Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Daimu Iddi Mpakate

All Contributions

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa, naomba nitoe shukurani kwa kuniteua leo kuwa mchangiaji katika bajeti ya kilimo.
Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo nikiwa salama kuongea katika Bunge lako kwa mara ya kwanza. Pia napenda niwashukuru wapiga kura wangu wa Tunduru Kusini na Tunduru kwa ujumla walioniwezesha leo kuwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kukosa fadhila, nakishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua kuwa mgombea wa Jimbo la Tunduru Kusini na hatimaye kuhakikisha kwamba ninashinda na leo niko ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, napenda kumpongeza Waziri wa Kilimo kwa hotuba yake nzuri ambayo ameiwasilisha leo. Nami napenda sehemu ya hotuba hiyo nichangie mambo mawili matatu ambayo najua yakirekebishwa, basi utendaji wetu utaendelea vizuri na wakulima wetu watapata manufaa mazuri na kulima zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ni suala la pembejeo. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri amelieleza vizuri. Kero ya voucher imekuwa ni donda ndugu, kwa kweli lilikuwa linatugombanisha na wakulima wetu; mahali penye kaya 2000, kaya 30 zinapata voucher, matokeo yake inaleta migongano katika vijiji vyetu.
Nashukuru sana kwa kuliona hili, lakini pamoja na kuahidi kwamba pembejeo zitauzwa kama soda, ni vyema Mheshimiwa Waziri uhakikishe kwamba unaweka bei dira, bei elekezi ya hizo pembejeo kama wanavyofanya EWURA ili kila mkulima ajue kwamba katika eneo lake pembejeo itapatikana kwa bei fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kufanya hivyo, wafanyabiashara ambao ni mawakala watakaosambaza pembejeo zile, watatumia mwanya ule ule kuendelea kuuza bei juu kuliko vile ilivyokusudiwa na Wizara. Naomba sana jambo hili litiliwe mkazo ili kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata fursa nzuri ya kupata pembejeo kwa bei nzuri na mahali walipo ili kuendeleza kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la muhimu ni suala la umwagiliaji. Ninachojua mimi katika dhana ya umwagiliaji ni kuhakikisha kwamba kilimo kinaendelea through out the year, kwamba mkulima anakuwa analima kifuku na kiangazi, lakini umwagiliaji uliopo sasa katika maeneo mengi, kilimo kile kinakuwa ni kilimo cha umwagiliaji wakati wa kifuku tofauti na kusudio lile la kulima through out the year. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wataalam wetu wanatakiwa waende mbali zaidi kuhakikisha kwamba ile mifereji inayotengenezwa kwa ajili ya kifuku peke yake, tuone namna nyingine ya kutengeneza mifereji kwa ajili ya kulima kipindi cha kiangazi. Maeneo mengi yaliyotengenezwa kwa ajili ya kilimo hiki yanatumika kifuku badala ya kiangazi kama inavyokusudiwa na dhana yenyewe ya umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba nielezee suala mtambuka la ushirika. Kwanza naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mmojawapo wa watumishi wa ushirika ndani ya miaka nane katika sekta ya korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri amesema kuhusu kuanzisha commission ya ushirika. Ni kweli ushirika umedorora lakini tunasahau wapi tulipojikwaa, tunaangalia tulipoangukia. Kamisheni hii kwa kweli haina nguvu kwa mujibu wa taratibu za kikazi. Utakuta kamisheni haina watumishi mikoani; kamisheni haina watumishi Wilayani, inategemea watumishi kutoka Halmashauri za Wilaya ambao katika utendaji wa kazi wanawajibika kwa Wakurugenzi wa Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hili ni tatizo, utendaji hauendi sawasawa kama kamisheni ilivyokusudia kwa ajili ya kufufua ushirika. Mbaya zaidi, hata hao watumishi waliokuwepo katika Halmashauri, hawatoshi kusimamia ushirika. Ni hali ya hatari, utakuta Wilaya ina vyama 20, 40, SACCOS pamoja na Vyama vya Wakulima, lakini Afisa Ushirika utamkuta mmoja au wawili. Inakuwa ni ngumu! Ni kazi kubwa kwa Maafisa Ushirika kuhakikisha kwamba vyama vile vinakwenda kama inavyokusudiwa na kama sheria inavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, commission ipewe nguvu, iwe na watumishi wa kutosha mpaka Wilayani ili waweze kusimamia Vyama vya Ushirika vizuri viweze kuwasaidia wakulima wao. Tunajua bila ushirika maeneo mengi kwa kweli inakuwa ni tatizo kubwa ingawa wenzangu wameeleza, ushirika ni jumuiya ya hiari, kwa hiyo, wanaushirika wenyewe wafanye yale yanayotakiwa ili kuhakikisha ushirika unaboreshwa kama inavyoeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo jambo la ushirika, kuna jambo la mikopo. Nashukuru ndugu yangu ameeleza kuomba kupeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ruvuma ni eneo mojawapo ambayo wanazalisha sana mahindi, lakini tukiangalia suala la mikopo hali siyo nzuri kwenye Benki zetu za kawaida. Riba inakuwa kubwa haimwezeshi mkulima kukopa na kupata return ya kuweza kurudisha faida na yeye mwenyewe kupata chakula kwa ajili ya maisha yake na familia yake ilivyo.
