Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie hoja iliyo mbele yetu.
Kwanza, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Lupa waliokichagua chama changu kwa kura nyingi sana, kuanzia Rais, Mbunge na Madiwani, kura nyingi sana nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema na kama alivyosema Mheshimiwa Rais, hatutawaangusha. Uchaguzi umekwisha, sasa iliyobaki ni kufanya kazi, ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ni kutekeleza ahadi ambazo wagombea tuliahidi kwenye
majukwaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu kuna genge limeibuka linaeneza uongo kwamba barabara ya lami kutoka Chunya kwenda Makongolosi aliyoahidi Mheshimiwa Rais haitajengwa! Eti haitajengwa kwa sababu kuna watu wamekula hela na hao watu wamekimbilia nje ya nchi!
Mheshimiwa Naibu Spika, wale ni waongo, ni watu ambao kwenye uchaguzi walishiriki na walikuwa wanatamba kwamba wangeshinda kwa kishindo! Wameshindwa kwa kishindo! Wanashindwa pa kutokea, wanaeneza uongo! Hilo wananchi wa Lupa ni jipu, mtajua namna
ya kulitumbua wakati ukifika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia Hotuba ya Mheshimiwa Rais nalinganisha sana na maneno, yaani nikiangalia hotuba yake na matendo yake, nalinganisha sana na maneno na matendo ya Yohana Mbatizaji zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Kwa ruhusa yako, naomba nisome
paragraph moja aliyosema Yohana Mbatizaji kwenye Injili ya Luka 3:7-14. Siyo maneno yangu haya, maneno ya Yohana Mbatizaji:
“Basi aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize. Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi toeni matunda yapatanayo na toba, wala msianze kusema mioyoni mwenu tunaye baba, ndiye Ibrahimu, kwa maana nawaambia kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumuinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti na kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
Makutano wakamuuliza, tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa wakamuuliza, Mwalimu tufanye nini na sisi? Akawaambia, msitoze zaidi kitu zaidi
kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamuuliza wakisema, na sisi tufanye nini? Akawaambia, msidhulumu mtu wala msishtaki kwa uongo tena mtoshewe na mishahara yenu.”
Mheshimiwa Naibu Spika, haya maneno ni ya miaka 2000 iliyopita! Ni maneno ambayo yako kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais Magufuli, yanafanana; anawaambia Watendaji wa Serikali, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, wote timizeni wajibu wenu, vinginevyo shoka liko shinani. Mti usiozaa matunda utakatwa! (Makofi)
Sasa msianze kulalamika, aah mimi, hapana! Timizeni wajibu wenu. Yohana Mbatizaji alikuwa anawaambia hawa, ili warithi Ufalme wa Mbingu. Mheshimiwa Rais Magufuli anawaambia Watendaji wa Serikali ili tuondoe umasikini kwa Watanzania, ili tulete maendeleo kwa Watanzania. Kwa hiyo, timizeni wajibu wenu, vinginevyo shoka liko shinani, mti usiozaa utakatwa na kutupwa motoni. Ninaomba hotuba hii hasa pale kwenye vipaumbele ambavyo ameweka Rais, Serikali mhakikishe Wakuu wa Mikoa wanayo, Wakuu wa Wilaya wanayo, Watendaji wanayo waangalie Rais ameweka vipaumbele gani kwenye hotuba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba hii anasema wakulima na wavuvi, hasa wakulima, wataletewa pembejeo kwa wakati, watawekewa huduma za ugani, watatafutiwa masoko panaposumbua! Jimboni kwangu mwaka uliokwisha wakulima wa tumbaku wamesumbuka sana, soko la tumbaku halipo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo hili ni jipu lako la kwanza, uhakikishe wakulima wa tumbaku wa Jimbo la Lupa na hasa nchi nzima, watafutiwe soko la zao lao kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, iko nchi ya Zimbabwe ambayo yenyewe imeingia ubia na Jamhuri ya Watu wa China kwamba tumbaku yote ya Zimbabwe inanunuliwa na China. Unajua Wachina wako wengi sana, wako watu 1.6 billion kwa hiyo, chakula kinahitajika kingi, vinywaji
vingi, hata tumbaku ya kuvuta inahitajika nyingi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, naomba jipu hili ulishike vizuri ili wakulima wa tumbaku wa Jimbo la Lupa na nchi nzima mwaka huu wapate soko la uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Hotuba hii ya Mheshimiwa Rais aliongea kwamba anataka kuleta Muswada Bungeni kubadilisha vipengele fulani vya Sheria ya Manunuzi, ili iharakishe, ilete unafuu wa kuleta huduma kwa Watanzania. Nawaambia wadau wote, nimeongelea Sheria ya Manunuzi miaka 10 Bungeni hapa kwamba jamani eeh, bajeti yetu inatakiwa ni trilioni 20! Ujue kwamba 70% ya hela hizo inaenda kwenye manunuzi! Sasa mkiona Rais mwenyewe wa nchi ameshtuka anasema tuongelee manunuzi, muichukulie very positively watendaji wote, ili mlete mapendekezo mazuri ya kuirekebisha sheria hiyo, ili iweze kuharakisha kupeleka huduma kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, pale ambapo muda wa tender ni siku 60, kwa nini, inachelewesha kupeleka huduma kwa Watanzania. Pale ambapo tender sum ya kujenga barabara kutoka hapa kwenda Iringa ni shilingi milioni 200, lakini variations zinazotolewa hapo inafika milioni 600, ni vitu vya kuviangalia hivyo. Pale ambapo Mtendaji au Accounting Officer kwenye Wizara, kwenye Idara, anasema ikifika shilingi milioni 50 lazima akapate kibali kwa Accountant General! Hilo ni la kuliangalia, ili hiyo nayo threshold iongezwe kutoka milioni 50 iende 500 au bilioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, sera ya magari; nimesema sana Serikali iwe na sera ya magari. Kuwe na sera ya magari siyo kwamba huyu ananunua hili, huyu ananunua hili, hapana, kuwe na sera ya magari kabisa. Kenya, Rwanda, Zambia na Malawi wana sera ya magari!
