Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Angeline Sylvester Lubala Mabula

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nami ni mara ya kwanza kuchangia hoja katika kipindi hiki cha bajeti, naomba pia nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuweza kunifanya niwepo hapa.
Pia nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ilemela kwa imani yao kubwa ambapo walipata mateso kwa miaka mitano bila huduma kwa jamii, lakini wakaamua kuachana na hiyo na kurudisha Chama cha Mapinduzi kuweza kuongoza Jimbo lile. Nasema sitawaangusha, tuko pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa dhamana hii kuweza kuwa msaidizi wake katika Serikali hii ya Awamu ya Tano. Nachukua fursa hii pia kupongeza na kuishukuru familia yangu hasa muwe wangu Julius Mabula, watoto kwa namna ambavyo wamekuwa wavumilivu kwa muda wote niko hapa; nawashukuru ndugu, jamaa na marafiki ambao wamekuwa karibu sana kuhakikisha kazi yangu ya uwakilishi inakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya, Makamu wa Rais na hasa kwa kuwa ni mwana mama, Waziri Mkuu, Mawaziri na Manaibu Waziri, Wabunge wote lakini pongezi za dhati sana kwa Wizara husika ambayo leo tunajadili hoja yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie machache kuhusiana na Wizara yangu kama jinsi ambavyo yameguswa na wachangiaji wakati wakichangia hoja ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nianze na migogoro. Naomba niseme wazi, migogoro ipo mingi, ndiyo maana Wizara imechukua hatua ya kupeleka waraka katika mikoa kuwataka waweze kuzungumzia migogoro iliyopo na chanzo chake ili tuweze kuona namna ya kuitatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke suala la migogoro ya ardhi ni suala mtambuka, haligusi Wizara moja, ndiyo maana limeingia sana katika mifugo na wakulima kule, lakini kwenye ardhi lipo, ukienda TAMISEMI lipo, ukiingia Maliasili na Utalii lipo, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) lipo. Kwa hiyo, suala hili kama Wizara tumeshaanza mchakato wa kukaa pamoja tuweze kulipitia kwa pamoja. Kwa hiyo, tukipata zile taarifa za mikoani, tutajua chanzo cha migogoro ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ardhi imekuwa ni tatizo na ni chanzo kikubwa, basi tutajua. Inatokana na wananchi kuvamia maeneo? Inatokana na wakulima kukosa maeneo ya kutosha? Au inatokana na wafugaji pengine kutopata maeneo? Je, mazingira tunayalinda? Kwa hiyo, ili tuweze kupata ufumbuzi wa kweli ni lazima hizi Wizara zikae pamoja kama ambavyo tumekwishaanza tuweze kuona chanzo na namna bora ya kuweza kutatua. Kama ardhi imekuwa ni tatizo, pengine tuweze kuona namna ambavyo tunaweza kulitatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mpango wa matumizi bora ya ardhi nao ni changamoto. Kwa hiyo, ni lazima pia tuangalie. Kuna wengine walitoa hoja kabla ya kilimo, suala la viongozi kupewa maeneo. Haikataliwi kama amefuata sheria, lakini suala la msingi ni je, sheria zimezingatiwa? Kwa hiyo, hapa tunasimamia ile Sheria ya Ardhi Namba (4) na Namba (5) ya mwaka 1999, kuona ni kweli limefuatwa. Kwa sababu kuna process ndefu ya kupata eneo. Lazima utapitia katika vikao husika. Vikao hivi kama vinakiukwa ndipo hapo ambapo unaona matatizo yanakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wakati mwingine tamaa za viongozi katika maeneo ya chini kuweza kutaka kumilikisha watu kwa kukiuka taratibu. Pia na siasa inaingia. Tukiondoa siasa katika suala la umilikaji wa ardhi, migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya ardhi itapungua sana, kwa sababu kila mmoja anaguswa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imezungumzia suala la kuwezesha vijana na sisi kama Wizara tunasema sawa. Wamezungumzia suala la kurejesha ardhi na kuwapa, lakini bado niseme Halmashauri zetu zitahusika sana kutambua yale maeneo na kuweza kujua ni jinsi gani vijana hawa tunawapa ili waweze kujikita katika uzalishaji ambao utakwenda vizuri katika kujipatia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala pia la wavuvi. Naomba ku-declare interest kwa sababu Jimbo ninalotoka ni la wavuvi. Kama Serikali ilivyozungumza, nami naomba, kwa sababu Sheria ya Uvuvi itakwenda kupitiwa upya, niwatake sana watu wa Jimbo langu na wale wote wanaotoka katika maeneo ya uvuvi waweze kuchangia mawazo yao ili sheria ile itakapokuwa imetoka, maoni yao yaweze kuwa yameingia. Walikuja kwa timu ya uongozi wakatoa kero zao nyingi, Waziri aliwapokea, tulikwenda nao na sisi tunasema kama Serikali tutayapitia haya kwa sababu kilio kinapotolewa ni lazima pia upitie, lakini nao wana sehemu kubwa ya kuchangia katika Muswada ule utakapokuwa umeanza mchakato wake, watoe mawazo yao ili tuweze kujua ni jinsi gani migogoro hii inakwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Upinzani wamezungumzia suala zima la Tume ile ya Bunge iliyoundwa katika kuchunguza migogoro na wakataka kujua ni maazimio mangapi yametekelezwa. Naomba niwahakikishe tu kwamba Wizara imeyashughulikia na kwa sababu yalikuwa yanagusa maeneo mengi, ndiyo maana ilikwenda kuwa chini ya Wizara ya Waziri Mkuu.
Kwa hiyo, yale ambayo yanatugusa, yapo, tumeainisha na tutayatoa wakati wa hotuba ya bajeti ya kwetu. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kila ambacho kimezungumziwa tuko tunaendelea nacho kukifanyia kazi tukijua wazi kabisa kwamba bila kufanya utatuzi huu itatuletea shida katika namna bora ya kupanga maendeleo katika Wizara na katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine ambalo limezungumziwa ni la kiusalama zaidi, kwenye usalama wa wavuvi ndani ya ziwa. Waziri mwenye dhamana tayari alishalichukua nalo linafanyiwa kazi kuhakikisha kwamba usalama wa wavuvi wetu unakuwa katika hali ambayo ni ya ulinzi zaidi. Bahati nzuri Waziri mwenye dhamana naye ana interest katika hilo. Naomba kusema tu kwamba tuko pamoja katika hilo.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAAZI: Niliambiwa dakika kumi, siyo tano Mheshimiwa.
NAIBU SPIKA: Ni kumi, ulishagongewa ya kwanza tayari.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge lako Tukufu, naomba nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa fursa aliyonipa ya afya njema na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kusema yale nitakayoyasema ikiwa ni katika hali ya kujibu baadhi ya hoja za Wabunge ambazo wamezitoa na nyingi tutazijibu kwa maandishi na watapata nakala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nichukue fursa hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameniamini na kunipa fursa ya kuweza kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na niseme sitamuangusha. Kwa kupitia kwake pia niwashukuru sana wananchi wa Ilemela ambao wamenipa dhamana hii ya kuwawakilisha Bungeni na hatimaye Mheshimiwa Rais akanipa wadhifa mwingine wa kuweza kumsaidia katika Wizara niliyoitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais. Ni wazi atatuwakilisha vizuri na ameonyesha njia kwa namna alivyoanza. Nimpongeze pia Waziri Mkuu kwa kuteuliwa kwake na hasa wananchi wa Jimbo lake la Ruangwa kwa kumchagua kuwa Mbunge na hatimaye akateuliwa kuwa Waziri Mkuu na Bunge hili likamthibitisha. Niwapongeze Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wamechaguliwa. Nimpongeze Spika pamoja na Naibu Spika na Wabunge wote kwa nyadhifa zenu ambao mnategemewa sana na wananchi kwa sababu ya kuwapa ridhaa kwa hiyo wana matumaini makubwa kutoka kwenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukurani zangu pia zimwendee sana Waziri na mtani wangu Mheshimiwa William Lukuvi kwa ushirikiano anaonipa katika kufanya kazi. Ni muda mfupi tu ambao tumekuwa pamoja naye lakini najisikia kuwa na faraja kubwa kwa sababu ni mentor mzuri ambaye anaweza kukuelekeza, akakushirikisha na ukaweza kufanya kazi vizuri. Na mimi nasema nitatoa ushirikiano kwake wakati wote kwa namna ambavyo anaelekeza nadhani imenifanya pia nitambue na nielewe Wizara kwa muda mfupi, nasema tutafanya kazi vizuri.
Pia niwashukuru watendaji wote wa Wizara pamoja na taasisi na mashirika yaliyoko chini ya Wizara wamekuwa na ushirikiano mzuri katika kufanya kazi hizi na hatimaye kwa muda mfupi sana huduma katika Wizara zimeboreka na watu wanahudumiwa vizuri na mrejesho tunaupata. Kwa hiyo, namshukuru sana Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na watendaji wote walioko katika idara nilizozitaja.