Tunaomba sana suala la benki lifanyiwe hima kuhakikisha kwamba Benki za Kilimo zinakwenda mikoani ili kuweza kuwasaidia wakulima walio wengi kwa kupata mikopo iliyokuwa nafuu ili waweze kuendeleza kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni suala la uhifadhi wa chakula, ni aibu! Nimesema nimekuwa kwenye sekta ya kilimo kwa muda wa miaka nane. Ukienda vijijini maghala ya kuhifadhia mazao hakuna na ndiyo maana utakuta sehemu kubwa iliyopo tunazalisha vizuri lakini uhifadhi wa mazao unakuwa ni tatizo. (Makofi)
Kuhusu ile programu ambayo ilikuwepo miaka ya nyuma ya kuhakikisha kwamba kila kijiji kinapata ghala la kisasa, basi naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja, atuhakikishie angalau vijiji vile ambavyo vinaonekana uzalishaji wa mazao ni mkubwa waanzishiwe miradi ya kujenga maghala kwa ajili ya kuhifadhi mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, kwa hayo machache, nashukuru sana kwa kuniruhusu kuchangia mawili, matatu, ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu bure ukweli kabisa sera hii imezibagua shule za Kata za kutwa na zile shule za Serikali ambazo zinahudumiwa kwa chakula kwa mabweni yaliyojengwa na wananchi na watoto/wanafunzi kukaa bweni wakati shule hizo bado zinaitwa za kutwa na hawapewi fedha za kununuliwa chakula kutoka nyumbani.
Hivyo ni vema suala hili likaangaliwa upya namna ya kusaidia shule hizo zenye mabweni zipewe chakula kama nyingine za Serikali. Wapiga kura wetu wanapiga kelele juu ya ubaguzi huo wa shule za bweni za wananchi hivyo kuongeza mzigo wa michango ya chakula. Shule hizo ni nyingi sana zilizopo kwenye Kata mbalimbali nchini kuliko shule za Serikali za bweni mfano Semeni, Likumbule, Wamasakata, Walasi, Malumba na Mbega Mchiteka Wilayani Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya posho za likizo za Walimu na madai ya zabuni mbalimbali. Kuna madai mengi hawajalipwa walimu katika shule mbalimbali kutokana na posho za likizo, uhamisho na posho nyingine mbalimbali. Kuna chuo cha maendeleo Nandembo watumishi wanadai 7,164,000 na wazabuni wanadai 5,447,000 na wametishia kusitisha kutoa huduma zao na kuna mtumishi mmoja Saidi Salanje alifariki mwaka 2011 lakini warithi wale hawajapata mafao yao ya kiinua mgongo mpaka leo hii. Ni vema madai hayo yakashughulikiwa mapema ili kuondoa malalamiko na kero zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukarabati shule za sekondari za Serikali, majengo ya shule za sekondari Tunduru, masonya na Frank Wiston zilijengwa muda mrefu zaidi ya miaka 30 iliyopita lakini hakuna ukarabati wowote uliofanyika katika majengo na yanatishia usalama wa wanafunzi na walimu wao. Hivyo, tunaomba majengo hayo yafanyiwe ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari; Kuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa sekondari hasa wa sayansi karibu shule zote za sekondari zilizopo Tunduru na walimu wa shule za misingi takribani mia tano jambo ambalo linashusha kiwango cha ufaulu wa watoto wetu katika masomo ya sayansi. Tunaomba tupewe kipaumbele cha kupewa walimu katika ajira ya mwaka 2016/2017 ili kupunguza pengo hilo na mwaka 2015/2016 hatukupewa hata mwalimu mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa vya kufundishia tunaomba Serikali kuliingilia kati suala la vifaa vya maabara ili watoto/wanafunzi wajifundishe kwa vitendo badala ya kuwaachia Halmashauri zetu, kwa sababu uwezo wa Halmashauri nyingi kupata vifaa hivyo kwa kutumia mapato ya ndani ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuboresha walimu kimasomo. Tunaomba Serikali itoe fursa kwa walimu wa vijijini kujiendesha kielimu ili kuwapa motisha wa kazi zao za kila siku. Ni vema kuimarisha vyuo vya Ualimu ili kupewa elimu na ujuzi wa kufundishia.