Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Jesca David Kishoa

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote, nikishukuru Chama changu kwa yote, lakini pia nimshukuru mume wangu David Kafulila ambaye pamoja na mimi kuwa mama ametambua ninayo nafasi ya kulitumikia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye mjadala. Tunajadili Mpango, lakini niseme kwamba mipango siyo tatizo katika Taifa, Taifa hili hatuna umaskini wa mipango, ila tuna tatizo la utekelezaji wa mipango. Tumeshakuwa na mipango mingi, ukiangalia kuanzia mwaka 1981 mpaka 1986 tumekuwa na Mpango mwingine kuanzia mwaka 1987 mpaka mwaka 2002, huu ulikuwa ni Mpango wa kumi na miaka mitano ambao ulikuwa umelenga kwamba mpaka kufikia mwaka 2002 Tanzania iwe nchi ambayo itakuwa ina mfumo wa ujamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukaja kuwa na Mpango mwingine wa miaka 25 kuanzia mwaka 2000 mpaka mwaka 2025 ambao lengo lake lilikuwa ikifika mwaka 2025, Tanzania iwe ni nchi yenye uchumi wa kati na mipango mingine mingi iliyofuata. Hata hivyo, hii mipango haitekelezeki na haitekelezeki kwa sababu kubwa mbili. Sababu ya kwanza, ni mfumo mbovu tulionao katika Taifa hili na sababu ya pili ni ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi zote ambazo tumeshafatana nazo katika masuala ya maendeleo kuanzia mwaka 1963; Malaysia, Singapore, Korea Kusini, nchi zote hizi mpaka hivi sasa zimeshakuwa wahisani wetu na zimekuwa wahisani wetu kwa sababu mipango yetu inashindwa kutekelezeka. Nimetangulia kwa kusema kwamba sababu kubwa ni mfumo mbovu, lakini pia na ufisadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo mbovu kwa maana gani? Kwa sababu ya muda nitazungumzia kwenye suala la elimu kwenye suala la mfumo mbovu. Leo hii tunazungumzia elimu bure, ni suala ambalo naamini kabisa kwamba Watanzania na wazazi wote wa nchi hii wamelifurahia, lakini tunazungumzia elimu bure wakati huo huo kuna changamoto nyingi. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri anasema hivi bado zimebaki changamoto ndogo ndogo pamoja na elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi changamoto ndogo ndogo zina uhusiano mkubwa na performance ya wanafunzi. Niseme hivi ni bora mngehakikisha mnaondoa hizi changamoto, halafu mkasema elimu bure. Mfano, mwaka 2015, Taasisi ya Haki Elimu ilitoa ripoti ikasema hivi; katika Taifa letu kuna upungufu wa madawati 1,170,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hesabu ya haraka haraka kama kwenye dawati moja wanakaa wanafunzi watatu watatu, inamaanisha Taifa letu kuna wanafunzi milioni tatu na ushee wanakalia mawe, kwenye nchi ambayo ni ya tano kwa idadi ya misitu Afrika nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwanafunzi anakaa kwenye mawe, mwalimu anakuja darasani kufundisha somo la historia, anaandika zama za kale za mawe, anajiuliza hizi ni za kale au ni za sasa? Ningeomba kwanza waelekeze kwenda kutatuta changamoto zilizopo kwenye mashule, halafu wakaja wakatuambia elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye suala la utawala bora, muundo wa suala la utawala bora kwa ujumla. Mfano mzuri ni hapa Zanzibar wala siyo mbali, unapuzungumzia Zanzibar leo hii ni aibu, hivi karibuni nilimsika Donald Champ, mgombea wa Republican Marekani, anasema Afrika wanahitaji miaka 100 kuendelea kutawaliwa kwa sababu hawajajitambua. Mpaka anafikia hatua ya kusema hivyo ni kwa sababu ya mambo kama yanayoendelea