Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Azza Hilal Hamad

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii, hongereni sana na nianze na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambapo katika ukurasa wa 113 anasema, naomba kunukuu; “Mikoa na Wilaya zenye maeneo tete ya chakula mwaka 2015/2016. Mkoa wa Shinyanga na Wilaya zake zote zilikuwa na hali mbaya ya chakula.”
Kwa taarifa hii tu ilikuwa inatosha kabisa kuona ndani ya kitabu cha bajeti cha Waziri, Shinyanga wameitizama kwa jicho gani. Kwa masikitiko makubwa baada ya miaka mfululizo Shinyanga kuwa na hali tete ya chakula hakuna mpango wowote ambao Serikali imeupanga kutuondoa katika hali hiyo. Ukiusoma ukurasa ule Mkoa wa Shinyanga na Wilaya na Majimbo yake yote hali ilikuwa tete. Nilitegemea basi katika bajeti hii ningeona kuna kitu tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa bajeti 2015/2016, Wabunge wote wa Mkoa wa Shinyanga tuligomea bajeti ya Wizara ya Kilimo na Waziri aliposimama kujibu alisema kuwa Wizara itatekeleza ahadi aliyoitoa aliyekuwa Waziri Mkuu kwenye ziara yake Wilaya ya Kahama kwamba Wilaya ya Kahama itakuwa Wilaya ya kimkakati kuuokoa Mkoa wa Shinyanga kwa kilimo kwa sababu ndiyo Wilaya pekee inayopata mvua za kutosha. Nilitegemea kuona Wilaya ya Kahama kuna jambo limefanyika, sijaona kitu chochote.
Naomba Waziri utakaposimama kuhitimisha uniambie ile ahadi iliyotolewa kwenye bajeti mwaka 2015/2016 ya kuifanya Wilaya ya Kahama kuwa ni Wilaya ya kimkakati kwa ajili ya kilimo kuokoa Mkoa wa Shinyanga iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii hii ya Kilimo, nilitegemea basi, Mikoa kama Mkoa wa Shinyanga ambao tunategemea maji ya juu, ningeona kuna bajeti ambayo imetengwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Sijaona hata Wilaya moja kwamba tunajikwamuaje na kilimo hiki kutoka kutegemea maji ya juu na kuwa tunavuna maji; sijaona ni wapi walipoonesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kwa mara nyingine naiamini Serikali yangu, hebu naomba muutazame Mkoa wa Shinyanga kwa macho mawili. Hatuwezi kuwa tunasoma kwenye vitabu tu, lakini utekelezaji hauonekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, katika Mabwawa ya Umwagiliaji, kuna bwawa ambalo lilikamilika mwaka 2015, Bwawa la Ishololo katika Jimbo la Solwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga; lakini nasikitika kusema bwawa lile sasa hivi limeshakatika, maji yote yametoka. Kwa hiyo, kwa mwaka huu bwawa lile hatujavuna maji. Sasa hawa wakulima tunaotegemea kwamba tumewatengenezea bwawa na hatimaye waweze kulima kwa umwagiliaji, bwawa hili limekatika na maji yote yametoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kusema kwa mara nyingine, nilishasema tuna miradi mingi ya umwagiliaji, naomba tuitengenezee mikakati miradi hii iweze kuhifadhi maji kwa wingi ili tuwe na kilimo chenye tija. Naomba nipate maelezo, miradi yetu ya umwagiliaji kwa nchi nzima, Wizara ya Kilimo mmejipanga vipi kuhakikisha miradi hii inavuna maji ya kutosha na kuwa na kilimo cha umwagiliaji chenye uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na Mikoa au Wilaya ambazo hazina mvua za kutosha isiwe sababu ya kutuadhibu tunaotoka katika maeneo yale, kwa sababu inavyoonekana wale wanaopata mvua mara mbili kwa mwaka ndio pia wanaotengewa fedha nyingi katika mradi wa kilimo. Naomba mtutazame, mwone tunawezeje kutoka hapo tulipo na kuweze kuwa na chakula cha kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye mifugo. Nasikitika kwa mara nyingine, Mkoa