Kwingine kote kuwe na Sera ya Magari! Hiyo Sera mkiiandika vizuri na mkaitia kwenye Sheria, kuna kitu Watendaji wa Serikali wanafanya sana hapa, una-acquire property ya Serikali by tender, lakini sasa katika kui-dispose sheria inasema u-dispose by tender! Magari wanajiuzia!
Hiyo naomba isimamishwe kwenye mapendekezo ambayo yataletwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, mwaka jana Serikali yetu nzuri ilitangaza kupitia kwa Rais na kwa Waziri Mkuu kwamba Mkoa wa Mbeya utagawiwa kuwe na Mkoa wa Songwe na wa Mbeya na kwamba Wilaya ya Chunya itagawiwa kuwe na Wilaya mbili; Wilaya ya Songwe na ya Chunya. Namwomba sasa Mheshimiwa Simbachawene atekeleze ahadi hiyo haraka, ili kila Wilaya katika hizo Wilaya mbili itengeneze Halmashauri yake ili kuharakisha kuwapelekea huduma wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kuna kitu kinanisumbua sana, kinanisumbua kweli, consistency! Nimeshindwa namna ya kusema Kiswahili, consistency! Wakati wa mjadala wa kusema Jamhuri yetu ya Tanzania tuwe na Serikali ngapi, mbili, tatu! Wanasema aah, hapana,
Zanzibari bwana wakae mbali kule, wakae mbali! Hapana, hapana, kuwe na Serikali yao huko! Sawa bwana! Wakati wa uchaguzi, wanasema aah, wale ndugu zetu bwana, lazima tuwasaidie wale, consistency! Nakushukuru sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali kwanza kwa kubuni mradi huu wa shilingi milioni hamsini kwa kila kijiji lakini pia kwa kutambua kuwa pesa hizi pekee hazitoshi na kuongeza fedha za ushauri na usimamizi. Hili jambo jema sana. Kila Wilaya kuwe na desk la consultancy na kuwe na wataalam wa kilimo, biashara, utafiti na kadhalika. Nashauri fedha nyingi katika hii shilingi milioni hamsini ikopeshwe vikundi vya kilimo. Washauriwe vizuri, walime vizuri, kitaalam na baadaye vikundi hivi visindike mazao hayo na kutafutiwa masoko. Tanzania ya viwanda itakuwa rahisi sana kama mapinduzi ya kilimo yatatangulia kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara ilete mageuzi sana kwenye masoko ya wakulima. Wakulima katika maeneo mengi wanauza mazao kwa walanguzi kwa bei ya chini sana. Vyama vya Ushirika viimarishwe, masoko ya uhakika yatafutwe. Utaratibu wa stakabadhi ghalani uenee maeneo yote Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Lupa, Maafisa Ushirika wa Wilaya na Mkoa wanakwamisha juhudi za wananchi kuanzisha Vyama vya Ushirika. Nina mfano wa Vijiji vya Lola na Lyesero, hawa wanakataliwa kuanzisha AMCOS kwa sababu ambazo hazina mashiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara itafute wanunuzi wa tumbaku wengine toka China waliopo wameanza maringo na ukiritimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza jana tulipewa kitabu, pamoja na cha bajeti, kitabu kingine kidogo chenye taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote hadi Aprili 16. Kwenye ukurasa wa 17, naomba ninukuu, kwenye Wilaya yangu ya Chunya, wanatoa taarifa ya minara iliyoweka inayofanya kazi ya mawasiliano na ambayo haifanyi kazi, kwenye Wilaya ya Chunya:
“Kata ya Kambikatoto mtoa huduma Vodacom, ruzuku dola 51,000, mnara haujawaka. Kata ya Lualaje, mtoa huduma TTCL, ruzuku dola 62,000, mnara haujawaka. Kata ya Mafyeko, Vodacom, ruzuku dola 121,000, mnara haujawaka. Kata ya Makongorosi, Vodacom, mnara haujawaka. Kata ya Matwiga, Vodacom, haujawaka”
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda tu rekodi iwe wazi kwamba minara haipo, kwa hiyo wanavyosema haujawaka ina maana upo lakini haujawaka, hii minara haipo. Kwa hiyo, kama ruzuku wameshapewa wapeleke minara, kama hawajapewa ruzuku basi wapewe ambao watapeleka minara. Minara haipo!
