Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Mbaraka Kitwana Dau

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie Mpango uliowasilishwa na Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia sote hapa tumeamka salama na tunaendelea na shughuli zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika namna ya kipekee kabisa niwashukuru wapiga kura wa Mafia kwa kuniwezesha kuwa Mbunge kwa kura nyingi sana na leo nimesimama kwa mara ya kwanza katika Bunge lako Tukufu nikichangia Mpango huu. Ninachotaka kuwaambia wananchi wa Mafia, imani huzaaa imani. Wamenipa imani na mimi nitawarejeshea imani. Ahadi yangu kwao, nitawapa utumishi uliotukuka uliopakwa na weledi wa hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wenyewe watakuwa mashahidi, wameshaanza kuona baadhi ya ahadi ambazo niliziweka kwao zimeanza kutekelezeka. Wananchi wa vijiji vya Juwani na Chole wa visiwa vidogo ambavyo hawakuwa na maji kwa muda mrefu, maji yameshaanza kutoka kule. Wananchi wa visiwa vidogo vya Bwejuu na Jibondo maji wataanza kupata baada ya wiki mbili kutoka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali makini na Serikali sikivu ya CCM kwa kuanza na sisi wananchi wa Mafia. Nimeongea na Waziri makini kabisa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi tukiomba watupatie meli ya MV Dar es Salaam ili kuondoa kero ya usafiri baina ya Kilindoni na Nyamisati. Kimsingi Waziri amekubaliana na hilo na naomba niwafahamishe watu wa Mafia kwamba Serikali imekubali kutuletea meli ya MV Dar es Salaam. Hivi sasa mchakato wa masuala ya kitaalam na ya kiutawala unaendelea na meli hiyo itakuwa Mafia ndani ya muda mfupi kutoka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee vilevile kuipongeza Serikali, tuliomba gati na niliongea na Waziri, Mheshimiwa Mbarawa, bahati mbaya hayupo, lakini ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani upo nakuona hapo, tuliomba gati lifanyiwe maboresho kwa kuletewa tishari kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kuwafahamisha wananchi wa Mafia na Bunge lako Tukufu kwamba tishari lile limefika Mafia juzi, taratibu za kuli-position kwenye gati lile zinaanza na usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni utaboreka zaidi.
Naomba ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani unifikishie salamu kwa Mheshimiwa Waziri, bado tuna matatizo upande wa pili wa Nyamisati, kule maboresho bado hayajafanyika. Tunatambua kwamba Mamlaka ya Bandari ilishatenga bajeti kwa ajili ya kufanya maboresho upande wa Nyamisati. Meli hii itakayokuja kama upande wa Nyamisati hakutafanyiwa maboresho itakuwa haina maana yoyote.
Kwa hiyo, nakuomba kwa namna ya kipekee ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani na nikimaliza kuchangia nitakuja hapo kwako nikuelezee in details. Maboresho ya Bandari ya Nyamisati ni muhimu sana katika kuhakikisha meli ile ya MV Dar es Salaam inafanya kazi zake baina na Kilindoni na Nyamisati bila ya matatizo yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee pia nikushukuru ndugu yangu, mzee wangu Mheshimiwa Profesa Muhongo. Nilikuletea concern yetu watu wa Mafia kuhusiana na kusuasua kwa mradi wa REA. Ukachukua hatua na ninayo furaha kukufahamisha kwamba nimeongea na watu wa TANESCO na tumekubaliana kwamba mradi ule utakabidhiwa baada ya mwezi Machi, hivyo basi nakushukuru sana. Pia tulinong‟ona mimi na wewe kuhusu suala la submarine cable kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni…
Mheshimiwa Mwenyekiti, submarine ndiyo solution …
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dau, naomba sana tuendelee kutumia lugha ya Kibunge.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nilikuomba Mheshimiwa Muhongo kwamba ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la umeme Mafia ni kuzamisha submarine cable kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni.
Kimsingi ukaniambia niendelee kukukumbusha. Mimi kwa kuwa wewe ni jirani yangu hapa kila nikifika asubuhi shikamoo yangu ya kwanza ni submarine cables…
MWENYEKITI: Kwa mujibu wa Kanuni ya 60, elekeza maongezi yako kwa Mwenyekiti.
MHE. MBARAKA K. DAU: Submarine cable itakuwa ndiyo salamu yangu ya kwanza ya asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nianze sasa kuchangia Mpango. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Ashatu wameleta Mpango mzuri sana. Mimi naamini madaktari hawa wawili watatuvusha, tuwape ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye ugharamiaji (financing) wa Mpango huu. Mpango uliopita ulipata matatizo makubwa sana kutokana na ukosefu wa fedha. Naamini kwa ari na kasi iliyoanza nayo Serikali ya Awamu ya Tano ambapo ukusanyaji wa mapato umekuwa mkubwa sana sambamba na kubana matumizi ya Serikali, financing ya Mpango huu wa sasa haitakuwa tatizo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, concern yangu ipo kwenye sehemu ya pili ya financing ya Mpango huu ambayo ni sekta binafsi. Sekta binafsi wanakuja kuwekeza lazima sisi wenyewe tuweke mazingira wezeshi kama mlivyosema katika Mpango wenu, kwamba ili watu waje kuwekeza hapa lazima mazingira yawe mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, ninachotaka kusema ni kwamba tuwe waangalifu na hawa wawekezaji wanaokuja. Nitatolea mfano kule Mafia na Mzee wangu Mheshimiwa Lukuvi naomba unisikilize vizuri sana hapa, tuna Kisiwa kinaitwa Shungimbili. Mafia imezungukwa na visiwa vingi tu lakini kimoja kinaitwa Shungimbili. Kisiwa hiki cha Shungimbili kimebinafsishwa au sijui niseme kimeuzwa au sijui niseme kimekodishwa bila ya Serikali ya Wilaya kuwa na habari. Namuuliza Mkurugenzi anasema hana taarifa, namuuliza DC wangu anasema hana taarifa, naomba sana…
MWENYEKITI: Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na usalama na leo tumekutana hapa tukiwa na afya njema ili kuweza kujadili masuala yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Mtukufu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyoiendesha nchi yetu mpaka sasa, kwa ukusanyaji mzuri na uongozi mzuri katika kipindi kifupi alichokua madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani zangu pia nizielekeze kwa ndugu yangu, Komredi, Mheshimiwa Waziri Mwigulu pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Olenasha, kwa kazi nzuri na hotuba nzuri waliyoiwasilisha leo asubuhi hapa. Combination yao ni nzuri sana na tunawategemea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niendelee kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo langu la Mafia kwa kunichagua na kuendelea kuniamini niweze kuwaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Kwa kusisitiza hili, ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba ile x-ray machine na ultrasound machine ambazo niliziahidi katika kampeni yangu, zimeshatoka bandarini na zinaelekea Mafia mwisho wa wiki hii, zitakuwa Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nukta hii, namshukuru sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kuweza kutusaidia kupata vibali muhimu vya TFDA na leo x-ray machine na ultra sound, tayari zinaelekea Mafia mwisho wa wiki hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru pia Taasisi ya MIDEF ambayo ndiyo iliyo-donate mashine hizi kwa Jimbo la Mafia. Na mimi mwenyewe pia nijipongeze kwa ushindi mkubwa nilioupata kwenye uchaguzi na kwenye kesi iliyofunguliwa na mgombea wa chama cha CUF. Nimeshinda, akakata rufaa na nimeshinda tena. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo.
Kwa upande wa Jimbo la Mafia, uchumi wa Jimbo la Mafia umebebwa na uvuvi na utalii. Kwa masikitiko makubwa sana kuna taasisi ya Serikali maarufu kama Marine Park, badala ya kuwa msaada kwa wananchi wa Mafia imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Mafia. Taasisi hii ya Marine Park, ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, naomba sana na utakapohitimisha nitahitaji kusikia kauli kutoka kwako kuhusiana na Marine Park.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wanatudhulumu watu wa Mafia kwenye mgao unaotokana na mapato ya watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 wanachukua Marine Park na asilimia 30 ambapo 10 zinakwenda kwenye Halmashauri na asilimia 20 inakwenda kwa vijiji husika ambavyo watalii wale wanakwenda. Mgao huu siyo sawa ukizingatia maeneo mengine kama Hifadhi ya Wanyamapori ambapo wananchi wa maeneo husika wanapata asilimia 60 na Serikali Kuu inapata asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapokuja kwenye Marine Park, wamekuwa wakitudhulumu wananchi wa Mafia. Tumelisema sana hili! Kila ukiongea nao wanakwambia kwamba hii ni sheria, hii ongea na watu wa Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda sana wakati unahitimisha hotuba yako Mheshimiwa, ndugu yangu rafiki yangu Komredi Mwigulu ulitolee maelezo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea suala la Marine Park, watu wa Marine Park wametoka katika kazi yao ya msingi ya uhifadhi na hivi sasa wamekuwa madalali, wanauza ardhi. Visiwa vitatu vya Mafia vidogo vidogo sasa vimeshauzwa na Marine Park. Visiwa hivyo ni Nyororo, Mbarakuni pamoja na Kisiwa cha Shungimbili. Huu mchakato wa kuuza pengine siyo tatizo kubwa sana, tatizo kubwa sana kwa nini hawataki kufuata taratibu? Huwezi ukauza ardhi au kuibinafsisha bila kuwashirikisha wananchi husika wa vijiji vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, kwa masikitiko makubwa sana, watu wa Marine Park wamevibinafsisha visiwa hivi kwa kutengeneza mihtasari fake kuthibisha kwamba wananchi wameshirikishwa. Ukweli ni kwamba wananchi hawajashirikishwa na nyaraka walizo-forge ninazo hapa, nitakuletea kwako hapo ili uzione na uweze kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mgao usio sawia wa maduhuli yanayotokana na watalii, vilevile pesa zinazotolewa pale kwa mujibu wa maelezo yao wenyewe Marine Park wanasema kwamba Marine Park ya Mafia ndiyo inaendesha Marine Park zote Tanzania. Mapato yanayotoka kule, sehemu kubwa yanaendesha Marine Park nyingine za nchi yote. Kisiwa kama Mafia kidogo chenye uchumi mdogo kwenda kukitwisha mzigo wa kuendesha Marine Park zote zilizopo Tanzania, kwa kweli hili siyo sawa. Hata huu mgao wa asilimia 70 wanautoa baada ya kutoa gharama zote, kwa maana ya gharama za uendeshaji. Hii tunaiona pia siyo sawa. Namwomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, hili nalo aliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tukirudi kwenye suala la uhifadhi wenyewe, Marine Park kazi yao ya uhifadhi yenyewe imewashinda ukianzia Moa, Pwani ya Tanzania mpaka Msimbati kule, mabomu yanapigwa usiku na mchana. Pale Dar es Salaam kuanzia Magogoni pale Ikulu kwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli mpaka Pemba Mnazi, mchana na usiku ni mabomu yanapigwa kama nchi iko kwenye vita. Tunashangaa uhifadhi gani wanaoufanya hawa wa Marine Park. Mheshimiwa Waziri Marine Park ni jipu na ninaomba sana ulitumbue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, mkononi mwangu hapa ninao waraka uliotolewa na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kilimo na Mifugo wakati ule Mheshimiwa John Pombe Magufuli, waraka wa tarehe 12 Agosti, 2008, ukitoa ruhusa kwa wavuvi ambao wamezuiwa wasitumie mitungi ya gesi migongoni mwao wanapokwenda kuvua katika kina kikubwa cha maji. Kina cha mita 50 mtu hawezi kuzamia kwa kuziba pua, ni lazima aende na mtungi wa gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana Marine Park wanawakataza wananchi na wanaendelea kuwakamata. Hivi ninavyozungumza, wapigakura wangu zaidi ya 20 wameswekwa rumande kwa sababu wamevua kwa ya kutumia mitungi ya gesi. Mitungi ya gesi Mheshimiwa Waziri, haiharibu mazingira, inamsaidia mvuvi aweze kwenda kina kikubwa zaidi kwenda kutoa nyavu zake zilizonasa. Haina uhusiano wowote na uharibifu wa mazingira, hata ndugu yangu Makamba anaweza akathibitisha hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo cha mwani, Marine Park...