wa Shinyanga tulikuwa na Kiwanda cha Kusindika Nyama. Kiwanda hiki mpaka leo hakifanyi kazi, kiwanda hiki kilibinafsishwa. Mheshimiwa Waziri naomba uniambie, toka mlipobinafsisha kiwanda hiki, mpaka sasa hivi kuna hatua gani? Maana zimekuwa ni hadithi. Kitaanza kazi mwezi ujao, kitaanza kazi kesho kutwa, hatuoni kazi inayofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Shinyanga tuna ng‟ombe wa kutosha, lakini ng‟ombe hawa wamekuwa wakinunuliwa kwa bei ya chini kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, hali ambayo inawafanya wafugaji wetu kutokufuga kwa ubora na kupata fedha ambayo haistahili kwa mifugo yao. Mimi nadhani ni muda muafaka sasa, tuangalie kwa maeneo ya wafugaji, basi viwepo viwanda ili mifugo hii iweze kuwa na thamani. Nilikwishawahi kusema, hata kwenye minada ambako ng‟ombe zetu zinanunuliwa, basi kuwepo na utaratibu wa kuweza kuuza mifugo hii iwe na thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huo naomba basi na naishauri Serikali angalau ng‟ombe hawa wawe wanapimwa kwa kilo ili wafugaji waweze kunufaika na kuuza ng‟ombe hao wapate faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa mifugo, katika hotuba ya Waziri sijaona popote ambapo kuna mabwawa au malambo ya kunyweshea mifugo yetu katika Mkoa wa Shinyanga. Ninapata shida, tunapowaambia wafugaji wasihame, tumewaandalia mazingira gani ya kuweza kukaa na hii mifugo ili wasiweze kuhama? Naomba Waziri aniambie, tunapotoa tamko wafugaji wasihame, ni mazingira gani tuliyowawekea ili wasiendelee kutangatanga na mifugo hii? Naomba sana mniambie, kwa Mkoa wa Shinyanga ni malambo mangapi ambayo mmepanga na ni mabwawa mangapi kwa ajili ya wafugaji? (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, naendelea kujikita katika Mkoa wangu wa Shinyanga. Katika hotuba ya Waziri na katika Kitabu cha Maendeleo pia. Nilijaribu kutazama hata viwanda vya kutengeneza/vya kuchakata ngozi, Mkoa wa Shinyanga hatuna hata kimoja. Sasa sijui mmetuweka katika fungu gani. Naomba myatazame muone kama kweli mnatutendea haki au kuna jambo gani la ziada ambalo mnaona litastahili kwetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema mvua za mwaka huu zimekwa ni nyingi, za kutosha lakini haitoshi kuwa na mvua nyingi, hatukuwa na miundombinu ya kujiandaa ili mvua zile ziwe na tija kwetu. Kwa kiasi kikubwa mazao mengi yameharibiwa na mvua, maji mengi tuliyoyapata yamepotea bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali na kuishauri, hebu kakaeni mjipange vizuri, hatuna sababu ya kuwa tunayapoteza maji haya bure, tutafute namna ya kuyahifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Kilimo itoe tamko. Pamoja na chakula kidogo walichokipata wananchi wetu, kuna wafanyabiashara ambao wanatoka nje wanakwenda mpaka mashambani kununua zao la mpunga kwa wakulima wetu. Wananunua mpunga ambao hata haujavunwa kwa bei ya kutupwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inakatisha tama! Wananchi wetu wanauza kwa sababu wana shida. Yote hii ni kwa sababu soko la mchele limekuwa likishuka mara kwa mara na hivyo mpunga wao umekuwa ukinunuliwa kwa bei ya chini, kwa bei ya kutupwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi niseme ni mkulima wa mpunga, kwa hiyo hili ninalolisema nalitambua vizuri na inanisikitisha sana kuona wakulima wenzangu wananunuliwa zao lao likiwa shambani kwa bei ambayo ni ndogo, baada ya miezi miwili watakuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa haraka haraka, naomba niungane na Mheshimiwa Bura kusema kwamba Wizara ya TAMISEMI