Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Lucy Simon Magereli

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti nipo. Naomba nikushukuru sana kwa kunipa fursa kuchangia. Niwie radhi kuwa nimeisikia sauti yako kuwa ningekuwa next, lakini ni suala jema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mapaji mengi, lakini kwa kujaaliwa fursa ya kuwepo hapa leo ili na mimi nitoe mchango wangu katika Wizara iliyoko mbele yetu.
Naomba kabla sijaendelea niungane na nimpongeze sana Mheshimiwa Mama Janet Mbene, kwa kweli mchango wako nimekusikia wakati wote uliposimama, uliiongelea ajenda ambayo na mimi ningetamani sana tuendelee kuiangalia kwa nguvu. Niulize tu kwa Mawaziri wahusika, Wizara ya TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora kwamba where is the woman?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Koffi Annan aliwahi kusema “There is no tool for development more effective than empowerment of a woman.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, there is no tool for development more effective than empowerment for a woman. Sasa nimezitazama hotuba, nimekwenda mbele, nimerudi nyuma, nimesikitishwa na namna ambavyo tunapewa empty promises. Mnafahamu population ya wanawake Tanzania ni kubwa, lakini kwenye elimu mmetuambia ni bure, lakini katika uhalisia hiyo elimu bure haina mkakati. Sasa tunapita around the bush kutafuta means and ways ya kui-subsidize hiyo elimu bure katika utaratibu ambao tulikuwa hatujajipanga; lakini bado katika hilo suala la elimu hata nilikopitia, swali langu lilibakia lile lile, where is a woman? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kwenye afya, nikatamani niwaulize, kwenye bajeti ambayo imekuja mbele yetu kimsingi imekuwa ya jumla na kwa jinsi hiyo inaendelea kuniacha niendelee kuuliza, where is the woman? Afya ya mwanamke, afya ya uzazi kwenye ripoti ya mpango nimeona mnasema vifo vya akina mama eti vimepungua kutoka 450 na kitu kuwa 410, kwa kuvipunguza vifo hivyo kwa idadi tu ya akina mama 30 hivi kutoka kwa akina mama 100,000 wanaojifungua, siyo jambo la kujisifia hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika mmelitoa with pride kabisa ndani ya ripoti mnasema vifo vya akina mama wanaojifungua wakati wa uzazi vimepungua; lakini fikiria ni uchungu kiasi gani eti akina mama mia nne na kitu wanakufa kati ya akina mama 100,000 wanaoingia kujifungua, halafu tunataka kusema it is an achievement. It is not! Where is the woman? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaalam mmoja aliwahi kusema you need a sense of history to know how to handle the future. Kama historia tuliyoibeba katika maisha yetu haijaweza kutuelekeza namna gani future yetu inaweza kwenda, ni dhahiri kabisa kwamba kwa sababu leo niliamua ku-centre hapo niwaeleze ya kwamba akina mama wamelia kwa muda mrefu, wamelia katika labor rooms wakati wakijifungua, wamelia kule jikoni ambako wanapika na kuni mbichi, moshi unawaumiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wamelia sana wanaposafiri kilometa nyingi kwenda kutafuta maji, wanawaacha watoto wao wadogo nyumbani, wanarudi wanakuta wameunguzana moto wakati wakijaribu kupika uji kwa sababu mama amechukua muda mrefu kwenda kutafuta maji; akina mama wamelia sana wanapolima mazao yao halafu yanakosa masoko; yakipata masoko yanapata masoko ya ajabu ajabu, wanakopwa, wanaibiwa na wachuuzi huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wamelia sana vijana wao walipomaliza shule wakakosa ajira ya uhakika, wakarudi mitaani wakawa vibaka, wamechomwa moto kwa sababu Serikali haijaandaa mpango maalum wa kuwasaidia vijana. Imewaacha akina mama wakilia na kulia. Akina mama wamelia sana wanaume zao walipoondoka vijijini wakawaacha peke yao na watoto, wakaenda mjini kuhangaika kutafuta ajira kwa sababu kilimo hakilipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnasema 80% ya Watanzania ni wakulima, lakini mmeshindwa kabisa kulitazama suala hilo katika mkakati ambao ni mahsusi. Mimi sitaki kwenda huko, nataka kuwauliza, where is the woman? Bei ya bidhaa inapopanda; jana niliongea na mama yangu ananiambia mwanangu sasa sukari hapa kwetu ni shilingi 2,500, nikamwambia mama vumilia. Eeh, 2020 bei itashuka, hamna matatizo. Akina mama wamelia sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora wanisaidie kulia na akina mama hawa kwa sababu maisha yao hata wakienda kujifungua wanakokotwa na mikokoteni ya ng‟ombe, wanapelekwa katika zahanati ambazo hazina huduma za kutosha; wakijifungua watoto wao wanafariki kwa sababu ya upungufu wa huduma; nilimsikia Mheshimiwa Malapo asubuhi anasema zahanati haina maji. Imagine mwanamke anayekwenda labor ward halafu hakuna maji, halafu utamwambia kufariki mtoto wako ni bahati mbaya. Bahati mbaya kwao tu, akina mama tu au na kwa wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kwenye janga kubwa la madawa ya kulevya, our youths are frustrated. We have a lot of miserable children around the streets na hili lote linatokea kwa sababu mipango ya Serikali haijamtazama mwanamke kama mwanamke. Nataka kuuliza tena katika bajeti zenu na katika mipango yenu, where is the woman?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaalam mmoja kutoka Singapore aliwahi pia kusema naomba nirejee, when women thrive, all the society benefits and succeeding generation are given a better start in life. You guys have gone through the same process. Ninyi wote mko na akina mama zenu, mlizaliwa.
