Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Stanslaus Shingoma Mabula

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kulikuwa na itilafu ya mitambo kidogo, naitwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana. (Makofi/Vigelele)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametupa fursa ya kuwepo hapa ndani, lakini nitumie nafasi hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Nyamagana kwa kufanya maamuzi sahihi kuwakataa watalii na kuleta wachapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maandiko matakatifu Hosea 4:6 inasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Kwa hiyo, nataka nikuthibitishie maandiko haya yako watu yanawahusu moja kwa moja. Kwa hiyo, tuliobaki humu tusiwe na shaka kwa sababu sisi tuna maarifa, tunayo kazi ya kulitumika Taifa na Watanzania. Mara zote nimekuwa ninasema tumeanza na Mungu, tutamaliza na Mungu na ndivyo itakavyokuwa. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake iliyokuwa imejaa na kusheheni mahitaji ya Watanzania. Watanzania wengi wakati wote tumekuwa na subira lakini tumekaa tayari kutegemea hiki ambacho Mheshimiwa Rais sasa anakifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda moja kwa moja kwenye kuchangia hotuba hii yako masuala ya msingi ya kuzungumza juu ya Jimbo langu la Nyamagana lakini juu ya Taifa zima kwa ujumla. Nianze na sekta ya afya. Mheshimiwa Rais amezungumza sana juu ya kuanzisha zahanati kwenye kila kijiji, kituo cha afya kwenye kila Kata, lakini kuhakikisha kila Wilaya ina hospitali na Mkoa una hospitali ya rufaa na Kanda zinazo hospitali za rufaa kwa ajili ya kuhudumia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo ninalotoka mimi la Nyamagana linazo hospitali 12 peke yake kwa maana ya zahanati, lakini siyo Nyamagana tu, ninaamini yako maeneo mengi sana. Kihalisia tunapozungumza kumhudumia mwananchi kwenye sekta ya afya, kuanzia ngazi ya Kijiji, ngazi ya Kata na ngazi ya Wilaya, tunapozungumza kuanzisha hospitali hizi ili zikamilike hospitali yako mambo mengi yanayohitajika, unazungumzia habari ya majengo, watumishi wenye nia njema na thabiti ya kuwatumikia Watanzania, unazungumzia vifaa tiba zikiwemo dawa ili kuhakikisha vyombo hivi na nyumba hizi zinapokuwa tayari Watanzania wenye matumaini na Serikali hii waweze kupata mahitaji yao, tukiamini afya ni suala msingi ambalo linaweza kuwa ni chombo peke yake kwa mwanadamu kinachomfanya awe na uhakika wa kupumua wakati anapopata matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini Nyamagana inabeba Hospitali ya Rufaa ya Bugando, hospitali hii ni kimbilio la wakazi zaidi ya milioni 14 wa Kanda ya Ziwa, lakini iko based kwenye Jimbo la Nyamagana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wanalalamikiwa sana, lakini inawezekana watumishi wanalalamikiwa sana sisi kama Serikali hatujafanya wajibu wetu. Niiombe Serikali ya Awamu ya Tano hospitali yenye vitanda zaidi ya 950 inayotegemewa na watu zaidi ya milioni 14 inaomba bajeti ya takribani bilioni saba kwa mwaka mpaka leo tuko zaidi ya miezi sita imepata milioni 106 peke yake, wananchi wataendelea kulalamika, watumishi wataonekana hawana maana kwa sababu hawatoi huduma zilizobora. Bili ya maji peke yake na umeme kwa mwezi ni zaidi ya milioni 60. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana tuangalie masuala haya kimsingi ili tuweze kutoa huduma. Nyamagana ni Jimbo peke yake lenye kilomita za mraba 256 kilomita 71 zikiwa ni maji lakini hatuna maji ya uhakika ya bomba kwa wananchi wa Jimbo la Nyamagana. Hili ni tatizo na lazima liangaliwe kwa undani. Liko suala la elimu limeshazungumza sana na mimi naunga mkono na wale waliolizungumza. (Makofi)
