Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, na nimshukuru Mwenyenzi mungu ambaye ameniwezesha afya njema na kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu bila kuwasahau wananchi wa Mtwara Vijijini ambao wameniwezesha kurudi kwa mara ya tatu katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa katika Bunge hili ambayo kwa kweli imegusa katika kila suala. Mimi kwa kifupi kama ambavyo umeshauri, ningependa nizungumzie maeneo machache.
Eneo la kwanza ningependa kuzungumzia suala la viwanda, ambalo Mheshimiwa Rais amesisitiza wakati wote kwamba Serikali yake itakuwa ni Serikali ya viwanda. Naunga mkona sana suala hilo, na napendekeza suala la wapi viwanda vijengwe, tuangalie vigezo vya kiuchumi zaidi. Mwenyenzi Mungu ameiumba nchi yetu kila eneo lipo zao au ipo rasilimali au malighafi ambazo amewajalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na Mkoa wangu ambao Mwenyenzi Mungu ameujalia gesi nyingi, ameujalia zao la korosho, bila kusahau bandari ambayo ni ya asili yenye kina kirefu. Kwa hiyo, naunga mkono Wizara ya Fedha na Uchumi ambayo kupitia Mpango wa Taifa wa miaka miwili, mapendekezo waliyoyatoa miaka mitano ijayo ambayo wamependekeza kuendeleza maeneo ya viwanda eneo la Mtwara likiwa ni mojawapo. Ningependekeza na ningeishauri Serikali kwamba suala la uendelezaji wa viwanda liende sambamba na uendelezaji wa miundombinu ambayo itawezesha viwanda vile kufanya kazi kwa ufanisi, ikiwemo reli ya kutoka Mtwara hadi Songea kwenda Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ile itawezesha sana kubeba malighafi kutoka Liganga na Mchuchuma kuja Mtwara na vilevile kusafirisha bidhaa ambazo zitazalishwa katika viwanda ambavyo vitakuwepo kule Mtwara. Mtwara imejaliwa gesi na sasa hivi bomba la gesi limejengwa hadi Dar es salaam, lakini bei ya gesi ni sawa Mtwara na Dar es Salaam. Wakati ukiangalia bei ya mafuta ni tofauti, Dar es Salaam tofauti na Mtwara, tofauti na Kigoma na tofauti na eneo lingine. Kwa kuweka bei ya gesi sawa Mtwara na Dar es Salaam au Mikoa mingine ndiyo kusema unataka kuua uwekezaji wa Mkoa wa Mtwara. Kwa sababu hakutakuwa na motisha yeyote mtu kwenda kuweka kiwanda Mtwara wakati bei ya gesi popote anapohitaji ataipata kwa bei ile ile. Kwa hiyo, nimuombe Waziri wa Nishati aliangalie suala hilo la bei ya gesi.
Mheshimiwa Naibu Waziri, suala lingine ambalo nataka pia nilizungumzie ni suala zima la uendelezaji wa bandari ya Mtwara na uwanja wa ndege wa Mtwara. Uchimbaji mkubwa wa gesi unafanyika baharini na wafanyakazi wanapelekwa kule kwa helkopta na kurudishwa kwa helkopta na wakati mwingine kama ilivyo katika eneo lolote la kazi wakati mwingine zinatokea ajali kule. Sasa ikitokea usiku ni suala gumu sana kuwaleta wale majeruhi huku nchi kavu kwa sababu uwanja wa ndege wa Mtwara hauna taa. Ukiachia taa ule uwanja ulijengwa mwaka1965, hata mzungumzaji nikiwa sijazaliwa, lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza hakuna ukarabati wa maana uliyofanyika katika uwanja ule, kwa hiyo, niombe Serikali iufanyie ukarabati uwanja ule uendane na uwekezaji ambao uko kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala zima la viwanda vya korosho na suala zima la ukamilishaji wa hospitali ya Rufaa katika Mkoa ule. Pia suala la maji, viwanda vyote vinahitaji maji, wananchi wanahitaji maji, lakini shughuli za binadamu nyingi zinahitaji maji. Ningependa kurudia tena kwamba suala la uwekezaji wa viwanda uende sambamba na uwekezaji wa miundombinu ambayo inabeba au inawezesha viwanda vile kufanya kazi ikiwemo umeme, barabara, reli, bandari, hospitali kwa sababu wafanyakazi pia wanahitaji kuwa na afya ili waweze kutumika vyema.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha afya njema na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili na niweze kuichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kwa pamoja na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Olenasha kwa kazi nzuri waliyonayo katika kuiongoza Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi zangu, napenda nichangie katika maeneo yafuatayo:-
Eneo la kwanza ni eneo la kilimo, hususan zao la korosho. Ulianzishwa mfuko wa kuendeleza zao la korosho na madhumuni ya mfuko ule, pamoja na mambo mengine lakini pia kujenga viwanda vya korosho. Mfuko ulianza kwa kutuahidi kwamba tutaanza kujenga viwanda vitatu vya korosho, maeneo yakachaguliwa, lakini mpaka sasa hivi, imebaki ni hadithi, hatujui huo mfuko unapata shilingi ngapi na zinatumika vipi?
Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri, huu mfuko ni lazima kwanza ukaguliwe na pia tuangalie, kwa sababu mara ya mwisho tumeoneshwa asilimia 41 tu ndiyo inayoenda katika kuendeleza zao la korosho. Kinachobaki kwa kweli hakieleweki, sana sana kinaenda kwenye utawala. Kwa hiyo, naomba uangalie sana katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kupunguza makato katika zao la korosho. Nimtahadharishe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kuna watu wamejipanga huko kuja kumwomba arejeshe baadhi ya makato.
Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba uendelee kuwa na msimamo wako huo huo, usibabaishwe wala usitetereshwe na baadhi ya watu wanaotaka kukuyumbisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni suala la uendeshaji wa minada, katika suala zima la Stakabadhi ya Mazao Ghalani. Huu mfumo ni mzuri sana na wananchi wanaupenda sana, tatizo uwazi hauko vizuri. Tumeelezwa katika kikao cha RCC kwamba korosho mwaka huu imenunuliwa mpaka shilingi 2,950 lakini kitu cha kushangaza, anakuja Afisa Ushirika anasimama anasema kwamba wanasiasa ndio wanaosumbua katika zao hili la korosho. Anasema kwamba sisi katika Wilaya yetu, koroshozimeuzwa kwa shilingi 2,060 tu. Sasa zile bei zinazotajwa kwenye RCC na ambazo wanatajiwa wananchi, kidogo kuna utata. Wakitafuta sifa, wanatutajia bei ya juu; wanapotaka kwenda kuwapa wananchi, wanashusha ile bei. Sasa tuelewe vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa ufafanuzi, atuambie mwaka huu Korosho zimeuzwa kwa shilingi 2,950 au zimeuzwa kwa shilingi 2,060? Tupate ufafanuzi wa hilo ili wananchi wetu waweze kupata haki. Sasa hivi tunavyozungumza, Tandahimba vyama 149 wanadai zaidi ya shilingi bilioni 1.4 na hayo ni maelezo ya Mkuu wa Wilaya na Masasi pia wakulima wanadai pesa zao za korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba wananchi wapate malipo yao. Wananchi wote wanaohudumiwa na MAMCU na TANEKU ambao wanadai malipo yao ya pili, walipwe ya mwaka huu na miaka mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilitaka kulichangia ni suala la wavuvi. Ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri utakuta kuna pembejeo za wakulima na pia kuna pembejeo na jinsi ya kuendeleza wafugaji. Ukija kwa upande wa wavuvi, sana sana kuna mikakati ya kuzuia uvuvi haramu; hatukatai, lakini tungependekeza suala hilo liende sambamba na kuwawezesha wafugaji kwa vifaa; vitendea kazi. Wavuvi wetu wengi wanavua kwa kutumia zile zana za zamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka wakati Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, akiwa Waziri wa Uvuvi, kwa kweli alikuwa na mipango mizuri sana ya kuwawezesha wavuvi. Na mimi katika Wilaya yangu alikuja katika maeneo ya Msangamkuu, wakawawezesha wavuvi katika Kijiji kimoja tu, alitoa zaidi ya shilingi milioni 250. Sasa baada ya yeye kuhamishwa Wizara ile, mipango ile yote iliishia pale pale. Naomba Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba uangalie mipango ile, pamoja na kwamba ilikuwa inapitia MACEMP lakini ilisimamiwa na Waziri Mheshimiwa Dkt. Magufuli kipindi kile akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Tunaomba wavuvi wawekewe mipango thabiti ya kuwaendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba niongelee suala la wafugaji. Wafugaji wanahangaika kwa sababu wanatafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao. Tunaomba katika bajeti yako ioneshe mnajenga majosho mangapi na mnawatengea maeneo gani waende lakini pia wapatiwe maji, kwa sababu kitu kikubwa kinachowafanya wanahangaika wanaende kugombana na wakulima ni kutafuta maji na malisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba maeneo yatengwe ya wakulima yajulikane na ya wafugaji yajulikane, lakini ya wafugaji, tunaomba mwongeze kuwawekea majosho pamoja na maeneo ya kunyweshea mifugo yao, hapo ndipo mtakapoweza kuwafanya wafugaji wasihame eneo moja hadi lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii naomba wasiachiwe Halmashauri peke yao, Halmashauri wana majukumu mengi sana ya kutekeleza katika ngazi zao zile. Tuiombe Wizara mama ndiyo itoe mchango wa kuziwezesha Halmashauri kule chini ili ziweze kujenga majosho. Tukiwaachia Halmashauri peke yao kwamba watenge maeneo wao, wao wajenge majosho, kwa kweli tutakuwa tunawaonea.
Wizara itenge pesa kwa kushirikia na hizo Halmashauri ili kujenga majosho pia na kujenga maeneo ya kunyweshea hiyo mifugo. Napenda nimalizie kwa kuwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo wa Mtwara Vijijini kwa kuniamini kwa kipindi cha tatu, kuwa Mbunge wao. Napenda niwahakikishie kwamba sitawaangusha, nitafanya kazi na wao bega kwa bega, kwa maendeleo ya Jimbo letu la Mtwara Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasisitiza tena suala la wavuvi kuwezeshwa, si suala tu la kwenda kuwakamata kuchoma nyavu zao na uvuvi haramu. Hakuna mtu anayependa kuvua kwa kutumia baruti, vijana wetu wanakufa; lakini wanafanya vile kwa sababu hawana mitaji, hawana zana za kuwawezesha kupata nyavu za kisasa, boti za kisasa na kupata injini za kuwawezesha kwenda kuvua katika kina kirefu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze, wavuvi ametutengea kiasi gani na za kufanyia nini? Maana yake siku zote tunasikia doria.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wavuvi na wenyewe wanatozwa tozo nyingi sana kwenye leseni; akitoka Mtwara anatozwa, akienda Kilwa anatozwa, akienda Msumbiji anatozwa. Tunaomba akilipia leseni, basi iwe ni hiyo hiyo, lakini kuna tozo nyingi sana; kila anachokwenda kukivua kule baharini kinatozwa. Kwa hiyo, nasema kabisa na lenyewe tuliangalie.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa wakulima wetu hasa wa zao la Korosho, tumesikia sasa hivi kuna suala commodity exchange, lakini sisi kama Wabunge hatujapata hata maelekezo, huo mfumo unaendaje ili tukawe wapambe wa kukusaidia mfumo huo kufanya kazi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na uzima na kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili nami niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nimshukuru na kumpongeza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kutuletea mwekezaji ambaye ana nia ya kujenga Kiwanda cha Sulphur kule Mtwara, namshukuru kwa hilo. Nampongeza kwa hotuba nzuri ambayo siyo tu imeandikwa vizuri, lakini pia amewasilishwa vizuri sana na kila mtu atakubaliana na hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema Serikali ya Awamu ya Tano ni ya viwanda na tunaunga mkono sana hilo. Ushauri wangu kwa Serikali yangu ni kuhakikisha tunatoa vikwazo vyote vile ambavyo wawekezaji wanakumbana navyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wangu wa Mtwara, naomba nianzie huko. Tunaye mwekezaji ambaye ameonesha nia ya kutaka kujenga Kiwanda cha Mbolea na tayari wenzetu wa EPZA wamemuonesha eneo la kujenga kiwanda tangu mwaka 2015 Aprili, lakini mpaka tunapozungumza sasa hivi, anashindwa kuanza kujenga kiwanda kwa sababu Wizara ya Nishati na Madini wameshindwa kumhakikishia upatikanaji wa gesi kwa zaidi ya miaka minne ijayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi wakati watu wa EPZA wanakuja kumuonesha eneo, walikuwa hawajazungumza na Wizara ya Nishati na Madini? Mwekezaji anaomba uhakika, kiwanda kile kitachukua zaidi ya miaka minne kukamilika, anaomba ahakikishiwe baada ya miaka minne kupewa gesi, mpaka leo Wizara ya Nishati na Madini haijampa uhakika kama watampa hiyo gesi. Kwa kweli kama Mwanamtwara, nasikitika sana, kwa sababu kiwanda hiki ni cha mfano. Mwekezaji alikuwa anafanya ubia na Halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara na tayari tulishakubali, eneo wamepewa, lakini gesi hajapewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja, atueleze amefanya juhudi gani za kumsaidia mwekezaji huyo kupata gesi ili Kiwanda cha Mbolea ambapo nchi inaagiza mbolea kwa zaidi ya asilimia 90, lakini anakuja mwekezaji anataka kujenga hapa, tunamwekea vikwazo. Hivi tuelewe kuna lengo gani ambalo sisi wengine hatulifahamu? Haiwezekani gesi itoke Mtwara lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza hakuna kiwanda hata kimoja kimepewa gesi katika mkoa ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo nataka kulichangia, ni suala la maeneo ya EPZA. Kama kweli tunahitaji kuwa na Serikali ya Viwanda, ushauri wangu ni kuiomba Serikali itafute fedha, ilipe fidia maeneo yote ambayo wanakusudia kuwa ni maeneo ya uwekezaji kwa maana EPZA na SES ili wawekezaji wanapokuja wasipate usumbufu wa aina yoyote wa kutafuta maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waziri atakapokuja atuambie, ana mikakati gani ya kuhakikisha kwamba maeneo ya EPZA yote yanalipiwa fidia kwa wakati ili yawe tayari, yasafishwe, yawekewe uzio tayari akija mwekezaji unamwonesha kwamba eneo la kuwekeza ni hili hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulianzisha