Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Mary Deo Muro

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja zilizoko mezani juu ya Mpango wa Miaka Mitano. Kwanza namshukuru Mungu kuniwezesha kufika katika Bunge lako Tukufu. Pia nashukuru chama changu kuniona nafaa kuiwakilisha jamii. (Makofi)
Awali ya yote, napenda kuungana na wale wote ambao wamechangia hoja inayohusu Tanzania ya viwanda kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kabisa kwamba Tanzania ya viwanda lazima iendane na afya ya wananchi, elimu, utawala bora, miundombinu, maji na ardhi. Nafahamu kabisa kwamba nia na madhumuni ya mpango huu ni kuleta ustawi wa jamii kwa wananchi wa Tanzania ndiyo maana Upinzani na Chama Tawala tunachangia kwa hoja nzito ili tuweze kuleta ustawi wa jamii kwa Watanzania wote. Lengo letu siyo malumbano, lengo letu ni kuhakikisha kwamba Watanzania ambao wanatumia pesa zao kwa ajili ya kutuweka hapa wanapata haki stahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye mada halisi. Ningependa kuongelea afya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa kwamba hakuna ufanisi katika Tanzana ya viwanda bila wananchi kuwa na afya bora. Tukiangalia maeneo mengi ya Tanzania tunakuta kwamba huduma za afya ziko hafifu. Kwanza nakumbuka asubuhi ya leo kulikuwa na msemaji mmoja ambae alitoa haja yake kuhusu hali halisi ya afya ya Watanzania na mazingira wanayoishi. Waziri husika alijibu kwamba Serikali siyo sababu ya wananchi kupata matatizo ya afya, isipokuwa wananchi wenyewe ndiyo sababu ya kupata matatizo ya afya au magonjwa ya kipindupindu na magonjwa ya mlipuko. Mimi napenda niulize Serikali iliyoko madarakani kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa kwamba kuna sekta zinazoshughulikia afya na kama kuna tatizo la kipindupindu ina maana kwamba sekta inayohusika haijawajibika. Nataka nijielekeze kwa mfano, natoka Mkoa wa Pwani Wilaya ya Kibaha, ilitokea mlipuko wa kipindupindu na sababu kubwa ni kwamba, Wizara ya Maji kwa Pwani haina mamlaka isipokuwa tunatumia DAWASCO ambayo kwa Pwani hakuna miundombinu ya kutoa maji machafu. Ina maana utiririshaji wa maji machafu ni lazima kwa sababu DAWASCO haijawajibika na watu wa Pwani wanahitaji mamlaka yao ili waweze kuiwajibisha pale inapokuwa haiwezi kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, narudi kwa Waziri aliposema kwamba siyo wao wanaosababisha, yeye kama Waziri anafahamu kabisa ni nani ambaye hakuwajibika mpaka mlipuko wa magonjwa utokee. Kwa hiyo, hawezi kusema kwamba yeye siyo sababu. Napenda kumwambia kwamba yeye na Watendaji wenzake hawakuwajibika. Walitakiwa wawajibike ili ugonjwa wa kipindupindu usitokee kwa sababu wapo ambao wako kwa ajili ya kazi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kwenda kwenye sekta ya elimu, tunaangalia Tanzania ya viwanda ambayo inatakiwa iende na elimu. Ni kweli tumedahili watu wengi kwa ajili ya sekta mbalimbali, lakini tuangalie sheria zinazo-govern uanzishwaji wa viwanda. Tunafahamu kabisa uanzishwaji wa viwanda siyo ufufuaji wa viwanda pengine ni uanzishaji wa viwanda kwa mashirika yanayotoka nje, wawekezaji kutoka nje. Hautaondoa umaskini Watanzania kama waanzishaji wa viwanda wanakuja wa watu wao kutoka nje, kama sheria za nchi haziwezi kusimamia kuhakikisha kwamba rasilimali watu iliyopo hapa ambayo ni watoto wetu ambao wamesomeshwa kwa pesa za Watanzania wanaajiriwa katika viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeiomba au niishauri Serikali kwamba, itakapoanzisha mpango huo ihakikishe kwamba inatunga sheria ambazo wawekezaji watakuwa nazo wakiangalia kwamba Tanzania ina watu ambao wanaweza kufanya kazi ambazo wanaleta watu wao kuja kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano, kuna bomba sasa hivi linatoka Ruvu chini kupeleka maji Dar es Salaam. Nimeshuhudia kwa macho yangu, mpaka yule wa kufukua udongo, yule mtu wa kufanya kazi za welding ni Mhindi wakati