Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Kiswaga Boniventura Destery

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake kwa kuniwezesha kufika ndani ya ukumbi huu na nawashukuru wananchi wa Jimbo langu la Magu kunipa Ubunge ili niweze kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwa kadri ambavyo imejikita kuonesha kwamba Watanzania wana mahitaji. Imegusa mahitaji ya kila Mtanzania lakini pia imeonesha huruma kwa Watanzania, naipongeza sana. (Makofi)
Sisi Watanzania tumepata kiongozi. Vitabu Vitakatifu vimeandika, ukisoma 2 Timotheo 2:20, unasema; “Nyumbani mwa Bwana kuna vyombo vingi, viko vyombo vya dhababu, vipo vyombo vya miti.” Mheshimiwa John Pombe Magufuli ndicho chombo cha dhahabu ambacho Mwenyezi Mungu Watanzania ametuandalia. Naomba tumuunge mkono wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na maji. Jimbo langu la Magu lina matatizo makubwa sana ya maji kama zilivyo wilaya zingine. Sisi wenye nguvu ukirusha jiwe linakwenda moja kwa moja ndani ya maji lakini Wilaya ya Magu haina maji. Tumeahidiwa na viongozi waliopita, Rais wa Awamu ya Tatu, Rais wa Awamu ya Nne mpaka leo Magu haina maji. Bahati nzuri Mheshimiwa John Pombe Magufuli wakati wa kampeni naye ameahidi.
Mimi sina shaka kwa sababu hotuba hii amezungumzia sana suala la maji na sina shaka kwa sababu Waziri wa Fedha ni type ileile ya Mheshimiwa Profesa Muhongo kwamba hataki ubabaishaji kwenye makusanyo ya fedha, nampongeza sana. Ili miradi hii itekelezeke lazima fedha zikusanywe na nawaomba wakaze kamba wasilegeze hata siku moja kwa sababu nchi hii ilikuwa imefikia pabaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua asali ni tamu sana lakini wako watu ambao hawanywi asali lakini kila mmoja anakunywa maji. Hebu tuangalie sasa suala hili, Serikali ifanye kila linalowezekana hata kukopa Benki ya Dunia ili kuweza kutekeleza miradi ya maji iliyoko kwenye nchi hii hasa Wilaya ya Magu. Wilaya yangu vijiji vingi havina maji na Wanamagu wana uvumilivu ukubwa sana na hili ndilo lililonileta Bungeni kwamba maji ndilo hitaji la wananchi wa Magu. Ili nirudi tena hapa Bungeni 2020 lazima maji yapatikane. Waziri wa Maji, Waziri wa Fedha, nisaidie hili ili Mheshimiwa Rais aliposema kwamba tumwachie jambo hili la maji Magu litekelezeke kweli kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo mradi ambao umeanza upembuzi yakinifu leo ni miaka miwili watu wanachakata, wanachakatia wapi? Mheshimiwa Rais alisema hawa watu wanaochakata watachakatia nje, Mtaalamu Mshauri anachukua miaka miwili anafanya upembuzi yanikinifu bila kukamilisha, hii ni kweli? Hii Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Pombe Magufuli ya „Hapa Kazi Tu‟ imwangalie huyu Mtaalamu Mshauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu bure Serikali imeanza vizuri. Mpango wa capitation ulikuwepo tangu mwaka 2002 lakini naomba niishauri Serikali kwamba wakati inatoa dola 10 kwa kila mtoto…
NAIBU SPIKA: Naomba umalizie Mheshimiwa.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Exchange rate ilikuwa ni Sh1,000 leo ni Sh.2,200. Kwa hiyo, waangalie hali ilivyo sasa ili kumudu uendeshaji wa shule hizi ili ziweze kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja lakini nina mambo mengi ya kuzungumza, kumbe ningeanzia mchana, basi niishie hapo.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu anayeneemesha neema nyingi nami akanineemesha neema ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze hotuba za Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwa kadri zilivyojielekeza kuhudumia na kutatua kero za wananchi. Nianze na eneo la elimu bure. Safari moja huanzisha nyingine, tumeanza, pamoja na changamoto, inapaswa sasa kama Serikali ione namna ambavyo itaongeza fedha hizi ili ziweze kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati suala hili la MEM linaanza 2002 capitation tulikuwa tunapeleka dola kumi kwa kila mwanafunzi. Wakati huo exchange rate ilikuwa ni shilingi1000 leo ni shilingi 2000. Maana yake kwamba ili zitosheleze lazima tupeleke mara mbili. Naishauri Serikali iweze kuliona hili ili iweze kuongeza kiwango hiki kinachotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure chekechea hadi kidato cha nne ni sahihi. Mimi najiuliza hivi mtoto wa maskini huyu anapofika kidato cha tano anatajirika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie kwa upana wake hata kama siyo bajeti hii, bajeti ijayo iweze kuwaangalia watoto hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo la maji, maji ni hitaji la kila mmoja wetu tulioko mahali hapa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Maji alitembelea Wilaya yangu ya Magu kwa kweli alinitendea haki na Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali ijielekeze kuhakikisha kwamba wale ambao tunazungukwa na Ziwa Victoria tunapata maji ya kutosha na wengine ambao wanazungukwa na Ziwa Tanganyika nao wapate maji ya kutosha. Haiwezekani watu tunasimama tunaliangalia ziwa lakini maji hatuna, hamtutendei haki.
Naishauri Serikali hii iangalie kwa sababu uchumi wa nchi hii wachangiaji wakubwa ni akina mama lakini inapofika saa tisa za usiku akina mama wanaondoka kwenda kutafuta maji. Ninapotembelea vijiji vyangu wanalalamika wanasema hata watoto asubuhi hawawaoni hawa akina mama. Naomba sana Serikali iangalie hata kama ni kukopa kwenye mifuko ya fedha tuwekeze kwenye maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishati. Namshukuru sana Naibu Waziri wa Nishati na Madini alitembelea Jimbo langu, tukatembea naye siku moja vijiji kumi, alinitendea haki Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uchumi ukue umeme unahitajika kila mahali. Tunapozungumzia viwanda vidogo wakati mahali ambapo vinahitajika viwanda hivi vijengwe umeme haupo. Niombe Serikali kwa jitihada ilizonazo kupitia REA Phase II na III tuweze kukamilisha vijiji vyote kwa kuvipatia umeme. (Makofi)
Naomba nizungumzie afya. Hotuba ya Waziri inasema vijiji 8,043 havina zahanati. Wewe ni shahidi kwenye vijiji vyako Jimbo la Bariadi ni vijiji vikubwa sana ukizingatia na Jimbo langu la Magu nalo lina vijiji vikubwa, kuondoka kijiji kimoja kufuata huduma ya afya kijiji kingine unachukua kilometa 15 na hakuna hata zahanati za private, hakuna hata maduka ya dawa. Niishauri Serikali kwa sababu wananchi wa Wilaya ya Magu wameanzisha maboma ya kutosha ya zahanati tupewe fedha za kukamilisha zahanati hizo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la viongozi wa kisiasa kwa maana ya Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji na Waheshimiwa Madiwani. Katika uongozi mgumu duniani sijui dunia au Tanzania hii, hakuna uongozi mgumu kama Mwenyekiti wa Kitongoji, Mwenyekiti wa Kijiji na Mheshimiwa Diwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa lazima tuelewane vizuri na naomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu kuna kipengele kwenye viapo vyenu kinasema utamshauri Mheshimiwa Rais kwa hekima, hapa ndipo mnatakiwa mumshauri kwa hekima. Mwenyekiti wa Kitongoji yeye ndiye anayefanikisha ujenzi wa madarasa, ujenzi wa zahanati na vitu vyote vilivyoko kule. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kitongoji leo mwananchi akikamatwa mahali popote yeye ndiye anayekwenda kuandika dhamana adhaminiwe, huyu ni mtu muhimu sana. Mimi leo nikitaka kufanya ziara yeye lazima aweko. Naomba Serikali tuelewane iweke siyo fedha nyingi, tuanze na za kuanzia ili hawa watu waweze kupata posho zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mheshimiwa Diwani mimi nimetokea huko niseme tu kwamba hawa watu ndiyo walionileta hapa kwamba tumpeleke mwenzetu anayetufahamu. Diwani aliyefanikiwa kuwa na gari halali usiku kucha gari yake ndiyo ambulance kupeleka wagonjwa hospitali. Leo maslahi yake tunayaona kama yanatosha hayatoshi. Niombe sana wasaidieni watu hawa na ndiyo wanaojenga siasa kwenye maeneo yetu, ni Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Madiwani. Naomba tuelewane vizuri hapa katika bajeti hii au bajeti ijayo. (Makofi)
Niendelee kusema kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ndiyo ambayo wananchi walikuwa wakiingoja, ni Serikali shupavu, Serikali ya kazi tu. Mwaka fulani Mheshimiwa Rais Nyerere alitangaza Kilimo cha Kufa na Kupona, Rais Magufuli ametangaza kazi ya kufa na kupona, huyo lazima tumpongeze. Wale wanaobeza ni mioyo ambayo haina shukurani. Maandiko Matakatifu yanasema mioyo ambayo haina shukurani hukausha mema mengi. Naiomba Serikali hii ya Awamu ya Tano, wale watu ambao hawashukuru ikaushe miradi ya maendeleo isipeleke kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu aombaye hupewa, huwezi kuwa unasimama unatukana Serikali inayokujali halafu unapewa miradi. Naomba Serikali hii isiwape miradi watu hawa ambao hawana shukurani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa wakisema Serikali hii haina meno, Serikali imeanza kutumbua majipu wao wanakuwa mawakala wa wale waliotumbuliwa.
Haiwezekani, tuipe heshima Serikali iweze kufanya kazi. Naomba tunapopanga miradi hii isimamiwe…
Na Wizara ili tuweze kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Dakika tano ni chache, nianze tu kwa kusema kwamba Wilaya za Magu pamoja na Wilaya ya Ilemela inavyo visiwa, vinahitaji vipate vivuko kwa sababu visiwa hivyo ni vijiji. Katika Kisiwa cha Besi, Wilaya ya Ilemela, pamoja na Kisiwa cha Ijinga, Wilaya ya Magu, tumeomba kwenye RCC lakini mpaka leo na ninaangalia kwenye bajeti sioni, naomba Mheshimiwa Waziri aliweke hili ili tuweze kusaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ambayo imeahidiwa na Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano, barabara ya Ngudu - Magu pamoja Nhungumalwa kwa kiwango cha lami. Upembuzi yakinifu umeshakamilika, lakini nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijawahi kuona fedha za kutosheleza ujenzi huu wa mradi wa barabara ya lami. Naomba sasa aliweke ili ahadi ya Mheshimiwa Rais ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Barabara ya Magu - Kabila - Mahaha; barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Magu pamoja na Bariadi. Mheshimiwa Rais ameahidi lami, lakini sijaona hata kwenye utaratibu wa upembuzi yakinifu, bali kuna hela kidogo tu ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza barabara hii. Naomba barabara hii nayo ya Magu - Kabila - Mahaha, iwekwe kwenye mpango mzima wa lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara inayofungua Mkoa wa Simiyu, kwa maana ya Bariadi - Salama - Sayaka - Bubinza na Kisamba. Barabara hii ni barabara ya karibu sana ikitengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuepusha watu wa Bariadi kwenda mpaka Lamadi; ni barabara muhimu kiuchumi kama tunataka kujenga uchumi kwenye kanda hiyo. Tunaomba sana barabara hii iwekwe, lakini kipande hiki cha Sayaka - Bubinza - Kisamba, huwa tunaomba kwenye Road Board, kwa sababu ni kipande kidogo, kipande daraja kihudumiwe na TANROADS, lakini mpaka leo hakijaweza kuwekwa. Niombe Mheshimiwa Waziri akiweke kipande hiki, ili kiungane na wenzetu wa Simiyu na kiwekwe lami kipande hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara ikijengwa tunaweza kuondoa msongamano wa Mwanza. Watu wa kutokea Mara wanapokwenda airport hawana sababu ya kuingia mjini…
MWENYEKITI: Ahsante! Ahsante,

