Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Risala Said Kabongo

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na shule za ufundi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Shule ya Ufundi Moshi (Moshi Technical School), shule hii ya ufundi ilikuwa ikitoa elimu ya ufundi kwa wanafunzi kutoka mikoa mingi Tanzania na baada ya masomo ya elimu ya sekondari wanafunzi hawa walijiunga na Vyuo vya Arusha Technical na Dar Technical pamoja na Ifunda Tech. Kwa sasa shule hizi za ufundi zina hali mbaya sana hasa Shule ya Ufundi Moshi; majengo yamechakaa sana vifaa vya ufundi vingi vimekufa na hivyo umuhimu wa shule hii kama ya ufundi, inaendelea kushusha taaluma za ufundi katika nchi yetu na hasa kipindi hiki ambacho tunakwenda kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda ambao unategemea nguvukazi kubwa ya vijana waliopitia taaluma ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri anapohitimisha aniambie ametenga bajeti kiasi gani kwa ajili ya kuimarisha shule za ufundi Tanzania. Hii itasaidia sana vijana wetu ambao wamekuwa wakikosa ajira baada ya kumaliza shule na kujiunga kwenye vitendo visivyo na tija kwa Taifa ambapo wangekuwa na utaalam wa ufundi mbalimbali wangeweza kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakaguzi wa shule. Kumekuwa na changamoto kubwa kwa wakaguzi wa shule ambao wengine wamepewa magari ya kuzungukia na kukagua shule, lakini tatizo la magari hayo wakati mwingine yanakosa bajeti za mafuta ya kuwawezesha wakaguzi kufanya kazi zao kwa ufanisi. Naomba kujua kuwa Waziri amejipanga vipi kuhusiana na changamoto hii na atalitatuaje kupitia bajeti yake ya 2016/2017 ili kuhakikisha wakaguzi wanapata fursa ya kufikia kwenye shule zote nchini na kufanya ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa shule. Uboreshaji wa shule za msingi na sekondari uangaliwe kwa karibu ili kuongeza tija, shule zetu ni chakavu sana, huduma za madarasa, vyoo havifai kwenye shule zetu, hakuna viwanja vya michezo, madawati, nyumba za Walimu. Pamoja na changamoto zote hizo, tatizo la vitabu ni kubwa sana, naomba Waziri anapohitimisha atuambie amejipangaje kwa bajeti yake ili kuweka sera za kusaidia huduma shuleni kupunguza gharama kubwa kwa wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mishahara ya Walimu. Mishahara ya Walimu ni midogo sana ukilinganisha na kazi kubwa anayoifanya Mwalimu. Naomba Waziri aangalie ni namna gani anaweza kuangalia upya suala la mishahara ili kuwapa motisha Walimu wetu. Hali ya maisha imepanda sana, hivyo kupelekea Walimu kushindwa kujikita katika ufundishaji na kujiingiza katika biashara ndogondogo baada ya vipindi vya darasani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia suala la elimu kwa watumishi waliopo kazini. Kumekuwa na wafanyakazi ambao wamekuwa wakifanyia kazi idara mbalimbali kwa muda mrefu na baadaye kutaka kujiendeleza kutokana na uzoefu wao wa kazi wanazozifanya. Wanapotaka kujiendeleza wanaambiwa cheti cha form four, ambacho pengine wakati huo hakikuwa kizuri ila amekuwa mzoefu wa kazi hata kwa miaka zaidi ya 10. Naomba Waziri anapohitimisha atuambie ni namna gani anaweza kutengeneza mfumo wa elimu ya juu kwa watumishi wa umma wanaohitaji kujiendeleza.