Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Gimbi Dotto Masaba

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Mazingira na Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba niwape pole wananchi wa Wilaya ya Itilima kwa kupatwa na msiba wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji uliotokea hivi karibuni kwa kuvamiwa nyumbani kwake na kupigwa hadi kuuawa. Nawapa pole sana na ni pole kwa Chama. Pia nichukue nafasi hii kukishukuru Chama changu ambacho kimeona umuhimu wa mimi kuwa Mwakilishi wa Mkoa wa Simiyu hasa kwa upande wa UKAWA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niende moja kwa moja kwenye Wizara ya Mazingira. Tunapozungumza suala la mazingira kwa uhalisia ni kwamba tunapaswa kuzungumza kwa mapana zaidi kwa sababu wananchi tulio wengi tumekuwa tukiamini kabisa kwamba mazingira ni kufagia tu. Naamini mazingira tunapaswa kuyatafakari kwa upana zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha taarifa yake, anasema anatarajia kuifanya nchi kuwa ya kijani. Sina hakika kama anaweza kuifanya nchi ya kijani ilihali hawaoneshi u-seriuos wa kubadilisha mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu, ukiangalia katika bajeti ambayo imetengwa kwa ajili ya kuboresha mazingira, haikidhi kile ambacho wanakizungumza. Tumejifunza pia kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, fedha iliyokuwa imetolewa pale ya mazingira ni kama shilingi 3.8 bilioni, lakini mpaka mwezi Machi, Wizara ilikuwa imepokea shilingi milioni 338 jambo ambalo linaonesha wazi kwamba hata ile fedha kidogo haitoki kwa wakati na kama ilitoka mwezi Machi tarehe 31, maana yake hata ile mipango iliyopangwa kwa mwaka wa fedha uliopita haijafanya kazi. Kwa hiyo, hata tukisema kwamba bajeti bado haikidhi, bado Serikali haitoi fedha kwa wakati. Nashauri kama kweli tunataka kufanya mabadiliko ya mazingira na Rais amefuta sherehe ya Muungano akimaanisha kwamba tuwe na nguvu ya mazingira Serikali itoe fedha hizo kwa wakati ili tuweze kuimarisha mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne, ilitoa kauli kwamba wafugaji wafuge ng‟ombe kisasa kwa maana ya kwamba ng‟ombe wanaleta uharibifu wa mazingira jambo ambalo siyo kweli. Nilidhani kwamba badala ya Serikali kutamka wazi kwamba wafugaji wapunguze ng‟ombe, ni vema basi ingeweza kutamka kwamba Mkoa wa Dar es salaam uanze kupunguza magari kwa sababu unaonesha wazi kabisa kwamba ni uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe kusema hivyo, badala ya kuwaambia wafugaji wapunguze ng‟ombe, Serikali ijipange kwenda kutoa elimu kwa hawa Wasukuma na wafugaji wengine wa mikoa mingine, badala ya kuwaambia wapunguze ng‟ombe, watoe elimu ya kuwafanya watengeneze biogas kama issue ni kwamba kinyesi cha ng‟ombe ndiyo kinacholeta uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha mazingira, bado minada yetu kwenye mikoa inafanya biashara, minada yote haina uzio, nashindwa kufahamu kwamba ni mazingira yapi ambayo tunayaboresha wakati minada tunayoiendesha tunathamini kukusanya ushuru badala ya kuimarisha minada ambayo haina uzio, haijulikani kinyesi cha ng‟ombe ni kipi na kinyesi cha mwanadamu ni kipi. Siyo hivyo tu bado minada hii haina vyoo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, tusizungumze mikakati ya kwenye makaratasi, hii mikakati ya kwenye makaratasi imepitwa na wakati. Waziri anasema anakwenda kuifanya nchi ya kijani, nataka anieleze kwamba nchi yetu inatumia usafiri wa meli, wasafiri wote wa meli naamini kabisa wanajisaidia kwenye bahari zetu, sasa nataka alieleze Bunge kwamba hivyo vinyesi vyote vinavyodondokea na mikojo yote kwenye bahari vinaenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujui hivyo vinyesi vinakwenda wapi na baadaye Wabunge tunakuja hapa tunasimama, tunasifia, tunasema namshukuru Waziri wa Maji ameniboreshea kwenye Jimbo langu maji safi na salama, wakati hujui yale maji kama kweli ni salama. Sasa tunataka kujua vile vinyesi vinakwenda wapi na ile mitambo inatumikaje? Naomba kufahamu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kidogo kwenye suala la Muungano. Nina imani kabisa kwa sasa inavyoonekana, kama Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauko hai. Nasema kwa sababu kwa sasa Zanzibar kwanza ina bendera yake, ina wimbo wake na mbaya zaidi bajeti ya Zanzibar haiji huku Bara. Naishauri Serikali kama inaamini kabisa kwamba Muungano ni salama, niiombe Serikali hii ipitishe maoni, tuone wangapi wanahitaji Mheshimiwa Mwenyekiti, sisomi nina akili. Mimi nilichojifunza humu Bungeni ukiona sindano inaingia utamsikia Mheshimiwa anatetea na hasa suala likitajwa jina la Rais, nashindwa kufahamu kwamba anatetea kwa misingi ipi, yeye ni Waziri hatakiwi kuonyesha itikadi yoyote. Lakini pia najua…….
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba Muungano siyo salama mpaka sasa hivi. Imeonesha wazi pia kwamba, Wazanzibari waliamua kuchagua Rais wao, lakini kwa sababu Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina mabomu, ina silaha, imeamua kupora ushindi waziwazi...
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu kwa leo. Ahsante sana

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na mifugo. Hoja kutoka Mkoa wa Simiyu, kwanza kwa kutozwa ushuru mara mbili aidha wauze au wasiuze, analipa ushuru shilingi 6,000/= ilhali wanaopelekea ng‟ombe Mnadani sio wote ni wafanyabiashara, bali wanapeleka ili wauze wapate mahitaji yao kama vile kununua chakula cha familia zao. Sasa unapomwambia auze au asiuze huu ni uonevu wa hali ya juu sana. Kwa maana nyingine ni wizi. Naomba Halmashauri ya Bariadi Mjini itazamwe katika hili na Mnada wa Dutwa Bariadi Vijijini kwani ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Waziri Mkuu alipokuja kwenye ziara yake Mkoa wa Simiyu alikutana na kero hii na alitoa ufafanuzi kwenye mkutano wa hadhara akisema mauzo yanafanyika mara tu biashara inapokuwa imefanyika. Alisema ni marufuku mwananchi kutozwa ushuru mara mbili, lakini kauli yake imepuuzwa, kwani bado wananchi wanaendelea kutozwa kila kichwa ng‟ombe sh. 6,000/= auze au asiuze, analipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, majosho mengi ya kuoshea mifugo yalishakufa kutokana na kukosekana fedha za kuendeleza majosho kutokana na ufisadi. Wananchi wa Maswa Meatu baadhi yao hawana mahali na kuchungia mifugo yao. Naomba Serikali irudishe pori la Maswa, lirejeshwe kwao ili liwasaidie kuondoa mgogoro wa wakulima na wafugaji, kwa sababu pori hilo limekosa sifa ya kuwa Hifadhi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Simiyu, wananchi wa Simiyu wengi wao ni wakulima wa pamba; wamekata tamaa kulima zao hili kutokana kuuzwa kwa bei ya hasara. Kwa muda mrefu hivyo wamekata tamaa na badala yake kulima zao la choroko kama sehemu ya zao la biashara. Kwa hiyo, naomba Serikali ilitazame kwa umakini zaidi kwani zao hilo limepotea kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali irudishe mbegu za pamba ambazo zilikuwa zinatumiwa zamani, zile zenye manyoya, kwani hizi nazo hazioti kabisa. Serikali ipandishe bei ya pamba badala ya kununua pamba kwa sh. 650/= mpaka sh. 750/= iuzwe sh. 1,500/=. Kwani mbona soda ambayo akina Mengi wanakologa maji na kuweka sukari wanafunika, lakini wanauza sh. 1,000/=? Iweje wananchi ambao ameiandaa pamba yake kwa muda wa