Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Richard Mganga Ndassa

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Naunga mkono, pongezi kwa Wizara kwa maandalizi ya hotuba. Naomba kutoa ushauri katika mazao ya biashara.
Zao la katani; leo hii pamba bei yake ilikuwa imedorora, tulikuwa tunaiita dhahabu nyeupe, katani leo White Gold. Miaka ya 70 katani katika soko la dunia, Tanzania tulikuwa tunaongoza, katani bora ilikuwa inatoka Tanzania. Soko la zao la katani limebadilika na kupanda bei ya katani (fibre), kwa tani ni dola 2,200 - 2,500. Serikali iangalie uwezekano wa kuliibua upya zao la katani.
Zao la pamba, nataka Serikali iwaambie wakulima wa pamba kuhusu mbegu zao (Kyuton) ambazo zimeua kabisa zao la pamba kutokana na wauzaji wa mbegu hizo zilizochakachuliwa kwa sababu ya rushwa. Leo naomba nipate maelezo ni nani hasa wamiliki wa kiwanda cha mbegu ziliozokuwa na manyoya. Hawa wameua kilimo cha pamba. Mbegu hizo zilipigiwa kampeni kubwa na viongozi kuanzia ngazi ya Taifa - Wizara na Wilaya, lakini tungependa kujua ni nani aliyewapeleka nje ya nchi Viongozi wa Juu wa Wilaya na Mkoa? Hii ni rushwa, sheria ishike mkondo wake kwa sababu kwa kufanya hivyo wamelizika zao la pamba kisa rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu usindikaji; Tume ya Mazao Mbalimbali tuliyozalisha; tuombe Serikali iangalie utaratibu wa kusindika na kuyaongezea mazao thamani. Mfano: mahindi, hakuna sababu ya kusafirisha mahindi, watumiaji wametaka unga siyo mahindi. Mpunga, watumiaji wanahitaji mchele na siyo mpunga, hapa naomba kwenye maeneo husika, kuwe na mashine za kusaga na kukoboa, lakini mazao haya yaani unga na mchele uwekwe kwenye mifuko ili kila mtu aweze kununua kufuatana na uwezo wake kilo 1, 2, 3 na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ng‟ombe, Watanzania wanataka nyama siyo ng‟ombe. Ng‟ombe wanakunya hovyo njiani, test ya nyama haipo. Kuku, Watanzania wanataka nyama ya kuku, unabeba kuku mzima na manyoya yake kwenda Dar es Salaam, kwa nini wasichinje hao kuku huko huko, nyama ikapelekwe kwenye supermarket na kadhalika.
Narudia tena, napenda na ningependa kujua ni hatua gani zilizochukuliwa kwa wale waliowatapeli wakulima wa pamba kwa kuwauzia mbegu za pamba zisizokuwa na manyoya zisizobeba, zilizosababisha kutoota vizuri tangu zilipotangazwa kwa mbwembwe sana na Viongozi wa Wizara yako. Ningependa kupata majibu yako.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa rasilimali tulizonazo za watu, mazao ya biashara tukiamua kwa dhati, tunaweza tukapiga hatua kubwa hasa tukijipanga vizuri. Ndani ya miaka mitano tuliyofunga mkataba na waliotuchagua, fursa zipo tukiamua hasa kwa kuanza na viwanda vidogovidogo ambavyo tunaweza kuanza navyo. Ili kuvilisha viwanda vya kati na baadaye viwanda vikubwa, kinachotakiwa ni kuundwa kwa mazingira mazuri ya uwekezaji, katika miradi mbalimbali kutokana na jiografia ya nchi yetu. Miradi hiyo ndiyo itakayounda ajira kwa Watanzania walio wengi na hao ndiyo watakaokuza uchumi wetu.
Kama nilivyoanza hapo juu kuwa tunayo rasilimali yetu ardhi, siasa safi na wajasiliamali. Hivyo tukiwatumia vizuri wajasiliamali, tukawawezesha tukawawekea mazingira mazuri kwa kila eneo, kufuatana na uzalishaji wao hasa katika mazao yanayotokana na ardhi, mito, maziwa, miti, mifugo na kadhalika huko waliko, ile idadi ya vijana kukimbilia mijini itapungua. Hebu tuisome ile Sera ya Taifa ya Biashara ndogo, na viwanda vidogo na tuitekeleze kwa kuisimamia. Sote twajua kilimo ndiyo kinachotoa, mapato kwa watu waishio vijijini, tukiamua kuanzisha viwanda vidogo vijijini vitaleta mabadiliko chanya, katika uchumi wa nchi yetu. Hasa vijijini kwa mazao yetu kuongezewa thamani, badala ya mkulima kuuza mazao yao kama yalivyo, viwanda vidogovidogo vitatumika kuyasindika mazao hayo. Mfano badala ya kuuza mahindi vijijini viwe na mashine za kusaga na kukoboa unga badala ya kuuza mpunga wauze mchele uliofungwa katika pakiti ndogo za kilo moja, mbili au tano huko huko vijijini tayari kupelekwa mjini kwa walaji, badala ya kuuza karanga na alizeti kama zilivyokuwepo, na viwanda vya kukamua