ushuru wa korosho ambayo inasafirishwa ghafi kwenda nje, yaani export levy ili kuhakikisha kwamba, badala ya wafanyabiashara kupeleka korosho nje, wazibangue hapa. Lengo la ushuru ule ilikuwa ni kuwakatisha tamaa wale wanaopeleka korosho bila kuzibangua ili wawekeze viwanda katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze tangu tumeanzisha export levy mpaka sasa hivi ni viwanda vingapi vimeweza kujengwa. Kama hakuna kiwanda chochote, ameshauri nini, kwamba kodi ile iongezwe kwa kiasi gani? Wasiwasi wangu ni kwamba, labda ile export levy ni ndogo kiasi kwamba hakuna sababu, mtu anaweza akalipa na bado akapeleka nje kuliko akizalisha korosho ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulichangia ni suala la kulinda viwanda vyetu. Kama tumeamua kweli kuwa nchi ya viwanda, ni lazima suala hilo liende sambamba na ulindaji wa viwanda vyetu vya ndani. Tanzania tuna uwezo wa kujilisha au kujitosheleza sisi wenyewe kwa mafuta ya kula, tuna uwezo wa kuzalisha alizeti. Tunayo Mikoa kama Singida, Tabora, Dodoma na kanda nzima ya kusini huku, tuna uwezo wa kuzalisha alizeti na kuweza kuzalisha mafuta ya kujitosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yatategemea iwapo tutakuwa tumeweka sheria ya kulinda viwanda vyetu. Kuna mafuta mengi sana ya kula yanatoka nje, wakisingizia kwamba mafuta hayo hayajakamilika, yaani yanakuja kusafishwa huku kwetu, lakini kimsingi yakifika hapa wanakuja tu kuya-park na kuanza kuyauza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, watuambie wana mikakati gani ya kulinda viwanda vyetu vya mafuta ya kula hapa nchini? Wenzetu Uganda wanafanya, Rwanda wanafanya, kwa nini sisi tuwe ni eneo ambalo mtu yeyote anayetaka kuleta mafuta ya aina yoyote ambayo hatuna hata uhakika wa usalama wa afya zetu, tunaruhusu watu kufanya hivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumsikia Mheshimiwa Waziri anatuambia katika upande wa viwanda vya mbolea na korosho kule Mtwara anatuletea viwanda vingapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, namwomba tu Mheshimiwa Waziri ajiandae kuja kuniambia kiwanda kile cha mbolea ana mikakati gani au anamwezeshaje yule ili aanze kujenga kile kiwanda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake ikiwemo uzima na afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba ambayo pia ameisoma kwa umahiri mkubwa sana. Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya Viwanda, napenda kuishauri Serikali kama tunataka kufikia lengo hili kwa ufanisi ifuatavyo:
Maeneo yote ya EPZA na SEZ ambayo hayajalipiwa fidia yakiwemo ya Kurasini, Bagamoyo na Mtwara wahakikishe kuwa fidia hiyo inalipwa kwa wakati na kusafishwa ili wawekezaji wasipate usumbufu juu ya upatikanaji wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu wezeshi, umeme wa uhakika, barabara na reli ni muhimu sana ili kuhakikisha tunazalisha bidhaa ambazo zitaweza kushindana na bidhaa nyingine kutoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kupata majibu kutoka kwa Waziri kuhusu suala la kiwanda cha Mbolea Msangamkuu Mtwara, ningependa kufahamu ni lini kiwanda hicho kitapatiwa uhakika wa kupewa gesi ili kiwanda hicho kianze kujengwa ninafikiri kushika shilingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kweli kuwa nchi ya Viwanda, Serikali yangu ni lazima tuweke sheria za maksudi kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu. Nchi yetu ina uwezo wa kuzalisha alizeti na mafuta ya alizeti na kulisha Afrika Mashariki, lakini tunashindwa kwa sababu ya mafuta ya kutoka nje ambayo hatuna hata uhakika wa usalama wa afya zetu. Naomba Serikali iondoe usumbufu kwa wawekezaji, tuangalie sheria zetu za kodi, utaratibu wa kupata ardhi kwa wawekezaji na kuthubutu kutoa maamuzi kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, viwanda vya korosho ni muhimu sana kwa maendeleo ya wakulima wa korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kabla ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya na uzima wa kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuweza kuichangia hotuba ya Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kumpongeza sana Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Ndani ya muda mfupi wameweza kutembelea mikoa mbalimbali na kuweza kutoa maelekezo mbalimbali, hali ambayo pia inawatia moyo hata watendaji wanaofanya kazi katika Sekta hii ya Afya. Hongereni sana na mwendelee kuchapa kazi hivyo hivyo na msimwangushe Mheshimiwa Rais. Nyie ni vijana na tunawategemea, mna nguvu pia mnao uwezo mkubwa sana, endeleeni kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika maeneo makuu matatu. Kwanza, namwomba Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, maeneo makuu matatu ambayo ni changamoto sana katika Sekta ya Afya; kwanza ni upatikanaji wa madawa na vifaa tiba; pili, ni suala la miundombinu ya kutolea huduma; na tatu, ni uchache wa watumishi katika Sekta ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upatikanaji wa madawa na vifaa tiba ni imani yangu kwamba Wizara ikidhamiria, ikiweka fedha za kutosha, ni suala ambalo linaweza likatatuliwa hata ndani ya miezi sita. Ni suala la dhamira tu, Serikali ikiamua inaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija katika suala la miundombinu, sasa hivi pamoja na juhudi zote zinazofanyika, lakini katika baadhi ya maeneo, miundombinu iliyopo kwa kweli imechoka na pia imeelemewa kutokana na idadi ya watu inayoongezeka kila siku, mfano mzuri ni Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa wanaoiamini hospitali ile kuliko hospitali nyingine zote katika nchi yetu. Ukienda pale, idadi ya wagonjwa ukilinganisha na idadi ya wodi pamoja na vitanda kwa kweli inatia huruma. Unawahurumia hata Wauguzi na Madaktari. Wagonjwa wanalala chini kwa sababu wodi ni chache, hata ukiongeza vitanda hakuna eneo ambalo unaweza ukaweka. Ifike wakati sasa suala la ujenzi wa hospitali ya Mlonganzila kwa kweli lipewe kipaumbele kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tunazo hospitali zetu za Kanda zipewe uwezo kwa maana ya Watendaji na vifaa ili ziweze kusaidia Muhimbili kupunguza mlundikano. Kwa upande wa kusini, Mikoa ya Mtwara na Lindi, tunayo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini ambayo inajengwa pale Mikindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika Bajeti yako Mheshimiwa Waziri, sijaona eneo lolote. Nimeangalia kwenye bajeti ya maendeleo, nimeona Hospitali ya Rufaa Mtwara shilingi bilioni mbili. Sasa sijui zile shilingi bilioni zinakwenda Ligula au zinakwenda Mikindani! Kwa sababu kama ni Mikindani, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, shilingi bilioni mbili kwa kweli hazitoshi, kwa sababu mpaka sasa hivi kilichojengwa pale ni majengo ya wagonjwa wa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kweli tuisaidie Muhimbili ni lazima tuhakikishe zile Hospitali za Rufaa za Kanda zinajengwa na zinawezeshwa. Sasa hivi mgonjwa yeyote pale Ligula akishindikana, inabidi asafirishwe kwenda Muhimbili. Wakati mwingine Mheshimiwa unalazimika kama Mbunge kununua viti sita kwenye ndege ili mgonjwa mmoja tu aweze kusafirishwa. Afadhali ikiwa ATC, shilingi milioni unaweza ukasafirisha mgonjwa, lakini ukija kwenye Precision, mpaka shilingi milioni 15 kusafirisha mgonjwa mmoja. Kwa kweli kwa wale ambao hawana uwezo hawawezi; na wakati mwingine hata Mbunge huwezi kutoa shilingi milioni 15 kusafirisha mgonjwa mmoja. Tunaomba hospitali ile ijengwe na iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwa upande wa watumishi, tuna vituo vya kutolea huduma zaidi ya 7,249 ukichanganya na sekta binafsi, lakini na mahitaji ya watumishi kwa upande wa Wauguzi ni zaidi ya 46,000 na waliopo ni kama 24,000. Tuna upungufu wa zaidi ya asilimia 49 ya watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika udahili wa watumishi wetu; nilikuwa naangalia, unakuta Madaktari kwa mwaka wanadahiliwa 1,670 wakati tuna upungufu wa Madaktari zaidi ya 4,000. Kwa upande wa Wauguzi, tuna upungufu wa Wauguzi zaidi ya 22,000, lakini wanaodahiliwa kwa mwaka ni kama 3,499. Hivi kweli tunaweza tukaondoa tatizo hili? Tulikuwa na tatizo la Wahasibu na tatizo la Walimu, Wizara mama zilikuwa zinatenga kiasi cha kutosha ili kuweza kuondoa matatizo haya. Sasa hivi tatizo la Walimu na Wahasibu ni kama limekwisha lakini kwa upande wa Sekta ya Afya, nawaomba wadogo zangu, Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla ni lazima tuje na mpango mahsusi, tupanue vyuo vyetu vya Wauguzi, Madaktari na kada zote za Sekta ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni lazima tuwalipie. Serikali itenge pesa kama ambavyo Wizara ya Fedha ilikuwa inatenga pesa kwa ajili ya Wahasibu; kama ambavyo Wizara ya Elimu na Wizara ya Kilimo zilikuwa zinatenga pesa kwa ajili ya kusomesha watumishi wao. Ni lazima Wizara ya Afya tufanye kama operation. Tunasema anayekwenda kuchukua degree ya Uuguzi atachukua mkopo, lakini wanaokwenda kuchukua Cheti, Diploma tunasema ajitegemee mwenyewe. Karo yenyewe ni zaidi ya shilingi milioni moja. Chakula kinazidi hata hiyo shilingi milioni moja. Kwa kweli kama tunataka kuondokana na upungufu huo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, ni lazima tuwe na mpango mahsusi na tuwekee kipaumbele, tutenge pesa za kutosha kuhakikisha tunadahili vijana wa kutosha hasa wale ambao tunawahitaji kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani kwa sisi tunaoishi vijijini, unakuta zahanati moja ina mtumishi mmoja, kule Muuguzi anafanya kazi masaa 24, hana Jumamosi, hana Jumapili; kukiwa na mgonjwa saa 5.00 za usiku anakwenda kuamshwa na sidhani kama kuna chochote wanachokipata. Ndiyo maana unakuta Wauguzi wetu wakati mwingine wanakuwa na lugha zisizostahili. Siyo kwamba wanapenda, ni uchovu wa kazi. Mzigo ni mkubwa wanaoufanya. Kwa hiyo, mtu mmoja halali, usiku kucha anaitwa kazini, asubuhi yuko kazini, Jumamosi yuko kazini, hivi unategemea awe na lugha nzuri? Wakati mwingine ni stress tu kutokana na uzito wa kazi ndiyo unaowafikisha wanakuwa na lugha wengine zisizostahili.
Kwa hiyo, kwa kweli lazima tuongeze udahili, hizi tunazosema kila kijiji kiwe na zahanati, kila kata iwe na kituo cha afya; bila kwenda sambamba na udahili, hizo zahanati na vituo vya afya zitakuwa ni nyumba tu za popo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nichangie, nirudi katika Mkoa wangu. Tunacho Kituo cha Afya cha Nanguruwe ambacho tulikiombea kuwa Hospitali ya Wilaya. Tumekamilisha karibu mahitaji yote yanayotakiwa. Tunayo majengo ya upasuaji, tunavyo vitanda vya kutosha, wodi za kutosha pamoja na Kituo cha Afya cha Nanyumbu; lakini mpaka sasa hivi bado tunasubiri kibali kutoka Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ummy alikwenda kutembelea Kituo cha Afya cha Nanguruwe, nina imani kabisa kwamba yeye mwenyewe amejiridhisha kwamba vipo vifaa vya kutosha na majengo ya kutosha. Tunaomba watoe kibali ili ianze kufanya kazi kama Hospitali ya Wilaya, tupunguzie mzigo hospitali ya Mkoa ya Ligula. Hii ikienda sambamba na hospitali au Kituo cha Afya cha Nanyumbu ambacho nacho kwa muda mrefu kimeshafikia mahitaji ambayo yanatakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mtwara Vijijini tunavyo vituo vya afya vya Mahurunga na Kitere. Tumeshajenga vyumba vya upasuaji; vifaa vyote vipo kwa zaidi ya miaka miwili, lakini hakuna huduma inayotolewa pale, tatizo ni lile lile la uchache wa Madaktari. Nakuomba Mheshimiwa Waziri utuletee Madaktari wa kutosha ili vituo vile vianze kutoa huduma ya upasuaji na tuweze kupunguza vifo vya akinamama na watoto hasa wakati wa kujifungua. Pia Mheshimiwa Waziri, wakati unaoandaa hao Madaktari, tunao Madaktari pale Hospitali ya Mkoa ya Ligula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo katika Wilaya yetu na hata kwa mkoa wetu suala la Mabusha. Kwa vile katika vituo vile huduma zote zipo, vifaa vyote vipo, kwa nini hao Madaktari wasiwe wanapanga siku angalau kwa wiki au kwa mwezi wanakwenda katika Vituo vya Afya vile ambavyo vina huduma za upasuaji, wakawa wanatoa huduma ile kwa wale ambao wanahitaji kufanyiwa operation za mabusha? Kwa sababu sasa hivi wanalazimika kuja katika Hospitali ya Mkoa, tunawagharamia, anafika pale anakaa zaidi ya wiki mbili anasubiri zamu. Mara leo sijui tunafanyia wawili, kesho tunawafanyia watatu; kwa nini wale Madaktari walioko katika mkoa wasiwe wanazunguka na wanakwenda katika maeneo hayo kutoa huduma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napendekeza kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake ni suala la uzazi wa mpango. Nimeangalia katika kitabu cha hotuba haraka haraka, sikuona eneo lolote lililozungumzia suala la uzazi wa mpango. Suala la idadi ya watu na uchumi wa nchi yetu ni muhimu sana. Maeneo mengine kama Wabunge tukienda kule wanatuambia bwana hizi huduma hatuzipati na wanazihitaji. Unakuta kule akinamama wengine tayari ana watoto 10 na uzazi wake ni wa matatizo, ni lazima ajifungulie katika hospitali ya Mkoa. Kwanini wasishauriwe uzazi wa mpango sahihi kwa ajili ya kuwawezesha na wenyewe kuboresha afya zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanapoteza maisha kwasababu tu kila baada ya mwaka mmoja ana mtoto au unakuta mtu tayari ameshajifungua kwa zaidi ya mara nane hali ambayo ni kihatarishi cha maisha yake kwa sababu kwa kweli baada ya kuzaa kwa zaidi ya mara nane, nadhani Mheshimiwa Kigwangalla, Naibu Waziri wa Afya ananielewa, ni kwamba kila kizazi kinachoongezeka pale ni hatari kwa maisha ya mama yule anayejifungua na hata mtoto anayejifungua. Ukiangalia vifo vingi vinavyotokana na uzazi ni aidha ni vya wale waliojifungua katika umri mdogo au kwenye umri uliopitiliza umri ule ambao kwa kweli mtu anaweza akajifungua salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusisitiza suala la Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini. Mheshimiwa Waziri akapokuja tungependa kusikia bajeti yake imetengwa wapi. Kama tunataka kupunguza vifo vya akinamama na watoto, tuangalie suala zima la magari ya wagonjwa. Siku za nyuma tulikuwa na magari ya wagonjwa, yana radio call ndani yake, kukiwa na tatizo wanaweza kuwasiliana kwa radio call na gari lolote lililoko karibu na eneo ambalo mgonjwa yupo linaweza likaenda kumchukua kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwa Mheshimiwa Waziri kwamba sasa hivi tuwe na magari ya wagonjwa ambayo pia ni surgical. Mgonjwa anapofuatwa, basi afuatwe na Daktari na akifika siyo kwenda kumchukua na kumkimbiza zaidi ya kilometa mia moja Makao Makuu ya Wilaya au ya Mkoa kwa ajili ya upasuaji. Gari ikifika, aweze kufanyiwa upasuaji kule kule inakomkuta badala ya kuanza kukimbizana naye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kujua hilo, kama tunao mpango wa kuwa na magari ya wagonjwa ambapo huduma za upasuaji zinaweza kupatikana humo humo ndani ya magari kama ambavyo nchi nyingine zinafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia afya na uzima na kuweza kupata nguvu ya kuweza kuwawakilisha wananchi wangu wa Jimbo Mtwara Vijijini na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla na Watanzania.
Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya kwa sababu Wizara hii ni zaidi ya Wizara tatu kama tulivyozoea kuziona, lakini nina imani kabisa kwamba ataweza kuzimudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kile kitendawili chetu cha wananchi wa mkoa wa Mtwara kuhusu barabara yetu ya uchumi angalau mwaka huu tunaziona kilometa 50 zikiwa zimetengewa pesa. Ametuhakikishia kwamba kilometa hizo 50 kutoka Mtwara mpaka Mnivata ujenzi utaanza katika mwaka wa fedha 2016/2017. Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isipokuwa ningependa tu kusisitiza, Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati anaomba kura alituahidi akishinda zile kilometa 159 zinazobaki kutoka Mtwara - Newala - Masasi watagaiwa wakandarasi kilometa zote ili ujenzi uweze kukamilika kwa wakati. Mheshimiwa Waziri nitapenda wakati unatoa ufafanuzi utuelezee utaratibu uliopo kwa zile kilometa ambazo zimebaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda pia nilizungumzie ni kuunganisha barabara zetu za mkoa na mkoa lakini pia kuunganisha nchi na nchi. Mheshimiwa Waziri tunazo barabra zetu zinazotuunganisha Mtwara na majirani zetu wa Msumbiji, kutoka Mtwara - Kilambo na kutoka Mtwara - Msimbati kimekuwa kilio cha muda mrefu, tumekuwa tukiomba zijengwe kwa kiwango cha lami kama ambavyo mipaka mingine yote inaungwanishwa. Kwa hiyo, nitataka kusikia ni lini mkoa wa Mtwara utaunganishwa na Msumbiji kupitia kivuko cha Kilambo na Msimbati kwa kujengwa kwa kiwango cha lami hasa ukizingatia kwamba Msimbati ndiko ambako gesi inatoka na tuna vitega uchumi vyetu vingi kule vya thamani ambavyo kwa kweli lazima tujenge barabara ya uhakika ambapo tutaweza tukaenda wakati wowote bila kujali mvua au jua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni bandari. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 tuliambiwa kwamba majadiliano na wawekezaji upande wa Mtwara yamekamilika kwa ajili ya kujenga gati nne katika bandari ya Mtwara, leo Mheshimiwa Waziri anatuambia kwamba majadiliano yale ambayo tuliambiwa yamekamilika hayakufanikiwa na badala yake inataka kujengwa gati moja yenye mita 350, hatukatai sawa lakini lengo lilikuwa ni gati nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utafiti wa gesi unaoendelea kule; zao letu la korosho na viwanda vingi ambavyo vinakwenda kule ikiwemo vya mbolea na hivyo vya kina Dangote kwa bandari iliyopo sasa hivi haitoshelezi na wakati mwingine inaleta usumbufu mkubwa sana hasa katika kusafirisha zao letu la korosho. Kwa hiyo, napenda Mheshimiwa Waziri atuambie gati zingine tatu zilizobaki mpango ukoje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunalo eneo la Kisiwa na Mgau ambapo eneo lingine tumempa Mheshimiwa Aliko Dangote ili ajenge bandari kwa ajili ya kusafirishia saruji na eneo lingine bandari yenyewe iliamua kuchukua kwa ajili ya kujenga bandari yake. Tathmini imeshafanyika, sasa hivi imebaki ni hadithi kesho, kesho kutwa. Amekuja Mheshimiwa Waziri Mkuu kule tuliambiwa baada ya siku tano fidia awamu ya pili italipwa. Lile eneo ambalo Dangote amepewa fidia ilishalipwa imekamilika, eneo ambalo bandari wamechukua kwa nini hamlipi? Dangote ameshalipa, wananchi wameshatumia pesa zao lakini wale ambao wanapaswa kulipwa na Mamlaka ya Bandari imebaki danadana. Sasa mnawagombanisha, kwa nini upande wa Dangote walipwe na upande wa bandari hamtaki kuwalipa?
Kwa hiyo, ningependa Mheshimiwa Waziri aje aseme ni lini watalipwa kwa sababu kila siku maelezo ni kwamba wanasubiri Bodi ya Bandari iundwe ili iweze kuridhia zile pesa kwa sababu pesa za kulipa fidia zipo shilingi bilioni 13, hiyo Bodi ya Bandari inaundwa lini ili mambo yaende? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulichangia ni kuhusu reli ya kutoka Mtwara - Songea - Mbamba Bay. Nimeona katika hotuba kwamba upembuzi yakinifu na usanifu umekamilika Februari 2016. Napenda kufahamu ujenzi wa reli hiyo ya kutoka Mtwara - Mbamba Bay na matawi yake ya kwenda Liganga na Mchuchuma utaanza lini? Kwa sababu uwekezaji unaofanyika kule Liganga na Mchuchuma, makaa ya mawe yaliyoko Ngaka bila kuwa na reli mradi ule Mheshimiwa Waziri itakuwa ni hadithi. Naomba Mheshimiwa Waziri aje atuambie ujenzi wa reli kutoka Mtwara - Mbamba Bay na matawi yake yanayokwenda Liganga na Mchuchuma utakamilika lini kwa Mtwara huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ukarabati wa uwanja wa ndege wa Mtwara. Iliwekwa katika bajeti lakini mpaka sasa hivi hakuna fedha iliyotoka hata kidogo. Pia tuliambiwa uwanja ule utawekewa taa, mpaka sasa hivi taa hakuna. Tunachofanya pale ni kuazima taa za muda za wenzetu wa BG, hivi siku BG wakitukakatalia tunafanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutonana na utafiti na uchimbaji wa gesi na mambo yanayoendelea kule Mtwara, kwa kweli ni lazima ule uwanja upate taa na ukarabatiwe. Uwanja ule ulijengwa mwaka 1965, hata mimi sijazaliwa na nimeshafikia mahali ambapo kama ni umri naweza nikasema zaidi ya nusu labda au nusu nimeshamaliza uwanja ule haujakarabatiwa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri anapokuja aje atuambie uwanja unakarabatiwa lini na unawekewa taa lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, tunayo makampuni ya mitandao ya simu na kila mara wamekuwa wakidai kwamba wanalipa kodi ya huduma (service levy) katika Halmashauri, lakini Halmashauri zetu nyingi hazipati ushuru huu na badala yake unalipwa katika Halmashauri chache. Niiombe Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia taasisi zake ikusanye ushuru huu makao makuu na ugawanywe katika Halmashauri zote bila kujali ukubwa wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi napenda niungane na wenzangu kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuichangia hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017 pamoja na Makadirio na Mapato ya Matumizi kwa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwa kumpongeza, kwa kuona umuhimu wa barabara yetu ambayo sisi wenyewe tunaiita ni barabara ya uchumi ya kutoka Mtwara kwenda Newala hadi Masasi, Mbinga hadi Mbamba Bay kuwa miongoni mwa miradi ya kipaumbele katika mwaka huu wa fedha. Mheshimiwa Waziri kwa hilo nakushukuru sana kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Mtwara hasa barabara kutoka Mtwara - Nanyamba - Tandahimba, Newala - Masasi imekuwa ni kilio cha muda mrefu, hii ni barabara yetu ya uchumi inasafirisha korosho zaidi ya asilimia 80. Kila mwaka barabara hii inatengenezwa lakini ukiisha msimu wa korosho inaacha mahandaki. Kwa hiyo ikijengwa kwa kiwango cha lami kwa kiasi kikubwa itaboresha mazingira ya ufanyaji biashara ndani ya Mkoa wetu wa Mtwara, kwa hiyo nakushukuru sana kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo nilitaka nilizungumzie ni suala la kupunguza ushuru wa korosho kwa wananchi. Napenda nilipongeze sana suala hilo kwa sababu siku nyingi tumekuwa tukilalamika wakulima wa zao la korosho wamekuwa wakikatwa makato mengi sana ambayo mengi hakuna hata moja linalowanufaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kato la shilingi 10,000 kwa kila kilo eti kwa ajili ya kikosi kazi kufuatilia ununuzi wa korosho. Kikosi kazi hicho ni watumishi wa Serikali, viongozi wa Serikali ambao wamepewa majukumu ya kufanya kazi hizo. Kazi walizopangiwa ni pamoja na kusimamia ununuzi wa zao la korosho, lakini walianza na shilingi moja, ikaenda shilingi tano, ghafla ikaruka shilingi 10 kila kilo ya korosho wao wanataka walipwe kama viongozi kwa ajili tu ya kusimamia ununuzi wa zao la korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu tulizonazo sasa hivi kwa mwaka tunazalisha zaidi ya tani 45,000, mwaka 2014 tulizalisha kwa mujibu wa korosho zilizosafirishwa nje ya nchi, tani 189,000. Mtwara peke yake inazalisha zaidi ya asilimia 80. Uchukue tu tani 100,000 zimetoka Mtwara na katika kila hizo tani 100,000 kila kilo moja mwananchi amekatwa shilingi 10 kwa ajili ya kuwalipa viongozi wanaosimamia ununuzi huo zaidi ya shilingi bilioni moja! Hivi tukienda kuwauliza hizo shilingi bilioni moja kwa biashara ya miezi mitatu wamezifanyia nini wataweza kutueleza? Wakati wana mishahara, wanatumia magari ya Serikali na kila kitu kimo wanafuatilia, mfano sasa hivi kuna utengenezaji wa madawati, wanalipwa shilingi bilioni moja kufuatilia utengenezaji wa madawati? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali na hasa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu zao la korosho analijua hahitaji kuelekezwa na mtu, ana uzoefu alioupata kutokana na Chama chake cha Ushirika Kikuu cha Mkoa wa Lindi cha Ilulu na baada ya kuwa wamechoshwa na Ilulu wakaanzisha Lunali ambayo kwa kiasi kikubwa inafanya vizuri. Kwa hiyo, katika eneo hili Mheshimiwa Waziri Mkuu wala hahitaji kushauriwa na mtu, anajua mbichi na mbivu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu mimi pamoja na Wizara ya Fedha napongeza sana kwa yale makato ambayo yamepunguzwa na fedha hizi tunataka sasa ziende zikamnufaishe mwananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule ndani eti kuna pesa zinakatwa kwa ajili ya unyaufu na korosho inaanza kunyauka baada ya miezi sita, lakini korosho zinafanywa minada kila wiki na ununuzi wa korosho unaanza mwezi wa kumi na unaisha kwa kuchelewa mwezi Januari. Sasa miezi hiyo mitatu hata kabla ya miezi sita kwa nini mwananchi akatwe eti ni unyaufu. Kwa hiyo niwaombe viongozi wenzangu wa Mtwara tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuunge mkono Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanakata shilingi 50 kila kilo ya korosho kwa ajili ya kusafirisha. Mimi katika Jimbo langu hakuna hata eneo moja ambalo linazidi zaidi ya kilometa 100, kwanza hazifiki. Sasa ndiyo kutaka kusema kwamba kila korosho inayosafirishwa tani 10 kutoka mahali popote, kilometa moja, kilometa mbili, kilometa tatu, tani kumi zinalipiwa shilingi 500,000. Kwa kweli huu ni unyonyaji wa hali ya juu, kwa hiyo, tumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilitaka nilichangie ni ukusanyaji wa kodi za Halmashuri na TRA. Mimi sina ubishani wowote, property tax zikusanywe na TRA na vyanzo vingine vyote wakusanye lakini mchango wangu ni kwamba pesa zile zikishakusanywa, zote zirudi Halmashauri na zirudi kwa wakati kama ambavyo TRA inakusanya mapato yake kila mwezi ikishakusanya inayagawa katika Sekta mbalimbali ili ziweze kutumika katika mwezi unaokuja. Kwa hiyo, Halmashauri kila mwezi ipate mapato yake yaliyokusanywa katika mwezi ule ili yaweze kufanyiwa kazi katika Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunakusanya naomba pia tuwajengee uwezo watumishi wa Halmashauri ili zoezi hili liwe la mpito. Tufike mahali Halmashauri kupitia huu ugatuzi tunaozungumza wakusanye wenyewe. Isiwe kwamba mwaka huu waanze TRA halafu iwe ndiyo forever, tutakuwa hatuzijengei uwezo Halmashauri halafu ni kinyume cha sera yetu ya Ugatuzi wa Madaraka (Decentralization by Devolution). Kwa upande wa fedha huku tunaanza kurudi nyuma, lakini kama ni zoezi la mpito naliunga mkono lakini msisitizo wangu, kila mwezi Halmashauri zipelekewe pesa zao kwa sababu pesa hizi zimewekwa kwenye bajeti na wanazitegemea kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo jingine ambalo ningependa nilichangie ni suala la mradi wa viwanda vya chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma. Miradi hii ni miradi ambayo ni kama viwanda mama ambavyo vyenyewe vitachochea viwanda vingine. Kwa hiyo, mchango wangu nilitaka niseme viwanda hivi pia viangalie na ujenzi wa reli ya kutoka Liganga na Mchuchuma kwenda Mtwara ambavyo vinaenda sambamba...
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga Naunga mkono hoja.