miezi sita mpaka saba anauza sh. 650/=. Naomba zao hili liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, njaa Mkoa wa Simiyu haikuwepo kwa miaka mingi sana, lakini Mkoa wa Simiyu kwa sasa unaongoza kwa janga la njaa. Hiyo ni kutokana na wananchi hawa kulima na baadaye kuuza mazao yao kwa hasara kabla ya wakati, baadaye kujikuta hawana chakula. Hivyo ,naomba Serikali iwape elimu kuhusu utunzaji wa chakula chao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mageti ya mazao kila kona na bila hata ya utaratibu maalum. Mageti haya yamesababisha vifo; nashauri wayawekee taa, kama hawawezi kuweka taa na hawalindi usiku, basi wayatoe kwa wakati wa jioni wayarejeshe asubuhi, kwani ni hatari sana. Serikali itoe maelekezo kwa Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hii Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kabla sijaanza kuchangia naomba nijikite moja kwa moja, kwenye Mkoa wetu wa Simiyu, ukiwemo na wewe mwenyewe Mwenyekiti, nadhani nikiutaja Mkoa wa Simiyu hata nisipozungumza chochote naamini roho yako inakuwa burudani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiongoza kupata chakula kwa wingi, lakini kwa kipindi hiki mkoa huu umekuwa ukiongoza kwa janga la njaa. Unaongoza kwa janga la njaa kutokana na kwamba wananchi wa Mkoa wa Simiyu wamekuwa wakitegemea kilimo cha msimu badala ya kutegemea kilimo cha umwagiliaji. Hivyo basi, kuliko wananchi hawa waendelee kutegemea kilimo cha msimu, naomba wananchi hawa wategemee kilimo cha umwagiliaji ili waondokane na janga la njaa ambalo linatukabili kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi hawa waondokane na njaa ni lazima Serikali itengeneze miundombinu ya kututengenezea mabwawa kwa maana ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji. Baada ya kututengenezea mabwawa hayo, naamini kabisa kwamba Mkoa wa Simiyu utakuwa umekidhi matatizo ya njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo imezungukwa na Ziwa Victoria, lakini ni Mkoa ambao ndiyo unaoongoza kwa ukosekanaji wa maji. Naomba nizungumzie kwa mfano Wilaya ya Busega Jimbo la Mheshimiwa Chegeni. Wananchi wa Wilaya ya Busega, walio wengi wanaoga maji ya kutoka Ziwa Victoria. Cha kushangaza wananchi hawa wanakunywa maji ya chumvi ya visima, ni jambo ambalo ni la kusikitisha na ni la aibu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kwa Bunge lililopita niliuliza swali kuhusiana na suala la utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Nilijibiwa kuwa mpango huu, unaendelea na hivi punde mradi utakamilika, lakini mpaka ninavyoongea hakuna kinachoendelea tunaendelea kupata takwimu tu na taarifa za kwamba mradi huu utakamilika jambo ambalo naona kwamba siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu kuna Idara za Maji, siku zote nimekuwa najiuliza kwamba hivi Idara za Maji zinafanya kazi gani, ilihali wananchi wa Mkoa wa Simiyu hawana maji, maji ambayo tumekuwa tukiyatumia wananchi wanatengeneza makazi yao na wanachimba visima kwenye majumba yao na wanakuwa wanatumia na walio wengi unakuta wanafanya biashara ndoo moja shilingi mia mbili, lakini unakuta kuna Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kupata majibu kwamba hii Wizara ya Maji inafanya kazi gani, ambapo wananchi wa Mkoa wa Simiyu hatuna maji. Kiukweli tunapozungumza kuhusu maji ni dhahiri kweli tunapata uchungu kutokana na kwamba Mkoa huu wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo ni mipya, lakini kiukweli mara nyingi umekuwa unasahaulika hata kutajwa kwenye Wizara zingine. Sijajua kwamba hatima ya Mkoa huu wa Simiyu ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia hapa kwenye kitabu