Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. William Mganga Ngeleja

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ahsante sana, nakushukuru sana. Na mimi naungana na
wenzangu kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa
Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri sana, yeye pamoja na
wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijazungumzia mambo
manne ambayo nimepanga kuyazungumzia, nina salamu za
pongezi kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Sengerema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, tunaipongeza
Serikali, lakini kwa hapa tunazungumza mbele ya Mheshimiwa
Waziri Mkuu, tufikie salamu kwa viongozi wote wakuu wa
nchi yetu pamoja na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa
namna ambavyo mnaratibu shughuli za maendeleo ya Taifa
letu. Tunazungumza kama Wabunge tukiwa tumejumuika
kutoka katika maeneo mbalimbali. Yapo maeneo ambayo
sisi wenyewe kutoka kwenye maeneo tunayofanyia kazi ni
mashahidi kwa namna ambavyo shughuli za maendeleo
zinafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa
namna ambavyo imeshughulikia jambo moja kubwa ambalo
lilishakuwa kidonda ndugu kwa Taifa letu nalo ni nidhamu
ya kazi. Taifa lilikuwa limefikia mahali pabaya. Sisi wote ni
mashahidi, tumekuwa tukifika kwenye taasisi za umma na
kuona namna ambavyo huduma zimekuwa zikitolewa miaka
iliyopita, lakini tuseme kweli kabisa, katika hii Awamu ya Tano,
tumeshuhudia mageuzi makubwa ya uwajibikaji kwa
Watendaji wetu. Kwa hilo tunamshukuru sana Mheshimiwa
Rais, lakini kiranja mkuu katika usimamizi wa Serikali,
Mheshimiwa Waziri Mkuu. Shukrani za pekee kwa namna
ambavyo unalifuatilia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Sengerema tuna
mambo makubwa yamefanyika, moja, namshukuru sana
Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Jimbo la Sengerema. TAMISEMI pale, Mheshimiwa Jafo na
Mheshimiwa Waziri Simbachawene, kile Kituo cha Afya cha
Ngoma A ambacho mmekitengea fedha, wananchi wa
Sengerema wamenituma nifikishe salamu zenu kwa shukrani
kwa namna ambavyo mnatufanyia kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Engineer Lwenge na msaidizi wako Naibu
Waziri, ule mradi mkubwa kabisa katika nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwa ngazi ya Halmashauri na Wilaya
unaofanyika Sengerema, sasa uko katika hatua za mwisho
kabisa. Shukrani kwenu pamoja na Serikali nzima kwa namna
ambavyo mmesimamia mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Simbachawene
tuna kiporo. Tumezungumza miezi michache iliyopita. Kwenye
hesabu za Mfuko wa Jimbo zilizofanywa hivi karibuni, yapo
baadhi ya Majimbo ambayo tulipunjwa. Halmashauri ya
Sengerema ni mojawapo hali iliyotokana na makosa ya
kimahesabu. Mmetuahidi kwamba kufikia mwisho wa mwezi
huu fedha zile zitakuwa zimeshafika, lile salio. Naomba
Mheshimiwa Simbachawene na Serikali kwa ujmla, jambo la
mapunjo ya Mfuko wa Jimbo mlifanyie kazi, fedha zifike
mahali pake, zifanye kazi kwa ajili ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizamie kwenye mchango,
la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaanzia kwenye
ukurasa wa 43. Umeanzishwa mfumo wa wazi wa
kielektroniki kufuatilia uwajibikaji na utendaji wa Serikali,
jambo hili ni kubwa sana. Ni muhimu tuipongeze Serikali.
Wamesema, kwa kupitia utaratibu huu, wata-track
utekelezaji wa ahadi ambazo zimefanywa na Serikali kupitia
Ilani ya Chama cha Mapinduzi, matamko, ahadi za viongozi
wakuu wa Serikali akiwepo Mheshimiwa Rais, Makamu wa
Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali
katika hili ni kwamba kwa sababu hatuna mashaka yoyote
kuhusu umakini na Serikali yetu, lakini pia kwa kutambua
kwamba sisi Wabunge ndio daraja la wananchi na Serikali, nilikuwa naomba uandaliwe utaratibu ambao Serikali kupitia
Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, watakuwa wanatushirikisha
Wabunge, tujiridhishe kujua yale ambayo tunaya-track katika
maeneo yetu ya kazi ni yapi? Miradi gani ambayo inaonekana
katika ule mfumo? Mahali ambapo pamesahaulika, sisi
tuwakumbushe kwa kusema hili nalo ni sehemu ya yale
mambo yaliyokusudiwa, yafanyiwe kazi kupitia huu mfumo
wa kielektroniki ambao utawasaidia Watanzania kufahamu
shughuli ambazo zinafanywa na Serikali.
Kwa hiyo, naomba na nilikuwa naamini kwamba
atakapokuwa anafanya majumuisho Mheshimiwa Waziri
Mkuu pamoja na wasaidizi wake, atatusaidia kuona umuhimu
wa kutushirikisha sisi Wabunge tujue miradi ambayo ukigoogle
ama ukibonyeza ule mfumo unakuletea miradi
iliyotekelezwa katika maeneo yetu. Tusipofanya hivyo,
narudia tena kusema kwamba, sina mashaka na utendaji
wa Watumishi wa Serikali, lakini binadamu ni binadamu. Sisi
ni jicho la pili kusaidia kufikia yale yaliyokusudiwa katika
kuyasimamia yaliyotekelezwa kwa namna ambayo
tunakusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia jambo
moja la kufanya maendeleo katika maeneo yetu ya kazi.
Tunapanga bajeti, kila mwaka tunaipitisha hapa. Tumekuwa
na changamoto ambayo sijapata jibu lake, tutasaidiana
kadri ambavyo siku zinaendelea. Suala la disbursement,
kufikisha pesa ambazo tunazipitisha hapa kwenye bajeti
kwenda kwenye maeneo yetu. Ninazungumzia kutotimiza
jukumu hili ama wajibu huu ambao sisi tunaufanya Kikatiba,
tumekuwa tukipitisha bajeti kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza hapa
Sengerema kwenye OC ambazo ndizo fedha ambazo
zimeidhinishwa kufutilia miradi mbalimbali ambayo
tunazungumzia hapa tuna asilimia 20 tu, lakini shughuli za
maendeleo tuna asilimia 30. Nafahamu Waheshimiwa
Wabunge wengi wanalalamika. Hilo siyo la kumnyooshea
mkono mtu yeyote, lakini ushauri wangu kwa Serikali, tusaidiane kupitia chombo hiki cha uwakilishi wa wananchi
tuone namna bora zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejifunza na mwaka 2016
tumeshauriana hapa, yapo mambo tulikubaliana kwamba
yako mambo hayakunyooka sana, lakini tutumie nafasi hii
katika Bunge hili tuelewane vizuri kwa mfumo huu wa bajeti
tulionao, tuone namna ambavyo tunaweza kutekeleza bajeti
ambazo tunazipeleka kule. Haina maana yoyote kupitisha
mafungu hapa kwa kiwango fulani halafu utekelezaji wake
unakuwa chini ya asilimia 50. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumza, hili ni
letu sote, halina itikadi ya vyama kwa sababu tunazungumzia
utekelezaji wa mambo ambayo kwa pamoja tumekubaliana
kuyatekeleza. Kwa hiyo, nashauri sana Kamati ya Bajeti
pamoja na Serikali kwa ujumla, tushauriane namna bora ya
kuhakikisha kwamba mafungu tunayoyapitisha, fedha
zilizokusudiwa zinafika mahali pake palipokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, ukisoma Mkataba wa Nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo sasa ziko sita, ukisoma
Ibara ya 49 inayozungumzia namna ambavyo tunaweza
kuimarisha mtengamano wa nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Inazungumzia habari ya Bunge Sports Club ikiwa
ni chombo mahsusi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kushiriki katika michezo hiyo ambayo
inafahamika kutokana na Mkataba wa Jumuiya ya Nchi za
Afrika ya Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia jambo hili kwa
sababu ninaona kuna masuala yanaingiliana na hii hotuba
ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hasa lile Fungu la Mfuko wa
Bunge. Bajeti ya Bunge Sports Club inatokana na huo mfuko.
Naomba Bunge pamoja na Serikali kwa ujumla tuone
kwamba ushiriki wa Bunge Sports Club katika michezo siyo
jambo la anasa ama la kwenda kutumia pesa hovyo, bali ni
nyenzo ya utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa
Waziri Mkuu, Watendaji wote wa Serikali na Bunge kwa
namna ambavyo mliwezesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 tulikwenda
kwenye mashindano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Mombasa; tuliondoka katika mazingira magumu kidogo,
lakini ninavyozungumza sasa hivi mambo yote yako level seat.
Shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Spika na Naibu Spika
pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo
mliwezesha jambo hilo. Tunasema ahsanteni sana. na
imeandikwa katika maandiko matakatifu, asiyeshukuru kwa
kidogo hatashukuru kwa kikubwa. Sisi tumepata kikubwa,
kwa nini tusishukuru? Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, mimi ni Mjumbe wa Kamati
ya Sheria Ndogo inayoongozwa na Mheshimiwa Mtemi
Chenge. Unapozungumzia fedha nyingi ambazo tunazipitisha
hapa, utekelezaji wake unakwenda kutekelezwa kutokana
na miongozo na sheria zilizotungwa katika Halmashauri, Taasisi
zetu mbalimbali zikiwemo Wizara za Serikali. Ninachotaka
kuzungumza hapa ni kwamba tunapozungumzia Sheria
zinazotungwa na Halmashauri zetu, ndiyo mpango wa fedha
wenyewe. Tumeshuhudia wote kama Taifa, wakati mwingine
viongozi wakuu wa Serikali wamekuwa wakitamka
matamko ambayo wakati mwingine katikati ya safari
wanaamua kuondoa tozo ambazo zimeshakubalika kwa
utaratibu wa kisheria kwa namna ambavyo tumekasimu
madaraka kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, silaumu katika hilo kwa
sababu kama kuna kero ni lazima ishughulikiwe hapo hapo,
lakini ninachosema, tuboreshe utaratibu wa namna
ambavyo tunaweza kukatiza katikati ya safari, kwa sababu
hizi Sheria Ndogo ndiyo zinaongoza mafungu ya kule
Halmashauri na hasa mafao yale ambayo yanakwenda kuwawezesha hata Madiwani wetu ambao sisi tulioko hapa
tunawategemea na ni Madiwani wenzetu kutekeleza miradi
mbalimbali ambako fedha nyingi zinakwenda. Tusiwakatishe
katikati ya safari. (MakofI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya bajeti hizi, kuwe
na utaratibu mzuri wa kukaa pamoja tuelewane kwamba
mwaka huu tutaondoa tozo hizi na hizi ili wasizifuate kwenye
bajeti zao wanazoziweka. Tukikatisha katikati tutakuja
kuwalaumu hawa wawakilishi wa wananchi wenzetu
kwamba hawatimizi wajibu wao, lakini kwa kweli mazingira
ambayo yamesababisha kumbe nasi tumeyachangia. (Maiofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa hili narudia
kusema, simlaumu mtu yeyote lakini naomba tulifanyie kazi
kwa uzuri kwa namna ambavyo tutaweza kuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa yale aliyotujalia.
Pili, nikupongeze wewe Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nakuomba unifikishie salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Spika pamoja na Wenyeviti ambao tumewachagua hivi karibuni kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kutuongoza. Naungana na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake ambayo kwa kweli, mimi nailinganisha na tangazo la vita, kwa namna ambavyo ilipangiliwa, lakini kwa namna ambavyo imetoa taswira ya kero za Watanzania na mikakati iliyopo ya namna ya kuzitatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wenzangu wamesema mengi, lakini kama ninavyosema hili ni tangazo la vita kuhusu maadui zetu wale ambao walianza kutajwa tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ujinga, umasikini, maradhi, lakini sasa yakaongezeka pia ufisadi, rushwa, uzembe na mambo ambayo yanakwaza maendeleo yetu, sina budi na mimi kupita katika baadhi ya maeneo ambayo Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya kurasa 36 aliyoyataja.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana kwa dhamira yake aliyoionesha na tayari ameshaanza kutenda kwa matendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hili ni tangazo la vita kwa sababu Mheshimiwa Rais baada ya hotuba yake na hata kabla hajaunda Baraza la Mawaziri na kwa nafasi hii pia nawapongeza sana wateule Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na watendaji wengine ambao wameteuliwa kumsaidia Mheshimiwa Rais; tayari Mheshimiwa Rais aliingia vitani, alishaanza kufanya kazi na akaanza kutumbua majipu kwa lugha ambayo imezoeleka sasa kwa Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza sana, lakini kubwa tunazungumzia uwezeshaji wa huduma kwa Watanzania ambao sisi ni mojawapo ya wadau wakubwa sana katika kuwezesha hilo. Lakini tunapozungumzia kuimarisha huduma za Watanzania tunazungumzia uwezo wa makusanyo ya Serikali na matumizi mazuri ya fedha inayopatikana kutoka kwenye makusanyo yanayofanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya na sisi Watanzania wote, tukiwemo sisi Wabunge, ni dhahiri na jambo la msingi kumuunga mkono na kumpongeza ni hili la kuongeza mapato. Kwa muda mfupi tu ambao amekuwepo Ikulu, kama Kiongozi wetu Mkuu wa Taifa, Mheshimiwa Rais amefanikisha kuongeza mapato ya Serikali yanayokusanywa kwa mwezi kwa kiwango ambacho kimetangaziwa Watanzania, kwa mwezi uliopita tuliambiwa makusanyo yalikuwa shilingi trilioni 1.4! Si jambo dogo!
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba kwa mwendo huu dira ambayo inaonekana sasa, tunajenga uwezo wenyewe wa Taifa kwenda kusimamia kwa kiwango kikubwa sana kuwezesha utekelezaji wa huduma mbalimbali na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais pamoja na mambo mengine, ametuambia na Watanzania tunakiri kwa matendo anayoyafanya kwamba, anataka kuiona Tanzania ya Viwanda katika kipindi chake cha utumishi wa takribani miaka 10 ijayo, tunaamini itakuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia viwanda tunazungumzia mambo mengi, lakini mimi hapa ni mwakilishi wa Jimbo la Sengerema ambako ninawashukuru sana wananchi hawa walionituma, nikiunganisha nguvu na wawakilishi wa Majimbo mengine kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, tunapozungumzia viwanda kwa vyovyote vile tutashuka chini kuzungumzia viwanda vinavyotuhusu katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuungana na wenzangu ambao wamekuwa wakizungumzia umuhimu wa kuwa na viwanda katika Taifa letu na kwa Kanda ya Ziwa na hasa Mkoani Mwanza, Jimbo la Sengerema, viwanda ambavyo navizungumzia hapa ni vile ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza sana, viwanda vya pamba. Nazungumza hapa nikiwa namuona Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, lakini nawaona pia, baadhi ya Mawaziri ambao wanahusika na mambo ambayo yanabeba uchumi wa Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nijielekeze zaidi kwenye maeneo haya, zao la pamba. Ninafahamu, Mheshimiwa Rais kwenye kampeni zake amelisisitiza sana, kufufua viwanda vya kuchambua pamba, lakini na viwanda vingine ambavyo vinategemea mazao ambayo tunayalima katika Kanda ile. Sisisitizi hili katika mtazamo wa Kikanda, nazungumzia yale ambayo wananchi wa Jimbo la Sengerema na Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa wanatarajia kuyaona yaki-reflect ile dhamira ya Mheshimiwa Rais katika kujenga uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili katika eneo la viwanda, si pamba tu! La pili, ni hasa mazao ambayo yanatokana na samaki, mazao yanayotokana na mifugo na mazao yanayotokana na kilimo kwa ujumla. Katika hili, naungana na Mheshimiwa Rais, juzi alipokuwa Arusha alisema na mimi nawaomba Waheshimiwa Wabunge eneo hili tumsaidie sana Mheshimiwa Rais pengine kwa kutolea maelekezo au kupitia Azimio kwa kadri itakavyokuwa ama kupitia taratibu za Kamati zetu mbalimbali za Bunge, hili la kulishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kuendesha na kusimamia baadhi ya viwanda ambavyo tunaviona vinaweza kutumia rasilimali ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo la kuachia lipite hivi hivi, kwa sababu tunaliweza, tunaweza kulifanya, malighafi iliyopo hapa hapa nchini, nikadhani kwamba ni jambo la msingi Bunge lako Tukufu tujipange tuone namna ambavyo tunaweza kum-support Mheshimiwa Rais kutekeleza hiyo azma ya kuweza kuwa na viwanda ambavyo Wanajeshi kwa ujumla wao wanashiriki katika kusukuma hili eneo la viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuzungumzia linahusu sekta ya afya. Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, pale Sengerema tuna hospitali ya mission ambayo imepewa hadhi ya kuwa hospitali ya Wilaya, na kwa utaratibu wa sera ya afya hiyo hospitali ina hadhi ya Hospitali ya Rufaa ya Kimkoa. Hospitali ile tumekuwa na matatizo ya muda mrefu, nimeyazungumzia sana, lakini kikubwa ambacho ninakizungumzia sasa hivi ni kwamba, ruzuku inayopatikana kwenye hospitali ile haitoshelezi na miaka kadhaa tumekuwa tukiomba na hatujafanikiwa sana katika ombi letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahesabu ya ruzuku yanatokana na vitanda 150 vilivyokuwa vinatajwa kipindi kile wakati Mkataba wa Serikali na wa-missionary wenye hospitali hii ulivyofungwa, leo hii ina vitanda zaidi ya 300. Ninachoomba Mheshimiwa Waziri wa Afya, ombi letu liko Wizarani pale, ninakuomba sana ombi letu ulizingatie la kuongezewa ruzuku kutokana na vitanda ambavyo viko pale vinavyohudumia wananchi wa Jimbo na Kanda ile ya Sengerema.
Mheshimiwa Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais inayoshughulika na masuala ya TAMISEMI, Mji wa Sengerema mnaufahamu Jimbo la Sengerema, Wilaya ya Sengerema mnaifahamu, Mji wa Sengerema una hadhi ya Mji Mdogo, lakini kwa miaka minne iliyopita tulileta ombi letu na tulikidhi vigezo wa kuubadili ule mji ufikie Halmashauri ya Mji. Nafahamu Serikali imekuwa ikishughulikia jambo hili, nina wajibu wa kukumbushia hili kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, kwamba tunamba ombi letu la kufanya Mamlaka Mji Mdogo wa Sengerema ifikie hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Simbachawene kuna lingine tuliongea na wewe la madawati, ombi langu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, sisi tulikuwa na Kikao cha RCC kule Mkoani, tumezungumza tukasema Wakuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya wamepewa malengo na Serikali ya kuhakikisha kwamba kila shule ya msingi na sekondari, inakuwa na madawati ya kutosha. Sasa sisi Wilaya ya Sengerema tumebahatika kuwa na msitu wa Serikali shamba la miti linafahamika liko Jimbo la Buchosa na kwa sababu Wakuu wa Wilaya na Mkoa wamepewa mamlaka ya kuomba ridhaa ama kupata vibali kutoka Mkoani, nilikuwa naomba sana tusaidiane pamoja na Mheshimiwa Profesa Maghembe tupate hivyo vibali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aelezwe na Wakuu wa Wilaya ili sisi tutengeneze madawati kwa ajili ya kusaidia vijana wetu wanaosoma katika shule za sekondari na sule za msingi kwa Wilaya na Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Bunge hili linahitaji kutengeza action plan, namna ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kuitekeleza hotuba hii ina mambo mengi. Sisemi hili kwa maana ya kwamba hatuiamini Serikali yetu, lakini sisi kama wadau muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo, na naamini unalifahamu na mkakati naamini wa Kamati ya Uongozi upo, sisi ni muhimu sana tutengeneze action plan kwa masuala yanayozungumziwa hapa tuone ni namna gani tunajipanga kumsaidia Mheshimiwa Rais na moja ni hili ambalo tumeshalifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kamati ya Sheria Ndogo imeundwa ni Kamati mpya, mimi ni mmojawapo ya Wajumbe katika Kamati hiyo, ninaamini kwamba tutakuwa na jukumu la kupitia sheria zote ambazo ni kero kwa wananchi na hasa zinawezesha kutoa ushuru ambao ni kero kwa wananchi katika Halmashauri zote za nchi yetu. Lakini tukishakuwa na action plan katika Bunge hili tutaisaidia sana Serikali kuikumbusha kutekeleza yale ambayo yamesemwa katika hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana, nakupongeza sana, naungana na wenzangu kwa mara nyingine tena kuunga mkono hoja, kuunga hotuba hii nzuri ambayo ni tangazo la vita kwa ajili ya kuondoa na kupunguza umasikini wa Taifa letu. Ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Kwanza na mimi naungana na wenzangu kukupongeza sana kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuipongeza Wizara kwa hotuba yao nzuri. Katika kuwapongeza pia nitawakumbusha baadhi ya mambo yanayohusu Jimbo langu la Sengerema lakini pia nitaomba maombi katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nina ombi langu la muda mrefu, naikumbusha Wizara, naamini watendaji wa Wizara pia wako hapa wanasikiliza. Wilaya ya Sengerema tuna Hospitali Teule ambayo kimsingi inamilikiwa na watu binafisi, ni Shirika la Kidini la Roman Catholic lakini ndiyo hiyo hiyo hospitali ambayo imekuwa ikisaidia wananchi wa Sengerema na maeneo mengine yanayozunguka eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote nimekuwa nikikumbusha na leo nakumbusha tena kwa mara nyingine na naamini nitapata majibu sahihi leo kwamba formula inayotumika pale kutoa ruzuku ya Serikali ambao ni utataribu wa kawaida ina-base kwenye vitanda 150 lakini leo hii hospitali ile ina uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kuzingatia uwezo wa sasa wa vitanda zaidi ya 375. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu liko Wizarani, naamini Katibu Mkuu yupo anaelewa, ambacho namuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, wakati wanatoa majumuisho ya ufafanuzi wa hoja zao kesho basi hoja hiyo ya ombi letu la Sengerema ambalo ni ombi la muda mrefu walitolee majibu. Hospitali ya Sengerema kwa kweli inasaidia Wilaya nyingi zilizoko upande wa Magharibi mwa Mkoa wa Mwanza, kwa hiyo, naomba nipate ufafanuzi kuhusu ongezeko la ruzuku kwenye Hospitali Teule ya Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu walioshauri kwamba Bohari ya Dawa ifungue maduka yake katika kila Hospitali za Wilaya. Tunafahamu juhudi zinazofanywa katika Hospitali za Rufaa pamoja na Mikoa, lakini haitoshi. Inawezekana kabisa kwamba changamoto yake ni kwenye bajeti lakini kama nilivyoshauri wakati nachangia Ofisi ya Rais na kama Wabunge wengine walivyoshauri, mafungu haya bado hatujaridhia, eneo hili la huduma ya afya ni muhimu sana, usambazaji wa dawa ni mojawapo ya jambo muhimu sana katika uendelezaji wa Taifa letu. Tungependa kuona huduma hii inawasogelea zaidi wananchi hasa katika hospitali za Wilaya. Tuangalie namna ambavyo tunaweza kurekebisha bajeti zetu tukawezesha hii Bohari ya Dawa kupitia Wizara ya Afya tuwasogezee wananchi huduma katika kufungua maduka ya dawa katika hospitali zetu za Wilaya. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilikuwa nasoma hotuba ya Wizara, uko ukurasa umeelezea Hospitali za Kikanda hasa za rufaa, nadhani ukurasa wa 52, wameelezea mambo mengi. Nina ombi hapa, Taifa kwa muda wote limekuwa linajitahidi sana kujenga hospitali za rufaa kikanda kurahisisha huduma kwa kusaidiana na sekta binafisi na hasa masharika ya dini. Nafahamu zipo hospitali kubwa ambazo zina hadhi ya rufaa ambazo zinamilikiwa na makampuni ama mashirika binafisi. Hata hivyo, bado Serikali pia haijawahi kusimamia juhudi zake za kufungua hospitali kubwa za rufaa zinazomilikiwa na Serikali. Ombi langu kwa Wizara ya Afya izingatie na itafakari upya mwelekeo wa ufunguaji wa hospitali za rufaa. Ombi langu naloliweka mbele ya Bunge lako Tukufu ni ujenzi wa hospitali inayomilikiwa na Serikali yenye hadhi ya rufaa katika Kanda ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 52 hapa utaona zipo kanda ambazo zimeainishwa zingine zina mikoa miwili, sitaki kusema hizi zenye mikoa miwili zidharauliwe, hapana! Ninachotaka kusisitiza pamoja na kwamba Kanda ya Ziwa tuna hospitali inayoitwa Hospitali ya Bugando kwa kweli imezidiwa. Sisi tunaotoka kule tunafahamu huduma zilizoko pale sasa hivi, sitaki kuwabeza juhudi wanazozifanya wauguzi na madaktari waliopo pale, lakini kimsingi wamezidiwa. Hii ndiyo Kanda ambayo ina mikoa mingi zaidi lakini ina hospitali moja tu ya rufaa ambayo kwa kweli kwa mazingira tuliyo nayo sasa hivi haimudu na haikidhi! Huko nyuma tulishatoa ombi hili na tukaahidiwa kwamba Serikali ilikuwa inatafakari kujenga Hospitali ya Rufaa katika Kanda ya Ziwa. Tunaomba sana Serikali kupitia Wizara hii itafakari na baadaye mtupe maelekeo na matumaini tunakoelekea ni wapi. Uwezekano wa kujenga Hospitali ya Rufaa kwa Kanda ya Ziwa upo au haupo? Hilo ni jambo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kushauri na kwa kweli ni kwa kuzingatia hali halisi tu ilivyo ni kuhusu hizi huduma za wazee. Tunaona juhudi za Serikali zinafanyika, madawati ya wazee yamefunguliwa kwa kila Hospitali ya Wilaya lakini jambo hili linahitaji ufuatiliaji wa makini. Nashukuru mmesema sasa hivi kutakuwa na madawati ya kutoa taarifa lakini sisi tulioko site tunafahamu, kama alivyosema Mheshimiwa Shabiby na Waheshimiwa wengine, kwa kweli madawati yale yamekuwa kama vile ya kutoa huduma za vipimo na kuandikiwa tu ambacho wewe kinakusibu maana wazee wakifika pale mara nyingi hawapati dawa. Naomba jambo hili tuliangalie kwa umakini na kwa macho mawili ili kuimarisha huduma za afya kwa wazee. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri sisi wote tuliopo hapa hata kama siyo wazee ni wazee watarajiwa tu, ndiyo nature ilivyo tutafika hatua hiyo, kwa hiyo, naomba sana wazee wetu tuwazingatie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, naishukuru sana Wizara, Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pia Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Ummy ameniahidi kwamba baada ya bajeti hii atafika Wilaya ya Sengerema, tunamkaribisha sana. Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, miezi miwili iliyopita alikuwa Sengerema tunamshukuru sana kwa juhudi zake alizofanya. Tunaomba tena msichoke kuwazungukia wananchi kwa sababu kadri mnavyofika ndivyo mnavyoimarisha utoaji wa huduma zinazotakiwa katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kujaalia yaliyotokea mwaka 2015 na hatimaye kupitia wananchi wa Jimbo la Sengerema wakaendelea kuniamini na sasa naungana na timu ya kikosi cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea maeneo matatu; la kwanza, nina masuala yangu ya Jimbo ambayo naamini Serikali kupitia Mawaziri husika wanaendela kuyafanyia kazi. Pia nitatoa ushauri kidogo na mwisho nitauzungumzia utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Waheshimiwa Wabunge wengi hapa kuunga mkono hotuba na mapendekezo ya bajeti yaliyoletwa hapa mbele yetu kupitia Mawaziri wawili hapa Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki na wasaidizi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hizi za Waheshimiwa Mawaziri hawa zimebeba mambo mengi sana; na kwa kadiri michango inavyoendelea inaonekana tu wazi ni dhahiri kwamba mambo mengi yamefanyika na kwenye mipango kuna mambo mengi yamepangwa kufanyika.
Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki, nafahamu ninyi mnawakilisha, lakini kuna mambo mnayoyasimamia ninyi yanaingiliana, ni maeneo mtambuka na maeneo mengine na sekta nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ambalo nataka niikumbushe Serikali, pale Sengerema nina ombi langu la muda mrefu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema. Hospitali yetu teule iliyoko pale imezidiwa. Ruzuku inayotolewa pale haitoshi. Nimekuwa nikiomba na leo nakumbusha tena, ni mwaka wa tatu nakumbusha. Ile ruzuku ambayo iliyotumika kipindi kile wakati hospitali ilikuwa na vitanda 150, sasa ina zaidi ya vitanda 375. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ombi hili liendelee kufanyiwa kazi na ninaamini, nimeshazungumza na Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, naamini wako hapa wanaendelea kulifanyia kazi, lakini nasisitiza kwamba wananchi wa Sengerema wanahitaji kuona matokeo ya ombi letu yakifanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nikumbushe, tuna ombi letu pale Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini sasa limerudi kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu viongozi hawa wako mbele yetu, Mawaziri hawa walioko katika Ofisi ya Rais, naamini kwamba, wanalifahamu. Tuna ombi la kupandisha hadhi Mji wa Sengerema kutoka Mamlaka ya Mji hadi Halmashauri ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusisitiza ni kwamba ombi lile pia limebaki kuwa la muda mrefu. Limechukua miaka kadhaa lakini ahadi za Serikali zimekuwa zinafanyiwa kazi. Naomba nisisitize kwa mara nyingine kwamba wananchi wa Wilaya ya Sengerema wana hamu kubwa kuona Mji wa Sengerema unapandishwa hadhi kutoka Mamlaka ya Mji kuwa Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia hizi bajeti lakini tukitambua katikati yake zipo Halmashauri ambazo hivi karibuni zimegawanywa, kumezalishwa Halmashauri nyingine ndani ya iliyokuwa Halmashauri moja. Ombi langu la ujumla, siyo kwa Wilaya ya Sengerema tu ambapo tumepata pia Halmashauri ya Buchosa, naomba Serikali itafakari, ione namna ya kuziongezea bajeti, kwa sababu bajeti tuliyopitisha mwishoni, Halmashauri zote ambazo ndani yake kumetokea Halmashauri nyingine ikiwemo Halmashauri ya Sengerema na Halmashauri ya Buchosa, nimesikia pia Halmashauri ya Chalinze na nyingine. Hili ni ombi la ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kuhusu suala la madawati. Kwa hali ilivyo na kwa mahitaji ya madawati yanayohitajika katika nchi yetu ya Tanzania, Halmashauri zote kwa vigezo vya mapato vilivyopo sasa, siyo rahisi sana kuliweza hilo jambo. Tunaomba Serikali izidi