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sera ya kuwekeza kwenye viwanda, nashauri tujikite zaidi kwenye viwanda vidogo vidogo vyenye kuongeza thamani ya mazao yetu badala ya viwanda vya kuzalisha bidhaa kamili kama hatuna “comparative advantage” ya bidhaa za aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali itafute mwekezaji wa Kiwanda cha kusindika samaki katika Kisiwa cha Mafia sambamba na kupata meli za uvuvi zenye zana za kisasa zenye uwezo wa kuvua katika bahari ya kina kirefu. Mafia ipo karibu na mkondo wenye kina kirefu kunapopatikana samaki wengi na wakubwa wa aina mbalimbali kama Jodari (Tuna) nguva (King fish) samsuri (Marley) na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa viwanda vya sukari umekuwa mdogo na hautoshelezi kulisha soko la nchi nzima. Ipo hoja na haja ya kuvutia mwekezaji kuwekeza katika bonde la Mto Rufiji ili kuondokana na tatizo la kuagiza sukari kila mwaka. Naishauri Serikali pia katika kipindi hiki kuelekea kujitosheleza kama uzalishaji wa ndani wa sukari, Serikali itoe vibali kwa kuagiza sukari kwa viwanda vyenyewe, mfano, Mtibwa, Kagera na kahalika.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kuwa hapa wote tukiwa salama na afya na kuweza kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa nimshukuru sana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ndugu yangu Mheshimiwa Makame Mbarawa na Naibu wake rafiki yangu Mheshimiwa Ngonyani kwa hotuba nzuri sana ambayo kwa kiasi kikubwa sana imejikita katika kuondoa matatizo na kero mbalimbali za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye uchangiaji. Kuna dhana hii ambayo ilikuwa ikizungumzwa sana ya maeneo ya pembezoni, maeneo yaliyosahaulika. Kwa bahati mbaya sana, kila inapojadiliwa maeneo ya pembezoni na yaliyosahaulika kisiwa cha Mafia kinasahaulika. Wananchi wa Kisiwa cha Mafia wana kila aina ya sababu na sifa zote za kuitwa watu ambao ni wa maeneo ya pembezoni na waliosahaulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo mtu akisafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza kuanzia saa 12 asubuhi akifika saa 3 au 4 lakini mwingine akaondoka na boti Dar es Salaam pale akielekea Mafia basi yule wa Mwanza atafika wa Mafia hajafika. Nayasema haya kwa sababu adha ya kusafiri kwa boti kutoka Dar es Salaam mpaka unafika Mafia inaweza ikachukua siku moja mpaka mbili na ndiyo maana kwa makusudi kabisa tukaamua wananchi wa Mafia wanapotaka kusafiri wanakwenda Kusini kidogo kwa kutumia barabara ya Kilwa mpaka maeneo ya Mkuranga, wengine wanakata kushoto wanakwenda Kisiju. Sasa matatizo yanaanza pale, barabara ya Kisiju - Mkuranga kilometa kama 46 ni ya vumbi, ni mbaya sana na imekuwa ikipigiwa kelele sana lakini bado haijashughulikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bandari ya Kisiju ni kama economic hub ya Kisiwa cha Mafia kwani mazao yote ya nazi na yanayotokana na bahari yanapitia bandari ya Kisiju lakini tatizo la uharibifu wa barabara ile ya Mkuranga – Kisiju ni kubwa. Nimeangalia kwenye Kitabu cha Mheshimiwa, nikakisoma mara mbili mpaka tatu sikuiona barabara ya Mkuranga - Kisiju ambayo ni kilometa 46. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha basi alitolee maelezo suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namna ya pili ambayo abiria wengi wanaitumia kufika kisiwa cha Mafia ni kwenda mpaka Bungu, Rufiji wanakata kushoto wanakwenda mpaka kwenye bandari ya Nyamisati. Baina ya Bungu na Nyamisati ni kama kilometa 41, pale napo pia barabara ni kama hakuna. Ina mashimo na kipindi kama hiki cha mvua inakuwa kama imekatika. Wananchi wa Mafia wanaposafiri na boti kutoka Kilindoni wakafika Nyamisati wana kazi nyingine pale ya kudandia magari mbalimbali na wengine bodaboda ili wafike Bungu na hatimaye kuja Dar es Salaam. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha ulielezee hilo pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Kisiwani Kwenyewe Mafia, kuna barabara kutoka Kilindoni - Rasi Mkumbi kilometa 55. Mkononi kwangu hapa nina Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndiyo tuliyoinadi kwa wananchi, ndani ya Ilani hii inasema wazi kabisa, Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano ijayo tutajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kilindoni - Rasi Mkumbi (Bweni). Hata hivyo, nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri sikuiona barabara hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana atakapokuja ku-wind up alitolee maelezo na hilo nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mafia kuna barabara inaitwa Airport Access Road kilometa 14 inatoka Kilindoni inakwenda mpaka Utende ambayo imetengenezwa kwa kiwango cha lami. Kwa masikitiko makubwa sana, barabara ile haijakabidhiwa huu unafika mwaka mmoja toka imekamilika. Naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri, itakapofika wakati mkandarasi anataka kuikabidhi barabara ile Serikali msikubali kuipokea kwani ina mashimo mwanzo mpaka mwisho na mpaka leo haijazinduliwa. Barabara ina matatizo, kuna jokes zinaendelea kule Mafia wanasema kama gari ikipata pancha ukipiga jeki badala ya ile gari kwenda juu basi jeki ndiyo inatitia chini kama vile umepiga jeki kwenye matope. Kubwa zaidi wenyewe wanaiita barabara ya Big G maana yake ina mashimo mashimo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nizungumzie kuhusu Bandari ya Nyamisati ambayo na yenyewe pia imo katika kitabu hiki cha Ilani ya CCM. Jana kwa bahati nilipata fursa ya kuongea na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) akanithibitishia kwamba bandari ile itajengwa lakini pesa zilizotengwa zilikuwa ni kidogo na walipoenda kufungua zabuni wakakuta ame-quote shilingi bilioni nane na wao Mamlaka ya Bandari hawana uwezo wa kulipia fedha hizo. Akanihakikishia Mkurugenzi Mkuu kwamba wamenunua dredger (mashine la kuchimbia na kuongeza kina kwenye bandari), kwa hiyo wamesema kazi hiyo wataifanya wao wenyewe.
Mheshimiwa Waziri naomba wakati utakapokuja ku-wind up uniambie na uwaambie wananchi wa Mafia ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya Bandari ya Nyamisati kazi ambayo wataifanya wenyewe Mamlaka ya Bandari? Vinginevyo kwa mara ya kwanza mimi sijawahi kutoa shilingi hapa lakini leo kama nisiposikia habari ya Bandari ya Nyamisati kiasi gani kimetengwa na mimi nitaingia kwenye record hapa ya kuzuia shilingi au pengine hata noti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mafia. Sasa hivi tuna kilometa 1.5 ili ndege kubwa ziweze kutua tunahitaji runway yenye angalau kilometa 2.5 ili watalii waweze kuja moja kwa moja katika Kisiwa cha Mafia. Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri iliyobaki pale ni kilometa moja tu, naomba sana mtupatie hiyo kilometa moja ili watalii waweze kuja Mafia na tuweze kunufaika na biashara ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MV Dar es Salaam…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dau nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, shukurani kwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wa Wizara kwa hotuba nzuri yenye kuleta matuamini kwa Watanzania. Mradi wa umeme wa REA kwa Kisiwa cha Mafia umebakiza vijiji na maeneo 10 kukamilika, navyo ni vijiji vya Gonge, Jojo, Mariam, Bani, Jibondu, Juani, Chole, Dongo na Maeneo ya Tumbuju, Bwejuu na Tongani. Ombi langu kwa Wizara ni vijiji na maeneo husika viingizwe kwenye mradi wa REA Phase III.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni uzalishaji wa umeme kwa sababu umeme Mafia unatokana na chanzo cha mafuta yanayoendesha majenereta yaliyopo. Kutokana na gharama kubwa ya ununuzi wa mafuta na matatizo ya usafiri wa mafuta hayo kwa njia ya bahari, ombi letu wananchi wa Mafia ni kwamba, Serikali sasa iunganishe na umeme wa SONGAS kupitia kupitishwa kwa submarine cable kutokea Nyamisati kwenda Kilindini takriban kilomita 50 ili kuondokana na adha ya kusafirisha mafuta mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utafiti wa mafuta na gesi, katika Kisiwa cha Mafia ni jambo linalofanywa mara kwa mara. Kwa habati mbaya sana wananchi wa Mafia wamekuwa hawapewi taarifa tunaomba Wizara na Waziri wakati atakapokuwa anajibu awaeleze wananchi wa Mafia kama mafuta au gesi vimegundulika Mafia au hapana ili kuondoa hali ya sintofahamu kwa wananchi wa Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kwenye ugunduzi wa gesi hasa maeneo ya kina kirefu cha bahari yaani off share maeneo ya Kusini mwa Tanzania. Mpakani mwa Wilaya ya Kilwa na Mafia, katikati ya bahari kuna visima viwili ambavyo kimpaka kimo katika Wilaya ya Mafia, lakini kutokana na matatizo ya usafiri shughuli za uchimbaji na utafiti zimekuwa zikifanyika kutokea Wilaya ya Kilwa.