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza nianze tu kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati kadri ambavyo imejielekeza namna ya kutatua matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Profesa Muhongo anaondolewa kwenye Wizara hii wananchi wa Tanzania walisikitika sana na wakati amerudishwa wananchi wa Tanzania wameshukuru sana, kwa hiyo, endelea kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba katika Wizara, Wizara hii ni ngumu sana, dunia yote hutafuta madini, hutafuta kupata utajiri kupitia madini, hii ni Wizara ngumu sana. Kwa hiyo lazima tukupongeze wewe pamoja na Naibu wako kwa kadri ambavyo mnachapa kazi Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina vijiji ambavyo vimepitiwa na REA Phase II, lakini vijiji hivyo ni Ng’haya, Bundlya, Kabila, Kigangama na Kisamba zimewekewa nguzo chache sana na sehemu zingine hata shule za msingi, makanisa na zahanati hazijapata umeme. Shahidi ni Naibu Waziri wa Nishati, tulitembelea maeneo hayo. Naomba mtakapokuja kujibu mseme pia kwamba mnaongeza vijiji hivyo ili vikamilike vionekane kwamba kweli REA Phase II, imevitendea haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyo vijiji viwili pia ambavyo havikuwekewa umeme, umeme huu umekwenda kwenye vijiji vingine, kwa mfano Nyashigwe, iko kwenye REA Phase II, lakini umeme wake umekwenda kitongoji cha Mawe ambacho ni kijiji cha Welamasonga. Kwa hiyo, kijiji hiki hakijawekewa umeme, mtakapokuja kutoa majibu mniambie je, mtakiingiza kwenye Phase III, aumtakipelekea umeme sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kijiji kingine cha Kitongo Ndagalu ambapo makao makuu ya kijiji ambayo ni center kubwa haijawekewa umeme, umeme umewekwa kitongoji cha Misungwi, napo mje mniambie ili wananchi hawa waweze kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ha utainga sasa hivi REA Phase II, basi uingizwe REA Phase III. Lakini umeme ambako wamekamilisha kama Kabila, Ng’haya haujawaka, naomba Wizara kwa maana ya Waziri muhimize ili kama umekamilika umeme huu uweze kuwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Magu havina umeme asilimia 70, ninaomba sasa kupitia REA Phase III, vijiji hivi viwekewe umeme, nimeongea na wewe Mheshimiwa Waziri, nimeongea na Naibu Waziri, nimeongea na Meneja wa Kanda, naomba sasa vijiji hivi kwa kweli viweze kupatiwa umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni declare interest nilikua mchimbaji mdogo mwaka 1993 katika machimbo ya Ulyankulu na huko ndiko nimeanzia maisha. Wachimbaji hawa wanateseka sana kila siku, wanahama kila leo, lakini wachimbaji hawa ni ajira yao. Tunapozungumzia Tanzanite, wachimbaji wale sio wa Arusha tu, wa Magu wapo, wa Bariadi wapo, wa Sengerema wapo. Tunapozungumzia almasi, wachimbaji wa nchi nzima wako kule na wa Magu wapo, tunapozungumzia dhahabu, wachimbaji wa Magu wapo. Kama walivyolalamika Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ninaomba hawa wachimbaji wadogo wadogo kama azma ya Serikali ni kuwatafutia maeneo iwatafutie maeneo ili waweze kupatiwa maeneo ya uchimbaji, hiyo ndio ajira yao ya kudumu.
Mhehimiwa Mwenyekiti, yako malalamiko kwamba mikataba ya madini tunapata fedha kidogo sana kama nchi. Ninaomba sasa haya nayo ni maeneo ambayo yanalalamikiwa na kila mmoja wetu ili yaweze kupitiwa na kuangaliwa ili Serikalil iweze kupata mapata ambayo kwa kweli yatanufaisha Taifa letu la Tanzania. Maana tunaweza kuwa na madini baadaye tukaachiwa mashimo na nchi isinufaike. Naishauri Serikali iangalie kwa uhakika ili kuhakikisha kwamba mikataba hii inawanufaisha watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ambayo yamewekewa umeme wa REA wananchi wanashukuru sana, sasa niguse tu kwamba tutakapokamilisha maeneo ya vijiji, viko vitongoji ambavyo navyo ni kama vijiji, kwa hiyo, tusiishie REA Phase III, lazima tuende na REA Phase IV. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo na niunge mkono hoja, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Maji kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameiwasilisha. Kwa kweli imesheheni mambo mengi ambayo yakitekelezwa yatatatua kero za Watanzania na kidogo sana katika Jimbo la Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, Magu kwa ujumla ina shida ya maji, miaka yote tumekuwa na shida ya maji. Kilio kikubwa cha Wan-Magu ni maji, mpaka najiuliza kwamba Wilaya ya Magu imekosea nini, imeikosea nini hii nchi mpaka tupate matatizo makubwa ya maji kiasi hicho ambapo Wilaya ya Magu imezungukwa na maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Waziri nimeona mradi mkubwa wa maji Magu Mjini, ambao utasaidia wananchi wa Magu wapatao 36,000, lakini wananchi 340,000 hawatakuwa na huduma ya maji, ninasikitika sana na ukizingatia kwamba hata Wilaya ambazo zinanizunguka majirani zangu kwa maana ya Wilaya Bariadi ambako wewe uko, nayo haina maji, Wilaya ya Busega nayo haina maji, Wilaya ya Kwimba nayo haina maji. Kwa hiyo, najikuta niko katikati pale hata majirani hawawezi kunisaidia, wewe unajua kabisa kwamba bhuzengano bhutikubhwaga makira. Lakini huo uzengano hauna chochote napata taabu sana, yaani kwamba ujirani huwa haunyimani mambo mazuri manono. Kwa hiyo, napata taabu kwa sababu majirani zangu hawana maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa maji kwa kweli kama hotuba inavyosema kama kweli wakandarasi wameshapelekewa vitabu, kama kweli unaweza kuanza mwaka huu utarudisha imani kwa wananchi wa Magu kwamba sasa wanaanza kupata huduma ya maji. Lakini kama nilivyosema wananchi 340,000 bado wanakunywa maji ambayo wanachangia na