Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri pamoja na Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Antony Mavunde kwa kazi nzuri wanayofanya katika shughuli zao za kumsaidia Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kazi nzuri mnayofanya. Ni mwaka mmoja tu tangu mmeingia madarakani lakini mambo mnayofanya ni mazuri sana, uchumi wa nchi hii umeendelea kuwa mzuri hadi sasa hivi viashiria vyote vya uchumi vinaonekana kwamba tunafanya vizuri sana kwenye uchumi. Pato la Taifa limeendelea kukua hadi sasa hivi linaendelea kukua kwa asilimia saba na mmeweza kuu-contain mfumuko wa bei ukaendelea kukaa kwenye tarakimu moja. Vilevile ni furaha ilioje niliposikia kwamba Tanzania iko kati ya nchi sita the best in Africa ambao uchumi wao unakuwa kwa kiasi
kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mengi ya kujivunia, tumeambiwa TRA sasa hivi makusanyo yameongezeka kutoka kwenye shilingi bilioni 850 mpaka kwenye shilingi trilioni 1.2 ndiyo maana mmeweza kuyafanya mambo makubwa kama kununua ndege. Anayependa apende, asiyetaka
asitake lakini makubwa yanafanyika ndani ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mmeweza kuwa mnapeleka shilingi bilioni 18.77 kwenye shule kwa ajili ya elimu bure kila mwezi, hongereni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia kwamba mabenki yako salama, mitaji na ukwasi upo wa kutosha. Hapa nina wasiwasi kidogo kwa sababu tukienda kule chini, tukienda mijini na vijijini tunaona kwamba mabenki ya biashara
yamepunguza kutoa mikopo. Tunahamasisha wajasiriamali wengi wajitokeze wafanye shughuli mbalimbali, wafanye shughuli za kilimo, biashara ndogo ndogo, tunahamasisha wananchi waanzishe viwanda vidogo na vikubwa, hivi kama mabenki hayatoi mikopo hawa mitaji watapata wapi? Niombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie ili Serikali sasa iweke mpango wa makusudi wa kuziwezesha hizi benki ili zianze kutoa mikopo kama walivyokuwa wanatoa kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo waliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita kwenye suala la kahawa. Kahawa ni zao la muhimu sana katika nchi yetu ya Tanzania, lakini lina umuhimu wa pekee kwa sababu tunaliuza nje linatuletea fedha za kigeni. Bei ya kahawa imeendelea kuwa chini kiasi ambacho inakatisha tamaa na ukilinganisha bei ya kahawa ya Tanzania na nchi jirani ya Uganda unakuta bei ya kahawa ya Uganda iko juu pamoja na kwamba nchi hizi zimepakana, ndiyo kitu kinachoshawishi watu wauze kahawa ya magendo kuitoa Tanzania kuipeleka Uganda. Bei ya kahawa kuwa chini ni kwa sababu bei ya kahawa ya Tanzania imegubikwa na tozo nyingi, ada nyingi, kodi nyingi. Wataalam wanasema hizi kodi na tozo zinafikia hadi 26. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, kuna kodi na tozo za zimamoto, OSHA, land rent, crop cess pamoja na kwamba sheria inasema crop cess inaweza kuwa kati ya asilimia tatu mpaka tano, sisi halmashauri zinatoza maximum, five percent. Kuna income tax, cooperate tax, VAT kwenye inputs zote zinazoingaia kwenye kahawa, research cess, Coffee Development Fund ambapo hela zinakatwa kwenye kila kilo, lakini sijawahi kuona huu mfuko unakwenda kumuendeleza au kuendeleza kilimo cha kahawa. Kuna labour charge, service levy, property tax, coffee bags duties, coffee industry licence et cetera mpaka zinafika 26.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo hizi ziko kwenye ngazi mbalimbali za uzalishaji pamoja na pale wanapouza nje. Ukienda pale mkulima anapouza kahawa kwenye chama cha msingi, kwenye chama kikuu cha ushirika, kule kwenye mnada Moshi ambapo wana-export kahawa kote kuna tozo kila mahali, lakini mzigo mzima anaubeba mkulima. Tozo hizi ndiyo zinasababisha bei ya kahawa inakuwa chini sana. Kwa msimu huu Mheshimiwa Waziri Mkuu, bei ya kahawa kwa Mkoa wa Kagera ni shilingi1,300, mtu anatunza ule mbuni kwa miezi tisa anapalilia, anakatia na kadhalika lakini anakuja kuishia kupata kati ya shilingi 1,100 na shilingi 1,300.
