Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Mgeni Jadi Kadika

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kumwezesha kuchangia hotuba hii. Elimu ni ufunguo wa maisha na Taifa. Ikiwa wananchi wake hawana elimu, basi Taifa hilo haliwezi kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu amesema, anayejua hawi sawa na yule asiyejua. Ni lazima anayejua ana upeo mkubwa wa kuona mbali. Kuhusu Walimu, wana kazi kubwa sana na wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanapata changamoto nyingi katika mazingira ya kazi, kwanza kufundisha wanafunzi wengi katika Idara moja, upungufu wa vifaa vya kufundishia, ukosefu wa matundu ya vyoo, maji hawana, nyumba za kuishi hawana, usafiri hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetangazwa kwamba elimu ni bure, wakati bado miundombinu ni mibovu. Kwanza tuiboreshe. Naishauri Serikali kwamba bajeti ya Wizara hii iongezwe ili iweze kuboresha miundombinu, madarasa yaongezwe ili kupunguza msongamano wa wanafunzi, vyoo, madawati, nyumba za Walimu na mishahara ya Walimu pia iboreshwe ili waweze kutoa hiyo elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, ikiwa mti huutunzi, hauna mbolea wala maji, utawezaje kutangaza tenda ya matunda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanapofika muda wao wa kustaafu, wanapata usumbufu mkubwa kupewa mafao yao. Wastaafu hao hudai mafao yao mpaka wanafariki hawapati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwatizame wastaafu hawa kwa jicho la huruma, pale tu wanapostaafu wapewe haki zao mapema ili wapate kuwasaidia katika maisha ya uzeeni na pia wapatiwe bima ya afya angalau waweze kuhudumiwa, kupata matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana kuwa mila potofu ya watoto wa kike kuchezwa unyago ni moja ya kichocheo kikubwa kupata mimba za utotoni, kwa sababu mtoto akishachezwa unyago, hujiona yuko huru na tayari amekamilika na kuingia katika daraja la ukubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipige marufuku kwa mtoto wa kike kuchezwa ikiwa bado ni mwanafunzi ili kupunguza tatizo hili. Vilevile sisi viongozi, wazazi, walezi tukemee kwa kupiga vita jambo hilo ili kumpa nafasi mtoto wa kike aendelee na masomo yake. Baadaye akimaliza kusoma atachezwa kama ndiyo mila zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Zanzibar, elimu ya juu bado kuna usumbufu mkubwa kuhusu mikopo ya wanafunzi. Wanacheleweshwa sana na hivyo kuchelewa kuanza kusoma. Tunaomba Serikali ya Muungano iweze kusimamia ili usumbufu uweze kuondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia, naomba kuwasilisha. Wako mjenzi wa Taifa.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, mwenye kunipa nguvu na afya njema nikaweza kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Maalim Seif Shariff Hamad kwa hekima yake na busara zake kuweza kuwatuliza Wazanzibari kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu. Kama si hekima zake basi sasa hivi tungekuwa tayari wengi wamekufa na wengi wamepata vilema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, sasa nakuja kwenye hoja. Mimi naanzia kuchangia hoja kwenye suala la UKIMWI. UKIMWI ni janga la Taifa na unapoteza nguvu kazi za vijana wetu katika Taifa hili. Pamoja na utafiti wa Serikali kusema kuwa UKIMWI umeshuka kuanzia asilimia 8.8 mpaka kufikia asilimia 5.1 lakini bado UKIMWI unaongoza. Utafiti unaonyesha mikoa mitano ya Tanzania ndiyo inaongoza kwa UKIMWI ambayo ni Mbeya, Iringa, Shinyanga, Dar es Salaam pamoja na Njombe. Mimi nataka kuzungumzia Mkoa wa Shinyanga kwa sababu ndiyo tulioutembelea na tukaona hali halisi ya wagojwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ninukuu wanasema, kuanzia Januari mpaka kufikia Disemba wagonjwa waliofika kwenye kituo cha afya na kupimwa wakaonekana ni waathirika katika Mkoa wa Shinyanga walikuwa ni wagonjwa 34,826, maambukizi mapya yalikuwa 953, hii ni asilimia kubwa. Nakuja kwa wajawazito, wajawazito waliofika kupimwa kati ya mwezi wa Januari mpaka Disemba walikuwa 81,509 na waliogundulika wameathirika ni wanawake 2,737, ni asilimia 3.4. Hii inaonyesha ni maambukizi makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri alizungumzia kuwa ataongeza vituo na dawa lakini hakuzungumzia chakula. Wagonjwa hawa wa UKIMWI wanapokula dawa za ARV basi ni lazima wapatiwe chakula kwa sababu dawa zina nguvu na wanazidi kuathirika. Kwa hiyo, naomba Serikali itenge fungu maalum la kuwasaidia hawa waathirika walio katika mikoa hii iliyoambukizwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja kwa wakunga jadi. Wakunga wa jadi ni watu ambao wanatoa msaada mkubwa katika kuwasaidia akina mama wajawazito vijijini. Naiomba Serikali wawape mafunzo hawa waliokuwa hawajapata na waliopata mafunzo waajiriwe, Halmashauri ziwatazame, ziwape angalau posho za kupata sabuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya afya na zahanati ziboreshwe kwa sababu miundombinu yake ni mibovu. Hakuna maji, umeme na vitendea kazi na isitoshe vituo vya afya vinajengwa mbali na wananchi. Kwa hiyo, ni shida, mzazi akipakiwa kwenye baiskeli mpaka akifika kwenye kituo cha afya basi huyo hali yake ni taabani, hana nguvu za kusukuma mtoto inampelekea kufariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali ifanye juhudi za makusudi ili kuwapatia wanawake hawa gari angalau kila kata au kila kituo kipatiwe ambulance. Wenzangu wengi wamesema na mimi naomba hilo ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Mheshimiwa Spika, sasa nazungumzia watoto wa mitaani. Watoto wa mitaani ni wetu lakini inakuwa ni kero. Watoto hawa ni kweli maisha ni magumu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo vya habari ni muhimu katika kuwaelimisha wananchi kwa kupata habari kwenye tv na redio pamoja na magazeti, lakini pia wakati wengine vyombo hivi hivi vinapotosha. Kwa hiyo wawe na umakini kwa sababu utaona habari ni ile ile lakini huwa tofauti wakati wa matangazo au machapisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo kilichofanywa na Serikali sio haki kuzuia vyombo vya habari kuonesha Bunge wakati wa vikao vya Bunge hii ni uonevu kwa sababu wananchi Bunge ni lao, vyombo ni vyao na Wabunge wanachangia ni Wabunge wao wamewatumia kero zao kwa nini wananyimwa uhuru wao wa kuona Wabunge wao waliowatuma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini wanamichezo wetu hasa wanawake wapokwenda nchi za wenzetu kucheza hawapati ushindi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la TBC ni chombo cha Serikali lakini chombo hiki hakiwatendei haki Watanzania kwa sababu hizo pesa wanazotumia ni za walipa kodi wa Tanzania, ukiangalia hiki chombo kina ubaguzi hasa wakati wa uchaguzi, tafadhali mtende haki. Serikali ni yetu sote hata ikiwa hatoki katika Chama cha Mapinduzi wakati uchaguzi umekwisha sasa kiongozi yeyote aliopo ni wetu sote acheni ubaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Nishati na Madini
Mheshimiwa Naibu Spika, nishati ya umeme ni nusu ya maisha ya binadamu hasa kwa wanawake kwa sababu mwanamke ni mdau mkubwa ndani ya nyumba; ikiwa umeme hamna au gesi basi kwake ni mtihani, itabidi afunge safari kutafuta kuni ili familia waweze kupata chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa ili aweze kupikia au kufanya biashara. Miti inakwisha na nchi inakuwa na ukame kwa sababu ukataji wa miti unaharibu vyanzo vya maji na wafugaji wanahangaika kutafuta maji kwa ajili ya kuharibika kwa mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madini, wachimbaji wadogo wadogo: Watanzania wengi ni wachimbaji wadogo wadogo ndiyo ambao wana mchango mkubwa katika kulipatia Taifa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo ili waweze kujiimarisha katika kazi zao, lakini la kusikitisha ruzuku hizi haziwafikii walengwa na kuanza kutoa malalamiko, mfano maeneo ya Mwanza, Geita na kadhalika. Naishauri Serikali iunde Kamati ya kusimamia jambo hili, ikibainika wahusika washughulikiwe, hayo ndiyo majipu ya kushughulikiwa kutumbuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishati ya mafuta ni muhimu sana katika maisha ya binadamu kama ilivyokuwa maji ni muhimu katika maisha ya binadamu na mafuta ni hali kadhalika, kwa sababu mafuta tunaendeshea magari, meli, ndege na pia kuendesha mitambo, kama hakuna umeme yanatumika kwenye jenereta. Hivyo, nishati ya mafuta inaleta uchumi katika Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha nchi hii haina formula ya bei maalum. Ukienda Dar es Salaam bei nyingine, Unguja bei nyingine, Ukienda Mtwara bei ni nyingine na nchi nzima bei hazilingani.