ngo‟mbe, mbwa na fisi huko vijijini, wana shida kubwa ya maji. Ni vema katika Mji wa Kabila ambao wewe unaujua vizuri Mahaha, Ng‟haya, Nkhobola Serikali ikawa na mpango mzuri wa kuwafikishia maji wananchi hawa hata kama siyo bajeti hii kwa sababu naona bajeti hii imelenga kutekeleza miradi hii, bajeti ijayo nifikiriwe vizuri zaidi katika Wilaya ya Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kijiji cha Nyang‟hanga ambacho kimetoa Wabunge wa Nne tangu Magu ianze kupata Wabunge, wote wanatoka kijiji hiki cha Nyang‟hanga hakina maji. Kijiji hiki Mheshimiwa Dkt. Festus Bulugu Limbu alifanikiwa kuchimba visima virefu vya maji, vina maji mengi ya kutosha kwa ajili ya kusambaza katika kijiji hiki cha Buhumbi pamoja na kijiji cha Nyang‟hanga, lakini kila mwaka nina- declare interest kuwa nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri tulikuwa tukiomba maombi maalum ya shilingi milioni 700 ili mradi huu uweze kusambaza maji hatukupatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri anihurumie Jimbo la Magu, atuhurumie kijiji hiki atafute fedha mahali popote ili aweze kutusaidia shilingi milioni 700 tuweze kusambaza maji katika kijiji cha Nyang‟hanga na Buhumbi.
Tunao mradi ambao unaendelea wa Sola Bubinza, huu ni mradi ambao umeanza tu lakini umekosa fedha, Wizara inajua, Katibu Mkuu anajua na Mheshimiwa Waziri anajua. Ninamuomba sasa kwa sababu ni mradi ambao ulikuwa unaendelea kuliko kupoteza fedha nyingi za walipa kodi wa nchi hii, tupewe fedha kwenye bajeti hii ili mradi huu uweze kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika sana, mradi huu unaopeleka maji Magu chanzo chake kinatoka Kata ya Kahangala, kijiji cha Bugabu. Lakini Makao Makuu ya Kata ambayo ni kilometa nane tu kutoka pale chanzo kilipo au bomba litakapopita hakimo kwenye mpango wa kuwekewa maji, hii ni haki kweli? Niombe Waziri atafute kila linalowezekana ili Makao Makuu haya ya Tarafa ya Kahangala ambako maji yanatoka yaweze kupata maji ni hela kidogo tu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri asaidie jambo hili. Tunayo Kata ya Mwamanga ambayo nayo ilikuwa na Mradi wa Matokeo Makubwa sasa wa awamu iliyopita. Kuna miradi ambayo ilianza lakini fedha zake hazijapatikana, niombe kwenye bajeti hii ni vizuri tukamaliza viporo ambavyo vilikuwa vimeanzishwa ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa Lugeye Kigangama, Mheshimiwa Waziri alifika kwenye mradi huu na Mheshimiwa Lubeleje pia alifika kwenye mradi huu. Unadaiwa shilingi milioni 94 tu ukamilike, chonde chonde naiomba Serikali yangu ya kazi, Serikali ya Awamu ya Tano itupe hizo shilingi milioni 94 ili mradi huu uweze kukamilika. Tuna kiangazi kikubwa sana, kwa kweli katika Wilaya ya Magu la sivyo tutapata taabu haingii akilini, kwamba shilingi milioni 94 zinakosekana ili mradi huu uweze kukamilika maji yameshavutwa yameshaletwa kwenye tank ni kusambaza tu kuunganisha koki mbalimbali, naomba nisaidiwe na Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Sanjo inazungukwa na maji lakini haina maji, na Tarafa ile inaongoza kwa kupata kipindupindu kwa sababu wanatumia maji ambayo hayajatibiwa, Tarafa ile ina Mji wa Kisesa, Mji wa Bujola bado una shida kubwa ya maji. Population ya pale inazidi hata Makao Makuu ya Wilaya ya Magu. Ninaomba angalau utafutwe mradi ambao unaweza kutokea Ilemela, Buswelu, Nyamongolo ulete maji katika Mji wa Kisesa, lakini hata Lutale, Kongolo pamoja na Chabula nao wanahitaji maji haya ya kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, ninajua kwamba fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya maji ni kidogo, lakini zitaleta impact sana kama miradi hii itatekelezwa. Tuombe mahala ambapo sisi hatujapata fedha tufikiriwe sana bajeti ijayo ili tuwemo kwenye utaratibu wa kusaidiwa miradi hii ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Ziwa imebaki kuwa jina tu, Wilaya zake zote hazina maji tunahangaikia Sengerema…
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Ahsante sana.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijaanza kuchangia nianze kuweka rekodi sawa sawa. Hapa ndani kwa sababu kuna Wabunge wenzangu wakati mwingine wanasema kwamba Mawaziri waache siasa. Nataka niongee tu jambo hili; kwanza siasa ni taaluma; na sisi tuliopo wote hapa tumeingizwa kwenye siasa. Siasa ni ngumu sana, lakini ni nzuri sana, tatizo ni tunavyoitumia tu kama wenzetu wanavyoitumia vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupata Ubunge ni kazi kweli kweli na suala la kupata Urasi ni kazi kweli kweli! Sisi ambao tumepita kwenye mchakato huu tunajua joto lake. Kwa hiyo, hata wote tunapokuwa humu tumebeba mizigo; wa kuteuliwa, sijui wa kutoka group gani, inategemea mizigo hiyo ina uzito gani; lakini uzito wa Jimbo ni uzito kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba duniani kote hakuna mtu anayehitaji kulipa kodi. Hata vitabu vya dini vimezungumza sana suala la kulipa kodi na aliyekuwa akitoza kodi wakati wa Yesu alikuwa ni mtu ambaye anachukiwa na Umma wote. Kwa hiyo, Serikali kukusanya kodi isiogope, ni jambo la kawaida, ndiyo uhai wa Serikali. Naiomba sana Serikali hii isirudi nyuma, ihakikishe inakusanya kodi ili wananchi waweze kupata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la maji. Suala la shilingi 50 kuongezwa kwenye dizeli na petroli ili iende kugharamia maji, ninasikitika sana, kwamba Serikali imeona kwamba ikiongeza shilingi 50 italeta mfumuko wa bei. Nataka kuuliza au mmeshatuuliza? Sisi Wabunge humu ndio watumiaji wa mafuta. Tumeshakataa kuongezwa hii shilingi 50? Sisi tumeshakubali tuongezwe shilingi 50 