Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Ester Alexander Mahawe

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante. Ninaomba tu niende haraka haraka kwa sababu, muda nao ni mfupi sana, lakini pia nashukuru kwa nafasi niliyoipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua suala la barabara ya Karatu - Mbulu limezungumzwa sana. Barabara hii ilimng‟oa Mheshimiwa Marmo baada ya miaka 25 kuwa Mbunge kwenye Bunge hili, kumbe ni kwa sababu tu mambo mengi kwa kweli hayapelekwi vile inavyokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa siyo hivyo tu, ilifika mahali wananchi wa Mbulu walikasirika wakaamua kuchagua debe la gunzi badala ya debe la mahindi mwaka 2010, lakini wamerudisha imani baada ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, Makamu wa Rais, kupita wakati ule wa kampeni na yeye binafsi kupita katika barabara ile ya Magara akaona jinsi ambavyo anapita juu ya maji, alipofika daraja la Magara, akaahidi wananchi ya kwamba daraja hilo lazima litatengenezwa katika kipindi hiki. Tunamshukuru sana pia Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, kupitia kwa Waziri wake wa Ujenzi nina hakika ya kwamba, hili litakuwa limemgusa kwa namna ya pekee maana tumelisema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili wa daraja la Magara kuna huduma muhimu kama shule na kituo cha afya, ambako wakati wa masika watu wa upande mwingine wa kutoka Mbulu hawapati huduma stahiki, wanafunzi wanashindwa kwenda shule wakati wa masika mpaka masika itakapokwisha. Tunaomba, haidhuru tujengewe daraja lile kama hatutaweza kupata barabara kwa kiwango cha lami ili kwamba wananchi hao waweze kuunganishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hiyo haitoshi; daraja hili upembuzi yakinifu ulikwisha kukamilika na kwa namna hiyo kwa ajili ya ahadi ya Serikali ya tangu mwaka 2011 wakati wa Rais Mstaafu Kikwete, wadau mbalimbali kama TANAPA waliweza kusogeza huduma zao karibu. TANAPA wamefungua geti na REA tayari wamepeleka umeme pale wakijua kwamba daraja hili linatengenezwa karibuni ili wananchi wa pale wapate kuhudumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tena habari ya barabara ya Mbulu - Haydom. Haydom kama tulivyosema ni Hospitali ya Rufaa, ni hospitali kubwa inategemewa na mikoa kama minne, tunaomba tusaidiwe ili kwamba, wannchi wetu waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ninaomba nizungumzie suala la FastJet. FastJet kwa kweli ni karaha, tunaambiwa kwamba hapa ni suala la soko, haiwezekani. Msafiri gani anasafiri bila begi?

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwanza kabisa naomba nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Mungu wa mbinguni kwa ajili yangu na wengine wote tuliojaliwa kuingia mwaka 2016 na kuletwa humu na wananchi wetu. Zaidi sana nielekeze pia shukrani zangu za dhati kwa Chama cha Mapinduzi ambacho kimenipatia fursa hii ya kuwawakilisha wanawake wa Manyara. Vilevile niwapongeze wanawake wa Manyara kwa kunipatia nafasi hii ili nije niwawakilishe katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba nielekeze michango yangu moja kwa moja nikianza na elimu. Naomba ku-declare interest ya kwamba mimi ni mwekezaji wa ndani katika masuala ya elimu, kwa maana ya shule za binafsi. Nipende kuanza kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako ambaye ameweza kusikiliza kilio cha Watanzania cha kuondoa GPA na kurudisha mfumo wa division. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichokuwa kinafanyika ni sawa na kuvalisha mtu mchafu gauni la gold. Kwa hiyo, niseme tu Mheshimiwa Profesa Ndalichako na timu yako hongereni sana maana mmedhamiria kuboresha elimu ya nchi yetu Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile hakuna nchi ambayo imewahi kuendelea duniani pasipo kuwekeza kwenye elimu, hata maneno matakatifu yanasema; “Mkamate sana elimu usimwache akaenda zake maana yeye ndio uzima wako.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu, kulingana na Mpango uliopo mbele yetu wa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imeazimia kuwekeza sana kwenye elimu kwa kuanza kutoa elimu bure, basi nafikiri ni wakati muafaka kuangalia changamoto zinazokabili tasnia ya elimu nchini. Kwa hiyo kwanza kabisa, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona ya kwamba, potelea mbali vyovyote inavyoitwa ya kwamba ni kupunguza makali kwenye elimu ama ni elimu bure, lakini iwavyo vyovyote ili mradi mtoto wa Kitanzania sasa anakwenda kupata elimu bila vikwazo vya aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwaambie tu ndugu zangu Wapinzani, msibeze kila kitu kinachofanywa na Serikali hii, Serikali inajitahidi sana ninyi si Mungu ama malaika ambapo mngepata nafasi hii kwamba mngeweza kuchange dunia in a day. Kila kitu kinakwenda taratibu, hatua kwa hatua, changamoto zilizopo kwenye elimu bure zinafanyiwa kazi na zinakwenda kwisha. Kwa hiyo, tambueni juhudi za Serikali kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye mchango wangu wa elimu. Naomba sasa pia Serikali ijitahidi sana kufanya kazi na sekta binafsi maana kuna wadau wengi sana wamewekeza kwenye elimu na ifike mahali watu hawa waonekane kama siyo competitors isipokuwa ni partners wanaoweza kusaidia kusomesha watoto wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu wawekezaji wa ndani katika suala la elimu wanakabiliwa na kodi zisizopungua 13, ndiyo maana inaonekana watu hawa wanatoa elimu kwa gharama ya juu sana mpaka mambo ya ada elekezi yanaingia humu. Shule za binafsi zinalipa property tax, income tax, service development levy, city levy, land rent, mabango ya shule yale yaliyo kwenye TANROADS tunalipa kwa dola. Sasa sijui mambo ya dola yanakujaje tena na halafu inaitwa TANROADS halafu tunalipa kwa dola, sasa si tuite tu USROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kodi ya corporate tax, working permits kwa walimu ambao siyo Watanzania. Mwalimu mmoja mpaka uweze kumpata anatumia sio chini ya shilingi milioni saba ndipo aweze kupata working permits na residence permit. Wakati huo huo tuna upungufu wa walimu wasiopungua laki tisa, tulionao ni laki mbili thelathini na nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna upungufu wa Walimu wa sayansi na hisabati wasiopungua elfu ishirini, Wizara ama nchi ina uwezo wa kutengeneza Walimu wasiozidi elfu mbili kwa mwaka. Kwa hiyo, tunachukua note less than ten years kutengeneza Walimu tunaowahitaji wa sayansi. Hii imekuwa pia changamoto kubwa kwa ajili ya maabara ambazo tumezijenga majuzi kati, tuna maabara kila mahali sasa, lakini changamoto kubwa imebaki kwa Walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali sasa kama inawezekana Serikali ione umuhimu wa kupunguza gharama za kuwapata Walimu kutoka nchi jirani kwa gharama ndogo residence permit na working permit ili waweze kusaidia katika shule zetu.
MHE. WAITARA M. MWIKABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kidogo suala la afya. Naomba katika suala la afya kwa sababu Serikali pia imeamua kuwekeza sasa kwenye afya ya wananchi wake. Nizungumzie kidogo hospitali ya Hydom, hospitali ya Hydom ipo katika Mkoa wa Manyara lakini ina-save Mikoa ya Singida na Mikoa ya Arusha kwa maana ya wenyeji wa Karatu na maeneo mengine hata ya Meatu. Kwa hiyo, ifike mahali sasa Serikali isaidiane kabisa kama ilivyoahidi kwenye mfumo huu wa PPP kusaidia hospitali ya Hydom kuendelea kutoa huduma njema na toshelevu kwa wananchi wake wa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tena kidogo suala la utalii, utalii wetu umekuwa na changamoto nyingi za kuandamwa na kodi nyingi, mfano wa TALA Licence ni dola 2000 kwa mwaka bila kujali anayelipa ni mzawa ama mageni. Nashauri Serikali ifike mahali wazawa wapewe first priority na kwa gharama rahisi kidogo ili wanapowekeza kwenye suala la utalii, basi vijana wengi wakapate ajira kupitia utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, magari mengi yamekuwa grounded, utalii umekuwa threatend na masuala haya ya Al-Shabab na hata Ebola. Wazungu kule nje hawajui umbali wa mahali Ebola ilipo na Al-Shabab ulipo, kwa hiyo, utalii umeshuka. Mimi naishi Arusha, kwa hiyo, niseme tu utalii umeshuka na imefika mahali hayo magari ya watalii sasa yamekaa tu yanafanya kazi za kubeba abiria wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto, nimesafiri mwenyewe Disemba mwaka uliopita, nimepita geti la Naabi pale wageni wanapoteza masaa yasiyopungua mawili mpaka matatu wakati wa kujiandikisha kuingia hifadhini. Sioni kwa nini hili liendelee wakati tupo kwenye dunia sasa ya sayansi na teknolojia. Muda mwingi mno unapotea foleni na jam inakuwa kubwa pale getini. Namwomba sana Mheshimiwa Jumanne Maghembe aweze kuangalia hilo ni kiikwazo. Mtu anayekwenda day trip kuingia pale chini crater na kurudi anapoteza masaa yasiyopungua matatu. Kwa hiyo, naomba hili nalo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba tu ni-declare interest mapema kwamba mimi ni mdau wa elimu pia, ni mwalimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa sera ya elimu bure ama elimu bila malipo, lakini inayogharamiwa na Serikali. Ninajua kila kitu kina mwanzo mgumu, mtoto hazaliwi leo akakimbia, hata nani angekuja na Sera hii na yeye angeweza kuyumbayumba hapa katikati. Hata ndege inapotaka kuruka huwa kuna tatizo mara nyingi na mwisho wa siku ikifika kwenye cruising point inasimama sawasawa na inakwenda. Mimi niseme tu niwatie moyo sana Mheshimiwa Waziri Mama Ndalichako pamoja na Mheshimiwa Engineer Mama Stella Manyanya, tunawaamini sana akinamama tuko nyuma yenu, pigeni mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kama inavyoeleweka elimu ni ufunguo wa maisha. Na hata neno la Mungu linasema, mkamate sana elimu asiendezake, mshike sana maana huyo ndio uzima wako. Ninaomba tu niiombe Serikali yetu sasa, hebu iwekeze sana kwenye elimu. Taifa lolote ambalo elimu yake haijakaa sawasawa linazalisha watumwa ambao watakwenda kutumia matajiri.
