Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Josephat Sinkamba Kandege

All Contributions

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukushukuru kwa fursa nyingine tena, naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao walipata fursa ya kuchangia kwa kuongea walikuwa jumla ya Wajumbe 19 na waliochangia kwa kuandika walikuwa jumla 17, jumla yake ilikuwa ni 36.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyoanza kusema asubuhi, umuhimu wa hoja hii nzito, naamini na wewe mwenyewe ni shahidi leo siku ya Jumamosi nisingependa kupoteza muda mwingi wa Waheshimiwa Wabunge, lakini wewe mwenyewe unaona jinsi ambavyo wametoa msukumo wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla naomba nikumbushe, wewe ni shahidi jinsi ambavyo kulikuwa na kazi kubwa ya uanzishaji wa Kamati ya Bajeti na uanzishwaji wa Sheria ya Bajeti na misingi ambayo ilikuwa imewekwa ili tuondokane na ile hali ambayo Bunge lilikuwa linafanya kama rubber stamping waliita watu hivyo. Tukasema tuondoke hapo, tufike mahali ambapo Bunge litashiriki katika mchakato mzima wa kuandaa bajeti na utekelezaji wake. Ombi ambalo ni vizuri na Serikali bahati nzuri wanasikia, isingependeza tukarudi nyuma tulikokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa ni vizuri kwanza tukajengea uwezo Ofisi ya Bajeti na sitarajii, maana hili limeanza kujitokeza pale ambapo Bunge linataka kuwa na uwezo wake mzuri sasa kumekuwa na tabia hata ule uwezo mzuri, wale watumishi wazuri ambao wanapikwa na Bunge wanaanza kuhamishwa wanapelekwa upande wa Serikali, haitapendeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukawa na uwezo mkubwa, twende na wengine ambao Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shahidi ukienda nchi kama Uganda, Kenya inafika mahali ambapo Kamati ya Bajeti, inakuja na bajeti mbadala ili kulinganisha na ile bajeti ambayo inaletwa na Serikali, huko ndiko ambako tunatarajia kwenda. Kwa hiyo, itakuwa si vizuri kama Serikali watatumia fursa ya kuanza kuchukua vile vichwa vizuri ambavyo vinatengenezwa wakapeleka upande wa kwao. Hilo lilikuwa la jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo na baada ya kutambua Wajumbe waliochangia, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, naomba kwa uchache nishukuru Serikali kwa sababu iko hapa wamesikia na mengi kimsingi na wao wamekiri kwamba ni ya kwenda kuyafanyia kazi, nitaje machache na kwa ujumla Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa kuongea kama watapenda niwataje majina lakini kwa kuokoa muda, naomba nisitaje hata wale ambao walichangia kwa kuandika naomba nisitaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya masuala ambayo yamesemwa kwa kiasi kikubwa ni vizuri nikasema. Kimsingi wajumbe wengi wamesisitiza juu ya suala zima la kulipa deni la TANESCO. Sisi sote ni mashahidi, uko umuhimu sana wa kuhakikisha kwamba deni hili linalipwa maana tunaamini Tanzania ya viwanda bila kuwa na uhakika wa umeme hatuwezi kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na suala zima la ushiriki wa private sector (PPP). Si rahisi kwamba masuala yote ya maendeleo tutaiachia Serikali kwa maana ya ile miradi mikubwa. Kwa hiyo, ni vizuri kama ambavyo Waheshimiwa wengi wamechangia kwamba fursa iwepo na itumike kuhakikisha kwamba private sector inashiriki kama injini ya kukuza uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, tumekuwa tukiongea muda mrefu tangu ukiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, mapendekezo ambayo yaliletwa Serikalini juu ya kuanza ujenzi wa barabara, kutoka Dar es Salaam kufika Morogoro na kwa kuanzia Chalinze zile njia tatu. Taarifa ambazo zilikuwepo ni kwamba private sector walikuwa wako tayari. Sasa hadithi imekuwa ya muda mrefu ni vizuri sasa Serikali ikaenda kwanza kutenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, katika Wajumbe wengi waliochangia yamesemwa maneno kwamba kuna hizi kauli za kutoka kwa Mheshimiwa Rais, anatamka pesa inapatikana. Niombe Waheshimiwa pamoja na nia njema ni vizuri tukaenda kutazama budget frame kwa ujumla wake, hiki ambacho kinatamkwa na Mheshimiwa Rais ukienda kwenye bajeti utakuta kipo. Siyo kwamba anaamka tu anatamka halafu pesa inapatikana. Mifumo ya bajeti iko sahihi. Kwa hiyo, ni vizuri kwa nia njema kwa sababu haya ambayo yanafanywa ni kwa ajili ya Watanzania ni vizuri tukafuatilia utaratibu wa bajeti twende kwenye vitabu, turejee tujue hayo ambayo yanatamkwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wameongelea kuhusiana na suala zima la kilimo ambalo na Kamati ya Bajeti kimsingi tumesisitiza kwamba ili twende kwenye Tanzania ya viwanda ni vizuri uwekezaji ukawekwa wa kutosha kuhusiana na suala zima la kilimo. Bahati nzuri Serikali imesikia, hii habari ya kwamba mvua zisiponyesha mara moja tu tunaanza kuwa na wasiwasi hatuwezi kwenda tukasema ni Taifa la kwenda kwenye uchumi wa kipato cha kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ziko nyingi, kama mtu hakuchangia hoja asitarajie kusikia hoja yake