Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Peter Ambrose Lijualikali

All Contributions

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Naam!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuzungumza kidogo. Naomba nizungumzie kwamba kama tunataka kutengeneza nchi ya viwanda ili twende kwenye uchumi wa kati mimi nafikiri kiwanda ni matokeo ya uwekezaji katika umeme. Lazima tuwe na umeme utakaoweza kufanya viwanda vifanye kazi. Kwa hiyo, niishauri Serikali kwamba ijitahidi sana kuwekeza katika umeme ili tuwe na umeme wa uhakika. Tukiwa na umeme wa uhakika viwanda ambavyo tunataka vije ama tuvifufue basi viweze kupata uwezo wa kufanya kazi vizuri. Huo ulikuwa ni ushauri wa kwanza. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nizungumzie hoja hii ya sukari. Tanzania kuna viwanda vinne ambavyo vinazalisha sukari. Kuna kiwanda cha Ilovo, kipo Jimboni kwangu Kilombero, kuna kiwanda cha Mtibwa, kuna cha TPC na kuna Kagera. Kiwanda cha Ilovo kimefunga uzalishaji wake tangu mwezi wa kwanza na hii ni kwa sababu ya maintenance, lakini leo ajabu karibu tani nane za sukari kutoka Ilovo zilikuwa kwenye godown hapo Tabata zimeuzwa leo. Hili godown lipo Tabata limeuza tani nane. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba tuna sukari ambayo imefichwa na wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais akiwa na nia safi, mimi nasema safi kwa sababu anazungumza vizuri ya sisi tuweze kupata sukari na viwanda viendelee, watu wanaficha sukari, wanasubiri maintenance za viwanda zikifanyika wao ndiyo watoe mzigo. Kibaya zaidi baada ya huu upungufu wa sukari hawa watu wanataka wapewe vibali vya kwenda kuagiza sukari yaani watu wanaoficha sukari kwenye ma-godown leo wanataka wao ndiyo wapewe vibali vya kwenda kuagiza sukari. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba hao watu kwa tabia yao hii ya kuficha kwanza hatuna uhakika kama wataagiza ambacho wameruhusiwa, maana yake ni kwamba wataongeza. Wakiongeza viwanda vyetu hivi vinne vya Ilovo, Mtibwa, TPC na Kagera vikianza production vitakuta tayari kuna mzigo mkubwa upo kwenye soko vitapunguza uzalishaji. Vikipunguza uzalishaji maana yake hawa wakulima wetu mfano wakulima wangu kule Sanje, Kidatu, Mkula wataathirika. Tunakwenda kuua hawa wananchi ambao wanaendesha kilimo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa, niiombe Serikali isiruhusu kabisa wafanyabiashara waagize sukari nje. Mimi najua kuna watu wamewekwa humu ndani waweze kuongea maneno haya, wamewekwa humu ili waweze kusema kwamba wafanyabiashara waruhusiwe, niombe Serikali, hivi viwanda vinne na kwa sababu Serikali hii inaweza sana, hawa Mawaziri wanafanya kazi bila kuwa na sheria, hawana kazi, basi niombe kama huo ndiyo utaratibu wetu hata kama viwanda hivi watasema kwamba sijui havina mamlaka haya, tuendelee hivi hivi tu, tufunike hivi hivi hawa wenye viwanda, viwanda hivi ndiyo viagize sukari ili kulinda viwanda hivi na wakulima. Nilikuwa nataka hili niliweke sawa watu wajue na Serikali ijue kwamba kuruhusu wafanyabiashara binafsi kuagiza sukari ni kuua viwanda na kuuwa wananchi watu wa Sanje na sehemu zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu Morogoro. Morogoro ina viwanda vingi sana lakini viwanda hivi watu wanafuga mbuzi, hapa ndipo wanaposema we have killed our past and we are busy killing our future. Tumeua past yetu na tuko busy kuua future yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi huwa najiuliza hivi nia ya Serikali ya privatization (kubinafsisha) hivi viwanda ilikuwa ni nini? Ilikuwa ni kuwapa watu nafasi ya kupata maeneo ya kufuga, kuuza mashine zetu kama scraper au nia ilikuwa tuongeze uzalishaji na ajira?