo vya habari akizungumza kuhusu wananchi wa kipato cha chini kushindwa kumiliki nyumba za kuishi au nyumba za biashara. Kama kweli Serikali inataka na ina dhamira ya kweli ya kuwasaidia wananchi wake ingeangalia upya hizi gharama za pango la nyumba za National Housing kwa sababu wananchi wengi wana kipato cha chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hizi nyumba za gharama nafuu ziangaliwe upya, bei ni kubwa sana, watu wenye kipato cha chini si rahisi kuzinunua. Kama tatizo ni kodi ya vifaa vya ujenzi Serikali ingeondoa ili kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi nchini. Nimpongeze Waziri kwa kuanza kupita katika maeneo yenye migogoro ya ardhi, kwasababu migogoro mingi ni kati ya wakulima na wafugaji, hifadhi na wananchi na mingine ni kati ya wawekezaji na wananchi. Ni kwanini Serikali isiwe na mpango wa kutenga kabisa maeneo kabla ya kuyagawa? Ni kwa nini yasitengwe maeneo ya wakulima ili Serikali iweze kuweka mahitaji yote katika maeneo hayo ili kuondoa hii migogoro? Serikali ina wataalam wa mipango miji, ni kwa nini miji yetu haina mipango? Kumekuwa pia na migogoro hata katika miji yetu sababu wananchi hawajengi majengo kwa mpango. Ni vema Serikali kabla ya kugawa viwanja ingetengeneza mpango mji na baada ya kugawa viwanja basi wasimamie majengo yanayojengwa ili kusiwepo na migogoro ya uvamizi hata ya viwanja vya wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi. Serikali ilijitahidi kufanya maboresho katika Mabaraza haya ya Ardhi ili mabaraza haya yaweze kutenda haki kwa wananchi. Mara nyingi kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya mabaraza kulalamikiwa kutotenda haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mabaraza haya kumekuwa na changamoto nyingi sana, ni vema Serikali ingeanza kutatua baadhi ya changamoto zinazoyakabili Mabaraza haya.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha bajeti yao ili tuweze kuijadili. Yapo mambo ambayo napenda kutoa ushauri na pia kupatiwa ufafanuzi wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini mkakati wa Serikali katika kukuza na kutangaza utalii Kimkoa au Kikanda? Mkoa wetu wa Iringa ni kati ya mikoa ambayo ina vivutio vingi ambavyo kama Serikali ingekuwa na mkakati wa kutosha naamini mkoa wetu ungeweza kuiingizia Serikali pato kubwa sana na pia tungeweza kutengeneza ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa una mbuga ya Ruaha National Park, katika Afrika ni mbuga ya pili kwa ukubwa lakini miundombinu ya barabara ni mibovu sana na bado Serikali haijaweza kuona umuhimu wa kuweka barabara ya lami ili kuvutia watalii wengi kwenda katika mbuga hiyo. Bado Serikali haiwezi kuona umuhimu wa kujenga au kukarabati kiwanja cha ndege cha Nduli, ni vema sasa Serikali ingeweza kuzifanyia upembuzi yakinifu baadhi ya miradi kama ya barabra na viwanja vya ndege ambavyo ni changamoto katika kukuza utalii wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu eneo la Isimila Olduvai Gorge lingeweza kuongeza pato kubwa sana la utalii lakini halitangazwi na halina maboresho kabisa. Mkoa wetu una kaburi na fuvu la kichwa cha Mtwa Mkwawa, bado hakuna matangazo ya kutosha ili tupate utalii wa ndani na nje ya nchi ili tuongeze utalii na vijana wetu kupitia watalii watengeneze ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TANAPA, shirika hili ni kati ya baadhi ya mashirika na taasisi za umma zinazofanya vizuri sana katika sekta hii ya utalii lakini ni tatizo gani linasababisha Serikali kutokuweka bodi? Mambo mengi na changamoto nyingi zinakosa maamuzi kutokana na shirika kukosa bodi. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapojibu atoe ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia kwa wananchi wanaoliwa na mamba, kwa kuwa kumekuwa na vifo mara kwa mara kwa wananchi na hasa wanawake wamekuwa wakipata ajali wanapokwenda kufuata maji katika Mto Lukosi katika Wilaya ya Kilolo, Kata ya Ruaha Mbuyuni. Je, ni utaratibu gani unatakiwa kutumika ili wananchi waweze kupatiwa haki zao na je, ni kwa nini wasisaidiwe na Halmashauri kuvuta maji ya bomba katika Mto huo Lukosi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zinazojitokeza katika kutoa vibali vya uvunaji miti msitu wa Taifa wa Sao Hill, kumekuwa na malalamiko makubwa sana ya wananchi katika utoaji wa vibali vya kuvuna miti katika msitu wa Taifa wa Sao Hill. Ninaomba kujua utaratibu unaotumika na Serikali inatambua hilo? Je, ili kuondoa tatizo hilo nini mkakati wa Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wabunge tumekuwa tukiombwa kuchangia katika taasisi za elimu, afya na hata jamii, je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwapatia vibali hivyo vya uvunaji ili kuweza kusaidia jamii na Serikali katika kupunguza changamoto ambazo huwa zinajitokeza wakati tukiwa kwenye ziara za kikazi katika Majimbo na Mikoa kwa ujumla? Ninaomba kupatiwa jibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi kwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha hotuba yao hapa Bungeni ili tuweze kuijadili. Yapo mambo ambayo naomba kupatiwa ufafanuzi wa baadhi ya mambo na mengine kuishauri Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubadilishana wafungwa wa Tanzania na nchi nyingine. Naomba ufafanuzi kama upo uwezekano wa Watanzania ambao wamekwenda nchi nyingine wakapata makosa ya kuhukumiwa kifungo. Je, kuna uwezekano wa wafungwa hao kurudishwa kuja kufungwa hapa nchini au kama kuna uwezekano wa kubadilishana na wafungwa walio hapa nchini kwenda kufungwa katika nchi zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda kujua kama Watanzania walio nje wakakutwa na makosa, Serikali inawasaidia msaada wa
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
221
kisheria sababu najua wengine wanafungwa kwa sababu hawana uwezo wa kuweka mawakili wa kuwatetea, kama nchi msaada gani unatolewa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vya Watanzania waishio nje ya nchi: Hivi karibuni yamejitokeza matukio ya mauaji ya kutisha baadhi ya vijana wa Kitanzania wanaishi nchi za nje kama USA kuuawa kwa kupigwa risasi je, ni jitihada gani ambayo Serikali yetu inachukua kubaini hayo? Ningependa kujua jitihada za Serikali kuhusiana na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali kuwaunganisha wajasiriamali wa Tanzania kuingia ubia na makampuni ya China. Serikali ya Awamu ya Tano, sera yake kubwa kufufua na kujenga viwanda kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi na kuongeza ajira na kwa kuwa nchi ya China katika hilo ipo mbali sana ina viwanda vidogo vidogo na vikubwa. Napenda kujua Tanzania imejipanga vipi kuhakikisha inaingia ubia na makampuni ya China yatakayoweza kusaidia ukuaji wa viwanda vyetu nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata bahati ya kutembelea Ubalozi wa China na UK. Kwa kweli jengo la Ubalozi wa China lilikuwa lina hali mbaya sana. Je, ni utaratibu gani huwa unatumika katika kupeleka pesa za ukarabati wa majengo hayo kwa sababu ni aibu sana Mabalozi wetu kuishi katika mazingira mabaya na magumu. Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi kwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha hotuba yao hapa Bungeni ili tuweze kuijadili. Yapo mambo ambayo naomba kupatiwa ufafanuzi na mengine napenda kuishauri Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubadilishana wafungwa wa Tanzania na nchi nyingine. Naomba ufafanuzi wa kama upo uwezekano wa Watanzania ambao wamekwenda nchi nyingine wakapata makosa ya kuhukumiwa kifungo, je kuna uwezekano wa wafungwa hao kurudishwa kuja kufungwa hapa nchini au kama kuna uwezekano wa kubadilishana na wafungwa walio hapa nchini kwenda kufungwa katika nchi zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda kujua kama Watanzania waliopo nje ya nchi wakikutwa na makosa, Serikali inawapa msaada wa kisheria, kwa vile najua wengine wanafungwa kwa sababu hawana uwezo wa kuweka Mawakili wa kuwatetea, kama nchi ni msaada gani unatolewa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vya Watanzania waishio nje ya nchi; hivi karibuni yamejitokeza matukio ya mauaji ya kutisha baadhi ya vijana wa Kitanzania wanaoishi nchi za nje kama USA kuuawa kwa kupigwa risasi; je, ni jitihada gani ambayo Serikali yetu inachukua kubaini hayo? Ningependa kujua jitihada za Serikali kuhusiana na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali kuwaunganisha wajasiriamali wa Tanzania kuingia ubia na makampuni ya China. Serikali ya Awamu ya Tano, sera yake kubwa kufufua na kujenga viwanda kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi na kuongeza ajira. Kwa kuwa nchi ya China katika hilo ipo mbali sana ina viwanda vidogo vidogo na vikubwa, napenda kujua Tanzania imejipanga vipi kuhakikisha inaingia ubia na makampuni ya China yatakayoweza kusaidia ukuaji wa viwanda vyetu nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata bahati ya kutembelea Ubalozi wa Tanzania nchini China na UK, kwa kweli jengo la Ubalozi wa Tanzania China lilikuwa na hali mbaya sana. Je, ni utaratibu gani huwa unatumika katika kupeleka pesa za ukarabati wa majengo hayo kwa sababu ni aibu sana Mabalozi wetu kuishi katika mazingira mabaya na magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri Profesa Kabudi na watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea bajeti yao ili tuweze kuijadili. Kuna mambo ambayo nataka kuyapatia ufafanuzi wake na kushauri pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ucheleweshaji wa kesi za ubakaji; Mkoa wetu wa Iringa ni kati ya mikoa inayokabiliwa na idadi kubwa sana ya kesi ya ubakaji na ulawiti. Inasikitisha sana Bunge lililopita nilileta swali langu hapa Bungeni na niliweza kutoa takwimu ya mwaka 2016 kesi 217 lakini zilizoweza kufikishwa Mahakamani ni kesi 27 tu lakini kila mwaka katika mkoa wetu matukio ya ubakaji yanazidi kuongezeka. Napenda kujua mkakati wa Serikali kuhusiana na jambo hili ni kwa nini kusiwepo na Mahakama Maalum ya kushughulikia kesi hizi. Matukio haya yamekuwa yakiwaathiri watoto wetu kiakili pamoja na mama zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ucheleweshaji wa mabadiliko ya sheria zilizopitwa na wakati; baadhi ya sheria zetu hapa nchini zimekuwa ni za muda mrefu sana na zimepitwa na wakati na kusababisha baadhi ya sheria zetu hapa nchini kutoendana na mabadiliko na kasi ya maendeleo ya Taifa na kuonekana kuwa zimepitwa na wakati. Mara nyingi sana sisi Wabunge tumekuwa tukileta hoja zetu hapa Bungeni lakini bado hatupatiwi majibu ya kuridhisha. Kwa mfano, 12 Aprili, 2017 nilileta swali kuhusiana na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 lakini bado majibu yake hayaridhishi. Je, ni lini sasa Serikali italeta hoja ya kufanya marekebisho ya kuboresha baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufinyu wa bajeti, Wizara hii ni muhimu sana na imekuwa na malalamiko mengi kwa wananchi kutomaliza kesi zao au kuchukua muda mrefu sana. Pia miradi mingi kutokamilika kwa wakati pamoja na bajeti yao kuwa kidogo sana lakini pia pesa yao imekuwa ikicheleweshwa sana na kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati hivyo kusababisha miradi hiyo kutumia pesa nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja hii ya Wizara Fedha. Vilevile na mimi nimuunge mkono mjumbe aliyepita kwamba Mheshimiwa Naibu Spika uzi ni huo huo, sheria ni msumeno. Lazima Bunge letu lifuate sheria na kanuni ambazo tumejitungia sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wake na watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea hii bajeti ili tuweze kuijadili. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ambaye kwa kweli utumbuaji wake majipu umesaidia sana kuongeza kipato TRA na kwa kweli hakuna mtu ambaye hajui kwamba tumbuatumbua majipu imeweza kutuongezea kipato kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu naanza na kitabu cha Waziri ukurasa wa 59 kuhusu Shirika la Bima la Taifa (NIC). Kwa kweli nina masikitiko makubwa sana na inaniuma sana. Hili Shirika la Bima lilikuwa shirika ambalo lilisaidia sana nchi hii, wafanyakazi wengi waliweza kuajiriwa, lilikuwa na majengo mengi na mali nyingi sana ambazo leo hii lingeweza pia kuongeza pato kubwa sana katika nchi hii. Hata hivyo, bado Serikali haijawa na mpango haswa wa kuhakikisha kwamba hili shirika linafufuka ili liweze kuwa chanzo kikubwa sana cha mapato katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika bajeti iliyopita ya mwaka 2015/2016, aliyekuwa Waziri wa Fedha alipokuwa anasoma bajeti yake alituambia kwamba Serikali ina mpango wa kuongezea uwezo Shirika la Bima la Taifa kwa Serikali kukatia bima mali zake zote ikiwa ni pamoja na za taasisi na TAMISEMI kupitia shirika hili. Mbona sasa hakuna mpango wowote wa kuhakikisha kwamba haya mashirika yanakatiwa bima katika Shirika hili la Bima? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuamini mpaka sasa hivi hili shirika halina hata bodi ya wafanyakazi, shirika hili Mkurugenzi wake Mkuu na Wakurugenzi wengi sana wanakaimu tu, sasa kweli hili shirika litajiendeshaje kama bado halijajiwekewa mkakati kama huo? Tuna taasisi karibu 200 katika nchi yetu lakini katika kitabu hiki amesema taasisi 15 tu ndiyo ambazo zinatumia hili Shirika letu la Bima ya Taifa. Niipongeze sana Wizara ya Nishati kwamba imeweza kukata bima katika bomba lake la gesi linalotoka Mtwara mpaka Kinyerezi. Najua ni mapato makubwa sana yanapatikana kwa kukatia bima kwenye Shirika letu la Bima la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua siku zote huwa tunawasifia Wachina wanaongeza pato na sisi tulienda kweli tukaona Wachina jinsi walivyokuwa wazalendo. Kama nchi hii haitakuwa na uzalendo mashirika yetu mengi sana yatakufa. Kwa sababu ipo TTCL, Posta bado hatutumii mashirika yetu vizuri, tunaona mashirika na taasisi za Serikali zinaenda kukata bima sehemu nyingine. Unaona tu Wachina wamekuja hapa wamewekeza lakini wameleta pia mashirika yao ya bima, wameleta pia walinzi wao, wameleta kila kitu mpaka wafagiaji. Lazima iwepo sheria kwamba haya mashirika yetu ya bima yatumike pia ili kuongeza Pato la Taifa letu. Nitamuomba Waziri atakapokuwa anajibu angalau atupe mkakati kwamba ana mkakati gani wa kuyafufua haya mashirika na ni kwa nini mpaka leo hii hakuna hata bodi ya wafanyakazi kwenye hili shirika na Wakurugenzi bado wanaendelea kukaimu siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia niendelee kuunga mkono kuhusiana na ile Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2011. Wabunge wengi sana siyo leo tu, siku zote tumekuwa tukiisema hii sharia, kwa nini hailetwi, kuna kitu gani kimejificha hapa nyuma? Kwa sababu hii sheria ingeletwa leo hii tusingekuwa tunalalamika, hii sheria ndiyo mkombozi. Naomba Mheshimiwa Waziri atujibu, tulipewa matumaini kwamba katika Bunge hili hii sheria ingekuja tungeweza kuibadilisha, mbona hakuna chochote, kuna tatizo gani katika uletaji wa hii sheria hapa Bungeni?
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu VICOBA, hakuna siri VICOBA ni mkombozi wa sisi wananchi hasa wanawake. VICOBA hii imetufichia mambo mengi sana, wanawake walikuwa wanadhalilika sana kwenye taasisi nyingine za fedha kwa kuchukuliwa mali zao lakini VICOBA imekuwa kama ndiyo mkombozi. Tuliambiwa kwamba VICOBA inaendeshwa bila kusimamiwa na sheria yoyote ya fedha na tuliambiwa sheria ingeletwa hapa ili tuweze kuipitisha lakini hakuna sheria iliyoletwa mpaka leo. Sasa wanatuambia nini kuhusiana na VICOBA kuendeshwa bila sheria yoyote ya fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu malipo ya wazabuni. Wazabuni wetu wanapata shida sana, ningeomba kujua ni lini Serikali italipa malipo wazabuni wanaozidai kwa muda mrefu sana Halmashauri na Wizara zetu. Wamekuwa wakizungushwa mno, wanaambiwa kwamba malipo yao yapo Hazina lakini wakienda Hazina bado hawalipwi, lakini hao wazabuni bado pia wanadaiwa kodi za Serikali. Sasa tutakusanyaje kodi kama hatuwalipi hawa wazabuni, watafanyaje biashara? Hawa wazabuni wamekuwa wakichukua mikopo kwenye benki, wanadaiwa riba, halafu TRA bado wanawatoza tena kwa nini wamechelewesha kulipa kodi zao. Serikali hii imesema kwamba itawasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati, huko ndiyo kuwasaidia wazabuni? Kwa sababu wazabuni walio wengi ndiyo ambao wanatoa zabuni kwenye Halmashauri zetu na kwenye Wizara zetu. Ningeomba kwa kweli uwepo mkakati wa kushughulikia suala hili kwa sababu ni muda mrefu sana wazabuni wamekuwa wakipata matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kuzungumzia kuhusu ucheleweshaji wa pesa za miradi katika Halmashauri na Wizara zetu. Huu ucheleweshaji siyo wa mara moja, siku zote pesa za maendeleo ya miradi zimekuwa zikicheleweshwa sana na ucheleweshaji huu wa miradi umekuwa ukisababisha miradi ile sasa inafanyika kwa gharama kubwa sana. Kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Iringa kuna ule mradi wa machinjio wa kisasa, ulitakiwa tuujenge kwa pesa kidogo sana, lakini kadri fedha ambavyo zinacheleweshwa kuletwa ule mradi pia gharama zake zinaongezeka. Pia ule mradi kama tungekuwa tumeumaliza kwa wakati ungeweza kusaidia chanzo kikubwa cha mapato kwa sababu tunategemea kwamba tutapata mapato hata ya dola kwa sababu tutasafirisha zile ngozi nje ya nchi.
Vilevile tulikuwa tunategemea kuajiri wafanyakazi wengi sana katika Halmashauri yetu kupitia mradi ule. Sasa utaratibu gani huwa unatumika, ni kwa nini hizi pesa za miradi zinacheleweshwa sana? Karibu sehemu zote watu wanalalamika ucheleweshaji wa pesa katika miradi ya Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi sana wamezungumzia kuhusu riba kubwa inayotozwa na baadhi ya taasisi za fedha. Taasisi nyingi sana zimekuwa zikitoza riba kubwa sana na wananchi wengi sana wanashindwa kufanya biashara.
Wananchi wengi sana sasa hivi wakichukua mikopo benki mali zao zinauzwa, imesababisha wananchi wengi sana kupoteza maisha au kupata hata pressure kwa sababu mikopo halipiki dhamana zinachukuliwa. Ukichukua sasa hivi mkopo benki ujue kwamba wewe umeajiriwa na benki hupati chochote zaidi tu utafanya ile kazi, kama umechukua kwa ajili labda ya uzabuni basi utafanya kazi ya uzabuni, zabuni yenyewe wanakusumbua.
Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie upya hizi riba ambazo mabenki yetu yamekuwa yakitoza, ikae na ione ni kiasi gani ambacho kinaweza kikasaidia. Kwa sababu biashara ni ngumu sana, watu wanatozwa katika majengo, kuna tozo nyingi mno ambazo ukienda kuchukua mkopo unaona riba imekuwa kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie kuhusu hizi mashine za EFDs. Wengi wamezungumzia suala hili, tulitegemea kwamba hizi mashine zingekuwa mkombozi, tungekusanya kodi nyingi sana. Tatizo utaona labda mtu mmoja au wawili ndiyo wana zile mashine wengine hawatumii, kwa hiyo, wengine wanalipa kodi wengine hawalipi, naomba hili suala liangaliwe. Pia Serikali ilisema ingetoa hizi mashine bure sijui zoezi hili limefikia wapi, ningependa kujua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri na hasa ya ziara zake mikoani na busara anazozitumia katika utatuzi wa changomoto mbalimbali. Pia niwapongeze Mawaziri Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Antony Mavunde na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nianze mchango kwa mambo yafuatayo; ucheleweshaji wa pesa za maendeleo katika miradi ya maendeleo. Kutokana na pesa za miradi kucheleweshwa katika Halmashauri zetu kunasababisha miradi mingi kutokamilika kwa wakati na pia kuongezeka kwa gharama za miradi variation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Manispaa yetu ya Iringa iliyopo katika Jimbo la Iringa Mjini kuna mradi wa machinjio ya Ngerewala. Mradi huu mzuri lakini umeanza toka mwaka 2007. Mradi huu ukikamilika ungeweza kutoa ajira kwa wananchi wa Iringa zaidi ya 200.
Mheshimwa Spika, nashauri ni vema Serikali ingetoa pesa katika mradi huu kiasi cha shilingi bilioni moja ili Halmashauri isiingie kwenye mkataba mbovu wa miaka 25. Pia atafutwe mtaalam mshauri ili asaidie mradi huu uendeshwe kwa faida kwa sababu hiki ni chanzo kizuri sana
cha mapato. Mfadhili akipata atapandisha bei ya uchinjaji na kusababisha wachinjaji kuchinjia mtaani na inaweza pia kusababisha bei ya nyama kupanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Jamii, nipongeze jitihada zinaofanywa na mifuko ya jamii ya NSSF, LAPF, PPF, GEPF, PSPF na NHIF kwa kukubali wito wa kuanza kujenga viwanda ikiwemo ufufuaji wa kinu cha kusaga mahindi. Lakini niiombe Serikali iweze kulipa madeni inayodaiwa na mifuko hiyo ili viwanda vijengwe ambavyo vitasaidia kukuza uchumi na kuongeza ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fao la kujitoa, pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kujali wafanyakazi pale wanapostaafu au wanapoacha kazi, lakini sheria ya kuzuia wafanyakazi kujitoa kwenye mifuko pale ajira zao zinapokomaa hadi mfanyakazi atimize miaka 60 hili ni tatizo kubwa sana kwa sababu ajira za wafanyakazi zimetofautiana. Mfano sekta ya ujenzi, sekta ya kilimo na sekta ya kazi za majumbani si rahisi wafanyakazi wa sekta hizo kufikisha miaka 60 tunashauri sheria hiyo itofautishe sekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la watu wenye ulemavu, niipongeze Serikali kwa kuwatambua watu wenye ulemavu nchini lakini bado wanachangamoto hasa katika suala la usafiri, bado vyombo vya usafiri sio rafiki, ni lini Serikali italiangalia hili? Pia ni kwa nini katika ile mikopo ya Halmashauri na wao wasitambulike kutengewa asilimia zao katika asilimia tano ya vijana na akina mama? Walemavu wengi ni wajasiriamali lakini hawakopeshwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumza kuhusu kumtua ndoo kichwani mwanamke. Katika Mkoa wetu wa Iringa limekuwa ni tatizo kubwa sana hasa katika maeneo ya vijijini. Kinachosikitisha Serikali imekuwa ikitumia pesa nyingi sana kwa miradi ya maji lakini maji hayatoki