Mheshimiwa Mwenyekti, tukijilinganisha na nchi jirani ambazo ni washindani wetu katika hili zao la kahawa kama Ethiopia wao wanakata 0.04% kama exchange rate sale price, Uganda wanakatwa 1% export levy, Kenya wanakata 3% tu kwa ajili ya cess, lakini Tanzania tuna different cess’s, licence fees, taxes na tozo mbalimbali zinazofikia zaidi ya 26 na kuifanya hiyo bei iwe chini sana na kuwafanya wakulima wa
kahawa wakate tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya mambo mazuri sana kwenye korosho, tumemuona. Ameweza kuifanya bei ya korosho ikapanda kutoka kwenye kilo moja shilingi 1,200 mpaka shilingi 3,800. Tumuombe chondechonde, mimi kama mwakilishi wa wakulima wa Mkoa wa Kagera na nyuma yangu wakiwa Wabunge wote wa Mkoa wa Kagera, tunamuomba hebu aangalie kwenye hili zao la kahawa, watu wamelia ni kilio cha siku nyingi. Hebu aangalie tunatoa ada, tozo na fees gani ili kumwezesha huyu mkulima na yeye mwenyewe aweze kufaidi jasho lake aweze kupata bei ya juu ili angalau kilo moja isiteremke chini ya shilingi 3,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati namalizia, unakumbuka kwamba watu wa Mkoa wa Kagera na Mwanza wanafanya biashara na Uganda kwa kupitia Ziwa Victoria. Meli ya Mv Bukoba ilizama, Victoria imezeeka inakarabatiwa kila kukicha lakini wafanyabiashara wanapata matatizo kwa sababu ili waweze kupeleka mazao yale ina… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.

The Chemist Professionals Bill, 2016

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya kwa kuleta muswada huu. Muswada huu ni muhimu sana kwa sababu wote tunajua umuhimu wa kemia katika maendeleo lakini vilevile teknolojia imepanuka sana kwa hiyo kuna changamoto nyingi zinazotokana na upanuzi huo therefore huu muswada umekuja kwa muda muafaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa muswada huu ni mkubwa, hii Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa ipo siku nyingi, lakini hawakuwa na sheria yao wenyewe, walikuwa wanatumia sheria za hapa na pale kukiwa na tatizo la mambo ya mazingira basi wanatumia Sheria ya Mazingira lakini kwa kutunga sheria hii sasa tutakuwa tumemuwezesha huyu Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa na sheria yake moja ambayo itaweza kuongeza ufanisi (principal legislation). Sheria hii ikishatungwa itaifanya maabara hii kuwa ya mwisho na ya rufaa. Hii itampa nafasi mtu ambaye hajaridhika na matokeo ambayo yametoka labda kwenye hizi maabara ndogo ndogo aweze kupata mahali ambapo anaweza akakata rufaa na akaweza kusikilizwa, kwenye maabara kama za TBS, TFDA basi kama mtu atakuwa hajaridhika huko anaweza kukata rufaa kwenye hiyo maabara. Hivyo basi, kifungu cha nne (4) kwenye Muswada huu kieleze wazi majukumu ya Mkemia Mkuu wa Serikali kusudi sasa kusiendelee kuwa na migongano ambayo ilikuwepo kati ya majukumu ya hii maabara pamoja na maabara zile ndogo ndogo zinazoshughulika na hayo mambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kifungu cha 10 kinazungumzia uteuzi wa Mkemia Mkuu na kinamtaka huyu atakayeteuliwa awe na shahada ya uzamili ya kemia au taaluma nyingine zinazofanana na hizo. Hata hivyo, tukumbuke sasa hivi vipo vyuo vingi, wengine degree tunapata tu kwenye internet, wengine tunapewa tu, ili kuondoa matatizo ambayo yanaweza kujitokeza tukakuta ameteuliwa mtu ambaye hana sifa zinazotakiwa hicho kipengele kiseme kwamba hiyo shahada ya uzamili iwe imetoka kwenye chuo kinachotambuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kifungu cha 16(4) kinachozungumzia usimamizi wa sampuli zinazopelekwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi, kinataka maabara isiwajibike kwa mabadiliko au muonekano wa sampuli utakaojitokeza wakati wa uchunguzi au hata baada ya uchunguzi.