siyo rafiki kwa Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Wabunge wenzangu, katika kitabu cha TAMISEMI hiki chenye majedwali kina kurasa 81, lakini kuanzia ukurasa wa 33 mpaka wa 81 wanaongelea elimu. Naomba Kamati ya Bajeti ikakae tujue hatma ya Wizara ya Afya ipo wapi kwenye ujenzi wa vituo vya afya na zahanati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye vifo vya mama na mtoto; taarifa inasema wanawake 42 kila siku wanakufa au wanapoteza maisha. Kwa nini wanapoteza maisha? Wanawake hawa wanapoteza maisha kwa sababu vituo vyetu vya afya havina majengo ya upasuaji, havina damu ya kuwaongeza akinamama hawa; akinamama wanapoteza maisha kwa kumwaga damu nyingi na kwa kukosa huduma ya upasuaji. Ndiyo maana nasema, naomba Kamati ya Bajeti ikakae tujue, waje na mpango wa kuhakikisha kwamba vituo vyote vya afya hata kwa kuanzia kila Jimbo tuambiwe watajenga vituo vingapi vya upasuaji katika vituo vyetu vya afya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kufanya hivyo, Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake, nawapenda sana, lakini nawaambia hawatafanya kazi vizuri kwa hilo kwa sababu vifo vitaendelea kuwepo na suluhu yake ni kuwepo kwa majengo ya upasuaji na upatikanaji wa damu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika Mkoa wangu wa Shinyanga. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inatakiwa kuwa na watumishi 680, lakini mpaka hivi ninaposimama hapa ina watumishi 341, ina upungufu wa watumishi 155, hiyo ni Hospitali ya Rufaa, lakini ina Madaktari Bingwa watatu tu, ina upungufu wa Madaktari 24. Katika upungufu wa Madaktari waliopo, hatuna Daktari Bingwa mwanamke hata mmoja! Hatuna Daktari Bingwa wa upasuaji hata mmoja! Naomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Mkoa wa Shinyanga uliomba shilingi bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa lakini mmetupa shilingi bilioni moja tu. Hivi kweli kuna dhamira ya dhati ya ujenzi wa hospitali hii? Tunategemea hospitali hii tunaijenga kwa shilingi bilioni moja? Hili halikubaliki! Naomba kama Serikali imedhamiria kweli kujenga Hospitali za Rufaa, basi wahakikishe wanatoa fedha ya kutosha, lakini siyo pesa kiduchu ambayo wanatupa, haiwezi kutufikisha popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naendelea katika Mkoa wangu wa Shinyanga. Duka la MSD katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga mpaka sasa hivi tunavyoongea halipo. Naiomba sana Wizara, nimwombe Mheshimiwa Waziri, amefika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga lakini sijui hili wanaliwekaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la dawa ni kubwa, ukienda pale Manispaa ya Shinyanga hata kwa wale wenye Bima ya Afya, ni maduka mawili tu ambayo wanatoa huduma hii. Sasa linakuwa ni tatizo kubwa na inafika mahali watu hawaoni sababu ya kuwa na Bima ya Afya, kwa sababu hata wanapokwenda kutafuta dawa, hawazipati. Naiomba Serikali iende ikafungue duka. Naomba MSD waende wakafungue duka pale Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa sababu asiyeshukuru kwa kidogo, hata kwa kikubwa pia hawezi kushukuru. Naipongeza kwa nini? Naipongeza kwa sababu Bunge lililopita kila siku tulikuwa tunaimba humu ndani, MSD wanadai, lakini bajeti ya mwaka huu imeonyesha dhamira ya dhati ya kulipa deni la MSD. Kwa hiyo, niseme nawapongeza sana, naomba mkalipe fedha hizo haraka iwezekanavyo, nina hakika tatizo la dawa kwa kiasi fulani litapungua.
Kwa hiyo, nawaomba sana madawa haya yaweze kupatikana. Vile vile naomba sana tunapokuwa…

