Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Salome Wycliffe Makamba

All Contributions

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namsikiliza kwa makini sana Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha Mpango wake na nikazidi kupata maswali mengi ya utekelezaji wa Mpango wake kwa sababu mambo mengi ambayo ameyaandika yanaonekana kwenye nadharia na huenda yasitekelezwe au yasitokee kabisa kama Mpango uliopita. Mheshimiwa Waziri anasema kwamba anataka kuweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafanya maendeleo ya viwanda Tanzania
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mazingira hayo mazuri ya kibiashara Mheshimiwa Waziri hakuyaeleza kinaga ubaga na hilo linanitia mashaka, kwa sababu nikifikiria moja kati ya vitu ambavyo ni vya kipaumbele ili tuweze kukuza viwanda Tanzania tunaongelea habari ya umeme, miundombinu lakini mpaka leo na hata ukiangalia katika bajeti tuliyonayo hakuna nguvu ya ziada ambayo Serikali imeiweka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata maendeleo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano wa mazingira ambayo tunaishi Watanzania leo, bei ya umeme bado iko juu na wanasema kwamba wamepunguza kwa asilimia mbili lakini effect yake katika punguzo hilo haionekani katika uhalisia wa maisha ya Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika mazingira ya sheria ambazo Mheshimiwa Waziri alitakiwa azieleze kwamba ndiyo zimerahisisha utekelezaji wa sera hii ya viwanda, sioni kama ameonesha kwa njia yeyote ila ameweka sheria kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wadogo wadogo, labda kama yeye alipokuwa anaongelea maendeleo ya viwanda alikuwa anaongelea wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wawekezaji wadogowadogo hasa wale wanaohusika na mazao ya kilimo wanawekewa vikwazo, wanawekewa sheria ngumu na wanawekewa tozo mbalimbali ambazo mwisho wa siku zinawafanya wazidi kukwama katika harakati hii ya kujiendeleza katika kutengeneza malighafi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano moja katika Jimbo la Kahama Mjini, Jimbo lile kuna watu wanashughulika na biashara ya upakiaji na uchakataji wa zao la mpunga, lakini leo hii ukiangalia tozo ambazo wanatozwa watu wale mpaka wanafikia hatua ya kukata tamaa kujihusisha na zao hili la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamewekeza fedha zao kwa ajili ya kutengeneza na kupaki zao hili la mpunga, lakini kuanzia asubuhi mpaka jioni umeme hauwaki, ukiwaka jioni Polisi wanapita wanasema hairusiwi mtu kufungua kiwanda usiku. Kwa hiyo, wanajikuta ndani ya mwezi mzima watu wale wanashindwa kufanya uzalishaji, kwa hivyo hata zile fedha ambazo wamewekeza mle wanashindwa kuzirejesha kama walizikopa kwenye mabenki, lakini pia wanashindwa kuzizalisha ili ziweze kuwaletea faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa ukiangalia ambao ni wazalishaji, Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, anataka kuendeleza viwanda, lakini nimesikitishwa na taarifa ya Waziri anasema kwamba bei za mazao zinapaswa zizidi kushuka. Swali hasa lilikuwa limeelekezwa kwenye zao la maziwa ambapo Mkoa wa Shinyanga tunafuga sana ng‟ombe, kwa sasa hivi lita ya maziwa ni shilingi mia nne mpaka shilingi mia tano na watu wale hawanufaiki, kumfuga yule ng‟ombe ni gharama, sindano moja inakugharimu kuanzia laki nne mpaka tano kwa ngombe mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ile shilingi mia nne, shilingi mia tano kwa lita ya maziwa unaambiwa izidi kushuka sasa sijui yauzwe lita moja shilingi mia mbili, hapo sijamuelewa vizuri! Kwa maana hiyo, ni kwamba, tunawakatisha tamaa wakulima, tushushe bei ya zao la maziwa, tushushe bei ya zao la pamba, tushushe bei ya zao la tumbaku, halafu unasema watu tuko katika harakati za kuzalisha malighafi ya kutosha ili tuweze kuendeleza viwanda Tanzania!