Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Frank George Mwakajoka

All Contributions

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze nitoe mchango wangu katika Wizara hii. Awali ya yote niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Tunduma, pia niitumie fursa hii kumshukuru sana Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa hotuba nzuri na hotuba ambayo ikifuatwa na Mheshimiwa Nape akiitumia ninajua Tanzania hii itabadilika kwa ajili ya Wizara yake.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa ambayo nataka kuizungumzia siku ya leo ni kuhusiana na matangazo ya TBC kwa wananchi. Jambo hili linasikitisha sana, wananchi wanasikitika sana kwa kuzimiwa matangazo yao ya live ili waweze kuona Wabunge wao wanafanya nini. Tumepata taarifa hapa mara nyingi CCM wanasema wanataka kutukomesha ili umaarufu upungue, tunataka kutoa taarifa katika Bunge hili kwamba tulikotoka ni maarufu na ndiyo maana tuko Bungeni. Kwa hiyo, hatuoni sababu hata moja ambayo tunafikiri CCM watatupunguzia umaarufu, sisi ni maarufu na tutaendelea kuwa maarufu na wao wataendelea kushuka umaarufu kwa sababu wamekuwa waoga kupita kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, tumepata taarifa mbalimbali hapa wanasema gharama ni kubwa, lakini kuna vyombo ambavyo vilijitokeza kwamba wangeweza kutoa matangazo kwa wananchi, jambo la kushangaza ni kwamba pia wamewekewa mgomo na sasa hivi wanafika mahala wanachambua taarifa ambazo siyo sahihi na ambazo hazina umuhimu kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana, Mheshimiwa Magufuli wakati anahutubia Bunge hili, alisema kwamba hii ni Serikali ya uwazi, sasa ni Serikali gani ya uwazi ambayo inaweza kufanya uwazi, bila kuweka masuala ya habari na kuweka taarifa hizi live wananchi waweze kusikia. Tunafikiri kama Upinzani tunajua kabisa kwamba Bunge ni chombo muhimu na kikao hiki ni kikao cha bajeti, ni jambo muhimu sana kwa wananchi wetu. Wananchi wanataka kujua wawakilishi wao waliokwenda Bungeni wanasema nini, ni fedha gani zinatengwa kwenda kwenye majimbo yetu na ni kazi gani ambayo Serikali itakwenda kufanya. Hatujaja hapa kuuza sura, kama wanavyosema Wabunge wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukiwauliza Watanzania, ni Waziri gani au ni mtu gani anayechukiwa sana katika nchi hii, watamtaja Mheshimiwa Nape Nnauye, kwa sababu tu ya kuzuia matangazo.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, watamtaja Nape Nnauye kwamba ni mtu ambaye anachukiwa sana katika nchi hii. Ninazungumza haya maneno kwa sababu tumejaribu kuangalia katika mitandao mbalimbali tumeona watu wanavyolalamika, wanavyolaani kitendo hiki na siamini kama Mheshimiwa Nape Nnauye atarudi Bungeni mwaka 2020.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, atang‟olewa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie jambo lingine ambalo linahusiana na michezo, tusifikirie kama tunaweza tukabadilisha michezo katika nchi hii kama tutaendelea kuendekeza siasa kwenye masuala ya msingi. Masuala ya kitaalam yaende kwenye utaalam, na masuala ya kisiasa yaende kwenye siasa. Leo nchi hii imetekwa na wanasiasa kila jambo linalofanyika wanasiasa ndiyo wao wanalolifanya, hata jambo la kitaalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi kupata timu bora ya Taifa, hauwezi kupata timu bora ya mpira kama hutaanzisha shule za vipaji maalum kwa ajili ya michezo, haitawezekana hii itakuwa ni ndoto ya alinacha, hata mngetenga bilioni 100 hapa, hata mngetenga trilioni 10 jambo hili halitaweza kubadilika, tutaendelea kubaki kichwa cha wendawazimu. Brazil ni nchi ambayo inatoa wachezaji wengi sana ambao wanacheza professional, lakini leo bado wanaanzisha shule za vipaji maalumu. Ukienda Ivory Coast, ukienda Ghana, ukienda Nigeria na maeneo mengine, sisi tumekalia siasa tunakaa tunazungumza humu, badala ya kuweka mipango na mikakati mizuri kwa ajili ya kutengeneza ajira za vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukubaliane kwamba mpira na michezo yoyote ni ajira kwa vijana wetu, tunahangaika ajira wakati tukitengezeza ajira za kuwawezesha vijana wetu kuwajengea viwanja na kujenga shule ambazo zinaweza zikawasaidia wao kuinua vipaji vyao, tutakuwa tumeongeza ajira katika nchi hii, lakini tunakalia siasa, tunafanya siasa hata kwenye masuala ya msingi, nataka nimuulize Waziri, wakati anakuja hapa kujibu maswali haya, anataka kujibu hoja zangu afike ajibu hoja.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wale vijana ambao walikwenda Brazil, wakaenda wakachukua kombe la Coca-Cola wako wapi wale vijana kama kweli Serikali hii ina dhamira ya kweli ya kuendeleza michezo na kuinua vipaji vya watoto na wananchi katika nchi hii. Wale watoto wako wapi, aje atuambie kama ni utaratibu, kama kweli vijana wanaotoka Tanzania wanakwenda kushiriki kombe la Coca-Cola nchini Brazil wanashinda wanakuja na kombe halafu vijana wale Mwaka mmoja wanapotea mpaka leo hawaonekani, leo tumekaa humu tunasema tunataka kutengeneza bajeti, ni bajeti ya aina gani tunayotengeneza ya kuinua michezo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ni maigizo, ni maigizo ndani ya Bunge hili na lazima Serikali ya Chama cha Mapinduzi iendelee kupokea ushauri na isipoendelea kupokea ushauri tutaikuta ikisuasua mwaka 2020 kwa sababu haitaki kufuata ushauri tunaoutoa katika Bunge letu hili hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumza hapa ni kuhusiana na wasanii. Leo ukienda kwenye redio zetu na televisheni zetu asilimia 90 ya nyimbo zinazopigwa na kuoneshwa kwenye tv ni wageni ndiyo wanaooneshwa. Tunataka uzalendo wa namna gani, tunataka tuwafundisheje wananchi wetu wapende miziki yetu na kuwathamini wasanii wetu kama hatutaweza kuchukua hatua. Ni lazima Serikali ikae na iangalie ni namna gani itawajengea uzalendo wananchi, kuhakikisha kwamba wanawapenda wasanii wao na wanatumia nafasi ya kujinufaisha kwa kutumia nguvu za wasanii wao.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tufike mahala tukubaliane, kwamba Serikali hii haijajipanga na la lazima ijipange, leo asubuhi nilikuwa najiuliza nasema, hivi kwa bajeti ilivyooneshwa humu katika bajeti hii ambayo imesomwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, nikawa nafikiria nikamuuliza Mheshimiwa Sugu nikasema, hivi kuna siku Nape amewahi kuwa mwanamichezo mpaka amepewa Wizara hii. Maana yake niliona ni maajabu yaliyomo humu, haya ambayo tunayazungumza hakuna hata moja lililoandikwa humu, sasa jambo hili ni la ajabu sana, Waziri unapimwa kutokana na mambo ya msingi ambayo yanaoneshwa humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba bajeti hii, hata TFF hawajashirikishwa, na ndiyo maana mambo ya msingi ambayo yalikuwa yanatakiwa yahusu mambo ya soka kwenye nchi hii hayaonekani humu. Tunaona tu semina zinakuwa nyingi, semina elekezi zinakuwa nyingi, hatutaweza kwenda huko, ni lazima turudi tuangalie misingi ya kujenga nchi yetu. Haitajengwa nchi hii kwa sababu tu ya kuzungumza na kuja kucheka cheka humu ndani, kuna watu wengine wanasimama humu ndani, amesimama Mheshimiwa Malembeka, anazungumza hapa anasema eti akina mama wamepewa mimba, inawezekana na yeye imegoma mimba, tutajuaje.