kwenye petroli pamoja na dizeli ili kugharamia Mfuko wa Maji Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu inasema mita 400 wananchi waweze kupata maji. Kwa namna hii tunayokwenda, hatutaweza kuifikia hiyo sera na mwaka 2020 tutapata taabu kweli kweli kurudi humu Bungeni, kwa sababu wakina mama wanateseka kila asubuhi, kila saa kumi na moja wanakwenda kuteka maji. Tuwahurumie! Wanapoteseka akina mama na sisi akina baba tunateseka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja nimewahi kusema asali ni tamu sana lakini wako watu hawaitumii asali, lakini kila mmoja anaguswa na maji; awe mtumia gari, anaguswa na maji aoshee gari lake. Kwa hiyo, naishauri Serikali hii ya Awamu ya Tano, Serikali ya kazi; kwa sababu unaweza kuwa na Serikali sikivu, ikawa inasikia tu, isifanye kazi. Sasa hii ni Serikali ya kazi, ifanye kazi kuongeza shilingi 50 ili akina mama waweze kupata maji ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongea haya kwa sababu nimetoka Jimboni, hali ni mbaya, akina mama wanasumbuka na mimi nina hali mbaya! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ungenionea huruma ukanipatia chupa ya maji hapa ili niweze kuongea vizuri huku nakunywa maji. Naomba hili, wala halipaswi kujadiliwa, iongezwe shilingi 50 kwenye mafuta, wala tusijadili hili; kama haitaongezwa, kama kuna kushika shilingi, mimi nitashika shilingi kwa sababu ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia kwenye fedha za ujenzi wa zahanati. Ilani yetu inazungumza kwamba kila Kijiji kiwe na zahanati; kila Kata iwe na vituo vya afya. Humu tuliomo ndani humu na wengine tunachagua mahali pa kwenda kupata matibabu, lakini mwananchi wa kawaida, maskini, hana hata mahali pa kwenda kupata matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati ni jambo la muhimu sana kujenga ili kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma hii. Sasa kama Ilani yetu inazungumza kwamba tuwe na zahanati kila kijiji, tuwe na kituo cha afya, wananchi wameshaandaa maboma ya kutosha, wanasubiri fedha za Serikali ili Serikali iwaunge mkono; tupelekeeni fedha hizo ili kupunguza matatizo ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali imekuja na mpango wa kupunguza kodi kwenye mazao, lakini nimeangalia kwenye zao la pamba; kilichoondolewa kile siyo tija kwa wananchi. Umeondoa mwenge, umeondoa kikao ambacho ni fedha ambazo zinalipwa na jina, ni hela kidogo sana hizo. Tunazungumzia shilingi 400,000 kwa jina; hiyo inaongeza nini kwenye bei ya pamba?
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo kodi mbalimbali cess za Halmashauri, kuna CDTF, mfuko wa kuendeleza zao la pamba; hizi zote inapashwa Serikali ifidie ili mkulima aweze kupata bei nzuri. Tusipofanya hivyo, zao la pemba linakwenda kufa. Sasa mnapozungumzia viwanda, kwa mazao yapi? Mnapozungumzia viwanda, kwa sababu viwanda vinavyoongeza ajira ni viwanda ambavyo malighafi yake ni pamba. Hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie ili tuweze kuona ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia wakulima wa pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko kodi ambazo Mheshimiwa Rais alikuwa anasema ataziondoa; kodi zenye kero, lakini naona kama hatujaziondoa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wana shida, akina mama ntilie, sokoni wauza nyanya na michicha wana shida. Tungeangalia jambo hili kwa mapana yake, upo ushuru hauna tija, hata Halmashauri haiongezei kitu chochote. Naomba anakapokuja kumalizia hapa atuambie, hizi kodi ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi, ushuru wenye kero, utaondolewa kwa namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie tu kuongeza usajili wa bodaboda. Hili ni kundi ambalo ni maskini sana, lakini ni kundi ambalo linarahisisha usafiri wa wananchi wetu vijijini ambako gari hazifiki. Yapo maeneo barabara haziko; wanaotusaidia ni hawa watu wa bodaboda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunapoongeza usajili maana yake tunataka kuwapunguza hawa watu. Kama tungeacha kodi ilie ile, ingechochea kuingiza bodaboda nyingi zaidi, ikachochea hao bodaboda kununua mafuta mengi zaidi na kuongeza uchumi wa nchi hii. Naomba hili nalo liondolewe; halina sababu na halina tija sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamezungumza suala la CAG, na mimi naendelea kusema nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, chombo hiki ni muhimu sana; chombo hiki ni cha kitaalam. Mheshimiwa Profesa Muhongo anasema haya ni mambo ya kitaalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama haya ni mambo ya kitaalam halafu tunayapunguzia fedha, itakuwa ni aibu. Halmashauri zitakuwa na hali mbaya na Wizara zitakuwa na hali mbaya. Naomba fedha ziongezwe ili tuweze kuhakikisha udhibiti wa fedha hizi tunazozipeleka, zinakuwa na uhakika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo duniani huwa hayajadiliwi. Suala la mafao kwa Wabunge ni jambo ambalo duniani halijadiliwi. Ku-maintain Jimbo ni sawasawa na kujenga kiwanda cha kati. Wabunge hawa wabishe. Ku-maintain Jimbo ni sawa na kujenga kiwanda cha kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba hili liondolewe mara moja, halina mjadala, halina nafasi ili kuhakikisha kwamba Wabunge hawa sio pensionable. Mbunge hapa akienda kupigwa dafrao, unaweza kumshangaa, ni hali ngumu. Naomba hili kwa kweli lisiingizwe, wala lisijadiliwe na liondolewe mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naendelea sasa kuipongeza Serikali, kazeni buti kukusanya kodi ili huduma za wananchi zipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia.