Sasa naomba ukiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ukiwa Waziri wa TAMISEMI, Afya na kadhalika usifikiri ya kwamba hakuna mama yako, shangazi yako, dada yako kijijini ukafikiri mipango hii tu inaweza kwenda bila kumtazama mwanamke katika jicho lenye uhakika, halafu ukadhani unakwenda kufanikiwa. When women thrive all the society benefits and succeeding generation are given a better start in life. What are we doing to give our succeeding generation a better start in life? Where is the woman? Where is the woman katika haya tunayoyafanya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakosea sana kama Taifa kuwaacha nyuma wanawake. Viwanda vidogo vidogo ni suala ambalo kwa kweli mnapokwenda kwenye mkakati wa viwanda lingekuwa limewatazama wanawake, ndiyo watu wenye commitment, ndiyo watu ambao wangezalisha malighafi ambazo zingesaidia viwanda vikubwa; lakini mmeyaweka in general. Kwa hiyo, naomba Mawaziri wanaohusika kwenye hili, tukienda kwenye hitimisho mnisaidie. Naomba mjibu hili swali, kwa sababu nobody can ever stay here and say he never recognize a woman in his life or in her life.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuambieni kwamba suala la umeme wa REA, mlipoona ni kazi nyepesi sana kufikiri ya kwamba ni mradi ambao mnatakiwa kubeza baada ya zile fedha za MCC kukatwa, mkadhani ni sawa sawa; akina mama wanapika gizani, akina mama wanaungua na mkaa na moshi. Hilo ndiyo jambo ambalo mngetakiwa kuliweka mbele ili hatimaye mwanamke apate ahueni. Aki-smile, you guys all smile. Make a woman smile. There is no life without a woman in this world man. Tukubaliane hivyo. Where is the woman? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani sana neno langu liwe sheria halafu niwalazimishe kufanya ninayotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa sababu naona muda wangu umekwisha, lakini naomba Waheshimiwa Mawaziri wanijibu, where is the woman in your plans?

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia jioni ya leo katika Wizara ya Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano.
Kabla sijaenda mbele nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa ya kuwepo ndani ya jengo hili, ninamshukuru amejibu ndoto zangu, ingawa ninachokiona haki ya Mungu ninastaajabu. Sikuwahi kufikiri kile chombo kinachoitwa Serikali ambacho tuliamini ni supreme haya ndiyo kinayoyafanya na kwa kweli ninasikitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea nimpongeze na nimtaje kwa heshima kabisa kiongozi wangu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, kamanda, kuwa mpinzani kwa miaka zaidi ya 20 siyo mchezo. Kazi uliyoifanya tumeiona, leo Bunge hili lina watu mahiri sana ndani yake ambao wataisaidia sana Serikali hii na si Bunge hili tu hata Bunge lililopita ndiyo kati ya Mabunge ambayo yaliwaamsha Watanzania wakajua ni nini kinachoendelea kwenye nchi yao na hatimae tuko hapa tulipo na tunafanya tunachokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye suala la daraja la Kigamboni. Nilimsikia Mheshimiwa Tizeba akichangia akisema, eti kwenye bajeti ya Wizara wameweka kivuko kingine cha Kigamboni; sawa sawa kabisa na mkiweke kwa sababu lile daraja mmetengeneza photo point, watu wakapige picha, siyo kwamba mmetengeneza liwasaidie chochote watu wa Kigamboni. Tulikuwa tunahangaika na vivuko vibovu…
…habari ndiyo hiyo, tulieni sasa mpate habari zenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunahangaika na vile vivuko vibovu despite the fact kwamba viko tu kilometa sifuri kutoka Ikulu, lakini huduma tuliyokuwa tunapata pale ni mbovu kabisa na leo Serikali ikaja ikatuahidi ya kwamba tunajenga daraja halafu maisha yetu yatabadilika, hayajabadilika chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lile daraja linaendelea kuchajiwa, Watanzania wa Kigamboni wanalipia lile daraja, tena eti mnasema mnaweza kumtenganisha Mtanzania wa Kigamboni na baiskeli na pikipiki na bajaji na hiace na gari la mzigo. Hivi mmemtenganishaje huyo Mtanzania wa Kigamboni? Mmempa ahueni gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za kivuko ndizo hizo hizo zilizohamishiwa kwenye gharama za daraja la Kigamboni, Mmempa ahueni gani mama ntilie? Mmempa ahueni gani yule Mtanzania anayesubiri kununua kifaa cha ujenzi akafanyie shughuli zake za ujenzi? Mmempa ahueni gani ikiwa lile guta tu ambalo linachukua bidhaa Buguruni na Kariakoo kupeleka Kigamboni linachajiwa gharama ile ile sawa na iliyokuwa inachajiwa kwenye gharama za kivuko? Hakuna mabadiliko, hakuna ahueni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kivuko mlituambia mnatuchaji kwa sababu kuna gharama za uendeshaji, well and good. Mmeleta daraja tunachajiwa gharama zile zile, eti mnasema anayekwenda kwa mguu tu ndiye amepata ahueni, amepata ahueni gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi niko Dar es Salaam nimekwenda mjini kwa shughuli za kikazi nikapigiwa simu nyumbani, mtoto anaumwa. Nimekwenda asubuhi nimelipa shilingi 2,000, nikarudi Kigamboni kumchukua mtoto nikalipa shilingi 2,000, nikarudi hospitali nikalipa shilingi 2,000, baada ya mtoto kutibiwa nikarudi nyumbani nikalipa shilingi 2,000, ni lazima nirudi kumalizia lile jukumu langu mjini nikalipa shilingi 2,000, jioni nilirejea nyumbani nimelipa shilingi 2,000, umenisaidia nini? And that not only me, Watanzania wengi wa Kigamboni wanapitia katika hatua hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifikirie upya kuhusu habari ya tozo za daraja la Kigamboni; mmetumia pesa za Watanzania, lazima ziwarejee.