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara ya Nishati na Madini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa la ukataji wa miti na kuvamia mapori kwa ajili ya uchomaji wa mkaa baada ya ujangili wa wanyama sasa ni ujangili wa misitu. Namtaka Waziri atoe majibu ni namna gani Serikali hii kupitia Wizara hii imejipanga kuzuia au kupunguza matumizi ya mkaa hasa mijini ambako kuna nishati mbadala ya gesi na soko kubwa la mkaa limeelekezwa huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukataji wa miti kwenye mapori umeendelea kusababisha mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha mafuriko sehemu kubwa nchini. Mafuriko haya yanatokana na ukataji wa miti ambayo huzuia kingo za mito na hivyo kusababisha mafuriko makubwa. Namtaka Waziri atoe majibu ya kina ni namna gani amejipanga kuokoa misitu kwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, namtaka Waziri atoe majibu ni kwa namna gani Serikali imeweka mkakati wa kudhibiti wachakachuaji wa mafuta ya magari ili kuondokana na adha ya uharibifu wa magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashuhudia matumizi ya solar kama umeme mbadala maeneo mengi nchini na hasa mijini. Namtaka Waziri anipe majibu ni kwa namna gani zinaweza kusaidia wananchi wa vijijini ili watumie nishati hii kwa wingi kwa kuuza solar kwa bei nafuu kwenye maduka ya Serikali ili wananchi wengi wafaidike na nishati hii. Naomba Waziri anipatie majibu haya kwa faida ya wananchi wetu wa vijijini.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchangia hoja iliyopo mezani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya ujenzi wa nyumba, mfano Shirika la Nyumba (NHC) nyumba zao ni gharama kubwa sana kuanzia shilingi milioni 50 mpaka milioni 270 na kuendelea. Nyumba hizi kimsingi hazimnufaishi Mtanzania wa kawaida mwenye kipato cha chini. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inapunguza gharama hizi ambazo kimsingi zinatokana na Serikali kutokuchangia gharama za miundombinu kama barabara, maji na umeme, gharama ambazo sasa zinatolewa na NHC kupitia mikopo ya ujenzi wa nyumba hizi, hali inayosababisha gharama ya ujenzi kuwa kubwa sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na miundombinu hii kumekuwa na suala la VAT ya asilimia 18 katika kununua nyumba hizi ambazo kimsingi VAT zimelipwa kwenye vifaa vya ujenzi. Ninaitaka Serikali itoe tamko kupitia Wizara hii ni lini itatoa VAT hizi kwa nyumba zote za Shirika la Nyumba ambalo ndilo mkombozi wa Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo mikopo ya magari, ningeshauri Serikali itoe mikopo ya nyumba za NHC kwa watumishi ili waweze kukatwa fedha kiasi. Hii itaondoa hali ngumu za wastaafu wetu ambazo wanapata baada ya kustaafu katika utumishi wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Ardhi imekuwa ikifanya kazi bila kuwa na bajeti. Tatizo la Tume hii inafanya kazi ya kuangalia eneo baada ya shughuli kubwa ya upimaji. Ningeshauri kama Tume hii itaendelea kuwepo ipewe bajeti ya kutosha na itoe ushauri kabla ya eneo kupimwa. Ninaitaka Serikali itoe majibu ya kina kuhusiana na Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, ninaitaka Serikali itoe tamko kuhusu wananchi wanaovamia vyanzo vya maji (waliopo ndani ya mita 60) ambazo wanatakiwa kuondoka. Mfano mzuri ni vyanzo vya maji vilivyopo Mkoa wa Arusha ambako kuna tatizo kubwa la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya maziko hasa ya mijini yamekuwa na changamoto kubwa sana. Ninamtaka Waziri anipe majibu kuwa Wizara yake imejipangaje kukabiliana na tatizo hili la maziko katika maeneo ya miji kama Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Kilimanjaro ambazo ardhi ni changamoto kubwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bomoa bomoa ninamtaka Waziri aniambie Serikali imejipangaje katika kulipa fidia kwa wananchi hawa ambao wanaendelea kubomolewa nyumba zao na fidia zinazotolewa haziendani na hali halisi ya gharama za ujenzi wa nyumba? Ni kwa namna gani wananchi hawa watafidiwa kulingana na hali halisi ya maisha ya leo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii muhimu ambayo inachangia Pato kubwa la Taifa. Kwanza kabisa nipende kuipongeza hotuba nzuri ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchango wangu mimi nitajikita kwenye suala zima la utalii. Tunapozungumzia utalii nitazungumzia mambo matatu muhimu ili tuwe na utalii endelevu. Ili tuwe na utalii endelevu tunahitaji vivutio vya utalii, ili tuwe na utalii endelevu tunahitaji namna ya kufikia vivutio hivyo, tunahitaji malazi ya kuwalaza wageni wetu wanapofika kwenye vivutio vya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala la vivutio vya utalii. Nchi yetu ya Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na vivutio vyenye ubora wa hali ya juu ukilinganisha baada ya nchi ya Brazil. Lakini cha kusikitisha sana pamoja na kwamba Wizara hii inachangia asilimia kubwa kwenye Pato la Taifa, kwa mfano nikiangalia asilimia 17.5 inachangia Pato la Taifa kupitia Utalii, lakini asilimia 4.8 inatoka kwenye misitu, asilimia 25 ya Pato la Taifa kupitia fedha za kigeni zinatoka kwenye suala zima la utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho nashangaa sana tunaona kitakwimu mapato haya ni makubwa lakini ukilinganisha na vivutio tulivyonavyo bado tunahitaji kuwekeza nguvu kubwa sana kwenye suala la kuboresha utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vivutio tulivyonavyo bado tunapata mapato kidogo sana, lakini tunapata watalii wachache sana ambao wanatembelea vivutio vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri, imejaa mambo mengi imejaa mipango mingi; lakini niseme ukweli tusiporekebisha changamoto za miundombinu, hasa miundombinu ya barabara bado suala la utalii tutakuwa tunaimba kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu na barabara ni changamoto kubwa hasa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Magharibi na Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Ukitaka kuwekeza katika Mikoa ya Kusini, Mikoa ya Magharibi na Mikoa ya Kanda ya Ziwa utakumbana na suala zima la changamoto ya barabara. Gharama zinakuwa ni kubwa sana kwa wageni wetu wanaotembelea hifadhi zetu na maeneo yetu ya utalii hii ni kwa sababu ya changamoto za barabara. Wawekezaji wengi wanashindwa kuwekeza katika sekta ya utalii ni kwa sababu ya changamoto ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia changamoto nyingine kubwa ni ya viwanja vya ndege. Tuna viwanja vya ndege vya kimataifa vya Kilimanjaro, Dar es Salaam, lakini sasa tuna uwanja wa ndege wa Songwe. Uwanja wa ndege wa Songwe ambao tunategemea ndio utakuza utalii wa Kusini hauwezi kufanya kazi peke yake usiposhirikiana na viwanja vidogo kwa mfano kiwanja a Iringa, kiwanja cha Katavi ambacho a ndege zinazokwenda kwenye hifadhi ile ya Katavi zinaweza kutua kule; hatuwezi kukuza utalii wa mikoa hii kama hatuwezi kuimarisha hivi viwanja vya ndege. Nikisema hapa leo gharama ya kutoka Dar es Salaam mpaka kwenye hifadhi ya Ruaha na kurudi ni karibu dola 700, (shilingi 1,400,000).
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni mtalii gani au mwekezaji gani anaweza kuwekeza kwenye utalii kwa gharama zote hizi? Ni mtalii gani wa ndani ambaye anaweza akatoka mfano Mkoa wa Iringa kwenda Hifadhi ya Ruaha kwa kulipa 800,000 kwa usafiri wa gari? Tutakuwa tunaimba utalii wa ndani, tutakuwa tunaimba uwekezaji lakini hatutoweza kuwekeza kama miundombinu hii haitafanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala zima la malazi. Suala la malazi ni changamoto kubwa, niwapongeze wawekezaji wa Mkoa wa Arusha ambao wao wameweza kuwekeza zaidi pia kwenye masuala ya hoteli. Hoteli nyingi zilizopo katika Mkoa wa Arusha zina hadhi za hoteli ya kitalii. Lakini hoteli hizi zinazidiwa wakati wa high season watalii wanalazimika kwenda kulala nchi jirani, wanalala Nairobi ni kwa sababu hoteli hizi hazitoshi, lakini pia hoteli zetu zilizojengwa kwenye mikoa yetu ya Nyanda za Juu Kusini mfano Mikoa ya Iringa, Mbeya, Mikoa ya Magharibi, Mikoa ya Kanda ya Ziwa bado ni changamoto kubwa kwa wageni wanaotembelea maeneo hayo. Kwanza huduma zinazotolewa kwenye hoteli zile ni huduma duni ambazo haziendani na hadhi ya huduma ambazo wageni wetu wanatarajia. (Makofi)
