Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Joyce John Mukya

All Contributions

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya michezo vimegeuzwa kuwa viwanja vya usheherekeaji wa sherehe mbalimbali na badala ya kuviendeleza kama viwanja vya michezo ambavyo vingeweza kuwasaidia vijana, wanawake na watoto katika kujenga, kufurahia kuimarisha afya zetu na kuchangamsha miili yetu na hata kutupa afya njema kila siku. Hatimaye viwanja hivyo vimegeuzwa kuwa sehemu ya kufanyia sherehe za Kitaifa na sherehe za Chama cha Mapinduzi (CCM). Mbaya zaidi viwanja hivi vimegeuzwa viwanja vya CCM, kwa sababu vyama vya upinzani hawaruhusiwi kufanya shughuli zao katika viwanja hivi isipokuwa Chama cha Mapinduzi tu. Nina ushahidi na hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie viwanja hivi vitumike kwa shughuli za michezo na kama ni shughuli nyingine basi kuwe na usawa na haki kwa sababu vyama au itikadi ni mapenzi ya mtu binafsi tu, lakini mwisho wa siku Utanzania wetu unabaki pale pale.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba hii kama nilivyoainisha hapo juu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea tatizo la wafanyakazi kutopata ajira za kudumu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nilishafanya kazi na Jumuiya kabla sijawa Mbunge kuanzia mwaka 2006 mpaka 2009 kama IT Assistant. Wakati najiunga pale nilikuta wafanyakazi wa temporary ambao wanafanya kazi kama vibarua, naweza kusema hadi leo hii ni muda wa miaka 10 na zaidi sasa, baadhi yao hawajaajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua toka kwa Mheshimiwa Waziri ni lini ajira za hawa wafanyakazi zitatangazwa ili waweze kuajiriwa? Kwa sababu wangekuwa hawatakiwi, wasingekuwepo kazini hadi leo hii. Naweza kukupa majina yao kama utahitaji pia na wengi ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine, ni Serikali yetu kutopeleka fedha za kuendesha Jumuiya kwa wakati. Mfano, tokea makubaliano ya bajeti iliyopita kati ya Partner States hadi leo hii nchi yetu ya Tanzania haijapeleka au kukamilisha mchango wake wa kuendesha Jumuiya hiyo. Hii ni aibu sana kwa nchi yetu na ukizingatia Jumuiya hii Makao Makuu yake yapo Tanzania. Ilitakiwa tuoneshe mfano kwa nchi wanachama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni wafanyakazi wa ngazi ya profession kutokupatiwa Diplomatic Passports. Kama yalivyokuwa makubaliano ya nchi wanachama, yaani Headquarters Agreement, wafanyakazi wa level hii wanaotoka nchi nyingine wana diplomatic passports isipokuwa nchi yetu. Hili nilishalisemea tena Bungeni mara mbili na Mheshimiwa Waziri akaahidi watapewa kwani ni haki yao, lakini hadi leo imekuwa ni hadithi tu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kujua ni lini watapewa haki yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wafanyakazi wa Jumuiya wamekuwa na shida ya kupata Work Permit. Ni aibu kubwa sana kwa hili jambo. Mtumishi ana mkataba wa miaka mitano, lakini bado Serikali haimpi Work Permit ya miaka mitano na kusababisha kero kubwa kwa nchi wanachama wanaokuja kufanya kazi nchini ambako ndiyo sehemu Headquarter ilipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Naomba Mheshimiwa Waziri anijibu maswali yafuatayo:-
(1) Ni lini Wizara hii itaanza kukaa na Wabunge wa EAC ili kujadili mambo mbalimbali, kama mtakavyojipangia ratiba, kama Wizara ya EAC ya Awamu ya Nne ilivyokuwa inafanya?
(2) Ni lini mtawapatia ofisi Wabunge wa Tanzania ambao wanaunda Bunge la Afrika Mashariki na waache kufanyia kazi hotelini au nyumbani mwao?
(3) Ni lini Serikali ya Tanzania itaanza kuwapa mikopo ya magari Wabunge wa EAC kama zinavyofanya nchi wanachama, mfano Kenya na Uganda, ili waache kutumia mishahara yao na posho kununua magari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi
pia nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika
hotuba hii ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee
alipoishia mwenzangu Mheshimiwa Zubeda kuhusu
walemavu. Walemavu wamekuwa wakidhalilishwa sana,
walemavu wamekuwa hawasaidiwi kimatendo. Kwenye
hotuba ya Waziri Mkuu katika ukurasa wa 47 amezungumzia