Lazima pesa za Watanzaia zilizotumika kujenga daraja la Kigamboni, mmejenga Malagarasi, mmejenga la Mkapa, mbona lile hamku-charge? Hawa Watanzania wa Kigamboni na wao wanalipa road licence kama ninyi. Zile gharama za barabara tunazokatwa kwenye lita moja ya mafuta na wao wanalipa, mbona mnawa-double charge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukubaliane ya kwamba mmewaonea sana watu wa Kigamboni, mmewanyanyasa sana, mmewanyonya mno kwa tukio hilo la kuamua kuwa-charge kwenye lile daraja, lakini tukubaliane pia kwamba, hamjawatendea haki hata kidogo. Utabaki kuwa msimamo wangu na Mheshimiwa Waziri naomba ulichukue hilo ulifanyie kazi utupe majibu, hutaki tutakuachia lile daraja sasa upigie picha tuendelee kupita kwenye Kivuko kwa sababu tunachajiwa kitu kile kile, adha yetu ni ile ile, lakini shukrani kutuongezea kingine basi, ili walau tuendelee kuteseka kwa sababu, sioni kama umekuja na mkakati wa maana sana juu ya kusaidia hatma ya Kigamboni na maendeleo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lile eneo la Kigamboni ukishaondoka tu pale darajani, pana njia nyembamba kama mrija wa biki. Kwa hiyo, mlipanda pale juu mkafanya kazi ya kisiasa, mka-celebrate mkaondoka, hamkujua watu wakishaondoka mjini basi kule mliko-cross mkasema cross overs sawa, baada ya kuondoka darajani unarudi Kigamboni, barabara pale iko wapi? Usanifu wa kina mnaoita, sijui na upembuzi yakinifu ulishafanyika, wale matajiri wanaomiliki matenki ya mafuta maeneo yale barabara iliyopangwa kutoka daraja la Kigamboni ilipaswa ipite maeneo yale, leo sijui mmekaa meza gani, mmejadiliana namna gani, wananchi wangu wananiambia mmebadilisha msimamo, eti mmeamua kwenda kupitisha daraja tena eneo la makazi ya wananchi ambao hawakufanyiwa tathmini, mnaendelea kutunyonya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye suala lingine, suala la Serikali kukopa holela; Serikali yetu eti imepata kimbilio la kwenda kukopa fedha China na wao wamejua kabisa ya kwamba wana ajenda yao. Na mkigonga tu hodi wanasema yes, what do you want men? Mmepewa dola milioni 500 kwa ajili ya fedha za maendeleo…
MHE. LUCY S. MAGERELI: ...hizo pesa zikapotea. zikayeyuka.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakandarasi wanaofanya miradi ya maendeleo hapa Tanzania, wakandarasi wa Kichina, wamedai fedha zao mlishakula! Mkatumia mwanya mwingine kwa sababu mnajua kukopa kiholela mmerudi Uchina, mmeomba dola milioni 500 zingine. Mlikataa msaada wa Marekani wa MCC mkidai ya kwamba eti hamtaki pesa zenye masharti! Mchina alipowapa dola milioni 500 akawaambia sharti la kwanza lazima wakandarasi wa Kichina wote walipwe, ambao wanaidai Tanzania siyo chini ya dola milioni 365. Mmekataa masharti yapi na mmepokea yapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tukubaliane kabisa ya kwamba, kwenye hili lazima muwe waangalifu kwa sababu kwanza mnakopa fedha nyingi sana kutoka source moja! Hatari hata kwa ustawi wa Taifa, hatari hata kwa usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie suala la mizigo bandarini. Naomba nieleze kwa masikitiko kabisa ya kwamba bandari ya Dar es Salaam ina hali mbaya na inekoelekea sijui inakwenda kufa sina hakika, kwa sababu kwa mwezi wa kwanza na wa pili tu kwa takwimu, naomba nirejee, mizigo iliyokuwa inapita kwenye bandari ya Dar es Salaam kutoka Zambia imepungua kwa 42%, container kwa 28%, magari kwa 55%. Mizigo iliyokuwa inakwenda Congo imepungua kwa 9%, container 31%, magari 50%. Mizigo iliyokuwa inakwenda Burundi imepungua kwa 27%, mizigo iliyokuwa inakwenda Malawi imepungua kwa 35.6%, container kwa 11%, lakini mizigo ya Uganda imepungua kwa 77%. Nchi nyingine zikiwa na bandari ndiyo zinazojivunia kwa sababu, ni moja ya mlango wa uchumi... Imeisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa ya kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Nje. Kwa utangulizi tu, nianze kwa kuonesha masikitiko yangu juu ya ukandamizwaji wa demokrasia unaofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili Bunge sasa limegeuka kuwa mwiba mkali sana kwa ustawi wa demokrasia ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono jitihada zote zilizofanyika siku ya jana kuhakikisha kwamba tunaleta attention ya kuwasaidia vijana wetu ambao hawakutendewa sawa. Whether mliikubali au mliikataa lakini ulimwengu unajua ya kwamba hapo mmekosea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Msigwa umefanya kazi yako vizuri, hongera sana. Naomba pia kuunga mkono hotuba