mafuta, badala ya kuuza matunda kama yalivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujengwe viwanda vya kukamulia juisi, viwanda hivi mbali na kuongeza thamani katika mazao hayo, vitaongeza ajira huko huko vijijini na itasaidia vijana kubaki vijijini. Serikali itambue uongozi katika ngazi za Wilaya, na Mikoa kushawishi wawekezaji katika maeneo yao kufuatia fursa zilizoko zitenge maeneo kwa wawekezaji kwa kuondoa urasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ile dhana ya kujitegemea ya ki-ujasiriamali nashauri Waziri wa Viwanda, awasiliane na Waziri wa Elimu ili kuingiza somo la ujasiriamali katika mitaala ya shule. Kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari, na katika mafunzo ya ufundi stadi, hii itasaidia kupanua elimu na matayarisho ya kazi ili kuongeza hali ya kupenda kuanzisha na kuendeleza ujasiliamali, ili kuwafanya vijana kubaki vijijini. Vijana wakifundishwa ujasiriamali kuanzia msingi, sekondari na katika mafunzo ya ufundi stadi, watabadili mitazamo yao watapenda kujiajiri tofauti na ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona nijikite hasa katika suala zima la ujasiliamali, huko vijijini ili kupunguza idadi kubwa ya vijana kuja mijini kutafuta kazi (ajira) ambazo nazo hapo naomba tujipange vizuri. EPZ tutazipata katika Wilaya zetu na Mikoa yetu, fursa zipo tukiamua na kila mtu akatekeleza na kutimiza wajibu wake ndani ya muda mfupi tutapata matokeo chanya na tutabadilisha maisha ya vijana na kuinua uchumi wa nchi yetu Tanzania. Naomba niwaombe wataalam wote wa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara yako wafanye kazi kwa kuzingatia weledi wao, tuangalie wapi tulikosea na tuparekebishe na tusonge mbele kwa ari mpya. Ili ile ndoto ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli na Watanzania kwa ujumla, Tanzania iwe nchi ya viwanda ili tuweze kuzalisha kwa matumizi ya ndani na baadaye tusafirishe nje ya nchi ili tupate pesa za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza ajira na vijana wetu waweze kubaki katika maeneo yao ya uzalishaji, Mheshimiwa Waziri tulikuwa na viwanda vingi sana kabla ya kubinafsishwa ningependa kujua ni jinsi gani agizo la Mheshimiwa Rais umelitekeleza. Hasa kwa wale waliojitwalia viwanda na kuvitelekeza mbali na kwamba hadi leo hawajalipa pesa zote kufuatia na mkataba wa mauziano (MOU), ni hatua gani umezichukua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha nguo, kiwanda cha zana za kilimo asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima wa pamba, nyuzi, matairi, korosho, kahawa, asali, nyama na kadhalika, ni kichocheo cha upatikanaji wa ajira fedha za kigeni lakini nchi yetu itaitwa nchi ya viwanda. Nchi haiwezi kuitwa nchi ya viwanda wakati viwanda vilivyopo havizalishi katika uwezo wake na havizidi 200-500 tunakuamini Mheshimiwa Waziri, lakini tunakuomba ukaze buti wewe na Wataalam wako, ndiyo mtaifanya nchi hii kuitwa nchi ya viwanda. Ushirikiano na Wizara zingine nchini hii ni kutokana na kutegemeana. Pia chuo chako cha CBE Dar es Salaam nilichosoma mimi kitazamwe upya, elimu inayotolewa pale ni tofauti na zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa utaratibu mzuri alionao wa kuwa msikivu, mtu mnyenyekevu na mwenye mahusiano mazuri sana hasa kwa vyombo vya habari wakiwemo wamiliki na waandishi wa habari. Nakuomba PR hiyo uiendeleze ili tasnia ya habari iweze kuwa nguzo kuu katika ustawi wa Taifa letu. Nakuomba uendelee kuvishauri vyombo vya habari na waandishi wa habari kwamba kalamu zao ziangalie na kuzingatia uzalendo kwa nchi yao Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Michezo Malya kina upungufu mkubwa, lakini kubwa ni kukiboresha chuo hiki ili kiweze kutoa degree ya michezo. Chuo cha Malya ni kiwanda cha kuzalisha walimu wa kufundisha michezo mbalimbali katika shule za msingi, sekondari na vyuo. Michezo ikifundishwa vizuri shuleni, vijana wetu wajipe ajira hasa katika sanaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TFF haisimamii vyema uendelezaji wa mpira wa miguu badala yake imekuwa ni chama cha kukuza vurugu badala ya mchezo wenyewe. TFF imekuwa chanzo cha migogoro kati ya vilabu na vilabu, tofauti na matarajio ya wengi. Ikumbukwe mpira wa miguu ni mchezo unaopendwa na watu wengi lakini Watanzania hawafurahishwi na uongozi wa TFF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, programu ya timu ya under 15, 17, 21 haionekani kusimamiwa vizuri. Michezo ni furaha, ajira, utalii, afya na kadhalika, tofauti na kwetu hasa TFF imekuwa ikilalamikiwa kuhusu matumizi mabaya ya fedha.