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote. Amenipa afya njema na hatimaye kusimama katika Bunge lako Tukufu. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika bajeti hii, natumia fursa hii kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuniamini kwa mara nyingine kuweza kuwatumikia. Nawaahidi sitowaangusha kama kawaida yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli. Mheshimiwa Rais hongera sana pamoja na Baraza lako la Mawaziri, chapeni kazi, tuko bega kwa bega na ninyi mpaka kieleweke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika hotuba ya Waziri wa TAMISEMI. Ukurasa wa 65 anasema ujenzi wa miundombinu ya Mikoa na Wilaya mpya. Baada ya kusoma hotuba ya Waziri wa TAMISEMI nimesikitika sana kwa sababu maeneo ambayo yanatazamwa ni maeneo mapya ya utawala, wakati kuna maeneo yaliyopo ya zamani hayana miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni Halmashauri mama kwa Mkoa wa Shinyanga, ni Halmashauri ambayo imezaa Wilaya zote na Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga. Hivi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga iko ndani ya Manispaa ya Shinyanga, majengo yake yako ndani ya Manispaa ya Shinyanga. Halmashauri za Wilaya ya Shinyanga ina Tarafa tatu, Kata 26, Vijiji 126, ina watu laki 355,930.
Mheshimiwa Naibu Spika, lilitoka agizo kwa Mkuu wa Mkoa kwamba tunapaswa kuhamia kwenye maeneo yetu ya utawala, tusifanyie vikao Manispaa ya Shinyanga. Kinachonishangaza unapotuambia tuhamie kwenye maeneo yetu ya utawala hatuna chumba hata kimoja cha ofisi, vikao vyote vya Baraza la Madiwani kwa sasa hivi vimehamia eneo moja la Iselamagazi ambapo ndiyo tulitenga kuwa Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanyia wapi vikao vyetu? Tunafanyia kwenye majengo ambayo ni ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Inasikitisha na inakatisha tamaa, kama tunasema tunataka kupunguza matumizi, unapunguzaje matumizi kwa kuondoa gari za Halmashauri zaidi ya sita kutoka Manispaa ya Shinyanga halafu zikafanye vikao zaidi ya kilometa 80, hayo matumizi unayapunguzia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri wa TAMISEMI aliangalie hilo. Hoja siyo kuangalia maeneo mapya, angalieni na maeneo ambayo ni ya muda mrefu ambayo yanahitaji miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisema hilo, naomba sasa nijielekeze upande wa afya. Nimepitia bajeti yote ya TAMISEMI katika vitabu vyote lakini sijaona, Mkoa wa Shinyanga tuna ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, sijaona tumepangiwa kiasi gani cha fedha. Siku zote nimekuwa nikisimama humu ndani nasema hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ina msongamano mkubwa wa wagonjwa, ukizingatia Wilaya zetu zote hazina hospitali za Wilaya isipokuwa Wilaya ya Kahama. Nilitegemea basi katika bajeti hii nitaona bajeti ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, lakini sijaona! Kama ipo naomba Waziri uniambie iko wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini gharama yake ni zaidi ya bilioni 10. Toka ujenzi huu umeanzishwa kwa nguvu za wananchi, Serikali imechangia milioni 270 tu mpaka hivi tunavyoongea, bado mnatuambia turudi kwenye maeneo yetu ya kazi, tunarudi kwenda kufanya kazi gani wakati hata miundombinu haituruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea nini iwapo hospitali hizi hatujazikamilisha, bado naendelea kusema hospitali ya Mkoa wa Shinyanga itakuwa na mrundikano wa wagonjwa kwa sababu hatuzitazami Wilaya zetu, miundombinu yake ikoje na wale ambao wameanzisha ujenzi wa hospitali hizi hamjatutengea