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua na mambo makubwa, mazuri yanayoonekana. Jambo la kwanza, bajeti ya maendeleo, Serikali ya Awamu ya Tano wameitoa kutoka asilimia 20 kwenda asilimia 40 ya maendeleo, jambo zuri sana, imejipambanua. Pia akiongea Mheshimiwa Rais ukimtazama usoni amejipambanua sana na wanyonge, watu wa chini. Ukimwangalia anavyoongea unasema huyu kweli inamuumiza, ukiwaangalia Mawaziri wanavyoongea na wanavyofanya kazi vijijini unaona kwamba kweli hawa wanataka kumkomboa mnyonge, wanataka kumkomboa Mtanzania, lakini kwa kuanzia na mnyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hawa wanyonge ambao wanatuumiza, bajeti tunayoipitisha hapa inakwenda kutatua matatizo yao, ndiyo bajeti hii ambayo Bunge linapitisha. Hakuna kitu kinaumiza au kinakera kama Bunge hapa linapitisha bajeti iende kwenye Wizara hii kiasi kadhaa, Wizara hii kiasi kadhaa, zikija Kamati kupitia bajeti mwaka unaofuata mwezi wa Tatu au wa Nne, unaambiwa Wizara hii imepewa asilimia 10, Wizara hii asilimia 17, Wizara hii asilimia 15. Sasa Serikali yetu nzuri, Serikali ya Chama cha Mapinduzi tunawapa KPI hiyo sasa, hiyo ndiyo tutawapima. Mwaka kesho tukifika mwezi wa Nne tunataka tuone bajeti ambayo tunapitisha hapa ya kuwakomboa wanyonge ikifika mwezi wa Nne imepita asilimia 80, asilimia 90. Tutawapima mwezi wa Nne mwaka kesho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naomba niongelee barabara ya Mbeya- Chunya- Makongorosi. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, kwanza napenda kuishukuru sana Serikali kwa kujenga angalau kutoka Mbeya kufika Chunya, nawashukuru sana. Barabara hii ina historia ndefu sana, hii ndiyo ilikuwa zamani ambayo Cecil Rhodes alisema ni barabara ya kutoka Cape kwenda Cairo ilipita toka Zambia- Mbeya- Chunya- Itigi- Manyoni- Babati- Arusha kwenda Cairo, ingawaje Serikali yetu baadaye ilipitisha sheria, Government Notice, kwamba itakuwa inatoka Mbeya- Iringa- Dodoma, lakini asilia ilikuwa Mbeya- Chunya- Itigi- Manyoni- Singida- Babati- Arusha, ndiyo Great North Road ilikuwa inapita hapo. Sasa naishukuru sana Serikali kwa kujenga angalau mpaka Chunya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi nauli kutoka Chunya kwenda Mbeya, kutoka Sh. 10,000/=, 15,000/= sasa hivi ni Sh. 3,500/=. Sasa hivi mazao kutoka Chunya kwenda Mbeya yanakwenda kwa urahisi. Ndiyo uzuri wa kuweka miundombinu mizuri kwa ajili ya wananchi, nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mwaka huu sasa barabara hii imepangiwa Shilingi bilioni 45.8 lakini zaidi ya asilimia 80 ya hela hizi zinalipa madeni, kwa hiyo, itakayojenga barabara kutoka Chunya kuelekea Makongorosi ni karibu bilioni tisa. Kama alivyosema Mheshimiwa Massare, jirani yangu, kipande kingine cha kutoka Mkiwa kwenda Itigi, bilioni sita. Yote katika hiyo 45 billion itakwenda kwenye kulipa madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ilianza kujengwa kabla ya barabara ya Iringa- Dodoma haijaanza, kabla ya barabara ya Msata- Bagamoyo haijaanza, hii itakwisha lini! Naomba sana Mheshimiwa Waziri aongezewe fedha kwa ajili ya kumalizia barabara hii kufika Makongorosi ili iendelee kutoka Makongorosi kwenda Rungwa na mwishoni kwenda Mkiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa watu wa Chunya ni lulu, ni mboni ya jicho, sana, tena sana. Sasa imejengwa juzi nimetoka Chunya mwezi wa pili nimekwenda TANROADS Mkoani kuwaambia kuna sehemu mbili zimeanza kubomoka sababu kuna malori yanabeba tumbaku, kuna malori yanabeba mbao ambayo yanaweka rumbesa, kutoka Chunya kuja Mbeya, lakini yakifika Mbeya yanagawa kwa sababu kuna weigh bridges, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iweke mizani ya kupima hiyo mizigo ya malori ili tuweze kuilinda hiyo barabara yetu, hata mkiweka temporary au mobile weigh bridge itasaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwakibete ameongelea Uwanja wa Songwe na mimi nitaongelea Uwanja wa Songwe huo huo. Uwanja wa Songwe ulianza kujengwa miaka kumi na nne iliyopita, Uwanja wa Kigoma umeanza kujengwa miaka minne iliyopita, Uwanja wa Bukoba miaka minne iliyopita, Uwanja wa Tabora miaka minne iliyopita, Uwanja wa Mafia miaka minne iliyopita, huu wa Songwe miaka kumi na nne iliyopita. Mara tatu, mara nne ndege zinatoka Dar es Salaam kwenda Mbeya zinageuza zinashindwa kutua, hasa mwezi wa Tano, wa Sita kwa sababu ya ukungu, kwa sababu uwanja hauna taa. Kwa hiyo, naomba uwanja huu nao uishe tunahitaji sasa hivi kuweka taa za kuzielekeza ndege kutua, kuweka fensi na kumalizia jengo la abiria. Sasa mwaka huu tumetenga bilioni 10 sijui kama zitatosha. Naiomba Serikali Uwanja wa Songwe ni gateway kubwa sana kwa Mikoa ya Kusini na nchi jirani, naomba uishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kiongozi mmoja wa nchi jirani…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mezani kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia nataka nitoe ushauri wa bure kwa Mheshimiwa Waziri. Pamoja na juhudi kubwa za kuweza kutatua maji katika jiji la Dar es Salaam kwa kuongeza uzalishaji kwenye Mto Ruvu na kuchimba Bwawa la Kidunda. Kimbiji ilikuwa ndiyo lango la Mto Rufiji kuingia baharini, pale Kimbiji chini kuna maji takribani cubic kilometre moja ambayo wakazi wa Dar es Salaam pamoja na kukua kwake wanaweza wakatumia kwa zaidi ya miaka 50. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri kwamba anapotafuta vyanzo vingine vya kupeleka maji Dar es Salaam na Kimbiji aifikirie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu alivyoibariki Mwenyezi Mungu pamoja na madini na kila kitu alichotupa ametupa vyanzo vingi vya maji, ukiacha bahari inayoanzia Tanga, Pemba, Zanzibar mpaka Mtwara; mito mingi, maziwa mengi. Lakini pamoja na mito yote tuliyonayo ukiangalia idadi ya watu waliokuwepo wakati wa uhuru na tuliopo sasa hivi tumeongezeka sana, wanyama wameongezeka sana, kilimo kimeongezeka sana, mito inapungua kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi. Ukiuangalia Mto Ruaha ulivyokuwa miaka ya 2006 - 2007 ukaungalia na leo inasikitisha, maji yanakauka ina maana mito yetu yote inakauka. Nashauri hizi Mamlaka za Mabonde ya Mito zote ambazo zimeunda naomba zipewe uwezo zaidi wa kusimamia vyanzo na kuboresha vyanzo vya mito hii vinginevyo vitakauka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Mbunge miaka mingi sijawahi kuona mara moja ambapo mawazo ya Serikali, mawazo ya Kamati, mawazo ya Kambi ya Upinzani yanafanana, lakini safari hii naomba ninukuu kwa ruhusa yako. Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chake ukurasa wa 8 anasema kuhusu maji vijijini, Waziri anasema; “miradi ya maji vijijini inatekelezwa chini ya Programu Ndogo ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kwa kuzingatia mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa (BRN), idadi ya watu wanaopata huduma ya maji vijijini imeongezeka kutoka milioni 15 sawa na asilimia 40 ya wananchi waishio vijijini mwezi Julai, 2013 hadi kufikia watu milioni 21.9 sawa na asilimia 72.” Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu anasema; “aidha, Mfuko wa Taifa wa Maji umeonyesha mafanikio makubwa katika kuwezesha upatikanaji wa fedha za kugharamia miradi ya maji vijijini, ambapo kiasi cha shilingi milioni 90 zilizotengwa zimeonyesha kutokidhi mahitaji ya miradi ya maji yaliyopo.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani anasema; “uanzishaji wa Wakala wa Maji Vijijini, katika Bunge la Kumi yalitolewa maoni kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusu uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini (Rural Water Agency) ikiwa ni lengo la kuongeza utoaji na usimamiaji wa huduma ya maji kwa wananchi katika maeneo ya vijijini.” Wote watatu wamekubaliana kwa hoja hii moja, ina maana Bunge lako lote linasimamia kwamba tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Wakala wa Barabara ilivyofanikiwa kutengeneza mtandao wa barabara nchini, tumeona mafanikio ya Wakala wa Umeme Vijijini sasa umefika wakati wa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho aoneshe dhamira na nia yake kwamba katika Muswada wa Fedha wa Bajeti hii tunayoizungumzia apeleke mapendekezo ya kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini ili vyanzo vya fedha vijulikane na viwekewe uzio ili Wizara ya Fedha isiweze kuvichezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwetu Chunya. Katika kitabu chako hiki Mheshimiwa Waziri kuhusu orodha ya Halmashauri zilizotengewa fedha za maendeleo kutekeleza maji vijijini kwa mwaka 2016/2017 sina matatizo, nimeiona Wilaya ya Chunya ipo kuhusu fedha zinazotoka nje kwa ajili ya maendeleo ya maji vijijini na mijini sina matatizo, tatizo langu ni mgawanyo wa fedha ukurasa wa 153 zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji (Quick wins katika Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo kwa mwaka 2016/2017. Nikiangalia pale naona Mbeya kuna Kyela- Mbeya, Mbarali - Mbeya, Tukuyu - Mbeya, Kasumulu - Mbeya – Mbozi, sijaona Chunya, najua ni makosa ya uandishi, kwa hiyo nakuomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuleta majumuisho yako hapa na Wilaya ya Chunya uiweke kwenye hizo Quick wins.