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke yeyote ni wajibu wake kubeba mimba, na hiyo ni mipango ya Mwenyezi Mungu, siyo mipango ya binadamu. Leo anakuja Bungeni badala ya kuchangia hotuba hii, anaanza kuzungumza mambo ambayo hayastahili. Ni lazima Serikali ifike mahala ibadilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza haya maneno wengine wanasema ukiwa humu huonekani, ukiweka maji kwa wananchi watakukubali, kuweka maji siyo hisani, ni kodi za wananchi. Serikali lazima ifanye hivyo kwa sababu imepewa mamlaka ya kufanya hivyo, na inakusanya kodi za wananchi. Kwa hiyo masuala ya msingi ni lazima tufike mahala tuyajenge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndugu zangu Watanzania, kwa nini tusijiulize miaka yote Filbert Bayi amestaafu kukimbia, mpaka leo hakuna mchezaji hata mmoja anayewakilisha vizuri nchi yetu huko nje, kwa nini hatujiulizi? Kwa nini tunaendelea kulala usingizi? Kwa sababu tu ya mambo ya kisiasa, tunatoa takwimu za uongo humu, wakati takwimu sahihi hatutaki kuzichukua na tuzifanyie kazi. Kutokana na hali halisi na kichefuchefu nilichonacho, ningeomba kwa kweli niishie hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jambo la kwanza kabisa nipende kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wangu wa Mji wa Tunduma kwa kunipa nafasi hii ya kuhakikisha kwamba nakuwa Mbunge, nawawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa nataka kuzungumza ni utawala bora. Tunapozungumzia utawala bora katika nchi hii hakuna. Jmbo lingine tunasema kwamba tunakaa kwa amani hatukai kwa amani bali tunakaliana kwa amani katika nchi hii; ndicho ambacho kinaonekana katika Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninazungumza haya kwa sababu nina mifano mingi sana ambayo nataka kuitoa mbele yako. Mfano wa kwanza nilivyosema kwamba hakuna utawala bora, nimeona katika uchaguzi kwa ajili wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, uchaguzi umefanyika tarehe 25/10 kupata Madiwani lakini Meya wa Jiji Dar es Salaam amekuja kupatika mwezi Machi, 2016. Jambo hili linaonesha ni jinsi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi haiko tayari kuheshimu utawala bora na pia kuheshimu demokrasia katika Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu kubwa pia kwa Kiongozi wa Kitaifa kushindwa kuwaheshimu viongozi wa chini. Alivyokwenda kuzindua na kufungua miradi ya maendeleo katika Jiji la Dar es Salaam alishindwa kumtambulisha Meya wa Jiji la Dar es Salaam na kumpa nafasi ili aweze kuzungumza ili kuwakilisha Jiji la Dar es Salaam. Jambo hili linanikumbusha mbali sana, namkumbuka sana Mwalimu Nyerere aliwaheshimu mpaka Wenyeviti wa Mtaa na Madiwani katika maeneo waliyokuwa wakiishi. Nashangaa utawala wa Dkt. Magufuli umekuwa unadharau viongozi wadogo na wao wakitegemewa kuheshimiwa baadaye jambo hili litakuwa ni ndoto kwao kwa sababu hawaheshimu utawala bora na demokrasia hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni madai ya Walimu. Kila wakati tunasikia Chama cha Mapinduzi wanajinasibu kwamba kuna elimu ya bure, mimi nasikitika sana katika Taifa hili hakuna Mtanzania hata mmoja anayependa elimu ya bure wala kitu cha bure. Tunasema elimu inayotolewa sasa hivi itolewe kwa kodi za Watanzania na siyo elimu ya bure. Kwa hiyo, tafsiri kuanzia leo tunahitaji elimu inayotokana na kodi za Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tusitegemee kupata elimu bora kama Walimu wanakuwa na madai makubwa, hawawezi kutimiziwa haja zao za kupata mishahara na wakati maisha yao na mishahara yao pia ni midogo. Ni vizuri Serikali hii ikajaribu kutazama kwanza huduma za Walimu ambao wanatoa elimu lakini pia ikaangalia ni namna gani inaweza ikaboresha maslahi ya Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusiana na mambo ya TAKUKURU. TAKUKURU ni taasisi muhimu sana katika Taifa hili na kama kweli tunahitaji uwazi na tunahitaji utendaji kazi mzuri ambao utaondoa mashaka ya rushwa katika nchi hii ni lazima TAKUKURU wapewe nafasi ya kuwa na uwezo wa kupeleka shtaka mahakamani bila kumpelekea mtu yeyote kufanya uchunguzi. Jambo hili katika rekodi mbalimbali linaonyesha kwamba kesi nyingi ambazo TAKUKURU wanajaribu kupeleka mahakamani wanashindwa kwa sababu kesi zile zinaandaliwa na watu ambao hawakuhusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri huu Vyama vya Upinzani vinatoa kila wakati ndani ya Bunge ni vizuri mkasikiliza kwa sababu tunatoa kwa faida ya Taifa hili na si kwa faida yetu sisi. Inaonekana kwamba hakuna hata siku moja mmesimama mkakubali kusikiliza ushauri huu na mnaendelea kuanzisha taasisi ambazo hazina meno, wala hazina tija na haziwezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika suala la biashara. Nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea kama wafanyabiashara wake wataendelea kuwa maskini na watakuwa hawatengenezewi mazingira mazuri ya kufanya biashara. Taifa hili wafanyabiashara wamekuwa kama wanyonge katika Taifa lao, wafanyabiashara sasa hivi wameshindwa kuangiza mizigo nje kwa sababu ya taratibu mbalimbali ambazo haziwapi nafasi ya kufanya biashara na kuwa na mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mataifa mengi duniani yanaandaa wafanyabiashara ili waweze kupata mitaji na baadaye wawe walipa kodi wakubwa katika Taifa lao. Nchi yetu ya Tanzania imeonekana kwamba sasa wafanyabiashara wote wanaoibuka katika Taifa hili wamekuwa wanabanwa na wanashindwa kutekeleza wajibu wao vizuri. Tunasema Serikali lazima ibadilike, iwatazame wafanyabiashara na iwaandae vizuri ili waweze kuwa wafanyabiashara wakubwa na waweze kulinufaisha Taifa hili na waweze kuwa walipa kodi katika Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni kutoa mfano wa Bandari ya Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam sasa inakwenda kufa siyo muda mrefu kwa sababu tumeshindwa kuingia kwenye ushindani wa kibandari na mataifa yaliyoko jirani na sisi. Angalia leo katika takwimu za mizigo ambayo inashuka katika Bandari ya Dar es Salaam, Zambia peke yake ni asilimia 34 ya mizigo imeshapungua wanashusha katika Bandari ya Beira. Kwa maana hiyo tumeshindwa kuingia kwenye ushindani wa kibandari kwa sababu ya kuweka masharti ambayo hayana tija kwenye bandari zetu. Lazima tufike mahali tubadike na tutazame ni namna gani tunaweza tukajenga uchumi bora kama tutaendelea kuua vyanzo vya mapato ambavyo tunavyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Kongo ni karibuni asilimia 46 wameacha kupita pale. Sababu ni kwamba Wizara ya Uchukuzi wameingia mkataba na Congo DRC Lubumbashi kuhakikisha kwamba mizigo yote wanayokuja kuchukua katika bandari ya Dar es Salaam wawe wanalipia kwanza. Wakongo wameona huu ni upuuzi, wameamua kuhamia kwenye Bandari ya Beira na sasa hivi wanapita kule wanaendelea na shughuli zao. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali inapoanzisha jambo ijaribu kupima na kutathmini jambo hili lina hasara gani katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tumepata taarifa na tunasikia kwenye vyombo vya habari Mheshimiwa Rais anawaambia vijana waende vijijini wakalime. Vijana kwenda kulima vijijini kunahitaji pia maandalizi ya kutosha, je, wana mashamba, wamewezeshwa kiasi gani kwamba wanaweza wakafika kijijini na wakaanza kulima kilimo chenye tija na kujiletea maendeleo? Tunaomba sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi wanapotoa matamko wajaribu kutazama ni nini ambacho wanamaanisha, wasiwaswage wananchi na kueleza kwamba ni lazima waende kijijini, hata yule mwananchi ambaye yuko kijijini anayelima haoni tija ya kuendelea kulima kwa sababu hakuna masoko ambayo yako na pia haelewi ni namna gani ya kulima kwa sababu tija hakuna katika kilimo hiki. Tunaomba Serikali ijipange, iwawezeshe Watanzania ili kuhakikisha kwamba Watanzania hawa hata kama wanakwenda kulima watakwenda kulima kilimo chenye tija ambacho kitawasaidia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunasikia matangazo mbalimali kuhusiana na vifo vya kina mama na watoto. Leo hii katika taarifa hii inaonesha kwamba mpaka 2018 watahakikisha kwamba kuna punguzo la vifo vya akina mama na watoto kwa asilimia 20, jambo hili ni aibu sana. Kwa kweli kifo kinafika mahala tunaweka takwimu za kupunguza asilimia 20, ni mambo ya ajabu kabisa. Lazima tufike mahali tujadili, hivi leo kama Wabunge wangekuwa wanatuwekea hapa wanasema jamani Wabunge tunakufa sana humu tupunguze asilimia 20 kwa bajeti ambayo tunaiweka, kila mmoja angekataa kwamba afadhali tuweke bajeti asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa tutazame jambo hili kwa umakini zaidi, tuangalie maisha ya watu, tuangalie maisha ya wananchi wetu kama kuna tatizo la kuweka fedha kidogo, fedha iongezwe kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanasaidia akina mama na watoto ili waendelee kuwa wazima na watu wanaobeba ujauzito wawe na uhakika kuzaa watoto na watoto wao kuwa hai muda wote. Jambo hili tunaona lazima lifanyike haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni matangazo ya television kukatishwa…
Bado Mheshimiwa, kengele ilikuwa bado Mheshimiwa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa kupata nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu liko mpakani kabisa mwa Zambia na Tanzania. Ni Jimbo ambalo ni lango kuu la nchi za Kusini na kati mwa Afrika. Jimbo la Tunduma linakuwa na wageni wengi sana ambao wanatoka nchi mbalimbali; South Africa, Botswana, Zimbabwe, Congo, Malawi na Zambia. Cha kushangaza katika Serikali yetu hii huwezi kuamini, Mji wa Tunduma hauna umeme wa kutosha kabisa. Wageni wengi katika Mji wa Tunduma sasa hivi wanakwenda kulala Zambia kwa sababu ya kuhofia usalama wao kutokana na giza kubwa linalokuwepo katika Mji wa Tunduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimshauri tu Mheshimiwa Waziri wakati anakuja hapa atuambie, ni lini Tunduma tutapata umeme wa kutosha ambao utasaidia kuwavutia wawekezaji na watu wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam ili waweze kutumia gesti zilizoko Tunduma na kuweza kukaa katika nyumba ambazo tumezijenga katika Mji wetu wa Tunduma kuliko kuwa na giza katika mpaka wetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu kubwa sana kwa nchi kama Tanzania ambayo sasa mpaka wa Tunduma ni mkubwa unaoingiza fedha nyingi. Miezi sita tu ulikuwa umeingiza karibuni shilingi bilioni 22 kwenye mpaka wetu wa Tunduma. Huwezi kuamini, hata maji Tunduma pale, imefika mahali mashine zetu za kuvutia maji kila siku zinakufa kwa sababu ya umeme kuwa mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka Mheshimiwa Waziri atuambie leo, kwamba ni lini atahakikisha umeme wa pale utakuwa vizuri? Kama wameshindwa kuleta umeme Tunduma, tuna transforma pale upande wa Zambia, miaka ya nyuma tulikuwa tunatumia umeme wa Zambia. Tunaomba watuunganishe na umeme wa Zambia ili wananchi wetu wa Mji wa Tunduma waweze kuwa na umeme masaa 24. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna mitaa mingi sana kwenye Mji wangu wa Tunduma haina umeme. Mitaa hiyo ni Namole, Msambatuu, Chiwezi na Mtaa wa Niumba, hawana umeme kabisa. Tunavyozungumzia mitaa, ina maana ni maeneo ambayo yako mjini, lakini huwezi kuamini, hakuna umeme kabisa. Wananchi wanalima vizuri, wanazalisha, lakini wanashindwa kupata huduma muhimu za umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri, atuambie, ni lini atahakikisha kwamba wananchi hawa, maeneo ambayo nimeyataja wanahakikisha kwamba wanapata umeme kwa kipindi hiki ambacho tunacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia imekuwa ni tatizo kubwa sana katika nchi yetu, kwamba katika Wilaya zetu ambamo wamepelekwa Mameneja wa Wilaya, wamekuwa wanalalamikiwa sana na wananchi katika maeneo yale, kuna mambo ya msingi sana ambayo ilitakiwa Wizara ifanye, lakini imefika mahali wanashindwa kufanya kwa sababu fedha ambazo zinakuwa zimepangwa kwenye bajeti kwa ajili ya kuweka umeme, unakuta fedha zile hazifiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, tunapotengeneza bajeti hapa Bungeni na tunapitisha, tunaomba hizi fedha ziende katika maeneo hayo ili zikawatumikie wananchi, waweze kupata huduma ya umeme. Kitendo cha kutengeneza bajeti hapa halafu baadaye bajeti zile zinashindwa kuwafikia wananchi kama tulivyokuwa tumepanga, ni kurudisha maendeleo nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukubaliane kabisa, hakuna nchi yoyote inaweza kupiga hatua kama nguvu ya umeme katika nchi hii itakuwa chini kiasi hiki. Wananchi wengi sana wamejiajiri, hasa vijana, wamejiajiri, wanachomelea, wana viwanda vidogo vidogo, lakini vile viwanda sasa hivi vimeanza kufa na wameshindwa kufanya kazi hizo kwa sababu ya kukosa umeme katika nchi hii. Tunaomba nchi hii iachane na mazoea ya kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki; wawe na muda mzuri wa kutekeleza na kufanya mambo ambayo yanaweza yakawasaidia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Tunduma nimeshamwambia Waziri wa Uchukuzi, Waziri wa Maji na sasa namwambia Waziri Profesa Muhongo, wahakikishe kwamba wanaleta umeme na huduma zote za kijamii kwenye Mji wa Tunduma kwa Wizara zote, zinapatikana pale kwa sababu sisi ndio tunaolinda Bandari ya Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam asilimia 60 ya mzigo unapitia kwenye mpaka wa Tunduma. Kwa hiyo, tuna….