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, nimesimama mbele yako kwanza, kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na kumshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kunipa afya kuweza kusimama na kuchangia katika mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuanza kwa kumwomba Rais wangu kipenzi, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, asiusaini mkataba huu kwa manufaa ya Watanzania. Tunamwomba sana kama Wabunge, kwa sababu mkataba huu hauna manufaa hata kidogo kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kutokusaini huu mkataba hatuwi wa kwanza na wala hatuwi kituko. Kwa upande wa SADC, Angola hawajasaini; kwa upande wa ECOWAS, Nigeria na Gambia hawajausaini mkataba huu. Kwa hiyo, sisi hatuwi wa kwanza kuukataa mkataba huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkataba huu hauna manufaa yoyote na Watanzania kwa sasabu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu, nchi kumi ambazo Tanzania tunafanya nazo biashara, nchi ambazo sisi tunachukua bidhaa, tuna-import kutoka kwao, ya kwanza ni Saudi Arabia; ya pili, ni China; ya tatu, ni India; ya nne, ni Falme za Kiarabu; ya tano, ni Afrika Kusini; ya sita, ni Uswiss; ya saba, ni Japan; ya nane, ni Marekani; ya tisa, ni Kenya; na ya kumi ni Andorra. Katika hizo nchi kumi, nchi za Ulaya ni Uswiss peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda kuangalia katika nchi ambazo sisi tunapeleka bidhaa zetu katika zile top five; ya kwanza ni China; ya pili ni India; ya tatu, ni South Africa; ya nne, ni Saudi Arabia; na ya tano, ni Kenya. Hakuna nchi yoyote ya Ulaya hapo.
Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia katika FDI; ya kwanza ni Uingereza ambayo na yenyewe ni inajitoa kwenye Jumuiya ya Umoja wa Ulaya; ya pili, ambayo ndiyo itakuwa ya kwanza, kwa sababu Uingereza inatoka katika Jumuiya ya Ulaya, ni India; ya tatu ni Kenya; ya nne, ni Netherland; inafuata China, Marekani, Afrika Kusini, Canada, Ujerumani na Oman. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nchi zenyewe za Ulaya unaziona ni kama mbili tu. Kama tunataka kuua biashara zetu, kama tunataka kuua viwanda vyetu, tuingie katika huu mkataba. Wanachotaka hawa ni kutaka kuchepusha mfumo wetu wa biashara. Wanataka kututoa tusifanye biashara na Saudi Arabia, China na India; na kwa sasa hivi, masuala ya biashara wanaotawala duniani ni China, India na Marekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa Jumuiya ya Ulaya wanataka kuturudisha tena tulikotoka. Wanataka tena scramble for Africa, hatuko tayari. Pia wanachokifanya Jumuiya ya Ulaya, kwa sababu makubaliano ya EPA ni kusaini Jumuiya ya Afrika kama nchi moja na sio mmoja, mmoja. Kwa hiyo, wanachotaka ni kuvunja Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Tuwaambie kabisa, Jumuiya ya Ulaya kwa kuanza kusaini na nchi moja moja badala ya kanda nzima kama Afrika Mashariki, wanataka kubeba dhima ya kuuwa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, narudia tena, namwomba Mheshimiwa Rais, kwa kweli asisaini mkataba huu. Kuna mtu amesimama hapa akasema tusomewe mazuri yaliyoko katika mkataba. Mkataba tumekabidhiwa, angeusoma huu mkataba akatueleza yeye mazuri. Yeye anasimama, anasema tusaini, lakini hajasema hata moja zuri, anakusudia nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda nimuunge mkono Mheshimiwa Bobali aliyesema hivi sisi, tuna kitu gani tunachoweza kwenda kuuza Ulaya? Sana sana sisi tunategemea malighafi; tunategemea kuuza nyama, samaki, lakini je, tuko tayari? Tunao uwezo wa kushindana na bidhaa kutoka Ulaya au sisi tunataka kufanywa soko la kuja kutupa bidhaa zao za kuja hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi za Caribbean ambazo zilijiunga, tafiti zinaonesha zimepoteza mapato yao kuanzia mwaka 2009 hadi 2013, wamepoteza zaidi ya Euro milioni 74.
Mheshimiwa Spika, narudia tena, tusisaini mkataba huu, hao wanaoshabikia, ndio wafadhili wao. Sisi hatuko tayari kusaini mkataba ambao pia katika kifungu cha 96 cha Cotonou ambacho kinaoanisha na Ibara ya 136 ya EPA pia haki za binadamu zimo, ambamo ushoga umo. Tuko tayari sisi kuingizwa kwenye ushoga kwa kupitia hii biashara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, narudia tena kusema siungi mkono hoja. Mkataba huu Mheshimiwa Rais tunakuomba usiusaini.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti nikushukuru kwa kunipa nafasi nichangie taarifa yetu ya Kamati ya Bajeti. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti ya Serikali kwa upande wa miradi ya maendeleo hadi kufikia asilimia 40. Tunachoomba tu kwamba pesa ziendele kwenda kwa wakati ili miradi itekelezwe kama ambavyo tumepanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niipongeze Serikali kwa hatua ya kusaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati. Reli ya kati ni kama mishipa ya fahamu ya mwili wa binadamu kwa uchumi ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuendelea kwa kutegemea bidhaa na malighafi zetu kubebwa na Lori moja moja kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma, Mwanza na kwenda nchi za jirani na hilo hilo lirudi lije lichukue kwa kweli hili haliwezi kutufikisha mbali lakini kwa hatua hii ya Serikali kusaini Mkataba wa kujenga reli tena kwa standard gauge kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kama hatua ya kwanza naipongeza sana na tunaomba vipande vilivyobaki basi vifanyiwe haraka ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa Serikali kulisisitizia ni eneno la EPZA. Kamati ilitembelea eneo la Mheshimiwa Benjamin Mkapa pale Mabibo, kwa kweli kule ndani kuna kazi nzuri sana inayofanyika na kuna ajira nyingi sana zinazotolewa kwa vijana wetu. Bidhaa zinazozalishwa pale ni za ubora wa hali ya juu na za mauzo ya nje ambazo zinatuingizia pesa za Kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kitu kama kile tulitegemea Dar es Salaam pale tuwe na EPZA kama mbili na ikiwezekana angalau kila mkoa tuwe na eneo la EPZA kwa sababu ni eneo ambalo linakuza ajira, linaingiza mitaji, linatuongezea teknolojia kutoka nje. Eneo la Kurasini tayari Serikali ilishalipia fidia kwa hiyo, tunaomba wawezeshwe EPZA kuweza kujenga miundombinu na hivyo kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika eneno la EPZA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, kwa sababu umenipa dakika tano, ningependa kusisitiza suala la utekelezaji wa mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mradi huu umezungumzwa kwa muda mrefu sana na ni mradi ambao kwa kweli utaleta viwanda mama, viwanda vya vyuma, viwanda ambavyo vitaleta viwanda vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua iliyofikiwa si mbaya kwa maana kwa upande wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe sawa, lakini upande wa chuma. Makaa ya Mawe yale na chuma tunategemea kwa kiasi kikubwa yasafirishwe kupitia Bandari ya Mtwara na reli ambayo tayari feasibility study ilishakamilika, upembuzi yakinifu ulishakamilika sasa hii tathmini ya fidia ilishakamilika, kwa hiyo, tunaomba fidia ile iweze kulipwa na ile reli kutoka Mtwara kwenda Mchuchuma na Liganga na matawi yake kwenda Mbamba Bay upewe umuhimu wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu chuma kile bila reli ile na makaa ya mawe yale bila reli ile kwa kweli hatuna barabara za kuweza mzigo mzito kama ule sana sana barabara zetu zitakuwa ni za kujenga baada ya miaka miwili zimeharibika halafu tunawalaumu waliojenga au waliosimamia kuzijenga lakini ni kutokana na mzigo mzito kwa hiyo nisisitize mradi wa Liganga na Mchuchuma na pia reli ya kutoka Mtwara, Liganga na Mchuchuma vitekelezwe kwa wakati muafaka ili kukuza uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana ulinipa dakika tano nisingependa unigongee kengele, naunga mkono hoja.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Kwanza nianze kwa kutoa pole kwa Wana-CCM wenzetu ambao walipata ajali na kupoteza
maisha kule Mkoa wa Kilimanjaro. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aweke roho zao mahali
pema peponi na pia awape moyo wa subira familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda niende haraka haraka
katika kuchangia hoja. Suala la kwanza nilitaka kumuuliza Waziri wa Miundombinu, hivi zile
Bombadier Mtwara zitaenda lini? Mimi nimezipanda kwenda Tabora, nimepanda kuja Dodoma,
kwa kweli ni ndege nzuri zinaenda kwa kasi, zinachukua muda mfupi sana. Mtwara ni miongoni
mwa viwanja bora sana ambavyo vimejengwa muda mrefu, kwa nini na sisi tunyimwe hiyo haki
ya kupelekewa Bombadier? Kwa hiyo, nilikuwa naomba atueleze lini hizo Bombadier zitaanza
kwenda Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nililotaka kulizungumzia ni kuhusu barabara ya
kutoka Mbwenkulu kwenda Nangurukuru. Kwa kweli ile barabara kile kipande kimechakaa,
kinatitia na kinasababisha ajali nyingi sana. Ukitoka Somanga kwenda Daraja la Mkapa kile
kipande ambacho kimejengwa na Caraf unaweza mpaka kuandika hata barua, yaani huwezi
kujua kama uko kwenye gari. Tunaomba na eneo lile la kutoka Mbwenkulu kwenda
Nangurukuru nalo lirejewe na liwe na ubora ule ule unaofanana kutoka Somanga kwenda
Darajani. Huwezi kuamini kama uko ndani ya gari. Tunaomba kwa kweli lile eneo lirudiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nilitaka nilizungumzie ni kuhusu umeme.
Katika Mji wa Mtwara juzi nimepokea message kwamba wanaomba samahani kwamba siku hizi
kuanzia saa moja mpaka saa nne usiku hakuna umeme. Sasa hivi anaeanza kupata umeme
kuanzia saa tano huo kweli si afadhali hata tungekuwa tunapewa saa moja mpaka saa nne?
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosababisha ni kwamba zile megawati 18 zimeshakwisha
sasa hivi, kwa hiyo ikitokea shoti kidogo kwenye jenereta moja ni tatizo. Tunaomba yaongezwe
majenereta hali ni mbaya katika Miji ya Mtwara na Lindi. Tunaomba Wizara ya Nisahati ije na
kauli inaongeza lini megawati lakini hata ile mitambo iliyopo wanaifanyia lini matengenezo ya
uhakiki? Huwezi kuwa na mahitaji megawati 18 na zilizopo megawati 18. Kwa kweli hapana,
tunaomba hilo waliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na suala lingine ambalo nilitaka nilizungumzie ni suala la
barabara kutoka Mtwara kwenda Newala - Masasi ni kilometa 30, tunataka kujua mkataba
unasainiwa lini Mheshimiwa Waziri? Mheshimiwa Rais alituambia akiingia madarakani kazi ya
kutoka Mtwara Mnivate inaanza na eneo lililobaki ataweka wakandarasi wanne ili wajenge kwa
wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba vile viatu vya Mheshimiwa Rais, ambaye alikuwa