Kwanza nianze na barabara yangu ya kutoka Magu - Kabila - Mahaha. Barabara hii ina kilometa 58, lakini mwaka huu haijatengewa fedha, matengenezo maalum au matengenezo ya mara kwa mara haina fedha. Nashukuru kwamba imetengewa fedha kwa ajili ya daraja ambalo Serikali inagharamika kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya daraja hili. Ninajua kwamba tayari upembuzi yakinifu umeshakamilika na mkandarasi ameshapatikana, tatizo ni fedha za kuendelea. Niiombe Serikali nikiamini kwamba bajeti ambayo tunayo tulitenga fedha kwa ajili ya kulijenga lile daraja angalau zitoke fedha za kuanzia lile daraja Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba tu Waziri kwa sababu sihitaji kulalamika, aiandike barabara hii ili aiwekee fedha angalau ipate fedha za matengenezo kwa mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii pia ni ahadi ya Rais kuwekewa lami alipokuwa kwenye kampeni Mheshimiwa Rais alipotembea aliona ametembea umbali mkubwa zaidi sana. Alipofika kule Kabila akasahau kwamba yuko Magu akasema yuko Kwimba, baada ya pale akasema basi barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami, naomba ahadi hii nayo iheshimiwe.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara hii ya Isandula - Ngudu ni barabara muhimu iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tangu 2005, hebu tupeni fedha ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara ambazo tuliziomba Road Board zipande kutoka Wilaya kwenda Mkoa, bahati nzuri Wizara yako Mheshimiwa Waziri ilileta wataalam wa kuzipitia, zikaonekana hizi zina qualify, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri sasa uzipandishe hizi barabara kwa sababu uwezo pekee wa Halmashauri hatuwezi kuzigharamia. Hizi ni barabara ya Kisamba - Sayaka - Salama na Simiyu kule Bariadi ni barabara muhimu sana ya kufungua uchumi. Tunayo barabara ya Ilungu kuelekea Kwimba mpaka Maswa ni barabara muhimu sana kiuchumi, tunayo barabara ya Kisesa - Kayenze - Ilemela inaweza kupunguza pia msongamano wa kuingia Jiji la Mwanza, tonayo barabara ya Nyanguge - Kwimba hizi barabara zote zime-qualify, ningetegemea kwamba bajeti hii zingeweza kupatiwa fedha, naomba zipatiwe fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara muhimu inayotoka Airport - Ilemela ambayo ikitengenezwa kwa kiwango cha lami mpaka Nyanguge inapunguza msongamano kabisa wa wananchi wote kutoka Musoma kuelekea Mwanza hawatapita Mwanza Mjini watakwenda airport itapunguza msongamano. Hebu muiweke vizuri kwa sababu tumeomba kila siku.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara ya kilometa
1.2 ya Kisesa – Bujora, barabara hii inapitiwa na viongozi wote wa kitaifa kila mwaka kwa ajili ya kwenda kwenye makumbusho, tumeiomba kama Road Board kila mwaka kiongozi wa kitaifa lazima apite, naomba na hii iingie ni kilometa 1.2.