tuna Watanzania tunawasomesha VETA hizo mnazosema zimeanzishwa wamekaa mitaani hawana kazi. Sasa unajiuliza je, huu umaskini tunaouimba hapa utaondolewaje kwa kiasi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiachana na hapo naomba niende kwenye kilimo, nimesoma, nimeangalia jinsi Waziri wa kilimo alivyojipanga, lakini naomba niongee machache juu ya hilo. Nimeona kilimo kina ufugaji, kina kilimo yenyewe, lakini nikiangalia kuna ufugaji, naomba ni-declare interest mimi ni mfugaji wa kuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mara nyingi sana kuku wakitoka Kenya wanajazwa pale Dar es Salaam kiasi kwamba wafugaji wa Tanzania tunashindwa, wajasiriamali wa Tanzania tunashindwa kuweza kufanya biashara. Sasa ningeomba Wizara katika Mpango huu wa Tanzania ya viwanda basi wahakikishe kwamba Wizara husika inasimamia kidete hali hii ili Watanzania wajasiriamali waweze kufaidika na kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeomba upangaji wa bei, mkulima amelima kwa shida zote, Serikali inakuwa mpangaji wa bei. Serikali inapanga bei wakati mkulima amelima kwa gharama zake. Anapokosa mapato mkulima anashindwa kuendeleza kilimo. Kwa hiyo, umaskini hatuwezi kuondoa kama Serikali haiwezi kusimamia kilimo ipasavyo, kutafuta masoko ambayo yana tija na kuhakikisha kwamba mkulima anapata faida ili kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu. Nimeangalia miundombinu nikaona kwamba kwa usafiri kwa mfano wa Dar es Salaam, msongamano wa Dar es Salaam nilivyouangalia, sisi sote tunafahamu kwamba time ni factor ya production, kama hatuwezi ku-save time tuna-consume time kwenye kutembea kwenye barabara masaa manne kutoka Kibaha mpaka ufike Dar es Salaam, masaa manne kutoka Mbagala mpaka city center ukafanye kazi, ina maana muda mwingi unapotea hapo katikati bila kutumika. Hii ina maana kwamba Tanzania ya viwanda watu watakuwa wanatembea kwenye magari masaa manne hawajafika kiwandani ina maana utekelezaji wake utakuwa mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende kwenye miundombinu ya maji. Nimesoma na nimesikiliza lakini nimeshangaa kusikia kwamba asilimia 68 ya Watanzania wanapata maji. Jamani mimi natoka kijijini kwetu Makambako chini kule hawajawahi kuona maji ya bomba hata siku moja. Nimekuja huku Kisarawe Mkoa wa Pwani wanachota maji ya visima, hiyo asilimia 68 ambayo wamei-calculate wakapata hapa sijaweza kuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama kweli tuna nia ya dhati ya kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na afya bora, hebu Serikali ijipange kuhakikisha maji ya uhakika yanapatikana kwa ajili ya kuwapa afya bora Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye ardhi. Ni kweli kabisa ardhi ndiyo mpango mzima wa Tanzania ya viwanda ya Mheshimiwa Magufuli, lakini naomba nitoe ushauri...
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha mchangiaji.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la wavuvi wa Mafia ni kule kuambiwa wahame eneo wanalovulia miaka mingi na kufanywa Hifadhi ya Taifa, hivyo wananchi kukosa eneo la uvuvi. Naishauri Serikali kuangalia upya jinsi ya kuwatafutia wananchi eneo la uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la majosho kwa ajili ya wafugaji wa Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Kibaha, eneo la Kwala ambako wafugaji wengi Wakwavi, Wamasai wanapoteza mifugo yao mingi na ECF (Ndigana Baridi) kutokana na kukosa majosho na dawa za mifugo kuwa juu. Nashauri Serikali irudishe mpango wa ujenzi wa majosho ili kusaidia wananchi. Pia kuwepo punguzo la bei ya dawa ili kusaidia wananchi kumudu gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri kusaidia udhibiti wa soko la mazao yatokanayo na mifugo, mfano, kuku wa nyama kuletwa kutoka nchi za jirani hivyo kuua soko la ndani la wafugaji. Mfano, wafugaji wa kuku wa mayai wanakosa soko la mayai kutokana na mayai toka nchi za jirani kuingia nchini.

