Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Ignas Aloyce Malocha

All Contributions

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuingia tena kwa mara ya pili katika mjengo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Wananchi wa Jimbo la Kwela kwa kuniwezesha, kwa kuniamini kunirudisha tena ili niweze kuwatumikia na wananchi hao walisimama kidete sana japo kuwa kulikuwa na mizengwe mingi sana lakini wananchi waliweza kusimama na hatimaye kuniwezesha kurudi katika ukumbi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Magufuli, kwa kasi hii aliyoianza ya kusimamia wananchi. Ni kasi ya hali ya juu na mimi nawapongeza wale ambao wanatambua kwamba kasi ile ndiyo iliyokuwa inahitajika katika nchi hii kwa sasa. Nawapongeza na Mawaziri wote ambao wametambua hivyo na wameanza na kasi hiyo, ninachowaomba Mawaziri wote mtambue kwamba mna watu wenu mpaka huko chini waimarisheni, wabadilisheni kifikra ili waendane na kasi hii ya Mheshimiwa Magufuli. (Makofi)
Kwa sababu Mheshimiwa Magufuli hawezi kufanya kazi peke yake bila sisi wote kujibadili kufanana na yeye, atachoka lazima tumsaidie na kumsaidia ni kuweka mtandao wa kasi kuanzia ngazi ya juu mpaka kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu katika kuchangia Mpango wa Maendeleo 2015/2016. Sisi tunatambua kwamba mpango huu wa maendeleo umelenga katika kukuza uchumi, katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na umaskini, katika kukuza pato la Taifa. Hata hivyo, nataka nichangie kwa upande wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua sisi wote kwamba nchi yetu sehemu kubwa ya wananchi wanategemea kilimo na katika kilimo, nataka nizungumzie jambo moja, lazima tujiridhishe hivi Watanzania wote waliopo mijini na vijijini wote wana ardhi ya kutosha kuwaendeleza? Hilo ni la kwanza kujiuliza, na mimi nasema baadhi ya maeneo yanawezekana yanatosha lakini maeneo mengi bado ni tatizo. Ni tatizo kwa sababu tumeachia watu wachache wameatamia maeneo makubwa, Serikali inazungumza kila siku haichukui hatua. Sijaona ni kwa sababu gani Serikali inachelea kuchukua uamuzi wa haraka, hii haitaji hata kusubiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara nyingi nimekuwa nikisimama hapa nikitetea wananchi wa Jimbo la Kwela kuhusu shamba la Malonje nimelizungumza kadha wa kadha hatimaye hata kwenye uchaguzi imeniletea mpambano mkubwa sana lakini Mwenyezi Mungu akisimama hakuna ubishi ndiyo maana niko leo hapa. Wananchi wa Jimbo la Kwela nitaendelea kuwatetea lazima shamba hilo lirudishwe mikononi mwa wananchi. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe Mwenyewe umefika mara ya mwisho ukasema mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuzungumzia suala la ardhi hii ya shamba hili la Malonje naomba utimize ahadi yako wananchi wale warejeshewe lile shamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine katika upande wa ardhi na mimi nataka niishauri Serikali. Serikali ni kweli ilitenga Mapori ya Akiba. Unaposema mapori ya akiba lazima uende na pande zote mbili, mapori ya akiba aidha kwa wanyama lakini mapori ya akiba kwa binadamu, tusiende upande mmoja. Wakati mapori yale yametengwa baadhi ya wananchi walikuwa hawajaongezeka lakini sasa hivi watu wameongezeka. Unaita pori la akiba lakini wananchi wananyanyasika hawana kwa kulima, pori hilo halina mnyama hata mmoja hata ndege mmoja, Jamani huu ni ubinadamu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Pori la Uwanda Game Reserve. Linatesa wananchi isivyo kawaida na halina faida yoyote kwa Serikali na nashukuru Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii nimeongea na wewe, nimekusimulia kwa kirefu sana na nikakuomba ufike, inawezekana maneno haya ninayozungumza usiyaamini, basi ufike ukaone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanakatiza mle kwenye lile pori la akiba, wananyang‟anywa majembe, wananyang‟anywa panga zao, wananyang‟anywa fyekeo, pikipiki, wanapigwa wana nyanyasika, wakati pori lenyewe halina mnyama hata mmoja. Jamani tumefika wapi hapo? Haya mambo mengine ni ya kuchukua hatua za haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uamini, maana mara nyingine mnachukulia sisi kama ni wanasiasa uende, namwomba Waziri wa Maliasili afike eneo lile. Hata hivyo, nikupongeze kwa sababu nilipokueleza ulitoa amri ya wananchi kurejeshewa vifaa vile walivyokuwa wamenyang‟anywa, nakupongeza katika hilo na naomba uendelee katika kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni umeme, tunatambua kabisa maendeleo hayawezi kuja bila umeme, lakini nitoe masikitiko kidogo katika Jimbo langu au Wilaya yangu ya Sumbawanga Vijinini, pamoja na Wilaya hii kuwa ya siku nyingi, pamoja na jitihada zote za Serikali, Jimbo langu halina umeme hata kijiji kimoja. Vijiji 114, Kata 27, watu zaidi ya 450,000, halina hata kijiji kimoja chenye umeme.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Wakati mwingine Serikali inaweza ikatutambua sisi viongozi, tunaotokana na Chama cha Mapinduzi kama vile tunaipinga Serikali hapana, ni masikitiko ya kuona wananchi wanahangaika, hivi Serikali hii inaendeshwa kwa upendeleo?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua Muhongo ni mchapakazi na nimeongea na wewe ninataka kwa kweli wananchi hawa wapate umeme, awamu ya kwanza ulisema utatoka Sumbawanga- Laela, ni nguzo tu zimelala, awamu ya pili ni Ukanda wa Ziwa Rukwa, kwa hiyo naishauri Serikali iweze kuhimiza kwa haraka ili wananchi hawa waweze kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni kupunguza ukubwa wa maeneo ya Utawala, nazungumzia Jimbo langu la Kwela ni Jimbo kubwa na lina watu zaidi ya 450,000 lina sifa zote za kugawanya na nilipozungumza hapa kwa mara ya mwisho na Waziri Mkuu Mstaafu ali-support, kwa sababu anafahamu. Hata Mheshimiwa Keissy juzi amezungumza, hata baadhi ya Wabunge ambao wamekwenda kule akina Paresso wanafahamu, Mheshimiwa Mbatia, Mheshimiwa Aeshi wanafahamu, ni Jimbo kubwa kuliko, wakati mwingine unasema nitafanyaje kazi katika Jimbo hili, ni kubwa ukienda upande huu wengine wanakusahau.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Naishauri Serikali na bahati nzuri uliyekuwa Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Manyanya uko hapa, naomba jambo hili tulivae wote, tuihabarishe Serikali inatuletea matatizo makubwa sana, Jimbo hili linatakiwa kugawanyika, kama tunatenda haki kwa sababu lina sifa zote. Yapo Majimbo yamegawanywa zaidi ya mara 3, hayana sifa zote. Lakini Jimbo langu limebaki pale pale.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mapendekezo tumeleta yote ya kuomba Jimbo, kuomba Wilaya, kuomba Halmashauri, hakuna hatua hata moja ambayo imechukuliwa, sasa jamani na hawa wananchi mnawaweka katika upande gani? Naishauri Serikali ijaribu kutenda haki kwa maeneo yote yenye matatizo kama haya, nimeona nilizungumzie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni miundombinu ya barabara, ninapozungumzia barabara nizungumzie barabara ya kutoka Kibaoni, kuja Kiliamatundu na kwa maana hiyo ukifika Kiliamatundu unatakiwa ukatishe uende Kamsamba, ukatokee Mloo. Ile barabara ina zaidi ya kilometa 200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali kwa sababu katika ilani mmeiweka katika kipaumbele cha kuifanyia usanifu. Hata hivyo, naomba isiwe usanifu ile barabara inatakiwa kutengenezwa kwa kiwango cha lami kwa sababu ina uchumi mkubwa sana. Hizi kilometa 200 ninazosema karibuni kila baada ya kilometa tano kuna kijiji cha wananchi wenye uzalishaji, ukitengeneza barabara hii utakuwa umeufungua ukanda ule kiuchumi, utaongeza pato kwa wananchi, utaongeza pato kwa Serikali. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kushughulikia barabara ile kwa kiwango cha lami, ikiwa ni pamoja na kutengeneza daraja la mto Momba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa miaka mitatu tunaambiwa upembuzi yakinifu tumechoka na maneno hayo, tunataka waanze kujenga. Ukijenga daraja hilo umeshawaunganisha wananchi na Wilaya ya Momba wanaotokea Mloo, uchumi utaenda kwa kasi kubwa sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kuchukua jambo hili katika masuala ya utekelezaji, kwa sababu linaumiza sana na ni ukanda wenye uchumi mkubwa sana, uzalishaji wa mpunga, ufuta, uvuvi. Sasa tunapozungumzia kutengeneza barabara si tuangalie na vigezo, vigezo ni kuongeza uchumi wa wananchi na Taifa zima kwa ujumla siyo unapeleka barabara huna hata matumaini ya kurejesha uchumi wenyewe.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.(Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nishukuru kupata fursa hii ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme ninaunga Mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa asilimia 100. Sababu ziko wazi, imesheheni karibu pande zote, mikakati yote, kutokana na utendaji wa kazi tunaouona kwa sasa wa Mheshimiwa Rais na Mawaziri wake hatuna mashaka, tusonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie upande wa hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa nane mpaka wa 10 katika eneo la siasa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maagizo kwenye Tume ya Uchaguzi kubaini sababu zilizopelekea wapiga kura milioni saba kutokupiga kura. Idadi hiyo ni kubwa sana, lazima na sisi tuweze kueleza baadhi ya sababu ambazo zinaweza kuwa kwa namna moja au nyingine zimechangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sababu ni umbali wa vituo vya kupigia kura. Watu walikuwa wanatembea kilometa 20 mpaka 10 kufuata kituo cha kupigia kura, sasa ni watu wachache ambao wanaweza wakamudu hali hiyo, lakini zipo sababu zingine za baadhi ya wananchi kukata tamaa zikiwemo sababu zifuatazo:-
Kwanza, wananchi kukata tamaa kutokana na baadhi ya Viongozi kutotenda haki, kuwa na upendeleo na ubinafsi uliokithiri. Hiyo ni sababu mojawapo inayowafanya wananchi wakate tamaa na ninaomba nieleze sababu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hatujaenda kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, Tume ya Uchaguzi ilitoa vigezo vinavyoweza kuwezesha Jimbo likagawanyika. Sisi wote tunajua, vigezo tunavijua lakini cha ajabu unakuja kuona majimbo ambayo hayakufikia vigezo hivyo yaliweza kugawanywa na kuacha majimbo ambayo vigezo vimezidi hata vigezo vilivyowekwa. Unashindwa kupata majibu, wananchi wanakata tamaa, wananchi wanaelewa, wananchi wanafuatilia sana vyombo vya habari na wanachanganua na wanaona wakati mwingine kama Serikali ina upendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wanakuwa wameomba mara kadhaa, wameomba Wilaya, wameomba Halmashauri, wameomba Jimbo hawajapata na ninao ushahidi wa kutosha, katika Wilaya yangu Jimbo la Kwela Halmashauri ya Wilaya imeomba Wilaya, imeomba Jimbo, imeomba Halmshauri haijapata wakati ina vigezo vilivyopitiliza. Hii inatokana na viongozi kutokutembelea maeneo yote, hii ni moja ya sababu muhimu sana ambayo inakatisha wananchi tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu nyingine ni kuchelewa kwa utatuzi wa Migogoro ya ardhi. Kwanza napaswa nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aliyepo sasa hivi, kwa kweli lazima tumpongeze anafanya kazi kubwa sana, tena yenye moyo na kujitoa muhanga, mimi nampongeza sana. Lakini ningeomba ajielekeze katika maeneo sugu ambayo yamelalamikiwa kwa muda mrefu kutoa ufumbuzi na utatuzi wa mara moja ili kutokukatisha wananchi tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza hivi ninaongelea suala la shamba la Malonje ambalo limekuwa ni sugu sana na kwenye uchaguzi limetupa shida sana, hasa mimi Mbunge ndiye nimepata kazi kubwa kana kwamba mimi ndiye niliyebeba mzigo huo. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni baadhi ya maeneo kutofikiwa na viongozi wa Kitaifa. Tangu tumepata Uhuru sasa hivi tuna Rais wa Awamu ya Tano, lakini yapo maeneo hawajawahi kumuona Rais hata wa Awamu ya Kwanza, ya Pili na Awamu ya Tatu, wanamuona tu kwenye luninga, sababu za msingi hazipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine kiongozi anaenda wanasema hakupitiki barabara ni mbaya nani atengeneze? Huko ni kutenga wananchi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba viongozi mnaotumbua majipu muangalie hayo ni majipu, kama Kiongozi anakuelekeza mahali pa kwenda kuzuri huko anaficha nini? Ni majipu nayo vilevile tunaomba tabia hiyo isiwepo tena, tunaimani na Serikali hii tabia hiyo itajifuta yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kubaki nyuma kimaendeleo, kukosa huduma muhimu. Kwa mfano, nitoe mfano kwa mambo mawili, barabara na umeme. Wilaya ya Sumbawanga Vijijini pamoja na kuwa kubwa mno, ina kata zaidi ya 28, vijiji 115 hakuna hata kijiji kimoja ambacho kina umeme, na wananchi wanasikia maeneo mengine kata mbili zina umeme na hata Kata jirani zina umeme, unadhani wananchi wanatafsiri kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri nyepesi ya wananchi wanadhani labda Mbunge wao hana uwezo, hasemi! kitu ambacho kila wakati tunazungumza. Kwa hiyo, ningeomba Serikali ijaribu kuweka uwiano isiwe na upendeleo, iweke uwiano kwa sababu nchi hii ni yetu sote. Iweke uwiano siyo kukimbilia upande mmoja, huko ni kuumiza wananchi bila sababu, niliona na lenyewe hilo nilizungumzie. (Makofi)
Suala lingine ni miundombinu ya barabara. Katika Jimbo langu ni mibovu mno, kwanza jiografia yenyewe ya Jimbo imekaa hovyo, miundombinu ni mibaya, hata viongozi wanaokuja, mfano Dada yangu Paresso alikuja wakati wa uchaguzi, Katika vitu alivyovitumia ni uchakavu wa miundombinu katika Jimbo langu, aliuliza hii ni Tanzania au ni Tanganyika? Nikamwambia Tanzania. Tulipata taabu kweli, hebu jamani jaribuni kuangalia maeneo haya, zipo barabara zaidi ya 10 hazipitiki. Sina sababu za kuzitaja kwa sababu naona muda hautoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninapenda kulizungumzia ni kuhusu kilimo. Katika Hotuba ya Waziri Mkuu upande wa akiba ya chakula, inaonesha kwamba wametenga kununua tani 100,000 hicho kiwango ni kidogo mno, na sijui vigezo gani mnavitumia? Sijajua vigezo gani mnavitumia hivi tani 100,000 mnapanga zinaweza kuwasaidia Watanzania kama mvua hazitapatinaka miaka miwili, mitatu? Hizo tani 100,000 zinaweza zikasaidia? Na bado miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji bado hatujafikia kiwango kizuri.