kama miradi ya Ilindi, Ng’uruhe, Ihimbo, Iparamwa Ruaha Mbuyuni na Mkosi. Lakini mkoa wetu una Mto Ruaha, Lukosi na Mtitu na chanzo cha Mto Mgombezi. Ni kwa nini mito hii isitumike katika kusambaza maji kuliko hiyo miradi ya visima iliyotengwa. Je, Serikali inawachukulia hatua gani hawa? Mheshimiwa Mwenyekiti, Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu niliochangia kwa kuongea, napenda pia niongeze mchango wangu kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia magari ya zimamoto katika viwanja vya ndege. Viwanja vingi vina changamoto kubwa sana ya magari ya kuzima moto kikiwepo na Kiwanja cha Nduli, Mkoa wa Iringa. Gari lililoletwa Mkoa wa Iringa lilitokea Kiwanja cha Tabora likiwa bovu na halijawahi kufanya kazi toka limeletwa. Hivyo kiwanja hakina gari la kuzimia moto, gari linalotumika ni la Ofisi ya Zimamoto kama kukiwa na ugeni wa viongozi na sasa hivi gari lile limepata ajali. Napenda kufahamishwa utaratibu unaotumika kupeleka haya magari katika viwanja au kama kuna vigezo vinavyotumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nizungumzie TCRA na mtambo wa TTMS. Nashukuru sana kwa uongozi wa TCRA kwa kutupatia semina ya uelewa wa taasisi yao ikiwemo na matumizi ya huu mtambo wa TTMS. Pamoja na huu mtambo kuwa ndiyo mtambuzi wa namna bora ya kupata taarifa za makusanyo ya makampuni ya simu ili Serikali iweze kutoza kodi stahiki kutokana na miamala ya fedha inayofanyika kupitia simu za mikononi, je, ni lini sasa ule mfumo wa Revenue Assurance Management System (RAMS) utafungwa? Tulipotembelea TCRA tuliambiwa kuwa wana mazungumzo na mkandarasi, nini mkakati wa Serikali kuhusiana na hilo? Napenda kujua kuhusu suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, niongelee kuhusu madeni ya TTCL. Pamoja na Serikali kumiliki hisa kwa 100% lakini bado shirika hili linatakiwa liendelee kujiendesha. Je, ni lini Serikali itaweka mkakati wa kuhakikisha madeni yote yanalipwa, sababu imeamua kulipa madeni yake? Wizara zote zilishafanya uhakiki wa madai, je, haya madeni ya TTCL Wizara wameshaanza kulipa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni Internet Data Center. Niipongeza Serikali kwa ujenzi wa kituo hiki kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi kumbukumbu. Hata hivyo, ukiangalia katika bajeti zetu kuna baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali pia zinatenga bajeti kwa ajili ya kuwa na data center zao. Je, ni kwa nini kituo hiki kisitumike kwa taasisi zote za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ni TAZARA. Nataka kujua ni lini ule upungufu wa ile Sheria Na. 23 ya mwaka 1975 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 4 ya mwaka 1995 itafanyiwa marekebisho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara hii. Kwanza kabisa nianze kutoa pongezi zangu kwa kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Naibu Waziri Engineer Ngonyani, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa taasisi zote katika Wizara hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, na mimi kwa kweli kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu nianze kupongeza kazi nzuri ambazo zimefanywa na Serikali ya Awamu hii ya Tano kama vile ujenzi wa Daraja la Kigamboni, ujenzi wa mabweni UDSM, uzinduzi wa ujenzi wa reli ya kati, uzinduzi wa miradi ya flyovers, TAZARA na Ubungo, Serikali kumiliki asilimia 100 TTCL, mradi wa ujenzi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam na ununuzi wa ndege ya ATCL na kubwa kuliko zote, Serikali kuanza kulipa wakandarasi na washauri shilingi bilioni 788 kutoka katika deni la shilingi bilioni 930.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali hili zoezi liwe endelevu ili miradi yetu ikamilike kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuzungumzia kuhusu ujenzi wa viwanja vya ndege. Naipongeza Serikali kuendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege kote nchini, ni pamoja na jengo lile la abiria Terminal III Kiwanja cha Mwalimu Nyerere.
Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa tulipotembelea tulikuta kuna changamoto ya pesa kutopelekwa kwa wakati, sasa naiomba Serikali ipeleke pesa kwa wakati ili jengo liweze kukamilika na liendane na ununuzi wa ndege zetu. (Makofi)
Niendelee kupongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja chetu cha Nduli. Hiki kiwanja kwa kweli tumekuwa tukikidai kwa muda mrefu, sasa tunaishukuru Serikali angalau imeweza kutenga pesa na sisi kiwanja chetu cha Nduli sasa kitajengwa na najua hata Bombardier sasa itatua pale. Nitoe tu ushauri, kwamba pamoja na kuwa huu mradi tayari wananchi wa pale wameshaukubali sasa waweke alama katika yale maeneo ambayo upanuzi utafanyika ili yale maeneo yasiweze kuendelezwa, kwa sababu yakiendelezwa wakati wa kulipa fidia itakuwa tatizo kubwa sana.
Vilevile niiombe Serikali sasa, kuna viwanja vingi sana havina hati miliki kikiwemo hiki cha Iringa. Kwa hiyo, sasa itengeneze hati ili wananchi wasiendelee kuvamia katika hivi viwanja vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na ujenzi wa barabara nchini. Niipongeze sana Serikali kwa kuendelea na ujenzi wa miradi ya barabara kwa kiwango cha lami.
Naomba niunge mkono ushauri, Mheshimiwa Serukamba alipokuwa akichangia amesema kwamba angalau zile barabara za Wilaya TANROADS iendelee kuzihudumia, kwa sababu tunaona hata sisi wenyewe tulipokuwa tunachangia watu wengi sana wanalalamikia barabara zilizopo katika vijiji kwamba miradi haiendi kwa wakati na vilevile tumeona kwamba hakuna wataalam wengi kwenye Halmashauri zetu. Kwa hiyo, kama barabara hizi zitamilikiwa na TANROADS tuna imani kabisa zitakwenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia labda uwepo upembuzi yakinifu katika miradi ya barabara zetu, kwamba zile za kiuchumi ziweze kupewa kipaumbele, kwa sababu tumekuwa na barabara nyingi za kiuchumi katika halmashauri zetu ambazo zinakuwa hazijengwi kwa kiwango cha lami kiasi kwamba sasa wakati wa mvua malori yanakwama. Kwa mfano pale Iringa tuna miti, kama Mgololo kule unaona wakati wa mvua malori yanakwama na kuna ajali nyingi sana zinatokea.heshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile ubovu huu wa barabara hasa vijijini unasababisha hata vifo vya akina mama na watoto. Kwa sababu ya miundombinu ambayo ipo katika barabara zetu zilizopo vijijini wakati wa mvua akina mama wengi hawafikiwi. Kwa hiyo, mimi niombe hizi barabara zipewe kipaumbele ili kupunguza pia vifo vya akina mama na watoto katika vijiji vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie pia barabara zilizopo katika Mkoa wetu wa Iringa. Tunashukuru sana Serikali katika bajeti hii imeweza kutenga pesa kuanza ujenzi wa barabara inayokwenda katika mbuga ya Ruaha. Muda mrefu sana tumekuwa tukiizungumzia barabara hii kwa sababu utalii utaongezeka katika mkoa wetu na mikoa iliyopo katika Nyanda za Juu Kusini. Kwa hiyo, mimi nishukuru kwamba japo kuwa wametenga pesa, lakini sasa ujenzi ufanyike kwa sababu kutenga pesa ni kitu kingine na kuanza ujenzi ni kitu kingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara za kiuchumi kama barabara ya Mafinga – Mgololo, Kinyanambo
– Isalavanu – Saadani – Rujewa, kuna Kiponzelo – Wasa, kuna barabara ile ya Kilolo mpaka Iringa Mjini. Tunaomba Serikali yetu izipe kupaumbele kwa sababu uchumi wa mkoa wetu unazitegemea sana hizi barabara ambazo ziko katika wilaya hizo nilizozitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie watu wenye ulemavu. Sisi wote hapa ndani ni walemavu watarajiwa. Nilipoongea na watu wenye ulemavu katika Mkoa wangu wa Iringa yapo mambo ambayo wanalalamikia hasa miundombinu katika magari. Inaonekana kwamba watu wengi wenye ulemavu bado Serikali haijawaangalia. Watu wanakuwa na baiskeli lakini hawawezi kupandisha kwenye gari kwa sababu hakuna miundombinu inayoruhusu mtu mwenye ulemavu kuweka baiskeli yake kwenye gari lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile majengo yetu bado si rafiki sana na watu wenye ulemavu kiasi kwamba yanasababisha hawa watu wenye ulemavu kukosa hata huduma nyingine. Utakuta mama mwenye ulemavu ni mjamzito anashindwa kupandisha ngazi kwenda kumuona daktari. Kwa hiyo, mimi ningeomba sheria iwepo ili watu wenye ulemavu pia wazingatiwe wakati wanajenga haya majengo yote yakiwepo hata majengo ya shule zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile TCRA labda iangalie, pia hata katika televisheni zetu bado hawajaweka watu kutafsiriwa zile lugha za watu wenye ulemavu. Kwa hiyo mambo yote hayo yazingatiwe. Hakuna pia michoro kwenye barabara kuonesha watu wenye ulemavu wanapopita, kwa hiyo mimi naomba haya mambo yazingatiwe kwa sababu sisi wote ni walemavu watarajiwa, huwezi kujua wewe lini utakuwa mlemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuzungumzia kuhusu Shirika la Posta Tanzania. Kwa sababu Serikali imeanza kuyafufua mashirika nchini, ni kwa nini sasa Serikali isitoe mtaji wa kutosha ili hili shirika liweze kujiendesha. Shirika hili lilikuwa na deni kama la shilingi bilioni 5.1 ambapo Serikali imelipa shilingi bilioni 2.5 tu kwa shirika.
Sasa mimi ningeomba sasa hivi hili shirika lizingatiwe kwa sababu lilikuwa lina mali nyingi sana hapo zamani. Kwa hiyo mimi naomba wapatiwe pesa zao zilizobaki ili na lenyewe liweze kujiendesha ili wafanyakazi wale pia waweze kufanya kazi kwa kujiamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nizungumzie mradi wa postal code na symbol za posta. Huu mradi kwa kweli umekuwa mara nyingi sana; kwanza ni muhimu sana kwa sasa hivi kwa sababu kwanza makazi yatatambulika, na isitoshe hatakukusanya kodi tutakusanya kwa urahisi kama nyumba zitakuwa zinatambulika kutokana na hizi symbol za posta, lakini mara nyingi sana imekuwa ikitengewa pesa kidogo sana kila mwaka, mimi naomba safari hii…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kuunga mkono hoja.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Naibu Waziri Mheshimiwa Kigwangalla na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha hotuba yao hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya ni moja ya sekta nyeti Tanzania inayosimamiwa na Wizara ya Afya pamoja na hospitali zote za rufaa, hospitali za wilaya pamoja na vituo vya afya na zahanati zilizopo chini ya Serikali za Mitaa, Manispaa na Wilaya hizi zipo chini ya Wizara ya TAMSEMI, pamoja na kwamba zote zinapatiwa miongozo ya kiutendaji kutoka Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na umuhimu wa Idara ya Afya katika Mkoa wetu wa Iringa, inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

