Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Japhet Ngailonga Hasunga

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utakuwa katika maeneo yafuatayo:-
Kwanza, mafunzo ya awali kwa Watumishi wa Umma. Serikali ihakikishe kwamba waajiriwa wote katika Utumishi wa Umma wanapoajiriwa kwa mara ya kwanza wanapatiwa mafunzo elekezi katika maeneo mbalimbali kama vile, uwajibikaji, maadili, OPRAS, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali. Bajeti ya mafunzo ipelekwe Utumishi ili Chuo cha Utumishi kitoe mafunzo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile viongozi wanaoteuliwa katika ngazi mbalimbali wapewe induction na orientation ya majukumu yao ya kusimamia rasilimali watu, fedha na mali za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni suala la OPRAS, lazima ifike mahali Serikali kuanza kuwachukulia hatua watumishi ambao hawajazi fomu za OPRAS. Pia Taasisi zisizofanya vizuri na zinazofanya vizuri, katika kutekeleza OPRAS zitangazwe hadharani ili wananchi wote wajue. Sanjari na hilo vigezo vya kupima taasisi mbalimbali vitayarishwe na kuanza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, ni fedha za TASAF awamu ya tatu katika baadhi ya maeneo; fedha hizi zinalipwa kwa wasiohusika kama pale Vwawa Mjini na baadhi ya vijiji, hebu fanyeni uchambuzi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nnem ni usimamizi wa malipo ya mishahara; kuna haja ya kuongeza jitihada za kusimamia mfumo wa mishahara (Lawson version 9), bado Watumishi hawaitumii sawa na kusababisha ucheleweshaji wa malipo kwa baadhi ya watumishi. Waajiriwa wapya ni waathirika sana wa hili. Pia watu wanaoachishwa kazi na kustaafu kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tano, ni kuboresha miundo ya Utumishi katika Kada mbalimbali. Hivi sasa miundo ya Kada nyingi imepitwa na wakati, lini mtaanza kuipitia upya miundo hiyo? Pia taasisi nyingi zimekuwa zinaanzishwa bila kuwa na miundo ya Taasisi husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la sita, ni kuhusu Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania. Kwa kuwa, Chuo hiki kilianzishwa ili kutoa mafunzo ya Uongozi, Menejimenti na Utawala Serikalini, je, ni lini hasa Serikali itaanza kukitumia Chuo hiki ipasavyo ili kitoe mchango unaohitajika katika kujenga rasimali watu iliyotukuka. Sanjari na hilo Chuo kinategemea kufundisha Watumishi wa Umma wangapi katika mwaka wa fedha 2016/2017. Pia ningependa kujua tafiti ngapi na katika maeneo yapi chuo kimepanga kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Vwawa kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwakilishi wao katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa na wananchi wa nchi hii na pia Baraza la Mawaziri na viongozi wengine wote ambao wamepewa dhamana ya kuiongoza nchi hii, nawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba niupongeze Uongozi wa Bunge, nikitambua kabisa kwamba kazi kubwa tuliyonayo ya Bunge hili ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Kama kazi yetu ni kuisimamia Serikali na kuishauri, maana yake kama mambo yatakuwa hayaendi vizuri, basi Bunge hili haliwezi kukwepa wajibu kwamba hatujafanya kazi yetu vizuri ya kuisimamia na kuishauri Serikali. Kwa hiyo, napenda nichukue nafasi hii kuwashukuruni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa kwamba sasa tumepata viongozi wazuri wanaoweza kuikokota na kuisukuma nchi yetu ikafika kuwa nchi ya kipato cha kati. Kwa muda mrefu tulikuwa tunatafuta viongozi, tulikuwa tunatafuta Rais ambaye ana maono ya mbali, sasa Mungu ametupa uwezo, tumebahatika tumepata Rais mwenye maono ya mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni tajiri sana kwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba, ambayo imejaa karibu kila kona. Tuna madini ya kila namna, tuna misitu, tuna mlima mrefu kuliko milima yote katika Afrika na wa pili duniani kwa urefu, tuna mbuga nyingi za wanyama, mito, maziwa, bahari na zaidi ya hapo tuna watu zaidi ya milioni 53. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni competitive advantage ambayo tunayo. Kwa maana hiyo, tuna vitu vingi vinavyoweza kuiwezesha nchi yetu kuendelea na kufika kuwa nchi ya kipato cha kati. Sasa tatizo kwa muda mrefu limekuwa ni nini? Tatizo kubwa ni tatizo la uongozi na hili ndio limekuwa likitusumbua sana. Sasa wakati huu tumepata viongozi, nadhani tutaweza kwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha kwa kuleta Mpango huu na kueleza dira na kuonekana mambo ambayo tunaweza kuyafanya. Mpango huu umezingatia dira ya Taifa na pia umezingatia Hotuba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naomba nichangie katika eneo la kilimo. Katika Mpango huu kilimo bado hakijapewa nafasi nzuri sana na hakijapewa mkazo kama ambavyo kingekuwa kimepewa. Sisi kule Wanavwawa ni wakulima, wananchi wa Vwawa wanalima sana, tunalima kahawa kwa wingi, mahindi, tunalima mazao mengi na tunaamini kabisa kama Serikali itatuwekea misingi mizuri, ikatupatia pembejeo kwa wakati, tuna uwezo wa kuzalisha chakula kwa kingi ambacho kinaweza kikatumika sehemu nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe wazo kwamba tusiseme mazao ya biashara, sasa kila zao ni zao la biashara, hata mahindi ni zao la biashara, hata maharage ni zao la biashara. Kwa hiyo, mazao yote yanayoweza kulimwa yapewe uzito unaostahili ili tuweze kuzalisha chakula kingi, tuweze kuzalisha kwa ajili ya kuuza sehemu zinginezo. Kwa hiyo, kilimo ni muhimu sana tukakipa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, ambayo ningependa nichangie, tumezungumzia viwanda, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa ni Serikali ya viwanda. Hata hivyo, viwanda ambavyo tumesema, nimesoma kwenye huu Mpango hatujaainisha, tunataka viwanda vingapi na viwe wapi? Hilo hatujalisema, lakini pia tulikuwa na viwanda vingi sana ambavyo vilijengwa katika nchi hii, nini kilitokea viwanda hivyo vyote vikafa? Tulikuwa na mikakati mingi ambayo tuliweka juu ya viwanda, tumejifunza nini katika mipango yote tuliyokuwa nayo katika kujenga viwanda vilivyopita? Sasa haya yanatakiwa yawe ni msingi mzuri wa kutuwezesha kuweka mikakati mizuri ya kuweza kujenga viwanda tunavyovihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ili tuweze kwenda sambamba kufika kwenye hiyo nchi ya viwanda, tunahitaji viwezesha, vitu vitakavyotuwezesha kufika huko, tunahitaji umeme, barabara na vitu vingine vingi. Sasa naomba nichangie kwenye suala la umeme; umeme wa REA umesambazwa nchi nzima katika vijiji vingi sana. Katika Jimbo langu kule watu wengi wamepata, lakini vijiji vingi bado havina umeme. Kuna Vijiji kama Nanyara, Nswiga, Irabii umeme unapita juu kwa miaka mingi, unawaruka wananchi unakwenda wapi, wananchi wale wanahitaji wapate ule umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema kwamba umeme ni muhimu sana na Mheshimiwa Waziri wa Nishati ameona kule kuna joto ardhi, kule kuna chanzo kizuri sana cha kuweza kuzalisha umeme. Naomba mkazo uwepo katika kuanzisha na kutumia nishati hii inayotokana na joto ardhi ambayo inaweza ikatusaidia sana kutukwamua katika suala hili la umeme ambalo ni muhimu sana katika kuipeleka nchi kuwa nchi ya kipato cha kati.
Suala lingine ambalo ningependa kuchangia, ili tuweze kuwa nchi ya kipato cha kati, tunahitaji wataalam wetu, tunahitaji watu wawe na ujuzi wa kuweza kufanya kazi na kuweza kutekeleza majukumu yetu. Sasa hivi vyuo vyetu tulivyonavyo na mfumo wa elimu tulionao, hauwaandai vijana kuweza kupata ujuzi unaohitajika sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tunayo kazi kubwa ambayo napenda nishauri, Wizara ya Elimu tutafakari kwa undani mitaala tuliyonayo inatuandaa, inawaandaa vijana wetu kwenda kuwa nchi ya kipato cha kati? Sasa hivi mkazo utatiliwa kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu. Naomba nishauri, lazima tuwe na vyuo vingi vinavyotoa elimu ya kati tertiary institutions ambazo zitatoa wataalam watakaoweza kushiriki kufanya kazi katika viwanda tunavyovihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye upande wa elimu, ningependa mitaala ile wakati inaandaliwa, iandaliwe vizuri, iwe ni demand driven rather than supply driven, halafu wapatiwe sehemu za kwenda kufanya field ili waweze kuiva na kukomaa hilo litatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka naomba nishauri mambo mengine yafuatayo:-
Kwanza, ili tuweze kufika na kutekeleza mpango huu ambao ni mzuri, nashauri, lazima tuweke nguvu sana katika ukusanyaji wa mapato, bila kukusanya mapato huu Mpango utakuwa hautekelezeki. Sasa hivi lazima tuweke mkakati wa kutosha wa kuhakikisha kwamba nchi inajitegemea kimapato kuliko kutegemea wafadhili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, tubadilike kifikra ili watu watambue kwamba wajibu wa maendeleo ya nchi hii ni sisi wenyewe ndiyo tutakaoleta maendeleo, ni wananchi wa nchi hii ndiyo watakaoleta maendeleo na si mtu mwingine.
La tatu, naomba kushauri, tumekuwa tukiimba kila wakati kwamba huko vijijini wananchi wanahitaji huduma za fedha, bila kupeleka huduma za fedha, bila kuanzisha hizi micro-institutions za kuweza kuwa-support wakulima, ku-support watu mbalimbali huko vijijini, ku-support vikundi mbalimbali, hatuwezi kuleta maendeleo ya kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri tuimarishe huduma za fedha mpaka vijijini ili wananchi wetu waweze kupata mikopo mbalimbali na kugharamia vitu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni vipaumbele, tunahitaji tuwe na vipaumbele vichache, ambavyo vitagharamiwa na Serikali. Viwanda naamini vitagharamiwa vitakuwa vinaendeshwa na watu binafsi siyo Serikali tena. Sitegemei kuona Serikali inaweka mkono mkubwa wa kuendesha viwanda wakati uwezo wetu ni mdogo, labda viwanda vile ambavyo ni strategic, lakini viwanda vitaendeshwa na private sector. Katika maeneo ya elimu, kilimo, uvuvi na ufugaji, afya na maji, miundombinu, barabara, viwanja vya ndege, umeme; hivyo Serikali lazima iwekeze vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba nishauri tumezungumzia sana kwamba tunahitaji viongozi ili waweze kuisukuma nchi hii. Hata hivyo, katika nchi hii hatuna utaratibu wa kuandaa viongozi, wala wa kuwafundisha, wala kuwaelekeza namna ya kutekeleza majukumu yao.
Sasa umefika wakati tuwe na mfumo mzuri wa kutambua viongozi wazuri na kuwaendeleza na kutambua vipaji vyao ili wakabidhiwe kufuatana na uwezo walionao. Hilo litatusaidia kuwa na viongozi wanaoweza kujenga, wazalendo wenye uwezo wa kuleta maendeleo ya kweli katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana na pia naomba Serikali izingatie mawazo yetu. (Makofi)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa Mpango huu ambao ametuletea, Mpango wa Pili wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 mpaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nimefurahishwa sana na Mpango huu ambao umeletwa mbele yetu. Mpango huu umeeleza bayana vipaumbele ambavyo Serikali inategemea kutekeleza katika kipindi hiki cha miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vipaumbele hivyo ambavyo ni msingi mkubwa sana wa maendeleo ya nchi yetu mambo yako mengi lakini suala la kwanza ambalo ni la msingi sana ni kuendeleza kilimo. Suala la kilimo inabidi lipewe kipaumbele cha kutosha. Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yetu, kilimo ndiyo kinachotoa ajira kubwa kwa wananchi wengi katika nchi yetu, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea kilimo. Pia tunapotaka kuipeleka nchi kuwa ya viwanda tunategemea zaidi kwamba malighafi nyingi na mazao mengi yatakuwa ni yale yanayotokana na kilimo na hivyo viwanda vingi ambavyo tunavianzisha vitakuwa vile vitakavyochakata mazao yanayotokana na kilimo. Naomba tuongeze jitihada kabisa za kuhakikisha tunakiimarisha hiki kilimo, pembejeo zile zinazohitajika katika kufufua kilimo hiki ziongezeke na bajeti ya kilimo iongezeke ili kwenda kujenga nchi ya uchumi safi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiofichika kwamba kama tukikifufua kilimo, tukiimarisha viwanda vinavyotokana na mazao ya kilimo, asilimia kubwa sana ya watu wetu wataajiriwa. Nashauri Serikali ihakikishe tunajenga viwanda vitakavyochakata mazao haya ya kilimo. Viwanda hivi vitasaidia sana kutoa ajira na msukumo mkubwa katika kuchangia pato la Taifa.
Kipaumbele cha pili ambacho kinaendana na hicho cha kilimo ni kuimarisha miundombinu mbalimbali ambayo ita-support hicho kilimo chetu. Miundombinu ya barabara, umeme na vitu vingine vinavyoendana na hivyo vitasaidia sana kuhakikisha nchi yetu inaendelea. Pia miundombinu hiyo itatoa ajira kwa vijana wetu wengi katika nchi yetu. Kwa hiyo, lazima tuweke nguvu zaidi katika kuimarisha hiyo miundombinu ya reli na vitu vinginevyo.