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie mchango wangu katika Wizara hii. Nimepitia kitabu cha bajeti katika kusoma nimeona uendelezaji wa miji sijaona Mji wa Tunduma. Kila mmoja anajua kuwa Mji wa Tunduma unakua kwa kasi kubwa na ni lango kuu la kuingilia nchi za Kusini na kati mwa Afrika. Hivyo, kutokuweka Mji wa Tunduma katika miji itakayoendelezwa ni kutokuitendea haki Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Kasi ya ujenzi katika Mji wa Tunduma ni kubwa sana na hatuna kiwanja hata kimoja kilichopimwa hivyo sasa ujenzi ni holela. Pamoja na kutokuona Mji wa Tunduma katika kitabu cha bajeti, naomba Waziri atuingize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika miaka mawili iliyopita tulifanya mchakato wa kutafuta namna ya kukopa katika taasisi za fedha na baadaye turejeshe baada ya kuuza viwanja, lakini tulikataliwa na TAMISEMI. Hivyo, tunaomba Wizara itusaidie kupata fedha katika taasisi za fedha ili kupima haraka Mji wa Tunduma kabla haujaharibika sehemu zote. Wananchi wanahitaji viwanja, hata leo ukipima viwanja 5,000 ndani ya miezi miwili hutapata kiwanja watakuwa wamemaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba sana Wizara itupatie pesa ili tupate master plan ya Mji wa Tunduma ili kurahisisha kazi za upangaji wa mji wetu wa Tunduma. Nashauri Halmashauri zote nchini zipate master plan katika kurahisisha kupima na kupanga miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua mpango wa kurasimisha makazi (MKURABITA). Mwaka 2012-2013 walikuja Tunduma na kupima baadhi ya maeneo kama Kata ya Maporomoko na Kaloleni katika mitaa ya Kaloleni, Danida, Kastamu, Nelo, Migombani na wakawahamasisha wananchi kufungua akaunti wakaanza kukusanya pesa na kuziweka katika akaunti ile mpaka leo hakuna kinachoendelea pamoja na kuchimba mawe yaani kuweka alama ya kuwa eneo limepimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini mpango huu uliowaacha njia panda wananchi wa kata hizo bila kujua nini kitaendelea utamalizika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mji wa Tunduma kuna migogoro ya ardhi kati ya wananchi wenye mashamba na Halmashauri baada ya Afisa wa Ardhi Mteule wakati bado tuko Mbozi kupima maeneo ya watu bila kuzungumza nao na bila kuwalipa fidia na kuwauzia wananchi wengine katika Kata za Mpemba, Katete, Chapwa na Chipaka huo ulikuwa mwaka 2011 na 2012. Hivyo tunaomba pia Waziri afike katika Halmashauri yetu awasaidie wananchi kwani wanamsubiri kwa hamu kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mpaka wa Tanzania na Zambia ni tatizo. Nyumba zimeingiliana, Watanzania wameingia Zambia na Wazambia wameingia Tanzania hivyo kuzua sintofahamu kwa wananchi wetu pamoja na Zambia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2017/2018 pamoja na Mwongozo wake.
Ningependa nianze moja kwa moja na upungufu wa mizigo kwenye bandarii yetu ya Dar es Salaam. Nilikuwa nafikiri ni vizuri zaidi Serikali hii ikajikita kukubali kushauriwa na Waheshimiwa Wabunge wanavyotoa ushauri wao, na pia niwashauri sana Wabunge wetu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tujikite kwenye majukumu yetu ya kuishauri Serikali na kuisimamia Serikali. Kazi ambayo inafanyika sasa hivi kwenye Bunge hili ninaifananisha sana na picha za zamani za kihindi ambazo wakati bosi anatembea, alikuwa anatembea na watu walikuwa wanaitwa masuzuki, yule suzuki alikuwa anakaa pembeni kwa bosi na bosi akigeuka tu hata akikohoa yeye anaondoa miwani kwenye macho akifikiri ameitwa au anaagizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri sana tukapunguza uoga na tukasimama kwa miguu yetu kama Wabunge ili kulisaidia Taifa hili. Taifa hili lina watu wengi ambao wamepewa majukumu, ni wasomi wazuri, lakini pia ni wataalam ambao tumewaweka kwenye Wizara mbalimbali kuhakikisha kwamba wanaisaidia Taifa. Wataalam hawa tumefika mahala sisi wanasiasa tumeanza kuwaingilia, wameshindwa kutekeleza wajibu wao kufuatana na utaalam unaowaruhusu waweze kufanya kazi hizo. Jambo hili tukubaliane kwamba Taifa hili haliwezi kwenda kwa mtindo huu kama wanasiasa tutaingilia shughuli zote za kitaalam na sisi tukawa kwenye maagizo badala ya kuangalia ni namna gani tunaweza tukaishauri Serikali na kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza wajibu wake ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi huwezi kuamini, nchi imebaki ni nchi ya matamko kila mmoja anatoa matamko pale anapoweza, hakuna mwongozo unaoonesha kwamba ni nani anatakiwa kufatwa hapa. Wataalam wetu sasa hivi wameshashuka thamani na utaalam wao haueleweki tena kwa sababu ya sisi wanasiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka sana wakati Mheshimiwa Rais ameapishwa na wakati anaanza kutembelea wadau mbalimbali kujaribu kupata mawazo alikutana na wafanyabiashara katika nchi hii. Wakati anakutana na wafanyabiashara kwenye nchi hii jambo la kwanza alilolizungumza aliwauliza ni nani mmoja wenu aliyenichangia hata shilingi moja wakati wa kampeni. Swali hili lilikuwa ni swali gumu sana kwa wafanyabiashara ambao waliitwa wakitegemea kabisa kwamba Mheshimiwa Rais angeweza kuwashukuru pia kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha kwamba wanaendeleza viwanda vyao, wanaendeleza biashara zao na wanalipa kodi katika Taifa hili mpaka alipolikuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini aliwauliza swali tu kwamba nani ambaye amewahi kunichangia wakati niko kwenye kampeni aseme hapa, tafsiri yake ni nini? Alikuwa anaweka gape, anatengana na wafanyabiashara na sasa hivi ndio maana baada ya muda mchache alitangaza wafanyabiashara wengi ni watu ambao wanaihujumu Serikali, ni wezi na ikaonesha kabisa kwamba Taifa hili linaonesha kabisa kwamba wafanyabiashara wote katika nchi hii ni watu ambao hawaaminiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lolote duniani kama halitawathamini wafanyabiashara na kukaa na wafanyabiashara na kubadilishana na wafanyabiashara mawazo ni namna gani Taifa lao liende, Taifa hilo haliwezi kupiga hatua hata siku moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilichokuwa nataka kukizungumza hapa nilikuwa nataka kusema kwamba ni lazima sasa Mheshimiwa Rais, lakini pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kurudi kukaa na wafanyabiashara, hakuna Taifa lolote linaweza likaendelea kwa sababu ya kutangaza kwamba yeye anapenda maskini, hakuna maskini anayependa kuwa na njaa, si siku nyingi maskini huyo akiwa na njaa akikosa dawa atamgeuka Mheshimiwa Rais kwa sababu hawezi kukubali kuendelea na mateso wakati anajua ana haki ya kupata maisha bora katika nchi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni mara nyingi sana wadau mbalimbali wanajaribu kutoa ushauri. Ninakumbuka sana Bandari ya Dar es Salaam tumezungumza mimi ni mjumbe wa Kamati ya PIC, tumezungumza sana tukiwa na Katibu wa Uchukuzi tukamweleza athari ambazo