Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Atupele Fredy Mwakibete

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa wingi wa rehema kwa jinsi ambavyo alituchagulia viongozi kwa ngazi zote; nikianza na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Joseph Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu; na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa.
Pili, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Busokelo ni Jimbo ambalo tunalima mazao ya chakula na mazao ya biashara. Mazao ya chakula tunayolima ni kama yafuatayo: ndizi, mahindi, maharage, viazi mviringo na viazi vitamu, matunda mbalimbali kama maparachichi, matunda damu na mengineyo. Mazao ya biashara ni kama yafuatayo: mbao, chai, kokoa, kahawa pamoja na hiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazao hayo yote, hatuna hata kiwanda kimoja kwa ajili ya kuchakata mazao hayo yote. Inasikitisha sana kuona mkulima, tena wa jembe la mkono analima kwa taabu sana, pembejeo haziwafikii kwa wakati, zinakuja wakati muda usiofaa. Kwa mfano, mbolea za kupandia zinakuja wakati wa kupalilia na mbolea za kukuzia zinamfikia mkulima wakati anavuna. Mbaya zaidi mkulima huyu akifanikiwa kuvuna,hapati sehemu za kwenda kuuza ama kuchakata (viwanda vidogo) ili mazao yao yapate thamani kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri awakumbuke wananchi hawa wa Busokelo kwa kututafutia wawekezaji wa mazao kama kokoa, ndizi na mahindi pamoja na viwanda vya mazao ya ng‟ombe mfano, maziwa (kiwanda cha maziwa) Kata ya Bonde la Mwakaleli (Isange, Kandete, Lubeta na Mpembo).
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kutafuta wawekezaji kwenye viwanda vya gesi aina ya cabondioxide gase Co2, pamoja na umeme wa joto ardhi Geothermal eneo la Ntaba, Kata ya Ntaba ndani ya Busokelo Mkoani Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana tuwe na kiwanda cha kusindika kokoa kwa sababu wakulima hawa wanalima kwa wingi sana hasa maeneo ya lufilyo, Ntaba na Kambasegela ili thamani ya kokoa ipande na mkulima aweze kupata zaidi kuliko hivi sasa na itaongeza morali zaidi kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya Jimbo la Busokelo ni mibaya sana hasa kipindi hiki cha mvua na hivyo imepelekea zaidi ya tani nyingi sana za ndizi na maparachichi kuharibika na hivyo kusababisha umasikini zaidi kwa wakulima hawa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, ni muhimu sana viwanda hivi vikajengwa maeneo husika ili hasara ambayo inatokana na kuharibika kwa miundombinu iweze kuepukika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia hayo hapo juu, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Spika, lakini kabla sijaanza kuchangia, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa sababu tangu uchaguzi umefanyika ametuteulia viongozi na tumepata jembe, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Pia napenda kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo mmekuwa nami tangu kipindi chote cha uchaguzi na hadi sasa tumepata nafasi ya kuingia Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nasema afya kwanza kwa sababu hakuna Mbunge au mwananchi yeyote ambaye anaweza akafanya shughuli za maendeleo pasipokuwa na afya. Katika kampeni zangu nilikuwa nasema afya kwanza na leo hii ikibidi naomba iwe slogan ya Taifa kama Mheshimiwa Waziri atakubaliana nayo. Napenda kuwashukuru Mawaziri kwa kazi nzuri mnazozifanya pamoja na Naibu Mawaziri kwa jinsi ambavyo mnajituma na kwa kweli hakika hapa kazi tu, tunaiona hii kazi inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri nimekuwa katika sekta hii ya afya kwa kufanya kazi na mashirika ya watu wa Marekani kupitia Jeshi la Amerika. Kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Waziri ataweza kupata ushauri wangu katika mambo mbalimbali. Nikianza kwanza na Jimbo langu la Busokelo. Busokelo ni Jimbo ama ni halmashauri mpya ambapo hadi sasa ninavyosema tuna watumishi wanne tu ambao ni specialist, kwa maana ya wanaume wawili na wanawake wawili. Ni sawa na kusema asilimia 100 hatuna watumishi kwa mujibu wa takwimu za kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 140.
Mheshimiwa Spika, lakini pia katika Halmashauri ya Busokelo, tuna kituo kimoja tu cha afya kwa maana ya kata 13, kituo kimoja. Najua hili lipo chini ya TAMISEMI lakini kwa sababu hizi ni Wizara ambazo zina mahusiano, napenda pia Mheshimiwa Waziri alifahamu hili. Pia hatuna hata hospitali ya wilaya tunatumia Hospitali ya Kanisa inaitwa CDH. Eneo tumeshaliandaa na tumeshaanza harakati lakini tunaomba pindi tutakapoomba msaada kutoka Serikalini muweze kutukumbuka katika hili.
Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu katika Kituo cha Afya cha Kandete ambacho ndicho kituo pekee, kinahudumia wananchi wengi sana kwa maana ya Bonde zima la Mwakaleli. Ukianzia na Kata za Itete, Kandete yenyewe, Isange, Mpombo mpaka Wangwa. Huduma zinazotolewa pale ni ambazo hakika, kama hujapata huduma pale maana yake inabidi usafiri umbali wa zaidi ya kilometa 50 kufuata huduma hizo mjini ambako ni Tukuyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba kituo hiki kiwezeshwe tukianzia na masuala ya mochwari hatuna na hata dawa nazo zinafika kwa kusuasua sana. Kwa mfano MSD wamepewa jukumu la kusambaza ama kusimamia tunasema Medical Store Department nchi nzima. Wakati mwingine MSD wanachokifanya utashangaa imebaki kama mwezi mmoja, ama miezi miwili kusambaza hizo dawa kwa maana zinakuwa expired lakini wanazisambaza. Kwa hiyo, zinakuwa hazina manufaa kwa wale wanaopelekewa kwa sababu kipindi kifupi tu zinakuwa tayari haziwezi tena kutumika kwa afya ya binadamu.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie sasa suala la huduma za UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania. UKIMWI ni janga la Kitaifa na Kimataifa na kwa bahati mbaya sana bajeti ya Serikali imekuwa kidogo sana ukilinganisha na uhitaji wa huduma kwa ugonjwa huu wa UKIMWI. Kuna mashirika mawili hapa nchini, kuna Global Fund na PEPFAR. PEPFAR ni President’s Emergency Plan For AIDS Relief, ni shirika ambalo liko chini ya Serikali ya Marekani, lilianzishwa enzi za Rais, Mheshimiwa Bush. Pamoja na kwamba tunatumia Global Fund ambayo ni nchi mbalimbali lakini asilimia kubwa bado inachangiwa na Serikali ya Marekani.
Mheshimiwa Spika,In case imetokea hawa Wamarekani wanasema sasa stop kuchangia Afrika na Mataifa mengine hakika Tanzania hatutakuwa sehemu nzuri. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kupitia Wizara hii waongeze bajeti ya kutosha katika masuala ya UKIMWI. Wakati mwingine wengi wetu tunaonesha kidole kimoja hivi kwamba yule yule ndiye anaishi na HIV lakini kwa tafiti ambazo tumefanya kwa miaka yote, kumbuka vidole vitatu vinakuonesha wewe.
Mheshimiwa Spika, niwape mfano mmoja, nilipokuwa nasimamia Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Ruvuma, Katavi, Rukwa, Mbeya, nililia sana nilipofika Hospitali ya Rukwa Mjini, nilimkuta bibi mmoja kizee sana ni mgonjwa, anasema mjukuu wangu hapa sina hata Sh.1,000 ya kununua dawa. Sasa umepataje huu ugonjwa? Anasema nilikuwa namlea mjukuu wangu na kwa sababu hatuna elimu ya kumtunza mtu wa aina hiyo ndiyo nikaupata maana alikuwa hatumii hata gloves. Hakika ilikuwa ni masikitiko makubwa, hata Sh.1,000 za kununua dawa hana. Kuna dawa kwa ajili ya kuzuia opportunistic infections, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla atakuwa anafahamu, Serikali haitoi hata wafadhili pia wamejitoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima kama Serikali tutie nguvu sana kwa upande huo kwa sababu dawa hizi za opportunistic infections zinazuia mambo mengi. Kuna zile ambazo zinazuia fungus, magonjwa ya ngozi na vitu vingi ukiachana na zile tunazoita TLE (Tenofovir/Lamivudine/Efavirenz) ambazo hizo zinatumika hasa hasa kwa upande wa matibabu kwa mama mjamzito na anayenyonyesha. Kwa hiyo, kwa sababu wafadhili nao wanajitoa kuleta hizi dawa za opportunistic infections, ni vizuri sasa tutenge bajeti ya kutosha ili kuzuia maradhi ambayo nimeyatamka hapo awali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nichangie kidogo katika suala la Hospitali ya Rufaa Mbeya. Hospitali hii inahudumia Kanda nzima, iwe Njombe, Iringa, Rukwa, Ruvuma, Katavi watu wanakwenda kutibiwa pale. Kipindi kile wakati inajengwa ilikuwa ni watu milioni mbili, lakini sasa ni zaidi ya watu milioni nane. Kwa hiyo, tunaomba Serikali hata kupitia Wizara ya TAMISEMI tuweze ku-expand ili iweze sasa kuendana na mahitaji ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, si hivyo tu hata Wabunge wenzangu wamezungumzia masuala la CT-Scan, hawana CT-Scan pale na hiyo ndiyo hospitali ya rufaa. Kama hakuna CT-Scan tusitegemee watu wale wanaweza wakapata huduma zilizo bora na sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, naomba nizungumzie suala la TEHAMA, mimi pia ni mtaalam wa mambo ya TEHAMA. Leo hii tunazungumzia ulimwengu wa sayansi na teknolojia ni lazima tuhusishe pia Wizara ya Afya. Mtu kutibiwa popote pale alipo. Tunazungumzia suala la uhaba wa Madaktari Bingwa lakini kuna solution ama majawabu ambayo yanaweza yakatusaidia kama tutaweza ku-adopt, inawezekana isiwe leo au kesho lakini tuwe na wazo kwamba kuna kitu hiki kinafanyika duniani na Mataifa