Kwa hiyo, mazoea ambayo tumekuwa nayo ya neema ambayo tunayo Tanzania tunadhani miaka yote tutakuwa tunapata mvua mfululizo ndiyo sababu ya kutenga kiwango kidogo ,tani 100,000 ni kiwango kidogo mno kwa Nchi ya Tanzania. Kwa hiyo, ningeshauri kiwango hiki kiongezwe ni kidogo sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Hiyo ni Rukwa peke yake kama anavyozungumza Mheshimiwa aliyepo nyuma yangu, naomba kiwango hicho kiongezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upande wa afya, tunalo tatizo la upungufu wa wataalamu, waganga, tunalo tatizo la ukosefu wa kumalizia zahanati ambazo zimeanza kujengwa na wananchi na vituo vya afya, madaktari hakuna, ukosefu wa magari ya kubeba wagonjwa.
Mfano, tatizo la Kituo cha Afya cha Milepa, maombi yamekuja huu ni mwaka wa tatu na kutokana na kuchelewa tumepoteza karibu akina mama wajawazito 10 kwa mwaka jana tu, nimetoa taarifa mara kadhaa, nimerudia kuomba mara kadhaa. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu mambo mengine kama haya uyachukulie ni mambo muhimu, yanatutia doa kwa Serikali yetu nzuri hii ya sasa. Naomba uyabebe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upande wa elimu. Tunalo tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi upande wa shule za msingi hata upande wa shule za sekondari.
Tumejenga shule nyingi za sekondari za kata, tunaomba tupate Walimu wa Sayansi na wapo walimu ambao wamepata mafunzo wamemaliza wanazagaa mitaani hatujui wataajiriwa lini? Tunaomba wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anakuja kutoa ufafanuzi atueleze wataajiriwa lini walimu wapya wa sayansi na kwa kiwango gani kinachoweza kukidhi hali tuliyonayo kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ukosefu wa hosteli hasa hosteli za wasichana. Shule za Kata zina tatizo kubwa la kukosa hosteli za wasichana, jambo ambalo linarudisha maendeleo nyuma la vijana wetu wa kike, sote tunafahamu watoto wa kike wana vikwazo vingi, kutembea kilometa 5 anapambana na vikwazo vingi, wakati mwingine tunaweza tukalaumu kumbe waharibifu ni sisi wenyewe tusioangalia matatizo kama haya. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikatilia umuhimu wa kujenga hizi hosteli kwa shule zetu za kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchukua fursa hii kuishukuru Serikali kwa haya ambayo wameandika humu, tunasubiri utekelezaji na vilevile kwa haya niliyoyasema ningeomba ufafanuzi hasa kuitenga Wilaya ya Sumbawanga kutoipa Jimbo au Wilaya au Halmashauri wakati inavigezo lukuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia kilimo huwezi kukosa kuzungumzia ukosefu wa ardhi ya kilimo kwa baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, wafugaji na hifadhi za Serikali, wakulima na hifadhi. Mfano mzuri upo mgogoro kati ya wakulima na Hifadhi ya Akiba ya Uwanda katika Jimbo langu la Kwela. Mwingine ni mgogoro wa wananchi na mwekezaji wa shamba la Malonje. Serikali imalize haraka migogoro hii bila kufanya hivyo inaweza kusababisha mapigano na kuleta maafa makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kwenye pembejeo. Pembejeo nyingi hazifiki kwa wakati, hazitoshelezi, wanaofaidika ni wachache na bei kuwa kubwa isiyolingana na bei ya mazao. Naomba Serikali iangalie suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchi yetu haiwezi kuwa na uchumi imara. Tunayo mito mingi inayotiririsha maji msimu wote, lakini bado hatujaitumia vizuri. Nichukulie mfano katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, miaka minne mfululizo tuliomba miradi ya umwagiliaji lakini hatujapata fedha za kujenga miradi hiyo. Miradi hiyo ni wa Msia, Uzia, Maleza, Nkwilo, Nankanga na Mbulu. Naomba Serikali itupatie fedha kwa ajili ya miradi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunalo tatizo kubwa la wakulima wetu kukosa soko la mazao na kuwafanya kukata tamaa na vijana wengi kukimbilia mijini baada ya kuona kilimo hakiwalipi. Hivyo, Serikali itafute masoko ya bei nzuri ya mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa maghala. Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha chakula kwa wingi lakini hakuna maghala ya kutosheleza kuhifadhi mazao. Matokeo yake ikifika wakati wa mvua mazao hunyeshewa na kuoza. Naomba Serikali itueleze ni lini Mkoa wa Rukwa utajengewa maghala.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetelekeza Ziwa Rukwa pamoja na ziwa hilo kutoa ajira kubwa kwa wananchi na hasa vijana. Serikali haijawahi kutoa mikopo ya vikundi vya wavuvi, kwa nini mmelitelekeza Ziwa Rukwa?

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mhshimiwa Mwenyekiti, Elimu ya Awali ni muhimu sana katika kumwandaa mtoto kuanza Darasa la Kwanza kwa mwaka unaofuata, hivyo ni vyema Walimu wa kufundisha watoto hawa wakawa rasmi na kupewa cheti cha kufuzu masomo hayo kwa kufaulu badala ya kuchukua Walimu waliochoka, wasio na taaluma hiyo kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Elimu ya Ufundi ni nyenzo muhimu sana kwa vijana wetu ambao hawakubahatika kuendelea na masomo ya elimu ya juu, hivyo ni jambo la muhimu vijana hao wakapata mafunzo ya ufundi ili elimu hiyo iwasaidie katika kumudu maisha yao, pia kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutambue kwamba sera ya Serikali ni kwamba kila Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi (VETA) angalau kimoja. Je, sasa nataka Mheshimiwa Waziri anieleze ni lini sasa Wilaya ya Sumbawanga vijijini itajengewa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA)? Ni lini Mkoa wa Rukwa utajengewa Chuo cha Ufundi VETA? Naomba majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ianzishe haraka Kidato cha Tano na Sita ili kwenda sambamba na uanzishaji wa sekondari kila Kata ili wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Nne wapate nafasi ya kuendelea na Kidato cha Tano na cha Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana na hasa kwa familia masikini ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwapeleka mbali. Nitolee mfano wa Wilaya ya Sumbawanga vijijini, inazo Shule za Kata zinazofika Kidato cha Nne 19, ikiwa tunayo shule moja tu ambayo imepandishwa kufikia Kidato cha Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Waziri atukubalie kupandisha shule zifuatazo kufikia Kidato cha Sita; Vuna Secondary School, Mazoka Secondary School, Mzindakaya Secondary School, Milenia Secondary School. Naomba majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitengo cha Ukaguzi kimezorota sana ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali, hivyo kitengo hiki kiimarishwe kwa kupewa vitendea kazi kama vile, magari pikipiki, vifaa vya Ofisi na Ofisi zao zijitegemee bila kuingiliwa, kuwe na mafunzo ya mara kwa mara, fungu la kutosha kwa maana ya OC ili kuwezesha kitengo hiki kufanya kazi vizuri na kwa uhuru bila mashindikizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapaswa kujipanga juu ya ujenzi wa hosteli ili kunusuru vijana wetu na hasa watoto wa kike ili kuwapa fursa nzuri ya kusoma na kuwaepusha na vishawishi wanavyovipata wanapokuwa huru katika mazingira ya uraiani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamejitahidi sana katika ujenzi wa maabara, hivyo tunaomba Serikali itoe vifaa vya maabara ili kuboresha na kuiimarisha, vijana wetu waweze kupata elimu bora katika masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itoe posho kwa Walimu wanaokwenda kukaa katika umbali na ukosefu wa huduma muhimu kama vile umeme, mabenki, mawasiliano na usafiri. Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuungana na wenzangu katika kuchangia Wizara hii. Kabla ya yote niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati, ndugu yangu Profesa Muhongo, Naibu Waziri na Katibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi siyo za unafiki, zinadhihirisha uwezo alionao, hasa kwa sisi ambao tulikuwamo katika awamu ile ya kwanza na awamu hii, tulikuwa tunamlilia arudi aokoe jahazi juu ya Wizara hii. Mwenyezi Mungu ameturudishia, ni haki yake kuwepo hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote tunatambua umuhimu wa nyenzo muhimu hii ya umeme kwamba, umeme ni nyenzo muhimu katika maendeleo. Umeme unaongeza uchumi, unaongeza ajira, unaboresha huduma mbalimbali, ni chanzo muhimu cha uchumi katika njia zote za uchumi; bila umeme hakuna viwanda, hakuna maendeleo, hakuna ustaarabu! Hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha umeme huo unamfikia kila Mtanzania mahali popote alipo, ili aweze kufaidika na kupata huduma zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa masikitiko yangu makubwa kwa upande wa umeme wa REA. Tumekuwa na REA I, REA II na sasa hivi tunakwenda REA III, lakini ni jambo la ajabu sana Wilaya yangu ya Sumbawanga pamoja na ukubwa wote vijiji karibu 150, watu zaidi ya laki nne na nusu, hakuna hata kijiji kimoja chenye umeme! Sasa Mheshimiwa Waziri, kama wewe ndiy ungekuwa Mbunge, sijui ungejisikiaje na wananchi wako wangekuelewaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kwanza mwelewe kwamba, wilaya yangu ina kanda mbili, kanda ya kwanza iko Ufipa Juu, unaanzia Sumbawanga kwenda Tunduma na ukanda wa pili unaanzia Stalike, kule tunapakana na Mheshimiwa Lupembe, mpaka huku tunapakana na ndugu yangu, Mheshimiwa Silinde. Sasa nianze na ukanda wa juu. Ukanda wa juu zipo kata 13 ambazo zinatakiwa kupitisha umeme, nimeona nitaje kata maana nikitaja vijiji ni vingi mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kata ya Msandamungano, Sandulula, Jangwani, Mpwapwa, Kaengesa, Kanda, Lyangalile, Mpui, Ikozi, Kalambanzite, Lusaka, Laela, Kasanzama, Myakula, Mlangalua; hizi ni kata za Ukanda wa Ufipa juu, lakini zipo Kata za Ukanda wa Ziwa Rukwa, maana kata yangu ina maeneo mawili tofauti, ndiyo maana mara nyingi nimekuwa nikilalamika jiografia ya hii Kata! Ukanda wa Ziwa Rukwa tunazo Kata 13 ambazo zina vijiji vingi; hakuna hata kata moja iliyopata umeme, ambayo ni Muze, Mto Wiza, Milepa, Ilemba, Kapenta, Kaoze, Kilya, Jamatundu, Kilangawana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maeneo ni makubwa. Ninapotaja hizi kata, nataja kwa sababu ni kata, lakini maeneo mengine kata moja inaweza ikagawanyika kuwa kata tatu kwa ukubwa wa kata jinsi ulivyo, lakini unashangaa ni vigezo gani vinatumika kutopeleka umeme katika maeneo haya! Sijajua kwa nini Serikali, mara nyingi, imekuwa ikifanya Wilaya ya Sumbawanga Vijijini kuwa ni ya mwisho katika kupeleka huduma mbalimbali! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata suala la barabara tumekuwa karibu wa mwisho kuletewa barabara, sijui mlishatazama namna gani; kwa maana hiyo, lazima Waziri anieleze sababu za msingi za kutofikisha umeme katika maeneo hayo. Tena eneo hilo la ukanda wa chini ni eneo lenye uchumi mkubwa, jamani umeme unahitajika! Watu wa kule wana uchumi mkubwa, yapo maeneo mnapeleka umeme, nguzo zimesimama, watu hawataki kuingiza ndani ya nyumba kwa sababu hawana fedha! Sasa mnapeleka tu kama formality wakati umeme unatakiwa kujizungusha urudishe pesa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maeneo ninayosema haya ni maeneo ya watu wenye uchumi mzuri, ukipeleka umeme wataingiza umeme kwenye nyumba zao, wataufanyia shughuli za maendeleo, wataongeza uchumi wao, wataongeza uchumi wa Taifa; kwa nini hamtaki kufanya hivyo? Nataka unapokuja hapa unipe vigezo vinavyokufanya usipeleke umeme katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie umeme tunaoutumia Mkoa wa Rukwa. Mkoa wa Rukwa wote tunatumia karibu megawatts tano kwa mkoa mzima na umeme huo mwingine tunaupata kutoka Zambia na mwingine unakuwa ni umeme wa generator. Ninachotaka kusema, tunavyo vyanzo vingi vya kuweza kuongeza umeme katika Mkoa wetu wa Rukwa. Kwa mfano, nikitaja umeme unaotokana na maji, Mto Nzovwe una maporomoko makubwa na ulishafanyiwa utafiti kwamba, unaweza kutoa megawatts nane ambazo zikiongezeka katika Mkoa wa Rukwa unaweza ukawa na megawatts nyingi zinazoweza kusambazwa na viwanda vikaweza kutekelezeka vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa ni kwa nini hawataki kuutumia mto huo ambao ulishafanyiwa utafiti na haukauki na bahati nzuri Mkoa wetu wa Rukwa ni karibu kila mwaka una mvua. Kwa nini wasitumie maporomoko hayo ambayo yameshafanyiwa utafiti wa kutoa megawatts nane! Kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri aje anieleze, ni kwa nini hawataki kutumia njia nyingine ya kupata umeme katika Mkoa wetu wa Rukwa ambao gharama yake inakuwa ni ndogo kuliko hata umeme wa generator? Sijui wataalam wetu, nashindwa hata kuwaelewa! Tatizo hili ni kutozunguka, kutotembea! Yapo maeneo mlishayatenga, mnarudia rudia, maeneo mengine hamtaki kwenda! Mnazunguka, mnarudia maeneo yale yale! Sijui ni kwanini? Sisi sote ni Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni juu ya utafiti. Lazima nchi yetu ijielekeze kwenye utafiti katika mambo mbalimbali kwa sababu, yapo maeneo mengi yana rasirimali, lakini nchi hii haijagundua! Ndiyo maana hata juzi nimekuja kugundua Mtwara mmegundua gesi, mmegundua mafuta, lakini rasilimali hizo zipo maeneo mengi ila hamjaweka upendeleo wa kufanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kuzungumzia juu ya Ziwa Rukwa. Ziwa Rukwa halina tofauti na Ziwa Albert la Uganda, jiografia ni ile ile na bahati nzuri nimeshafika, lakini nataka anieleze ni utafiti gani umeshafanyika wa Ziwa Rukwa ili kuangalia kuna kitu gani na mkishajua maana yake mtaweza kulitunza. Ndiyo maana mmelitelekeza, hamna habari nalo, suala la mazingira hamna habari, lakini naamini upo uchumi mkubwa katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala lingine la utafiti, kuna shamba ambalo nimekuwa nikizungumzia mara kwa mara, Shamba la Malonje. Yule Mtaalam wa Kenya alilizungukia lile shamba akasema, lile shamba, 1/8 ya lile shamba lina madini ya kopa, lakini watafiti wetu hawajakwenda kuangalia ni kitu gani kinafanyika! Matokeo yake mwekezaji akija anang‟ang‟ania kwa sababu, anajua pale kuna faida kwa baadaye. Kwa nini, watafiti hamtaki kufanya kazi inayostahili, ili kuweza kuboresha nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka tu kusisitiza kwamba, Mheshimiwa Waziri sisi sote tunafahamu uwezo wake na msukumo wake. Siwezi kuunga mkono kwa sababu, wananchi watanishangaa! Huna umeme hata kijiji kimoja, vijiji 150, halafu leo hii unasema unaunga mkono, watakushangaa! Mpaka nipate maelezo ya Mheshimiwa ndipo naweza kuunga mkono hoja, lakini kwa sasa siwezi kuunga mkono hoja wananchi watanishangaa, kwanza ni aibu kubwa, ni aibu kubwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasisitiza Mheshimiwa Waziri anieleze ni kwa namna gani atapeleka umeme katika Wilaya ya Sumbawanga Vijijini? Mkija Sumbawanga Mjini mnadhani ndio Sumbawanga Vijijini, hata Kijiji kimoja! Ni aibu kubwa sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuchangia kuhusu shamba la Malonje. Ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa shamba la Malonje kati ya wananchi na mwekezaji? Mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu, wananchi wameteseka kwa kukosa ardhi ya kulima. Naomba Mheshimiwa Waziri atoe maelezo kuna maeneo kadhaa yenye migogoro Waziri huyu ameimaliza huu unamshindaje au kuna mikono ya wakubwa? Naomba maelezo kwani wananchi wamechoka na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali. Naomba Serikali imalize haraka mgogoro huu kuepusha shari inayoweza kutokea. Ahsante.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kushukuru kwa kupata nafasi hii ili niweze kuungana na wenzangu katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango. Lakini kabla ya yote nikupongeze wewe kwa umahiri wako na msimamo, umeonesha umahiri wa hali ya juu na kiti kimeku-fit, hongera sana mama, hongera sana jembe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu wake na watendaji wote walioko ndani ya ofisi yake, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. Mheshimiwa Waziri tunamfahamu umahiri wake hata kabla hajaingia ndani ya Bunge, uwezo wake tunaujua, isipokuwa michango yetu ni ya kumsaidia tu ili aweze kufunga goli vizuri kama ataitumia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuchangia nianze kwa kusema kwamba mapato yote, uchumi wote ili kuboresha uchumi, kuongeza mapato huwezi ukatenga vitu viifuatavyo katika kuviboresha, ikiwemo barabara, reli, umeme, maji, afya, elimu, kilimo, tena kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake ameeleza mikakati ya ujenzi wa reli ya kati na mambo mengine, lakini katika hili nataka nitoe ushauri kwa upande wa barabara. Yapo maeneo katika nchi hii ambayo hayawezi kupitiwa na reli, ama kwa sababu ya jiografia au ukanda wenyewe kwa jinsi ulivyokaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni vyema kabisa maeneo haya na yenyewe yakatazamwa kwa upekee kwa maana ya kuwajengea barabara za lami. Kama unapitisha reli upande huu, upande huu hawana reli ni vizuri basi tukatenda haki na upande wa pili ukapeleka nguvu ya barabara za lami, kwa sababu reli haiwezi ikapita pande zote katika nchi hii. Kwa hiyo, mgawanyo mzuri ni kuweza na wenyewe kuwapelekea barabara ya lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia suala hili nizungumzie upande wa jimbo langu, Ukanda wa Ziwa Rukwa kutoka Kibaoni, unakuja Kilyamatundu unakwenda Kamsamba hadi Mlowo, ukanda ule huwezi ukapitisha reli lakini ni ukanda mkubwa tena wa uchumi wa hali ya juu. Nasikitika sana Serikali haijaangalia ukanda ule, una uchumi mkubwa, barabara yake ni kilometa zaidi ya mia mbili na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu Serikali imeazimia kujenga Daraja la Mto Mumba ambalo wameshatangaza tenda yake, ili kuimarisha barabara hii ni vyema wakajenga sasa lami ili iweze kutoka Kibaoni mpaka Kamsamba ikatokee Mlowo ili kuunganisha watu wa ukanda ule na mikoa mingine. Bila kufanya hivyo wale watu utakuwa umewaacha kisiwani, ile barabara ya lami unayoona Sumbawanga kwa wale watu haiwafai wala hawana matumizi nayo kabisa kwa sababu ni ukanda ambao umejitenga, kwa hiyo, nailitaka nisisitize hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la CAG, wenzangu wamelizungumza kwa utaalam mkubwa sana, na kwa utafiti wangu karibu asilimia 90 ya Waheshimiwa Wabunge wamegusa jambo hili. Nina imani amesikiliza na mimi nimeona nigusie kwa sababu CAG ndiyo jicho, ndiyo dira ambayo inatuonesha kitu gani kimefanyika. Unapomtenga mtu huyu ni kama unataka kuficha uovu wako na sipendi Serikali hii ambayo Rais wetu amedhamiria kuondoa mafisadi halafu na mtu ambaye anaweza akawa jicho lake akapata kifungu kidogo. Kwa hiyo, nashauri kama wenzangu walivyoshauri, ofisi hii iweze kuangaliwa kwa kipaumbele cha hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la migogoro ya ardhi, Serikali imetenga bilioni tano kwa ajili ya fidia ya migogoro ya ardhi, lakini kiwango hiki ni kidogo sana, karibu nchi yote imetapakaa migogoro ya ardhi. Bilioni tano haitoshi kuweza kufidia maeneo mbalimbali katika nchi nzima ya Tanzania, ni kitu ambacho hakiwezekani. Kama tuna azma kabisa ya kuondokana na migogoro hii ningeomba Serikali iweze kuangalia ni namna gani inaweza kufanya katika suala zima la kuongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la mapato kutokana na wananchi kudai risiti wakishapata huduma na namshukuru Mheshimiwa Rais amepiga kauli mbiu sana kwenye TV tunamsikiliza. Sasa kauli mbiu hii ya Mheshimiwa Rais isiishie kwenye TV maana yake ni indicator kutuambia sisi viongozi wote, Waheshimiwa Wabunge, Wenyeviti na raia wote wenye nia njema, huko tunakofanya mikutano kipaumbele iwe ni kuwaelimisha wananchi wetu kudai risiti anapopata huduma na hasa huko vijijini. Tumuunge Mheshimiwa Rais, anazungumza kwenye TV, sisi twende nayo kwenye mikutano ya hadhara kutoa elimu kwa wananchi wetu ili waweze kudai risiti pindi wanapopata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mashine za kutoa risiti. Ili tuweze kuleta ufanisi vizuri ni vyema kabisa mashine hizi zikatolewa bure na si bure, kwa sababu mtu akitoa mashine atakapokuwa anazitumia ndiyo nia njema ya kuleta mapato kwenye Serikali. Kwa hiyo, nashauri, ni vyema kabisa mashine hizi zikatolewa bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limezungumzwa na karibu Waheshimiwa Wabunge asilimia 90, ni kuondoa msamaha wa kiinua mgongo kwa Waheshimiwa Wabunge. Suala hili ukiliangalia, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni kama limechomekwa, halijaja kwa muundo rasmi, limechomekwa. Sasa kama limechomekwa ni kazi rahisi, lichomoe tu, hakuna sababu ya kuhangaika nalo. Lichomoe, kwa sababu lingekuwa limekaa kwa mpangilio lingegusa viongozi wote wa kisheria ambao wanatakiwa kusamehewa na msamaha huo, lakini kwa sababu limepachikwa basi wewe usipate kazi ngumu, lichomoe, wala halina hata uzito wowote, lichomoe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, watu wengine wanaweza wakadhani sisi Waheshimiwa Wabunge tunajisemea, sisi siyo Wabunge wa maisha, tupo leo, kesho watakuja Wabunge wengine, kwa hiyo hatujizungumzii sisi, tunazungumzia hata watakaokuja. Maana mtu mwingine anaweza kusema hawa Waheshimiwa Wabunge wanajitetea, hapana, sisi siyo Wabunge wa milele, wangapi walikuwepo hapa hawapo, hata Mawaziri hawapo. Kwa hiyo, tunazungumza kwa niaba ya Watanzania na kwa nia njema. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kwa haya machache yametosha. Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mgogoro katika Hifadhi ya Akiba ya Uwanda kutokana na ongezeko kubwa la watu waliopo katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi hiyo mipaka yake kutoeleweka, askari wanyama pori kutoza wafugaji fedha ili walishe mifugo yao ndani ya hifadhi; kukodisha ardhi iliyomo ndani ya hifadhi ili wakulima waweze kulima; askari wa wanyama pori kuruhusu wananchi wasio na uwezo wa fedha walime mazao yao na mazao yakishakomaa hutumia ujeuri wa kupora mazao yao wanayauza na kuingiza fedha hizo mifukoni mwao; kuwanyang‟anya pikipiki, baiskeli, majembe ya plau na majembe ya mkono, fyekeo, panga na kadhalika, jambo ambalo linahatarisha amani. Kama Serikali haitachukua hatua haraka ipo siku yatatokea mapigano kati ya askari hao na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi hiyo kwa sasa haina sifa, ni hasara tu kwa Serikali, inawanufaisha Askari tu. Hivyo kutokana na uhaba wa ardhi, nashauri, hifadhi hiyo ipunguzwe au kufutwa kabisa, wananchi wagawiwe ardhi hiyo waendeleze uchumi wao kwa kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anieleze nini faida ya hifadhi hiyo kwa Serikali na kwa wananchi hadi sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hifadhi ipunguzwe kama siyo kufutwa kabisa. Mipaka ijulikane, Serikali itoe misaada ya kuwajengea shule, zahanati na kuwapatia madawati ili kuwatia moyo wananchi. Pia nashauri Mheshimiwa Waziri atembelee eneo hili la hifadhi ili ajifunze na baadaye aweze kutoa uamuzi sahihi kuliko kusikiliza kwa mbali. Ahsante.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakuru sana kwa kunipa nafasi
niungane na wenzangu katika kuchangia taarifa hizi zote mbili, Kamati ya Miundombinu na
Kamati ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza naomba nianze na Kamati ya Miundombinu,
kwanza naipongeza Kamati kwa taarifa nzuri, nampongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na
watendaji wote katika Wizara hii kwa utendaji mzuri. Kwa kweli kiuwajibikaji wanawajibika vizuri
na nadhani tatizo kubwa litakuwa ni pesa. Sasa labda nizungumzie suala moja ambalo naona
kwangu kama linanitesa, ni vipaumbele vya Serikali katika suala la barabara za lami,
tunafahamu kwamba sisi wote kwamba kuunganisha Mikoa na baadae itakuja Wilaya.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nazungumzia Mkoa wa Rukwa unasemekana
tumeunganisha barabara ya lami ni sawa, ni katika ukanda wa upande wa juu. Mkoa wa
Rukwa umegawanyika katika pande mbili; ukija ukanda wa Bonde la Ziwa Rukwa barabara
kuanzia kibaoni unakuja, Kiliamatundu, unakuja Kamsamba, unakuja Mlowo; ni ukanda
mwingine tofauti kabisa ambao hauwezi kufaidika kabisa na barabara ya lami ya kutoka
Tunduma mpaka Sumbawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu imekingwa na mlima ambao gari haiwezi kubeba
mzigo wa zaidi ya tani tatu, lazima iwe inabeba nusunusu na barabara hii bahati nzuri
inaunganisha Mikoa mitatu; Katavi, Rukwa na Songwe. Barabara hii ina kilometa karibu 200 na
ni barabara ya siku nyingi hata wakati wa ukoloni ilikuwepo ndio maana sababu ya kuwepo
wakati wa ukoloni ni umuhimu wake; potential zilizopo katika maeneo yale, kilimo ni bonde la
ufa linakubali mazao karibu mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sijaua ni kwanini Serikali haijatilia umuhimu wa kuweka
lami katika barabara hii, na juzi wakati wamekuja watu wa MCC II waliuona umuhimu wa
kuweka lami barabara hiyo kulingana na vigezo vilivyokuwa vimewekwa, ni bahati mbaya tu
waliweza kujiondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kuiambia Serikali kwa nini haitaki kuona umuhimu
huo ambao hata watu wa MCC wamekuja kuiona na wakoloni waliona; kwa nini haitaki kuona
umuhimu wa kutenegeza barabara hii katika kiwango cha lami? Ni barabara ambayo ina eneo
la bonde la ufa na ina rutuba, inakubali mazao yote, inalima mpunga, matunda; ina mito
isiyokakuka karibu kipindi chote cha mwaka na mvua za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba Waziri atakapokuwa anakuja
kutoa maelezo atueleze ni kwa nini Serikali haitaki kuangalia barabara hii na ninajua sababu
yake ni viongozi kutokupita katika maeneo yale na bahati mbaya sana Mawaziri karibu walio wote ni wageni. Nawaomba safari hii mjaribu kutembelea ile barabara mtaona umuhimu,
itawagusa mpaka kwenye mioyo yenu, naombeni sana mtusaidie katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nishukuru kwa ujenzi ambao mnatarajia kuanza wa
daraja la Mto Momba, niwashukuru sana. Lakini faida ya ujenzi wa daraja lile ni kuunganisha
sasa ile barabara kwa lami; lakini kama mtalijenga mkaacha barabara ya vumbi itakuwa haina
maana yoyote. Kwa hiyo, na mimi nashauri kabisa jitihada za kujenga hilo daraja tunapongeza
lakini ziende sambamba na kufanya barabara ile iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwa upande wa Kamati ya Nishati na Madini; kwanza
nampongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake wote na Kamati kwa taarifa yao nzuri.
Lakini nataka kusema ni muhanga wa REA katika Jimbo langu. Jimbo langu nimeeleza mara
kadhaa kwamba ni jimbo ambalo limeachwa kabisa halina miundombinu ya umeme; na kwa
jinsi lilivyokaa kijiografia sijajua ni kwa sababu gani linaendelea kuchelewa. Ninafahamu wazi
kwamba tumepangiwa kuletewa umeme katika REA III.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini sisi tunakuwa nyuma kiasi hicho, kila jambo
tunakuwa nyuma na tunakaa gizani? Na bahati nzuri yapo maeneo mnapeleka umeme
mnapeleke watu hawataki kuutumia, umeme umeenda watu hawataki kuutumia, lakini lie eneo
ni eneo ambalo ukipeleka umeme watu watautumia kwa sababu vipo viashiria vya uchumi
vingi sana na ndio maana utakuta karibu eneo lote watu wamefunga solar; sasa watu
wanaojimudu kununua solar ukiwapelekea umeme utakuwa umewasaidia sana.
Ninamuomba Mheshimiwa Waziri ulione hili, nataka kipaumbele katika suala la umeme
katika maeneo yale yote; nikiungana na Mheshimiwa Kikwembe kule hatuna umeme kabisa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu cha ajabu mmekuja kupitisha nguzo mkapitisha Muze,
mkapitisha kwenye Kata zangu mkapeleka Mpanda sijui mlipeleka wapi huko; kwa hiyo
wananchi wangu wanaziona nguzo tu. Juzi niliongea na Meneja wa TANESCO kwamba
naomba basi ulete hata umeme wa TANESCO potelea mbali wananchi watalipa; wamewasha
kijiji kimoja cha Muze wananchi wamelipa karibu shilingi laki moja na kitu; wanajitoa wamalipa.