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba ya Viwanda na Biashara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani inatakiwa ifanyiwe marekebisho kutokana na upungufu, kwani ilishindwa kumfidia mkulima pindi mzigo wake ulivyopotea katika maghala makuu. Mzigo ukipotea ghala kuu sheria inamtaka mtunza ghala amfidie mweka mali, lakini sheria haimlazimishi kulipa, matokeo yake mweka mali anakuwa anadai mali zake bila mafanikio. Hivyo ninaomba sheria hii irekebishwe ili itoe msisitizo wa mtunza ghala kulipa mara moja pindi akipoteza mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tozo nyingi sana zinazotolewa na Serikali pamoja na Halmashauri bila kumfahamisha tozo hizo wakati mfanyabiashara anapata leseni ya biashara. Ni vyema mfanyabishara apewe orodha ya tozo zote anazopaswa kulipa wakati anapewa leseni ya biashara. Kuna ule ushuru wa vipimo, kodi ya majengo, ushuru wa mazingira, tozo mbalimbali kama EWURA, Halmashauri na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna ukiritimba wa kupata vibali mbalimbali. Ni vyema mfanyabiashara akahudumia sehemu moja ili kuharakisha uwekezaji wa wafanyabiashara. Kwa mfano, vibali vya ujenzi, vibali vya mazingira, vibali vya Taasisi mbalimbali kama EWURA na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingi vimebinafsishwa, lakini wafanyabiashara wamebadili matumizi ya viwanda hivyo bila kujali kuwa viwanda hivyo vilijengwa kwa madhumuni fulani ili kuwezesha mazao yetu kuongeza thamani. Ni vyema viwanda hivyo vifufuliwe kama ilivyokusudiwa ili kuongeza ajira kwa vijana wetu. Tuna malighafi nyingi sana tunazalisha, lakini tunauza ghafi badala ya kuongeza thamani ya mazao hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna ucheleweshaji wa huduma mbalimbali katika vitengo vilivyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwa ni pamoja na kufumbia macho sekta ndogo ya biashara ndogo ndogo (Wamachinga) ambao wanaendesha biashara bila utaratibu maalum ambao ungewezesha kundi ili kuwa na leseni za biashara na kuiongezea mapato Serikali kupitia leseni hizo.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia hoja ya Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Walemavu, Wazee pamoja na Watoto. Kwanza kabisa, napenda niwapongeze Mawaziri hawa wote wawili kwa ku-translate Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika hotuba yao iliyofanya kila mmoja asisimke. Nasi ni wajibu wetu kuchangia kuongeza nyama ili pale ambapo pamepungua waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, naungana na wasemaji wenzangu waliozungumza awali kuhusu suala la wazee; tumezungumza bima, tumezungumza suala la dirisha maalum la wazee, lakini tunaleta msisitizo mkubwa kwa sababu Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumeinadi sana vijijini kuhusu pensheni ya wazee zaidi ya miaka 65. Katika maelezo yake au hotuba yake haijaonyeshwa vizuri ni lini program hii itaanza au ikoje ili Waziri atakapokuja atueleze hawa wazee wataanza lini kufikiriwa suala hili la pensheni ya wazee wenye umri zaidi ya miaka 65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nitazungumzia suala la Hospitali ya Wilaya ya Tunduru. Hospitali hii ni ya muda mrefu, tangu miaka ya 1990 huko, lakini hadi hivi sasa ina majengo yaliyochakaa na mbaya zaidi hakuna wodi ya upasuaji. Wagonjwa wakipasuliwa, wakitoka theater wanachanganywa na watu wengine pamoja na madonda yao waliyokuwa nayo. Hii ni hatari, inahatarisha zaidi afya ya wale wagonjwa ambao wanafanyiwa upasuaji. Kwa hiyo, naomba Serikali ifikirie namna ya kuweza kusaidia hospitali ile kupata wodi kwa ajili ya wagonjwa ambao wamefanyiwa upasuaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kulikuwa na chuo pale ambacho kilikuwa kinafundisha Manesi mbalimbali ambao walikuwa wanatoka vijijini, lakini chuo kile kiliungua moto zaidi ya miaka kumi iliyopita na mpaka leo majengo yale hayajafanyiwa renovation na kile chuo kimekufa moja kwa moja. Ile nafasi ambayo walikuwa wanapata vijana wa Tunduru kusoma pale na baadaye walikuwa wanaajiriwa