Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Sixtus Raphael Mapunda

All Contributions

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchana wa leo. Awali ya yote nachukua fursa hii kuwashukuru sana wananchi wapenda amani wa Jimbo la Mbinga Mjini kwa heshima kubwa waliyonipatia, nami
nawahakikishia tu kwamba sitawaangusha, nitawawakilisha kama wanavyotarajia. (Makofi)
Pia nachukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kwa kutoa hotuba nzuri, iliyosheheni weledi, iliyoangalia kila sekta na kwa maoni makubwa na mapana kwa maslahi ya Taifa hili la
Tanzania. Nawaomba tu Watanzania wote tuendelee kumwombea ili azma yake ya kuleta maendeleo ndani ya nchi hii ifanikiwe. Kusema ni rahisi, kutenda ni vigumu. Watapita wengi watakejeli, watapita wengi watasema lugha ambazo wanadhani zinastahili ili kuipunguza
thamani hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mimi niseme tu kwamba Mheshimiwa Rais ametenda, amesema, ameelekeza na utekelezaji tumeuona.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme neno moja tu kwa kifupi. Tunapozungumzia habari ya amani, umoja, mshikamano na utulivu wakati wa chaguzi, naomba niwakumbushe jambo moja.
Watanzania tunaofanya active-politics tuko milioni tisa tunaotokana na vyama vya siasa. Milioni 50 ya Watanzania wote wanaobaki hawako kwenye active politics. Inapofika wakati wa uchaguzi, sisi milioni kumi tunajiona ndio wababe, tunaoweza kufanya kila kitu, tukawaacha
Watanzania wengine, tunachoma matairi barabarani. Askari wakituzuia sisi wanasiasa, tunasema aaah, mnahatarisha amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tofauti kati ya kuhatarisha amani na kusimamia amani. Alichokieleza Mheshimiwa Rais katika hotuba yake, uchaguzi ulikwenda vizuri, zile rabsha rabsha mlizokuwa mnaziona za vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa ni kuhakikisha kwamba nchi hii
inakuwa hamna amani. Nawashukuru sana Jeshi la ulinzi pamoja na Polisi kwa kazi kubwa waliyoifanya. Sisi tutaendelea kuwatia moyo, fanyeni kazi kusimamia amani ili maendeleo yapatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye sekta moja; sekta ya kilimo ukiondoa sekta nyingi ambazo Mheshimiwa Rais alizielezea katika hotuba yake. Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais anakiri kwamba asilimia 95 ya chakula tunachokipata hapa nchini kinatokana na Sekta ya Kilimo, lakini anakubali kwamba asilimia 30 ya mapato ya kigeni yanatokana na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niseme tu mambo machache kuhusu takwimu ya mwaka 2014, sekta gani ziliongoza kwenye kuleta pato la kigeni? Ukiondoa dhahabu ambayo ilileta shilingi bilioni 2,705, sekta zote zilizofuatia kwenye zile sekta tisa, zilikuwa
ni sekta zenye uhusiano na kilimo. Korosho ilileta shilingi bilioni 647, Pamba ilileta shilingi bilioni 558, Tumbaku ilileta shilingi bilioni 319, Kahawa ilileta shilingi bilioni 204, Mkonge ulileta shilingi bilioni 111, Chai ilileta shilingi bilioni 72 na Karafuu ilileta shilingi bilioni 50. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Ukiangalia zile top ten unakutana na sekta ya kilimo kwenye uchumi wa nchi wetu. Pamoja na mchango wa kilimo kwenye uchumi wa nchi yetu, bado wakulima wadogo wadogo wana changamoto nyingi sana ambazo
tunaiomba Serikali yetu itusaidie kwa haraka sana kuzitatua changamoto hizi. Changamoto ya kwanza ni ya pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru Serikali inatusaidia pembejeo kwenye kilimo cha mazao ya chakula, lakini ukifika kule kwangu Mbinga Mjini. Mbinga Mjini imegawanyika katika maeneo mawili. Kuna milimani ambako tunazalisha Kahawa na mabondeni tunalima mahindi,
lakini wote hawa ni Watanzania, wote hawa wana mchango kwenye uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa watu wa kule Mondeki, Miyangayanga, Luwaita, Utili kwenye milima kule, wale watu wanalima Kahawa, hawawezi kulima mahindi. Kutokuwapatia ruzuku ni kuwafanya wadumae na mwisho wa siku kilimo kitakuwa mzigo baada
ya kilimo kuwa msaada kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni ukosefu wa centers za kufanya utafiti ambazo tunaweza tukajua eneo hili mbegu gani inaweza ikafaa, eneo hili aina gani ya mbolea inaweza ikafaa, mwisho wa siku tuweze kuleta kilimo chenye tija. Tukiulizana hapa sasa hivi ni maeneo
gani, kuna hizi research centers ziko kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa eneo husika, jibu utakalolipata litakuwa bado viko kwenye mchakato au vimekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ukosefu wa wataalamu, hawa tunaowaita Mabwana Shamba na mabwana mifugo. Tuzunguke kule vijijini tuulize lini Bwana Shamba alikwenda kumsaidia mkulima aweze kupanda kwa wakati, aweze kufanya palizi yake kwa
wakati na kumpatia ile elimu ya kilimo bora. Utakuta kwenye sekta hii, sehemu ya wataalamu, Mabwana Shamba na Mabwana Mifugo hatujafanya vizuri sana. (Makofi)
Lingine ni kushuka kwa bei ya mazao. Mkulima analima kwa nguvu zake mwenyewe. Inapofika masuala ya bei, haitabiriki. Pembejeo ziko juu, gharama za uzalishaji ziko juu. Matatizo haya yote yanasababisha kilimo kidumae na malengo tunayotaka ya kuajiri asilimia 75 ya Watanzania wote kutoka vijijini kwenye Sekta ya Kilimo, Mfugo na Uvuvi itapata tatizo kubwa. Changamoto nyingine inayotokana na hili eneo la kilimo ni kodi na tozo mbalimbali zinazowaumiza wakulima. Ukienda kwenye zao la kahawa, kodi na ushuru unaotozwa kwa wakulima unawatesa sana. Unakuta kuna kodi inaitwa Tanzania Coffee Research Institute ambayo ni 0.75, halafu kuna kodi nyingine inaitwa Tanzania Coffee Development Fund ambayo mkulima anatozwa 0.10 kwa kila kilo.
Lingine, kuna leseni ya TCB. Leseni ya TCB kabla ya mwaka juzi ilikuwa ni dola 24, sasa hivi imefika kuwa dola 24,000. Hivi mkulima wa kawaida atawezaje kwenda sambamba na ongezeko hili la dola kwenye TCB? Hali inakuwa ngumu sana. Naiomba Serikali, ili kumwongezea Mheshimiwa Rais nguvu ya kuleta maendeleo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mapunda, muda umekwisha!
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Ahsante sana. Naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo. Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu kwa jinsi alivyoitoa hotuba yake kwa umahiri na ufundi mkubwa, iliyogusa kila sekta. Hakika hotuba hii ime-reflect katika maana ya utendaji, hotuba iliyotolewa na Mheshimiwa Rais siku analizindua Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri Mkuu imegusa mambo mengi ambayo kama hayo yote tutakwenda kuyafanyia kazi kama alivyoyawasilisha hapa, nina uhakika ndani ya miaka michache nchi yetu itakuwa katika kiwango cha hali ya juu sana cha maendeleo. Niwaombe Mawaziri wote, kadiri Waziri Mkuu alivyoeleza kwenye hizo sekta, tuziongezee nguvu ili maendeleo kwa Watanzania yapatikane kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya mambo yote mazuri ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyaeleza, kuna maeneo machache naomba nijikite ili kuiomba Serikali iongeze nguvu sana ili tuweze kuendelea kwa wakati.
Jambo la kwanza ameelezea nishati ya umeme. Umeme ni jambo muhimu sana kwenye maendeleo ya Taifa lolote lile. Tuko kwenye mfumo wa gesi na aina nyingine zote za umeme ambazo zimewekwa katika programu ya mwaka 2016/2017. Niwaombe sana mtusaidie na sisi watu wa Songea katika maana ya Mkoa wa Ruvuma kama mlivyoeleza kuweka mfumo mpya wa umeme wa gridi ya Taifa kilowatt 220 kutoka Makambako Songea na nina imani hautaishia Songea utafika Mbinga utakwenda mpaka Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la viwanda. Suala la viwanda ni zito na ni kubwa sana na ni moja kati ya sera ya Awamu hii ya Tano. Kama tutawekeza kwenye viwanda hasa vile viwanda ambavyo vilisinzia na vingine vilikufa au vingine vinafanya kazi chini ya kiwango, nina uhakika ajira itapatikana kwa vijana na maendeleo makubwa yatapatikana kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Mbinga tuna kiwanda cha kahawa. Niiombe Serikali ikitazame kile Kiwanda cha Kahawa Mbinga na kiende hatua ya pili sasa kuweka kiwanda kingine cha Instant Coffee ili kahawa ile ikishakobolewa siyo lazima tuipeleke Brazil, India au Ujerumani, tutengeneze pale pale kahawa na sasa tuwe na kahawa made from Mbinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliongelee ni suala la afya. Kati ya changamoto ambazo zinatukabili kule Mbinga ni Hospitali yetu ya Wilaya. Hospitali yetu ya Wilaya ilianzishwa kama kituo cha afya. Kwa bahati nzuri maendeleo ya Mji wa Mbinga yakapelekea kuwa na Wilaya ya Mbinga ambayo baadaye ikazaa Wilaya ya Nyasa. Hata hivyo, hizi wilaya zote mbili, Wilaya ya Mbinga na Nyasa zinategemea Hospitali ya Wilaya ya Mbinga, Hospitali ya Mbuyula ambayo kwa sasa inahudumia Halmashauri nne za Nyasa, Mbinga Vijijini, Mbinga Mjini na sehemu ya Halmashauri ya Songea Vijijini. Niombe sana Serikali iwekeze kwenye ile hospitali ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ninayoomba Serikali iongeze nguvu ni kwenye huduma ya maji safi na salama. Ule mji unakua kwa kasi sana lakini mpaka sasa hatuna mradi mkubwa wa maji wa kuweza kuwasaidia wananchi wa Mbinga wanaoongezeka siku mpaka siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza hotuba nzuri sana ya Waziri Mkuu, nimepata muda kidogo kuisoma hotuba ya Kambi ya Upinzani. Hii hotuba ya Waziri Mkuu ina page 82, imegusa kila maeneo, hii iliyowasilishwa na Mheshimiwa Freeman Mbowe ina vi-page kama tisa vile, font ni kubwa sana na double space, haiwezi hata kidogo ikajibu hoja ya page 82. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiondoa hayo, ameiwasilisha hoja hii na amepotosha watu hapa kana kwamba watu hawasomi au hawafikiri. Nimwombe Mheshimiwa Mbowe akasome mambo yafuatayo. Kwanza, akaisome vizuri Katiba aielewe, akishaielewa vizuri akasome Sheria ya Bajeti, halafu vile vile akasome na Appropriation Act ya mwaka 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongelea kutengeneza bajeti lazima uweke sheria itakayosimamia utekelezaji wa bajeti ile na sheria hiyo inaitwa Appropriation Act. Kwa muktadha wa shughuli yetu ya leo ile Appropriation Act ilikuwa ya mwaka 2015 ambayo ina section sita au kwa lugha nyingine ina vifungu sita. Katika vile vifungu sita kuna kifungu cha 6 kinasema mamlaka ya Serikali kubadilisha matumizi kadiri itakavyoona inafaa kwa maslahi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Mbowe alinukuu vipengele vya Katiba sasa mimi nimuambie Katiba ni sheria mama, inatafsiriwa kwenye sheria na ukitoka kwenye sheria ukafika kwenye bajeti utekelezaji wa bajeti unakwenda kwenye Appropriation Act. Sasa mimi nampeleka kwenye Appropriation Act ya mwaka 2015, kifungu cha sita (6) kinachosema, power of the Minister to reallocate certain appropriated moneys. Imeelezea kifungu cha kwanza (1) mpaka cha tano (5) ila kwa faida ya kikao hiki mimi nakisoma vizuri kifungu kile cha tano (5), kinasema hivi, nanukuu:-
“The Minister may, by certificate under this hand, reallocate any sums arising from savings in the Consolidated Fund to any of the purposes specified in the second, third and fourth columns respectively of the Schedule to this Act, and where this occurs, the provisions of section 3 and 4 shall take effect as if the total sum granted out of the Consolidated Fund and the amounts appropriated for the purpose specified in such certificate were raised by the amount or amounts specified in the certificate”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anachotuambia hapa ni nini? Anachotaka kutukoroga hapa ni nini?