fedha hata kidogo. Inasikitisha, naomba mtutazame Mkoa wa Shinyanga na mtazame Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, imeanzisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Kwa sasa hivi taratibu imeanza kufanya kazi lakini kuna baadhi ya majengo hayajakamilika na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imeomba ombi maalum la shilingi milioni 600 angalau kujaribu kusogeza tu zile huduma, sijui ombi hilo mpaka sasa hivi limefikia wapi? Hiyo yote ni kujaribu kuondoa msongamano mkubwa uliopo katika hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Naiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri namwomba sana atutazame kwa jicho la huruma Mkoa wa Shinyanga kwa sababu hatuwatendei haki wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yanayotakiwa katika hospitali ya Wilaya ya Kishapu ni bilioni tatu, lakini tumeomba milioni 600, sijui imefikia wapi, nitaomba majibu Waziri utakapokuwa umesimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuishauri Serikali, huu utaratibu wa kila mwaka kuanzisha majengo mapya kama Wilaya imeanza mpya, Halmashauri mpya, mnaanzisha majengo, hebu tuusitishe, tumalize kwanza miradi iliyopo. Hakuna sababu ya kila siku kuanzisha miradi wakati tuna magofu mengi hayajakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila ninaposimama humu ndani huwa nasema, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga tuna zaidi ya zahanati 28 ambazo tumeanza kujenga ambazo hazijakamilika. Tuna zaidi ya vituo vya afya nane ambavyo havijakamilika, sijaona kwenye bajeti hii tunafanya nini. Niombe tusianzishe miradi mipya, tukamilishe kwanza ile iliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa watumishi katika Wizara ya Afya. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mahitaji yake katika watumishi wa afya ni 726, watumishi waliopo ni 227, upungufu ni 499. Tunategemea watu hawa wanafanya kazi kwa kiasi gani? Nawaomba sana tuangalieni muweze kutuongezea watumishi ambapo tuna upungufu mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekee upande wa maji. Nasikitika sana Bunge lililopita la mwezi wa Pili Mheshimiwa Naibu Waziri Suleiman Jafo alijibu swali langu la Mradi wa Maji wa Mji Mdogo wa Tinde, alisema ndani ya Bunge kufikia mwezi wa Nne Mradi wa Maji wa Mji Mdogo wa Tinde utakuwa umekwishaanza kufanya kazi, lakini mpaka hivi ninavyoongea hapa mradi haujakamilika na SHIWASA hawajapewa fedha ambayo ilikuwa imebaki. Nawaomba sana mtakaposimama kujibu, Waziri wa Fedha aniambie ni kitu gani ambacho kimesababisha mradi huu ulikuwa ukamilike kutoka 2014 na mpaka leo ni milioni 100 tu inayosumbua ili mradi ukamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, nijielekeze katika mradi wa TASAF. Mradi wa TASAF wa awamu ya tatu ni mradi mzuri sana, kinachosikitisha Kamati zilizowekwa pamoja na baadhi ya watendaji wanautumia mradi huu kwa kudanganya, kuweka watu ambao hawastahili kupata ruzuku hii. Niombe ukafanyike uhakiki wa kila kaya kwa wale ambao wamechukua ruzuku hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niwashauri Serikali, Mheshimiwa dada yangu Kairuki, kwa sababu TASAF imeazimia kuwasaidia watu hawa upande wa afya, isiwe ombi, iwe ni sheria kwa watu wote wanaopewa ruzuku kutoka TASAF wakatiwe bima ya afya moja kwa moja na wasipewe zile pesa wapewe huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Subira upande wa Wabunge wa Viti Maalum. Imekuwa ni mazoea Wabunge wa Viti Maalum hawaruhusiwi kuingia kwenye Kamati za Fedha. Ukienda Halmashauri zingine wanaingia. Namwomba sana Waziri