zimetokea kwenye Bandari ya Dar es Salaam, wateja ambao walikuwa wakitumia Bandari ya Dar es Salaam wakubwa ilikuwa ni Kongo pamoja na Wazambia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Tunduma niko pale Tunduma, kwa takwimu za mwaka 2014/2015 kwenye nchi hii asilimia 71 ya mizigo inayoshuka kwenye Bandari ya Dar es Salaam inapita kwenye mpaka wa Tunduma, lakini leo hii ukienda kuangalia tulikuwa na foleni ya malori karibuni kilometa nane ili kuvuka mpaka lakini leo huwezi kukuta gari hata moja liko barabarani limepanga foleni wanasema hali ni nzuri wakati hali bado ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wana Tunduma tumeathirika lakini pia Taifa tunaliona linaathirika kupita kiasi sasa wadau mbalimbali wanajaribu kutoa ushauri nakumbuka Mheshimiwa Sugu hapa alisema ndani ya Bunge hili akasema mtindo huu ambao Serikali imeanza kufanya kazi ya kuikusanyia Serikali ya Kongo kodi ni jambo ambalo linasababisha wateja wengi wa bandari yetu wakimbie waende Beira, waende Mombasa lakini pia wengine wameenda hadi Durban wanapitia kule japokuwa ni mbali lakini wameona afadhaili wapitie kule, hatukuweza kusikiliza tukaendelea kukomaza shingo zetu mpaka bandari inataka kukatika hapa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ndugu zangu, ninakumbuka sana wafanyabiashara pamoja na wadau wa bandari tuchukulie watu wa TATOA. Watu wa TATOA wamejaribu kuishauri Serikali mara nyingi, wameishauri Kamati ya Viwanda na Biashara, wakawaeleza wakasema tatizo kubwa la upungufu wa mizigo hapa ni tatizo la Serikali kutokusikiliza ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo walizungumza walijaribu kutoa mfano wa kampuni moja tu ya Impala ambayo ilikuwa ikipitisha kwa mwezi mzima tani laki tano kwenye bandari ya Dar es Salaam. Wakasema magari ambayo yalikuwa yakipakia mzigo na kwenda kupakuwa mzigo Kongo yalikuwa ni zaidi ya 30,000 kwa mwezi na magari haya yalikuwa yakitumia lita 2,500 kutoka Dar es Salaam kwenda Lubumbashi kwenda kuchukua copper na kila lita moja ya mafuta Serikali ilikuwa inachukua shilingi 600 kwa ajili ya kodi, lakini pia wakasema kwamba copper tani moja walikuwa wanalipa dola 600 kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam lakini leo hii hakuna kinachoendelea na juzi kwenye takwimu za Durban imeonesha Kampuni ya Impala imesafirisha tani laki saba kutoka Kongo na Zambia wamekwenda kupita kule kwa sababu ya ukiritimba tuliokuwa nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana mambo ya uchumi hayana utani, nchi za wenzetu zilizoendelea tunazoziona zina maendeleo mazuri si kwamba zinacheza na uchumi, uchumi sio jambo la kucheza nalo, leo watu wanasimama, Mheshimiwa Rais anasimama, Waheshimiwa Mawaziri wanasimama wanasema hata ikija meli moja, kauli hizi kwa kweli zinafika mahala zinawakatisha tamaa Watanzania na wanafikiria hawa ni viongozi kweli ambao tumewatanguliza kwa ajili ya kuleta ustawi wa Taifa hili. Ndugu zangu haitawezekana ukipata meli mbili au tano badala ya kupata meli 20 mpaka 30 huwezi kufananisha hata ungepandisha ushuru kiasi gani ni lazima tutakuwa na hasara katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana leo tunazungumzia uchumi kushuka kwenye Taifa hili watu wanakomaa hapa wanasema uchumi haujashuka wakati huduma za jamii, fedha katika Halmashauri zetu hazijafika leo watu wanasema uchumi haujashuka katika Taifa hili. Tunataka tuseme ni lazima Serikali ifike ikubaliane na ushauri mbalimbali unaotolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni kuhusiana na wafanyabiashara katika nchi hii. Wafanyabiashara wengi sasa wamekuwa na wasiwasi wameanza kuhamisha biashara zao wanakwenda Kongo, Zambia, Malawi na maeneo mengine wanahamisha biashara kwa sababu hawana uhakika wa biashara zao katika nchi hii. Kuna wafanyabiashara ambao wamekamatiwa mizigo yao, kuna wafanyabiashara ambao tayari wamefungiwa akaunti zao bila sababu za msingi na bila taarifa za msingi na wanafunguliwa akaunti bila kuambiwa nini kilichoendelea, jambo hili wafanyabiashara wamekuwa na wasiwasi wameona kabisa Serikali hii inaonesha kabisa haiwezi kuwatendea tena haki na wanaamua kuhamisha biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nikwambie tu takwimu zilizopo ukienda nchini Zambia kuna Watanzania zaidi ya milioni tatu wameamua kwenda kufanya biashara Zambia, lakini Malawi kuna Watanzania zaidi ya milioni moja na laki tano wanafanya biashara kule Malawi. Serikali imekaa kimya wanalipa kodi kule wananemesha nchi ya Malawi na Zambia kule Serikali imekaa kimya kwa sababu ya masharti magumu ambayo Serikali imeweka. Nataka nitoe mfano mmoja wa masharti ambayo Serikali inatakiwa iyatazame. Mimi niko mpakani mwa Zambia na Tanzania ukilipia mzigo wako eneo la custom pale ZRA - Zambia ukiondoka kwenda kufika Lusaka mzigo ule watu wa ZRA wanakuja kuchunguza risiti zako kama umelipia vizuri na mzigo ndio ule uliolipia, wakikuta mzigo ndio uliolipia wanachokifanya wao ni kukuruhusu ushushe mzigo na uendelee kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Tanzania mtu anatoa mzigo nje akishafikisha kwenye Bandari ya Dar es Salaam analipa ushuru, akishauchukua ule mzigo anafika Kariakoo watu wa TRA walewale wanakwenda kuchukua kodi, anatoka pale anakuja mtu wa Mbeya ananunua mzigo watu wa TRA walewale wanakwenda wanachukua mzigo ule kodi, anatoka pale anapeleka; mtu ananunua Mbeya pale anapeleka Sumbawanga watu wa TRA walewale wanakwenda kuchukua kodi, mzigo unatoka Sumbawanga mtu wa Nkasi anakwenda kununua mzigo mtu wa TRA yule yule anakwenda kufata mzigo Nkasi, ni sheria za wapi za kukusanya kodi katika dunia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndiyo vikwazo vikubwa vya wafanyabiashara katika nchi hii, ni lazima tufike mahali nchi yetu tunaipenda na hatuna nchi nyingine ya kukimbilia zaidi ya nchi hii; na sio nchi ya mtu mmoja ni nchi ya Watanzania wote tunahitaji kuipigania na lazima Wabunge tushikamane kwa jambo hili tuzungumze kwa nguvu zetu zote ili kuboresha uchumi wa nchi hii wananchi wetu waweze kupata madawa watoto wetu waweze kusoma na shughuli zingine ziweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa najaribu kujiuliza elimu bure Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaonesha ni jinsi gani ilivyofeli kwenye elimu bure. Wakati tunafanya mahesabu imeonesha kabisa kwamba karibuni shilingi bilioni 15.7 zinakwenda kila mwezi kwa ajili ya kulipia gharama za elimu bure kwa watoto 8,340,000; tafsiri yake ni kwamba kila mtoto anapewa shilingi 1,884.