Zanzibar, tunadhalilisha Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, mnaweza mkasema kwamba labda kwa sababu mpo madarakani, lakini ni hivi Marekani wamesema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa fair and free, Ulaya wakasema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa fair and free, mtasema aaa! Hao ni wa mbali, SADC hapa Kusini kwetu wamesema uchaguzi wamesema ulikuwa fair and free, AU wamesema ulikuwa fair and free. Tatizo ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 nikiwa na miaka mitatu, mlianzisha kitu kinaitwa multipartism mkimaanisha mfumo wa vyama vingi ambao mlikubaliana kwamba kila baada ya miaka mitano kutakuwa kuna utaratibu vyama vinagombea mbalimbali kinachochukua nafasi kinashika dola. Sasa niseme tu kwamba, kinachoendelea Zanzibar ni suala la kukosa ustaarabu tu na siyo vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Rais Mafuguli aweke mkono wake Zanzibar. Nasema hivi kwa sababu gani? Hata awe mzuri kiasi gani Zanzibar akiharibu hawatamwelewa, kuna msemo unasema hivi: “You cannot stand for something you don’t know and likewise it doesn’t matter how much you know about something, if you cannot stand up on it. Kinachoendelea Zanzibar kama Magufuli hataingia, maana yake ni kwamba Wazanzibari hawatamwelewa, maana ingekuwa Kilimanjaro angeingilia halafu ninyi mnahubiri kwamba hii ni nchi moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Magufuli, suala la Zanzibar alitazame kwa jicho la kipekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ufisadi unaturudisha nyuma sana, namwomba Mheshimiwa Magufuli, kwa sababu ninaposema ufisadi namaanisha ni miongoni mwa sababu inayopelekea hii mipango tunayoijadili hapa isitekelezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufisadi unaoendelea sasa Mheshimiwa Magufuli anatakiwa auone na auangalie kwa ukamilifu kwa sababu huu ni muda sasa amemaliza kutumbua vipele, atumbue majibu makubwa mengine anakaa nayo mezani. Imefika wakati ni lazima tuseme, kwa sababu kinachoendelea katika Taifa hili tukikaa kimya, tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka jana, kuna ripoti ililetwa hapa, tulieni siyo ESCROW, kuna mjadala ulikuja hapa ukiachana na ESCROW, lilikuwa ni suala la mabehewa. Mwaka jana Taifa letu limeingia hasara ya bilioni 238, hizi zilikuwa ni fedha za wananchi ambao zilikwenda kununua mabehewa, matokeo yake, mabehewa yalikuwa fake. Haya siyo maneno yangu, hii ni ripoti PPRA ambayo ilileta ripoti kwenye Kamati ambayo nipo mimi. Mabehewa yanaonekana kwanza ni fake, lakini cha ajabu hata kampuni iliyopewa tenda ni kampuni ambayo haikufanyiwa due diligence kwa maana ya ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa limeingia hasara ya bilioni 238 kwa sababu ya mtu tu kuwa mzembe kuwajibika, halafu leo jipu linahamishwa mkono wa kushoto, linapelekwa mkono wa kulia. Mheshimiwa Magufuli alitumbue na jipu hili liko humu ndani, tunaye Mheshimiwa Mwakyembe, leta ripoti hapa, ripoti kuhusiana na masuala ya mabehewa, mlikataa kuileta hapa kwa nini mnaficha, kama ni safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwakyembe umeaminiwa na Serikali na Magufuli lete ripoti hapa, tusijisahaulishe haya mambo tunayakumbuka tuliona hata tukiwa nje. Tunaomba tutendeeni haki wananchi wa Tanzania kwa sababu Bunge liliazimia ripoti iletwe Bungeni, naomba ripoti iletwe hapa Bungeni na tuweze kuifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hiyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nashukuru kwa kupata fursa hii kuchangia kwenye hii Wizara ambayo ina uhusiano mkubwa sana na mkoa ambao nauwakilisha kwa maana ya Mkoa wa Singida. Mkoa wa Singida ni miongoni mikoa ambayo inafanya vibaya sana katika suala la taaluma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuendelea, naomba mama yangu, Mheshimiwa Waziri Ndalichako, wakati unakuja kuhitimisha nakuomba uje na majibu ya kwanini Walimu takriban 366 wanaotokea Mkoa wa Singida Wilaya ya Iramba hawajapandishwa madaraja toka mwaka 2013 na wakati katika mkoa huu Wilaya nyingine zote Walimu wao wamepandishwa madaraja, lakini kasoro Wilaya ya Iramba peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote humu ndani tunatambua kwamba dunia ya sasa ni dunia ya ushindani, silaha pekee kwenye dunia ya ushindani ni elimu; lakini cha kusikitisha ni kwamba elimu inayotolewa katika Taifa letu ni elimu duni kabisa. Ni elimu ambayo haijakidhi vigezo. Nasema hata kwa sababu hapa nina taarifa ya USAID ya mwaka huu ambayo inaonyesha kwamba asilimia 70 ya wanafunzi hawajui kusoma Kiswahili, Shule ya Msingi na wakati huo huo asilimia 90 ya wanafunzi hawajui kusoma Kiingereza. Kwa tafsiri nyingine ya watu, hata kuandika barua ya kuomba kazi hawawezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Vyuo Vikuu vilivyopo katika Taifa letu, kuna baadhi ya Vyuo Vikuu kwa sasa vimeamua kupanua magori kuhakikisha kwamba wanaanza kusajili wanafunzi kutoka Form Four kwa sababu kuna wanafunzi wa Form Six hawajakidhi vigezo kuingia Vyuo Vikuu. Takwimu ya TCU ya mwaka 2015 inaonyesha kwamba kuna nafasi 25,000 zimeshindwa kuwa fulfilled kwa sababu wanafunzi hawajakidhi vigezo vya kwenda University. Hii inasikitisha sana na ni aibu! (Makofi)
Sasa katika kutafakari, nikaangalia, msingi wa haya ni nini? Sababu kubwa, kwanza ni kwa sababu hakuna mkazo kwenye suala la elimu. Hakuna mkazo ambao Serikali imepelekea kwenye suala zima la elimu. Niseme tu, nafikiri hii ni kwa sababu anguko la elimu katika Taifa hili haliwahusu Mawaziri, wala haliwahusu vigogo katika Taifa hili. Ila kwa sababu hiyo hapa we are not talking the same language! Hatuongei lugha moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo mmoja wa Kiswahili unasema hivi: “kilio na mwenyewe.” Katika hali ya kawaida katika cabinet hii, msiba wa elimu, hamna member hapa kwenye cabinet ambayo inamhusu kwa namna yoyote ile. Kwa sababu asilimia kubwa watoto wao wanasoma nje na wengine wanasoma shule za private. (Makofi)
Kwa hiyo, ifike mahali tulitazame hili kwa sura nyingine. Mfano mzuri ni UK. Uingereza, Waziri kumpeleka mtoto wake kusoma shule ya private ni kashfa kubwa sana. Naomba kupitia Bunge hili Tukufu nimwombe Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli atangaze rasmi Mawaziri wote wa Taifa hili, watoto wao wasome shule za government. Wasome shule za Serikali! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye suala la madawati, ni aibu! Eti wanafunzi milioni tatu na nusu, wingi wote huo wa wanafunzi, wanakaa chini. Upungufu wa madawati ni karibia 1,174,000. Ukiangalia gharama zinazoweza madawati haya, siyo chini ya shilingi ya bilioni 90 mpaka 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ni vema wakaona kwamba kuna umuhimu hata suala hilo wakalipeleka kwenye jeshi, jeshi likatutengenezea madawati wakawa wanalipa taratibu; au wakatumia mifuko ya hifadhi kuhakikisha