Waziri wa Ujenzi aliyekutangulia ujitahidi ili viweze kukuenea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika taarifa za Kamati hizi mbili. Pia nichukue fursa hii kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa ajili ya kuishauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kwanza wa miaka mitano wa maendeleo ulikuwa na lengo la kutoa vikwazo vya kimaendeleo ambavyo vilikuwepo kipindi kile ikiwa ni pamoja kuongeza upatikanaji wa umeme, kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli na barabara pamoja ya kuboresha bandari zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Pili ambao tunao ambao una lengo la kuhakikisha kwamba tunakuwa na uchumi wa viwanda. Naliunga mkono sana hilo lakini wasiwasi wangu nahisi tunaweza tusifike mbali kwa sababu bado vile vikwazo ambavyo vilikuwepo katika mpango wa kwanza vinaelekea kwamba bado tunaendelea kuwa navyo na vingine si kwamba vikwazo halisi vipo lakini baadhi tu ya watu wanaamua kuvifanya viwe vikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri wa Viwanda na Biashara, vile viwanda wanavyosema anatembea navyo mfukoni kwangu kwa kweli amenisaidia sana na tumefikia hatua nzuri. Nilimwomba kiwanda kwa ajili ya sulphur kwa sababu sisi kule ni wakulima wa korosho na sulphur kwa kiasi kikubwa tunaagiza kutoka nje, basi tuliomba angalau hata kufunga waje waifungie kule kwetu lakini pia tunaweza kutengeneza kwa sababu tunayo gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari mwekezaji amekuja, Mtwara amekwenda, ardhi tumempatia sasa hivi yuko hatua za mwisho na nina imani kabisa huko TIC atamaliza lakini wasiwasi wangu ni upande wa nishati, upande wa upatikanaji wa gesi na upande wa umeme, ndiyo maana nikasema kwamba vile vikwazo bado vipo. Gesi inatoka Mtwara lakini mpaka tunapozungumza hapa tunavyo viwanda zaidi ya viwili, vingine vinashindwa kujengwa; bado Wizara haina nia ya dhati ya kusaidia wawekezaji kuwapatia gesi au kuwapatia umeme wale ambao wanataka kuwekeza Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu; mwakani tutakapokuwa tunajadili Kamati ya Viwanda na Biashara iunganishwe na Nishati na Madini kwa sababu tulikotoka tulikuwa na changamoto sana ya ardhi kwa wawekezaji wetu kwenye viwanda. Sasa hivi hatuna tatizo kwenye ardhi, hatuna tatizo na Wizara ya Viwanda na Biashara, tatizo kubwa lililopo ni upande wa Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara tunavyozungumza sasa hivi umeme ni wa shida, mitambo inakufa kila mara, megawati 18 zinazozalishwa mahitaji zimeshazidi megawati 18 na hatuoni mipango ya uhakika ya kuhakikisha tatizo hilo linakufa. Tunacho kiwanda cha mbolea, tayari wamekuja Wizara ya Viwanda na Biashara imewasaidia imetoa eneo lake la EPZA, Wizara ya Miundombinu wamejenga barabara ya lami mpaka katika hilo eneo, lakini mpaka sasa hivi watu wa Wizara ya Nishati hawajaonesha nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba kiwanda kile kinakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndani ya Serikali kwa mtazamo wangu, wenyewe kwa wenyewe wanakwamishana na kwa kiasi kikubwa nahisi hata vile viwanda tunavyovihisi kwamba viko mfukoni si ajabu vinakwama kwenye nishati. Kwa hiyo, tuseme bila kigugumizi kwamba Wizara ya Nishati isaidie Wizara nyingine katika kuhakikisha kwamba viwanda, kama uchumi wetu ni wa viwanda, nishati kwa kiasi kikubwa itatumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiingii akilini kwamba Mtwara ile mpaka sasa hivi hawajamuingizia umeme hata mtu mmoja, hawajamuingizia gesi hata mtu mmoja na wala hawana mpango. Pia nimuombe Waziri wa Viwanda na Biashara atuelezee mpango mkakati wa kuendeleza viwanda katika Mji wa Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo ardhi, eneo la EPZA, wengine wanalia fidia sisi fidia ilishatolewa tangu mwaka 2000, eneo lipo kuzunguka bandari, hakuna matatizo ya fidia wala nini, wanasubiriwa wawekezaji. Eneo ambalo Dangote amejenga kiwanda ni hekta 17,000, yeye amepewa 4,000 tu nyingine zipo za kumwaga hazihitaji fidia, hazihitaji kitu chochote, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara atuelezee na Waziri wa Nishati na Madini mikakati yao ya kuhakikisha gesi inatumika katika viwanda katika Mji wa Mtwara. Ni haki yetu watu wa Mtwara na sisi kupata maendeleo ya nchi hii na wala hatuombi favour. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka nizungumzie, kama nilivyotangulia kusema eneo la EPZA Mtwara tunalo fidia ilishalipwa tangu kipindi cha Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, eneo lipo wazi. Sambamba na EPZA ya Mtwara, tunayo Kurasini, tunayo pale Benjamin Mkapa na katika mikoa maeneo mbalimbali, EPZA ndiyo njia rahisi kama walivyotangulia kusema, ya kuhakikisha nchi inaendelea kwa haraka. Watu wanakuja na mitaji yao, wanakuja na teknolojia yao, sisi tunachopata pale, kwanza tunapata ajira, tunapata teknolojia mpya na pia tunapata pesa za kigeni. Hivi kwa nini tusihakikishe kwamba hii EPZA inakwenda kwa kasi, hata China tunaosema wameendelea walianzia na EPZA, kule akina Shenzhen, maeneo mengi, akina Guangzhou, kote walianza kama EPZA, kwa nini tusiige hayo mambo mazuri na sisi tukaweza kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wale wanaosema kwamba viwanda vile ambavyo vilibinafsishwa vihakikishe vinafanya kazi iliyokusudiwa. Kule kwetu Mtwara viwanda vya korosho watu walipewa kwa bei ya kutupa lakini hakuna hata mtu mmoja anayebangua korosho, wengi kazi yao wamefanya maghala wanayakodisha kipindi cha ununuzi wa korosho wanaona inawalipa kuliko kufanya viwanda, korosho zetu zinakwenda nje zikiwa hazijabanguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kuhakikisha kwamba viwanda vile kama watu madhumuni waliyopewa, kwa sababu hawakupewa kwa bei ya soko, walipewa kwa bei ya kutupa, wahakikishe aidha, wafanye kazi iliyokusudiwa au wanyang‟anywe wapewe watu wengine ili waweze kufanya kazi iliyokusudiwa. Haiwezekani kiwanda cha korosho leo kinageuzwa ghala la kuhifadhia korosho, kwa kweli hilo tulisimamie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri wa Viwanda na Biashara, anahangaika katika kutafuta viwanda. Sisi kama Wabunge katika maeneo yetu lazima na sisi tumuunge mkono, amenipa mwekezaji nimekwenda naye nimemtembeza katika maeneo yote ya ardhi na akachagua eneo analolipenda na tumefikia hatua nzuri, nina uhakika kile kiwanda kitafika, lakini wasiwasi wangu Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Ardhi kwa sababu ili uweze kuwekeza vitu vikubwa muhimu ni ardhi, nishati na wenzetu hao Wizara ya Viwanda na Biashara ambao tunategemea waweke mazingira mazuri. Kwa sababu hawezi kujenga viwanda Waziri wa Viwanda na Biashara. Kazi ya Waziri wa Viwanda na Biashara ni kuweka mazingira mazuri ambayo anayaweka, Waziri wa Ardhi hana matatizo kwenye uwekezaji, ardhi, migogoro anatusaidia kutatua, lakini Nishati na Madini kwa kweli kama tunataka tuwe na uchumi wa viwanda Wizara ya Nishati na Madini kwa kweli iamke. Ndiyo tunapata umeme wa REA vijijini, lakini ule ni kuwasha tu vikoroboi badala ya vikoroboi sasa tunaleta bulb, tunahitaji umeme uzalishe, uinue uchumi wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami ningependa kuchangia hoja. Niwapongeze watoa hoja wote na hivyo nianze kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ningependa kuzungumzia suala la elimu na hasa masuala mazima ya ufaulu. Katika wilaya nyingi na mikoa mingi ambapo matokeo ya kidato cha pili na kidato cha nne yamekuwa siyo ya kuridhisha, asilimia kubwa uamuzi au hatua zilizochukuliwa ni kushusha vyeo walimu wakuu au wakuu wa shule. Mimi sidhani kama mwalimu peke yake anaweza akawa ndiyo sababu ya shule kufeli au kufaulu. Mimi napenda nishauri katika zile Wilaya ambazo kila mtihani uliofanywa zimekuwa za mwisho hebu tufanye utafiti wa kina tujue kwa nini wilaya hizo zimefanya vibaya. Haiwezekani kwenye Mkoa wangu Wilaya moja hiyo hiyo matokeo ya kidato cha nne wa mwisho, matokeo ya darasa la saba ya mwisho halafu tuone hatua ya kuchukua ni kushusha vyeo tu walimu, sidhani! Naomba tufanye tathmini ya kina ili tujue tatizo tuweze kuwasaidia na zile Wilaya na zenyewe zifanye vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye sekta ya afya na nianze kuzungumzia suala la uchache wa watumishi katika sekta ya afya. Kwa kweli hali ni mbaya, ukienda katika vituo vyetu vingi vya afya, hospitali majengo ni yanaridhisha, unakuta hospitali zetu sasa hivi nyingi ni safi, madaktari wanajitahidi hata wauguzi, kauli zinaridhisha lakini uchache wao unawaangusha. Katika baadhi ya Wilaya tunashindwa kutoa baadhi ya huduma kama upasuaji, kufungua baadhi ya zahanati, kwa sababu ya uchache wa watumishi. Niombe Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, wakati tukiendelea na uhakiki basi kama tulivyofanya kwa sekta ya elimu na sekta ya afya nayo tuiangalie, hali ni mbaya hasa katika Mkoa wangu wa Mtwara ambao ninaufahamu. Nina vituo vyangu vya afya ambavyo vimeshindwa kuanza huduma za upasuaji kwa sababu hatuna watumishi wa kuweza kutoa huduma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vifo vya akina mama limezungumziwa sana hasa kutokana na changamoto za uzazi. Mojawapo ikiwa kuzalishwa na watumishi ambao kwa kweli hawana utaalamu. Niombe hivi vituo vya afya, mlishaanza kuvifanyia tathmini na kuvipa madaraja, zoezi hili likamilike nchi nzima ili vile vituo ambavyo havina uwezo wa kuzalisha akina mama waambiwe kwamba siku zako zikifika pale huwezi kusaidiwa, wajue ili ajiandae, ikiwezekana aende akakae karibu na eneo ambalo ataweza kusaidiwa. Kwa sababu kama atahitaji damu wakati wa kujifungua, kama atahitaji operation wakati wa kujifungua ndiyo kusema kama atakuwa eneo ambapo hakuna huduma hizi huyo mama ndiyo tumeshampa cheti cha kifo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka kulichangia ni tafiti zinaonesha maeneo ambayo wanaume wanafanyiwa tohara maambukizi ya UKIMWI yako chini sana kuliko maeneo ambayo hayafanyiwi tohara ambapo maambukizi ya UKIMWI yako juu sana, na hivyo hivyo maeneo ambayo tohara haifanyiki maambukizi ya kansa ya shingo ya kizazi pia yako juu. Niiombe Wizara ya Afya hili suala la tohara kwa wanaume lisiwe la hiari liwe la lazima. Kwa sababu kama tafiti zote zinatuambia maeneo mengine wanaume ambao hawajatahiriwa maambukuzi wako zaidi ya asilimia 21 kuliko wale ambao wametahiriwa. Kwa nini tusiseme ni lazima? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba, ile Mikoa ambayo wanatahiriwa, lile tendo wasiite suna, maana yake mtu anasema anakwenda kutahiriwa unaita suna, kitu kama ni suna maana yake siyo lazima, niwaombe kwa wale wanaotahiriwa tuseme faradhi ili kila mtu ahamasike. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wote tulikuwa Morena, tumeambiwa haya, siyo kama nimeyatoa kichwani, ni taarifa zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani, Wizara ya Afya wanazo. Tupeleke taarifa sahihi, kuhusu suala la tohara kwa wanaume. Tutawanusuru akina mama wetu tutapunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara ya Afya, tunazo hospitali zetu za Kanda, Kanda ya Kaskazini tunayo KCMC, Kanda ya Magharibi au ya Ziwa tunayo Bugando na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini tunayo Hospitali ya kule Mbeya, Kanda ya Kusini peke yake ndiyo imebaki ambayo haina Hospitali ya Rufaa ya Kanda, ujenzi umeanza lakini ni wa kusuasua. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, tusaidie katika hilo, gharama ya kumsaidia mgonjwa mmoja kuja hospitali kutibiwa kwa kumsafirisha kwa ndege kutoka Mtwara, Precision Air inafika mpaka shilingi milioni 12. Mimi mwenyewe nimesafirisha kijana ambaye alipata ajali ya gari kwa shilingi milioni nane kwa ATC, kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, ni wangapi wanaweza gharama hizo? Kwa hiyo, tuwaombe wenzetu wa Wizara ya Afya mkamilishe ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo Hospitali za Rufaa za Mikoa, naomba tuzifanye ziwe kweli Hospitali za Rufaa za Mikoa. Unakwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa unakuta ina oxygen machine moja, wakija wagonjwa wawili mmoja anakuwa kwenye mashine mwingine hata kama anahitaji ile huduma hawezi kupata. Tuombe muweke MRI, muweke CT Scan, X-ray machines, angalau hata kwa Kanda. Kwa sababu tunazungumzia suala la ugonjwa wa kansa ya kizazi ndiyo ugonjwa ambao unaua sana akina mama, lakini huduma hiyo inapatikana hospitali ya Ocean Road peke yake, na ugonjwa huo mgonjwa akiwahi unatibika. Kwa hiyo, niombe basi huduma hii ipelekwe angalau kwenye Kanda. Hivi ni wangapi wenye uwezo, unatoka Rukwa, unatoka Kagera kwenda Dar es Salaam na kila dozi inapokuja uende, kwa kweli, ndiyo kule utatibiwa bure, lakini mara nyingi gharama za kwenda kule huwa wanajigharamia. Kwa hiyo niombe kwa kweli hili lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la kuweka vifaa MRI, CT Scan na X ray machines siyo lazima Serikali ifanye, tunaelewa kwamba Serikali haina uwezo wa kugharamia kila kitu na tunaona unapokwenda kwenye hospitali pale Muhimbili kama mashine haifanyi kazi unaambiwa ukapime nje, kwa nini msiingie ubia mkafanya PPP, hizo mashine wakaja kuziweka kwenye hospitali zetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wizara ya Afya mshirikiane muingie ubia, vitu kama MRI, CT Scan, X-Ray, kila baada ya miaka mitano teknolojia inabadilika na hatuwezi kwenda na kasi hiyo, lakini akiweka mtu binafsi ikipita muda wake unamwambia