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kusaidia Wizara kuwa na vyuo vikuu vya uhakika ili kukuza sanaa na michezo nchini. Naomba Wizara ijikite katika kuibua vipaji kwa kuendeleza michezo shuleni ikiwa ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu wa michezo, pia kwa wanafunzi wanaoshinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuwepo uhuru wa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na Televisheni ya Taifa kubaki ya Taifa na siyo kwa ajili ku-report taarifa za chama chochote bali itumike kama chombo huru kwa ajili ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuunga mkono vyombo vya binafsi kwa mchango mkubwa vinaotoa kwa Taifa. Naishauri TBC kuongezwa mtaji ili iweze kuwafikia watu wengi katika jamii.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nakishukuru chama changu kwa kunipa nafasi ya kuingia Bungeni na kuwa sehemu ya Bunge kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nianze kuchangia kuwa mimi ni mmoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu ambayo ilikuwa inatembea nchi nzima kuangalia uhalisia wa mambo yanavyoendelea katika Kamati hiyo. Nilichokiona ni kwamba nchi yetu ya Tanzania, kama tuna nia ya dhati, kwa sababu niliangalia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) ambao uliletwa hapa Bungeni. Nikaangalia na Pato la Taifa linakotoka, vyanzo vya Pato la Taifa la kuendeleza mpango huo, nimekuta kuna tofauti kubwa sana kwa sababu vyanzo kama bandari ambayo tulitarajia ilete pato ambalo litaweza kuendesha shughuli za nchi inadidimia na inazama kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Bandari ya Dar es Salaam kama ungewapa waendeshaji wengine ingeweza kutumika kama chanzo kikubwa ambacho kingeweza kuinusuru Tanzania kuishia kuwa na wakopaji wa kila siku, kwa sababu tumefika pale bandarini tumekuta kuna vitu viwili, kuna kitu kinaitwa MCL, tumekuta kuna TPA ambayo ndiyo mama. Katika kuangalia hali ile tumekuta kwamba watu wawili hamuwezi kuendesha kitu kimoja kwa nia tofauti. Kwa hiyo, unakuta kwamba bandari badala ya kupata mapato, ikafanya kazi vizuri, yeye anakuwa mwangalizi wakati MCL ambaye hana kipato anashindwa kufanya kazi vizuri. Na sehemu zote hizi kuna watumishi ambao wako pale wanafaidika na hamna kitu kinachotokea ambacho kinarudi kwenye Serikali kama mapato ambayo yanaweza kuendeleza nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza malalamiko ya watu wengi mikoani wanataka maji, barabara, n.k., lakini nimeangalia mapato ya Tanzania kupitia vyanzo halisi, hakuna. Kwasababu kama ni bandari, nimeenda bandarini nimekuta kuna migogoro na migongano ya kimaslahi. Kuna watu wamefika pale wamefanya ni mahali pa kuchukulia hela wakati nchi haipati pato lolote. Unakuta kuna migongano ya kimaslahi, kuna TRA inafanya yake, kuna TPA wanafanya yao, yaani kuna migongano ya kimaslahi imefikia mahali ambapo hatuwezi kupata kitu chochote. Tumefukuza wadau ambao walikuwa wanaleta hela pale bandarini kwasababu ya migongano ya kimaslahi. TRA anataka vyake, TPA anataka vyake sasa wamefika mahali hakuna kinachoendelea ni wawekezaji kuondoka na kutuacha tukiwa watupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia tulivyofika airport kwenye viwanja vya ndege, nimefika Mwanza; kile kiwanja cha Mwanza nimeona kwenye majedwali inaonesha kwamba wanapewa shilingi bilioni 30, ni kweli tulikuwa Mwanza, tumekuta kuna uendelezaji wa jengo la kuongozea ndege ambalo limejengwa vizuri kwa East Africa nafikiri linaongoza, lakini ukiangalia lile jengo limesimama kwa muda karibu mwaka haliendelezwi kwa sababu halina hela. Na nimeangalia kwenye hotuba ya Waziri inaonesha kwamba anatoa shilingi bilioni 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipofika pale tulikuta kwamba kuna shilingi bilioni 20 ambazo Serikali ilitakiwa itoe haikutoa, leo hii unampa shilingi bilioni 30 wakati ana deni halafu mradi ulishasimama. Mobilization ya material mpaka ifike kuanza tena ina maana ni hela zaidi ya hiyo, na hivyo ndivyo vyanzo vya mapato ambavyo Serikali kama ingejikita kwenye vile vyanzo ambavyo ni deal tungeweza tukapata mapato na tukaendesha hizo shughuli zote tunazosema, za maji, za barabara na kadhalika. Hapa hata tupige kelele kama vyanzo hivi tumeshavikalia haiwezekani hata siku moja kutoka hapo!