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbowe aliongea kwa Kiingereza, mimi najua alikuwa na maana ya kupotosha watu wasielewe Kiingereza. Kwa Kiswahili kisichokuwa rasmi, Waziri ana mamlaka kwenye hii Sheria ya Bajeti tuliyoipitisha kwa maslahi ya nchi anaweza akaondoa kifungu kimoja under certificate kwa matumizi mengine yenye muktadha ule ule unaofanana kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuchukua pesa ambayo ilibaki kwenye matumizi from July, August, September, October ambapo Bunge halikuwepo tukaenda kununua madawati kwa mujibu wa sheria aliyetunga yeye mwenyewe na alikuwa amekaa pale, leo anajidai kasahau, huku kujisahaulisha kunatokana na nini? Niwaombeni, watu kama hawa tuwaangalie vizuri wenye ndimi mbilimbili, huku unauma huku unapulizia…
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Unafikiri sisi wote hapa ni matutusa? Humu hakuna zero, watu tunafikiri kwa kutumia vichwa, hatufikirii kwa kutumia matumbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba niungane na wale waliochangia jana kumpongeza Waziri kwa jinsi anavyofanya kazi zake vizuri na tukijua kwamba Wizara hii ni kubwa na ndiyo iliyobeba uchumi wa nchi yetu. Kwa jinsi anavyofanya kazi zake, nimpongeze na nitakuwa miongoni mwa wale watakaokuwa wanakesha Makanisani kumwombea awe na nguvu hizo ili matumaini kwa Watanzania walio maskini yapate kufikia katika kiwango kinachostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye kuchangia hoja hii kwenye mambo matatu. Jambo la kwanza ni suala la ruzuku ya pembejeo. Waziri ameeleza vizuri na amefafanua changamoto zilizojitokeza. Nimwombe atakapofika kufanya majumuisho aweke mambo yafuatayo ili angalau wakulima wapate faraja na wapate ahueni waweze kuiona kesho yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuweka ruzuku ya pembejeo lakini kimsingi ile ruzuku ukiitazama vizuri kuna maeneo haiwasaidii wakulima ambao wanatarajiwa. Ruzuku ile ya pembejeo kuna asilimia mkulima anapaswa kulipa ili apate ile seti ya mbolea ya kupandia, mbolea ya kukuzia, pamoja na mbegu, anatakiwa atoe hela wakati yeye hana hela. Ukiangalia kwenye tathmini nani ana sifa ya kupata ile ruzuku unajikuta yule ambaye anapelekewa hana uwezo hata wa kununua huo mfuko au nusu mfuko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara ifanye mambo yafuatayo:-
Kwanza ipeleke ile ruzuku kama mkopo mapema, ipeleke mbolea ya kupandia, ya kukuzia na ipeleke mbegu. Baada ya mavuno sasa wale wakulima ndiyo walipe ile gharama ya pembejeo. Tukifanya hivi hali itakuwa nzuri sana kwa wakulima wangu wa mahindi kule Lipilipili, Luangai, Masimeli, Ruvuma Chini, Mpepai, Mzopai na Kikolo. Ukiyafanya haya Mheshimiwa Waziri utawafanya watoke kwenye mstari wa umaskini waende juu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mbinga na hususan Jimbo la Mbinga Mjini limegawanyika katika maeneo mawili. Eneo la kwanza ni milimani la wakulima wa kahawa na eneo la pili ni bondeni ambao ni wakulima wa mahindi. Hawa wote ni Watanzania ambao wanahitaji Serikali kwa namna yoyote ile iwasaidie. Huo mfumo wa ruzuku ya pembejeo umeelekezwa kwenye mazao ya kilimo cha mahindi tu hawajaelekeza kwenye zao la kahawa. Wale ndugu zangu wa milimani hawakupenda kuzaliwa kwenye maeneo ambayo hayastawishi mahindi, ni Mwenyezi Mungu aliwaumba wakakaa kule milimani ambako ukipanda mahindi hayawezi yakastawi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali itazame hili kwa jicho la upekee kidogo, itoe ruzuku vile vile ya dawa na mbolea kwenye mazao ya biashara hususan kahawa. Tukifanya hivi, ndugu zangu wa kule Miyangayanga, Mateka, Mundeki, Luwaita, Kagugu, Sepukira, Utiri, wataweza kupata ahueni ya maisha yao na wataiona kesho yao katika hali nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye sehemu ya pili ambayo wenzangu waliongelea jana kuhusu tozo nyingi zinazowakumba wakulima wa kahawa na wakulima wa mazao mengine. Kuwa specific, niliongelee zao la kahawa. Mnunuzi wa kahawa huwa analipia leseni kwenye Bodi ya Kahawa, analipa Dola 1,024 lakini akitaka kwenda kununua kahawa aidha amekwenda Mbinga, Mbozi au Kagera, akifika kule atakutana tena na leseni nyingine ya ununuzi wa kahawa kwenye halmashauri husika. Hizi gharama ambazo unampelekea mnunuzi wa kahawa zikisambaa zinakwenda kumuumiza mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiondoa gharama hii, kuna makato mengine hata ukiyatazama unashindwa kuyaelewa. Kuna gharama ya kulipia Tanzania Coffee Research Institute – TACRI ambapo kwa kila mkulima aliyeuza kahawa kwa kilo moja ya kahawa unailipia 0.075 kwenda kwenye kitengo hiki cha research. Vile vile wanakatwa kuna kitu kinaitwa Tanzania Coffee Development Fund ambayo ni 0.10 wanalipa kwa kila kilo ya kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza haya makato yakishatokea na ikatokea labda sehemu fulani wakulima wamepata magonjwa ya mlipuko, sijawahi kuona sehemu yoyote pesa inatoka kwenye hii Mifuko kwenda kuwasaidia wakulima. Matokeo yake wakulima wanatafutiwa mfumo mwingine wa kulipwa, wanakuwa double charged! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, hebu aangalie huo Mfuko kwa ajili ya maboresho ya kilimo cha kahawa unafanya kazi gani? TCDF, ile 0.10 anayokatwa kila mkulima kwenye kilo yake ya kahawa inaenda kufanya nini? Sisi kule Mbinga tumepata ugonjwa wa vidung’ata, kule wanauita viporomba, ukashambulia kahawa matokeo yake wale wakulima wakakatwa kila mkulima kwenye kilo yake kulipia hiyo na wakati walikwishalipa wakijua kabisa kuna Mfuko ambao utawasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni ushuru. Kwa mujibu wa sheria mkulima atapaswa kulipa 0% - 5% kwa kila kilo kwa ajili ya ushuru wa halmashauri. Hii range ya 0% - 5% imewekwa kwa halmashauri kuamua waweke wapi. Nimejaribu kuuliza hata kwa wenzangu wa Mbozi nao kule ni 5% haishuki, imebaki kwenye 5% pale pale nao wanaumia kama tunavyoumia sisi Mbinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanasababishwa na hizo tozo nyingi ambazo huko juu wanazichukua. Wakizichukua hizi tozo huko juu wanasababisha halmashauri zishindwe kuendeshwa na kwa sababu watu wa karibu ni wale wakulima, watawabana tu wakulima, hali hii haitaweza kuondoka hata siku moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni uhakika wa masoko na bei kwa mazao yote, mazao ya kilimo na mazao ya biashara katika ujumla wake. Kuna jambo nadhani hatujalifanya vizuri katika kutazama. Hivi tatizo la mkulima ni bei, uzalishaji au gharama za uzalishaji? Maana haya mambo matatu usipoyaweka katika level zake unaweza ukatatua tatizo ambalo si tatizo. Ukitizama kila mkulima analalamika, tumelima soko hakuna. Sisi tunakwenda ku-address soko na wakati tatizo ni gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachomfanya mkulima alalamike na anung‟unike ni ile pesa ambayo inaitwa mtaji, kaenda kuichukua kwenye SACCOS, VICOBA, UPATU, akaiingiza kwenye matuta yake mawili, mwisho wa siku anapata kidogo kuliko kile alichokiweka. Niiombe Serikali ijaribu kuangalia namna nzuri itakayowezesha kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima ili azalishe katika hali nzuri. Hata kama soko likiyumba badaye maumivu yanakuwa madogo sana kwa sababu, gharama ya uzalishaji ilikuwa ni ndogo kuliko ile gharama ya kuuzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii tena kurudia kwanza kumshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri aliyoifanya na anayoendelea kuifanya. Pili, nimshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake iliyoonesha uelekeo na kuonesha Serikali ya Awamu ya Tano itakwenda kufanya nini. Mwisho kabisa, nimshukuru kaka yangu Comrade Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba kwa kazi anayoifanya. Nikuombe kaka yangu wewe pigana, pambana kweli kweli lakini katika kufanya shughuli zako usisahau kutenga siku kadhaa twende Mbinga ukaone jinsi gani wakulima wanavyosulubika kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Nimezifuatilia hotuba zile mbili vizuri na michango michache ya waliotangulia, wamenilazimisha kufikiri baadhi ya mambo ambayo ningependa niyaseme jioni ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijiuliza hivi kwa nini kulikuwa na Serikali? Nikajiuliza kwa nini kulikuwa na Polisi, Magereza, Bunge na Mahakama? Ikanirudisha nyuma kwenye kumbukumbu yangu kipindi kile ulimwengu ulipokuwa hauna utawala kwenye state of nature na human nature. Nikawakumbuka akina Thomas Hobbes walivyokuwa wanaongelea; nikawakumbuka akina John Locke, Montesk, Jean-Jacques Rousseau na wengine wengi walivyokuwa wanaelezea dunia ilikuwaje kipindi kulikuwa hakuna utaratibu uliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema hivi, kabla ya kuwa na huu mfumo tunaouona leo dunia ilikuwa nasty, ilikuwa brutal, ilikuwa inakatisha tamaa. Maisha yalikuwa mafupi, vita ilikuwa kwa kila mtu, kwa yeyote. Tena Thomas Hobbes anasema kwa lugha ya Kilatini, katika kipindi kile kulikuwa na bellum omnium contra omnes, maana yake war of all against all, yaani vita ya wote dhidi ya wote. Ndiyo tukatengeneza huu mfumo. Huu mfumo ulivyotengenezwa ulikuwa ni kwa ajili ya ku-control tabia za wanadamu na hulka yake. Usipom-control, atatumia mamlaka yake vibaya. Mwisho wa siku unapata kile kitu kinaitwa survival for the fittest. Wenye nguvu na wenye mabavu wataendelea kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? nasema hivi ku-respond yaliyosemwa hapa na waliotangulia. Askari wanatumia nguvu zilizopitiliza katika kipindi cha chaguzi na wakaelezea maeneo na maeneo. Niwaambie kitu kimoja, kama wako makini, wao ndiyo wamewafanya Askari wafikie hatua hiyo, kutokana na ile ile hulka ya mwanadamu, akishajua kwamba hakuna kitu kinachom-control anafanya vitu vya ziada, anapambana katika jinsi anavyoona yeye mwenyewe inamfaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichotokea kwenye uchaguzi uliopita ambao mwenzangu ameusema pale wote ni mashahidi, nani ambaye alikuwa hajui kulikuwa na watu wanaitwa red brigade wakavalishwa kininja wakapewa mazoezi ya kupambana? Sasa mlitaka Askari waangalie red brigade wakiwa wamevaa kininja wamepambana ili nchi iwe ya makambale, vita of all against all. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanafanya kazi yao vizuri, ninyi mnakwenda mnasema yale yasiyowezekana. Nawaombeni ndugu zangu tuelewane. Tusipofika kwenye hatua hiyo, tunarudi kwenye state of nature, tunarudi kwenye human nature. Vitu hivi lazima viwe regulated! Lazima vitengenezewe utaratibu ili twende vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utaratibu huu wa migawanyo ya majukumu, hawa ndugu zetu Askari nao lazima tuwaangalie ili wafanye kazi zao vizuri, watulinde vizuri, ili tufike siku wafanye ile kazi inayotarajwa kuifanya nchi hii iwe nchi ya wote yenye amani inayofuata sheria na utaratibu. Wana mambo ya msingi, inabidi lazima nao tuwaangalie. Waliosema Askari kwake kambini, walikuwa wana maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani leo Askari akatoka nyumbani kwa baba John alikopanga, akaenda ofisini, halafu anarudi akamkamate baba John, hiyo haiwezekani. Turudi kwenye utaratibu wa zamani kuwaandalia Askari maeneo ya kukaa na kuwapatia facilities zitakazowasaidia wakafanye operations zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi dakika zilizobaki ataongea Mheshimiwa Kingu.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia asubuhi ya leo. Awali ya yote, nichukue fursa hii kama walivyosema waliotangulia kumshukuru sana na kumpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Comrade William Vangimembe Lukuvi. Kwa kweli ukiitazama Wizara yake, ukitazama majukumu yaliyopo katika Wizara hiyo na jinsi anavyofanya kazi na ile flexibility yake ya kwenda kwenye migogoro ya ardhi, kwenye masuala yanayohusu ardhi kila kona ya nchi yetu, kwa kweli inatupatia matumaini makubwa. Huenda mwarobaini wa migogoro ya ardhi ndani ya nchi yetu umeshapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya ya utangulizi, naomba nijielekeze kwa kifupi kwenye mambo matano ambayo naomba Serikali iyatazame kwa kiwango cha hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ya nchi yetu ipo vile vile ila inapungua kutokana na shughuli za bahari, size inapungua, lakini binadamu wanaongezeka kila kukicha. Kwa hiyo, watu wanazaliana, wanaongezeka, lakini ardhi bado ipo vile vile. Tusipokuwa na mpango mahususi wa kuitazama Tanzania ya leo, ya kesho na ya miaka 50 ijayo, tutakuja kuzalisha migogoro ya ardhi ambayo tutashindwa kabisa kuja kuituliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona miji inakua, sasa hivi Jiji la Dar es Salaam limekua katika kiwango cha hali ya juu, sasa linatusumbua jinsi ya kupanga. Wapi upitishe barabara, ni shughuli! Wapi upitishe maji safi, ni shughuli! Wapi upitishe maji taka, ni shughuli! Wapi upitishe nguzo ya umeme, ni shughuli! Hata sasa tunapotaka kwenda kwenye huo mpango wa gesi ambapo inapita kama mtandao wa maji, tutashindwa kwa sababu kila utakayemgusa, utalazimika kumlipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea Dar es Salaam lingekuwa ni kosa letu la mwisho kufanya kwenye miji mikubwa na miji inayofuata yote isiwe na matatizo ambayo yametukuta Dar es Salaam. Sasa tunaona majiji yanayokuja tena, yanapita kwenye matatizo yale yale ya Dar es Salaam. Nenda kaangalie Tanga, matatizo ni yale yale; Arusha inakuja kwa kasi, matatizo ni yale yale; Mwanza ndiyo kabisa, tena itafungana kuliko Dar es Salaam; nenda kaangalie Mbeya, matatizo ni yale yale. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri na Serikali, hii miji inayokua na ambayo mingine tuna-predict baada ya miaka 10 itakuwa miji mikubwa, tumalize mpango wa ramani ya miji. Miji ijulikane itakuwa na sura hii, tusirudi tena kwenye migogoro iliyopita huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii unaenda kutatua mgogoro wa Kigamboni; Kigamboni imekuwa darasa zuri sana kwenye mipango miji. Tupange mji, barabara itapita wapi, nyumba itakuwa wapi, uwanja utakuwa wapi na ikiwezekana twende kwenye hatua ya pili; na ramani ya nyumba pale iweje? Sasa atakapofika mtu apate kiwanja chake ajenge nyumba kwa mujibu wa ramani jinsi ilivyo. Tunazunguka nchi za watu, tunaona haya mambo yapo, siyo mageni. Namwomba Mheshimiwa Waziri alipe kipaumbele hili suala, litaweza kuja kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, hii Wizara ina changamoto kutokana na centers nyingi za decision making kwenye ardhi. Kijiji kina mamlaka, Halmashauri ina mamlaka, Wizara ina mamlaka. Ukiondoka kwa upande mwingine, unakwenda kwenye Wizara nyingine, ina mamlaka vile vile kwa mujibu wa sheria kwenye ardhi hiyo hiyo. Sasa matatizo ya Wizara moja au matatizo ya sehemu moja yenye mamlaka kisheria, yanaweza yakapelekea madhara kwenye eneo lingine.