ya Kamati ya Mambo ya Nje, mmefanya kazi nzuri, mmetendea haki mlichokiona na huo ndiyo ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ku-declare kwamba ni mjumbe wa Kamati hii na katika kutekeleza majukumu yetu ya Kamati, nieleze tu masikitiko yangu kwamba hii ndiyo Wizara ambayo tulikuta hata cha kuzungumzia hakipo, kila unakogusa tabu, shida, karaha, fadhaha. Ukizungumzia shughuli za utendaji wa watendaji katika Wizara ya Mambo ya Nje yaliyoko kule fadhaha, ukitazama Balozi zetu zilizoko nchi za nje fadhaha, bajeti ya maendeleo waliyotengewa hawakupata hata senti moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika kwa kweli kuona hotuba hii ambayo nimeisoma mwanzo mwisho, sijajua Waziri anaogopa, ana hofu au ana mashaka, lakini nilitarajia aje na hotuba ambayo ni ya kitaalam, ina mikakati na ina mipango lakini Mheshimiwa Waziri amekuja na hotuba ya kisiasa. Nikajiuliza yale tuliyoyaona wakati wa Kamati, japo sawa Waziri mpya kwa this time, nikajua atayaona na kwenye hotuba yake ndiko atakakokuja na yale ambayo aliyaona ni upungufu na ataonesha mikakati yake na way forward lakini Mheshimiwa Waziri ameandika siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye hotuba yake ukurasa wa 111, amesema malengo ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017, nimeyasoma yote ni siasa. Nisome mawili ya mwanzo tu, la kwanza kutangaza nchi yetu kama moja ya nchi duniani zenye mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa, kwa kufanyaje?
Lla pili, anasema kuongeza uwakilishi wetu nchi za nje kwa kufungua Balozi mpya ofisi za Kikonseli na kuimarisha rasilimali watu na fedha wakati haya ndiyo ambayo kwenye Kamati tumezunguka tukiyatazama, hizo Balozi tulizonazo tu ziko hohehahe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia Mheshimiwa Mbunge, mama wa CUF anasema alikwenda Msumbiji akakuta katika Ofisi ya Balozi mama ntilie anaingia anauza chai, hakuna hadhi. Mimi iko Balozi tulifika tukakutana na mende, panya na popo. Sasa akituambia tu kwa maneno mepesi kama alivyosema katika lengo lake la pili kwamba anataka kufungua Ofisi za Balozi wakati viwanja tulivyonunua havijajengwa, viwanja vilivyotolewa havijajengwa, nyumba tulizopewa kwa ajili ya Ubalozi ziko hoi, ndiyo hizo zenye popo na mende, sasa anafunguaje Balozi nyingine mpya wakati zilizopo hii ndiyo hali yake? Basi fine, tulitegemea aseme at least kwa details kwamba tutafanya moja, mbili, tatu, tutakarabati lakini tutaongeza na hili yaani tulitaka hata kuona nyingi ngapi? Ndiyo maana nasema hii ni siasa kwamba tutafungua Balozi mpya, ngapi, wapi na kwa gharama ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni huduma za kibalozi. Watendaji wetu katika Balozi zetu mbalimbali wana hali mbaya, huduma ni shida lakini hata vipindi vyao vya kuhudumia vinapokwisha fedha ya kuwarejesha nyumbani ni tatizo. Badala yake, kama alivyosema Mheshimiwa Msigwa, uteuzi wa nafasi za Balozi katika nyakati fulani zimeonekana ni adhabu kwa wale watu ambao wanaonekana ni threat kwa wanasiasa fulani. Kilicho kibaya ni kwamba unapigwa jina Ubalozi halafu unaachwa hapo. Kwa hiyo, pale Foreign Affairs kuna watu wenye titles za Ubalozi wengi tu, wakiona unakerakera kwa kuweko hapa basi wanakutafutia mahali wanakwenda kukuficha pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakaporejea ningetamani haya ninayoyazungumzia atuoneshe kimkakati hasa kwamba anakwenda kuchukua hatua gani na atupe na time frame. Kwa sababu hata suala la Sera ya Mambo ya Nje, hii ambayo imetumikiwa kwa miaka kadhaa sasa ya Economic Diplomacy, hakuna tulicho-achieve. Kwa sababu kingekuwepo angekuja nacho akatuonesha kwamba kwa kipindi kilichopita tumefanya yafuatayo lakini hotuba yake imeongea siasa mwanzo mwisho na hakuna ambacho kiukweli amemudu kutupatia kama takwimu za kuonyesha achievement na if so, what is next? Je, tunakuja na sera nyingine au bado tunaendelea kutumikia hiyohiyo iliyoshindwa? Mchangiaji mmoja amesema tumeleta wawekezaji wa kutosha. Sawa, walipotosha wakafanya nini? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utangazaji wa vivutio na fursa za uwekezaji Tanzania, kama alivyosema Mheshimiwa Mwanjelwa, natamani sana labda tungeweka sasa goals na kila Afisa wa Balozi aliyeko Ubalozini ambaye ana wajibu wa kutekeleza haya mwisho wa bajeti ya mwaka mmoja atuambie ame-achieve nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hawauwezi kumdai ame-achieve nini kwa sababu hawawa-finance, hawawa-facilitate wale watu, kwa hiyo hawa-perform. Wamekaa kule wanaendelea ku-enjoy diplomatic securities lakini kiukweli najua hawawezi kukubali ku-set goals na kuanza kufanya assessment ya performance kwa sababu hawajawa-facilitate maafisa wetu walioko maeneo ya Balozi ili waweze kutekeleza wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niiombe Serikali itusaidie katika Wizara ya Mambo ya Nje, bajeti wanayopewa haikidhi haja hasa kwenye miradi ya maendeleo. Ile ndiyo sura ya Tanzania katika maeneo ambayo tuna uwakilishi lakini kama kweli tuna Balozi ambazo mapaa yanavuja na umekaa sitting room mende anapita, kiukweli hata kama tungetaka wafanye nini isingewezekana kwa sura ile. Mwaka jana wametengewa bajeti ya shilingi bilioni nane lakini hawakupata hata senti moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Diplomasia. Kama kweli majukumu tuliyokipatia Chuo cha Diplomasia ndiyo tunayotaka kitekeleze, basi Serikali inatakiwa kuja na kauli ituambie kwamba hicho chuo kweli ni Chuo cha Diplomasia au wameshabadilisha ajenda. Kile chuo kwa miaka mitatu mfululizo hawajapata senti moja ya pesa za maendeleo halafu tunasema wawafundishe Mabalozi wetu, wake wa Marais na kadhalika, hiyo haiwezekani unless tuwe na mkakati mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi leo nichangie katika hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na mimi nitajielekeza eneo moja mahsusi kabisa la ukuaji wa uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ukurasa wa 10, kuna quotation pale alitoa iko kwa lugha ya Kiingereza lakini ilitolewa pia tafsiri isiyo rasmi ambayo na mimi ningependa pia niirejee, nayo inasema hivi; “Ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi unapotokea kwenye sekta ambazo watu maskini wanafanya kazi kama vile kilimo. Unatokea katika maeneo ambayo watu maskini wanaishi, kwa mfano, maeneo ambayo hayajaendelea na yasiyo na rasilimali. Unatumia nyenzo za uzalishaji ambazo watu maskini wanazo, kwa mfano, nguvu kazi isiyo ya kitaalamu na unapunguza bei za bidhaa ambazo watu maskini wanatumia kwa mfano chakula, mafuta na nguo.” Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye kati ya maeneo aliyoyazungumzia kwamba yamefanya vizuri sana ni eneo hili la ukuaji wa uchumi. Maoni yangu mimi binafsi ni kwamba ukuaji wa uchumi hauwezi kuja kama katika uchumi wa leo hatuwezi kuishirikisha sekta binafsi. Sekta binafsi imetengwa kabisa na kwa bahati mbaya kuna baadhi ya kauli ambazo
zimekuwa zikitolewa na Kiongozi Mkuu wa nchi ambazo kwa kweli ukizitafakari kwa undani unaona kabisa kwamba kuna a missing link somewhere ambayo inatupelekea sisi kwenda kudumaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuombe Mheshimiwa Rais, lakini na Serikali kwa ujumla kwamba ile kampeni yake aliyoianzisha ya malaika waishi kama mashetani, sasa umefika wakati muafaka kwamba kauli hiyo ifutwe kwa sababu ugomvi huo wa kuwataka wale malaika
sasa warudi kuishi kama mashetani umegeuka kiama kwa wale wenyewe mnaowaita mashetani kwa maana ya Watanzania wa hali ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inaposhindikana sekta binafsi au wawekezaji walioko ndani ya nchi hii kuendesha na kukuza mitaji yao lakini kutoa michango yao katika uchumi wa nchi, mwisho wa siku anayeathirika siyo yule ambaye ni mwenye kipato hicho cha juu ambaye kwa reference ya Mheshimiwa Rais ni malaika lakini anayeathirika ni yule ambaye anaitwa shetani. Sasa na mimi kwa sababu niko kwenye kundi hilo la mashetani, naomba nilete ujumbe wangu maalum nikisema tunaomba waacheni malaika waendelee kuwa malaika, waacheni waendelee kufanya zile karamu zao kwa sababu zile karamu, yale makombo yanayodondoka kwenye zile meza za malaika kwetu sisi ndiyo riziki, ndiyo neema. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotaka malaika wageuke mashetani, shida kubwa iko kwa Watanzania wa chini. Sasa nastaajabu tunapoona hotuba zinazosema kwamba kuna ukuaji wa uchumi. Tuwaache malaika wanaoshughulika na sekta ya ujenzi waendelee lakini tuwasaidie waweze kuendelea kwa ustawi kwa sababu wanapofanya kazi zao za ujenzi sisi mashetani tunaokotaokota makombo kwa kupata kazi za ajira za ujenzi lakini wakiagiza bidhaa in bulk kwa maana ya bidhaa nyingi basi na sisi tunapata ahueni kwa sababu zinapokuwa nyingi sokoni na sisi tunapata kuzipata katika bei ya ambayo ni ya ahueni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitolee mfano wa mzalishaji na mwekezaji mmoja Bakhressa ambaye katika kibano ambacho amekipata kwa