Mkuu atuangalie Wabunge wa Viti Maalum, mnatuogopa nini kuingia kwenye Kamati za Fedha? Kila unapokwenda Wabunge wa Viti Maalum hawaruhusiwi kuingia kwenye Kamati za Fedha, naomba sana Wabunge wa Viti Maalum turuhusiwe kuingia kwenye Kamati za Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwaomba Wenyeviti wa Vijiji waweze kulipwa posho ukizingatia asilimia 20 haifiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuuona mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nitumie fursa hii kuwatakiwa heri wale wote waliojaaliwa kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Wizara ya Fedha, Ofisi ya CAG, binafsi sioni kama tumeitendea haki Ofisi ya CAG kwa sababu pesa zote tunazozipeleka katika Halmashauri zetu bila kumuwezesha CAG hakuna tunachokifanya. Kwa sababu hatafanya kazi yake kwa uhakika, atafanya pale ambapo atakuwa amepafikia vinginevyo kama tunasema labda fedha hizi tunazozipeleka kule ziende zikaliwe na wale ambao wamezoea kula fedha za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisema hilo naomba nisemee mafao ya Wabunge. Mbunge ninakatwa kodi kila mwezi shilingi 1,063,000; inanishangaza sana kuona mafao yangu ya mwisho ninakwenda tena kukatwa kodi. Wakati ninapomaliza Ubunge mimi silipwi tena ile pensheni wanayolipwa watumishi wengine. Nimuombe Waziri wa Fedha atakapokuja hapa atuambie ni kwa nini na kwa nini iwe kwa Wabunge tu na kwa nini iwe ni mwaka huu? Kwa hilo Waziri wa Fedha naomba utupe mchanganuo mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninajikita zaidi leo katika hotuba ya Waziri wa Fedha ukurasa wake wa 30 mpaka ukurasa wa 31.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kusema Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tulisema kwenye majukwaa tutajenga vituo vya afya kila kata na tutajenga zahanati kila kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikichukua kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha hotuba yake ukurasa wa 31 naomba nimnukuu anasema; “Tutaimarisha mifumo, majengo na miundombinu mingine katika shule za awali, shule za misingi, za sekondari, upanuzi wa vyuo vikuu, ukarabati, ujenzi wa vyuo vya elimu ya juu, upanuzi wa vyuo vya ufundi, miradi ya kuboresha Hospitali za Rufaa, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Magonjwa Kuambukiza Kibong’oto na kuanzisha programu ya kuzalisha ajira na programu ya maendeleo ya ujuzi, mazingira na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sehemu yoyote ambayo ametuambia upande wa afya tunakwendaje kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya kujenga kituo cha afya kwa kila kata, hakuna kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya. Haitoshi kwenye Wizara ya TAMISEMI nilichangia nikasema hakuna sehemu yoyote ambapo TAMISEMI wameonesha kwamba ni wapi tunakwenda kutekeleza ujenzi wa vituo vya afya na zahanati katika vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamtaka Waziri aniambie, tunaposema tunakwenda kujenga vituo vya afya, tunategemea Halmashauri ikajenge vituo vya afya kwa mapato ya ndani? Halmashauri inayokusanya milioni 300 itakwenda kujenga vituo vya afya kwenye Kata zake? Hili haliwezekani! Sijui ni kwa nini Serikali yote kuanzia TAMISEMI mpaka Waziri wa fedha hawakuitizama Wizara ya Afya.
Mheshimwia Naibu Spika, tunaposema tunataka vituo vya afya kila kata. Tuna kata 3,963, vituo vilivyopo vya Serikali ni vituo 497 tu ambavyo vinatoa huduma ya afya na vituo hivi havijakamilika. Katika vituo 497 vinavyotoa huduma, ni vituo 106 tu vinavyotoa huduma ya upasuaji, sasa tunapokwenda kusema, tunataka kuondoa vifo vya mama na mtoto, tunaviondoaje wakati vituo vyetu vya afya havina majengo ya upasuaji? Tunaposema tunaboresha afya kwa wananchi wetu, tunaboreshaje wakati hata vitu vilivyopo havijakamilika?