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inasema kwamba kila mtoto wa shule ya msingi anatakiwa kulipiwa shilingi 10,000 tunataka kujua shilingi 8,116 zinakwenda wapi na zitapatikana namna gani (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama kweli bajeti ni shilingi bilioni 15.7 tafsiri yake ni kwamba ukifanya mahesabu ya haraka haraka kwa watoto 8,342,000 utakuta ilihitajika fedha bilioni 83 kwa mwezi lakini inapelekwa bilioni 15 leo mnatuambia kwamba huduma za watoto mashuleni zinakubalika, kazi hiyo haipo, Serikali imeshindwa na iwaambie wananchi kwamba imeshindwa na mzigo huu wananchi waendelee kuubeba mzigo huu. Ndio maana madarasa sasa hivi hayajengwi, ndio maana ukienda ukiona msongamano wa watoto unazidi kuongezeka kwa sababu Serikali imewadanganya wananchi na kazi haifanyiki hata kidogo katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tulikuwa Bungeni humu, tukaishauri Serikali tukasema kitendo cha kuwaambia watumishi wakusanye ushuru kwenye Halmashauri zetu manpower ya watumishi wetu ni wachache katika Halmashauri zetu, tukasema hili jambo litakuwa ni gumu, leo katika Mji wa Tunduma ambapo kwa kipindi hiki cha mavuno tulikuwa tunakuwa na asilimia 40 mpaka 45 ya makusanyo leo tuna asilimia 18 tu, leo hii tumekaa hapa vyanzo 42 havijakusanywa hata shilingi moja ukimuuliza Mkurugenzi anasema watumishi ni wachache siwezi kuwagawa watumishi katika Halmashauri yangu. Serikali ikafidia fedha hizi ili tuweze kufanya maendeleo katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kuhusiana na kilimo, nilikuwa najaribu kuangalia kwenye Mpango huu naona kabisa kwamba kilimo kinaendelea kushuka…
MWENYEKITI: Ahsante.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kuwapa pole sana wananchi wangu wa Mji wa Tunduma kwa ajali ya moto ambayo imetokea katika soko kuu la Mji wa Tunduma na kuteketeza maduka mengi ambayo wamepoteza mali zao nyingi sana, nawapeni pole sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze na suala la utawala bora katika nchi hii. Nchi hii utawala bora kwa kipindi cha Awamu ya Tano inaonesha kabisa utawala bora katika nchi hii sasa umetoweka kabisa. Nasema kwamba utawala bora umetoweka, sasa hivi hali ya watumishi katika nchi hii imekuwa ni tete, kila mtumishi amekaa akisubiri matamko, ana wasiwasi na shughuli ambazo anakwenda kuzifanya, haamini kama kesho ataamka akiendelea kuwa mtumishi wa umma katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hali ilivyo katika nchi hii sasa hivi. Jeshi la Polisi sasa wanakamata watu hovyo hovyo, Jeshi la Polisi wanaagizwa, Jeshi la Polisi wanasema wameshindwa kufanya kazi zao bila maagizo kutoka juu, hili jambo tumeliona hata kwenye uchaguzi uliopita. Katika uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa, Madiwani na Wabunge tumeona hali ilivyokuwa tete katika uchaguzi huu. Imeonesha kabisa kwamba katika kituo cha uchaguzi hasa siku ya kupiga kura walikuja Polisi wengi ambao walikuwa wana mbwa na silaha nyingi kabisa, kiasi kwamba waliwatisha wapiga kura lakini pia walizuia hata Mawakala ambao walikuwa wanatakiwa kuhakiki uhesabuji wa kura wasiingie katika vituo vya kupigia kura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba kutokana na jambo hili, hata leo Chama cha Mapinduzi wanajinafasi kwamba wamepata kura nyingi na wameshinda lakini tunataka kusema kwamba asilimia kubwa ya matokeo yaliyojitokeza yanaonesha kabisa yalihujumiwa. Tunasema yalihujumiwa na hili tunalizungumza hapa watu wengi watazomea na wataona ni jambo ambalo kama vile tunatania, lakini tunazungumza ukweli na hili lina mwisho. Itafika mahali Watanzania watachukia na watakataa dhuluma pamoja na uonevu unaojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana jambo la uchaguzi na jambo la haki za watu wanapokwenda kupiga kura ni lazima lilindwe. Sheria za nchi sasa hivi hazifuatwi na viongozi wengi wanakaa madarakani kwa sababu eti amesimamia vibaya uchaguzi na kuiba kura kuhakikisha kwamba CCM wanashinda uchaguzi. Jambo hili linasumbua sana na watu sasa hivi wameanza kukata tamaa ya kwenda kupiga kura.
Mheshimiwa Mweyekiti, nikupe mfano mmoja; Kata ya Kijichi wapiga kura walikuwa karibuni 16,800 mwaka 2015 kwenye Uchaguzi Mkuu lakini safari hii wapiga kura waliojitokeza ni 5,000 tu. Hii inaashiria kwamba Watanzania wameanza kukata tamaa na wanaona hawana haja ya kwenda kupiga kura kwa sababu hata wakipiga kura, kura zao na matokeo yao yanahujumiwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka kusema kwamba ni vizuri pia Serikali hii ikajua kwamba hizi ni haki za watu na watu wanavyokwenda kufanya uchaguzi, waacheni wafanye uchaguzi wamchague kiongozi wanayemtaka atakayeweza kuwaongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine imetokea sasa hivi, kila jambo linalozungumzwa na mtu hata kiongozi akisema kwake kuna njaa wanasema umekuwa mchochezi. Ni vizuri Serikali ikajaribu kutoa ufafanuzi, uchochezi maana yake nini? Jambo la kweli ambalo linazungumzwa nalo limeshakuwa uchochezi. Nchi hii watu watashindwa kuzungumza, watakaa kimya na wakikaa kimya tunakoelekea siyo kuzuri hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa kwenye kampeni maeneo mbalimbali. Ukizungumzia hali halisi ya chakula katika nchi hii nashangaa baadhi ya viongozi ndani ya Serikali hii wamekwenda kutoa matangazo katika mikoa mbalimbali kwamba mtu yoyote atakayesema kwamba kuna njaa anatakiwa kukamatwa. Haya ni mambo ya ajabu kabisa. Njaa haifichiki hata siku moja, njaa iko wazi.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kukushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii, lakini pia naishukuru sana Kamati kwa maoni yake ambayo wamejaribu kutoa na ushauri mbalimbali walioutoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, siku zote nikisimama nikiwa nachangia hasa kuhusiana na mambo ya bajeti au na masuala ya fedha, najaribu kuzungumza sana kuhusiana na siasa kuondoka kwenye masuala ya kiutendaji. Masuala ya kiutendaji yakiingiliwa sana na siasa kama tunavyofanya sasa hivi katika nchi hii, lazima tukubaliane kabisa kwamba hatutaweza kufanya vizuri na tusitegemee kabisa kama Taifa hili litabadilika kama wataalam wetu ambao tumewasomesha kwa gharama kubwa na tumewapa majukumu wanashindwa kutekeleza wajibu wao, wanashindwa kuishauri Serikali kitaalam na sisi tunatoa maagizo kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia na nimejaribu kupima bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 na ushauri mbalimbali ambao umetolewa na Kamati. Ukijaribu kuangalia utaona kabisa kwamba sisi wakati tuko Bungeni humu tunatengeneza bajeti hii, sisi kama Upinzani tulitoa Bajeti Elekezi, ili kidogo vitu ambavyo viko mle viweze kuchukuliwa kama msaada wa kusaidia bajeti hii. Kilichotokea, tulionekana watu wa hovyo, tulibezwa humu ndani na baadaye ilionekana kwamba hata bajeti yetu isingeweza kusomwa na watu hawakuipitia kuangalia nini ambacho kinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana wenzetu ambao walikuwemo humu wanapitisha hii bajeti, leo wanalalamika na wao. Nami nashangaa, hata wewe Mheshimiwa Mapunda! Hata wewe fulani! Nashangaa sana, yaani wanalalamika wakati bajeti walipitisha wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba uko