Mheshimwa Naibu Spika, ahadi ya Rais ya kilometa tano za lami Magu Mjini, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri ulikuja Magu nikakutembeza kwenye barabara zile ukaziona zilivyo, hebu tusaidie kwenye bajeti hii angalau ahadi hii ya kilometa tano za lami ianze ili wananchi waweze kupata huduma inayokubalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi nataka nijikite kwenye taasisi hii ya marine. Taasisi hii ya Marine Services ina uhakika wa kuingiza kipato kwenye nchi hii, nina uhakika mkiijali inaweza kuchangia uchumi kwenye nchi hii pia shirika hili linaweza kujiendesha. Mheshimiwa Waziri hili shirika ni kama limetelekezwa, tunazo meli 15 katika maziwa yetu haya matatu, sekta binafsi wako ambao wana meli kule Ziwa Victoria wanafanya vizuri wana meli na kila mwaka wanaongeza meli, kwa nini Marine isihudumiwe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti iliyopita tulitenga fedha, lakini mpaka leo fedha hizi Marine hawajapewa taasisi hii. Ni kama dhahabu ambayo iko ndani hatujaipeleka sokoni, hebu tuisaidie Marine ili iweze kuchangia uchumi na iweze kujiendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya kabisa wapiga kura wetu kule ni wafanyakazi wa taasisi hii mishahara hawalipwi, bima ya afya wamefungiwa, kuna mambo kede wa kede. Ushauri wangu ni kwamba kwa sababu hii ni taasisi ambayo iki-link na bandari; ika-link na reli naamini mizigo yote ambayo inakwenda Uganda inaweza ku-support sana kupata fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunacho kivuko ambacho alikiongelea hapa Mheshimiwa Mabula, Ilemala pale tumeomba kivuko cha Kayanze, Bezi na Ijinga. Wananchi walioko visiwa vile ni zaidi ya wananchi huku wako 600,000 Bezi lakini na Ijinga wapo zaidi ya 400,000. Kwa hiyo, wakipata kivuko hiki kinatasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo Serikali imefanya, makubwa sana kwa muda mfupi na wala hayawezi kuelezeka. Na mimi nilikuwa najiuliza sana, Mheshimiwa mmoja alikuwa anasema kwamba kipindi hiki tumepata Rais wa ajabu, nilishindwa kumuelewa, lakini sasa nimeanza kumuelewa kwamba kweli tumepata Rais wa ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kinaitwa Bombardier ndege mbili zimekuja, nne bado zinakuja jumla ndege sita, kwa muda mfupi, huyu ni Rais wa ajabu haijawahi kutokea! Kuna kitu kinaitwa standard gauge tukitafakari kidogo Waheshimiwa Wabunge hili ni jambo kubwa la kihistoria, nasema huyu ni Rais wa ajabu. Kupambana na ufisadi haijawahi kutokea, kupambana na dawa za kulevya haijawahi kutokea, kupambana na rushwa haijawahi kutokea, huyu ni Rais wa ajabu lazima, tumpe hongera zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote haya yanayofanywa na Serikali kwa miradi yote ya kiuchumi na huduma za kijamii hili ni tendo la huruma, na sisi viongozi tunapaswa kuwa na huruma. Mithali ya pili maandiko matakatifu ambayo siyo ya kwako wewe sura ya 19:17 unasema, amhurumiaye maskini anamkopesha Mungu naYe atamlipa kwa tendo lake jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa huruma hii ya Mheshimiwa Rais na Serikali yake na Waheshimiwa Mawaziri na watendaji wake wakuu wa Serikali, wanafanya kazi ya huruma wanamkopesha Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwakunipa nafasi hii ya kuchangia. Nianze kwanza kwa kutoa shukrani kwa Wizara hii ya Maji kwa maana ya Mawaziri wote na Watendaji Wakuu wa Wizara kwa namna ambavyo wanafanya kazi. Wako watu asubuhi walisema Mawaziri hawa ni wazee, lakini nataka niseme aliyewateua bahati nzuri amefanya nao kazi, hawa ni Mawaziri makini kwelikweli na ni wachapakazi kweli. Ukienda ofisini kwao, ukiwaita jimboni wanakuja haraka kuja kuona shida ulizonazo. Kwa hiyo, kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais. Wakati anaomba kura alifika Magu akasema hapa shida moja ni maji na mimi wakati naomba kura niliwaeleza wanachi kama maji hayatapatikana sirudi 2020. Bahati nzuri wakati anazunguka hivi karibuni kwenda Simiyu alipita Magu akasema nakwenda kumuagiza Waziri wa Maji ili aweze kuja kusaini mkataba haraka na wakandarasi wawe site. Hivi ninavyozungumza mkataba ule tuliusaini hadharani kule Nyasaka ambapo utahudumu kata nne kule mjini Jimbo la Ilemela pamoja na kata tatu Jimbo la Nyamagana lakini mradi huu unaunganisha pia na Lamadi na Misungwi. Magu wakandarasi wako site.Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ahadi yake ya kweli na Wanamagu watapata maji, Magu ilikuwa imesahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengi, mradi huu wa Magu Mjini utahudumia wananchi 46,000 lakini Tarafa ya Ndagalu ambayo haina bwawa, haina mto, vijiji 21 wakazi 86,000 wana hali mbaya kutokana na kukosa huduma ya maji. Kwa hiyo, pamoja na kwamba bajeti hii inasemwa haitoshi na mimi nikisema hii inatosha maana yake tarafa hii haitaingizwa. Hata hivyo, niendelee kusema tunapokuwa na shilingi bilioni 600 zikaenda zote shilingi bilioni 600 mwaka huo tunahama hapo, tukiongeza ifike shilingi bilioni 900 halafu hatuna uwezo wa kuwa nazo haitusaidii. Mimi niombe shilingi bilioni 600 hizi ziende zote, wale ambao mmepangiwa miradi tutahama kwenda maeneo mengine. Pamoja na hayo,