Aidha, pia nishukuru sana Ofisi ya TAMISEMI ambayo nayo tumekuwa tukishirikiana sana katika kutatua kero mbalimbali. Ardhi ni suala mtambuka na mambo mengi yanaletwa ardhi lakini yanagusa Wizara nyingi, kwa hiyo, nishukuru kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shukrani zangu nisisahau familia yangu, namshukuru sana mume wangu Julius Mabula, watoto wangu David, Javine, Diana na Dorothy, baba na mama wazazi Silvester Lubala ambao wameweza kunilea na kunifanya niwe kama nilivyo. Nashukuru ndugu, jamaa na marafiki ambao wote wamekuwa karibu sana katika kunitia moyo na kuweza kufanya kazi kwa umoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Wabunge wote wa Mkoa wa Mwanza ambao tunashirikiana sana katika kazi zetu kuhakikisha kwamba Mkoa unakwenda vizuri. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa dini madhehebu yote Mapadri, Mashehe, Maaskofu katika madhehebu mbalimbali ambao kwa muda wote wamekuwa wakiniombea na kunipa ushauri wa kimwili na kiroho na wamenifanya kwa kweli nisimame imara katika kazi zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie shukurani zangu si kwa umuhimu kwa kukishukuru sana Chama changu ambacho kimeniamini kikaniteua na kunifanya nigombee katika Jimbo ambalo kwa miaka mitano tulikuwa tumepangisha lakini mpangaji akashindwa masharti ya upangaji tumemwambia apumzike ili tuweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani zangu naomba sasa nianze kujibu baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Wabunge katika michango yao ya maandishi na wengine kwa kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia ile taarifa ya Kambi ya Upinzani ambayo Waziri Kivuli aliiwasilisha hapa na nimshukuru tu kwamba taarifa yake ilikuwa ni nzuri kwa jinsi alivyoileta ina changamoto na mambo ambayo ameyasema hapa tutakwenda kuyatolea taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ya Upinzani imezungumzia suala la uporaji holela wa ardhi katika maeneo mbalimbali, wamezungumzia ufisadi wa ardhi unaofanywa na viongozi na hakuna hatua zinazochukuliwa na wamezungumza kuhusu watu wa chache kuhodhi ardhi. Katika haya yote niseme utoaji wa ardhi kwa wawekezaji unazingatia zaidi sheria za nchi. Wizara inaelekeza mamlaka ya ugawaji kuzingatia sheria hiyo na Wizara imekuwa ikilisimamia hilo na imetoa mwongozo kwa Wakuu wote wa Wilaya ili kupitia katika vikao vyao ili ardhi isitolewe kiholela kama ambavyo imekuwa ikileta migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hatua zinachukuliwa kwa ardhi ambayo inapatikana kinyume na utaratibu. Wizara imeagiza Halmashauri zote nchini kufanya ukaguzi na uhakiki wa mashamba pamoja na viwanja ili kuweza kuratibu na kuona yapi ambayo yanamilikiwa isivyo kihalali ili hatua ziweze kuchukuliwa. Katika kutekeleza hilo pia ni wazi wote ni mashahidi tumeandaa kitabu ambacho kila mmoja anacho kimeainisha migogoro yote ambayo ipo. Mingine kweli inatokana na watu kukiuka taratibu, lakini mingine pia ni kwa utendaji pengine ambao umekiuka maadili ya kazi kwa watendaji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la fidia ambalo amelizungumzia. Sheria ya Ardhi na kanuni zake zimeweka utaratibu wa kukadiria na kulipa fidia ya ardhi na fidia yake inatofautiana kutegemeana na eneo ambapo ardhi ipo. Kwa hiyo, kuna ardhi nyingine unakuta bei yake iko juu na nyingine iko chini. Pia hapa tutambue kuna wengine ambao wanalalamika lakini ardhi zao zilitwaliwa kabla ya ile sheria ya mwaka 2002 ambayo imeingiza ardhi pia kuweza kuthamanishwa. Kwa hiyo, wengi wanarudi kudai kuongezewa fidia lakini wakati huo huo walishathaminishwa kwa sheria ya kabla ya sheria mpya ambayo imeingiza na ardhi kuwemo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ukaguzi wa ardhi ambalo limetolewa na Mheshimiwa Mdee, lakini na hapa mmeliongelea. Niseme Wizara ilishaanzisha kitengo kinachoshughulikia ardhi kwa ajili ya uwekezaji na pia imeziagiza Halmashauri zote nchini kufanya ukaguzi wa mashamba. Hii tunayofanya katika kunyang‟anya baadhi ya mashamba ambayo yametelekezwa sehemu kubwa pia tutachukua ili kuweza kuwa na akiba ya ardhi katika mtazamo huo kwa sababu siyo yote itakayogawiwa kwa wananchi na siyo yote ambayo watapewa tena wawekezaji lazima tutakuwa na sehemu ambayo itakuwa ni kwa ajili ya akiba kwa matumizi ya baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutolipwa fidia ambalo limezungumziwa na hasa wamezungumzia pia maeneo ya jeshi, walizungumzia maeneo ya Kaboya na maeneo mengine yako Mwanza, Ilemela na mengine yametajwa eneo la Kusini. Niseme Waziri wa Ulinzi wakati anazungumzia aliainisha vizuri kabisa namna ambavyo wanakwenda kulipa fidia katika ile migogoro ambayo wanatofautiana sana kati ya jeshi na watu. Kwa hiyo, niseme jeshi limeweka utaratibu wa kutambua mipaka yao na kujipanga katika kulipa fidia. Wameliweka wazi hili na nisingependa kulirudia kwa sababu tayari iko kwenye hotuba ya Waziri wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa suala la wananchi wa Kata ya Kahororo kutolipwa fidia. Tukumbuke kwamba maeneo mengi ambayo yanachukuliwa na wawekezaji au taasisi mbalimbali suala la kulipa fidia linakuwa siyo suala la Wizara ya Ardhi ni la mwekezaji au taasisi inayochukua. Hili suala la Kahororo ni suala la Mamlaka ya Maji ya Bukoba ambapo thamani yake ni shilingi 1,961,609,000. Kwa hiyo, hizi zinatakiwa kulipwa kwa wale wananchi kwa kadri walivyothaminishwa katika uthamini uliofanyika mwaka 2014 kwa wananchi 186 na kiasi hiki kinatakiwa kulipwa.
Kwa hiyo, suala la ulipaji wa fidia lazima pia tuangalie ni nani anayehusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara ilishatoa Waraka kwamba hatutapokea jedwali lolote linalotaka watu waliofanyiwa uthamini kwa ajili ya kulipwa fidia kama hatutaridhishwa au kuhakikishiwa kwamba kuna pesa iliyotengwa. Kwa hiyo, nitoe rai kwa Halmashauri zote wakileta madai yoyote ya fidia na wakitaka wathamini waende ni lazima tuwe tumejiridhisha kwamba kuna pesa imetengwa na watu watalipwa ili tuweze kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna maeneo ya EPZ ambayo nayo yanadaiwa fidia. Kuna baadhi ambayo yalichukuliwa na yalikuwa yanalipwa fidia kulingana namna fedha zinavyopatikana. Maeneo ambayo yamecheleweshewa fidia kwa muda mrefu Serikali itaangalia uwezekano wa kuyarejesha mikononi mwa wananchi ili yaweze kutumika kwa kazi nyingine kwa sababu imekuwa ni kero kubwa na wananchi wamekuwa wakilalamika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makampuni makubwa ya nje kuhodhi maeneo sehemu mbalimbali. Niseme tu Serikali inafanyia kazi orodha ya mashamba kama tulivyosema tayari tumeshaliweka katika utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia pia suala la Mabaraza ya Ardhi na hili limezungumzwa na Wabunge wengi kwa uchungu sana. Naomba niseme tu kwamba ni wazi kama ilivyozungumziwa Mabaraza ya Ardhi hayako ya kutosha lakini hayana watendaji wa kutosha na kesi zake zinakaa kwa muda mrefu. Niseme tu kwa mwaka huu tumepeleka maombi maalum kwenye Wizara inayohusika kuomba tupatiwe Wenyeviti kwa ajili ya Mabaraza hayo yatakayofunguliwa. Tutafungua Mabaraza 47 na tutaanza na matano. Katika kuyafungua Mabaraza hayo kuna maeneo mengine ambayo yanahitaji ushirikiano wa Wilaya husika kwa sababu shughuli ya kuwa na maeneo na ofisi kila mahali inakuwa na ugumu wake kulingana na rasilimali zilizopo. Hata hivyo, tumebaini mahitaji halisi ya Mabaraza haya kwa lengo la kuboresha na tayari vifaa mbalimbali vimeanza kupelekwa katika maeneo kusudiwa. Aidha, kuhusu watumishi kama nilivyosema tumewakilisha ombi maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme katika suala la Mabaraza ya Ardhi naomba tu tuwe na imani kwamba tunakwenda kulitatua tatizo hilo muda ambao si mrefu kuanzia sasa ili wananchi waweze kupata haki kwa wakati. Pia tutaangalia katika zile Wilaya kama watakuwa hawajapangiwa kuwekewa Baraza ambapo unakuta Wilaya moja inahudumia Wilaya zaidi ya tatu au nne, tutaangalia ni Wilaya gani ambayo