Swali je, wananchi wa Mafia wananufaika vipi na visima hivi ambavyo kimipaka vipo Mafia lakini shughuli za uchimbaji zinafanyika Kilwa?
Suala lingine ni bomba jipya la gesi kutoka Kusini kuja Dar es Salaam, ujenzi umekamilika kwa asilimia 100. Swali, je, ni lini bomba litaanza kusafirisha gesi kutoka Kusini kwa matumizi ya kibiashara? Swali lingine, ni lini umeme ghafi utachakatwa na kuweza kutumika kwa matumizi ya majumbani?
Mheshimiwa Naibu Spika, natanguliza shukurani na naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hotuba hizi mbili alizozileta Waziri wa Fedha na Mipango, Hali ya Uchumi na Bajeti ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na salama, leo tumekutana hapa kujadili mambo yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru sana Dkt. Phillip Mpango, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kutuletea bajeti ambayo nimeiita ni bajeti ya kihistoria. Haijapata kutokea katika historia ya nchi yetu Bajeti ya Maendeleo ikawa asilimia 40 ya bajeti yote ya Taifa. Kwa kweli pongezi nyingi sana zimwendee Mtukufu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa dhamira hii ya dhati ya kuwaondoa wananchi wa Tanzania katika lindi la umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napata faraja kubwa sana, nilikuwa najaribu kufanya tathmini ndogo hapa, nikagundua miundombinu peke yake imetengewa asilimia 25.4, elimu asilimia 22 na bajeti ya afya ni asilimia 9.2. Hapa kwenye bajeti ya Wizara ya Afya, Abuja Declaration inatutaka tutenge bajeti ya asilimia15. Wanasema Rome haikujengwa siku moja, kidogo kidogo ndani ya bajeti mbili, tatu zijazo tunamwomba sana Dkt. Mpango Azimio hili la Abuja la asilimia 15 katika bajeti ya Wizara ya Afya lifikiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze moja kwa moja kwenye kuchangia bajeti. Ushiriki wa sekta binafsi na sekta ya umma katika miradi ya pamoja kimekuwa ni kilio cha siku nyingi sana, tumelizungumza sana hili na ninayo furaha na nahisi faraja kubwa sana, kupitia kwenye bajeti hii nimeuona ushiriki huu wa sekta binafsi na sekta ya umma kwa maana ya PPP, tatizo langu ni dogo tu!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha basi atuletee na mchanganuo, kwa sababu tumeona tu humu miradi, mimi naiona kama ni blanket imewekwa humu, miradi kama ya barabara ile ya Chalinze – Dar es Salaam express way, mradi wa Reli ya Kati, miradi hii ya umeme ya phase III kule Kinyerezi ipo tu kwa ujumla ujumla!
Mheshimiwa Naibu Spika, tungeomba sana hebu watupatie break down na frame work, timeline kwamba miradi hii tunafanya labda tutaanza na mradi wa reli ya kati standard gauge, labda tarehe fulani mpaka itakapofikia mwaka wa fedha miaka miwili, mitatu, mbele mradi huu utakuwa umekwisha; labda mradi wa bandari ya Bagamoyo utaanza tarehe fulani mwaka wa fedha fulani na utakwisha hivi, ili tupate kwa ujumla wake haya mambo yanakwendaje; lakini kutujazia tu miradi ya jumla bila ya kutupa timeline inatusumbua sana, kwa sababu tunajenga matumaini, lakini ndani yake hatujui miradi hii itakuja lini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye suala la utalii. Nilizungumza hapa kwenye Wizara ya Maliasili na Utaii ilipoleta bajeti yake na nashukuru sana Mheshimiwa Waziri namwona pale na namwomba Mheshimiwa Waziri anitegee sikio. Takwimu zinatuambia kwa miaka miwili kati ya mwaka wa fedha uliopita na mwingine wa nyuma yake, utalii wetu umeshuka kwa karibu watalii laki moja, sasa sitaki kujielekeza kwenye sababu gani zimepelekea watalii kupungua. Nataka nijielekeze kwenye namna ambavyo tunaweza tukatangaza utalii wetu ili tupate watalii wengi na kuhakikisha kwamba tunapata mapato katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumza utalii mara nyingi tunajikita kwenye vitu viwili tu, Mlima Kilimanjaro na Mbuga, wakati Tanzania na Naibu Waziri wakati anajibu swali hapa juzi alisema wazi kwamba Tanzania ni ya pili duniani kwa vivutio vya kitalii, sasa hivi vivutio vingine vitatangazwa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Kisiwa cha Mafia na nilizungumza hapa wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwamba kule Mafia tuna samaki anaitwa ‗Papa Potwe‘, huyu samaki ni samaki wa ajabu, anatabia kama za dolphin, ni samaki rafiki, watalii wanapenda sana kuja kuogelea naye. Je, ni wangapi wanajua habari za samaki huyu ‗Papa Potwe‘?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunaomba sana mtengeneze package ya vivutio vyote ili muweze kwenda kuviuza huko nje, kwa sababu Halmashauri hatuna uwezo wa kumtangaza ‗Papa Potwe‘! Ni lazima tusaidiwe na nguvu ya Serikali. Kwa hiyo naomba sana tutanue wigo katika utalii wetu katika kuutangaza na kuhakikisha kwamba tunapata mapato mengi ili kuendeleza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango, hili nililizungumza kwako kama mara moja au mara mbili hivi, masikitiko yangu makubwa kuona kwamba Kisiwa cha Mafia hakikuingizwa katika zile flagship project kwa ajili ya Mpango wa Pili wa Maendeleo, kwa maksudi kabisa! Mimi nilikuwa naiona Mafia kama ndiyo Zanzibar mpya! Tuifungue kiutalii Mafia ili watalii waje.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale tuna matatizo mengi na tunahitaji investment ndogo sana kuifungua Mafia. Barabara inayotoka Kilindoni mpaka Rasimkumbi kilometa 55 ikitengenezwa hiyo ikitiwa lami pamoja na bandari yetu na ndugu yangu Ngonyani pale ananisikia, kuhusu bandari ya Nyamisati, Mamlaka ya Bandari imetenga nafahamu kwamba bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ile, ikikamilishwa sambamba na bandari ya Kilindoni na kuongezwa kwa runway, airport ya Mafia…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Maliasili na Utalii. Mheshimiwa Waziri nianze kwa kuunga mkono hoja yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili suala la utalii ni suala ambalo lipo interconnected, tunazungumzia utalii ambao uko under utilized. Utalii ili uwe utalii, utalii ili uweze kufanya kazi sawasawa ni lazima sekta nyingine saidizi ziweze kusukuma twenda sambamba, kwa mfano, suala la miundombinu kuanzia barabara na maeneo mengine ya usafiri, hata huduma za viwanja vya ndege. Matatizo yetu ya usafiri na utalii yanaanzia pale airport ya Dar es Salaam na Kilimanjaro. Mtalii anakuja anakutana na mazingira ambayo ni very unfriendly, hawezi kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtalii anakaa anasubiri wale wanaochukua visa on arrival anakaa masaa matatu, mwingine anakaa kwenye foleni pale airport yenyewe, kuna joto, air condition hazifanyi kazi anaanza ku-experience matatizo akiwa pale kiwanja cha ndege. Sasa tunapozungumzia kukuza utalii tuangalie na aspect kama hizi tuhakikishe kwamba vituo vyetu vya airport na maeneo mengine ambayo watalii wanakuja wanaanza ku-experience mambo mazuri, pamoja na vitanda kule kwenye hoteli zetu ziwe za kutosha na miundombinu mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii dhana ya utalii tumejikita zaidi kuangalia mbuga pamoja na Mlima Kilimanjaro na vivutio kama hivyo. Lakini dhana ya utalii ni pana zaidi ya Mlima wa Kilimanjaro na mbuga. Kwa mfano, mimi natokea kisiwani Mafia, Kisiwa cha Mafia ni kisiwa tajiri sana kwa utalii, lakini mazingira ili uingie Mafia ni magumu kweli kuanzia usafiri kwa maana usafiri wa bahari na usafiri wa ndege. Lakini kubwa zaidi ni namna gani Serikali inatangaza utalii katika maeneo mbalimbali ya vivutio hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia tuna samaki anaitwa a whale shark au kwa jina lingine la Kiswahili anaitwa Potwe, samaki huyu ana tabia kama za dolphin, ni samaki friendly anaweza akaogelea na watalii, hana matatizo. Lakini dunia nzima samaki huyu anapatikana Australia na Mafia tu. Ni wangapi miongoni mwa Watanzania tunalijua hilo kwa utalii wa ndani peke yake ikilinganishwa na utalii wa nje? Kwa hiyo tunahitaji kwanza kutangaza na kuwekeza katika miundombinu ili vitu hivi vinapokuwa connected pamoja, basi utalii wetu utasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia kuna vivutio mbalimbali kama scuba diving, sport fishing na utalii wa kwenda kuangalia papa Potwe, lakini bado Serikali haijatia mkazo kuweza kutusaidia kutangaza utalii huu. Kikubwa zaidi Mheshimiwa Waziri pale kisiwani Mafia hatuna hata Afisa wa Utalii utawezaje kukuza utalii kwenye destination muhimu kama ya Mafia bila ya kuwa na Afisa wa Utalii wa Wilaya? Tumelizungumza hili sana, tumeandika barua lakini mpaka leo hatujapata Afisa wa Utalii.
