Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

All Contributions

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA - MWENYEKITI KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi tena. Sitamaliza hiyo robo saa kwa sababu Kamati yangu wamechangia watu watatu; hapakuwa na maneno mengi sana. Nadhani hiyo ni kuonesha alama wanazoipa Kamati, nadhani zaidi ya asilimia 90 hawakuwa na mambo ya kusema. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wawili wamechangia humu ndani, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete na Mheshimiwa Dkt. Semesi. Mheshimiwa Juma Othman Hija alichangia kwa maandishi. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, yeye ametoa rai kwamba kila Mbunge ajiheshimu mwenyewe kwanza. Sisi tunakubaliana naye na ndiyo msimamo wa Kamati yangu kwamba kama hapa ndani kila mmoja atajiheshimu, nafikiri hata kazi ya Kamati hii itakuwa rahisi sana. (Makofi) Mheshimiwa Dkt. Semesi amependekeza Kamati iwe na Wajumbe 50 kwa 50. Nataka nimweleze kwamba Kamati hizi hapa ndani zinaundwa kulingana na uwiano wa Wabunge kwenye Vyama. Kamati zote zilizomo humu ndani kile Chama ambacho kina Wabunge wengi ndicho kina Wajumbe wengi. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Kamati zote zinategemea hiyo. Ukichambua hizi Kamati, ni yale yale ninayoyakemea kwamba kwa utaratibu wa humu ndani, kama mmoja anaongea, wewe unanyamaza. Nadhani ndiyo mnaona umuhimu wa Kamati yangu, kwamba wako watu ambao lazima tushughulike nao ili hapa ndani pawe shwari. (Kicheko/Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukitoka hapa, nenda kachambue Kamati yote, in reality, ratio iko 7:3 nenda Kamati zote. Kwa hiyo, siyo kwamba hii Kamati ya Maadili isan exception, hapana. Ndivyo ilivyo kwa muundo wa Kamati zote. La mwisho, niseme tu kwamba anayeunda hizi Kamati, sio Wajumbe wa Kamati, ni Mheshimiwa Spika. Mheshimiwa Mwenyekiti, watatu, ndugu yangu hapa, Mheshimiwa Juma Abdallah Juma, yeye amechangia kwa maandishi, anaipongeza kazi ya Kamati na anapendekeza kanuni ziangaliwe upya ili kuwabana wanaofanya fujo ndani ya Bunge. Ninachotaka kusema ni kwamba, Kamati ya Kanuni ndiyo inayotengeneza kanuni, sisi tunafanya kazi kwa kutumia kanuni zilizotengenezwa na Kamati ya Kanuni na kupitishwa na Bunge Zima. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimalizie tu kusema kwamba sisi kama Kamati ya Maadili, tunatoa rai na kama tulivyosema pale mwanzo, hapa ndani kuna maendeleo makubwa sana. Ukilinganisha vurugu zilizokuwepo mwanzoni wakati Bunge linaanza na tulivyo leo, yapo mabadiliko makubwa. Kwa mtu yeyote ambaye akili yake haina matatizo, anaelewa kwamba tumepiga hatua. Yule ambaye hataki kuelewa, mwache aendelee kutokutaka kuelewa kwa sababu ndiyo watu wengine walivyo, lakini hali ya hapa katika Bunge nadhani kwamba tumeanza kwenda vizuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimalizie... Mheshimiwa Mwenyekiti, si ndiyo haya haya ninayokemea? Mimi si ndiyo nimepewa nafasi hapa kusema? Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie kwa kusema hivi, tukiwa hapa ndani, naomba tuendelee kuheshimiana, kuvumiliana, kuzingatia kanuni, kuheshimu kiti na nimalizie kusema tu kwamba ukizomea wakati mwingine wanasema, haujajenga hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka leo tuondoke wote na msemo huu ambao katufundisha Baba yetu Mwalimu Nyerere. Alitufundisha hivi, argue, don’t shout. Tuondoke na spirit hiyo, Baba yetu katufundisha, “argue don’t shout.” Kama mwenzio anaongea, kapewa nafasi, nawe ghafla bin vup, unabonyeza unasema „nini wewe?” “Mambo gani hayo?” You are shouting. Argue, don’t shout. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba Bunge lako Tukufu likubali kuipokea taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge pamoja na mapendekezo yake ili yakubaliwe na kupitishwa na kuwa maazimio ya Bunge. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kusema na kwa sababu katika Bunge hili ni mara yangu ya kwanza kuzungumza. Nataka niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Newala Mjini kwa kunirejesha tena katika jengo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mengi ya kusema kabla sijaenda mbali. Nikiwa ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Klabu ya Yanga nataka kuipongeza klabu yangu ya Yanga kwa kuchukua ubingwa. Vijana wetu tunawapongeza, mmefanya yale tuliyowatuma mfanye, tunataka mfanye hivyo na nchi za nje pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza maraisi waliotokana na Chama changu kwa kushinda uchaguzi. Tupo awamu ya tano ya maraisi, na faraja niliyonayo kwamba wote waliopokezana vijiti wametoka Chama cha Mapinduzi.
Nampongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kushinda, nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, naipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais, Mabaraza ya Mawaziri yote ya Muungano na lile la Baraza la Mapinduzi Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna kazi moja tu ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri chapeni kazi. Ukimsikia mtu anakuambia mnakwenda kasi muulize nilipoapishwa niliambiwa niende speed gani? Kwa hiyo, mimi nataka kupongeza sana. Lakini wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. (Makofi)
Ndugu zangu uongozi wa nchi ni kupokezana. Kabla ya Magufuli tulikuwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kafanya mambo mengi nchi hii. Mimi nataka niwape mfano ambao ni my personal experience.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimaliza shule form four mwaka1967 wengi mlikuwa hamjazaliwa. Shule inaitwa St. Joseph College Chidya, nikapelekwa kwenda Ilboru, kwa sababu ya matatizo ya mawasiliano ya Mtwara na Arusha mimi nilikuwa natembea wiki nzima kwa gari katika barabara ya vumbi kutoka Newala, Nachingwea, Tunduru, Songea, Njombe, Iringa, Morogoro nikifika Chalinze napanda basi kwenda Arusha; wiki nzima niko njiani, hatukuwa na barabara ya lami. Akaja Mzee Mwinyi akatuanzishia daraja, Mzee Mkapa akatujengea daraja, Jakaya akatuwekea lami. Leo unatoka Newala kwa gari saa nane mchana na saa mbili jioni upo Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya kazi nzuri, ametuwekea sekondari kila kata, amejenga barabara za lami nchi hii, kama ilikuwa ni kushindana ndiye anayeongoza kwa kujenga barabara za lami nyingi kuliko waliomtangulia. Kigoma mlikuwa mnalalamika tupo gizani, ameondoa tatizo la umeme, amewawekea daraja mto Malagarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwanza tunampongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameiongoza nchi salama miaka kumi amemaliza, kijiti amemkabidhi Mheshimiwa John Pombe Magufuli, sasa sikilizeni kazi ya Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya miezi sita tu vijana wanasoma bure toka fstandard one mpaka form four, ndani ya miezi tu. Ndani ya miezi sita amesema ile Mahakama ya Ufisadi mliyokuwa mnaidai tarehe 01 mwezi Julai inaanza. Miezi sita bado…
(Hapa baadhi Wabunge walizungumza bila kutumia vipaza sauti)
Mtu mzima naongea mambo ya kuzomea zomea wakati hujaruhusiwa, mtu mzima anaongea. Mimi nilidhani mnawafanyia vijana wenzenu hata mimi size ya mzee wenu? (Makofi)
MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hii disturbance iliyotokea utaniongezea muda. (Makofi/Kicheko)
Kwa hiyo nasema nchi ipo salama. Ametoka Rais wa CCM amemkabidhi kijiti Rais wa CCM, ilani ya uchaguzi iliyokuwa inatekelezwa sasa Mheshimiwa John Pombe Magufuli amechukua pale alipoacha Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ndiyo maana nchi ipo shwari, haijashikwa na watu wababaishaji, imeshikwa na watu makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kusema hayo niseme mengine. Kwanza nataka niombe sana Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ana nia nzuri na nchi hii, Mawaziri wake wana nia nzuri na nchi hii, hebu tuwape ushirikiano ili Tanzania pawe mahala pazuri pa kuishi. Mbona kila nchi nje huko wanatupongeza? Wanawashangaeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kusema hayo nataka kwenda kwenye barabara. Nataka niishukuru Serikali yangu ya CCM Serikali sikivu, watu wa Mtwara tumeomba barabara ya lami