suala la walemavu lakini hakuna mkakati wowote
unaoonesha kwamba walemavu watasaidiwa kimatendo.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali
kama ambavyo tunatoa asilimia 10 kwenye Halmashauri zetu
kutoka kwenye own source, naomba kwenye asilimia hizo
hizo 10 iwe ni lazima kwa wanawake asilimia tano wawepo
walemavu at least watano au 10 kwenye watu 30 na walemavu wengine watano kwenye watu 30 ambao ni
vijana. Naomba sana kwa sababu walemavu hawa
wanaonekana kwa macho tofauti na wanawake na vijana
ambao mara nyingi wamekuwa wakitumika kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanasiasa mara nyingi
wamekuwa wakiwatumia wanawake na vijana kwa ajili ya
kuwatafutia kura kwa vipindi vya uchaguzi vijavyo lakini
naomba sana suala la walemavu wamekuwa hawana
msaada dhahiri unaoonekana. Naomba sana suala la
walemavu, aliliongelea sana Marehemu Dkt. Elly Macha,
naomba tumuenzi marehemu Mheshimiwa Macha kwa
kuwasaidia walemavu wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hela za maendeleo; ni
dhahiri kwamba Serikali yetu imeshindwa kabisa kuisaidia nchi
hii kwa hela za maendeleo. Asilimia 34 tu mpaka bajeti
inakwisha ya mwaka 2017, hakuna hela za maendeleo
ambazo zimeenda kwenye Halmashauri zetu ambazo
zinaenda kuwasaidia moja kwa moja wananchi kule chini.
Ingekuwa hakuna own source katika Halmashauri zetu,
mfano, Arusha Mjini tunaendesha Halmashauri kutokana na
own source zetu wenyewe. Mpaka Februari mwaka 2017
imeenda shilingi milioni 320 kati ya bilioni tatu ambayo ni
asilimia 11 tu iliyopendekezwa mwaka 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana
tunavyoendelea hivi tunaenda kuua zile Halmashauri zetu,
wananchi hawatapa maendeleo na kwa Halmashauri
ambazo ziko vijijini hawana own source za maana,
wanashindwa kuendesha vikao, wanashindwa kulipana hela
za vikao, wanashindwa kufika kwenye vikao kutokana na
umbali ama distance kulipana mafuta na gharama za usafiri
kwa sababu tu Serikali haipeleki hela za maendeleo kule chini.
Naomba sana hili mliangalie kwa jicho la pekee sana.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongele suala la
utawala bora; kumekuwa na tabia mbaya sana Viongozi
wa Serikali wanachukua madaraka mikononi na kuanza kutumia hela za Halmashauri au hela za Mikoa na Wilaya
walizopangiwa kuanza kutumia bila kuwashirikisha Kamati
za Fedha na Uchumi za Halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limetokea mwaka
jana Septemba. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa
Mrisho Gambo aliita Walimu wa AICC pale Simba Hall
akaongea nao, wakahojiana, Walimu 701 wakampa madai
yao akamuamuru Mkurugenzi wa Jiji, Ndugu Athuman J.
Kihamia awalipe wale Walimu shilingi 169.8 milioni, hii siyo
sawa. Hata kama Walimu wale walikuwa wanatakiwa
walipwe zile pesa lazima ilitakiwa vikae vikao vya Kamati
ya Fedha na Uchumi, lazima vikae vikao lakini siyo Mkuu wa
Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mkuu wa Mkoa
alikuwa anaumia sana na wale Walimu angeingia kwenye
Mfuko wake wa Mkoa na kutoa hela kwa ajili ya kuwalipa
wale walimu. Hilo alilofanya siyo sawa, alipoambiwa
akasema nawakomesha na hapa nimeanza tu lakini
mtakoma. Pesa zile zilikuwa kwa ajili ya kuwalipa Madiwani,
ilikuwa ni stahiki za Madiwani kwa ajili ya vikao, kwa ajili ya
vocha, kwa ajili ya usafiri lakini Madiwani ambao
wanaongozwa na Chama cha CHADEMA walivumilia yote
na leo wanaenda kwenye vikao wanalipwa sh. 40,000 mpaka
sh. 60,000 mbali walivyokuwa wanalipwa sh.120,000 kwa
kikao kimoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la
Faru Fausta; Serikali hii imejitanabaisha kuwa inapunguza
matumizi na mpaka sasa hakuna mtu yeyote ambaye
analipwa milioni 17 kwa mwezi, lakini Faru Fausta analipwa
milioni 64 kwa mwezi hiyo ni mara tatu. Gharama za Faru
Fausta huyo ambaye ni Mzee ana miaka 54 ni kwa ajili ya
gari lake ambalo linabeba chakula chake, kwa ajili ya
chakula kinachotoka nchini Kenya aina ya LASEMI, kwa ajili
ya kulipa Walinzi 15 ambao wanamlinda kwa masaa 24 na
nguvu za Kijeshi. Faru Fausta huyu ni Mzee lakini ukiongea na
