Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Suzana Chogisasi Mgonukulima

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Manispaa ya Iringa ina mradi wa machinjio ya kisasa ambao Kitaifa ni wa pili kwa ubora na una uwezo wa kuchinja ng‟ombe 100 na mbuzi 100 kwa siku, mradi huu umebaki kidogo kumalizika kutoka Serikali Kuu. Manispaa ya Iringa iliomba shilingi milioni 200/= ili kumalizia, gharama ya mradi ni bilioni moja. Hadi leo hii fedha hiyo haijatolewa hata senti na iliomba bajeti ya mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo ukimalizika, ajira zitaongezeka kwa vile machinjio hiyo ina uwezo wa kuajiri watu 200. Naomba Waziri anijibu: Je, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 mradi huo umeutengea fedha kama Manispaa ilivyokuwa imeomba?

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa mkakati madhubuti (strategic plan) wa kutangaza rasilimali na vivutio vyetu kunasababisha nchi nyingine kunufaika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri mwenye Wizara husika wakati atakapokuja kuhitimisha hoja aje na mpango mkakati unaoelekeza kutoa fursa kwa taasisi au watu wenye uwezo ili waweze kutangaza vivutio na rasilimali zetu kimkakati zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwa ni vigumu sana kuona ujangili katika nchi yetu unakuwa kwa kasi wakati kuna watumishi walioajiriwa kwa kazi ya kulinda wanyama, hata pembe za ndovu zikikamatwa mwisho wake zinapopelekwa hakujulikani, hata mrejesho wowote katika Bunge hili Tukufu ili kupata taarifa yoyote endelevu juu ya kesi endapo watuhumiwa wameshinda kesi wananchi kinyemela. Hii ndiyo sababu kubwa inayokuza kazi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali isione vigumu kutoa taarifa muhimu kama hiyo katika Bunge lako Tukufu tena taarifa hizi zinapotolewa jina la mtuhumiwa litajwe kufanya hivyo hivyo ujangili utapungua.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni ya viwanda, napenda kushauri katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/2018, sekta ya kilimo ipewe kipaumbele cha kwanza ili kuwezesha pembejeo za kilimo kupatikana kwa wakati na itengwe bajeti ya kutosha. Kwa kufanya hivyo, wananchi watalima mashamba ya mazao ya biashara na chakula na kuwezesha viwanda vyetu kukua kwa kasi na kuinua uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maendeleo ili iweze kwenda na wakati ni lazima fedha za miradi zinazopitishwa na Bunge lako Tukufu zipelekwe kipindi husika. Angalia bajeti mwaka 2016/2017 hadi robo ya mwaka hata senti tano ya miradi ya maendeleo hazijapelekwa kwenye Majiji, Manispaa, Halmashauri na Miji Midogo.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa Fungu 52 inaonesha kuwa hadi mwezi Machi, 2017 Wizara ilikuwa imepokea sh. 314,673,230.000.95 sawa na asilimia 43 ya bajeti ya Wizara, zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida pamoja na miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuhusu fedha za maendeleo, randama zinaonesha kuwa hadi mwezi Machi, 2017 ni asilimia 34 tu ya fedha za ndani ndizo zilizotolewa na Hazina na kwa fedha za nje ni asilimia sita tu ya fedha hizo zilikuwa zimetolewa na Hazina kwa kipindi hicho. Hii ina maana kwamba bajeti ya maendeleo kwa fedha za ndani haijatekelezwa kwa asilimia 63 na kwa fedha za nje haijatekelezwa kwa asilimia 94. Kwa utekelezwaji huu duni wa bajeti ya maendeleo katika fungu hili, maoni yangu ni kwamba Serikali iwe makini kabisa na afya za Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Fungu 53, kwa mwaka wa fedha 2016 - 2017 Bunge liliidhinisha jumla ya shilingi bilioni