MWENYEKITI: Ahsante muda wako ulikuwa ni dakika tano tu.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuanza kwa kuunga mkono hoja. Pili, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri Profesa Jumanne Maghembe na Naibu wake Engineer Ramo Makani kwa hotuba nzuri na yenye kuleta matumaini kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Serikali sikivu ya CCM kutanua wigo wa vivutio vya utalii kwa muda mrefu kumejengeka dhana kuwa utalii maana yake ni mbuga za wanyama na maeneo ya fukwe peke yake. Dhana hii si sahihi, kwani utalii una wigo mpana zaidi. Kwa mfano katika jimbo langu la Mafia (Kisiwa) kuna samaki aina ya papa mkubwa sana anaitwa Mhaleshark (Potwe) ni one of the species of shark, papa huyu ni adimu sana duniani, kwa sasa anapatikana Australia na Mafia tu dunia nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Australia ni ghrama kubwa kwa mtalii kwenda kumuona samaki huyo na moja ya sifa za whaleshark ni papa rafiki ana tabia zinazofanana na dolphin (pombuwe) mtalii anaweza kuogolea naye bila ya kupata madhara yoyote ile. Hivyo mtalii Australia anatumia gharama kubwa ikiwa ni pamoja na kukodi helikopta kwenda maeneo ya mbali sana kuogolea na papa. Lakini kwa upande wa Mafia papa huyu anaonekana umbali usiozidi mita 300 kutoka bandari kuu ya Kilindini Mafia. Ombi letu wana Mafia Serikali kupitia Bodi ya Utalii itusaidie kuutangazia ulimwengu upatikanaji na papa huyo ili kuongeza watalii wengi Mafia sambamba na maboresho ya hoteli zetu za kitalii na miundombinu ya kuingia na kutoka Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uvunaji wa mikoko katika Kisiwa cha Mafia mwekezaji Tanspesca amewekeza kiwanda cha kamba katika kijiji cha Jimbo na kupewa kibali na Wizara ya Utalii kukata baadhi ya mikoko. Tunaiomba Wizara sehemu ya mapato yatokanayo na kukatwe kwa mikoko hiyo ibaki katika Halmashauri ili kuweza kusaidia shughuli za uhifadhi katika Kisiwa cha Mafia ikiwemo kupanda mikoko mingine kufidia ile iliyokatawa.
Suala lingine ni kukosekana kwa Afisa Utalii katika Wilaya ya Mafia. Pamoja na potential kubwa ya utalii katika Wilaya ya Mafia bado mpaka sasa hatuna Afisa wa Utalii wa kuratibu shughuli za utalii kisiwani Mafia, tunaomba Wizara kulifanyia kazi jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine nawashukuru Waziri na timu yake yote na naunga mkono hoja. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mahiga, Naibu wake na timu nzima ya Wasaidizi wao katika Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia hoja kwa kuelezea masikitiko yangu ya utoaji wa Visa katika Balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia tunataraji Serikali sasa imefika wakati tuanzishe utaratibu wa kutoa Visa online, utaratibu huu sasa wa watu kutakiwa waende wenyewe moja kwa moja ni wenye usumbufu na umepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Wizara ione umuhimu pia wa kufungua ofisi za ubalozi wa Tanzania Korea ya Kusini, kule kuna potential kubwa ya kunufaika na fursa za teknolojia na watalii kutembelea nchi yetu. Pia Balozi zetu kutumika vizuri kwa kutangaza Tanzania kiutalii na fursa nyingine za kibiashara ili nchi yetu inufaike na uwepo wa Balozi hizo badala ya utaratibu wa sasa wa kutoa Visa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia ione umuhimu wa kuongeza kasi ya kujenga au kununua majengo kwa ajili ya Balozi zetu wenyewe, baada ya miaka 55 ya uhuru badala ya kuendelea kupanga wakati nchi nyingine ndogo kama Eritrea zimejenga nyumba zao wenyewe. Umefika wakati sasa Serikali iongeze kasi ya ujenzi au ununuzi wa majengo yetu wenyewe kwenye Balozi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa hii ili nami nipate kuchangia Hotuba za Bajeti mbili hizi, Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na afya njema. Nielekeze pongezi zangu kwa Mheshimiwa Waziri, George Simbachawene pamoja na dada yangu, Mheshimwa Waziri, Angella Kairuki kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, teknolojia inakuwa kwa kasi sana siku hizi. Leo tumeshuhudia maelezo hapa mtu anamaliza semester mbili ndani ya miezi minne, habari kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo nimefunga, nimefunga kwa maana nina swaumu au nimejizuia kula. Nimefanya hivyo kwa makusudi tu ili nimwombe Mwenyezi Mungu aniongoze katika haya nitakayoyazungumza leo niseme iliyo kweli, basi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu ambacho nakiamini cha Quran, Sura ya 33, Aya ya 70 baada ya audhubillah mina shaitwan rajim, Mwenyezi Mungu anasema Bismillah Rahman Rahim; ya ayuha ladhiina aamanuh, takkullah wakulu kaulan sadida. Hii ni Aya ya Mwenyezi
Mungu. Tafsiri yake; Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu, muabuduni Mwenyezi Mungu na semeni kauli zilizo za kweli’”
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mwenyezi Mungu aniongeze niseme ile iliyo ya kweli. Wilaya ya Mafia, Hospitali ya Wilaya ya Mafia ambayo mimi ni Mbunge wao haina huduma ya X-ray takribani miaka minne sasa. Nilipokuwa najinadi niliwaahidi wananchi wa Mafia kwamba
nikipata fursa hii nitajitahidi kushirikiana na watu mbalimbali Hospitali ya Mafia iwe na X-ray mpya kabisa. Nimetimiza, true to my words, nimetimiza ahadi hiyo, mwezi wa Nne mwaka wa jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa masikitiko makubwa sana huu ni mwezi wa Nne mwaka 2017. Mwezi wa Nne mwaka 2016, X-ray machine ile mpya imefika Mafia na katika nukta hii kwa namna ya kipekee kabisa ningeomba nitambue msaada mkubwa sana aliyeutoa mama yetu kipenzi, Mheshimiwa Salma Kikwete alipokuja Mafia. Sina uhakika kama kanuni zinaruhusu Mbunge anayeongea ampigie makofi Mbunge aliyekaa, lakini naomba Bunge tumpe makofi makubwa sana Mheshimiwa mama Salma.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya X-ray ile kufika Mafia zikaanza figisufigisu. Mtu wa kwanza; na bahati mbaya simwoni hapa; Mheshimiwa Waziri wa Afya; akatuambia kwamba hamruhusiwi kuifunga kwa sababu tuna mkataba na Kampuni inaitwa Philips na kampuni hii ndiyo pekee
inayoruhusiwa kufanya ukarabati na matengenezo ya ile Xray ya zamani. X-ray ya zamani ni chakavu, ni ya teknolojia ya miaka ya 1970, ukiitengeneza inaharibika. Sasa leo wanasema kuna mkataba na Philips, mpaka leo umefika sasa mwaka mmoja X-ray ile bado ipo kwenye stoo, nawauliza wahusika wanatuambia mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mafia ni kisiwa, huna namna kusema kwamba labda mgonjwa utamhamishia hospitali ya jirani, sasa wagonjwa wetu sisi referral hospital yetu lazima umpandishe kwenye boti kwa masaa tano kwenda, referral hospital Temeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa huko wakati wa Pasaka, tumepeleka wagonjwa wawili Hospitali ya Temeke, tunafika Temeke na kwenyewe nako tunaambiwa X-ray ni mbovu kwa zaidi ya mwezi mmoja, haohao Philips. Tunawauliza wahusika wanasema mkataba na Philips umekwisha toka mwaka wa jana. Mafia tunazuiwa tusifunge kwa sababu kuna mkataba na Philips, Temeke wanasema X-ray mbovu Philips mkataba umekwisha, tushike lipi? Hili la Temeke watalizungumza wenyewe akina Mheshimiwa Mangungu na Mheshimiwa Mariam Kisangi na ndugu yangu
Mheshimiwa Mtolea lakini mimi najikita kwenye Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika…
T A A R I F A...
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba naipokea Taarifa ya Mheshimiwa Waziri kwa tahadhari kubwa sana. Kwanza hajanipa time frame, kwa sababu hili jambo limekuwa likienda kwa danadana kwa muda mrefu sana. Hicho chumba ambacho wamekitoa mwanzo walisema sisi wenyewe tujenge halafu tuhamishie ile mashine mpya kule. Midhali yeye amesema leo kwamba
wametupatia chumba hicho; mimi nafahamu kule hatuna chumba cha ziada; lakini kama ataweza kutupatia kingine cha kujenga haraka kwa hizo milioni 50, tutashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niliache hili suala kwa sababu nilikuwa nilielezee kwa upana zaidi. Niingie kwenye suala la pili. Kwenye ukurasa wa 11 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia migogoro ya mipaka baina ya wilaya, mikoa, vijiji na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule Mafia mipaka yetu ni bahari, hakuna namna nyingine ya kupakana na kijiji cha karibu, tunaopakana nao karibu ni ndugu yangu Bwege kule upande wa Kilwa. Tungeomba sana mipaka ya bahari ije iwekwe, kwa sababu kule mafia kuna exploration za mafuta zinafanyika, kwa kiasi kikubwa sana zimo ndani ya eneo la Mafia lakini kutokana na logistics yale makampuni yanafanya
wakitokea Kilwa. Sasa matokeo yake chochote kinachopatikana kinaonekana ni sehemu ya Kilwa wakati kimipaka, kihalisia ile ni sehemu ya Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaomba sana wataalam watakapokuja, sijui wanatumia vitu gani vya kisayansi ili kutofautisha mipaka kwenye bahari lakini waje watuoneshe. Kuna kisiwa kimoja kinaitwa Kisiwa cha Ukuza, kisiwa hiki ni sehemu ya Mafia, lakini shughuli zote za kijamii zinafanyika kutokea Kilwa, tungeomba sana Mheshimiwa Waziri hilo nalo atusaidie kutupatia ufafanuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati; tumeomba zahanati…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dau, naambiwa muda wako umekwisha.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa pongeza nyingi kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, Mheshimiwa January Yusuf Makamba na Naibu wake Mheshimiwa Luhaga Mpina
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuelezea ari kubwa ya kimazingira inayokikabili Kisiwa cha Mafia na visiwa vidogo vidogo vinavyoizunguka Mafia. Mabadiliko ya tabia nchi kwa kiasi kikubwa vinatishia kuviondoa kabisa kwenye uso wa dunia visiwa vya Bwejuu, Jibondo, Chole na Juani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la kina cha bahari limepelekea kiasi kikubwa cha ardhi ya visiwa hivyo kumeguka. Kwa Muktadhi huu natarajia Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hoja yake aje atueleze wananchi wa Mafia hatua ambazo Serikali inachukua katika kuokoa visiwa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia ni Kisiwa chenye vyanzo vichache vya maji lakini kutokana na kukua kwa shughuli za kijamii vyanzo hivi vimeanza kuvamiwa na mvuto hali hii inatishia upatikanaji wa maji safi na salama, nichukue fursa hii kwa namna ya kipekee kumwomba Mheshimiwa Waziri au Naibu wake kuja kutembelea Mafia ili kujionea hali ilivyo kimazingira .