mengine yaliyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa Telemedicine. Telemedicine ni suala la kutibu mgonjwa popote pale alipo. Kwa maana ya kwamba unaweza ukafanya naye appointment lakini utafanya baada ya kumsaidia kwa kutumia hata hizi simu za mkononi, wengi wetu tunatumia tu WhatsApp, Facebook na vitu vingine lakini simu inaweza ikafanya vitu vingi zaidi ya hivi. Kwa hiyo, Wizara naomba ilichukue wazo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimeshiriki sana kuandaa na kufanya analysis za Wizara kwa maana ya kutumia tools zinaitwa database, C2C database, DHIS - District Health Information System, LAS - Lap Assessment Response System. Hizi database ni nzuri sana kwa maana ya kwamba inaweza ikaunganisha nchi nzima kufanya analysis ya tuko wapi, ni mkoa gani unaongoza na tufanye nini kwa ajili ya intervention zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninachoiomba Wizara ni kwamba, inabidi hizi system ziwe integrated. Kwa mfano, C2C database ina version nyingi sana lakini ni muhimu sasa iwe ni web-based sasa hivi ni stand-alone, nikisema stand-alone najua mnafahamu nyie Madaktari hasa wale wataalam wa Wizara kwa maana ya kwamba ukipeleka kituoni iko pale pale inabidi tena uhamishe kwa njia ya flash ama external kuipeleka sehemu nyingine. Pamoja na hayo hii LAS - Lapla Response System imekuwa na combined na Post Training Follow-up na itasaidia sana kwa maana ya ngazi ya Wilaya. Kwa ngazi ya Wilaya itakuwa inatuma ripoti moja kwa moja kwa Wizara na haya ndiyo maboresho katika sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza naomba nizungumzie suala la huduma kwa mtoto, maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Kwenye hotuba ya Waziri, ukurasa wa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uzima na afya njema hata tumepata kufika kuiona siku ya leo. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumwongoza vema Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na leo hii anafanya kazi iliyotukuka katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru Mungu pia kwa jinsi Mawaziri wanavyofanya kazi vizuri, Mawaziri wote, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wengine. Lakini kipekee sana niwashukuru baadhi ya Mawaziri ambao walifika Jimboni kwangu, nikianzia na kaka Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, ulinyeshewa sana na mvua kipindi kile! Pia Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, pamoja na Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, tunawashukuru sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nichangie kama ifuatavyo:-
Nikianza na suala la uwanja wa ndege wa Songwe, uwanja huu umejengwa zaidi ya miaka 14 sasa, tangu ambapo ulipendekezwa, tunashukuru Serikali ilipofikia, lakini bado unahitaji kuboreshwa zaidi! Uwanja huu ni muhimu sana kwa sababu unaunganisha Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini iwe Mbeya, Njombe, Katavi, Rukwa na Ruvuma, tunautumia uwanja huu wa Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja huu wa Songwe, nilikuwa nasoma kwenye vitabu umetengewa shilingi bilioni 10, lakini bilioni 10 hii naamini kwa suala la kujenga taa pamoja na kujenga ujenzi kwa maana ya fence, hakika Mheshimiwa Waziri hazitatosha kwa bajeti ambayo imetengwa pale! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini uwanja huu utakapojengwa, utafungua fursa nyingi sana za kiuchumi Nyanda za Juu Kusini. Wawekezaji wengi sana ambao wamekuja ili wawekeze, lakini wanasema hatuwezi kusafirisha mizigo kutoka Mbeya, ama kutoka Songwe, ama kutoka Njombe mpaka kwenda Dar es Salaam halafu ndipo iende Ulaya, wanataka ndege Emirates zitoke huko ziende moja kwa moja Mkoani Mbeya kwa ajili ya kuchukua hizo raw products na pia ziweze kuwa processed. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia uwanja huu ni muhimu kwa sababu kuna baadhi ya viwanda ambavyo vilikwishaanzishwa pale, vinashindwa kuendelea kwa sababu hakuna njia madhubuti; ukiangalia TAZARA, nayo haifanyi vizuri. Kwa hiyo, tunaomba uwanja huu uweze kukamilika kwa wakati ili uweze kufungua fursa nyingi za kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika suala la barabara, suala la barabara kwa Jimbo langu la Busokelo ni changamoto kubwa sana. Nakumbuka kuna barabara ambayo iliahidiwa ni zaidi ya miaka 12 sasa inasemwa itajengwa kwa kiwango cha lami. Nikichukua kitabu cha Ilani ya Chama chetu ukurasa wa 49, hii ni Ilani ya Chama mwaka 2015 imeandikwa ile barabara pale kwamba Katumba – Mbambo - Tukuyu, kilomita 80 kwa kiwango cha lami, lakini kwa miaka yote hiyo hata hivi ninavyoongea, nakumbuka nilishawahi