Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Lathifah Hassan Chande

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa maendeleo uweke kipaumbele suala la maji na miundombinu katika Mkoa wa Lindi. Mkoa wa Lindi unakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji safi, takribani asilimia 85 ya wananchi wa Mkoa wa Lindi hawapati maji safi kupelekea kunywa na kutumia maji ya mito na mabwawa pamoja na wanyama. Kitu cha kusikitisha zaidi hospitali ya Mkoa wa Lindi nayo ina tatizo la uhaba wa maji safi kupelekea wagonjwa kuletewa maji ya vidumu kutoka majumbani.
Hii ni hali mbaya inayopelekea wagonjwa kuwa hatarini kupata magonjwa ya mlipuko, nilitegemea mpango wa maendeleo ungekuwa na mipango ya miradi mbalimbali ya maji katika Mkoa wa Lindi na maeneo yote nchini ambako kunakabiliwa na tatizo la maji.
Miundombinu ilipaswa ionekane kwa mapana katika mpango wa maendeleo kati ya mwaka 2012 - 2015 shilingi bilioni 6.4 zilitengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilomita 230 inayotoka Nangurukuru kuelekea Liwale. Hali ni hiyo hiyo katika barabara ya Nachingwea – Liwale. Serikali iweke mpango wa kuzijenga hizi barabara katika kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu; Serikali haijaainisha ina mpango gani juu ya wanafunzi waliofaulu kwenda Vyuo Vikuu, mpaka dakika hii hakuna kinachoeleweka juu ya wengi na hawa wanafunzi waliofaulu vizuri na kukosa mikopo. Serikali itambue kwamba elimu inaelekea kuanguka kama haitoandaa mpango wa kueleweka juu ya mikopo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu afya; nchi nzima inakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa dawa katika hospitali, vifaa tiba na chanjo. Hii imejikita katika Wilaya zote za Mkoa wa Lindi na maeneo mbalimbali nchini. Huu mpango ulipaswa uoneshe maboresho katika sekta ya afya, akinamama na watoto wanaendelea kupoteza maisha yao wakati wa kujifungua kwa kukosa vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kilimo; mpango wa maendeleo umekosa shirikisho la soko la mazao kwa wakulima wa mazao mbalimbali kama ufuta, mbaazi na kadhalika. Ni vema Serikali ingepanua wigo kwa wakulima kwa kuwatafutia masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mawasiliano; mpango wa maendeleo uzingatie suala la kuhakikisha hata maeneo yote nchini yanapata mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uchumi; uchumi unaendelea kuanguka na matumizi kuongezeka hata baada ya wafanyakazi hewa kutambulika. Watumishi wengi wamesimamishwa kupeleka kila mwezi wanaendelea kupokea mishahara. Halmashauri zifikishiwe pesa kwa wakati kwa kutekeleza maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliahidi elimu bure kwa wanafunzi, lakini hii haijaainishwa katika mpango wa maendeleo, kwani elimu bure haina maana yoyote kama wazazi bado wanaendelea kutoa michango. Pia kumekuwa na ucheleweshaji wa pembejeo, mpango huu ungeainisha ni kwa kiwango gani Serikali itahakikisha wakulima wanafikishiwa pembejeo kwa wakati.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

HE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote napenda kwanza kuanza kwa kuchangia sekta ya ujenzi hususan barabara. Katika Mkoa wetu wa Lindi tunashukuru barabara imejengwa ambayo tunaunganishwa kutoka Mkoa wa Lindi hadi Mkoa wa Mtwara na kuelekea Ruvuma. Sasa utata unakuwepo katika barabara za kuelekea kwenye Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni suala la kusikitisha sana kwa sababu inafika wakati unaenda kwenye Wilaya ya Liwale na Nachingwea lakini inakuwa kama ile ni barabara ya kuelekea kijijini. Naiomba Serikali iangalie katika kujenga barabara zinazoelekea katika hizo Wilaya ili nazo ziweze kuwa katika kiwango cha lami kuliko kila siku kuendelea kuiboresha katika kiwango cha vumbi. (Makofi)