tuuongeze huu mfuko wa shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta ifike shilingi 100 ili usaidie kuharakisha kutekeleza miradi hii. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Ndagalu na Tarafa ya Sanjo wana hali mbaya kama nilivyosema. Hawana mito, hawana mabwawa na bahati mbaya kabisa wanakwenda kuchota maji kilometa 58 wengine, wanaamka saa tisa za usiku. Nazungumza haya kwa sababu Mheshimiwa InjiniaLwenge ameshawahi kufanya kazi kule Mwanza na Magu anaijua vizuri, Ndugu Kalobelo anaijua vizuri Magu. Wanaamka saa tisa na unajua Wasukuma muda ule wa mapema baba mwenye mji anakaa kwenye kimunya anachunga ng’ombe kwa hiyo kuingia kulala ni saa saba, naye amechoka, anafika kwenye kitanda puu, akiamka saa tisa amuangalie mwenzake ili atafute mtoto hayupo yuko kwenye maji. (Kicheko/Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana tuwahurumie hawa wananchi, ni tatizo kubwa. Kwa hiyo, muone kwamba wazalishaji wakubwa wa uchumi ni akinamama, muda mwingi wanaumalizia kuchota maji kuliko kuzalisha. Niombe, kama tutaongeza Mfuko wa Maji, Tarafa za Ndagalu na Sanjo ziangaliwe kwa umakini wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu hapa bado wanabeza Serikali hii ya Awamu ya Tano na bado wanasema 2020 haitarudi. Nataka niwahakikishie kwamba Serikali hii inarudi kwa kishindo kifua mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya maneno yanathibitishwa na Biblia Takatifu. Wakorintho 10:23, inasema, vitu vyote ni halali bali si vitu vyote vifaavyo. Ikaongeza, vitu vyote ni halali bali si vitu vyote vijengavyo. Vyama vyote ni halali lakini chama kinachoweza kujenga ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Vyama vyote ni halali lakini chama ambacho kinaweza kuwa kizuri ni Chama cha Mapinduzi. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, mnazungumza kwamba mmemezwa demokrasia kwenda kuwaeleza watu mtaenda mkaeleze nini? Kama ni demokrasia, juzi MArehemu Mheshimiwa Dkt. Macha amefariki tukatarajia mtaleta mtu yuleyule (mlemavu), hamkuleta mlemavu, ninyi mna demokrasia gani?