Suala la miundombinu pia limezungumzwa ziko barabara ambazo hazipitiki, Nyamagana Mheshimiwa Rais wakati amepita ameahidi kuimarisha barabara zinazosimamiwa na TANROAD na zile ambazo alifikiri kwa ahadi yake zitatekelezeka, kutoka Buhongwa kupitia Lwanima, Kata ya Sahwa, Kishiri kuunganisha na Igoma, Fumagira kuunganisha na Wilaya za Misungwi na Magu. Lakini kutoka Nyakato kupita Busweru kwenda Kabusungu, kwenda kutokea Bugombe, Igombe na kuunganisha na Kata nyingine, hii barabara ili iweze kupitika kwa mama yangu Mheshimiwa Angelina kwa sababu haya ni majibu pacha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la miundombinu naomba niseme kwamba liko tatizo kubwa, Serikali hii imejipambanua kukusanya mapato ni lazima tuhakikishe tunapata vyanzo vya mapato. Mwanza ni kituo kikubwa ambacho kinaunganisha mikoa ya Kanda ya Ziwa, nchi za Afrika Mashariki na Kati na Maziwa Makuu hakina airport ya maana ambayo inaweza kuongeza mapato kwa asilimia kubwa. Tuone umuhimu wa kujenga airport ya maana, Internation Airport ambayo itasaidia mtalii anayekwenda Ngorongoro kutokea Arusha akipita kule atokee Serengeti aje aondokee Mwanza, akishukukia Mwanza apite Serengeti aende Ngorongoro aondokee Arusha. Lakini bandari tunaunganisha mikoa zaidi ya sita hakuna bandari ya maana Mwanza hili na lenyewe liangaliwe kwa maana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, juu ya ukusanyaji wa mapato. Nimuombe Waziri wa TAMISEMI, hakuna siku itakaa Halmashauri hizi ziweze kujitegemea asilimia 50 mpaka 100 maana yake ni kwamba uwezo huo ni mdogo sana lazima tujipange kukusanya mapato.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mabula muda wako umekwisha.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja asilimia mia. (Makofi)

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia na mimi angalau kidogo na nitajikita zaidi kwenye viwanda vyetu katika Jiji letu la Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa nyingine tena leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka miaka michache iliyopita Mji wa Mwanza ulikuwa maarufu sana kwa viwanda vya samaki na watu wake wengi sana walipata nafasi za maendeleo, za kiuchumi na uchumi kwa kweli ulikua sana. Hata asilimia tunayoizungumza leo inayochangiwa kwenye pato la Taifa na Mkoa wa Mwanza imetokana sana na imetengenezwa na viwanda vya samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa viwanda hivi vya samaki leo ni viwanda ambavyo vinajiendesha kwa hali dhoofu sana. Nasema dhoofu sana kwa sababu zao hili la samaki miaka mitatu nyuma kiwanda kimoja cha samaki peke yake kilikuwa na uwezo wa kukata tani 250 kwa siku kikiwa kimeajiri wafanyakazi wasiopungua 600; na hawa walikuwa ni vijana kabisa wa kike na wa kiume. Leo tunapozungumza hapa, kiwanda kimoja cha samaki kati ya viwanda saba kinakata tani zisizopungua 20 mpaka 72 kwa siku, kikiwa kimepunguza wafanyakazi kutoka 500 mpaka 750 kufikia wafanyakazi 96 mpaka120. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba vijana wengi wamepoteza ajira lakini vijana wengi hawana pa kwenda ndiyo sababu unaona Mji wa Mwanza unazidi kujaa kwa vijana ambao hawana kazi, kila mmoja anatamani kufanya biashara ya umachinga, kila mmoja anatamani kufanya biashara ya umama lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu! Tatizo liko kubwa! Mheshimiwa Waziri viwanda hivi vinakufa kwa sababu zao la samaki linapungua. Zao la samaki linapungua kwa sababu gani? Uvuaji wa njia za sumu umekuwa ni mkubwa zaidi na badala yake samaki hazipatikani kwa njia rahisi, lakini wenzetu wamezalisha samaki hizi na kwenda kuzivuna na kuzipanda makwao, leo unaweza kupata samaki wengi sana kutoka Ugiriki na kutoka Urusi na wameongeza ushindani zaidi kwenye soko letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, quality ya samaki wanaovuliwa sasa kwa sababu uvuvi haramu umekithiri, hii sumu inasambaa sana. Unapozungumzia uvuaji katika Ziwa Victoria, mikoa hii inayotumia sana uvuaji huu kwa Ziwa Victoria, lakini zipo nchi za jirani, Uganda na Kenya, wanafanya biashara kama sisi. Sasa wazo langu hapo Mheshimiwa Waziri, ni lazima tuangalie njia mbadala. Tutafanyaje kuhakikisha tunaokoa, uvuvi huu haramu unaondoka na tunabaki na uvuvi sahihi ambao unaweza kusaidia viwanda hivi?