T A A R I F A...
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante siipokei, naomba akae nayo kwa sababu mimi naelezea kile nilichokiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu kama tutaendelea kupanga bajeti ambazo hazitekelezeki ina maana wananchi wetu tutakuwa tumewatenga mbali sana. Hapa UKAWA na CCM wote tumetoka kwa wananchi, tunahitaji kuwafanyia wananchi ili wapate neema, lakini kama tunafika hapa halafu tunaulizana taarifa wakati mimi nina taarifa sahihi na mimi ndiye niliyezunguka nikaona reality, ninasema haya kwa sababu niliyashuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tungekitengeneza vizuri na tukawekeza vizuri kwa hizo hela zilizotengwa siku tulipokwenda Mwanza tungekuta kwamba lile jengo kwenye kiwanja kile liko mbali sana na umaliziaji. Kiwanja cha Mwanza kinajaa maji, ndege kubwa zinashindwa kutua kwa sababu wakati mwingine kunakuwa na ukungu, hamna viongozea ndege ambavyo wakati wa ukungu ndege zinaweza zikatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vyote hivyo kwa shilingi bilioni 30 haiwezekani. Nimesema hayo kwasababu kama tunaimarisha bandari, viwanja vya ndege tunaweza kuwa na pato ambalo tunaweza kuendesha nchi na tunaweza kupata hayo yote ambayo mmeomba, barabara, maji, afya na kadhalika. Fahamu kwamba afya, maji, elimu hivi vyote ni consumer wa mapato kutoka vyanzo kama bandari na viwanja vya ndege. Viwanja vya ndege vikizalisha vizuri ndipo tunaweza tukapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa niunge mkono msemaji aliyepita. Tumepita mawasiliano, tumekuta kweli wanasema kwamba watazima huo mtambo, lakini tukajiuliza nchi yetu ya Tanzania ambayo ina wataalam ambao wanawezakugundua, wapo kwa ajili ya kujua kwamba hizi ni bidhaa fake na hizi ni bidhaa ambazo sio fake. Kama wapo na wanalipwa na wanaruhusu vitu viingie, halafu wateja wanunue, hawa maskini wa kule kwetu, halafu waambiwe mitambo ile inazimwa kwa simu zao fake halafu wakose simu, hivi tunawezaje kulifanya hili Taifa liingie katika uchumi wa kati kama sasa hivi bibi yangu na mama yangu kule kijijini aliyenunua simu fake hatakuwa na simu kuanzia mwezi wa sita? Tunatakiwa tufike mahali tuangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikuwa wapi wakati simu fake zinaletwa hapa nchini? Kile chombo ambacho kinadhibiti uingizaji wa simu fake kilikuwa wapi? Hao ndio waliotakiwa washughulikiwe, kwamba kwa nini mmeruhusu simu fake zikaingia lakini si yule bibi yangu kule nyumbani ambaye hajui na simu nilimpelekea tu mimi na mimi nikiwa najua nimempelekea simu nzuri. Mnafahamu kabisa simu ndiyo mawasiliano ambayo kila mmoja anaweza akawasiliana na mwenzake. Leo hii tunapowazimia watu karibia milioni 20 hawatakuwa na simu, Taifa tunalipeleka wapi? Na kama Taifa litakosa mapato hayo maji mnayoyaomba humu ndani mtayapata wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba jamani kama kweli tuna nia ya dhati tuhakikishe kabisa Serikali inafuatilia. niishauri Serikali fuatilieni vitu, kama kweli mlikuwepo wakati simu zinaingizwa fake mna kitu cha kujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudi kwenye mawasiliano. Nimeona kwamba kuna watu wanachota hela pale. Kuna makampuni yanachota hela pale kwenye mfuko wa uendelezaji minara…
MWENYEKITI: Ahsante!