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nia ilikuwa ni kuongeza ajira na uzalishaji hivi inakuwaje tunakuwa na viwanda yaani kama Taifa tumejiminya, tumepata viwanda, tukasema wenzetu mviendeleze halafu wanachukua hivyo viwanda wanaanza kufugia mbuzi, wanakata mashine, wanauza kama scraper, kama Taifa hii ni aibu! Sidhani kama Serikali hii ya Awamu ya Tano inayosema Hapa Kazi Tu itaruhusu kwamba hizi ndizo kazi zenyewe. Yaani kazi ya Mwalimu Nyerere ilikuwa kuunda viwanda halafu watu wengine waje kukata scraper! Sidhani kama hii ndiyo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mifano hapa, pale kwangu Mang‟ula pana kiwanda kinaitwa MMT, nina handover letter hapa ambayo hii Serikali ilikabidhi hiki kiwanda kwa Mama Rwakatare, Mama Rwakatare huyu huyu ambaye alikuwa Mbunge, handover hii hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu walikuwa hawajui kama mlikuwa mnaona vifaa kama mapanga na kadhalika vyenye picha ya mamba ilikuwa ni Mang‟ula. Kiwanda tumekabidhiwa kikiwa kizuri, kikiwa kina kila kitu lakini pale sasa hivi kuna mbuzi tu ndiyo wanachungwa pale lakini unakuta eti mtu naye anajiita mwekezaji, amewekeza nini huyu? Umewekeza kwa kuua uchumi wa nchi? Kile kiwanda kilikuwa kinatoa ajira pale, Serikali ikaamua kutoa, ikasema endeleza na nimuombe Waziri twende kule akaone kiwanda hiki ambacho kilikuwa kina manufaa katika nchi yetu leo kimekuwa cha kufunga mbuzi. Hatuwezi kujenga Taifa la hivi na tukiongea hivi hatumuonei mtu, tunaongea ukweli kwa sababu ya faida ya Taifa letu. Kuna watu huko hawana ajira, tumetoa viwanda watu wanafugia mbuzi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kama haitoshi, kuna kiwanda kingine kilikuwepo pale Mang‟ula, wengine mnafahamu vizuri wakati reli hii ya TAZARA inajengwa vifaa vya kutengeneza yale mataruma vilikuwa pale Mang‟ula. Mwalimu Nyerere kaacha viwanda vizuri, kiwanda vya Ilovo, kiwanda vya Mtibwa spare zake ilikuwa wanazipata Mang‟ula. Leo kiwanda mtu anachukua semi-trailer anapakia chuma chakavu anapeleka kuuza, sisi tupo tu hapa, Taifa lipo, Serikali ipo! Kiwanda kinahujumiwa, nchi inaliwa tunasema wawekezaji, what kind of this business? Are we serious?
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: We are not serious and never be serious. We have killed our past and we are busy killing our future. Ukiuliza, anaongea mpinzani, anaongea UKAWA, come on lets be serious! Tunazungumzia uchumi wa nchi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri twende tukaone kule! Kiwanda ambacho mnasema mmempa mtu mkaone…
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naitwa Peter Lijualikali, siyo Juakali. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutimiza jukumu langu la Kikatiba kuwepo mahali hapa na nitaanza na TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango wa kuisaidia miji ili iweze kuendelea nimeona hapa kuna miji 18 ambayo Mheshimiwa George Simbachawene ameiweka kwenye hotuba yake, kwenye hii miji siuoni Mji wa Ifakara, ni mji mpya ambao ninadhani kwa changamoto ambazo mji huu unao kama za barabara na juzi tulikuwa na mafuriko makubwa sana ambapo Mto Rumemo umekuwa na kawaida ya kumwaga maji kuja Mjini Ifakara, sasa nimeshangaa tangu bajeti ya 2016 miji ni ile ile 18, kuna miji mipya mwaka jana imetangazwa na Ifakara ikiwemo, lakini mji wangu wa Ifakara hauonekani kwenye huu mpango.