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mji wa Chunya ni katika miji mikongwe nchini au wilaya kongwe, nitaichukua Bagamoyo, Ujiji na Chunya. Visima vya maji ambavyo viko Chunya pale vilianzishwa mwaka 1938 wakati huo wananchi pale Chunya walikuwa 2000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi pale Chunya wananchi wanaelekea kuwa 20,000. Tunachimba kisima hiki, hakitoshi, tunachimba kisima kingine hakikidhi. Hata Mheshimiwa Rais alipokuja kuomba kura Chunya alikuta shida kubwa ya pale Mjini Chunya ni maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, fedha za quick wins zije ili tuweze kutatua matatizo ya maji Chunya Mjini na kwenye mji mdogo wa Makongorosi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishukuru sana Serikali kwa kujenga bwawa la maji la Matwiga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kunipa nafasi hii niwe mchangiaji wa pili kwenye hoja ambazo zimeletwa na wenyeviti wa Kamati. Kamati hizi mbili zimefanya kazi nzuri sana na wenyeviti mmetuletea taarifa ambazo zipo kamili, nawashukuru sana na nawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwa kutoa mifano kama miwili hivi au mitatu. La kwanza kuna mkoa hapa nchini ambao miaka ya 70 nyani walikuwa wengi sana mkoani huko na walikuwa wanashambulia sana mahindi kiasi cha kuleta njaa kwa wananchi. Wananchi wa Mkoa huo wakaamua sasa kwamba nyani ni kitoweo, wakaanza kula nyani; wanakamata nyani wanakula, nyani wakatoweka kabisa na chakula chao kwa miaka iliyofuata kikawa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili kuna mkoa mwingine miaka hiyo hiyo ya 70 ilivamiwa sana na nzige; wananchi wa mkoa huo wakaamua kwamba nzige ni chakula wakawa wanakamata sana wanakaanga, wanakula; nzige wakatoweka. Maana yangu ni kwamba kukitokea maovu zipo njia nyingi za kuyashambulia ili yaishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano madawa ya kulevya ni ovu, yanaharibu wananchi na society; kwa hiyo, inaweza kutumia njia zozote kushambulia mpaka ziishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wizi ni dhambi; mwenye mamlaka ya kukamata mwizi ni polisi; sasa mtu akija shambani kwako anaiba mahindi unaogopa kukamata kwa sababu sio kazi yako kumkamata unasema ni kazi ya polisi utavuna mabua. Nadhani tutumie njia zote ili kuhakikisha kwamba maovu kama madawa ya kulevya yanatoweka nchini kwetu. Anakamata nani ni suala lingine, nani anayekamata ni kwenye vyombo vinavyohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka baada ya hapo niongelee masuala mawili tu machache ambayo Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ameweka mezani. Nianze na Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Wiliam Mkapa ambayo ipo hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali za rufaa hapa nchini zipo tano au sita; Muhimbili, Bugando, KCMC, Mbeya na Benjamin Wiliam Mkapa. Hiyo hospitali ya Benjamin Wiliam Mkapa ni kama Jakaya Kikwete Heart Institute; ina vifaa vya kisasa kweli kweli lakini watumishi hakuna. Ile hospitali ilikuwa na madaktari wanajitolea; vijana kutoka vyuoni wanajitolea wako pale kama saba au nane, wamejitolea kwa zaidi ya mwaka mmoja; wanasubiri Serikali itakaporuhusu ajira waweze kufikiriwa nao, sio kulazimisha Serikali kuwaajiri bali waweze kufikiriwa kuajiriwa. Mkurugenzi wa hospitali hiyo baada ya vijana kutumika pale amewaondoa, halafu baada ya miezi miwili baada ya kuwaondoa amewarudisha baadhi yao wengine amewaacha huko mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wenyeviti wa Kamati mlishughulikie suala hili, naona kama si haki hata kama Serikali imesitisha ajira lakini hawa vijana wamejitolea kuokoa maisha ya wananchi; na hawasemi kwamba utakapokuwa tayari kuajiri waajiriwe wao, hapana; wanajitolea tu na uwape posho kidogo, naomba Wenyeviti mlichukue hilo na mlishughulikie ili muweze kuishauri Serikali vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye hospitali hiyo hiyo kama nilivyosema ina vifaa vya kisasa kweli kweli, sasa hapo mimi huwa naenda kutibiwa; kuna mashine ya MRI (Magnetic Reasoning Imaging) ya kisasa kweli kweli, haijafungwa bado ipo pale imekaa tu na mtu anayetaka kipimo cha namna hiyo inabidi umpeleke Muhimbili au kwingine lakini mashine iko hapa, kwa nini haifungwi? Tunahitaji lazima Mheshimiwa Rais atoe amri ya kufunga hiyo mashine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mashine ya CT Scan ya kisasa kwelikweli, haijafungwa; iko mashine ya X- Ray, sasa hivi wanatumia mobile mashine ya X-Ray; iko mashine ambayo ni fixed, kubwa, ya kisasa kweli haijafungwa; tunahitaji nani aje atuambie tufunge hizo mashine? Mheshimiwa Mwenyekiti na Kamati yake naomba sana walishughulikie suala hili, waishauri Serikali iweze kufunga vifaa hivi na kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye Hospitali ya Muhimbili, kama alivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii; Taasisi ya Jakaya Kikwete inafanya kazi nzuri sana, imepunguza Watanzania kwenda kutibiwa nje; unafanya vipimo na unatibiwa hapa hapa, naipongeza sana Serikali kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge mwenzangu aliyetangulia, tuiangalie taasisi hiyo, ipewe pesa ya kutosha ili lengo lake la kupunguza kabisa na kuweka sifuri ya Watanzania kwenda kutibiwa nje