kwamba mifuko ya hifadhi inakopesha wanajeshi halafu Serikali inakuwa inailipa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la ukaguzi. Unapozungumzia ukaguzi, ukaguzi una uhusiano mkubwa sana na performance ya mwanafunzi, kwasababu ukaguzi unapelekea kumtambua Mwalimu bora na ubora wa elimu wanayoitoa. Kwa Taifa letu ni aibu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Best Education Statistics za mwaka 2015, zinaonesha karibia asilimia 81 ya shule zote za Msingi hazijafanyiwa ukaguzi, lakini wakati huo huo asilimia 76 ya Shule za Sekondari hazijafanyiwa ukaguzi. Halafu mwaka 2015 mkatenga fedha shilingi bilioni 22.4 kwa ajili ya kupeleka kwenye ukaguzi, mkachukua shilingi bilioni 20 mkawalipa wakaguzi kama mshahara, halafu shilingi bilioni 2.4 ikatumika kwa ajili ya ukaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sawasawa na Mbunge hapa amlipe dereva wake mshahara kila mwezi, halafu asiwe anamwendesha, awe anaendesha mwenyewe. Naona huu ni ubadhirifu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mmoja anaitwa Aristotle aliwahi kusema hivi: “mizizi ya elimu ni michungu, lakini matunda ya elimu ni matamu.” Mimi nabadilisha kwa Taifa letu, “mizizi ya elimu ni michungu na hata matunda ya elimu ni machungu vile vile.” Tafsiri halisi ya elimu ni ili mtu atoe ujinga awe na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazomzunguka. Kwa Taifa letu, watoto wetu wanakwenda shuleni ili mradi wavae uniform wafanane na wengine. Ni masuala ya aibu, ambayo ni lazima tuyafanyie kazi haraka iwezekananyo, maana tunachekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naomba Waziri, mama yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako kama itakupendeza, muda wowote nikupatie majina haya ya Walimu wote ambao wana madai yao kwa ajili ya kuweza kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja, ahsante.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, napenda kutoa pongezi kwa Kamati ambayo imewasilisha muda siyo mrefu, kwa sababu kuna mambo ya msingi wameweza kuyaweka bayana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukianza na suala la Serikali kuchelewa kupeleka fedha za miradi katika maeneo husika, hasa katika eneo la umeme; mimi ni miongoni mwa wahanga katika tatizo hili. Umeme wa upepo Singida, kwa muda mrefu, toka miaka ya 1990 mpaka
Bunge lililopita, Serikali imekuwa ikipiga danadana kuhusiana na suala hili. Majibu ni yale yale! Kila siku Mheshimiwa Waziri husika anapokuja kuzungumzia suala hili, analeta majibu yale yale ambayo anayazungumza toka Bunge lililopita na bahati nzuri ni Waziri yule yule kutoka Bunge
lililopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali, kama wameshindwa kupata fedha kutoka nje ambazo wanazitegemea, basi ni heri atumie fedha za ndani kutekeleza mradi huu, kwa sababu ni muda mrefu sana. Tumepewa majibu haya haya kila siku, wananchi wa Mkoa
wa Singida wamechoka na Wabunge wa Singida naamini hapa wataniunga mkono katika hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba katika suala hili la umeme wa upepo wa Singida, Serikali, kama kuna uwezekano wa kuchukua fedha kutoka ndani, ichukue na itekeleze mradi ule kwa sababu kiukweli tumechoka. Upepo wenyewe labda tungekuwa tumepewa na mtu;