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchafu unaotupwa katika Bahari yetu ya Hindi kwa kiasi unatokana na mifuko ya Plastic (maarufu kama mifuko ya rambo). Kwa namna ya kipekee kabisa napenda kuomba Serikali yangu Tukufu kupiga marufuku matumizi ya mfuko na vifungashio vya plastic
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusoma Jarida moja la uchunguzi la Kimataifa, likitoa Matokeo ya Uchunguzi ya kuonyesha kuwa kama hali ya utupaji taka baharini ilivyo sasa ikiendelea vivi hivi ifikapo mwaka 2050 ndani ya bahari kutakuwa na takataka nyingi (hususan) mifuko ya plastic kuliko idadi ya samaki. Hivyo, ipo haja sasa ya kupiga marufuku mifuko ya plastic.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukataji miti kwa madhumuni ya kuchoma mkaa, sasa ni janga la Kitaifa. Naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua kupiga marufuku uchomaji na usafirishaji wa mkaa. Niiombe Serikali kupunguza bei ya gesi ili wananchi wengi waweze kuhama kwenye kutumia mkaa na kutumia gesi asilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niwatakie Watanzania wote kwa kusherehekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Sheria na Katiba Palamagamba Kabudi. Nianze na hali za Mahakama zetu nchini hususan Mahakama za Mwanzo. Hali za majengo, watumishi na vitendea kazi ni mbaya sana. Katika Wilaya ya Mafia tuna Mahakama ya Mwanzo moja tu na imechakaa na haina watumishi wa kutosha. Wananchi wa Mafia wanalazimika kusafiri masafa marefu kwenda kufuata huduma za Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuiomba Serikali ituongezee Mahakama za Mwanzo angalau mbili katika maeneo ya Utende na Vunjanazi sambamba na kuimarisha vitendea kazi na kuongeza watumishi wa Mahakama ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haki ya dhamana kuu mahabusu kwenye rumande zetu kuna mahabusu wengi wanashikiliwa katika mahabusu zetu wakati wapo wenye kukidhi vigezo vya kumchukulia dhamana. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hoja alitolee ufafanuzi hili jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo umuhimu wa Serikali kuongeza bajeti ya Wizara hii ili kuhakikisha suala la utoaji wa haki nchini linafanyika kwa weledi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba kuunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakukushuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumpa pongezi kubwa sana mtoa hoja, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa na timu yake yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nielekeze pia pongeze zangu kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zake thabiti na za dhati katika kuhakikisha kwamba analifufua Shirika letu la Simu la TTCL, imewekwa pale management ya vijana, management nzuri kabisa. Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, muasaidie sana hawa katika kuwaongezea mtaji ili waweze ku-compete vizuri katika soko hili ambalo lina ushindani mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nianze kujielekeza katika katika kuchangia hotuba hii. Katika hiki kitabu, ukurasa wa 49 na 50 unazungumzia ujenzi na ukarabati wa vivuko mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mafia, sisi kule hatuna namna yoyote, lazima tupate boti au meli ya aina yoyote ili kututoa kwenye kisiwa kikubwa na kutuleta huku sehemu ya bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mwaka 2016 wakati nachangia hotuba hii, nilimuomba Mheshimiwa Waziri, naye anakumbuka kwamba sisi watu wa Mafia tuna matatizo sana ya usafiri wa kuingia na kutoka Mafia. Akatuahidi kwamba ile iliyokuwa MV Dar es Salaam, ambayo ilikuwa imeegeshwa pale, haina shughuli yoyote, tulipoiomba akatukubalia, lakini akasema ina matatizo kidogo ya kimkataba na ya kiutaalam; wakishayamaliza watatuletea Mafia iweze kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumesikia tangazo, mwenye mamlaka ameichukua ile meli, amewapelekea watu wa Jeshi, hatuna tatizo na hilo. Tatizo letu ni kwamba je, Mheshimiwa Waziri baada ya kutuondolea ile MV Dar es Salaam, katika hotuba yako, nimeisoma na kuirudia hapa kwenye maeneo ya vivuko hivi na ferry mbalimbali, hakuna mkakati wowote wa kuondoa tatizo la usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni katika kisiwa cha Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwa sababu naye anatokea kisiwani vilevile, baadhi ya maeneo mengine yamepangiwa kwa alternative route, wengine wanaona kama vile kuzunguka; mnawajengea vivuko wafupishe safari zao, lakini sisi hatuna namna, lazima tupande boti. Sasa hatusemi kwamba maeneo mengine wasipelekewe vivuko, lakini haya maeneo ambayo yana alternative route japokuwa ya kuzunguka, yasubiri kwanza mtupe kipaumbele sisi ambao hatuna namna yoyote, lazima tuvuke maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa majibu ya kusema kwamba jaribuni kuwashawishi private sector waje wasaidie, tumefanya sana na Mheshimiwa Waziri ni shahidi, tumeongea na Bakhresa, tumeongea na Zacharia, bado wanasitasita kuleta usafiri baina ya Kilindoni na Nyamisati. Sasa hili moja kwa moja ni jukumu la Serikali sasa, mtuletee huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenye kiti chako hapo, uniandike jina langu kabisa, nitazuia shilingi mpaka nipate majibu, ni lini Serikali itakuja na mkakati thabiti kabisa kuhakikisha kwamba inapatikana meli au boti ya kisasa ili kuondoa tatizo la usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni Mafia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, gati la Nyamisati. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, walituahidi mwaka 2016 hapa wametenga shilingi bilioni 2.5 na kweli zimekuja tumeona mkakati unaanza pale, wataalamu wapo, utafiti wa udongo umeshaanza na ujenzi na tenda imetangazwa wiki iliyopita na ujenzi utaanza hivi karibuni. Tunaipongeza sana Serikali na tunashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa gati lile utachukua mwaka mmoja kukamilika. Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, wananchi bado wanapata matatizo. Bandari ya Nyamisati haina sehemu ya abiria, kuna banda tu bovu bovu pale, hakuna vyoo, hakuna maji, hakuna hata ngazi ambayo inaweza ikarahisisha abiria kupanda kwenye boti na kushuka. Tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri kupitia Mamlaka ya Bandari, naamini wapo, watusaidie pale. Na mimi binafsi nimefanya juhudi, nimeandika barua kwa Katibu Mkuu wa Ujenzi na nimemsikia asubuhi hapa akitambulishwa, Ndugu Nyamuhanga kwamba tunaiomba ile ngazi iliyokuwa pale inatumika kwa ajili ya MV Dar es Salaam ambayo haifanyi kazi kwa sasa, mtuletee Nyamisati kwa kipindi hiki cha muda wa mwaka mmoja wakati ujenzi unaendelea, isaidie. Sijajibiwa ile barua, wala sina taarifa zozote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, ninaamini Serikali ni sikivu na Mheshimiwa Waziri sasa nalileta kwako rasmi, tunaomba sana mtupatie ile ngazi angalau kwa muda huo wa mwaka mmoja tuweze kuondoa tatizo la kupanda na kushuka katika gati la Nyamisati.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi, kilometa 55 ilikuwa ni ahadi ya Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alipokuja kuomba kura Mafia mwaka 2005 na 2010 tena na kwenye Ilani ya Uchaguzi, 2015 - 2020 imo, kwamba barabara ile itafanyiwa upembuzi yakinifu. Nimekiangalia hiki kitabu kuna mahali nimeona kuna shilingi bilioni 1.5. Tafsiri yake sijaipata, lakini naomba utakapokuja kuleta majumuisho hapa, uniambie labda hiyo ndiyo kwa ajili ya usanifu na uchambuzi wa kina kuhusu barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, hususan Mheshimiwa Naibu Waziri yeye alikuja Mafia na tukamwambia kwamba Mafia ni kisiwa, kuna tatizo la udongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kuikarabati ile barabara, wataalamu wanasema udongo uliobaki utafaa kwa miaka miwili tu, baada ya hapo utakuwa umekwisha na mkitaka kujenga barabara ya lami itabidi udongo muutoe Dar es Salaam gharama itakuwa ni kubwa sana.