49.9. Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ilikuwa shilingi bilioni 41 na shilingi bilioni 8.848 zikiwa ni fedha za maendeleo. Hata hivyo, fedha za maendeleo hadi kufikia Machi, 2017 ni sh. 497,718,250/= sawa na asilimia 5.62 tu ya shilingi bilioni 8.8 zilizoidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni kwamba bajeti ya maendeleo katika fungu hili la Maendeleo ya Jamii haikutekelezwa takriban kwa asilimia 95. Fungu hili ndilo linalohusika na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii; na kwa maana hiyo, utekelezaji duni wa bajeti wa vyuo hivyo haviwezi kuwa na uwezo wa kujiendesha na kuzalisha wataalam wa kusaidia jamii zetu kujiletea maendeleo kwa kuweza kuibua fursa zilizo katika jamii zao.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutoa shukrani zangu za dhati na napenda nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijaalia uzima na afya njema ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, napenda nitumie nafasi hii kuwashukuru wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Iringa kwa kunipa kura za kuweza kuwa mwakilishi wao. Pamoja na hilo sitakisahau Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kupokea kura za wanawake wa Iringa kwa kuwa wamenituma kuwa mwakilishi wao na kunipa go ahead. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, hii Wizara ni nyeti sana kwa muono wangu mimi na nilivyoiona. Hata hivyo, baada ya kuipitia hotuba hii kuna ugonjwa huu wa UKIMWI, ugonjwa huu una magonjwa nyemelezi kuna typhoid, homa za hapa na pale. Magonjwa haya yanapelekea hawa wenzetu ambao wana ugonjwa huu wa UKIMWI kuondoka haraka kwa sababu ya kukosa kutibiwa. Naiomba Wizara hii iweke Bima ya Afya kwa hawa wagonjwa ili wakiwa na magonjwa haya nyemelezi waweze kutibiwa. Hakutakuwa na sababu ya kupewa dawa za ARV wakati wakiugua magonjwa nyemelezi wanakosa dawa za kutibiwa typhoid ili waweze kupona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Wizara hii ije na mpango mkakati juu ya elimu ya ulaji wa vyakula. Magonjwa sugu yasiyoambukiza kama moyo, saratani, sukari na mengine ambayo tunayafahamu, haya yanasababishwa na vyakula ambavyo Watanzania sasa hivi tunakula. Ni ukweli usiopingika tunapenda Watanzania wawe wajasiriamali ili wainue vipato vya maisha, lakini sambamba na hilo hawa wajasiriamali wanaolima mboga mboga, wanaofuga kuku ambao ndani ya siku 14 unakuwa ni mlo sahihi, hawa ndio wanaopelekea haya magonjwa kulipuka. Mkulima wa nyanya, mkulima wa mboga aina ya chinese dawa anamwagilia leo asubuhi, jioni wanachuma mboga wanakwenda kuuza. Sumu zote zinaingia kwenye mwili wa binadamu na kupelekea haya magonjwa yasiyoambukiza kukua kwa kasi katika Taifa letu
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nchi yetu ya Tanzania ni kubwa sana. Ina square mita za mraba 947,303. Mheshimiwa Waziri mwenye Wizara hiyo nina uhakika hataweza kufikia maeneo yote. Ushauri wangu naomba atumie vipindi vya redio na tv kuelimisha Watanzania kuhusu mlo bora. Tutafika pale ambapo tumekusudia Watanzania.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna hili shirika la MSD. Wizara kama haitajikita kuhakikisha inakuwa na mpango mkakati wa kuweza kulipa madeni yanayopelekea shirika hili kuidai Serikali, tutapiga makelele usiku na mchana dawa hazifiki kwenye Halmashauri, haitawezekana kwa sababu MSD inaidai Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni mambo ya fedheha pale inaposadikika kuwa nchi zinazoisaidia Tanzania kwenye magonjwa, maambukizi kuleta dawa kama dawa hizi za UKIMWI, zinapofika bandarini na shirika letu kushindwa kwenda kukomboa kwa sababu wanaidai Serikali, wale waliotusaidia wanatuona sisi ni wa