tumepewa na Mwenyezi Mungu, ilikuwa ni suala la Serikali kutekeleza mradi huu na kuweza kutimiza ahadi ambazo wanazitoa kwa wananchi wa Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, Singida ninyi Chama cha Mapinduzi mnajua ni champion wa kutoa kura kwa Chama cha Mapinduzi mfululizo miaka yote, lakini ni miongoni mwa watu ambao kwenye miradi mmewasahau. Naomba suala la umeme wa upepo wa Singida, Serikali ilichukulie kwa uzito wa kipekee, kwa sababu ni ahadi za muda mrefu sana ambazo zimekuwa hazitekelezeki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuachana na hayo, naomba pia nizungumzie suala ambalo limekuwa likizungumzwa miaka nenda miaka rudi karibu Mabunge yote; ni suala la mikataba kuwekwa wazi. Namaanisha mikataba ya gesi pamoja na mikataba ya madini specific. Suala hili la mikataba kuwekwa wazi limeshazungumzwa kwa muda mrefu sana. Wamezungumza Awamu ya Nne, wamezungumza Awamu ya Tatu na Awamu ya Tano tena tunalizungumza suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Serikali yoyote ambayo inajipambanua kwamba yenyewe ni ya uwajibikaji, uwazi na ya kutumbua majipu, suala la mikataba kuwekwa wazi lilikuwa siyo suala la kuanza kuihoji, lilikuwa ni suala ambalo lilipaswa kutekelezeka tu. Miongoni mwa vitu ambavyo tulipaswa tuvizingatie ni pamoja na sisi kuwa Wajumbe kwenye organizations ambazo zinazungumzia masuala ya mikataba kuwa wazi. Mfano, sisi ni member kwenye OGP (Open Governance Partnership), lakini toka mwaka 2011 tumekuwa member katika organization hii,
bado vitu vyetu tunafanya kwa mazingira ya usiku usiku; Bunge usiku, mikataba usiku.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado sisi toka mwaka 2009 ni member kwenye Shirika la EITI (Extractive Industry Transparency Initiative). Hii ni aibu. Ukiachana na sisi kuwa member katika hizi taasisi, lakini bado Awamu ya Nne Bunge hili lilipitisha sheria ya kutaka mikataba kuwa wazi na
Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akasaini, lakini danadana zikaanza kupigwa baada ya kufika kwa Waziri husika kwa maana ya kutunga kanuni ambazo zinaweza zikasababisha sheria hiyo kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu ni kutofahamu, linapokuja suala la sheria ambazo zina maslahi kwa umma, kwa mfano, mwaka 2016 tulipitisha sheria ambazo zinafunga vyombo vya habari, zinafunga demokrasia, zimepitishwa Rais akasaini immediately na Waziri husika
akatunga kanuni na zikaanza kutekelezwa, lakini zinapokuja sheria kama hizi ambazo zina maslahi kwa umma, kwamba mikataba iwe wazi, sheria hizi zinakaa muda mrefu sana. Mfano, toka Awamu ya Nne mpaka sasa, bado Mheshimiwa Waziri hajatunga kanuni na mpaka dakika
hii hajasema sababu ni nini. Labda ni kutofahamu, au ni kufahamu lakini ni kiburi tu kwamba mikataba ikiwa wazi kuna faida gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba inapokuwa wazi, kwanza wananchi wanakuwa na confidence na Serikali yao. Pia mikataba inapokuwa wazi, wale wawekezaji katika eneo husika wanakuwa na mahusiano mazuri na watu wa eneo lilo ambalo linawazunguka kwa kuamini
kwamba wanayoyafanya ni mambo ambayo wanayajua kwa maana yako wazi. Lingine, mikataba kuwa wazi inasaidia sana zile organisations na NGOs ambazo zinafanya tafiti mbalimbali kuwa na correct details, figures ambazo ni sahihi kuhusiana na mkataba husika au investment husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nchi mbalimbali ambazo unaweza ukafikiri labda ni Tanzania tu tutakuwa wa ajabu sana, lakini zipo nchi nyingi sana ambazo zimeweka mikataba wazi; na kwa sababu ya muda nashindwa kuzitaja lakini nitazitaja chache, ninazo hapa zote.