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na ninayo machache ya kuchangia kwenye Wizara hii. Kwanza namshukuru Mungu kuwa na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchangia eneo la mwanamke na nishati; nimeamua kuchangia eneo hili kwa sababu nimeona ni jinsi gani mwanamke anahangaika na nishati kuanzia asubuhi mpaka jioni na saa nyingine ashindwe hata kutayarisha chakula kwa kukosa nishati. Nafahamu kabisa kwamba, ndani ya jengo hili wanaume wengi wanakuta chakula kiko mezani, hawajui mwanamke amehangaika kiasi gani mpaka akifikishe mezani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia safu ya uongozi kwenye nishati naona ni wanaume wawili wamekaa pale, lakini hakuna mwanamke ambaye angesimama kwa niaba ya wanawake wa Tanzania ambao wanahangaika siku nzima kutafuta kuni ili waweze kutayarisha chakula kwa ajili ya familia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za katikati hapo nyuma, kulikuwa na mradi unaitwa biofuel ambao tulitarajia kabisa ungeweza kutumia gharama ndogo ya kumfikia kila mwanamke alipo, akapata moto poa, ambao ungeweza kumrahisishia kupika na kufanya kazi za upishi kwa urahisi, lakini mpaka sasa hivi hatuoni dalili zozote za ule mradi wa mibono ambao ungeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kueneza vijiji vingi nishati mbadala. Tunaona kuna biogas na zimetengewa pesa hapa bilioni 3.2, lakini ukiangalia kwa Tanzania ilivyo kubwa, mpaka akafikiwe mwanamke aliyeko kule kijijini pembezoni, akapate biogas itakuwa ni karne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mwanamke ataendelea kulia machozi jikoni huku akichochea vyungu, akichochea sufuria, ili mwanaume akae ale mezani, ambaye haingii jikoni na mwanaume hapati uchungu kwa sababu siye anayepika! Mwanamke ndiye anayehangaika, apike, atafute wapi kuni, atatafuta mkaa, atatafuta chochote kile, lakini chakula kiive! Namwomba Waziri anapokuja angalau atuambie amemuangaliaje mwanamke wa Kitanzania? Jinsi gani anaweza akasaidika na bajeti hii ambayo ameileta mezani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, atakapokuja kujibu, naomba Waziri aje na majibu sahihi, sana sana atuambie labda ule mradi wa biofuel umeishia wapi? Watu walishaanza kulima na mibono ilishaletwa mpaka majiko, umeishia wapi? Leo ukija kwenye bajeti hii ya 3.2 billion kwa Tanzania nzima wakati unaweza ukatumia biofuel ikaenda kwa haraka na kwa nafuu zaidi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Mkoa wangu wa Pwani. Mkoa wangu wa Pwani, Wilaya ya Kibaha, kuna mradi ambao ulikuwa unaendelea wa TANESCO wa Gridi ya Taifa, walitathminiwa wakaambiwa kwamba watalipwa. Ni Vijiji vya Kiluvya, Mwanalugali na Mikongeni, lakini tangu wametathminiwa kwenye mpango wa miaka mitano ilielezwa kwamba, wamelipwa lakini mpaka sasa hivi hawajalipwa na kinachoendelea hatuelewi! Wananipigia simu kila siku wanasema utakaposimama, tuulizie kwa Waziri, Je, hela zetu tutalipwa? Kama hatulipwi, tuendeleze maeneo yetu? Kwa hiyo, Waziri atakapokuja kujibu, ningependa kupata majibu ya maswali ya Wanakibaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuchangia yafuatayo. Kwa mfano, tunaona TANESCO imebeba mzigo mzito sana, inazalisha umeme, inasambaza, inauza! Hivi kweli, hili shirika binafsi litaweza kufanya kazi zote hizo? Kwa nini Serikali isije na mpango mwingine ambao uta-faster maendeleo ya Tanzania tunapoelekea kwenye Tanzania ya viwanda? Nadhani kungekuwa na mpango wa ziada wa kuisaidia TANESCO isifanye kazi zote peke yake; kuzalisha, kusambaza, kuuza, ndiyo maana unakuta saa nyingine…
MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi yanachelewesha kesi hivyo kuchochea migogoro ya ardhi. Kesi inachukua miaka kumi; nini matokeo yake kama siyo kukuza migogoro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro kati ya wananchi wa Mwanalugali - Kibaha Mjini na Halmashauri Kibaha Mjini ambao wameporwa ardhi tangu mwaka 2004 kwa madai ya kufidiwa mpaka leo, nini maana yake? Mgogoro kati ya wananchi wa Bagamoyo na EPZ katika shamba ardhi ya Bagamoyo; mgogoro wa ardhi kati ya wafugaji na Vigwaza na wakulima, nashauri wafugaji watengewe maeneo ya mifugo ili kupunguza migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la CDA ni kubwa. Wafanyakazi wa CDA kupora ardhi za wananchi na kujimilikisha. Mhudumu ana viwanja kumi eti kwa sababu wanapopima wanajipa viwanja na kuviuza kwa bei nafuu. Ushauri wangu ni kwamba mambo ya ardhi yarudi mamlaka ya Mji wa Dodoma. Wananchi wamechoshwa na CDA kwa jinsi inavyofanya kazi kwa maslahi ya wafanyakazi wenyewe.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifute hifadhi ambazo hazina wanyama tena na maeneo hayo yagawiwe kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali isisitize kwa mabalozi walioko nchi za nje kufanya kazi kwa ukamilifu kutangaza vivutio vyetu na kuwe na library zao za maliasili yao katika ofisi zao zinazoelezea jinsi Tanzania ilivyo ikiwa ni pamoja na tamaduni zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoteli za Tanzania ziboreshwe, pia kuwepo na vyuo vikuu vya kufundishia wahudumu wa hoteli hizo Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu ni mali, Serikali ijipange kupanda miti, pia kutoa zawadi kwa kushindanisha wapandaji bora, waweza kuwa ni Taasisi kwa Taasisi au Wilaya kwa Wilaya.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Umaskini na Athari Zake; kukithiri kwa umaskini kunazalisha uhalifu na ndio unaoondoa amani katika Taifa. Hivyo basi nashauri hatua za kuondoa umaskini zifanye jitihada za haraka ili kunusuru nchi na majanga ya uvunjifu wa amani kunakopelekea magereza kujaa wahalifu na kupelekea Taifa kubeba mzigo mkubwa wa kuwatunza wafungwa badala ya kuelekeza fedha hizo kwenye maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ongezeko la Watu. Ifikapo 2020/2026 idadi ya watu itafikia milioni 63 ambayo kama utekelezaji wa mpango wa miaka mitano hauwiani na ongezeko hilo italeta shida kwenye huduma za jamii wakati huo, hivyo ndoa za utotoni zithibitiwe kupunguza ongezeko.
Mheshimiwa Naibu Spika, Elimu. Bila elimu yenye tija Taifa haliwezi kufika kwenye uchumi wa kati. Elimu yetu haisaidii kijana kujiajiri, ni vyema kila Mkoa kukawa na scheme for irrigation ili kumeza ombwe kubwa la vijana wanaomaliza shule ili kuwafanya wasigeuke kuwa wahalifu katika Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madhara ya ukosefu wa ajira kwa vijana kunasababisha uhalifu kuongezeka hivyo kusababisha ongezeko la ajira za Polisi na Magereza na hivyo kuongezeka kwa matumizi kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukosa ajira kunasababisha utumiaji madawa ya kulevya hivyo kuligharimu Taifa kuwatibu kwa gharama kubwa na pia kutokana na hali ngumu ya maisha na utumiaji madawa ya kulevya, UKIMWI umeanza kushika kasi sehemu nyingi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tuangalie nguvukazi ya Tanzania ambayo iko asilimia 60 ya wananchi wa Tanzania kuwa mzigo kwa nchi, hivyo Taifa lijipange kunusuru tatizo hili ambalo miaka ijayo Taifa halitaweza kulimudu, hilo ni kundi la vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo, naomba iainishwe vijana wametengewa ekari ngapi ili waweze kujiajiri, pia njia ambazo Taifa litawawezesha.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's