litimie. Kwa hiyo, namwomba Mwenyekiti wa Kamati waliangalie vizuri hilo na kuweza kuishauri Serikali; hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa hapo hapo, kuna Mturuki ambaye ametoa fedha kwa Muhimbili; amejenga maabara pale Muhimbili, Maabara ya Hermatology ya kupima kwa ndani sana vipimo vya mwili na damu mpaka kwenye details za vinasaba. Ameijenga maabara ile, iko pale, ame-train Watanzania sita au saba wa kuweza kui-manage hiyo maabara ili Serikali, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyingine ziachane na kupeleka sampuli Nairobi, Afrika Kusini, Uingereza na Marekani ambako tunatumia fedha nyingi sana. Hiyo maabara ipo tayari na naambiwa Kamati wamepita hapo na kuna vifaa vingine amevituma vipo njiani vinakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Hospitali ya Muhimbili haipeleki hizo sampuli kwenye maabara hiyo ambayo ipo mlangoni hapo, bado inapeleka Afrika Kusini, Uingereza na Marekani, kwa nini? Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati naomba hilo alishughulikie aishauri Serikali vizuri. Maabara iko pale, mtu wa Mungu ameijengea Tanzania; tuitumie hiyo ili iwe kama ilivyo Taasisi ya Jakaya Kikwete kupunguza kupeleka fedha zetu nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naomba kuunga mkono hoja za Kamati zote mbili.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuniwezesha na mimi kuweza kutoa mchango wangu kwenye hoja iliyo mbele yetu. Naomba nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, kwa mawasilisho yake mazuri sana aliyoyafanya kwenye hotuba yake. (Makofi)

Vilevile kuwasilisha hotuba nzuri ina maana hotuba hii ilitayarishwa na timu ya wataalam wenye weredi mkubwa sana, napenda nichukue nafasi hii, kumpongeza Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na wataalam wote kwenye Wizara hii kubwa ambao wamewezesha kutengeneza hotuba nzuri kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuipongeza na kuishukuru Serikali hii ya awamu ya tano ambayo kwa makusudi mazima imeamua kuwekeza karibuni asilimia 40 ya bajeti yetu kwenye miundombinu. Ukiwekeza kwenye miundombinu sawasawa na kuweka akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo, kwa sababu miundombinu inachochea maendeleo na uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naomba nije kwenye barabara yangu ya Mbeya - Chunya - Makongorosi. Napenda nimfahamishe Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye anaifahamu sana hii barabara. Kwanza ninamsifu sana ametoka Mbeya mpaka Itigi anaikagua barabara. Hii barabara zamani ndiyo ilikuwa njia ya The Great North Road inayotoka Cape kwenda Cairo, ilipita Chunya, Itigi ikaja Manyoni kwenda Arusha - Nairobi mpaka Cairo. Serikali kwenye miaka ya 1960, 1961, 1962 ndio waliibadilisha route hiyo ya Great North Road kwa kutumia GN kwa kuifanya itoke Mbeya - Iringa - Dodoma - Babati kwenda Cairo, lakini originaly ilikuwa ni hiyo ya Chunya, Itigi, ndiyo hii The Great North Road kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nakusifu sana umeikagua unaifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali imejenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Mbeya mpaka Chunya, kilometa 72 tunawashukuru sana wananchi wa Chunya, mmetupunguzia sana matatizo. Sasa hivi kutoka Mbeya kwenda Chunya ni shilingi 3,500 au 4,000 ambapo ilikuwa shilingi 10,000 au shilingi 12,000 sasa hivi mazao tunayolima Chunya yanafika haraka kwenye masoko, kwa hiyo mimi napenda kuishukuru sana Serikali kwa jambo hili kubwa ambalo wamelifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mwaka huu Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 22 barabara hii kujengwa kwa lami kutoka Chunya kwenda Makongorosi hadi Mkola kilometa kama 42. Kwenye kitabu chake nimeiona na ninajua kwa sababu niko karibu sana na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, tender imetangazwa sasa hivi wako kwenye evaluation, najua ujenzi utaanza siku za karibuni, ninawawashukuru sana. Naomba barabara hii ambayo ni ya muhimu sana tuiendeleze mpaka ifike huko inakohitajika kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona vilevile kwenye kitabu kwamba, barabara hii hii kwa mwaka huu inaanza kujengwa kutoka Mkiwa kwenda Itigi ili mwaka ujao itoke Itigi kuja tukutane katikati na Mheshimiwa Massare, kwa hiyo naishukuru sana Serikali kwa niaba ya wananchi wa Chunya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niongelee barabara ndogo ambayo inatoka kijiji cha Kiwanja inakwenda kwenye kijiji cha Mjele kwenye Mkoa mpya wa Songwe, Wilaya mpya ya Songwe Barabara hii inashughulikiwa na Halmashauri ya Chunya, lakini kwa kuwa sasa hivi Mkoa wa Songwe ni Mkoa mpya na Chunya iko Mkoa wa Mbeya kwa hiyo hii barabara inaunganisha mikoa miwili, inaunganisha Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo, naomba