hamisha leta nyingine inayoendana na teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika Wizara hii, pamoja na ukubwa na majukumu mengi lakini wanaonekana kuweza kuyamudu na kuimudu Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza napenda nipongeze kazi ya upanuzi wa Bandari ya Mtwara ambao tayari umekwishaanza. Ni imani yangu kwamba upanuzi ule wa bandari utasaidia sana katika kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Mtwara, Lindi na Ruvuma hasa ukizingatia kwamba sisi ni wakulima wakubwa wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupanua bandari ile sasa hivi hakutakuwa na sababu hata kilo moja kusafirishiwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam hasa inayozalishwa katika Mikoa ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la Liganga na Mchuchuma kwamba kule kuna uzalishaji wa makaa ya mawe, kuna chuma, tuna kiwanda kikubwa sana cha Dangote ambacho kinategemea hiyo bandari pia tunategemea chuma itakayozalishwa kule, makaa ya mawe na yenyewe pia yasafirishwe kupitia Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri suala la upanuzi wa Bandari ya Mtwara basi liende sambamba na ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na Liganga na Mchuchuma. Suala la upembuzi yakinifu limekamilika, tathmini ya mimea pamoja na nyumba maeneo ambapo reli itapita imeshakamilika. Kwa hiyo, namwomba sana suala hilo nalo liende pamoja ili ile bandari isije ikaleta mzigo mkubwa ukalazimika tena kusafiri kwa magari ambao utaharibu barabara ambayo kwa kweli tumekaa muda mrefu sana baina ya Mtwara na Ruvuma hatujawa na barabara ya kueleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine napenda kumpongeza sana Waziri na Serikali pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kuanza kujenga reli ya kati. Reli ya kati ni sawa na mifumo ya damu au mifumo ya fahamu ndani ya mwili wa binadamu, reli hiyo ndiyo itakayoifanya bandari ya Dar es Salaam iweze kufanya kazi yake vizuri. Kwa hiyo, namwomba tu waharakishe hicho kipande cha kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ambayo ni reli ya kisasa sana. Vipande vinavyobaki basi watangaze kwa haraka ili ujenzi huo ikiwezekana uweze kukamilika kwa muda mfupi sana, kwa sababu huo ndiyo ukombozi wa nchi yetu na maendeleo yetu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine napongeza pia ndege ya Bombardier kuanza kutua Mtwara na Songea. Tarehe 30 imeenda kwa mara ya kwanza, nimeambiwa kwamba kutakuwa na ratiba nzuri tu zinazoeleweka. Ushauri wangu naomba ile ndege ya kwenda Mtwara inaunganisha pamoja na Ruvuma, unatoka Mtwara unaenda Ruvuma saa nzima, unatoka Ruvuma kwenda Mtwara dakika hamsini karibu na tano, halafu ndiyo utoke pale kwenda Dar es Salaam karibu tena dakika 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba route ya Ruvuma ikiwezekana iwe ni ya Ruvuma peke yake ili mtu akitoka Dar es Salaam anafika Ruvuma na akitoka Ruvuma anafika Dar es Salaam. Kutoka Mtwara mpaka ufike Ruvuma upite tena Mtwara kwa kweli inachukua muda mrefu sana na kama shirika kweli linataka kushindana na mashirika mengine ambayo yanaenda Mtwara hapo hamtaweza kushindana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kwamba route ya Mtwara iunganishwe na ya Comoro kwa sababu kutoka Mtwara kwenda Comoro ni saa moja na kutoka Comoro kwenda Mtwara ni dakika kama 25 au nusu saa. Kwa hiyo, hapo utaweza ushindani. Huo ndiyo ushauri wangu kwamba hiyo route ya Dar es Salaam – Ruvuma – Mtwara waiangalie tena ikiwezekana Mtwara iambatanishwe na ya Comoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilichangie ni suala la barabara ya kutoka Mtwara – Newala kwenda Masasi. Niishukuru Serikali kazi inaonekana kwamba inakaribia kuanza, Mkandarasi amepatikana na ameshaanza kukusanya vifaa tuna imani muda wowote ataanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika bajeti iliyotengwa mwaka huu ambao tunaenda nayo ni bilioni 21 na bajeti ambayo ipo sasa hivi ni bilioni saba. Kwa mujibu wa mkataba ule ni zaidi ya bilioni 90 na mkataba ni wa miaka miwili, sasa kwa pamoja tumetenga kwa miaka miwili bilioni 29, mkataba unataka bilioni karibu 90 na kitu. Sasa huyo Mkandarasi atajenga kwa fedha zipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie hilo, vinginevyo tutakuwa tunamfanya Mkandarasi anakuwa site anaondoka. Mheshimiwa Waziri tunashukuru kwa sababu lazima ushukuru kidogo ulichokipata, tunashukuru kwamba sasa hivi ile ndoto imeanza kutimia, lakini pia iangaliwe bajeti ili barabara ijengwe kwa ubora unaokusudiwa, kwa sababu kama pesa zitakuwepo mkandarasi hana kazi ya kuondoka site na kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la Uwanja wa Ndege wa Mtwara. Uwanja ule umejengwa kabla sijaanza hata darasa la kwanza na hata sijui umejengwa lini kwa sababu nimepata akili nimeukuta ule uwanja upo tayari. Tangu kipindi hicho sidhani kama kuna ukarabati wowote
wa uhakika uliofanywa na sasa hivi ndege zikitua pamoja na kwamba ni uwanja wa lami lakini utafikiri umetua kwenye matuta. Kwa hiyo, nawaomba Wizara wauangalie uwanja ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna masuala ya utafiti wa gesi yanakuwa yakifanyika pamoja na kwamba sasa hivi yamesimama. Kule kazi zinafanyika usiku baharini, uwanja hauna taa na kama mnavyofahamu Mtwara jua linaanza kutoka na linawahi kuchwa. Sasa siku nyingine mnaondoka abiria mnakaribia uwanja mnaambiwa uwanja umeshaingia giza mnarudi tena Dar es Salaam. Nawaomba waukarabati uwanja ule pia wauweke taa. Taa zinazotumika pale ni za wachimbaji wa gesi na hawaruhusu taa zao kwa sababu ni mobile wanaziweka pale tu panapokuwa na dharura na kwa maombi maalum. Kwa hali, ambayo tumefikia sasa hivi Mtwara kwa kweli tunaomba uwanja ule ukarabatiwe na uwekwe taa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa wale ambao wameenda Mtwara, lile jengo la abiria lipo ndani ya uwanja, nalo waliangalie waone uwezekano wa lile jengo kuliweka kama majengo mengine yalivyoojengwa. Haiwezekani jengo yaani unashuka kwenye ndege unaingia moja kwa moja kwenye jengo la abiria kwa sababu kwanza ni hatari kwa abiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena kumpongeza Waziri pamoja na timu yake, niombe tu yale ambayo nimeuombea Mkoa wangu na kuiombea nchi yangu basi yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na wataalam wao kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao. Nipongeze Serikali kwa kuanza kujenga reli kwa kiwango cha SGR, pia nimpongeze Waziri kwa kazi ya ujenzi na upanuzi wa barabara ya Mtwara. Naomba Serikali kuona umuhimu wa kukarabati uwanja wa ndege wa Mtwara kwani umechakaa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuiomba Serikali kuhusu kuharakisha na kuongeza kiwango cha pesa kwa barabara ya Mtwara, Newala, Masasi kwa mujibu wa mkataba. Serikali pia ianze ujenzi wa reli ya Mtwara - Mchuchuma na Liganga Mbamba bay. Reli hii ni muhimu sana kwa uendeshaji wa bandari ya Mtwara.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia. Napenda nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake pamoja na watendaji wote wa sekta ya afya ambayo kwa kweli wanafanya kazi nzuri, ngumu na yenye changamoto kubwa lakini bado wanaonesha kuimudu, kwa hiyo napenda nimpongeze sana. Mheshimiwa Waziri amesoma hotuba yake vizuri ambayo inaonesha anajiamini lakini pia sekta hii anaijua vizuri. Ameonesha malengo bayana ambayo anakusudia katika bajeti hii kutatua kero ambazo ziko ndani ya sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunisaidia kunipatia gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kitele, kwa kweli namshukuru sana. Pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri TAMISEMI kwa kutoa ufafanuzi kuhusu suala la upanuzi wa Kituo cha Afya Nanguruwe na Nanyumbu kuwa hospitali ya Wilaya, kwa sababu ilileta mkanganyiko mkubwa sana, kwa hiyo nawashukuru sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa maombi yafuatayo kwa Serikali. Ombi la kwanza ni kwamba bajeti hii iliyotengwa kwa kweli inatosha. Tunachoomba ni Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba pesa hizo zinakwenda kwa wakati ili yale tuliyoyapanga yaweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili, namwomba Mheshimiwa Waziri wa UTUMISHI, kwa dhati kabisa, kama ambavyo wanatoa vibali vya kuajiri Walimu basi awamu hii wajitahidi na Sekta hii ya Afya itolewe vibali vya kuajiri. Kwa kweli hali ni mbaya sana kwenye vituo vya afya hasa kutokana na huu uhakiki wa vyeti uliofanyika, vijijini kwetu huko kumeathirika zaidi kuliko hata mijini. Kwa hiyo tunaomba watoe vibali vya kuajiri Madaktari, Wauguzi pamoja na Matabibu. Kama wangesema sekta moja tu ipewe kibali, basi mimi ningesema ni sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika maombi ya mkoa wangu, Mkoa wa Lindi na Kanda ya Kusini kwa ujumla. Kila Kanda ina Hospitali ya Kanda ya Rufaa. Kanda ya Kusini ujenzi ulianza karibu miaka 10 iliyopita, lakini kwa miaka hii miwili mfululizo naona kama ujenzi umesimama inatengwa bilioni mbili na hiyo haitoki. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Ummy mdogo wangu afanye huruma kwa ndugu zake wa Kusini, atakapokuja basi atuambie ametuandalia nini cha matumaini ili kuhakikisha hospitali ile inakamilika kabla ya mwaka 2020 ili huduma ziweze kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti iliyopita Kamati ya Bajeti iliweka maombi na mapendekezo ya kuongeza tozo kwa ajili ya kupata pesa za kujenga vituo vya afya na zahanati katika kila Halmashauri. Lengo ikiwa ni kuboresha huduma za afya na pia kupunguza vifo vya akinamama na watoto. Serikali iliomba ipewe muda ifanye tathmini ili katika bajeti hii, waje na mpango mahususi wa kujenga kituo cha afya angalau kimoja kwa kila Halmashauri na zahanati angalau nne kila Halmashauri. Sasa upande wa TAMISEMI bahati mbaya wakati wa bajeti yao sikuwepo, lakini pia nimesoma kwenye makabrasha yao sikuona na upande wa sekta ya afya sioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile tathmini Mheshimiwa Ummy nina uhakika wamemaliza. Kwa hiyo, tutaomba atakapokuja kutoa ufafanuzi au kutoa majibu atuambie, wametenga kiasi gani na baada ya kufanya tathmini wameona gharama ni kiasi gani na mwaka huu wanahisi ni kiasi gani kitatosha ili kuweza kujenga hivyo vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo pia nataka nilizungumzie ni suala la udahili wa kada zote za afya, iwe Madaktari, Wauguzi, Wafamasia kwa kweli uongezwe na sio udahili tu, lakini waajiriwe na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu Afya na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii pamoja na wataalam wao kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Waziri kwa kukipatia gari kituo cha afya cha Kitere, suala ambalo nina imani litasaidia sana katika kuboresha huduma za rufaa kwa wagonjwa hasa akina mama na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri kuongeza watumishi wa afya katika vituo vya afya vya Nanguruwe, Kitere na Mahurunga ili viweze kutoa huduma bora kwani vituo hivyo vinavyo vifaa vya kisasa vya kutolea tiba, lakini baadhi yake vinashindwa kutumika kutokana na uchache wa wataalam wenye weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali pia kuongeza udahili wa wauguzi, maafisa tabibu, wafamasia na wataalamu wa maabara na kufadhili masomo yao ili tuweze kuwapa masharti ya kwenda kufanya kazi katika maeneo yenye upungufu kwa muda maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kuonesha nia ya dhati katika ujenzi wa hospitali ya Kanda ya Kusini. Kwa Kusini Mkoa wa Lindi na Mtwara ni kanda pekee isiyokuwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda na kwa miaka miwili mfululizo kiasi kinachotengwa kwa hospitali hiyo kwanza ni kidogo na pili, fedha hizo hazitolewi. Kwa kifupi ni kama ujenzi umesimama, Mheshimiwa Waziri iwapo hutatoa mikakati inayotia moyo na yenye kuonesha nia ya kukamilisha ujenzi wa hospitali hii nakusudia kuondoa shilingi kwenye mshahara wa Waziri na kwenye bajeti ya Wizara.