Sasa nichukue wakati huu kumuomba Mheshimiwa Waziri Simbachawene aweze kukumbuka Mji wa Ifakara kwa maana ni mji mpya, mji ambao una changamoto, ningependa kuona unaingia kwenye huu mpango ili mji uweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye suala lingine la utawala bora na hapa nitasema kidogo. Mwaka jana wakati tunakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na mara zote tumekuwa tukisema Tume hii siyo huru na mfano hapa upo; kwamba Tume ya Uchaguzi ilikuja Ifakara, Kilombero ilikuja kuhakiki majimbo mapya na huu ni mpango wa kila baada ya miaka mitano. Mwenyekiti wa Tume hii akasema Ifakara kwa kuwa ni Halmashauri ya Mji ina-qualify automatic kuwa Jimbo la Uchaguzi, sehemu ikishakuwa Halmasahauri maana yake ina-qualify kuwa Jimbo automatic. Kile kigezo cha population hapa hakipo tena kwa sababu hii ni mamlaka inayojitegemea. Kunakuwa na Baraza la Madiwani, Halmashauri, Mkurugenzi na Idara kamili which means ina-qualify kuwa na Mbunge hapa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Jaji Lubuva kukiri kwamba Ifakara ina-qualify kuwa jimbo nikashangaa anakuja kutangaza majimbo mapya Ifakara haipo. Nikashangaa sana na nikasema kama Serikali ya CCM inaongoza mambo yake kisheria na kwa miongozo ya Katiba ni kwa nini Ifakara iachwe, wakati sheria na vigezo vya Ifakara kuwa Jimbo vilikuwa vinaipa Ifakara kuwa jimbo. Na nikasema kama Tume ya Uchaguzi inao wataalam, ina wanasheria na wanajua fika kwamba Ifakara ina-qualify kuwa jimbo lakini kwa makusudi wakanyima Ifakara kuwa jimbo tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi siyo huru, haifanyi kazi zake kisheria ni uhuni unaofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho tumekuwa tukisema upinzani kwamba hii Tume hii irekebishwe nafikiri kuna haja ya hii kitu kufanyiwa kazi na katika mazingira kama haya kama Tume inakubali kabisa kwamba Ifakara inapaswa kuwa jimbo halafu wanashindwa kulifanya jimbo kwa nini tusikubali kwamba pia Lowassa mlimwibia? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kitu kipo wazi, yaani kitu kipo wazi tu kisheria kwamba hii sehemu inafaa kuwa jimbo Mwenyekiti wa Tume anakubali kwamba hii sehemu inafaa kuwa jimbo lakini anafanya lisiwe jimbo kihuni tu, kwa nini tusikubali kwamba Tume hii CCM mmekuwa mkiitumia kihuni ili mfanikiwe ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye hii hii utawala bora yametokea mpaka mimi nakuja kukamatwa na polisi wananikwida kwa sababu ya huu uhuni leo eti polisi mwenye „V‟ koplo anakuja kumkamata Mbunge kihuni kabisa. Leo hii kila mtu anasema Lijualikali ulionewa unastahili kwenda Kilombero na bahati yangu kwenda Kilombero nazuiwa na polisi na nina kesi mahakamani kwa sababu hiyo, halafu mnasema eti hapa kuna utawala bora!Huo utawala bora uko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo nadhani Taifa hatupaswi kuyaendeleza. Ninadhani tuna kila sababu ya kurekebisha siasa zetu. Kama sehemu inastahili haki zake sehemu inastahili na haya unakuta hata katika Mkoa wa Dar es Salaam, Madiwani wengi ni wa UKAWA, lakini Serikali ya CCM mmetafuta namna zozote mnazoziweza ili mshinde Jiji. Mmefanya kila namna mnahangaika, mnajua kabisa hamna haki hiyo, lakini mnahangaika mnavyoweza ili muweze tu kushinda.