ina kesi nyingi na inahitaji huduma hiyo kwa haraka. Kwa hiyo, tutaangalia badala ya Mwenyekiti kuwa katika eneo ambalo halina kesi nyingi basi itabidi tumhamishie katika eneo ambalo lina kesi nyingi ili aweze kuhudumia na atakuwa anakwenda kama visiting chairperson kwenye lile eneo kwa maana ya Mwenyekiti wa Baraza. Kwa hiyo, tuseme tu kwamba hili tutalifanyia kazi kulingana na namna ambavyo tutakuwa tumeyapata. Kwa hiyo, tunaanza na hayo ambayo tayari yapo matano, lakini yale mengine 47 yote yako katika mchakato mzuri wa kuweza kuyaanzisha, kote tutakwenda kuanzisha kama ambavyo tumesema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la National Housing. Kambi ya Upinzani kwenye hotuba yao nao wamelizungumza, lakini wachangiaji wengi sana pia wamezungumzia suala hili na wamezungumza kwa uchungu sana. Niseme walikuwa na haki ya kuyasema hayo yote kwa sababu National Housing ni kioo cha jamii na ni shirika pekee baada ya uhuru linafanya vizuri zaidi kuliko mengine yaliyoanzishwa kipindi hicho na mtakumbuka lilianzishwa mwaka 1962 baada tu ya uhuru. Kazi wanayoifanya sasa na wote ni mashahidi, mmeweza kusifia msimamizi wa shirika hilo lakini tuseme pongezi hizo zinaenda kwa watumishi wote katika idara husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wamezungumza sana kwamba nyumba zinazosemwa ni za gharama nafuu si za gharama nafuu. Naweza kukubaliana na wanachozungumza kwa sababu ya hali halisi ya namna ambavyo National Housing wanavyopata maeneo yale na namna wanavyohangaika na miundombinu. Kama Wizara tumetoa maelekezo, tumesema kama National Housing sasa wanataka kujenga nyumba za gharama nafuu ni lazima waendelee kuwa wabunifu, waendelee kufanya utafiti kuweza kujua ni kwa namna gani watajenga nyumba za gharama nafuu kwa kuangalia vifaa. Achilia mbali lile suala la VAT ambalo tumelizungumzia, hili bado tunalizungumza Kiserikali kuweza kuona ni jinsi gani VAT itakuwa waved ili waweze kupata nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa sasa hivi tunaloangalia ni namna ya kushirikisha taasisi zingine kama TANESCO, Idara ya Maji, Idara ya Ujenzi (barabara) ambao ni Halmashauri zenyewe, waweze kufanya maandalizi ya ile miundombinu mapema ili National Housing wanapokwenda kule basi waweze kufanya kazi kwa pamoja. Lingine pia Halmashauri zetu pamoja na kwamba tunalalamikia National Housing kutowafikia, lakini bado hatujawapa fursa ya kuweza kuja kupata maeneo ambayo yatapunguza gharama. Kwa sababu wakija pale NHC wanatakiwa walipe fidia, watengeneze miundombinu hiyo, tumewaambia wajipange vizuri na wafanye networking na mashirika mengine ambayo yanashughulika na huduma nilizozisema ili waweze kuona ni jinsi gani hizo nyumba zitapungua gharama kulingana na namna ambavyo wamejipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa NHC wameshafikia Halmashauri 25 na wameshajenga nyumba ziipatazo 1,076 kwa maana ya zile za gharama nafuu. Kwa hiyo, niseme kwamba wapo katika utaratibu ambao unakwenda sambamba na mahitaji jinsi yalivyo ili kuweza kuona wanafikia wananchi kutegemeana na hitaji la Halmashauri. Niwaombe Halmashauri ambazo ziko tayari katika hilo basi waweze kuwapa nafasi ya kuweza kufika katika maeneo haya na kuwapa maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia hati za kimila kutotambulika. Naomba niwataarifu tu Waheshimiwa Wabunge kwamba hati za kimila kuna Benki ambazo tayari zinazitambua na zinapokea. Ttunayo benki ya CRDB, TIB, Exim Bank, NMB, Meru Community Bank ambazo tayari zimeshazitambua hizi hati za kimilila na zinatoa mikopo. Niseme haya yote yanafanyika na bado Serikali inaendelea kuongea na taasisi za fedha ili waweze kuthamini na kutambua kwamba zile hati ni hati ambazo zinahitaji kutambulika kama ambavyo benki zingine zimeanza kuzitambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia masuala ya upangaji miji na huduma za jamii katika maeneo mbalimbali. Uvamizi wa maeneo bila kuwa na mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi hatutafika. Kama tulivyosema ni asilimia 15 tu ya ardhi ambayo imepangwa lakini ni jukumu pia la Halmashauri zetu kupima ardhi. Halmashuri zetu zinapaswa kutenga bajeti kidogo kidogo angalau wakapima kwenye maeneo yao. Tukikaa tukisubiri Wizara tutafanya kazi hiyo lakini itatuchukua muda mrefu.
Kwa hiyo, niombe Halmashauri zetu ziweze pia kuchukua wasaa wa kuweza kuyapima yale maeneo na kuweka matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro hii ambayo ipo. Kwa sababu kama tutaachia Wizara, kazi itafanyika kama tulivyoanza katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi lakini tumeona kwamba huu ni mradi wa miaka mitatu ambayo ni mingi sana tutafikia vipi maeneo yote kama mlivyosema. Niseme hilo ni la kwetu sote tushirikiane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutokuwa na Maafisa Ardhi Wateule, Halmashauri pendekezeni majina ya wale ambao wamefikia sifa hizo, mlete kwa Kamishina. Kwa sababu tayari tunao Makamishna Wasaidizi kwenye Kanda nane, watafanya kazi ya kuwateua watumishi hao ili waweze kufanya kazi hiyo.
Suala la upungufu wa watumishi bado tunalifanyia kazi kama nilivyosema pia tumeomba watumishi wengine waweze kuongezwa katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba mambo yaliyozungumzwa ni mengi ambayo yanahitaji pia kuwa na utulivu katika kuweza kuyapitia moja baada ya lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo nataka kusema ni kwamba masuala haya na hasa ya upimaji na mipango miji, tuna master plan ambazo zimeandaliwa katika miji yetu ya Mwanza, Arusha, Dar es Salaam ambao ulikuwa umeharibika sana unaandaliwa upya kwa kuzingatia mpango kabambe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana tuwaelimishe wananchi wetu wasiwekeze katika maeneo ambayo watakuja kupata shida baadaye kwa sababu master plan zinakuwa zimeandaliwa lazima waangalie waweze kujua katika eneo lake katika mpango uliopo panatakiwa kujengwa nini? Kwa hiyo, kama ni suala la umilikishaji na uendelezaji aweze kuendeleza katika hali halisi ambayo ndiyo mpango uliopangwa ili asijepata hasara baadaye anaambiwa abomolewe kwa sababu amejenga kinyume na taratibu au hakuzingatia mpango mji kwa kule ambako tayari mipango miji imeandaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge wa Misenyi amezungumzia habari ya kupanga mji mzuri kule kwao. Eneo lolote ambalo wamejiandaa katika kuweka kamji kadogo kazuri katakakofuata sheria na taratibu walete, Wizara ipo tayari tutasaidiana pia na wenzetu wa National Housing kuhakikisha kwamba huo mji unapangika vizuri na unajengwa majengo mazuri. Hata kama siyo National Housing tutaangalia pia nani anaweza akafanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge walilalamikia kuhusu ubovu wa majengo yanayojengwa na kulazimu kubomolewa. Naomba niwaambie, katika jengo lililobomolewa pale Dar es Salaam National Housing hakuwa amejenga yeye lilijengwa na mtu mwingine, majengo yote ya Nationa Housing yanakwenda vizuri. Kwa hiyo, wale wanaotaka kuwa na miji mizuri bado msisite kutumia Shirika la Taifa ambalo linaweza likafanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamejadiliwa lakini niseme haya ambayo nimeyadodosa tu kwa kuyapitia moja moja, kidogo kidogo bado niseme kwamba tutayajibu yote na Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa na yeye atajibu baadhi ya hoja. Niseme kwa wale wanaojenga maeneo yasiyofaa na kupatiwa huduma za maji, umeme na kadhalika, utoaji wa huduma kwa wakazi waliojenga maeneo hatarishi unafanywa na mamlaka na taasisi kwa kutoa huduma kwa msingi wa kibiashara na hata wale waliobomolewa ambao pengine walikuwa wana hati, Wizara ilishawaambia walete ili tuweze kutambua. Kama alikuwa na hati halali ya Wizara, tunajaribu kupitia na kuweza kuona tutawapa alternative ipi ya kuweza kuwapatia viwanja vingine. Habari ya kuwekewa maji, umeme isiwe ni sababu ya kujenga kwenye maeneo ambayo ni hatarishi. Wale wanafanya kazi zao kibiashara ukimwambia alete maji analeta kwa sababu