Vilevile ningependa kutoa ushauri kwa Serikali, watoe masharti nafuu kwa wawekezaji hawa mnaotaka kuwekeza katika sekta ya utalii, kuwekeza kwenye tour operators. Kwa mfano mwekezaji anataka kuwekeza Kusini unatofautishaje mwekezaji wa Kusini na mwekezaji wa Kaskazini, kwanza mwekezaji wa Kusini ana changamoto ambazo nimezitaja, vivutio vile viko mbalimbali, barabara ni mbovu, lakini pia mwekezaji huyu hajavutiwa. Wizara haijampa mwekezzaji huyu ya yeye kuwekeza katika mikoa hii ya Kusini. Kwa mfano ukiwekeza katika suala zima la utalii, la tour operator unatakiwa kulipa dola 2,000 na sijui kwa nini ni dola kwa Mtanzania mimi nilitegemea labda watalipa Tanzania shillings lakini analipa dola, dola 2000 kuwekeza tour operator.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu tour operator anahitaji kulipa TRA, anahitaji kulipa SUMATRA malipo yamekuwa ni mengi. Lakini huyu tour operator nitamtofautishaje na tour operator anayekuja kuwekeza Kusini? Wanaokuja kuwekeza Kusini, Mikoa ya Magharibi na Mikoa ya Kanda ya Ziwa wapunguziwe angalau ifike hata dola 1000 ili waweze kuvutiwa kuja kuwekeza katika mikoa ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiboresha maeneo haya ya uwekezaji, mahoteli yetu, tour operator, tunaweza pia tukatoa ajira nyingi sana kwa wazawa ambao wengi wamemaliza vyuo. Kwa mfano Chuo cha Taifa cha Utalii kimetoa wanafunzi wengi wa certificate pamoja na diploma tangu mwaka 2006, lakini wanafunzi hawa hawajaajiriwa, hawana ajira hata kwenye Wizara.
Kwa hiyo, ningeomba pia Waziri anapokuja kuhitimisha hapa atuambie pia ni ajira ngapi zimetoka kwa wanafunzi hawa waliomaliza katika chuo hiki kama ilivyo Mweka na Pasiansi?. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningependa kuongelea suala pia la Maafisa Utalii katika mikoa yetu. Ninaomba Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na TAMISEMI iangalie namna ambavyo itaweza kuajiri Maafisa Utalii kwenye mikoa yetu, wilaya zetu, lakini pia kwenye halmashauri. Hii itasaidia sana kuibua vivutio mbalimbali vilivyoko kwenye mikoa yetu kwa kushirikiana na wataalam. Vilevile itasaidia kuondoa umaskini kwa wananchi wanaozunguka katika maeneo yanayozunguka hifadhi zetu au maeneo yetu ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wanaoishi kwenye maeneo hayo wamekuwa ni maskini kwa sababu hawana namna ya kutumia vile vituo vyao bila miongozo ya hawa maafisa utalii. Ukiangalia suala zima la utalii wa kitamaduni, utalii huu sasa hivi umepotea hauthaminiwi, lakini ukiangalia nchi nyingi zimekuwa zikitumia utalii wa kitamaduni kuweza kunufaisha wananchi wanaozunguka karibu na maeneo ya hifadhi, wamekuwa wakitumia tamaduni zao, wamekuwa wakitumia taaluma zao kwa mfano wengine wamekuwa ni wachoraji na wameweza kufaidika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siungi…