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikia kauli mbalimbali za Serikali zikibeza misaada, lakini ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri inasema wazi kwamba gharama kwa ajili Mpango huu wa Maendeleo itakuwa ni trilioni 107 na Serikali itatoa trilioni 59 tu, hiyo baki inayobaki tunategemea kuitoa wapi? Bila shaka fedha hizo huenda zingetoka kwa wahisani au wafadhili na labda kukopa kwenye mabenki ambapo mwisho wa siku inaonekana kwamba fedha hizo tunashindwa kuzirejesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kutoa kauli badala yake inazidi kuwabeza hawa watu. Sasa hivi tuko katika ulimwengu wa teknolojia, wanazipata hizi taarifa na hakuna mtu yeyote anayeshtuka na kuona kwamba yule mtu anayetusaidia angalau kidogo tunatakiwa tumheshimu, badala yake tunatoa kauli za kukejeli na kauli za dharau, wakati leo hii waziri anathibitisha wazi kwamba ana zaidi ya nusu ya gharama ya bajeti ambayo hajui atakapoitoa. Matokeo yake anategemea kwenda kuzidi kuwabana watu kwa kuchukua property tax za Halmashauri, anategemea kwenda kuwabana watu kwa kuchukua kodi mbalimbali ambazo Halmashauri inakusanya kwa ajili ya kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika mazao mbalimbali ambayo leo hii yalitegemewa yatunufaishe Watanzania. Wakati tunachambua sheria ndogo za Halmashauri, tulionamkulima amebebeshwa mzigo mkubwa sana. Kwa mfano, moja kati ya sheria ndogo mkulima anaambiwa achangie mpaka fedha kwa ajili ya Mwenge, hivi kweli Mwenge, kwa nini Serikali Kuu isitoe hiyo pesa kama kweli inaona hilo jambo ni la muhimu sana hata inambebesha mkulima mdogo kutoa hiyo pesa ikiwa ni moja kati ya tozo ambayo imelimbikizwa katika zao lake lile ambalo anategemea kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni sehemu ambayo Mheshimiwa Waziri ananieleza juu ya kuboresha ufundi stadi ili kuweza kupata watu ambao wataweza kufanya kazi katika hivi viwanda ambavyo vinategemewa kuanzishwa. Katika mikoa tumeona kuna VETA moja tu katika kila Mkoa na mtu anavyotaka kufungua Chuo cha Ufundi Wilayani kuna ukiritimba mwingi na process ndefu ambayo inamkwamisha mtu binafsi kuweza kufungua Chuo cha Ufundi au Chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri afahamu kabisa kwamba tunayo sera ya kwamba mwekezaji anatakiwa kuajiri watu wanaozunguka eneo alilowekeza. Walio wengi na miradi mingi inawekezwa maeneo ya vijijini na maeneo yale hayana watu ambao wana elimu ya juu na wanategemea kupata watu ambao angalau wanaweza kuwa na elimu ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa mgodi wa Buzwagi na Bulyanhulu ambayo ipo katika Vijiji vya Kakola na Wilaya ya Kahama, maeneo yale watu wengi siyo kwamba wana elimu ya juu, lakini hakuna Chuo cha Ufundi kwa ajili ya kuendeleza wale watu, unamkuta mtu anafanya kazi ya kibarua zaidi ya miaka minne, mitano, kwa sababu hana jinsi ya kusoma angalau masomo ya jioni ili aweze kupanda kutoka ile rank aliyopo kwenda juu, inambidi aendelee kufanya kazi ile itakayomtesa kwa miaka nenda miaka rudi halafu leo Waziri anasema anataka kuendeleza ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado sijaelewa vizuri mkakati wa Waziri anaposema anataka kuuza viwanda, kwa sababu kwa upeo nilionao ni kuwa viwanda vikubwa vinatokana na viwanda vidogovidogo ambavyo vinaanzishwa na wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii pale Kahama tunalo soko la wakulima, wale watu wamejiunga kwenye ushirika na wamekusanya fedha zao wamejitahidi wameweza kutengeneza lile soko na leo linaonekana ni moja kati ya masoko makubwa katika Mji ule. Hata hivyo, leo ukiangalia soko lile Serikali imekubali ule ushirika kuupeleka ukauzwa kwa mtu binafsi, wakati Sheria ya Ushirika iko wazi kwamba soko lile lilitakiwa liuzwe kwa ushirika mwingine ulio hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linaungwa mkono na Serikali, kibali kimeshatoka, soko lile ambalo wananchi wamekusanya jasho lao linapelekwa kupewa mtu binafsi, wakati wale watu waliweka nguvu. Nilitegemea Serikali iwasaidie, iwawezeshe, iwape mtaji ili lile soko liweze kuwa kubwa, liweze kukidhi mahitaji ya ndani na ya nje ya Mji ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutilia mkazo katika elimu. Kama kweli tunataka kwenda katika biashara ya viwanda