Naomba Mheshimiwa Waziri akihitimisha majumuisho aniambie fedha zinatolewa na FIFA kwa miaka mitatu ya nyuma yaani mwaka 2013 - 2015 zililetwa na zilitumikaje? Tujue fedha za wafadhili mbalimbali walioichangia timu yetu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanaume na wanawake, tujue pesa za ligi kuu (VPL) mkataba ukoje hasa upande wa timu shiriki? Yapo malalamiko mengi kwa washiriki wa ligi ya VPL.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ligi daraja la kwanza iliyomalizika hivi karibuni imemalizika kwa migogoro ndiyo maana nimesema kuwa TFF badala ya kuendeleza soka inaendeleza migogoro na upendeleo wa dhati kwa baadhi ya timu. Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze ni namna gani atakiendeleza Chuo hicho cha Malya? Pamoja na kutopatiwa pesa zake za OC, ni vyema wazabuni wakalipwa madai yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Michezo Tanzania (BMT) hivi kazi yake ni nini? Sioni wanachokifanya, wapo wapo tu. Sioni maendeleo katika michezo mbalimbali iliyo chini ya Baraza. Kila chama ni vurugu, siyo kwenye riadha, ngumi, wavu na kadhalika. Je, ni busara kuendelea na hilo Baraza hilo? Kama ni jipu, litumbuliwe. Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kwanza asubuhi hii, nijaribu kujadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. La kwanza, naomba tumwombee Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri sana anayoifanya, lakini naye pia amekuwa akituomba sisi Watanzania wote kwa dini zetu zote, tumwombee sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, hili ni ombi, sisi kama Wabunge tumekuwa na maneno mengi sana humu ndani ambayo kwa kweli hayana tija sana kwa Watanzania. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wa pande zote mbili; upande wa CCM lakini na upande wa wenzetu; Watanzania wanaotusikiliza na kutuona, wanategemea tutoe michango ili kusudi wataalam walioko hapa waweze upata ushauri mzuri zaidi. Hili kwa kweli naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee hapo kwamba, ni vizuri kwa sababu tunazo Kanuni zetu, zituongoze katika kuendesha Bunge letu. Endapo limetokea tatizo, Kiti chako kisisite kuita Kamati ya Uongozi, kwa sababu tukienda na utaratibu huu kama ilivyo sasa, juzi kuna wanafunzi kutoka Msalato walikuwa wamekaa pale, lakini baada ya kuanza kurushiana maneno na kutupa vitabu, wale wanafunzi ambao walikuwa wamekuja kwa ajili ya mafunzo, waliondoka humu ndani. Sasa kwa utaratibu huo, wanapotoka Walimu wao na wao wenyewe wanatuelewaje sisi kama Wabunge? Kwa hiyo, nashauri sana hili tulizingatie kwa sababu sisi ni jicho la Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mheshimiwa Waziri nataka aniambie, kupitia hotuba yake hasa ujenzi wa Mwanza Airport, imetengwa shilingi bilioni 30. Ni za nini? Ni za kujenga uwanja au ni za kukarabati? Kwa sababu tumekuwa tukisema mara kwa mara, jinsi mnavyotenga pesa kidogo kidogo hizi, hazitoshelezi hata kidogo. Ujenzi wa Mwanza Airport gharama yake ili ikamilike, siyo chini ya Dola bilioni 60 mpaka 90. Sasa leo mkitoa shilingi bilioni 30, pesa hizi hazitoshi. Nashauri Mheshimiwa Waziri, hebu suala hili alitazame upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nizungumzie reli ya kati. Namshauri Mheshimiwa Waziri, nimeongea na Naibu wake, mabehewa wanayopeleka kutoka Mwanza…