Mheshimiwa Waziri, Mwanza kwa sasa ukipata mbinu mbadala ya kuhakikisha viwanda hivi vinaendelea na uzalishaji wake kama zamani, vinarudisha ajira kubwa iliyoangaka. Huna sababu ya kufikiria kujenga viwanda vipya vya samaki kwa sasa Mwanza. Hivi tulivyonavyo, kama tunakwenda kujenga viwanda vipya, hivi tunaviweka kwenye kundi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kiwanda cha Mwatex pale, miaka kumi iliyopita, tangu tukibinafsishe mpaka leo, wafanyakazi kutoka 700 na kitu mpaka 30 na kitu kwa siku. Hata walioondoka hawajalipwa mpaka leo, imekuwa ni kero na kasheshe kila kukicha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tuangalie hivi tulivyonavyo kwanza kabla ya kufikiria mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho kiwanda cha Tanneries pale, nilikuwa nataka kumpa taarifa rafiki yangu Mheshimiwa Msigwa, bahati mbaya tu nilichelewa, nilitaka tu nimtaarifu kwamba unapozungumza Kiwanda cha Tanneries hakihusiki na kuzalisha nyama, bali kinahusika na kutengeneza na kuzalisha mazao yanayotokana na ngozi. Kiwanda hiki kimeuzwa na kimekuwa godown, hakuna shughuli inayofanyika pale na tumepoteza vijana wengi ambao naamini Serikali mngefikiria vizuri, leo vijana wetu wangekuwa wanafanya kazi pale. Kwa maana siyo kwamba ng‟ombe nao wamekufa, ngozi hazipatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, majeshi yetu leo yangekuwa yanapata bidhaa za viatu kutoka pale, mikanda yao wangetoa pale na kadhalika. Sasa hivi tunavyozungumza, makampuni ya ulinzi yamekuwa mengi na maarufu sana nchini hapa. Wote hawa wanahitaji bidhaa za viatu hizi na mikanda yao ni hii hii ya bei za kawaida. Leo hata mikanda tunaagiza kutoka China na bahati mbaya sana inakuja ya plastiki ambayo haidumu, unanunua leo, kesho imekatika inabidi ununue mwingine.
Mheshimiwa Waziri nakuomba, tunayo kila sababu ya kuangalia umuhimu wa kiwanda hiki ambacho kilikuwa kinasaidia watu wa Mwanza kupata ajira na kadhalika, uangalie uwezekano wa kukifanya kirudi na sisi tukitumie kwa manufaa ya Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza suala la uboreshaji wa viwanda tulivyonavyo, tunazungumza suala la anguko kubwa la ajira. Kama ajira hii ambayo vijana wengi wanaitegemea, leo kila tukija hapa, nami kila nikisimama nazungumza juu ya ukuaji wa Mji wa Mwanza. Leo yapo maeneo tupetenga kwa ajili ya EPZ, hizi EPZ zinafanya nini? Tunajenga leo, tunatenga leo, matokeo yake ni baada ya miaka 30. Waachiwe watu maeneo haya wafanye biashara zao nyingine za kawaida, maana kuendelea kutunza maeneo makubwa, na mimi nikupe mfano, walikuja watu wa NDC toka mwaka 1974 wakachukua eneo la zaidi ya ekari 305, sawa na ekari 705. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya yamekaa toka miaka ya 1980 mpaka leo, eneo halijaendelezwa na tumeambiwa eneo hili ni kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo. Pia maeneo mengi yanayochukuliwa hayalipwi fidia kwa wakati. Tunajua Halmashauri zetu hazina uwezo mkubwa wa ukusanyaji wa mapato. Hebu nikuombe Wizara yako ione umuhimu na maana halisi ya kuhakikisha maeneo yote yanapotengwa kwa ajili ya viwanda, aidha vidogo vidogo au viwanda vikubwa, tafsiri yake tunataka kupunguza mzigo, lakini tunataka kukuza uchumi, zaidi ya yote tunataka kuajiri vijana wengi zaidi ili tufikie kwenye malengo ambayo ilani yetu inasema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatuwezi kuboresha maeneo haya, hatuwezi kuokoa kundi kubwa la vijana ambao wanamaliza vyuo. Sio wanaomaliza vyuo tu, wako watu wana vipaji wanaweza kufanya kazi. Viwanda hivi tunavyovizungumza ni viwanda vinavyochukua watu wenye tabia tatu, wenye elimu ya chini, elimu ya kati na elimu ya juu, wote hawa wanataka ajira. Ni lazima tufike sehemu, kama tunataka kuepukana na matatizo ya msongamano wa vijana machinga, mama lishe na kadhalika kwenye maeneo mengi, lazima tuhakikishe tunajenga viwanda, lazima tuhakikishe viwanda hivi vinahimishwa, vinakuwa sawasawa na vinafanya kazi zake kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nakuomba tu kwamba nitakuunga sana mkono lakini kubwa ninalotaka kulisema, Mheshimiwa Mwijage sisi tuna imani na wewe. Tunayo imani kubwa, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano amekuamini na sisi tunakuamini. Imani yetu tuliyonayo kwako tunataka kuona, tunajua huu ndiyo mwanzo, tunataka kuona hapo ulipo na hayo unayoyasema unayasimamia, unayafanyia kazi. Na wewe ni jembe la shoka, hatuna shaka, hizi nyingine ni kelele tu tumeshazizoea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka uone watu hawana adabu, haiwezekani unazungumza, unatukana, unamaliza unaondoka bila kusubiri majibu. Hawana nia njema na Watanzania hawa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Meshimiwa Mwenyekiti, tunataka watu ambao ukitoa hoja ya misingi kwa ajili ya Watanzania, ukitoa hoja kutetea vijana kwamba wanatafuta ajira, lazima ubaki upate majibu yake. Waangalie wako wapi? Mheshimiwa Kubenea yuko wapi hapa? Mheshimiwa Msigwa yuko wapi hapa? Wametukana, wameondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka niseme Waheshimiwa Wabunge, iko tofauti na lazima tukubali. Tofauti ya Mbunge wa CCM na Mbunge wa Upinzani ni kubwa na itabaki pale pale. Sisi ndio Wabunge wenye Serikali na hiyo ndiyo tofauti, hakuna namna nyingine. Sisi ndio wenye Serikali, ni lazima tuiunge mkono Serikali hii, tufikie malengo ya watu wetu kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mhesimiwa Mwenyekiti, mtu mwingine, rafiki yangu Mheshimiwa Mussa pale anashangaa kila tunachokisema tunazungumzia ilani. Kwenye ushindani kule si kila mtu alinadi ilani yake. Haya ndiyo matunda ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Leo ukisimama hapa unazungumza, mwisho wa siku unaomba. Ndugu yangu Mheshimiwa Mussa ameomba reli ya kati ianzie Tanga. Bila Ilani ya CCM usingeomba reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwashukuru sana na niendelee kuhimiza, naunga mkono bajeti asilimia mia moja, viwanda kwa ajira za vijana wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi ya kuchangia angalau kwenye Wizara hizi mbili niweze kusema maneno machache.