na zahanati zetu zilizoko vijijini kwa mikataba na vijiji wakisubiri ajira ya Serikali Kuu, sasa imekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atupe majibu halisi, chuo kile ni lini kitakarabatiwa ili kiweze kuwafundisha vijana wetu ambao wanaweza kusaidia jamii zetu kwa sababu tunalalamika sana kwamba wahudumu ni wachache katika zahanati zetu na mbaya zaidi Wilaya ya Tunduru, pamoja na kuwa na zaidi ya vijiji 150, lakini kuna zahanati 49 tu, vituo vya afya vitano na gari ni moja tu ambalo lipo kwenye Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, akinamama wanatembea umbali wa zaidi ya kilometa 30 kufuata huduma ya afya, ni mbaya sana. Naomba sana, pamoja na kwamba Wizara ya Afya inatekeleza sera, naamini pacha wake ambaye ni Serikali za Mitaa, analijua hili na naomba alifahamu na ikiwezekana baadaye waweze kufika kule waangalie hali mbaya ya Wilaya ile; kwa sababu Wilaya ile ni kubwa ukilinganisha na Mkoa wa Mtwara. Wilaya ya Tunduru ni kubwa na Mkoa wa Mtwara una Wilaya tano. Naomba sana hili tufikiriwe kwa sababu tuko katika hali mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia katika hotuba hii ni suala la wafanyakazi wa ustawi wa jamii. Ni kweli ni tatizo, kama nilivyochangia katika Idara ya Kilimo, suala la ushirika linafanana sambamba na ustawi wa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara hii tumeisahau sana; watumishi ni wachache, huduma hakuna, usafiri hakuna, incentives hawapewi; sasa tunategemea vikundi vya akinamama vya maendeleo vyote vipate huduma kutoka kwa hawa watumishi wa ustawi wa jamii, lakini bahati mbaya nao wako katika hali mbaya, hoi, huduma hawapewi. Naomba sana wathaminiwe ili waweze kufanya kazi yao nzuri ya kuwasaidia ndugu zetu huko vijijini waweze kujikwamua kiuchumi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho naomba nichangie suala la upungufu wa madawa. MSD ni tatizo. Mara nyingi sana dawa nyingi zinazofika katika Hospitali, Zahanati zetu na Vituo vya Afya, zinakuwa zimepitwa na wakati. Sijajua ni kwa nini muda mwingi dawa zile zinakuwa zimepitwa na wakati. Mbaya zaidi wananchi wanasikia namna MSD wanavyoteketeza dawa ambazo zimepitwa na wakati, huku vijijini hakuna dawa. Naomba sana suala la MSD kupata dawa na kusambaza kwa wakati liwe la muhimu sana ili watu wetu wapate huduma ya dawa kwa wakati ili kufufua matumaini ya watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba sana Vyuo vya Maendeleo ya Jamii. Tunduru tuna Chuo cha Maendeleo ya Jamii, kipo pale Nandembo, lakini hakina huduma. Kwa mwaka kinafundisha chini ya watu 200. Sasa sijui maendeleo haya tunayoyataka kwa wananchi wetu wakati chuo kile hakiwezi kuchukua watu zaidi ya 200 kwa mwaka! Kwa kweli ni hatari! Tunaomba sana Serikali itilie mkazo chuo kile iweze kuwapeleka wataalam wazuri, iwapelekee fedha waendeshe program zao za kila siku ili watu wa Tunduru nao waweze kufaidika na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba sana Serikali iangalie suala la usafiri katika zahanati zetu zilizoko na vituo vya afya ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, upungufu wa Maafisa Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ni mkubwa sana kiasi kwamba inasababisha maeneo mengi kutokupimwa kwa wakati na watu kujenga holela. Hata hivyo, wafanyakazi waliokuwepo wanashiriki kwa namna moja au nyingine na kujihusisha na rushwa kwa kupima maeneo ya wazi hata maeneo ya hifadhi ya barabara kama ilivyojitokeza kwa mwekezaji mmoja anayeitwa Cross Road Petrol Station kujenga petrol station eneo la barabara. Kwa mujibu wa mchoro wa awali sehemu hiyo iliwekwa kwa ajili ya kutengeneza junction ya barabara kuu ya Masasi - Tunduru - Songea na barabara ya Bomani jambo ambalo limesababisha mgogoro mkubwa na mkandarasi anayejenga kwa lami barabara ya Tunduru - Matemanga ambapo mwekezaji huyo anadai fidia kwa vile ana hati miliki ya eneo hilo ingawa ni sehemu