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nichangie Wizara hii ya Mambo ya Nje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua Serikali inawatumiaje Mabalozi waliopo nje ya nchi katika kutangaza nchi yetu kwa maana ya ushiriki katika majukwaa ya kiuchumi. Mfano sekta ya utalii inachangia pato la Taifa kutokana na fedha za kigeni takribani asilimia 25. Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha naomba aniambie wana mpango gani wa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza Tanzania ili kuendana na kasi ya kukua kwa uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya Mabalozi hawajui vizuri nchi na vivutio vilivyopo. Ofisi za Mabalozi hazina wataalam wa utalii ambao wanaweza kuitangaza nchi yetu kupitia Balozi zetu. Naomba Mheshimiwa Waziri anipe majibu wana mpango gani kuwa na Maafisa wa Utalii katika Balozi zetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu ni namna gani wanafunzi wanaosoma nje ya nchi wanapata misaada kupitia Balozi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2017/2018 ni uhuishwaji wa viwanda nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda haviwezi kuwa endelevu kama hakutakuwa na malighafi ambazo kimsingi zinatokana na kilimo. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba bila kuwa na mapinduzi ya kilimo ndoto ya Tanzania ya viwanda haitafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu kilimo chetu bado ni duni sana kuweza kuzalisha malighafi za kulisha viwanda hivyo vinavyokusudiwa. Hivi karibuni nimetembelea Mkoa wa Songwe, wakulima wanapata shida sana kutokana na ukosefu wa pembejeo za kilimo na zile chache zinazotolewa kwa mfumo wa vocha na mawakala zinakuwa za urasimu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali kwa mapendekezo ya Mpango huu wa 2017/2018 iweke bajeti ya kufanya tathmini ya idadi ya wakulima ili pembejeo zinazotolewa ziendane na idadi ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, masoko ya mazao ya wakulima hayaeleweki, naomba Waziri atuambie kwa mpango huu wa 2017/2018 Serikali imejipangaje kufungua masoko ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika. Kumekuwa na changamoto nyingi sana kwenye suala la afya nchini, kwa mfano Hospitali ya Wilaya ya Vwawa inayotegemewa na Mkoa mzima wa Songwe ina upungufu mkubwa wa madawa, Madaktari na vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya ziara kuangalia huduma ya mama na mtoto, wanawake 14,695, sawa na wanawake 15 – 20 kwa siku wanajifungulia hapo. Wagonjwa 150 – 200 wanahudumiwa kama outpatient kila siku katika hospitali ya Wilaya. Huku idadi ya Madaktari wakiwa watatu na uhitaji ni Madaktari 23. Sambamba na watumishi 507 na uhitaji ni watumishi 1,112. Watoto wa umri wa miaka 0 – 28 wanafariki kwa siku na kupelekea idadi yao kuwa 180 kwa takwimu za 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waziri anahitimisha aniambie kwa mpango huu wa 2017/2018 wana mkakati gani wa kupandisha hadhi hospitali ya Wilaya ya Vwawa kuwa hospitali ya mkoa ili kuwa na bajeti ya kutosha kukabiliana na changamoto katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako majengo yaliyoachwa na wakandarasi waliojenga barabara ya Sumbawanga – Tunduma ambayo yapo kilomita tatu kutoka Tunduma Mjini eneo la Chipaka na Serikali ilitoa commitment ya kufanya majengo yale kuwa hospitali ya Wilaya naomba commitment hiyo iwekwe kwenye mpango ili kusaidia kupunguza tatizo la huduma za afya, ukizingatia kwamba Tunduma ni mpakani na watu wanaohitaji huduma ya afya ni wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la Black market. Soko hili lipo ndani ya mpaka wa Zambia na wafanyabiashara wengi, zaidi ya 1000, wa upande wa Tanzania wanafanya biashara zao katika mpaka huo; hii inasababisha ukosefu wa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kufahamu je, katika mpango huu wa 2017/2018, Serikali imeweka utaratibu gani wa kuwarudisha wafanyakazi katika eneo la Tanzania ili kuongeza mapato katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma?