ikijibiwa, hayo ambayo nayajibu ni yale ambayo yamechangiwa kwa ujumla na yakapewa uzito na bahati nzuri, hiki ninachokisema nimekisomea. Kwa hiyo, sikukiokota mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto za kibajeti, Wajumbe wengi wamechangia. Wabunge wameainisha kuwa katika taarifa ya Kamati hali ya uchumi kwa mujibu wa taarifa ya kutoka Benki Kuu na mwenendo wa mfumuko wa bei, Serikali inashauriwa kuhakikisha kwamba inakaa chini na kutathmini mwelekeo uliokuwa umetolewa awali na hali ya sasa. Ni vizuri tukaanisha ili tukapata namna ambavyo tunaenenda kama tuko kwenye right track. Hili niombe Serikali kujisahihisha si vibaya, tutazame wapi tuna-miss point ili isije ikafika mpaka dakika ya mwisho ndio tukajikuta tume-miss kile ambacho tulikitarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kuhusiana na mafunzo kwa Bunge zima. Imechangiwa na Wabunge wengi ni hoja ya msingi ni vizuri Serikali mkajipanga maana exposure ni jambo la msingi sana. Pamoja na ufinyu wa bajeti lakini ni lazima tuhakikishe kwamba Wabunge wanajengewa uwezo ili wafanye kazi yao ya kikatiba ya kuhakikisha kwamba wanaisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeongelewa hoja kuhusiana na Serikali kukopa ndani na sisi Kamati tumeliona, tukaishauri Serikali. Serikali ina muscles za kutosha ina uwezo mkubwa wa kwenda kutafuta mikopo nje, ni vizuri hii mikopo ya ndani tukaiachia sekta binafsi ili wahangaike na hizi fedha ambazo watazipata kwa urahisi. Tumeiomba Serikali iharakishe zoezi la kufanya sovereign rate ili waende kutafuta mitaji huko nje kwa sababu inapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la shilingi milioni 50 ya kila kijiji, wewe ni shuhuda ulishiriki wakati tunajadili na tukakubaliana kwamba pesa hizi zinazotolewa si pesa ya ruzuku, ni pesa ambayo ni ya mkopo na pesa ya mkopo lazima ujihakikishie kwamba huyu unayemkopesha anaenda kuzirejesha vipi kwa sababu pesa hii ni revolving fund. Tunaiomba Serikali iharakishe mchakato ili pesa hizi zikitolewa zikifika kwa wananchi ziweze kurejeshwa ili wananchi walio wengi, Watanzania wengi waweze kupata fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda hautoshi naomba sasa nijikite katika maazimio ambayo tunaomba Bunge lako liiitake Serikali kwenda kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako Tukufu lipokee maoni na mapendekezo ya Kamati kuwa Azimio la Bunge kwa utekelezaji wa Serikali ili taarifa hiyo ije iletwe namna ambavyo Serikali imetekeleza na kwa kuzingatia ushauri mzuri ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia pande zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo nami niweze kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ndiye anayeniwezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kila sababu ya kuwashukuru wananchi wa Kalambo, tulikubaliana kwamba nuru mpya ya Kalambo, kwa pamoja tunaweza; na hakika wamenirejesha kwa kishindo, nawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ulioletwa unaleta matumaini makubwa sana. Tanzania ya viwanda inawezekana. Viwanda vipi ambavyo tunaenda kuvijenga? Ni hakika Serikali lazima ijenge viwanda vya kimkakati lakini, ni wajibu wa sekta binafsi kushiriki katika viwanda vidogo vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotaka kujenga kiwanda maana yake ni lazima rasilimali fedha iwepo ya kutosha. Bila mtaji wa kutosha hakuna viwanda ambavyo tunaweza kujenga. Serikali ikijenga viwanda vya kimkakati, tukaiachia Sekta binafsi, wanaenda kutoa pesa wapi Hawawezi kwenda kukopa katika mabenki ya kibiashara, kwa sababu unapowekeza katika kiwanda hutarajii return ya haraka. Lazima ni mtaji mkubwa ambao return yake utaipata kidogo kidogo.?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, haiwezekani tuka-plan kwenda kushindwa. Tunapokuwa na Benki ambayo hatujaipa mtaji, kwa maana ya TIB, hakika ni kwamba tume-plan kwenda kushindwa. Tusikubali kufanya kosa hili, tuhakikishe tunaiwezesha Benki yetu ya TIB ili itoe fursa kwa wananchi kwenda kukopa kwa riba ambayo ni rahisi kulipika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashuhuda kwamba asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima na hasa ambao wako vijijini. Sitafarijika hata kidogo na wala sitaki kuamini kwamba Serikali imesahau mpango mzima wa SAGCOT. Tumesema lazima tuwekeze katika kilimo, ikaja mipango mizuri, naamini na hili litakuja; ni kwa sababu inawezekana bado wanakumbuka, ikija detail report itaainisha masuala yote ya kuhakikisha kwamba tunajitosheleza katika kilimo na tena kilimo cha kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali, kwa utaratibu wake na Mpango waliokuja nao wa kuhakikisha kwamba tunaenda kubana matumizi, kutumia pale tu ambapo itaongeza tija. Ni jambo jema. Serikali imeagiza kwamba kuanzia sasa pesa zake zote ambazo Taasisi zimekuwa zikiweka katika Benki za kibiashara, zipelekwe Benki Kuu maana zote ni mali ya Derikali. Sina ubishi! Ubishi wangu unakuja pale ambapo kama utaratibu tutakaoenda kuufanya utasababisha mashirika yetu ambayo yashaanza kufanya vizuri, tukaya-suffocate. Haitapendeza!