Mheshimi Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

The Media Services Bill, 2016

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye amenijalia afya na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuweza kuchangia Muswada huu wa masuala ya huduma za habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuweza kuuingiza Muswada huu Bungeni baada ya zaidi ya miaka 20 pamoja na vikwazo mbalimbali ambavyo vimejitokeza. Kwa hiyo, nampongeza sana Waziri na Naibu wake pamoja na Maafisa wa Wizara yao kwa kazi kubwa sana ambayo wameifanya kuhakikisha Muswada huu unaingia ndani ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nichukie fursa hii kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati iliyoshughulikia Muswada huu. Kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana na katika mazingira magumu. Pia niwapongeze wadau wa habari ambao kwa kweli wamekubali kutoa maoni yao na kuweza kwa kiasi kikubwa kuboresha Muswada huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masuala ya kawaida Muswada kuandaliwa na Serikali na kuupeleka kwa wadau na kwenye Kamati. Lengo la Serikali kupeleka kwa wadau na kwenye Kamati ni kuhakikisha kwamba wadau wanatoa maoni yao, yale maeneo ambayo wanaona yana upungufu wanayazungumzia ili Serikali iweze kuyarekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la ajabu sana Muswada ambao umekaa zaidi ya miaka 20 mdau kila siku ukiambiwa unasema muda hautoshi. Hivi tunao Muswada wowote ambao umejadiliwa zaidi ya miaka 20 ndani ya Bunge hili? Ndiyo maana nawapongeza wale wadau ambao kwa kweli hawakukubali kuburuzwa na hao ambao wamekusudia kuwaburuza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri na Serikali kwa ujumla kwa kufuta kifungu cha 50(4),(9),(10) na (11) ambavyo vilikuwa vinaruhusu polisi kuchukua mashine au mitambo iliyohusika katika kuandika habari ya uchochezi. Hii inaonesha kabisa kwamba Serikali na Waziri wametambua mabadiliko ya teknolojia. Kwa sababu katika mabadiliko ya sasa ya teknolojia, mmiliki wa mtambo anaweza akauweka mtambo wake automatic na mchapishaji akaandika taarifa yake akaleta softcopy kwa ajili tu ya kuchapisha na mmiliki wa mitambo ule asiwe na nafasi ya kusoma lile chapisho mwanzo mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kumchanganya na yeye kwenye makosa kwa kweli naona haikuwa sahihi, lakini naipongeza Serikali yangu kwa kupokea maoni ya wadau na kuviondoa vipengele vyote vinavyohusiana na kuchukua mitambo ambayo imehusika katika kuandika chapisho lenye uchochezi au ambalo kwa kweli linaleta madhara kwa baadhi ya wananchi. Hiyo yote imetokana na mapendekezo ya wadau, Kamati na usikivu wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kabisa kwamba Muswada huu ni mzuri na unalenga kuboresha tasnia hii ya habari. Pia unalenga kulinda haki na wajibu wa vyombo vya habari. Hakuna haki isiyokuwa na ukomo, lazima tasnia kama hii ipewe haki, lakini pia ipewe ukomo na mipaka, ihakikishe haki hiyo wanaitumia vizuri bila kuathiri usalama wa nchi, bila kudhuru wengine na bila kukashfu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hapa Tanzania ni mashahidi, Rwanda imeingia katika machafuko na miongoni mwa sababu ni pamoja na uchochezi wa vyombo vya habari. Ndiyo maana mmiliki mmoja wa vyombo vya habari ni miongoni mwa waliohukumiwa kufungwa. Kwa hiyo, tasnia hii hatuwezi tukaicha tu ielee yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana naipongeza Serikali yangu, unalenga kuwatetea na kuwasaidia waandishi wa habari. Ukiangalia katika kifungu cha 21 Muswada unaanzisha Mfuko wa Mafunzo ya Habari. Sasa kama Muswada unaanzisha Mfuko kwa ajili ya kumwendeleza mwandishi wa habari na tasnia ya habari, hivi unasimamaje mwanasiasa mwenzangu ukasema kwamba Muswada huu unakusudia kuua sekta ya habari au uhuru wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu cha 10 cha Muswada huu inaanzishwa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari. Katika kifungu cha 12 kazi za bodi hiyo zimeainishwa ambapo mojawapo ni kutoa ithibati kwa wanahabari, kusimamia kanuni na maadili za nidhamu miongoni mwa wanahabari na kusimamia viwango. Haya ni mambo ya kawaida kwenye taaluma mbalimbali. Hatujaanza na taaluma/tasnia ya habari kwani Bunge hili hili limeshapitisha kuwa na bodi kama hizi kwa Wahasibu (NBAA), tunayo Bodi ya Wahandisi, Bodi ya Wakadiriaji Majengo, Chombo cha Wanasheria, Baraza la Madaktari, Mafamasia, Wauguzi, Wakemia, hiyo ni mifano michache tu. Sasa kama taaluma nyingine zinasimamiwa kwa nini taaluma hii nayo isisimamiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nipingane na wale wenzangu wanaosema kwamba enzi hizo mtu alikuwa anaajiriwa kuwa mwandishi wa habari bila hata kusomea. Hivi jamani hii nchi baada ya miaka 50 bado tunataka tuendelee kuajiri bila kusomea, yaani mtu atoke chuoni leo aende akawe Mkurugenzi wa Habari Maelezo au mtu bila kusomea hata kidato cha sita hajafika unataka na yeye awe mwandishi wa habari bila cheti, kwa kweli hapana. Ni lazima tuzingatie viwango, lazima tuweke viwango, lazima tuondokane na makanjanja na lazima tuwape heshima wale ambao wamepoteza muda, rasilimali zao kwa ajili ya kujiendeleza katika tasnia hii ya habari, uwatofautishe na wale wanaoandika kwa mazoea tu, lazima tuweke madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukienda katika utumishi wa umma Serikali ilikuwa inaajiri darasa la saba, form four ambaye hana cheti hana chochote hata mimi mwenyewe nimeanza kazi mwaka 1992, fresh from school, form six nikaajiriwa kama PCA (Planning and Controller Assistant) cheo hicho hakipo. Kwa hiyo, tusilazimishe mambo ya miaka 20 leo tuendelee kuwa na watu wa aina hiyo. Enzi hizo wakati watu wanatoka Makerere Tanzania hatukuwa na Chuo cha Uandishi wa Habari hata kimoja chenye kutoa digrii, sasa hivi vimejaa, wasomi wamejaa bado tuendelee na watu wa darasa la saba kuwaita waandishi wa habari? Kwa kweli ni kuidhalilisha tasnia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Muswada huu narudia tena kusema kwamba una lengo la kuwasaidia waandishi wa habari. Katika kifungu cha 58 kinataka kila mwajiri kuweka bima na hifadhi ya jamii kwa kila mtu aliyeajiriwa katika chombo cha habari husika. Wenyewe ni mashahidi, tunao waandishi wetu wa habari wengine wanafikia mpaka kufariki amefanya kazi kwenye chombo zaidi ya miaka sita hana ajira, bima na hajalipiwa kwenye Mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii. Tunao waandishi wa habari wanapata ajali hawana hata bima, hawawezi hata kutibiwa, wengine mpaka wanapata ulemavu wa kudumu hakuna hata bima ya kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli napenda niipongeze Serikali yangu kwa kuliona hili na kuja na sheria inayowatetea waandishi wa habari. Kwa sababu ukisema awekewe bima na alipiwe hifadhi ya jamii ndiyo moja kwa moja unamaanisha kwamba huyu ni lazima atakuwa na mkataba unaoeleweka, unaomwezesha kulipwa mshahara unaojulikana na sehemu ya huo mshahara ukamlipie kwenye Hifadhi ya Mifuko ya Jamii. Kwa kweli nashangaa kusikia kwamba eti kwa kuwa na hiyo bima na kulipiwa hifadhi ya jamii unanyanyasa, unadidimiza sekta ya habari. Waswahili wanasema ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu katika kifungu cha 21 kama ambavyo nilisema kinaanzisha Mfuko wa Mafunzo ya Wanahabari ambao utaweza kutoa mafunzo kwa wanataaluma ya habari, kukuza programu za uendelezaji maudhui ya ndani ya nchi na kukuza na kuchangia utafiti wa maendeleo katika nyanja za habari na mawasiliano ya umma. Hivi Mwenyezi Mungu awape nini wanahabari? Mie kwa kweli nasema huu Muswada kwanza hatukutakiwa hata tuujadili kwa siku mbili, tungeweza kuujadili kwa siku moja, tukaumaliza ili wenzetu wanahabari nao wajione wako sawa na wanataaluma wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilishangaa sana namsikia mwanahabari anasema eti mnatutaka tuvae suti wakati tunaenda kuandika habari. Ndugu zanguni huu Muswada tunavyoandika au tunavyopitisha sheria lazima tuangalie na sheria nyingine za Kimataifa zinasemaje? Sisi kama nchi tunayo makubaliano mbalimbali ambayo tumeingia na mojawapo ni makubaliano ya Mkataba wa Geneva wa kuwalinda raia na waandishi wa habari katika operesheni mbalimbali au katika maeneo ya vita. Sasa utalindwaje kama hutofautiani na watu wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuvaa mavazi rasmi katika maeneo maalum ni kwa lengo la kuwalinda wanahabari wenyewe. Usiangalie leo unaandika katika mazingira ya amani, unaweza ukapelekwa Sudan huko ukafanye coverage, lakini kwa vile umeshazoea huku kwenu hakuna kuvaa uniform eneo lolote hata katika mazingira magumu utafika kule utachekesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili linalenga kuwalinda wenyewe waandishi wa habari katika mazingira maalum. Kwenye operesheni za polisi, kijeshi hivi wewe usipovaa vazi rasmi la kukutofautisha, siyo kwamba kila siku uwe umevaa hiyo sare lakini katika mazingira maalum, Serikali ina wajibu wa kukulinda mwandishi wa habari usidhurike. Sasa itakulindaje kama haiwezi kukutofautisha na vibaka wengine na wale ambao wamekusudiwa kwenda kufanya operesheni. Kwa hiyo, ili iweze kukutofautisha na wengine na iweze kukulinda ni lazima ikuweke katika vazi linalokutofautisha. Tunaposema vazi siyo lazima iwe uniform chini juu hata ukivaa reflector ni vazi maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Kamati yake pamoja na Uongozi wote wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo kwa kweli niliona nilizungumzie ni kwamba, kwa mtazamo wangu, Muswada huu unampunguzia sana Waziri mamlaka kuliko ambavyo watu wanafikiri. Kwa sababu zamani Waziri mwenyewe alikuwa anaweza kufungia magazeti, chombo cha habari, lakini kwa Muswada huu masuala karibu yote ya kitaaluma yatapelekwa kwenye bodi na Waziri atabaki na masuala machache tu yanayohusiana na uchochezi, amani au usalama wa nchi. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba Muswada huu unakusudia kukandamiza tasnia ya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe tu wenzetu, kama kweli tumekuja hapa kuwatetea wananchi wanyonge tuungane kuhakikisha kwamba Muswada huu unapita kwa sababu unawalinda sana waandishi wa habari. Hata hivyo, kama nyuma ya pazia kuna mtu ametutuma kuja kumtetea ili hao waandishi wa habari wasiolipwa mishahara, wasiokuwa na mikataba, wasiolipiwa bima waendelee kunyanyaswa, hebu mkae ninyi wenyewe mzungumze ndani ya nafsi yenu, mumwogope Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Haiwezekani mtu awe na chombo cha habari, ameajiri watu hawana mshahara, hawana bima anawalipa anavyotaka yeye.Kwa kweli huo siyo uhuru wa habari tunaoutaka, tunataka uhuru ambao pia unajali maslahi ya wale wanaoleta habari.
Mheshimiwa Sugu hata kama inauma vumilia, hata kama sindano imeingia imekuchoma vumilia ndiyo uanaume. Watakaposimama wanaume wenzako utafanyaje kama dada yako tu akisimama unatapatapa hivyo, mwanasiasa lazima uwe na ngozi ngumu, uwe na uwezo wa kusikiliza wenzako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ukiona mtu anapiga kelele ujue tayari imemgusa huyo na sindano imeingia. Ndiyo maana Chama cha Mapinduzi, chama kikomavu, mnazungumza, tunawasikiliza na tunagusa vifungu.
Ni kwa sababu tumesimama hapa kutetea wanyonge, waandishi wa habari lakini wengine hapa wanachofanya ni kuwaonyesha waliowatuma kwamba nilizungumza. Sisi tunawawakilisha wananchi, wanyonge, tusimame na tuzungumze kwa niaba ya wanyonge, tuache kutumiwa na matajiri wachache wenye vyombo vya habari ambao wanataka kuendelea kukandamiza waandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naona yanatosha, yamewaingia, wameelewa na nina imani Serikali yangu yale inayohitaji kuyafanyia kazi yamechukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.4), Bill, 2016