Mhshimiwa Naibu Spika, hii pia inaleta adha kubwa kwa watumiaji wa hizi barabara hususan Wana-Lindi pale wanapohitaji kutoka Wilaya moja kwenda Wilaya nyingine. Imepelekea hadi akina mama wanapoteza maisha yao pale ambapo wanahitaji kuhamishwa kutoka Hospitali ya Wilaya na kupelekwa kwenye Hospitali Mkoa ya Lindi, kutokana adha hii ya barabara kuwa mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu umefanyika kutoka barabara ya Nanganga kuelekea Ruangwa. Sasa sijui ni kwa kuwa kuna Waziri Mkuu ambaye ana interest pale, kwa sababu inawezekanaje kuwe na mpango wa kujenga barabara ya kutoka Nanganga kwenda Ruangwa na iachwe hii inayoelekea Nachingwea na Liwale?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuliangalia hilo ili kuwatoa wananchi wa eneo hilo kwenye adha ya tatizo la usafiri, especially kipindi hiki cha masikika, usafiri inakuwa ni shida. Kwa gari dogo unatumia siku mbili kutoka Nangurukuru hadi kufika Liwale kwa kupitia barabara ya Njinjo ambayo ina urefu wa kilometa 230. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata wafanyabiashara wanaishia kuharibikiwa na magari njiani na kutoweza kuendelea kutokana na ubovu huu wa barabara na kupelekea hadi kufika siku saba, ambayo ni wiki nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali iweze kuangalia hili na pia ikiwezekana Waziri husika aweze kutupa jibu; lini atahakikisha kwamba barabara hizi za kutoka Nanganga - Nachingwea hadi Liwale na kutoka Nangurukuru hadi kufika Liwale zitajengwa katika kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia katika sekta ya uchukuzi juu ya matumizi ya bandari yetu katika kukuza mapato ya Taifa letu. Hadi sasa hivi shehena zinazopita katika bandari zetu zinaendelea kushuka na zimeshuka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2014/2015 hadi kufika asilimia 0.1. Hii ni ishara mbaya sana kwa mapato ya nchi yetu. Maana yake ni kwamba mapato ya bandari yanaendelea kushuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi, 2017 takwimu za TRA zinaonyesha kwamba mapato yaliyotokana na forodha, ikiwemo bandari ni shilingi trilioni 4.3. Sasa kama kusingekuwa na upungufu wa shehena katika Bandari, maana yake haya mapato yangeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia bajeti nzima ya mwaka 2016/2017 ni shilingi trilioni 29.54, lakini tumeendelea kushuhudia mapato ya bandari yanavyozidi kushuka kwa kasi. Sasa je, tutaweza vipi kuboresha vyanzo vyetu vya mapato kwa usimamizi mbovu kama huu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumebarikiwa kijiografia kuwepo katika Ukanda wa Maziwa Makuu, lakini hii lawama Serikali haiwezi kuikwepa kutokana na kuwa na sera mbovu juu ya uratibu wa shughuli za bandari. Hili ni janga kwa Taifa letu.
Napenda kuishauri Serikali iweze kuboresha sera zake juu ya uratibu wa bandari ili tuweze kutumia vizuri baraka hizi tulizopewa na Mwenyezi Mungu ya kuwa strategically positioned na hatimaye kuweza kuongeza mapato yatokanayo na bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia juu ya hii sekta ya uchukuzi kuhusiana na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Naungana mkono na juhudi zilizotumika katika kufufua Shirika hili la Ndege la ATCL, lakini siungi mkono njia zinazotumiwa na Serikali katika kusimamia Shirika hili la Ndege. Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu kitendo cha Serikali kununua ndege kwa gharama ya shilingi bilioni 500 na kuzikodisha hizi ndege kwa Shirika la ATCL naona ni kitu ambacho ni kibaya kwetu sisi kama Taifa ambalo kwa sasa hivi uchumi wetu upo dhaifu na bajeti ikiwa ime-under perform. Kwa nini tumeshindwa kuendelea na mfumo wa Public Private Partnership (PPP) ambapo wenzetu wa Kenya tukiangalia Kenya Airways asilimia 29.7 shares zinamilikiwa na Serikali ya Kenya huku asilimia 26.8 zinamilikiwa na Shirika la Ndege la KLM.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wamejiingiza katika soko mitaji, soko la hisa Dar es Salaam, Uganda na Nairobi ambapo umma nao umeweza kumiliki hizo shares nyingine zilizobaki. Kwa nini ishindikane kwetu sisi? Tuna mambo mengi ambayo tunahitaji ku-prioritize na siyo kununua ndege. Kwa sababu tungeweza kuendelea huu mfumo wa PPP, japo tulifanya vibaya, hii siyo kwamba tuachane kabisa na huu mfumo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili suala la Serikali kununua ndege kwa gharama hizo za shilingi bilioni 500 kwangu mimi naona siyo sahihi kwa sababu tuna mambo mengi. Vijijini maji hamna, dawa hamna katika sekta ya afya, elimu pia haijaboreshwa kwa kiwango kile inavyotakiwa, lakini tunahangaika kununua hizi ndege. Napenda kupata majibu juu ya kwa nini Serikali imeshindwa kuendelea na huu mfumo wa PPP? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuishauri Serikali iweze kusisitiza ATCL iweze kukabidhi mahesabu yake kwa sababu hadi Februari Waziri Mkuu aliagiza CAG iweze kupatiwa mahesabu ya madeni na mali juu ya management nzima ya ATCL tangu waweze kupatiwa hizi ndege mwaka 2016. Nashauri kwamba wakabidhi mahesabu haya ya tangu 2009 ambayo tangu mwaka 2009 walishindwa kuyakabidhi kwa CAG. Kwa sababu kuna poor management ya ATCL inayopelekea kuongezeka kwa madeni na kutokuweza kujua exactly mali zetu za ATCL ziko kiasi gani mpaka dakika hii. Kwa hiyo, kikubwa napenda pia kushauri Serikali iweze kufanya hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo. Ahsante, nashukuru.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea juu ya sera ya Serikali ya kuhakikisha kila kata nchini inapata kituo cha afya. Mpaka sasa hivi imeonesha hii sera imeshindikana na kupelekea katika kata za nchi nzima 3,959, kata 448 tu ndiyo zimepata vituo vya afya. Sasa tukienda kwenye Mkoa wa Lindi, tuna kata 138 lakini cha kusikitisha sana ni kata 19 tu ambazo zina vituo vya afya. Kibaya zaidi ni kata moja tu yenye kituo cha afya ambacho kinatoa huduma ya dharura ya upasuaji ya mama mjamzito, hii kata iko Kilimalondo - Nachingwea. Hii imepelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi kuwa tegemezi kubwa kwa ajili ya kutoa huduma ya afya especially kwa akina mama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kibaya zaidi na kutegemewa kote kwa hii hospitali ukiangalia majengo yake tangu mwaka 1954 hayajawahi kufanyiwa ukarabati wowote. Vilevile hakuna nafasi ya kutosha, hata tukisema pawe expanded palepale kibaya zaidi labour ward ina uwezo wa kuhudumia akina mama wajawazito 30 tu kwa wakati mmoja wakati wa kujifungua, hii ni hali mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile vifaa muhimu kama x-ray hakuna, sasa hivi ni miezi mitatu ilikuwepo x-ray moja tu ambayo mpaka sasa hivi haifanyi kazi, kwa hiyo hilo pia liangaliwe. Pia watumishi hawatoshelezi mahitaji ya hospitali ile ya Mkoa. Wauguzi wengi wamestaafu, hakuna specialists wa kutosha na hii tumbua tumbua yenu hii kwa maana hiyo hata hao wachache waliopo tumbua tumbua kwa sababu ya kutuaminisha kwa ajili ya kuwa na vyeti fake, matokeo yake hawa wachache pia wataendelea kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ihakikishe inatekeleza sera yake ya kuhakikisha kila kata inafikiwa na kupatikana vituo vya afya katika hizo kata, pia kutokana na kwamba tayari kuna eneo limetengwa kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Mkoa wa Lindi, basi kwa nini Serikali
isifikirie angalau unit ya labour iweze kuwepo pale, ambayo itakuwa na facilities zote zinazohitajika kwa ajili ya mama anapokuwa anajifungua, hii itasaidia kupunguza hata maternal mortality rate. Pia kuweza kuajiri watumishi zaidi watakaoweza kukidhi mahitaji yaliyopo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bima ya afya, takwimu zinaonesha kwamba ni asilimia nane tu ya Watanzania ambao wako kwenye mfumo wa bima ya afya, ni dhahiri mnafahamu ni mzigo kiasi gani wa gharama uliyopo kwa wananchi juu ya huduma hii ya afya. Napenda kuishauri Serikali iweze kupunguza tozo zisizokuwa za msingi ili hata private sectors waweze kutoa huduma hii ya afya kwa gharama zilizo nafuu ili wananchi waweze kufikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa tiba na dawa; Serikali imekuja na mfumo ambao uko centralized, ambapo dawa zote zinasambazwa na Medical Stores Departments, ni dhahiri kwamba usambazwaji wa dawa kikamilifu umeshindikana, maeneo yote yanashindikana kufikiwa…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabla ya yote napenda kutoa pole zangu kwa familia zote zilizokumbwa na msiba huu mkubwa, kwa kweli ni janga kubwa katika Taifa letu. Vilevile ningependa kutoa pole kwa Mbunge wa Mkoa wa Arusha Mheshimmwa Godbless Lema. Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi, Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika Wizara hii hususan juu ya Sera ya Serikali ya 2002 iliyoelekeza kwamba wananchi waweze kupata huduma ya maji ndani ya umbali usiozidi mita 400, lakini ni dhahiri kwamba imeonesha hadi sasa hii sera imeshindikana kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba maji ni uhai. Mwanadamu akose kila kitu lakini si kukosa maji. Sasa pale ambapo Serikali inaweka mipango ya maendeleo, hata kama ikaweza kufanyia kazi mipango yote isipokuwa hili suala la maji basi nisawa sawa na bure. Kwa sababu mwananchi analazimia kutumia muda mwingi katika kutafuta maji kuliko katika kufanya shughuli za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inavyosema kwamba uchumi unakua kwa asilimia saba ni bure kama mwananchi analazimika kutembea umbali wa hadi kilometa tano hata kumi kwa ajili ya kutafuta maji. Hii sera imeshindikana si kwa vijijini tu, mfano mkubwa ni mkoa wetu wa Lindi ambako maji ni janga kubwa mno kiasi cha kusababisha maji kuwa yenye thamani kama dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Hospitali ya Sokoine hakuna maji, kweli hospitali inakosa maji au kwa kuwa Mawaziri mnapata maji hadi majumbani mwenu? Akina mama wanaenda kujifungua hospitali huku hakuna huduma ya maji wagonjwa wanaenda hospitali wanaolazwa pale wanakosa huduma ya maji, jambo ambalo linasababisha kuwa prone katika kupata magonjwa ya mlipuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wauguzi wanakosa huduma ya maji, madaktari wanakosa huduma ya maji kweli Serikali inaliona hili tatizo na kukaa kimya bila kukuchua hatua yoyote? Kusema ukweli hili ni suala la kusikitisha mno kwa sababu hadi vyoo navyo vinakosa maji pale hospitalini, naomba mliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hapo tu unapoingia vijijini vile vile hali ni mbaya zaidi katika mkoa wetu wa Lindi. Hatuna maji katika Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Mchinga, Mtama pamoja na Kilwa. Ni sawa sawa na kwamba sisi hatustahili kuwa na haya maji, kitu ambacho ni muhimu kuliko vitu vyote ambavyo binadamu anahitaji. Ukienda Liwale si vijijini tu, ukienda Ruangwa siyo vijijini tu bali hata mjini tunakosa maji, naomba mliangalie hili. Wananchi wanalazimika kutembea umbali wa kilometa tatu hadi kilometa kumi kwa ajili tu ya kutafuta maji, na mwisho wa siku hawapati maji safi na salama kwa sababu wanaishia kufuata na kutumia maji ya madimbwi na maji ya mabwawa ambayo pia wanyama wanatumia maji hayo hayo.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni mwaka wa pili sasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ijinasibu kuwa hii ni Tanzania ya viwanda. Kwanza kabisa, napenda kuzungumzia juu ya rasilimali tulizonazo. Gesi asilia iligundulika kwa mara ya kwanza katika visiwa vya Songo Songo, Mkoani Lindi mwaka 1974. Ikagunduliwa Mtwara Vijijini (Mnazi Bay mwaka 1982 na Ntorya mwaka 2012), Mkuranga Mkoa wa Pwani mwaka 2007 na Lindi, Kiliwani mwaka 2008.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiasi cha gesi asili iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa futi za ujazo trilioni nane. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji mafuta na gesi asilia uliojikita zaidi kwenye maji ya kina kirefu cha bahari na kiasi cha gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha maji ni takribani futi za ujazo trilioni 33.7. Jumla ya gesi asili iliyogunduliwa nchi kavu na baharini inafika takribani futi za ujazo trilioni 41.7. Rasilimali hii ya gesi asilia inaweza kutumika katika maeneo mbalimbali yakiwemo kuzalisha umeme, malighafi ya kuzalisha mbolea na kemikali, nishati viwandani, majumbani na kwenye taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Mkoa wa Lindi