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali ipange mpango maalum kwa kupanga bei ambayo inalingana ili wafanyabiashara wasiwanyonye wananchi, wengine ni wanyonge katika nchi hii wanahitaji kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa mchango huu, naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu ameijalia nchi hii kuwa na neema na mali nyingi yapasa kumshukuru. Maliasili ya wanyamapori inaingiza faida kubwa ya Pato la Taifa kwa kuvutia watalii wa nchi mbalimbali na Serikali imepata pato la asilimia 25 siyo kidogo. Tunajua kuwa TANAPA inafanya kazi kubwa katika kuchangia pato kubwa katika sekta ya utalii katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji ni lazima Waziri wa Maliasili na Utalii akae na wenzake wa Wizara ya TAMISEMI, Kilimo, Mifugo na Halmashauri ili waende pamoja katika kutatua migogoro hii ili kuleta amani juu kwa wakulima na wafugaji na kuleta suluhisho la kudumu ndani ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya kihistoria yaliyomo katika nchi hii yaboreshwe ili tuzidi kuvutia watalii katika maeneo yetu kama vile Kilwa au kule Zanzibar sehemu ya Chwaka, Tumbe na maeneo mbalimbali ili tuzidi kuukuza utalii na kuzalisha kipato zaidi.
Kuhusu suala la mazingira hususani ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa au kukata miti kwa biashara ya mbao vibali vinatolewa kiholela. Kwa kufanya hivi hii misitu itakwisha na ukame utashamiri katika nchi hii. Kwa hiyo, ni lazima Serikali iwe makini na kile wanachokifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango wangu huu, naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu deni la matibabu ya ndugu yetu, Marehemu Nassor Moyo ambalo hadi leo Serikali ya Uingereza inadai Tanzania. Deni hili ni aibu kubwa kwa nchi yetu, ni vyema Mheshimiwa Waziri alipatie ufumbuzi suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabalozi wetu walioko nje ya nchi wanadharauliwa kwa sababu nyumba wanazoishi haziridhishi na hazina ubora, hii ni dharau. Mabalozi wanaoishi katika nchi yetu ya Tanzania wanaishi nyumba za hadhi na ubora wa hali ya juu. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri suala hili alisimamie kwa nguvu zake zote ili lirekebishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Watanzania walioko nchi za nje wanapopatwa na matatizo au dharura, ni njia gani za mawasiliano watumie kupata msaada wa Kibalozi? Naomba Mheshimiwa Waziri atufafanulie suala hili.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sina budi kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuchangia hoja hii ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Dar es Salaam. Ni bandari ambayo inaipatia pato Serikali yetu kwa kiasi kikubwa, lakini leo hii tunakosa mapato makubwa kutokana na kodi kubwa kuongezeka na wafanyabiashara kukimbia bandari yetu kwa kuogopa kula hasara. Wafanyabiashara wa Congo, Zambia, Malawi, wote hao wamekimbia na kuifanya Bandari kuwa kavu. Kuna upungufu wa makontena, magari ya mizigo hayaingii, wengi wamekosa ajira na uchumi kudorora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge kazi yetu ni kuelekeza Serikali na kuishauri na kuikosoa pale inapofanya vibaya na kuisifu pale inapofanya vizuri. Sasa umefika wakati wa Mawaziri kusema ukweli, wasimdanganye Mheshimiwa Rais kwa kuogopa kutumbuliwa, hii ni nchi yetu sote, Watanzania wanatutegemea, tunakokwenda siko. Uchumi unaporomoka kutokana na mipango mibovu kuanzia matajiri mpaka mama ntilie. Mheshimiwa Waziri tunakwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano, kipaumbele chake inajipanga kufufua viwanda na kujenga viwanda, lakini haiwezi kufanikiwa ikiwa miundombinu ya umeme na maji ni mibovu, ni lazima kwanza ijipange. Serikali kwa kusimamia kupatikana kwa umeme wa uhakika ili wanapokuja wawekezaji kuingia nao mkataba waweze kufanya kazi na kuipatia nchi uchumi na vijana wetu kupata ajira na kupatikana maendeleo. Porojo za kwenye makaratasi hazitoshi tufanye maamuzi ya kiutekelezaji ndiyo dira ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya umeme wa uhakika inaweza kuendesha viwanda na kukidhi matumizi mengine ya wananchi wa kujikwamua kimaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo bado hakijapewa kipaumbele kwani benki hazitoi mikopo ili miradi ya kilimo iendelee; ni usumbufu mkubwa. Pembejeo hakuna, vitendea kazi kama vile matrekta, mbegu bora hakuna za kutosha, hivyo wakulima wapate mbolea mapema na bei zipunguzwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo maji vya vingi vimekauka kutokana na uharibifu wa mazingira na ukataji wa miti hovyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Waziri atatuambia nini kuhusu upatikanaji wa mikopo ya fedha kutoka benki ili wakulima waweze kufaidika kwa kupata mahitaji yao ili kukuza uzalishaji na kupunguza umaskini?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huu, naomba kuwasilisha.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Kibaha Vijijini (CCM)

Contributions (1)

Profile

Hon. Riziki Saidi Lulida

Special Seats (CUF)

Contributions (8)

Profile

View All MP's