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni suala la control, naomba niikumbushe Serikali irejee Sheria ya Bajeti Kifungu cha 17, inaeleza kabisa kazi ya Treasury Registrar kwamba mashirika yote ambayo yako chini ya TR watapeleka bajeti zao kule, ataidhinisha na hata kama kuna suala la kwenda kuwekeza, ni lazima wawe wamepata idhini kutoka kwake. Hiyo ni control ya kutosha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile ambavyo wananchi na Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tunapata wasiwasi, ni kwamba utaratibu wa kuhamisha pesa zote kupeleka Benki Kuu, inaweza kuziua Halmashauri zetu. Hakika pia inaweza ikaua mashirika yetu. Sisi ni mashahidi kwamba mwaka 2015 tulivyokuja hapa tulisema kwamba ni vizuri Taasisi zetu zikawezeshwa ikiwa ni pamoja na TPDC ili iweze kushiriki katika uchumi wa gesi na mafuta. Sasa kama utaratibu itakuwa hatuwezeshi wakawa na fungu la kutosha, wakaweza kuwekeza, hakika ushiriki wa Watanzania kwa kupitia shirika letu hautaweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nyie ndugu zangu nyote ni mashahidi kwa jinsi ambavyo Shirika letu la Nyumba la Taifa lilivyokuwa na hali mbovu, leo hii limekuwa ni miongini mwa mashirika machache ambayo yanapigiwa mfano kwa namna ambavyo wanawekeza na naamini na Kalambo watakuja. Sasa zile taratibu kwa wale watu wanaofanya kazi vizuri tusianze kuwa-frustrate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesoma katika Mpango kuna suala zima la kununua ndege. Ni jambo jema sana, lakini haitapendeza tunaposema tunataka kufufua Shirika letu la Ndege, zinanunuliwa ndege mbili, lakini kwa utaratibu ambao utakuwa umewekwa kwa makusudi, wakashindwa hata kununua mafuta kwa sababu OC haijawafikia. Itakuwa hatutendi haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala zima la Wakandarasi wa ndani. Wakandarasi wa ndani wamekuwa wakiidai Serikali kwa muda mrefu. Kutowalipa Wakandarasi tafsiri yake ni nini? Barabara zetu hazijengwi zikakamilika kwa kiwango kwa wakati unaotakiwa. Tafsiri yake ni kwamba, miradi mingi inajengwa kwa gharama kubwa, kwa sababu kwa kutowalipa, wanalazimika kuidai Serikali riba, lakini hali kadhalika wanashindwa kulipa kodi kwa sababu wao wanaidai Serikali na Serikali haijalipa. Nasi tunataka kuwe na mzunguko wa kutosha; walipwe na Serikali, walipe kodi, lakini pia waweze kutoa ajira kwa Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee, Serikali ihakikishe kwamba miradi ile ya barabara ambayo imeshaanza, ikiwa ni pamoja na mradi wa barabara kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda; Mradi wa barabara kutoka Sumbawanga kwenda Kalambo Port, unakamilika kwa wakati ili tuhakikishe kwamba kasi ya Tanzania ya kwenda kuwa nchi ya kipato cha uchumi wa kati, inawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tukubaliane, kupanga ni kuchagua. Haiwezekani tukatekeleza yote, ndiyo maana tukubaliane kwamba bila kujenga reli kwa standard gauge, hakika uchumi ambao tunataka upae na kufika uchumi wa kipato cha kati hatutaweza. Niwasihi ndugu zangu wote bila kujali unatoka eneo gani la Tanzania, tukubaliane mkakati wa kuhakikisha kwamba reli inajengwa. Bahati nzuri nyie ni mashahidi, kuna fungu ambalo lilitengwa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwekeza lazima utarajie kupata kule ulikowekeza. Tujiulize, kutokana na bomba la gesi, ni kiasi gani kinapatikana kama return kwa Serikali na hicho ambacho kinapatikana kipo kwenye mfuko upi? Kama siyo hapo tu, mkongo wa Taifa, pesa nyingi sana imewekwa, tunataka tujue, baada ya kuwekeza return yake iko wapi? Iko mfuko upi kwa manufa ya Watanzania? (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi jioni ya leo hii niwe miongoni mwa wachangiaji wako. Awali ya yote, nalazimika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama leo nikiwa na nguvu ya kutosha na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wananchi wa Kalambo, nuru mpya Kalambo ambayo tumeiahidi tutaitimiza na hasa kwa kasi hii kila mtu ana kila sababu ya kuunga mkono Serikali inayoongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Kubeza ni kama namna tu ambavyo mtu ambaye ameanza safari unamwambia ongeza speed. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu najielekeza katika suala zima la bajeti ya mikoa. Nashindwa kuelewa kama hili limekuwa likitokea kwa bahati mbaya au ni katika design ambayo imewekwa. Ukipitia katika budget allocation, ukienda Mkoa wa Katavi, kupitia TAMISEMI wametengewa shilingi bilioni 3.9, unaujumlisha na Mkoa wa Lindi shilingi bilioni 6.1, unakwenda Mtwara na ya Mtwara imeongezeka hivi karibuni na sababu zinaweza zikawa zinapatikana lakini ni shilingi 10.7, ukienda Mkoa wa Rukwa ni shilingi bilioni 6.7, inawezekana pia hawakujua na Shinyanga nayo imetengewa kidogo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kandege, ni kitabu kipi hicho unachotumia?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki hapa.