kuleta swali na Mheshimiwa Naibu Waziri, alilijibu kwamba ifikapo mwaka huu mwezi Septemba ama Oktoba itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tukija katika bajeti ukifungua ule ukurasa wa 243, imeandikwa upgrading to DSD of Katumba-Lwangwa- Mbambo- Tukuyu road kilometa 83, lakini hapa inaonyesha ni kilometa moja tu! Tunamwomba sana, Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni ya enzi na enzi, alikuja Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa aliahidi, lakini alikuja Mzee, Mheshimiwa Dkt. Kikwete aliahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 28 Agosti, 2015 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, saa sita na dakika thelathini mchana aliahidi barabara hii na wananchi walipiga sana makofi wakiamini kwamba itajengwa. Hakika tunawaombeni sana, kwa sababu barabara hii, kule tuna vitu vingi kwanza kuna gesi asilia. Hii gesi asilia, kuna viwanda viwili ambavyo vinafanya extraction na exploration za minerals, lakini zinaharibika kwa sababu barabara haziko imara!
Mheshimiwa Naibu Spika, si gesi asilia tu, kuna suala zima la geothermal, karibu tutaanza kuchimba, umeme wa kutumia joto ardhi pia unatoka kule! Nakumbuka alipokuja Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo yeye mwenyewe alijionea ile barabara hadi akauliza Mheshimiwa Mbunge hapa vipi, nikasema na mimi nitalia kilio kwa Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu ili aweze kutuwezesha kwa barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu, hivi ninavyoongea Mheshimiwa Waziri, barabara ile nilipita mwezi wa nne hakika ilikuwa ni worse, worse, worse, nusura nipate ajali! Watano walikufa kwa sababu ya mvua ambazo zimenyesha sana kipindi hiki. Kwa hiyo, tunaomba mtukumbuke, mtukumbuke kwa maana ya kwamba, sehemu ambapo ilitakiwa tusafiri umbali wa kilometa pengine 20 inatulazimu tuzunguke sana. Kama mnakumbuka kipindi ambacho kumetokea mafuriko ya kule Kyela, watu wa Kyela wanalazimika kupita Ipinda, waje Mbambo, waje Masoko, waje Tukuyu wanatumia barabara hii na ndiyo kiunganishi pekee cha Halmashauri zote tatu, maana yake Halmashauri ya Rungwe, Wilaya ya Rungwe, Busokelo na Kyela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaombeni sana na si hivyo tu, ni zaidi ya tani 20 kama si 30 zimeharibika wiki mbili zimepita kwa sababu ya barabara kutopitika, kwa maana ya kwamba malori yameweza kuzuia njia na hakuna abiria anayeweza kupita pale na utelezi ni mkali sana. Kwa hiyo, wananchi ambao wanalima wanashindwa kwenda kupeleka mazao yao kwenda mjini kwa sababu hakuna magari yanayokwenda kule kuchukua bidhaa zao, kwa hiyo tunawaombeni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini siyo hivyo tu, kuna suala zima la madaraja. Madaraja ni changamoto kubwa, ni changamoto kubwa kwa sababu sasa mvua zilivyonyesha zimesababisha baadhi ya madaraja hayo kuondoka, kwa maana ya kwamba wananchi wanatumia tunaita madaraja utepe. Sasa baadhi ya wanafunzi hawawezi kwenda ng‟ambo ya pili ya mto kwenda kusoma kwa sababu hawawezi kuning‟inia kwenye zile nyaya ama zile kamba ambazo zimewekwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kama kuna emergency plan yoyote iweze kutusaidia ili haya madaraja yaweze kujengwa hasahasa daraja la Nsanga. Halafu kuna daraja ambalo lipo Kata ya Kisiba ambalo linaitwa Kibundugulu, hii Kibundugulu imesababisha hata kwenye mitandao, ambao mna WhatsApp, baadhi ya akinamama wanatembea juu ya kamba, inasikitisha sana! Kwa mfano, kama huyo mama ni mjamzito kwa vyovyote vile hawezi kuvuka pale kwa sababu inahitaji apite mmoja baada ya mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaombeni sana Wizara hii kupitia Wizara ya Miundombinu mtusaidie kutengeneza hata emergency, wakati bado tunaendelea kusubiri hiyo long plan kwa ajili ya kutusaidia kujenga madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hayo, pia kuna suala hili la mitandao ya simu; mitandao ya simu ina-diverge sana kulipa kodi na kwa bahati mbaya sana pengine sijui tuna mtambo ama hatuna mtambo, lakini ni muhimu kupitia TCRA wawe na mtambo ambao unaweza uka-filter ama ukajua ni kiwango gani cha course ambazo kila siku zinaingia na kiwango gani cha mapato hata kama ni hizi M-pesa, Tigo pesa ili Serikali ipate mrabaha wake sawasawa, iwezekanavyo. Kwa maana hiyo basi, ni muhimu kuanzisha mitambo kama nchi zingine ambapo inarahisisha sana kutokuwa katika quarrels na Serikali kwa maana ya kufuatilia masuala ya kodi, mara hapa, mara pale, wewe unaingia tu kwenye system unajua bwana wewe umefanya hivi na hivi then lipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsanteni sana!