anajua tu kwamba ni eneo ambalo anapeleka huduma. Kwa hiyo, niseme tupo pamoja katika kuhakikisha tunapanga miji yetu ili tuweze kuona kwamba ni jinsi gani tutakwenda pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima ambalo tumesema ni la utatuzi wa migogoro ambalo Waziri wangu atalizungumzia kwa kirefu. Hili suala ni mtambuka na kama ambavyo tumelieleza tutakwenda kukaa pamoja na Wizara zinazohusika ambazo ni Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Maliasili na Utalii, Kilimo, Uvuvi na Mifugo na Maji tuweze kuona kwa sababu migogoro mingi imekuja kwenye Wizara lakini ukiangalia kitabu chetu tulikuwa tunaainisha pia kuona kwamba mgogoro huu utatatuliwa na Wizara ngapi, kama ni ya kwetu tumeonesha na Wizara nyingine anayofuatia tumeionesha. Haya yatafanyika katika utaratibu ambao utakuwa umewekwa vizuri ambao utatusaidia sisi sote kuepuka hiyo migogoro ambayo inajitokeza mara kwa mara na si lengo la Serikali kuweza kusema kwamba tuweze kuhatarisha maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba haya yote tunayokwenda kuyafanya tunategemea zaidi ushirikiano wa Wabunge. Tayari kama Wizara tumeshawezesha kwa maana ya kupata zile nyaraka muhimu. Kwa hiyo, tunategemea pia mtakuwa ni sehemu ya utoaji wa elimu. Kwa sababu siku zote tunasema ardhi ni mtaji bila kufahamu sheria na kanuni zinazotawala ardhi bado itakuwa ni shida. Kwa hiyo, nyaraka hizo ni nyenzo mojawapo ambayo tumeitoa itakayotusaidia sisi sote, Wabunge pamoja na Waziri mwenye dhamana katika maeneo hayo ili kuweza kuona kwamba kazi hii tunaifanya katika muda muda mfupi kwa kusaidiana na hatuzalishi migogoro mingine kwa sababu taratibu tutakuwa tumezizingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimalizie kwa kuwashukuru sana Wabunge kwa ushirikiano wao na Wizara. Baada ya kuwa tumepokea hoja na migogoro, Wizara itaishughulikia yote na baadaye tutaona namna bora ya kuweza kuona kwamba Taifa ambalo halina mgogoro linapatikana. Kwa sababu kazi tuliyopewa na Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha migogoro iliyopo inakwisha na tusizalishe mingine lakini ni mimi na wewe ambao tutakwenda kuhakikisha migogoro inakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimuachie Mheshimiwa Waziri aweze kuendelea kwa sababu najua kila ambalo limeandikwa litafanyiwa kazi na litakwenda kutolewa ufafanuzi kama ambavyo tumepanga. Nashukuru kwa kunisikiliza.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwanza kwa kuishukuru sana Kamati na kuunga mkono pengine na kusema kwamba tunapokea ushauri ambao wameutoa ikiwa ni pamoja na ile addendum ambayo imeletwa kama Serikali tumeipokea na tutakwenda kuifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wamezungumzia masuala ya migogoro na kama mwenzangu wa kilimo alivyozungumza, suala hili la migogoro ni mtambuka. Nitapitia wachache ambao nimejaribu ku-note, ukiangalia suala la migogoro, zaidi ya Wabunge 15 wamezungumzia. Naomba nianze kwa kusema kwamba ushauri uliotolewa na Kamati tumeupokea kama ulivyo, wamezungumzia suala la National Housing kwamba nyumba ni za gharama nafuu, lakini ubora si mzuri sana. Hilo tumelipokea na tutakwenda kupitia tena kuona ni jinsi gani ambavyo watakwenda kuboresha. Sehemu kubwa pia hata ile size ya nyumba zinapoungwa mbili wengi wamesema hawazipendi sana katika kutembelea waliyazungumza hayo. Kwa hiyo, tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikija kwa hoja ya Mheshimiwa Sakaya ambayo alizungumzia habari ya Kamati iliyoundwa na Wizara tano ambazo hazijajulikana zinamaliza muda wake lini pamoja na Mheshimiwa Grace Kiwelu na Mheshimiwa Pauline Gekul wote walitaka kujua taarifa hizi zitakuja lini.
Mimi niseme tu kwamba tarehe 13 Februari, taarifa ya kwanza itatoka na wamepitia katika mikoa mitano, wamekwenda Tabora, Katavi, Morogoro, Geita na Kagera. Kwa hiyo, taarifa ya kwanza tutaipokea kutoka katika mikoa hiyo. Baada ya hapo awamu ya pili wanakwenda katika Mkoa wa Arusha, Manyara, Tanga na Pwani, kwa hiyo, tutawapa ratiba kamili watakapokuwa wanakwenda kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sakaya pia alitaka kujua namna ambavyo tunaweza tukasaidia Halmashauri kuhakikisha kwamba viwanja vinapimwa na kuondoa hii migogoro. Niseme tulikuwa na ule mfuko na bado upo lakini haufanyi kazi vizuri sana kwa sababu Halmashauri zetu zinakopa na hazirudishi. Jumla ya Halmashauri 27 zilishakopeshwa kiasi cha shilingi 962,676,000 lakini kati ya hizo Halmashauri 11 hazijalipa, bado zinadaiwa. Kwa hiyo, pesa ambayo ilitakiwa irudi ni shilingi 1,155,211,224.
Kwa hiyo, niwaombe tu Halmashauri ambazo zinadaiwa mrejeshe ikiwemo Halmashauri ya Magu, Mji Mdogo wa Makambako, Kagera, Bunda kwa maana ya Chato lakini kuna Singida, Sengerema, Iringa, Tumalenga, Ruvuma, Songea na Tarime. Hizi ni Halmashauri zinazodaiwa, tuwaombe sana mrejeshe ile mikopo ili na wengine waweze kutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la kusaidia, tuseme tu kwamba kanda zetu tumejaribu kuziimarisha, lakini tatizo tulilonalo kwa nchi nzima tuna upungufu wa watumishi wa sekta ya ardhi kwa asilimia 64. Kwa hiyo, utaona kwamba kuna upungufu mkubwa ambapo kwa kweli kuweza kukidhi haja inakuwa ni ngumu. Pamoja na upungufu huo, tunazo Halmashauri kama saba ambazo hazina kabisa wataalam hao, kwa hiyo, unaweza ukaona changamoto jinsi ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ambavyo tunajaribu kuimarisha kanda zetu, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge pale mnapokuwa na ratiba za upimaji shirikisheni ofisi zetu za kanda, kwa sababu tunatarajia watakuwa tayari wamekamilika na timu nzima za wataalam lakini pia na vifaa vya upimaji. Kwa sababu unakuta kanda moja pengine inasimamia Halmashauri zaidi ya 18 mpaka 36, basi niombe tu ile ratiba iweze kwenda vizuri ili hawa nao wasaidie katika kupima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sehemu kubwa ni jukumu letu katika Halmashauri zetu kuona ni jinsi gani tunapanga mikakati yetu vizuri kuweza kuweka utaratibu wa kupima kila mwaka na kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi, tukiweka angalau vijiji vitatuau vinne kila mwaka tutasogea. Gharama siyo kubwa ni kati ya shilingi milioni sita mpaka 7 na kuna vijiji vingine vina uwezo basi tuwashirikishe wale waweze kuona ni jinsi gani wanaweza wakahudumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ku-subsidized nyumba za National Housing hili tulichukue tu tulifanyie kazi, kwa sababu ni mashirika mengi yanayojenga, bado TBA, WatumishiHousing, NSSF kila mmoja atataka kunufaika na punguzo hilo. Kwa hiyo, niombe tulichukue tutaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la mashamba ambapo wamezungumzia kwamba kasi ni ndogo pengine na gharama ya kuweza kuyapima. Mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwenye maeneo yetu sisi ndiyo tuna mashamba hayo na tunatambua jinsi gani ambavyo hayajaendelezwa. Kazi ya Wizara ni kupokea kile ambacho mmeona hakifanyi kazi vizuri na kimekiuka taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwaombe wakati wanafanya kazi zao wale watumishi wa idara husika iwe ni sehemu ya kazi zao. Mmaana hapa mmesema hakuna pesa anahitaji pesa lakini akiweka kama ni sehemu ya kazi zake za kila siku, yule anayefanya kazi za uandani anapokwenda kufanya kazi kule basi afanye na kazi hii itasaidia sana katika kuona ni jinsi gani tunaweza tukapunguza au tukatoa taarifa za haya mashamba. Tusisubiri hela za kuja kupimiwa au kukaguliwa kutoka Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Njeza amezungumzia suala la mipango miji, naomba nikiri tu hili nalo ni kutokana na upungufu tulionao. Pia tunaomba sana kwa sababu wenzetu wa Mbeya wako katika mpango kabambe wa master plan basi hilo nalo liingie katika mpango huo, itasaidia sana katika kuona ni jinsi gani tunaweza tukaweka mpango mzuri katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ile project ya Kawe, imezunguziwa kwamba amepewa mtu binafsi kwa US dollar milioni 6.5.