MWENYEKITI: Sawa, ili wote tuwe pamoja.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Ndiyo, maana ndiyo bajeti, hii nyingine ni porojo, sisi tunataka twende kwenye facts. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shinyanga imetengewa shilingi bilioni 9.2 na Singida ni shilingi bilioni 9 ukijumlisha mikoa yote hiyo na ukija ukilinganisha na hii yote na ukajumlisha Mkoa wa Manyara ambao ulikuwa sehemu ya Mkoa wa Arusha, mikoa hii miwili wametengewa jumla ya shilingi bilioni 38.3. Jumlisha pesa ya mikoa yote hiyo niliyotangulia kuitaja haifikii pesa ambayo imetengwa kwa ajili ya mikoa miwili na mikoa ambayo ilikuwa mkoa mmoja. Hili nimekuwa nikilisema, ifike mahali ambapo sasa Serikali ituelewe, haiwezekani ile mikoa ambayo tunasema iko nyuma kiuchumi ambayo haijaendelea, hiyo ndiyo ambayo iendelee kutengewa bajeti ndogo, hatuwezi kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya hawa ambao wanapata 27, hebu katafute kura, katafute jinsi gani ambavyo wanaitambua Serikali iliyopo madarakani kaangalie wametoa kura kiasi gani? Inawezekana kuna wataalam ambao wametangulia wako huko waka-design formula ambayo watahakikisha daima wao ndiyo wanapata pesa nyingi katika mikoa yao. Jambo hili halikubaliki! Tunaomba Serikali ituambie ni utaratibu gani ambao wanautumia katika budget allocation. Haiwezekani ambaye yuko nyuma useme ataendelea kuwa nyuma daima dumu. Hii nchi ya kwetu sote, keki kama ndogo tugawane kwa usawa.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi imekuwa ikisikika kwa wale ambao imegawanywa mikoa na Wilaya, Wilaya zingine zinafanana na kata zangu mbili, ukiwaambia kwamba na sisi tunaomba tuongezewe mgao wanasema hapana, huu ni ulaji lakini ni kwa sababu tayari wao ukubwa wa Wilaya ni sawasawa na kata zangu mbili. Mtu kama huyu ukimwambia kwamba Serikali iendelee kugatua madaraka kupeleka huko chini hawezi kuelewa kwa sababu tayari yeye alishatosheka. Naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, nimetoa sample tu ya hiyo mikoa na iko kwenye kitabu hiki. Wakati unakuja kuhitimisha ni vizuri ukatuambia formula gani ambayo inatumika katika kugawanya keki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niseme jambo ambalo limekuwa likinitia simanzi. Katika mikoa yote Tanzania, ukiachia hii ambayo ndiyo imeanza hivi juzi, Mkoa wa Rukwa ndiyo mkoa pekee kwa taarifa nilizonazo ambao hauna Chuo cha Ufundi kwa maana ya VETA. Kwa hiyo, naomba Serikali hii ili sisi tusilazimike kukimbilia huko ambako kuna vyuo, kupitia Wizara zote kwa namna mtakavyoweza kujikusanya ujenzi wa VETA Rukwa iwe miongoni mwa vipaumbele. Kwa sisi Kalambo tayari tulishatenga eneo na tunafuata ramani ili tuanze ujenzi tukiamini kwamba Serikali nayo itatuunga mkono hivi karibuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi na kwa bajeti finyu kama hii ambayo umeiona kupitia TAMISEMI hali kadhalika hatuna Hospitali ya Wilaya. Niiombe Serikali, huko ambako mlishapeleka vinatosha, sasa hivi tuelekeze nguvu maeneo ambayo tunaita peripherals ili wananchi wakienda sehemu zote za Tanzania wasijione ukiwa kwamba ukifika maeneo fulani inakuwa kama vile haupo Tanzania. Niiombe Serikali, bado hatujachelewa, naona Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko pale ana-take note, Mikoa yote ambayo ni under privileged ipewe kipaumbele tuhakikishe kwamba inapata allocation ya fedha ya kutosha na wananchi wako tayari kuiunga Serikali yao mkono si tena kwa hila bali kwa upendo wa dhati kutoka moyoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niyaseme machache ili yachukuliwe kwa uzito niliotaka ufike, kimsingi naunga mkono bajeti. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ili nami nisije nikamaliza kama Mheshimiwa Mwambe bila kuunga mkono, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu, afya na uwezo wa kusimama jioni ya leo, niungane na Watanzania wenzangu na Wabunge wenzangu ili kuishauri Serikali katika kuhakikisha kwamba kasi ya maendeleo na hasa umeme inaenda kutendeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kushauri kwa kuisaidia Serikali na hasa nimesikia hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri, akiwa anaelezea jinsi ambavyo bajeti imeongezeka kwa kiasi cha asilimia 50. Naomba nimkumbushe, hiyo asilimia 50 atakuwa amesahau shilingi bilioni 79, kwa hiyo, inapaswa iongezeke kwa kiasi cha zaidi ya asilimia 50. Hiyo shilingi bilioni 79 iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma katika Sheria ya Bajeti na hasa katika uanzishaji wa Mfuko wa REA, fungu lile ni ring fenced. Maana yake ni nini? Pesa hiyo haiwezi kwenda kutumika kwa shughuli nyingine yoyote. Kwa mujibu wa sheria inatakiwa iende upande wa REA. Sasa nini kilichotokea? Serikali inawezekana walijikopesha kiasi cha shilingi bilioni 79 ambacho wana wajibu wa kuhakikisha kwamba kinarudi na kinaenda REA, kwa sababu lengo lake ni kupeleka umeme vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kile ambacho ametaja kwamba ni ongezeko la asilimia 50, ukichukua na hii bakaa unayovuka nayo, naomba urekebishe vitabu vyako visome kwamba kuna shilingi bilioni 79 ambayo inapaswa iongezeke katika bajeti yako. Najua Serikali wamejikopesha na muungwana akikopa ana kawaida ya kulipa na Serikali hii inayoongozwa na CCM italipa ili dhana ya kuhakikisha kwamba umeme unafika kila vijiji Tanzania inaenda kufikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo napenda kuchangia ni kuhusiana na suala zima la uzalishaji wa umeme. Ukimsikiliza Mheshimiwa Waziri, tunajipongeza tumezalisha umeme wa kutosha, lakini ukitazama projection tuliyokuwa nayo na nini ambacho tulitarajia kuzalisha, bado kasi yetu haitoshi. Tulisema kwamba tungezalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe pale Kiwira, ilikuwa tuzalishe umeme pale Mchuchuma, lakini haya yote hatujaweza kufanya. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri anapokuja kumalizia hotuba yake, atuambie baada ya miradi hii kutofanya kazi, tunajielekeza wapi kwenye vyanzo vingine vya uhakika ili kasi ya kupata umeme wa kutosha kwa ajili ya kutosheleza Watanzania na kuuza kwa nchi jirani tunakwenda kuifikia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimwongezee vyanzo vingine vya umeme, ukienda Mkoa wa Rukwa pale, kuna makaa ya mawe maeneo ya Namwere pale. Wachunguzi wanasema kwamba makaa yale yanafaa kwa kuzalisha umeme. Namwomba Mheshimiwa Waziri aelekeze nguvu kule. Kama haitoshi, maporomoko ya Kalambo, maporomoko ya pili Afrika baada ya Victoria Falls ambayo hayajatumika vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii, hebu tutumie chanzo hiki kwa ajili ya kuzalisha umeme na kazi ni ndogo tu. Kama imewezekana kuwa na mahusiano mazuri tukaanza kuzalisha umeme kule Rusumo, ni rahisi kabisa kwenda kwa majirani zetu Zambia kwa sababu yale maanguko yako mpakani mwa Tanzania na Zambia. Hebu tufanye utafiti, maanguko yale tutumie kwa ajili ya kuzalisha umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze upande wa REA. Tumeambiwa tunaenda REA Awamu ya Tatu, ni jambo jema. Hata hivyo, ni lazima tujitathmini; katika hii Awamu ya Pili tumenufaika sawa? Haiwezekani maeneo kama Wilaya ya Kalambo ilikuwa na umeme sifuri, halafu unaposema tunaenda Awamu ya Tatu bila kutazama huyu ambaye alikuwa na sifuri amepata nini? Naomba kuwe na exception katika mtazamo kabla hatujakwenda REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri na maeneo mengine ambayo umeme ulikuwa haujafika, barua nimepeleka ofisini kwake, kwa uchache tu nimtajie vijiji ambavyo vimetajwa kwenye barua niliyopeleka kwake, ni pamoja na Kijiji cha Mwazye ambako anazaliwa Muadhama Polycarp Pengo, hakuna umeme pale. Pia Kijiji cha Kazila, Kijiji cha Kamawe, Tatanda, Sopa, Ninga, Kanyezi, Musoma na vyote hivyo viko kwenye barua. Alikuja Makamu wa Rais Mstaafu, akawaahidi wananchi; amekuja Mheshimiwa Rais, akatoa ahadi, naomba aende kutekeleza kabla hatujaenda hiyo awamu ya tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la TPDC. Ukitaka kushiriki vizuri, lazima uwekeze ili katika mnyororo wa uzalishaji na utafutaji wa mafuta na gesi, Shirika letu la TPDC ambalo ni kwa ajili ya Watanzania wote liwe na nguvu, linatakiwa liwekeze kwa maana ya mtaji. Ukisoma ile sheria, imeeleza kabisa kwamba ili uweze kushiriki, lazima uwekeze kiasi cha pesa ambacho kinatakiwa. Naomba Mheshimiwa Waziri kwa kupitia Wizara yake tutazame kwa jicho la huruma, jicho la maslahi mapana kwa ajili ya Watanzania wote tuhakikishe kwamba tunawekeza vya kutosha TPDC. Hii itaondoa hii dhana ambayo watu wengine wamekuwa wakisema eti wagawane wao lakini Watanzania kwa ujumla wetu tusiwe na shirika letu ambalo ndiyo kwa ajili yetu sisi sote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itasaidia sana, itaondoa kelele ambayo imekuwa ikijengeka kwamba eti mzawa ni kumjali mmoja mmoja. Hebu tujaliwe kwa ujumla wetu tuwekeze katika kampuni yetu kama ambavyo Mataifa mengine wamefanya. Statoil, lile ni shirika la Kiserikali, Petrol Brass ni shirika ambalo part ni Serikali na watu binafsi. Kwa hiyo, ni vizuri tuhakikishe nguvu hii tunapelekea huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini haya machache ambayo nimeyaongea yamechukuliwa kwa uzito na yatafanyiwa kazi. Nakushukuru.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukushukuru na kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama jioni ya leo ili niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na ripoti ya Kamati ya Bajeti maana mimi ni sehemu ya taarifa ile, hivyo naiunga mkono kwa asilimia mia moja. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yote kwa ujumla. Baada ya pongezi hizo naomba nitoe michango kidogo kwa sababu naamini mengi yameandikwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kuipongeza kwa moyo wa dhati kabisa TRA kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, hii achievements ambayo imeonekana ni ushirikiano miongoni mwao na wanaweza kufanya vizuri zaidi, naomba tuwatie moyo. Sisi Wabunge tuwe ni sehemu ya kuhimiza ulipaji wa kodi, bila kulipa kodi nchi hii haiwezi kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachia mbali Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mapato kwa maana ya Commissioner General, Wakuu wa Idara karibu wote ni Makaimu. Sasa haiwezekani, watu ambao wanafanya kazi nzuri na mpaka wanavuka malengo waendelee kukaimu hili halifai. Naiomba Serikali kwa kupitia Bodi husika hebu hawa watu ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu kama Makaimu muwa-confirm na kama hawatoshi, muwaondoe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la pili ambalo naomba kuchangia na hili limejitokeza bayana kwenye taarifa yetu, ni namna ya ushirikishwaji wa Bunge kwa kupitia Kamati ya Bajeti pale ambapo Mheshimiwa Waziri wa Fedha anakwenda kukutana na Mawaziri wenzake Arusha. Jambo hili halijaanza katika mwaka huu wa fedha, lilianza mwaka wa fedha 2015/2016 na ukisoma report yetu hatukuridhika na kile ambacho kilijitokeza na Waziri mwenye dhamana wa kipindi hicho, aliahidi kwamba halitajitokeza, lakini safari hii limejitokeza tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba, wenzetu tunavyokutana nao kwa maana ya Mawaziri wa Fedha wa nchi nyingine, wanakwenda wakiwa wamejiandaa, wamehusisha Mabunge ya kwao kwamba baadhi ya mambo wanakwenda nayo wakisema haya ni ya kufa na kupona. Wanakwenda kuyatetea, wanajenga hoja na wanahakikisha kwamba yanapita.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri, kuna msururu wa vitu vingi sana ambavyo vimepitishwa. Imekuja orodha ya nondo nyingi, unasema haya yametoka wapi? Alishauriana na akina nani? inachekesha mahali fulani unakuta kwamba, wanasema tuondoe kodi ili tuweze kulinda viwanda vya kutengeneza viberiti kwa sababu hatuna misitu ya kutosha!