ni lazima tuhakikishe tunatoa elimu ambayo ni ya ubunifu na wananchi wana uwezo wa kutoa ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda. Elimu tuliyonayo leo hii ni ile ya kukariri, ndiyo maana unasikia mara leo Mama Mheshimiwa Ndalichako anasema kuna GPA, mara anarudi kwenye Division, ni kwa sababu hatuna system ambayo inaweza kutambua njia sahihi ya utoaji wa elimu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuko serious hatuwezi kusema tunaenda kuendesha elimu kwa njia ya mtu kutoa matamko tu kwenye magazeti. Elimu inatakiwa iboreshwe kwa kufanyiwa utafiti na ikidhi mahitaji ya Watanzania na siyo kwa kukidhi mahitaji ya Serikali ya CCM inasema hivi, kesho inakuja Serikali nyingine inasema mnawayumbisha watoto mnawa- frustrate, naomba Serikali iwe serious tunapoongelea masuala ya elimu kwa ajili ya mabadiliko ya viwanda hatuongelei tu suala la kufurahisha chama fulani au chama fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ningependa kuongelea suala zima la miundombinu. Barabara za Mitaa na barabara za TANROAD, barabara hizi zimegeuzwa kama mitaji. Tunayo barabara ambayo inatoka Kahama inaelekea Kakola pale Jimbo la Shinyanga kuunganisha na Jimbo la Msalala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inafahamika wazi kwamba uwezo wa ile barabara haiwezi kubeba magari ya ukubwa wa namna ile ambayo yanapeleka mizigo mbalimbali kuelekea mgodini na kuelekea Geita, badala yake TANROAD imegeuza ile barabara kama mtaji, kila mwaka ile barabara inafanyiwa repair, inamwagiwa kifusi na ku-level, sasa hivi ni zaidi ya miaka kumi tangu mgodi ule umeanzishwa barabara ile inafanyiwa repair kila mwaka na mamilioni ya fedha yanapotea. Naomba Waziri husika alitazame hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea maendeleo ya viwanda hatumaanishi kudunduliza pesa, bora kama fedha ni ndogo basi tuwekeze mahali ambapo tunaona kwamba italeta tija na italeta maendeleo ya nchi hii, lakini siyo tunaruhusu watu wanatumia hii kama ni njia ya kujinufaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Pia ningependa kuchukua fursa hii kuipongeza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa hotuba nzuri iliyoonesha weledi na uzamifu katika suala zima la Katiba na Sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeeleza yote watu watapiga makofi lakini mwenye macho na masikio atasikia neno hili ambalo watu wa Upinzani tumeeleza Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema inahitaji digrii ya ujinga kukubali kupewa kazi bila job description halafu useme huo ni uamuzi wa bosi wako kama anaweza akakupa au asikupe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia hotuba hii kwa kushauri Serikali mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa kama Wabunge kazi yetu kubwa ni kuisimamia na kuishauri Serikali ili iweze kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutekeleza hayo ningependa kushauri na kuwaomba wanasheria waliopo humu na Mawaziri waliopewa dhamna hii waishauri Serikali itekeleze majukumu hayo kwa kumshauri Rais ipasavyo juu ya utekelezaji wa majukumu hayo kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wafahamu wazi kwamba Urais ni taasisi na siyo mtu binafsi.
Mheshimwa Rais tamko lolote atakalolitoa iwe ni kwa masihara au yupo anakunywa chai au anafanya kitu chochote kwetu sisi tunaiona kama ni agizo na tunaichukulia kama ni sheria, kwa hivyo, Mawaziri wahakikishe kwamba Rais wao anapotoa matamko basi yawe ni ya kujenga na siyo kubomoa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba suala la uendeshwaji wa nchi hii, tukiangalia suala la sukari, suala la vyombo vya habari, suala la utekelezaji wa haki za binadamu, uendeshwaji wa mahakama ni suala ambalo kimsingi Rais wa nchi hii alipaswa kukalishwa chini na kuelezwa ni lipi aliongee kwenye jamii ambalo mwisho wa siku litaleta matunda na siyo kuibomoa nchi hii na kuirudisha mwaka 1980 enzi za uhujumu uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, madhara makubwa, leo asubuhi tumepata taarifa kwamba bei ya sukari imefika shilingi 3,200...
