Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Esther Lukago Midimu

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya. Vile vile nampongeza Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anazozifanya, wananchi wote wanaziaminia. Pili, nawapongeza akinamama wa Mkoa wa Simiyu kwa kunipa kura ili niweze kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu na nawaahidi utumishi uliotukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza sana Mawaziri wote wawili kwa hotuba yao nzuri. Naanza na uboreshaji wa maslahi ya Madiwani. Madiwani wanafanya kazi katika mazingira magumu sana hawana hata usafiri. Naiomba Serikali yangu sikivu iweze kuwapatia hata pikipiki ili waweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya Wilaya ya Maswa; hospitali ya Wilaya ya Maswa ina tatizo la umeme, umeme siyo wa uhakika unasuasua, miundombinu imekuwa ya kizamani. Naiomba Serikali yangu iweze kuboresha miundombinu ya hospitali ya Wilaya ya Maswa. Vile vile hospitali ya Wilaya ya Maswa ina majengo ambayo yameshakamilika, jengo la OPD, theater na wodi ya wazazi, lakini hayajaanza kutumika. Naomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi hayo majengo yaanze kutumika yaweze kuhudumia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika Wilaya hospitali ya Maswa ina tatizo la maji. Jambo la kusikitisha Maswa Mjini kuna maji na hospitali ya Maswa na Maswa Mjini ni pua na mdomo, lakini hospitalini hakuna maji. Naiomba Serikali yangu ifanye haraka ivute maji kutoka pale Maswa Mjini ipeleke hospitali ya Maswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya katika Wilaya ya Itilima, Wilaya ya Itilima tunayo zahanati kubwa sana Kata ya Luguru. Hiyo zahanati ina majengo mengi sana. Tunaomba kibali kwa zahanati hiyo ili iweze kupandishwa hadhi iwe kituo cha afya. Tuna jengo kubwa la upasuaji limejengwa na Mfuko wa Mkapa Foundation na vifaa tiba tayari vipo, tatizo hatuna wataalam wa upasuaji. Naiomba Serikali yangu itupelekee Madaktari Bingwa wa upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kituo cha afya Zagayu. Kituo cha afya cha Zagayu kina wafanyakazi watano ambapo mahitaji ni wafanyakazi 32. Tunaomba mtupelekee watumishi 32 ili waweze kuhudumia vizuri. Tunacho kituo cha afya Kata ya Nkoma, tunaiomba Serikali itupatie kibali kama kuna uwezekano tukipandishe hadhi kwa Wilaya ya Itilima tuwe na Hospitali ya Wilaya, kwa sababu wananchi wa Itilima wanahangaika sana, wakipata matatizo wanaenda kutibiwa Bariadi, Somanda. Tukikipandisha hadhi kile kituo cha afya cha Itilima, nina imani hata msongamano wa wagonjwa Somanda utapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya maji; naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuahidi kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kuleta Mkoani Simiyu kupitia Wilaya zake za Busega, Bariadi, Maswa, Itilima na Meatu. Naiomba Serikali yangu ihakikishe hayo maji itakapovuta, maji yapitie kwenye shule zote za Mkoa wa Simiyu za Sekondari, vituo vya afya vyote na zahanati ili yaweze kusaidia kwa sababu maji ni muhimu kwenye vituo vya afya na hospitali, ukizingatia na sera yetu ya sasa hivi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kila Kijiji kutakuwa na zahanati na kila Kata kutakuwa na kituo cha afya. Naomba na maji yafike huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna vijiji katika Wilaya ya Maswa havina maji kabisa ambavyo ni Gudekwa, Masanwa, Mwabalatulu na Isegenge, akinamama wa vijiji vile wanahangaika sana. Naiomba Serikali yangu iweze kuchimba visima virefu kwa hivyo vijiji nilivyovitaja ili mradi akinamama waweze kupata maji. Wameshindwa kufanya kazi zao za ujasiriamali na mambo mengine ya maendeleo wamebaki kutafuta maji, wanasafiri kilometa nane mpaka kilometa 10. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya elimu; naishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kujenga shule nyingi za Kata, naipongeza sana. Naiomba Serikali yangu kama kuna uwezekano kwa Mkoa wetu wa Simiyu iweze kutenga kila Wilaya shule ya bweni kwa watoto wa kike, kwa sababu watoto wa kike wanahangaika sana, watoto wa kike tukijenga shule za bweni tutawaepusha na vishawishi vya chipsi na bodaboda wakiwa wanarudi makwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Bariadi tuna Chuo cha Ufundi, Bunamhala, chuo kile naomba kiboreshwe, vijana wengi wapate ujuzi ili waweze kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mkoa wetu una changamoto, una upungufu wa nyumba za Walimu 1,471, madarasa 563 na matundu ya vyoo 2,107. Tunaiomba Serikali iweze kutuletea pesa kupitia TAMISEMI ili tuweze kukamilisha ujenzi huu. Vile vile naomba Serikali iweze kuweka Chuo cha VETA Mkoani Simiyu na iweze kutuletea pesa haraka sana tuweze kujenga hospitali ya Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, naunga mkono hotuba ya Waziri Mkuu kwa asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa namshukuru Waziri kwa hotuba yake nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nianze kuchangia mchango wangu. Mkoa wetu wa Simiyu ni wakulima wazuri wa pamba lakini cha kusikitisha zao hilo linaenda kufa kabisa, wananchi wamekata tamaa kabisa kwa sababu ya bei kushuka. Suluhisho pekee la bei ya pamba ni kutuletea kiwanda cha nguo na nyuzi. Mkituletea kiwanda cha nyuzi, nina imani vijana wengi watapata ajira na bei ya pamba itapanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Simiyu tuna viwanda vitano vya kuchakata pamba. Naona na wenye ginneries wamekata tamaa, nashindwa kuelewa kwamba zao la pamba likifa viwanda vile vitafanya kazi gani. Naomba mtuletee kiwanda cha nyuzi na kiwanda cha nguo, nina imani hata wao watauza marobota yao karibu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mkoa wetu ni wa wafugaji, tunaomba mtuletee kiwanda cha nyama. Nasema hivyo kwa sababu wafugaji wetu wanaibiwa sana, wakipeleka mnadani ng‟ombe mmoja anauzwa shilingi laki mbili mpaka shilingi laki tatu lakini ng‟ombe huyo huyo ukimlisha na kumnenepesha ukimpeleka kiwandani unamuuza shilingi laki nane mpaka shilingi milioni moja, naomba mtuletee kiwanda cha nyama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Simiyu kuna akinamama wajasiriamali wakubwa na wazuri sana, wana vikundi vikubwa. Naomba Serikali iwaletee viwanda vidogo vidogo vya SIDO vya kusindika mazao ili waweze kujikwamua na umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwangu yalikuwa ni machache tu ya kuomba viwanda, Serikali yangu ni sikivu, naomba ituletee viwanda hivyo katika Mkoa wetu wa Simiyu. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazozifanya. Kwa namna ya pekee nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya. Kwa muda mfupi amefanya kazi na zimeonekana, Mwenyezi Mungu ambariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza ahadi ya kuleta maji kutoka Ziwa Victoria mpaka Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake tano za Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu, na hela tayari zimeshakuja, wananchi wana imani na Rais wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu maji yakifika Mkoa wa Simiyu iweze kusambazwa kwenye shule za msingi na sekondari pamoja na vituo vya afya na zahanati. Nasema hivyo kwa sababu wanafunzi wanahangaika sana, muda mwingi wanachota maji usiku, asubuhi wakienda darasani wanashindwa kusoma wanasinzia tu, ni bora Serikali itoe kipaumbele katika mashule yetu yapate maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Simiyu ni wachapakazi wazuri na ni wakulima wazuri, nina imani maji yakifika watalima kilimo cha umwagiliaji, njaa itakuwa ni ndoto katika Mkoa wa Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali yangu kwa ajili ya kutuletea shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ukarabati wa mabwawa Wilaya ya Itilima na mabwawa yale ni Mwamapalala, Nobora, Sunzula, Sawida, Chinamiri na Lugulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu sasa iweze kusambaza maji kwenye kata ili kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mwanamke ndoo kichwani. Iweze kusambaza kwenye kata zifuatazo, kata za Nkuyu, Migato, Mwaswale, Mwamtani, Nkoma, Kindilo na Sawida. Maeneo haya niliyoyataja wanawake wanahangaika sana, muda mwingi wanaupoteza kutafuta maji kuliko kufanya kazi za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ukizingatia wanaochota maji ni wanawake si wanaume. Mwanamke anachota maji usiku, saa zingine anakutwa na matatizo huko njiani. Naiomba Serikali iweze kuzingatia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's