Kwa hiyo, mimi naomba tu Serikali yetu iendelee sasa, hii ingekuwa ni Wizara ambayo ilipaswa ipate bajeti kubwa kuliko Wizara nyingine zozote kwa umuhimu wake. Itoshe sasa walimu na ualimu kutokupewa kipaumbele katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu waliopata division four karibu na zero ndio wanaokwenda kusoma ualimu, unategemea nini na hawa watu ndio wanaotuanzishia msingi wa elimu nchi hii. Msingi wowote, hata kama ni nyumba unajenga huwezi ukaanza na msingi mbovu huko juu ukaweka zege, hiyo nyumba ni lazima itadondoka at the end of the day. Wale aliofaulu wakapata first class ndio wanaosubiri kuwapokea hawa watoto watakapofika Chuo Kikuu wakati hawa watoto wana mwanzo mbaya. Ifike mahali walimu nao wapewe nafasi ya ku-up grade, waweze kuboresha elimu zao na wapewe nafasi ya kwenda kujiendeleza. Na ikiwezekana hata watu wanaotokea division one na two waende wakasomee ualimu kwani kuna dhambi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo litazamwe sana, imekuwa hivyo kwa miaka mingi, tutaendelea kumtafuta mchawi, mchawi ni sisi wenyewe ambao tunaweka sera mbovu kwenye elimu, mwisho tunabakia kulalamika kila iitwapo leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa naomba tu nizungumzie pia, suala la mitaala. Mitaala hii imekuwa ikibadilishwa kila wakati, ifike mahali kuwe na Standing Orders kwenye Wizara ya Elimu, sio kila Waziri anayeingia anaingia na lake, tunachanganywa. Wakati tukiwa tunasoma wengi wetu tulioko hapa, nakumbuka kuna kitabu kimoja cha Kiswahili, kitabu chenye lile shairi linalosema karudi baba mmoja toka safari ya mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka nilikuwa naimba lile shairi nikiwa darasa la kwanza japo haikuwa level yangu kwa sababu, lilikuwa linaimbwa na ndugu zangu walionitangulia, kulikuwa kuna system nzuri. Nani ametuloga tukaondoa hiyo system? Tuangalie tulikoangukia ili tuweze kuboresha elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyowahi ku-declare interest, nimesema mimi ni mdau katika shule binafsi. Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 inaeleza kwamba shule sio biashara, shule ni huduma. Mwalimu Nyerere alisema watu wa asasi za kidini na wenye mapenzi mema waweze kuisaidia Serikali katika kutoa elimu, lakini leo tunashindwa kuelewa tumekuwa maadui? Kwa nini isifike mahali Serikali ikaona sisi ni partners badala ya competitors wakati tunawasomesha Watanzania hao hao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi peke yake ambayo shule zisizo za Serikali zinalipa kodi. Tumetembea nchi mbalimbali humu duniani, wanapata capitation grant kutoka kwenye Serikali zao, wanalipiwa walimu wao mishahara. Sisi tunafanya kila kitu wenyewe, tunakopa mikopo 24% interest kwenye mabenki, unanunua ardhi, unajenga shule, unalipa mishahara, unalisha watoto, unafanya kila kitu, leo tunaambiwa ada elekezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hii ni sawa na kwamba mtoto wako mimba umebeba mwenyewe, mtoto umemlea mwenyewe, shule umempeleka mwenyewe, anayekuja kuoa anakupangia mahari. Sasa namna hii tutafika? Ikiwa tu bado tuna ukakasi na tuna mahitaji makubwa kwenye shule zetu za Serikali, tutakapoanza tena kuzitibua hizi zisizo za Serikali ambazo hata kwa kunukuu tu niseme, shule 50 bora mwaka jana katika kidato cha nne zilikuwa zimetoka kwa shule binafsi, yaani tunavuruga huku wakati hata huku bado hatujaweka sawasawa! Kwa kweli, hatutendewi haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mlolongo wa kodi. Ada elekezi si tatizo, lakini mimi nilikuwa ninaishauri Serikali ituondolee huu msururu wa kodi ili kwamba tuwasaidie hata watoto watokao kwenye mazingira magumu. Niseme tu ukweli, mimi shuleni kwangu nina watoto 67 yatima ninaowa-sponsor mwenyewe. Watoto hawa wametelekezwa, ni shule ipi ya Serikali ambayo inaangalia hawa watoto wa namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamiliki wa shule binafsi wanajitahidi sana kuchukua watoto hawa. Serikali iondoe hizi kodi ili tuweze kuwasaidia watoto wengi wa namna hii, tupunguze wingi wa watoto wa mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalipa kodi zifuatazo, inawezekana Wabunge hawafahamu ama wananchi huko nje hawajui; na hizi kodi unapozi-impose kwetu hakuna mwingine atakayezilipa ni mlaji