Kwanza nianze kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Rais pamoja na Baraza lake lote la Mawaziri kwa namna ya kipekee ambavyo wamekuwa wakifanya shughuli zao na kuwajibika kwa kiwango cha hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuwashukuru sana wapigakura wa Jimbo la Nyamagana kwa kazi kubwa sana waliyoifanya. Niwahakikishie kwamba ninapokuja Bungeni hapa, nakuwa nimekuja kazini na kazi moja kubwa ni kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kuwalipa yale waliyoyafanya baada ya tarehe 25 Oktoba, 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa shughuli nyingi za kimaendeleo ambazo imeendelea kuzifanya katika Jimbo la Nyamagana, lakini yapo mambo machache ambayo tunapaswa kushauriana na kuambizana ili tuweze kuyarekebisha na tuweze kuendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kidogo juu ya habari ya mapato, nizungumze juu ya habari ya ajira kwa vijana, lakini nizungumze juu ya namna ambavyo Halmashauri zinaweza kuongeza mapato kutokana na uwekezaji wa taasisi mbalimbali.
Sote tunafahamu, Jiji la Mwanza ni sehemu ya Mkoa wa Mwanza ambao ni mji wa pili kwa ukubwa Tanzania; lakini ni ukweli ule ule usiofichika kwamba Nyamagana na Jiji la Mwanza ndiyo mji unaokua kwa kasi zaidi Barani Afrika katika nchi yetu ya Tanzania. Tafsiri yake unaipata katika ongezeko la watu; 3% ya kuzaliana na 8.2% ya wahamiaji na wageni wanaoingia kila wakati kwenye Jiji la Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuikumbusha Serikali yangu, Jimbo la Nyamagana ni sehemu ambayo ni kitovu cha Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Unapoanza kuzungumza habari ya msongamano wa watu, habari ya msongamano wa vifaa wa vyombo vya usafiri, lakini habari ya msongamano wa wafanyabiashara ndogo ndogo ambao kwa kweli huwezi kuwaondoa kwa sababu ndiyo sehemu wanayoweza kupata fursa nyingi zaidi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuiomba Wizara ya TAMISEMI kwamba Halmashauri peke yake haiwezi kukabiliana na taizo hili, lakini kupitia masuala mbalimbali, kwa mfano, tunapozungumza juu ya uboreshaji wa Miji na upanuaji wa Mji, naiomba Wizara ya TAMISEMI kupitia kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene; mara kadhaa tumekuwa tunazungumza na unanipa ushirikiano wa kutosha, nakupongeza sana. Sina shaka Halmashauri hizi zimepata dawa ambayo kwa kweli ukiendelea hivi, naamini tutafikia kwenye lengo tunalolitazamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo kubwa sana la wafanyabiashara ndogo ndogo na leo nitajikita hapa sana. Bila kutafuta ufumbuzi kutoka juu, bila kuisaidia Halmashauri kuweza kupanua Mji; tunapozungumza kupanua barabara ya kutokea Buhongwa kupita Kata ya Sahwa kwenda Lwanima, kutokea Igoma kuunganisha Fumagila kukamata barabara inayotoka Usagara kwenda Kisesa; tusipopanua Mji hatuwezi kuwaondoa machinga katikati ya Mji! Tusipopanua Mji hatuwezi kupanua fursa za vijana ambao wanapaswa kujitanua na kufuata yaliko makazi! Huwezi kuwaondoa machinga kuwapeleka sehemu ambako hakuna wakazi, hakuna watu, hakuna biashara! Inakuwa ni vigumu sana; lakini ndio wakwetu hawa, wanaingia kwa kasi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakumbuka miaka ya nyuma, ni miaka michache tu iliyopita, watu wengi walitumia nafasi hii kujinufaisha sana kupitia vijana hawa wanyonge na maskini wanaotafuta maisha yao ya kawaida. Kwa sababu waligundua ukweli na kuamini Chama cha Mapinduzi peke yake kupitia watu wake wanaweza kukisaidia, Nyamagana wameamua kufuta habari ya upinzani na wakakirudisha Chama cha Mapinduzi. Sasa ni lazima tuwatendee haki kwa kuwaboreshea miundombinu, kuimarisha maeneo yao ya biashara ili wafanye kazi zao vizuri na Mji ubaki unapumua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba nizungumze juu ya uwekezaji. Tunafahamu Halmashauri hizi hazina mapato mengi. Nawashukuru sana LAPF kwa uwekezaji wao mzuri na mkubwa, nafahamu wamefanya Morogoro na baadaye wamekuja kufanya Mwanza. Tumefanikiwa kujenga Shopping Mall ya kisasa, Eastern Central Africa unaikuta Mwanza peke yake. Hii itatusaidia kuongeza ajira zaidi ya vijana 270.