kutafakari kwa siku zilizobaki hizi mpaka mwezi wa sita. Kama katika bajeti hii tunapokwenda kupitisha tunaweza kufanya adjustment katika baadhi ya maeneo, tuziwezeshe Halmashauri zetu kupata fedha za kutengeneza madawati ili tuongeze kasi ya kutengeneza madawati kwa kuhudumia wanafunzi ambao sisi tunawalea kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano wa Jimbo la Sengerema. Jimbo la Sengerema tunahitaji madawati 23,000 leo. Maana yake unazungumzia zaidi ya shilingi bilioni moja; kwa hakika hatuwezi kuzipata kwa miezi michache iliyobaki pamoja na juhudi ambazo zinaendelea. Sisemi kwamba wananchi wakae au Halmashauri na viongozi wa Mkoa wakae tu, lakini ninachosisitiza ni kuona ni namna gani ambapo sisi kama Bunge tunaweza kushirikiana kurekebisha bajeti iliyoko hapa ili tuokoe pia tatizo ambalo ni la Taifa na siyo tatizo la eneo moja moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, nashauri kwamba tunapokwenda kuhitimisha mgawanyo wa mafungu huko mbele ya safari, tutafakari suala la kuwezesha upatikanaji wa madawati kwa kurekebisha bajeti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mimi niko kwenye Kamati ya Sheria Ndogo. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu jana ameliarifu Taifa habari njema sana, kwamba sasa wameongeza threshold ya Mamlaka ya Halmashauri kupitia vitengo vyao vya sheria kwa maana ya ile mikataba kwamba sasa Halmashauri zote zishughulikie mikataba yote isipokuwa inayozidi kuanzia shilingi bilioni moja na kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo hili tulipe uzito, tukiwezeshe kitengo cha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na hasa Wanasheria walioko katika Halmashauri zetu. Tunaofanya nao kazi, tunaona udhaifu ulioko pale, lakini wakati mwingine ni kwa sababu ya matatizo ya kibajeti. Kwa hiyo, ninachoshauri hapa ni kwamba bajeti yao tuiongeze kwa Kitengo cha Sheria kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili wanasheria walio kule kwenye Halmashauri zetu waweze kufanya kazi zao vizuri zaidi. Siyo zaidi ya hapo tu, pia kuongeza ikama ya Watumishi katika Halmashauri zetu. Tukifanya hivyo tutafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa sana kuhusu utawala bora, lakini naungana na Watanzania walio wengi kuunga mkono hatua zote zinazochukuliwa na Mheshimiwa Magufuli kwa sasa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliweka sawa Taifa letu. Historia inaonyesha, nchi zote duniani ambazo zimefanikiwa kupata maendeleo ya kasi, zimepitia vipindi vigumu lakini pia baadhi ya hatua zilizochukuliwa na viongozi wao wa kitaifa ni pamoja na hizi ambazo amechukua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nitatolea mfano wa nchi ya Singapore. Wote tunafahamu wanaofuatilia historia. Yule Waziri Mkuu wao wa kwanza aliyeiongoza ile nchi kwa miaka 31, yule Lee Kuan Yew aliongoza toka mwaka 1959 mpaka mwaka 1990. Mojawapo ya changamoto alizokutana nazo kipindi kile ni wakati ambapo walivunja muungano wao na nchi ya Malaysia wa mwaka 1965, ni muungano uliodumu kwa miaka miwili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuvunjika, Waziri Mkuu Yew alipata shida sana kutafakari nini kitafuatia, kwa sababu ni nchi ndogo ambayo ukubwa wake ni sawa sawa na nusu tu ya Jiji la London. Alijiuliza kwa sababu walikuwa hawajajiandaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zinazochukuliwa leo na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni kwa ajili ya manufaa ya Taifa hili. Nazungumza haya bila kubeza na kwa namna yoyote ile bila kudharau kazi iliyofanywa na watangulizi wake.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba ni kengele ya kwanza hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya bila kubeza kazi iliyofanywa na watangulizi wa Mheshimiwa Rais wa Awamu Tano, lakini kwa hakika Taifa tulipokuwa tumefikia na sisi wote ni mashuhuda, Taifa hili linahitaji kuumbwa upya. Tunalifinyanga upya ili tusonge mbele kwa pamoja. Kama alivyofanya Waziri Mkuu wa Singapore, Taifa hili linahitaji juhudi hizo. Waziri Mkuu wa Singapore yule baada ya ule muungano wa Malaysia kuvunjika, alijifungia wiki sita, akaenda Kisiwani kule akakata simu hakuwa na mawasiliano na Baraza lake la Mawaziri, hakuwa na mawasiliano na Wabunge wenzake, akasema yeye anajifungia kutafakari mustakabali wa Taifa lile.
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuapishwa, aliendesha hii nchi pamoja na Waziri Mkuu kama jeshi la mtu mmoja, akitafakari mustakabali wa Taifa hili. Hatua zinazochukuliwa leo zisitufanye sisi kama Taifa kutoka njia kuu. Tunafahamu hapa wapo watu wanalalamika kwamba hatua anazozichukua zinazidi kiwango, lakini fikiria yanayotokea! Soma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali, yanayosemwa haya, ni nini kifanyike kudhibiti? Kwahiyo, naungana na wenzangu na ninawashawishi wenzangu kwamba tuungane pamoja kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia habari za wenzetu kusema Ibara ya 18 ya Katiba imevunjwa. Tuache kuwapotosha wananchi. Kinachosemwa kwenye Ibara ya 18 hapa, ni wananchi kupata kuwa na haki ya kupata taarifa, utaratibu umeandaliwa na Bunge hili. Kilichobadilika ni ratiba tu. Kwa nini tunang’ang’nia live? Kuna haki gani inayosemwa “live” katika Katiba yetu? Hakuna haki live inayooneshwa katika Katiba yetu. Kwa nini hawa wenzetu wanapiga kelele? Mambo mengine yanakatisha tamaa sana. (Makofi/Kelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma ukurasa wa 17 wa taarifa ya wenzetu, wanasema Serikali isafishe mtandao wa ufisadi uliojengwa na Wakurugenzi wa Halmashauri na wahasibu wao wa kutoa tender kwa upendeleo. Unalikuta jambo hili limeandikwa katika taarifa ambayo inawasilishwa hapa na inajenga historia ya maamuzi na mapendekezo yanayotolewa na Kambi ya Upinzani. Ni jambo la aibu! Kwa sababu jambo hili la tender kutolewa, sisi Waheshimiwa Wabunge hapa ni sehemu ya Madiwani kule, ni jambo la kusimamia sisi; siyo jambo la kuja kulalamika hapa. Unamlalamikia nani? Kama ni udhaifu wa Halmashauri yenu, ni wa kwenu. Miongozo na taratibu zipo wazi hapa! (Makofi)
Mhesimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema tu kwamba tusiwapotoshe Watanzania kwa sababu ya hasira tulizonazo. Wote tunafahamu tulivyokumbushwa, huu mchezo hauhitaji hasira, ni lazima uwe tayari. Ukiwa na hasira utapata taabu kidogo, kwa sababu ya mambo yanavyokwenda. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimalizie kwa kusema naunga mkono hoja asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa hiyo fursa uliyonipatia ya dakika tano, nashukuru sana. Nimesimama hapa kuungana na Waheshimiwa Wabunge wanzangu kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo inatuunganisha Watanzania endapo mambo haya yatatekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea kuchangia, wiki moja iliyopita Taifa zima lilipata habari ya mauaji yaliyotokea Jimboni Sengerema. Nasimama hapa kwa niaba ya Wanasengera na Watanzania wengine kuwaombea marehemu wetu waliouwawa kikatili sana, Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia navishukuru sana vyombo vya habari kwa jinsi ambavyo vimezungumzia jambo hili na kupeleka ujumbe mahsusi kwa jamii. Kwa fursa hii navishukuru na kuvipongeza sana vyombo vya dola kwa namna ambavyo vimefanya kazi kubwa na kwa kweli sasa hivi watuhumiwa wameshatiwa mbaroni na naamini kwamba haki itatendeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa sababu ya matumaini kwamba yakitekelezeka yaliyomo humu ndani Taifa litakuwa linasonga mbele kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ninalotaka kuzungumzia ni masuala ya jimboni kwangu. Nimeona pale kuna masuala ya ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi, zimetengwa shilingi milioni 600, naipongeza sana Serikali kwa ajili ya kupata Mhandisi Mshauri ili afanye usanifu, mambo ya design na mambo mengine ili hatimaye ujenzi wa daraja uanze, naishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwaka jana tulipitisha bajeti ya ununuzi wa kivuko kingine hapo hapo Busisi Kigongo na hapa tumeelezwa kwamba taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu, taratibu za kufanya upembuzi yakinifu ulishakamilika na sasa taratibu za manunuzi ya hicho kivuko yanaendelea vizuri. Nashukuru sana na naipongeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku nne zilizopita tulikuwa na sakasaka na hekaheka kule Sengerema kwenye kivuko cha Kamanga. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana pamoja Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wako kwa kutatua hilo tatizo na sasa vivuko vyote vinafanya kazi, kwa hiyo nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwangu nimetengewa fedha za matengenezo ya barabara lakini nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri nafahamu kwamba hii ni bajeti ya kwanza kama walivyozungumza Wabunge wengine, siyo rahisi sana mambo yote yaliyoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na hata kwenye mipango yetu yakawa reflected kwenye bajeti hii. Nonachoomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho asisahau kuzungumzia barabara ya Kangama - Sengerema kilometa 35 ambapo ukisoma Ilani ya Uchaguzi, ukurasa wa 60 utaona imehaidiwa kujengwa kwa lami. Pia kuna barabara nyingine ya Sengerema – Nyehunge, Jimbo la Buchosa kwa Mheshimiwa Dkt. Tizeba, kilometa 68 iko kwenye ahadi. Tuna barabara nyingine ya kutoka Busisi, Jimbo la Sengerema kwenda Jimbo la Nyang‟hwale na kuelekea Msalala hadi Kahama kwenye Jimbo la Mheshimiwa Maige. Hii ni barabara ambayo imeahidiwa na Mheshimiwa Rais kujengwa kwa lami. Ni barabara inayounganisha mikoa mitatu, mkoa wa Mwanza, Geita pamoja na Shinyanga. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho azungumzie hilo pia kutupa matumaini kwamba mipango ya utekelezaji itafanyika lini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la reli limezungumzwa sana na hasa nazungumzia reli ya kati. Kitu ambacho nataka niseme, hizi hotuba zinavyokuja hapa zina miongozo yake, hotuba tunazozijadili hapa zinaletwa kwa miongozo. Mojawapo ya mazingatio ambayo hotuba hizi zinatakiwa kuyazingatia ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa sababau ndiyo Serikali iliyoko madarakani lakini pia na ahadi na maagizo au maelekezo ya wakuu wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia ujenzi wa reli ya kati, jambo hili siyo jipya wala siyo geni, tumelizungumza kwenye Mpango wa Maendeleo, tumelizungumza katika mazungumzo yetu ya kawaida na pia tumekuwa tukizungumza katika bajeti zilizopita. Kwenye Ilani yetu unafahamu, ukisoma ukurasa wa 66, ahadi ya 69 utaona tumesema upembuzi yakinifu ulishakamilika, kwa hiyo ilikuwa ni kwenda sasa kufanya upembuzi wa kina zaidi ili hatimaye ujenzi uanze na kikwazo kikubwa ilikuwa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hili kwa uchungu kwa sababu inavyokuja ni kama vile ujenzi wa reli ya kati haujawekwa wazi hapa. Ukisoma ukurasa wa tano na wa sita wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri inasema, hotuba hii imetayarishwa kwa kuzingatia Ilani ya uchaguzi, mambo mengine pamoja na maagizo ya Serikali. Tarehe 25 Aprili, Serikali kupitia Msemaji wa Ikulu, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano…
NAIBU SPIKA: Kengele ni moja Mheshimiwa Ngeleja, dakika tano zimekwisha.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. WILIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimshukuru sana na jirani yangu Mheshimiwa Kiswaga kwa ukarimu wake kwa kunipa dakika tano hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo pamoja na Naibu wake Dkt. Kalemani kwa kazi kubwa wanayoifanya. Lakini nianze kwa kupeleka salamu maalum za shukrani kuungana na watanzania wengine kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna alivyosimamia uamuzi wa kushirikiana na Uganda kujenga lile bomba la mafuta kutoka Uganda kuja kupitia Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba ujenzi wa bomba lile ulikuwa na ushindani mkubwa, ni hitajio la kila nchi inayopatikana ndani ya mipaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wae ule, pia umebadilisha siasa za nchi za Afrika Mashariki, kwa hivi tunampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo tunakupongeza sana kwa namna ambavyo ulisimamia utekelezaji ule ukiongoza kikosi cha wataalam hongera sana pamoja na timu nzima ya Serikali. Dkt. Kalemani miezi miwili iliiyopita ulikuwa Sengerema, tunakupongeza sana kwa ziara iliyoifanya, mafanikio yake tumeshayaona, lakini kuna moja nilitaka nikukumbushe Mheshimiwa Kalemani, tulivyokuwa pale katika ule Mgodi wa Nyanzaga ulisema uliwapa siku 14 wale wachimbaji wenye leseni ile ambayo wamepewa ambayo ni ya Acacia, ulisema utawaandikia barua uwape notice ya siku 14, waeleze kama wana nia ya kuendeleza ule mgodi ama laa, na kama hawatakuwa na nia Serikali ichukue uamuzi mwingine kwa kutoa leseni ile kwa watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatarajia kwamba Mheshimiwa Waziri, utakapokuwa unafanya hitimisho/majumuisho yako ya jioni ya leo basi utatoa hatima na mwelekeo wa Mgodi wa Nyanzaga ambao unapatikana katika Jimbo la Sengerema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 30 wa hotuba ya Mheshimiwa Profesa Muhongo ambayo kwa kweli imebeba mambo mazito na mazuri, mojawapo ya mambo yanayozungumziwa pale ni kufikisha umeme katika baadhi ya maeneo ambayo hayafikiki kirahisi, hayafikiwi na umeme wa Gridi ya Taifa. Na mazingira ya maeneo hayo yanayozungumziwa ni pamoja na visiwa, Jimbo la Sengerema ambavyo msemaji ndio anaiwakilisha ina maeneo ambayo hayafikiki kirahisi, nina visiwa kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alivyokuwa anachangia jana Mheshimiwa Dkt. Tizeba alisema hapa, lakini mimi nataka niungane naye kwamba katika yale aliyozungumza ni pamoja na visiwa vya Juma Kisiwani, Chitandele, tuna kisiwa cha Chikomelo kule pamoja na Lyakanyasi. Nilikuwa naomba mtakapokuwa mnatafakari kuyafikia maeneo ambayo hayafikiki kirahisi msije mkasahau visiwa vinavyopatikana katika Jimbo la Sengerema na Wilaya ya Sengerema kwa ujumla ikiwemo Jimbo la Buchosa kwa ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba na maeneo mengine ambayo tunakumbwa na hilo jambo ambalo tuko katika maeneo ambayo hayafikiki kirahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri inatukumbusha kwamba malengo ya Serikali kufikia mwaka 2020 katika eneo la uzalishaji umeme tunakusudia tuwe tumefikia uzalishaji wa umeme kiasi cha megawati 4,915 kutoka kwenye 1,500 tulipo sasa. Nilichotaka kusema nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kufafanua, kuna miradi mingi imetajwa hapa, lakini kwa mahitaji haya na mkakati wa Serikali sasa hivi wa nchi ya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, tunaamini demand itaongezeka zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka atusaidie katika mipango tuliyonayo, je,ni pamoja na uendelezaji wa miradi ya Hydro, inayotokana na nguvu ya maji ama vinginevyo kwa sababu tuna potentials kama Stiegler’s Gorge lakini tuna Mpanga, Ruhuji, Mnyera, Rukose, tuna kule Kilombero, tuna maeneo mengi ambayo yanaweza kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji. Tunataka kujua tu kama katika mpango wetu wa kulitoa Taifa hili, kufika hapo mblele tunakususia kujumlisha hii miradi mikubwa ambayo inaweza kuzalisha umeme kutokana na nguvu ya maji/