ajabu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichangie kuwa kwa sababu tayari zile hela za Wabunge, zilishaelekezwa kwenye madawati, zingekuwa bado, hizi ndiyo zilitakiwa ziende zikalipe kwenye shirika la MSD ili Serikali iweze kulipa, waweze kupata dawa zao na kuweza kupeleka kwenye Halmashauri zetu kama tulivyoazimia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya afya kwa kuipandisha hadhi hospitali ya Mkoa wa Iringa kuwa Hospitali ya Rufaa. Hospitali hii ilikuwa imeelemewa sana na wagonjwa waliokuwa wamejazana kwenye vitanda wawili wawili. Kwa wagonjwa wa kawaida unaona ni nafuu, lakini kwa akinamama wajawazito, tunafahamu akinamama wajawazito shape zao huwa zinabadilika. Sasa shape zile kulaza kitanda tunachokijua cha wastani wa Wizara ya Afya watu wawili si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya Wizara kuipandisha hospitali ya Mkoa kuwa Hospitali ya Rufaa, Manispaa ya Iringa wameweza kujenga hospitali ya Wilaya. Jengo la utawala limekamilika, wodi ya wagonjwa wa nje limekamilika, wodi ya wazazi imekamilika. Baada ya kukamilika wodi ya Wazazi Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mheshimiwa Peter Simon Msigwa amepelekea vitanda 30 na magodoro yake kwa ajili ya kuwasaidia akinamama wajawazito hao. Kwa sababu hospitali ya Wilaya tumesema iko TAMISEMI, lakini TAMISEMI nafikiri wewe Waziri wa Afya ndiyo mwenye Mamlaka, naomba basi, kwa sababu hospitali hii imekosa vifaa tiba, kwenye bajeti yako ya mwaka 2016/2017 hebu waambie TAMISEMI watusaidie hivi vifaa vifike pale Hosptali ya Frelimo.
Mheshimiwa Spika, upande wa walemavu, Waziri nikisema hapa mimi kama mama mtu mzima, mwenye nusu karne, suala la kwenda kujifungua ni suala nyeti sana. Maeneo tunayoishi, tumeona wenzetu wenye ulemavu wa viungo wanapopata shida wakati wanapokwenda kujifungua. Kwanza kabisa mapokezi ya wale manesi yako tofauti na mtu ambaye yuko kama nilivyo mimi na pili, vitanda vile wanavyoenda kujifungulia si rafiki na wenyewe na maungo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namuomba Waziri mwenye dhamana kwa namna ya pekee, ndani ya mwaka huu wa bajeti hebu alipe kipaumble suala la wanawake walemavu wanapokwenda kujifungua. Nitaona umelitendea haki Taifa, nitaona umeweka tija sura ya mwanamke kwa mwanamke anapopata nafasi ya namna hiyo anakuwa na huruma ya pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo. Nakuja kwenye tatizo la meno na macho. Ni ukweli usiopingika karibu ya robo tatu ya Watanzania tunavaa miwani sasa hivi na tunaotoa meno ni takribani milioni 20. Naomba Wizara yenye dhamana iangalie mpango mkakati wa jinsi ya kutoa elimu ya vyakula vinavyoweza kupunguza watu tusiwe vipofu mapema na tusianze kutoa meno chini ya umri usiotakiwa. Masuala yote hayo yanasababishwa na hivi vyakula ambavyo tunakula, lakini kwenye mpango huu wa hotuba ya Waziri sijaona mahali ambako amewekea kipaumbele suala la macho na meno. Hivyo, nikaona ni wakati muafaka baada ya kuwa nimepata nafasi ya kuchangia, niweze kulisemea hilo.
Mheshimiwa Spika, mimi naishi Mkoa wa Iringa na nimezaliwa Iringa. Naiomba Wizara ya Afya kuhusu afya ya uzazi wa mpango ni hatari. Kwa nini nasema ni hatari? Napenda kama inawezekana sheria itungwe ndani ya Bunge hili inayokataza utengenezwaji wa viroba. Viroba ni pombe zinazonunulika kwa bei ndogo sana, kwa maana hiyo unakuta hawa watoto wa under eighteen wanaanza kulewa toka asubuhi na ndiyo inapelekea waanze kuzaa kabla ya umri wao, wakati akili ya kulea mtoto yenyewe haijakomaa. Dada na kaka kama yamkini wanaweza kuwa wameoana, je, kupata Taifa linaloongezeka kwa kasi, lisilokuwa na malezi ya kielimu, ya kiafya Taifa hili tunalipelekea wapi?
Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimetoa dondoo kuwa uzazi huu unasababishwa na ulevi wa pombe hizi zinazonunulika kwa bei ndogo ndogo. Tuliombe Bunge letu Tukufu, tutakapokuja kujadili, hebu tutunge sheria ya kutokutengeneza pombe hizi za viroba zinazouzika kwa shilingi mia tano, mia tano tuifute kabisa. Tanzania hii tunayokusudia itakwenda kwa kasi kwa sababu tutapata watu watakaozaa watoto ndani ya umri unaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba niunge hoja ya Kambi ya Upinzani kwa asilimia mia moja kwa maana ndiyo inayotoa mwongozo ili Serikali iweze kufanya vizuri.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia jioni ya leo kwenye Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nianze na kundi la walemavu. Ninarudia tena kusema Mheshimiwa Ummy - Waziri wa Afya, matatizo wanayoyapata wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua bado yako pale pale. Niliongea mwaka wa jana katika Bunge hili lakini wakati nikiwa field huko kwenye majimbo nimekuta wauguzi wengi wanawanyanyapaa sana wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, kwa dhamana ya nafasi yako, hili ulichukue na ulifanyie kazi, wale watakaobainika wanaendeleza vitendo vya kuwanyanyapaa wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua wachukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 mpaka mwaka 2012 Hospitali ya Mkoa wa Iringa ilipata hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa. Tatizo ambalo linaikumba hospitali ile ni ukosefu wa madaktari bingwa. Hitaji la madaktari ni 24, hadi sasa hivi hospitali yetu ile ya rufaa ina madaktari watano, hivyo kusababisha kazi ya kiutendaji ya kuokoa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Iringa kuwa ngumu sana. Mheshimiwa Waziri, naomba hili ulichukue kwenye mgawo wako wa madaktari hao wanaopata ajira, basi Madaktari Bingwa uwapeleke kwenye Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuja kwenye Mfuko wa Bima. Afya kwa wazee wetu wa Taifa hili imekuwa ni tatizo. Serikali imejikita kuwasaidia wazee hawa huduma ya magonjwa ya homa, tumbo, lakini si pale wanapopata magonjwa yale ya moyo, ini, figo, vipimo hivi lazima walipie. Sasa kama Serikali inataka kusaidia kundi la wazee; hivi vipimo nilivyovisema gharama yake ni kubwa; na Serikali haitaki kuwekeza mkono wake, hii huduma ambayo tunasema tunataka kuwasaidia wazee naona sio sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi Wizara ichukue jukumu hili kuhakikisha hawa wazee ambao Serikali imesema itawatibia bure, iwe bure ya magonjwa yote hata hayo niliyoyaainisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Hospitali ya Mkoa wa Iringa kupata hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa, Manispaa ya Iringa tulijenga Hospitali ya Wilaya ambayo iko maeneo ya Frelimo na inaitwa Hospitali ya Frelimo. Hospitali hii ina wauguzi wakutosha, madaktari wakutosha, kinachokuja kuleta shida ni upungufu wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi ninapozungumza sasa hivi hospitali hiyo yenye wauguzi wa kutosha na madaktari wa kutosha haina vifaa vya uuguzi ambapo tumekosa kupata vipimo vya full blood picture, x-ray, ultra sound ambapo ingekuwa vipimo hivi viko pale, hospitali hii ingepokea msongamano wa wagonjwa ambao wanatakiwa kutibiwa pale ili wasiende kutibiwa kwenye hospitali ya rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ningependa nijikite kwenye unyanyasaji wa watoo wadogo wa kike. Sipo sambamba na wachangiaji waliosema, mtoto wa miaka chini ya miaka 18 kuozeshwa na kuwa mama wa nyumba ni makosa makubwa sana kiafya. Kwanza