ya hifadhi ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ucheleweshaji wa michoro/ramani za viwanja vilivyopimwa ni kero kubwa sana. Tangu mwaka 2012 mchoro wa viwanja vilivyopimwa bado haujarudi kutoka Wizarani ili walionunua viwanja waanze kutafuta hati ya viwanja vyao. Kwa hiyo, ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Tunduru. Mimi nikiwa mmojawapo nimeshindwa kupata mkopo kwa kukosa hati ya nyumba yangu kwa vile mchoro bado haujapitishwa na Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, tatizo la viwanja vilivyopimwa kupewa watumishi badala ya wananchi wa kawaida. Watumishi hao baadaye huviuza viwanja hivyo kwa bei ya juu kwa wananchi wa kawaida wakati wao wamevinunua kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, mipaka ya vijiji inavunjwa sana na watumishi wa ardhi kwa kusogeza na kutoa beacon zilizowekwa wakati vijiji hivyo vimeanzishwa na kusababisha migogoro ya kijiji na kijiji. Kwa mfano kijiji cha Namasalau na Kitando, Semli na Chikomo/Mchesi/Muungano suala hili limeleta ugomvi wa wakulima kwa wakulima kutokana na Ofisi ya Ardhi kutotoa ramani za awali za vijiji hivyo. Hivyo, ni vyema Ofisi ya Ardhi wakatoa ramani ya Wilaya ya Tunduru kwa kila kijiji ili wajue mipaka yao ya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi. Mikopo mingi ya mabenki kwa wafanyakazi inatolewa kwa walio Dar es Salaam tu, wa mikoani ni wachache sana ambao wanafanikiwa kupata mikopo hiyo. Hivyo ni vyema Serikali ikasimamia mabenki waweze kukopesha wafanyakazi waliopo mikoani na wilayani ili waweze kujenga sehemu za kuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, Shirika la Nyumba ya Taifa lijielekeze kujenga nyumba wilayani na mikoani ambako mahitaji ya makazi kwa ajili ya wafanyakazi ni makubwa sana. Shirika lijielekeze huko badala ya kuendelea kujenga nyumba Dar es Salaam na miji mikuu ya majiji na manispaa pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, nashauri Wizara iondoe wafanyakazi wasio waadilifu wanaotoa hati mbili katika kiwanja kimoja; wanaopima maeneo ya wazi na kubadilisha matumizi bila utaratibu; wanaodai rushwa ili kuwapa huduma wananchi ya kupatiwa hati ya viwanja vyao kwa mkoani na wilayani. Pia kupata hati ya kiwanja ni gharama kubwa sana na inachukua muda mrefu sana, naomba nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nane, maeneo yanayochukuliwa na Halmashauri wananchi walipwe kutokana na thamani ya ardhi kwa wakati huo badala ya kuangalia mazao pekee yaliyoko kwenye kiwanja hicho.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia bajeti hii ya Serikali. Katika mchango wangu kwanza naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, nitaongea maneno mawili matatu kuhusiana na kilimo, ushirika pamoja na tozo za zao la korosho katika maeneo yale ambayo yanalima korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kuzungumzia suala la ushirika ninaamini Sheria Na. 6 ya mwaka 2013 ilianzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika, lakini katika bajeti yetu ya kilimo ipo chini ya asilimia tano, sidhani kama Tume hii ya Maendeleo ya Ushirika imepewa kipaumbele kwa ajili ya kuendeleza wakulima wetu, kwa sababu wakulima walio wengi vijijini wanategemea sana ushirika ili kupata masoko ya mazao yao pamoja na pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutegemea huko, jambo kubwa lililopo kwenye Tume ya Ushirika, ninaomba Serikali tangu sheria hii imeanza huu ni mwaka wa tatu Tume ile haina Mwenyekiti wa Tume imekuwa ni jina peke yake, Makamishna hawapo. Naomba sana katika bajeti hii iangalie namna ya kuiwezesha Tume hii iweze kufanya kazi kwa kuteua Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika na kupata Makamishna wake ili waweze kusimamia ushirika usimame vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna matatizo mengi sana ya ushirika, lakini yanatokana na uongozi kukosa viongozi walio imara