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Kuwepo kwa mall hii peke yake siyo tu kuongeza ajira, inaongeza kipato kwenye Halmashauri kwa sababu Halmashauri imewekeza kupitia ardhi yake, LAPF wamewekeza fedha. Kwa hiyo, tunagawana mapato siku ya mwisho na Halmashauri zinaendelea ku-generate income tofauti na kutegemea ushuru mchache ambao unatokana na kero mara nyingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la afya. Sote tunafahamu namna ya kumlinda mama na mtoto wakati wanapojifungua. Tunapozungumza kuboresha zahanati na vituo vya afya, tunapozungumzia habari ya maduka ya dawa, tumeanzia ngazi ya juu sana. Hatukatai, ni vizuri hatua zimeanza kuchukuliwa, lakini unapoboresha kwenye Hospitali ya Mkoa ukasahau kuboresha kwenye Hospitali ya Wilaya, tafsiri yake ni kwamba mzigo wote wa Wilayani unaupeleka Mkoani; unaondoa chini huku ambako watu wengi wanahitaji msaada, hatuwezi kufanikiwa. Hii ndiyo maana tunasema, siyo rahisi sana, lakini tunajitahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niwashukuru sana kwa kuanza kupeleka maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Hawa wakiwajibika na wao sawasawa Halmashauri zitapunguza mzigo kwa sababu watakuwa wanashirikiana katika kuhakikisha wanapeleka maendeleo kwa wananchi na mifano mizuri mnayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu, kwenye Jimbo la Ilemela pale kwa mama yangu, Mama Angelina Mabula, iko zahanati moja ya muda mrefu, Zahanati ya Sangabuye. Zahanati hii imeanza kitambo, lakini mpaka leo inapata fedha za zahanati wakati ni kituo cha afya. Halikadhalika zahanati iliyoko kule Nyamuhungolo, hakuna wataalam lakini inavyo vifaa vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie tu kwa kusema nikiwa naendelea na mimi nashangaa sana kwenye suala la elimu; tumesema elimu ni bure, watu wanalalamika. Wakati inaanzishwa, wakati tuko kwenye kampeni, watu walikuwa wanajinasibu kutoa elimu bure, leo wanashangaa Serikali ya CCM kutoa elimu bure, wanasema ni fedha za walipakodi. Unapozungumza elimu bure, tafsiri yake ni nini? Nani unataka atoe fedha mkononi kama siyo Serikali yenyewe? Na mimi nashangaa! Nilikuwa najiuliza, hawa watu ni kiumbe cha namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tukitaka kuangalia hapa; namshukuru sana Mheshimiwa Zitto Kabwe kwa kuona thamani na umuhimu wa elimu hii ambayo CCM imesema, elimu ya kuanzia chekechea, msingi na sekondari ni bure. Kwake kule kwenye Halmashauri akiwa na mwaka mmoja tu na Chama chake, amesisitiza kuanzia kidato cha tano na cha sita. Ninyi mna miaka 23 mmefanya nini kwenye elimu kama siyo kulalamika leo? Nimekuwa najiuliza, tunahangaika hapa, kila siku ni kutukana, kulalamika! Tunataka kujua! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ungetusaidia. Mara zote mimi nimejiuliza, hawa UKAWA ni viumbe wa namna gani? Ni chura au ni popo hawa? Maana ndiyo peke yake huwezi kujua! Chura anabadilika kila wakati, lakini kinyonga huwezi kujua! Kinyonga anabadilika kila wakati, lakini popo huwezi kujua kama ni ndege au ni mnyama? Kwa hiyo, hii tunaipata wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 22 Aprili, 2016 hapa Mwenyekiti wao alisema, katika mazingira kama haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiko tayari kuendelea kushiriki na uvunjaji wa Katiba, Sheria na haki za msingi za wananchi. Leo wanashiriki hapa, wameungana na sisi, hawajaungana na sisi? Ukishindwa kupambana naye, ungana naye. Hii ndiyo dhana halisi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa wameshashindwa kupambana na sisi…
