Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

All Contributions

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nianze kwa kumshukuru tena Mungu kupata nafasi hii kutoa na mimi mchango wangu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara na Mazingira, na ni Mwenyekiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe mchango wangu baada ya kuwa nimekutana na wadau wengi sana pamoja na Kamati yangu, tulikutana na wadau wenye viwanda, wafanyabiashara lakini pia tulikutana na mamlaka za udhibiti, ziko nyingi, tulikutana nazo kama 19 hivi. Tulikutana pia na waagizaji wa bidhaa na wale ambao wanapeleka bidhaa nje. Pia tulikutana na Wizara ya Viwanda na Biashara. Kila tulipokutana swali langu la kwanza kwa Waziri lilikuwa ni kwamba hivi tunafanya muujiza gani ili tuweze kutekeleza hii azma ya Mheshimiwa Rais ya kuwa na viwanda katika miaka 10 ijayo? Waziri ni shahidi na hata Wajumbe wenzangu ni mashahidi, tuliuliza sana swali hili na kwa kweli hatukupata jibu kwa maana kwamba yale yote yaliyowasilishwa kwenye Kamati ni business as usual. Kwa kweli ni vizuri sisi Wabunge wote wa Kambi ya Upinzani na sisi wa Chama cha Mapinduzi tutoe ushauri ambao utatutoa hapa tulipo utupeleke mbele. (Makofi)
Baada ya kutafakari, naomba niseme mambo kama sita hivi kwa kifupi, nadhani muda utanitosha. Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano una maneno mazuri sana na unasema vizuri sana, naturing industrialization in Tanzania. Maneno haya ni mazuri na Mheshimiwa Rais ameya-reflect wakati anafanya kampeni na sisi sote lazima tufikirie kwenda huko. Tukifanya kazi kama tunavyofanya tunaweza tusifike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ni lazima tuwe na quick wins sasa, vitu ambavyo tutavifanya kwa haraka tuone mabadiliko. Jambo la kwanza katika quick wins, ni viwanda vilivyopo na wafanyabiashara waliopo; tuwaondolee kero zao, tutengeneze mazingira mazuri, waweze kupanuka badala ya kufa. Walituambia wana kero sana na Waheshimiwa Wabunge wamesema, kero ni nyingi. Regulation ya udhibiti, kila mtu anakuja kudhibiti kiwanda kidogo. OSHA anakuja, nani anakuja mpaka unafunga. Kwa hiyo, Regulatory Authorities hizo bado zinachelewesha huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walisema mambo mengi; utitiri wa kodi, tozo na vitu vingi sana. Jambo lingine walilosema hao wenye viwanda vilivyopo, walisema service wanayopewa na hizi institutions, wakati mwingine wanazilipia kwa bei kubwa. Serikali inatakiwa itoe service hii bure kwa hivi viwanda ili viweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, walilosema miundombinu. Umeme unakatika sana. Pamoja na kwamba tuna mipango mizuri, tunaishukuru Serikali, lakini bado umeme uwe stable, reliable. Siyo unakatika! Kwenye kiwanda ukikata dakika tano, umechelewesha production kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia walisema kulinda bidhaa za ndani. Kuna hatua tunaona zinachukuliwa, tunaishukuru Serikali. Tulinde bidhaa za ndani dhidi ya bidhaa za nje. Viwanda na wafanyabiashara waliopo wana mambo mengi sana ambayo siwezi kuyasema, lakini Waheshimiwa Wabunge wamesema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali mmeonesha vizuri sana kwenye hotuba, lakini pia kkwenye Mpango, viwanda vya kimkakati. Ukisoma kwenye mpango vimejatwa vizuri; viwanda vya chuma, vimetajwa viwanda vinavyotumia mazao ya kilimo na viwanda vingine kama vya mazao ya uvuvi na mazao ya mifugo. Ukienda kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, unaona ni kiwanda kimoja tu cha chuma ndio cha kimkakati, lakini viwanda vingine; sijui kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua mbu, sio cha kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuangalie hasa viwanda vinavyotumia mazao ya kilimo. Hivi ni vya kimkakati kweli, sivioni kwenye speech! Kwa hiyo, tunaomba hilo liwe jambo la pili. Tunavyotaka kujenga viwanda vipya, ni hivi vitakavyohamasisha industrialization katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kuhamasisha wawekezaji. Tuliongea na wawekezaji wengi wa ndani na nje, wote walisema wanaonekana kama wezi. Mtazamo wa Watanzania wengi na mtazamo wa hata viongozi wengine, mwekezaji wa ndani anayepewa eneo kubwa anasumbuliwa, anaonekana mwizi, yule wa nje ndio kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, wawekezaji hawa wanahitaji misamaha. Japokuwa tulipitisha sheria mwaka jana, ile ya VAT ya mwaka 2015 nadhani, na mimi nilisimama hapa nikasema hii VAT ukiweka kwenye vifaa kwa ajili ya kutafuta madini, kwa ajili ya kuanzisha kiwanda, utafukuza wawekezaji. Kwa hiyo, nasema tena, tutazame hii misamaha tusiiogope.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ni kufufua viwanda vilivyokufa. Kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge, viko viwanda vya mazao ya kilimo kama pamba. Igunga kule tulikuwa na Manonga Ginnery, ilikufa. Hatutazamii kufufua viwanda vya namna hii. Kule Tabora ndugu yangu amesema; viwanda vya nyama Mwanza, Shinyanga na kadhalika tumeviacha; viwanda vya chuma Tanga na kadhalika, tuvifufue hivi. Kuna viwanda vingine kama CAMATECH na Mang‟ula, vitu vya namna hii tuvitazame, tuvifufue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niseme maeneo ya kuwekeza (EPZA), tulipe madeni. Serikali itafute fedha ilipe madeni, Shilingi bilioni 191. Fedha hizi zitafuteni mlipe ili mpate maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani, naomba nimalizie kwa kusema, tulikubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba ili tuweze kupata gist ya mambo haya, tuitishe Mkutono wa wadau na tulikubaliana tuitishe Dodoma kabla ya bajeti. Tulisema wadau ambao tunataka tuwaitishe, tuzungumze tufanye dialogue hii, tujue; tukipata yale maneno ndiyo tuyaingize kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mwaka kesho tutakuwa na mpango mzuri zaidi kwa sababu tutakuwa tumepata mawazo ya wenzetu. Kwa hiyo, wadau ambao tulikubaliana, Mheshimiwa Waziri na hii lazima uitishe labda hata wiki ijayo ili tupate mambo haya kwa ajili ya mwaka kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE.DKT. DALALY P. KAFUMU: Mhehimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi hii kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, na nakushukuru na wewe Mwenyekiti kwa kunipa nafasi. Lakini kama wenzangu walivyosema tuwapongeze Waziri na Naibu Waziri, pamoja na wataalam kwa kazi nzuri wanayofanya katika mazingira haya magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wana changamoto nyingi sana, mimi nilikuwa mmoja wao wakati fulani, kwa hiyo najua changamoto walizonazo, wanahitaji kuhudumia wananchi, lakini pia wanahitaji kuhakikisha wawekezaji wanaendelea kuja katika nchi yetu. Mnatakiwa kukaa katikati, ukihamia upande mmoja unaweza kuharibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nitasema maneno machache ya kutoa ushauri tu kwamba ukiangalia ukurasa wa 62 wa hotubua ya Mheshimiwa Waziri, kipengele 136, naomba nisome, kinasema; “Pamoja na bei ya madini ya dhahabu na nikeli kushuka katika soko la dunia, Serikali imeendelea kuhamasisha uendelezaji wa miradi mikubwa ya madini,” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri kwa kusema haya maneno, lakini ningependa sasa haya maneno ya-reflect katika vitendo vya Serikali katika kuhamasisha uwekezaji mkubwa. Sasa hivi ukipita mitaani huko ukisikiliza wawekezaji na wachimbaji wadogo kuna kilio kwamba Serikali imegeuka kidogo. Zile juhudi tulizofanya kuanzia mwaka 1995 Awamu ya Tatu na ya Nne zinakwenda tofauti kidogo, kwa hiyo mimi ningependa niwashauri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, hebu ongezeni juhudi za kuhamasisha wawekezaji waje tusipohamasisha hatutakuwa na migodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi utafutaji na ninyi ni mashahidi umepunga kweli na utafutaji unapopungua maana yake ni kwamba hatutakuwa na migodi siku za usoni, hii migodi ikifungwa basi. Napenda niseme kwamba Kamati ya Bomani ilitushauri