Naomba niseme tu kwamba tungeweza hata kuishukuru Serikali kwa namna ilivyoweza kuokoa, kwa sababu lile lilikuwa imewekwa chini ya PSRC na ndipo hapo Wizara ikaomba kupitia National Housing ili kuweza kuchukua ile fifty, fifty angalau eneo lingine lirudi Serikalini. Isingekuwa hivyo basi basi eneo lote lilikuwa limeshaondoka. Mimi nasema kwa kweli lile eneo na gharama yake ni kubwa kwa maana ya kwamba lina-appreciate kila siku. Kwa hiyo, kitendo cha kuchukua asilimia 50 ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri binafsi, Naibu Waziri na Watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba katika REA III vijiji 23 vifuatavyo vipatiwe umeme, ili waweze kwenda na kasi ya maendeleo sawa na maeneo mengine:-
Vijiji vya Lutongo, Kabusungu, Kilabela, Kilino, Isanzu, Igogwe, Shibula, Bulyanhulu, Ilalila, Chabakirua, Masemele, Igombe A, Igombe B, Mhonze A, Buganda, Zenze A, Zenze B, Iseni, Ilekako, Igalagale, Kasamwa, Imalang‟ombe na Isesa. Kazi mnayoifanya ni nzuri sana na inatia moyo, endeleeni kuchapa kazi msikatishwe tamaa na watu wasioitakia mema nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeambatanisha Shule za Sekondari zisizo na umeme. Naomba zipatiwe umeme maana ziko nje au vijijini; Mwinuko, Nundu, Kilimani, Shibula, Kirumba, Kabuhoro, Kangaye, Ibinza, Lukobe, Mihama na Sangabuye.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja. Aidha, niwapongeze sana Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya pamoja na kuwa na changamoto nyingi, Mungu mweza wa yote awatie nguvu, mtende kazi bila kuchoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni tamaduni za makabila; niwaombe katika suala la utalii muangalie pia historia na tamaduni za makabila mbalimbali kwani chaweza kuwa kivutio kikubwa cha utalii, kupata historia na utamaduni wa makabila husika. Mfano Kituo cha Bujora na Kayenze Mkoa wa Mwanza, kwa Wanyamwezi Tabora (Mwinamila), tamaduni na historia za Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Makumbusho ya Mkwawa - Iringa, kuna mengi ya kuvutia watalii, lakini pamesahaulika sana. Historia ya Mkwawa hakuna asiyeifahamu lakini kituo chake kimesahulika sana na pamechakaa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia kwa waathirka wa kung‟atwa na fisi; Jimboni kwangu katika Kata ya Sangabuye na Bugogwa zaidi ya watu nane waling‟atwa na fisi na wawili hali zao zilikuwa mbaya sana. Halmashauri italeta madai ya wananchi wakidai fidia kwa madhara waliyoyapata. Vilevile kwa habari nilizopewa, ninaomba walete ushahidi wao baadhi yao walipwe fidia siku za nyuma. Ninaomba mara watakapoleta madai yao yashughulikiwe mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wafugaji na wakulima; ni vyema kama ambavyo imesemwa mara nyingi na Wizara yetu imelizungumzia, tupange kukutana na Wizara zinazohusika ili tumalize kero hii, watu wawe wafugaji wasiosumbuliwa. Iwapo kuna haja ya kumega maeneo ambayo yamevamiwa na makazi ya watu, tupime uzito ili kuondoa kero na kelele za mara kwa mara. Lengo la Serikali ni kuondoa kero, lakini kuwafanya wananchi waheshimiu sheria za nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu liwe endelevu ili watambue mipaka yao, zaidi sana wawe sehemu ya kulinda mazingira na hifadhi zetu.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DR. ANGELINA S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja. Ombi langu wananchi wa Kata ya Kanyerere na Kata jirani katika Wilaya ya Magu wana tatizo kubwa la usafiri kuweza kufikia visiwa vya base (Ilemela) na kisiwa cha Mashoka – Magu. Katika Kikao cha RCC kilichofanyika Mkoa wa Mwanza Januari, 2017, waliahidi kupeleka kivuko baada ya kufanya tathmini ya abiria, mizigo na shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika visiwa hivyo na kuona vinastahili kuwa na kivuko. Ombi langu ni utekelezaji wa ahadi hiyo.

(1) Barabara ya Sabasaba - Kiseke hadi Buswelu ilikuwa ahadi ya Waziri alipotembelea Jimbo langu, naomba barabara hiyo kuwa ni kiungo cha Makao Makuu ya Wilaya na Kata zaidi ya saba ijengwe. Aidha, barabara hiyo itarahisisha pia kuwa kama mchepuko wa wasafiri waendao Mara na Shinyanga.
(2) Barabara ya Airport, Kayenze hadi Nyanguge nayo pia itasaidia mchepuo kuelekea Mara na Serengeti katika Mbuga za Wanyama na kuchochea utalii katika maeneo hayo.
(3) Tunahitaji minara ya simu katika Kata ya Kayenze na Sangabuye hawana mawasiliano ya uhakika katika baadhi ya mitaa ya Kata hizo za Kabusungu, Igumamoyo, Imalang’ombe na kadhalika.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. ANGELINA S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoifanya katika Wizara hii kwa kushirikiana na Naibu Waziri na timu nzima ya wataalam. Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki muendelee kuwatumikia Watanzania. Vilevile nichukue fursa hii kutoa shukrani kwa mara nyingine kwa mgao wa gari la wagonjwa, hakika mlitusaidia kwa kiasi kikubwa sana kusaidia huduma ya mama na mtoto katika jimbo langu hususan Kituo cha Afya Sangabuya ambako gari lilipelekwa na Kituo cha Afya Karume linakotumika pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba Manispaa ya Ilemela haina Hospitali ya Wilaya mpaka sasa, kwa juhudi za Halmashauri na kwa msaada wa Serikali Kuu jengo la wagonjwa wa nje tayari limepanuliwa. Tunaomba Wizara isaidie ukamilishaji wa hospitali hiyo ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ina vituo vya afya vitatu tu kati ya 19 vinavyotakiwa. Pamoja na mapungufu hayo, vituo tulivyonavyo bado vina mapungufu mengi sana. Naomba Wizara yako katika majengo ya theatre yatakayojengwa nchini walau kituo kimoja kipate, hasa kituo cha Buzuruga ambacho kina mapungufu mengi. Kwa kuainisha Kituo cha Afya Buzuruga, kinahudumia wagonjwa takribani 25,877 lakini hakina jengo la upasuaji, wodi ya wanaume wala wodi ya akina mama waliojifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Karume kinahudumia wagonjwa 25,654 lakini hakuna nyumba za watumishi pamoja na jengo la wagonjwa wa nje. Kituo cha Afya cha Sangabuye hakina nyumba za watumishi, hakuna wodi ya watoto, hakuna wodi ya wanaume. Tunaomba walau tupate jengo la wodi kwa wanaume na watoto.

MheshimiwaMwenyekiti, tuna upungufu mkubwa wa watumishi katika kada ya wateknolojia maabara, wateknolojia dawa, wahudumu wa afya pamoja na watunza kumbukumbu za afya.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja na kuwapongeza kwa kazi nzuri katika Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni Mkoa wa Mwanza pamoja na kuwa makazi ya makabila zaidi ya manne, lakini Wasukuma ni wengi zaidi. Kuna utamaduni wa Kisukuma ambao umejengeka na kuhifadhiwa kwa njia ya ngoma na vitendea kazi vilivyokuwa vinatumika enzi za mababu zaidi sana historia ya uchifu kwa koo tofauti za Wasukuma umehifadhiwa vizuri.

Aidha, namna ya maisha waliyoishi na kuweza kudumisha amani ya maeneo yao lakini pia Kituo cha Bujora kimetunza kumbukumbu zote vema ambapo watalii wanaweza kutembea na kujifunza mengi. Rai yangu naomba Kituo cha Bujora kiingizwe katika maeneo ya vivutio vya utalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Victoria mbali na kuwa ziwa la pili kwa ukubwa duniani bado halijatangazwa vema, tunaweza kutangaza kivutio hiki kwa kuwekeza katika michezo ya ziwani kwa kuweka sports boats (speed boats) ambapo watalii wanaweza kushiriki kikamilifu. Aidha, wanaweza kufanya uvuvi (sport fishing) ambapo Ziwa Victoria ni tulivu, uvuvi wa aina hiyo ya utalii unaweza kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uwanja wa ndege wa Mwanza upo katika upanuzi, bado watalii wanaweza kutumia uwanja huo kwenda Serengeti ambapo ni karibu zaidi tofauti na KIA ambako ndiko watalii wengi wanapitia.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja na niwapongeze kwa kazi nzuri pamoja na changamoto zote wanazokumbana nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nishauri tu katika kuboresha sekta ya uvuvi ni vyema season fishing ikapewa kipaumbele, italeta tija sana katika sekta hii. Tuyatambue mazalia ya samaki na kisha tuweke programu maalum ya kutekeleza season fishing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tutoe kipaumbele katika cage fishing. Tuwekeze kwa vijana ili ufugaji wa samaki ufanyike katika mfumo wa kuwa na plot ndani ya ziwa ama bahari kwa kuweka wigo katika maeneo yatakayowekezwa katika uvuvi kwa njia ya uvuvi wa wigo ziwani ama baharini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kuhusu ufugaji wa ng’ombe ni vyema wafugaji/wachungaji wakashauriwa kufuga ufugaji wa kitaalam na kuwaelekeza wafugaji wetu kufuga kitaalam ili wawe na tija katika ufugaji wao badala ya kuwa na ufugaji wa kuhamahama kitendo ambacho kinachangia sana katika kuleta migogoro ya wakulima na wafugaji.