upungufu mwingi sana ambao tuliukataa na tulishauri humu ndani. Tulianza na suala la VAT, tukajaribu kueleza hali halisi kwamba ndugu zangu mkiweka VAT kwenye masuala ya utalii mtapunguza pato la Taifa kwenye Idara ya Utalii. Tukawaambia ondoeni, angalieni wenzenu Kenya na Mataifa mengine yanafanya hivyo. Watu mkabeza mkasema haiwezekani, tunaweka sisi. Leo hii kila mmoja anashangaa humu ndani utafikiri hakuwemo Bungeni wakati wanapitisha bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu kwamba, sisi Wabunge tumepewa dhamana na wananchi kwa ajili ya kuishauri Serikali na kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, wajibu wetu ni lazima tuutekeleze tukiwa ndani ya Bunge hili. Tukiendelea kuendekeza siasa ndani ya Bunge hili ni lazima tufike mahali ambapo tutaendelea kushindwa na kufeli na kila siku tutakuwa tunashtuka humu utafikiri hatukupitisha na kujadili sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kusema, tunachotaka kushauri hapa ni kwamba, ni lazima turudi kwenye misingi. Lazima Serikali ikubali kushauriwa na kama Serikali haitakubali kushauriwa, itaendelea kufunga masikio na kuendelea kuona Wabunge wanachozungumza ni hamna! Mheshimiwa Magufuli, kama Rais wetu, ni lazima akubaliane na sisi kwamba, sisi kama Wabunge tuliopewa majukumu haya, ni lazima akubali ushauri wa Wabunge. Sisi ndio tunaoishauri Serikali na kuisimamia Serikali, kwa hiyo, akubali ushauri wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulizungumza sana kuhusiana na hali halisi ya watumishi kukusanya mapato kwenye Halmashauri zetu. Leo Halmashauri zetu kwenye nchi hii, zote ambazo zilipelekwa kwenye majaribio, ziko chini ya 24% kwenye nchi hii katika makusanyo yake. Ni kwa sababu, watumishi waliokwenda kukusanya yale mapato wameshindwa kufikia malengo kwa sababu, watumishi ni wachache katika Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali tunazungumza hapa tunasema kwamba, makusanyo yanakwenda vizuri. Nataka kusema tu kwamba, fedha ambazo zimekusanywa kwenye Halmashauri zetu ziko chini kabisa. Sasa Serikali sijui kama nayo itachukua nafasi ya kuweza kufidia fedha ambazo tumeshindwa kukusanya kwenye Halmashauri zetu. Sielewi kama zitafidiwa fedha hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia kwenye Taarifa ya Kamati hapa, ukisoma kwenye ukurasa wa 26 kwenye kipengele cha 2.52 - Matumizi ya Serikali. Ukiangalia, utaona kabisa katika quarter ya kwanza katika Halmashauri, fedha kwenye Halmashauri zetu haikupelekwa hata shilingi kwenye upande wa utawala. Kwa hiyo, fedha ambazo zinatumika sasa hivi kwa ajili ya kuendeshea shughuli za utawala kwenye Halmashauri zetu, zinatumika fedha za vyanzo vya ndani, kitu ambacho kinarudisha utendaji kazi wa Halmashauri zetu. Nasi kama Halmashauri, tunashindwa kutekeleza majukumu ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba, ni lazima tukubaliane tukiwa tunatengeneza bajeti hii tujue kwamba ni bajeti ya Serikali, siyo bajeti ya vyama vya siasa. Kwa hiyo, lazima tunapoingia kwenye bajeti hizi, tukae tukubaliane, tusikilizane, tupokee ushauri wa kila mmoja wetu ili kujenga nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia shughuli mbalimbali ambazo zimefanyika na mambo ambayo yameshindwa kufanyika katika bajeti hii. Ukijaribu kuangalia katika hali halisi, Serikali yoyote duniani ina wajibu wa kuwajengea wafanyabiashara wadogo wadogo na wafanyabisahara wakubwa mazingira ya kufanya biashara ili wafanyabiashara wakubwa waweze kupata mitaji mikubwa ili waweze kulipa kodi ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yoyote makini inaendesha Serikali yake kwa kutumia kodi. Leo hii Watanzania wengi katika nchi hii wameshindwa kufanya biashara kwa sababu ya masharti magumu ambayo Serikali imeyaweka. Pia, Serikali hii haichukui hata jukumu la kuwaelimisha walipakodi wa nchi hii, ni nini ambacho kinalipwa katika Serikali hii. Wananchi hawaelewi; Watanzania hawajui! Watanzania wanajiuliza, kinacholipwa ni mtaji? Ni faida au ni kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania sasa hivi wanaviziwa, wanapangiwa fedha ambayo haiwezekani, wengine wanafunga maduka, wengine wanaacha biashara zao, wanahamisha biashara zao, Serikali haichukui jukumu la kuwafundisha na kuwaeleza wananchi nini ambacho kinatakiwa kilipwe kama kodi ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajibu wa Serikali ni kuhakikisha kwamba inawaelimisha wananchi nini ambacho kinalipwa ili wananchi walipe kodi na Serikali iweze kupata fedha, lakini Serikali haina muda huo. Ni lazima tukubaliane, kama wananchi wataendelea kuwa maskini, biashara zao zitaendelea kufungwa na Serikali hii. Maduka sasa hivi tunahesabu. Ukienda Dar es Salaam wanakwambia maduka 300 yamefungwa; ukienda Mwanza wanasema maduka 200 yamefungwa; ukienda Mbeya wanasema maduka 300 yamefungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema inatekeleza wajibu wake wakati watu wanaendelea kufunga maduka na uchumi unazidi kushuka katika nchi hii. Kwa hiyo, ninachotaka kusema, ni lazima Serikali ijikite kabisa kuwaelimisha wananchi na kuweka ustawi wa biashara zao ili wafanyabiashara wafanye biashara, mitaji ikue na waweze kuwa walipa kodi katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine la mikopo. Wanafunzi wamepewa mikopo mwaka 2016, lakini kitu cha kushangaza, sasa hivi ukienda mashuleni, ukienda UDOM hapa sasa hivi kuna wanafunzi ambao wameambiwa hawana sifa tena za kukopeshwa. Tunataka Serikali itupe ufafanuzi; kama mtoto alipata mkopo awamu ya kwanza, leo hii wanasema kwamba hana sifa ya kupata mkopo, tafsiri yake ni nini? Serikali haina fedha? Au nini kilichotokea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi sasa hivi hawaelewi kinachoendelea. Watoto wao wanapata shida, hawaelewi nini kitakachotokea hapo mbele ya safari. Kwa hiyo, tunataka tupate majibu; kama Serikali haina fedha, iseme kwa wananchi kwamba Serikali haina fedha ili wazazi wa wototo hawa waangalie ni namna gani watahangaika na watoto wao kuliko kuanza kuwahangaisha watoto ambao wameshalipiwa mkopo kwa Awamu ya Kwanza na leo hii wanaambiwa kwamba hizo fedha hazipo na watoto hawana sifa za kuweza kupewa tena mikopo. Ni jambo la kushangaza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kilimo. Wakati tunapitisha bajeti hapa, tulishangaa sana. Huko nyuma tulikuwa tunasema wakulima wanapata pembejeo kidogo, Serikali iongeze bajeti, lakini mwaka 2016 hapa wakati tunatengeneza bajeti, tulishangaa Serikali inaondoa shilingi bilioni 47 kwenye ruzuku ya Serikali kwa ajili ya wakulima, tukashangaa. Serikali hii inajinafasi kwamba inataka kuwa ni Serikali ya viwanda, huku inaondoa shilingi bilioni 47 kwenye bajeti. Leo hii mnashangaa kwa nini kuna 0.5 ambayo imeshuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnashangaa kitu gani wakati mliondoa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.