tukatengeneza sera nzuri, tukatengeneza na sheria nzuri, tumekosea wapi sasa mpaka tuanze kurudi nyuma? Ukiwasikiliza wawekezaji wengine wanasema Tanzania ninyi mnataka kurudi kwenye ujamaa, ukisikiliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nashauri Mheshimwia Waziri, hebu tutoke hapo tulipo, tutengeneze mikakati sasa ya kuhamasisha. Kwa mfano tulikuwa tunaenda sana kwenye mikutano hii ambayo wawekezajiwote duniani wanakusanyika, tunawaalika. Miaka miwili iliyopita hatujaenda na wale wawekezaji wanaona Tanzania haimo tena kwenye kazi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaombeni sana tujitahidi tuwahamasishe wawekezaji, wasikate tamaa, ninyi ni mashahidi leseni nyingi sasa hivi zimekaa idle kwa kweli, japokuwa tumetengeneza mfumo mzuri lakini hazifanyi kazi kwa sababu tumekosea wapi, wataalam wa nishati na madini toeni ushauri jamani kitu gani kimetokea? Mimi inaniuma sanamnapoona juhudi zile za Serikali ya Awamu ya Tatu na ya Nne zinakwenda nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia majirani zetu Mozambique hata Malawi walitangaza geophysical results zao mwaka jana, sasa hivi wawekezaji wanaenda kule kutafuta dhahabu hii hii ambayo imeteremka bei. Kwa hiyo, mimi naomba sana na sisi tutazame tena wapi tumejikwaa, tuamke, ni ushauri tu ambao kwa kweli utatusaidia kwenda mbele upande wa madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine napenda niseme juu ya ushiriki wa watanzania, tunaishukuru Serikali kwa kuwasaidia wachimbaji wadogo kuwapa hii mitaji. Lakini hebu wasaidieni pia na katika kutafuta madini. Geological Survey of Tanzania moja ya kazi yake kwa sera ile tuliyotengeneza ni kuyaangalia hayo maeneo ya wachimbaji wadogo na kuyapa value kidogo ili waweze kufanya kazi zao vizuri. Lakini pia ni kuwasaidia katika environmental impact assessment ili waweze kuwa na tija katika uwekezaji wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kulisema ni ushauri ambao hua natoa kila mwaka na sasa hivi natoa, mnaweza msinielewe sasa lakini baadaye mtanielewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), ni wakala unaofanya kazi nzuri kama walivyosema, lakini unalipa Taifa hili gharama kubwa kwa sababu unafanya kazi zinazofanywa na taasisi zingine. Ngoja nitoe mfano, wanaangalia kampuni itaweza kulipa kodi, kazi ambayo inafanywa na TRA mnaweza mkasema ni audit, lakini kazi ni ile ile ukimuuliza mwekezaji anayekaguliwa na TMAA, mwekezaji anayekaguliwa na TRA anayekaguliwa na yule mkaguzi wa kisheria kazi wanazofanya ni zile zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunafumia hela nyingi kufanya jambo moja, ukiangalia wanafanya kazi ya ukaguzi wa mazingira, NEMC anakwenda kufanya jambo lile lile. Wanafanya kazi ya kuangalia madini yanavyopelekwa nje, wametengeneza ma-desk pale kwenye viwanja vya ndege, kazi hii ilitakiwa kufanywa na Ofisi ya Kamishna wa Madini kwa Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Mimi nasema skills na taaluma tuliyoijenga pale, hebu tuiweke mahali inapostahili, mimi ningependekeza na nimewahi kupendekeza kwamba hii kazi ifanywe na mtu mmoja sio watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaweza tukaifanya TMAA ikawa Idara ya TRA yenye Kamishna wake wa ukaguzi wa migodi na hizo skills zote tukamuachia TRA, itasaidia sana badala ya kufanya kazi mara mbili. Taarifa ninayoipata lazima iende TRA na kama amekosea mtu, TRA ndio anaechukua hatua, TRA akiacha inakuwaje? Kwa hiyo TMAA imewekwa hapo kufanya kazi za watu wengine ili watu wengine wachukue hizo information. Tunatumia fedha nyingi sana, kufanya jambo lile lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri tena, sasa hivi naweza nisieleweke nasema lakini siku za usoni nadhani nitaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kama nitapata muda, nataka nizungumzie mikataba ya madini. Mikataba ya madini watu wengi wanaisema tofauti, Sheria ya Madini…
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Ahsante sana.