i) Chumba cha uangalizi wa wagonjwa wa nje wa dharura (OPD) hivyo kusababisha msongamano mkubwa katika wodi kwa zile huduma zinazohitajika uangalizi wa muda mfupi.

(ii) Wastani mdogo wa daktari kwa wagonjwa. Hivyo kufanya kuwa na msongomano mkubwa katika vyumba vya madaktari wachache wanapokuwa zamu, hivyo kuongeza work load kwa madaktari.

(iii) Kuna wodi nzuri za watoto zilizojengwa kwa ufadhili wa Hospitali ya Vicensa ya Italy na mzalendo mmoja familia ya ASAS lakini hakuna Daktari Bingwa wa Watoto (Pediatrician) pamoja na idadi kubwa ya watoto wanaolazwa hospitalini hapo.

(iv) Hakuna kitengo cha ENT (sikio, pua na koo) wala Daktari wa ENT. Hivyo case zote za ENT lazima zipewe rufaa au kusubiri visiting doctor ambayo inakuwa ni kero kwa wagonjwa wenye matatizo yanayohusiana na tatizo hilo.

(v) Vitendea kazi muhimu wodini ni vichache kama vile oxygen cylinder na oxgen concentrators, pulsonetor za kupima kiwango cha oxygen kwa mgonjwa, BP machine hazina uwiano inaostahili kwa ugonjwa (wodi nzima inakuwa na mashine moja tu), vipimo vya sukari kwa wagonjwa wa sukari waliopo wodini wanaohitaji uangalizi wa kina.

(vi) Kitengo cha afya ya akili hakikidhi haja na mahitaji ya wagonjwa wa afya ya akili kwa sababu kina vyumba vinne yaani viwili kwa wanaume na viwili kwa wanawake, vyenye uwezo wa kukaa na wagonjwa wawili kila chumba, hivyo uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wa akili ni wagonjwa wanne tu, ambavyo ni hatari kwa hospitali yenye kiwango cha Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ukizingatia Mkoa.

(vii) Wagonjwa wanaostahili msamaha hawapati huduma za dawa kama inavyostahili kutokana dawa nyingi kutokuwepo hospitalini, hivyo kusababisha shida zaidi kwa wagonjwa wasio na uwezo, wazee na wenye magonjwa ya kudumu kama sukari, akili, TB na HIV.

(viii) Nyumba za madaktari zaidi ya asilimia 85 ya madaktari na wahudumu wengine wa afya wanakaa maeneo ya mbali na hospitali kutokana na kukosekana nyumba hasa nyakati za usiku kwa wagonjwa wetu.

(ix) Kukosekana kwa huduma zingine za msingi kama CT Scan, MRI, ECG, ECHO katika hospitali ya Mkoa hivyo kusababisha rufaa zingine zisizokuwa na lazima ambapo ni kero kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo.

(x) Mifumo ya ki-eletronic inayowezesha daktari kupata majibu ya mgonjwa kutoka maabara na taarifa nyingine za mgonjwa kwa haraka kama ilivyo hospitali nyingine za private.

(xi) Pia dawa muhimu hazipo hospitalini kila wakati, hivyo kusababisha wagonjwa kuhangaika kwenda kutafuta maduka binafsi na kero zaidi inakuwa wakati wa usiku ambapo hayo maduka binafsi yamefungwa, inaweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya Wanawake; niipongeze Serikali kwa kuweka dirisha la kuweza kuhudumia wananchi wa Mkoa wa Iringa, lakini ili ile dhamira ya kuanzisha benki hii kwa ajili ya wanawake ipate kutimia. Pia kuwepo na mobile agency kwa ajili ya huduma hii kufikishwa vijijini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vituo vinavyolea watoto yatima; pamoja na wamiliki wa vituo hivi vya watoto yatima kuisaidia Serikali katika wimbi hili la watoto yatima na watoto wa mtaani, lakini kuna changamoto nyingi zilizopo katika vituo hivi. Kuna vituo havina hata uwezo wa kuwatibu watoto hawa wanapougua au kupata ajali. Hivyo ni vema Serikali ikaweka utaratibu wa kusaidia vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nianze na kumpongeza Dkt. Harrison Mwakyembe Waziri, Naibu Waziri Anastazia Wambura, Makatibu Wakuu na watendaji wa Wizara kwa kuwasilisha hotuba hapa Bungeni ili tuijadili. Yapo mambo ambayo nahitaji kuyachangia ambayo ni:

Moja, ufinyu wa Bajeti; siku zote Wizara hii imekuwa ikipatiwa bajeti finyu sana na kusababisha Wizara hii kufanya kazi zake katika wakati mgumu sana na mbaya zaidi pamoja na kupatiwa bajeti kidogo lakini hata bajeti iliyopangwa haipelekwi kwa wakati hivyo kusababisha Miradi mingi iliyopangwa kutokamilika kwa wakati. Ni vema Wizara hii ingepewa kipaumbele kwa sababu pia imekuwa ikifanya kazi ya vijana wetu inayohusiana na sanaa.

Mheshimiwa Spika, uvamizi wa viwanja vya michezo katika Halmashauri, vijana wetu wanakosa haki yao ya msingi kutokana na uvamizi uliofanywa katika viwanja vilivyoachwa wazi kwa ajili ya michezo kuvamiwa na kugawiwa kwa watu kujenga. Nakumbuka Serikali ilitoa tamko kuwa waliovamia viwanja vya wazi waondolewe lakini mpaka leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Serikali kwa ajili ya jambo hilo. Hivyo, ningependa kupatiwa ufafanuzi wa agizo hilo la Serikali sababu vijana wengi hawana maeneo ya michezo.

Mheshimiwa Spika, Vazi la Taifa; ningependa kujua mpango wa Serikali kuhusiana na vazi la Taifa, nakumbuka Serikali ya Awamu ya Nne ilishawahi kutuletea taarifa kuhusiana na mchakato wa kupata vazi hilo lakini mwisho wake mpaka leo hatujui limefikia wapi.

Mheshimiwa Spika, (TBC) Shirika la Utangazaji la Taifa; naomba Serikali ifanye jitihada za kutosha kuhakikisha TBC inapatiwa pesa ya kutosha ili iweze kusikika nchi nzima. Tunasikia vibaya kuona maeneo ya mipakani wanapata mawasiliano toka nchi jirani. Pia vitendea kazi viboreshwe viendane na hadhi ya chombo cha Serikali.

Mheshimiwa Spika, watu wenye ulemavu; naomba Serikali iwatendee haki watu wenye ulemavu kwa kuweka Sheria ya kuhakikisha wamiliki wote wenye Television wanaweka watafsiri wa lugha katika Television ili watu wenye ulemavu wa kusikia nao waweze kuona. Pia itawasaidia kupata ajira kwa watu waliosomea kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, michezo ya UMISETA; naiomba Serikali yetu iweke kipaumbele kikubwa sana katika kutenga pesa kwa ajili ya michezo hiyo ili tuweze kuibua vipaji vya watoto wetu ili tuviendeleze kwa ajili ya kusaidia nchi hii kwa upande wa maendeleo ya michezo. Michezo ni ajira, michezo ni afya na michezo inajenga mahusiano.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu; Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla na Watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha vizuri hotuba yao hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya ni moja kati ya sekta nyeti Tanzania inayosimamiwa na Wizara ya Afya pamoja na hospitali zote za rufaa, hospitali za wilaya pamoja na vituo vya afya na zahanati zilizopo chini ya Serikali za Mitaa (Manispaa na Mitaa). Hizi zipo chini ya Wizara ya TAMISEMI pamoja na kwamba zote zinapata miongozo ya kiutendaji kutoka Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na umuhimu wa Idara hii ya Afya, Mkoa wetu wa Iringa unakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

(i) Kukosekana kwa chumba cha uangalizi wa wagonjwa wa nje wa dharura OPD (Casuality/Emergence) hivyo kusababisha msongamano mkubwa wodini kwa zile huduma zinazohitaji uangalizi wa muda mfupi;

(ii) Uwiano mdogo wa daktari kwa mgonjwa, hivyo kufanya kuwa na msongamano mkubwa katika vyumba vya Madaktari wachache wanaokuwa zamu na kuongeza workload kwa Madaktari;

(iii) Kuna wodi nzuri za watoto zilizojengwa kwa ufadhili wa Hospitali ya Vicensa ya Italia na mzalendo mmoja, familia ya ASAS, lakini hakuna Daktari Bingwa wa watoto (pediatrician) pamoja na idadi kubwa ya watoto wanaolazwa hospitalini hapo;

(iv) Hakuna Kitengo cha ENT (sikio, pua na koo) wala Daktari wa ENT hivyo, case zote za ENT lazima zipewe rufaa au kusubiri visiting doctor ambapo ni kero kwa wagonjwa wenye matatizo hayo;

(v) Vitendea kazi muhimu wodini ni vichache kama vile oxygen cylinder na oxygen concentrators, pulsometor za kupimia kiwango cha oxygen kwa wagonjwa, BP machines hazina uwiano unaostahili kwa ugonjwa (wodi nzima inaweza kuwa na mashine moja tu) na vipimo vya sukari kwa wagonjwa wa sukari waliopo wodini wanaohitaji uangalizi wa kina;

(vi) Kitengo cha Afya ya Akili hakikidhi haja na mahitaji ya wagonjwa wa afya ya akili kwa sababu kina vyumba vinne yaani viwili kwa wanaume na viwili kwa wanawake vyenye uwezo wa kukaa na wagonjwa wawili kila chumba. Hivyo, uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wa akili ni wagonjwa nane tu ambayo ni hatari kwa hospitali yenye kiwango cha Hospitali ya Mkoa ya Rufaa;

(vii) Wagonjwa wanaohitaji msamaha hawapati huduma za dawa kama inavyostahili kutokana na dawa nyingi kutokuwepo hospitalini. Hali hii husababisha shida zaidi kwa wagonjwa wasio na uwezo, wazee na wenye magonjwa ya kudumu (sukari, akili, TB na HIV);