Nimefarijika sana na jitihada za Serikali za kuamua kufufua Shirika letu la Ndege. Katika ulimwengu huu kila nchi ina shirika lake na Shirika la Ndege ndiyo linatoa mchango mkubwa sana katika kuendeleza nchi. Tumeona nchi mbalimbali jinsi zinavyofanya. Kwa kweli inasikitisha sana kuona shirika letu limekuwa likisuasua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi jitihada ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuzichukua katika kulifufua shirika hili lazima tuziunge mkono kwa udi na uvumba ili kuhakikisha linakua na linatoa ajira nyingi kwa vijana wetu lakini pia tuweze kulitumia katika kuharakisha kuchochea maendeleo katika sehemu mbalimbali. Shirika letu sasa hivi lina ndege moja au mbili …
WABUNGE FULANI: Hamna.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hizi ndege ambazo tumepanga kuzinunua zikinunuliwa naamini zitachochea sana maendeleo ya nchi yetu. Kwa hiyo, tuongeze hizo jitihada. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuleta maendeleo ya kweli lazima huduma mbalimbali zikiwemo huduma za masuala ya fedha ziimarike. Hivi sasa mabenki mengi yamekuwa yakifanya biashara maeneo ya mijini hayakuweza kwenda vijijini. Sasa hivi Benki ya Wakulima imeanzishwa lakini bado iko Dar es Salaam. Nashauri kama ni Benki ya Wakulima ianzishwe mikoani ili wakulima wapate nafasi ya kwenda kukopa huko na tuweze kufufua kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mabenki yetu mengi yalikuwa yanafanya biashara kwa kutegemea fedha za Serikali. Kwa hiyo, naomba niunge mkono jitihada za Serikali, sasa hivi za kuhakikisha fedha zote za Serikali zinakuwa Benki Kuu ili mabenki haya yaende sasa kutafuta wateja huko vijijini na hii itasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, wakati Serikali inachukua jitihada za kubana matumizi na hivyo kuondoa fedha nyingi za Serikali kwenye mabenki maana yake sasa mabenki nayo lazima yafanye jitihada za makusudi za kuhakikisha kwamba riba za mikopo zinashuka. Sasa hivi riba ziko juu sana, wananchi wakikopa baada ya miaka miwili, mitatu unakuta deni ni mara mbili ya kile ambacho alikuwa amechukua hali ambayo haisaidii kuchochea maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani kwa kuangalia riba zile za kukopa na riba ambazo wanazitoa kuna spread kubwa ambayo nafikiri Serikali pamoja na mabenki yachukue hatua zinazostahili kuhakikisha kwamba yanarekebisha hiyo hali ili kusudi benki hizi zichochee maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mpango huu umejikita katika utoaji wa huduma za jamii hasa suala la elimu. Suala la elimu limepewa uzito mkubwa na naunga mkono kwani bila kuimarisha elimu hatuwezi kuwa nchi ya kipato cha kati. Elimu hii ndiyo itakayotuwezesha tupate watalaam wazuri, tupate watalaam wa kati wanaohitajika katika viwanda vyetu. Lazima mitaala ya elimu zetu kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu ipitiwe upya ili iendane na mahitaji halisi ya wakati tulionao. Hilo naamini linawezekana kwa kutumia watalaam na uwezo uliopo tunaweza tukafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vyetu vinahitaji wataalam, sasa hivi vijana wengi wamekuwa wakikimbilia sana kwenda kusoma kwenye vyuo vya elimu ya juu wanakuwa ni ma-engineer, lakini nadhani kuna haja ya kuimarisha elimu ya mafundi wale wa kati na hasa vyuo vyetu hivi vya VETA na vyuo vinginevyo. Hivi ndivyo vitakavyoweza kuchukuwa vijana wengi na kuwapa ujuzi unaohitajika katika viwanda vingi. Kwa hiyo, hizi jitihada lazima ziungwe mkono kwa hali na mali ili tuhakikishe kwamba tunafika kule tunakokusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kupongeza Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha kwamba elimu yetu inakuwa bure kwenye shule za msingi na sekondari mpaka kidato cha kumi na mbili. Kwa kweli hili ni suala zuri sana lazima tuipongeze Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tumeanza kuitekeleza hii sera imeonyesha matumaini na matunda makubwa kwani watoto wengi wameweza kwenda shule na kuandikishwa. Sasa lazima tuhakikishe kwamba tunaunga mkono jitihada hizi na tunashirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuhakikisha hii azma inatekelezeka. Zipo changamoto ambazo tutakabiliana nazo na ni kitu cha kawaida. Unapoamua kuanzisha kitu chochote lazima ukabiliane na changamoto ambazo naamini tutashinda na tutafika mahali pazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia suala la afya. Jitahada za Serikali ya CCM sasa hivi ambazo tumejikita nazo na tumeiweka kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi kwamba kila kijiji kuwe na zahanati na tunataka kila kata kuwe na kituo cha afya lakini vituo hivi vya afya vinahitaji pia viwe na wataalam. Jitihada ambazo wananchi wameanza kuonyesha kwa kujenga zahanati na vituo vya afya, Serikali iongeze mkakati wa kuhakikisha inawaunga mkono na pale ambapo wamekamilisha vianze kufanya kazi kama ambavyo inakusudiwa. Wananchi wamejitoa sana kuhakikisha wanajenga hivi vituo vya afya na zahanati, Serikali itekeleze wajibu wake pale ambapo tunaona kwamba panatakiwa kutekelezwa ili kusudi maendeleo yapatikane haraka kadri inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Mpango huu ni mzuri, mpango wa kuimarisha reli ya kati, mpango wa kujenga reli kwa standard gauge ni wa muhimu sana kwani utatusaidia sana kuchochea maendeleo katika mikao yote. Hii ndiyo njia pekee itakayotusaidia nchi yetu kuweza kuunganishwa na hizo nchi zingine na kupunguza gharama za uendeshaji ambazo sasa hivi zimekuwa ni kubwa sana. Sasa hivi barabara zetu zinabeba malori makubwa ambayo yanasababisha barabara zetu zisidumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tukiimarisha reli hii naamini itakuwa limesaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo machache, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JAPMheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni hifadhi ya jamii. Kwa kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi iliazimia kuanza kuwalipa pensheni wazee wote waliofikia umri mkubwa bila kujali walikuwa waajiriwa au laa, je, ni lini hasa ahadi hii ya kulipa pensheni kwa wazee hawa ambao wanaisubiri sana itatekelezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ni kwa lini Sera ya Hifadhi ya Jamii itaanza kutekelezwa kwa wananchi wote yaani wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara ili kila mwananchi afaidi mafao ya hifadhi ya jamii? Pia kuna mkakati gani wa kupunguza malalamiko ya wananchi ambao husumbuliwa sana na Mifuko ya Jamii kama NSSF na PPF? Je, hatua za kuboresha mifumo hii zimechukuliwa vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, sekta binafsi. Hivi sasa sekta binafsi ndiyo mhimili mkuu wa kukuza uchumi wa nchi yetu ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wengi zaidi. Hata hivyo, waajiri wengi wa sekta hii hususani kilimo, ulinzi, huduma za hotelini, biashara na viwanda wamekuwa hawatoi mikataba na barua za ajira na wakati mwingine masharti ya kazi ni magumu sana na ya kinyonyaji, mazingira yanatisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia baadhi ya waajiri hulipa mishahara duni ambayo haiendani na uzalishaji na haina tija. Lazima Serikali ihakikishe kwamba waajiri wote wanakuwa na mikataba na barua za ajira zinatolewa kwa wafanyakazi wote. Hili liende sambamba na kuimarisha Idara ya Kaguzi za Kazi ili ifanye kazi ya ukaguzi mara kwa mara na kutangaza hadharani waajiri ambao wanakiuka sheria za kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Serikali kuboresha kilimo. Ni lazima Serikali ije na makakati mpya wa kuinua kilimo ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa ruzuku, usambazaji wa pembejeo, masoko, chakula, kama vile kahawa, mahindi, maharage na kadhalika. Je, Serikali imefanya uchambuzi ili kuimarisha kilimo kwenye maeneo yenye tija na kujenga mazingira wezeshi ili kuongeza thamani ya mazao? Nashauri pale ambapo wananchi wanaweza kuuza nje mazao yao waruhusiwe kwani itasaidia kuongeza fedha za kigeni. Pia mkakati wa kuanzisha kilimo kikubwa ili kutoa ajira kwa vijana wetu umefikia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni mkakati wa kuanza kutengeneza magari na vipuli. Serikali lazima ifanye maamuzi magumu ya kimkakati ili kuanzisha kiwanda cha kutengeneza magari na vipuli vyake. Kiwanda hiki kitasaidia kuchukua vijana wetu wengi ambao wana ufundi mkubwa. Kuna mafundi wazuri katika mikoa yetu. Ni muhimu kuanza kutengeneza magari ambayo yatatumia gesi na mafuta. Pia itasaidia kufanya utafiti na kuziangalia projects za wanafunzi wa vyuo vya ufundi ambazo ni nzuri sana. Maamuzi haya ni muhimuHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwenye maeneo yafuatayo:
sana ili kutoa ajira na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kununulia magari na vipuli.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAPHET H. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumushi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwa kazi kubwa ambayo wameifanya na ambayo wameendelea kuifanya. Kwa kweli nawapongeza sana tena sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kuchukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa ujumla, Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa ikifanya kazi nzuri sana katika kuhakikisha kwamba maendeleo ya nchi hii yanasonga mbele. Kwa kweli hongera sana Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia kwanza katika mapato ya halmashauri. Katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwa undani sana hatua ambazo Serikali inakusudia kuchukua ili kuhakikisha kwamba inaimarisha mapato na mimi naunga mkono hizo jitihada ambazo Serikali inategemea kuchukua. Hata hivyo, kuna haja ya kuwa na mfumo mzuri kabisa, mfumo madhubuti wa kuhakikisha vyanzo vyote vya mapato vya Halmashauri vinasimamiwa vizuri. Bila kuwa na mfumo mzuri wa kusimamia mapato, tutapata matatizo makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali inasema tutaachana na mawakala ambao walikuwa wanakusanya Halmashauri zitaanza kukusanya zenyewe kwa kutumia mfumo wa electronic. Nashauri kwamba wakati tunakwenda kwenye huu mfumo basi ni vizuri Halmashauri zitakapowapangia wale watendaji wanaokwenda kukusanya wahakikishe kwamba wanawapa malengo na malengo hayo yasimamiwe vizuri ili wale watakaoshindwa kufikia malengo wachukuliwe hatua za dhati kabisa. Kwa sababu bila kufanya hivyo usimamizi wa mapato bado utaendelea kuwa mgumu na maeneo mengi kutakuwa na matatizo mengi sana ambayo tulikuwa tunayapata huko nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nimeshukuru suala la property tax kwamba sasa itakuwa inakusanywa na Halmashauri. Mimi nataka niongezee tu kusema kwamba property tax ilikuwa haikusanywi vizuri na ni eneo ambalo lina mapato mengi. Ukiangalia nyumba ambazo zipo katika maeneo ya mijini na maeneo mengine ni nyingi sana lakini nyingi zimekuwa hazilipi property tax. Kwa hiyo, ni vyema Halmashauri ziweke utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba majengo na maeneo yote yanalipa hiyo property tax ambayo itasaidia kuinua vyanzo vya mapato vya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo napenda nichangie ni kuhusu malipo ya walimu ambao walisimamia mitihani ya kidato cha nne mwaka jana. Walimu hawa walifanya kazi nzuri sana, walisimamia kwa uadilifu, walisimamia kwa uaminifu mkubwa na kazi yetu ikawa imekamilika vizuri. Kwenye Wilaya yangu ya Mbozi wale walimu mpaka leo hawajalipwa, naambiwa walilipwa posho ya siku tatu tu. Hili ni tatizo kubwa kwani linawavunja moyo sana walimu hawa ambao bado wana kazi kubwa sana ya kufanya na kuchangia katika maendeleo ya nchi hii. Juzi Mheshimiwa Waziri alitoa tamko kwamba sasa wanafanya jitihada kuhakikisha kwamba haya malipo yanakamilika. Naiomba Serikali itutamkie ni lini hasa ambapo walimu hawa watalipwa hayo malimbikizo yao ya hela zao za kusimamia mtihani, itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo napenda kuchangia ni hili suala la fedha shilingi milioni 50 ambazo tumejiwekea kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambazo tutapeleka katika vijiji na vitongoji. Hizi fedha zikienda tutakuwa tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana, zitatusaidia sana. Hata hivyo tuwe na mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba hizi fedha zitakapokuwa zinatolewa basi wale wanaokopa utaratibu wa kurudisha ieleweke ni wapi watakuwa wanarudisha na wengine watakuwa wanakopa na wengine wanarudisha. Kwa hiyo lazima, tuwe na mfumo ambao unaeleweka vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu afya. Kule Mbozi katika Jimbo langu la Vwawa, wananchi wameitikia wito sana wa kujenga zahanati na kushiriki katika ujenzi wa vituo vya afya. Zahanati nyingi zimejengwa ziko zaidi ya 40 na zimekamilika toka mwaka jana mpaka sasa hivi bado hazijafunguliwa. Naomba Serikali ije na mkakati ituambie ni lini hasa hizo zahanati zitafunguliwa ili zianze kufanya kazi kusudi wananchi waendelee kupata huduma zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda kuchangia kuhusu mafunzo ya awali kwa watumishi wa umma. Mafunzo ya awali kwa watumishi wa umma ambao wanaajiriwa kwa mara ya kwanza ni muhimu sana. Hivi sasa tumekuwa tukishuhudia kumomonyoka kwa maadili katika maeneo mengi. Watumishi wa umma wanapoajiriwa wakitoka mitaani wanakuwa bado hawajui miiko na utamaduni wa kufanya kazi kwenye utumishi wa umma. Sheria hii imeweka ni lazima ndani ya miezi sita wanatakiwa wapate mafunzo lakini hivi sasa waajiri wengi wamekuwa hawatekelezi agizo hilo. Naishauri Serikali ni vyema kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kile cha miezi sita wale watu wanapokuwa wameajiriwa kwenye utumishi wa umma wapatiwe mafunzo ili waweze kujua ni namna gani wanatakiwa kuendesha kazi zao na namna gani Serikali inatenda kazi zake. Hiyo itatusaidia sana katika kupunguza matatizo ambayo yamekuwa yaliyopo katika utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo la mafunzo ya awali lakini pia mafunzo elekezi. Mafunzo elekezi ni muhimu sana kwa watumishi wa umma hasa wale ambao wanakuwa wamefikia katika ngazi za kati na wanajiandaa kwenda kwenye ngazi za juu. Bila kupata mafunzo ya uongozi, mafunzo ya menejimenti hawa watu wanakuwa ni vigumu sana kuelewa. Kuna wengine wanakuwa ni wataalam wa fani zingine lakini unapokuwa umepata madaraka ya uongozi unatakiwa uongoze watu, kwa hiyo, ni lazima ujue masuala ya uongozi yanasemaje. Maana unatakiwa usimamie fedha, usimamie mali mbalimbali sasa lazima upate mafunzo ya kutosha kuhakikisha wanatenda kazi zao inavyotakiwa. Kwa kweli nashauri wote wapatiwe mafunzo haya elekezi hiyo itasaidia sana.