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimshukuru Mungu tena kwa kunipa nafasi hii mara ya nne kuchangia katika Bunge lako.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali kwa mambo makubwa mawili. La kwanza, Serikali kutenga fedha nyingi kwenda kwenye maendeleo kwa sababu fedha hizi zitawafikia wananchi.
La pili, azma ya Serikali ya kujenga viwanda (nchi ya viwanda), hili ni jambo zuri na tunalipongeza. Tutakuwa na changamoto nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge wanazisema lakini nadhani tukitekeleza haya mambo mawili nchi yetu itafika mahali pazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie mambo kadhaa. La kwanza ni hili jambo la gratuity ya Wabunge, naomba nianze na hilo. Sheria ya mwaka 1999 ya Political Service Retirement Benefit iliwekwa makusudi kwamba viongozi hawa wa kisiasa spectrum yote mpaka DC, wamefanya kazi kubwa sana ya kuhangaika na wananchi, wanapewa retirement ya namna ile kwa kuwapongeza na kuwapa zawadi na hii ilikuwa ni hekima tangu mwaka 1981 sheria ilipotungwa na kurekebishwa. Sasa leo kama hekima ya Serikali ni kuiondoa, nadhani watafakari vizuri zaidi kama alivyosema Mheshimiwa Ngeleja ili kama ni lazima basi spectrum nzima ya viongozi iweze kulipa kodi kwenye mafao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amelisema tena Mheshimiwa Waziri wangu mstaafu ni kuhusu sekta ya uchimbaji wa madini ambapo kwenye nchi zingine ni injini ya uchumi wa nchi zile. Serikali ilianza vizuri sana miaka ya 1990 mpaka miaka mitano iliyopita kuhamasisha uchimbaji mkubwa pamoja na uchimbaji mdogo, lakini mwaka huu uchimbaji mkubwa sijausikia kabisa. Tutafanya makosa makubwa sana kwa sababu sekta hii ni sekta inayoleta FDI ya kutosha, ni sekta inayoleta ajira na mifano ya Afrika ipo. Botswana, South Africa, Mali, Ghana, Burkina Faso hata DRC Congo ni nchi ambazo uchumi wao unategemea sana madini, sasa sisi tunaacha kuwaalika wawekezaji wakubwa waje kuwekeza katika nchi yetu kufanya kazi hii, tunafanya makosa. Naomba Serikali tutafakari tena kuna kitu gani kimetokea, sheria nzuri tunayo, nilisema wakati nachangia kwenye madini na narudia tena jamani Serikali tuhamasishe uwekezaji katika spectrum yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni misamaha ambayo walikuwa wanapewa mashirika ya kidini wanapoingiza vitu kwa ajili ya shughuli zao. Serikali inasema watalipa halafu watarudishiwa, mimi nina mifano katika sekta ya madini, unapo-export unasamehewa VAT na unalipa hiyo VAT kurudishiwa ni ngoma. Makampuni yanaidai Serikali hii shilingi bilioni zaidi ya 100, wameshindwa kabisa kurudisha. Tusifikirie kurekebisha jambo kwa kuongeza kodi, turekebishe mfumo. Sisi kila kitu kikiharibika kwenye kodi tunaenda kwenye kodi badala ya kurekebisha mfumo ambao umefanya hii kodi isikusanywe. Kwa hiyo, naomba sana mashirika ya dini yanapoleta vitu kwa ajili ya kuhudumia wananchi wetu yasamehewe kama kawaida, turekebishe utaratibu wa kukusanya hizo kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nazungumza kidogo kidogo ili niweze kuchangia mambo mengi, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu watumishi wa umma. Mheshimiwa Rais alipoingia katika Serikali yake amefanya kazi moja nzuri sana ya kuhakikisha discipline inarudi katika utumishi wa umma. Amefanya ziara za kushtukiza na amefanya mambo makubwa na sisi tunamuunga mkono. Hata hivyo, kuna changamoto imejitokeza kwa wale wasaidizi wa Mheshimiwa Rais wameshindwa kurudi kwa wafanyakazi na kuwapa motisha (morali) ya kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtaalam mmoja wa mambo ya psychology ya institutional structures alisema hivi:-