Mheshimiwa Mwenyekiti,la mwisho, kwa sababu ni dakika tano tu, tarehe 21 Aprili, Shirikisho la Wachimbaji na Watafutaji wa Madini walitoa taarifa wakifafanua ushiriki na uwezesho na namna ambavyo wao wamechangia katika uendelezaji wa uchumi wa Tanzania. Katika baadhi ya mambo waliyoyazungumzia walitoa hisia zao na taarifa zilitoka kwenye vyombo vya habari vingi tu kwamba mpaka sasa hivi wameshachangia kiasi kikubwa. Lakini hoja ninayoizungumzia hapa ni kwamba tunaiomba Serikali itoe ufafanuzi itakapokuwa inafanya majumuisho, kwa sababu mchango wa kwenye Pato la Taifa wa sekta ya madini sasa hivi ni asilimia tatu pointi kadhaa. Lakini sisi tuna dira ya Taifa hapa inasema katika sekta ya madini tunakusudia mchangowa Taifa uwe umeshafikia asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema kwa sababu maandalizi ni sasa, miaka tisa, kumi iliyobaki sio mingi sana, pengine katika hatua hii Mheshimiwa Waziri, pamoja na Serikali nzima inaweza kukusaidia kutoa mwelekeo kwamba mikakati iliyopo kutoka kwenye asilimia tatu na ukizingatia changamoto zinazopatikana katika sekta ya madini duniani sasa hivi, ni mikakati ipi tuliyonayo ya kutoka hapa kusogea mbele kufikia hiyo asilimia 10 ifikapo mwaka 2025?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naungana na Watanzania wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa tunayoifanya katika kuendeleza sekta. Lakini pia nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, wameanza vizuri sana wamefanya kazi kubwa sana, tunakushukuru sana na tunawatakia kila la heri.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nianze kwanza kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na watumishi wote wa Bunge, kama mtakavyokumbuka kwa mujibu wa Katiba ya Bunge Sports Club ambapo wamiliki wake na wanachama ni Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watumishi wote, tarehe 1 Juni, 2016 kwa pamoja mlinichagua kuwa Mwenyekiti wa Bunge Sports Club. Natumia fursa hii kuwashukuru sana. Ahsanteni sana. Ninaahidi kutowaangusha katika masuala ya burudani na michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara ya Fedha na Mipango kwa hotuba yao nzuri, imetupa mwelekeo, lakini shukrani za pekee ni kwa Mheshimiwa Rais, amekuja na bajeti ambayo 40% inakwenda kwenye maendeleo ya Taifa. Tunashukuru sana kwa sababu, ni kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida, kwa taratibu za kawaida za mijadala kama hii, ukiona watu hawaliongelei jambo, maana yake wanakubaliana nalo. Kwa hiyo, hata mimi mwenyewe sitatumia muda mwingi sana kwa mambo ambayo hayana mjadala mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee mambo machache. Ukurasa wa saba wa Kitabu cha Hotuba cha Mheshimiwa Waziri anatukumbusha malengo makuu ya hotuba hii ya bajeti kwamba, la kwanza ni kutatua kero za wananchi, lakini la pili ni kujenga uchumi wa kipato cha kati kiuhalisia kwa kusimamia kwa umakini na utulivu kuhusu uchumi wetu huu uliopo sasa. Kwa kweli uchumi wetu uko vizuri. Pamoja na kwamba ni nchi maskini, lakini wote tunakumbuka kwamba kwa taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia mwaka jana, 2015 mwanzoni Tanzania sasa siyo miongoni mwa nchi masikini sana duniani, tumeshajinasua kutoka kwenye lile kundi. Kwa hiyo, kwa namna yake kwa aina fulani tuna utulivu wa kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye hoja niliyokuwa naisema, yale mambo ambayo hayazungumzwi sana, hayana utata hapa, tunakubaliana nayo; lakini yako mambo yanahitaji Serikali na Wabunge tuyatafakari kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nihoji kuhusu hili lengo la pili la kuusimamia utulivu wa uchumi wetu kwa umakini na kwa ubora ili kuongeza tija na hasa katika suala la ajira. La kwanza, hivi tunapokuwa tunaanzisha kodi ya VAT kwenye huduma za utalii wakati tunafahamu kabisa majirani zetu, washindani wetu wameshaondoa hiyo kodi, huu ni usimamizi makini wa uchumi ambao tunakusudia kuufikia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kama alivyosikia Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla mlivyosikia, Waheshimiwa Wabunge tukiwa wawakilishi wa wananchi, kuna hajo na kuna jambo la kutafakari hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anafanya rejea kwenye hotuba yake wakati anawasilisha, alisema baadhi ya nchi ambazo zimekuwa na utaratibu huo ni pamoja na Kenya, lakini kesho yake kuna gazeti moja liliandika Mheshimiwa Waziri wa Fedha apigwa chenga. Kwa sababu nchi ile siku hiyo hiyo, bajeti zetu kwa kuwa zilisomwa pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati tuna-introduce hiyo kodi, wenzetu wanaiondoa na ni jambo la kusikitisha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri asikate tamaa, hatujachelewa, tuko pamoja hapa tunajadili. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali kwa ujumla, wasikilize mawazo na ushauri wa Wabunge kwa sababu ni wawakilishi wa wananchi na ni kwa nia njema, hatushindani, hakuna nani zaidi hapa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba suala hili tulitafakari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, natafakari tu. Ukisoma ukurasa wa 64 tunaongeza ada za usajili wa pikipiki kutoka shilingi 45,000 ilivyo sasa mpaka shilingi 95,000. Nataka niikumbushe Serikali na inafahamu zaidi kuliko sisi. Taarifa iliyotolewa mwezi wa tano mwaka huu na Benki ya Dunia inasema; na mtu mwingine anaweza kusema tusitegemee sana taarifa za Benki ya Dunia, lakini hawa ni washirika wetu, kila siku tunawasifu hapa. Wamesema zaidi ya 50% ya Watanzania ni maskini na katika hao miongoni mwao milioni 12 ni maskini zaidi. Chini ya mstari wa umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia waendesha bodaboda na wamiliki badoboda, pikipiki hizi, ndio kundi la milioni 12. Leo tunapandisha ada ya kusajili vyombo hivi kutoka shilingi 45,000 mpaka shilingi 95,000, tutafakari tu kwa pamoja. Hii kweli tunajenga! Tunasimamia uchumi wetu kwa utulivu na kwa umakini ambao tunauzungumza hapa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tutembee kwenye maneno yetu. We must walk the talk, kwamba hivi ni kweli, hawa ni wapiga kura wetu. Nataka niseme la ziada katika hilo. Ukiongeza hii ada ya kutoka shilingi 45,000 kwenda shilingi 95,000 wanaoathirika miongoni mwetu ni sisi Wabunge hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yaliyopo kwa Waheshimiwa Wabunge kuwasaidia na ujue kwamba fedha hizi ni za mfukoni, kwa sababu Mfuko wa Jimbo hauruhusu mambo haya. Kwa hiyo, nasema Serikali tushiriki kwa pamoja, tusaidiane, tulitafakari tu. Huu ndiyo umakini na utulivu tunaozungumzia? Nadhani hapana. Hata hivyo, halijaharibika jambo, ndiyo maana tunajadili wiki nzima kuhusu jambo hili. Kwa hiyo, naishauri sana Serikali itafakari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina tafakari nyingine tena ukurasa huo wa 64, kuhusu ada ya usajili kwa namba za magari binafsi. Kwa waliokuwa wanapenda kuandika majina yao kama mtani wangu Mheshimiwa Profesa Maji Marefu, imepandishwa kutoka shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 10 kwa kila baada ya miaka mitatu; natafakari tu. Inavyoonekana ni kama Serikali haitaki kuwaona hawa. Nadhani inasema hawa watu ni kama wanajidai. Ni kama wanaleta mbwembwe, ni kama wanaleta “ubishoo.” Kwa sababu hii kodi ni ya hiyari tu, kwa sababu halazimiki mtu kusajili kwa jina lake. Anaweza kusajili kwa namba za kawaida, lakini kwenye eneo hili pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Waziri anakusudia kupata shilingi bilioni 26. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza, kama tuna umakini na utulivu kuimarisha uchumi wetu tulivu kama ulivyo, inakuwaje tunawaongezea hawa? Kwa sababu hawa wanasajili kwa hiyari yao tu. Anyway, kwa nini tunawaongezea sasa? Ni kwa sababu hatutatki tuone watu wamesajili kwa kutumia majina yao? Hii haiwezi kuwa sawa. Tunaishauri Serikali itafakari, tuone kama kuongeza huku tunaweza kufikia lengo tulilokusudia la kuongeza mapato, kwa sababu wataona kama unawapiga penalty na matokeo yake hawataendelea kusajili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilikuwa nalitafakari, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukurasa wa 44 ukaoanisha na Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anawasilisha ukurasa wa 35, katika mambo ambayo tunakusudia tuimarishe kiuchumi ni sekta ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuuliza, natafakari tu, naiomba Serikali itupe ufafanuzi, kwa nini hatuzungumzii uwekezaji mkubwa wa madini? Kwa sababu hotuba hii ya fedha inazungumzia uchimbaji mdogo. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inazungumzia uchimbaji mdogo, kwa nini hatuzungumzii wachimbaji wakubwa na hapa sizungumzii wachimbaji kutoka nje, tunaweza kuzungumzia wachimbaji wa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo madini yetu tuliyoyachimba hapa hayajafikia 20% kwa hiyo, tuna rasilimali ya madini zaidi ya 80%. Kwa nini hatuweki mkakati wa kuendeleza sekta hii itusaidie katika uchumi wetu? Kwa hiyo, natafakari tu, naomba Serikali itusaidie. Kwa nini hatutaki kuzungumzia uchimbaji mkubwa? Au sasa ndiyo mwisho? Naamini kwamba sio mwisho, lakini tunashauriana na ninaamini kwamba tutafika tunakokusidia.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naamini ya kwanza hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia yanayozungumzwa sana. Kodi kwenye gratuity, kiinua mgongo kwa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hilo eneo linasema, Mheshimiwa Waziri anasema, kodi hii imeanzishwa kwa sababu ya kuweka usawa katika walengwa, walipa kodi. Fine, jambo zuri, tunakubaliana, hatubishani nalo. Nasi hatuhitaji special treatment, lakini kwa sababu msingi ni huo huo kwamba tusibaguane, kwa nini imeletwa kwa Wabunge tu wakati sisi ni kada ya watu wengi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaishauri Serikali itafakari, watufafanulie tu, kwa nini wasilete watu wote wenye hadhi ya kisiasa hawa; wapo wengi wametajwa; Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine wa kisiasa. Kwa sababu msingi wa kuweka hii kodi ni kutokuwa na ubaguzi katika wanaolipa kodi. Sasa kwa sababu tumelengwa sisi na msingi wa utungaji sheria, tunakumbushwa waliosoma sheria, mojawapo ya misingi mikubwa inayozingatiwa ni kutokuwa na kodi baguzi. Sasa tunapolengwa sisi Wabunge tu na wengine wakaachwa; hii ndio inayotuchonganisha na wananchi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali itafakari. Kwa sababu mwishoni tutakuwa na muswada, turekebishe tu kwamba kama ni makundi yote yanayopata hadhi hii yote yawekwe hapa, itakuwa fine; lakini isiwe ni Waheshimiwa Wabunge peke yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine bajeti hii si tunakwenda kukusanya na kutumia? Sasa nilikuwa naangalia, hili suala la gratuity yetu limejitokeza kwenye fungu gani hapa kwenye hiki kitabu? Kwamba leo tunaweka hapa; au ni maandalizi ya kisaikolojia ili tusonge mbele? Natafakari tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma pale, kuna eneo limesema ukusanyaji wa kodi za majengo. Hapa naiunga mkono Serikali, nina sababu zangu. Hapa naomba niiunge mkono Serikali kwa sababu pamoja na wenzangu ambao wamezungumza kwa maoni tofauti, baadhi yao na tumegawanyika hapa, lakini msingi wa Serikali iliokuja nao hapa inasema inakwenda kuimarisha ukusanyaji. Naamini Serikali inasikia kwamba yako maeneo TRA hawajajiandaa vizuri, mojawapo ni Wilaya ya Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu mwezi wa tatu, TRA ni pamoja na Halmashauri, zilikaa pamoja; uwezo wao kwa kweli wa kuyafikia maeneo yote kuhusu eneo hili ni mdogo, lakini kwa sababu Serikali kuna eneo inasema imedhamiria kwenda kuimarisha uwezo wa TRA na kwa sababu lengo ni ukusanyaji, lakini mapato yatazirudia Halmashauri, Majiji na Manispaa kama ambavyo imekusudiwa, tuwape Serikali muda kama alivyosema Mheshimiwa Zungu na Waheshimiwa wengine walivyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuipe muda Serikali ikashughulikie hili jambo, lakini kilicholengwa kwenda kwenye Halmashauri kisiende kinyume na hapo. Tuipe nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nasema katika kufanya mambo makubwa ya msingi lazima kuna kuthubutu. Na mimi nina ushuhuda kwa sababu, wakati mwingine nimeshakuwa muhanga nikiwa Waziri wa Nishati na Madini. Wakati nimekwenda China mwaka 2009 nikiongoza msafara wa Serikali kuzungumzia bomba la gesi la kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam wako watu walitubeza sana wakasema Tanzania haiwezi kujenga bomba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati niliitwa kwenye nchi moja kubwa sana duniani, nikaambiwa kwa nini mnafanya hivyo badala ya kuiachia sekta binafsi? Kwa nini msije tukawapa fedha sisi hapa? Tuliwaambia kuna nchi hapa ziliathiriwa na msukosuko wa uchumi wa dunia zilikwenda kukopa fedha kwenye nchi ya China, na sisi tuna historia ya nchi ya China ya urafiki wa miaka mingi, ndiyo maana tumekatiza kwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika hili nilikuwa naomba tukubali tuipe Serikali muda, kazi yake…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Jitu Vrajlal Soni

Babati Vijijini (CCM)

Supplementary Questions / Answers (5 / 0)

Contributions (16)

Profile

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Special Seats (CHADEMA)

Questions / Answers(2 / 0)

Contributions (8)

Profile

Hon. Zubeda Hassan Sakuru

Special Seats (CHADEMA)

Questions / Answers(2 / 0)

Contributions (4)

Profile

View All MP's