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, mabehewa wanayopeleka Mwanza kuja Dodoma au Tabora ni machache mno. Unapeleka mabehewa matatu ya abiria kutoka Tabora kwenda Mwanza; kuna msongamano wa abiria kule, lakini watu weo Mheshimiwa Waziri wanawadanganya eti kwamba abiria ni wachache, siyo kweli. Inawezekanaje eneo lingine wakapeleka mabehewa 15 lakini Tabora - Mwanza, mabehewa matatu; wanasababisha watu walanguliwe. Nashauri suala hili litazamwe kwa mara ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, zipo ahadi za Mheshimiwa Rais mbili; ya kwanza ni ujenzi wa barabara ya lami kutoka Magu mpaka Hungumalwa, sijaiona humu ndani. Ahadi ya pili, wataalam nafikiri walikuwepo siku ya uzinduzi wa Daraja la Mto Simiyu pale Marigisu. Mheshimiwa Rais aliahidi kuweka mita hamsini hamsini kwa kiwango cha lami, lakini sijaona humu. Nashauri hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri, barabara ya kutoka Nyanguge kwenda Musoma na barabara ya kutoka Mwanza - Shinyanga Border barabara hizi zimekuwa zikitengewa pesa mara kwa mara; hivi kwa nini tusiangalie namna nyingine nzuri zaidi ili kusudi barabara hizi zikwanguliwe zote kwa mara moja, halafu ijengwe upya kuliko hivi ilivyo sasa? Tutakuwa tunatenga pesa mara kwa mara lakini pesa hizo hazina maana. Kwa hiyo, nashauri wajaribu kubadilika kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, siku ile niliuliza swali hapa na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesifia hizi ndege zinazotoa huduma humu ndani kwa maana ya kwenda Mwanza na Mbeya. Pamoja na kusifia, lakini ndege hizi zinaumiza sana wasafiri wetu. Bei ni kubwa mno! Kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya, sh. 700,000/=, ukienda na kurudi sh. 1,400,000/=; kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam, sh. 800,000/=; kwenda na kurudi ni shilingi milioni moja na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ukichukua ndege kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, siyo chini ya sh. 800,000/=. Hebu tuangalie, ndiyo tunataka huu usafiri, lakini basi usafiri huu usije ukawa kama ni adhabu kwa Watanzania. Nashauri chombo ambacho kipo chini ya Mheshimiwa Waziri kisimamie vizuri ili kusudi wananchi wetu wengi wapande usafiri huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, nawapongeza sana Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa taarifa nzuri ambazo wanatupa sisi Watanzania. Ombi langu kwa upande huu, kama vifaa vyao ni vichache kwa sasa na wanafanya kazi katika mazingira magumu, hebu waongezewe vifaa ili kusudi mamlaka hii iweze kufanya kazi yake vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tunazo taasisi zetu mbili; TPA kuna Kaimu, hakuna Bodi. Kuna maamuzi mazito yapo pale yanatakiwa yatolewe na Bodi. Nataka uniambie, Bodi ile itaundwa lini? ATCL kuna Kaimu, hakuna Bodi na bahati nzuri unasema unataka kupeleka ndege pale. Hivi utaamua mwenyewe pale au itaamua Bodi? Vyombo vile Mheshimiwa Waziri, ni lazima kuwe na Bodi ili iweze kusimamia majukumu yote yaliyopo pale kwa sababu yapo kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri, najua mengine hayapo chini yake, lakini bado ana uwezo wa kumwomba Mheshimiwa Rais ili kusudi taasisi hizi hasa TPA kwa sababu kuna mambo mengi mazuri pale, sasa nani anayasimamia? Nani anaamua? Namwomba sana, Mheshimiwa Waziri, hayo nayo ayachukue.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba Mwanza Airport Mheshimiwa Waziri asipoleta majibu ya kutosha humu ndani nitakamata shilingi. Namwambia mapema kabisa! Shilingi nitaondoka nayo mpaka nipate majibu kwa sababu kila mwaka wanasema watatenga fedha. Mwaka 2015 ilikuwa ni hivyo hivyo, tukatenga fedha nyingi chini ya Mheshimiwa Mtemi Chenge, tukaahidiwa, lakini hakuna fedha iliyotoka. Safari hii namwambia Mheshimiwa Waziri tutaungana watu wote wa Kanda ya Ziwa ili tupate majibu ya kutosha kuhusu Mwanza Airport. Wamesema wengi sana humu ndani na jana Mheshimiwa Maige alisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Mheshimiwa Waziri akilinganisha viwanja vya ndege, sikatai maeneo mengine, kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. Mwanza Airport, hivi hawaijui kwamba ina faida gani kwa nchi hii? Nashauri sana. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu alete majibu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya kati na yenyewe ina maneno. Standard gauge wanayosema sijui, lakini bado nasema viwanja vya ndege Mwanza Airport na reli ya kati. Vitu hivi viwili wakisimamia vizuri, nina uhakika tutasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Nianze moja kwa moja, sitaki nipongeze, niende Ukurasa wa 78 wa Kitabu cha Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana kwa sababu, ametenga asilimia 94 kwa ajili ya maendeleo, lakini hasa kwenye Sekta ya Nishati. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, lakini ili tuipate hiyo trilioni moja nashukuru kwa sababu, bahati nzuri nyuma yangu hapa kuna Waziri Mkuu na ningemwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize vizuri, naomba mumshtue hapo! Hili Jimbo la Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Shabiby, hili Jimbo la Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, eneo lote lile lipate umeme, lakini na maeneo mengine ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tuliomo humu ndani tunaiomba sana Serikali hii, asilimia 94 ambayo ni sawa sawa na trilioni moja; Mheshimiwa Waziri wa Fedha tumekuwa tukisema mara nyingi sana humu ndani kwamba, pesa hizi zitoke, lakini bahati nzuri au mbaya pesa hizi hazitoki! Hata zile fedha ambazo tumeziwekea uzio na zenyewe mnazipeleka sehemu nyingine, lakini ili nchi hii iendelee na ili iwe ya viwanda lazima tuwe na umeme wa kutosha. Tutaimba nyimbo hapa, lakini kama hatuna umeme wa kutosha, umeme wenye uhakika, hatuwezi tukafikia yale malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hapa, Serikali kupitia Waziri Mkuu, mtakapokaa kwenye vikao vyenu huko hii trilioni moja iliyoombwa na Wizara ya Nishati na Madini itoke ili kusudi huyu Waziri wa Viwanda anapozungumzia viwanda, lazima apate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukipata umeme wenye uhakika REA wakasambaza umeme vijijini wale vijana wanaokuja mjini hawatakuja mjini tena kwa sababu kuna umeme vijijini. Naomba sana Serikali zile pesa ambazo tulikuwa tumetenga kwa ajili ya umeme Tanzania, tozo, pamoja na zile ambazo zilibaki mwaka jana, lazima wapelekewe wenzetu wa TANESCO ili kusudi waweze kufanya kazi yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili na hili nimekuwa nikilisema mara kwa mara, Serikali imeshindwa kulipa TANESCO madeni yake, sijui tatizo ni nini! Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati, hii si Serikali kwa Serikali, hivi hawawezi kukaa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha wakaondoa hili deni ili kusudi vitabu vya TANESCO viwe visafi! Maana kila siku tunakuta madeni, madeni, madeni! Hebu wakae chini hili tatizo walimalize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie bomba la gesi; huu ni ushauri kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Bomba hili lina gharama kubwa, linatakiwa liwe na ulinzi wa kutosha na wasiweke pale Waswahili, waweke Jeshi la Ulinzi liende lisimamie ulinzi wa bomba lile kwa sababu, gharama yake ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu, mitambo ya kusindika gesi, LNG; bado hatujachelewa, tuongeze speed kwa sababu, huwezi ukazungumzia trillion cubic meters za gesi tuliyonayo, wamesema 57 trillion, halafu huna mtambo wa kusindika hiyo gesi! Lazima tuwe na mtambo wa kusindika hiyo gesi, vinginevyo tutabaki hapa, hata manufaa yatakuwa hayapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bomba la mafuta la kutoka Uganda kuja Tanzania, Tanga. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuchangamkia, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, hii ndiyo fursa yenyewe, tusiiachie hata kidogo, lakini lazima kuwe na ulinzi wa kutosha katika usimamizi wa ujenzi wa bomba hili la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, REA. Niwapongeze sana REA kwa kazi nzuri sana wanayofanya na niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa umoja wetu, kwa kazi nzuri sana aliyofanya REA, hata kama huwapendi kwa sura zao, basi wapende kwa matendo yao, wamefanya kazi nzuri mno. Cha msingi hapa, sisi kama Wabunge, ni kuibana Serikali, ili itoe pesa za kutosha ili miradi iliyobaki ya REA II na REA III tunayokwenda kuanza, iweze kukamilika ndani ya muda unaotakiwa. Lazima tuibane Serikali humu ndani na tuishauri Serikali kwamba, kwa sababu, tunakwenda kwenye REA III tuibane Serikali ili kusudi iweze kutoa pesa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo dogo upande wa REA, lakini ni vizuri wakarudi nyuma ili wajifunze kwamba, tulifanikiwa REA I, kulikuwa na matatizo gani? Changamoto zilizopo, tumekwenda kwenye REA II changamoto ni zipi tulizoziona? Sasa tunakwenda kwenye REA III zipo changamoto nyingi, hasa urukaji wa vijiji na vitongoji; wanaweka umeme hapa, wanaruka, wanakwenda wanaruka, wanaruka, wanaruka!