Kwa mfano, migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi, unakutana na Wizara tatu ziko kwenye sakata moja; unakutana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, unakutana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; unakutana na Wizara ya Maliasili na Utalii; unakutana na TAMISEMI tena nao wapo humu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi Wizara nne zisipokaa zikajadili kwa kina, zikaona baadhi ya sheria nyingine ambazo tunaona zinaleta migongano ya kimaslahi, migongano ya kimadaraka zifutwe, hatutatoka hapa. Leo hii ninavyoongea, kule Mbinga tuna mgogoro wa ardhi. Halmashauri inamiliki ardhi ina mamlaka ya kupima kama kawaida kwa mujibu wa sheria; kijiji kimemkaribisha mwekezaji kwenye ardhi ambayo wapo pale wanakijiji. Baadhi ya wanakijiji wamekubali kumpokea mwekezaji, wengine hawataki. Imekuwa ni mivutano mikubwa. Sasa Wizara huku juu wanaweza wakadhani kule chini mambo yanakwenda sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kigonsera, Kijiji cha Mihango, Waziri anaweza akaja akapatiwa maafa ambayo kwa kweli yatakuwa hayawezi kuelezeka kwa sababu pale wanakijiji wapo juu wanakasirika kwa nini mwekezaji anakuja? Tunatambua kwamba wawekezaji ni muhimu sana katika Sekta ya Kilimo, nami na-encourage sana waendelee kuwepo kwa sababu kweli kuna mambo mengi tunayapata kupitia hawa watu, isipokuwa uelewa wa watu wetu, ukoje. Hii mifumo ya mamlaka katika ardhi inakuwa ni kikwazo kikubwa sana kuiwezesha Wizara yako kufanya kazi smoothly katika speed ya Mheshimiwa Waziri. Nawaomba wafanyeni watakaloweza kulifanya, hao wanne ambao ni wadau wakubwa wa ardhi, wakae, wapange mpango mzuri, tukitoka hapo mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, migogoro mingi ya ardhi ndani ya nchi yetu ina uhusiano na nani mmiliki? Nani kapima? Kapima wapi? Kwenye Halmashauri zetu, wana mamlaka ya kupima ardhi, lakini uwezo wao wa kupima ardhi ni mdogo. Naiomba Wizara itengeneze program maalum ya kutafuta vifaa vya upimaji kwa nchi nzima. Ikishapata hivyo vifaa vya upimaji kwa nchi nzima, kwa sababu kila Halmashauri tuna Maafisa wa Mipango Miji, waende wapime ardhi yote kusiwe na mgogoro, eneo la makazi mtu akitaka kununua kiwanja aende sehemu tayari kimeshapimwa, akalipie apate hati yake, ajenge aendelee na maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwangu pale maeneo ya Lusonga, Mji sasa unakua ardhi haijapimwa. Ukienda Lusewa, Mji wa Mbinga unakua, hakuna kupima. Ukienda Mateka, Kilimani, Tanga, Luwaita, haya maeneo yote ya miji hayajapimwa. Kesho mji utakuwa mkubwa, tutakuja kwenye migogoro mikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nadhani litakuwa la mwisho, nisemee kuhusu ujenzi wa hizi nyumba za bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naipongeza Serikali kwa kuifufua sasa National Housing Corporation i-operate katika kiwango cha hali ya juu. Tunaona nyumba zinajengwa lakini zile nyumba hazinunuliki. Mtu wa kawaida hawezi akanunua kabisa, ni ghali! Mbaya zaidi, tumeingia katika mortgage financing, mtu anakwenda kukopa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba akajisitiri, anaenda kwenye mkopo wa riba kwenye hiyo nyumba; yaani unanunua nyumba una riba, Nationa Housing Corporation wamechukua vifaa kwa ajili ya ujenzi wa ile nyumba, wanakatwa Value Added Tax kwenye yale mambo, ukiyaweka yale yote gharama zinakuwa kubwa sana. Hii siyo njia sahihi ya kumsaidia mtu kwenye ujenzi wa nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kitu kimoja kifanyike. Kama Serikali, tumeamua sasa tujenge nyumba za bei nafuu, twende kwenye mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tuiwezeshe National Housing Corporation ijenge kwa pesa zake, iuze na ipangishe. Zile nyumba zilizokuwepo miaka ya 1960 na 1970 mbona ilikuwa hakuna mambo kama haya tunayoyaona leo! Tuna flats zipo kila sehemu, ukiuliza wanasema hii ya National Housing Corporation, kila Mkoa zilikuwepo! Namwomba Mheshimiwa Waziri, najua haya mambo anayaweza. Kaa na National Housing Corporation, wasikilize changamoto zao, waweke vizuri wajenge nyumba za bei nafuu ili kila Mtanzania sehemu ya kulala isiwe tatizo tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara asubuhi ya leo. Wizara ya Maliasili na Utalii ni miongoni mwa Wizara mtambuka inapokuja mahusiano yake na wakulima, inapofika mahusiano yake na wafugaji. Nchi yetu ina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 947,300. Kati ya hizo ardhi ambayo tunaweza kutumia kwa ajili ya kufuga, kulima, kujenga na shughuli nyingine za miundombinu ya kijamii ni takribani kilomita za mraba 885,800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilomita za mraba 61,500 ni kwa ajili ya water bodies, kwa ajili ya bahari, mito na maziwa. Kwa maneno mengine shughuli zote tunazozitumia kwa ajili ya ustawi wa maisha yetu, tunategemea kilomita za mraba 885,800 ambazo wakulima wanazihitaji hizo hizo, wafugaji wanazihitaji hizo na hifadhi wanahitaji hizo hizo. Ukifuatilia hotuba ya Mheshimiwa Waziri unakuja kugundua asilimia 33 ya hizo kilomita za mraba nilizozitaja ndiyo mbuga na hifadhi za misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tunaendelea kuongezeka kwa idadi kila siku na ng‟ombe wanazidi kuzaliana na kuongezeka kila siku. Katika hiyo 885,800 kilomita za mraba, kuna ukame unaikuta hilo hilo eneo, kuna mafuriko, lakini kuna shughuli nyingine za volcano kwa mfano kule Oldoinyo Lengai ikipiga volcano pale huwezi kulima, huwezi kufuga. Kwa hiyo, ardhi bado inaendelea kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa watu wamesema wafugaji wanahitaji malisho na hizi sababu nilizozitaja ndizo zinazowafanya wahamehame. Tumesahau kwamba na wakulima nao wanahamahama kutafuta chakula, kutafuta sehemu nzuri ya kulima kwa hoja hizo hizo kama za wafugaji. Tukisema leo tuangalie tu mgogoro kati ya wakulima na wafugaji kwenye sehemu ya malisho ya wanyama, tukienda kutazama mgogoro kati ya hifadhi na wakulima kwenye yale maeneo ya buffer zone kama maeneo ya Mto Kilombero, eneo lina rutuba nzuri wakulima wanakuja eneo la hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukienda upande wa selous kule wakulima wamekata miti wanaingia eneo la hifadhi. Ukija Kilosa, Mikumi the same, kila sehemu utakuta mkulima anaongezeka kutafuta maeneo ya kilimo kwa sababu eneo analolima kwanza rutuba nayo inapungua, ikipungua rutuba aina yetu ya kilimo kwa sababu siyo kilimo cha kisasa tunakutana na matatizo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye upande wa mifugo, takwimu zinatuonesha tuna zaidi ya ng‟ombe milioni 25 na hawa ng‟ombe wanazaliana kila mwaka kwa zaidi ya milioni moja. Baada ya miaka 10 tutakuwa na ng‟ombe milioni 35. Nashangaa humu ndani tunasema tuna wafugaji, mniwie radhi humu ndani tuna wachungaji hatuna wafugaji. Huwezi ukajiita mfugaji unahama pori moja unakwenda pori lingine na huwezi ukajiita mkulima, hatuna wakulima, tuna wabangaizaji wanaotafua maeneo kwa ajili ya kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri kitu kimoja, juzi nilisema hizi Wizara nne, tano zikae pamoja kwa ajili ya kupanga vizuri, tukisema leo tutenge maeneo kwa ajili ya ufugaji, ng‟ombe wanazidi kuongezeka, ardhi bado ni ndogo na aina yetu ya ufugaji tunaona kabisa hatuwezi kuja ku-solve hili tatizo. Baada ya miaka10 tuna ng‟ombe milioni 35 tutawatengea maeneo gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaondoa kule Ihefu tumewapeleka Lindi, yale maeneo Lindi yaliyopangwa kwa ajili ya wafugaji leo watu wanalima ufuta. Kwa tatizo lile lile wakulima wana matatizo, wafugaji wana matatizo. Sasa hili haliwezi likajibiwa kwa Waziri kuja kutuambia hili tatizo atalimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tujadiliane hivi, lakini baada ya bajeti mimi niiombe Serikali, ikae Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Maliasili na Utalii na Wizara ya Mazingira. Lazima haya tuangalie, tunakwenda tunamsahau wa mazingira huyo, ukame ukija, tunamsahau wa mazingira huyu, mafuriko yakija na haya maeneo yanayotengwa yanatengwa kwa hoja za ikolojia. Tukisema tulime kote, tufuge kote, mwisho wa siku mvua tutakosa, nchi nzima itakuwa jangwa. Kwa hiyo, hoja siyo hoja ya hisia, siyo hoja ya kusema mimi ni mkulima nataka wakulima wangu wakae vizuri, mimi ni mfugaji nataka ng‟ombe wangu akue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku tutalima wote, tutafuga wote, tutashindwa sehemu ya kufuga, ardhi itageuka jangwa na hata tunaohama hama wakulima kutafuta maeneo mazuri ya hifadhi yenye udongo wa rutuba kwa ajili ya kupata mahindi mazuri, kwa ajili ya kupata maharage mazuri, ufuta, itafika muda haya maeneo mvua haitafika, na hiyo mito tunayotegemea kumwagilia nayo mvua haitakuwepo, maji hayatakuwepo, samaki hawatakuwepo. Kwa hiyo, sekta moja ikikorofisha itapelekea sekta nyingine kuharibikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwa nia njema kabisa, tutajadili kila kona kuhusu Maliasili na Utalii kwenye eneo la migogoro ya wafugaji, kwenye maeneo ya matumizi bora ya ardhi, lakini hatutafika mwishoni kama hakutakuwa na mpango mkakati wenye sura mbili. Kwanza mpango wa dharura, uitwe transformation strategy, kuwatoa wakulima wanaohama hama wawe centralized katika kilimo cha kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuwaondoa wachungaji wanaohama kuchunga chunga wawe centralized, wafuge ng‟ombe wao vizuri wazaliane na wawe na tija. tukienda hapo tutafika mbele kwa haraka na ardhi yetu tutaitunza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna kosa moja tunalifanya, tunapoongelea vyanzo vya mapato na nguvu kazi ya Taifa letu tunatazama wakulima, tunatazama wafanyakazi tunasahau kuwatazama wafugaji kama sekta rasmi ambayo ipangiwe mipango kama tunavyopanga mipango kwenye maeneo ya kilimo. Tunamwangalia mkulima, yaani mfugaji anakwenda kwenda tu, ndiyo kwa maana leo yuko Lindi, keshokutwa anatoka, hatuwezi kwenda kwa staili hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, wafugaji sasa kwa sababu sio wafugaji, tuwa-transform kwenda kuwa wafugaji, wawekwe kwenye utaratibu mzuri, tija tutaipata. Hatuwezi leo kusema tuna ng‟ombe milioni 25, halafu pato hatulioni. Baada ya miaka 10 tutakuwa milioni 35 halafu wao wanazunguka tu nchini, haiwezekani hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwa nia njema kabisa hizi Wizara nne zikae pamoja, zije na mkakati mkubwa, hii migogoro haitakuwepo na wala tusitoe hapa maneno ya kuwafurahisha wakulima, kuwafurahisha wafanyakazi ili migogoro itulie, haitatulia. Ardhi ni ndogo sana, msijidanganye mnatoka hapa mpaka Dumila mnaona yale si mapori, yale ndiyo kwa ajili ya kuleta vertilization ni AC ile ya kuleta hali ya hewa nzuri. Sasa siku mki-clear ile miti, cha moto mtakiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kuendelea bila kuwa na mambo manne yafuatayo:-