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu, Wizara ya Nishati na Madini. Nakushukuru wewe kwa kazi nzuri unayoifanya, pia nimshukuru Mungu kwa kutupa nafasi hata kufika mahali hapa siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mungu zaidi kwa jinsi ambavyo alimwongoza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumchagua Profesa Sopeter Muhongo katika Wizara hii ya Nishati na Madini. Profesa hakika unaitendea haki sana Wizara hii. Pia niwashukuru wale wote ambao ni Watendaji Wakuu, Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa REA Tanzania, Dkt. Lutengano Mwakahesya, Mkurugenzi wa Geothermal Tanzania na Watendaji wengine wote katika nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo mchango wangu nielekeze zaidi nikianza na umeme wa vijijini (REA). Mpango huu wa umeme vijijini hakika mwaka jana wengi wetu tumeokoka sana katika mpango huu wa REA. Tumeokoka kwa sababu pamoja na kwamba siyo vijiji vyote vimepata, naamini katika awamu hii ya III vijiji vingi vitapata umeme huu. Nikija katika Jimbo langu la Busokelo, Busokelo ni miongoni mwa Majimbo ambayo tumenufaika na mpango mzima wa REA. Pamoja na kwamba kuna changamoto za hapa na pale, kuna baadhi ya maeneo kama Lupata, ukienda Isoko, ukienda Mpata, ukienda na maeneo mengine ya Kilimansanga bado umeme huu haujafika lakini tuna imani kwamba vijiji 30 vilivyosalia, tunaamini katika mpango huu wa awamu ya III vitapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la mpango wa umeme vijijini, kwa vile vijiji ambavyo vilikuwa awamu ya pili, tunaomba watendaji pamoja na wahusika wote vikamilike kabla ya Juni ili wananchi wale kwa sababu tulishawaaminisha kwamba watapata umeme, na walituamini, tunaomba kabla ya Juni kwisha waweze kupatiwa huo umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la madini. Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ambayo imebarikiwa sana katika nchi yetu ya Tanzania. Tuna madini ya aina nyingi sana, ukienda kule Chunya utakuta kuna gold, ukienda huku Ileje utakuta kuna madini, ukienda Kyela makaa ya mawe, ukija Busokelo, kwa hiyo tuna madini ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na madini aina ya calcium yanayopatikana pale Mlima wa Panda Hill. Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake haya madini sijayaona hapa, lakini naamini kwamba atatuma timu yake waweze kufanya exploration na extraction kule, basi wananchi wale watafaidi sana haya madini kwa sababu tunaamini hata utengenezaji wa mbolea aina ya NPK inatokana na madini hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, nikisoma kitabu cha hotuba na Waziri ameandika vizuri sana, very technical, ukurasa wa 62 kuna madini aina ya niobium, madini haya pia Mbeya yanapatikana na kazi kubwa ni kutengeneza vifaa vya elektroniki ikiwemo pamoja na engine za ndege tunaita jet, lakini pamoja na kutengenezea vitu mbalimbali, mambo kama kompyuta na simu. Kwa hiyo, tunaomba kama yataweza kuendelezwa, pamoja na kwamba upembuzi yakinifu ulishafanyika na utafiti umefanyika, sasa kazi kubwa iliyobaki ni kwamba yaanze kufanyiwa kazi kwa maana ya kuchimbwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha hotuba yake hapa atuambie kwamba ni lini hasa rasmi wananchi wa Mbeya, katika maeneo ya Panda Hill, Mbeya na Tanzania kwa ujumla watanufaika na haya madini ili waweze kuinua uchumi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika suala la geothermal (jotoardhi). Geothermal ni umeme ambao unatokana na nguvu ama joto lililoko ardhini na Busokelo tumebahatika kuwa na sehemu inayopatikana hiyo geothermal. Kwa hiyo naomba nimshukuru Waziri kwanza kwa sababu nakumbuka siku ile alikuja, alifika katika eneo hili la Mto Mbaka na alituahidi kwamba mara tu baada ya uchunguzi ama baada ya utafiti kukamilika mwezi wa Septemba wataanza kuchoronga visima vya huko, kwa hiyo tunaomba asitusahau.