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri kwa sababu, wanapita kuangalia ni wapi wameweka umeme, ni vizuri kama ni kijiji kimoja basi kijiji chote kiweze kupata umeme. Si vizuri sana wanaweka umeme kwenye nyumba, wanaruka wanakwenda kuweka kwenye nyumba hii, wanaruka! Si vizuri sana, tungependa sana umeme kwenye kijiji X umeme uwepo. Kwenye maeneo ya Jimbo langu, nilishawasilisha kwa Ndugu Msofe maombi, sitaki niseme hapa, lakini nimwombe sana, maeneo ambayo yamerukwa, vijiji ambavyo vimerukwa, naomba katika awamu ya III umeme uweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho. Naomba kusisitiza tena, najua Waziri wa Fedha hayupo, lakini najua Waziri wa Nishati yupo na Waziri Mkuu ananisikiliza. Pesa tunazokubaliana humu kwamba, pesa hizi zinatakiwa zitumike kwa kazi fulani, naomba zitumike kwa kazi hiyo hiyo, zisitumike kwa kazi nyingine na haya ni makubaliano ya Bunge. Nasisitiza tena, tukikubaliana kwamba, pesa hizi zinakwenda kwa ajili ya umeme, kama ni tozo za mafuta ziende zikasaidie kule, kusaidia wananchi wetu ili waweze kupata umeme wenye uhakika, basi ziende.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila umeme wenye uhakika hakuna maendeleo, bila umeme wa uhakika hakuna viwanda. Mheshimiwa Mwijage, ni vizuri wakakaa kwa sababu huko mbele bila umeme wa uhakika, viwanda tunavyozungumza Dar-es-Salaam au maeneo mengine vijijini, havitapatikana! Ni lazima tupate umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni bajeti ya Serikali wala siyo ya Dkt. Mpango. Wapo watu wengine wanalaumu kama vile Dkt. Mpango hii bajeti ni ya kwake, hii ni bajeti ya Serikali inayosomwa na Waziri wa Fedha Dkt. Mpango. Kwa hiyo niwaombe sana tunapojadili tujadili bajeti, tusijadili mtu alivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri kwa Dkt. Mpango kwa sababu yeye ndiye Waziri wa Fedha, yapo mawazo mazuri sana ya Kamati, nashauri kwa mfano suala zima la maji ile tozo kutoka sh. 50/= kwenda sh. 100/= Wabunge wote, Watanzania wote, kama itaongezwa iwe sh. 100 kwa ajili ya maji, nina uhakika Watanzania watanufaika, naomba suala hili ulitazame kwa jicho jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai, mtoto mdogo anategemea maji, akinamama kule wanategemea maji, maji yakiwa mengi vijijini kero kwa chama changu itapungua. Nakuomba sana juu ya hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, imependekezwa, Mheshimiwa Waziri najua yeye ni muungwana sana, chombo chetu kikuu, kisemeo cha Serikali ni TBC, TBC ndiyo mdomo wa Serikali, TBC ndicho chombo ambacho kinaweza kusema kwamba hapa sasa Serikali ifanye hivi, namwomba hebu atumie busara na watalaam wake, hili nalo alione. Mheshimiwa Waziri tukifanya hivyo kwa kweli tutakuwa tumefanya jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimelifurahia sana na niipongeze sana Serikali, nimekuwa Mbunge wa siku nyingi kidogo humu ndani, Wabunge wote wa Vyama vyote tulitakiwa tuipongeze sana Serikali kwa kutenga asilimia 40 ya pesa ya bajeti kwenda kwenye maendeleo, haijawahi kutokea. Nilitegemea Wabunge wote watapongeza kwa sababu pesa hizi asilimia 40 ya bajeti ya trilioni 29 inakwenda kwenye shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri kwamba, ingekuwa ni amri yangu kwa sababu kweli tumetoka kwenye asilimia 23 tumekwenda sasa kwenye asilimia 40 lazima tuipongeze sana Serikali. Mbali na hilo katika ukurasa wa 98 wa kitabu chako, ninakushauri ile aya ya 102 unapoanza kwanza mpaka namba kumi nishauri hii ndiyo iwe kama ndiyo amri kumi kwa sababu yako