Wizara ya Maliasili wanakwambia eti kwamba anaingiza
fedha nyingi za kigeni sawa na bilioni 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini kama Wazungu au
Watalii wanakuja Tanzania kumuangalia Faru Fausta peke
yake. Naamini Watalii wanakuja Tanzania kuangalia utalii,
kujifunza kutalii Tanzania lakini wakifika Tanzania
wanakutana na Faru Fausta. Naomba sana Serikali kwa
sababu inajidai kwamba inapunguza gharama na kutumbua
majipu, ianze kumtumbua Faru Fausta ambaye ni Mzee sana
sasa hivi na wanasema kwamba nyumba yake ikishakamilika
atatumia milioni 20.4 tu sawa sawa na milioni 244 kwa
mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado gharama hizi ni kubwa
sana. Kule chini Ngorongoro wale Wamasai na wale wakazi
wa Ngorongoro wanahangaika, hawana mahali pa kulisha
mifugo yao, Serikali imeshindwa hata kuwajengea majosho
kule juu kwa ajili ya kulisha mifugo yao, Faru Fausta ambaye
ni Mzee anahudumiwa kwa milioni 64 kwa mwezi, hii siyo
haki na siyo sawa kwa wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie katika suala
la elimu bure; elimu bure ni kwenye makaratasi tu, ukienda
kule chini elimu bure hakuna cha elimu bure zaidi ya kulipa
ile UPE. Walimu wamekuwa kwanza wanahangaika, hakuna
walimu wa sayansi, hakuna walimu wa hisabati, imefikia
wazazi wakae vikao na walimu na wanafunzi kutafuta
walimu wa hisabati na walimu wa sayansi. Inabidi walimu
wakae vikao na wanafunzi na wazazi kulipa walinzi, kulipa
maji kwa ajili ya wanafunzi wao waweze kusoma, hii siyo
sawa kabisa hapa hakuna elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Ma-DC na
Ma-RC badala ya kupigana na Wapinzani kwenye Wilaya
zenu na Mikoa yenu, tafuteni njia mbadala ya kusaidia a elimu
bure ambayo ni sera ya Serikali yenu. Kama mnaweza
kuchangisha hela za Mwenge, Mheshimiwa Gambo Arusha
alinunua pikipiki 200 kwa kusaidiana na wadau wa Mkoa
wa Arusha sasa Mheshimiwa Gambo fanya hili la elimu bure
kwa watoto ambao wanakua sasa hivi. Naomba sana hili
mliangalie kwa jicho la pekee kabisa, hakuna elimu bure
hapa ni utapeli tu wa makaratasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende katika suala
la utalii; suala la utalii tangu kodi na tozo za utalii zipande
limekuwa halina faida kwa nchi yetu. Kama mnavyofahamu
nchi ya Kenya ndiyo imekuwa mpinzani mkubwa sana kwetu
kwa suala la utalii. Nchi ya Kenya imeondoa kodi ya VAT,
nchi ya Tanzania imeweka kodi ya VAT, nchi ya Kenya
imeondoa kodi kwenye magari ya utalii wakati wa
matengenezo, nchi ya Kenya imeondoa Visa kwa watoto
na kuwafanya watalii ambao wana familia waende Kenya
na siyo Tanzania. Nchi ya Kenya imeondoa Park fees Tanzania
vyote hivyo mmeviweka, Tanzania mnataka utalii wa aina
gani ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Tanzania,
naomba sana nchi yetu, naomba sana Waziri Mkuu
anavyokuja kujibu utalii Tanzania umeshuka katika ukurasa
wa 20 amesema kwamba utalii umepanda kwa asilimia 1.2
siyo kweli. Wageni hawa ambao wanaingia nchini ni wageni
ambao wanakuja kwenye mambo ya kibiashara na
mikutano lakini takwimu za utalii zinasema wageni wote
wanaokuja Tanzania ni watalii siyo kweli, siyo watalii wa
vivutio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wageni wengi wanatokea
Rwanda, wanatokea Burundi, wanatokea South Africa na
hii ni kwa sababu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Naomba
sana Mheshimiwa Waziri Mkuu anapopewa takwimu zipitie
na watu wako, anapokuja hapa kwenye Bunge ziletwe
takwimu ambazo ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee mimea
vamizi katika crater ya Ngorongoro. Kumekuwa na mimea
vamizi sana katika crater ya Ngorongoro. crater ya
Ngorongoro kuna uoto wa asili. Mimea vamizi imeharibu
crater ya Ngorongoro, Waziri January Makamba alienda lakini
hali ni mbaya na mbaya zaidi mimea hii inakua kwa kasi
sana. Sehemu ambako mimea hii inakua, wanyama
hawawezi kwenda kula. Sasa inaharibu uoto wa asili kule.
Naomba sana Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Waziri Mkuu
ashirikiane…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Hussein Ibrahim Makungu

House of Representatives (CCM)

Profile

View All MP's