The Valuation and Valuers Registration Bill, 2016

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kabisa kwa kunipa fursa ya kuja kutoa mchango wangu lakini wakati huohuo kuweza pengine kujibu baadhi ya hoja ambazo wachangiaji wamezisema. Napenda tu nianze kwa kuwashukuru wachangiaji wote ambao wametoa hoja zao tukianza na Waziri mwenyewe mtoa hoja, Mwenyekiti wa Kamati na Mwakilishi wa Kambi ya Upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote katika taarifa zao wamesema vizuri na karibu sehemu kubwa wanaunga mkono Muswada huu. Pia wachangiaji wote kila aliyesimama alikuwa anapongeza maana yake ni kwamba Muswada huu umekuja wakati muafaka ambapo pengine imekuwa ni kero ya muda mrefu, lakini sasa ndiyo muda wake wa kuweza kuitungia sheria ili wanataaluma hawa waweze kufanya kazi zao kwa weledi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kupitia hoja za Waheshimiwa Wabunge ambazo wamezitoa na zile ambazo pengine sitazizungumzia hapa basi nina imani Mheshimiwa Waziri atakuja kuzizungumzia. Msemaji wa kwanza Mheshimiwa Sabreena alizungumzia suala la uteuzi wa Mthamini Mkuu akasema usifanywe na Mheshimiwa Rais. Hata hivyo, tunasema kwamba kutokana na uzito na umuhimu wa nafasi yenyewe bado kama Serikali tunaona ni muhimu Mheshimiwa Rais aweze kuteua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tumepanua wigo badala ya kuteua kutoka ndani ya watumishi wa umma peke yake anao pia wigo mpana wa kuweza kuangalia pia hata walioko nje ya Serikali. Kwa maana hiyo, bado kuna nafasi kama kuna Mthamini aliyebobea nje ya Serikali kwa maana ya mtumishi wa umma basi atapata fursa hiyo. Jedwali la Marekebisho limepanua wigo huo na nadhani litakuwa limeshapita huko na mtakuwa mmeliona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia akazungumzia uzoefu wa Mthamini Mkuu kuwa wa miaka 10 kuwa ni mingi sana hivyo kusababisha pengine vijana kukosa nafasi hii. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge niseme nafasi tunayoizungumzia ni ya Mthamini Mkuu na ni nafasi moja. Sasa ukimpa muda mfupi wakati nafasi hii ni nyeti na Taifa linamtegemea zaidi katika zoezi la uthamini haitakuwa sawa. Ukipunguza miaka hii na sisi tunahitaji mtu mwenye weledi mkubwa na nafasi yenyewe ni moja, kidogo tutakuwa hatujatenda haki sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunasema kwamba kutokana na umuhimu wa nafasi yenyewe na majukumu ya Mthamini Mkuu wa Serikali jinsi yalivyo anahitaji kuwa na uzoefu wa kutosha ili kuweza kusimamia eneo hilo, uzoefu ni kigezo cha yeye kupewa nafasi hiyo. Sasa anavyosema vijana watakosa ajira au muda ni mwingi bado tunasema kwamba ile nafasi inahitaji mtu aliyebobea katika nafasi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye suala la usajili, kigezo cha uzoefu wa miaka mitatu Mheshimiwa Sabreena alipendekeza ipungue iwe mwaka mmoja. Ili mtu aweze kusajiliwa kuwa mthamini ni lazima awe na uzoefu wa kutosha wa kumudu majukumu yake. Sheria inayopendekezwa imepunguzwa muda kutoka miaka mitano na kuweka miaka mitatu. Tukumbuke pia tuna taaluma zingine kama za wenzetu watu wa CRB ambazo pia ni taaluma kama hii ambayo tunakwenda kuizungumzia, hizi ni rare professional, tunahitaji watu ambao wamefanya kazi kwa weledi chini ya watu na wamesimamiwa na wanaweza wakajisimamia wenyewe baada ya kuwa wamepata uzoefu wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulipunguza kutoka kwenye hiyo miaka mitano na kuleta mitatu baada ya wajumbe ndani ya Kamati pia kusema kwamba huu ni muda mwingi sana. Sasa ukiupunguza ukawa mmoja maana yake pia tunakuwa hatujapata yule mtu tunayemtaka na tukumbuke kazi hii ni kazi ambayo imeleta migogoro mingi sana na bado kuna migogoro mingi kwa hiyo, hatuhitaji kufanya majaribio katika hili. Mfano, nimetoa kwa wenzetu hawa wa engineering registration, nao wanakwenda kwa miaka mitatu na hii ni rare professional. Kwa hiyo, kwa nini tunasema miaka mitatu na siyo mwaka mmoja ni kutokana na unyeti wa kazi yenyewe wanayokwenda kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sabreena amezungumzia pia suala la kwamba wazawa hawakupewa kipaumbele au kutiliwa mkazo bali wageni ndiyo wamependekezwa. Nadhani katika pendekezo hili kifungu cha 25 kwenye huo Muswada kimetoa muda wa mtu asiye mzawa kutokana na kazi anayoifanya ambayo ni ya muda usiozidi mwaka mmoja, ana limit ya kufanya kazi hiyo siyo kwamba wamependelewa. Vilevile leseni anayoipata ni ya mwaka mmoja tu, baada ya hapo tena hatuko naye. Kwa hiyo, hakuna upendeleo isipokuwa tumejaribu kuweka muda wa mwaka mmoja kwa wale ambao siyo wazawa wa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza Muswada wa Uthamini utakavyodhibiti hasara iliyosababishwa na wathamini. Katika kifungu cha 67 cha Muswada huu kimeorodhesha adhabu kutokana na makosa mbalimbali ya uthamini na hasara iliyofanywa kwa vitendo na mthamini. Kwa hiyo, tuna imani kama wataisoma sheria vizuri siyo rahisi kwenda kinyume na kile ambacho kimepangwa na ndiyo maana na adhabu zake ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Elias Kwandikwa yeye amezungumzia mkanganyiko uliopo katika Ibara ya 26 na 27 katika suala zima la usajili. Tunachosema hapa ni kwamba sheria hii inasomeka sambamba na sheria nyingine, hivyo lazima hizi sheria tuziangalie. Unapoangalia vigezo vilivyowekwa huyu mwingine ni mtu aliyesajiliwa lakini mwingine ni mtu ambaye bado yupo kwenye practical anahitaji kusajiliwa, yupo katika matazamio, kwa hiyo, huwezi kuwalinganisha katika makosa yao. Huyu mwingine yupo full registered na tayari ameshaanza ku-practice, huyu mwingine anajitangaza tu bado hajaweza kupata ile full registration ya kuweza kufanya kazi hizo maana yake akifanya kosa lile anapewa adhabu. Kwa hiyo, adhabu za hawa watu wawili haziwezi kulingana, lazima yule mmoja ambaye anatambua sheria inaambana namna gani akifanya kosa lazima adhabu yake iwe kubwa kuliko huyu mwingine ambaye anajitangaza kwamba yupo kati ya wale wathamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chumi yeye amezungumzia Ibara ya 20 na 21 haisemi adhabu gani itatolewa kwa watakaokiuka maadili ya sheria iliyopendekezwa. Adhabu zote zinatokana na taaluma ya uthamini na zimeainishwa katika Ibara ya 67 kama nilivyozungumza hapo juu, kimeorodhesha adhabu zote kulingana na kosa alilofanya. Kwa hiyo, hapa hakuna mkanganyiko wowote ambao upo, hasara itakayofanyika pale lazima itakwenda sambamba na ukiukwaji wa maadili ya taaluma, ataadhibiwa kwa mujibu wa Ibara ya 67.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameomba pia Muswada uweke kifungu kitakachoweka haki ya mlalamikaji. Utaratibu wote kuhusu malalamiko dhidi ya Wathamini waliosajiliwa utaainishwa katika kanuni. Ukitaka kuweka kila kitu katika sheria tungekuwa na Muswada mkubwa sana ambapo sasa inakwenda kutokea sheria ambayo imejaa mambo mengi, lakini kuna mambo mengine ambayo yataainishwa kwenye kanuni. Kwa hiyo, hayo anayoyazungumzia yatakwenda kuonekana katika kanuni zitakapokuwa zimeandaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia pia Ibara ya 8 kuhusu Wathamini Wakuu Wasaidizi ambapo anapendekeza wawe na shahada moja na uzoefu wa miaka mitano isiwe sawa na sifa ya Mthamini Mkuu. Tukumbuke huyu Mthamini Msaidizi atakwenda kufanya kazi katika Ofisi za Kanda na tunatarajia atafanya kazi sawasawa na zile anazofanya Mthamini Mkuu aliyeko pale Wizarani. Kwa hiyo, ili aweze kufanya kazi yake vizuri na kwa uhakika ni lazima na yeye sifa zake zifanane na yule Mthamini Mkuu kwa sababu kule kwenye kanda atafanya shughuli zote za uthamini kulingana na majukumu atakayokuwa amepewa. Kwa hiyo, ukisema yeye awe na sifa za chini kidogo maana yake tutakuwa tunazishushia pia hadhi kanda zetu ambazo tumesema tuna kanda nane na kila kanda itafanya kazi zote kama ambavyo zitafanywa Wizarani. Kwa hiyo, bado sifa ya yeye kuwa sawasawa na Mthamini Mkuu tunasisitiza ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chumi pia ameongelea suala la Ibara ya 68 Mthamini Mkuu awajibike kwa uzembe wa kitaalam utakaosababishwa. Mthamini Mkuu kwa makosa ya kitaaluma atawajibishwa na Bodi na ndiyo maana katika uundaji wa Bodi pia wao watakwenda kuweka kanuni (rules) ambazo