MHE. JAPHET H. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza jina langu naitwa Japhet Hasunga, siyo Joseph.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kwanza kushukuru kwa kupata nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii. Pia napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa hotuba nzuri ambayo ameitoa na mchanganuo mzuri ambao ameuwasilisha leo hii, kwa kweli nimefurahi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa uchambuzi wa kina walioufanya na kuiwasilisha katika Bunge lako Tukufu. Kwa kweli ni nzuri sana na imejenga msingi mzuri wa nini kinatakiwa kufanyika katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuchangia katika Sera ya Elimu ya shule za msingi na sekondari ya mwaka 2014. Sera hii ni nzuri sana ambayo imeandaliwa na iliwasilishwa na ilishirikisha wadau mbalimbali ambayo imeweka bayana hatua ambazo zinatakiwa kuchukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba nchi yetu inabadilika kwa hali tuliyonayo na kwenda mahali ambapo ni pazuri. Elimu ni kitu muhimu sana, elimu ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi yoyote na hii ndiyo itakayotusaidia kutufikisha kuwa nchi ya kipato cha kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu hii sasa hivi vijana wetu wengi ambao wamekuwa wanamaliza elimu ya msingi, wanamaliza wakiwa ni wadogo sana, wengi wanaanza darasa la kwanza wakiwa na miaka mitano, miaka sita wanamaliza shule ya msingi wakiwa na miaka kumi na mbili, kumi na tatu. Hivyo hawa-qualify kujitegemea wala hawawezi kujiajiri wala kuajiriwa, kwa sababu itakuwa ni kinyume na sheria za ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo sera hii ilikuwa inasema elimu ya msingi sasa itajumuishwa na elimu ya sekondari mpaka kidato cha nne. Mtoto akianza shule ya awali aende moja kwa moja shule ya msingi, akimaliza shule ya msingi anaunganisha moja kwa moja kwenda kidato cha kwanza. Kwa hiyo, ina maana watoto wote sasa watakuwa wanakwenda mpaka kidato cha kwanza wanamaliza mpaka kidato cha nne. Hapa mpaka wanamaliza sasa watakuwa wamefikisha umri ule ambao kidogo wanaweza wakaanza kujitegemea au wakaajirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili nafikiri ni la msingi sana. Sasa nataka Wizara wakati wa majumuisho itupe maelezo ni hatua gani au mikakati gani wameiweka kuhakikisha kwamba sera hii sasa inaanza kutekelezwa kama ambavyo tulikusudia. Kwa sababu ifikapo mwaka 2018 ni kesho kutwa tu tutakuwa tumefika. Tungependa kikifika kipindi hicho watoto wote sasa wawe na uwezo wa kufika hadi kidato cha nne, badala ya kuishia darasa la saba ambapo wanakuwa kidogo hawajaandaliwa vya kutosha hilo ni la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna suala la watoto wanaopata mimba wakiwa shuleni. Mimba inapatikana kwa bahati mbaya, nasema ni kwa bahati mbaya siyo kwa makusudi, watoto wengi wamekuwa wakipata mimba kwa bahati mbaya mashuleni. Sasa watoto hawa wanapopata mimba, ni bahati mbaya unakuta kwamba baada ya muda wanaondolewa mashuleni kwa sababu eti wana mimba. Hii inakuwa ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia ni kinyume na dira ya Wizara ya Elimu ambayo imeitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ninukuu, ukurasa wa nne pale, ameeleza dira vizuri sana, kwamba dira ya Wizara ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa. Hivi ndivyo dira inavyosema na hii dira haijabagua mtoto wa kike wala kiume. Kwa hiyo ina maana watoto wote ni muhimu na mtoto wa kike sasa hivi ndiyo muhimu sana kumwelimisha kuliko hata mtoto wa kiume. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kabisa kwamba hawa watoto ambao kwa bahati mbaya wanapata mimba basi wapewe nafasi ya kuendelea kusoma pale wanapokuwa wamejifungua ili kusudi waendelee kuelimika maana nao ni Watanzania kama Watanzania wengine. Hili ni la msingi sana na litatusaidia kuhakikisha kwamba sasa jamii yote ya Kitanzania Watanzania wote wanapata elimu sawa na ile ambayo tulikuwa tunakusudia. Nadhani kwamba hilo ni suala la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa nichangie katika hii Wizara ni kuhusu Mitaala. Mitaala ya elimu yetu kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu lazima hii mitaala iangaliwe kwa undani ili iendane na maarifa na stadi zinazohitajika sokoni. Iwaandae vijana wetu kujitegemea, iandae wataalam watakaochangia na watakaoweza kushiriki katika maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa mitaala yetu haijaainisha vipaumbele ambavyo Taifa kama Taifa linahitaji. Watu wanasoma tu wengine wanajiunga katika vyuo mbalimbali, sasa vyuo hivi viendane na mahitaji halisi ya soko, ndiyo itatusaidia sana kwenda na wakati. Hili ni la muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa nilichangie ni kuhusu tafiti yaani research na project mbalimbali ambazo vyuo mbalimbali vimekuwa vikiwapa vijana wanafanya katika maeneo mbalimbali. Sasa hivi vyuo vingi havijatilia mkazo sana katika upande wa utafiti, vyuo vikuu vingi havifanyi utafiti wa kutosha. Bila kufanya utafiti wa kutosha hatuwezi kupata wataalam, hatuwezi kupata maendeleo halisi. Lazima vifanye utafiti na Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha hao wataalam wetu wanafanya utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti hizi ndizo zinatakazosaidia kuboresha mazingira na kuleta maendeleo katika nchi yetu. Kuna maeneo mengi ambayo vijana huwa wanafanya na kuna baadhi ya project ambazo vijana huwa wanapewa wakiwa mashuleni. Wanafanya project nzuri sana. Naishauri Wizara iandae utaratibu mzuri wa kuhakikisha zile project ambazo vijana wanafanya wakiwa vyuoni zingine zinafaa sana kuendelezwa, zingine zingefaa sana katika kuanzisha viwanda vidogo na kadhalika. Wanafanya ubunifu mzuri sana ambao nafikiri ni muhimu sana kama Wizara itakuwa na utaratibu mzuri, wa kuziangalia hizo project na kuangalia namna ambavyo Serikali inaweza ikazi-fund ili ziweze kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa nichangie ni kuhusu Vyuo vya Ufundi, Vyuo vya VETA, pamoja na Vyuo Vikuu, Jimbo langu ni Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Songwe na hiyo naipongeza Serikali sana. Pamoja na kuwa ni Makao Makuu ya Mkoa sasa hivi hatuna chuo hata kimoja, hatuna chuo cha Serikali wala cha watu binafsi. Sasa ni wakati muafaka naomba Wizara yako iangalie utaratibu, iweke utaratibu wa kuhakikisha kwamba Jimbo la Vwawa hasa Wilaya ya Mbozi tuna jenga chuo cha VETA ambacho kitawaajiri vijana mbalimbali waliopo katika Wilaya ile. Wale vijana wako maeneo mengi, iwe ni katika fani mbalimbali wapate ule ujuzi ambao utasaidia sana katika kuchangia maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Vyuo vya Elimu ya Juu kikiwemo Chuo Kikuu Huria, tungeomba vianzishe matawi haraka ili wananchi wale ambao ni wengi sana katika ile Wilaya waweze kupata elimu ile ambayo inahitajika katika hili eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa nichangie ni kuhusu suala la hii SDL, hii kodi ambayo sekondari za watu binafsi na vyuo vya watu binafsi vinatakiwa kulipia, SDL ya five percent. Kwanza naomba ku-declare interest kwamba mimi ni mdau na nina maslahi katika hili, hili suala sasa hivi sekondari zote za watu binafsi pamoja na vyuo binafsi vinaendelea kudaiwa SDL kwamba lazima vilipwe, wakati navyo vinatoa mafunzo ya ufundi ambao vinawaandaa vijana wale wale na sera za nchi hizi zinasema elimu siyo sehemu ya biashara, elimu ni kutoa huduma. Sasa kama ni huduma kwa nini vidaiwe SDL badala ya kupata mgao kutoka Serikalini unaotokana na hizi fedha, wanaambiwa wao wachangie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kwa kweli halikubaliki kabisa, ningeomba kabisa kabisa kwa dhati Serikali iliangalie upya ili hizi shule za watu binafsi, vyuo vya watu binafsi, vipewe msaada, vipewe mgawo wa hii SDL ili viweze kujenga ujuzi, stadi na maarifa mbalimbali yanayohitajika katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri haya masuala ya msingi sana na naamini tukiweka misingi mizuri ya kuimarisha elimu yetu nchi yetu itapiga hatua sana. Wale wanaobeza kwamba nchi yetu elimu yetu inashuka, hapana haishuki tuendelee kuiboresha, tuweke mikakati mizuri, tuiimarishe, naamini nchi yetu itapiga hatua sana. Wenzangu wale ambao wanategemea kwamba eti mwaka 2020 tutaishia hapa labda CCM itaporomoka, nataka niwaambie CCM mwaka 2020 tutashinda huenda Viti vyote vya Ubunge kwa sababu ya kazi nzuri ambayo tutaifanya. Hii Wizara naomba ifanye kazi nzuri na mambo yatakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu upo katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni ukosefu wa mfumo wa kimenejimenti ambao ni unganishi (Integrated Land Management System). Mfumo huu utashirikisha Wizara karibu zote ambazo majukumu yao yanategemea kuwepo kwa ardhi ya kutosha. Kwa mfano Wizara ya Kilimo na Uvuvi, Nishati na Madini, Uchukuzi na Ujenzi, Viwanda na Biashara, Mazingira, Maji, Elimu na Afya. Mpango jumuishi ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gharama kubwa za upimaji wa ardhi wakati teknolojia imeimarika, kuna haja ya kupunguza gharama ili watu wengi wapime ardhi, kwa hili itasaidia kuifanya ardhi kuwa mtaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukua kwa miji bila ya mpangilio mzuri, hii inaleta bomoa bomoa katika maeneo mengi. Pia kuna haja ya kuongeza kasi ya kupima miji yetu.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Na mimi naomba nichukue nafasi hii kuchangia machache katika hii hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango katika hotuba zake mbili ya Hali ya Uchumi pamoja na Bajeti nzima ya Nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na nianze kabisa kwa kuunga mkono hoja yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mambo aliyoyazungumzia vizuri katika kitabu cha hali ya uchumi ni suala la kilimo, lakini kilimo kinaonekana kimekuwa kinakua kwa kiwango kidogo sana. Kilimo inaonekana kimekua kwa asilimia 2.3 ukilinganisha na sekta nyingine. Hii inatia wasiwasi wakati tumekuwa tukiimba kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo, kilimo ndiyo kila kitu, ndiyo kinatakiwa kuchangia kwa kiwango kikubwa Pato la Taifa, kilimo ndiyo kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, kilimo ndicho ambacho kinaweza kikachangia katika kuimarisha thamani ya fedha yetu kwa kutuletea fedha za kigeni. Sasa hivi fedha zetu zimekuwa zikishuka thamani sana kwa muda mrefu ukilinganisha na dola, ni kwa sababu uzalishaji umekuwa siyo mzuri na mauzo yetu nje ya nchi yamekuwa siyo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo hiki kikiimarika kinaweze kusaidia vizuri sana ukiangalia katika hotuba zote tulizozitoa, ukiangalia katika maelezo yote aliyotoa tumeimba sana kilimo ni uti wa mgongo, lakini hakuna mikakati ya dhati inayoonekana kabisa kwamba kweli tunaenda kuiimarisha kilimo. Nataka kusema bila kuimarisha kilimo hii tunayosema uchumi umeimarika, umekuwa itakuwa ni hadithi, kwa sababu watu walio wengi asilimia kubwa wanategemea kilimo, bila kuwasaidia wao hizo sekta nyingine haziwagusi moja kwa moja. Kwa hiyo, ni lazima tuweke mikakati ya makusudi ya kuhakikisha kwamba kilimo kweli kinawekewa mikakati itakayosaidia kuimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kabisa ruzuku ambayo itatolewa kwenye pambejeo ni ndogo sana, sasa kama kweli tunataka kuimarisha kilimo tuongeze zuruku. Mimi nina uhakika kabisa Mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini na hasa kwenye Jimbo langu la Vwawa wakulima wakipatiwa pembejeo za kutosha tutalima vizuri sana na tutazalisha kwa ziada nchi itapata ziada nyingi sana.
Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iangalie upya sera ya kilimo ili kuhakikisha kwamba pembejeo zinafika kwa wakati na zinapatikana. Kilimo cha kahawa kiweze kufufuliwa, mahindi, pareto, tumbaku na mazao mengine yatachangia sana katika kuimarisha uchumi wa nchi hii. Hii kwa kweli haijanifurahisha kuona kwamba kilimo sasa hivi kimechangia kwa asilimia 2.3 tu wakati ndiYo kilikuwa kinaongoza kuliko sekta nyingine zote, hilo ni la msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo ningependa nichangie ni kuhusu Mfuko wa Maji Vijijini. Naipongeza Serikali imesema kwamba kutakuwepo na Mfuko wa Maji Vijijini na utaendelea kuwepo, lakini huu mfuko fedha ambazo zinapatikana zinaonekana bado ni ndogo. Sisi tungependa kabisa vijiji vyote vipate maji ili tuondokane na hili lazima tuje na mkakati wa makusudi kwa kipindi kifupi, iwezekane kabisa kipindi cha miaka miwili, mitatu tumalize kabisa hili tatizo la maji vijijini. Ili kumaliza hilo ni lazima tuweke tozo kwenye mafuta, kama tukiweka kwa mfano ikiwa shilingi mia tutapata fedha za kutosha kabisa zitakazoweza kusambaza maji katika vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaita Mfuko wa Maji, lakini hivi fedha nyingi zimekuwa zinatumika kwenye maendeleo ya maji mijini, kama ni za vijijini ziende kweli vijijini hiyo ndiyo itakayoweze kutusaidia na kuleta kweli kuinua hadhi. Mimi ninaamini kabisa kama maji tukiyasambaza vijijini wale wananachi wa vijijini maisha yao yatakuwa mazuri na watapata maji safi na salama na pia wataweze kulima hata kumwagilia bustani pale walipo katika maeneo yao itasaidia sana. Nafikiri hilo ni suala la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni kuhusu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa kweli niseme kabisa mimi nimesikitika na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya ofisi hii, hii inatokana bajeti yetu imeongezeka! Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali anatakiwa kukagua Wizara zote, anatakiwa kukagua Idara zinazojitegemea zote, Wakala zote, Balozi zote, Mashirika ya Umma na haishii hapo tu anatakiwa kwenda kukagua miradi yote ambayo tumeipitisha. Ukiangalia kwenye bajeti yetu miradi ni mingi sana tunayoenda kuitekeleza, asilimia 40 ya bajeti inaenda kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipompa fedha za kutosha Mkaguzi nani atakayekwenda kufuatilia hiyo miradi na kuhakikisha kwamba hizo fedha kweli zimetekeleza yale ambayo tunayapitisha hapa Bungeni? Kwa hiyo, nashauri lazima iangaliwe upya ikiwezekana Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unapitia upya mid year review ya bajeti lazima tuhakikishe Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anapatiwa fedha za kutosha ili aweze kutekeleza majukumu yake ambayo yapo Kikatiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hatakiwi uhuru wake kuingiliwa, kwa sasa hivi kinachojionesha ni kwamba atakuwa anaanza kuomba omba fedha na akianza kubembeleza kuomba fedha maana yake atakuwa na compromise independence yake, sasa hili ni suala ambalo lazima tuliangalie sana na huyu ndiye mwakilishi na ndiyo jicho la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kwamba inaisimamia ipasavyo Serikali. Kwa hiyo, naomba lazima hili suala liangaliwe vizuri ili angalau tuweze kwenda mbele, hili ni la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naelewa azma ya Waziri anayoisema, labda tuangalie Waziri je, mlipokagua mlikuta hela zake zinatumika vibaya? Kama mmekuta kwamba matumizi yake yalionekana mabaya basi ni sawa sawa. Lakini kama haijaonesha hivyo ni vema akapewa fedha za kutosha ili akafanye kazi ile ambayo tumeikusudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa nichangie ni kuhusu kiinua mgongo cha Wabunge. Wenzangu wamechangia vizuri na mimi nisingependa nilisema sana. Nilitaka kusema sikuona sababu ya azma ya Serikali ya kulileta kwenye Bunge hili la kwanza kwa nini limeletwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, naelewa Kanuni za uhasibu za kimataifa zinavyosema, zinataka kiinua mgongo kitakacholipwa baada ya miaka mitano kinatakiwa kisambazwe katika miaka yote ambayo mfanyakazi ametumikia, yaani kama Mbunge ametumika kwa muda wa miaka mitano basi iwe prolated katika kipindi cha miaka mitano. Kwa hiyo, ina maana lazima ianze kuwa provided kwenye vitabu vya uhasibu kuanzia mwaka wa kwanza, hiyo azma naielewa, lakini haitakatwa kodi na haitatolewa, haiwezi kutolewa sasa hivi kwa sababu itakuja kutolewa mwaka wa mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna sababu gani ya kuzungumzia masuala ya kodi kwa leo wakati hii kodi haitakatwa chochote mwaka huu? Kwa hiyo, hili suala kuna haja ya kuliangalia vizuri. Mimi nadhani hili linatuletea matatizo. Wenzangu wamelizungumzia vizuri nisingependa niliseme. Najua lazima liwe provided kwenye books of accounts, lakini lifanyiwe kazi vizuri ili li-cover wote wanaotakiwa kulipa kodi walipe, siyo tu iende kwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la mwisho ambalo ningependa nilichangie ni kuhusu shirika letu la ndege. Nimefurahishwa sana na Serikali kwamba tunataka sasa kulifufua shirika letu, lakini hili shirika lina madeni mengi sana na makubwa. Hizi fedha ambazo zimetengwa nisingependa ziende tena kwenye hili shirika, ningependa lianzishwe shirika lingine au hilo livunjwe lianzishwe lingine ndiyo lipewe hizo fedha na ndege tatu, hapo tutaweze kuona mchango halisi. Hizi fedha zikitolewa kama zilivyo mwisho zitaenda kulipa madeni mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwenye maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha utalii katika nchi yetu, nchi yetu ina vivutio vingi kama mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro, maziwa na masalio ya kale. Serikali iongeze matangazo nchi za nje ili kuvutia watalii wengi zaidi pia usalama na amani ya nchi ni muhimu sana kuongeza hoteli na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna misitu mingi ambayo lazima ilindwe na kuvuna kwa utaratibu mzuri, haiwezekani nchi kukosa madawati katika shule zetu. Kuna wananchi wengi hasa katika maeneo ya Nanyara, Songwe na kadhalika wananyanyaswa sana na maliasili. Wengi wanapanda miti ambayo wanakata ili kuchomea chokaa, cha ajabu wanatozwa shilingi 15,000 kwa mti mmoja bila receipt naomba mfuatilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimondo cha Ndolezi Mbozi ni muhimu kikajengewa fence ili kukihifadhi na kuimarisha utalii katika eneo hilo ni muhimu sana.

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru wa kupata nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia machache ambayo ninayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nianze kwa kuzipongeza Kamati zote mbili kwa taarifa nzuri ambazo zimetolewa. Kwa kweli ni nzuri sana na naamini kama Serikali itazifanyia kazi basi hali itakuwa ni nzuri. (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, suala la pili ambalo napenda kuchangia ni kuhusu taarifa za Mkaguzi Mkuu (CAG). Kwanza CAG ndiyo mwakilishi wa Bunge hili, ndiyo jicho la kwenda kuangalia kukoje huko katika taasisi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaenda haraka haraka kwa sababu ya muda, chukulia ripoti ya Serikali Kuu ya mwaka huu. Katika ripoti ya mwaka 2014/2015, katika Serikali Kuu taasisi 18 zilipata hati yenye mashaka na taasisi moja ilipata hati isiyoridhisha kwenye Serikali za Mitaa ndiyo inatisha. Ukiangalia kwenye Serikali za Mitaa mwaka 2011/2012 hati zenye mashaka zilikuwa 29, hati isiyoridhisha ilikuwa moja na hati chafu ilikuwa moja. Mwaka 2014/2015 kwenye Serikali za Mitaa ndiyo kunatisha, hati zenye mashaka 113, hati zisizoridhisha tatu na hati chafu moja, hii maana yake nini? Maana yake hali siyo nzuri katika taasisi zetu katika kusimamia fedha za umma na hapo lazima Serikali ichukue hatua stahiki kuhakikisha kwamba tunazuia hii hali ambayo ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hati yenye mashaka maana yake ni kwamba vitabu na hesabu zilizopo hazioneshi sura halisi ya taasisi. Sasa kama hivyo ndivyo ilivyo tusipochukua hatua hali itaendelea kuwa mbaya katika taasisi zetu. Naishauri Serikali yangu tuendelee kuchukua hatua stahiki ili tuhakikishe mambo yanakuwa mazuri katika miaka inayokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ambalo nataka nilizungumzie ni kuhusu taasisi chache ambazo zinafanya kazi kama TRA. Zipo taasisi ambazo zenyewe zinazalisha, zinafanya biashara, zinanunua raw material, zina-process goods halafu zinaenda kuzalisha zinauza kama TANESCO na zinginezo. Hata hivyo, zipo taasisi zinazofanya kazi kama TRA kwa mfano EWURA na TCRA hawana gharama zingine za uzalishaji zaidi ya tozo, zile tozo ni mali ya Serikali, lazima Serikali iweke mkono wake kuhakikisha kwamba zinaingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Hiyo ndio itakayoongeza mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, kwa sababu ya muda nakwenda haraka haraka lakini nizungumzie matatizo ambayo yamejitokeza. Labda niweke taarifa vizuri, nimesikia watu wameliongelea suala la Lugumi labda pengine niweke taarifa vizuri. Kwanza niseme mimi ndiyo nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Lugumi iliyokuwa inashughulikia huo mkataba. Katika mkataba ule hadidu za rejea ilikuwa ni moja kwenda kuangalia kama ile mitambo ilinunuliwa na kufungwa, ndiyo ilikuwa kazi yetu. Hatukuwa na kazi nyingine zaidi ya hiyo na tulizunguka nchi nzima, Mikoa yote, Wilaya zote tukathibitishe kama zilinunuliwa na kufungwa. Naomba niweke rekodi sawa kwamba tulikuta kwa asilimia karibu 99 vilinunuliwa na kufungwa. Kilichokuwepo kwenye taarifa ya CAG alisema katika vituo vyote vile ni vituo 14 tu ndiyo mitambo ilikuwa inafanya kazi zake sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilithibitishie Bunge lako hili hata Kamati Ndogo ilipoenda ilikuta ni vituo 15 ndiyo vilikuwa vinafanya kazi yake sawasawa. Hiyo ndiyo iliyokuwepo kwenye ripoti ya Kamati yetu. Kama vituo 15 vinafanya kazi yake sawasawa kulikuwa na tatizo gani? Ile mitambo ina kazi tatu, kazi ya kwanza ilikuwa ni kuchukua picha na maelezo ya wahalifu; kazi ya pili ilikuwa ni kuhifadhi kumbukumbu zile kwenye njia ya electronic na kazi ya tatu ilikuwa ni kutuma sasa zile taarifa kwenye mitandao ili kuweza ku-share na vituo vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka niliambie Bunge lako vizuri kwamba katika kazi ya kwanza na ya pili ilikuwa haihitaji kabisa mtandao wa internet. Hapa ndipo Kamati ilikuwa inauliza kama vifaa vyote hivi vilinunuliwa ni kwa nini sasa vilikuwa havitumiki kufanya kazi ya kwanza na ya pili, ndiyo swali lililokuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilichotaka kusema ni kwamba mitambo yote ilinunuliwa, imewekwa lakini ilikuwa haijaanza kutumika. Hiyo ndiyo hoja ambayo tunayo kwenye Kamati na naomba ieleweke hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa muda huu.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-
(1) Mdororo wa uchumi umesababishwa na sera za uchumi wetu. Wakati Serikali imetumia sera zote mbili za fiscal policy kubana matumizi na kuongeza kodi katika bidhaa na huduma mbalimbali. Benki Kuu imekaa kimya kabisa bila kuchukua hatua zozote katika kupunguza riba za mabenki na kusimamia mzunguko wa fedha nchini. Hali hii ndiyo iliyosababisha mabenki kuporomoka na kushuka kwa uchumi. Fedha zimepungua kwenye mzunguko.
(2) Kupungua kwa uzalishaji bidhaa na kushuka kwa ajira nchini. Hivi sasa viwanda na makampuni mengi yameanza kupunguza wafanyakazi kama kwenye sekta ya utalii, hoteli na taasisi za elimu.