La kwanza, ni uwezo wake kukusanya kodi; la pili, nidhamu ya kutumia kile ilichokusanya; la tatu, kujenga mazingira ya kodi endelevu yaani kodi isiyo ya muda mfupi, kutengeneza mazingira wananchi waendelee kulipa kodi kwa wakati wote; na la nne ni kutengeneza mazingira mapya ya kupata kodi mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Awamu ya Tano imeonesha nia ya dhati, imeonesha dhamira ya dhati kwenye haya niliyoyasema kwa kiwango kikubwa sana. Tumeona mikakati ya kubana mianya ya wakwepa kodi, lakini tumeona mikakakti inayopelekea kukusanya kodi kwa wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tumeiona Serikali hii katika mipango yake imeelekeza asilimia 40 kwenye shughuli za kimaendeleo, hii ndiyo inakuwa tafsiri sahihi ya kuelekeza kile ulichokikusanya kwenye eneo sahihi, yaani shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maamuzi haya ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenye hii bajeti si madogo, ni kwa mara ya kwanza imewekeza pesa nyingi kwenye shughuli za kimaendeleo. Sisi Waheshimiwa Wabunge katika ujumla wetu ni wajibu wetu kuishauri Serikali na kwa wingi wetu tuna uhakika tukipeleka sauti yetu kwa Serikali watatusikiliza. Ndugu zangu Walatini wana methali yao, huwa wanasema quot capita, tot sententiae wakimaanisha kwenye wengi hapaharibiki neno. Huu wingi wetu wa Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge lako Tukufu tukiipitia hii bajeti katika ujumla wake, tuna mawazo mazuri ambayo tunaamini Serikali wakiyabeba yatatufikisha kule tunakotaka kwenda kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeainisha mambo mengi, kwa asilimia kubwa ni mazuri sana, lakini kuna mengine machache inabidi tuyaboreshe kidogo na tuiombe Serikali iwe flexible kwenye kutusikiliza. Wasione ugumu kuyapokea yale tunayowaeleza, nia yetu ni njema kama wao walivyokuwa na nia njema, kama wenzetu wanavyosema quot capita, tot sententiae, palipo na wengi hapaharibiki neno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mambo ambayo Mheshimiwa Waziri amekuja nayo mazuri, nimependa wameondoa tozo na ushuru kwenye Sekta ya Kilimo. Wameondoa kwenye korosho, pamba na kahawa, lakini nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwenye zao la kahawa, ameondoa kodi moja, leseni ya kusindika kahawa ya Dola 250, lakini siku zote tumekuwa tukisema na Mheshimiwa Rais amezunguka kwenye kampeni yake nchi nzima ameeleza wakulima wa kahawa wanasulubika sana, wana kodi na tozo 26.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ameiondoa moja tu Mheshimiwa Waziri, nimwombe, tulisema kuna ushuru wa halmashauri wa asilimia tano, tuliomba Serikali shusheni angalau uwe wa asilimia tatu ili wakulima wetu wapate ahueni. Kuna leseni ya kununua kahawa ya Sh. 300,000, kuna tozo ndogondogo, kama sisi kule kwetu Mbinga kuna tozo ya Sh. 20 kwa kila kilo kwa ajili ya wale wadudu vidung’ata, kuna leseni ya Bodi ya Kahawa ya Dola 1,024. Kuna tozo ya TACRI ya asilimia 0.75 kwa kila kilo ya kahawa, kuna mchango wa Tanzania Coffee Development Fund (TCDF) wa 0.10, kuna ushuru wa ulinzi zaidi ya 200,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hayo yote tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri ile Dola 250 waliyotoa ya usindikaji ni ndogo sana kwa wakulima wa kahawa, aziangalie zile kodi zote katika ujumla wake, akifanya hivi itampendeza Mungu na akifanya hivi maendeleo tutayapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tunatoa misamaha ya kodi, lengo la Serikali kutoa misamaha ya kodi si kupunguza mapato yake, ni kutengeneza mazingira yule mtu ambaye anasamehewa aende akawekeze au akafanye jambo lingine ambalo litaleta kodi nyingi kwa watu wengi kwa wakati mmoja, ndiyo maana Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa misamaha ya hizi kodi ili kutengeneza mazingira mazuri ya kukusanya hizo kwa mlango mwingine, hiyo ndiyo maana na dhamira ya dhati ya kuweka hiyo misamaha ambayo Serikali imeiweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kwenda, tena kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya kiwango cha hali ya juu ya viwanda. Viwanda haviwezi kufika kama Serikali haitakusanya mapato, viwanda havitaweza kufika kama Watanzania hawatakuwa na uwezo wa kujiletea kipato na kuweza kujikwamua katika maisha yao ya kila siku. Kwa sababu viwanda vinahitaji kwanza mashine kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine viwanda vinahitaji raw material, hawa wakulima lazima wawe na uwezo wa kuzalisha sana pamba, wawe na uwezo wa kuzalisha kahawa, wawe na uwezo wa kuzalisha katani, wawe na uwezo wa kuzalisha tumbaku ili viwanda vyetu viendelee kujiendesha kwa muda wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya mambo yote ndiyo inakuja ile hoja ya tatu kwa Serikali makini ambayo inataka maendeleo; lazima itengeneze mazingira kwa wananchi wake waweze kulipa kodi kwa wakati wote. Hawawezi kulipa kodi kama wana mazingira magumu ya kuzalisha. Ndipo namwomba Mheshimiwa Waziri na timu yake, najua Serikali ya CCM ni sikivu, Serikali ya Awamu ya Tano ina maono, inatufikisha mbali, wakakae na timu yake akirudi aje atuelezee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo Mheshimiwa Waziri alilisema juzi kwenye hotuba yake, sasa anaingiza VAT kwenye utalii. Hili jambo ni jambo zuri sana, lakini nilipoisoma hotuba yake inasema reference kwanza tuliweka sheria mwaka jana, tulikuwa na mikataba tukasema mwaka huu tuimalize halafu tuendelee, lakini amei-refer Kenya wenzetu wameiondoa, ami-refer Rwanda, amei-refer South Africa; juzi wenzetu wa Kenya wameiondoa VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, aende akaangalie kitu gani kilitufanya sisi tusiiweke, kitu gani kimewafanya Kenya juzi waiweke, ili aitazame katika mapana yake, siyo kwa sababu tu South Africa wanafanya, kwa sababu tu Rwanda na Kenya wananfanya, sidhani kama ilikuwa ni dhamira.
Mheshimiwa Naibu Spika, nahisi Mheshimiwa Waziri ana hoja za kutosha za kutushawishi sisi tuamini au tuelewe kwamba kuweka ile kodi ya VAT kwenye utalii itatuongezea mapato sio kutukimbizia. Tukumbuke kwa sasa utalii unatuletea Dola karibu bilioni 2.5 kwa mwaka jana, 2015. Nadhani hii ilitokana na sisi tulikuwa na mazingira mazuri ya kuwezesha watalii wakafanya kazi. Leo hii wenzetu Kenya, wanasema ile the last token tuliyokuwa nayo inayomzidi Kenya kwenye ushindani, mwenzetu ndiyo kaibana ile, ameondoa sisi tumeweka, naomba Mheshimiwa Waziri alitazame hili kwa mapana zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, Mheshimiwa Waziri alisema sasa tutakwenda kutengeneza sheria ambayo itaondoa misamaha kwa taasisi za kidini. Hii naomba niseme kidogo na nimuunge mkono ndugu yangu, Mheshimiwa Richard Ndassa aliyeongea juzi. Hili jambo Mheshimiwa Waziri tulitizame kwa mapana kidogo. Unajua haya madhehebu ya kidini huduma wanayotoa ni huduma, hawafanyi biashara. Wamewekeza kwenye hospitali, wamewekeza kwenye elimu, wamewekeza kwenye maji safi na salama, wamewekeza kwenye shule, ndiyo kazi wanayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumwambia mtu leo, anataka alete mashine ya CT Scan kwenye hospitali ile ya mission au ile ya taasisi ya kidini, alipe kwanza ushuru wote halafu baadaye tufanye assessment arudishiwe, nina uhakika hawatanunua hizo mashine, kwa sababu kwao kazi yao ya kwanza si huduma za kijamii, wao kazi yao ya kwanza ni kumtumikia Mungu na kuleta injili na kupeleka aya ili wanadamu wamfikie Mungu, ile wanatusaidia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkizingatia haya maeneo yote ninayoyasema, nendeni mkaangalie zahanati zilikojengwa, hospitali zilikojengwa; mnaikuta Mvumi kule, utaikuta Hospitali ya Mvumi, nenda Lugarao utaikuta kule, nenda Ikonda, nenda utakuta Hospitali ya Peramiho, Hospitali ya Ndanda, Hospitali ya Lituhi, Hospitali ya Litembo, Hospitali ya Ifakara; hizi zote zinatoa huduma na nawaambia kabisa ukifika kule unajikongoja una shida, wanaweza wakakuhudumia hata bila kukutoza halafu uje uwalipe baadaye, hiki kitu hakipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, kwenye suala la afya tuwape msamaha, kwenye suala la elimu tuwape msamaha na kwenye suala la maji safi na salama. Kwa mfano kwangu mimi kule Mbinga, toka dunia imeumbwa maji ya kwanza ya kunywa yalikuwa ya Buruda Otmar, (Brother Otmar) leo hii akitaka kubadilisha mabomba eti alipe kwanza ushuru sisi tupate maji safi na salama. Mheshimiwa Waziri, namwomba sana kwa dhati ya moyo wangu, alitazame hili jambo vizuri sana, sisi tulioko humu ndani nia yetu ni njema sana, hatutaki watu wakwepe kodi na tutashirikiana nao wasikwepe kodi, quot capita, tot sententiae. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niwapongeze kwa mpango mzuri waliotengeneza. Ukiusoma mwanzo mpaka mwisho hupati shaka kwa yanayoenda kutekelezwa na hasa walipogundua kuingia na mfumo wa program wa kibajeti ambao mimi naamini wakijielekeza kwenye program itawasaidia huu Mpango ukatekelezeka vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzuri wa Mpango huu, nimeusoma kurasa zote lakini huu Mpango una changamoto moja, umekosa kitu kinachoitwa rejea. Tukipata nafasi ya kurejea mafanikio ya Mpango uliopita, unatupa nafasi nzuri ya kushauri Mpango huu tuutekeleze vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walatini wana msemo repetitio est mater studiorum wakimaanisha marejeo ni mama wa mafunzo. Tutakwenda na mpango huu, tusipopata fursa ya kurejea mwaka mmoja uliopita kwamba tulipanga nini, tumefanikiwa nini, tufanyeje ili tusirudi nyuma, hatutafika. Hilo ndilo jambo linalotia shaka mpango huo mzuri. Tusipopata marejeo ya mafanikio ili twende vizuri zaidi; ya upungufu ili turekebishe, hatutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango aje angalau na summary ya tulikotoka, tulipo na tunakokwenda ili tuutendee haki huu mpango ili tufanye vizuri ndani ya mwaka ujao na baada ya miaka mitano tuseme Tanzania tuliikuta hapa, tumeitoa mwaka 2015, tunaiacha hapa 2020 kwa mpango unaoeleweka na unatabirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1981 Chama cha Mapinduzi kilitoa mwongozo. Kwenye ule mwongozo kuna maneno mimi napenda sana kuyatumia na huwa napenda sana yawe sehemu ya maisha ya viongozi wenye utu. Yale maneno yanasema hivi, “kujikosoa, kukosolewa na kujisahihisha siyo dalili ya kushindwa bali ni njia sahihi ya kujipanga na kufanikiwa vizuri zaidi.” Tukiona pale tulipokosea aidha kwa kuambiwa au kwa sisi wenyewe kuona maana yake tumejikosoa, siyo kwamba tumeshindwa, inatupa njia nzuri ya kutoka hapa tulipo, twende mbele zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Nasema hivi kwa sababu huu mpango umekuja na programs ambazo tunaamini tumezipa vipaumbele. Kuna miradi ya vielelezo. Unaposema miradi ya vielelezo tafsiri yake ni kwamba kwenye haya mambo baada ya mwaka mmoja tutasema hiki ndicho kielelezo kinachotuonesha kwamba tumefanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeelezea vizuri sana kuhusu viwanda, lakini nikiangalia sioni sehemu ambapo kuna mikakati itakayokuja kukabiliana na changamoto za viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuatilia sana nchi zilizokuwa na viwanda, aidha zile za zamani za Ulaya zilizoanza na coal and steel industries, Wajerumani na Waingereza; au zile za Mashariki ya Mbali zilizoanza na textile industries baadaye zikaendelea, hawa wote walikuwa na misingi minne ambayo namwomba Mheshimiwa Waziri Mpango aiangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa kwanza wa viwanda ni power (energy) na gharama za energy; msingi wa pili wa ni qualified personnel (manpower); watu wenye uwezo wa kuviendesha hivyo viwanda; msingi wa tatu ni malighafi (raw materials). Utavilishaje hivyo viwanda? Msingi wa nne siyo katika maana ya udogo wake, is financing. Una uwezo gani wa kuviendesha, kuvi-finance, kuvigharamia hivyo viwanda aidha kwa mapato yako ya ndani au kwa kushirikiana na watu wengine wenye mitaji kuja kwenye mifumo ya kuwekeza kwa kushirikiana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiyaangalia haya yote, yananipa sababu za kutosha kumwomba Mheshimiwa Waziri ayaangalie maeneo mawili kwenye mkakati wake. Eneo la kwanza kubwa ni mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na mradi wa chuma wa Liganga. Kwa nini nilianza na kusema repetition est mater studiorum? Huu Mpango ulikuwa mwaka 2007, ndiyo kwa mara ya kwanza tunataka sasa Mchuchuma na Liganga ije iwekeze kutuletea chuma, ije ituwekee umeme wa kutosha na iongeze umeme mwingine kwenye gridi ya Taifa, it was 2007. Leo tunapoongea, we are approaching ten years.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nasema marudio ndiyo mama wa mafunzo. Tusiporudia kutaka kujua tulipotoka, tutadhani tunakuja na kitu kipya kumbe kitu kipya kilipata changamoto nyingi sana na hizo changamoto hatukupata fursa ya kuzirekebisha. Kwenye huu mpango, Mchuchuma, mmesema itazalisha Megawatt 600. Kati ya Megawatt 600, Megawatt 250 ndiyo zitazalisha umeme kwa ajili ya chuma kile cha Liganga na 350 ndizo sasa watauziwa TANESCO kuingia kwenye grid ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa za wazi zinasema haya mambo yote yako sawasawa isipokuwa kuna mvutano mmoja kwenye power purchase agreement ambapo mbia anataka tununue umeme kwa 13% sisi tunataka tununue umeme kwa 7%; lakini tukumbuke agenda ya umeme ni ya mradi mmoja tu na agenda ya chuma ile siyo hoja pale ya sisi kujadiliana tumeuziana umeme kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuendelea na mradi wa chuma cha Mchuchuma kwa sababu tu ya bei ya umeme. Kwa nini kwenye zile Megawatt 250 ambazo ndiyo za mbia, azalishe 250, atuletee chuma sisi tuzalishe chuma, tuachane na 350 ambao tutaununua kwa sh. 7/= au sh.13/=. It is wastage of time! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mpango, kwa dhati ya moyo wangu, hebu a-focus kwenye hili kwa sababu nalo lina maneno ya hujuma; hujuma zina sura mbili. Wanasema, bwana, kusikiliza maneno ya mtaani siyo jambo zuri, lakini yakisemwa kwa muda mrefu yanawafanya watu waamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema huu mradi unahujumiwa; kwanza unahujumiwa na mashirika makubwa na makampuni makubwa ya upande mwingine kwa sababu mradi kapewa Mchina, wanataka usuesue usifike kwa wakati, lakini wa pili wanasema, eh, kwa sababu Kusini siku zote ni Kusini, basi Kusini iwe ya mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mambo hayatujengi sisi kama Wabunge, haya mambo yanatufarakanisha, yanatufanya sisi watu wa Kusini tuendelee kuwa maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie Kusini siyo Kusini kama mnavyofikiri, kama Kusini ingekuwa inamaanisha chini, Mto Nile usingetoka Ziwa Victoria kwenda Kaskazini. Nataka kukwambia Kusini ni juu na Kaskazini ni chini kwa lugha kama hiyo. Niombe kabisa, tusifike sehemu tukawafanya watu wa Kusini ionekane kwamba wanahujumiwa katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujipe muda wa kutosha kwenye hoja nzima ya Mchuchuma na Liganga. Kwa nini nasema hivi? Kanuni ni mbili tu; tukifanikiwa kwenye Mchuchuma katika maana ya kuleta chuma na chuma kile hakitafika peke yake, kitakuwa na madini mawili, tutapata vanadium na titanium. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku chuma sasa ndipo tutakapoongelea mataruma yale ya kwenda reli ya kati yapatikane pale; mtakapotaka sasa madaraja yenu, vitu vitoke pale. Ndiyo zile kanuni nne nilizozisema; angalia sehemu zote, angalia eneo la power; power tunayo. Sasa unafanyaje kukifanya kiwanda cha textile industry kiende vizuri? Power yetu ni ghali, tuangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utatengeneza kiwanda cha nguo, tuna soko kubwa la nguo, tutashindwa ku-compete kitakufa. Kwa sababu nguo ya Thailand, China na Uturuki itauzwa bei ya chini kwa sababu ya cost of production, haya mambo yote Mheshimiwa Mpango yaweke katika mizani yake, tutatue hili tatizo Watanzania tutoke hapa tulipo twende mbele zaidi. Watanzania wanataka viwanda, nami nataka viwanda, nawe unataka viwanda; lakini viwanda lazima tuvipange vizuri kwa kuangalia kila element, tusiache untouched stone, kila jiwe likanyagwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Mkataba huu wa ubia baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote niwapongeze waliotangulia kuupinga huu mkataba kwa nguvu kubwa na maneno mazuri yalio-base kwenye content nikianzia na mchangiaji wa mwisho Cosato Chumi aliyechangia kabla ya mimi, michango ya Mheshimiwa Kabwe Zitto, Mheshimiwa Azzan Zungu, Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mheshimiwa Hussein Bashe na wengine wote, wameenda vizuri sana kwenye content, na Mheshimiwa Hamidu Bobali na chama chake na Mheshimiwa Khatib Said Haji.
Mheshimiwa Spika, sitakwenda kwenye content nitagusa mambo ya jumla ambayo ninadhani jumba lako hili Tukufu ni vema likajua ili tuweze kwenda katika mtiririko mzuri. Kuna watu wamesema hapa, nakubaliana Tanzania siyo kisiwa na wengine wamesema tusiikimbie hii ndoa, hii ndoa ni muhimu ni nzuri ina mazuri yake ni vema tukayatafuta mazuri yaliyoko sirini yasiyoonekana ili tuone kuna nia njema ndani ya hili. Naomba niseme machache yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, nchi yoyote inapoamua kufanya urafiki na Taifa lingine lolote, kuna mambo inapoteza kama Taifa na kuna mambo inayapata kama Taifa, kwa maneno mepesi, mahusiano yoyote baina ya mataifa yanaunganishwa na principle ya statism, principle ya self-help na principle ya survival. Katika mazingira yoyote yale unapoingia kwenye makubaliano na Taifa lolote lile, kanuni ya kwanza inayopaswa kuku-guide, una interest gani kama Taifa kwenye ule mkataba.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, unalopaswa kuliangalia, utanufaika kwa kiwango gani katika ule mkataba? Lakini kuna mazingira mengine, unaweza usinufaike, ila ule mkataba ukakusaidia kuishi uione kesho yako, labda kuwakimbia maadui hiyo ndiyo inayoitwa national survival.