(viii) Nyumba za Madaktari, zaidi ya 85% ya Madaktari na wahudumu wengine wa afya wanakaa maeneo ya mbali na hospitali kutokana na kukosekana nyumba. Hii ni changamoto hasa inapohitajika huduma ya dharura kwa mgonjwa hasa nyakati za usiku;

(ix) Kukosekana kwa huduma nyingine za msingi kama CT Scan, MRI, ECG, ECHO katika Hospitali ya Mkoa na kusababisha rufaa nyingine zisizokuwa na lazima ambapo ni kero kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo;

(x) Kukosekana kwa mifumo ya kielektroniki inayowezesha daktari kupata majibu ya mgonjwa kutoka maabara na taarifa nyingine za mgonjwa kwa haraka kama ilivyo hospitali nyingine za private;

(xi) Kila wakati kukosekana kwa dawa muhimu hospitalini na kusababisha wagonjwa kuhangaika kwenda kutafuta dawa kwenye maduka ya watu binafsi na kero zaidi inakuwa wakati wa usiku ambapo na hayo maduka binafsi yanapokuwa yamefungwa, inaweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Benki ya Wanawake. Niipongeze Serikali kwa kuweka dirisha la kuweza kuhudumia wananchi wa Mkoa wa Iringa. Hata hivyo, niiombe Serikali itoe mtaji wa kutosha ili ile dhamira ya kusaidia benki hii kwa ajili ya wanawake ipate kutimia. Pia nashauri kuwepo na mobile agency kwa ajili ya huduma hii kufikishwa mpaka vijijini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu vituo vinavyolelea watoto yatima. Pamoja na wamiliki wa vituo hivi vya watoto yatima kuisaidia Serikali katika wimbi hili la watoto yatima na watoto wa mtaani lakini kuna changamoto nyingi zilizopo katika vituo hivi, kuna vituo havina hata uwezo wa kuwatibu watoto hawa wanapougua au kupata ajali. Hivyo, ni vema Serikali ikaweka utaratibu wa kusaidia vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Maghembe, Naibu Waziri, Engineer Ramo Makani, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea bajeti yao ili tuweze kuijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Wanyama ya Ruaha National Park ni hifadhi ya pili kwa ukubwa katika Afrika na hifadhi yenye wanyama wengi sana. Cha kushangaza hifadhi hii barabara inayoenda katika mbuga hii haina lami na kiwanja cha ndege cha Iringa hakuna ndege kubwa inayotua katika kiwanja hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijajua Wizara hii inafanya juhudi gani kuhakikisha miundombinu ya kuwezesha watalii wanaofika na kufanya matangazo ya kutosha ili tupate watalii wa kutosha? Ni kwa nini Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Serikali haiwekezi kama ilivyo Kaskazini? Kwani kuna vivutio vingi sana. Ni vizuri Serikali ingetupatia mkakati wa kuendeleza mbunga hiyo na utalii wa Nyanda za Juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kitabu kilichotolewa na TFS kilichotoa mwongozo wa kutoa vibali, tunashukuru kwa kutangulia kutoa kipaumbele kwa wenye viwanda na wananchi watakaozunguka msitu; lakini nitoe ushauri wangu kwa Serikali kuwa katika mwongozo wake ungeongeza na yale makundi maalum; makundi ya akina mama wajane, akina mama wenye vyama vinashughulikia makundi ya kijamii. Kwa sababu tumeshuhudia mara nyingi wananchi wanaozunguka msitu hawafaidiki na rasilimali hiyo, wakati wao ndio walinzi wakuu wa mazingira hayo, hata wakati mwingine moto ukitokea wanakuwa wakitoa msaada mkubwa. Naiomba Serikali jambo hilo liangaliwe tena na tupatiwe majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie upya suala la fidia kwa wananchi wanaopatwa na maafa. Kwa mfano, Mkoa wa Iringa kuna wananchi walipata matatizo ya kuuawa na mamba wengine kupata ulemavu.

Pia tembo walileta uharibifu wa mali na vifo katika Kata ya Nyanzwa, lakini tunashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Engineer Ramo alishawahi kufanya ziara katika eneo hilo na kilio kikubwa kilikuwa ni fidia kidogo sana ukilinganisha na uharibifu unaojitokeza. Ni vigezo gani huwa vinatumika au ni lini sheria itarekebishwa ili ianze kukidhi vigezo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Iringa una vivutio vingi sana ambavyo bado hatuoni kama Serikali inavitendea haki ya kuvitangaza ili viweze kuchangia pato na kukuza utalii katika eneo la Nyanda za Juu Kusini. Tunaona kama upo ubaguzi. Nini mkakati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Nabu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii ambayo ni muhimu sana kwa sisi akina mama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Mawaziri wake ambao wako katika Wizara hii. Vilevile nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia ambaye alikuja Iringa kwa ajili ya kukagua vyanzo vya maji. Niiombe tu Serikali iangalie yale maagizo aliyoyatoa siku zile alivyokuwa Iringa basi yazingatiwe. Tuna imani kwamba kama yatazingatiwa angalau Iringa na sisi vile vyanzo vinaweza vikawasaidia wanawake wa Iringa na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niunge mkono Wabunge wote waliochangia kuhusu Mfuko ule wa Maji uongezewe kutoka kwenye shilingi 50 mpaka shilingi 100. Nina imani kabisa ili mwanamke atuliwe ndoo kichwani ni muhimu mfuko huu ukaongezewa kiasi hicho. Pia tuangalie kwenye vyanzo vingine vya mapato kama wenzetu wengine walivyosema ili tu Mfuko wa Maji upate fedha. Kama walivyosema wenzangu na mimi nawaunga mkono kwamba maji ni kitu muhimu sana katika maisha ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu katika Mkoa wetu wa Iringa tumekuwa na matatizo makubwa sana, tumekuwa na vifo vingi sana vinavyosababishwa na ukosefu wa maji. Nitatoa mifano miwili ambayo imetugusa sana wananchi wa Iringa. Kwanza, kuna mwanamke ambaye alikuwa amejifungua watoto mapacha akaenda kwenye Mto Lukosi kwenda kuchota maji yule mama akauawa na mamba. Hili ni jambo ambalo kwa kweli linatuumiza, aliacha watoto wadogo sana.

La pili, juzi tu hata mwezi haujaisha, kuna mtoto wa shule ya sekondari ya Lukosi alikwenda pale kuchota maji akatokea mbakaji mmoja akamchukua yule mtoto kutaka akambakie upande wa pili. Watu walipotokeza akamtupa kwenye maji yule mtoto akafa. Kwa kweli ilitusikitisha sana kwa sababu yule binti alikuwa bado mdogo. Kwa hiyo, tunaomba sana Mkoa wa Iringa unauhitaji mkubwa sana wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika vituo vya afya vingi vilivyopo vijijini bado maji ni tatizo, inasababisha akina mama wakati wanajifungua wanapata mateso makubwa sana. Aidha, mama anaamka asubuhi kwenda kwenye shughuli ya kutafuta maji badala ya kwenda kwenye shughuli ya maendeleo. Hii pia inamkosesha mama kuendelea na miradi aliyonayo, kutwa nzima anatafuta maji, anamuacha pia hata mzee, hata ndoa nyumbani zinavunjika kwetu Iringa kwa sababu ya maji kwa sababu mama anaondoka saa
9.00 za usiku kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisisahau kuwazungumzia wananchi wa Mji Mdogo wa Ilula. Bahati nzuri Mheshimiwa Rais alipokuja kuomba kura alikuja kwenye Wilaya ya Kilolo, lakini kwenye Mji Mdogo wa Ilula. Ule mji kama alivyosema Mheshimiwa Mgonokulima kwa kweli maji ni tatizo kubwa sana. Siku ile wananchi walikuwa wana mabango ynayozungumzia tatizo la maji wakimwambia Rais wanavyopata shida ya maji. Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba angeweza kuleta maji baada tu ya kuchaguliwa na akatuambia kwamba Waziri atakayemchangua atakuja mara moja kuja kusikiliza tatizo la maji. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri hebu aende Kilolo pale Ilula ukawaeleze kwa nini mpaka leo maji hayajaletwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mkoa wa Iringa hauna tatizo la maji bali ni usambazaji wa maji. Tunavyo vyanzo vingi sana vya mito kama Mto Ruaha, Mto Lukosi, Mto Mtitu na kadhalika, ni kwa nini Serikali isitumie mito hiyo kutatua tatizo hili la maji kwa sababu tumeona miradi mingi sana ya visima haifanyi kazi. Nilishauliza hata swali, tunayo mito mingi kama Mto Lukosi umezunguka maeneo mengi sana, lakini mpaka leo hii haujaweza kutumika ili uweze kuwasaidia wananchi wa Iringa kutatua tatizo la maji linalowakabili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba tu nipate majibu, katika mji huo huo wa Ilula, kulikuwa kuna wafadhili wa Austria. Je, ule mradi umefikia wapi kwa sababu tulijua kwamba ungeweza kuwasaidia wananchi wa pale Ilula?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja lakini nitaandika kwa maandishi kwa sababu mengi sana sijayazungumza. Nashukuru sana kwa kupata nafasi hii.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri Dkt. Tizeba, Naibu Waziri Mheshimiwa Olenasha, Watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea bajeti yao ili tuweze kuipitisha Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kuongelea kuhusu bima ya kilimo. Ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kuwapatia elimu wananchi ili waweze kuweka bima kwa ajili ya kilimo? Kwa sababu kilimo chetu nchini kimekuwa hali ya hewa haitabiriki na pia Serikali haijaweza kuwa na uwezo wa kutoa pesa ya kutosha kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji. Tulipotembelea nchi ya China tulijifunza mengi yanayohusu kilimo mojawapo ni kuwaelimisha wananchi kuwa na Mashirika ya Bima ya Kilimo ili pia itawasaidia hata kukopesheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Benki ya Kilimo. Tunaipongeza Serikali kwa kuanzisha Benki ya Kilimo nchini ambayo ilikuwa ndiyo kilio chetu na tukiamini ndiyo mkombozi kwa wakulima ambao ndiyo walio wengi. Ni kwa nini benki hii Makao Makuu yasiwekwe Dodoma ambako ndiyo katikati ya mikoa yote iwe rahisi na kuweza kufikika kirahisi? Vilevile ni kwa nini benki hii isiweze kufunguliwa madirisha katika mikoa na wilaya ili kuwatendea haki wakulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kilimo cha umwagiliaji. Mkoa wa Iringa una eneo linaweza kumwagiliwa lenye jumla ya hekta 54,446, kati ya hekta hizo zinazomwagiliwa kwa sasa ni hekta 25,575 sawa na asilimia 47 ya eneo lote. Mazao makuu yanayolimwa kwa skimu za umwagiliaji ni pamoja na mpunga, mahindi, nyanya, vitunguu, mbogamboga na matunda. Mkoa wetu una jumla ya skimu za umwagiliaji 48 katika mchanganuo ufuatao; Iringa 32, Kilolo tisa (9), Mufindi tano (5) na Manispaa ya Iringa mbili (2).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii miradi ya Manispaa ya Iringa ni miradi ya muda mrefu sana, Serikali imekuwa haitoi pesa kwa ajili ya miradi hii na tunategemea miradi hii ingeweza kusaidia vijana wetu hawa wa mjini waweze kujiajiri kupitia kilimo. Je, Serikali inatumia vigezo gani kutoa pesa kwa miradi hii ya kilimo cha umwagiliaji? Pia baadhi ya miradi ya umwagiliaji maji kutokamilika vyema na mingine haihitaji ukarabati wenye gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za jumla katika kilimo katika Mkoa wetu wa Iringa ni kama zifuatazo:-