(3) Lazima Serikali ianze kurasimisha Sekta binafsi na kuziunga mkono ili zichangie katika pato la Taifa.
(4) Kuhamasisha kilimo kikubwa cha mazao ya chakula na biashara kwa kutoa support inayohitajika pamoja na masoko ya bidhaa.
(5) Kuendelea kuhakikisha kuwa Serikali inahamasisha na kusimamia sera ya elimu ikiwa ni pamoja na kuanzisha mitaala yetu ili iendane na mahitaji ya soko na kuongeza udahili ili nchi iwe ya wasomi wengi.
(6) Kuangalia vipaumbele ambavyo vina competitive advantages kufuatana na mazingira na jiografia ya nchi yetu. Lazima uchambuzi wa kina ufanyike. Kwa mfano; Bahari, Bandari, Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Wanyama, Madini, Olduvai Gorge na kadhalika.
(7) Kuimarisha matumizi ya reli ya TAZARA ili kupunguza gharama za uzalishaji na uharibifu wa barabara katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa, ubabaishaji na kadhalika.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata hii nafasi ili kuweza kuchangia katika taarifa hii ya Kamati. Kwanza naipongeza sana Kamati kwa taarifa nzuri ambayo wameiandaa ambayo na mimi pia ni Mjumbe wa hii Kamati, kwa hiyo nashukuru sana kwa taarifa nzuri hii.
Mheshimwa Mwenyekiti, tunapozungumzia maendeleo na tunapotaka maendeleo ya nchi lazima tuangalie ni vipaumbele gani ambavyo vitaashiria na vitafanya nchi ionekane imeendelea. Nasema hayo nikianzia na suala la kilimo. Katika kilimo asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, nchi yetu hii tumesema tunataka sasa kujenga nchi ya viwanda, hatuwezi kujenga nchi ya viwanda, hatuwezi kukamilisha hilo kama hatutaimarisha kilimo. Viwanda vinategemea malighafi na malighafi hizo lazima zitoke kwenye kilimo. (Makofi)
Hata ukiangalia nchi za wenzetu, ukiangalia Ulaya industrial revolution ya Europe ilianzia kwanza na agricultural revolution, ilianzia kwanza na mapinduzi ya kilimo; mapinduzi yale ya kilimo yakaleta mapinduzi ya viwanda. Kwa hiyo, tunaposema maendeleo lazima tuweke tuzungumzie bayana kabisa, tuwe na mkakati wa makusudi wa kuimarisha kilimo chetu na ambacho ndicho kinatoa ajira kwa watu wengi, ambacho ndiyo kitatupatia malighafi za kutosha kwenda kwenye viwanda na kitachangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa letu. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, hivi sasa kilimo chetu kinategemea mtu mmoja mmoja kilimo kidogo, hii haitatupeleka mbele kama Taifa. Lazima pia tuweke mkakati wa makusudi wa kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo yatakayosaidia katika kuimarisha Pato la Taifa.
Mheshimwa Mwenyekiti, hivi sasa tunavyozungumzia kilimo nchi yetu sasa inakabiliwa na ukame katika maeneo mengi ambao tunaamini itaathiri kwa kiwango kikubwa sana maendeleo yetu ya kilimo. Mikoa ya Nyanda za Juu kama kule kwetu Songwe sasa hivi bado mvua zinanyesha na tena zinanyesha vizuri sana na wananchi wamelima mazao yanakwenda vizuri, tatizo lipo kwenye pembejeo, pembejeo sasa hivi kule Mkoani Songwe zimepanda vibaya sana. Katika kipindi cha nyuma Serikali ilitamka kwamba kwa mfano mbolea ya kukuzia ingeuzwa shilingi 26,000 lakini hivi leo ninapoongea pembejeo zimepanda sana kule Mbozi, mbolea ya kukuzia ni zaidi ya shilingi 50,000, sasa hii itasaidiaje? Hatuwezi kuendelea kwa namna hiyo. Kwa hiyo, naiomba Serikali itafute uwezekano wa kusaidia kilimo ili angalau tuweze kuinua pato la Taifa na kutoa ajira kwa wananchi walio wengi, hilo ni suala la kwanza.
Mheshimwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu usimamizi wa bajeti na nidhamu ya bajeti. Mimi nashukuru uchambuzi wa Kamati ulivyofanywa, lakini naomba nitoe ushauri wangu, fedha nyingi zinatoka kwenye Wizara ya Fedha, zinapopelekwa kwenye Serikali za Mitaa na kwenye taasisi za umma ni namna gani Serikali inasimamia na kufuatilia kwamba hizo fedha zinatumika kama zilivyopangwa, hilo ni suala la msingi sana.
Mheshimwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na tabia kwamba katika baadhi ya maeneo watu wamekuwa wakibadilisha matumizi ya bajeti kinyume na Sheria ya Bajeti, hii siyo sawasawa. Mimi naamini Bunge baada ya kuidhinisha bajeti, bajeti inatakiwa itumike kama ilivyo na kama kuna mabadiliko basi hatua zinazoweza kuchukuliwa zifuatwe, kuliko sasa hivi mabadiliko ya bajeti yanatokea, bajeti tunapanga hapa inakuwa sasa haitekelezeki, kwa kweli hiyo itakuwa haitusaidii kama nchi, ni vema tukawa na msimamo na tukasimamia vizuri bajeti ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, lazima tuweke vipaumbele vichache vinavyoonekana kwamba kwa mwaka huu tunataka tuwe na kipaumbele gani? Tusichukue vipaumbele vingi, hiyo itatufanya kwamba tusionekane kama mwaka huu kipaumbele ni kusambaza maji tuhakikishe mwaka huu tunasimamia kusambaza maji. Kwa hiyo, bajeti ya maendeleo ilenge katika hayo maeneo, mwaka unaofuata tunaelekeza tena upande mwingine, hiyo, itatusaidia sana katika kuweza kuharakisha kuleta maendeleo na kuwa na nidhamu nzuri ya matumizi ya fedha.
Suala lingine ambalo ningependa kuchangia linahusu mapato yasiyotokana na kodi. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuvuka malengo ya mapato yanayotokana na kodi kwa kweli naipongeza sana Serikali. Katika mapato ambayo hayatokani na kodi yaani non-tax revenues tumeweza kufikia asilimia 54; sasa asilimia 54 ni ndogo. Lazima tuwe na mikakati ya kutosha, tuchukue hatua zinazowezekana kuhakikisha kwamba tunaimarisha hili eneo maana lina vyanzo vingi, tunaweza tukapata mapato mengi.
Mheshimwa Mwenyekiti, ninaamini kama tukisimamia vizuri mashirika ya umma yakafanya kazi yao inavyotakiwa, yakafanya kazi kwa ufanisi, mashirika kama EWURA ambao wanakusanya fedha nyingi, mashirika kama TCRA, Civil Aviation, Reli, Shirika la Ndege na Bandari. Tukisimamia haya mashirika vizuri yataisaidia sana nchi hii kuweza kupata fedha na kupata mapato mengine yasiyokuwa yana kodi. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nchi nyingi zinahitaji kuwa na bandari; sisi tuna bandari nzuri. Bandari yetu ile tukiimarisha nina uhakika kabisa tunaweza tukapata fedha nyingi sana na ikiwezekana mara mbili ya bajeti tuliyonayo, lazima tuweke mkakati wa kutosha katika kuhakikisha hilo eneo tunafikia malengo. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nichangie pia kwenye eneo la ulipaji mzima wa kodi. Mimi naamini Watanzania lazima tuwe ni wazalendo wa kweli. Sasa hivi elimu ya mlipa kodi bado haitoshi, wananchi walio wengi bado elimu haitoshi ya ulipaji kodi. Katika maeneo mengi mimi nimeona pamoja na jitihada za Serikali, pamoja na mkazo ambao umekuwa ukitiliwa katika kukusanya kodi na watu kuwahamasisha maeneo mengi ukienda dukani mtu anakuuliza; nikupe risiti au nisikupe risiti? Risiti ni haki, risiti ni wajibu wa kila mtu kutoa na wanapopanga bei zao lazima wajue kwamba kuna wajibu wa kulipa kodi, kwa hiyo, lazima hilo lizingatiwe.
Mheshimwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Fedha iweke mkakati kwamba, sisi Viongozi wa Siasa, Wizara ya Fedha na Serikali lazima tufanye jitihada za makusudi za kuhamasisha ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu ya kulipa kodi, bila kulipa kodi hatuwezi kuleta maendeleo, tutakuwa tunaimba tu. Lazima wananchi wetu walipe kodi na lazima tuisimamie vizuri.
Mheshimwa Mwenyekiti, VAT (Value Added Tax) nina uhakika kama tutaisimamia vizuri itasaidia sana……
Mheshimwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
kwanza napenda kumpongeza Waziri Mkuu kwa kuja na
hotuba nzuri. Naomba kuchangia maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira kwa vijana. Hivi
sasa kuna vijana wengi ambao wamehitimu katika vyuo
mbalimbali vya ngazi zote lakini kuna tatizo la vijana
kukosa kazi za kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe. Tatizo la ajira lina athari kubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii. Lazima
Serikali ije na mpango mahususi wa kuwaajiri au
kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo; hivi sasa kilimo
kinaajiri watu zaidi ya asilimia 75; ili nchi iendelee lazima
kutoa pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu. Ahadi ya
Waziri Mkuu kuwa na bei elekezi ni muhimu sana. Lakini pia
mbegu nzuri, kilimo cha kisasa na umwagiliaji ni lazima kwa
kipindi hiki. Baadhi ya maeneo tuanzishe mashamba
makubwa ya kuanzia kilimo na kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa za kulevya;
naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za kupambana
na dawa za kulevya. Ni muhimu vita hii iendelee kwa nguvu
zote ili kuiokoa nchi, vijana na Taifa kwa ujumla. Naomba
Serikali iongeze nguvu zaidi kuwakamata wauzaji,
wasambazaji na watumiaji. Tungependa kusikia Kamishina
wa Kupambana na Dawa aongeze kasi na kutupatia taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, rushwa; hivi sasa kuna
rushwa sana katika maeneo ya Serikali za Mitaa kwa mfano
Mbozi hali ni mbaya sana. Naomba vyombo vinavyohusika
vichukue hatua za haraka kwani wananchi wanateseka
sana.