kutoka Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi. Hotuba ya Waziri inasema bajeti ya mwaka huu kuanzia tarehe 1 Julai, 2016 barabara inajengwa. Naomba watu wa Tandahimba, Newala, Masasi, Mtwara, kazi mliyotutuma tumeifanya majibu ya Serikali ndio hayo, barabara itajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili barabara ya mkoa. Mheshimiwa Waziri Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mtwara tumeomba barabara ya mkoa kutoka Newala – Nyambe – Ndanda ichukuliwe na mkoa kwa sababu, watu wa Tandahimba na Newala Hospitali yetu ya Rufaa ni Ndanda. Tunaomba ombi hilo lichukuliwe barabara iwe ya mkoa ili iweze kutengenezwa vizuri kwa sababu, Halmashauri zetu uwezo umekuwa mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Newala tulikuwa na uwanja wa ndege ambao umetumika sana wakati wa vita vya Msumbiji. Bahati mbaya nyumba zimejengwa karibu sana mpaka uwanja wa ndege ule umefutwa, lakini Halmashauri imeomba ipewe barua rasmi ya kuufuta uwanja wa ndege wa Newala, hilo jambo halijafanyika, tunaomba lifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, Wilaya tumetafuta eneo la kuweka uwanja wa ndege, Waziri uliwatuma wataalam kuja kuona, wametuambia shughuli gani tufanye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba suala la ujenzi wa uwanja wa ndege Newala, utakapokuwa unajibu, watu waliozoea kuwa na uwanja wa ndege tangu enzi ya mkoloni sasa inapokuwa hatuna uwanja wa ndege tumerudi nyuma. Tutapenda kusikia kauli ya Serikali kuhusu lini mnaanza kujenga uwanja wa ndege wa Newala, lakini kwa hatua za awali tunaomba wale watu wafidiwe eneo lile mlichukue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Newala tuko mpakani na Mto Ruvuma; nimeona hapa hotuba kivuko hapa, kivuko hapa, sisi tuna mawasiliano ya karibu sana na Msumbiji. Kuna daraja kule la Umoja, kuna daraja la Kilambo, lakini Tandahimba na Newala pale tuna vivuko vingi na nafikiri ndio tunaingiliana zaidi na watu wa Msumbiji kwa sababu ya kupakana, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri, Wizara iangalie uwezekano wa kutuwekea kivuko katika Mto Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara inaitwa barabara ya Ulinzi, hii ni barabara inatoka Mtwara inaambaa ambaa kandokando ya Mto Ruvuma mpaka Tunduru mpaka mkoa wa Ruvuma. Barabara hii haijatengenezwa miaka yote na Serikali kuu, muda mrefu mmeaicha kuitengeneza, tunapata tabu kusomba korosho kwa sababu ya hali ya barabara na korosho za Mtwara nyingi zinatoka katika bonde la Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nilikuletea barua, bado uko mgeni Wizarani kwamba, vijiji vya bonde la Ruvuma Wilaya yangu ya Newala, hawana mawasiliano ya simu. Walikuwa wanatumia simu za Msumbiji ambazo dakika moja tu shilingi 1,000, lakini haraka haraka ulituma watu wako, watu wa Halotel wakaja, bonde la Ruvuma leo Halotel ni Halotel kweli kweli. Tatizo lile la watu wa Newala, watu wa Tandahimba kutumia simu za Msumbiji umetuondolea tuko ndani ya Halotel ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Waziri, mimi nataka nikushukuru sana kwa uharaka wako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru, lakini kwa kumalizia uwanja wa ndege wa Mtwara uwe uwanja wa Kimataifa wa Mtwara. Ninakushukuru.