TAARIFA....
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli unabaki pale pale kwamba tumetumia miezi mitano, tumefanya vurugu, mpaka zimekuwa forged hati za mahakama ambazo mahakama imekataa. Nabaki kwenye msingi ule ule kwa nini mpaka mahakama isingiziwe? Kwa nini mpaka tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nimekosea kusema Rais, na Rais anisemehe sana na ninyi mnisamehe lakini nina hoja ya msingi hapa, hii hoja hatuwezi kuidharau, kwa nini mpaka tufikie huku? labda nimesema hivi kwa sababu nimekwazwa moyoni, nimeumia moyoni yaani ni kwa nini nifanyiwe hivi, Rais yupo, Waziri Mkuu yupo, mpo wote kwa nini vitokee hivi? Kwa hiyo, ni kweli naomba mnisamehe, najua mnajua kwamba mlikosea na Mungu awasamehe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye hoja nyingine, kuna kitu...
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda umeisha jamani.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ndiyo nimeyasema sasa hivi hapa, this is not fair, haya nimeyasema sasa hivi tu, ameongea mbele yangu muda amechukua hapa na umeona kabisa, ndiyo nimesema sasa hivi mambo haya, hamsikii tunasema hapa ndani lakini hamsikii, hatuwezi kwenda hivi kama Taifa!

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa leo ni mara ya kwanza nasimama ndani ya Bunge lako kuzungumza tangu nimetoka Gereza la Ukonga, ambako nilikuwa natumikia kifungo batili cha miezi sita, nashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kilombero, kwa namna ambavyo wananipenda, wananiheshimu na wanajua mchango wangu kwao, kiasi ambacho nilipokuwa nimefungwa hawakukata tamaa, walikuwa wanakuja kuniona, walikuja kwa wingi Idete, mpaka ikaonekana wanaweza wakavunja Gereza, maana walikuwa wengi sana, ikabidi nihamishwe. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe shukrani za pekee kwa Chama changu, Mwenyekiti wangu wa Chama Taifa Mheshimiwa Mbowe, Wakili wangu msomi Mheshimiwa Tundu Lissu, pia ninawashukuru watu wote waliokula njama, walionifanyia fitna na uhuni ili nifungwe, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mhehsimiwa Mwenyekiti, vilevile niwashukuru Wabunge wa CCM wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB) Mheshimiwa Mbowe anazungumza yanayonisibu gerezani na kutaka Bunge lichukue attention nawashukuru kwa kumzomea, ila mjue mlikuwa hamzomei Mwenyekiti, hamkuwa mnamzomea Mbowe ila mlinizomea mimi, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kabisa ninawashukuru wafungwa wa Gereza la Ukonga na wale wa Gereza la Idete, maana naamini maisha yangu yalikuwa mikononi mwao. Wangeweza kufanya ubaya wowote lakini waliniheshimu, wakanitunza na niseme Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu programu ya Parole ambayo ni misamaha kwa wafungwa. Misamaha hii ambayo inatumika vibaya na vizuri. Gerezani nimekuta kuna wafungwa wazee ambao wamefungwa miaka ya 1970 mpaka leo bado wapo gerezani, lakini Serikali mmekuwa mkitoa msamaha kwa wafungwa wanaofungwa miezi sita, vifungo vidogo. Nataka nimwambie Waziri, nilimwambia tukiwa wawili na leo ninasema mbele ya Bunge, vifungo hivi vya miezi sita, wahalifu wakubwa wa Taifa hili, wanatumia vifungo vidogo kufanya uhalifu wanakuja gerezani, wanakaa kwa muda mchache, halafu wanatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mtu anajipa kesi ndogo ambayo anajua atafungwa miezi sita, anajua atakaa miezi mitatu, atapata msamaha. Anakuwa na kesi hiyo mahakamani, anakwenda anafanya tukio kubwa la mauaji au ujambazi ile kesi ndogo inamfunga, anakuwa amejikinga na lile tukio kubwa ambalo amelifanya mtaani. Waziri wa Mambo ya Ndani unatoa msamaha kwa huyu mfungwa pasipokujua umemsaidia kuficha kesi kubwa ambayo alikuwa nayo mtaani.