Ndugu zangu, mkumbuke kwamba hii maabara itakuwa inapima kemikali, sumu, vinasaba, dawa za kulevya na sampuli za kesi za jinai, kwa hiyo, lazima tuwe waangalifu. Ikitokea mtendaji ambaye syo mwaminifu hiki kifungu cha 16(4) kinaweza kikatumika vibaya, ukakuta mtu unapeleka sampuli ukihisi kwamba ni sumu iende kupimwa ikapimwa lakini ukaambiwa kwamba hii haikuwa sumu ilikuwa ni chumvi au ukapeleka bhangi unakwenda kuangalia unakuta imeshakuwa mchicha. Kwa hiyo, napendekeza kwamba hicho kifungu kielezwe vizuri kusudi hao watu ambao siyo waaminifu wasiweze kukitumia vibaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku hizi wanaume wengi wanawapa wanawake mimba, lakini wanawakana watoto. Wengine wanawapa mimba wanafunzi, wanawatelekeza, watoto wa watu wanaishia kufukuzwa shule na kwa sababu hawawezi kupata kazi kwa hiyo watakuwa hawana kipato, wataendelea kuwa maskini na watoto wao wataendelea kuwa maskini. Pia wote tunaona ukatili kwa watoto unaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna takwimu zimetolewa juzi juzi na Dawati la Jinsia na Watoto katika Jeshi la Polisi ambapo wamebaini kwamba kwa mwaka huu tu tangu mwezi Januari mpaka Julai, watoto 2,571 wamebakwa. Je, wamebakwa na nani? Unaweza ukakuta hata mtu mwingine unaishi naye humo ndani ndiye mbakaji, lakini hujui. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwabaini wanaume wanaowakana watoto, wanawapa mimba wanawake lakini wanaogopa majukumu wanawakana watoto, kuwabaini wanaowapa wanafunzi mimba na kuwabaini hao wanaobaka watoto na kuwalawiti, Maabara hii ya Mkemia Mkuu wa Serikali inaweza ikatumika au itatumika kupima DNA ambayo itakuwa ni kipimo sahihi kuonesha ni nani amefanya tukio hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili watendaji wasije wakashawishiwa kwa rushwa kubwa au ndogo, napendekeza adhabu iongezeke ambayo iko kwenye kifungu cha 53. Adhabu kwenye kifungu hiki iongezeke ili isomeke kwamba fine isiwe chini ya shilingi milioni tano na kifungo kisiwe chini ya miezi kumi na mbili kusudi mtu aweze kupewa adhabu kubwa kufuatana na kosa atakalokuwa amelifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ipendekeze kwamba sheria hizi zikishapita basi kanuni zitungwe haraka sana kusudi hizi sheria ziweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijajitendea haki na nitakuwa sijawatendea haki wana Kagera, mimi kama Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kagera ambaye ni mwakilishi bila ya kulizungumzia hili ambalo limetokea Mkoani Kagera.
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kuwapa pole wenzangu wote ambao wako kule walioathirika kwa matatizo makubwa waliyoyapata ambayo yametokana na tetemeko la ardhi. Najua imetokea Kanda ya Ziwa lakini Mkoa wa Kagera umeathirika vibaya sana na hasa hasa Bukoba Mjini. Leo hii tumeambiwa watu 17 wameshafariki, tumesikia katika taarifa mbalimbali na kwamba watu zaidi ya 252 wamejeruhiwa, nyumba zaidi ya 840 zimeanguka, nyumba zaidi 1,264 zimepata nyufa kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie ukifika pale Bukoba Mjini utakuta karibu nyumba zote zina nyufa, Bukoba Vijijini nyumba nyingi zina nyufa, Misenyi, Muleba na kadhalika lakini vifaa vya ndani vimeharibika kwa kweli ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana na kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona umuhimu wa tatizo hili na akaamua kuahirisha ziara yake ili aweze kulishughulikia akiwa hapa hapa. Namshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa kwa upendo wake, kwa kuwajali watu na uharaka alioutumia kufika Bukoba kwenye site akaweza kuwafariji watu lakini akashiriki vilevile kwenye hatua za awali za mazishi. Niwapongeze viongozi wa Mkoa ambao wako kule kule, kuna Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Mstahiki Meya wa Manispaa, Madiwani, Kamati za Maafa wote hawalali sasa hivi kila mtu anahangaika afanye nini. Nimshukuru Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye yuko huko kwa sasa wanapanga mipango na kuangalia wanasaidiaje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru na Wabunge wa CCM na Wabunge wa Upinzani ambao wamekwenda kule…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba Serikali iongeze nguvu ya kuweza kupeleka vitu haraka kwa sababu watu wanalala nje na mvua zimeanza.

The Media Services Bill, 2016

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia muswada huu.
Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Nape, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Anastazia Wambura, kwa kuleta muswada huu mbele ya Bunge hili, muswada ambao umesubiriwa kwa muda mrefu sana. Naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Peter Serukamba kwa kuweza kujadili na kurekebisha muswada huu kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya muswada huu ni ndefu sana, ina zaidi ya miaka 20. Tumeelezwa hapa, kwa mara ya kwanza muswada huu uliletwa Bungeni mwaka 1993, lakini wanahabari wakalalamika kwamba walikuwa hawajashirikishwa vya kutosha na kwamba muswada huu ulikuwa unabana uhuru wa habari, kwa hiyo, ukaondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu ukaendelea kurekebishwa, ilipofika Machi, 2015 ukaletwa tena Bungeni, wanahabari wakalalamika kwamba hawajashirikishwa tena, lakini vilevile wakawa wanahoji, kwa nini umeletwa chini ya hati ya dharura, muswada ukaondolewa tena. Serikali ikaendelea kuurekebisha huu muswada, ilipofika mwaka huu mwezi wa nane, ikatangaza kwenye Gazeti la Serikali na ilipofika tarehe 16 Septemba, muswada huu ukasomwa mara ya kwanza humu Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mwezi mmoja, wadau wa habari wakaitwa mbele ya Kamati ili watoe maoni yao, wakasema hawana maoni kwa sababu muda umekuwa mfupi. Kamati ikawapa muda wa siku kumi zaidi. Baada ya siku kumi wengine wakaleta maoni lakini wengine wakaendelea kusema kwamba muda ulikuwa hautoshi wanataka mpaka Februari, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwa kweli mimi ilinishangaza sana kwa sababu, huu muswada umesubiriwa zaidi ya miaka 20 na hao hao wanahabari. Wanahabari wameendelea kulalamika kwamba Sheria ya Magazeti inawatesa, wamepata nafasi, muswada wenyewe wenzangu una kurasa 28 tu, mtu ambaye una interest na huu muswada utashindwaje kusoma kurasa 28 katika karibu siku 43 walizopewa ukajadili na ukaweza kutoa maoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo wale wale waliosema hawana maoni, wakawa wanaonekana kila siku kwenye vyombo vya habari, wanatoa maoni juu ya huu muswada kifungu kwa kifungu. Kwa sababu hii Kamati ilikuwa sikuvu, tukaendelea kuyasikiliza hata yaliyokuwa kwenye vyombo vya habari, na kwa kiwango kikubwa yote yameingizwa kwenye huu muswada ambao upo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye vifungu. Ukiangalia kifungu cha 7(1)(b)(iv), hiki kinaonekana bado kina ukakasi kwa sababu kinazungumzia wajibu na haki ya vyombo vya habari kwamba kutangaza na kuchapisha habari au muswada ambao ni muhimu kwa Taifa kwa kadri Serikali itakavyoelekeza.
Ndugu zangu, hapa Serikali inachosema ni kwamba ikitokea kwa mfano dharura, leo hii kimekuja kimbunga kama vimbunga tunavyoona huko Amerika, inatakiwa watu wa Dar es Salaam centre pale waondolewe na kupelekwa Kibaha, au ikitokea vita mahali popote hapa Tanzania, wanategemea kwamba vyombo vyote vya habari vitakuwa vinatangaza juu ya hiyo vita; kisije kikatokea chombo cha habari wakati huo kikaendelea na programu zake za kawaida na wengine wanatangaza burudani. Kwa wakati huo watatakiwa kutangaza kitu hicho muhimu ambacho ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 7(3) kinaipa ukuu hii sheria ambayo tunaitunga sasa. Ikitokea mgongano kati ya sheria hii na sheria yoyote ile, basi hii sheria ndiyo itatumika kuamulia huo mgongano. Mimi hiki nakiona kama ni kitu kizuri kwa sababu sheria ambayo inaweza kumtetea au kutetea chombo cha habari ni hii hapa. Kwa hiyo, naona ni vizuri kiendelee kuwemo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia vifungu vya 9, 17, 10, 50(4); Kifungu cha 9 kabla ya kurekebishwa kilikuwa kinampa Mkurugenzi wa Habari uwezo wa kukataa maombi ya kutoa leseni kwa yeyote ambaye hajatimiza vigezo au kufuta leseni kama mwenye leseni atakuwa hakuzingatia masharti.
Kifungu cha 17(1) kilikuwa kinatamka kwamba Waziri ndio mamlaka ya mwisho ya nidhamu, lakini kwa sasa kifungu cha 10 kinampa uwezo mhusika ambaye hajaridhika kwenda kukata rufaa mahakamani na akasikilizwa. Kwa hiyo, wale ambao wanajadili, tusipotoshe umma, hivyo vipengele vingine vilishafutwa au vilishaondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 56 kilimpa Mkurugenzi wa Habari au Afisa Polisi kutwaa kifaa kwa sababu kama angekuwa anaona kwamba chombo cha habari kinaendeshwa kinyume na sheria.