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa kuongoza Wizara hii, lakini nataka nikupe pole kwa kazi ngumu iliyoko mbele yako, kati ya wewe na wapiga kura wangu, wanaotegemea Mradi wa Maji Makonde, ambao upatikanaji wa maji badala ya kupanda umeporomoka. Tunapata maji asilimia 30 ukilinganisha na vijiji vingine au Wilaya zingine ambako wameshafika asilimia 65 vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea Waziri hoja yangu ni kwamba wala hatutaki Tandahimba, Newala Mtwara kunakofika huu mradi, hatutaki hela za kuendesha mradi, tunataka hela za kukarabati mradi ili kuongeza uzalishaji wa maji. Mchango wa wananchi wanaotegemea mradi huu kwa Serikali kila mwezi ni mdogo sana, kwa sababu maji mnayotuuzia ni kidogo sana, hatuna tatizo la kuchangia maji kwa sababu tangu tulivyoaanza Makonde Water Corperation tulikuwa tunanunua maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ujumbe wangu siyo kupitisha mafungu ya kuwezesha uendeshaji wa Mradi wa Maji Makonde, hoja leo hapa utakapokuwa unamalizia kesho kutwa, ueleze nini Wizara yako inafanya kuongeza uzalishaji maji kwa Mradi wa Maji Makonde. Mheshimiwa Waziri wewe umefika kule lakini nataka kukuomba, Naibu Waziri alikuja juzi wakati mvua inanyesha, watu wa Tandahimba, Newala ni hodari kwa kuvuna maji, kila nyumba ya bati utakayoiona tunachimba kisima, tunavuna maji ya mvua, mimi naishi kijiji kwangu, sina maji ya bomba katika nyumba yangu, nina visima viwili, napata maji ya shower na ya kunywa kwa sababu tunachimba visima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Tandahimba na Newala kama wangelitegemea tu maji ya bomba ya Serikali hali yetu ya maisha ingekuwa ngumu sana. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ninachoomba hapa siyo utueleze unafanya nini katika administration uendeshaji wa Mradi wa Maji Makonde, aaah aah! Utakapokuwa una- wind up utoe maelezo nini Wizara yako inafanya kuongeza uzalishaji wa maji katika Mradi wa Maji Makonde. Hiyo ndiyo hoja yangu, umri huu siyo wa kutoa shilingi, lakini kama hutatufikisha huko, kuna vijana wengine humu ndani wanategemea mradi huo huo mimi nitakaa pembeni huku nawapigia kwa chini chini (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Maji Makonde, Tatizo la maji Newala, Tandahimba ni kubwa kwa sababu ya jiografia, ile inaitwa Makonde plateau, niliposoma jiografia niliambiwa a plateau is arised flat peace of land. Plateau ni kitu gani, ni eneo ambalo limeinuka, na juu kuko flat ndivyo ilivyo uwanda wa Makonde ukija kwetu Tandahimba na Newala, ukienda Masasi, Mto Ruvuma, Lindi, Mtwara unateremka, ndiyo maana katika eneo la kwetu hatuna agenda visima vifupi haipo. The water table is so below unaweza ukachimba hata maili ngapi sijui, siku hizi mnatumia kilometa, unaweza ukachimba sijui kilomita ngapi hujapata maji, hatuna visima vifupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia hapa the oldest scheme ya maji ambayo inaendeshwa na Taifa ni Mradi wa Maji Makonde, lakini naona tumepewa shilingi bilioni mbili. Shilingi bilioni mbili upeleke maji Tandahimba yaende mpaka Mtwara, mradi mwingine wa Kitaifa three hundred thirty thousand Euro, mradi mwingine twenty thousand billion, mradi mwingine three point; Mradi wa Maji Makonde shilingi bilioni mbili, Waziri naomba hili jambo ulitazame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sitaki kwenda katika historia, watu wa Newala - Tandahimba baada ya kuona shida zetu za maji ni kubwa, enzi ya mkoloni 1953 tulianzisha kampuni iliyokuwa inaitwa Makonde Water Corporation, kwa wazee waliokuwepo hisa ilikuwa shilingi 20 kampuni ikaenda kukopa hela Uingereza ikaanzisha Mradi wa Maji Makonde na mwaka 1954 mradi ukafunguliwa kwa sababu palikuwa na cost sharing kila mwaka tulikuwa tunapeleka maji vijiji vipya, maji yakawa yanapatikana bila matitizo every domestic point.