katika Idara ya Maendeleo ya Ushirika. Pamoja na hilo watumishi waliopo kwenye ushirika ni wachache, ninaomba sana kwa sababu tunapitisha bajeti hii basi waliangalie namna ya kuongeza watumishi kwenye Idara hii ya Tume ya Ushirika ili waweze kusimamia Vyama vyetu vya Ushirika viweze kufanya kazi vizuri. Kwa mfano, vyama vya Mkoa wa Mtwara, Lindi, Pwani Ruvuma ambavyo vinajihusisha na shughuli za biashara ya korosho vinatumia zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya biashara ya korosho, usimamizi haupo makini kwa kuwa Maafisa Ushirika wamekuwa ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba wanaongeza watumishi walio na elimu ya ushirika pamoja na uwezo wa kufanya na kusimamia ukaguzi wa vyama vya ushirika mara kwa mara, kwa sababu vyama hivi vina-transact fedha nyingi sana kinyume na Sheria ya Fedha inavyotaka. Vyama vyetu vya Msingi viongozi walio wengi ni darasa la saba, mtu wa darasa la saba anafanya transaction ya shilingi bilioni mbili, bilioni tatu! Kwa kuwa Maafisa Ushirika ndiyo wasimamizi tunaomba Maafisa Ushirika wenye taaluma ya kusimamia na kukagua vyama hivi vya msingi waajiriwe waweze kuendelea kusimamia vyama hivi ili tupunguze malalamiko ya watu na wakulima wengi huko vijijini hasa kwenye Mikoa ya inayozalisha korosho na Mikoa inayozalisha tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja naomba niende kwenye tozo ya zao la korosho kama ilivyopendekezwa katika bajeti hii. Nakubaliana kwenye mchakato wa kutoa tozo katika unyaufu. Nimekuwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani zaidi ya miaka nane, mfumo ulivyoanza kulikuwa na tozo 17, taratibu namna utendaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani ulivyoendelea zimepunguza zile tozo mpaka zikafikia saba kwa umuhimu wake ili kuweze kumsaidia mkulima aweze kupata hela yake. Kwa mapendekezo yaliyojitokeza naomba nieleze yale ambayo ninayaona mbele ya safari yataleta mkanganyiko katika kutekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni suala la ushuru wa kusafirisha korosho wa shilingi 50. Mfumo wa stakabadhi ghalani unataka ghala lolote lenye uwezo wa kuhifadhi kwa wakati mmoja tani 200 uweze kupewa kibali cha kuhifadhi korosho. Maghala yetu yaliyopo vijijini mengi yapo chini ya uwezo huo. Mbaya zaidi ubora wa yale maghala hauruhusu kuifadhi korosho kwa muda mrefu; mbaya zaidi maghala yale hayana umeme, ni vumbi tu, hakuna chochote ambacho kinaweze kustahili kuweka korosho kwa muda mrefu ili mfumo wa stakabadhi ghalani uweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo tunalalamika wataalam wa ugani hawapo katika maeneo mengi, kwa kuhakiki ubora kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani tunahitaji Maafisa Ugani katika kila Chama cha Msingi. Katika sekta ya korosho kuna vyama 739 ambavyo vinajihusisha na biashara ya korosho, kwa hiyo, tunahitaji Maafisa Ugani 739 ili kuhakikisha kila chama kinakuwa na Mhakiki Ubora ambao utasadia kuhakikisha zao linakwenda v izuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi tunahitaji kipimo kinachotumika kupima ubora wa korosho kwa content ya moisture na nut counting pamoja na ubora wenyewe wa korosho kama ilivyo kile kipimo kinauzwa shilingi milioni sita kwa bei ya mwaka 2014/2015 tulinunua shilingi milioni sita, tunahitaji vipimo 739 kwa kila chama cha msingi ili viweze kuhakiki huu ubora. Kwa matatizo haya naamini kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani ukihamia kwenye maghala ya chama cha msingi moja kwa moja tayari tutawakaribisha Wahindi waende moja kwa moja kwenye maghala ya vyama vya msingi wawe wanatembea na moisture meter yao na watakuwa tayari kuwadanyanya wakulima wetu matokeo yake bei ya korosho itakuwa imeshuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kuondoa tozo hii maana yake tunaondoa wakulima kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani. Sambamba na hilo usimamizi wote unaofanyika kwenye vyama vya msingi unafanywa na Chama Kikuu kwa sababu Chama Kikuu ndicho chenye wahasibu…