muda mfupi wa Serikali ya Awamu ya Tano, amebadilisha kabisa mkakati wake wa uwekezaji na kwa kiasi kikubwa mtaji wake sasa anauhamishia maeneo mengine ya Afrika kwa maana ya nchi nyingine za Afrika. Hatua hiyo tu inaleta ujumbe straight kwamba kuna ajira ambazo zimeathirika. Kuna hao mashetani sasa ambao kwa yule malaika Bakhressa kuadhibiwa na kupangiwa kodi ambazo haziko realistic na masharti mengine ambayo hayatekelezeki kibiashara, amepunguza wafanyakazi lakini zingatieni ndiye anayezalisha mpaka maziwa na maji ya shilingi 500 na sisi mashetani tunapata ahueni ya kunywa maji ya chupa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo kama la Breweries, tuache malaika hawa wa Breweries wazalishe kwa sababu wakizalisha sisi mashetani wa kule mashambani, mazao yetu ya ngano na shairi yanapata soko la uhakika. Pia wale wanaojishughulisha na shughuli za usafirishaji na sisi vijana wetu wako kwenye kuwa madereva wa hayo magari lakini wako katika kuwa utingo wa hayo magari na kutoka hapo na sisi tunapa riziki na vijana wetu wanakwenda shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo kwa mfano la bandari. Wakati bandari ina-operate katika kiwango chake ilitusaidia sana sisi tunaoitwa mashetani kupata kiasi kikubwa cha ajira na vijana wetu kutumika katika eneo la bandari ambapo kwa sasa kutokana na kiwango cha uingizaji na utoaji wa mizigo kushuka, vijana wengi sana wamepoteza ajira bandarini. Vilevile yale magari yaliyokuwa yanaondoa mizigo bandarini na kupeleka mikoani na nchi za jirani napo palikuwa kuna kundi kubwa la Watanzania ambao walikuwa wanahudumia kama madereva, utingo lakini mama ntilie katika maeneo tofauti walikuwa wanapata riziki zao kutokana na eneo hilo. Naamini sasa nimeeleweka ninapojaribu kusema ya kwamba tuwaache malaika waendelee kuwa malaika kwa sababu sisi mashetani tunapotea kwenye karamu za meza zao, wanapodondosha
na sisi ndiyo tunaishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipata taarifa juzi kupitia vyombo vya habari kwamba Private Sector Foundation wanakuja Dodoma kwa ajili ya kuonana na Serikali, naamini taarifa hiyo mnayo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu, hao ndiyo watu ambao unatakiwa kuwapokea na mimi sijui niombe kama Mheshimiwa mwingine aliyesema, muache Waziri Mkuu atusikilize. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba hawa watu wa private sector wanapokuja Dodoma kuja kuonana na Serikali wapewe fursa, wapewe usikivu…
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimaanisha kumueleza Waziri Mkuu nilisikia kupitia vyombo vya habari kwamba The Private Sector Foundation wanakuja Dodoma kuja kuonana na Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba uwapokee hao watu na uwasikilize kwa sababu kama nilivyosema awali makombo ya kwenye meza za karamu zao kwetu sisi ni neema. Hebu acheni private sector sasa ishamiri, itoe ajira kwa Watanzania, izalishe bidhaa nyingi ili bidhaa zishuke bei lakini muwape na access ya ku-import ili bidhaa ziwe nyingi kwenye masoko na kwenye mzunguko ili na sisi tunaokuwa referred kama mashetani, naupenda sana huo msemo sana kwa sababu ni fahari kweli kuitwa na Rais wako kwamba wale wote ambao tuna kipato cha chini basi sisi ni mashetani na sisi tupate kuneemeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nataka niende kwenye suala moja la msingi ambalo nimeliona na niombe attention. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, kuna suala limejitokeza ambalo naendelea kulistaajabiwa. Jambo hili ni kwamba, Mheshimiwa Rais ametoa kibali kwa mwekezaji mmoja wa hapa Tanzania, Dangote, achukue mgodi wetu wa makaa ya mawe, achimbe mwenyewe, asafirishe mwenyewe, atumie mwenyewe, huu ni utaratibu gani? Huu ni wizi wa namna gani wa wazi na hadharani? Sasa leo tunahangaika na mchanga wa ACACIA bandarini nimeona mpaka leo Tume imeundwa wakati kuna mahali tumemfungia fisi buchani halafu tutamuuliza umekula kilo ngapi? Hivi uwezekano huo kweli upo? Mheshmiwa Naibu Spika, kati ya mambo sasa ambayo Bunge hili linatakiwa liisimamie Serikali na kulitazama upya ni hili suala la Mgodi wa Makaa ya Mawe. Haya ni kati ya makosa makubwa kabisa ambayo tumeyafanya hata kama lengo ni kumbembeleza mwekezaji basi hapa tumekwenda kinyume kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo lingine la wawekezaji na mitaji yao. Kauli za Mheshimiwa Rais zimeendelea kuwa tata kila mara na kusababisha wawekezaji wengi kupata mashaka kuhusu mitaji yao wanayoiwekeza ndani ya nchi hii lakini na wanaotaka kuja sasa na wao wanaongeza mashaka ya kwamba wawekeze ama la.