ambaye ni mzazi. Iko hivi, tunalipa Land Rent, Property Tax, Business License, Sign Boards Levy, City Service Levy, Corporation Tax, SDL, Workers Compensation Fund, Work Residence Permit Fee, Fire, OSHA, taja yote tunalipa. Tunafanya biashara gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaisadia Serikali kusomesha Watanzania, kabla ya hapo watu walikuwa wanasomesha watoto Kenya na Uganda. Tumejitoa muhanga, wengine wamekufa kwa pressure kwa ajili ya kudaiwa na mabenki, wengine mna ushahidi hapa wameshindwa kulipa madeni ya benki mtu anakufa na pressure na wamiliki wengi wa shule wana-suffer na masuala ya pressure na sukari kwa sababu ya ugumu wa kuendesha hizi shule. Leo ni nani mwenye shule ambaye ana biashara nyingine pembeni ya uendeshaji wa shule? Kama ulikuwa unaendesha nursery school uta-up grade utafungua primary, bado ni elimu ileile! Utatoka primary utaanzisha secondary, utatoka secondary utaenda colleges! Yet tunawasomesha Watanzania hawa hawa, kwa nini Serikali isitupatie dawati pale Wizara ya Elimu, ili kwamba, na sisi tuweze kutoa maoni yetu pale? Ili kusaidia mitaala hii inayotungwa watu wakiwa wamejifungia vyumbani bila kupokea maoni ya wadau wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilifanyika semina ya walimu wa darasa la kwanza na la pili hapa Dodoma, hatukuelezwa watu wa shule binafsi kwamba, kuna semina ya namna hiyo na wakati kwenye shule zetu kuna wanafunzi wa namna hiyo. Tunatengwa, sisi tumebaki yatima, Serikali ituangalie sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia tukaambiwa tupake magari rangi ya njano, tunaongezewa gharama, gari moja ni shilingi milioni tatu mpaka tano, mwingine ana magari 50 ni shilingi ngapi hizo? Nani atazilipa kama sio mzazi wa Kitanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi tukubali, kama ni hiyo ada elekezi basi ije tujue kwamba ada elekezi imekuja, lakini hatulipishwi kodi za namna hii zinaumiza sana. Tuna madeni kwenye mabenki kwa ajili ya kujenga madarasa wanakosoma watoto wa Kitanzania, hata mtu akifa leo anaacha shule inaendelea kusomesha Watanzania, lakini wewe umekufa na pressure kwa ajili ya uendeshaji wa shule za namna hii. Tutaendelea hivi mpaka lini? Itafika mahali hawa wadau watafunga hizi shule zao basi turudishe watoto Kenya na Uganda kama ndicho tunachokitafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa shule yenye watoto 350 ambao ada yake labda makusanyo kwa mwaka ni kama shilingi milioni 216, lakini shule kama hii inalipa kodi shilingi milioni 85, kwa faida ipi anayotengeneza mwenye shule? Weka tu chakula cha mtoto shilingi 10,000 hata kwa siku 90 anazokaa mtoto shuleni ni shilingi ngapi? Tunaumizwa. Ifike mahali sasa kilio chetu kisikilizwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nilikuwa nafikiri there is no fair play here. Wizara ya Elimu ama TAMISEMI ina shule zake, watu binafsi wana shule zao, lakini anayetu-monitor ni Wizara ya Elimu. Ni sawa na mchezaji wa simba awe referee wakati yanga na Simba wanacheza, hivi kweli hatapendelea timu yake? (Makofi)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaomba dakika zangu kumi, kila nikichangia ninapewa dakika mbili, dakika tano wakati wengine wametumia dakika kumi; naomba unitendee haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpe tu pole Mbunge wangu Mheshimiwab Issaay, inatia hasira wakati mwingine lakini pole sana kaka yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema, ni kweli kwamba sekta ya utalii inatoa mchango wa asilimia 25 ya pato la fedha za nje katika nchi yetu, lakini ni kweli wakati mwingine inakuwa inaumiza baada ya kuona kwamba uharibifu mkubwa unafanywa na wanyama... Wabunge naomba tusikilizane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu mkubwa unafanywa na wanyama, lakini badala yake fidia ama kifuta jasho kinachotolewa ni kweli kwamba ni kidogo sana. Hii ndiyo inayopelekea kwa kweli watu kupata shida wakati wa kampeni za uchaguzi baada ya kuona kwamba hawatendewi haki. Inafika mahali labda wanyama wanaonekana wa thamani kuliko mwanadamu. Ni kweli kwamba hili linapaswa kuangaliwa kwa umakini sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme kwa upande wa Wilaya ya Babati Vijijini, wanyama walifanya uharibifu na Mheshimiwa Jitu Soni kwa zaidi