Mheshimiwa Naibu Spika, ooh! Ahsante, naomba kuunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuchangia hotuba hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Tunduru kuna hifadhi kadhaa za misitu ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Selous iliyopo Jimbo la Tunduru Kaskazini pamoja na Hifadhi ya Misitu ya Mwambesi, Muhesi na kadhalika. Mwaka huu tembo wamekuwa wakipita katika hifadhi hizo na kuzagaa katika vijiji mbalimbali kama Mtina, Angalia, Mchesi, Kazamoyo na Kalulu na kuharibu mazao ya wananchi na wanadai malipo ya uharibifu huo wa tembo bila mafanikio. Kumekuwa na malalamiko mengi ya wakulima ambayo hayajafanyiwa kazi na Idara ya Wanyamapori, wanyama hao wanasumbua sana hivyo kuna uhitaji mkubwa wa watumishi wa Idara ya Wanyamapori ili kusaidia kufukuza wanyama hao waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Tunduru Kusini kumekuwa na kero kubwa ya fisi kuua watu. Mpaka sasa watu wawili wameuawa na fisi na watu wawili wameuawa na mamba katika Mto Ruvuma na wawili wamejeruhiwa lakini utaratibu wa kulipwa fidia unachukua muda mrefu. Mpaka sasa wahanga hao hawajalipwa, mbaya zaidi majibu wanayopewa yanawakatisha tamaa. Ni vyema utaratibu wa kuwalipa wahanga hawa wa wanyamapori ukafanyiwa marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TFS inashirikiana na Watendaji wa Vijiji kukata miti/magogo bila kufuata utaratibu wa kisheria na wanashirikiana na wafanyabiashara kukata miti hovyo bila kufuata utaratibu. Kwa mfano, katika Kijiji cha Semeni na Muungano, mfanyabiashara mmoja amekata magogo bila ridhaa ya mikutano mikuu ya vijiji hivyo na hata ushuru wa vijiji hivyo haujalipwa na kuna mgogoro mkubwa unafukuta na wanataka viongozi wa Halmashauri wa Kijiji na Mtendaji kupelekwa mahakamani. Hivyo, TFS inamaliza misitu ya Tunduru kwa kuruhusu magogo na mbao kukatwa hovyo bila kufuata utaratibu wa kisheria na sasa wanakata magogo Kijiji cha Machemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya hifadhi za misitu na wakulima. Ni vyema mipaka ya hifadhi hizo ikaangaliwa upya ili kutoa maeneo kwa wakulima kutokana na ongezeko la watu mfano Muhesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wa hifadhi na wanyamapori kutumia nguvu kubwa kuwanyanyasa watu kwa kuwapiga, kuharibu mazao yao, kuwanyang‟anya vitu vyao bila makosa. Ni vyema wakatumia ustaarabu katika kuwaelimisha wakulima badala ya kutumia nguvu. Ni vyema sheria ikatumika zaidi badala ya nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Operesheni Tokomeza. Jambo hili limekuwa mradi wa watu kwani kila mwaka wanaokamatwa ni watu walewale, wanateswa, wanapigwa, wanatoa rushwa ili waachiwe bila kupelekwa mahakamani. Ni vyema basi watuhumiwa wote wapelekwe mahakamani wakachukuliwe hatua badala ya kila mwaka wanakamatwa, wanateswa, wanawekwa ndani, wanatoa rushwa, wanaachiwa bila kuwapeleka mahakamani. Jambo hili linasababisha wananchi kuichukia Serikali yao bila sababu. Inaonekana kuwa umekuwa mradi wa watu fulani badala ya kufuata utaratibu. Ni vyema utaratibu wa kisheria ukafuatwa na haki za binadamu zikazingatiwa zaidi. Hakuna anayependa uharibifu unaofanywa, bila kuwachukulia hatua makundi mengine yanajitokeza, ila wakifungwa watu wataogopa kujishirikisha na biashara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kutenga maeneo ya hifadhi ni vyema elimu na mikutano ikafanyika katika vijiji husika ili kuondoa migongano na migogoro ya kutoelewa manufaa ya misitu. Naamini wananchi wakipewa elimu migogoro hii itapungua kwa kiasi kikubwa na hifadhi zisaidie vijiji vinavyopakana ili kutoa imani na nguvu ya watu wa maeneo hayo kulinda hifadhi hizo. Hifadhi zikisaidia vijiji jirani vijiji vingine vitahamasika katika kuanzisha hifadhi zao ili kupata manufaa wanayopata wenzao.