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru ingawa naona muda umekuwa mfupi, ahsante.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, na kushukuru sana kwa kunipa fursa nichangie na mimi Bajeti ya hii Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na nianze kwa kueleza na kukubaliana kwamba ninaunga mkono hoja zote katika ripoti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye hoja ya suala la Daraja la Kigamboni. Hili mimi nitaendelea tu kulisemea tu sana kwa sababu imekuwa ni changamoto kubwa. Tozo katika Daraja la Kigamboni zimekuwa kero kuliko msaada, gharama zinazotozwa pale kwenye lile daraja ni kubwa kuliko hali halisi ya wananchi wa Kigamboni. Tulitarajia kama ambavyo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati anazindua lile daraja alivyosema, kwamba daraja lile lifungue fursa za kuwasaidia Watanzania, wananchi wakazi wa Kigamboni kubadili mfumo wa maisha yao lakini pia kujipatia fursa za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wakazi wa Kigamboni bado ni aina ya wananchi ambao wanawaza watoto wao watakula nini, watapata wapi ada ya shule, lakini pia wanawaza hata namna ya kugharamia mavazi ukilinganisha na hali halisi ya uchumi ilivyo leo na ukiangalia hali halisi ya uchumi wa Tanzania, mimi nafikiri bado hatujafikia mahali pa kulipia tozo za huduma muhimu na nyeti kama barabara na madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili naomba kabisa Mheshimiwa Waziri litazamwe upya, ikiwezekana kama iko lazima sana kwa sababu daraja hili limejengwa kwa ubia wa NSSF na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania basi lile eneo la NSSF lifanyiwe utaratibu fedha zile ambazo zilitolewa kama mchango wa NSSF kwenye ujenzi wa lile daraja zilipwe, kwa sababu daraja hili kulingana na jinsi ambavyo nimesoma kwenye hotuba yako itakuwa ni connection ya interchange ile barabara ya haraka ya Chalinze, sasa kama ndivyo je, ni eneo lile tu la kuvuka pale kwenye daraja litakuwa linalipiwa ama na barabara zote za interchange zitakazo unganisha na daraja la Kigamboni zitakuwa zitalipiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama zote zitalipiwa bado tufahamu kabisa kwamba ni changamoto kubwa kwa Watanzania wa sasa hivi na hali ya uchumi ilivyo jamani hatujafika huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie baadhi ya vipaumbele ambavyo vimeoneshwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu eneo la Kigamboni nikianzia na barabara ya Kongowe – Mjimwema – Kivukoni ambayo kulingana na taarifa zilizopo katika kitabu cha Waziri ni ya kilomita 25 na imepangiwa shilingi bilioni 1.290. Mheshimiwa Waziri niombe sana kwamba barabara hii ni muhimu sana kwetu na tangu mwaka jana ilikuwa katika bajeti yako, lakini kwa bahati mbaya nadhani ilipata fedha kidogo mno ambapo utaratibu wa upanuzi ulianzia tu eneo la pale kwa Mwingira mpaka kufika Mji Mwema na imeishia hapo.

Kwa hiyo, nikuombe sana katika bajeti yako ya utusaidie kutengwa fedha za upanuzi wa hiyo barabara kwa sababu ndicho kiunganishi kikubwa cha kutoka eneo la Kivukoni mpaka kwenda kuunganisha na Kongowe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimeona Mheshimiwa Waziri amelitaja daraja la Mzinga, nikuombe sana lile daraja msimu wa mvua tunapata matatizo makubwa sana, na mwaka juzi daraja lile lilikatika kabisa tuliishi kwa msaada wa ujenzi uliofanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo, nimeona umetenga fedha pia kwa ajili ya daraja hilo, tunaomba pesa hizo zipatikane na hilo daraja lijengwe ili kuweze kuwa na connection baina ya wakazi wa Kigamboni na eneo la Temeke; lakini ukizingatia na hiyo express way ambayo nimeona mnaijenga, nimeona inakwenda mpaka eneo la Mbagala ambayo na amini ile barabara ya Kongowe itakuwa ni feeder road kwenda kwenye hiyo interchange ambayo umeizumzumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye barabara ya Tungi – Kisiwani – Kibada. Mheshimiwa Waziri wakati wa hotuba yako wakati wa uzinduzi wa daraja la Kigamboni kwa maneno yako mwenyewe kabisa ulisema umejipanga na utakwenda kumalizia lile eneo la kilomita 1.5 lililobaki baada ya daraja kwenda mpaka pale kwa Msomali, na ulisema fedha zipo na ujenzi ungekamilika mapema iwezekanavyo. Hata hivyo lile eneo limebaki na sura kama alivyosema Mheshimiwa Shabiby jana, kwamba umevaa koti zuri safi na tai lakini chini umevaa kaptula na makobazi.