nyonga zake zenyewe hazijakomaa kuweza kuendeleza mambo ya mipango mingine ya kiutu uzima na hivyo tunawafanyia hayo matendo kiunyama kwa sababu tendo la ndoa kwa mtoto wa miaka chini ya 18 hana hisia nalo kwenye akili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Wizara hii kama sheria inakingana, kuwa haiwezekani kutungwa sheria hiyo, basi tutalazimisha Wizara ya Elimu iweke kiwango cha elimu ya mtoto wa kike ni Kidato cha 12, ili kama itaonekena kuna mzazi yeyote yule ana binti yake ameolewa chini ya miaka 18 aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tutakuwa tumewakwamua kundi la watoto wa kike ambao kwa tamaa za wazazi wao… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tanzania inataka iwe nchi ya viwanda, tuboreshe sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kwamba mikopo kwa wakulima inapatikana. Tukifanya hivyo tutakuwa tumewawezesha wakulima kulima kilimo bora. Kilimo bora kinatokana na wakulima kuwa na mbegu bora na mbolea kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sera ya elimu bure, ni miaka miwili kama Taifa tumeona kuwa elimu bure inaathari kutokana na kuporomoka kwa ufaulu wa wanafunzi. Katika mpango huu uliopendekezwa na Waziri wa Fedha, je,kuna mkakati wa makusudi wa kutatua matatizo yanayoikabili sekta ya elimu? Elimu ya kutosha inatakiwa kutolewa kwa wananchi wajue kuna baadhi ya shughuli za elimu kama wananchi wanapaswa kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu uliopendekezwa kwa mwaka 2018/2019, hakuna sehemu iliyoonesha ukuzaji wa viwanda katika Mkoa wa Iringa ambavyo vilikuwepo katika Mkoa huo. Mkoa wa Iringa miaka ya nyuma ulikuwa na viwanda vya COTEX, Cocacola, IMAC, SIDO na Tyre,viwanda hivi viliwasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Iringa na maeneo mengine ndani ya nchi yetu kupata ajira, lakini katika mpango uliopendekezwa sijaona sehemu yoyote inayoonesha kwa mwaka 2018/2019 kuhakikisha viwanda hivyo vinaimarishwa ili kupatia ajira wananchi wa Mkoa wa Iringa na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili lipewe kipaumbele.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo Wizara ya Maji. Maji ni uhai wa kila kitu, ikitokea jambo lolote hapa mtu mwingine ameanguka ghafla hapa Bungeni akifika pale hospitalini Madaktari wataanza kumwongeza drip la maji. Hivyo, tuone umuhimu wa maji unavyotakiwa katika maisha ya mwanadamu. Hata magari, meli, ndege vyote hivyo vinahitaji maji. Hata sasa hivi moto ukitokea jengo lolote utaona tunasema gari la zimamoto liko wapi, maji yaje ili waweze kuzima moto. Kama kweli maji ni uhai basi ifikie wakati muafaka wa kuona Serikali inaona jambo hili ni la umuhimu kitaifa na wazingatie kwamba kwa kukosa maji ni kukosa kuwa na maendeleo katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu inasema tunataka kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani. Imeonekana suala la maji siyo tatizo la kifamilia ila ni tatizo la mwanamke ambapo si kweli. Tatizo la maji ni tatizo la kitaifa na hivyo tulijue kama ni tatizo la kifamilia ni janga la kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kutokana na kuwa mwaka jana tulikuwa tumeweka ongezeko la bei ya mafuta ya dizeli na petroli kwa ajili ya kuhakikisha maji yanafika vijijini lakini imeonekana ongezeko ya bei ya mafuta haya limetatua changamoto ya maji kwenye miji yetu. Changamoto ya maji kwenye miji si kubwa kama ilivyo kwenye vijiji. Hivyo basi katika bajeti hii naomba Wabunge wote tuombe tuwe na ongezeko tena la tozo kwenye mafuta tufikie Sh.100, basi asilimia 70 iende vijijini na asilimia 30 iende mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla suala la maji ameachiwa mwanamke utaona hata wakati wa uzinduzi, Waziri anakinga maji kwenye ndoo anamtwisha mwanamke kwa nini basi akikinga maji asimtwishe mwanaume wakati suala hili ni tatizo la kifamilia? Naomba tuelewe kwamba suala la maji siyo tatizo la mwanamke ni la kifamilia, hivyo basi, kama ni tatizo la kifamilia, isionekane ni kumtua ndoo mwanamke kichwani bali ni pamoja na waume zetu tuliokuwa nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niingie kuzungumzia Mkoa wangu wa Iringa, mkoa wenye neema na uliobarikiwa ambao una vyanzo vya maji, tuna Bwawa la Kihansi, Bwawa la Mtera, Mto Lukosi, Mto Mtitu na Mto mdogo Ruaha. Cha ajabu pamoja na kuwa tuna vyanzo vyote hivyo kuna vijiji vina shida ya kuliko mtu anavyoweza kufikiria. Vijiji hivyo ni Nyakavangalala, Lyamgungwe, Lupembelwasenga, Luhota, Mkalanga, Usolanga na vingine vingi katika mkoa huu pamoja na Mji Mdogo wetu wa Ilula ambapo chemchem ya Ibofye iko jirani sana na nafikiri ni kama mita za mraba zisizopungua arobani na tano. Tumeshindwa kuweka miundombinu ili watu wa Mji Mdogo Ilula waweze kupata maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi navyozungumza Mji Mdogo wa Ilula wanauziwa maji ndoo ya lita ishirini kwa Sh.500. Huo ni Mji Mdogo tena uko kwenye barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kuelekea Zambia. Naomba Mawaziri wenye Wizara hii washughulikie tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo hicho cha Ibofye kwanza kabisa kwenye bajeti ya mwaka 2000-2005, Bunge hili lilipitisha bajeti ili waende kufanya kazi ya miundombinu katika chanzo hicho, wakati huo akiwa Mheshimiwa Mbunge Mlawa. Hadi leo navyozungumza sielewi hata hizo fedha zilikoishia. Naomba Mawaziri wahusika walifuatilie suala hili iliwaelewe. Ndiyo maana tunasema tutakapoweka ongezeko kwenye bei ya mafuta kuwe na bodi maalum itakayofuatilia ongezeko la fedha hizi ili ziende kwenye miradi tuliokusudia wa kupunguza uhaba wa maji kwa wananchi katika taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Iringa ni kati ya mikoa ile minne inayozalisha sana chakula nchini Tanzania.

Nataka niseme njaa tunaitaka kwa makusudi kwa sababu ya kutokuwa na mbinu mbadala kwa wakati muafaka wakati nchi yetu ina wataalam waliosomea na kubobea. Tatizo letu ni kwamba wakati wa mvua hatuna mabwawa ya kutunza maji ya mvua ili wakati wote tuweze kuendelea na kilimo cha umwagiliaji. Kutokana na hilo, tuone ni wakati sasa wa kuhakikisha bajeti hii inayokuja kuombwa na Waziri mwenye dhamana imeongezeka ili tuweze kujenga mabwawa maeneo hayo ambayo nasema ni lazima tuwe na mabwawa yanayotunza maji ya mvua tuweze kuondokana na tatizo la maji. (Makofi)

Katika Mkoa wangu wa Iringa akinamama wengi wajasiriamali ni wakulima wa mazao ya mbogamboga. Hivyo kukosa mifereji ya umwagiliaji iliyo bora wanashindwa kumudu shughuli zao za kilimo na kuweza kujikwamua katika dimbwi la umasikini walilokuwa nalo ukizingatia kazi kubwa ya kulea familia ni ya mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri mwenye dhamana katika Mkoa wangu wa Iringa katika maeneo haya yote niliyoelekeza na vijiji ambavyo sikuorodhesha hapa kutokana na wanawake wale walivyo na juhudi kwenye kilimo ahakikishe amepeleka mradi wa maji ili waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo cha mbogamboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Kata yetu ya Mahenge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi naunga mkono hoja ya Upinzani asilimia mia kwa mia.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's