Serikali na Wizara muichukue barabara hii iweze kushughulikiwa na TANROADS badala ya kushughulikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kidogo kwenye hii hii barabara ya Mbeya - Chunya - Makongorosi. Barabara hii ina matatizo makubwa mawili, naleta kilio kwako Mheshimiwa Waziri. Tatizo la kwanza barabara hii baada ya kujengwa kilometa 72 ukipita sasa hivi kama ulivyoona ulivyopita kumeanza kuonekana matobo mawili, matatu, manne; kwa barabara ambayo haijamaliza hata miaka mitano siyo vizuri, haina afya hii. Kwa hiyo, naomba sasa hivi mnavyofanya evaluation kwa kuiendeleza barabara hii kutoka Chunya kwenda Makongorosi na Mkola, kandarasi ambaye alijenga huku nyuma ambaye hata miaka mitano haijapita mashimo yanaonekana asipewe kazi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili hili labda tungechukua mfano wa barabara ambayo inajengwa na Serikali kutoka Ruaha ambayo sasa hivi imefika mpaka Mafinga imekwenda Igawa, barabara imejengwa kwa kiwango cha juu sana. Labda wakandarasi wengine wa barabara hapa nchini wangekwenda kujifunza kwa mkandarasi huyu anayejenga barabara kutoka Ruaha kwenda mpaka Igawa kwenda mpaka Tunduma. Kwa hiyo hilo ni tatizo la kwanza, kwamba kumeanza kujitokeza mashimo madogo madogo, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri na viongozi wako mlielewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la pili, Chunya tunalima tumbaku, sasa wasafirishaji wa tumbaku wanaobeba tumbaku kutoka Chunya kuleta Morogoro kutoka Chunya kuja Mbeya wanapakia malori ya rumbesa kwa sababu wanajua kwamba kule sijui hakuna mizani; wanapakia malori ya rumbesa ili akifika Mbeya ndipo anagawa hilo lori yanakuwa malori mawili. Sasa hiyo rumbesa inaiumiza sana barabara ya lami ambayo mmetujengea inaumizwa vibaya sana. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri nipewe hata weighbridge moja au mbili hata mobile weighbridges ili tuweze kuilinda hii barabara, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongee kidogo kuhusu uwanja wa Songwe. Naishukuru Serikali kwa awamu zilizopita na awamu hii, mmejenga uwanja wa ndege wa Songwe ambao unainua sana uchumi wa Mikoa ya nyanda za juu Kusini; Mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Katavi, Rukwa, majirani wa Zambia wa Congo tunatumia uwanja wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeona hapa karibuni wakati wa masika huu, ndege zinatoka Dar es Salaam kufika Songwe kama kuna ukungu zinashindwa kutua, kwa hiyo naomba katika hii bajeti tunayoimalizia mwaka huu, Serikali iweke taa kwenye uwanja huo ili madhumuni ya Serikali ambayo ilikuwa imepanga kwa ajili ya uwanja huu yaweze kutimia. Vilevile naomba Serikali imalizie jengo la abiria kwenye uwanja wa Songwe, naomba tafadhali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee reli ya TAZARA, reli ya Uhuru ambayo walijenga Waasisi wa Taifa hili. Serikali inafanya jambo jema sana kuwekeza kwenye miundombinu, kutengeneza bandari, kujenga reli ya kati kwa standard gauge, bandari za Mtwara, Dar es Salaam, Tanga Serikali inawekeza ili iweze kuvuna kwenye uchumi wa jiografia wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hatuwezi kukamilisha jambo hili kama tutaelekeza tu kwenye reli ya kati na bandari zile basi bila kuingalia reli ya uhuru. Reli ya uhuru yenyewe haihitaji kujengwa, reli ya uhuru inahitaji kukarabatiwa kidogo ifanye kazi, nadhani ni sheria ambazo zimeiweka reli ya uhuru. Naomba Serikali ishirikiane na Serikali ya Zambia tuangalie sheria hizo ni sheria gani ambazo zinaikwamisha reli hii bila sababu, ili bandari zikikamilika, reli ya kati ikikamilika na reli ya uhuru ikikamilika nchi iweze kuvuna kutumia uchumi wa jiografia ambao Mungu ametuwezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye reli ya kati zimeanza block trains ambazo zinabeba mizigo inayokwenda Isaka au inayokwenda Burundi au Rwanda na reli ya TAZARA nayo ingeweza kufanya hivyo, tungeweza kufanya bandari kavu ikawa Mbeya au Makambako au Tunduma tukawa tunatoa block trains kwenda Dar es Salaam, Tunduma, Mbeya au Makambako. Naomba sana, tunapotaka kuboresha miundombinu ya kutumia uchumi wa Jiografia wa nchi hii basi tuiangalie na reli ya TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa barabara ya mchepuko (bypass), Mheshimiwa Mwanjelwa aliiongelea jana; ya kutoka Uyole kwenda Mbalizi. Sasa hivi congestion ni kubwa mno kutoka Uyole kwenda Mbeya Mjini na kuelekea Mbalizi. Barabara ni ndogo, ni ya siku nyingi, biashara ni kubwa mno, fursa ziko nyingi sana za biashara kwenye Mkoa wa Mbeya. Kwa hiyo, hii hadithi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina kila mwaka, naomba barabara hii ya bypass iweze kujengwa ili tuweze kuuokoa Mkoa wa Mbeya kwa uchumi ambao unaweza kudidimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja.