Mheshimia Naibu Spika, ukubwa wa barabara inayotoka darajani ni kubwa mno ya njia tatu pande zote mbili lakini inakwenda kuingia katika barabara ndogo halafu mbaya na chafu sana, tena wakati huu wa mvua ukifika eneo lile hata kupita na gari ndogo ni shughuli kubwa na pevu. Kwa hiyo tunaomba kipande hicho cha kilometa 1.5 kimaliziwe kama ambavyo uliahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hiyo hiyo ya Mheshimiwa Waziri ya siku ya uzinduzi wa daraja la Kigamboni alisema lile eneo la darajani, mpaka pale kwa Msomali kwa maana ya kuunganisha barabara ya Kivukoni kupitia Tungi, Vijibweni mpaka Kibada usanifu umeshakamilika na barabara ile ilipaswa kuanza, ujenzi ungeanza Mei 2016 lakini mpaka ninavyozungumza leo hakuna kinachoendelea eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sielewi kilichotokea yawezekana ni ufinyu wa bajeti lakini tunaomba sasa msimu huu kwa maana bajeti hii inayokuja mtusaidie eneo lile liweze kukamilika na barabara ile ikamilike kwa sababu ndio barabaara ambayo ina wasaidia wananchi wengi wa kazi ya maeneo ya Kisarawe II, kata za Kibada, Mji Mwema kupita kwa ajili ya kuja kukutana na eneo la daraja la kuvuka kuja mjini. Barabara ile ya sehemu ile ni mbaya sana na kisehemu cha lami kilichojengwa kuanzia Tungi mpaka Vijibweni karibu kuelekea hospitali eneo limeshaharibika kabisa lina hali mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia nizungumzie au ni muulize Mheshimiwa Waziri atusaidie. Katika bajeti iliyopita ulitupangia fedha kwa ajili ya barabara ya Kibada - Mwasonga kuelekea Tundwi Songani. Najua unaufahamu umuhimu wa barabara hii, ndiyo barabara ambayo magari makubwa sana ya yanayotoka Kimbiji kuelekea Kiwanda cha Saruji cha Nyati yanakopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile kwa kweli imepata uharibifu mkubwa sana kutokana na matumizi makubwa ya yale maroli na kwa hiyo wananchi wa kawaida na usafirishaji wa kawaida unashindwa kuendelea kabisa katika eneo lile kwa sababu mara nyingi yale magari yanapoharibika au yanapokwama katika barabara ile wakazi wanashindwa kuendelea na maisha yao ya kawaida. Kwa hiyo, sasa sielewi imekuaje kwamba barabara hii ya Kibada – Mwasonga – Tundwi kuelekea Kimbiji haijatengewa fedha msimu huu wala haujaizungumzia wakati 2016/2017 ilikuwepo kwenye bajeti yako Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia nizungumzia barabara ambayo nimeona umeizungumzia katika kitabu chako ukurasa wa 35, barabara ya bandari ambyayo ni ya kilomita 1.2 lakini barabara ya Mivinjeni kilometa moja na Dock Yard kilometa 0.7. Barabara ile Mheshimiwa Waziri nikusihi sana kwamba tungependa itengewe fedha lakini itanuliwe kiasi cha kutosha, kwa sababu msongamano wa yale maroli pale bandarini unatupashida shida sana.

Mheshimiwa Naibu Soika, kweli unafiri ni haraka sana kutoka Kigamboni kwa kuvukwa kwa daraja na kuondoka haraka kufika mjini lakini ukishaondoka darajani tu unakutana na hii barabara ya bandari imejaa foleni ndefu, unakutana na barabara ya Mandela imejaa foleni ndefu, kwa hiyo, shughuli ile inabaki kuendelea kuwa shughuli vilevile. Hata kama kungekuwa na nafuu barabara ya bandari bado utaratibu wa kuegesha magari yale makubwa ni mgumu mno na barabara hii inashindwa kupitika. Kwa hiyo, tunaomba mtusaidie utaratibu wa kutengeneza parking maalum ya yale magari ili barabara zibaki huru zitembee kwenda na kurudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana, nimeona umetenga bajeti yako pia ukurasa wa 214 umetenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa gati ya pale Kivukoni, Kigamboni. Eneo lile nalo ni shida kubwa sana, vivuko vile tunashukuru vinafanya kazi na vinatusaidia sana kwa sababu sisi kwa bahati mbaya tumejikuta na hilo janga la kujikuta barabara kwa maana ya daraja tunalipia na kivuko tunalipia, hewala kama ndivyo ilivyowapendeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikuombe basi mtusaidie sana Bajeti hii fedha za utanuzi wa gati pale zipatikane kwa sababu hata kama pantoni imefika imetia dock pale utaratibu wa utokaji wa magari unakuwa taratibu mno kwa sababu eneo ni finyu mno. Kwa hiyo, pantoni kupakia ruti nyingine iende inachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa haya ya leo, ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's