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Na hii nayo inasababishwa na tamko ambalo Mheshimiwa Rais alilitoa, tunaamini matamko, sheria, kanuni na taratibu za nchi hii zinafanyika kwa kushirikisha wadau, endapo tatizo au suala la sukari na ukuzaji wa viwanda lingeshirikisha wadau ambao ni watumiaji wa sukari pamoja na wafanyabiashara wa sukari, huenda tusingefikia kwenye hatua hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya mahakama zetu tukubaliane mbali na itikadi zetu za kisiasa ni tatizo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu. Tunakosa uhuru wa mahakama kwa sababu mahakama hizi kinyume na sheria mbalimbali zilizowekwa ikiwa ni pamoja na sheria za kimahakama na uendeshaji wa nchi hii zimekosa uwezo na uwezeshaji. Nimeshangaa sana Mheshimiwa Mbunge aliyepita aliposema kwamba tusiongelee kwa sababu hii ni mihimili inayojitegemea, lakini sisi kama Wabunge ndiyo tunaopitisha bajeti ambayo inakwenda kuiendesha hiyo mihimili mingine. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuhakikisha tunatetea na tunasimamia maslahi ili mihimili hii iweze kuwa independent na iweze kufanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mahakama zetu zimekuwa zikikabiliwa na changamoto za miundombinu, malipo ya wafanyakazi na madaraja ya mahakimu; mahakimu wawili wana cheo kimoja, wana daraja moja lakini wanalipwa mishahara tofauti. Suala hili linapaswa kuzungumziwa humu kinyume na mjumbe aliyetoka kuongea anasema kwamba huo ni mhimili unaojitegemea sijui kama yeye ana mfuko wa kuwapelekea mahakama pesa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara ya Mahakama inakabiliwa na changamoto kubwa ya rasilimali. Mwaka wa fedha uliopita Wizara ya Katiba na Sheria ilipangiwa fungu lakini pesa hazikupelekwa ndiyo tunaona inazidi kudorora siku hadi siku. Tumeshuhudia kwenye kesi za uchaguzi, Majaji wanakosa impartiality katika decisions zao, ni kwa sababu ya umaskini wa hali ya juu ulioko katika ngazi ya mahakama. Mahakimu wanapewa baiskeli kwa ajili ya kwenda kazini, wanakosa nyumba, hawawezi kujikimu na hii inapelekea kushindwa kusimamia majukumu yao wakiwa kama mhimili wa Serikali unaojitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijatoka kwenye suala la mahakama mwaka 2012 ulitolewa waraka ambao ulikuwa unaongelea kada ya Mtendaji wa Mahakama. Lengo la kuwa na kada ya Mtendaji wa Mahakama ilikuwa ni kuboresha utendaji kazi wa kiutawala katika ngazi ya Mahakama. Kinyume na mategemeo, kada hii imeshindwa kutekeleza majukumu yake badala yake hali imezidi kuwa mbaya lakini watu hawa wanalipwa na Serikali. Ningeomba Waziri wa Katiba na Sheria aliangalie suala hili kwa umakini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba niongelee suala la Law School. Tanzania tumekuwa na mfumo ambapo mwanafunzi anapomaliza shahada yake ya sheria analazimishwa kwenda kusoma Law School, lakini Law School imekuwa tofauti na shahada ya sheria. Tanzania vyuo vinavyotoa shahada ya sheria viko Mwanza, Mbeya, Arusha na maeneo mbalimbali na Law School ya Tanzania iko Dar es Salaam. Wanafunzi wanalazimishwa kusafiri kutoka huko wanakosomea ambako walichagua mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya Law School. Usipofanya hivyo, pamoja na miaka minne aliyoipoteza wakati unasoma shahada yako ya sheria mwanafunzi yule hawezi kutambulika kama ni mwanasheria kamili na hawezi kupata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na tatizo hilo, wanafunzi hao walio wengi walikuwa wanasomeshwa kwa kutumia mkopo. Cha kusikitisha ni kwamba anapokwenda Law School suala la mkopo inabidi lifanyiwe pre-assessment tena na wanafunzi hawa hawapewi mkopo. Kwa taarifa tu, sasa hivi ada ya Law School ni shilingi milioni moja laki tano na zaidi. Watoto waliokuwa wanasoma shahada ya sheria walikuwa wanalipiwa mkopo na Serikali lakini linapofikia suala la kwenda Law School linakuwa ni jukumu la mzazi kujua yule mtoto atafikiaje kwenye hatua hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili inabidi liangaliwe kwa umakini. Tunayo majengo yako UDOM pale wanakaa buibui, tunayo majengo na watu ambao wanaweza kutekeleza suala hili, lakini leo watu wachache wamejirasimisha zoezi hili wameweka Law School Dar es Salaam. Watu wanalazimishwa kusafiri mpaka Dar es Salaam, hawana makazi, wengine hawajawahi hata siku moja kufika Dar es Salaam, wanalazimishwa wakakae pale wasome Law School kwa sababu kuna maprofesa wachache au watu wachache wanaotaka kunufaika na mfumo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda suala la Law School lishirikishe wadau hasa wanafunzi wanaokwenda kwenye shule hiyo. Pia ifahamike kuna watu ambao hawakusoma Law School zamani lakini leo kila gazeti utakalolishika linatangaza kazi lazima uwe umepitia Law School. Kwa yule ndugu yangu ambaye hafahamu kiingereza kama alivyoomba afundishwe Law School ni ile shule ya sheria ambayo ni lazima uende kusoma ili uweze kuwa Wakili kwa mujibu wa Law School Act ya mwaka 2007.
MHE. SALOME. W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, namuone huruma sana Mheshimiwa anayesimama na kusema kwamba anakaa Dar es Salaam lakini hajawahi kuona mahakama. Mahakama si kama tangazo la Vodacom au la Tigo linalobandikwa kwenye jukwaa.
MHE. SALOME. W. MAKAMBA: Mahakama ni institution ambayo iko kwa mujibu wa sheria na anachoelezwa ni fact kwa mujibu wa sheria. Unaweza ukakaa Dar es Salaam ukafahamu ratiba ya vigodoro Dar es Salaam nzima lakini usijue ziko mahakama ngapi.