The Public Procurement (Amendment) Act, 2016.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia katika huu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kuleta marekebisho haya ya sheria hii ambayo imekuwa ni kikwazo kikubwa katika majukumu mbalimbali ya Serikali huko nyuma. Kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kwanza niipongeze Serikali kwa kuamua kuleta vifungu vya kupunguza muda wa mchakato wa manunuzi. Tumekuwa tunatumia muda mrefu sana katika mchakato wa manunuzi. Na wakati mwingine katika baadhi ya taasisi kama huna wataalam, kama wale wa PMU hawajajiandaa inaweza ikafika mpaka mwisho wa mwaka bado mko kwenye mchakato wa manunuzi, kwa hiyo hii ya kupunguza muda, kwa kweli naipongeza sana Serikali ni kitu kizuri sana tulichokuwa tunakisubiri; hili ni suala la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nimefurahishwa sana katika muswada huu, ni hii ya kuiondoa wakala wa ununuzi wa bidhaa za umma yaani GPSA kuiondoa katika kupanga bei. Hili lilikuwa ni tatizo kubwa, GPSA ilikuwa inalalamikiwa kila mahali na bei ambazo zilikuwa zinawekwa katika mikataba zilikuwa ni kubwa sana haziendani na hali halisi. Sasa kuiondoa kwamba wasipange bei nadhani hii inakwenda vizuri sana na sheria ya sasa ambayo kwa marekebisho haya yanataka taasisi zitumie bei ya soko; kitu ambacho ni muhimu sana. Hii ilikuwa ni changamoto kubwa sana lazima tutumie bei ya soko, unakuta mfuko simenti unauzwa shilingi 15,000 bei ya soko, kwenye mikataba shilingi 20,000, 30,000 hii haikubaliki. Kwa hiyo marekebisho haya ni ya muhimu sana lazima tuyaunge mkono, mimi nafikiri ni suala la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na GPSA kuna tatizo lingine lipo TEMESA. TEMESA haijazungumzwa kwenye hii sheria nayo imekuwa ni matatizo kwenye utengenezaji wa magari na vipuri, bei ambazo zimekuwa zinawekwa na TEMESA ukienda mitaani ziko tofauti kabisa. Sasa hilo halikubaliki, lazima Serikali itazame hapo ifanye nini ili kuweza kurekebisha kusudi tuweze kutengeneza magari katika bei ambazo zinakubalika kwenye soko. Siyo zile ambazo zinawekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho nilitaka kuchangia kwenye hii nimefurahishwa sana na hii sheria kwa kuleta sasa upendeleo maalum kwa kampuni za kizalendo, zinazomilikiwa na Watanzania. Hii ni suala la msingi sana kwa sababu mara nyingi kwenye upande wa construction makampuni mengi yaliyokuwa yanafanya kazi nyingi yalikuwa ni ya kigeni, na makampuni ya ndani yamekuwa hayapewi kazi kwa sababu ya kukosa mambo fulani fulani. Sasa hii ambayo imewekwa kwenye sheria ya kuwapa upendeleo wa makusudi, maalum nadhani ni suala la msingi sana ambalo limewekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini haijaishia hapo na wataalam wa ndani kwamba tutumie wataalam wa ndani ili kuwajengea uwezo waweze kuchangia katika maendeleo ya nchi; hii nafikiri itatuletea maendeleo endelevu. Hatuwezi kuwa na maendeleo endelevu tukiendelea kutegemea wataalam kutoka nje, hatuwezi kuwa na maendeleo endelevu tukiendelea kutegemea makampuni yanayotoka nje, lazima tuyajengee uwezo makampuni ya ndani, haya ndio yatakayoweza kuleta maendeleo endelevu. Hili nafikiri ni suala la msingi sana ambalo naliunga mkono.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu ununuzi katika Serikali za Mitaa, tumekuwa na changamoto kubwa sana kwenye Serikali za Mitaa na huku ndio kuna matatizo mengi sana, mara nyingi kampuni nyingi ambazo zimekuwa zikifanya kazi kwenye Serikali za Mitaa zimekuwa zikiwa na matatizo mengi, nadhani kuna haja sasa ya kurekebisha vizuri, kulikuwa na kanuni zile zinazohusu manunuzi kwenye Serikali za Mitaa na kanuni za hii, mimi namwomba Mheshimiwa Waziri, hizi kanuni ziwe harmonized tuwe na kanuni moja inayo-apply sehemu zote; hizi kanuni ambazo mara nyingine ziko huku, nyingine huku zina toa loopholes kwa watu kutumia zile nafasi vibaya na kufanya fedha za umma zipotee kwa kiwango kikubwa. Hili ni suala la msingi ambalo lazima tulizingatie katika kuweza kuhakikisha kwamba mambo yetu haya yanakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kwenye Halmashauri kuna tatizo lingine, mimi nilikuwa nafikiri mwelekeo mzuri Halmashauri zingeshauriwa pale zinapoweza kununua baadhi ya vifaa zinunue zenyewe halafu zifanye kazi ziajiri vibarua wa kufanya kazi; ingekuwa ina maana sana. Mimi sielewi kwa nini ni lazima kama Halmashauri inaweza kununua grader kwa nini tumpe contractor, kwa nini sheria ilazimeshe kwamba lazima ipewe tender? Mimi nilikuwa nafikiri ni lazima sasa kama tuna grader tuajiri vibarua wa kuweza kufanya hizo kazi na tulime barabara kwa wingi hilo lingekuwa ni la msingi sana. Kwa hiyo ningeomba sheria iliangalie hilo, na ione namna gani tutakavyoweza kulitekeleza iatusaidia sana katika kuweza kusaidia kuleta maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi sheria ilivyo inataka kila kitu kiende kwenye tender hatuwezi kuweka kila kitu kiende kwenye tender, haiwezekani hilo ni la msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo nilitaka kuchangia ambalo naliona sasa lilikuwa ni tatizo la mfumo huu wa ununuzi ni suala la bei, sheria ilikuwa imeweka kigezo kwamba bei huwezi uka-negotiate, huwezi uka-bargain bei ikapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtu ameweka bei za ajabu; nataka kweli afanye kazi au yupo peke yake au wapo wangapi kwa nini tusiruhusiwe, sheria hii sasa inaruhusu kuanza ka-bargain bei mimi ninadhani hili ndio suala la msingi sana, lazima tu-bargain bei, iendane na hali halisi pale tunapoona kwamba bidhaa ambazo mzabuni ameweka haziendani na hali halisi, tumwambie bei ya soko sio hiyo rekebisha kama unataka kazi na irekebishwe ili kazi ziweze kwenda na tuweze ku-save hela za umma na tuweze kupata thamani halisi ya fedha za umma.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo ningependa nilichangie ni kuhusu value for money, ni kitu muhimu sana, haiwezekani katika hali ya kawaida mimi nikienda dukani nanunua kitu kwa shilingi 500 ukisema unatoka kwenye taasisi ya umma wanakwambia shilingi 5,000 hii haikubaliki kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haikubaliki kwa sababu; sababu nyingine ambazo wanazitoa nyingine zina maana lile suala la kusema kwamba eti malipo ya Serikalini yanachukua muda mrefu sana kwa hiyo zile bei zinakuwa na interest hii nadhani ni message inafika kwenye Serikali mliangalie hilo. Hakuna sababu ya kuchelewesha sana malipo walipwe kwa wakati na hili tuachane nalo. Lakini bei lazima tuzingatie bei ya soko na tuzingatie thamani halisi ya bidhaa tulizonunua, sasa hivi vitu vingi unakuta haviendani na hali halisi value for money haiwi-considered hasa hili ni tatizo kubwa ambalo ninaamini kabisa katika hii sheria ni muhimu sana ikalitekeleza na ikaliangalia, naamini Wizara wataliangalia kwa undani zaidi ili tuone ni namna gani tunaweza kulitatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa nirudie kwenye lile suala la kanuni za ununuzi wa umma, kuna baadhi ya vipengele vilikuwa vinakinzana na sheria kuu.
Mheshimiwa Waziri naomba ukaviangalie vizuri vile vipengele vinavyokinzana, vipengele vingine vilikuwa vinaweka utaratibu huku tofauti unakuta kwenye kanuni zinakuwa ni tofauti. Hasa naomba hizi ukaziangalie vizuri ili ziwe harmonize ziendane na sheria inavyotaka. Lakini zaidi ya hapo hizi kanuni zisichelewe, sheria hii inatakiwa ianze kufanya kazi; mimi niliamini inaanza kufanya kazi tarehe 1 mwezi wa 7, kesho kutwa. Lakini sasa kama kanuni zitachelewa zitasababisha hii sheria iendee kutumika na tuzidi kuchelewa zaidi. (Makofi)
Kwa hiyo, nilikuwa naomba muliangalie hili muziharakishe hizi kanuni zije kwa wakati ili haya marekebisho ambayo yamepitishwa na hii sheria yaweze kufanya kazi ile ambayo tunaitarajia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda niseme naunga mkono hoja, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.

The Valuation and Valuers Registration Bill, 2016

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mawazo yangu machache juu ya sheria hii ambayo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda niipongeze Serikali kwa kuleta muswada huu kwa wakati ambao ni muafaka. Naamini kabisa muswada huu utatupunguzia matatizo mengi sana ambayo yamekuwepo maeneo mengi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nijikite katika maeneo machache. Eneo la kwanza ambalo ningependa kulisemea ni kuhusu huyu Msajili ambaye anatajwa katika sheria hii. Nimeona muda wa Msajili huyu ambaye ametajwa kwamba atateuliwa na atapewa miaka mitatu na baadaye anaweza akateuliwa tena kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nadhani Msajili ndio mtendaji mkuu. Kipindi cha miaka mitatu ni kipindi kifupi sana. Bodi ina miaka mitatu, Msajili miaka mitatu. Sasa mara nyingi hapa kwa sababu Msajili ndio mtendaji, panaleta mvutano kidogo. Wakati mtakapokuwa mnafanya uteuzi wa Bodi tutajikuta hata Msajili mwingine tena atakuwa anateuliwa, kiasi kwamba mwendelezo wa ofisi utakuwa unakosekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka kushauri, kama inawezekana, Msajili angekuwa anateuliwa kwa kipindi cha miaka angalau minne au mitano. Hiyo ingesaidia kwamba wakati bodi inateuliwa lakini kunakuwa na Mtendaji ambaye tayari yuko pale na ofisi inaweza sasa ikawa na mwendelezo wa kuweza kutekeleza majukumu yake. Tumeona katika Bodi nyingi, Wasajili wanakuwa na muda mrefu kidogo, wanakuwa na miaka minne au mitano, hii inasaidia sana katika kuweza kuimarisha utendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kulizungumzia ambalo linaelezwa katika sheria hii ni hili suala ambalo sheria inamtaka Msajili kuwasilisha taarifa kwa Waziri kwa miezi mitatu na Waziri baadaye ataiwasilisha hiyo taarifa katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni kwamba taarifa ambayo atakuwa anaiwasilisha ambayo itawasilishwa na bodi hii miezi mitatu baada ya mwaka kumalizika, hiyo taarifa naamini itakuwa bado haijakaguliwa. Ili taarifa iweze kuwasilishwa hapa Bungeni ni vyema basi taarifa hiyo ikawa imekaguliwa na mtu mwingine ameiona, ameiangalia kwa undani na akaona hii taarifa sasa inafaa kabisa kuja kuwasilishwa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naona kabisa hii taarifa ya miezi mitatu itakuwa ni taarifa ambayo ni unaudited na hivyo haitaweza kutoa picha halisi ya utendaji wa taasisi inayohusika au wa bodi yetu inayohusika. Kwa hiyo, napendekeza kwamba kwa utaratibu mzuri kabisa, inafaa taarifa hiyo iwe ni ile ambayo itatolewa labda ni miezi sita baada ya kufunga mwaka ambapo sasa hiyo taarifa itakuwa imekaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu; taarifa hiyo itakuwa sasa ni taarifa ya mwaka mzima ambayo itakuwa na majukumu mbalimbali ambayo yametekelezwa na hiyo Bodi pamoja na huyo Msajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo taarifa itakuwa sasa inakidhi mahitaji yetu ambayo tunayahitaji, kuliko hivi sasa ambapo taarifa yenyewe inakuwa ni ya miezi mitatu itakuwa bado haijakamilika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilikuwa nataka kulizungumzia, zipo njia nyingi ambazo zinatumika katika kufanya uthamini. Njia hizi zinategemea na lengo hasa la uthamini ni nini. Lengo ni kupata mkopo, lengo ni kutoa fidia au lengo ni sababu gani? Zipo sababu nyingi.
Sasa nilikuwa nafikiri kwamba umefika wakati hizi njia ili kusiwe na migongano, Mthamini mmoja anaweza akaleta taarifa fulani halafu ikagongana na Mthamini mwingine, ni vyema basi tukawa tunachagua njia, zikaelezwa katika kanuni zitakazotolewa na Mheshimiwa Waziri, tukaeleza kama ni mkopo kwamba tutatumia kigezo fulani; tutatumia njia fulani kwa ajili ya kuthaminisha. Kama ni fidia, basi lazima tuainishe kwamba ni njia hii ambayo ndiyo inafaa zaidi, hivyo hii ndiyo itakayofaa kuweza kuthaminisha mali zilizoko katika eneo fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hiyo itatusaidia katika kupunguza migongano ambayo inaweza ikajitokeza kutokana na Wathaminishaji kuwa wawili au watatu ambao wote wana sifa lakini wanatoa ripoti zinazotofautiana. Nadhani ni muhimu sana tukaziangalia hizo njia ambazo tunazitumia katika kufanya hizo valuation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna njia nyingi zimetajwa katika hii sheria na vigezo vingi vimetajwa, kama tutazingatia labda gharama za soko, kama tutazingatia soko, yaani mali hiyo ina thamani kiasi gani, yaani market value au tutazingatia gharama (cost recovery program) au historical cost na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vigezo hivi viendane na sababu hasa ya kufanya uthamini. Naamini kabisa kama zikiendana na sababu ya kufanya uthamini, inaweza ikasaidia sana na inaweza ikapunguza migogoro ambayo imekuwa mingi sana katika hii sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nashukuru, naona kabisa kwamba hii sheria ni nzuri na ni sheria ambayo itaweza kukidhi mahitaji yetu, itasaidia sana kupunguza migogoro ambayo imekuwepo katika maeneo mengi sana.
Kwa hiyo, naomba itakapokuwa imepitishwa, basi Mheshimiwa Waziri mwiharakishe katika kuitangaza na kuhakikisha kwamba inaanza kutumika ili kusudi kule kwenye kanda na kwenye Halmashauri zetu ziweze kuanza kuitumia hii sheria na iweze kutatua matatizo ambayo yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo machache, ahsante sana.