Baada ya mradi kuchukuliwa na Serikali kusema sasa hapana, tuachieni tunaendesha sisi tumerudi nyuma. Nimekaa Bungeni hii term ya tatu, nilipoingia upatikanaji wa maji Newala ulikuwa 22 percent miaka yangu kumi ya kufurukuta pamoja na uzito niliokuwa nao tumeongeza asilimia nane tu. Kama miaka kumi asilimia nane mpaka tufike hiyo asilimia 65 itatuchukua miaka mingapi? (Makofi)
Mheshimiwa Waziri ninachotaka kusema Mradi wa Maji Makonde una matatizo makubwa yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo hayo ni pamoja na uchakavu wa mitambo, mabomba yale enzi ya mkoloni hayakuwa plastic yalikuwa ni ya chuma yameoza yametoboka kwa hiyo maji yanayopotea njiani ni mengi. Hatuna pampu za kutosha, wataalam hawatoshi, vituo vichache vya kugawia maji, kwa ujumla uzalishaji mdogo wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri utakapokuwa unajibu narudia tena ueleze mwaka huu Serikali inafanya nini kuongeza uzalishaji wa maji Makonde, nakuomba uje kiangazi, Waziri wako alikuja wakati wa masika hakuona shida ya watu, wakati wa masika ndoo moja ya maji shilingi 1,000!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingine ndugu yangu pale Mheshimiwa Bwanausi ameelezea, mradi wa maji Chiwambo ulikuwa unafika mpaka Newala hauji tena, Mradi wa Maji wa Luchemo tulipata mafuriko mwaka 1990 mashine zile zikasombwa na maji tangu 1990 mpaka leo hakuna replacement. Mheshimiwa Waziri naomba sana fufueni Mradi wa Luchemo tuunganisheni watu wa Newala na Mradi wa Chiwambo kwa ndugu yangu Mheshimiwa Bwanausi na ninashukuru ameuzungumzia hapa, naomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwamba tunapata taabu Viongozi, mradi wa maji wa Kitangari – Mitema, Mji mdogo wa Kitangari upo kilomita tatu kutoka pale, hawapati maji. Maji yale ya Mitema yanasukumwa yanafika mpaka Tandahimba, hapa kwenye source ya maji hawapati maji.
Mimi mnanipa taabu sana maana inabidi niwabembeleze wapiga kura wangu, wanataka wapige shoka maji yale ili tukose wote, nawaambia hapana subirini Serikali inachukua hatua, sasa mwisho nitaitwa muongo, hivi umri huu na mvi hizi niitwe muongo Mheshimiwa Waziri unafurahi? Hivyo, tuaomba tatizo la maji la Mji Mdogo wa Kitangari lishughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo sugu ambalo watumishi wa maji Newala hawataki kusikia. Tumepitisha maazimio kwenye Halmashauri, marufuku kupeleka maji katika visima vya watu binafsi, palekeni maji katika domestic point za public pale ambapo kila mmoja anapata maji. Maafisa wako wanachofanya wanapeleka maji katika nyumba za watu binafsi, wanawajazia maji baadae wale wanawauzia wananchi maji ndoo shilingi elfu moja, ukiwaambia kwa nini hampeleki katika domestic point ambayo watu wote tunapata pale hawana majibu! Jawabu nini corruption. Hebu Waziri tamka kesho kutwa utakapo wind up na uwaagize watumishi wa maji Newala kwamba….
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nakutakia kila la kheri mdogo wangu unijibu vizuri kesho kutwa. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, barabara ya Newala -Kitangari – Mtama inahudumiwa na TANROADs. Hii barabara inaunganisha Mkoa wa Mtwara na Lindi, lakini ni barabara ya vumbi. Wananchi wa Newala wanaomba barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami, maana pia ndiyo njia kuu wanayotumia watu wa Newala kwenda Dare es Salaam na Dodoma. Tunashukuru kwa jitihada za Serikali maana sehemu korofi kama za Kitangari na mlima Kinolombedo zimejengwa kwa kiwango cha lami. Ni vizuri kuongeza kilomita zilizojengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Uwanja mpya wa Ndege wa Newala. Baada ya eneo la Uwanja wa Ndege wa zamani kupima viwanja, Uongozi wa Wilaya umetenga eneo jipya la Uwanja wa Ndege. Wataalam wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege walitembelea Newala na kuelekeza ukubwa unaohitajika na mwelekeo wa Uwanja. Nilipouliza swali Bungeni, Mheshimiwa Waziri alinijibu kuwa Serikali italipa fidia eneo la uwanja, wakati inafanya mipango ya Ujenzi. Wananchi wa Newala wanaomba Serikali ilipe fidia eneo la Uwanja wa Ndege ambalo halina mazao mengi ya kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami toka Newala Mjini kuelekea Masasi palitengenezwa mfereji wa kutolea maji barabarani. Mfereji huu umeleta uharibifu mkubwa kwa kutengeneza korongo kubwa zinazotishia usalama wa nyumba za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika katika Kijiji cha Mkunya, korongo kubwa lililosababishwa na mvua linahatarisha usalama wa nyumba za wananchi. Alipotembelea Wilaya ya Newala, Mheshimiwa Waziri Mbarawa alikagua eneo la korongo la Newala Mjini, akaahidi kutafuta fedha za kujenga makorongo hayo vizuri. Wananchi wa Newala tunakumbusha ahadi ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's