Mheshimiwa Spika, yawezekana kuna wengine wanayatafuta mazuri kwenye Mkataba huu kwa sababu tu ya ule woga katika makubaliano kuna mchawi asiyeonekana, yaani wanatafuta ku-survive sehemu ambayo hakuna survival. Niwaombe ndugu zangu Wabunge, historia ya nchi yetu tumeshirikiana na mataifa mengi katika nyakati tofauti. Kuanzia karne ya tano tuliposhirikiana na nchi za Mashariki ya Mbali na nchi za Uarabuni mpaka kipindi nchi za Ulaya zilipoingia, kipindi cha ukoloni na mahusiano baada ya uhuru. Wote mmeona kila Tanzania tulipojikwamua kutoka kwenye makucha ya kutaka kuendelea kumekuwa na uhusiano wa mjomba wa kuturudisha nyuma.
Mheshimiwa Spika, tumetoka kuanzia mwaka 1961 mpaka leo tunaongea mwaka 2016, kuna mikakati mingi sana tumeipanga kama Taifa, kuna mikakati mingi sana tumeipanga kama nchi na majirani zetu, kuna mikakati imefanikiwa na mikakati haikufanikiwa. Ni jukumu letu sasa kujiuliza kama Taifa, haya mahusiano tuliyowahi kuyafanya nyuma yalitusaidia kwa kiasi gani? Na haya mahusiano tunayotaka kuyafanya sasa yana tija kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, niwakumbusheni ndugu zangu Wabunge, tulishawahi kugawanywa katika block mbili, block ya East na block la West. Mnakumbuka kipindi cha cold war. Nchi yetu kama Taifa ilisimama ikasema hatutageuka kulia wala kushoto tutakwenda katika mfumo ambao tunaona nchi yetu ina maslahi nayo, hatukugombana na Wamarekani na Waingereza na wala hatukugombana na marafiki zetu wa Urusi.
Mheshimiwa Spika, leo tunavyokwenda kuujadili mkataba huu, ni mkataba wa kwanza ndani ya nchi yetu kuwekwa fungu moja as a bargaining block against European Union. Haikuwa kutokea huko nyuma na wala hatukuwahi na experience ya kundi zima tukawa na interest sawa, tukawa na historical background sawa, tukawa na matamanio sawa, tukawa na ndoto sawa, leo tukae kwenye meza ya majadiliano against a huge block - European Union.
Mheshimiwa Spika, ninaona kuna tatizo, kuna matatizo mawili; tatizo la kwanza si mahusiano yetu na Jumuiya ya Ulaya na wala siyo mahusiano yetu na majirani zetu wanaotuzunguka, tuna tatizo la kwanza la content, mambo yaliyopo ndani ya mkataba ambayo tunayapinga. Kwa bahati mbaya sana kwa hatua tuliyofikia, hatuna fursa ya kuchambua kifungu kimoja baada ya kingine, tuna fursa moja tu sasa hivi ya kuukataa, kwa sababu ya kukubali hatunayo. Baada ya kukataa hayo mazuri msiyoyaona hapa mnayodhani yapo, ndiyo yatakuja.
Mheshimiwa Spika, leo hii hapa tujadili nini, tu-suspend, uende halafu urudi, hapana. Hatuna fursa hiyo, tuna fursa leo ya kusema Serikali isaini mkataba au Serikali isisaini mkataba. Kutokana na hoja zote zilizotolewa ndani humu na Wabunge, nakubaliana na ninaiomba Serikali isisaini mkataba huu. Kwanza, haujatupa room ya kufanya marekebisho, kama kutaonekana huko mbele kuna haja ya kurekebisha vifungu tutakwenda.
Mheshimiwa Spika, tuna marafiki zetu wametangulia, ndugu zetu Walatini wana msemo amicorum omnia communia wakimaanisha between friends all is common au wakimaanisha for friends all things are shared. Sasa kwa style ya wenzetu wanavyokwenda tunaona ile principle ya amicorum omnia communia haipo, hatuoni kitu hapa kinachoenda in common. Walishakaa Wakuu wetu wa nchi wakasema tujipe muda wa miezi mitatu, wenzetu wamekwenda speed.
Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kusema machache yafuatayo; umefika wakati sasa kwa Watanzania kutoka kwenye giza nene la urafiki wa kinafiki wenye lengo la kudidimiza na kuua ndoto ya Tanzania kuwa na viwanda. Umefika wakati sasa kwa Tanzania kutoridhishwa na aina hii ya urafiki mpaka pale mishipa yetu ya fahamu itakapojiridhisha kwamba urafiki huu haufanani na ule urafiki wa paka na panya kukumbatiana na kubusiana ilhali shimo la panya la kutorokea liko mbali.
Mheshimiwa Spika, wakati sasa umefika kwa Watanzania kutokuwa na kiu ya kutaka kunywa maji ambayo yako kwenye kikombe cha mateso, uchungu na maumivu makubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa maneno haya, siungi mkono hoja na ninaiomba Serikali isipitishe na isisaini mkataba huu. Ahsante sana.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye taarifa ya Kamati. Awali ya yote niungane na walioipongeza Kamati kwa kazi nzuri walioifanya ya uchambuzi na kutupatia mwelekeo, huenda bajeti ijayo ikawa nzuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imefanya kazi kubwa ya kutuonesha maeneo gani tunapaswa kuyafanyia kazi kama nchi, Kamati imetusaidia kutuonesha hali halisi ya nchi yetu iko wapi katika masuala ya kiuchumi na vilevile kutuwekea mazingira mazuri ya kutuwezesha kufanya tathmini na kujipanga kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuipitia taarifa hii nimeona kuna mambo mawili, matatu tunapaswa kujifunza na wataalam wetu watusaidie. Sina hakika kama tumewahi kujiuliza swali kitu gani kinacho-run uchumi wa nchi yetu. Ukiangalia kwa umakini vipimo vinavyotumika kuielezea Tanzania inaendelea au haiendelei ukitafakari kwa makini unakuja kugundua tunaishi Kitanzania na tunafikiri Kiulaya. Mwisho wa siku tukitafsiri fikra za Ulaya kwenye maisha ya Kitanzania tunakuja na majibu kwamba uchumi unakua halafu tunaona idadi ya maskini inaongezeka. Kwa nini hili linatokea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya World Bank inaeleza itakapofikia mwezi August inflation rate itashuka, inaweza ikafika 4.5 kutoka kwenye 6.5. Hata hivyo, katika kipindi hiki uchumi wa nchi yetu unaonekana unaendelea kuimarika na wakatoa sababu kwa nini tunaendelea kuimarika. La kwanza wanalolisema ni kwamba Tanzania ina political stability nzuri yaani nchi yetu ina utulivu wa kisiasa kiasi kwamba tuna fursa zote za kufanya nchi yetu ikaendelea. La pili, nchi yetu ina fursa za kiuchumi nyingi za kutosha ambazo bado nyingine hazijatumiwa katika kiwango cha kusema hii nchi ni kuzimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaposema kiwango cha umaskini kimeshuka halafu taarifa hiyohiyo inakwambia maskini wanaongezeka unaweza ukasema hii hai-make sense, ni kwamba tumeshindwa kutafsiri maisha ya Watanzania. Hivi kuna utafiti gani umefanyika baada ya kujengwa kwa barabara ya Dodoma - Iringa kupitia Mtera ukafika katika vile vijiji vilivyojengwa baada ya ile barabara wanauza nyama za mbuzi pale, kuna mtu ameweza kujua pato lao kwa siku ni shilingi ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu amewahi kufika Mbinga akakuta matuta kumi ya viazi yanayomfanya mwananchi pale aishi akienda dukani anakwenda kununua tu sabuni, chumvi na mafuta ya taa, akakaa Januari mpaka Desemba akauza magunia yake mawili ya mahindi akampeleka mtoto wake shuleni akasoma halafu mwisho wa mwaka mnasema huyu kwa siku yuko chini ya dola, vipimo gani tunavyovitumia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wataalam wetu mtusaidie. Katika kipindi hiki nchi yetu imeendelea sana ndiyo maana wanasema uchumi wa nchi unakua. Anayesema maisha ya Watanzania hayakui ni kwamba hajakwenda into details, hajaenda kuangalia familia kwa familia tukoje. Hivi tuseme ule ukweli, kama kweli hapa ndani wote tuna familia na kuna watu tunawalea, kama tupo chini ya dola kweli tungeishi? Mnaelewa maana ya chini ya dola, maana yake tunaishi chini ya Sh. 2,000 kwa siku mtu ana familia ya watoto saba hakuna mtu anayekufa na njaa, does it make sense? Kuna vitu vingine mimi sivielewi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe wataalam, tukitaka tulingane na nchi nyingine zilizoendelea kama Asian Tigers, tukiwafuata tutapotea. Tukitaka tukajifunze Botswana kama wengine wanavyosema tutapotea. Mfumo wa Tanzania ni wa kipekee, unahitaji study yake ya kipekee utaleta matokeo tunayoyataka. Tukienda hivi, wachumi hawa wamesoma sana wamekuja na makabrasha na hawa si ndiyo walioshauri bajeti iliyopita, si ndiyo hawa wanaokuja na vyanzo vya mapato vilevile!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme kabisa, tunahitaji a serious discussion, we need serious research kuhusu uchumi wa kipekee wa Kitanzania unapoishi na watu wanaoishi chini ya dola wakati huohuo wakaweza kusomesha, wakaweza kula, wakaweza kujenga, hii hali sio ya kawaida. Tutadanganyana tu na haya makaratasi hapa, tunasema uchumi umepanda, uchumi umeshuka, tutapelekwa kulia, tutapelekwa kushoto hatutafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikasema, kinachotutesa sisi na narudia tena, ni kufikiri Kitanzania, kuishi Kitanzania lakini tunadhani kwamba mifumo ile ya Ulaya ya uchumi ndiyo inayofaa kutafsiri uchumi wetu. Mipango ya Ulaya ya kukuza uchumi na projection zao ndiyo tunadhani zinatufaa kwa Watanzania, zimefeli na hazikuwahi kufanikiwa kutuletea majibu yanayotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kaangalie hali ya maisha ya kawaida ya Mtanzania, sawa, kuna vitu kama nchi lazima tuvifanye, tukivifanya hivyo tuna uhakika ile gap inayoonekana watu kuongezeka kuwa maskini kwenye maandishi ikapotea ni kwenye suala la infrastructure. Bajeti zijazo zijielekeze kwenye infrastructure, reli ya kati iimarike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi reli ya kati ilipokuwa inafanya kazi mtu wa maisha ya chini alikuwa anakula wale dagaa wanaotoka Kigoma, walikuwa wakifika Dar es Salaam ndiyo chakula kinachokuwezesha kuishi, unanunua kilo moja kwa Sh. 200, 300 leo hii kilo moja ya dagaa wa Kigoma anayeweza kula ni from royal family, kwa nini? Kwa sababu reli ya kati imeshindwa kuleta ule mtiririko uliokuwa una-cover matatizo mengine. Sasa tukiimarisha reli ya kati haya mambo mengine yote yatakwenda vizuri. Tukifungua barabara, kama nilivyosema, leo mimi nikitoka Dar es Salaam kwenda Mbinga sihitaji kupita Iringa, nitapita Masasi nitaongea na Ndugu yangu Mheshimiwa Mwambe dakika mbili nasonga mbele naingia Mbinga haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali kama hii, leo inapasuliwa barabara hii ya Arusha kwa kupitia Msalato unapunguza kilometa nyingi ambazo tulikuwa tunazitumia kwenda Singida. Hali kadhalika ukatoboa barabara ya Kigoma – Mpanda – Sumbawanga na ukatoka Sikonge – Mpanda ukaja Tabora utaratibu unakuwa mzuri. Haya ndiyo maendeleo, tusiende kwenye hizi figures ambazo zinaonesha namba, hazina uhalisia katika hali ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nakubali maendeleo ni watu, hatuwezi kusema kuna maendeleo ya vitu tukayatofautisha na maendeleo ya watu. Tukawa na barabara, viwanda, watu wakawa wanasononeka hawana furaha wanaishi maisha ya hovyo, haya siyo maendeleo. Maendeleo ya nchi yetu ni maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante

The Media Services Bill, 2016

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru na mimi kupata nafasi ya kuchangia muswada huu jioni ya leo.