hauna hata kiwanda kimoja cha kuzalisha mbolea za viwandani licha ya gesi kuwepo mkoani hapo. Ni wakati sasa wa Serikali kutafuta na kuelekeza wawekezaji wa kuzalisha mbolea katika Mkoa wa Lindi ukizingatia ukamilikaji wa barabara ya Masasi-Ruvuma kupitia Tunduru utafanya usafirishaji uwe rahisi wa mbolea hiyo hasa ukizingatia Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ndiyo watumiaji wakubwa wa mbolea hiyo ya viwandani. Ujenzi huu wa viwanda utasaidia vijana wa Lindi ambao zaidi ya asilimia arobaini (40%) hawana ajira, jambo ambalo litapunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la ajira kwa vijana Mkoani Lindi na Kanda ya Kusini kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia juu ya usindikaji na kuongeza thamani mazao. Mkoa wa Lindi unazalisha kwa wingi mazao kama korosho, ufuta, muhogo, mbaazi na mengine mengi. Kwa sasa duniani kote faida ya kilimo chochote kiko kwenye usindikaji na uongezaji thamani ya zao husika. Mkulima wa Lindi na Mtwara bado hajanufaika na anachokizalisha kwa kuwa mteja wake mkuu ni mlanguzi ambaye ananunua kwa mkulima na kuuza kwenye masoko na makampuni makubwa kwa bei itakayompa faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoani Lindi kulikuwa na viwanda vya korosho ambavyo vilikuwa na mashine za kubangua korosho lakini sasa viwanda hivi havifanyi kazi.

Matokeo yake korosho zinauzwa bila kuongezwa thamani na kupelekea kupunguza kipato. Naiomba Serikali ijikite katika kufufua viwanda hivi Mkoani Lindi na pia katika kujenga viwanda vingine hata kwa kushirikisha private sectors ili kuweza kumnufaisha mkulima, kutoa ajira kwa vijana, kudhibiti walanguzi na hatimaye kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na viwanda vya nguo hapa nchini, vipo wapi sasa? Mitumba leo inapigwa marufuku huku Serikali haijaleta njia mbadala wa kuleta nguo za bei nafuu kuweza kukidhi mahitaji ya majority. Makubaliano ya East African Common Market ni kwamba mitumba marufuku ikifika 2019. Wenzetu Rwanda wameanza kuwapa mafunzo akinamama kutengeneza nguo za gharama nafuu kwa kutumia materials zinazopatikana kwa wingi. Imebaki miaka miwili tu tutapiga marufuku mitumba ya Ulaya badala yake tutanunua za bei rahisi kutoka Rwanda na China. Sisi tutanufaika na nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kiwanda Morogoro kinaitwa Mazava ambacho kinazalisha sport wear lakini bidhaa zote zinapelekwa Ulaya na Marekani wakati Tanzania hakuna product yoyote sokoni. Tunahitaji kuwa na viwanda vya nguo vitakavyoweza kuzalisha, kujiendesha pia wakati huo huo nguo ziweze kuuzwa kwa bei nafuu. Tukiwa na viwanda vyetu vitakavyozalisha kwa wingi itasaidia kushusha gharama za uzalishaji na bei ya kuuza itakuwa rahisi na mwananchi wa kawaida ataweza kumudu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Kenya wana kitu kinaitwa Vision 2030. Kwenye manufacturing wana-target kutoka kwenye kumiliki soko kwa 7% hadi kufikia 15% ambayo ni zaidi ya mara mbili. Kwa maana hiyo viwanda walivyonavyo sasa wataviongeza mara mbili. Kipaumbele kimoja cha Wizara ya Viwanda na Biashara Kenya ni kutengeneza skilled technical human resources.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya vitu vinavyoangusha watu wetu hapa hawana uwezo wa kushindana kimataifa, skill level iko chini. Kwa hiyo, hata tukijenga viwanda bila kuwa na programu maalum ya kunyanyua skill za watu wetu, bado effect kwenye uchumi wa viwanda itakuwa ndogo maana kazi zitakuja kuchukuliwa na watu wa mataifa ya jirani ambao wameandaliwa Kenya na Rwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushauri Serikali ijikite katika kujenga viwanda na vilevile kutayarisha vijana kwa kutengeneza skilled technical human resources ili waweze kupata ajira katika hivi viwanda. Vilevile Serikali iboreshe miundombinu ili kuwezesha movement ya bidhaa zinazotengenezwa, maana kuongelea Tanzania ya Viwanda bila kuwa na uhakika wa miundombinu ya barabara ni sawa na kuongelea mwili wa binadamu bila damu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's