(a) Mtawanyiko mbaya wa mvua/ukame unaochangiwa na mabadiliko ya tabianchi;

(b) Uhaba wa mikopo yenye riba nafuu na isiyohitaji dhamana kubwa kwa kuwa wakulima wengi hukosa vitu vya kuwekea dhamana;

(c) Kuendelea kupungua kwa rutuba katika udongo suala linalosababisha wakulima wengi kuwa na mahitaji ya matumizi makubwa ya mbolea;

(d) Bei kubwa ya pembejeo za kilimo hasa mbolea na mbegu bora kunakosababisha wakulima gharama za uzalishaji wa mazao ya kilimo kuongezeka mara kwa mara;

(e) Magonjwa ya mimea hasa nyanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inasaidiaje changamoto hizo kwa sababu asilimia 75 ya wananchi wa Iringa ni wakulima na ndiyo wanaochangia pato la mkoa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na Waislam wote nchini kwa kuwatakia mfungo mwema katika mwezi huu Mtukufu. Naomba mchango wangu nimtangulize Mwenyezi Mungu. Nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu wote wa Wizara pamoja na Watendaji wa Wizara kwa kutuletea hii bajeti ili tuweze kuijadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Benki ya Wanawake. Tanzania ina mabenki mengi lakini Benki ya Wanawake ni benki pekee ambayo ina wateja karibu asilimia 74 ya wateja wote. Sisi wanawake tunao wajibu mkubwa kabisa wa kuipigania benki hii. Mwaka 2010 Serikali ilitoa ahadi ya kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 10 kwa miaka mitano yaani itatoa bilioni mbili kila mwaka katika Benki ya Wanawake lakini toka ahadi hiyo ilipotolewa ni shilingi bilioni 5.75 tu ambayo imetolewa mpaka sasa hivi. Je, hizi bilioni 4.25 Serikali itatoa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu benki hii tumeona inakuwa ikifanya kazi vizuri sana, karibu mikoa sita sasa hivi imefungua madirisha lakini bado ina kazi kubwa kuhakikisha kwamba benki hii inafungua madirisha katika mikoa yote ili wanawake wote waweze kupata haki ya kupata mitaji kama ambavyo Serikali ilitaka, kwamba wanawake waweze kupata mitaji kupitia benki hii ya wanawake. Sasa nitaomba labda wakati Waziri anahitimisha atueleze na asipoeleza vizuri itabidi tushike shilingi ya mshahara wake ili wanawake wote nchini waone kwamba benki hii inatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kuzungumzia kuhusu TIB (Tanzania Investment Bank), naungana mkono na wote waliosema kwamba upo umuhimu wa benki hii kupewa mtaji wa kutosha kwa sababu ndio benki pekee inayosaidia kuleta kwa haraka zaidi maendeleo ya nchi hii. Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa viwanda lakini bila kuiwezesha benki hii tutapata shida sana, kwa sababu ndio pekee itakayosaidia kuwezesha miundombinu ya viwanda. Serikali iliahidi kuipatia mtaji shilingi bilioni 500 na tena iliahidi kutoa trilioni tatu lakini ilipatiwa shilingi bilioni 150 tu. Sasa niombe Serikali itakapokuwa inajibu itueleze nini mkakati wa kuhakikisha benki hii sasa inawezeshwa ili huu uchumi wa viwanda uweze kwenda kwa kasi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Naipongeza sana mifuko hii kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanya katika jamii yetu kama ujenzi wa daraja la Kigamboni, ujenzi wa majengo ya UDOM na kadhalika. Niiombe Serikali ilipe madeni ya mifuko hii ili iweze kuendelea kuisaidia jamii na Serikali pia. Kipekee naomba nichukue nafasi hii kuishukuru LAPF, NSSF, PPF na Shirika la Bima (NIC) kwa kuniunga mkono katika programu yangu ya ukarabati wa majengo kongwe kwa shule za msingi katika Mkoa wa Iringa. Niombe na mifuko mingine basi iendelee kutusaidia ili kuendelea kusaidia jamii zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alisema mifuko hii sasa hivi ianze kuwekeza katika viwanda ili isaidie pia na kuongeza ajira nchini. Pia nimshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama alipokuja Iringa kutembelea kinu cha National Milling alisema kwamba NSSF itatoa mtaji. Najua kwamba ikitoa mtaji katika kile kinu itasaidia pamoja pia na kupata soko kwa wakulima wetu wa Iringa vilevile kuongeza ajira katika mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumzia kuhusu madeni ya wazabuni. Naipongeza Serikali kwa kuanza kulipa madeni ya wazabuni kiasi cha shilingi bilioni 796 kati ya deni la shilingi trilioni tatu iliyokuwa inadaiwa, lakini bado wazabuni wengi sana wakimemo wa Mkoa wa Iringa wanaidai Serikali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali ingetangaza katika gazeti ili wazabuni waliohakikiwa na wale waliolipwa madeni waweze kujua, kwa sababu kuna wengi walikuwa wanaidai, lakini hawajui hatma ya madeni yao mpaka leo hii, kama yatawekwa wazi angalau hata sisi tunapokwenda kwenye mikutano maswali yanapungua, wanakuwa wanajua kabisa hatma ya madeni yao ni yapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee kuhusu Ofisi ya Ukaguzi (CAG), kwanza niipongeze kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikiifanya, ofisi hii inafanya kazi nzuri sana lakini changamoto kubwa ni utekelezaji wa ushauri wa mapendekezo yanayotolewa katika ripoti yake. Bado Serikali hawajaweza kuyafanyia kazi yale mapendekezo ambayo yanatolewa. Vilevile wapewe fedha ya kutosha, kwa wakati na waweze kukagua mapema ili kusaidia nchi yetu panapokuwa na matatizo, tuweze kujirekebisha halafu tuendelee mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu TRA; TRA imekuwa ikifanya kazi nzuri sana tu lakini nafikiri sasa hivi wafanyabiashara wale wadogo wadogo wamekuwa wakikadiriwa kodi kubwa sana hata wale wakubwa kiasi kwamba wanashindwa kufanya biashara zao vizuri. Vilevile kuna utaratibu wa kumkadiria kodi mtu anayetaka TIN ya biashara, anatakiwa alipe kadirio hilo kabla hata ya kuanza biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limekuwa ni tatizo sana, watu wengi wanakwepa kuomba TIN kwa sababu wanakuwa wana mitaji midogo, sasa akijua kwamba akienda pale atatakiwa akadiriwe ile kodi yake kabla hata hajaanza biashara halafu baadaye tena ndio alipie anashindwa kujisajili. Sasa ningeomba Serikali iangalie kwa sababu shida yao ni kurasimisha hizi biashara ili kuweza kupata kodi kwa urahisi zaidi, lakini sasa hii itasababisha biashara nyingi kutorasimishwa, watu wanaogopa kwenda kuzirasimisha kwa sababu wanatakiwa walipe kodi hata biashara zao hawajui kwamba watazifanyaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna utaratibu wa kumtaka mfanyabiashara aambatanishe invoice ya madai kwa mtu aliyempatia huduma kabla hata yeye hajalipwa. Ukitolea tu mfano wale wazabuni wanaofanya kazi na Serikali utakuta kwamba wanapeka invoice lakini kuja kulipwa madeni inachukua muda mrefu sana. Sasa TRA wanataka uambatanishe na ile invoice ya risiti wakati hata bado hujalipwa. Hili pia ningeomba Serikali iliangalie na iweke utaratibu mzuri wa kumsaidia huyu mfanyabiashara ili aweze kufanya biashara yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine, utaratibu wa kutaka wafanyabiashara kununua hizi EFDs, nafikiri wenzangu wengi sana wamesema. Mfanyabiashara anakuwa na mtaji kidogo sana, sasa anapokwenda kununua hii EFD tayari mtaji wake unakuwa umeathirika. Kwa hiyo, hata hii niungane na wenzangu kwamba Serikali hebu iangalie uwezekano wa EFDs mashine ziweze kutolewa bure. Nakumbuka hata Mheshimiwa Rais alishawahi kutoa ushauri kwamba TRA wawapatie hizi EFDs mashine wafanyabiashara wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukulie tu mfano kama TANESCO utakuta TANESCO wanakufungia ile mashine yao kwa hiyo inasaidia, inapunguza hata gharama za kufuatilia. Hii ni kwa sababu tayari mtu anakuwa amefunga ile mashine na hata ile kodi inayokadiriwa sasa inasaidia, kwamba unalipa kweli kodi halali, lakini si kama wanavyokadiria kodi kubwa wakati pato unalopata sio. Kwa hiyo, naomba hizi EFDs ziweze kupatiwa bure kwa wafanyabiashara wote, hata Mkoa wa Iringa bado hatujapatiwa hizi mashine za EFDs. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lile la tax clearance kwa mfanyabiashara anayedaiwa kodi. Naona kama sio sahihi kwa sababu utakuta mfanyabiashara huyu, wengi sana wamefunga biashara zao sasa hivi kwa sababu ya hizi tax clearance. Hii ni kwa sababu wamekadiriwa kodi kubwa ambayo kwa kweli hailipiki na hawa wafanyabiashara wamekuwa wakifanya biashara bila kupata faida. Utakuta huyu mkadiriaji bado hajaangalia na bado hajamsikiliza huyu mfanyabiashara matatizo makubwa ya kibiashara anayoyapata. Sasa hivi wengi wamekopa benki na utakuta wengi wao bado wanaidai Serikali na wengi wao bado wana matatizo makubwa kwenye biashara zao. Kwa hiyo, ningeomba Serikali iangalie sana hawa wafanyabiashara kwa sababu ni sawasawa na ng’ombe… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria muda wa mzungumzaji kuisha)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha bajeti yao ili tuijadili. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kumteua Dkt. Ave Maria Semakafu kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hii, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuunga mkono hotuba ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na hasa ukurasa wa 29 wa kitabu chao. Serikali itoe tamko rasmi juu ya wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakifukuzwa shule kutokana na kupata ujauzito kurudishwa shuleni ili waendelee na masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya walimu, niipongeze Serikali kwa kulipa madeni ya walimu kwa kuanza kulipa shilingi billion 33.1 sawa na asilimia mbili. Naiomba Serikali iongeze kasi ya ulipaji madeni hayo.