Kwa hiyo, naomba sana mtuharakishie ujenzi ule wa barabara ya lami Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi kilometa 55 tu ili tusije tukakumbwa na tatizo la ukosefu wa udongo ambao unakwisha kutokana na matengenezo ya kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu alifanya ziara Mafia Septemba, 2016, tukamwambia kilio chetu, ATCL ije Mafia, usafiri ni taabu, ni gharama kubwa sana usafiri wa ndege Mafia. Round moja tu ya kwenda one way ni shilingi 160,000; kwenda na kurudi inakwenda shilingi 300,000 mpaka shilingi 320,000. Tumeona ATCL wameanza route ya kwenda Mtwara, tunaomba sana ile ya kwenda Mtwara ipitie Mafia
– Mtwara; ikitoka Mtwara – Mafia – Dar es Salaam; itatusaidia sana kutuondolea tatizo hili la gharama kubwa ya usafiri wa ndege. Tukifika sisi Magharibi pale, jua likizama Mafia, huna namna ya kutoka. Akipatikana mgonjwa huna namna ya kutoka kwa sababu ndege zinazokuja pale ni ndogo na usiku uwanja ule hauna taa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nukta hiyo labda nizungumzie tena huu Uwanja wa Ndege. Tunaishukuru Serikali iliutanua, lakini bado kuna hilo tatizo la taa. Uwanja hauna taa na ikifika usiku, akitokea mgonjwa amepata dharura, basi mjue huyo mgonjwa chance za kupoteza maisha ni kubwa zaidi kwa sababu hakuna namna ya kutoka ndani ya Mafia ila ni kupitia bahari na ukiingia kwenye boti ni safari ya saa tano mpaka sita.
Kwa hiyo, tunaomba sana na Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Mafia, tukakwambia hili jambo, ukasema utalitilia kipaumbele. Nimejaribu kuangalia kwenye kitabu hiki, sijaona uwekaji wa taa na utanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia. Naomba sana wakati unakuja kuhitimisha hoja yako utuelezee mikakati ya kuhakikisha kwamba Uwanja wa Ndege wa Mafia unawekwa taa na unaongezwa ukubwa ili kuongeza fursa za kitalii pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki mbili zilizopita nilileta swali hapa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza mtoa hoja, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa na timu yote iliyofanikisha mchakato wa Makadirio ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Mwenyekiti, barabara ya Airport Access Road - Kilindoni mpaka Utende Wilayani Mafia yenye urefu wa kilometa 14 pamoja na kukamilika kwake, lakini kwa masikitiko makubwa imejengwa chini ya kiwango. Ni matumaini yangu Mkandarasi atalazimishwa kuirudia barabara ile na hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa kuitia hasara Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia kutokana na jiografia yake kuwa ni kisiwa, tunategemea sana Uwanja wa Ndege. Ikitokea dharura hususan nyakati za usiku, ndege haziwezi kuruka kwa kuwa uwanja hauna taa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea dharura ya mgonjwa kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, anaweza kupoteza maisha, kwani ili afike Dar es Salaam, atahitaji kusafiri kwa boti kwa takriban masaa nane hadi kumi ili afike katika Hospitali ya Rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, boti ya uokoaji katika Bandari za Kilindoni na Nyamisati ndiyo usafiri wa wengi katika Kisiwa cha Mafia. Ila hatari kubwa iliyo mbele ni kwamba hatuna huduma za uokoaji, yaani Coast guard kutokana na idadi kubwa ya wasafiri kati ya bandari hizi mbili. Tunaiomba sana Serikali iweke Kituo cha Coast guard ili likitokea jambo la dharura waweze kutoa msaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu boti ya abiria kati ya bandari ya Nyamisati na Kilindoni Mafia. Wananchi wa Mafia tupo katika wakati mgumu kwenye usafiri wa kuingia na kutoka Mafia. Tumejaribu kushawishi wafanyabiashara waje wawekeze kwenye usafiri wa baharini, lakini mwitikio mpaka sasa umekuwa ni hasi mno. Hivyo tunaiomba Serikali ichukue jukumu la kutuletea kivuko cha kisasa baina ya bandari hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 2.5 na tender ya ujenzi imeshatangazwa na ujenzi utaanza muda siyo mrefu. Kwa kuwa ujenzi utachukua zaidi ya mwaka, mazingira ya sasa ya bandari ile siyo mazuri kabisa. Hakuna vyoo, hakuna jengo la abiria na ngazi ya kupanda na kushukia abiria. Niliandika barua kwa Katibu Mkuu wa Ujenzi kuomba ngazi iliyokuwa ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa haitumiki ili itusaidie pale Nyamisati. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wakati wa kujibu hoja, nipate ufafanuzi juu ya ombi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara kutoka Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi yenye urefu wa kilometa 55, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi; na imo katika Ilani ya CCM 2015 -2020. Nimeangalia kwenye kitabu hiki sijaona fedha zozote zilizotengwa kwa ujenzi wa barabara hii. Naomba Mheshimiwa Waziri atupe majibu wananchi wa Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kutoa pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mafia inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa ni ukosefu wa huduma ya x-ray.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia ni kisiwa na kutokana na changamoto ya usafiri hospitali hii wananchi wanapata taabu sana kuwasafirisha kufuata huduma ya x-ray Wilayani Temeke, Dar es Salaam. Mimi binafsi kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali nimefanikiwa kupata x-ray mpya na ya kisasa na tayari ipo Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa x- ray imefika Mafia toka mwezi Aprili, 2016 mpaka leo hii bado ipo store, haijafungwa. Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja Katibu Mkuu wanafahamu suala hili, ukweli nashindwa kuelewa ni kwa nini hamtaki kutoa ruhusa x-ray ili ifungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kujenga chumba kipya kwa ajili ya x-ray mpya siyo wazo baya ila ombi letu ni x-ray mpya ifungwe katika chumba cha x-ray ya zamani na ile ya zamani chumba kipya kitakapokuwa tayari ifungwe. Hii itasaidia sana kwani kwa sasa wananchi wanapata usumbufu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hopitali ya Mafia pia haina jokofu la kuhifadhia maiti. Suala hili ni muhimu sana kutokana na kukua kwa sekta ya utalii na shughuli za kijamii kuongezeka, inapotokea dharura ya mtu au watu kufariki ambao siyo wenyeji kwa Mafia usumbufu mkubwa unajitokeza kama ilivyotokea kuanguka ndege ya Comoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuipandisha hadhi zahanati ya Kironywe kuwa kituo cha afya; Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Mafia yenye jumla ya vijiji 23 na kata nane haina kituo cha afya hata kimoja. Tayari hatua za awali tumeshazikamilisha tunaomba Wizara sasa iharakishe mchakato huu ili Wilaya tuwe na kituo kimoja cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati za Bwejuu, Mlongo, Gonje na Jimbo zilitengewa fedha ili kumalizia mabomba, lakini mpaka sasa tumekapokea robo tu ya fedha hizo. Kwa namna ya kipekee zahanati ya Bwejuu ambayo ipo katika kisiwa kidogo cha Bwejuu ambapo hakuna huduma yoyote ile ya kitabibu, hakuna hata sanduku la msaada wa kwanza (first aid kit) tunaomba Serikali iharakishe upatikanaji wa fedha hizo ili wananchi wapatoa 1,000 wa kisiwa cha Bwejuu wapate huduma hii muhimu.

Kuhusu Mfuko wa Bima ya Afya tunaomba Serikali iboreshe CHF ili iweze kutumika mpaka ngazi ya Mkoa na pia huduma za upasuaji zijumuishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mgao wa vitanda na mashuka kipaumbele tupewe Wilaya za pembezoni kama Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri Dkt. Harrison Mwakyembe na timu nzima waliofanikisha hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, niipongeze timu yetu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa mafanikio na heshima kubwa inayoiletea Tanzania. Niiombe Serikali bila kujali matokeo ya mashindano yatakayofanyika Gabon baada ya mwezi huu, Serikali isiwatupe vijana hawa, kwani wameonesha uwezo na vipaji vya hali ya juu, kutokana na umri wao kuwa mdogo tuwekeze zaidi kwao na naona akina Samatta wengi kutoka kwa vijana hawa.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF); ni ukweli usio na shaka hali katika shirikisho hili sio nzuri, migogoro na malalamiko ambayo kwa kiasi kikubwa tulishaanza kuisahau wakati wa uongozi uliopita chini ya Rais Leodgar Chills Tenga kwa sasa imerudi kwa kasi sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri asimamie vizuri shirikisho hili na kwa kuwa watafanya uchaguzi mwaka huu wapate viongozi wazuri ambao wataipeleka Tanzania mbali kupitia mchezo huu wa soka.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Natambua Wizara hii inawajibika kwenye Wizara hii kupitia maudhui na usajili wa vyombo vya habari. Tumeshuhudia magazeti na vipindi vya runinga vinavyoenda nje ya maadili, tumeshuhudia magazeti yakiandika habari za uongo na uzushi dhidi ya viongozi, Mheshimiwa Waziri mwenyewe ni muathirika wa jambo hili. Ushauri wangu, Serikali ichukue hatua kali ikiwa ni pamoja na kufungia maisha magazeti au Televisheni zinazothibitika kufanya vitendo hivi vya kuchafua majina ya watu.