MHE. SALOME. W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu kwa maandishi ili na mimi niweze kushauri Serikali katika kuboresha sekta hii muhimu ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Elimu itoe fursa kwa watu binafsi wenye uwezo kuwekeza katika elimu ya ufundi VETA. Hii itasaidia kuipunguzia mzigo Serikali unaotokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mimba za wanafunzi, Wizara ilete Muswada Bungeni utakaoonesha jinsi ya kuwabana na kuwawajibisha wale wanaohusika na mimba hizo. Pia Serikali iweke mtaala maalum kwa wasichana wanaozalia shuleni ili tusije wapa haki ya kusoma na kujikuta tunakandamiza haki ya watoto waliozaliwa mfano haki ya kunyonya, kuwa karibu na wazazi lakini pia tusijeleta mzigo mkubwa wa kulea kwa bibi watakaokuwa wakilea watoto hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujitahidi kutoa motisha kwa Walimu ili kuwapa morali katika utendaji kazi wao. Natoa mifano michache ya baadhi ya Walimu niliokutana nao katika Wilaya ya Kyerwa kwenye moja ya ziara zangu. Walimu hawa walipandishwa vyeo miaka miwili iliyopita lakini mpaka leo hawajaongezewa mishahara. Nafahamu changamoto ya bajeti inayoikabili Serikali yetu ila nashauri tusiwapelekee barua za kuwapandisha vyeo kama hatuna uhakika na malipo yao. Baadhi ya Walimu hao ni kama ifuatavyo:-
(1) Rutaihwa Kazoba
(2) Geofrey Kamondo
(3) Rugeiyamu Damian
(4) Selestine Tibanyendera Ishengoma
(5) Erick Twesige Anacleth
(6) Philbert Jeremiah Kazoba
(7) Tabu Herman
(8) Ndyamukama Cylidion
(9) Heavenlight Baguma
(10) Frida Buyoga
(11) Onesmo Alphonce
(12) Philbert Kinyamaishwa
(13) Diomedes Kajungu
(14) Yohatam Samwel
(15) Diomedes Kajungu
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali hao ni baadhi ya Walimu waliopo katika Wilaya ya Kyerwa ambao nilipofanya ziara yangu ya kiutendaji niligundua hao na wengine wengi ambao majina yao sijayataja wamepandishwa vyeo kwa takribani miaka miwili sasa na mpaka leo hawajaongezwa mishahara. Naomba Mheshimiwa Waziri ufuatilie matatizo haya katika Wilaya ya Kyerwa na upatapo nafasi naomba unijibu hoja zangu hizi kwa maandishi ili niweze kupeleka mrejesho kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kumwomba Waziri ashirikiane na Wizara ya TAMISEMI ili kuweza kusukuma vipaumbele ambavyo kimsingi Wizara hii mnakutana navyo moja kwa moja katika kutekeleza Sera ya Elimu nchini. Nakutakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yako, ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati na Madini. Naamini nafasi hii haijaja kwangu kwa bahati mbaya kwa sababu, natokea Mkoa wa Shinyanga ambao umebarikiwa kuwa na baraka ya madini kwa sababu, nina migodi mitatu mikubwa; migodi miwili ya dhahabu, Mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi iliyoko Jimbo la Msalala na Jimbo la Kahama. Nimebarikiwa kuwa na Mgodi wa Williamson Diamonds ulioko Mwadui Shinyanga, lakini pia nina mgodi, medium scale mining wa El-Hilary ulioko Buganika, Kishapu, ukiacha migodi mbalimbali midogo midogo inayohusika na uchimbaji na uchenjuaji dhahabu ambayo imezunguka Mkoa mzima wa Shinyanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Shinyanga ni Mkoa ambao unachangia takribani asilimia tisa ya pato la Taifa hili na hii ni baada tu ya Mkoa wa Dar-es-Salaam na hii inatokana na uwepo wa nishati na madini katika mkoa huo. Pamoja na baraka hizi ambazo Mkoa wangu wa Shinyanga umebarikiwa kuwa nazo leo nikisema niondoke na watu wachache hapa kwenda kuangalia hali halisi ya mkoa huu, ukilinganisha na baraka hizi ambazo tunazo, mambo yanayoendelea kule ni mambo ya kusikitisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga hasa maeneo ya uchimbaji, walipoletewa habari hii ya uwekezaji wa sekta ya madini walifikiri kwamba, itakuwa ni faraja kubwa kwao na itawakwamua na umaskini, lakini kwa bahati mbaya watu hawa, badala ya mijadala ya kuwahamisha ili kuweza kuwapisha wawekezaji kufanyika kama inavyoelekeza Sheria ya Madini ya mwaka 2002 na 2008 badala yake watu hawa walihamishwa kwa kufukuzwa kama wakimbizi kwenye ardhi yao wenyewe. Mbali na hivyo, watu hawa walilipwa fidia ambayo intervention ya Serikali katika ulipaji wa fidia hizi, ikawa ni kinyume na matarajio ya wakazi hawa, hasa maeneo ya Kakola, ambako kuna mgodi wa Bulyanhulu na maeneo