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna viwanda, kiwanda chetu kilichokuwepo cha Moshi kimekufa, leo tunasema kwamba hatuna miti ya kutosha kwa ajili ya kukidhi viwanda vyetu, hivyo viwanda ni viwanda vipi? Ni kwa manufaa ya nani? Kwa faida ya nani? Naamini, mapendekezo ambayo yametolewa na Kamati ya Bajeti kwamba jambo hili litazamwe lisijirudie, hakika halitajirudia, maana Mheshimiwa Waziri ni msikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu yangu nyingine ni kuhusiana na suala zima la mradi wa maji na hasa maji vijijini pamoja na suala zima la ujenzi wa zahanati na vituo vya afya. Tumependekeza kwamba iongezeke tozo ya sh. 50/= ili jumla iwe sh. 100/= kwenye tozo za mafuta kwa maana ya petrol na diesel. Hii itatuwezesha kutupatia kiasi cha shilingi bilioni 250 na tumependekeza kwamba mgawanyo wa pesa hizi bilioni 220 iende kutatua tatizo la maji vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Mbunge hata mmoja ambaye anaweza akaniambia kwamba kwenye Wilaya yake hawana tatizo la maji, hayupo! Kwa hiyo, ni vizuri tukatoka jasho jingi kulikoni tukasubiri kuja kuvuja damu nyingi. Naomba Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla mlisikilize. Pia tumependekeza kwamba bilioni 30 iende kusaidia kumalizia ujenzi wa zahanati. Ni nani asiyejua kwamba ukirudi kwenye vijiji vyetu, wananchi wameitikia kwa moyo wa dhati wakajenga Zahanati zikafika usawa wa lenta, leo ukienda unamwambia mwananchi ashiriki kwenye shughuli nyingine ya maendeleo wakati maboma anayatazama hapati huduma ya afya, hawatuelewi. Kwa hiyo naomba hii shilingi bilioni 30 iende kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, karibia mwisho, nimesikia Serikali wana mapendekezo kwamba safari hii wanaenda kufanya adjustment kwa inflation rate ya five per cent, ni jambo jema! Lakini jambo hili haliwezi likaenda in a blanket form, lazima kuwe na exceptions, ukiongeza kwenye bia haina tatizo kwa sababu wauzaji wa bia wameongeza bei tangu mwezi Februari, bia zimeongezeka kutoka sh. 2,300/= mpaka 2,500/=. Kwa hiyo hiki ambacho mnafanya adjustment is ok! Wala haitaathiri chochote, kwa sababu walishaanza ku-enjoy!
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo langu nalipata kwenye suala zima la vinywaji baridi na hasa soda na juisi. Hivi leo hii tunasema kwamba tunaweka excise duty ya asilimia tano kwenye soda na wakati huo Serikali hiyo inasema kwamba tunataka Mtanzania mnyonge ambaye ndiyo mnywa soda, leo hii ndiyo tunaenda kumwwekea five percent! Ukitazama kipindi hiki ndiyo kipindi ambacho wenzetu waliojaaliwa kufunga wanafunga, anataka wakati anapata futari yake apate na juisi, apate na soda. Ndiyo kipindi kweli Serikali mnataka mkaongeze hiyo? Bei ya soda haijapanda kwa ujumla kama miaka mitano, leo hii mnataka itoke sh. 500/=, iwe sh. 600/=, halikubaliki hili! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vyanzo vingi, let‟s think outside the box.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja iliyoletwa mbele yetu. Aidha, baada ya kuunga mkono hoja naomba nichangie baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine ikiwa ni mara yangu ya nne kuongelea suala zima la maporomoko ya Kalambo pamoja na Hifadhi ya Msitu wa Kalambo kuwa chini ya TANAPA nimekuwa nikileta ombi hili na nitaendelea kurudia nikiamini ipo siku Serikali itanielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maporomoko ya Kalambo yako mpakani mwa nchi ya Tanzania na Zambia. Pamoja na maanguko ya maji kuwa mazuri sana upande wa Tanzania kuliko upande wa Zambia lakini kwa upande wa Zambia wameyatangaza maporomoko haya kwamba ni maporomoko ya pili Afrika baada ya yale ya Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linashindikana kutokana na uwezo mdogo wa Halmashauri ya Kalambo kwa maana ya uwezo mdogo wa kifedha na weledi katika tasnia ya utalii. Hivi ninavyoongea tembo wanaokadiriwa 17 mpaka 25 wapo ndani ya msitu wa Kalambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara kwa mara nyingine maporomoko ya Kalambo na Msitu wa Hifadhi ya Kalambo viwe chini ya TANAPA ili wahifadhi na kutangaza vivutio hivi vya utalii.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi jioni ya leo ili kuchangia. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam kwa ujumla, mengi nimechangia kupitia Kamati ya Bajeti. Kwa leo kuna machache ambayo nadhani iko haja ya kuongezea ili kumtengeneza ng‟ombe vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza wachangiaji wengi ni kama vile dhana haieleweki kwamba Serikali inataka na sisi tujazie ya kwetu, badala yake watu wanakuja wanalalamika kama vile essence ya kuwepo wao kuchangia haina maana. Tungewasikia wapi kama fursa hii isingepatikana, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge ni fursa ya kuchangia ili tuwe na mpango mzuri kwa ajili ya kulivusha Taifa hili, Taifa ni la kwetu sote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma maoni ya Kambi ya Upinzani wanachokisema ni kama vile wana nchi ya kwao kiasi kwamba hata boti hili likienda vibaya wao wana option ya pili, haitujengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo ambayo nimeyatoa kwa utangulizi naomba nichangie kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee ukurasa wa saba wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri ambayo katika matazamio yake anatarajia kwamba bei ya mafuta itaendelea kuwa nzuri. Naomba tukumbushane OPEC walishakubaliana kwamba watapunguza uzalishaji wa mafuta, tafsiri yake ni nini? Kama uzalishaji wa mafuta utapungua maana yake bei itapanda, sasa katika mipango yetu lazima tulijue hili na tukishalijua sasa tujiandae