Kifungu cha 50(4) kilikuwa kinaruhusu mashine ya kupiga chapa iliyotumika kuchapa taarifa ya uchochezi kuchukuliwa au kuzuiliwa na Afisa wa Polisi kabla ya hata kusikilizwa. Hayo mambo yote yamefutwa tusiwadanganye Watanzania, hayapo tena kwenye muswada huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inaanzisha utaratibu, sheria hii imeweka mchakato, sheria imeweka hata na Kamati ya Malalamiko. Hivyo ukiangalia hata 56(2), wale waliokuwa wanaogopa kwamba Waziri ana mamlaka kubwa, anaweza kuamka asubuhi akafungia chombo chochote au gazeti lolote analolitaka, hayo hayapo kwa mujibu wa sheria hii tunayotunga, yote yameondolewa; kila mtu atapewa haki na mahakama. Kama hujaridhika na uamuzi wa Waziri unaweza kwenda ukakata rufaa kwenye mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 18 cha Muswada huu, kinaanzisha Bodi ya Ithibati ya Wanahabari na vilevile kifungu cha 23 kinaanzisha Baraza Huru la Wanahabari. Hii sasa maana yake ni nini? ni kwamba sasa tunakwenda kuifanya tasnia hii kuwa taaluma kamili. Sasa tunakwenda kuijengea taaluma hii heshima, tunakwenda kupunguza makanjanja ambao walikuwa wanaharibu tasnia hii kwa kuandika habari ambazo ziko substandard tukiweza kuweka Bodi pamoja na Baraza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 18 kinazungumzia juu ya ithibati ya wanahabari; mtu hataruhusiwa kufanya kazi ya habari kama hatakuwa amethibitishwa na utaratibu unaowekwa na sheria hii. Nimewasikiliza waliokuwa wanaongea na nimewashangaa sana. Wanataka kutuambia kwamba katika karne hii na baada ya sayansi na teknolojia iliyokuwa mpaka kiwango hiki, mtu yeyote anayejua kufunga kidonda, tumuite daktari; mtu yeyote yule ambaye amekwenda kwenye semina ya wiki moja, akirudi kwa sababu ilikuwa inahusu sheria awe mwanasheria; na mtu yeyote anayejua kushika kalamu na karatasi akaandika aitwe mwanahabari, haiwezekani. Hii Bodi ya Ithibati lazima iwepo na wanahabari wenyewe ndiyo kitu wanachokitaka, wanataka iwe taaluma, iheshimike ili na viwango vya mishahara yao viweze kufahamika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanapotosha, wanadanganya watu kwamba kuna kiwango cha elimu, kwamba mtu ambaye hana degree hawezi kuitwa mwanahabari. Hakuna mahali popote kwenye muswada huu yalipoandikwa hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii imetambua kwamba sasa tutakuwa na Bodi ya Ithibati, tutakuwa na Baraza Huru la Wanahabari; yote hii itakuwa na wanahabari ambao wamebobea. Watakaa chini, wataweka vigezo vya nani awe mwanahabari. Hivi vigezo vitawekwa kwenye kanuni kwa sababu ukiweka kwenye sheria, vikitakiwa kubadilishwa ni rahisi kubadilisha kanuni kuliko kubadilisha sheria.
Kwa hiyo, hivi vigezo vitawekwa kwenye kanuni. Hivyo jamani msiwadanganye watu, waache tuwaboreshee wawe na tasnia nzuri ambayo itakuwa inaheshimika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 11 kinazungumzia juu ya muundo wa bodi, hakijazingatia jinsia. Napendekeza waweke kifungu kidogo kimoja cha kuweza kuzingatia jinsia. Hebu angalia Wanahabari wote Waandamizi, karibu wote ni wanaume. Kwa hiyo, hiki kipengele kikiachwa hivi hivi unaweza ukakuta Bodi nzima ina watu wa jinsi moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, muswada huu ni mzuri, utaifanya tasnia hii kuheshimika, itakuwa ya kitaaluma, lakini kwa kupewa ithibati, kitawafanya wamiliki wa vyombo vya habari waweze kuwalipa wanahabari mshahara unaostahili na vilevile wataweza kuwakatia bima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, tumwombe Mheshimiwa Waziri baada ya sheria hii kuwa imesainiwa aharakishe kuandaa kanuni ili sheria hii ianze kutumika mara moja kwa sababu imesubiriwa kwa zaidi ya miaka 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's