Mheshimiwa Spika, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC); usikivu wa TBC Redio upo chini ya asilimia 25 kwa nchi nzima, niiombe Serikali iongeze bajeti ya TBC ili iweze kuwekeza katika mitambo na kuongeza usikivu hadi vijijini ambapo ndipo wananchi walipo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa hotuba yao nzuri ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukanda wa Kusini (Southern Circuit) upo nyuma sana kiutalii pamoja na ukweli kwamba kuna vivutio vingi vya kitalii. Kwa mfano, Kisiwa cha Mafia katika Mkoa wa Pwani kimejaaliwa kuwa na vivutio vifuatavyo:-

Kwanza kuna whale shark, samaki huyu aina ya papa (potwe) wamebaki wachache sana na katika nchi chache duniani. Moja ya sifa nyingi za samaki huyu ni rafiki kwa mwanadamu kama livyo pomboke (dolphin) na watalii wanapenda sana kucheza na kuogelea naye. Kwa sasa samaki huyu anapatikana Australia, Philippines na nchi chache za Bara la Amerika ya Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na umuhimu wake na mvuto wake kwa watalii hakuna juhudi zozote kutoka upande wa Serikali katika kumtangaza samaki huyu. Juhudi pekee ni zile zinazofanywa na mmiliki wa hoteli na mtalii mwenyewe. Tunaiomba Serikali sasa itangaze kivutio hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kuna scuba diving, hiki ni kivutio kingine kinachopatikana kisiwani Mafia. Mandhari ya chini ya bahari ya Mafia imesheheni samaki wa aina mbalimbali ambazo zinawavutia watalii kuja na kufanya uzamiaji wa bahari. Tunaiomba Serikali sasa itangaze kivutio hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni sports fishing ambapo ni uvuvi wa mchezo maarufu kama catch and release ambapo watalii wanavua samaki na kupiga nao picha halafu huwarejesha baharini akiwa hai. Ni kutokana na vivutio hivi pamoja na vivutio vingine vya Kusini vya Mji wa Kilwa na magofu yake, mbuga ya Selous na hot spring Utete Rufiji; Serikali sasa ije na mpango mkakati wa kutangaza vivutio hivi vya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu. Ni ukweli usio na shaka kumekuwa na ongezeko la utalii nchini. Lakini kuna utata mkubwa namna ambavyo takwimu hizi zinakokotolewa. Nimeomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kujibu atupe ufafanuzi juu ya kadhia hii. Je, watalii hesabu inachukuliwa kwenye mipaka yetu au viwanja vya ndege na mipaka ya bandari na bandari zetu au wakati wanaingia kwenye vivutio vyetu? Je, watalii wanaoingia Zanzibar moja kwa moja na kuondokea huko huko hawa wamo katika idadi ya watalii milioni 1.2 walioingia Tanzania mwaka wa jana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja. Ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa mtoa hoja, Waziri Dkt. Hussein Mwinyi kwa kutuletea hotuba nzuri sana yenye kuleta matumaini kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Kisiwa cha Mafia ambacho kipo mpakani kabisa na Comoro kule. Takribani miezi miwili, mitatu iliyopita tulipata bahati ya kutembelewa na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Mwamunyange, katika juhudi za kuhakikisha kwamba wanafungua kikosi pale cha Jeshi katika Kisiwa cha Mafia ili kuhakikisha kwamba suala la ulinzi na usalama linaimarika pale kisiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo jema sana na sisi watu wa Mafia tumelipokea kwa mikono miwili. Lakini kuna mambo mawili hapa ni vizuri niyaweke kwa attention ya Mheshimiwa Waziri ayaangalie yaweze kutusaidia ili hili jambo liwe jema zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza; site ambayo wameichagua pale sisi na wenzetu pale Wilayani tumeiona kwamba sio site nzuri kwa sababu ni katikati ya Mji wa Kilindoni pale. Lakini kuna site ambayo iko maeneo ya Jimbo takribani kilometa 30 kutoka Mjini Kilindoni pale; tulikuwa tunapendelea na tungefurahi sana kama jeshi lingekwenda kule ili kukataa hizi crush na wananchi kwa sababu kule kidogo kumejitenga na watu wapo wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini angalizo la pili tungependa pia Kikosi cha Maji kiwepo pale kwa sababu sisi tunapakana na bahari kuu na kule kuna maharamia wale wa Kisomali na pia kuna meli za uvuvi ambazo zinakuja kuvua kule bila ya kibali cha mamlaka husika. Kwa hiyo, tungependa sana kije kikosi cha maji pale ili waweze ku-patrol ile bahari na kuhakikisha kwamba hakuna aina yoyote ya uvuvi wa kuvamia wa meli kubwa zinazokuja kuvua pale Kisiwani Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ningependa nijielekeze sasa kwenye suala la vijana wanaoingia kwenye JKT. Mimi kwa ufahamu wangu kila wilaya imetengewa sehemu yake ya vijana watakaokwenda JKT kila mwaka, lakini kwa bahati mbaya na masikitiko
makubwa sana Mheshimiwa Waziri, inapofika Wilaya ya Mafia wale washauri wa mgambo sijui wanatoka wapi, sijui wapo chini yenu au wako chini ya nani, Mshauri wa Mgambo wa Mafia siku zote lazima ataandikisha vijana kutoka nje ya Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, hili tunaomba sana mwaka huu lisijirudie, na kama litajirudia basi kuna hatari ya kuvunjika kwa amani katika Kisiwa cha Mafia, kwa sababu vijana wenye qualification wapo, lakini Mshauri wa Mgambo analazimisha kuwaleta vijana kutoka nje ya Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapowachukua wale huku nyuma tunaanza kuulizwa na wazazi, vijana wamemaliza shule za kata hizi, form four wanakosa nafasi, kwa nini nafasi hizi wanakwenda kuzichukua watu wanaotoka nje ya Mafia? Serikali imefanya hivi kwa makusudi kwa sababu ya kuleta uwiano ili Jeshi letu liwe na uwakilishi mzuri, kwamba kijana kutoka kila wilaya ya Tanzania anakuwepo katika Jeshi. Sasa zinapokuja nafasi zetu sisi mshauri wako wa mgambo Mheshimiwa Waziri anatuletea watu kutoka nje ya Mafia, inatukera. kwa hiyo kwa mwaka huu sasa tunasisitiza, hili jambo lisijirudie, kama ni kuvumilia tumevumilia kwa miaka ya nyuma huko inatosha sasa, enough is enough. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima. Nielekeze shukrani zangu kwa mtoa hoja Mheshimiwa Waziri Dkt. Charles Tizeba na Msaidizi wake ndugu yangu, Mheshimiwa William Olenasha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ilibahatika kuwa na wataalam wenye kuijua Sekta yao. Nampongeza sana pia Katibu Mkuu upande wa Uvuvi, ndugu yangu Dkt. Yohana Budeba ambaye kiasili naye ni mvuvi kama mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa huzuni kidogo kwa sababu haya nitakayoyazungumza leo, kwa kiasi kikubwa sana ndiyo kilio cha wananchi wa Mafia. Kuna Taasisi ya Serikali inaitwa Hifadhi ya Bahari na naamini wapo hapa. Taasisi hii imekuwa ni kero kwa wananchi wa Mafia. Lazima nianze kusema mapema kabisa, hakuna mtu wa Mafia yoyote anayepinga uhifadhi, wote tunaunga mkono uhifadhi; lakini aina ya uhifadhi unaoendelea Mafia na hii Taasisi ya Hifadhi ya Bahari, maarufu kama HIBAMA siyo uhifadhi bali ni uporaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hifadhi kama jina lake lilivyo, wanatakiwa wahifadhi, lakini badala yake hifadhi ya bahari wamekuwa ni waporaji na wauzaji wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nimuulize ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba, hawa amewatuma waje kuuza ardhi au waje kuhifadhi maeneo ya mazalia ya samaki? Tunataka aje na majibu mazuri kabisa, kwa sababu hivi sasa, hivi ninavyozungumza, hifadhi wameshauza visiwa viwili. Kisiwa cha Shungimbili kimeuzwa, sasa hivi wako katika mchakato wa kuuza Kisiwa cha Mbarakumi na baadaye wanakwenda Nyororo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Hifadhi inasema wakati wanawaondoa hawa wavuvi katika hivi visiwa sheria inasema haya ni maeneo tengefu; na maeneo tengefu hayatakiwi kuwa na makaazi ya kudumu. Wanachofanya hifadhi, wanawaondoa wavuvi, vile visiwa wanaviuza kwa wawekezaji. Sasa inapingana na dhana nzima ya maeneo tengefu. Pale Shungimbili wameuza, imejengwa hoteli ya nyota tano; usiku mmoja dola 10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie, toka imeuzwa kisiwa kile, Halmashauri ya Mafia haijapata hata senti tano, hatuujui mkataba uko wapi? Tuna sababu gani sisi tena ya kuipenda Hifadhi ya Bahari?