Katika Mkoa wa Iringa, walimu wanaidai Serikali shilingi 1,238,841,517.00, lakini tangu wamehakikiwa hakuna hata Wilaya moja iliyolipwa kabisa. Naomba kujua utaratibu unaotumika au vigezo vinavyotumika kulipa haya madeni katika mikoa na Wilaya zetu. Inakatisha tamaa sana kuona mwalimu anafundisha bila ari na chama kinataka kuandaa maandamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu bure, niipongeze Serikali kwa ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Niipongeze Serikali kwa programu hii, imeonesha kuwa kuna changamoto nyingi sana zilizojitokeza katika utekelezaji wa sera hiyo, lakini bila kuanza tusingezibaini changamoto hizo. Lakini ni vema Serikali iwe na mkakati wa kuzishughulikia changamoto kwa wakati ili azma ya Serikali iweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuta Kodi ya Ujuzi (SDL) na uchangiaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika vyuo vikuu binafsi, ukisoma ukurasa wa 33 katika kitabu cha Kamati, unazungumzia kwa kirefu kuhusu hilo, naomba niunge mkono hoja. Hivyo vyuo havifanyi biashara bali vinatoa huduma kwa manufaa ya nchi yetu. Kuwepo kwa tozo hizi kunapelekea kuwa na changamoto ya kupanda kwa ada na kupungua kwa ajira ili vyuo viweze kujiendesha, Serikali iliangalie upya jambo hili na kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za elimu zilizopo katika vyuo vyetu vya Iringa, bei za nyumba katika maeneo yanayozunguka vyuo vya Iringa ni kubwa mno, ni vema Serikali ingetoa bei elekezi. Mikopo bado inachelewa sana, hasa wanafunzi wa elimu ya vitendo (field and research).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu ya watu wenye ulemavu, niipongeze Serikali kwa kusambaza vifaa vya kujifunzia na kufundishia lakini bado miundombinu katika shule nyingi si rafiki na watu wenye ulemavu kabisa. Mazingira ya vyoo vya shule nyingi bado si rafiki kwa watoto wa kike hasa wawapo kwenye siku zao. Uwiano uliopo kati ya idadi ya wanafunzi na idadi ya matundu ya vyoo bado si ya kuridhisha kwa viwango vya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hali mbaya sana ya majengo ya shule; hali ya majengo ni mbaya sana, mfano katika Mkoa wetu wa Iringa shule nyingi tangu zijengwe hazijawahi kukarabatiwa, sera ipo vipi? Mtoto anasoma katika mazingira magumu sana, hakuna vioo, hakuna floor, hakuna ceiling board.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maktaba katika shule zetu, sera inasemaje kuhusiana na hili? Hali ya maktaba za shule za msingi na sekondari si nzuri, watoa huduma za maktaba (wakutubi) hawapati ajira kwenye maktaba za shule. Shule inapohamishwa inatakiwa iwe na maktaba lakini si shule zote zenye maktaba. Kama tusipozisimamia hizi maktaba hatutakuwa tumemtendea haki huyu mtoto tunayetaka kumjenga kielimu na kuwa na mazoea ya kujisomea ambayo ingemsaidia hata akienda elimu ya juu kuwa na utaratibu wa kusoma.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie changamoto zilizopo katika Mkoa wetu wa Iringa kama ifuatavyo:-

(i) Ukosefu wa fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa kwa baadhi ya miradi kama Tanangozi, Kidabaga, Malangali na Mbalamaziwa;

(ii) Ukosefu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mipya vijijini kama Mkonge – Igoda, Ukelemi na Uyela – Nyololo, Njiapanda na Makungu;

(iii) Uwezo mdogo wa wakandarasi na wataalam washauri kifedha na kitaalam katika kujenga na kusimamia mradi wa maji;

(iv) Ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya uchangiaji wa huduma ya maji na uendeshaji wa miradi ya maji vijijini; na

(v) Upungufu wa wataalam wenye sifa katika Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya LAAC
ilipotembelea katika Mkoa wetu wa Iringa ilibaini yafuatayo:-

(i) Miradi mingi ilikosewa wakati wa usanifu, hivyo, visima vingi kwa sasa havina maji na kama yapo basi sio ya kutosha;

(ii) Miradi mingine chanzo cha maji kimehama na hivyo kukosa maji katika chanzo;

(iii) Baadhi ya wakandarasi hawana uwezo wa kifedha na kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati; na

(iv) Ucheleweshwaji wa wakandarasi kupatiwa malipo wanapowasilisha certificates mpaka kupelekwa mahakamani kwa baadhi ya miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua tatizo linalosababisha Serikali kutotumia mito mingi tuliyonayo katika mkoa wetu kama Mto Ruaha, Mto Lukosi, Mto Mtitu katika kutatua tatizo kubwa la maji badala ya miradi ya visima inayotumia pesa nyingi na hakuna maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya umwagiliaji. Katika Mkoa wetu wa Iringa na hasa Jimbo la Iringa, ipo miradi miwili ya umwagiliaji ya Ruaha Irrigation Scheme, huu upo Kata ya Ruaha na Mkoga Irrigation Scheme, huu upo katika Kata ya Isakalilo. Miradi hii ni ya siku nyingi sana, Serikali haijaweza kuitengea pesa ili iweze kukamilika na kutoa ajira kwa wananchi. Nataka kujua vigezo vinavyotumika kupeleka hizi pesa za miradi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, uvunaji wa maji. Ni lini Serikali itatoa elimu katika suala hili ili Halmashauri zetu ziweke utaratibu wa kuhakikisha maji yanavunwa wakati wa mvua nyingi ili kuwa na akiba ya maji wakati wa kiangazi? Hayo maji yangeweza kusaidia katika shughuli za kibinadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bustani za mboga (vinyungu). Mkoa wetu wa Iringa ni mkoa ambao wananchi wake wanafanya shughuli za kibiashara hasa za mbogamboga kutumia maeneo hayo nyevunyevu kujipatia kipato lakini Serikali imepiga marufuku. Sasa nini mpango
wa kuwasaidia hawa wananchi waliokuwa wanategemea kilimo hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango; Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa uwasilishaji wa bajeti yao hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ikifanya juhudi za kurasimisha biashara zisizo rasmi, Wizara ya Fedha kupitia TRA haioneshi juhudi za makusudi kuwakomboa wananchi wa hali ya chini kuinuka kiuchumi na kuweza kuchangia pato la Taifa kutokana na taratibu ngumu zilizowekwa kwa wafanyabiashara katika kuanzisha na kuendesha biashara zao. Taratibu hizo ni pamoja na:-

(i) Kumkadiria kodi mtu anayetaka TIN ya biashara na anatakiwa alipe kadirio hilo kabla ya biashara kuanza;

(ii) Kumtaka mfanyabiashara aambatanishe invoice yake ya EFD receipt wakati wa kuwasilisha invoice ya mradi kwa mtu aliyempatia huduma kabla hata yeye hajalipwa, mfano Idara za Serikali ambapo malipo yenyewe hayalipwi kwa wakati;

(iii) Kuwataka wafanyabiashara kununua EFD machine kwa fedha zao chache za mtaji wakati EFD ni machine inayoiwezesha TRA kukusanya mapato yake. Ni kwa nini tusifanye kama TANESCO ambapo mita ya umeme inakuwa mali ya TANESCO hivyo kuipunguzia gharama ya ufuatiliaji wa madeni ya kodi? Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano alitoa na kuzigawa bure ili zisaidie kukusanya kodi lakini utaratibu huo ulifanyika kwa kipindi kidogo tu na haukuendelea tena;

(iv) Kuzuia ugawaji wa Tax-Clearance kwa mfanyabiashara anayedaiwa kodi jambo ambalo si sahihi kwani kunamkwamisha mfanyabiashara huyo kuendelea kufanya biashara ili aweze kupata fedha ya kulipia deni la kodi anayodaiwa ukitilia maanani kuwa hata leseni haitolewi kwa mtu asiyekuwa na Tax Clearance. Kwa nini usiwepo utaratibu mwingine wa kumruhusu huyu mtu akaendelea kufanya biashara wakati mwingine anakuwa anakadiriwa makadirio ya kodi makubwa kuliko pato halisi. Akinyimwa Tax Clearance anashindwa kuomba kazi matokeo yake anafunga biashara. Serikali inawavunja moyo wasifanye biashara halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuanza kulipa madeni ya wazabuni kiasi cha shilingi bilioni
796.22 kati ya kiasi cha shilingi trilioni tatu kinachodaiwa. Hata hivyo, bado wazabuni wengi wanadai labda ni vizuri Serikali itangaze katika magazeti wazabuni waliohakikiwa na wale waliolipwa madeni ili waweze kujua sababu kuna wengine walikuwa wanadai lakini hawajui hatima yao mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake ilianzishwa ili kuweza kuwasaidia wanawake kupata mtaji wa biashara baada ya kuona udhalilishaji mkubwa wanaopata katika baadhi ya taasisi. Mwaka 2010 Serikali ilitoa ahadi ya kuipatia Benki ya Wanawake shilingi bilioni 10 kwa miaka mitano maana yake shilingi bilioni mbili kila mwaka. Mwaka 201/2012 – Serikali ilitoa shilingi bilioni mbili; 2012/2013 – Serikali ilitoa shilingi bilioni 1.75 na 2013/2014 – Serikali ilitoa shilingi bilioni 1.5. Jumla Serikali imeweza kutoa shilingi bilioni 5.75. Je, shilingi bilioni 4.25 itatolewa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIB (Tanzania Investment Bank), Tanzania tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda lakini bila kuiwezesha benki hii tutapata shida sana, sababu ndiyo benki itakayosaidia kuwezesha miundombinu ya viwanda. Serikali iliahidi kuipatia mtaji wa shilingi bilioni 500 na tena shilingi trilioni tatu lakini walipatiwa shilingi bilioni 150 tu. Je, nini mkakati wa kuisaidia benki hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuwapongeza, Waziri Mheshimiwa Lukuvi, Naibu Waziri Mheshimiwa Angelina Mabula, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kuleta bajeti hapa Bungeni ili tuijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Migogoro ya Ardhi, niipongeze Wizara na Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii kwa kuendelea kutatua migogoro mingi nchini ikiwemo ya wakulima na wafugaji. Ni kwa nini Serikali isingetenge maeneo ya wafugaji peke yake na yakaainishwa na yakawekewa miundombinu kwa ajili ya kuwezesha wafugaji kutohama hama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ipo migogoro inayowahusu Maafisa Ardhi katika Halmashauri zetu. Tunashukuru hata hivi Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wanafanya juhudi kubwa sana kuwasaidia wanyonge waliokuwa wakipokonywa ardhi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanagawiwa ardhi ya eneo moja zaidi ya watu wawili na kusababisha usumbufu mkubwa sana, lakini huwa tunapata tabu sana, Afisa anayeharibu Halmashauri moja badala ya kubadilisha anahamishiwa eneo lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Wataalam wa Ardhi; Halmashauri zetu nyingi nchini bado zina upungufu mkubwa na kunasababisha wananchi wengi kupata usumbufu mkubwa wanapotaka kupimiwa ardhi au kupata hati na sasa hivi na hili la vyeti feki nalo limechangia kwa kiasi kikubwa sana kuendelea kuwa na idadi ndogo ya wafanyakazi. Ni vizuri Serikali ikaweka utaratibu wa kujua nafasi hizi mapema ili kusaidia utendaji katika Halmashauri zetu na kupunguza kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mipango Miji, ni kwa nini miji yetu mingi haijapangwa, je kazi ya Maafisa Mipango Miji ni nini? Kumekuwa na mwingiliano mkubwa sana wa shughuli katika miji yetu kama vile hakuna wataalam. Ushauri wangu ni vizuri Maafisa Mipango Miji wangekuwa wanasimamia ile michoro iliyopangwa au kama miji haujapangwa basi wasigawe viwanja kabla ya kupitishwa michoro. Hata hivyo, kuna maeneo ambayo hayajapimwa ungekuwepo utaratibu maalum ili kuweza kusaidia jamii, kwa sababu kuna baadhi ya maeneo hayafikiwi kihuduma, wananchi wamekuwa wakipata mateso makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu NHC, niipongeze Serikali kwa ajili ya kazi nzuri inayofanywa na Shirika hili, lakini tuombe majengo haya yajengwe hata katika miji midogo sababu hata wafanyakazi wanapata shida sana wanapohamishiwa mikoani. Ni kwa nini Halmashauri zetu zisitenge maeneo na kuingia ubia nao ili iweze kusaidia upungufu uliopo katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, haya mashirika yanayojenga nyumba kwa ajili ya Walimu kama Watumishi Housing nao wangefika katika Halmashauri zilizopo pembezoni ambako kuna matatizo makubwa sana ya nyumba za watumishi wakiwemo Walimu hata kama ya
kawaida sana ya vyumba vitatu au viwili ili kuyafanya maeneo hayo pia wafanyakazi waweze kuishi kama mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko ya ukarabati wa nyumba za mjini, naomba kujua je kuna sheria yoyote iliyotolewa na Serikali nyumba za kati kati ya mji zisikarabatiwe zijengwe maghorofa. Sababu kunakuwa na malalamiko kwa wananchi wa Manispaa ya Iringa kutopatiwa vibali vya kukarabati nyumba zao hata kama ni magofu na kusababisha majengo mengi kuwa na hali mbaya sana. Sababu hawana uwezo wa kujenga maghorofa sasa tunaomba Serikali itupatie ushauri. Sasa hivi hakuna wawekezaji kabisa kutokana na hali ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