Sasa wanalipa kwa gharama hiyo je, ukipeleka umeme wa REA si wananchi wengi watafaidika
na umeme huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo lingine ambalo nilikuwa naomba Mheshimiwa
Waziri unisaidie umeme ambao mnapeleka REA III kwangu upande wa Kusini Mashariki,
mmefikisha nguzo katika Wilaya ya Mbozi kwa kijiji cha Kamsamba; kijiji cha Kamsamba kinacho
tutenganisha ni mto. Mmeshapeleka nguzo mmefunga na transfoma kwa maana REA II
watapata umeme wale watu, nina vijiji zaidi ya nane ambavyo vimepangana vinauangalia
umeme utawashwa Kamsamba halafu huku hakuna umeme, zaidi ya vijiji nane na vyenye
uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo, kuwasha
umeme Kamsamba halafu kinachotutenganisha ni mto haizidi hata mita 500; kwa nini umeme
usivuke ukaja kuvisaidia vijiji vyangu zaidi ya nane ambavyo vina uhitaji huo umeme na
kupunguza gharama?
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu tukubaliane vile vile hata kisiasa mnakuwa mmeniweka
mahali pabaya; wananchi wanashangaa kijiji kimoja kimepata umeme ng‟ambo ile, vijiji zaidi
ya nane viko huku vinachelewa kwa Mheshimiwa Silinde ni mambo ya ajabu sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa utakapokuwa unakuja ueleze ni kwa nini usitumie ule ule umeme kuvusha huku.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ukanda ule una mito mingi sana isiyokauka na
nilishaeleza hapa kuna mto mmoja unaitwa Mto Nzovwe ulishafanyiwa utafiti kwamba unaweza
kutoa megawati kumi; nashangaa kwanini Serikali haitaki kutumia chanzo hiki kuongeza umeme
katika Mkoa wa Rukwa na umeme ambao una unafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka Waziri utakapokuja kama ukipata nafasi
unipe maelezo juu ya jambo hili. Nilikuwa na jirani yangu Mheshimiwa Mipata anasema kwake
umeme unakatika katika kwa hiyo, mliangalie na suala la kukatika katika umeme kwenye
baaadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja lakini naomba
maelezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuweza kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuungana na wenzangu katika kuchangia taarifa za Kamati mbalimbali, Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Kamati ya Maliasili. Kwanza naunga mkono taarifa za Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza nizungumzie mgogoro kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi za akiba za ardhi. Tulishazungumza mara kadhaa hapa kwamba zipo baadhi ya akiba za hifadhi ambazo hazina faida zaidi ya miaka 50 na ukimuuliza Waziri hii akiba ya hifadhi hii imeleta faida gani kwa Taifa hili au kwa wananchi hawa zaidi ya askari wa wanyamapori au askari wa misitu kuitumia kwa manufaa yao, kukamata wananchi na kuwatoza rushwa halafu kuwaruhusu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie hifadhi ya akiba ya Uwanda Game Reserve. Hifadhi hii ni zaidi ya miaka 50 na wakati hifadhi hii imetengwa idadi ya wananchi ilikuwa kidogo lakini sasa hivi hifadhi hii inazungukwa na vijiji zaidi ya 15, zaidi ya wananchi 26,000. Kwa hiyo, wananchi wanashindwa walime wapi, lakini hifadhi hii ukiiangalia faida yake haipo matokeo yake askari wanatumia hifadhi hii kwa manufaa yao binafsi. Mwananchi akisogelea hii hifadhi hata kwa kupita tu anakamatwa, anadaiwa pesa, asipokuwa na pesa anakamatwa anarundikwa ndani na wengine wamekuwa vilema, wengine wamepoteza maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, tarehe 2 Januari, 2017, mwananchi mmoja anaitwa Luanda Salanganda Malele amepigwa risasi kwenye goti na askari anayeitwa Limomo baada ya kumkuta nje ya hifadhi. Akaambiwa kuna mtoto wako tumemkamata, akawaambia mimi sina mtoto aliyekamatwa, wakamdadisi kumdai pesa akakataa wakamwambia wewe una mazoea ya kujidai mjuaji tukikuomba pesa hutupati, wakaanza kumtishia kwa risasi. Katika kumtishia akakimbia akaenda kwenye nyumba ya jirani wakamtandika risasi kwenye goti, goti limechanikachanika sasa hivi yuko Muhimbili anasubiri kukatwa mguu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sisi kama binadamu Mwenyezi Mungu kweli anaweza akapenda maonevu ya namna hii? Hizi hifadhi zimewekwa kwa ajili ya binadamu tena tunaita hifadhi ya akiba, tulishasema kwa nini Serikali isipite kufanya utafiti wa kina kuona hifadhi ambazo hazina faida, hata kama zina faida wanaangalia maslahi makubwa ya wananchi waweze aidha kurekebisha mipaka au kuziondoa kabisa. Kwa mfano, Uwanda Game Reserve haina manufaa kabisa kwa Taifa zaidi ya kusumbua wananchi kwa kuwakamata kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna Kamati inapita au Waziri aende kwenye hifadhi hii, akakutane na wananchi aweze kuzungumza nao wamueleze matatizo yao, vinginevyo yatatokea mapigano makubwa sana kwa hali iliyopo sasa hivi. Sisi tumebeba mzigo wa kila siku kutuliza hali hii ya hewa, kwa hiyo, tunaomba Serikali au Waziri afanye utaratibu wa kwenda kukutana na wananchi ili aweze kuwasikiliza na kutafuta muarobaini wa mgogoro huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni uhaba wa ardhi. Lazima tukubali ipo baadhi ya Mikoa au Wilaya zina uhaba wa ardhi na zina uhaba wa ardhi kwa sababu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika,
ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuwa
miongoni mwa wachangiaji katika hotuba ya Mheshimiwa
Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wachangaiaji
waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu
kwa speed tunayokwenda nayo sasa hivi. Niwatie moyo
kwamba endeleeni kukaza uzi mambo yanakwenda
barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia upande
wa kilimo. Sisi wote tunatambua kwamba asilimia kubwa ya
Watanzania wanategemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 85.
Hata hivyo, ukiangalia hali halisi ya Serikali kutilia maanani
suala hili sijaona. Serikali haijazama kwa undani zaidi kuona
kwamba kilimo ndiyo kinachoweza kuwasadia Watanzania
hawa wengi na mtiririko wa vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu hatutaweza kuwaajiri wote wangeweza kukimbilia
kwenye kilimo kama tungeweka mipango yetu vizuri. Kilimo
kinalipa kwa mtu ambaye atakuwa amejipanga vizuri na
Serikali imeweka mazingira mazuri. Kwa hiyo, naiomba Serikali
itilie maanani sana upande wa kilimo ambacho ndiyo
kinaweza kuokoa Watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu mbolea
na pembejeo. Toka nimeingia katika Bunge hili sijawahi kuona
mwaka ambao pembejeo kwa maana ya mbolea na mbegu
imewahi msimu wa kilimo hata siku moja. Ni miaka yote
imekuwa ikichelewa na sijajua ni kwa sababu gani. Kama
tuna dhamira thabiti ya kuwasaidia wananchi tupeleke
pembejeo kabla ya msimu kuanza. Ningefurahi mwaka huu
jambo hili iwe ni mara ya kwanza Serikali kuwahisha
pembejeo kwa wakulima kabla ya msimu kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo lingine la
kupeleka mbegu fake na dawa fake za palizi. Yapo maeneo
ambayo yanatengeneza mbegu fake na dawa fake za palizi
wakulima wetu wananunua na kwenda kuyatumia yanatia
hasara kubwa sana. Naomba vyombo vinavyohusika vijaribu
kufuatilia makampuni haya ambayo yanapeleka mbegu fake
na dawa fake za palizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado lipo tatizo kubwa la
upungufu wa ardhi katika maeneo mbalimbali. Vijana wengi
wanapenda kulima, lakini lazima tukubali baadhi ya maeneo
ardhi haitoshi. Hii ni kutokana na watu wachache kukumbatia
ardhi. Vilevile Serikali ijaribu kuangalia yale maeneo ambayo
tulitenga kwa kazi nyingine iyatoe kwa vijana hawa waweze
kujiendeleza kwa kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni
umwagiliaji. Sisi wote lazima tukubali kwamba kilimo ni sahihi
kisicho na risk ni kilimo cha umwagiliaji. Huwezi ukalinganisha
kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha mvua. Kilimo cha mvua
kina risk nyingi sana, unaweza ukapata mafuriko, upepo
mvua au kukosekana kwa mvua. Ndiyo maana hata benki
ukienda kuomba mradi wa kilimo kwa kutegemea kilimo cha mvua hupati mkopo. Ukienda na kilimo cha umwagiliaji
utapata mkopo kwa sababu wanajua kwamba ni kilimo cha
uhakika.