“Leaders must know how to develop their EQ and put into practice to attain emotional intelligence, they need for insparing others to achieve. These emotionally excellent leaders are able to create a heart of an emotionally intelligent organization. An emotionally intelligent organization is one where its leaders and their followers exhibit a high level of emotionally excellence which allows them to connect one another and deliver in the organization.”
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi nchi yetu ni organization ambayo viongozi wanaosimamia wafanyakazi na wafanyakazi wenyewe lazima wawe na uhusiano ambao siyo wa paka na panya, uhusiano wa kuogopana, hatutapata mafanikio mazuri katika kufanya kazi.
Kwa hiyo, naomba wasaidizi wa Rais (Mawaziri na wasaidizi wao) hebu warudi kwenye Wizara zao. Mimi nimekaa kwenye Wizara, mtumishi usipompa hamasa ya kufanya kazi atagoma kimya kimya, huwezi ukapata matunda ya kazi yake. Leo hii ukienda kwenye Mawizara watu wameinama wanasema naogopa kutumbuliwa. Viongozi mnaosimamia watumishi, wahamasisheni watumishi wapende kazi yao, wasiogope, wajisikie kufanya kazi kuipenda nchi yao vinginevyo productivity itaharibika, tutaendelea kutumbua lakini hatutapata mafanikio mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nataka niseme habari za Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora ni mkubwa kuliko mikoa yote Tanzania na ndiyo maana tumeomba tuugawe. Mkoa wa Tabora una matatizo ya maji kuliko mikoa yote Tanzania. Mkoa huu unahitaji kutazamwa kwa jicho tofauti. Tunaomba ule mradi wa kuleta maji Mkoa wa Tabora kutoka kule Malagarasi utekelezwe ili Tabora tupate maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye elimu Tabora tunaonekana wa mwisho, lakini ni kwa sababu ni mkubwa, usimamizi unakuwa ni mgumu sana kwa viongozi wetu. Leo ninavyoongea Mkuu wa Mkoa wa Tabora hana gari, hawezi kutembea kabisa kuzungukia maeneo yake unategemea elimu itakuwaje? RAS naye pia hana gari na ma-DC wetu nao hawana magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iuangalie Mkoa wa Tabora na itusaidie tuweze kufanya kazi kuwahudumia wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu mdogo. Kwanza nimshukuru Mungu tena kwa kunipa nafasi hii kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu nichangie kama Wabunge wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri kwa speech lakini pia nampongeza kwa kazi ngumu aliyonayo mbele yake. Tunajua yeye ni mtaalam ataweza kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie mambo mawili tu, na kama nitakuwa na la tatu basi nitachangia. La kwanza, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 31 kifungu 3.4.10 anasema katika mwaka wa 2015/2016 Wizara imepitia Sheria ya Manunuzi ya Umma namba saba ya mwaka 2011 na kupendekeza marekebisho ya Sheria hiyo. Napenda niseme kati ya vichaka au sehemu ambazo zinatumika kumaliza fedha ya Taifa hili ni Sheria ya Manunuzi. Bei za tender za Serikali huwa ni za ajabu kweli, ni kwa sababu ya sheria hii. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kwa kweli sheria hii iletwe kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma sheria ambazo mmetupa tuangalie za marekebisho miscellaneous, hii sheria siioni, mtaileta nini? Maana yake ndiko huko fedha zinakopotelea. Tunaomba kama mnaweza kuileta hata kwa hati ya dharura tutashukuru kwa sababu matumizi ya Serikali yanatumika vibaya kulingana na sheria hii ya mwaka 2011. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka kusema ni juu ya kazi ya BOT (Benki Kuu ya Tanzania) na hili jambo niliwahi kusema na narudia tena, labda baadaye litaeleweka. Ni vizuri kusema sema hata kama ni jambo la uongo linaweza kuwa la kweli. Sisi tunachimba dhahabu katika nchi yetu, tuna migodi minne sasa inayotoa dhahabu. Kazi ya BOT ni kutunza fedha za kigeni lakini kutunza dhahabu safi na dhahabu ina represent utajiri wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati tulijaribu kununua dhahabu tukapata hasara kwa sababu tulinunua dhahabu, tulivyoipeleka