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naunga mkono hoja ya mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018. Pili, napenda kutoa mapendekezo au ushauri wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo liangaliwe kwa upana zaidi ili kumsaidia mkulima kupitia vyama vya ushirika waweze kusaidiwa kwa urahisi zaidi kwani takribani asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima. Hivyo, ili kuwahudumia vizuri inapaswa kuangalia chombo chao kinachowaunganisha kupitia vyama vyao vya ushirika vya mazao ili aweze kupata huduma kwa urahisi zaidi wakiwa pamoja kama elimu ya kilimo biashara, matumizi bora ya mbegu za mazao yao, kupata mikopo kupitia mabenki kwa kutumia vyama vya ushirika na mashamba yao kama dhamana ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia pembejeo za kilimo zipatikane kwa urahisi na kwa wakati ili wakulima waweze kuendana na msimu wa kilimo ulivyo katika maeneo mbalimbali. Vilevile aina ya pembejeo kwa kila eneo izingatiwe zaidi kulingana na udongo wa maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ujenzi wa maghala bora ya kuhifadhia mazao ni muhimu katika maeneo ya vijijini na Hifadhi ya Taifa ya Chakula kwa kuwa baada ya kuvuna vyakula hivyo ni vyema vikahifadhiwa vizuri kwa matumizi ya kipindi kijacho ambapo uzalishaji hamna. Ni vyema basi Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2017/2018 ukazingatia ujenzi wa maghala haya kwani kwa mfano maghala ya Hifadhi ya Taifa ya Songea mahindi mengi yapo nje ambapo yana hatari ya kuharibika katika kipindi cha mvua, asilimia 50 ya mahindi yamehifadhiwa nje maghala yamejaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuimarisha ushirika na mazao ni vyema basi Mpango wa Maendeleo wa Taifa ukatilia mkazo wa kuimarisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kuiwezesha kifedha. Ni vyema Tume hii ikaimarishwa kiutaalam katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Halmashauri za Wilaya kwa kuongeza watumishi wenye uwezo wa kusimamia ushirika na kurudisha imani ya wakulima kuamini vyama vyao vya ushirika. Ni vyema Makamishna wa Tume ya Ushirika wakateuliwa ili kuipa nguvu Tume hii kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kuimarisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika, ni vyema kuimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kwa kukiongezea uwezo kifedha na watumishi ili wapate muda wa kukagua vyama vya ushirika kila mwaka kwa maendeleo ya ushirika na wakulima wetu. Karibu wakulima wote wa Tanzania kwa njia moja au nyingine wanahudumiwa na ushirika wa mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu soko la mazao yetu, ni vyema Serikali ikasisitiza kuuza mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kama inavyofanyika katika mikoa inayolima korosho ambapo mafanikio makubwa yanaonekana kwa wakulima wa Mkoa wa Lindi na Mtwara na imehakikishia Halmashauri zetu kuwa na uhakika wa kupata ushuru wa mazao kupitia mfumo huu. Mkulima anakuwa na uhakika wa kupata malipo yake ya mazao kupitia mfumo rasmi wa kiuchumi. Naiomba Serikali kuangalia uwezekano wa mazao yote ya biashara na chakula kuingia katika mfumo huu kwani unaruhusu wanunuzi kushindana katika bei.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono hoja ya mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's