Naomba Waziri wa fedha atuambie kama kwa mwaka huu hakuna
kitu chochote kinafanyika katka ujenzi huu, nina hakika Halmashauri hatuwezi kujenga vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano tu; Wilaya ninayotoka tuna kata 26, unakwendaje kujenga vituo vya afya vyote kwa kutegemea mapato ya ndani? Hili Wizara ya Fedha waliangalie halijakaa vizuri kabisa, hatutakwenda kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Ninaomba atakaposimama, ajibu wamejipanga vipi kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga vituo vya afya kwa kila kata ili kuhakikisha kwamba tunapunguza au tunaondoa kabisa vifo vya mama na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vifo vya mama na mtoto vinatokea kwa sababu gani? ukienda kwenye Kituo cha afya, huduma ya upasuaji haipo, huduma ya damu salama haipo. Vifo vya Watoto vinatokea ni kwa sababu ya upungufu wa damu. Ukienda kwenye kituo cha afya, damu salama haipo. Tunasemaje tunatapunguza vifo vya mama na mtoto wakati majengo ya upasuaji na huduma ya damu salama haipo kwenye vituo vyetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali, badala ya kusema tunakwenda kujenga vituo vipya vya afya, tuvichukue hivi 497 ambavyo vipo na vinatoa huduma, tuhakikishe vinatoa huduma zote zinazostahili katika vituo vya afya, kuliko kwenda kuanzisha majengo mapya ya ujenzi ambao pia tunaacha yale ambayo yanatoa huduma na hayajakamilika. Hayajakamilika kwa sababu gani? Unakuta hakuma wodi ya mama, hakuna wodi ya watoto, hakuna wodi ya akina baba, hakuna wodi ya akina mama wala hakuna jengo la upasuaji. Kwa hiyo, niishauri Serikali iende ikakamilishe kwanza vile vituo 497 wahakikishe kila kituo kinapata jengo la upasuaji, ndipo hapo tutakaposema kwamba huduma ya afya sasa tunakwenda kuiboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, niende kwenye shilingi milioni 50 za kila kijiji. Imetengwa kwenye bajeti, asilimia sita tu ya asilimia 50 kwenye kila kijiji. Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015, tulisimama tukasema kila kijiji kitapata shilingi milioni 50. Tuna maswali mengi kwa wananchi wetu, nikitizama kwenye bajeti hii ni shilingi bilioni 59 tu ambazo zimetengwa kwenye bajeti hii ambayo ni sawa na asilimia sita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inanitia hofu kama tutakwenda kwa asilimia sita mwaka huu, ndani ya miaka mitano, tutakuwa hatujafikia lengo ambalo tumelikusudia kwa wananchi wetu. Niungane na Kamati, niishauri Serikali badala ya kutoa asilimia sita, itoe asilimia 20 kwa mwaka huu wa fedha. Tukijipanga kwa kutoa asilimia 20 kwa mwaka huu wa fedha, maana yake utatoa shilingi bilioni 196, ndani ya miaka mitano tutakwenda kuvifikia vijiji vyote tulivyonavyo, bila kufanya hivyo tutafikisha miaka mitano na hatutakuwa tumevifikia vijiji vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda bado unaniruhusu, naomba niongelee suala la maji. Tatizo la maji ni kubwa sana. Nimuombe Waziri wa Fedha, kuna miradi mingi ya muda mrefu ambayo bado inadai fedha, wakandarasi wanadai fedha. Hebu nendeni mkakamilishe miradi hiyo, walipwe wakandarasi hao na miradi iweze kufanya kazi. Nitoe mfano mdogo tu, kuna mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Tinde ambao mpaka leo haujakamilika kwa shilingi milioni 100 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninaunga mkono hoja.