Kwa hiyo, mnawafunga watu kwa miezi michache mnawatoa, baada ya muda mfupi kumbe walitakiwa wapate msamaha watu wenye vifungo vikubwa, hii ingesaidia kuwafanya watu wenye vifungo vya muda mfupi peke yao waone kwamba hii siyo kinga.

Mheshimiwa Waziri, hili nilikwambia na leo nasisitiza Parole muwe mnaangalia vifungo, msijali kwamba hiki ni kikubwa mkaona hawa hawafai, hawa wenye vidogo basi ndiyo tuwatoe, vidogo vinatumika kuficha maovu makubwa. Kwa hiyo, naomba hili muangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ukiwa Ukonga na magereza mengine, nimeshuhudia askari wakifanya njama pamoja na maafisa wa mahakama, wale admission officers wafungwa wanakosa kupata haki zao za kupata Hati za Hukumu pamoja na upande wa mashtaka, kunakuwa na uhusiano mzuri kati ya mahakama pamoja na askari wa admission. Mfungwa akiomba apate nakala ya hukumu akienda kule mahakamani anaambiwa muone askari fulani, askari yule anamwambia mfungwa lazima utoe hela, ndiyo upate hati ya mashtaka na mwenendo wa mashtaka. Hii maana yake ni kwamba askari wako lazima uwaangalie. Vitengo vya Admission vinatenda rushwa, vinazuia wafungwa kupata haki yao, naomba hilo Mheshimiwa Waziri uangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu hii programu mnasema ya urekebishaji. Mimi nilipokuwa gerezani nilitegemea ningeona huo urekebishaji mnaousema, kwamba wafungwa mnawarekebisha kwa programu ambayo ni tangible. Nione kuna programu ya urekebishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho nimekiona sasa sijui kama huu ndiyo urekebishaji wenyewe, nimeona marungu, mfungwa anapigwa marungu mpaka mguu unageuka. Unapigwa rungu mpaka mguu unashindwa kutoka.Nimeona wafungwa wanafanyishwa, labda niseme nilipoingia mara ya kwanza gerezani, askari wako walinikamata wakanipiga mitama, sijafanya chochote nimeingia hapo. Sasa sidhani kama Mbunge naweza nikafanyiwa hivyo wafungwa wa kawaida sijui wanafanywaje na siamini kama huu ndiyo urekebishaji au nilifanyiwa hivyo kwa sababu mimi ni Mbunge wa Upinzania labda, lakini kama hizo ndiyo programu za urekebishaji, vile ambavyo wafungwa wanafanyiwa mle ndani, wafungwa wanauwawa, wanapigwa risasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,mimi nimefanyiwa mambo ajabu kama hayo katika Gereza la Idete, askari ananiambia nitakuuwa. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri uliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuambie wewe ni Waziri mpaka wa wafungwa, usifikiri kwamba wewe ni Waziri tu kwa watu ambao wako mtaani, nenda gerezani kasikilize vilio vya wafungwa. Wafungwa wana matatizo makubwa sana nenda kawasikilize, wanavyofanyiwa mambo ya ajabu mle ndani. Nilikwambia tukiwa wawili na leo nakwambia, nenda kasikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoamini kabisa mtu yeyote wa Mungu anajua kabisa vitabu vinasema waonee huruma wafungwa, wagonjwa, walemavu na wajane. Hizi kauli za wamenyeke tu, Mheshimiwa Rais anasema hawa wafungwa wamenyeke