Nawashukuru kuendelea kuungana na sisi! Na mimi nakushukuru sana. Dhamira ya Chama hiki ni kuendelea kuongoza na kuweka maendeleo sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa namalizia, namshukuru sana Waziri wa Wizara ya Michezo, Habari, Sanaa na Utamaduni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Nyamagana tumehangaika kwa muda mrefu juu ya uwanja wetu wa Nyamagana, leo ninavyozungumza tayari nyasi ziko bandarini na muda mfupi kazi inaendelea katika uwanja wa michezo wa Nyamagana. Tafsiri yake, tunataka kuimarisha! Ukiimarisha michezo umekuza ajira kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuzungumza juu ya hali halisi ya bajeti yetu ambayo tunaitegemea na Watanzania wengi sana wanaitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye mada kutokana na muda. Cha kwanza naomba niwashukuru sana watu wa Wizara ya Maji. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuangalia umuhimu wa kutoa kodi kwenye dawa zinazotibu maji kwa sababu kuondoa kodi hii kunazisaidia sana Mamlaka za Maji kuweza kutekeleza miradi yao midogo midogo kwenye kila eneo ambapo wapo. Hata hivyo, kutoa kodi kwenye dawa peke yake haitoshi, tungetamani sana na vifaa vinavyohusika katika shughuli za utengenezaji wa maji kama mabomba, pipes na nuts na vitu vingine ambavyo vinafanana na hivyo viondolewe kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha pili tumezungumza juu ya kujenga vituo vya afya na zahanati na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano. Hata hivyo, ingependeza sana tuseme tutajenga vituo vingapi na kila Halmashauri ijue tutaipa vituo vingapi ambapo mwisho wa siku tutafahamu tunao wajibu kwenye kila Halmashauri kujenga vituo vitano, kujenga zahanati tatu na kadha wa kadha, kama ambavyo tunaona Wizara ya Maji na Wizara ya Miundombinu wameelekeza vyanzo vyao kwa namba.
Mheshimiwa Naibu Spika, tungetegemea sana namba hizi kwani zingetusaidia kwa sababu tunatambua tunayo sera ambayo inasema kila zahanati inapojengwa kuwe na wakazi wasiopungua 10,000, tunafahamu iwe na umbali wa kilometa zisizozidi 10 lakini leo tunataka kujenga vituo vya afya kwenye kila Kata. Vituo vya afya hivi tunafahamu ni sawa na hospitali kwa sera ya sasa inavyotaka, ni lazima kuwe na OPD, ni lazima kuwe na maternity ward, ni lazima kuwe na ward ya wanaume na wanawake. Tutavijenga kwa mpango upi, kila Halmashauri itawezeshwa kwa kiasi gani, kuhakikisha vituo hivi vinajengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine ni juu ya kodi ya usajili wa bodaboda. Tunafahamu kwamba kodi hii inamhusu mtu anayeingiza pikipiki hii nchini, lakini huyu anapokwenda kuinunua bado hamjatoa maelekezo vizuri kule kwenye Halmashauri. Mngeelekeza vizuri kule kwenye Halmashauri, ziko kodi za leseni wanazotakiwa kulipa watu wa bodaboda hawajawahi kulipa hata shilingi moja. Sababu ni nini? Hakuna maeneo sahihi ya kuwapanga na kuwaelekeza kwamba hivi ndivyo vituo vyenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu wa bodaboda yenye magurudumu mawili anapaswa kulipia leseni Sh. 22,000, mwenye gurudumu tatu analipa Sh. 23,000. Uliza Halmashauri yoyote haijawahi kulipwa fedha hii kwa sababu Wakurugenzi wamekuwa wagumu kutenga maeneo ambayo yatasaidia sana kuhakikisha kodi hii inalipwa. Ukichukulia Mkoa wa Mwanza peke yake, kuna bodaboda zisizopungua 18,000 mpaka sasa hivi, kwa Sh.22,000 unapoteza zaidi ya shilingi milioni 396. Sasa tukiangalia haya tunaweza tukaona namna gani tunaweza kuwasaidia vijana hawa pamoja na gharama zingine ambazo zinaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunazungumza juu ya shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji, wengine tunakotoka sisi kuna mitaa, tumeizungumzia vipi hii mitaa? Nimshukuru kwa kugundua Mikoa mingi ya Kanda ya Ziwa maana katika mikoa mitano, mikoa minne yote inatoka Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najiuliza ikabidi nifanye utafiti kwa nini Mwanza tunaitwa maskini, kwa nini Kigoma wanaitwa maskini lakini nikagundua kulingana na idadi ya watu wengi tulionao Kanda ya Ziwa, umaskini wa watu wetu, watu wenye kipato kikubwa ni wachache na watu wenye kipato cha kati ni wachache na maskini ndiyo wengi zaidi kuliko maeneo mengine. Kwa sababu mmelijua hilo tungetamani sana tuone tunasaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwanza uwezo wetu wa umaskini ni asilimia 35, Mheshimiwa Waziri ameongelea Geita umaskini uko kwa asilimia 48 na Kagera ni asilimia 43 na mikoa mingine. Sasa hizi shilingi milioni 50 tunazozizungumza tungetamani sana zianzie mikoa hii maskini, kwenye mitaa ili watu wake walioonekana kuwa na umaskini mkubwa waweze kusaidiwa na waweze kujikwamua na wao angalau wasogee kwenye kipato cha kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza suala la kuhamisha kodi ya majengo kutoka kwenye Halmashauri kwenda kwenye TRA, iko mifano mingi. Mwaka 2007 walijaribu Dar es Salaam ikashindikana na leo tunarudi upya. Pamoja na sheria nyingi ambazo amezitaja humu ndani lakini Mheshimiwa Waziri hajatuambia kama anakumbuka Halmashauri hizi kupitia TAMISEMI Tanzania Bara na Ofisi ya Rais Zanzibar (TAMISEMI) ziliingia mkataba mwaka 2006 na World Bank (GIZ) na kupata fedha nyingi na malengo ya fedha zile ilikuwa ni kuboresha Miji, Makao Makuu ya Miji, Manispaa na Majiji na zimefanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukipitia mradi wa TSCP, ukienda Mwanza, Mbeya, Arusha, Kigoma utaona haya ninayoyazungumza. Pia wameenda mbali zaidi wakaziwezesha Halmashauri hizi kupata fedha na kutengeneza mfumo wa GIS ambao umesaidia watu wamepewa mafunzo, wameelimisha watu, kwa ajili ya kuhakikisha wanapata data za majengo yote kwenye kila mji, leo tunakwenda kuondoa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na sheria hizi alizozitaja, tunasahau iko Sheria Na. 2 ya mwaka 1983 inazozitambua mamlaka hizi za mitaa kwamba ndiyo mamlaka pekee zenye haki ya kukusanya kodi ya majengo. Hatukatai, inawezekana ninyi mmekuja na mfumo mzuri zaidi ambao sisi hatujui lakini kama Halmashauri na sisi kama wadau tunafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Halmashauri hizi zimeingia kwenye mikataba mikubwa hii tunayoizungumza, zimepewa vifaa kwa ajili ya kuboresha ukusanyaji wa taka, zimepewa vifaa kwa ajili ya kutambua majengo yaliyopo na thamani yake, kuondoa kodi hizi hawaoni kama ni athari kwa Halmashauri hizi? Ni lazima watuambie vizuri lengo na makusudi ni nini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa hapa suala la kumpunguzia uwezo, mimi naita kumpunguzia uwezo CAG. Nilipokuwa nasikia michango ikabidi nitafiti zaidi, lakini Mheshimiwa Waziri atagundua mwaka huu wa fedha unaokwisha tulikuwa tumempangia CAG shilingi bilioni 74 ukijumlisha na fedha za wadau wengine alipaswa kuwa na shilingi bilioni 84. Mpaka tunavyozungumza CAG kapata shilingi bilioni 32 peke yake na maeneo aliyoyakagua ni ya matumizi peke yake, maeneo ya mapato ameshindwa kukagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kashindwa kufika kwenye mikataba mingi ya mgawanyo wa rasilimali za Taifa kama gesi kwenye madini na kadha wa kadha. Katika maeneo 27 ameenda maeneo sita peke yake. Leo tunamtengea shilingi bilioni 44 out of 74 ya mwaka huu unaokwisha, je, hawezi kupata shilingi bilioni 22 chini hata ya zile alizozipata mwaka huu? Hili ni lazima tuliangalie. Inawezekana wao wameliangalia vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusitafakari vibaya, ni lazima tuhakikishe maeneo tunayotaka yakaguliwe vizuri na sawasawa tujiridhishe. Huyu CAG ndiyo tunamtegemea sisi, ili TAKUKURU afanye kazi yake vizuri anamtegemea CAG na ndiyo maana ata-Audit ripoti ya TRA mwaka huu imechelewa kwa sababu wamekosa fedha hizi, ni lazima tukubaliane tunachokiamua kiwe na maslahi kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa tunafahamu kwamba tunayo matatizo mengi. Tunazungumza viwanda lakini karibu miji yote nchini ardhi iliyotengwa kwa ajili ya viwanda siyo zaidi ya asilimia 2.5 na wakati matarajio na matakwa ni kuwa na asilimia 10 kwenye kila Halmashauri, ni wapi tumeweka?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naomba niunge mkono hoja, lakini lazima tuangalie kinaga ubaga ni nini tunataka kuwatengenezea wananchi wa Taifa hili ili wafikie malengo ya Mheshimiwa Rais yaliyokusudiwa. Nakushukuru sana.