The Government Chemist Laboratory Authority Bill, 2016

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuja na miswada hii miwili ambayo ni miswada muhimu sana na ambayo tumekuwa tukiisubiri kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naipongeza Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa jinsi ambavyo imeuchambua huu muswada pamoja na Kambi ya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, muswada huu utaleta manufaa mengi sana katika nchi yetu. Kwanza tunaamini kabisa kwamba matokeo ya uchunguzi wa kikemia sasa utakuwa na msemaji mkuu na utakuwa na hadhi inayostahili ndani ya nchi na pia nje ya nchi kwa sababu sasa utalindwa na sheria hii ambayo tunaenda kuitunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, kuanzishwa kwa kamati za kitaaluma ambazo zinashirikisha wadau wa aina mbalimbali, hili ni suala ambali ni la msingi sana na huu muswada utatusaidia sana katika kutatua matatizo mbalimbali ambayo yamekuwepo. Lakini pia katika muswada huu tunaona wakaguzi wa maabara watateuliwa na kupewa kazi za kufanya. Wamewekewa mipaka, wamewekewa maslahi yao, lakini pia wamewekewa mipaka na maeneo ambapo wataishia katika kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika muswada huu tunaona sasa unatamka bayana kwamba maabara zote nchini itakuwa lazima zisajiliwe na sasa zitakuwa zinasajiliwa na kutambulika kisheria. Hiyo itatuwezesha kuondokana na matatizo mbalimbali ambayo yamekuwepo, na uholela ambao umekuwepo katika utengenezaji wa kemikali katika maeneo mengi, na hivyo wananchi wataweza kunufaika na muswada huu na miongozo ambayo itakuwa imetolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kwanza nichangie katika baadhi ya vifungu hivi vya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Nianze na hivyo na kama muda utaruhusu nitaenda sehemu nyingine. Kwanza nianze na hili la kwanza la idadi ya wajumbe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mchango wangu wa jumla, kwanza mimi nakubaliana kabisa kwamba bado Mheshimiwa Waziri apewe mamlaka ya kufanya uteuzi wa Wajumbe wa Bodi, hilo sina matatizo nalo kabisa. Lakini mimi kitu ambacho natofautiana, idadi ya Wajumbe wa Bodi ni kubwa mno katika hizi taasisi za umma. Katika huu muswada inaonekana wanatamka kwamba Wajumbe wa Bodi watakuwa sita, ukijumlisha na Mwenyekiti, pamoja na Mkemia Mkuu, watakuwa wanane. Mimi idadi hiyo naiona ni kubwa sana. Hii inaongeza mzigo wa uendeshaji wa mamlaka. Bodi nyingi ukiangalia ziko sita, saba, nane, mimi nashauri muswada huu ungekuwa na Wajumbe wa Bodi wanne, ukawa na Mwenyekiti na Msajili wanakuwa sita maximum; wanatosaha kabisa kuweza kutekeleza majukumu ambayo yameainishwa kwa mujibu wa sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunaona katika katika hii Bodi ya Mamlaka ambayo itafanya majukumu mengi yenye wadau wengi inachukua zaidi wajumbe kutoka kwenye Serikali na taasisi zake. Mimi nadhani kuna haja ya kuhakikisha kwamba sekta binafsi nao wanakuwemo katika hii mamlaka. Na hii sekta binafsi tunaweza tukaangala kwa mfano, wawakilishi kutoka labda waajiri yaani ATE kule wanaweza wakaleta mtu mmoja akawakilisha wale wadau wa sekta binafsi au kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi; kukawa na mwakilishi huko anaeweza kutusaidia pia katika kuleta mchango na kuchangia katika hii mamlaka na hivyo kutetea maslahi ya hii sekta binafsi; hilo ni suala nafikiri ambalo lingeweza kusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika hizi Bodi naona katika hii Sheria wameweka kwamba akidi katika mkutano ni theluthi mbili. Theluthi mbili ni kubwa sana. Hiyo itafanya baadhi ya vikao vingi viwe vinaahirishwa; na wale Wajumbe ambao wanakuwa wamefika siku hiyo ukiahirisha kikao unakuwa umeshawahribia ratiba. Kwa hiyo, katika Bodi mimi nashauri wangeweka akidi iwe ni nusu badala ya theluthi mbili. Nusu ya Wajumbe inatosha kabisa kuweza kuhakikisha kwamba wanashiriki na wanafanya kikao halali kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika kifungu cha 8(1) kinataja majukumu ya bodi. Majukumu hayo ambayo yanatajwa ukiangalia ni majukumu mazuri tu yameainishwa vizuri sana. Lakini kuna baadhi ya majukumu ambayo yametajwa pale mimi nilikuwa nadhani katika kifungu (h) na (j) nadhani hii kazi pengine iliandikwa labda kwa uharaka zaidi hawakuliangalia vizuri. Najua Mkemi Mkuu wa Serikali ilikuwa ni wakala wa Serikali, na ukishakuwa wakala unakuwa na bodi ambayo tunaiita ni Ministerial Advisory Board, kwa ajili ya kumshauri Waziri ili aweze kufanya maamuzi ya kimkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naona bado katika hizi kazi za bodi wameandika hivyo hivyo. Pale kwenye (h) wameandika itamshauri Waziri katika kufanya strategic policy matters for implementation of the authority. Mimi nadhani hizi ni kazi za wakala. Kwa Bodi ambayo imetajwa, kwa Bodi ambayo ni executive, kwa Bodi yenye maamuzi mimi sidhani kama kazi yake ni kufanya hivyo. Hizo ni kazi zake ambazo zinatakiwa ifanye kama Bodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ukiangalia (j) inasema Bodi itamshauri Waziri. Naomba niisome kwa Kiingereza; “Advice the Minister on performance of the management on the set targets and carries out the policy priorities.”
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sidhani kama bodi itakuwa inampelekea Waziri ni kazi ya bodi hii ku-set target zake si kazi ya kumshauri Waziri. Mimi nadhani hizi kazi pengine walioitayarisha hii sheria wangeangalia vizuri, hizo ni kazi zile zilizokuwepo kwenye wakala, kwa sasa hivi ni kazi za Bodi yenyewe wala sio kazi za Waziri, ni za kwake mamlaka ya bodi hiyo iweze kufanya hayo maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 9(1) kinatamka kamati za kitaaluma za huduma za sayansi, jinai nakadhalika. Na kifungu hiki kinasema hizi kamati za kitaaluma zitateuliwa na Mheshimiwa Waziri. Sasa huyu Waziri tutamrundikia mambo mangapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilidhani hizi ni kamati za kuisaidia ile mamlaka, kuisaidia ile Bodi; hizi zingekuwa za kufanywa na ile Bodi; ziteue kamati za kuweza kuisaidia, za kitaaluma. Sasa kumpa Waziri mimi naona kama tunamuongezea majukumu mengi sana ambayo ufanisi wake sasa unaweza usiwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 11(2) kinataja kazi ambazo Mkemia Mkuu wa Serikali anatakiwa kuzifanya, ikiwa ni pamoja na kutoa miongozo kwa ajili ya utekelezaji wa sheria hii, kuzuia matumizi mabaya ya kemikali kuzuia vitu mbalimbali vya kikemikali na bidhaa zingine za kikemikali. Sasa mimi nilikuwa nadhanai hayo yote ni majukumu ya bodi. Tunaposema sasa ni majukumu ya huyu Mtendaji Mkuu tunaisahau bodi nadhani kidogo pale panakuwa hapajakaa vizuri. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri tuangalie kwamba hayo ni majukumu ambayo ni ya Mtendaji Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 13(1) kinampa tena Waziri kuteua Wakemia wa Serikali badala ya Bodi, mimi nilifikiri kazi zote hizi zingekuwa za Bodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna adhabu ambazo zinatajwa katika vifungu vingi katika hii sheria, mimi nashauri hizi adhabu zote zingehuishwa zikaandikwa katika sehemu moja badala ya kutajwa kila mahali, karibu sehemu sit azote zinataja adhabu hii, adhabu hii na kuna sehemu nyingine inasema wale watu wakifanya uzembe anafungwa miezi sita; adhabu shilingi milioni tano lakini kufungwa miezi sita. Mimi nadhani hizo zianishwe vizuri ziangaliwe ili ziweze kuleta maana halisi hasa iliyokuwa imekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu spika, kifungu cha 25 kinataka maabara zote zisajiliwe, maabara ambazo zipo zote zitasajiliwa na mimi nakubaliana, mimi sina matatizo lakini nataka ufafanuzi hapo Mheshimiwa Waziri atakaposimama. Najua kwenye shule za sekondari huku tuna maabara, shule zote za sekondari zina maabara. Taasisi za umma zimetajwa kwamba pamoja na taasisi za mafunzo, lakini nataka nijue hata maabara za sekondari zote zitasajiliwa au itakuwaje? Na imeweka kabisa kwamba lazima kila maabara isajiiwe. Sasa hiyo tungependa tupate labda ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kifungu cha 37(1) mpaka (3) kinampa Waziri mwenye dhamana na mamlaka hii kuidhinisha bajeti badala ya Bodi. Ukisoma pale Bodi haijatamkwa kwamba itaidhinisha bajeti hiyo. Sasa nilikuwa nafikiri kazi mojawapo ya bodi ni kupitia mpango kazi, kupitia bajeti ya mamlaka na kuidhinisha na baadye ndipo kuijumlisha katika bajeti kuu. Sasa naona hapa kinasema kwamba bajeti hiyo itaidhinishwa na Waziri, hilo kidogo naona kama halijakaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 39 na 40 kinazungumzia taarifa iliyokaguliwa ya mamlaka; na kinasema eti mamlaka inatakiwa iwasilishe taarifa mizezi mitatu baada ya mwaka kuisha; na hiyo miezi mitatu hiyo taarifa iwe imekaguliwa. Nadhani hapo tutakuwa tunachanganya. Kwanza kufunga kwenyewe mahesabu ni miezi mitatu mpaka Mkaguzi Mkuu amalize anahitaji miezi mingine kadhaa. Kwa hiyo hivi ilivyoandikwa; na niliona hata jana tulipitisha sheria nyingine imeandikwa hivyo hivyo; mimi nadhani kwamba tungefata uhalisia kabisa kwamba haiwezekani taarifa ikatayarishwa kwa miezi mitatu ikawa imekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hiyo inaendana sambamba kabisa na hata kwenye hili baraza la wanataaluma wa kemia. Kifungu cha 22(2) kwenye Baraza la Wanataaluma pale kuwasilisha taarifa ya ukaguzi miezi mitatu. Mimi siamini kabisa kwamba taarifa ya miezi mitatu itakuwa imekamilika. Nafiki hapa tutakuwa tunaandika halafu mambo hayawezi kutekelezeka. Kwa hiyo, nilikwa nashauri marekebisho haya yafanyike ili kusudi taarifa ije katika wakati ambao tunajua kwamba kweli itakuwa imekamilika na kifungu cha 23 nacho kinasema hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika zile taarifa ambazo zimeandikwa, taarifa za fedha za mwaka ambazo zinatakiwa kuwasilishwa zimeandikwa pale. Zote zinazohusiana na fedha wametaja. Sasa mimi nilifikiri ni muhimu basi katika zile taarifa iwekwe pia taarifa ya wakurugenzi ya utendaji wa taasisi, yaani tunaita directors report kwa kitaalamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, directors report ndiyo itakayoonesha majukumu makuu ya taasisi, jinsi walivyotekeleza majukumu yao na shughuli zote jinsi ambavyo zimekwenda.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba waangalie hilo, waangalie hayo yote na mengine nitayawasilisha nitakapokuwa nawasilisha naunga mkono hoja asante sana.