Mlituletea hapa wagombea wawili tukasema waongezeni, mkaleta sita mkawanyima kura hata ninyi, hata Makamu Mwenyekiti mmemnyima kura, hao wote wangejiuzulu wakarudi CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, msiseme kwamba hakuna demokrasia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba watuvumilie kidogo, tuwe na uvumilivu wa kisiasa ili tuelewane kidogo, ninyi mmezungumza asubuhi hapa.

TAARIFA...

HE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza taarifa siikubali kwa sababu chama kina mamlaka ya kubadilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii Rais Dkt. Magufuli, kama ni upele umepata mkunaji sasa. Unajua ili uwe jemedari lazima upigane vita, huwezi kuwa jemedari bila kupigana vita. Rais Dkt. Magufuli amepigana vita ya ufisadi, rushwa, vyeti hewa na mambo mengi, kwa hiyo, amefanya kazi ambayo alikusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais Dkt. Magufuli wakati ....Yeye atafanya kazi, hatajali chama…

Wale ambao wanatoka vyama vya upinzani tutapata wapi Rais wa namna hii? Kwa hiyo, naomba niwaambie Wabunge wenzangu wajue kwamba dereva mliyenaye atawafikisha salama na CCM itashinda mwaka 2020. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga, muda wako umekwisha, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja lakini tuvumiliane kisiasa, tuwe na ngozi nene.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Sanjo ina vijiji 24 na wananchi 120,000. Ina hali mbaya sana, haina hata bwawa wala mito, lakini imezungukwa na Ziwa Victoria. Maji yanatakiwa yatoke Lutale ambapo ndiyo chanzo, yaende Vijiji vya Kageye, Kayenze, Itandula, Langi, Makamba, Shilingwa, Kongolo, Chabula, Bugando, Nyashiwe, Ihayabuyaga, Welamasonga, Matale, Sese, Ihushi, Isangijo, Busekwa, Bujora, Kisesa, Kanyama, Wita, Welamasonga na Igekemaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Ndagalu ina vijiji 26 wakazi 86,000. Tarafa hii haina hata mto wala bwawa sasa wanafuata maji kilometa hadi 58. Tunaomba watu hawa muwaonee huruma, chanzo cha maji kitoke Nsola kwenda Misungwi, Kitongo, Lumeji, Nyang’hanga, Iseni, Mwamibanga, Buhumbi, Nyashoshi, Ng’haya, Mwabulenga, Nkungulu, Kayenze ‘B’, Chandulu, Bugatu, Salama, Kabila, Ng’wamagoli, Jinjimili, Nhobola, Kabale, Nyasato, Mahaha, Shishani, Isolo, Igombe, Ndagalu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa hii ya Ndagalu hata visima virefu havipo. Naomba tusaidiwe hata kwa dharura visima virefu kila kijiji pamoja na bwawa la Kabila likarabatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Katibu Mkuu, Engineer Kalobelo alifika akaona shida iliyopo akatuma wataalam kutoka MWAUWASA walifanya ziara wakaandika andiko la miradi hii miwili na Mkurugenzi alileta kwenye bajeti, Baraza likapitisha na tukapeleka hata Wizara ya Maji kwa Mkurugenzi wa Maji Bwana Mafuru, pamoja na kwa Naibu Katibu Mkuu Engineer Kalobelo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kutoona miradi hii kwenye bajeti. Jamani wanionee huruma hata waniwekee fedha za kuanzia ili kila mwaka waendelee kuniwekea, hususan naamini tutaongeza sh.50/= kwa kila lita ya mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukinisaidia hii, utakuwa umeokoa maisha ya Watanzania wengi sana wa Jimbo la Magu.

Mhshimiwa Naibu Spika, natanguliza shukurani.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Mansoor Shanif Hirani

Kwimba (CCM)

Contributions (3)

Profile

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Kibaha Vijijini (CCM)

Contributions (5)

Profile

View All MP's