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwa haraka niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa na Mheshimiwa Rais pia Mheshimiwa Mbunge aliyeshinda katika mapambano makali kule Dimani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nikipongeze Chama changu cha Mapinduzi kwa kuchukua karibu Kata zote katika Uchaguzi ule wa Madiwani. Hiyo imeonesha kwamba sasa kazi imeanza na njia huko mbele ni nyeupe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niende kwenye muswada ambapo ninataka niangalie tu katika Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato (Income Tax Cap. 332).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sheria iliyokuwepo uamuzi wa kusamehe kodi ulikuwa mikononi mwa Waziri wa Fedha, katika marekebisho ambayo tunataka kuyafanya sasa hivi ni kwamba kwa ile miradi ambayo tunaona kwamba ni ya kimkakati na ina maslahi ya Kitaifa, basi maamuzi takwenda kufanywa katika Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina pingamizi lolote na hicho, lakini kimsingi maamuzi ya Baraza la Mawaziri hayawezi kupelekwa kwenye Kamati yoyote na hayawezi kuhojiwa na Kamati yoyote, kama ambavyo vile tulikuwa tunaweza kumhoji Waziri wa Fedha pale ambapo misamaha inaenda, au akivuka kile kiwango ambacho tulikuwa tunakitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni kwamba kwa kufanya katika Baraza la Mawaziri na tumesema kwamba tutaangalia miradi ile ambayo ni ya kimkakati, sasa ipi ni miradi ya kimkakati na ipi ina maslahi ya Kitaifa? Wasiwasi wangu ni kwamba inaweza ikaongeza wigo wa misamaha. Waswahili wanasema wasiwasi ni akili! Ni wasiwasi wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile maamuzi ya Baraza la Mawaziri hayawezi kuombwa kwenye Kamati na hayawezi kuhojiwa kwenye Kamati, nilikuwa napendekeza kwamba basi Baraza la Mawaziri lifanye mapema maamuzi yake kabla ya mwaka wa fedha au bajeti ya mwaka unaokwenda haijapitishwa ili yale yaweze kuingizwa katika Jedwali la Misamaha ya Kodi wakati wa kujadili pamoja na Finance Bill, ili kusiwe na mgongano na kusiwe na matatizo yoyote. Lakini tukisema wakati bajeti inaendelea, halafu ndiyo Baraza la Mawaziri lifanye maamuzi ya kutoa misamaha ya kodi katika hiyo miradi ambayo itaonekana kimsingi ni ya kimkakati, itakuwa kwa kweli kidogo kuna matatizo kwa sababu Kamati haitaweza kuhoji wala Baraza la Mawaziri halitaweza kuhoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nilikuwa nashauri, ninakubaliana na mapendekezo ya Serikali, lakini nilikuwa nashauri tu kwamba maamuzi ya kusema miradi ipi isamehewe, itakayowezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kwa maslahi ya Taifa yafanywe mapema kabla ya mwaka wa fedha haujafika na yajadiliwe pamoja na Finance Bill.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, sina matatizo nayo, ushauri wangu ulikuwa ni huo. Nimalizie tena kukipongeza Chama changu cha Mapinduzi kwa ushindi tuliojizolea.

The Finance Bill, 2017.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami napenda niungane na wenzangu kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada wa Sheria ya Fedha kwa Mwaka 2017. Kwa kweli sikuhitajika nisimame nichangie kwa sababu Wizara ya Fedha imechukua karibu zaidi ya asilimia 80 mapendekezo ya Wabunge na ya Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, isipokuwa nimesimama kuweka sawa baadhi ya mambo ambayo yanaonekana yanapotoshwa kwa makusudi kwa misingi ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa wa kirahisi rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza ambalo nataka nilisemee ni kuhusu kupata Miswada miwili. Wakati nawasilisha hotuba yangu nilisema kwamba Miswada hii huu wa pili ni matokeo ya mchakato mzima wa majadiliano yaliyoanzia kwenye Kamati za Kisekta, Kamati ya Bajeti na kupitia katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria zilizoongezwa kwanza ni Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kieletroniki. Sheria hii imependekezwa kupitia katika Kamati yangu, tukiomba suala la uuzaji wa share lisiishie kwa Watanzania peke yake, liende mpaka kwa watu wengine ili kuhakikisha kwamba tunavuta mitaji lakini tunachangamsha soko letu la mitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili wakati tunatoa hayo mapendekezo Mheshimiwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani alikuwepo na yeye ni miongoni mwa waliochangia, sasa sijui kwamba wakati tulivyokuwa tunaiomba Serikali tulitaka watuambie kwamba walichukue mpaka mwakani? Nilitegemea kwamba tupongeze kwa Serikali kuchukua yale ambayo tumeyapendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, tumependekeza ndani ya Bunge. Sheria ya Usalama Kazini tumelalamika kwamba kumekuwa na suala la ukaguzi wa mara kwa mara ni kero, ni usumbufu. Kama Waziri amekuja na Muswada ambao vitu hivyo havimo, Wabunge tumeomba, Serikali imekubali, imeongeza hizo sheria, badala ya kushukuru Serikali tunasema tumeshtukizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwahakikishia…

T A A R I F A ...

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu wakati tunajadili haya mambo mpaka tunaafikiana alikuwa ni mtoro, akiingia, anatoka. Kwa hiyo, hawezi akajua tulifikiaje katika marekebisho hayo. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwamba haya yaliyoletwa na Serikali kama ziada ni mapendekezo ya Kamati, ni mapendekezo ya Wajumbe, nami naipongeza sana Serikali, nampongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango kwa kupokea mapendekezo ya Kamati na kuyafanyia kazi na kuandika upya Muswada wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali isipokuwa wale wenzetu walipenda, kwamba yale tuliyomshauri Waziri wa Fedha asiyakubali ili waje walalamike kwamba Waziri huyu siyo msikivu. Sasa anakuwa msikivu wanalalamika, sijui tuwekwe wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo napenda nilichangie, sikuwa na sababu ya kuchangia kwa sababu bajeti ni nzuri. Suala la kusema kwamba tumeanza sera za ubaguzi ndani ya Bunge hili. Hakuna ubaguzi, tulichokiuliza na ambacho tunasimamia ni suala la kukaa zaidi ya miezi mitatu hapa tunaijadili bajeti, tunatoa mapendekezo, Serikali inayachukua, halafu mtu anakuja anasema siungi mkono, au anasema hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na njia tatu, ulikuwa na uwezo wa kusema hapana, ulikuwa na uwezo wa kusema ndiyo na ulikuwa na kusema sina maamuzi. Huna maamuzi kwa sababu yapo uliyoyakubali na yapo ambayo hujayakubali. Hakuna aliyesema kwamba hana maamuzi, badala yake wamesema wanakataa, sasa kama bajeti umeikataa…

T A A R I F A ...

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu napongeza pale napopongeza, nisipokubaliana na hilo ninatoa ushauri jinsi gani Serikali yangu ifanye na pale Serikali yangu inavyochukua ule ushauri wangu nilioutoa ndipo ninapokuja nasema naunga mkono Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wazima hivi au ile maana ya abstain watu hawakujua maana yake ndiyo maana hakuna hata mtu mmoja aliyesema abstain. Waswahili wanasema ukiligoroga lazima ulinywe, mmeikataa bajeti kwa hiyo madhara ya kukataa bajeti lazima yawafikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru naona sindano zangu zimeingia vizuri sana na ndiyo maana watu wote sasa wanashindwa, wanagugumia kama ambavyo watoto wakichomwa sindano wanalia. Poleni sana mwakani mjifunze jinsi ya kuunga mkono bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Yussuf Kaiza Makame

Chake Chake (CUF)

Contributions (3)

Profile

Hon. Hussein Ibrahim Makungu

House of Representatives (CCM)

Profile

View All MP's