The Tanzania Agricultural Research Institute Bill, 2016

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kwanza kuipongeza Serikali kwa kuja na Miswada hii miwili ambayo ni Miswada muhimu sana katika maendeleo ya nchi yetu. Tumeona kabisa katika Miswada hii taasisi hizi inaonekana zitafanya kazi ya kufanya utafiti katika masuala ya kilimo na masuala ya uvuvi lakini pia itadhibiti na kuratibu shughuli zote zinazohusiana na maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Miswada imekuja kwa wakati muafaka, lakini naomba nichangie kwa maeneo machache. Nianze na maeneo ya jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii Miswada yote miwili na mambo ambayo yanaelezwa katika hii Miswada miwili ni mazuri sana. Nianze kwanza na ukubwa wa Bodi. Nimekuwa nikisema na tutaendelea kusema, kwamba Bodi hizi ni gharama kubwa kuziendesha; Bodi hizi zinatumia fedha ya walipa kodi; na Bodi hizi zikiwa kubwa kiasi hiki, ufanisi wake unakuwa ni mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye hii sheria imeandikwa Bodi itakuwa na wajumbe tisa, ukijumlisha na Mwenyekiti pamoja na Mkurugenzi wanakuwa 11. Hiyo Bodi ni kubwa sana. Bodi hizi zikiwa kubwa namna hii, zinatuletea matatizo. Zinaongeza gharama za uendeshaji kwenye Serikali. Kwa hiyo, naomba waliangalie upya, hakuna sababu yoyote Bodi kuwa kubwa kiasi hicho. Bodi nzuri zinakuwa na Wajumbe wanne na Mwenyekiti labda na Mkurugenzi, wanakuwa sita maximum; lakini Bodi ya Wajumbe 11, kidogo inanipa wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimeona katika muundo wa hizi taasisi, ni taasisi za utafiti nakubali, lakini najua kabisa katika hizi taasisi, nyingi ikiwemo Chuo cha Kilimo Uyole na vingine vingi, vilikuwa pia vinafanya kazi ya kutoa wataalam wanaohusiana na masuala ya kilimo na masuala mbalimbali. Wataalam hawa wa mafunzo mbalimbali ambayo walikuwa wanayatoa yalikuwa yanatolewa halafu wanasajiliwa, yanatambulika katika nchi. Vyuo hivi vilikuwa vimesajiliwa na Baraza la Taifa la Vyuo vya Ufundi (NACTE) na hivyo mafunzo waliyokuwa wanayatoa, iwe ni katika Astashahada au katika Stashahada au katika ngazi nyingine yoyote ni mafunzo yaliyokuwa yanatambulika na bado ilikuwa ni kazi muhimu sana katika kuchangia kupatikana kwa wataalam katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika huu Muswada sijaona mahali ambapo wanagusa hizi kazi kwamba pamoja na kazi za utafiti, lakini pia vyuo hivi vitafanya kazi ya kuzalisha hawa wataalam ambao tunawahitaji sana katika haya maeneo. Kwa hiyo, nafikiri ni suala la kuliangalia pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, hizi taasisi ni nani atakayekuwa anazisimamia? Taasisi za Elimu ya Juu tunajua kwamba kuna TCU wanazisimamia; taasisi nyingine za mafunzo tunajua kuna NACTE wanazisajili, wanazisimamia. Hizi taasisi za utafiti, ni nani ambaye ni regulator wa hizi taasisi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vitafuata muundo wa Baraza la Taifa la Vyuo vya Ufundi (NACTE) maana yake hata muundo wake lazima ufuate ule muundo ambao ulishapitishwa wa taasisi hizo. Ambapo kunakuwa na Director General au Mkuu wa Chuo, anakuwa na wasaidizi wake, inaeleweka kabisa na muundo upo wazi wazi. Sasa hii tunayoiweka kwenye hii taasisi moja naona kunakuwa; mmesema kutakuwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kuna Mkurugenzi Mkuu anateuliwa na Rais, Naibu Mkurugenzi Mkuu anateuliwa na Waziri, Wakurugenzi wanateuliwa na Bodi. Naona kama tunajaza mambo ambayo yataleta migongano mbele ya safari kiutendaji. Yatagonganisha tu! Mtu atashindwa kutekeleza majukumu yake anasema bwana kwa nini unaniambia hivi? Wewe umeteuliwa na Rais, nami nimeteuliwa na Waziri; inaleta migongano. Kwa nini huyu Naibu sasa asiteuliwe na Bodi? Kwa nini tuweke mpaka hadi aende kuteuliwa na Waziri? Mimi sioni sababu. Nafikiri hilo kuna haja ya kuliangalia vizuri ili muundo wao uwe ni mzuri na uendane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata kwenye taasisi ya kilimo, nimeona hakuna Naibu, lakini naamini kabisa wale Wakurugenzi wanatosha kabisa na wale watakaosimamia vile vyuo ambavyo vimezungumziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 22 mpaka 25 kimetoa masharti kwa watafiti wote watakaofanya utafiti wa masuala ya kilimo, wote lazima wasajiliwe na hii taasisi. Pia miradi watakayokwenda kuifanyia utafiti lazima isajiliwe, ni kitu kizuri tu, sina matatizo, isipokuwa naangalia, wapo watu walikuwa wanafanya utafiti wa masuala ya kilimo, wapo wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo vyetu wanafanya utafiti huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, sasa tunataka kusema kwamba, hawa vijana ambao wanasoma au mtu kama yupo shuleni anasoma na anasoma Ph.D kwenye haya masuala, ni lazima kwanza akapate kibali kwenye hii taasisi ndiyo aendelee na utafiti. Sasa hilo naliona kidogo kama linakinzana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba kuna haja ya kuangalia vizuri hizi ili kusudi tunaposema kwamba kila utafiti lazima usimamiwe, nakubaliana, lakini kuwe na utaratibu unaoeleweka kwa wale ambao wapo kwenye mafunzo ili kusudi tuepukane na matatizo ambayo tumekuwa tukikutana nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tumekuwa na matatizo mengi sana. Tumeona kwa mfano, mwaka jana na mwaka juzi kule kwetu ilitokea kule Mbeya, watu walikuwa kwenye utafiti, wamefanya utafiti, wamepata mbegu mbovu, mbegu mbaya, badala ya kuzitupa, wamepeleka sokoni, wamewauzia wananchi wetu. Wamenunua mbegu mbaya na hadi ikaharibu kabisa kilimo. Sasa hiki siyo kitu kizuri, kwa hiyo, ni suala la msingi ambalo lazima tuliangalie katika mtazamo huo wa kudhibiti mambo yanayoendana na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Miswada hii haijaonesha namna tutakavyokuwa tunashirikiana na vyuo vingine kama Chuo Kikuu cha Kilimo. Kwenye huu Muswada haijataja tutakuwa tunashirikiana nao vipi? Wale wataalam ambao wapo kule, watashiriki vipi katika hii taasisi? Kwa hiyo, nafikiri kuna haja ya kuliangalia vizuri na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nataka kuzungumzia kuhusu mapato. Katika taasisi yoyote kuna mapato yanayotokana na shughuli wanazozifanya, lakini pia kuna mapato ya ushauri na pia kuna mapato yanayotokana na utafiti, yaani funded research. Zile funded research nimeangalia katika vile vyanzo haijazungumzwa. Ule ushauri wa kitaalam watakaokuwa wanatoa, haujazungumzwa pale. Sasa nafikiri kwamba ni vyema wakaangalia ili kusudi viweze navyo kuwa ni sehemu ya mapato ya taasisi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo sijafurahishwa nalo, nimeona kwenye taasisi hizi sheria inasema watarithi mali na madeni ya taasisi zilizokuwepo. Tunapoanzisha taasisi kama hizi, tukisema zirithi na madeni yaliyokuwepo kwenye vyuo hivyo, vitashindwa kusonga mbele. Hayo madeni Serikali ingeyachukua ili vikianza vianze fresh badala ya kurithi madeni. Hili sioni kama linakuja vizuri. Kwa hiyo, ni suala la kuliangalia vizuri badala ya kurithi na madeni ambayo yapo nafikiri tungekuwa na utaratibu mwingine ambao ungeweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona kwenye adhabu zinazotolewa katika utekelezaji wa hizi sheria. Adhabu hizi napendekeza ziangaliwe vizuri. Naona kuna adhabu unakuta kwamba wanasema fine ya fedha, shilingi milioni 20; kifungo ni mwaka mmoja, fine ya fedha shilingi milioni 10; kifungo, miezi sita. Nadhani hizi adhabu zingehuishwa; afadhali ingekuwa inasema labda mwaka mmoja mpaka miaka mitano au muda gani; hii ingetusaidia sana katika kuweza kuweka vizuri hizi taratibu ambazo nafikiri ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niongelee pia kuhusu suala la utafiti. Umefika mahali ambapo Serikali lazima itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kugharamia taasisi mbalimbali zitakazotoa mchango katika nchi yetu. Kila mwaka tumekuwa tukiimba kilimo ni uti wa mgongo, sijui uvuvi, sijui nini na nini; bila kutenga fedha za utafiti, tutakuwa tunaimba kila siku, tutakuwa tunapiga kelele bila sababu yoyote. Lazima fedha za kutosha zitengwe na tuweke kama ni kuwekeza. Kufanya utafiti ni kuwekeza na matokeo ya tafiti…
MWENYEKITI: Ahsante.

The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.4), Bill, 2016

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa kupata hii nafasi ili niweze kuchangia katika muswada huu ulioko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta muswada huu mzuri, muswada ambao unakwenda kutatua matatizo mengi ambayo yamekuwa yakiikabili nchi yetu, kwa kweli tunampongeza sana.
Pia naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa jinsi ambavyo wamechambua muswada huu na maoni yake ambayo wameyatoa ili kuboresha muswada huu, na nadhani kwa kweli wamefanya kazi nzuri, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningependa nichangie maeneo machache, lakini la kwanza ambalo ningependa nianze nalo ni hili suala la mikopo yenye dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkopo wowote duniani una masharti yake, mkopo wowote ambao mtu anahitaji au taasisi inahitaji una masharti ambayo lazima kigezo hicho kizingatiwe. Sasa kwenye nchi yetu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kwamba kuna Serikali mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika hilo, imeweka mipaka baadhi ya masuala ambayo yanashughulikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na masuala ya fedha ni mojawapo ya suala la Muungano, kwa hiyo hili ni lazima lishughulikiwe na sheria za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na matatizo kwa muda mrefu na kumekuwepo na malalamiko ya pande hizi mbili kwamba katika baadhi ya mikopo ambayo imekuwa ikitolewa imekuwa haizingatii sheria, imekuwa haizingatii masharti na kanuni za mikopo. Mimi naona hii Sheria inayoletwa mbele yetu sasa inakuja kutatua haya. Sasa hatuwezi kuzungumzia ya nyuma, tukasema miaka mingi imepita, aaa, sasa wakati umefika ndiyo maana sasa Serikali ya Awamu ya Tano inataka kutatua haya ili tuweze kusonga mbele, kwa hiyo mimi nadhani hii ni nia njema kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema taasisi yoyote ambayo inaomba mkopo wa aina yoyote; kumekuwepo na tabia ya taasisi nyingi katika nchi hii zimekuwa zikiomba mikopo na zinaomba dhamana ya Serikali lakini inapokuja kulipa zimekuwa zinasuasua hazilipi, sasa hii sheria inaboresha, sheria hii sasa inakuja kutatua haya matatizo. Inasema taasisi yoyote ambayo itakopa ambayo ina miradi ya maendeleo, maadamu miradi hiyo itakubalika, basi ikope lakini tuangalie wana uwezo wa kulipa? Kama hawana uwezo wasipewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sheria jinsi ilivyoweka mimi nakubaliana nayo kabisa kwamba lazima tuangalie uwezo wa kulipa wa taasisi yenyewe na taasisi ikionekana ina uwezo ndiyo ipewe mkopo, haina iwezo isipewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri hii sheria tena imeweka masharti magumu. Imeweka masharti kwamba kama taasisi itakopa na itashindwa kulipa, basi wale viongozi wachukuliwe hatua hii sheria ni nzuri sana, wachuliwe hatua kweli kwa sababu dawa ya kukopa ni kulipa. Huwezi ukasema unakopa halafu unakimbia kulipa, dawa ya deni ni kulipa na ndiyo maana tunasema, hata Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sasa inaruhusiwa kukopa katika miradi ile ambayo inaona kwamba ina manufaa kwa nchi yao, lakini pia lazima tuzingatie uwezo wa Zanzibar wa kulipa hayo madeni, ndicho kinachoelezwa katika hii sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wakope halafu wasilipe, kwa hiyo kama watakopa, sheria hii inawaruhusu lakini tunasema tuangalie balance sheet yao wana uwezo wa kulipa maana ni masuala ya Muungano? Sasa wasipolipa itakuja kuwa ni tatizo la Muungano. Ili lisiwe tatizo lazima tuangalie uwezo wao. Tukiona hiki wana uwezo tutawaruhusu wakope, walipe, waiendeleze Zanzibar hilo mimi sidhani kama lina tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo hili mimi naunga mkono kabisa Sheria hii ilivyokaa imekaa vizuri na Wazanzibar nadhani ni wakati muafaka sasa wataendelea vizuri, watafanya vizuri lakini tunawashauri wakope na walipe na watalipa kwa taratibu zilizopo, watalipa principle, watalipa na riba ile inayotakiwa. Hatutazidisha riba, riba iliyokubalika ndiyo hiyo hiyo walipe. Kwa hiyo, mimi nadhani sheria imekaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ambalo ningependa nichangie ni suala marekebisho ya hii sheria inayohusu mikopo ya elimu ya juu
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Mikopo ya Elimu ya Juu, hii sheria sasa imesema vijana wetu wanaosoma kwenye vyuo vya elimu ya juu kulikuwa na malalamiko mengi. Kulikuwa na mambo mengi ambayo yapo. Sheria hii sasa inarekebisha inasema; hata vijana sasa wenye diploma waruhusiwe kukopa mimi nadhai hii sheria ni nzuri sana ya kuiunga mkono. Maana yake tuna vijana ambao wana stashahada katika fani mbalimbali, kwa mfano; fani za afya, mafundi mchundo tunahitaji, hatuhitaji watu wawe na degree, tunahitaji hawa wote wapate elimu itakayotusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda kuwa nchi ya viwanda hao ndio wanaohitajika kwenda kufanyakazi, sasa ili tuwapate lazima wapate mikopo. Kwa hiyo huu utaratibu mimi naomba niseme kwamba nauunga mkono kabisa, sheria hii irekebishwe, vijana wetu wale wote wenye stashahada wapate mikopo na ikiwezekana badala ya kusema fani fulani fulani, fani zote ziruhusiwe kukopa, maana ni mikopo, watalipa. Watalipa hawa, wakikopa watalipa. Kwa
hiyo, mimi nashauri kabisa kwamba hawa vijana ni wakati muafaka waangaliwe.
masharti yaliyowekwa kwenye mikopo; kuna haja ya kupitia. Tunaweza tukaweka kwa mfano katika hii fani ya stashahada tukasema mtu yoyote ambae ana-upper second and above au ana-first class, ana-upper second uruhusiwe kukopa badala ya kuwawekea kwenye taaluma kwamba taaluma fulani ndiyo wakope wengine wasikope. Wote waruhusiwe washindane ili kuwe na uwazi katika utoaji wa hii mikopo. Mimi nadhani hili litatusaidia sana katika kuweza kuleta maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nichangie kidogo kuhusu misamaha ya kodi. Sheria hii imezungumzia juu ya misamaha ya kodi ambayo imekuwa ikitolewa na Waziri na imeweka utaratibu mzuri kwa jinsi Waziri anavyoweza kutoa misamaha ya kodi. Mimi nadhani hili limekuwa ni tatizo la muda mrefu sana. Nchi yetu tunashindwa kuendelea kwa sababu ya misamaha mingine isiyokuwa na tija, na niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano imepunguza sana misamaha ya kodi kwa kweli nawapongeza sana, imepunguza sana hii. Lakini tuendelee kuboresha kabisa ili misamaha ya kodi itakayokuwa inatolewa itolewe iwe ni ile yenye tija tu, iwe yenye tija tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wanaozungumzia Kuhusu Utaratibu, ndiyo maana sisi tumeshinda Kata 22 kati ya ngapi, tunawapongeza. Sisi tumeshashinda hapa tunazungumzia kuleta maendeleo, jinsi ya kuwatumikia Watanzania hayo Kuhusu Utaratibu…mimi nachangia. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mweyekiti, mimi nadhani waangalie kitu cha kufanya haya mambo ni ya msingi, tunazungumzia maendeleo ya nchi hii. Kwa hiyo, misamaha ya kodi itakayokuwa inatolewa tuangalie wale wote wanao-qualify zile taasisi...
ile misamaha ya kodi iwe ni misamaha yenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti mimi nadhani haya ni masuala ya msingi sana ambayo sheria hii iliyoko mbele yetu inaenda kuyatatua, lazima sote tuiunge mkono kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nimalizie kwa kusema nawapongeza Wabunge wapya ambao wameteuliwa na ambao wameapa jana, washirikiane nasi katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Nchi yetu hii wananchi wanahitaji maendeleo ya kweli na naomba tushirikiane tulete maendeleo, ahsanteni sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's