The Legal Aid Bill, 2016

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niwe mchangiaji wa kwanza kwenye Muswada huu ambao nauona ni wa muhimu sana kwa mustakabali wa wananchi maskini wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka ku-declare interest, Mheshimiwa Waziri aliyeleta Muswada huu hapa Bungeni leo ni ndugu yangu mimi wa damu, ni pacha wangu lakini kwa hili natofautiana nae. Sasa hivi amekuwa Waziri karibu mwaka mmoja na mwezi, alikuwa wapi kuleta Muswada huu toka mwanzo na Mawaziri wengine waliomtangulia walikuwa wapi kuleta Muswada mzuri kama huu hapa Bungeni? Naomba nitofautiane naye ndugu yangu na Mawaziri wote waliotangulia, walikuwa wapi kuleta Muswada mzuri kama huu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Mheshimiwa Tundu Lissu mdogo wangu anasema hizi Taasisi za kujiandikisha amezitaja nyingi Chuo Kikuu wapi na wapi lakini kwangu mimi Chunya kijijini Taasisi hazipo, hamna Taasisi hizi Chunya kwa hiyo Mkombozi ni Muswada huu, sasa Waziri Mwakyembe alikuwa wapi nimetofautiana naye kweli kweli, ulikuwa wapi ndugu yangu?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe experience yangu kwenye masuala mawili, matatu. Kwenye uchaguzi uliopita huu, nimekwenda Kata ya Matwiga naenda kuomba kura kwa wapiga kura. Nimekuta hapo mtu ananikimbilia wa jamii ya wafugaji anasema baba yake amekamatwa amewekwa ndani na Mtendaji. Anasema umeweka mifugo yako mahali ambapo haparuhusiwi (tresspass), anasema Mtendaji, kama hukutoa shilingi milioni tano kwa mifugo yako hii nakupeleka Polisi kesho uende Mahakamani sasa dawa yake ni Muswada huu. Nilimfuata huyu Mtendaji kwenda kumuomba amuachie yule mfugaji kwa sababu mfugaji hana kosa na mfugaji hajui sheria akamtoa, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, juzi hapa niko Wilayani Chunya natekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, niko na Mkuu wa Wilaya anaitwa Bi. Rehema Madusa mchapakazi kweli huyu mama. Kuna Ma-DC ambao wanagongana na Wabunge lakini mimi na DC huyu tuko kitu kimoja. Ameniita anasema, Mbunge njoo kuna tatizo, tatizo gani? Anasema kuna wafugaji wametoka wilaya nyingine wamekuja huku, wanakula mazao ya wakulima, wameshikiana mikuki wanataka kupigana, tumeita Kikao mimi niko pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikamwambia Mkuu wa Wilaya tatizo hapa ni Mwenyekiti wa Kijiji. Mwenyekiti wa Kijiji anawaita wafugaji njooni wekeni mifugo yenu hapa, wanampa chochote, anawaruhusu. Kumbe ardhi ile siyo ya wafugaji ni ya wakulima. Kwa hiyo, tatizo kubwa katika ugomvi ambao nimeuona hapa nchini wa wakulima na wafugaji ni aidha Mtendaji au Mwenyekiti wa kijiji. Sasa hawa wakulima wetu, wafugaji wetu sheria hawajui, huu ndiyo tiba yake, muarobaini wake ndiyo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwambia vijijini kama kwangu mimi Chunya, mfugaji awe wa kabila lolote awe Msukuma au awe nani hajui sheria kabisa kabisa. Anachoambiwa na Mwenyekiti, anachoambiwa na Mtendaji ndiyo hicho hicho. Sasa huu ndiyo tiba yake hiyo. Nakushuru sana Mheshimiwa Mwakyembe umeuleta pamoja na kwamba nimekulaumu, lakini pia nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, haki za binadamu, Mheshimiwa Ritta leo asubuhi alikuwa analalamika anasema Mkoani Iringa watoto wadogo wanabakwa sana. Kwanza Mungu alivyomuumba mwanadamu, Mungu akatofautiana na Malaika mmoja. Huyo Malaika amekuwa Shetani. Imefika Watanzania siku hizi wanatenda mambo ambayo hata Shetani anashangaa. Unaendaje kubaka mtoto wa miaka mitatu? Shetani mwenyewe hajawahi kutenda dhambi kama hiyo, hajawahi anawashangaa wanadamu na ndiyo maana labda hata mvua tunakosa kwa sababu tunatenda mambo ambayo hata Shetani hatendi. Sasa wanaobaka watoto muarobaini wao ndiyo huo umefika. Wanawaonea wananchi, haki za binadamu, muarobaini wao umefika. Wanaowaonea akinamama kwenye mirathi muarobaini wao umefika, wanaowaonea wakulima na wafugaji kwenye ardhi yao, muarobaini wao ndiyo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahi sana, nasema hawa watakaoteuliwa kwangu mimi, hawa wasaidizi watoa msaada bila malipo, Mawakili bila malipo; watakaokuwa kwangu Chunya nimefurahi Mheshimiwa Waziri amesema tayari wameshapata mafunzo kwa hiyo, iliyobaki ni kusajiliwa na waanze kazi. Mimi kwangu Chunya watakaoanza, nina mambo mawili; la kwanza nitaomba Kamati yangu ya mfuko wa Jimbo tuwanunulie pikipiki ya kuweza kusambaa vijijini kwenda kutoa msaada kama huu. Kama haitawezekana mfuko wa Jimbo kutoa fedha hizi, mimi nitatoa hela yangu ya mshahara niwanunulie pikipiki ili waweze kutoa msaada huo wa sheria kwa wananchi wote wanaotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hata sura yangu inaonesha nimefurahi sana Muswada huu kuja sasa hivi. Naomba Wabunge wenzangu wa vyama vyote tuunge mkono upite haraka iwe sheria ili tuweze kuwasaidia wananchi ambao wananyanyaswa, wanateswa kwa sababu tu hawajui sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's