chake ametutengea fedha Wilaya ya Itilima ambayo mimi natoka na ni Mwenyekiti wa chama katika Wilaya hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nimekuta wametenga shilingi milioni 200 ni sawa, lakini nimeona Wilaya ya Busega hakuna fedha ambazo zimetengwa kutekeleza mradi huu wa maji. Pia katika Jimbo la Mheshimiwa Mwenyekiti pale Bariadi sijaona fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa maji, nimeona Jimbo la Maswa hakuna fedha yoyote ambayo imetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijajua huu mpango unakwenda vipi, kwa sababu fedha nilizoziona pale Wilaya ya Itilima inayo, Wilaya ya Mwanuzi ipo, ni wilaya kama mbili hivi. Kwa hiyo, sasa nashindwa kuelewa kwamba huu mradi unakwenda kutekelezwa vipi? Hii inaonesha wazi kwamba jinsi ambavyo pamoja na kwamba tunatoa hizi taarifa, ijulikane kabisa kwamba sidhani kama kuna mpango wowote unakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mpango unakwenda kutekelezwa, ni dhahiri basi tuanzie pale kwenye vyanzo vya maji, kwa mfano Wilaya ya Busega, ndiyo iko karibu sana na ziwa, kwa nini hatujaona mpango wowote wa kutoka pale Busega, lakini pia Bariadi ndiyo inayofuata hatujaona mpango wowote ambao unaelekea pale, kwa maana kwamba kuna fedha yoyote ambayo inakwenda kutimiza huu mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize kwenye suala la upatikanaji wa mabwawa katika mkoa huu. Mkoa wa Simiyu una maeneo makubwa sana ya kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano, kama maeneo ya Matongo, Mwamtani, Meatu, Malampaka, Malampaka ni walimaji wazuri wa mipunga na mazao mengine. Kwa hiyo, ni vyema Serikali hii ikajikita sana kututengenezea mabwawa ili Wasukuma waendelee kulima kilimo cha umwagiliaji. Tumechoka kuletewa chakula cha msaada kutoka Serikalini ambacho tukiletewa tunapewa kilo tatu.
Ndugu zangu Wasukuma tunazaa mpaka Mungu aseme wametosha, ukiniletea kilo tatu, kwa kweli hiyo mimi naona siyo sahihi. Kwa hiyo, niombe sana kwamba ifike mwisho, mkoa wetu usiwe tegemezi kwenye chakula cha msaada na badala yake tujisimamie na tuweze kuendana na kasi hii ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masikitiko yangu makubwa ni kwamba, ziwa linatuzunguka, lakini hatupati maji safi na salama. Kwa mfano, Mikoa kama ya Mara, Mji wa Tarime hauna maji, kuna bwawa moja tu la wakoloni ambalo hata usafi halifanyiwi la miaka nenda rudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Mkoa wa Mara, Mkoa wa Simiyu, Mikoa hiyo ipate maji safi na salama ili tuendane na kasi ya Serikali hii ya Awamu ya Tano. Kwa hiyo, niombe sana na Wabunge wenzangu tunaotoka Mkoa wa Simiyu tusichoke kupiga kelele kuhusu mkoa wetu angalau tuone ni jinsi gani Serikali yetu itaweza kutusaidia ili tupate angalau hata robo tatu ya mafanikio ambayo tunayatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa Mheshimiwa Waziri, Wabunge waliokuja Awamu hii ya Tano tusipopeleka maji Mkoa wa Simiyu nawahakikishia 2020, hakuna Mbunge atakayekuja hapa, hakika wananchi wamechoka kunywa maji ya chumvi. Sasa hivi tumeanza kupata matusi kutoka kwa Wabunge wenzetu kwamba tumeoza meno, si kwamba tumeoza meno kwa sababu hatupigi miswaki, hapana tumeoza meno kwa sababu tunatumia maji ambayo yana chumvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri, badala ya kuendelea kupata matusi haya basi ifike mahali…