Naomba Serikali izame kwa undani zaidi kuhakikisha
inainua kilimo cha umwagiliaji. Tunayo mito mingi, mabonde
mengi, maziwa mengi, kuna tatizo gani la Serikali kutozama
katika kilimo cha umwagiliaji ambacho tunajua kwamba ni
kilimo cha uhakika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri yangu iliweza
kuomba miradi ya umwagiliaji katika vijiji kadhaa vya Uzia,
Ilemba, Msia, Milepa hatujawahi kupewa hata mwaka
mmoja. Naomba safari hii tuweze kupewa angalau hata kwa
mradi mmoja hasa ule mradi wa Mareza ambao una hekta
7,000 ambazo zinaweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao upungufu wa
maghala kwa baadhi ya mikoa inayozalisha sana kwa mfano
Mkoa wa Rukwa. Ukienda pale kwenye maghala ya Serikali
utakuta mahindi yamepangwa nje jambo ambalo ni risk
mvua zitakapokuwa nyingi. Tungeomba Serikali iweze
kujenga maghala ya kutosha katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende Wizara ya Afya,
katika ukurasa wa 40, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelezea
vizuri sana kwamba kumekuwa na ongezeko la fedha za
kununua dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016
kwenda shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017. Tunapongeza
kitendo hicho na tunaomba Serikali iendelee kuongeza fedha
mwaka hadi mwaka kwa suala la ununuzi wa dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lazima tukubali, sera
yetu ya Serikali kupitia Chama cha Mapinduzi iliji-commit
kwamba lazima kuwe na zahanati kila kijiji, kituo cha afya
kila kijiji na Wilaya kuwa na Hospitali ya Wilaya. Sera hiyo
ilieleweka vizuri sana kwa wananchi na ndiyo maana
wamejitoa kujenga maboma mengi sana katika maeneo
mbalimbali ya nchi yetu kwa sababu wanajua ingeweza kuwasaidia. Cha ajabu maboma hayo hayajamalizika
kutokana na Serikali kutopeleka fedha kwenye halmashauri.
Ni nguvu za wananchi na wakati mwingine unakuta Mbunge
anajitolea kupitia Mfuko wake wa Jimbo lakini Serikali kama
Serikali tungeomba ipeleke fedha ili miradi hiyo iweze
kumalizika mapema iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye Jimbo
langu kuna maboma karibu 13 ambayo wananchi
wamejenga, mengine yamefikia hatua nzuri mengine bado
katika vijiji vya Ilambo, Maleza, Kirando, Kiryamatundu,
Mtapenda, Kasekela, Lyapoo, Nakazi, Mumba, Jangwani,
Kizumbi, Kawila na kasekela. Wananchi wamejitoa kujenga
majengo haya, naomba Serikali iweze kupeleka pesa kwenye
halmashauri zetu ili iweze kukamilisha majengo haya.
Kadhalika, vituo vya afya wananchi wamejitoa michango
yao, nguvu zao, wamejenga majengo kwenye Kata za
Mfinga, Muza, Ilemba, Kaoze, Kipeta na kalambazite.
Tunaomba Serikali ipeleke fedha ili iweze kumalizia majengo
hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ukosefu wa
magari ya kubeba wagonjwa katika vituo vya afya. Ninavyo
vituo vya afya vinne ambavyo havina magari vya Milepa,
Lahela, Mpui na Msandamugano lakini sanasana
nizungumzie Kituo cha Afya Milepa ambacho kimejengwa
kwenye mazingira magumu kulingana na jiografia ilivyo. Kile
kituo kimepoteza akina mama wengi na watoto. Mheshimiwa
Waziri Ummy nimekueleza mara kadhaa hata Naibu Waziri
nimewaeleza athari kubwa inayotokea ya vifo vya akina
mama kutokana na kituo hiki kukosa usafiri. Nina imani kwa
maelezo ya leo kwa huruma yako tungeomba uwapatie gari
la wagonjwa katika kituo hiki cha afya cha Milepa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao upungufu mkubwa
sana wa watumishi kwenye zahanati zetu hasa mikoa ya
pembezoni. Unakuta zahanati inaongozwa na Mhudumu
Muuguzi sasa unategemea nini katika mazingira ya namna hiyo? Tunaomba Serikali iweze kuliangalia hilo na ikiwezekana
kutoa ajira kwa watumishi wenye sifa wa kuweza kuongoza
hizo zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile
nikumbushie maombi ya Halmashauri ya kuomba
halmashauri, wilaya na jimbo. Jambo hili wengine wamekuwa
wakiona kwamba labda tunafanya mzaha. Mimi nataka
nieleze ukweli, kama Watanzania tuna huduma, Mheshimiwa
Waziri Mkuu umefika katika maeneo yale, tena nikushukuru
sana, hukupangiwa kwenda, mimi ndiye niliyekuomba na
ukafika. Hata hivyo, nakuambia, sehemu uliyofika ni moja ya
nane ya eneo langu. Ulijionea hali halisi ilivyo, jiografia ilivyo
na ukubwa wa jimbo ulivyo. Pamoja na Serikali kuweka
msimamo wa kutoongeza maeneo, myaangalie maeneo
nyeti kama haya. Mimi nazungumza kwa niaba ya wananchi.
Wananchi ndiyo wamenituma nizungumze jambo hili
isionekane mimi ndiye ninayezungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wananchi wapiga
kura zaidi ya 200,000 na idadi ya wananchi karibu 400,000…waaminifu kwa Chama
cha Mapinduzi inakuwaje hawa watu msiwaangalie? Kama
tulifanya makosa ya kutoa halmashauri kwenye maeneo
ambayo hayana sifa basi yavunjeni hayo mtoe haki kwa wale
ambao wanastahili kupewa haki kuliko kuweka kizuizi watu
wengine wasiweze kuomba. Mimi nadhani hili ni tatizo kubwa
sana katika eneo langu. Nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu
uweze kulibeba kama ulivyokuwa umelibeba toka siku ile
wala siyo jambo la kupuuza. Wananchi ndiyo kilio chao
kikubwa kutokana na mazingira na huduma mbovu
wanayoipata kutokana na mazingira yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nililotaka
kuzungumzia ni upande wa elimu. Tuna upungufu mkubwa
sana wa walimu wa sayansi kwa shule zetu za sekondari hata shule za msingi. Vilevile umaliziaji wa maabara ambazo
wananchi wameshajenga, tungeomba Serikali iweze
kumalizia hizo maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni uanzishwaji wa
shule mpya...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika,
naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's