kwenye smelting ikaonekana ni makapi lakini sasa tuna nafasi nzuri ya kupata dhahabu safi kwa kuwaambia makampuni watulipe nusu ya mrabaha katika dhahabu safi, hatuna tatizo. Hivi tunashindwa nini kuchukua dhahabu safi tukalipwa, tukaitunza ili baadae watoto wetu tutakapokufa tunawaambia bwana dhahabu hiyo mnaona mashimo hayo, ipo pale tani 200, 300 zimekaa. Uzuri wa kuwa na dhahabu kwenye reserve yetu tunaweza kurekebisaha hata thamani ya shilingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, thamani ya shilingi ikiteremka tuna-release kidogo inakuwa nzuri. Kwa hiyo, tuna wajibu sasa hivi kutunza dhahabu. Najua niliuliza swali mwaka jana, Serikali ikapiga chenga lakini nasema hatuna sababu ya kutokutunza dhahabu kwenye benki yetu. Nchi zingine kama Marekani wana tani 8,000 kwenye reserve yao. Ujerumani wana tani zaidi ya tani 3,000 hata Libya nchi inayopigana ina dhahabu 116 tani. Na nchi nyingi ambazo unaziona ni tajiri zote zina dhahabu kwenye reserve yao. Kwa nini tusifanye hivyo, kwa vile na sisi tunachimba dhahabu. Nchi za Afrika, iko South Africa, ina tani zaidi ya 100 kwenye reserve yao, sisi tuna shida gani? Sisi zero! Kwanini? Kwa hiyo naomba sana Serikali mtafakari jambo hili. Tafuteni wataalam waangalie namna tunavyoweza kufanya jambo hili tukapata dhahabu. (Makofi)
Jambo la tatu, ni matumizi holela ya dola katika nchi yetu. Dola inatumika mahali popote. Ukienda leo mahali popote hata Karikaoo unaweza ukatoa dola ukanunua, hata salon umekwenda kutengeneza nywele ukanunua kwa dola. Dola zetu zinapotea. Haziingii kwenye mfumo halali wa nchi, kwa hiyo dola zinaibiwa, zinapotezwa, zinabebwa kwa sababu tumeruhusu hili jambo. Ukienda South Africa ninyi mashahidi, huwezi kulipa hata hoteli ya kitalii kama huna dola, lazima ukatafute hela yaki-South Africa. Nenda nchi za Ulaya, hivyo hivyo, nenda Thailand, kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna ruhusu kila mahali dola inatumika, tunapoteza fedha. Serikali tunaomba tena, nilishawahi kuuliza swali mkapiga piga chenga, mimi naomba jamani uchumi wetu unaharibika kwa sababu tuna mifumo ambayo haisimamimii fedha zetu vizuri. Hili ni jambo sio zuri sana. Tunaomba Serikali msimamie jambo hili tungeni sheria. Tungeni sharia tuko tayari sisi Wabunge tutunge sheria ili fedha za kigeni ziweze kubaki kwenye reserve ya Taifa letu vinginevyo tuna kazi kubwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Ubelgiji huwezi ukatumia hela ya nje lazima uibadilishe iwe Euro sasa sisi tuna shida gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne na la mwisho, naomba nisipigiwe kengele, leo niko very smart. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuelimishwa kidogo, la kwanza ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya shilingi milioni 50. Amesema mama yangu pale, kwenye bajeti huko kote nimeangalia sioni, hivi tumeiwekea bajeti wapi?
Inawezekana nimeisoma vibaya, kwenye vitabu vyote nimeangalia hakuna mahali ambapo tumeweka fedha kwa ajili ya kutekeleza ile ahadi ya Rais, basi nielimisheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni MCC. MCC tuliiachia ikaondoka hatuna mradi wa MCC tena, labda kama kuna mazungumzo mapya. Hata hivyo, bado kuna subvote 1007 inasema imeweka hela shilingi milioni 500 kwa ajili ya MCC, ni kitu gani hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Anthony Calist Komu

Moshi Vijijini (CHADEMA)

Questions (2)

Supplementary Questions (5)

Contributions (2)

Profile

Hon. Esther Nicholus Matiko

Tarime Mjini (CHADEMA)

Questions (5)

Supplementary Questions (10)

Contributions (11)

Profile

Hon. Mbaraka Salim Bawazir

Kilosa (CCM)

Questions (0)

Supplementary Questions (1)

Contributions (3)

Profile

Hon. Vicky Paschal Kamata

Special Seats (CCM)

Questions (0)

Supplementary Questions (1)

Contributions (2)

Profile

View All MP's