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba pamoja na timu yake ya wataalam waje katika eneo hili kwa sababu wananchi wakati tunahimiza kwamba wasifanye maendeleo yoyote kwa sababu hili eneo litakuwa ni sehemu mojawapo ya kuzalisha umeme na sisi tutakuwa tunauza maeneo mengine, walisikiliza ile kauli kwa sasa hivi wanasubiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo geothermal pekee tu, katika Jimbo la Busokelo pia tuna gesi aina ya carbondioxide. Hii gesi imeanza kuchimbwa tangu mwaka 1984, lakini kwa bahati mbaya hata hivi sasa ninavyoongea tuna viwanda viwili, kimoja kipo Kanyelele na hii gesi inatoka Kijiji cha Mpata, lakini pia kuna kiwanda kingine karibu na Tukuyu Mjini kwa ajili ya gesi hii na gesi hii inatumika zaidi katika masuala mazima ya kwenye soda, kwenye bia na maeneo mengine ambayo yanasababisha vitu visioze wala visiharibike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya, kwa makampuni ambayo yamewekeza kule, kuna kitu tunaita social responsibility kwa maana ya jamii inayozunguka, huwa hawafaidiki na gesi hii. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, kwa nguvu zako zote pamoja na watendaji wako wote kuisimamia vizuri gesi hii aina ya carbondioxide kwa sababu wananchi wanaona yanakwenda magari na kurudi kuchukua, lakini hawaoni wananufaikaje na hii gesi. Hii ni changamoto kubwa sana, kwa sababu nakumbuka kipindi tunaomba kura ni miongoni mwa mambo ambayo yalitusababisha tupate wakati mgumu sana. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri alizingatie hilo atakapokuwa anajumuisha hotuba yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na suala hilo, ukienda Kata ya Lufilyo kuna madini ambayo yanapatikana kule kwa ajili ya kutengenezea marumaru na ukiangalia Tanzania nzima hii, mara nyingi sana tuna-rely kwenye marumaru za ku-import kutoka China lakini kule kuna madini ya kufanya hivyo. Katika Kijiji hiki cha Kikuba, Kata ya Lufilyo, kuna maji ama maporomoko ambayo yanaweza yakasababisha umeme wa Hydro Electric Power kwa maana ya umeme wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi, tunaomba wataalam ama watafiti waanze kuja kuchungulia kule kwa ajili ya kuleta wataalam ili waweze kutuambia ni kitu gani pengine baada ya hapo kitafuata ili wale wananchi wasiangalie tu yale maji yanakwisha pasipo faida yoyote, naamini tukiwekeza katika umeme itatusaidia sana kama nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la matumizi ya umeme. Mara nyingi sana tunasema umeme; naishauri Serikali tuanze kutoa elimu kwa jamii kwamba umeme huu siyo kwa ajili ya kuwasha taa, siyo kwa ajili ya kupiga pasi tu, siyo kwa ajili ya kuangalia TV ama runinga, tufikiri katika uwanja mpana hasa kwa maana ya kuleta viwanda vidogovidogo, vile vya kuchakata hata kwa mikono yao. Nafikiri umeme utakuwa na faida sana na REA hii itakuwa na faida sana kwa wananchi kama tutaanza kutoa elimu ya namna hiyo. Maana wengi wetu wanafikiri kwamba umeme ni kwa ajili ya kuwasha taa na pengine kuangalia vitu vingine, lakini kumbe umeme ni zaidi ya matumizi hayo. Nafikiri elimu hii ikiwafikia na kama Wizara watakuwa na mipango ya kutoa elimu hiyo kwa jamii itapendeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie suala zima la Serikali kuhusika asilimia mia moja katika kuwekeza kwa maana ya nishati ya umeme. Umeme ni gharama kubwa sana, tunaomba Serikali kwa jinsi ambavyo wameshaanza kutafuta wadau wengine waendelee hivyo hivyo. Hakuna Taifa lolote duniani ambalo kwa nguvu zao wenyewe wanaweza wakajitosheleza katika nishati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri nilipata nafasi ya kutembea Mataifa mengine duniani, kama Ujerumani, utakuta nyumba moja ya familia moja inakuwa na vyanzo vitano vya nishati ya umeme; utakuta kuna maji, utakuta kuna solar, utakuta kuna umeme wa upepo utakuta kuna umeme wa biogas, geothermal na kadhalika, hata ukikatika umeme wa aina moja, basi umeme wa aina nyingine ule una-take up, hivyo katika nchi yetu pia tuanze kufikiri katika mfumo huo, tusi-rely tu katika vyanzo vya umeme wa aina moja, kwa maana kwamba kuna gesi halafu pia kuna umeme wa maji, lakini pia tuanze kufikiri zile energy ambazo ni renewable kwa maana ya kwa mfano geothermal.