ya miaka mitano amekuwa akifuatilia kifuta jasho cha wananchi husika, lakini katika pesa ambazo zinafikia zaidi ya shilingi milioni 100 ameambulia kupata shilingi milioni 12, tunaomba Wizara hii sasa iweze kuangalia namna gani hawa wananchi walioathirika wanaweza kupata fidia hiyo japo kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitoe shukrani za dhati kwa TANAPA kwa kuweza kufungua geti la Sangaiwe pamoja na geti la Mamire ili kuweza kuruhusu wananchi kufanya biashara zao ndogo ndogo. Niombe Wizara iweze kutusaidi kukusanya hiyo 0.3 levy ili kwamba mapato haya yaweze kuwa ya msaada kuliko inavyofanyika sasa, maana hoteli zinazozunguka hifadhi hizo zimekataa kata kata kulipa tozo hizo za 0.3 percent.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo naomba pia niseme miaka michache iliyopoita wakati wa Operation Tokomeza mama mmoja kule katika Kata ya Galapo, Mkoani Manyara aliauwa, ikaundwa Tume ya Kijaji mpaka sasa hatujapata jibu lolote kuhusu mauaji yale. Tunaomba Wizara itusaidie kujua nini kiliendelea kuhusu mauaji yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na zaidi sana naomba ni-declare interest kwamba mimi pia ni mdau wa utalii. Kuna utitiri mkubwa wa kodi zisizopungua 15 katika uwekezaji huu wa utalii. Haiwezekani wananchi wetu wakalifikia goli la kuondokana na umaskini wakati kodi ni nyingi kupita kiasi. Mheshimiwa Mchengelwa ametoka kuzungumza habari ya night bed levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui ni nini maana ya mtalii. Inawezekana mtu akitoka Arusha kwenda Dar es Salaam kwenda kumuuguza mgonjwa wake Muhimbili na akawa analala kwenye hoteli pale Dar es Salaam anaweza akawa anaitwa mtalii. Tatizo ni kwamba kodi hii haiko-fair. Kama ni Mount Meru Hotel inalipa one point…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi hii ya night bed levy kwa kweli imekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wadogo. Unakuta mtu hoteli yake anauza vyumba kwa shilingi 30,000 au 50,000 analipa the same amount na mtu ambaye ana hoteli ya kitalii, au let us say hoteli ya Mount Meru ama hoteli nyingine kubwa za nyota nne au nyota tano. Sasa usawa uko wapi? Hili litazamwe na Wizara hii, Mheshimiwa Maghembe tunaomba ulitupie jicho, night bed levy imekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wadogo kama wale wenye guest houses wanatozwa kodi kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo huo niseme pia TALA license imekuwa ni kilio cha muda mrefu. Hapo Kenya wanatoza dola 300 kwa TALA license, lakini pia wanatoza kwa gari hawatozi kwa kampuni. Huku kwetu una gari moja, tano, mbili, mia tano unatozwa dola 2,000 kwa nini? Hili kimekuwa kilio kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulipia TALA license unalipa land rent, unalipa tax zote 15, huyu mtu anapataje faida? Anawezaje kutusaidia kuongeza ajira kwa vijana wetu? Nilisema tena watu wengi wameweka magari yao nyumbani, wameshindwa kufanya biashara ya utalii kwa ajili ya utitiri wa kodi. Ifanyike review kwenye kodi hizi ili utalii wetu uweze kuleta tija katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu, inawezekana sana kuhakikisha kwamba pia na misitu yetu inatusaidia. Ukienda nchi za watu watoto wanagombana na wazazi wao kubadilisha ipad, laptop mpya, smart phones, sisi tunajadili habari ya dawati wakati misitu iko hapo. TFS wanakusanya zaidi ya shilingi bilioni 50, ni ukataji wa miti tu unaendelea, hakuna miti inayorudishwa kupandwa. Tutakwenda hivi mpaka lini? Mtoto kukaa kwenye dawati Tanzania inakuwa ni privilege, kweli? Tutaondoka lini huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nafikiri kwamba tunaweza kurekebisha hali hii, kama tuna sera mbovu basi tuziangalie tena, tuzirekebishe ili kwamba yote yanayoendelea katika nchi hii yawe ni kwa maslahi ya Mtanzania maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme haraka haraka juu ya Mlima Hanang. Mlima ule ni wa tatu kwa urefu hapa Tanzania, lakini kuna uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea katika Mlima Hanang. Tunaomba ikiwezekana mlima huu ukabidhiwe kwa TANAPA ili waweze kuulinda maana uharibifu unaofanyika pale ni mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nisiendelee sana, niwaachie na wenzangu wengine dakika chache zilizobaki.