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini naomba niseme ninaitwa Azza Hillal Hamad.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama ndani ya ukumbi wako kuweza kuchangia Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe kwa ruhusa yako, nitumie fursa hii kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki ambao wameondokewa na wapendwa wao katika ajali ya gari ya aina ya Noah iliyotokea tarehe 6 Novemba, siku ya Jumapili katka Mji mdogo wa Tinde poleni sana Mwenyezi Mungu awape subira niko pamoja na ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia katika Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Ukiangalia katika ukurasa wa 40 wa Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa mfuko wa wanawake na vijana asilimia kumi katika Halmashauri ambazo zimekafuliwa, tumekagua Halmashauri 164 katika Halmashauri 164, Halmashauri 112 hazikupeleka fedha ipasavyo katika mfuko wa wanawake na vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri 112 halmashauri 6 ziliagizwa na Kamati kuandika barua ya kuji-commit kulipa fedha hizo kabla ya tarehe 30 Septemba. Cha kusikitisha Halmashauri hizo mpaka hivi ninavyoongea au mpaka Kamati inaleta taarifa ndani ya Bunge hazijaleta barua hizo. Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Halmashauri ya Jiji la Tanga na Halmashauri ya Ruangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri hizo zilizokaguliwa kuna Halmashauri ambazo hazikuchangia kabisa hata shilingi moja kwa mwaka 2014/2015 ziko ukurasa wa 43. Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Halmashari ya Tunduru, Halmashauri ya Mpanda, Halmashauri ya Tunduma, Halmashauri ya Ludewa, Sengerema na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfuko wa wanawake na vijana umekuwa kama ni hisani kwa halmashauri. Watu wanafanya pale ambapo wanaona kwamba inafaa na Wakurugenzi wengi katika Kamati wamekuwa wakijibu kwamba wanatumia fedha hizi kwa sababu ya maagizo yanayotoka juu. Wengi wanasema wanatengeneza madawati, wamejengea maabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini fedha hizi zimekuwa kama shamba la bibi? Ni kwa sababu tu hakuna sheria ambayo ipo katika Halmashauri zetu inayowaelekeza Wakurugenzi kupeleka fedha hizi kwa wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukilisema kwa muda mrefu hili ni tatizo sugu kwa Halmashauri. Wanafanya hivi kwa sababu tu wanawake hawa na vijana hawawezi kwenda kwenye Halmashauri kudai haki yao kwa sababu haipo kisheria. Lakini kama Halmashauri inafikia kupewa maagizo na Kamati, kuandika barua ndani ya Kamati na Halmashauri inakaidi maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Halmashauri hizi haziheshimu wala hazitambui mamlaka zilizopo juu kwa maana ya kwamba waraka huu wa kupeleka mfuko wa akina mama na vijana asilimia kumi ulipelekwa kutoka TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe na niishauri Serikali kwa kuwa Halmashauri zimekuwa hazipeleki fedha hizi, ni vyema basi Serikali ikaleta Muswada wa Sheria wa Mfuko wa Wanawake na Vijana ili wanawake na vijana hawa ambao wako kule na wanakosa nafasi ya kupata mikopo katika mabenki kwa sababu ya masharti yaliyopo ya mabenki waweze kukopeshwa fedha hizi kama haki yao ya msingi. Vinginevyo tutabaki kulalamika lakini fedha hizi hawatazipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaishauri Serikali mlete muswada wa sheria kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana ili tuweze kuwakomboa wanawake na vijana waliopo kule majimboni kwetu. Katika taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Halmashauri pia ina tatizo sugu. Tatizo hili ni kwamba asilimia 20 ya vyanzo vya mapato zilivyofutwa Halmashauri haipeleki kwenye mitaa na vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia ukurasa wa 45 wa taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa utaona kuna Halmashauri ambazo tumezitolea mfano hazijapeleka kwa miaka mitatu mfululizo fedha za vijiji na mitaa. Halmashauri hizo ni Halmashuri ya Kilwa, Halmashauri ya Ngara, Halmashauri ya Hai, Halmashauri ya Rombo, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwauliza hata fedha hizi kisingizio ni hicho hicho; maagizo kutoka juu. Sasa najiuliza, kwa Halmashauri ambazo wanaweza kupeleka fedha hivi wao wanafanya nini kutengeneza madawati? Kama siyo kwamba ni uongozi mbovu uliopo katika Halmashauri hizi wanashindwa kukaa na kuamua watatengeneza vipi madawati wanakwenda kuchukuwa haki ambayo siyo ya kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatutaondoa tatizo la rushwa katika ofisi za Serikali za Mitaa katika ofisi za vijiji kwa sababu ofisi za Serikali za mitaa na ofisi za vijiji hawana nyenzo za kufanyia kazi. Ile haki yao ambayo wanatakiwa kuipata hawaipati; unakuta Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji na Mtaa, hana hata fedha ya kununua karatasi, unategemea nini kwa mwananchi aliyekwenda ana shida yake? Kama siyo kwamba ataombwa fedha ili aweze kukamilishiwa shida iliyompeleka ofisini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali badala ya fedha hizi kuzipeleka kwenye Halmashauri zetu na Halmashauri zinafanya ni shamba la bibi basi fedha hizi zipelekwe moja kwa moja katika vijiji na mitaa ziweze kuwafikia walengwa vinginevyo kila siku tutapiga kelele Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa hawawezi kupata haki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka nikitoka hapo niende, suala la Wakuu wa Idara na Vitengo kukaimu. Halmashauri nyingi zimekuwa zikikaimiwa nafasi hizi lakini cha kusikitisha wengine makuwa wakikaimu kwa muda mrefu na matokeo yake nafasi ile anakuja kupewa mtu mwingine, yeye aliyekaimu hapewi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Lameck Okambo Airo

Rorya (CCM)

Questions / Answers(4 / 0)

Contributions (1)

Profile

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sumbawanga Mjini (CCM)

Supplementary Questions / Answers (2 / 0)

Contributions (7)

Profile

Hon. Vicky Paschal Kamata

Special Seats (CCM)

Supplementary Questions / Answers (1 / 0)

Contributions (2)

Profile

Hon. Khamis Ali Vuai

Mkwajuni (CCM)

Profile

View All MP's