The Public Procurement (Amendment) Act, 2016.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii Procurement Act.
Kwanza kabisa na mimi nianze kumpongeza Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kuleta hii sheria kwa sababu tumekuwa tukiipigania muda mrefu sana na tunaamini sasa uletwaji wa hii sheria itatusaidia pia hata Serikali kuongeza pato la Serikali na watu ambao walikuwa wanakwepa kulipa kodi na wale ambao walikuwa wanafanya tender kwa upendeleo hasa angalau itasaidia hii sheria kuleta haki sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze Kamati ya Bajeti kwa sababu kwa kipindi tu kifupi wameweza kutuletea hotuba yao nzuri japokuwa tumechelewa kuisoma, lakini ninaimani kwamba sheria hii sasa inaenda kutendewa haki. Pia nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu siku zote huwa anakuwa anatuletea sheria nyingi, lakini tunakuwa hatumpongezi, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kupongeza Serikali kwa kuiondoa GPSA kupanga bei kwa sababu kwa kweli ilikuwa ni tatizo kubwa sana kwa kutupangia bei kwa wazabuni.
Mheshimiwa NAibu Spika, jambo la pili, nilikuwa nataka kujua hii GPSA bado ilikuwa inachagua wazabuni wachache ili waweze ku-tender hizo zabuni. Sasa je, katika sheria hii inasemaje maana yake zamani wakati GPSA haipo hizi tender zilikuwa zinatangazwa magazetini na kila mtu anatendewa haki, ku- tender hizo zabuni. Sasa labda sheria ituambie je, GPSA wameondolewa na ile kuchagua wazabuni wachache katika ku- tender hizi zabuni?
La pili pia hii GPSA ilikuwa inatoza ile asilimia mbili ya gharama ya mkataba je, na hii asilimia mbili imeondolewa? Nilikuwa nataka nipatiwe majibu ya hilo pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ukisoma hotuba ya Waziri ukurasa wa saba namba “E”, niipongeze kwa sababu imeweka mfumo utakaotoa upendeleo kwa makundi maalum kwa akinamama, vijana, wazee na makundi maalum ya walemavu. Lakini nilikuwa naomba labda sheria hii ingeweka wazi, je, ni asilimila ngapi sasa hayo makundi yatapatiwa? Labda nitoe mfano, kama watatoa asilimia 30, kwa sababu kina mama wengi sana wamekuwa wakifanya biashara tunaona kabisa tofauti labda na vijana na haya makundi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda kama itatoa asilimia 30, ingetamka kwamba asilimia 15 basi wapatiwe akina mama na asilimia 15 yagawane haya makundi mengine. Hili litawasaidia akina mama wengi sasa hivi wamekuwa wakifanya biashara lakini wanaona kwamba hawapatiwi huo upendeleo ambao watapatiwa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukisoma pia kipengele “G” namba hiyo saba inasema kwamba; kuweka sharti la kutumia mfumo wa electronic katika ununuzi na kuongeza uwazi na uwajibikaji. Labda kanuni zingeeleza jinsi ya kuelimisha kutumia hizi mashine za EFDs kwa sababu itasaidia kama wangewekewa uwezo wa kujua hizi mashine, kwa sababu utawakuta akina mama wengine wako huko vijijini, hakuna umeme, hakuna nini, sasa labda wangetoa elimu na kuwajengea uwezo ili waweze kuzitumia hizi mashine kuliko ilivyo, haijaeleza vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nilikuwa naomba labda katika sheria hii tungeona kipaumbele cha Serikali kuwalipa wazabuni kwa wakati. Kwa sababu utakuta kwamba zamani wazabuni Serikali ilikuwa haiwalipi kwa wakati, wanaweza wakapewa tender labda kwenye mashirika au taasisi za umma, lakini malipo yao yanachukua muda mrefu sana. Je, hii sheria sasa itaibana Serikali kuweza kuwalipa hawa wazabuni kwa wakati? Kwa sababu utakuta wazabuni wanadaiwa na wazabuni wanatakiwa sasa waki-issue invoice, wanatakiwa pia watoe risiti na TRA wanatakiwa sasa wakusanye kodi kwa hao wazabuni. Lakini wazabuni hawajalipwa, TRA wanawadai, na TRA usipolipa wao wanatakiwa wakupige penalt. Sasa je, sheria hii inamlindaje mzabuni?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huo, naomba tu kuunga mkono sheria hii.

The National Shipping Agencies Bill, 2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada huu. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali yetu kwa kuleta Muswada huu pamoja na kuwa ulichelewa sana, lakini nashukuru kwamba umeweza kuletwa.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia Wanasheria wa Bunge kwa kweli walitusaidia sana kuhakikisha tunavielewa baadhi ya vifungu sisi Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu kwa sababu Muswada huu kidogo ulikuwa ni mgumu kwetu na mpaka ulituletea matatizo wewe unajua, lakini tunawashukuru sana Wanasheria na tunamshukuru sana pia Mwanasheria Mkuu ambaye kwa kweli alijitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba huu Muswada unaingia humu ndani bada aya kuishawishi Kamati.

Mheshimiwa Spika, pia nisisahau kuipongeza Kamati ya Miundombinu na Mwenyekiti kwa sababu najua kwamba huu Muswada tumeutendea haki muda mrefu sana umeletwa kwenye Kamati yetu na tukaweza kuuchambua na kuna ushauri mwingi sana tuliutoa na tuipongeze Serikali kwamba mambo mengi sana ambayo Kamati ya miundombinu ilikuwa imeomba kwamba yabadilishwe kwa kweli walileta na tukayafanyia marekebisho.

Mheshimiwa Spika, naomba tu kuishauri Serikali kwamba, Miswada kama hii ambayo ina manufaa kwa Serikali angalau tuwe tunapatiwa semina za kutosha hasa Bunge zima ili tuweze kuishauri vizuri Serikali kwa sababu hata sisi Kamati tuliomba muda mrefu sana tuwekewe semina ili tuweze kuuchambua vizuri huu Muswada kwa ajili ya manufaa ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1973 Serikali ilianzisha chombo kama hiki kilichokuwa kinaitwa NASACO, lakini itakumbukwa kuwa, kufilisika kwa NASACO kulisababishwa kutokuwepo kwa Taasisi ya Serikali katika uwakala wa meli na hivyo Serikali kutokuingia moja kwa moja katika kuona nyaraka ambazo zilikuwa zinaingizwa katika shehena. Kwa hiyo, utaona kwamba sasa hivi huu Muswada utasaidia Serikali yetu itakuwa inaweza kuona nyaraka ambazo zipo katika meli ambazo zinaingia na kutoka.

Mheshimiwa Spika, tangu mfumo wa biashara huria uruhusiwe katika sekta hii mwaka 1999, udhibiti haujawahi kuwa mzuri licha ya maboresho kadhaa ya Sheria. Baadhi ya Sheria zilifanyiwa marekebisho lakini hazikujitosheleza kama Sheria ya SUMATRA ya mwaka 2002, Sheria ya Uwakala wa Meli ya mwaka 2002 na Sheria ya Udhibiti wa Mizigo ya mwaka 1981. Upungufu wa Sheria hizo ulisababisha changamoto mbalimbali ambazo zilichangia upotevu mkubwa wa mapato na kukosesha nchi yetu manufaa ya kuwa na Bandari.

Mheshimiwa Spika, labda tu nitoe mfano kwa sababu nishawahi kwenda kutembelea huko Singapore utaona kwa
wenzetu Singapore, Bandari yao ndiyo uchumi wao na wanafanya vizuri sana. Sisi tulikwenda kuona kwa sababu ule Muswada na wao wana chombo kama hiki, kwa hiyo utakuta kwamba wana Sheria ambazo wamezitunga hazina mianya ya rushwa rushwa, hazina mianya ya kuachia wafanyakazi wa Serikali kuweza kuingiza vitu ambavyo vilijitokeza katika NASACO. Kwa hiyo, nashauri Serikali yetu na yenyewe pamoja na kwamba tunapitisha huu Muswada lakini iweze kuzingatia, itengeneze Sheria ambazo zitadhibiti ile mianya ambayo ilisababisha hata NASACO kufilisika kwa sababu utakuta kuna wajanja tu wachache waliacha nafasi kidogo ile mianya wakaweza kuua hii NASACO, kwa hiyo naiomba kabisa Serikali iangalie na izingatie.

Mheshimiwa Spika, sipendi kuchangia sana kwa sababu tayari nafikiri Kamati yangu ya Miundombinu imeweza kutoa ushauri mkubwa sana na naomba kabisa Serikali ichukue ule ushauri wa Kamati kwa sababu ndiko na mimi nilikuwa huko ili iweze kupitia ule ushauri ili iweze kuboresha hiki chombo. Tuna imani kabisa huu Muswada utakapopita, basi tutaitendea haki Bandari yetu na kwa kweli hata hizi nyaraka zote za usafirishaji zitadhibitiwa na chombo cha Serikali na vile vile rasilimali zote za madini, petrol zitasimamiwa na chombo hiki cha Serikali.

Mheshimiwa Spika, huu Muswada ni muhimu sana na niwaombe tu Wabunge wote waweze kupitisha na wasiwe na wasiwasi kwa sababu tunajua kwamba tulikuwa na Muswada wa Makinikia ule ambao Wabunge wengi walikuwa wameonesha wasiwasi lakini saa hivi kutokana na jinsi ambavyo Sheria zimekaa vizuri na zikaweza kupitishwa hata huu pia nina imani kabisa kama tutaupitisha na tukauwekea Sheria nzuri nina imani kabisa sasa Bandari yetu tutaitendea haki.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, kwa kweli nishukuru na niombe Wabunge wote tupitishe huu Muswada ili nchi yetu iweze kutendewa haki,

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's