Mheshimiwa Naibu Spika, hoteli ile ya nyota tano iliyojengwa pale, wale wanaoitwa wawekezaji wamebadilisha mpaka jina. Mheshimiwa Simbachawene nimemwona hapa, labda watusaidie wenzetu waliopo Serikalini, mamlaka ya kubadilisha majina ya maeneo, ni mamlaka ya nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, inayoitwa Thanda Hoteli, wala si majungu unaweza uka-google ukaiona, Thanda –‘T’ for tangle, ‘h’ for hotel, ‘a’ for alpha, ‘n’ for November, ‘d’ for delta and ‘a’ for alpha. Thanda hoteli utaiona pale ukiisha- google tu, unaona Thanda Hoteli Mafia. Thanda Ireland Hoteli Mafia. Hakuna kitu kama hicho Mafia. Mafia kuna Kisiwa kinaitwa Shungimbili, hakuna kisiwa kinaitwa Thanda Ireland. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie mamlaka haya ya kubadilisha mpaka jina la kisiwa wameyapata wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, wamejenga pale hawana hata building permit. Building permit anatoa Mkurugenzi wangu wa Halmashauri, yeye mwenyewe anashangaa anasema mimi naona majengo yanaota tu pale kama uyoga. Sasa tunataka kujiuliza wakati wanavichukua visiwa hivi kuvifanya maeneo tengefu, hoja ilikuwa kwamba kuna kiumbe kinaitwa kasa. Kasa anakwenda kupanda pale kutaga mayai.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo mmeshawauzia hawa wawekezaji, wameweka miamvuli pale Wazungu wanapunga hewa muda wote; huyo kasa atapanda juu kwenda kutaga mayai saa ngapi katika mazingira kama hayo? Kuna mambo ya ajabu sana yanaendelea pale Mafia. Kuna aina ya uporaji unaoendelea pale. Sasa tunawauliza ninyi mmekuja kuhifadhi, mmekuja kuuza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema wala sitatoa shilingi, lakini nitakachofanya, tutamwandikia Mheshimiwa Rais tumwambie kwamba Mafia inauzwa. Visiwa viwili vilishauzwa, watauza cha tatu, watauza na kisiwa kikubwa, mtatuhamishia sehemu nyingine kwa sababu tumewaambia miaka miwili, hamtaki kusikia. Kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana. Hata wananchi kuulizwa basi juu ya ule uwekezaji! Sheria zinasema, hawa watu wa hifadhi wamekuwa na kiburi na ni wababe sana. Wao wanaamini hiyo inayoitwa Sheria ya Hifadhi ina supersede sheria zote za nchi; Local Government Act mpaka Katiba ya nchi haimo. Wanakwambia hii hifadhi imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge, kwa hiyo sheria nyingine zote hazifai, inayofaa ni Sheria ya Hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana yule bwana anakuja pale anajenga hoteli, hahitaji building permit, hawataki kuwashirikisha wananchi, wananchi hawakuulizwa na hakuna mihtasari. Leo hapa nina hii document; nilipowauliza mbona wananchi hamkuwauliza? Wanasema wananchi tumewauliza, wakaenda kukaa na watu wanane pale Kirongwe baadaye ndiyo wanasema wananchi tumewauliza sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana nimwulize ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba, kaka yangu, tena rafiki yangu sana; mambo haya yangefanyika kule Buchosa, yeye angekubali? Yeye ana visiwa kule; vingeuzwa visiwa vya Buchosa angekubali? Kwa sababu kila siku namwambia kitu hiki hiki kimoja hataki kusikia, kwa nini? Tunataka aje na majibu thabiti kabisa, kwa nini hifadhi ya bahari wanaendelea kuuza visiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo unaoitwa uhifadhi. Nenda pale Kigamboni Dar es Salaam kule Kijiji Beach, South Beach kule maeneo yale kaa kuanzia asubuhi mpaka jioni, yanapigwa mabomu utafikiri nchi iko kwenye vita na Ikulu iko pale pale. Hawa watu wa hifadhi wanaacha kwenda kukamata wapiga mabomu pale, wanakwenda kuuza visiwa kule Mafia, hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wanahamisha wananchi wa Nyororo, wavuvi wa pale, wamekaa karibuni miaka 15 wanawaondoa wanataka kuweka hoteli nyingine ya Nyota tano. Kisa nini? Wanasema sasa haya ni maeneo ya tengefu. Tunasema maeneo tengefu kusiwe na makazi ya kudumu. Kwa nini mnawatoa wavuvi halafu mnajenga hoteli? Hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jibondo, kisiwa kingine hiki; ndugu yangu Kwandikwa anafahamu sana haya. Wananchi wa Jibondo hivi sasa wako siege hawawezi kwenda kufanya shughuli zozote, wamezuiwa na watu wa hifadhi wasivue. Sasa tunawauliza, mmekuja kuwasaidia wananchi kuwahifadhi au kuwamaliza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuona kwamba uvuvi umeshindikana, wakaamua kulima kilimo cha mwani baharini. Wakalima wakapata mwani mwingi sana, wakaweka katika ma-godown yao. Imekuja meli kupakia ule mwani na kupeleka sokoni. Hifadhi ya bahari wanasema ile meli inavunja matumbawe, inaharibu mazingira. Kwa hiyo, hairuhusiwi kuingia, ule mzigo umeozea ndani. Nataka tuwaulize tu ndugu zangu, hivi ninyi hamna huruma? Hawa watu wa hifadhi hamna huruma? Watu mzigo umejaa ndani, hawaruhusiwi kwenda kuuza...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mwijage, kwa hotuba nzuri ya bajeti yenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuweka mbele mapinduzi ya viwanda. Juhudi hizi tumeanza kuona matunda chanya na Tanzania ya viwanda sasa inaonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kisiwa cha Mafia wamehamasika katika kilimo cha miwa na kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kupata mazao mengi, lakini tatizo limekuwa ni kutokuwepo na kiwanda cha kuchakata miwa ili kupunguza ukubwa wa mzigo na kujirahisishia usafirishaji wa mazao. Namwomba tu Mheshimiwa Waziri kupitia Shirika la SIDO, aangalie uwezekano wa Mtaalam kuja na kiwanda rahisi kusaidia wakulima wa miwa wa Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kisiwa cha Mafia pia ni maarufu kwa ulimaji wa zao la nazi. Kwa kuwa zao la nazi linatoa mafuta na tui kwa matumizi ya mwanadamu, nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano wa kutupatia kiwanda kitakachochakata mazao yatokanayo na nazi ili kusaidia kukuza kipato cha mwananchi wa Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais mwaka anazindua Bunge hili la Kumi na Moja alionesha masikitiko yake ya kukosekana kiwanda cha kusindika samaki kwa ukanda mzima wa Pwani kuanzia Mkoa wa Tanga mpaka Msimbati Mtwara. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa ukaribu suala hili la kiwanda cha kusindika samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijadili suala Kitaifa la viwanda. Niiombe tu Serikali yangu kwenye kuelekea viwanda, mkazo uwekwe kwenye kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi badala ya Serikali kujenga viwanda vyake yenyewe. Serikali haifanyi biashara, Serikali isubiri kutoza kodi na kupata fursa ya kutoa ajira kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, naomba Serikali ianzishe vyuo aina ya VETA katika makambi yetu ya Jeshi la Kujenga Taifa. Aina ya viwanda inayokuja sasa, lazima tuandae vijana wetu kwenye kada za kuendesha mashine (Machines Operators). Hii itasaidia kwao kupata ajira kwenye viwanda hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuoanisha uanzishaji wa viwanda na kilimo chetu. Sisi mazao yetu mengi ya matunda yanaoza mashambani kwa kukosa kiwanda cha kusindika matunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ukweli kwamba tuna kiwanda cha Azam pale Mkuranga, lakini kiasi kikubwa wanaagiza matunda concentrate kutoka nje ya nchi. Hii inatokana na ukweli kwamba matunda yetu hayalimwi kitaalam na kupelekea shamba moja kutoa matunda yenye ladha tofauti na kushindwa kutengenezwa juice. Kilimo cha kisasa ndiyo namna pekee ya kuoanisha ladha ya mazao haya ya matunda ili yaweze kutumika kutengeneza juice.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii ya kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini. Naipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kufuta kodi zenye kero kwa wakulima na wavuvi wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kero kubwa ya taasisi ya Serikali ya Hifadhi ya Bahari Mafia (HIBAMA) kwenye mgao wa maduhuli yatokanayo na watalii wanaoingia katika maeneo ya hifadhi, Halmashauri ya Mafia inapata asilimia 10 ya pato halisi, yaani baada ya kutoa gharama za uendeshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza asilimia 10 ni kiwango kidogo sana ukizingatia mzigo unaobebeshwa na Halmashauri kwenye kuendesha shughuli za afya, elimu na miundombinu. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri yeye ndiye mwenye kutengeneza kanuni, kwa kipekee tunamwomba sasa aridhie ombi letu la kubadili kanuni ili kiwango hiki kiongezwe kutoka asilimia 10 mpaka kufikia asilimia 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni hili la pato halisi (net income), baada ya kutoa gharama zote za uendeshaji za hifadhi ya bahari zikiwemo semina, safari, likizo na malipo ya ziada, baada ya saa za kazi ibaki zile gharama za kukusanya mapato tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uwekezaji unaofanywa na hifadhi ya bahari katika visiwa vya Shungimbili, Mbarakuni na Nyororo. Kimsingi sisi watu wa Mafia hatupingi mwekezaji, bali namna ya uwekezaji na mchakato mzima ndiyo unaacha maswali mengi bila majibu. Kitendo cha kutowashirikisha wananchi hakikubaliki hata kidogo. Ni ushauri wetu kwamba suala la mwekezaji liachwe kwenye ngazi ya Halmashauri kutoka hifadhi ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ongezeko la vijiji vya eneo la hifadhi ya bahari. Hifadhi ilianza na vijiji vinne tu, lakini leo imeongezeka mpaka kufikia vijiji 13 na Wilaya ya Mafia ina jumla ya vijiji 23. Ukweli huo zaidi ya nusu ya vijiji ipo chini ya himaya ya hifadhi ya bahari na sasa wananchi wanakatazwa hata kulima mbali ya kuvua. Kilio chetu ni kwa nini mchakato wa kuongeza vijiji vya eneo la hifadhi haikushirikisha wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubinafsishaji wa kisiwa cha Nyororo na Mbarakuni usitishwe mara moja kwa maslahi ya Taifa hili ili kasa waweze kupata maeneo ya kutagia mayai yao, kuokoa kiumbe huyo asipotee katika sura ya nchi yetu.

Mheshimiwa Waziri, Meneja Mkuu wa Hifadhi ya Bahari awajibishwe kwa kosa la kuuza kisiwa cha Shungimbili kinyume na utaartibu wa kushirikisha wananchi na mwekezaji kujenga bila ya kuwa na kibali cha ujenzi (building permit). Vilevile huyu Meneja Mkuu alimwongopea Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara ya kiserikali Mafia kuwa Halmashauri ya Mafia haidai hifadhi fedha za maduhuli, lakini baada ya Waziri Mkuu kuondoka, Hifadhi ya Bahari walilipa Halmashauri shilingi milioni 44. Kitendo hiki cha kumdanganya kiongozi mkubwa huyu mbele ya Mkuu wa Wilaya ni kitendo cha utovu wa nidhamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa bajeti yenye matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mafia ni kisiwa na kutokana na jiografia yake hiyo hakuna mito yenye kutiririka mwaka mzima. Ukweli kuwa chanzo kikuu cha maji kisiwani Mafia ni uchimbaji wa visima virefu na vifupi. Kwa masikitiko makubwa miradi ya maji iliyoletwa Kisiwani Mafia ni michache sana hivyo kisiwa cha Mafia kina shida kubwa ya maji. Kupitia Bunge lako Tukufu kwa namna ya kipekee, tunaiomba Serikali ituongezee miradi ya maji kutokana na mazingira magumu ya upatikanaji wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kuvusha maji kutoka Kisiwa Kikuu cha Mafia eneo la Kiegeani kwenda Kisiwa kidogo cha Jibondo takriban kilometa tisa umekuwa kwenye hatua mbalimbali za michakato kwa takribani miaka mitano sasa. Kupitia Bunge lako hili Tukufu tunaomba Serikali iharakishe mchakato huu kwani Kisiwa cha Jibondo kwa asili na ardhi yake ni mawe matupu na hakuna namna yoyote hivyo kulazimisha kuchimbwa kisima kilometa tisa nje ya Kisiwa Kikuu cha Mafia na kupitisha mabomba chini ya maji mpaka Kisiwa cha Jibondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kwa kuwa mradi huo haupo wananchi wanalazimika kukodi mashua za uvuvi kuja Kisiwa Kikuu na madumu ya maji na kuchota maji na kuvuka nayo. Nyakati za pepo kali za kusi na kaskazi zoezi hili linakuwa gumu na wananchi wanatumia maji ya chumvi ambayo ni hatari kwa usalama wao. Hivyo, tunaiomba Serikali kuharakisha mradi huu ili kuondoa adha hii kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's