Mheshimiwa Naibu Spika, geothermal is an energy ambayo inakuwa renewable, inaweza ikazalisha umeme na kuzalisha na kuzalisha, lakini tuki-rely katika umeme wa maji, sisi wote ni mashahidi hapa, kwa sababu wakati mwingine, kama kipindi cha miaka miwili iliyopita nchi yetu ilikuwa katika janga kubwa, kwa hiyo umeme ama mabwawa ambayo tunategemea yalikuwa hayatoi maji sawasawa kama vile ambavyo tulitegemea. Pia tukija katika gesi, gesi ile ukisha-extract hatutegemei tena kwamba itaendelea kuwepo vilevile kwa miaka na miaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niunge mkono Wizara hii na hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha aniambie ni lini umeme wa joto ardhi (geothermal) utaanza kuchimbwa uliopo Kata ya Ntaba. Je, wananchi wa maeneo hayo watanufaikaje na mradi huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji ambavyo vilikuwa kwenye awamu ya pili ya REA ila hadi sasa vijiji hivyo havijapata umeme. Tunaomba vijiji hivyo vipate umeme vilivyopo ndani ya Jimbo la Busokelo visivyopungua 30.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie migogoro ya ardhi iliyopo, moja kwenye Bonde la Mwakaleli kati ya TANAPA na wananchi wa Bonde la Mwakaleli katika Kata za Kandete, Luteba na Isange. Tunaomba irudishwe mipaka ya zamani ili wananchi hawa wapate nafasi za kufuga na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa Kyeruku uliopo Kata ya Kisegese, Kijiji cha Ngeleka, kwa sababu shamba hili wananchi wanalihitaji kulilima ili wajikomboe kwenye umaskini na kwa sasa shamba hili lipo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Busokelo tumetenga maeneo tayari kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za NHC, wananchi hawa wapo tayari kununua nyumba hizo.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri Serikali kwenye Mpango wa mwaka 2017/2018 kama ifuatavyo:-
(i) Kilimo; kuongeza nguvu kubwa ya kuwasaidia wakulima kwa kuongeza pembejeo za kilimo na mbegu yenye ruzuku, kwa mikoa inayozalisha mazao mengi ya chakula na biashara.
(ii) Mifugo; ni muhimu kupunguza ama kuondoa kabisa migogoro ya wafugaji na wakulima, kwa kuwatengea maeneo maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.
(iii) Elimu; ni muhimu kwa Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kuanza mean test mapema kwa ajili ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanaoomba mikopo, ili kupunguza matatizo yanayotokana na kukopeshwa kwa wahitaji hao. Elimu ya shule zetu iwe ni kwa vitendo zaidi kuliko nadharia.
(iv) Afya; ni muhimu kupanga bajeti ya afya ambayo itakuwa inalenga kujitegemea kama nchi kuliko kutegemea wafadhili. Mfano, magonjwa kama ya UKIMWI, dawa zake zinategemea zaidi Global fund na President‟s Emergency Plan for Aids and relief from America (PEPFAR) ambapo Serikali bajeti yake ni kidogo sana na hivyo inaweza kupelekea maafa makubwa kama wafadhili hawa watajitoa na ukizingatia kuwa sera za nchi zao zinabadilika.
(v) Telemedicine; ni muhimu Wizara ya Afya kufanya matibabu kwa njia za mtandao yaani telemedicine.
(vi) Barabara (Miundombinu); kuna umuhimu mkubwa wa kujenga barabara ya kutoka Katumba-Lwangwa –Mbambo-Tukuyu iliyopo Mkoani Mbeya Wilayani Rungwe. Barabara hii inatakiwa kujengwa kwa kiwango cha lami ili wananchi wa Majimbo yote matatu yaani; Busokelo, Kyela na Rungwe wanufaike kwa kuweza kusafirisha mazao mbalimbali kama ndizi, mpunga, kokoa, viazi mviringo, chai, mbao, mahindi na mazao mengine mengi, lakini pia usafirishaji wa gesi asilia aina ya carbondioxide (Co2).