maagizo kumi, hii ndiyo iwe amri kumi, sitaki kusema kwa sababu ya muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri maelezo aliyoyaeleza hapa kuanzia kipengele cha Kwanza, Pili, Tatu, Nne, Tano, Sita, Saba, Nane, Tisa na Kumi, iwe ndiyo mwongozo kwa Maafisa Masuuli wote Tanzania. Atakayekiuka haya wala tusimwonee aibu, kwa sababu ili pesa hizi ziende kufanya kazi yake vizuri, hii asilimia 40 ya bajeti yote kama hizi amri kumi alizoziorodhesha zikisimamiwa vizuri, nina uhakika tutasonga mbele, tukifanya hivyo na naomba nirudie kusema tena hapa, Maafisa Masuuli wote waandikiwe secular kuhusu hizi amri kumi wazitekeleze. Mimi naziita amri kumi kwa sababu kwa jinsi alivyozipanga na kama kila mtu akifuata moja baada ya nyingine, nina uhakika tutafika mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naunga mkono, kwanza niipongeze sana TRA kwa kufanya kazi vizuri sana. Tunawaamini, mmepewa jukumu zito, lakini niwaombe hasa kwa upande wa kodi za majengo, tukisimamia vizuri kodi za majengo, Dar es Salaam tukafanya tathmini ya kutosha, Mwanza tukafanya tathmini ya kutosha, Arusha na maeneo mengine tukafanya tathmini ya kutosha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuna pesa nyingi sana pale, tutaboresha miji yetu, tutaboresha miundombinu yetu, kwa sababu pesa zilizoko pale zilikuwa zinapotea bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine kwa Waziri wa Fedha na Wabunge wenzangu, naomba kuhusu misamaha ya kodi, sikubaliani nayo, lakini hebu mkae vizuri na Wataalam wako mwangalie hasa upande wa madhehebu ya dini, tusiwahukumu kiujumla tukae, tufanye tathmini ya kina, najua mmeshafanya, kwa sababu madhehebu ya dini mengine yanatoa huduma upande wa hospitali, upande wa shule. Kwa hiyo, naomba sana kuhusu hili, mkae mfanye tathmini ya kutosha ili tusilete mgogoro na madhehebu ya dini. Najua Serikali yangu ni sikivu hili italifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine niipongeze Serikali na niweke tu msisitizo, nimesema leo kazi yangu ni kushauri bajeti ijayo ndiyo tutakwenda kwa detail. Kuhusu ujenzi wa reli naipongeza sana Serikali, ununuaji wa ndege hili wala msichelewe, msisikilize yale maneno ya kule, kwa sababu najua Serikali imekaa. Nawashangaa watu wengine tulikuwa tukisimama humu tunasema Tanzania hatuna ndege sasa Serikali imekuja na mpango mzuri wa kununua ndege tatu, watu wengine wanaanza kuhoji! Jamani hivi tunataka Serikali ifanye nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nashauri asiwe na kigugumizi kununua hizi ndege tatu, atwange mzigo, alete ndege tatu hizo ili kusudi Watanzania watumie ndege zao, siyo ndege zile zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni ununuzi wa meli, chonde chonde! Meli hizi kwa jinsi ambavyo mmejipanga kama Serikali zinunuliwe bila kusuasua, hivyo maeneo ambayo tumeshaahidi kuwa tutanunua meli au kukarabati tufanye bila kuchelewa. Ili tufanye hivyo niwaombe sana wenzetu wa TRA kwa sababu tunawategemea. TRA ni kama mshipa kwenye mwili wa binadamu, ukikatika mshipa mmoja au ukisimama mshipa mmoja, ina maana eneo moja lita-paralise, kwa hiyo ili tutekeleze haya ambayo Dkt. Mpango Waziri wa Fedha ameyaainisha humu ndani ni lazima makusanyo yakusanywe na yasimamiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukusanya matumizi yetu yawe na nidhamu, tukifanya hivyo tutakwenda vizuri. Kwa kweli naunga mkono sana bajeti hii kwa sababu ina mambo mengi sana mazuri na imegusa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo Waziri wa Kilimo ni muhimu kuliangalia, hebu tazama kwenye tozo za mazao, tumeyasema mwanzo tozo ni nyingi, ni kero, hebu ziondoeni kwa sababu zinawapa matatizo watu wetu, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho Waziri wa Ardhi, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Maliasili wakae pamoja waangalie namna ya kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, yale maeneo ambayo sasa hayana sifa tena ya kuwa mapori ya hifadhi, wakae na waangalie namna nzuri wayagawe ili watu wetu, wakulima na wafugaji waweze kuyatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini naomba niwashauri katika maeneo mbalimbali ili kuboresha na kustawisha Wizara ambayo ni nyeti katika kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Mheshimiwa Waziri na viongozi wenzako nashauri kuchukua mapendekezo mazuri yaliyotolewa na Kamati pamoja na ushauri mzuri unaotolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa mustakabali wa nchi.