Mheshimiwa Mwenyekiiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kwanza niwapongeze tu walioandaa bajeti hii, lakini pia nielekeze zaidi mchango wangu kwenye suala zima la afya. Afya ni jambo la msingi sana kuzingatiwa katika uwekezaji wowote ule unaotakikana kama tulivyosema kwamba tunataka kutengeneza Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Tanzania ya viwanda ambayo tunataka kuitengeneza bila kujali ama kuweka kipaumbele kwenye afya za watu wake ambao wengi ndio wazalishaji, wengi ndio wanaofanya kilimo cha mkono, ama ni wakulima wadogo wadogo ambao wako vijijini; hawa watu tusipowapelekea zahanati za kutosha, tusipopeleka Vituo vya Afya vya kutosha, tusipowapelekea watumishi wa kutosha wa kada za afya, hawa watu wanawezaje kusaidia uzalishaji na hatimaye viwanda vyetu vikafanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona upungufu kidogo katika bajeti yetu hii kwamba ingawa Serikali imeweka kipaumbele kwenye Sekta ya Kilimo na kuainisha kwamba mazao ya kilimo yatakuwa moja ya malighafi kwenye viwanda hivyo, bado vipaumbele vinaenda kwenye kujenga reli, barabara, Viwanja vya Ndege na kadhalika; lakini kwenye vyanzo vya kilimo ambavyo ndivyo vitakuwa malighafi, kusababisha uzalishaji ukue hakujawekewa mkazo huku; na asilimia 80 ya wanawake walioko kijijini ndio wakulima, lakini bajeti hii haioneshi ni jinsi gani afya ya mwanamke huyu imezingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi upande wa Mkoa wa Manyara na Wilaya zake zote, hatuna watumishi wa kutosha katika kada ya afya na hatuna vituo vya kutosha. Kwa mfano, katika Kata ya Eshikesh, mama mjamzito anatembea kilometa 40 kwenda kwenye Zahanati ya Yaeda Chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya hii ya Mbulu Vijijini haina Hospitali ya Wilaya wala gari la wagonjwa. Akinamama hawa wanapata shida kusema ule ukweli; siyo Mbulu tu, tuna maeneo kama Simanjiro, mahali ambapo gari la wagonjwa ni moja, hawana Hospitali ya Wilaya, wanatumia Hospitali ya KKKT. Mama akishindwa kujifungua, anatakiwa apatiwe operation lakini anatakiwa alipe shilingi 400,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi yule mama wa Kimasai anayetembea na punda, anayepoteza muda wote kwenye maji, ni saa ngapi ametafuta shilingi 400,000 za kuweza kumsaidia yeye kwenda kujifungua? Nafikiri tungehakikisha kwamba kipaumbele kinawekwa kwanza kwenye afya, watu wetu wakiwa na afya njema watazalisha kwa tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, nizungumzie hili suala la asilimia tano ya akinamama na vijana. Tulijinadi sana kwenye kampeni zetu kupitia asilimia tano kwa akinamama na vijana. Sasa inaonekana sehemu kubwa ya own source inakusanywa na Serikali Kuu. Changamoto ipo kubwa; mara nyingi, hata leo Mheshimiwa Umbulla ameuliza hapa, akinamama ama Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye Kamati ya Mipango na Fedha ya Halmashauri zetu, ndiyo maana hizi fedha zimekuwa misused wakati mwingi. Hakuna mtu wa kuzisimamia; tunaziona tu kwenye makaratasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwahakikishia akinamama ambao ndio wamekipa Chama chetu kura nyingi ya kwamba tunakwenda kudai asilimia hizi. Je, tunarudije kwao? Tunaomba hizi fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya akinamama, kwa mwaka huu haidhuru, basi kwa mara ya kwanza zifike katika ukamilifu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna shilingi milioni 50 kila Mtaa na kila Shehia na kila Kijiji. Nako tulijinadi kwa sababu ni ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tu kwamba pamoja na Mikoa 10 inayotaka kutengwa hapa ya pilot run, nashauri ili wananchi wetu mioyo yao isikunje ngumi, kwa nini isitumike mikoa yote, halafu haidhuru vichukuliwe vijiji hata kama ni vitano kwa kila mkoa? Maana changamoto na mazingira hayafanani. Haidhuru na sisi tupate cha kusema tukirudi kwa wananchi wetu. Hawa kumi tu, tuseme Mkoa wa Manyara, haufanani na Dar es Salaam; Mkoa wa Manyara haufanani na Kilimanjaro; changamoto zinatofautiana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sijajua kwamba labda hawa walioweka hivyo kwamba wanachukua mikoa kumi wamezingatia nini. Ila nashauri tu, kama inawezekana, mikoa yote ichukuliwe na vijiji haidhuru vitano vitano kila Mkoa ili tuone kwamba tunawezaje kuokoa maisha ya wananchi wetu kupitia mikopo hii ya shilingi milioni 50 kupitia SACCOS.