Nchi ya Liberia, Ghana, Congo, USA, Colombia, Canada; nchi karibu zote zimeweka mikataba wazi. Kwa nini Tanzania tunaendelea kuweka mikataba hii katika hali ya usiku? Naomba kama Bunge, ikiwezekana tutunge sheria ambayo itambana Waziri, kwamba ndani ya miezi sita
atunge kanuni ambazo sheria itaanza kutekelezeka, lakini siyo afanye anavyotaka yeye.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine ambalo limenishtua kidogo na napenda kushare na Wabunge wenzangu humu ndani. Naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha alielezee kwa ufasaha kabisa, kwa sababu siyo vyema kuliona linaandikwa kwenye majadala ya Kimataifa halafu kama Wabunge humu ndani hatuna information sahihi. Kuna kampuni inaitwa BG Group ya Uingereza ambayo inamiliki vitalu vya gesi Tanzania. Ilifanya transfer share kwenda Kampuni ya Shell ambayo ni kampuni kutoka Uholanzi. Kisheria na kiutaratibu wakati kampuni inafanya transfer shares, ni lazima kama Serikali tupate kitu kinaitwa Capital Gain Tax, lakini ni aibu kwa Serikali hii, transfer share imefanyika lakini Serikali haijapewa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha hapa aseme kama kodi hii imelipwa au kama suala hili lina ukweli kiasi gani? Siyo vyema kuona linazungumzwa na kama Wabunge hatulifahamu lakini pia kama Serikali haiji kutoa maelezo
yoyote kwa maana ya Wizara. FCC hawana majibu, nimewauliza na wakasema watatoa kwa maandishi, mpaka leo hawajanipa; TRA hawana majibu, lakini pia Wizara tunaomba majibu leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine la uwekezaji katika gesi asilia.
Unapozungumzia…
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabla ya kuendelea nianze na quotation moja aliitoa mtaalam mmoja wa masuala ya uongozi anaitwa John Maxwell, anasema hivi:- “If you want to recognize the intelligence of the leader look people around him.”
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mkuu wetu wa Nchi amezungukwa na watu aina ya Goodluck amezungukwa na watu aina ya Bashite what do we expect. (Kicheko/ Mheshimiwa Naibu Spika, sikutegemea kama tunaweza kuwa na aina ya viongozi ambao wanaweza kuja Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuchangia katika suala zima la utawala bora baadaye nitamalizia na utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kwa sasa hivi imekumbwa na tatizo kubwa sana katika suala la uchumi na tatizo hili linatokana na ukosefu wa utawala bora katika Taifa letu. Leo hii nchi yetu tumekosa fedha za MCC takriban Dola 463,000,000 kutoka Marekani kwa sababu ya ukosefu wa utawala bora. Leo hii tumekosa mikopo kutoka nje.
Mheshimiwa shemeji yangu naona hayupo hapa leo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, amekwenda Ulaya, amezunguka nchi zote, amekosa mikopo kwa sababu kigezo namba moja cha mkopo ni lazima kuwe na good governance katika Taifa, lakini tunakosa fursa hizi kwa
kutokuwepo na utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka leo Bajeti ya Mwaka 2016/2017, imetekelezeka kwa asilimia 34 tu kwa sababu kubwa ya ukosefu wa utawala bora. Wakati huo huo tunakosa misaada kutokana na ukosefu wa utawala bora katika Taifa hili. Wawekezaji wanakimbia, wafanyabiashara wanakimbia; kwa sababu hakuna mwekezaji ambaye ana akili timamu anaweza kuwekeza kwenye nchi ambayo muda wowote mkataba unaweza ukavunjwa kwenye majukwaa. Hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuwekeza kwenye nchi ambayo haifuati misingi ya utawala wa Sheria , hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika yapo mambo humu ndani tunaweza kutofautiana kwa sababu ya itikadi zetu, lakini yapo mambo ambayo lazima tuungane kwa ajili ya maslahi ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, utawala wa sasa unaendeshwa kwa double standard, Serikali haina consistency. Kwa mfano unaweza kukuta kwamba watu ambao wako ngazi ya chini wanavunja Sheria na wanachukuliwa hatua kali, lakini wapo watu ambao wapo kwenye mamlaka kubwa wanavunja sheria na wakati mwingine wanalindwa mpaka na mitutu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi ni mdau mkubwa sana wa vita juu ya ufisadi, lakini jitihada za Mheshimiwa Rais wetu zinakosa uhalali kwa sababu ya kuwa na double standard. Kuna maeneo anaonekana anachukua hatua na kuna maeneo anaonekana hachukui hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkutano uliopita kuna suala nililizungumza humu ndani, nilizungumzia suala la uvunjaji wa Sheria ya Finance Act ambayo iliundwa mwaka 2012 section namba 29 inasema kwamba hakuna transfer share yoyote ambayo itafanyika bila kulipwa Capital Gain Tax.