(vii) Geothermal (Nishati ya Umeme); ni muhimu kama nchi kuweza kuanza kuwekeza kwenye umeme wa joto-ardhi ambao unapatikana Jimbo la Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya eneo la Kata ya Ntaba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nategemea mapendekezo yangu yatapewa kipaumbele.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa na mimi
niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu, ya Kamati ya Miundombinu. Kwanza niipongeze
kamati kwa jinsi ambavyo wameleta taarifa ambayo iko vizuri na ipo very detailed pamoja na
Mwenyekiti wa Kamati hii. Nina mambo machache ya kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni suala la viwanja vya ndege, nikisoma ukurasa wa
17 inaonesha kabisa viwanja vya ndege vingi katika nchi yetu vinaendelea kujengwa. Lakini
kuna viwanja ambavyo vilikuwa vilikuwa vinaendela kwa muda mrefu hadi sasa hivi
wanapoleta hii ripoti havijapelekewa pesa hata senti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na kiwanja cha ndege cha Songwe. Kiwanja cha
ndege cha Songwe mwaka 2015/2016, kilitengewa shilingi bilioni tano lakini hawakuletewa
fedha hizo, mwaka 2016/2017, tumetengewa bilioni saba hadi wanaandika ripoti hii
hawajaletewa hata senti tano, maana yake nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanja hiki, ni mfano mzuri kwa mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini, Mkoa wa Mbeya, Rukwa, Katavi, Njombe, Iringa mpaka Songea. Kwa maana nyingine
kwa wale wote ambao wanatumia ndege zinazokwenda Mbeya ni hivi karibuni ni majuzi tu
fastjet imerudi kwa sababu ya kutoweza kutua katika kiwanja kile. Imerudi kwa sababu ukungu
ambao unatanda eneo lile, hakuna taa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nchi na kama Taifa tunataka tuwekeze zaidi katika
masuala ya viwanda, na wawekezaji wengi wanataka watumie usafiri huu wa njia ya ndege
kwa ajili ya kuja kuwekeza viwanda vyao hapa nchini. Kwa hiyo, naiomba Serikali kwamba, kwa
bajeti ambazo zimetengwa katika viwanja ndege mbalimbali kati nchi hii; ukizingatia
Mheshimiwa Rais, nampongeza kwa sababu ameshanunua ndege nyingi katika nchi hii, na
bado tunaendelea kununua kama Serikali. Kwa hiyo, viwanja hivi viweze kupelekewa fedha zao
kwa wakati na viweze kutengenezwa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine muhimu zaidi ni suala la barabara kwa za
kuunganisha kwa kiwango cha lami. Nizipongeze Serikali ya Awamu ya Nne na ya Tano zote
zinaendelea kuthubutu kuunganisha maeneo mbalimbali katika nchi yetu kwa ajili ya
kuunganisha wananchi, lakini pia kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Nimuombe pia
Mheshimiwa Waziri, kwamba kuna barabara ambayo imeahidiwa mara nyingi, na nimeisema
hapa Bungeni kwa miaka mingi; barabara ya Katumba - Lwangwa - Mbwambwa - Tukuyu,
kilomita 83, na wewe Mheshimiwa Naibu Waziri uliona jinsi ambavyo wananchi tulipokea kwa
furaha na tupo tayari hata kutoa maeneo yetu kwa ajili barabara iweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la mawasiliano. Mawasiliano katika nchi
yetu yamekuwa kwa haraka sana, lakini jambo ambalo linasikitisha kidogo kwa wenzetu hawa
wa TCRA kumekuwa na utapeli mkubwa sana kupitia mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba Wizara, lakini pia na wataalam,
kuna wataalam wazuri katika nchi hii ambao wanaweza wakaishauri Serikali ni mechanism gani
zitumike kwa ajili ya kuwabana wale wote ambao ni matapeli kwa njia ya mawasiliamo na
ninaamini kwa kuwa na mimi pia niko kwenye fani hiyo tunaweza tukasaidiana na watu wengi
kuiwezesha Serikali ili wananchi wake wasitapeliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la umeme/nishati. Nakupongeza sana
Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo pamoja na Naibu wako kwa kazi nzuri mnazozifanya.
Suala la REA III na REA II imekuwa ni changamoto katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiw Naibu Spika, mara nyingi Mheshimiwa Waziri umekuwa ukisistiza kwamba
wakandarasi wanapokuja katika maeneo yetu lazima wawasiliane na viongozi ambao ama ni
Waheshimiwa Wabunge ama Madiwani. Lakini kwa bahati mbaya sana wakandarasi
wanakwenda eneo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.

The Media Services Bill, 2016

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Muswada wa Sheria ya Habari kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuundwa kwa ithibati ya wanahabari. Hii itasaidia kuwezesha tasnia hii ya habari kuheshimika kama ilivyo bodi za taaluma zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza hisa zaidi kwa wamiliki wa vyombo vya habari kwa Watanzania 51% na wageni toka nje 49%. Hii itasaidia sana uimarishwaji wa ulinzi kwa nchi na kupunguza habari zisizo za kweli kwa Mataifa ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bima ya afya. Muswada huu wa sheria unatoa umuhimu wa bima ya afya kwa wananchi wote na itawasaidia wakati wanapopata matatizo wakiwa kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri. Ningependa kushauri kuwa pamoja na umuhimu wa Muswada huu, ni vizuri tukazingatia umuhimu wa kuandika kanuni mapema ili baada ya Mheshimiwa Rais kusaini, sheria hii ianze mapema kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Muswada huu.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's