zinawasimamia hawa wathamini. Kwa hiyo, yeye adhabu yake itatokana na Bodi ambayo imemsajili na katika utendaji wake wa kazi yupo chini ya Bodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia suala la utata wa ukomo wa muda pale ambapo siku itakapoanza kufanyika maendelezo au katika muda wa miaka miwili iliyoelekezwa toka siku ya kujaza fomu na ni lini kipindi hicho kitaanza kuhesabika. Tumesema kipindi kitahesabika baada tu ya taarifa ya mthamini kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali, hapo ndipo tunapohesabu ile miaka miwili. Baada ya hiyo miaka miwili kwisha kama bado malipo ya fidia hayajafanyika maana yake ule uthamini tena hauhesabiki, utakwenda kuanza uthamini mwingine mpya lakini kwa kuzingatia ile hali halisi iliyokuwepo kwa wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama viwango vya malipo vitakuwa vimebadilika, basi tutachukua vile vilivyopo lakini kwa kuangalia ile hali halisi iliyokutwa wakati uthamini wa kwanza unafanyika. Hapatakuwa na zoezi la kurudi kule site kufanya uthamini upya isipokuwa uthamini ule ule uliofanyika mara ya kwanza ndiyo huo huo utakaorudiwa tena, lakini kwa kutumia viwango vipya ambavyo vimewekwa katika utaratibu wa bei zile za fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chumi kaongelea pia suala la notice kabla ya mthamini hajaingia kwenye eneo la wananchi na nini kifanyike. Tuseme hili limezingatiwa kwenye Jedwali la Marekebisho katika Ibara ya 55(1).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sophia Simba yeye ameongelea habari ya elimu itolewe kwa wananchi kuhusu haki zao juu ya sheria hii. Serikali inasema tumezingatia ushauri huu na utakwenda kufanyika kwa sababu kwa vyovyote vile unapokuwa na sheria mpya ni lazima pia elimu itolewe ili watu waweze kutambua. Kwa sheria hii kila mmoja nadhani atakuwa anaisubiri kwa hamu kwa sababu tayari watu wameumizwa sana, watu wamelia sana. Kwa hiyo, ushauri wake tumeuzingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwenda Ilala ili kuweza kumaliza tatizo nalo tumelizingatia tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia amezungumzia sheria zinazogusa masuala ya uthamini zihuishwe ili kuondoa masuala ya mgongano. Hili nalo tumelizingatia katika Jedwali la Marekebisho katika Ibara ya 72.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali yeye amezungumzia tafsiri ya property kwamba iongezwe baadhi ya maneno. Tafsiri inayopendekezwa haitofautiani sana na iliyopendekezwa kwenye Muswada. Hivyo Ibara ya 2 imetoa tafsiri kwamba ni mali zinazohamishika na zile zisizohamishika na aina za mali ambazo zinafanyiwa uthamini na pia inakuwa imezingatia matakwa ya tafsiri ambayo imependekezwa. Kwa hiyo, imeguswa hatuhitaji pengine kuweka ufafanuzi mwingine zaidi ya ule ambao upo kwa sababu unapozungumzia mali zinazohamishika na zisizohamishika tayari unakuwa umegusa aina nyingi ya mali ambayo ipo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia pia suala la ugatuzi wa madaraka katika huduma inayotolewa na Mthamini Mkuu iwe inapatikana hadi vijijini kwenye Halmashauri. Muswada unaopendekezwa Waheshimiwa Wabunge umezingatia suala hili katika Ibara ya 10, kutakuwa na Wathamini Wateule katika kila Halmashauri. Hawa wathamini siyo kwamba watakuwa chini ya Wizara ni sawasawa na kwenye Halmashauri zetu ambapo tunao Maafisa Ardhi Wateule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na kule kutakuwa na Mthamini Mteule kwa sababu Wathamini watakuwepo wengi, lakini lazima wawe na kiongozi wao ambaye atakuwa anawajibika pia katika kutia saini zile fomu za uthamini unapokuwa umefanyika uthamini. Kwa hiyo, hawa wapo kule kwenye Halmashauri siyo kwamba watakuwa Wizarani. Kwa hiyo, hili limezingatiwa pia katika muundo mzima ulivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 52 kuhusiana na ukomo wa miaka mitatu ni mingi. Jedwali katika Ibara ya 52 limerekebisha na tumezungumzia miaka miwili kama hapo juu nilivyozungumzia nini kinakwenda kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Richard Phillip Mbogo yeye anasema hajaona kifungu cha kukata rufaa kwa mtu ambaye hajaridhika. Sheria hii siyo kwamba itakwenda kusimama peke yake bali itakwenda kusomwa sambamba na sheria zingine na Sheria ya Ardhi imeweka utaratibu wa ukataji rufaa kwa watu ambao hawajaridhika na uthamini. Kwa hiyo, sheria hii siyo kwamba inakwenda kusimama peke yake. Katika maeneo ambayo pengine hayakutajwa hapa, basi kuna sheria ambayo inakwenda kugusa wapi mtu anaweza kwenda kukata rufaa au kulalamika pale ambapo anakuwa hajatendewa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 57, Mheshimiwa Phillip amezungumzia habari ya kwamba inaipa Bodi mamlaka makubwa na kufanya Bodi kusema itakavyo. Kwa hiyo, yeye anashauri kanuni ya Waziri itaje adhabu ambazo Bodi itazitoa. Muswada huu umefafanua taratibu na mamlaka kati ya Bodi na Waziri, kwa hiyo, hilo litazingatiwa katika utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia Ibara ya 49 anasema sababu za kufanya uthamini ziwe standard na zitajwe katika kanuni zitakazotolewa na Waziri. Waheshimiwa Wabunge Ibara ya 49 imetaja madhumuni mbalimbali ya uthamini yanayotambulika kitaaluma. Kwa hiyo, haya yote yameorodheshwa na yatakwenda kufanyika kulingana na sheria itakavyokuwa, hatuhitaji tena kutaja moja baada ya nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Pauline Gekul yeye amezungumzia kwamba Wakuu wa Wilaya hawakutajwa. Hili litazingatiwa katika kanuni kwa sababu hata ile ya awali walivyokuwepo walikuwa wametajwa katika kanuni, hawakutajwa katika sheria. Kwa hiyo, bado wapo watafanya kazi zao, lakini watatajwa kwenye kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akauliza kwa wananchi ambao bado hawajalipwa fidia mpaka leo sheria hii ikishapita hatma yao ni ipi? Sheria hii itaanza kutumika pale itakapokuwa imetangazwa, kwa hiyo, kwa ile migogoro mingine yote ya nyuma ambayo ipo sasa, sheria ya zamani iliyopo itaendelea au tuseme sheria zilizopo za ardhi bado zitaendelea kusimamia hilo. Kwa hiyo, hapatakuwa na hitaji lolote la kuweka pale kwa sababu kuna sheria. Kama kuna mtu pengine anaona kwamba hajatendewa haki basi itashughulikiwa kwa njia ya kimahakama, anaweza akachukua hatua ya kwenda kulalamika lakini bado anaweza akatendewa haki kwa mujibu wa utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 7(2)(a), anasema kifungu kitaje aina ya adhabu. Hii imezingatiwa katika Ibara ya 67 ambayo imeainisha adhabu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia ukomo wa mwaka mmoja, hii imezingatiwa katika Ibara ya 52 ambapo tumetaja miaka miwili na siyo mmoja kama ambavyo anapendekeza na nimeshaliongelea hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akauliza endapo mtu alichukua ardhi kwa ajili ya maendelezo akaamua kuiachia ardhi hiyo nini hatma yake. Tunasema basi endapo mtu alisimamishwa kuendeleza shughuli zake halafu mtu akaamua tena kusema kwamba hafanyi tena hii kazi, akaamua kuachia basi huyu mtu anayo haki pia ya kushtaki kwa maana kwamba sheria zingine zitachukua hatua. Kwa sababu ni kitu ambacho alikisema anataka kukichukua halafu kaacha kuchukua na huyu kamkwamisha katika maendelezo yake na katika shughuli zake, basi anayo haki pia ya kulalamika katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezingatia yale yote aliyoyazungumza Mheshimiwa Maufi, nadhani amezungumzia Ibara ya 52 ukomo wa miaka, akazungumzia suala la Wathamini Wasaidizi kuepusha migogoro lakini kazungumzia pia suala la CV aliyepo, yeye anadhani anatosha. Basi vyombo vinavyohusika kwa uteuzi vitakuwa vimesikia kilio chako pengine inaweza ikawa kama unavyoomba lakini tuseme Inshallah Mwenyezi Mungu atabariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Omary Mgumba naye kazungumzia Ibara ya 52 ambayo tayari tumeshalizungumzia. Katika suala la CV kukaa na ule uthamini, tumesema ikishafika kwa CV haitakiwi izidi siku saba na itawekwa kwenye kanuni kwa sababu ni lazima izingatiwe kwa maana kama kazi yote imeshafanyika kazi yake yeye ni kujiridhisha, hatutarajii kwamba atakaa nayo muda mrefu. Kwa hiyo, ndani ya siku saba lazima awe amemaliza na ameitoa kwenda kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Silinde ameongea mambo mengi ambayo yana ushauri pia tunashukuru lakini kwa suala la uthamini kufanywa na makampuni mawili hilo ni kosa, hakuna mahali ambapo makampuni mawili yatafanya uthamini kwa wakati mmoja halafu useme ni uthamini umefanyika, hilo ni kosa tayari. Hiyo inaweza ikafanyika pengine kuona kwamba kuna kitu hakikwenda sawa, mtu ame-appeal basi inateuliwa kampuni nyingine au watu wengine kwenda kufanya lakini haiwezekani wathamini kutoka makampuni mawili kufanya kazi moja halafu tulinganishe kazi zao nani kasema vipi, hilo ni kosa pia katika taaluma ambayo wanakwenda kuifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini akasema anataka kujua pia thamani ya nyumba kabla ya mambo ya uthamini kuendelea. Tukumbuke kwamba unapotaka kujenga nyumba kuna mtu anayeitwa Quantity Surveyor ambaye anakuwa ameshaonesha kwenye bill of quantity. Kwa hiyo, masuala ya bill of quantity yale yale ndiyo yatakayokuwa yamechukuliwa kama thamani ya kile ambacho kimejengwa pale kwa maana ya nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Japhet Hasunga yeye amezungumzia muda, tayari tumekwishalizungumzia. Pia mengi aliyoyazungumzia masuala ya Bodi kujulikana kabla na kadhalika mengine yatazingatiwa kwenye kanuni kwa sababu huwezi kuya-mention yote kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, katika hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge sehemu kubwa tumezizungumzia kwa sababu karibu yote yanajirudiarudia katika maeneo yale yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Salma Mwassa kwa kuchangia na ameonesha Mheshimiwa ni mbobezi katika taaluma hiyo kama Mthamini na ali-declare interest na tumepokea ushauri ambao ameuzungumza. Pia napenda tu kumfahamisha yale aliyopendekeza tayari Jedwali la Marekebisho limeshayazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muundo wa Bodi amesisitiza kutaja habari ya wanne kwa watano lakini hakusema sasa wanne ni wanawake au wanaume, kasema tu nne kwa tano, kwa hiyo, inaweza ikawa wanawake watano wanaume wanne. Niseme hili ni katika zile barua za kutaka yale mashirika au zile taasisi kuleta majina yao. Kwa hiyo, Waziri anapowaandikia kuleta majina maana yake ni kwamba atakuwa ametaja pale kwamba angalau apendekezwe mwanamke lazima aseme. Unaweza ukakuta majina yaliyoletwa au yaliyopo karibu yote ni ya wanawake, tunaweza tukawa na Bodi ya wanawake watupu, tunaweza tukawa na Bodi ya mchanganyiko lakini hii pia inakwenda na sifa, lazima wawe na sifa zile zilizotajwa kwa maana lazima awe registered na anaweza kufanya kazi hii. Kwa hiyo, suala la gender litazingatiwa na linaendelea kuzingatiwa kutegemeana tu pia na qualification za watu ambao wapo. Hili tunalipokea na litafanyiwa kazi pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine yalijirudia, kwa hiyo nisingependa kuyazungumzia. Suala la muda wa valuation, Mheshimiwa Mgumba alikuwa anapendekeza hizi valuation zifanyike kwa muda wa miaka miwili. Huwezi kuwa na valuation ya muda mrefu namna hii, lakini hapa pia tunaangalia na scope yenyewe ya valuation. Unaweza ukawa na magari yako mawili, matatu huhitaji kuwa na muda mrefu. Kwa hiyo, muda utakuwa-determined pia na ukubwa wa kazi yenyewe wanayokwenda kufanya. Ukiweka miaka miwili kuna mingine ambayo unakuta ndani ya siku moja imefanyika, huhitaji kuwa na muda mrefu. Kwa hiyo, hili huwezi kulipangia kwamba baada ya muda huu iwe imekwisha kwa sababu ukubwa wa kazi yenyewe pia unategemea na namna ambavyo kazi inakwenda kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Japhet Hasunga ameongelea habari ya taarifa kuletwa hapa kwamba miezi mitatu ni kidogo. Hilo tumeliona na tumepokea ushauri wako. Ni kweli kwa sababu unapomaliza mahesabu ndani ya miezi mitatu yanatakiwa yawe yamekwenda kwa Mkaguzi wa Hesabu. Mkaguzi wa Hesabu huwezi ukampangia muda kwamba ndani ya mwezi mmoja awe amemaliza vinginevyo hesabu zitakuja hapa hazijakaguliwa. Kwa hiyo, tumeliona hili na tumeangalia pia taasisi nyingine zinafanyaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa NIMR wana miezi sita kwa sababu tunajua kwamba ukishamaliza ndani ya miezi mitatu umepeleka kwa Mkaguzi Mkuu kule naye ana muda wake wa kufanya hesabu na siyo kwamba ana ya kwako tu na taasisi nyingine zimepeleka pale, kwa hiyo tumeweka muda wa miezi sita…
Ndani ya miezi sita tuna imani kazi ya ukaguzi itakuwa imekwisha na Waziri atapata fursa nzuri ya kuzileta hesabu hizo Bungeni zikiwa zimekaguliwa. Kwa hiyo, tumechukua ushauri wake Mheshimiwa Japhet Hasunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mtuka kwa sababu yeye pia ni mwana taaluma wa uthamini, ushauri alioutoa tumeuchukua tutaufanyia kazi. Sehemu kubwa ambayo amezungumzia ni pale ambapo anasema kwamba Wajumbe wa Bodi wako tisa na zipo kama Kamati nne, sasa wakiunda Kamati zile ina maana Kamati moja inaweza ikawa na watu wawili au watatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ile Ibara ya 13 imeongelea kama Bodi itahitaji mtu pengine kwa taaluma yake kutakuwa na wale co-optedmembers kutoka nje ambaye atakuja tu pengine kwa ajili ya kutoa uzoefu wake katika taaluma fulani. Unaweza ukawa unafanya shughuli ya mambo ya mahesabu, unahitaji pengine mtu aliyebobea, kwa hiyo, atakuja kama co-opted member kuweza kutoa ushauri wake pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, habari ya kuwa na Wajumbe wa Bodi tisa hilo lipo kisheria, huwezi kusema kwamba utakuwa nao wengi zaidi ili uweze kuwa na Kamati zilizo na watu wengi, kwa hiyo, wanaweza wakawa watatu. Wala siyo vibaya mtu mmoja kuwa na Kamati mbili lakini bado wata-co-opt members kutoka nje pale wanapoona kwamba wanahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia suala la exemption ya fee kwa taasisi za Serikali na hasa zile zinazofanya uthamini wa mara kwa mara. Kama Serikali tumelichukua hilo na nadhani litakwenda kuwekwa katika kanuni kwa sababu ni kweli kuna maeneo ambapo unapofanyika uthamini wa mara kwa mara unaweza ukakuta kwamba ile taasisi haiwezi kulipia hizo fee ambazo unaziweka lakini nature ya kazi yake inataka aende kwenye shughuli ya uthamini. Kwa hiyo, hili tumelichukua litazingatiwa wakati wa kuweka kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hoja zile ambazo zimetolewa nadhani karibu sehemu kubwa tumezizungumzia na sehemu kubwa pia zitaonekana kwenye Jedwali la Marekebisho ya Serikali ambalo limeletwa. Changamoto kubwa ambayo inakuwepo katika kazi hii na ambayo imesababisha Muswada huu kuwepo, tulikuwa na makanjanja wengi ambao wanajiita Wathamini lakini ni Wathamini hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke pia taasisi zetu nyingi hasa za fedha zimeibiwa sana na hawa vishoka, sasa Muswada huu unakwenda kuweka nidhamu kwa taaluma husika. Kama wanataaluma wamekuwa wakitajwa na sheria nyingine na walikuwa kwenye Bodi ile ya ma-Quantity Surveyor lakini ukiangalia kazi zao zinavyofanyika wanahitaji kuwa na sheria yao ya kuwasimamia, kwa sababu sehemu kubwa pia hata Serikali imeingia hasara sana kwa watu ambao hawazingatii sheria na wakati mwingine hawana chombo kinachowabana au kinachowaongoza katika kazi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi Muswada huu ulivyokuja tunaomba sana Wabunge wote walione hili na wote ni mashahidi huko tuliko watu wanavyolalamika, wanavyoonewa na wanavyolalamikia ule uthamini ni kwa sababu tu baadhi ya watu siyo wote walikuwa hawafanyi kazi zao kwa weledi. Kwa hiyo, inabidi kuwaweka katika mfumo ambao watadhibitiwa na Bodi yao, lakini watadhibitiana wenyewe kwa sababu pia wana association zao lakini wataheshimu ile kazi ambayo wanakwenda kuifanya. Ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi, waweze kuheshimu taaluma yao, ni lazima kuwe na chombo ambacho kinawafuatilia na kuangalia namna ambavyo wanatekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue fursa hii pia kushukuru tena kwa mara nyingine na nikiwaomba Waheshimiwa Wabunge waone umuhimu wa kupitisha Muswada huu ili tuweze kufanya kazi katika taratibu ambazo zipo kisheria na watu wanabanwa, wanaheshimu na tupunguze pia migogoro ambayo imekuwa ikiwakwaza watu wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's