hawafai, wafanye kazi mpaka wachubuke,mimi nilifungwa kihuni, nimeonewa, sina kosa, lakini Rais alisema kwamba nimenyeke. Ningekuwa sina Wakili msomi kama Mheshimiwa Tundu Lissu maana yake yake na mimi ningebaki ninamenyeka. Sasa kuna watu wangapi ambao nchi hii wanamenyeka kwa uhuni tu ambao wamefanyiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri, wale wafungwa ni binadamu, wafungwa ni watu. Yeyote aliyepo hapa ipo siku chochote kinaweza kikatokea. Sheria mnazotunga hapa, wakati mimi nasema haya wewe umevaa crown upo juu unafikiri uko sahihi, ipo siku na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena kuhusu maisha ya askari. Mheshimiwa Waziri nikuulize, hivi leo ukiambiwa uchague, ukae kwenye choo chako au ukae kwenye nyumba wa Askari wa Magereza wa Idete wewe utachagua ukae wapi? Kati ya choo chako wewe Waziri, choo chako wewe Mbunge na chumba cha Askari wa Magereza uambiwe ukae kwa siku moja utakaa wapi?

Utakaa chooni kwako. Nyumba ya askari wa nchi hii wa magereza ni mbaya choo chako ni kizuri. Wabunge vyoo vyenu ni vizuri, vyoo vya askari wenu, na hawa askari pamoja na yote haya mnayofanyiwa, bado sisi ambao tunaongea haya maneno mnatupiga virungu, Mungu anawaona ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza tangu mwaka 2012 mpaka leouniform hawajapewa. Nimekuta askari wanajinunulia wenyewe uniform.Wananiambia Mbunge hii uniform nimenunua mwenyewe kwa fedha zangu na hivi unavyoona hivi haifanani na nguo za askari wengine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo fair, package allowance mnawapa askari wengine, wanajeshi wengine mnawapa package allowance leoMagereza wale mpaka leo hamjawapa, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru lakini askari polisi msitumike vibaya na hawa jamaa, Mungu anawaona.

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nataka nizungumzie ushuru wa mazao ambao Mheshimiwa Waziri ametoa kwa mazao ya kilimo. Alisema kwa hawa wakulima ambao wanasafirisha mizigo yao kwa maana ya mazao kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine, kama ni mzigo usiozidi tani moja wasitoe ushuru.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana mimi nina Halmashauri mbili, ya Ifakara na Kilombero. Wananchi wangu hasa wa Ifakara wengi wanalima Halmashauri ya Kilombero wanakuja Ifakara hapa katikati huwa kuna barrier ambapo huwa wanawekwa pale Askari Polisi wenye bunduki kwa ajili ya ushuru. Kama Halmashauri ya Kilombero tulisema mkulima kutoka Ifakara anayelima Kilombero, akirudi na magunia yasiyozidi 20 anapita bure.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa hili agizo kwamba tani moja ndiyo ipite, tani moja ni wastani wa magunia 10 maana yake ni kwamba tayari tumesha-confuse utaratibu wetu kule Ifakara. Maana yake tunawaambia wananchi wa Ifakara kama tulikuwa tunasema wapite na magunia 20 sasa wapite na magunia 10 tu kwa mujibu wa sheria hii, tayari ni confusion. Maana yake ni kwamba hapa sasa hatusadii.