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna mgongano wa maslahi. Pale mwongozo unapoelekeza kuwa mapato yote ya mamlaka ya Serikali za Mitaa yawasilishwe Serikali kuu, changamoto kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kwamba fedha hizi huwa zinachelewa sana kuteremka chini huko kwenye Halmashauri zetu. Sasa itakuwaje ikiwa fedha hizi zinakusanywa na Serikali Kuu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasoma kiambatanisho cha masuala ya afya; elimu ya watoto wetu wa kike ni tatizo. Imeelezwa sana, kwamba tunaomba kodi ziondolewe kwenye vifaa vyote vinavyosaidia akinamama pamoja na mabinti mashuleni. Kwenye towel zao kodi iondolewe. Binti anakosa shule siku saba katika mwezi. Mwisho wa siku inaonekana watoto wa kike ni vilaza; kumbe ni kwa sababu hawa-attend shule inavyotakiwa kama wanavya-attend watoto wa kiume.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili litazamwe upya, tuwasaidie watoto wetu wa kike. Utakuta miundombinu kwenye shule, watoto 400 vyoo viwili au watoto 600 vyoo vitatu, watoto wa kike wanapataje kujisitiri? Je, bajeti hii inamwangaliaje mtoto wa kike? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kushea hii keki sawasawa, naomba tuwekeze zaidi kwa akinamama ambao ni waaminifu hata wanavyochukua mikopo kwenye mabenki, wamekuwa wakirejesha kwa uaminifu mkubwa. Kwa hiyo, naomba sana akinamama watazamwe kwa jicho la pekee ili waweze kusaidia pato hili la Taifa hasa kupitia kilimo na ujasiriamali. Hakuna asiyejua kwamba akinamama ndiyo wanaokimbia kimbia asubuhi mpaka jioni kutafuta riziki za familia zao, kupitia biashara ndogo ndogo. Akinamama hao watazamwe kwa jicho la pili ili waweze kusaidia katika kukua kwa uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna upungufu mkubwa wa urari baina ya matumizi ya kawaida na yale ya maendeleo. Matumizi ya kawaida ni karibu mara tatu ya yale ya maendeleo. Kwa hiyo, nashauri tu kwamba, bajeti hii iangalie ni jinsi gani inaweza ikawekeza zaidi kwenye bajeti ya maendeleo, japo imepandishwa mpaka asilimia 40, lakini kama inawezekana, iendelee kusogea hata ifike mahali iwe asilimia 50 kwa 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi naomba nisisuburi kengele inayofuata, niseme tu kwamba yangu ni hayo. Zaidi sana, nawalilia akinamama waweze kusaidiwa na bajeti hii pamoja na watoto wa kike ili waweze kupata elimu sawasawa pamoja na watoto wa kiume.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga hoja mkono.

Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni

MHE. ESTHER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa naomba niunge mkono hoja. Tunafahamu kabisa michezo ni furaha, michezo ni elimu na michezo ni afya, niseme tu kama nchi ni kweli kwamba tumechelewa kukubaliana na Azimio hili. Kwa hiyo, kwa kuwa imeletwa sasa basi niwaombe na Wabunge wenzangu kwa pamoja tupitishe Azimio hili ili nchi yetu iweze kufaidika kama faida zilivyoorodheshwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme inafahamika kabisa kwamba madhara ya kutumia dawa hii ni makubwa kama yalivyoelezwa. Kama nchi sidhani kama tuna sababu ya kutokupitisha Azimio hili kwa sababu hatuna woga, tuna Watanzania wachezaji wazuri sana ambao wameiletea nchi hii heshima kwenye football, kwenye riadha na kadhalika. Kwa uchache tu nitambue heshima waliyoileta wanariadha hawa wafuatao:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna watu kama akina Simon Robert, John Stephen, John Bura, Nada Saktai, Focus Wilbroad Aweso, Francis Nada na Zebedayo Bayo, hawa watu wamefanya kazi kubwa katika nchi hii. Niseme tu tusiogope; tuwekeze kwenye michezo, tunao watu ambao bado wanaweza wakailetea nchi hii heshima.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia michezo inahitaji uwekezaji, tuendelee kuwekeza kama ilivyokuwa zamani kwenye UMISHUMTA na UMISETA tuendelee kutengeneza vijana wenye vipaji kuanzia katika utoto wao ili waweze kuiletea nchi yetu heshima na wakipata kuwekewa misingi na miundombinu mizuri nina hakika wala hatuhitaji kutumia madawa ya kuongeza nguvu maana vijana hawa watakuwa wameandaliwa vizuri na hatimaye wataweza kufanya vizuri katika michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwamba hawa watu waliowahi kuiletea nchi yetu heshima hatukuona namna yoyote tukiwaenzi, namna yoyote ya kuona kwamba walileta mchango mkubwa wa fedha, wa heshima katika nchi yetu; hii inawakatisha tamaa wale wengine wadogo ambao wanaibuka katika tasnia hii ya michezo kama riadha, football na michezo mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri kwamba juhudi za hawa watu zitambulike, kuwe na namna maalum ya kuhakikisha kwamba hawa watu wanakumbukwa. Sasa hivi hawa karibu wote niliowataja hapa ukiacha Filbert Bayi ambaye atleast yeye amejiingiza kwenye masuala ya elimu, wengine wote wanapata shida, wanakufa katika umaskini uliotopea kule vijijini, wengine wamejiingiza kwenye ulevi na maisha duni yanawaandama kama watu ambao hawakuwahi kuifanyia nchi hii kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme tu kwamba hakuna asiyefahamu kwamba Manyara kwa ujumla, mimi of course nimetoka Manyara, kwa ujumla Manyara imeiletea sana heshima Tanzania katika suala zima la riadha. Kwa hiyo naendelea kuiomba Serikali iendelee kuwekeza katika Mkoa wa Manyara tupate Sports Academy kule Manyara ambayo inaweza ikasaidia kuendelea kuibua vipaji. Bado tuna watoto hawa wa kifugaji wengi tu ambao kwa mazingira ya Manyara hayana tofauti na mazingira kama ya Ethiopia, wanaweza wakaibeba nchi hii na bado heshima ya nchi ikarudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashukuru tu kwa mchango huu na naunga mkono hoja.