ya Kahama Mjini ambako upo mgodi wa Buzwagi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa mpaka leo wamekuwa na kilio cha muda mrefu. Zaidi ya miaka 10 wanalalamika kuhusu unfair compensation iliyofanyika kwenye maeneo yale, lakini Serikali ambayo tunaamini kwamba, inaweza kushughulikia matatizo yao haioni umuhimu wa kushughulikia matatizo hayo na wale wananchi wa-feel kweli Serikali ipo kwa ajili ya kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ni wapole na ni watulivu, pamoja na maumivu makali waliyoletewa kwa sababu ya unfair compensation, malipo ya fidia ambayo hawakuridhika nayo, walikubaliana kuvumilia mgodi wakiamini ipo siku Serikali itakuja kutatua matatizo yao. Pamoja na Serikali kutokutatua matatizo yao na kuwaahidi kwamba, watapata kazi kwenye migodi ile, mpaka leo wananchi wale hawapati ajira na wakifanikiwa kupata ajira basi, watapewa zile ajira ambazo mwisho wa siku zitawaacha katika hali ya umaskini mkubwa na utegemezi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaozunguka eneo la mgodi wakipata kazi kubwa katika migodi hii ambayo tunaamini ni ya wawekezaji watapata kazi ya kufagia, kufyeka, upishi na hakuna program zozote za msingi ambazo ni madhubuti zimewekwa na Serikali zinazoweza kuwaendeleza wananchi wale! Japokuwa tunasema wamefanya kazi kwa muda mrefu tuna-assume kwamba, wana-on job training, basi angalau i-certify ujuzi walionao ili siku moja watu wale waweze kuja kupata kazi ambazo zitawaingizia kipato na cha akiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitishwa sana na matukio yaliyojitokeza kwenye Mgodi wa Bulyanhulu miaka ya 2000, 2002, 2005; wafanyakazi wale walipata ulemavu, wengi wao wakiwa ni ma-operator. Wale ambao tulipata bahati ya kwenda kutembelea migodini kuna Watanzania wenzetu wanaofanya kazi ya ku-operate mitambo katika migodi ile, lakini pamoja na maradhi waliyoyapata kwa sababu ya kufanya kazi ngumu na nyingine zikiwa underground, watu wale walipelekwa kutibiwa na mgodi na wakiwa wanaendelea na matibabu yale, wale watu walirudishwa kazini na kufukuzwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi zao ziko Mahakamani. Mpaka leo wanahangaika wengine wanakufa kwa sababu ya magonjwa, lakini Serikali inayojiita Serikali sikivu, sijaona hatua mahususi, hatua madhubuti za kusaidia kutetea watu hawa na leo hii tunajisifu hii ni Serikali ya Hapa Kazi Tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha mbali suala la watu kufukuzwa kazi, kuna watu ambao leo migodi ya Tanzania, migodi ya wawekezaji imekuwa ni Serikali ndani ya Serikali ya Tanzania. Wafanyakazi wanapokosea katika migodi ile adhabu wanayopewa bila kujalisha ukubwa wa kosa alilolifanya anapewa adhabu ya kufukuzwa kazi na anafungiwa haruhusiwi kufanya kazi mahali popote pale maisha yake yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala limewaathiri watu wengi ambao kama nilivyotoka kusema awali, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga maisha yao yote yamekuwa ni maisha ya madini. Unapomwambia kwamba, haruhusiwi kufanya kazi tena ina maana unamzuia yule mtu kupata kipato halali na hakuna adhabu Tanzania hii, labda kama ni adhabu ya kifo, inayomfanya mtu kupewa adhabu ya milele, lakini hicho ndiyo kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo migodi inafungwa! Tumeona Mgodi wa Tulawaka umefungwa na Mgodi wa Buzwagi huenda mwakani ukaanza closure plan na migodi mingine itafungwa. Kinachotokea nyumba zinazozunguka migodi hii zimekuwa zikipata athari kubwa ya uwepo wa migodi hiyo, kama athari za milipuko na athari za kemikali inayoweza kuvuja kutoka migodini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo Tulawaka imeshafungwa na Buzwagi itafungwa. Vijiji vya Mwendakulima, Vitongoji vya Ikandilo, Chapulwa, Mwime, Mbulu, Kakola, kule Msalala watu wanalia, nyumba zao zimepata crack, zimepasuka kwa sababu ya athari ya milipuko! Nimewahi kushiriki kwenye Kamati kwa ajili ya kuangalia athari za milipuko na Kamati hizi zilishirikisha watendaji wa Serikali ambao ni Majiolojia na Maafisa Madini. Afisa Madini anakuja kwenye Kamati ya Uchunguzi wa Athari ya Milipuko na kalamu na karatasi; utawezaje kuchunguza athari ya mlipuko kwenye nyumba bila kuwa na vifaa ambavyo vinaweza kukupa data zinazoeleweka Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea ku-improve sekta ya madini na uwekezaji, tunaongelea kuwapa vifaa Wataalam wa Serikali ili tuweze kupata ripoti ambazo zipo impartially, ambazo zinaweza kusaidia na kutetea maslahi ya wafanyakazi wetu na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda Nyamongo kuna kesi, hata leo ukifungua kwenye google, kuna kesi inaitwa the Tigiti River; ile kesi watu waliripoti, Wabunge walipiga kelele Bungeni na mto ule ulikuwa unatiririsha maji yanayotoka mgodini ambayo yalisemekana kwamba yana sumu, yalitiririshwa kwenda kwenye vijiji na ng‟ombe wakafa na watu wakaathirika, lakini Serikali ikapuuza kelele za Wabunge, kama ambavyo mnafanya sasa! Matokeo yake ripoti ya Umoja wa Mataifa na Mataifa mbalimbali ndiyo iliyofanyiwa kazi. Hivyo, leo tutaendelea kupiga kelele humu ndani na kama kawaida Serikali itapuuza, lakini naamini sisi tukiongea msipofuatisha na mawe yataongea na ipo siku mtatekeleza matakwa ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee kwenye suala la uchimbaji holela. Katika Wilaya ya Bukombe kuna Pori la Kigosi Moyowosi na Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 2009 inasema, hairuhusiwi kuchimba madini hasa ya dhahabu except for strategic minerals. Lakini leo…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndiyo huo!

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuwawakilisha wananchi wangu wa Shinyanga katika bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyeki, napenda kuongea na Mheshimiwa Waziri na kumwomba atusaidie matatizo ya ushirika pale Kahama. Mheshimiwa Waziri wote tunafahamu Sheria ya Ushirika namba 20 ya mwaka 2003 inasema wazi kwamba Ushirika ukifilisika mali zake zitakwenda katika Ushirika mwingine. Hilo limekuwa likifanyika tangu mwaka 1984, mwaka 1986, lakini cha kushangaza hivi karibuni pale Kahama Chama cha Ushirika kimepewa Kampuni. Wamepewa Kampuni kinyume na utaratibu na Mahakama imetengua lakini mpaka leo Chama kile cha Ushirika
kimeng’ang’aniwa na Kampuni na wale wananchi ambao walijiunga pamoja, ambao ni wakulima wadogo wadogo wakatengeneza Ushirika, wakajenga vibanda, wamenyang’anywa maeneo yao. Suala hili nimeshalipigia kelele mara nyingi humu Bungeni na hakuna msaada wowote unaoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri alitazame jambo hili kwa jicho la pekee. Wale wakulima ni watu ambao ni wanyonge, hawana pesa, hawawajui watu wakubwa, lakini kwa sababu walioko pale ni mapapa, ni mafisadi, wamewanyang’anya maeneo yao wale watu, vibanda zaidi ya 200 vimechukuliwa, soko lile limemilikishwa kwa mtu mmoja ambaye ndiye mwenye hisa nyingi kwenye Kampuni ile na wale watu wanakosa pa kukimbilia. Namfahamu vizuri Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Tizeba ni mtetezi wa wanyonge. Namwomba sana aje kwetu pale atusaidie kutatua tatizo hili kwa sababu limekuwa ni tatizo sugu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wale watu wakihoji kuhusu Ushirika Mheshimiwa Waziri wanakamatwa, wanaenda kuwekwa ndani, wanaanza kuhojiwa, wanatishwa, vitisho hivyo ni unyanyasaji kwa raia wanyonge wa Tanzania hii. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie kutatua tatizo la ushirika kwa sababu limezidi, kwanza ni kinyume cha Sheria, Mahakama imeshatengua Kampuni ile kumiliki, ile hati iliyopo pale ya Kampuni imetenguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza wanatakatisha hati ile, wanafanya kui-renew ili ionekane kwamba ni hati halali. Kweli tatizo hili limezidi, limekuwa la muda mrefu lina miaka zaidi ya 27, tunaomba Mheshimiwa Waziri tafadhali aje atusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo niongelee suala la upigaji chapa ng’ombe, tumezinduliwa mradi sasa hivi wa kupiga chapa ng’ombe. Wanasema ni kwa ajili ya sababu za kiusalama wanataka kutambua ng’ombe na wale wanaokuja kutoka nchi za jirani. Hata hivyo, wanasema upigaji chapa hawa ng’ombe gharama yake ni Sh.3,000/= kwa kila ng’ombe. Sisi Wasukuma tunasifika kwa ufugaji. Familia za vijijini Sh.3000/=, Sh.1,000/= ya kula tunahangaika kutafuta hiyo Sh.3,000/= tutaitoa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ndizo tozo za kero ambazo zilipigwa marufuku na Mheshimiwa Magufuli. Kama wanaleta mradi basi watafute namna ya kuutekeleza mradi ule bila kuwaumiza wananchi na Mheshimiwa Waziri anafahamu kabisa kwamba kupiga chapa ng’ombe kunashusha thamani ya ngozi ile inapotakiwa kuuzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunasema tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, tunasema tuwakwamue wananchi kwenye umaskini, leo tunaenda kuwapiga chapa ng’ombe wao na tunawatoza Sh.3,000/=. Tunaomba majibu tunahitaji kujua ni njia gani itatumika kuwapiga chapa bila kuwabughudhi, bila kuwakera wakulima hawa ambao ufugaji kwao ni biashara, ufugaji ni maisha, lakini ufugaji kwao ndiyo chakula cha kila siku na ndio utamaduni wetu vile vile. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie sana majibu juu ya hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala la punda. Usukumani punda wanatumika kwa ajili ya kubeba mizigo, maji, ndio usafiri kule kwetu. Hata hivyo, hivi leo nikikueleza punda wanauawa, punda wanauzwa, wamekuwa ndio biashara. Mheshimiwa Waziri, China wanabiashara ya ngozi, wananunua ngozi hizi za punda na wanatengeneza anti aging, dawa ambayo inayozuia kuzeeka na inaongeza nguvu za kiume pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ya Mheshimiwa Waziri, biashara hii…

MWENYEKITI: Mheshimiwa umesemaje? (Kicheko)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la punda lina dawa ambayo inatumika kule China kupunguza kuzeeka, lakini pia inaongeza nguvu za kiume. Kwa sababu hiyo thamani ya punda ni Sh.50,000/= mpaka Sh.190,000/=, lakini thamani ya ngozi ya punda ni pound 160, ngozi peke yake. Juzi Mheshimiwa Mwijage wakati anapitisha bajeti yake hapa alisema amepiga marufuku uuzaji wa punda. Hii haitoshi, tunatakiwa tuisimamie kama tunavyopiga marufuku mambo ya pembe za ndovu na biashara nyingine, kwa sababu hii itapelekea kupotea kwa hawa punda ambao ni mifugo tunayoitegemea sisi kama njia ya usafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumeamua kuingia kwenye biashara hiyo basi tuwe na mechanism ya kuongeza hawa punda wawepo wawe ni wanyama wa biashara, waongezeke tuwe na jinsi ya kuboresha, kwa sababu hii mifugo iko chini ya Wizara yako na hii mifugo sisi tunaitumia kama njia ya usafirishaji kule kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ethiopia wana mifugo milioni 7.5 hii ya aina ya punda, lakini kuna nchi ambazo zimepiga marufuku na wameweka sheria, nchi kama Burkina Faso, Niger na Pakistan wameshaweka Sheria. Kusema tu haitoshi, tunafungua mianya ya wale watu ambao watakuwa wanafanya ujangili wa mifugo hii. Tusifungue mianya kwa sababu hatimaye itatuathiri sisi wenyewe. Tuweke sheria ambazo zitazuia, lakini kama unataka kufanya biashara hiyo na wafanye kwa njia halali na kuwe na misingi ya kuzuia upotevu wa wanyama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu kwa kweli Ushetu, Tarafa ya Mweli hakuna hata josho, tarafa nzima ina kata karibu sijui ngapi, hakuna hata josho la kuoshea ng’ombe. Sasa bajeti ya Kilimo na Mifugo haifiki hata trilioni moja na tunategemea eti huu uti wa mgongo wa Kilimo Kwanza; sijui hata hiyo sera iliishia wapi; tunategemea eti malighafi itokane na mazao wa kilimo na mifugo, eti uti wa mgongo wa nchi hii ni kilimo, wakati huo huo hata bajeti yenyewe haiakisi malengo ya nchi hii ya Tanzania ya kutokana na malighafi za kilimo na mifugo. Hivi kwa nini tuendelee kuwadanganya Watanzania? Mimi sina wasiwasi na ukusanyaji wa kodi katika nchi hii, wasiwasi wangu ni allocation ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atueleze mkakati wake wa kuongeza kilimo na mifugo kwa nchi hii kuelekea ku-connect na wazo la Tanzania ya viwanda ukoje? Ukiangalia ni theory tu, utekelezaji wa theory hii mimi siuoni, naona tu ni maneno yanasemwa na mwakani wanatumia kitabu kile kile wanabadilisha mwaka wanabadilisha vitu vidogo wanarudisha kitu kile kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, anaakisi vipi, anashirikiana vipi na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutengeneza barabara ili atusaidie kule Ushetu, Kinamapula, Nyandele sijui Wandele sijui wapi, anatusaidia vipi kuleta barabara tuweze kulima kilimo cha tumbaku? Pamba imeshakufa, zao la biashara tulilonalo Shinyanga sasa hivi ambalo tunalitegemea ni tumbaku, lakini hakuna miundombinu iliyoboreshwa kila siku ni hadithi mtatekeleza lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's