Pia katika kutatua migogoro ndani ya hifadhi Waziri kupitia wataalam wake watatue migogoro kwa kuzingatia hekima, busara na taratibu za kisheria zilizopo, wasitumie mabavu, tunajua sheria zipo lakini tatizo ni ushirikishwaji hafifu au elimu duni ya uhifadhi ikichangiwa na rushwa.
Mheshimiwa Waziri, Shirika la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi za Taifa 16 hadi leo halina bodi kwa mujibu wa Sheria Sura 282 ya mwaka 2002 na kama ilivyorejewa kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa ya mwaka1959 Sehemu ya II inayoanzisha Hifadhi ya Taifa na Bodi ya Wadhamini. Nashauri kufuatana na uzito na umuhimu wa taasisi hii Waziri umwombe Mheshimiwa Rais ateue Mwenyekiti wa Bodi na wewe uteue Wajumbe wa Bodi haingii akilini taasisi kubwa kama hii kukaa miaka zaidi ya minne bila Bodi ya Wadhamini.
Naomba niulize, TANAPA kutokuwa na bodi ni nani anaamua maamuzi ambayo uamuzi wake unatakiwa uamuliwe na bodi. Mheshimiwa Waziri Chuo cha Mweka nikiwa Mjumbe wa Bodi kwa wakati huo Rais wa Awamu ya Nne alitamka kwa kumwambia Waziri wa wakati huo Mheshimiwa Mwangunga kuwa chuo hicho kiwe chuo cha mfano (center of excellence) lakini hayo hatuyaoni, kumbuka chuo hicho ndicho kiwanda cha kuzalisha wataalamu katika tasnia ya wanyamapori hasa katika hifadhi zetu zote nchini. Nashauri chuo hicho pamoja na kile cha Pasiansi visimamiwe vizuri ili kutoa wataalam na askari wanaoweza kwenda kusimamia vizuri maeneo ya uhifadhi.
Nimalize kwa kuwaomba viongozi wote walio chini ya Wizara hii kumsaidia Waziri ili yaliyoainishwa ndani ya kitabu hiki yaweze kutekelezwa. Lakini kwa pekee nimpongeze CEO wa TANAPA kwa kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa pamoja na kutokuwa na Bodi ya Wadhamini.
Mheshimiwa Waziri moja ya changamoto kubwa ni kutopata takwimu sahihi za watalii hasa katika eneo la Selous, Serikali iangaie njia nzuri zaidi hasa kwa hawa wenye hoteli ziwe na takwimu sahihi ili kudhibiti mapato ya Serikali lakini kuwe na motisha kwa wafanyakazi na Selous iimarishe usimamizi kwa kila hoteli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika pori la akiba la Selous lina jumla ya kambi za kuweka wageni (camp sites) nane na zisizopewa wawekezaji hadi leo hawajaendeleza, nashauri wanyang‟anywe ili wapewe wengine na kuendelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya makazi, kilimo, ufugaji na matumizi endelevu nashauri kuainisha na kuhakiki mipaka ya mapori ya akiba kwa mujibu wa GN kupitia Wizara ya Ardhi, kutoa elimu ya uhifadhi na kufanya tathmini ya mapori tengefu. Pia nashauri kuzishirikisha Wizara na taasisi zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Utalii (TTB) na TANAPA kwa pamoja na NCCA hawajaonyesha jitihada za kutangaza utalii nje na ndani ya nchi. Je, ni kwa nini taasisi hizo ikiwemo Bodi ya Utalii hawatilii mkazo suala zima la kutangaza na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha watalii hasa wa Marekani na Wafaransa ili ile idadi ya watalii iongezeke na nchi ifaidike na utalii kwa kuongeza mapato zaidi.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Hussein Nassor Amar

Nyang'hwale (CCM)

Questions (1)

Supplementary Questions (6)

Contributions (4)

Profile

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Siha (CHADEMA)

Questions (2)

Supplementary Questions (1)

Contributions (4)

Profile

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Serengeti (CHADEMA)

Questions (4)

Supplementary Questions (5)

Contributions (4)

Profile

Hon. Agnes Mathew Marwa

Special Seats (CCM)

Questions (0)

Supplementary Questions (1)

Contributions (4)

Profile

Hon. Miza Bakari Haji

Special Seats (CUF)

Questions (1)

Supplementary Questions (1)

Contributions (0)

Profile

View All MP's