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kwa kupata nafasi walau dakika tano hizi niseme machache ambayo nadhani yanaweza kutusaidia kuendelea mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kuungana na mapendekezo ya Kamati zote mbili nikiamini kwamba ni moja ya maeneo muhimu sana ambayo kama Serikali itayafanyia kazi tunaweza kupiga hatua ambayo tunaitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninavyofahamu mimi suala la ukaguzi, katika Halmashauri zetu, Taasisi zetu na maeneo mbalimbali ambayo kwa kweli CAG anapaswa kufanya kazi huko zinasaidia kuimarisha utendaji bora na matumizi bora ya fedha za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na uimarishaji huo, kama Kamati hizi mbili kama ambavyo zote zimesema haziwezi kupewa nguvu ya kufanya kazi ya kwenda field na kukagua kilichopo itakuwa bado ni sawa na kupiga mark time. Sababu moja kubwa ya msingi, kupata Hati Safi hakumaanishi yale yote yaliyofanyika yana ubora wa kiwango kinachostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunaamini kupata Hati Safi ni uandishi mzuri wa vitabu, lakini Kamati zinapokwenda field zinakutana na vitu tofauti; toka asubuhi Wabunge wameongea hapa. Sasa tunafikiri upo umuhimu, tunaamini kwamba, mambo haya yakifanyika vizuri sina shaka tutakuwa tumefikia malengo ambayo yametarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi, limezungumzwa suala la miradi kutokamilika kwa wakati. Naamini katika Halmashauri zote nchini miradi mingi sana ilianza. Hapa imetajwa miradi ya maabara, ikaja ya miradi ya vituo vya afya, zahanati, madarasa na kadha wa kadha. Vyote hivi, kama haviwezi kupelekewa fedha kwa wakati ni lazima tutakuwa tunakutana na hoja za ukaguzi mara kwa mara na hatuwezi kufikia malengo kwa kweli ambayo wananchi wanatazamia kuyaona sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Fedha za Mfuko wa Vijana na Wanawake; liko tatizo na mimi sina shaka Mheshimiwa Simbachawene atakuwa analifanyia kazi suala hili vizuri akishirikiana na Mheshimiwa Jenista kwa sababu moja tu ya msingi kwamba, fedha hizi imekuwa ni tabia, fedha hizi imekuwa ni mazoea, hazitoki kadri sheria inavyosema na Wakurugenzi wamefanya kama fedha hizi ni za miradi ya kwao pekee yao, si fedha za Serikali kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, ningeomba uwekwe utaratibu tena ikiwezekana kwa maandishi kuisisitiza sheria hii kwamba ikiwezekana kila mapato ya mwezi yanayopatikana hata kama vitakuwa vinapata vikundi vitano mpaka 10, lakini mwisho wa mwaka watakuwa wana kiasi kikubwa ambacho wameshakitoa na itakuwa inaonesha uhalisia wa kile tunachokizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa ambao sisi tunaotokana na Chama cha Mapinduzi tumetoa ahadi nyingi na ahadi hizi kwa vikundi mbalimbali ambavyo vimeshaundwa kama haziwezi kutekelezeka bado tutakuwa hatuna maneno mazuri ya kuwaridhisha wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye Kamati ya PAC yapo mambo mengi hapa yamezungumzwa na muda uliopita huko nyuma tulisema hapa, kwamba pamoja na CAG kupisha bajeti ambayo tumeipitisha kwenye Bunge hili, lakini ipo miradi, kwa mfano ipo mikataba mikubwa, mikataba ambayo kipato chake tunaamini ni mgawanyo wa Taifa hili. Kwa hiyo kama hatutaweza, kwa mfano, mikataba ya gesi, CAG asipoweza kwenda kukagua huko na haya tunayoyaona bado hatuwezi kuona kile ambacho tunakitarajia miaka 10, miaka mitano ijayo katika kuhakikisha tunamsaidia Mtanzania huyu ambaye ni maskini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni juu ya Kamati kushindwa kufanya kazi. Kamati hizi haziwezi kufanikiwa, Kamati hizi haziwezi kuleta matunda chanya kwa sababu kama nilivyosema, upatikanaji wa Hati Safi ni uandishi bora wa vitabu. Wako wahasibu mabingwa wa kuandika vitabu vizuri. Tutaendelea kusifia Hati Safi lakini miradi kule nyuma ni hewa, miradi haitekelezeki, miradi imekufa. Ni lazima tuhakikishe Kamati hizi zinakwenda kukagua miradi ambayo tunadhani imetumia fedha nyingi za Serikali na kodi ya wananchi pia katika kuhakikisha tunamsaidia Mtanzania huyu ambaye ni maskini na mnyonge.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa sababu ya muda; suala la PSPF, fedha nyingi bado hazijalipwa, tunafahamu Serikali imejiwekea mkakati wa kulipa zaidi ya bilioni 150…
Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru na naunga hoja mkono.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's