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ilivyowasilishwa hapo mbele. Miaka ya hivi karibuni Tanzania imewahi kuingia kwenye mgogoro na nchi jirani ya Malawi kuhusu mpaka ndani ya Ziwa Nyasa. Mgogoro huo ulitaka kufifisha mahusiano mema ya kidiplomasia baina ya Malawi na nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa mahusiano ya nchi, namwomba Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge, mgogoro huu umepatiwa ufumbuzi au bado? Kama bado, Waziri aje hapa atueleze, nini kinaendelea? Je, huo mpaka ndani ya Ziwa Nyasa, nchi yetu ina eneo la ukubwa gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Umoja wa Mataifa (UN) umetutaka mataifa yote yapige vita Mataifa yanayotuhumiwa kuzalisha makombora ya nyuklia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna taarifa zinaeleza kwamba baadhi ya Balozi za nchi yetu huko ng‟ambo zipo taabani kifedha. Namwomba Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge hili hali halisi ya kifedha kwa ofisi za Balozi za Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilikutana na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam ambapo walieleza kwamba mizigo imepungua kwa kiasi cha asilimia 42 na mingi ni ile inayopita kwenda nje ya nchi hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo ya wadau kupungua kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kumesababishwa na kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa huduma zinazotolewa katika mizigo au bidhaa inayopitia bandari hiyo kwenda nchi jirani (VAT on auxiliary services on transit goods) za Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Uganda. Kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani katika tozo mbalimbali za bandari kunaongeza gharama ya huduma na biashara katika Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza ushindani na bandari nyingine kama zile za Nacala, Beira, Mombasa na Durban. Hivyo basi, ili tuweze kufikia uchumi wa kati, ifikapo mwaka 2025 ni lazima tuiangalie bandari yetu na pia tupunguze ushuru ili tuweze kuzalisha mapato mengi katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

The Media Services Bill, 2016

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu ni hatari kwa Wanahabari na maendeleo kwa ujumla, umelenga kuondoa kabisa uhuru wa habari. Muswada unasema Mwandishi wa habari akipewa taarifa na Afisa wa Serikali kuhusu jambo fulani anaweza kushtakiwa Mwandishi pekee na si aliyetoa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, jambo la kutaifisha mitambo ya kutangazia au kuchapisha magazeti halipaswi kuungwa mkono. Waziri amepewa mamlaka ya kuelekeza nini chombo cha habari ki-report kwa wakati huo, hii itavinyima vyombo vya habari kukosa uhuru wa wake. Waziri au Serikali anaweza kuelekeza waandishi wote waandike habari hata za CCM pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za Tanzania zinamzuia Mwandishi wa habari kupiga picha au kuandika chochote wanapokuwa gerezani. Pia wanazuiwa ku-record au kutangaza live wakati Mahakama inaendesha kesi. Sasa Je, kwa namna hii, Tanzania kuna uhuru wa vyombo vya habari? Tunataka sheria hizi kandamizi zifutwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria hii mpya imwondolee madaraka makubwa Waziri wa Habari. Kwa mfano kifungu cha 54 - 55 amepewa mamlaka makubwa sana, hivyo nashauri badala yake Baraza la Habari ndilo liwe na mamlaka ya kuvionya na kukemea vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania si yetu sisi wana UKAWA tu bali ni ya watu wote, hivyo Chama Tawala wakilazimisha kupitisha Muswada huu wajue wazi hawatukomoi sisi wana UKAWA tu bali wanaukomoa umma wa Watanzania na wao pia, siku moja utawageukia tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wa CCM kama kweli wapo hapa kwa ajili ya kula posho za vikao hata kama tungeandika mpaka tukatokwa na povu Muswada lazima upite tu.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's