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kampuni inaitwa Shell ilifanya transfer share kutoka kampuni ya BG. Shell ilinunua vitalu vya gesi kutoka kampuni ya BG, lakini hakuna Capital Gain Tax ambayo imelipwa. Cha kusikitisha sana wakati tupo kwenye Kamati, Mkutano uliopita niliuliza viongozi wa FCC wakasema kwamba swali lako tutajibu kwa maandishi mpaka leo hawajajibu. Nika-take trouble kupitia Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, section namba 29 nikasema kwamba, toeni sababu kwa nini mpaka leo Capital gain tax haijalipwa lakini mpaka leo, toka tarehe nne TRA nao hawajajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Muhongo alijaribu kupiga bla bla, lakini nashukuru alikiri kwamba kuna wizi unafanyika kwenye makampuni haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii kampuni ya Shell, hii ni kampuni ambayo wiki mbili zilizopita, nina ushahidi hapa, imekuwa reported kwenye vyombo vyote duniani kwamba imetoa rushwa ya trilioni mbili kwa ajili ya kukidhi maslahi yake kwenye Serikali ya Nigeria. Baada ya kugundulika ndipo wakaamua kuitumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi kwenye Serikali yetu kampuni hii lazima tuone kwamba kuna harufu ya rushwa hapa. Haiwezekani fedha za wananchi takribani dola milioni 500, takribani kama trilioni moja na ushee, ni hela nyingi sana, zinaweza kutengeneza hiyo standard gauge ambayo Mheshimiwa Rais anataka kuitengeneza kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro; lakini imepotea katika mazingira hayo na hakuna ambaye amechukuliwa hatua na vitu vinafunikwa funikwa na hakuna ambaye anahoji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Mheshimiwa Rais wetu anataka tutengeneza imani na yeye, aanze kuchukua hatua ambazo zinalenga kote kote, achukue hatua kwa watu wake, achukue hatua kwa watu ambao anafikiri kwamba hawamuhusu, wote kwa pande zote mbili
achukue hatua kwa sababu mnatupotezea imani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka naomba pia nichangie upande wa utumishi. Kuna uhusiano mkubwa sana kwenye suala la uwajibikaji na maslahi, hivi vitu viwili vinakwenda sambamba. Hapa nilipo nina chati kutoka Chuo cha Walimu, Kanda ya kati lakini nitaongelea
specifically Singida. Walimu wa Mkoa wa Singida toka mwaka 2013 mpaka leo hawajapa stahiki zao, takribani bilioni 2.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kutegemea matokeo makubwa Singida na ndiyo maana elimu imekuwa ikianguka kila siku, tumegundua miongoni mwa sababu ni pamoja na hii. Naomba niishauri Serikali jambo moja; kama ambavyo wanafanya kwa wakandarasi, mkandarasi anapokuja kulipwa fidia zake, anapokuja kulipwa malipo yake analipwa kwa riba. Vivyo hivyo tupeleke utaratibu huu kwa upande wa watumishi wa Serikali, specifically Walimu pale mnapokuja kuwalipa muwalipe kwa riba kwa sababu fedha zile kwa wakati ule value yake ni tofauti na wakati huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atutazame upya kwa sababu inasikitisha sana elimu yetu imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu sana na Walimu wamekuwa wakilalamika sana, wanaishi maisha magumu, wanakosa stahiki zao. Moja kwa moja hiyo automatically inapelekea utendaji mbovu kwenye elimu wanayoitoa kwa wanafunzi wetu. Tutaendelea kuzalisha watoto ambao hawana vigezo, hawana sifa, kwa sababu tunashindwa kuwasaidia Walimu kupata stahiki zao.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's