tunafanyaje kama Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwombe Mheshimiwa Waziri, ni manufaa yapi ambayo tulipata kama Taifa baada ya bei kushuka? Kwa sababu haiwezekani tuache liende kama linavyoenda bei ikishuka hakuna ambacho Serikali inafanya, bei ikipanda hakuna ambacho Serikali inafanya. Ni vizuri tukawa na mkakati maalum kwamba pale ambapo inatokea bei kushuka tuone faida moja kwa moja ambayo inapatikana kutokana na anguko la bei ya mafuta. Lakini ingependeza sana kama ungeanzishwa Mfuko Maalum ili kuweza ku-stabilize pale ambapo bei zikipanda sana basi kuwe na namna ya kuweza ku-absolve shock ambazo zinajitokeza wakati bei za mafuta zimepanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote ni mashuhuda kwamba pale ambapo bei ikipanda hata siku moja tayari siku inayofuata tunaambiwa nauli zinapanda na kila kitu kinapanda. Sasa ni vizuri katika mipango yetu tukajiandaa tunaitumiaje fursa kama hiyo pale inapotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mpango wa maandalizi ya bajeti kuna prediction kwamba hali ya chakula itakuwa nzuri. Naomba nipingane na hili kwasababu kwa taarifa tulizonazo ni kwamba kuna ukame unatarajiwa kuwepo. Kwahiyo, hatuwezi tukasema hali ya chakula itakuwa nzuri, sio sahihi. Kwa hiyo, kwenye mipango yetu lazima factor hiyo tuiweke na tuseme sasa hiki kinachotokea tunafanyaje ili hali ya uchumi wetu isije ikaharibika kwa kiasi kikubwa. Ni vizuri katika mipango ambayo inawekwa tukaweka hiyo factor kwa sababu ipo; kama jambo una uhakika litatokea ukajifanya kwamba hulijui utakuwa husaidii Taifa. Ni vizuri tukalijua, tukajiandaa kwamba tunafanyaje kama Taifa ili tusije tukapata tabu kutokana na upungufu wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza wenzangu kuhusiana na kupungua kwa mizigo bandarini. Ni kweli, lakini ambacho ningeomba kiingie na kionekane vizuri kwenye mipango yetu, sisi sote ni mashuhuda kwamba bandari ya Dar es Salaam haina uwezo wa kupokea meli kubwa za kuanzia 3G, 4G uwezo huo hatuna, nini kifanyike? Tumekuwa tukisikia muda mrefu kwamba bandari ambayo itajengwa Bagamoyo itakuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kupokea meli za ukubwa wa fourth generation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipata fursa ya kutembelea bandari ya Mombasa ukaona uwekezaji uliofanywa na wenzetu na hawakuishia kwenye Bandari ya Mombasa wameenda sasa Bandari ya kule Lamu, kiasi kwamba tusitarajie. Hata kama tutafanya upanuzi wa geti namba 13, 14 bila kuanza seriously ujenzi wa bandari ya Bagamoyo hakika tunajiandaa kwenda kushindwa kama Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri katika mipango yetu tukajielekeza katika hilo kwamba hata ungepanua vipi Bandari ya Dar es Salaam imeshafika mwisho. Kwahiyo, ni vizuri katika mipango yetu tukajielekeza katika kuanza kujenga bandari ya kisasa ambayo itakuwa na uwezo wa kupokea meli za kisasa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia taarifa na hii pia tulikutana nayo hata wakati tumekutana na Wizara ya Fedha. Kuna fikra ndani ya Serikali kwamba mpango unaokuja sasa hivi juu ya currency yetu ni kuhama kutoka utaratibu wa fluctuation floating twende kwenye fixed na fikra iliyopo Serikalini ni kwamba tu-peg shilingi yetu kuibadilisha na dola kwa shilingi 2,193 kama sijakosea, ni jambo jema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tafsiri yake ni nini? Ni kwamba tayari tunajiandaa kwamba shilingi yetu inakwenda kuanguka, faida ya ku-devalue shilingi inakuwa ni rahisi kwa mtu ambaye anakuja kuwekeza kwetu kwa ile direct foreign investment lakini disadvantage ambayo tunakuwa nayo ni kwamba itakuwa ni gharama sana kwa mtu ambaye anataka kupeleka mizigo nje kutoka Tanzania akija kubadilisha na pesa yetu atakuta anapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri hii hali ya kuacha soko ndio liamue na tutafute namna nzuri ambayo itahakikisha kwamba shilingi yetu haiyumbi sana, ndiyo namna iliyokuwa nzuri kulikoni habari ya kwamba unasema fixed, ukishafanya fixed ikija kutokea kipindi uchumi umeanguka maana yake tutalazimika ku-devalue shilingi yetu kwa kiasi kikubwa sana. Ni vizuri ikafanyika tathmini na utafiti wa kutosha kabla hatujafikia hatua hiyo, tujue madhara ambayo tumekuwa nayo kwa kuachia bei ya soko ni yapi na hicho ambacho tunatarajia kukifanya faida yake ni ipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapendeza sana tukiwa na makampuni ya Kitaifa kwa ajili ya Watanzania, sioni katika mpango unaokuja nia thabiti ya kuhakikisha kwamba TPDC inawezeshwa kwa niaba ya Watanzania ili kuweza kushiriki katika upstream na downstream katika suala zima la mafuta na gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikataba iliyopo mizuri kabisa inaonesha kwamba, wakiweka mtaji basi ushiriki wao na share ambayo watakuwa wanapata ni kubwa, lakini pale ambapo hawezeshwi kwa maana ya capital, kitabaki kugawanywa kile kidogo ambacho kimebaki. Sasa kwa Taifa ambalo tungependa kampuni ya Taifa kama zilivyo State Oil, Petrolbras ni kwamba Serikali zao ziliwekeza ndiyo maana makampuni haya yakawa na uwezo mkubwa. Ni vizuri na sisi tukahakikisha kwamba TPDC inawezeshwa kwa ajili ya Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la uvuvi wa bahari kuu. Silioni hili likijitokeza dhahiri lakini limekuwa likisemwa siku nyingi. Nakumbuka katika bajeti iliyotangulia ya 2015/2016 ilikuja Wizara ya Uvuvi wakisema kwamba wanahitaji pesa kwa ajili ya kununua meli ya doria. Ikatengwa nadhani kama shilingi milioni 500 wakapewa, hadithi ya hiyo pesa imetumikaje mpaka leo haijulikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, haiwezekani