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kuunga mkono hoja kwa kuipongeza Serikali ya CCM chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli, kwa kazi kubwa wanayofanya ya kurejesha nidhamu na uwajibikaji katika nchi yetu. Japokuwa hali hii kwa kuwa ni ngeni kwa wengine na kinyume cha matazamio yao wameitafsiri katika namna hasi. Ombi langu, tuendelee hivi hivi huku tukibaki katika lengo letu la kumkomboa Mtanzania kutoka kwenye lindi la umaskini, ujinga na maradhi na kuwapeleka kwenye nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijikite kwenye hoja yangu. Bila kusahau naomba ku-declare interest kwamba mimi ni mdau wa elimu wa shule binafsi. Naomba nielekeze mchango wangu kwenye ushirikiano kati ya Umma na Binafsi (PPP) katika uwekezaji kwenye sekta zote muhimu nchini ikiwemo elimu, afya, viwanda, miundombinu na kadhalika. Nafahamu kuwa Serikali yetu sikivu ya CCM ina nia njema sana katika hili hivyo naomba nitoe ushauri ufuatao:-
(i) Kubainisha wazi na bayana majukumu ya kila upande katika utekelezaji wa sera ya PPP katika sekta ya elimu (utungaji wa sera, sheria, miongozo, uchangiaji wa gharama za elimu, usimamizi wa taasisi za elimu, upimaji na udhibiti ubora);
(ii) Kuwa na mifumo imara na endelevu ya mawasiliano (dialogue structure) baina ya pande zote mbili ili kupeana taarifa za mara kwa mara na uzoefu mbalimbali wenye tija kwa maendeleo ya nchi; na
(iii) Kuwe na mifumo imara yenye kujengeana uwezo baina ya pande zote mbili kwa vile kila upande unacho cha kujifunza kutoka kwa mwenzake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Serikali itakapofungua milango katika PPP ni hakika tutaona mafanikio na mabadiliko makubwa ya kiuchumi ndani ya muda mfupi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri pia Serikali kuweka vipaumbele vinavyotekelezeka. Mpango huu ni mzuri lakini umekuja na vipaumbele vingi sana. Tukiendelea hivi tutabaki kupapasa tu na hatutafika tuendako.
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo yetu ya kodi si rafiki hali inayopelekea kutishia kuongezeka hali ya rushwa hasa katika chombo chetu cha kodi (TRA). Kuwe na mazingira rafiki na dialogue structure baina ya TRA na mlipa kodi badala ya vitisho na kuuza kwa mnada mali za wafanyabiashara kwani kwa kufanya hivyo Serikali inakosa pesa na wale wafanyabiashara wanakuwa wamefilisika na mwisho tunaishia kuumia kama nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu ina mpango wa kutupelekea kwenye Tanzania ya viwanda, basi niishauri Serikali iweke nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji ili viwanda vyetu viweze kufanya kazi kwa kipindi chote cha mwaka. Endapo hatutawekeza kwenye kilimo cha kisasa ambapo asilimia 80 ya Watanzania ndiyo wahusika wakuu katika hili, ni bayana hatutaweza kumwondoa huyu Mtanzania maskini kwenye lindi la umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nitoe ushauri wangu kwa Wizara ya Afya. Ni dhahiri kwamba ni pale tu watu wetu watakapokuwa na afya njema ndipo tutakapoweza kufanikiwa katika mambo yote. Mtu mgonjwa asiyeweza kutibiwa kwa wakati hawezi kamwe kufanya uzalishaji wa aina yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nigusie suala la ukosefu wa dawa MSD. Suala hili linaipeleka Serikali yetu pabaya sana. Naomba hili suala la dawa lifanyiwe kazi kwa gharama yoyote ile ili kulinusuru Taifa na vifo vya watoto na kizazi kijacho kwa kukosa chanjo za muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo haya ya Mpango bado hayajaweka bayana ni jinsi gani huduma ya maji zitafika vijijini ili kumtua ndoo mama wa Kitanzania. Asilimia zaidi ya 80 ya muda wa wanawake hawa wazalishaji inapotea kwenye kusaka maji usiku na mchana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tena kupongeza juhudi za Serikali kwa jinsi pia inavyoshughulikia suala zima la mikopo ya elimu ya juu inayotishia amani ya wapiga kura wetu. Busara ya hali ya juu itumike ili kumaliza tatizo hili na kila mhusika abaki akiwa ameridhika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niunge mkono hoja, ahsante sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's