The Tanzania Fisheries Research Institute Bill, 2016

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nichangie Muswada huu. Muswada huu umekuja kipindi muhimu sana lakini tunachotaka kukizungumza sisi kama Watanzania ni lazima tubadilike sana katika kuhakikisha kwamba tunatekeleza wajibu wetu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti mbalimbali zimekuwa zikifanywa katika nchi hii lakini tatizo kubwa ni kwamba zikishafanyika zinawekwa katika makabati haziwafikii wananchi na hata siku moja hawajaona ni namna gani tafiti hizi zimewasaidia. Ndiyo maana ukiangalia sasa hivi utaona wakulima wetu hawajui walime nini katika maeneo yao kwa kuongozwa na hawa watu ambao wamefanya utafiti. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali tunapokuwa tumepitisha Miswada hii na kuwa sheria ni lazima zianze kufanya kazi tena kwa vitendo kabisa.
Mheshimiwa mwenyekiti, nilikuwa najaribu kupitia Muswada huu na niliangalia baadhi ya maeneo ambayo nataka kuchangia sasa hivi lakini sijaona sehemu ambayo Msajili wa Hazina ametajwa. Jambo hili limenisikitisha kwa sababu ukisoma Sheria za Msajili wa Hazina zinaonesha kwamba Msajili wa Hazina ndiye mtu pekee ambaye anasimamia mashirika pamoja na taasisi mbalimbali ambazo zinaanzishwa katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza katika sheria hii sijaona inataja Msajili wa Hazina anahusika kuyasimamia mashirika pamoja na taasisi ambazo zinaanzishwa. Naomba sheria zote zinazotungwa sasa hivi zimtaje Msajili wa Hazina kama ndiye msimamizi mkuu wa mashirika na taasisi mbalimbali zinazoanzishwa katika nchi hii. Nia na madhumuni ni kumpa nafasi kubwa Msajili wa Hazina kuhakikisha kwamba anasimamia mashirika au taasisi hizi ambazo zinakwenda kuanzishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimeliona liko tofauti ni uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi, inaonesha kwamba Mheshimiwa Rais ndiye atachukua jukumu la kumteua Mwenyekiti wa Bodi lakini tumeona mashirika na taasisi mbalimbali ambazo Mheshimiwa Rais ameteua Wenyeviti hawa 90% ni wazee ambao walikuwa wameshastaafu na leo wamerudishwa kazini. Kwa hiyo, wanapata nafasi hizi kama vile fadhila kutoka kwa Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaomba sasa uteuzi huu wa Mwenyekiti wa Bodi ni lazima Mheshimiwa Rais ashauriane na Msajili wa Hazina ili Msajili wa Hazina aweze kumsaidia Mheshimiwa Rais ni namna gani anaweza akapata Mwenyekiti wa Bodi ambaye anaweza kuisaidia Bodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana sasa hivi unaona mashirika na taasisi nyingi zinakufa na hazifanyi kazi ipasavyo kwa sababu watu wanaoteuliwa kwa kweli ni wazee na ambao hawawezi kutoa mawazo mazuri na wakafanya kazi nzuri. Kwa hiyo, tunashauri sheria hii ifanye mabadiliko na kuhakikisha kwamba wakati Mheshimiwa Rais anamteua Mwenyekiti wa Bodi lazima ashirikiane na Msajili wa Hazina ili kuboresha uteuzi huo tupate Mwenyekiti wa Bodi bora na anayeweza kusaidia taasisi au shirika kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona mashirika mbalimbali ambayo Mheshimiwa Rais amekuwa akiteua Wenyeviti wa Bodi ufanisi wake umekuwa ni mdogo sana. Kwa hiyo, tunaomba sana TR aweze kushiriki kwa 90% katika uteuzi wa viongozi mbalimbali au viongozi wa Bodi ambao wanateuliwa katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria hii haijatuonesha tafiti mbalimbali ambazo zitafanyika kama zitakuwa zimekosewa na kusababisha hasara kwa wakulima au wafugaji wetu, ni namna gani wananchi hawa wanaweza wakafidiwa na Serikali kwa sababu ya utafiti ambao unakuwa umefanyika vibaya. Tunachokiona pale ni kwamba kama watakuwa wamefanya utafiti na baadaye utafiti ule ukasababisha hasara kwa wakulima na wafugaji ni kwamba wale watu hawawezi kushtakiwa wala hakuna hatua zozote ambazo zinaweza zikachukuliwa dhidi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaleta mkanganyiko na tunaomba sana tujue juu ya suala hili. Hata Wabunge wengine wamesema wamenunua mbegu za mahindi wakipanda hazioti na kuingia hasara kwa sababu msimu unakuwa umeshapita. Kwa hiyo, lazima pia sheria ioneshe kwamba kama utafiti utafanyika vibaya na ukasababisha hasara kwa wananchi wetu ni lazima wananchi hawa ambao wamepata hasara waweze kufidiwa ili maisha yao yaweze kuendelea kama ambavyo walitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nilikuwa naangalia orodha ya vituo vya utafiti katika Jedwali sijakiona Kituo cha Utafiti cha Mbimba kilichopo Wilayani Mbozi katika Mkoa wa Songwe. Kituo kile kinaendelea kufanya utafiti kwa muda mrefu lakini hakipo hapa. Kwa hiyo, wakati Mheshimiwa Waziri anakuja kuhitimisha atueleze ni kwa nini Kituo hiki cha Mbimba kilichopo Wilayani Mbozi katika Mkoa wa Songwe hakionekani kabisa kama ni kituo ambacho kipo wakati ni cha muda mrefu. Kwa hiyo, tutaomba pia tupate maelezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kuhusu kituo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni katika kifungu 27(1), kinasema kwamba Taasisi ya Utafiti inaweza ikakopa na ili iweze kukopa ni lazima Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Kilimo watoe idhini. Naomba tuendelee kupitia Sheria za TR (Msajili wa Hazina) kwani ndiye mtu pekee ambaye amepewa majukumu na mamlaka ya kuamua kwamba shirika au taasisi hii inaweza ikakopa kutokana na mpango kazi ambao inao kama inaweza ikarejesha zile fedha au zinaweza zikaleta tija katika Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba wakati tunamzungumzia Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Kilimo ni lazima pia TR ashiriki kujua endapo mkopo huo ambao taasisi inaenda kuchukua utaleta tija katika Taifa hili na siyo Waziri mwenye dhamana pamoja na Waziri wa Fedha kushiriki peke yao. Kwa hiyo, naomba sana…

MWENYEKITI: Ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's