Mheshimiwa Spika, mimi nasema tani na ningependa unisikilize mpaka mwisho kwa sababu katika hicho kizuizi wanapokaa askari hapo, mkulima hata kama ana gunia tano za mpunga, hawezi kuchukua fuso au usafiri mkubwa kwa ajili ya kubeba hizi gunia tano, maana yake lazima wakulima watachanga, watakodi usafiri mkubwa waweke kwenye hilo gari waweze kuja Ifakara. Haiwezekani mkulima atoke na mzigo Idoko akiwa na gunia 10 atembee nazo mpaka Ifakara, hawezi kukodi maana yake lazima wachange wawe wengi. Wakifika pale wanaambiwa huu mzigo ni wa mtu mmoja wakati wale ni wakulima wengi wamechanga gari.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hili Mheshimiwa Waziri aliangalie, aende kule Ifakara aweke sawa, haiwezekani mkulima mmoja akodi gari wakati ana magunia matano au sita maana yake lazima wakulima wengi wachange kwenye hili gari moja ili wawe na mzigo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niseme nina shida ya barabara pale, barabara yangu ya kutoka Kidatu mpaka Ifakara ni mbovu kwa miaka mingi. Sasa Mheshimiwa Waziri nimeambiwa imetengwa shilingi milioni 300 kwa ajili ya fidia, maana barabara hiyo sasa hivi ndiyo inataka kujengwa, hivi kutoka Kidatu mpaka Ifakara pale kuna nyumba ngapi, ni nyingi sana. Hii fidia ya shilingi milioni 300 ni takribani nyumba mbili tu hizi, hawa wengine fidia yao iko wapi? Kwa hiyo, naiomba Serikali kama ina ya dhati ya kujenga barabara hii, fidia iongezwe siyo hii hela ndogo ambayo imewekwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo lingine, hotuba ya Mheshimiwa Msigwa, hii hotuba ya akili ndogo nafikiri itaishi milele. Kwa sababu mambo yanayotokea leo katika nchi hii yameshasemwa miaka mingi sana na hata Msigwa alisema akili ndogo haiwezi kuongoza akili kubwa. Leo ambacho kinatokea hapa ni kwamba akili ndogo ile ambayo ilikuwa inapiga makofi wakati sheria mbovu zinatungwa hapa Bungeni, ile akili ndogo wakati akina Zitto wanasema hawa Mawaziri wanakwenda kusaini mikataba nje, Waziri anapewa ndege aende nje akaingie mkataba mlikuwa mnapiga kelele nyie mnasema kwamba huyu Zitto mwongo, hafai na ametumwa, Zitto akafukuzwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati haya yanatokea huyu Rais wetu alikuwa pale amekaa. Wakati Mnyika anaongea haya maneno kwamba nchi hii inaibiwa, nchi hii inafilisiwa, mlikuwa mnapiga makofi nyie, akili ndogo hiyo inapiga makofi. Akili kubwa akina Msigwa, Zitto na Mnyika wakati wanasema haya maneno walionekana wabaya.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu unakuja hivi, kwa kuwa tumeshasema na kama Taifa tumeona kwamba Acacia ni wezi na kwa kuwa na Rais amesema hawa watu wanatakiwa wafanyiwe kazi, kwanza lazima kinga ya Rais itolewe, tufanye amendment hapa, Marais wa nchi hii wasiwe na kinga ya kutokushtakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu hainiingii akilini wakati leo unamwambia Karamagi, unamwambia mzee wangu Chenge kwamba wahojiwe Marais waliopita wanaachwa. Haiwezekani Chenge alifanya makosa Rais asijue, haiwezekani Cabinet ilikuwa haijui. Tufanye amendment ya sheria Marais wote na hii vita siyo iwe ni one man army, isiwe vita ya jeshi la mtu mmoja ndiyo lipigane iwe vita ya Taifa zima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ni kuomba radhi, CCM lazima muombe radhi kwa hasara ambayo mmeleta kwenye Taifa hili. Leo hapa mnajifanya mnapiga makofi, mnashangilia wakati nyie mmeua watu, watu wamekosa madawa kwa sababu ya uamuzi wenu wa hovyo. Kwa hiyo, huo ndiyo ushauri wangu, amendment ije, Rais aombe radhi, Bunge liombe radhi na CCM muombe radhi kwa maamuzi mliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Wanu Hafidh Ameir

House of Representatives (CCM)

Contributions (1)

Profile

View All MP's