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Binafsi nitoe pole kwa misiba iliyolipata Bunge letu kwa kipindi cha mwaka huu. Kipekee nikushukuru kwa upendo wako kwa Wabunge hata tunapokuwa na matatizo unakuwa mstari wa mbele kutusaidia. Naomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu mahali pema peponi. Mheshimiwa Sitta, Mheshimiwa Hafidh na Mheshimiwa Dr. Elly Macha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuungana na Wabunge wenzangu katika kuangalia changamoto mbalimbali za miundombinu ya maeneo mbalimbali katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na Mkoa wangu wa Songwe ambao ni mkoa mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto za barabara katika Mkoa wa Songwe, mfano, barabara inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Momba inayoanzia Chapwa, kupitia Vijiji vya Nanole, Chiwezi, Msambatu, Chindi, Msagao hadi Chitete. Naomba Waziri anapohitimisha aniambie ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya barabara hii ili kusaidia maendeleo ya Mkoa mpya wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imepitiwa na barabara kuu ya Tanzania kwenda Zambia kwa takribani urefu wa kilometa 50 kati ya eneo la Doma na Mikumi na kwamba barabara hii ilianzishwa kabla ya mwaka 1964 kabla Hifadhi ya Taifa ya Mikumi haijatangazwa. Wakati barabara hii haijawekwa lami, magari yalikuwa machache na yalipita kwa mwendo mdogo. Baada ya barabara kuwekwa lami magari yaliongezeka sambamba na mwendokasi hivyo kusababisha ajali na vifo vingi vya binadamu na wanyamapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto hizo, TANAPA mwaka 1999 waliainisha na kujenga matuta maeneo yenye mapito ya wanyama. Jumla ya matuta 12 yalijengwa na alama za barabarani kuwekwa katika kilometa 50 zilizo za hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizokusanywa na TANROAD mwaka 2012 katika kituo cha Doma zilionesha kuwa kulikuwa na magari 1,750 kwa siku yanayopita katika barabara hii ambayo asilimia 60 yalikuwa ni magari ya mizigo na mabasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aina hii ya magari ndiyo inayosababisha ajali za kuwagonga wanyama. Hifadhi kwa kushirikiana na TAWIRI mwaka 2014 walihesabu na kubaini idadi ya magari imeongezeka na kuwa 1,991 kwa siku. Matokeo ya utafiti 2014 yanaonesha ifikapo 2025 gari
zinazopita hifadhi zitakuwa 4,699 kwa siku. Idadi hiyo ya magari ni kubwa sana kuweza kuimudu kwa siku hivyo, ni lazima tuchukue hatua madhubuti kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua mikakati ya Serikali kwa bajeti hii ya 2017/2018 kuhusu ujenzi wa barabara mbadala ya Melela – Kilosa – Mikumi yenye urefu wa kilometa 141.78 ili kupunguza idadi ya magari yanayopita katika hifadhi na kuokoa uwepo wa Hifadhi ya Mikumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Ahsante.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Afya ni kigezo kimojawapo katika maisha ya mwanadamu. Hivyo basi, sekta ya afya ni muhimu sana katika mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa wa UKIMWI kwa akina mama ambao wamejifungua salama, kumekuwa na uhaba wa dawa kwa akina mama wajawazito na waliojifungua salama. Mfano, mama mjamzito anachukua dawa hospitali ya Vwawa na anaishi Usangu. Baada ya kupata mtoto na mtoto kufikisha miaka miwili mama anatakiwa kurudi kituo chake cha kwanza ili kuendelea na dawa. Ikifika wakati wa kurudi hospitali ya awali mama anaacha kwenda kuchukua dawa kwa sababu mbalimbali. Kwa mfano, umbali wa vituo vya afya vya kuchukulia dawa, gharama za usafiri, majukumu ya malezi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya msingi kwa Wizara ni kwa nini Wizara isiweke mpango wa kutoa dawa kwenye ngazi ya zahanati zilizoko karibu na wananchi ili kuendelea kuokoa nguvukazi hii ya Taifa letu. Mfano, mtu anatoka Ichesa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Vwawa kilometa 45 hadi 50, barabara ya vumbi na usafiri wa bodaboda. Hii inasabishia watumiaji wa dawa kuacha dawa na kuendelea kuwa na madhara yatokanayo na magonjwa nyemelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto za vifaa tiba kwenye hospitali zetu, bado wajawazito wanatakiwa kuwa na vifaa vya kujifungulia. Mfano gloves, code tie inayotumika kufunga kitovu cha mtoto anapozaliwa, pamba na gauze. Je, Waziri anatusaidiaje kwenye suala la vifaa hivi kwa wanawake wanaojifungua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa aina ya folic acid kwa wajawazito bado zimekuwa adimu sana kwenye hospitali zetu, badala ya kutolewa bure mama mjamzito analazimika kununua kwenye maduka ya dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie kuhusiano na upungufu wa Madaktari Bingwa kwenye hospitali zetu za rufaa sambamba na wakalimani wanaotumia lugha za alama kwa walemavu wanaokwenda kutibiwa katika hospitali zetu.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's