kile ambacho tunapata kwenye bahari kinazidiwa na maziwa ya Victoria na Tanganyika. Maana yake kuna tatizo kubwa ambalo hatujafanya kiasi kwamba wanakuja Wakorea kuvua samaki wengi sana wanatajirika kutoka katika maji ya kwetu lakini sisi kama Taifa tunapata nini? Ni vizuri sasa likajitokeza waziwazi kwamba kama Taifa tunafaidika vipi na bahari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusiana na General Tyre; sisi sote ni mashahidi, Wabunge wote tunatumia magari, kwa hiyo hatuna jinsi lazima tununue matairi kwa ajili ya magari, kwa hiyo soko lipo wazi hata kama mngekuwa na uhakika wa ku-service gari za Wabunge tu una uhakika wa kupata tairi ambazo zina ubora lakini soko lipo la kutosha nchi zote hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kasi ya kufufua General Tyre ni vizuri ikaonekana dhahiri; haipendezi tukaendelea kutazama tu kwenye makaratasi, inatosha tunataka utekelezaji. Kama imeshindikana tuambizane kwamba idea hii imeshindikana, labda tuanze thinking nyingine, lakini ukirejea kama miaka minne, mitano General Tyre inatajwa, Mchuchuma na Liganga inatajwa, kule Natron inatajwa, itoshe kutajwa tunataka kwenda kutenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini katika Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo tunataka maneno kidogo vitendo viwe vingi, vitendo vikiwa vingi huna haja ya kusema sana wenzako watakuwa wanatafuta namna gani ya kukosoa. Lakini pale unapotenda kama ambavyo tumetenda kuhusiana na suala zima la ndege, kuna wengi walibeza wengine wakasema ni ndege chakavu, lakini ukija hata asiyekuwa na macho atapapasa, atajua kwamba hii siyo ndege chakavu, ni ndege mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na naunga mkono hoja.

The Chemist Professionals Bill, 2016

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika muswada ulioletwa hapa Bungeni. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wote walioshiriki katika uandaaji wa muswada huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati najaribu kupitia taarifa ya Kamati ya sekta husika, kimsingi wameridhia pamoja na mapendekezo machache sana ukizingatia kwamba Muswada huu umefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa ndiyo maana naendelea kuwapongeza, hongereni sana kwa Muswada mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie katika maeneo machache kama ifuatavyo na la kwanza, ni ukweli usiopingika kuhusu umuhimu wa maabara ya Mkemia Mkuu lakini kwa kipindi kirefu sana kulikuwa na ufinyu mkubwa sana wa kibajeti kiasi kwamba zile kazi ambazo walitakiwa kuzifanya kwa ufanisi hawakuweza kuzifanya. Kwa kuletwa kwa Muswada huu na kuwa na subvote yake ambayo itasomwa kupitia Wizara husika, naamini Idara hii itatengewa pesa za kibajeti za kutosha. Tafsiri ya bajeti ni kwamba unaipa uwezo mkubwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuweza kutimiza wajibu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Ofisi hii ilikuwa na ufinyu mkubwa sana wa bajeti. Taarifa zinaonesha kwamba kuna kipindi walikuwa na uwezo wa kuwa na mapato ya shilingi bilioni mbili. Naomba niipongeze Wizara kwa kushirikiana na Mkemia Mkuu wa Serikali wamepandisha kiwango cha mapato kutoka shilingi bilioni mbili mpaka kufika shilingi bilioni 10. Ukitaja shilingi bilioni 10 inaweza ikaonekana kama ni pesa nyingi lakini ukilinganisha na majukumu yake na hasa kutokana na kuongezeka kwa kesi za kijinai ambazo zinahitaji uchunguzi ufanyike ili kesi ambazo zimerundikana ziweze kupatiwa ushahidi kiasi hiki cha pesa hakitoshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi sote ni mashuhuda kwamba wakati polisi wamekuwa wakikamata hayo yanayoitwa madawa ya kulevya lazima taarifa kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ipatikane ambayo inathibitisha kwamba haya kweli ni dawa za kulevya au sivyo. Nitaomba niunganishe na wachangiaji wengine ambao wanasema kwamba ni vizuri kazi hii ikaachiwa polisi, mimi nasema hapana. Nasema hapana kwa sababu gani?
Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa mashuhuda tukipata taarifa kwamba kuna watu ambao wanabambikiziwa kesi kutokana na baadhi ya polisi kutokuwa waaminifu sasa kama tutampa na kazi yeye ndiyo a-prove kwamba sampuli hii ni madawa ya kulevya au la maana yake tunataka akamate yeye mwenyewe, afanye uchunguzi yeye mwenyewe, akatoe ushahidi yeye mwenyewe jambo hili halikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi itasaidia kwamba hata pale ambapo mahakamani unapelekwa ushahidi kutoka kwenye chombo ambacho ni independent ushahidi ule utaaminika na kila mtu atajua kwamba ametendewa haki. Sikubaliani hata kidogo pamoja na polisi kuwa na kitengo chao cha forensic, lakini wafanye kazi zile ambazo zitawasaidia katika kufanya uchunguzi wao ili kubaini matukio lakini siyo kupata uhakika kwamba ushahidi unaopelekwa mahakamani wao wawe ndiyo wameutengeneza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni mashuhuda kuna kipindi tuliambiwa zimekamatwa dawa za kulevya mara unaambiwa kwamba ilikuwa ni unga wa muhogo, sijui unga wa mahidi. Sasa tukienda kwa utaratibu huu sidhani kwamba tutakuwa tunatenda haki. Kwa kukitengea kitengo hiki bajeti ya kutosha tuna imani kabisa Ofisi za Kikanda zitaimarishwa na uchunguzi ambao unafanyika majibu yake yatapatikana kwa kipindi muafaka na hivyo huu mlundikano wa sampuli nyingi ambazo lazima zipelekwe Dar es Salaam itakuwa imepungua kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema kwamba muswada huu umetendewa haki na Kamati ya Kisekta niishie kwa kutoa huo mchango mdogo na kuunga mkono hoja. Nashukuru sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's