Mheshimiwa Mwneyekiti, kwa muda mrefu sana tasnia ya habari haikuwahi kupata hadhi inayostahili ndani ya nchi yetu. Pamoja na kazi nzuri ya tasnia ya habari katika kuhabarisha, kufundisha, kukosoa, kuwasaidia watu wenye matatizo kwa kuvumbua changamoto mbalimbali hata kufikia hadhi ya kuitwa muhimili wa nne wa dola, bado tasnia hii haikuwahi kulindwa, haikuwahi kuenziwa, haikuwahi kupata heshima inayostahili; moja, kwa mwandishi wa habari mwenyewe; pili, kwa chombo cha habari; na tatu, kwa mmiliki wa chombo cha habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na tasnia nyingine kama uhandisi, madaktari, wahasibu, wanasheria ambao wana chombo chao maalum kinacho-govern their conduct na kinachowalinda waendelee kulinda ile profession yao, wakue na watoe huduma bora. Hii tasnia kubwa ya habari haikuwahi kupata heshima hii. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza ndani ya nchi hii, heshima ya tasnia ya habari inapatikana. Kwa takribani miaka 23 toka tumeanza kusema kupigania haki za waandishi wa habari, haki za vyombo vya habari, tumeongea from unseen morning to unseen night bila kupata ufumbuzi wa kudumu kwa hawa waandishi wa habari. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Walatini wana msemo; “verba volant, scripta manent” wakimaanisha spoken words fly away, but written remain. Kwa nini nasema hivi? Kwa miaka 23 mnasema kuhusu haki za waandishi wa habari, you don’t write, you don’t put down, you don’t put in laws na matokeo yake wanalalamika na hamuwasaidii. Leo Serikali kwa mara ya kwanza inakuja na kujibu hili. Maneno tunayoyaongea yanapepea hewani, lakini tukiyaweka katika maandishi yanadumu. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kuisaidia tasnia hii ya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu tutakaoenda kuupitisha unatutatulia matatizo yote tuliyokuwa tukiyaongea kutokana na upungufu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. Kwa muda mrefu tumelalamika hapa Waziri anaweza akaamka asubuhi akalifungia gazeti. Kwa kupitia muswada huu, kuna marekebisho yaliyofanyika kwa kuweka Bodi. Sasa hivi tuna Bodi ya Ithibati, Mfuko wa Mafunzo na tuna Baraza Huru la Habari. Haya yote ni mambo mapya yanapatikana kwenye sheria hii yaliyotokana na upungufu wa sheria zilizopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema sasa tofauti ya uelewa ambao ninao na ninaamini wanaelewa lakini wanafanya makusudi kuwa hawaelewi; ni kwamba tunachokifanya hapa ni kufanya a total transformation ya tasnia ya habari from occupation to profession. Kuna watu hapa wameongea maneno mengi mimi mpaka nikachoka, nikasema dah, hili mpaka kaka yangu Mheshimiwa Zitto kalisema? Kwa jinsi ninavyomfahamu kaka yangu Mheshimiwa Zitto siyo mvivu wa kufikiri, anakuja anasema time is standing still, ana-compare mwaka 1961 kipindi wasomi wanahesabika, leo hii turudi kule tulipotoka? No bwana hatuwezi kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto ametoka hapo amekwenda na mfano wa pili wa Mheshimiwa Harrison Mwakyembe aliyeanza na tasnia ya habari akaenda akafika akawa mwanasheria. Tafsiri yake ni nini? Harrison Mwakyembe angekuwa mwandishi wa habari na angeendelea kuwa na taaluma ya uandishi wa habari, leo asingekuwa lawyer. Tunachokifanya hapa leo, tunataka waandishi wa habari wote wawe…
Siyo tafsiri yake wawe ma-lawyer, wawe na hadhi inayofanana na ma-lawyer; wawe na hadhi inayofanana na madaktari; wawe na hadhi inayofanana na ma-engineer. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo tunasema…, aah my God! (Kicheko/Makofi)
Anasema uandishi wa habari is passion. Mimi nikusaidie kaka yangu, kila kitu ni passion. Passion ni wito. Mcheza mpira, ana passion; mwanasheria, ana passion; daktari ana passion; kila mtu ana passion. What we are doing here ni kuifanya ile passion iwe profession. Ndiyo maana tumekuja na muswada. Msituondoe kwenye mstari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa watu siyo kwamba hawajui, wanajua ila wanafanya kusudi. Hivi kweli hakuna tofauti kati ya journalist as a profession na mtu mwenye uwezo wa kuandika habari? Tofauti ipo clear.
Huyu journalist tunamfanya anakuwa na profession kutokana na taaluma yake. Hii haizuii mawazo yako Mheshimiwa Zitto kama mchumi, haizuii mtu mwingine yeyote mwenye mawazo yake ya kilimo akayaandika kama makala yakatumika kwenye vyombo vya habari. Sasa kwa nini mnapotosha mambo ambayo yapo wazi dhahiri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu nahisi mnataka uandishi wa habari uendelee kuwa kindergarten usifike university. Tunachokifanya leo ni kuvusha daraja kuwaondoa waandishi wa habari kutoka eneo moja ambao mnawachukualia wa kawaida, tena mpaka mnawaita majina ya hovyo makanjanja, sasa wanakuwa na taaluma inayoheshimika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tofauti kubwa sana nimeisema kati ya reporter, radio presenter na mwandishi wa habari. Mimi nikikaa kwenye tv ku-broadcast kuelezea kipindi fulani I am not a journalist, mimi ni presenter.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa sasa msitake kwa sababu kuna watu hawakusomea uandishi wa habari, kwa karama ambazo Mwenyezi Mungu aliwaumba, wakikaa kwenye tv wanaongea vizuri sana, wakikaa kwenye redio wanaeleweka, haimaanishi kwamba wale hawatafanya kazi zile. Hii ndiyo hali ambayo ukiangalia muswada kuanzia page ya kwanza mpaka mwisho haijakataza mambo hayo, haijakukataza Mheshimiwa Zitto na taaluma yako ya uchumi kutoa mawazo ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, umemtolea mfano Mbarak Islam, yule alietoa taarifa ile ya kwanza. Yule katika lugha ya kawaida ni source ya taarifa, source ya taarifa, siyo taaluma. Mimi naweza nikawa source ya taarifa, wewe unaweza ukawa source ya taarifa na mtu yeyote anaweza akawa source ya taarifa. Kwa hiyo, msichanganye haya mambo eti ionekane kwamba hii Serikali ina nia mbaya kwenye muswada. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwaambie waandishi wa habari, mimi nawapenda sana na kwenye hili tunawaondoa hapa mlipo muwe kwenye taasisi inayotambulika kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ndugu yangu Mheshimiwa Kubenea umeongea kuhusu shares; unajua mambo mengine haya, kabla hujaongea soma soma kidogo. Shares za nani? Zile shares hazisemi kwamba mimi hapa nikifungua gazeti langu na mwenzangu hapa shares zisomeke. Shares zinazoongelewa hapa ni zile za mmiliki anayetoka nje ya nchi; mambo mawili tofauti. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hili linafanyika? Kwa nini tunasema siku zote; tena hawa wanaosema, wamekuwa wakisema mashirika ya nje yakiingia humu ndani yana-control each and everything. Kinachofanyika hapa ni kuwawezesha Watanzania wawe na sauti ya asilimia 51 dhidi ya 49 ya wale wageni wanapokuja kuanzisha chombo cha habari. Hii ni hali ya kawaida kabisa. Nilitegemea washangilie na kufurahi sasa Serikali inataka ku-empower Watanzania wawe na uwezo wa kumiliki vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno haya machache naomba niseme yafuatayo; huu muswada ni mzuri sana, nawaomba wote tuunge mkono akiwemo na dada yangu Mheshimiwa Esther naye aunge mkono.
La pili, lazima tutofautishe tunachokifanya hapa, is not a status quo, siyo hadithi ya miaka 40, tunataka tutoke hapa tulipo twende mbele zaidi. Kama kuna maswali yoyote yanayotokana na modality, piga hatua kwanza, time can’t stand still. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Juma Hamad Omar

Ole (CUF)

Contributions (1)

Profile

Hon. Suleiman Masoud Nchambi

Kishapu (CCM)

Supplementary Questions / Answers (4 / 0)

Contributions (3)

Profile

View All MP's